Categories
Ezekieli

Ezekieli 43

Utukufu Warudi Hekaluni

1 Kisha yule mtu akanileta kwenye lango linaloelekea upande wa mashariki,

2 nami nikaona utukufu wa Mungu wa Israeli ukija kutoka upande wa mashariki. Sauti yake ilikuwa kama ya ngurumo ya maji yaendayo kasi, nayo nchi ikangʼaa kwa utukufu wake.

3 Maono niliyoyaona yalikuwa kama maono yale niliyokuwa nimeyaona wakati Mungu alipokuja kuangamiza mji na kama maono niliyokuwa nimeyaona kando ya Mto wa Kebari, nami nikaanguka kifudifudi.

4 Utukufu waBwanaukaingia hekaluni kwa kupitia lango linaloelekea upande wa mashariki.

5 Kisha Roho akanichukua na kunileta katika ule ua wa ndani, nao utukufu waBwanaulilijaza Hekalu.

6 Wakati yule mtu akiwa amesimama kando yangu, nilisikia mtu mmoja akisema nami kutoka ndani ya Hekalu.

7 Akasema, “Mwanadamu, hapa ni mahali pa kiti changu cha enzi na mahali pa kuweka nyayo za miguu yangu. Hapa ndipo nitakapoishi miongoni mwa Waisraeli milele. Kamwe nyumba ya Israeli hawatalinajisi tena Jina langu takatifu, yaani, wao wala wafalme wao, kwa ukahaba wao na kwa sanamu zao zisizokuwa na uhai za wafalme wao katika mahali pao pa juu pa kuabudia miungu.

8 Walipoweka kizingiti chao karibu na kizingiti changu na miimo yao ya milango karibu na miimo yangu, pakiwa na ukuta tu kati yangu na wao, walilinajisi Jina langu takatifu kwa matendo yao ya machukizo. Kwa sababu hiyo niliwaangamiza kwa hasira yangu.

9 Basi sasa na waweke mbali nami ukahaba wao na sanamu za wafalme wao zisizo na uhai, nami nitakaa miongoni mwao milele.

10 “Mwanadamu, elezea hilo Hekalu kwa watu wa Israeli, ili wapate kuona aibu kwa ajili ya dhambi zao. Wao na wapime hicho kielelezo.

11 Wakishaona aibu kwa ajili ya yale yote waliyotenda, wafahamishe kielelezo cha hilo Hekalu, yaani mpangilio wake, maingilio yake ya kutoka na kuingia, kielelezo chake chote, na masharti yake yote na sheria zake zote. Yaandike haya mbele yao ili wapate kuwa waaminifu kwa hicho kielelezo chake na kufuata masharti yake yote.

12 “Hii ndiyo sheria ya Hekalu: Eneo lote linalozunguka Hekalu juu ya mlima litakuwa takatifu kuliko yote. Hii ndiyo sheria ya Hekalu.

Madhabahu

13 “Hivi ndivyo vipimo vya madhabahu kwa dhiraa ndefu, yaani, dhiraa moja na nyanda nne:Tako lake liwe na kina cha hiyo dhiraa moja na upana wa hiyo dhiraa moja, ikiwa na ukingo wa shibiri mojakuizunguka pembeni. Hiki kitakuwa ndicho kimo cha madhabahu:

14 Kimo cha msingi kuanzia usawa wa ardhi mpaka kwenye mfereji sehemu ya chini kimo chake ni dhiraa mbili na upana wake ni dhiraa moja na kuanzia kwenye ukingo mdogo hadi kwenye ukingo mpana kimo chake ni dhiraa nne na upana wake ni dhiraa moja.

15 Pale pawashwapo moto madhabahuni kimo chake kitakuwa dhiraa nne, na pembe nne zinazoelekeza juu kutoka pale pawashwapo moto.

16 Pale pawashwapo moto pa madhabahu ni mraba, urefu wake ni dhiraa kumi na mbilina upana wa dhiraa kumi na mbili.

17 Pia sehemu ya juu ni mraba, urefu wake dhiraa kumi na nne na upana wa dhiraa kumi na nne, ikiwa na ukingo wa nusu dhiraa na mfereji kuizunguka madhabahu. Ngazi za kupandia madhabahuni zitaelekea upande wa mashariki.”

18 Kisha akaniambia, “Mwanadamu, hili ndiloBwanaMwenyezi asemalo: Haya ndiyo yatakayokuwa masharti ya kutoa dhabihu za kuteketezwa na kunyunyiza damu juu ya madhabahu itakapokuwa imejengwa.

19 Utatoa fahali mchanga kuwa sadaka ya dhambi kwa makuhani, ambao ni Walawi, wa jamaa ya Sadoki, ndio watakaonikaribia kuhudumu mbele zangu, asemaBwanaMwenyezi.

20 Itakupasa kuchukua baadhi ya hiyo damu ya mnyama huyo na kuiweka juu ya hizo pembe nne za madhabahu na juu ya ncha zake nne za sehemu ya juu kuzunguka ukingo wote, ili kuitakasa madhabahu na kufanya upatanisho kwa ajili yake.

21 Itakupasa kumchukua huyo fahali mchanga kwa ajili ya sadaka ya dhambi na kumteketeza mahali palipoagizwa katika eneo la Hekalu nje ya mahali Patakatifu.

22 “Siku ya pili yake utamtoa beberu asiye na dosari kwa ajili ya sadaka ya dhambi, nayo madhabahu itatakaswa kama ilivyotakaswa kwa yule fahali.

23 Utakapokuwa umemaliza kazi ya kuitakasa, utamtoa fahali mchanga pamoja na kondoo dume toka kwenye kundi, wote wawe hawana dosari.

24 Utawatoa mbele zaBwana, nao makuhani watanyunyizia chumvi juu yao na kuwatoa kuwa sadaka ya kuteketezwa kwaBwana.

25 “Kwa siku saba itakupasa kutoa beberu kila siku kwa ajili ya sadaka ya dhambi, pia itakupasa kutoa fahali mchanga na kondoo dume kutoka zizini, wote wawe hawana dosari.

26 Kwa siku saba itawapasa kufanya upatanisho kwa ajili ya madhabahu na kuitakasa na hivyo ndivyo watakavyoiweka wakfu.

27 Mwishoni mwa hizi siku saba, kuanzia siku ya nane na kuendelea, itawapasa makuhani kutoa sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka za amani juu ya madhabahu. Kisha nitawakubali ninyi, asemaBwanaMwenyezi.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/EZK/43-d0abc399774505642729302e3f2b8aca.mp3?version_id=1627—

Categories
Ezekieli

Ezekieli 44

Mkuu, Walawi, Makuhani

1 Ndipo yule mtu akanirudisha mpaka kwenye lango la nje la mahali Patakatifu, lile linaloelekea upande wa mashariki, nalo lilikuwa limefungwa.

2 Bwanaakaniambia, “Lango hili litabaki limefungwa. Haliruhusiwi kufunguliwa, wala hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kuingilia kwenye lango hili. Litabaki limefungwa kwa sababuBwana, Mungu wa Israeli, ameingia kwa kupitia lango hili.

3 Yeye aliye mkuu peke yake ndiye anayeweza kukaa penye njia ya hilo lango na kula chakula mbele zaBwana. Itampasa aingie kwa njia hiyo ya lango la ukumbini na kutokea njia iyo hiyo.”

4 Kisha yule mtu akanileta kwa njia ya lango la kaskazini mpaka mbele ya Hekalu. Nikatazama nami nikauona utukufu waBwanaukilijaza Hekalu laBwana, nami nikaanguka kifudifudi.

5 Bwanaakaniambia, “Mwanadamu, angalia kwa uangalifu, usikilize kwa bidii na uzingatie kila kitu ninachokuambia kuhusu masharti yote yanayohusu Hekalu laBwana. Uwe mwangalifu kuhusu wale wanaoruhusiwa hekaluni na wale wasioruhusiwa kuingia mahali patakatifu.

