Categories
Yeremia

Yeremia 32

Yeremia Anunua Shamba

1 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwaBwana, katika mwaka wa kumi wa utawala wa Sedekia mfalme wa Yuda, ambao ulikuwa mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Mfalme Nebukadneza.

2 Wakati huo jeshi la mfalme wa Babeli lilikuwa limeuzunguka mji wa Yerusalemu, naye nabii Yeremia alikuwa amezuiliwa katika ua wa walinzi katika jumba la kifalme la Yuda.

3 Basi Sedekia mfalme wa Yuda alikuwa amemfunga huko akisema, “Kwa nini unatabiri hivyo? Wewe unasema, ‘Hili ndilo asemaloBwana: Ninakaribia kuutia mji huu mkononi mwa mfalme wa Babeli, naye atauteka.

4 Sedekia mfalme wa Yuda hataweza kuponyoka mikononi mwa Wakaldayo, lakini kwa hakika atatiwa mikononi mwa mfalme wa Babeli, naye atazungumza naye ana kwa ana na kumwona kwa macho yake mwenyewe.

5 Atamchukua Sedekia hadi Babeli, mahali atakapoishi mpaka nitakapomshughulikia, asemaBwana. Kama utapigana dhidi ya Wakaldayo, hutashinda.’ ”

6 Yeremia akasema, “Neno laBwanalilinijia kusema:

7 Hanameli mwana wa Shalumu mjomba wako atakuja kwako na kusema, ‘Nunua shamba langu huko Anathothi, kwa sababu wewe kama jamaa ya karibu ni haki na wajibu wako kulinunua.’

8 “Kisha, kamaBwanaalivyosema, binamu yangu Hanameli alinijia katika ua wa walinzi na kusema: ‘Nunua shamba langu lililoko Anathothi katika nchi ya Benyamini. Kwa kuwa ni haki yako kulikomboa na kulimiliki, jinunulie.’

“Nilijua kwamba hili lilikuwa neno laBwana.

9 Hivyo nikalinunua shamba hilo lililoko Anathothi kutoka kwa binamu yangu Hanameli, nami nikampimia shekeli kumi na sabaza fedha.

10 Nikatia sahihi na kuweka muhuri hati ya kumiliki, nikaweka mashahidi, na kupima ile fedha kwenye mizani.

11 Nikachukua ile hati ya kununulia, nakala iliyotiwa muhuri yenye makubaliano na masharti, pia pamoja na ile nakala isiyo na muhuri,

12 nami nikampa Baruku mwana wa Neria, mwana wa Maaseya, hati hii mbele ya binamu yangu Hanameli, na mbele ya mashahidi waliokuwa wameweka sahihi kwenye hati hii na mbele ya Wayahudi wote waliokuwa wameketi katika ua wa walinzi.

13 “Nilimpa Baruku maelezo haya mbele yao:

14 ‘Hili ndilo asemaloBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: Chukua hati hizi, yaani nakala zote zenye muhuri na zisizo na muhuri za hati ya kununulia, na uziweke kwenye gudulia la udongo wa mfinyanzi ili zidumu kwa muda mrefu.

15 Kwa kuwa hili ndilo asemaloBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: Nyumba, mashamba na mashamba ya mizabibu yatanunuliwa tena katika nchi hii.’

16 “Baada ya kumkabidhi Baruku mwana wa Neria hii hati ya kununulia, nilimwombaBwana:

17 “EeBwanaMwenyezi, umeumba mbingu na nchi kwa uwezo wako mkuu na kwa mkono ulionyooshwa. Hakuna jambo lililo gumu usiloliweza.

18 Wewe huonyesha upendo kwa maelfu, lakini huleta adhabu kwa ajili ya dhambi za baba mapajani mwa watoto wao baada yao. Ee Mungu mkuu na mwenye uweza, ambaye jina lako niBwanaMwenye Nguvu Zote,

19 makusudi yako ni makuu, na matendo yako ni yenye uwezo. Macho yako yanaona njia zote za wanadamu, nawe humlipa kila mmoja kulingana na mwenendo wake, na kama yanavyostahili matendo yake.

20 Ulitenda ishara za miujiza na maajabu huko Misri, na umeyaendeleza mpaka leo, katika Israeli na miongoni mwa wanadamu wote, nawe umejulikana na kufahamika hivyo mpaka leo.

21 Uliwatoa watu wako Israeli kutoka Misri kwa ishara na maajabu, kwa mkono wenye nguvu na ulionyooshwa na kwa matisho makuu.

22 Uliwapa nchi hii uliyokuwa umeapa kuwapa baba zao, nchi inayotiririka maziwa na asali.

23 Waliingia na kuimiliki, lakini hawakukutii wala kuifuata sheria yako. Hawakufanya kile ulichowaamuru kufanya. Hivyo ukaleta maafa haya yote juu yao.

24 “Tazama jinsi tumezungukwa na jeshi ili kuuteka mji huu. Kwa sababu ya upanga, njaa na tauni, mji utatiwa mikononi mwa Wakaldayo ambao wanaushambulia. Ulilosema limetokea kama vile unavyoona sasa.

25 Ingawa mji utatiwa mikononi mwa Wakaldayo, wewe, EeBwanaMwenyezi, uliniambia, ‘Nunua shamba kwa fedha, na jambo hilo lishuhudiwe.’ ”

26 Ndipo neno laBwanalikamjia Yeremia kusema:

27 “Mimi ndimiBwana, Mungu wa wote wenye mwili. Je, kuna jambo lolote lililo gumu nisiloliweza?

28 Kwa hiyo, hili ndilo asemaloBwana: Ninakaribia kuutia mji huu mikononi mwa Wakaldayo, na mwa Nebukadneza mfalme wa Babeli ambaye atauteka.

29 Wakaldayo ambao wanaushambulia mji huu watakuja na kuuchoma moto na kuuteketeza, pamoja na nyumba ambamo watu wamenikasirisha kwa kumfukizia Baali uvumba katika mapaa na kumimina sadaka za vinywaji kwa miungu mingine.

30 “Watu wa Israeli na wa Yuda hawakufanya kitu kingine ila uovu mbele zangu tangu ujana wao. Naam, watu wa Israeli hawakufanya kitu kingine ila kunikasirisha kwa kazi ambazo mikono yao imetengeneza, asemaBwana.

31 Tangu siku ulipojengwa hadi sasa, mji huu umenikasirisha na kunighadhibisha kiasi kwamba ni lazima niuondoe machoni pangu.

32 Watu wa Israeli na wa Yuda wamenikasirisha kwa uovu wote waliofanya: wao, wafalme wao na maafisa wao, makuhani wao na manabii wao, watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu.

33 Walinigeuzia visogo vyao, wala si nyuso zao. Ingawa niliwafundisha tena na tena, hawakupenda kusikiliza wala kuitikia adhabu.

34 Waliweka miungu yao ya kuchukiza sana katika nyumba iitwayo kwa Jina langu na kuinajisi.

35 Wakajenga mahali pa juu pa kuabudia miungu kwa ajili ya Baali katika Bonde la Ben-Hinomu, ambapo walitoa wana wao na binti zao kafara kwa Moleki, ingawa kamwe sikuamuru, wala halikuingia akilini mwangu, kwamba watafanya chukizo kama hilo