6 Iambie nyumba ya kuasi ya Israeli, ‘Hili ndiloBwanaMwenyezi asemalo: Matendo yenu ya machukizo yatosha, ee nyumba ya Israeli!

7 Zaidi ya matendo yenu yote ya machukizo, mmewaleta wageni wasiotahiriwa mioyo na miili katika patakatifu pangu, mkilinajisi Hekalu langu, huku mkinitolea chakula, mafuta ya wanyama na damu, nanyi mmevunja Agano langu.

8 Badala ya kutimiza wajibu wenu kuhusiana na vitu vyangu vitakatifu, mmeweka watu wengine kuwa viongozi katika patakatifu pangu.

9 Hili ndiloBwanaMwenyezi asemalo: Hakuna mgeni asiyetahiriwa moyo na mwilini anayeruhusiwa kuingia patakatifu pangu, wala hata wageni wanaoishi miongoni mwa Waisraeli.

10 “ ‘Walawi walioniacha wakati Waisraeli walipopotoka wakatoka kwangu na kutangatanga kwa kufuata sanamu zao, watachukua adhabu ya dhambi zao.

11 Wanaweza wakatumika katika mahali patakatifu pangu, wakiwa na uangalizi wa malango ya Hekalu, nao watachinja sadaka za kuteketezwa na dhabihu kwa ajili ya watu na kusimama mbele ya watu ili kuwahudumia.

12 Lakini kwa sababu waliwatumikia watu mbele ya sanamu zao na kuifanya nyumba ya Israeli ianguke kwenye dhambi, kwa hiyo nimeapa kwa mkono ulioinuliwa kwamba ni lazima wachukue matokeo ya dhambi yao, asemaBwanaMwenyezi.

13 Hawaruhusiwi kukaribia ili kunitumikia kama makuhani wala kukaribia chochote changu kilicho kitakatifu au sadaka iliyo takatifu kupita zote, bali watachukua aibu ya matendo yao ya kuchukiza.

14 Lakini nitawaweka katika uangalizi wa Hekalu na kazi zote zile zinazotakiwa kufanyika ndani yake.

15 “ ‘Lakini makuhani, ambao ni Walawi na wazao wa Sadoki, ambao walitimiza wajibu wao kwa uaminifu katika patakatifu pangu wakati Waisraeli walipopotoka, watakaribia ili kutumika mbele zangu. Itawapasa wasimame mbele zangu ili kutoa dhabihu za mafuta ya wanyama na damu, asemaBwanaMwenyezi.

16 Wao peke yao ndio wenye ruhusa ya kuingia mahali patakatifu pangu. Wao peke yao ndio watakaokaribia meza yangu ili kuhudumu mbele zangu na kufanya utumishi wangu.

17 “ ‘Watakapoingia kwenye malango ya ukumbi wa ndani, watavaa nguo za kitani safi, hawaruhusiwi kamwe kuvaa mavazi ya sufu wakati wanapokuwa wakihudumu kwenye malango ya ukumbi wa ndani wala ndani ya Hekalu.

18 Watavaa vilemba vya kitani safi vichwani mwao na nguo za ndani za kitani safi viunoni mwao. Hawatavaa chochote kitakachowafanya kutoa jasho.

19 Watakapotoka ili kuingia katika ukumbi wa nje mahali watu walipo, watavua nguo walizokuwa wakihudumu nazo na wataziacha katika vyumba vitakatifu nao watavaa nguo nyingine, ili kwamba wasije wakaambukiza watu utakatifu kwa njia ya mavazi yao.

20 “ ‘Hawatanyoa nywele za vichwa vyao wala kuziacha ziwe ndefu, bali watazipunguza.

21 Kuhani yeyote asinywe mvinyo aingiapo katika ukumbi wa ndani.

22 Wasioe wanawake wajane wala walioachika, inawapasa kuoa wanawake bikira wenye heshima wa Israeli au wajane wa makuhani.

23 Watawafundisha watu wangu tofauti kati ya vitu vitakatifu na vitu vya kawaida na kuwaonyesha jinsi ya kupambanua kati ya vitu najisi na vitu safi.

24 “ ‘Katika magombano yoyote, makuhani watatumika kama mahakimu na kuamua hilo jambo kufuatana na sheria zangu. Watazishika sheria zangu na maagizo yangu katika sikukuu zangu zote zilizoamriwa, nao watatakasa Sabato zangu.

25 “ ‘Kuhani asijitie unajisi kwa kukaribia maiti, lakini, kama mtu aliyekufa alikuwa baba yake au mama yake, mwana au binti yake, ndugu yake au dada ambaye hajaolewa, basi aweza kujitia unajisi kwa hao.

26 Baada ya kujitakasa, atakaa hali hiyo kwa muda wa siku saba.

27 Siku atakapoingia katika ukumbi wa ndani wa mahali patakatifu ili kuhudumu, atatoa sadaka ya dhambi kwa ajili yake mwenyewe, asemaBwanaMwenyezi.

28 “ ‘Mimi nitakuwa ndio urithi pekee walio nao makuhani katika Israeli. Msiwape wao milki, mimi nitakuwa milki yao.

29 Wao watakula sadaka za nafaka, sadaka za dhambi na sadaka za hatia na kila kitu kitakachotolewa kwaBwanakatika Israeli kitakuwa chao.

30 Yote yaliyo bora ya malimbuko ya vitu vyote na matoleo yenu maalum vitakuwa vya makuhani. Inawapasa kuwapa malimbuko ya kwanza ya unga wenu ili kwamba baraka ipate kuwa katika nyumba zenu.

31 Makuhani hawaruhusiwi kula chochote, ikiwa ni ndege au mnyama, aliyekutwa akiwa amekufa au aliyeraruliwa na wanyama pori.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/EZK/44-e04fe73cdf5e32e3ae40081a84dfc016.mp3?version_id=1627—

Categories
Ezekieli

Ezekieli 45

Mgawanyo Wa Nchi

1 “ ‘Mtakapogawa nchi kuwa urithi, mtaitoa sehemu ya nchi kwaBwanakuwa eneo takatifu, urefu wake dhiraa 25,000,upana wake dhiraa 20,000eneo hili lote litakuwa takatifu.

2 Katika hiyo, itakuwepo sehemu mraba ambayo ni mahali patakatifu kila upande dhiraa 500 ikiwa imezungukwa na eneo la wazi lenye upana wa dhiraa hamsini.

3 Katika eneo takatifu, pima sehemu yenye urefu wa dhiraa 25,000 na upana wa dhiraa 10,000.Ndani ya hilo eneo kutakuwa mahali patakatifu, Patakatifu pa Patakatifu.

4 Itakuwa sehemu takatifu ya nchi kwa ajili ya makuhani, wale wanaohudumu ndani ya mahali patakatifu na ambao hukaribia ili kuhudumu mbele zaBwana. Patakuwa mahali pa nyumba zao pamoja na sehemu kwa ajili ya mahali patakatifu.

5 Eneo la urefu wa dhiraa 25,000 na upana wa dhiraa 10,000 litakuwa la Walawi wale wanaotumika hekaluni, kama milki yao kwa ajili ya miji ya kuishi.

6 “ ‘Utatoa mji kama mali yao wenye upana wa dhiraa 5,000na urefu wa dhiraa 25,000, karibu na sehemu takatifu, itakuwa mali ya nyumba yote ya Israeli.

7 “ ‘Mkuu anayetawala atakuwa na lile eneo linalopakana na lile eneo lililowekwa wakfu upande huu na upande huu na eneo la mji. Eneo la mji litaenea upande wa magharibi kuanzia upande wa magharibi na upande wa mashariki kuanzia upande wa mashariki, likiendelea kwa urefu kutoka magharibi hadi mpaka wa mashariki sambamba na mojawapo ya sehemu za makabila.

8 Nchi hii itakuwa milki yake katika Israeli. Nao wakuu wangu hawataonea tena watu wangu bali watairuhusu nyumba ya Israeli kuimiliki nchi kulingana na makabila yao.

9 “ ‘Hili ndiloBwanaMwenyezi asemalo: Yatosha, enyi wakuu wa Israeli! Acheni mbali ukatili wenu na uonevu wenu mkafanye lile lililo haki na sawa. Acheni kuwatoza watu wangu isivyo haki, asemaBwanaMwenyezi.

10 Tumieni mizani sahihi na vipimo sahihi vya efana bathi.

11 Efa na bathi viwe sawa, bathi iwe sehemu ya kumi ya homeri na efa iwe sehemu ya kumi ya homeri, homeri itakuwa ndicho kiwango cha kukubalika kwa vyote viwili.

12 Shekeli moja itakuwa gera ishirini.Shekeli ishirini, jumlisha na shekeli ishirini na tano, jumlisha na shekeli kumi na tano zitakuwa mina moja.

Sadaka Na Siku Takatifu

13 “ ‘Hili ndilo toleo maalum mtakalotoa: moja ya sita ya efa kutoka kila homeri ya ngano na moja ya sita ya efa kutoka kila homeri ya shayiri.

14 Sehemu ya mafuta iliyoamriwa, yaliyopimwa kwa bathi, ni sehemu ya kumi ya bathi kutoka kila kori moja(ambayo ina bathi kumi au homeri moja.)

15 Pia kondoo mmoja atachukuliwa kutoka kwenye kila kundi la kondoo mia mbili kutoka kwenye malisho yaliyonyeshewa vizuri ya Israeli. Hivi vitatumika kwa ajili ya sadaka ya nafaka, sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani ili kufanya upatanisho kwa ajili ya watu, asemaBwanaMwenyezi.

16 Watu wote wa nchi wataungana pamoja na mkuu anayetawala Israeli ili kutoa hii sadaka maalum.

17 Huu utakuwa ndio wajibu wa mkuu anayetawala kutoa sadaka ya kuteketezwa, sadaka ya nafaka na sadaka ya kinywaji kwenye sikukuu, Mwezi Mwandamo na Sabato, kwenye sikukuu zote zilizoamriwa za nyumba ya Israeli. Atatoa sadaka za dhambi, sadaka za nafaka, sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nyumba ya Israeli.

18 “ ‘Hili ndiloBwanaMwenyezi asemalo: Katika mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya huo mwezi utamchukua fahali mchanga asiye na dosari na kutakasa mahali patakatifu.

19 Kuhani itampasa achukue sehemu ya hiyo damu ya sadaka ya dhambi na kuipaka kwenye miimo ya Hekalu, kwenye pembe nne za juu za ukingo wa hayo madhabahu na juu ya miimo ya lango la ukumbi wa ndani.

20 Itakupasa kufanya vivyo hivyo katika siku ya saba ya mwezi huo kwa ajili ya mtu yeyote ambaye hutenda dhambi bila kukusudia au bila kujua, hivyo utafanya upatanisho kwa ajili ya Hekalu.

21 “ ‘Katika mwezi wa kwanza siku ya kumi na nne utaadhimisha Pasaka. Sikukuu itaendelea kwa siku saba, wakati huo wa hizo siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu.

22 Katika siku hiyo mkuu anayetawala atatoa fahali kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya watu wote wa nchi.

23 Kila siku wakati wa hizo siku saba za sikukuu atatoa mafahali saba na kondoo dume saba wasio na dosari kuwa sadaka ya kuteketezwa kwaBwanana beberu kwa ajili ya sadaka ya dhambi.

24 Pia atatoa sadaka ya nafaka efa moja kwa kila fahali na efa moja kwa kila kondoo dume, pamoja na hini mojaya mafuta kwa kila efa.

25 “ ‘Wakati wa hizo siku saba za sikukuu, ambayo huanza katika mwezi wa saba kwenye siku ya kumi na tano, mkuu anayetawala atatoa mahitaji yale yale kwa ajili ya sadaka za dhambi, sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka na mafuta.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/EZK/45-2d6ce2a5485b62a15f54344cd88bc98d.mp3?version_id=1627—

Categories
Ezekieli

Ezekieli 46

Sheria Nyingine Mbalimbali

1 “ ‘Hili ndiloBwanaMwenyezi asemalo: Lango la ukumbi wa ndani linaloelekea upande wa mashariki litakuwa linafungwa kwa siku sita za juma, ila siku ya Sabato na siku ya Mwezi Mwandamo litafunguliwa.

2 Mkuu anayetawala ataingia kupitia baraza ya njia ya lango la ukumbi na kusimama karibu na nguzo ya lango. Makuhani watatoa sadaka za mkuu anayetawala za kuteketezwa na sadaka za amani. Mkuu anayetawala atasujudu kwenye kizingiti cha njia ya lango, kisha atatoka nje, lakini lango halitafungwa mpaka jioni.

3 Siku za Sabato na za Mwezi mwandamo watu wote wa nchi wataabudu mbele zaBwanapenye lile ingilio la ile njia.

4 Sadaka ya kuteketezwa aletazo mkuu anayetawala kwaBwanasiku ya Sabato itakuwa ni wana-kondoo sita na kondoo dume mmoja, wote wasiwe na dosari.

5 Sadaka ya nafaka inayotolewa pamoja na huyo kondoo dume itakuwa efa moja na sadaka ya nafaka inayotolewa na hao wana-kondoo itakuwa kiasi apendacho mtu pamoja na hini ya mafuta kwa kila efa.

6 Siku ya mwezi mwandamo atatoa fahali mchanga, wana-kondoo sita na kondoo dume, wote wasiwe na dosari.

7 Atatoa kuwa sadaka ya nafaka efa moja pamoja na fahali mmoja, efa moja na kondoo dume mmoja na pamoja na wana-kondoo kama atakavyo kutoa, pamoja na hini ya mafuta kwa kila efa.

8 Wakati mkuu anayetawala aingiapo, atapitia kwenye baraza ya njia ya lango, naye atatoka nje kwa njia hiyo hiyo.

9 “ ‘Wakati watu wa nchi wanapokuja mbele zaBwanakatika sikukuu zilizoamriwa, yeyote aingiaye kwa lango la kaskazini kuabudu atatoka nje kwa lango la kusini na yeyote aingiaye kwa lango la kusini atatoka nje kwa lango la kaskazini. Hakuna mtu yeyote atakayerudi kwa kupitia lango lile aliloingilia, lakini kila mmoja atatoka nje kwa lango linalokabili lile aliloingilia.

10 Mkuu anayetawala atakuwa miongoni mwao, akiingia nao ndani wanapoingia, naye atatoka nao nje wanapotoka.

11 “ ‘Kwenye sikukuu na kwenye sikukuu zilizoamriwa, sadaka ya nafaka itakuwa efa moja pamoja na fahali mmoja, efa moja pamoja na kondoo dume mmoja, pamoja na idadi ya wana-kondoo kama mtu apendavyo kutoa, pamoja na hini ya mafuta kwa kila efa.

12 Mkuu anayetawala anapotoa sadaka ya hiari kwaBwana, ikiwa ni sadaka ya kuteketezwa au sadaka ya amani, lango linaloelekea mashariki litafunguliwa kwa ajili yake. Atatoa sadaka yake ya kuteketezwa au sadaka yake ya amani kama afanyavyo katika siku ya Sabato. Kisha atatoka nje, naye akiisha kutoka nje, lango litafungwa.

13 “ ‘Kila siku utamtoa mwana-kondoo wa mwaka mmoja asiyekuwa na dosari kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa kwaBwana, utaitoa kila siku asubuhi.

14 Pia kila siku asubuhi pamoja na hiyo sadaka utatoa sadaka ya nafaka, ikiwa na sehemu ya sita ya efa pamoja na theluthi moja ya hiniya mafuta ya kuchanganya na ule unga. Utoaji wa sadaka hii ya nafaka kwaBwanani amri ya daima.

15 Kwa hiyo mwana-kondoo na sadaka ya nafaka na mafuta vitatolewa kila siku asubuhi kwa ajili ya sadaka ya daima ya kuteketezwa.

16 “ ‘Hili ndiloBwanaMwenyezi asemalo: Ikiwa mkuu atawalaye atatoa zawadi kutoka kwenye urithi wake na kumpa mmoja wa wanawe, hiyo zawadi itakuwa pia kwa wazao wake, itakuwa mali yao kwa urithi.

17 Hata hivyo, kama atatoa zawadi kutoka urithi wake na kumpa mmoja wa watumishi wake, mtumishi anaweza kuiweka mpaka mwaka wa uhuru, kisha itarudishwa kwa mkuu anayetawala. Urithi wake ni wa wanawe peke yao, ni mali yao.

18 Mkuu anayetawala hana ruhusa kuchukua urithi wowote wa watu na kuwaondoa kwenye mali zao. Mkuu atawalaye atawapa wanawe urithi wao, kutoka kwenye mali zake mwenyewe, ili kwamba pasiwe na mtu wangu yeyote atakayetengwa na urithi wake.’ ”

19 Kisha mtu yule akanileta kwa kupitia kwenye ingilio lililokuwa kando ya lango mpaka kwenye vyumba vitakatifu vinavyoelekea kaskazini, ambavyo ni vya makuhani, naye akanionyesha mahali fulani upande wa mwisho wa magharibi.

20 Akaniambia, “Mahali hapa ndipo makuhani watakapotokosea sadaka ya hatia na sadaka ya dhambi na kuoka sadaka ya nafaka, kuepuka kuzileta katika ukumbi wa nje na kushirikisha utakatifu kwa watu.”

21 Baada ya hapo akanileta kwenye ukumbi wa nje na kunizungusha kwenye pembe zake nne, nami nikaona katika kila pembe ya huo ukumbi kulikuwa na ukumbi mwingine.

22 Katika pembe nne za huo ukumbi wa nje kulikuwa na kumbi nyingine, zenye urefu wa dhiraa arobaini na upana wake dhiraa thelathini, ambapo hizo kumbi kwenye hizo pembe nne zilikuwa na vipimo vilivyo sawa.

23 Mzunguko wa ndani wa hizo kumbi nne ulikuwa na ukingo wa jiwe, zikiwa na sehemu zilizojengwa kwa ajili ya moto kuzunguka chini ya huo ukingo.

24 Akaniambia, “Hizi ndizo sehemu za kupikia ambazo wale wanaohudumu kwenye Hekalu watatokosea dhabihu za watu.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/EZK/46-2670619042ff791d89347c9c9e183386.mp3?version_id=1627—

Categories
Ezekieli

Ezekieli 47

Mto Kutoka Hekaluni

1 Yule mtu akanirudisha mpaka kwenye ingilio la Hekalu, nami nikaona maji yakitoka chini ya kizingiti cha Hekalu yakitiririkia upande wa mashariki (kwa maana upande wa mbele wa Hekalu ulielekea mashariki). Maji yalikuwa yakitoka chini upande wa kusini wa Hekalu, kusini mwa madhabahu.

2 Ndipo akanitoa nje kupitia lango la kaskazini na kunizungusha mpaka kwenye lango la nje linaloelekea mashariki, nayo maji yalikuwa yakitiririka kutoka upande wa kusini.

3 Mtu yule alipokwenda upande wa mashariki akiwa na kamba ya kupimia mkononi mwake, akapima dhiraa 1,000kisha akanipitisha kwenye hayo maji ambayo yalifika kwenye vifundo vya miguu.

4 Akapima dhiraa 1,000 nyingine na kunipitisha kwenye hayo maji ambayo yalifika magotini. Akapima dhiraa nyingine 1,000 na kunipitisha kwenye hayo maji ambayo yalifika kiunoni.

5 Akapima tena dhiraa 1,000 nyingine, lakini wakati huu yalikuwa mto ambao sikuweza kuvuka, kwa kuwa maji yalikuwa na kina kirefu ambacho ni cha kuogelea, mto ambao hakuna mtu yeyote ambaye angeweza kuvuka.

6 Akaniuliza, “Je, mwanadamu, unaona hili?”

Kisha akanirudisha mpaka kwenye ukingo wa huo mto.

7 Nilipofika pale, nikaona idadi kubwa ya miti kila upande wa ule mto.

8 Akaniambia, “Haya maji yanatiririka kuelekea nchi ya mashariki na kushuka mpaka Araba,ambapo huingia Baharini. Yanapomwagikia kwenye hiyo Bahari,maji yaliyoko humo huponywa na kuwa safi.

9 Popote mto huu uendapo kila kiumbe hai kinachoyaparamia hayo maji kitaishi, nako kutakuwa na samaki wengi mno, mara maji haya yafikapo huko. Maji hayo yatakuwa hai na kila kitu kitakachoishi kule mto uendako.

10 Wavuvi watasimama kando ya bahari, kuanzia En-Gedi hadi En-Eglaimu huko patakuwa mahali pa kutandaza nyavu za kuvulia samaki. Samaki watakuwa wa aina nyingi, kama samaki wa Bahari Kuu

11 Lakini madimbwi yake na mabwawa yake hayatakuwa na maji yanayofaa kunywa, bali yatabakia kuwa maji ya chumvi.

12 Miti ya matunda ya kila aina itaota kwenye kingo zote mbili za mto huu. Majani yake hayatanyauka wala haitaacha kuwa na matunda katika matawi yake. Kila mwezi kutakuwa na matunda, kwa sababu maji yatokayo patakatifu yanaitiririkia. Matunda yake yatakuwa chakula na majani yake yatakuwa dawa.”

Mipaka Mipya Ya Nchi

13 Hili ndiloBwanaMwenyezi asemalo: “Hii ndiyo mipaka ambayo kwayo mtagawanya hiyo nchi kuwa urithi miongoni mwa hayo makabila kumi na mawili ya Israeli, pamoja na mafungu mawili ya Yosefu.

14 Mtagawa kwa usawa miongoni mwao. Kwa sababu niliapa kwa mkono ulioinuliwa kuwapa baba zenu, nchi hii itakuwa urithi wenu.

15 “Huu ndio utakuwa mpaka wa hiyo nchi:

“Upande wa kaskazini utaanzia Bahari Kuu kwa njia ya Hethloni kupitia Lebo-Hamathi hadi maingilio ya Sedadi.

16 Berotha na Sibraimu (ambao uko kwenye mpaka kati ya Dameski na Hamathi), hadi kufikia Haser-Hatikoni, ambao uko katika mpaka wa Haurani.

17 Hivyo mpaka utaendelea kuanzia Baharini hadi Hasar-Enoni, ukiambaa na mpaka wa kaskazini wa Dameski, pamoja na mpaka wa Hamathi upande wa kaskazini. Huu utakuwa ndio mpaka wa kaskazini.

18 Upande wa mashariki mpaka utapita kati ya Haurani na Dameski, kuambaa Yordani na kati ya Gileadi na nchi ya Israeli, hadi bahari ya masharikina kufika Tamari. Huu utakuwa ndio mpaka wa mashariki.

19 Upande wa kusini utaanzia Tamari hadi kufikia maji ya Meriba-Kadeshi, kisha utaambaa na Kijito cha Misri hadi Bahari Kuu. Huu utakuwa ndio mpaka wa kusini.

20 Upande wa magharibi, Bahari Kuu itakuwa ndio mpaka hadi kwenye sehemu mkabala na Lebo-Hamathi. Huu utakuwa ndio mpaka wa magharibi.

21 “Mtagawanya nchi hii miongoni mwenu kufuatana na makabila ya Israeli.

22 Mtaigawanya kuwa urithi kwa ajili yenu na kwa ajili ya wageni wanaoishi miongoni mwenu na ambao wana watoto. Wao watakuwa kwenu kama wenyeji wazawa wa Israeli, pamoja na ninyi watagawiwa urithi miongoni mwa makabila ya Israeli.

23 Katika kabila lolote mgeni atakapoishi hapo ndipo mtakapompatia urithi wake,” asemaBwanaMwenyezi.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/EZK/47-d3f55158735d6aa2e920f380f131826c.mp3?version_id=1627—

Categories
Ezekieli

Ezekieli 48

Mgawanyo Wa Nchi

1 “Haya ndiyo majina ya makabila na sehemu zao: Kwenye mpaka wa kaskazini, Dani atakuwa na sehemu moja, mpaka huo utafuata barabara ya Hethloni hadi Lebo-Hamathi, Hasar-Enani hata mpaka wa kaskazini wa Dameski karibu na Hamathi utakuwa sehemu ya huo mpaka wake kuanzia upande wa mashariki hadi upande wa magharibi.

2 “Asheri atakuwa na sehemu moja, itapakana na nchi ya Dani kuanzia mashariki hadi upande wa magharibi.

3 “Naftali atakuwa na sehemu moja, itapakana na nchi ya Asheri kuanzia mashariki hadi magharibi.

4 “Manase atakuwa na sehemu moja, itapakana na nchi ya Naftali kuanzia mashariki hadi magharibi.

5 “Efraimu atakuwa na sehemu moja, itapakana na nchi ya Manase kuanzia mashariki hadi magharibi.

6 “Reubeni atakuwa na sehemu moja, itapakana na nchi ya Efraimu kuanzia mashariki hadi magharibi.

7 “Yuda atakuwa na sehemu moja, itapakana na nchi ya Reubeni kuanzia mashariki hadi magharibi.

8 “Kupakana na nchi ya Yuda kuanzia mashariki mpaka magharibi itakuwa ndiyo sehemu utakayoitoa ili kuwa toleo maalum. Itakuwa na upana wa dhiraa 25,000na urefu wake kuanzia mashariki mpaka magharibi utakuwa ule ule wa sehemu moja ya kabila, mahali patakatifu patakuwa katikati ya eneo hilo.

9 “Hiyo sehemu maalum mtakayotoa kwaBwanaitakuwa na urefu wa dhiraa 25,000 na upana wa dhiraa 10,000

10 Hii itakuwa ni sehemu takatifu kwa ajili ya makuhani. Itakuwa na urefu wa dhiraa 25,000 upande wa kaskazini, upana wa dhiraa 10,000 upande wa magharibi, dhiraa 10,000 upande wa mashariki na urefu wa dhiraa 25,000 upande wa kusini. Katikati yake patakuwa mahali patakatifu paBwana.

11 Hii itakuwa kwa ajili ya makuhani waliowekwa wakfu, Wasadoki, waliokuwa waaminifu katika kunitumikia nao hawakupotoka kama Walawi walivyofanya wakati Waisraeli walipopotoka.

12 Itakuwa toleo maalum kwao kutoka sehemu takatifu ya nchi, yaani, sehemu takatifu sana, inayopakana na nchi ya Walawi.

13 “Kando ya nchi ya makuhani, Walawi watakuwa na mgawo wa urefu wa dhiraa 25,000 na upana wa dhiraa 10,000. Urefu wake utakuwa jumla dhiraa 25,000 na upana wa dhiraa 10,000.

14 Hawataruhusiwa kuuza wala kuibadilisha hata mojawapo. Hii ndiyo sehemu nzuri ya nchi kuliko nyingine zote, hivyo haitakuwa mikononi mwa watu wengine, kwa sababu ni takatifu kwaBwana.

15 “Eneo linalobaki lenye upana wa dhiraa 5,000na urefu wa dhiraa 25,000, litakuwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya mji, kwa ajili ya ujenzi wa nyumba na malisho. Mji utakuwa katikati yake

16 nao utakuwa na vipimo hivi: upande wa kaskazini dhiraa 4,500,upande wa kusini dhiraa 4,500, upande wa mashariki dhiraa 4,500 na upande wa magharibi dhiraa 4,500.

17 Sehemu ya malisho kwa ajili ya mji itakuwa na eneo la dhiraa 250upande wa kaskazini, dhiraa 250 upande wa kusini, dhiraa 250 upande wa mashariki na dhiraa 250 upande wa magharibi.

18 Eneo linalobaki, linalopakana na sehemu takatifu likiwa na urefu sawa nalo, litakuwa dhiraa 10,000 upande wa mashariki na dhiraa 10,000 upande wa magharibi. Mazao yake yatawapa watumishi wa mji chakula.

19 Watumishi wa mji wanaolima shamba hili watatoka katika makabila yote ya Israeli.

20 Eneo lote la hiyo sehemu litakuwa mraba, yaani, dhiraa 25,000 kila upande. Kama toleo maalum mtatenga sehemu takatifu, pamoja na milki ya mji.

21 “Eneo linalobaki pande zote za eneo linalofanya sehemu takatifu na milki ya mji litakuwa mali ya mkuu atawalaye. Eneo hili litaenea upande wa mashariki kuanzia kwenye dhiraa 25,000 za sehemu takatifu hadi mpaka wa mashariki na kuelekea upande wa magharibi kuanzia kwenye dhiraa 25,000 hadi mpaka wa magharibi. Maeneo yote haya mawili yanayoenda sambamba na urefu wa sehemu za makabila yatakuwa ya mkuu anayetawala, na sehemu ile takatifu pamoja na mahali patakatifu pa Hekalu itakuwa katikati yake.

22 Kwa hiyo milki ya Walawi na milki ya mji vitakuwa katikati ya eneo lile ambalo ni mali ya mkuu anayetawala. Eneo la mkuu anayetawala litakuwa kati ya mpaka wa Yuda na mpaka wa Benyamini.

23 “Kuhusu makabila yaliyobaki: Benyamini atakuwa na sehemu moja, itakayoanzia upande wa mashariki hadi upande wa magharibi.

24 “Simeoni atakuwa na sehemu moja, itakayopakana na nchi ya Benyamini kuanzia mashariki hadi magharibi.

25 “Isakari atakuwa na sehemu moja, itakayopakana na nchi ya Simeoni kuanzia mashariki hadi magharibi.

26 “Zabuloni atakuwa na sehemu moja, itakayopakana na nchi ya Isakari kuanzia mashariki hadi magharibi.

27 “Gadi atakuwa na sehemu moja, itakayopakana na nchi ya Zabuloni kuanzia mashariki hadi magharibi.

28 “Mpaka wa kusini wa Gadi utapita kusini kuanzia Tamari hadi maji ya Meriba-Kadeshi, kisha kupitia upande wa Kijito cha Misri hadi Bahari Kuu.

29 “Hii ndiyo nchi mtakayogawanya kuwa urithi kwa makabila ya Israeli, nazo zitakuwa sehemu zao,” asemaBwanaMwenyezi.

Malango Ya Mji

30 “Haya yatakuwa ndiyo malango ya mji ya kutokea: Kuanzia upande wa kaskazini, ambayo urefu wake ni dhiraa 4,500, utakuwa na malango matatu,

31 malango hayo ya mji yatapewa majina ya makabila ya Israeli. Malango hayo matatu ya upande wa kaskazini moja litakuwa lango la Reubeni, lango la Yuda na lango la Lawi.

32 “Upande wa mashariki, wenye urefu wa dhiraa 4,500, utakuwa na malango matatu: lango la Yosefu, lango la Benyamini na lango la Dani.

33 “Upande wa kusini, wenye urefu wa dhiraa 4,500, utakuwa na malango matatu: lango la Simeoni, lango la Isakari na lango la Zabuloni.

34 “Upande wa magharibi, wenye urefu wa dhiraa 4,500, utakuwa na malango matatu: lango la Gadi, lango la Asheri na lango la Naftali.

35 “Urefu wote kuzunguka utakuwa dhiraa 18,000.

“Nalo jina la mji huo kuanzia wakati huo na kuendelea litakuwa:

Bwana yupo hapa.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/EZK/48-5cec6eda75021edc2158555d445f17bc.mp3?version_id=1627—

Categories
Danieli

Danieli Utangulizi

Utangulizi

Kitabu hiki kinatoa kumbukumbu za Danieli wakati wa utumishi wake wa muda mrefu katika falme za Babeli na Uajemi. Alipokuwa mateka katika jumba la mfalme huko Babeli, Danieli alipandishwa cheo na kupewa wadhifa wa juu baada ya kumwambia Nebukadneza ndoto yake na tafsiri yake. Katika mwongo wa mwisho wa maisha yake, Danieli alipata funuo kadha wa kadha kutoka kwa Mungu zilizowiana na ndoto ya Nebukadneza, zikionyesha kuinuka na kuanguka kwa falme za dunia zilizostawi, ambazo hatimaye zinafikia mwisho wake na kusimamishwa kwa ufalme wa milele. Danieli, kama Myahudi mcha Mungu aliyekuwa mwombaji na msomaji wa Maandiko, alikuwa anahusika na watu wake wa Israeli sana. Alihakikishiwa na Mungu kwamba wangefanywa imara tena.

Mwandishi

Danieli.

Kusudi

Kuelezea habari za Wayahudi waliokuwa mateka lakini wenye imani, na walioonyesha jinsi Mungu anavyoweza kuokoa wale wanaomtumaini kutokana na kusudio lolote baya, akionyesha uweza wake kwamba ndiye anayetawala mbingu na nchi, na kwamba falme zote za wanadamu ziko chini yake.

Mahali

Babeli.

Tarehe

536 K.K.

Wahusika Wakuu

Danieli, Shadraki, Meshaki, Abednego, Nebukadneza, Belshaza na Dario.

Wazo Kuu

Danieli aliandika kitabu hiki Wayahudi walipokuwa utumwani ili kuwatia moyo waendelee kumwamini Mungu ambaye anatawala historia yote.

Mambo Muhimu

Maono ya Danieli yanaonyesha mpango wa Mungu kwa vizazi vyote, pamoja na kutabiri wazi kuhusu Masiya.

Mgawanyo

Matukio wakati wa utawala wa Mfalme Nebukadneza (

1:1–4:37

)

Maandishi ukutani (

5:1-30

)

Danieli katika tundu la simba (

5:31–6:28

)

Maono wakati wa utawala wa Belshaza (

7:1–8:27

)

Ndoto ya Danieli na majuma sabini (

9:1-27

)

Mafunuo ya mwisho ya Danieli (

10:1–12:13

).

Categories
Danieli

Danieli 1

Mafunzo Ya Danieli Huko Babeli

1 Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, Nebukadneza mfalme wa Babeli alikuja akazingira Yerusalemu kwa jeshi.

2 Bwana akamtia Yehoyakimu mfalme wa Yuda mkononi mwa Nebukadneza, pamoja na baadhi ya vyombo kutoka Hekalu la Mungu. Hivi akavichukua hadi kwenye hekalu la mungu wake huko Shinari, naye akaviweka nyumbani ya hazina ya mungu wake.

3 Kisha mfalme akamwagiza Ashpenazi, mkuu wa maafisa wa mfalme, kumletea baadhi ya Waisraeli kutoka jamaa ya mfalme na kutoka jamaa kuu,

4 vijana wanaume wasio na dosari mwilini, wenye sura nzuri, wanaoonyesha kipaji katika kila aina ya elimu, wenye ufahamu mzuri, wepesi kuelewa, na waliofuzu kuhudumu katika jumba la kifalme. Alikuwa awafundishe lugha na maandiko ya Wakaldayo.

5 Mfalme akawaagizia kiasi cha chakula na divai ya kila siku kutoka meza ya mfalme. Walikuwa wafundishwe kwa miaka mitatu, na hatimaye waingie kwenye utumishi wa mfalme.

6 Baadhi ya hawa vijana walitoka Yuda: nao ni Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria.

7 Mkuu wa maafisa akawapa majina mapya: Danieli akamwita Belteshaza, Hanania akamwita Shadraki, Mishaeli akamwita Meshaki, na Azaria akamwita Abednego.

8 Lakini Danieli alikusudia kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha mfalme na divai, naye akamwomba mkuu wa maafisa ruhusa ili asijinajisi kwa njia hii.

9 Basi Mungu alikuwa amemfanya huyo mkuu wa maafisa kuonyesha upendeleo na huruma kwa Danieli,

10 lakini huyo mkuu wa maafisa akamwambia Danieli, “Ninamwogopa bwana wangu mfalme, aliyeagizia chakula na kinywaji chenu. Kwa nini aone nyuso zenu zikiwa mbaya kuliko za vijana wengine wa rika lenu? Mfalme atakata kichwa changu kwa sababu yenu.”

11 Ndipo Danieli akamwambia mlinzi aliyeteuliwa na huyo mkuu wa maafisa kuwasimamia Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria,

12 “Tafadhali wajaribu watumishi wako kwa siku kumi. Usitupe chochote ila nafaka na mboga za majanitule, na maji ya kunywa.

13 Baadaye ulinganishe sura zetu na vijana wanaokula chakula cha mfalme, ukawatendee watumishi wako kulingana na unachoona.”

14 Basi akakubali jambo hili, akawajaribu kwa siku kumi.

15 Mwisho wa zile siku kumi, walionekana kuwa na afya na kunawiri zaidi kuliko yeyote kati ya wale vijana waliokula chakula cha mfalme.

16 Hivyo mlinzi wao akaondoa chakula chao na divai yao waliopangiwa kula na kunywa, akawapa nafaka na mboga za majani badala yake.

17 Mungu akawapa hawa vijana wanne maarifa na ufahamu wa kila aina ya maandiko na elimu. Naye Danieli aliweza kufahamu maono na aina zote za ndoto.

18 Mwisho wa muda uliowekwa na mfalme kuwaingiza kwake, mkuu wa maafisa akawaleta mbele ya Mfalme Nebukadneza.

19 Mfalme akazungumza nao, akaona hakuna aliyelingana na Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria. Hivyo wakaingia katika utumishi wa mfalme.

20 Katika kila jambo la hekima na ufahamu kuhusu kile mfalme alichowauliza, aliwaona bora mara kumi zaidi kuliko waganga na wasihiri wote katika ufalme wake wote.

21 Naye Danieli akabaki huko mpaka mwaka wa kwanza wa utawala wa Mfalme Koreshi.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/DAN/1-4ee83ff26b72d26874b0f661463536f0.mp3?version_id=1627—

Categories
Danieli

Danieli 2

Ndoto Ya Nebukadneza

1 Katika mwaka wa pili wa utawala wake, Nebukadneza aliota ndoto. Mawazo yake yakasumbuka na hakuweza kulala.

2 Hivyo mfalme akawaita waganga, wasihiri, wachawi na wanajimu ili wamwambie ndoto yake aliyokuwa ameota. Walipoingia ndani na kusimama mbele ya mfalme,

3 akawaambia, “Niliota ndoto inayonisumbua, nami nataka nijue maana yake.”

4 Ndipo wanajimu wakamjibu mfalme kwa lugha ya Kiaramu,“Ee mfalme, uishi milele! Waambie watumishi wako hiyo ndoto, nasi tutaifasiri.”

5 Mfalme akawajibu wanajimu, “Nimeamua hivi kwa uthabiti: Ikiwa hamtaniambia ndoto yangu ilikuwa ipi na kuifasiri, mtakatwa vipande vipande na nyumba zenu zitafanywa kuwa vifusi.

6 Lakini mkiniambia ndoto yangu na kuielezea, mtapokea kwangu zawadi, tuzo na heshima kubwa. Basi niambieni ndoto yangu na mnifasirie.”

7 Wakajibu kwa mara nyingine, “Mfalme na awaambie watumishi wake ndoto yake, nasi tutaifasiri.”

8 Ndipo mfalme akajibu, “Nina hakika kuwa mnajaribu kupata muda zaidi, kwa sababu mnatambua kuwa nimeamua hivi kwa uthabiti:

9 Ikiwa hamtaniambia ndoto yangu, ipo adhabu moja tu kwenu. Mmefanya shauri kuniambia habari za kunipotosha na mambo maovu, mkitumaini kwamba hali itabadilika. Hivyo basi, niambieni hiyo ndoto, nami nitajua kuwa mwaweza kunifasiria.”

10 Wanajimu wakamjibu mfalme, “Hakuna mtu duniani ambaye anaweza kufanya analotaka mfalme! Vilevile hakuna mfalme hata awe mkuu na mwenye uweza namna gani, aliyeuliza kitu kama hicho kwa mganga au kwa msihiri, wala kwa mnajimu yeyote.

11 Anachouliza mfalme ni kigumu mno. Hakuna yeyote awezaye kumfunulia mfalme isipokuwa miungu, nao hawaishi miongoni mwa wanadamu.”

12 Jambo hili lilimkasirisha na kumghadhibisha mfalme mno hata kuagiza kuuawa kwa wenye hekima wote wa Babeli.

13 Hivyo amri ikatolewa ya kuwaua wenye hekima, nao watu wakatumwa kuwatafuta Danieli na rafiki zake ili wawaue.

14 Wakati Arioko, mkuu wa askari wa walinzi wa mfalme, alikuwa amekwenda kuwaua watu wenye hekima wa Babeli, Danieli akazungumza naye kwa hekima na busara.

15 Akamuuliza huyo afisa wa mfalme, “Kwa nini mfalme ametoa amri kali hivyo?” Ndipo Arioko akamweleza Danieli jambo hilo.

16 Aliposikia jambo hili, Danieli akamwendea mfalme, akamwomba ampe muda ili aweze kumfasiria ile ndoto.

17 Ndipo Danieli akarudi nyumbani kwake na kuwaeleza rafiki zake Hanania, Mishaeli na Azaria jambo hilo.

18 Aliwasihi waombe rehema kutoka kwa Mungu wa mbinguni kuhusu siri hii, ili yeye na rafiki zake wasije wakauawa pamoja na wenye hekima wengine wa Babeli.

19 Wakati wa usiku lile fumbo lilifunuliwa kwa Danieli katika maono. Ndipo Danieli akamhimidi Mungu wa mbinguni,

20 na akasema:

“Lihimidiwe jina la Mungu milele na milele;

hekima na uweza ni vyake.

21 Yeye hubadili nyakati na majira;

huwaweka wafalme na kuwaondoa.

Huwapa hekima wenye hekima,

na maarifa wenye ufahamu.

22 Hufunua siri na mambo yaliyofichika;

anajua yale yaliyo gizani,

nayo nuru hukaa kwake.

23 Ninakushukuru na kukuhimidi,

Ee Mungu wa baba zangu:

Umenipa hekima na uwezo,

umenijulisha kile tulichokuomba,

umetujulisha ndoto ya mfalme.”

Danieli Aifasiri Ndoto

24 Ndipo Danieli akamwendea Arioko, ambaye mfalme alikuwa amemteua kuwaua wenye hekima wa Babeli, akamwambia, “Usiwaue wenye hekima wa Babeli. Nipeleke kwa mfalme, nami nitamfasiria ndoto yake.”

25 Arioko akampeleka Danieli kwa mfalme mara moja na kumwambia, “Nimempata mtu miongoni mwa watu wa uhamisho kutoka Yuda ambaye anaweza kumwambia mfalme maana ya ndoto yake.”

26 Mfalme akamuuliza Danieli (aliyeitwa pia Belteshaza), “Je, unaweza kuniambia nilichoona katika ndoto yangu na kuifasiri?”

27 Danieli akajibu, “Hakuna mwenye hekima, msihiri, mganga au mwaguzi anayeweza kumweleza mfalme siri aliyouliza,

28 lakini yuko Mungu mbinguni afunuaye siri. Amemwonyesha Mfalme Nebukadneza kitakachotokea siku zijazo. Ndoto yako na maono yaliyopita mawazoni mwako ulipokuwa umelala kitandani mwako ni haya:

29 “Ee mfalme, ulipokuwa umelala kitandani, yalikujia mawazo kuhusu mambo yatakayotokea baadaye, naye mfunuaji wa siri akakuonyesha ni kitu gani kitakachotokea.

30 Kwangu mimi, nimefunuliwa siri hii, si kwa sababu nina hekima kubwa kuliko watu wengine wanaoishi, bali ni ili wewe, ee mfalme, upate kujua tafsiri, na ili uweze kuelewa kile kilichopita mawazoni mwako.

31 “Ee mfalme, ulitazama, na mbele yako ilisimama sanamu kubwa, kubwa mno kupita kiasi, sanamu iliyongʼaa na kutisha kwa kuonekana kwake.

32 Kichwa cha ile sanamu kilikuwa kimetengenezwa kwa dhahabu safi, kifua chake na mikono yake vilikuwa vya fedha, tumbo lake na mapaja yake vilikuwa vya shaba,

33 miguu yake ilikuwa ya chuma, na nyayo zake zilikuwa chuma nazo sehemu nyingine zilikuwa udongo wa mfinyanzi uliochomwa.

34 Ulipokuwa unaangalia, jiwe lilikatwa, lakini si kwa mikono ya mwanadamu. Lile jiwe liliipiga ile sanamu kwenye nyayo zake za chuma na udongo wa mfinyanzi, na kuivunja.

35 Ndipo ile chuma, ule udongo wa mfinyanzi, ile shaba, ile fedha na ile dhahabu vikavunjika vipande vipande kwa wakati mmoja, na vikawa kama makapi katika sakafu ya kupuria nafaka wakati wa kiangazi. Upepo ukavipeperusha bila kuacha hata alama. Lakini lile jiwe lililoipiga ile sanamu likawa mlima mkubwa mno na kuijaza dunia yote.

36 “Hii ndiyo iliyokuwa ndoto, nasi sasa tutamfasiria mfalme.

37 Ee mfalme, wewe ni mfalme wa wafalme. Mungu wa mbinguni amekupa wewe utawala, uweza, nguvu na utukufu.

38 Mikononi mwako amewaweka wanadamu, wanyama wa kondeni, na ndege wa angani. Popote waishipo amekufanya wewe kuwa mtawala juu yao wote. Wewe ndiye kile kichwa cha dhahabu.

39 “Baada yako, ufalme mwingine utainuka, ulio dhaifu kuliko wako. Baadaye utafuata ufalme wa tatu, ule wa shaba, nao utatawala juu ya dunia yote.

40 Hatimaye, kutakuwako na ufalme wa nne, wenye nguvu kama chuma, kwa maana chuma huvunja na kupondaponda kila kitu; kama vile chuma ivunjavyo vitu vipande vipande, ndivyo ufalme huo utakavyopondaponda na kuvunjavunja nyingine zote.

41 Kama vile ulivyoona kuwa kwa sehemu nyayo na vidole vilikuwa vya udongo wa mfinyanzi uliochomwa na kwa sehemu nyingine chuma, hivyo huu utakuwa ufalme uliogawanyika; hata hivyo utakuwa na sehemu zenye nguvu za chuma ndani yake, kama vile ulivyoona chuma imechanganywa na udongo wa mfinyanzi.

42 Kama vile vidole vyake vya miguu vilikuwa kwa sehemu chuma na sehemu udongo wa mfinyanzi, hivyo ufalme huo kwa sehemu utakuwa na nguvu na kwa sehemu udhaifu.

43 Kama vile ulivyoona chuma kikiwa kimechanganyikana na udongo wa mfinyanzi uliochomwa, ndivyo watu watakavyokuwa mchanganyiko, wala hawatabaki wameungana tena, kama vile chuma kisivyoweza kuchanganyikana na udongo wa mfinyanzi.

44 “Katika siku za wafalme hao, Mungu wa mbinguni atauweka ufalme ambao kamwe hautaangamizwa, wala hautaachiwa taifa jingine. Utaziponda zile falme zote na kuzikomesha, bali wenyewe utadumu milele.

45 Hii ndiyo maana ya maono ya jiwe lililochongwa kutoka mlimani, lakini si kwa mikono ya mwanadamu, lile jiwe ambalo lilivunja chuma, shaba, udongo wa mfinyanzi, fedha na dhahabu vipande vipande.

“Mungu Mkuu amemwonyesha mfalme kile kitakachotokea wakati ujao. Ndoto hii ni ya kweli na tafsiri yake ni ya kuaminika.”

46 Ndipo Mfalme Nebukadneza akaanguka kifudifudi mbele ya Danieli kumpa heshima, akaagiza wamtolee Danieli sadaka na uvumba.

47 Mfalme akamwambia Danieli, “Hakika Mungu wako ni Mungu wa miungu, na Bwana wa wafalme, na mfunuaji wa siri zote, kwa maana umeweza kufunua siri hii.”

48 Ndipo mfalme akamweka Danieli nafasi ya juu, na kumpa zawadi nyingi tele. Akamfanya kuwa mtawala wa jimbo lote la Babeli, na kumweka kuwa mkuu wa wenye hekima wote.

49 Zaidi ya hayo, kwa ombi la Danieli, mfalme akawateua Shadraki, Meshaki na Abednego kuwa wasimamizi wa jimbo la Babeli, huku Danieli akibaki katika ukumbi wa mfalme.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/DAN/2-5f025cd69caa5915457c7a76108715d3.mp3?version_id=1627—

Categories
Danieli

Danieli 3

Sanamu Ya Dhahabu Na Moto Mkali

1 Mfalme Nebukadneza alitengeneza sanamu ya dhahabu, yenye kimo cha dhiraa sitini,na upana wa dhiraa sita,akaisimamisha kwenye tambarare ya Dura katika jimbo la nchi ya Babeli.

2 Kisha mfalme akaita wakuu, wasimamizi, watawala, washauri, watunza hazina, waamuzi, mahakimu na maafisa wengine wote wa jimbo kuja kuizindua sanamu ambayo Mfalme Nebukadneza alikuwa ameisimamisha.

3 Basi wakuu, wasimamizi, watawala, washauri, watunza hazina, waamuzi, mahakimu na maafisa wengine wa jimbo walikusanyika ili kuizindua sanamu ile Mfalme Nebukadneza alikuwa ameisimamisha, nao wakasimama mbele ya hiyo sanamu.

4 Ndipo mpiga mbiu akatangaza kwa sauti kubwa, “Enyi watu wa kabila zote, mataifa na watu wa kila lugha, hili ndilo mnaloamriwa kulifanya:

5 Mara mtakaposikia sauti ya baragumu, filimbi, marimba, zeze, kinubi, zumari na aina zote za sauti za ala za uimbaji, lazima mwanguke chini na kuabudu sanamu ya dhahabu ambayo Mfalme Nebukadneza ameisimamisha.

6 Mtu yeyote ambaye hataanguka chini na kuiabudu sanamu hiyo, atatupwa saa iyo hiyo ndani ya tanuru iwakayo moto.”

7 Kwa hiyo, mara waliposikia sauti ya baragumu, filimbi, kinubi, zeze, kinanda na aina zote za ala za uimbaji, watu wa kabila zote, mataifa na watu wa kila lugha wakaanguka chini na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu ambayo Mfalme Nebukadneza alikuwa ameisimamisha.

8 Wakati huo baadhi ya Wakaldayo walijitokeza na kuwashtaki Wayahudi.

9 Wakamwambia Mfalme Nebukadneza, “Ee mfalme, uishi milele!

10 Ee mfalme, umetoa amri kwamba kila mmoja atakayesikia sauti ya baragumu, filimbi, kinubi, zeze, kinanda, zumari na aina zote za ala za uimbaji lazima aanguke chini na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu,

11 na kwamba yeyote ambaye hataanguka chini na kuiabudu atatupwa saa iyo hiyo ndani ya tanuru iwakayo moto.

12 Lakini wako baadhi ya Wayahudi ambao umewaweka juu ya mambo ya jimbo la Babeli: yaani, Shadraki, Meshaki na Abednego, ambao hawakujali wewe, ee mfalme. Hawaitumikii miungu yako wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.”

13 Mfalme Nebukadneza, akiwa amekasirika na mwenye ghadhabu kali, akawaita Shadraki, Meshaki na Abednego. Hivyo watu hawa wakaletwa mbele ya mfalme,

14 naye Nebukadneza akawauliza, “Je, ni kweli kwamba ninyi Shadraki, Meshaki na Abednego hamuitumikii miungu yangu wala kuiabudu sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha?

15 Basi wakati mtakaposikia sauti ya baragumu, filimbi, marimba, zeze, kinubi, zumari na aina zote za ala za uimbaji, kama mtakuwa tayari kusujudu na kuiabudu hiyo sanamu niliyoitengeneza, vyema sana. Lakini kama hamtaiabudu, mtatupwa saa iyo hiyo ndani ya tanuru iwakayo moto. Naye ni mungu yupi atakayeweza kuwaokoa ninyi, kutoka mkono wangu?”

16 Shadraki, Meshaki na Abednego wakamjibu mfalme, “Ee Nebukadneza, hatuhitaji kujitetea mbele zako kuhusu jambo hili.

17 Ikiwa tutatupwa ndani ya tanuru iwakayo moto, Mungu tunayemtumikia anaweza kutuokoa na moto, naye atatuokoa kutoka mkononi mwako, ee mfalme.

18 Lakini hata ikiwa hatatuokoa, ee mfalme, tunataka ufahamu kwamba, hatutaitumikia miungu yako wala kuiabudu sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.”

19 Ndipo Nebukadneza akawa na ghadhabu kali sana kwa Shadraki, Meshaki na Abednego, nayo nia yake ikabadilika kwao. Akaagiza tanuru ichochewe moto mara saba kuliko kawaida yake

20 na kuwaamuru baadhi ya askari wake wenye nguvu zaidi katika jeshi lake kuwafunga Shadraki, Meshaki na Abednego na kuwatupa ndani ya tanuru iwakayo moto.

21 Hivyo watu hawa, walifungwa na kutupwa ndani ya tanuru iwakayo moto wakiwa wamevaa majoho yao, suruali, vilemba na nguo zao nyingine.

22 Amri ya mfalme ilikuwa ya haraka sana na tanuru ilikuwa na moto mkali kiasi kwamba miali ya moto iliwaua wale askari waliowapeleka Shadraki, Meshaki na Abednego.

23 Watu hawa watatu walianguka ndani ya tanuru iwakayo moto wakiwa wamefungwa kwa uthabiti sana.

24 Ndipo Mfalme Nebukadneza akashangaa, akainuka kwa haraka na kuwauliza washauri wake, “Je, hawakuwa watu watatu ambao tuliwafunga na kuwatupa ndani ya moto?”

Washauri wakajibu, “Hakika, ee mfalme.”

25 Mfalme akasema, “Tazama! Naona watu wanne wakitembeatembea ndani ya moto, hawajafungwa wala kudhurika, naye mtu yule wa nne anaonekana kama mwana wa miungu.”

26 Ndipo Nebukadneza akaukaribia mdomo wa ile tanuru iwakayo moto na kupaza sauti, “Shadraki, Meshaki na Abednego, watumishi wa Mungu Aliye Juu Sana, tokeni! Njooni hapa!”

Ndipo Shadraki, Meshaki na Abednego wakatoka ndani ya moto.

27 Nao maliwali, wasimamizi, watawala na washauri wa mfalme wakakusanyika kuwazunguka. Waliona kwamba moto haukudhuru miili yao, wala unywele wa vichwa vyao haukuungua, majoho yao hayakuungua, wala hapakuwepo na harufu ya moto kwenye miili yao.

28 Ndipo Nebukadneza akasema, “Ahimidiwe Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego, ambaye amemtuma malaika wake na kuwaokoa watumishi wake. Walimtumaini na kukaidi amri ya mfalme, nao wakawa tayari kufa kuliko kutumikia au kuabudu mungu mwingine yeyote isipokuwa Mungu wao.

29 Kwa hiyo ninaamuru kwamba watu wa taifa lolote au lugha yoyote watakaosema kitu chochote dhidi ya Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego wakatwe vipande vipande na nyumba zao zifanywe kuwa malundo ya kokoto, kwa maana hakuna mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii.”

30 Kisha mfalme akawapandisha vyeo Shadraki, Meshaki na Abednego katika jimbo la Babeli.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/DAN/3-655d7a63af06b510f0e85976e4d007c5.mp3?version_id=1627—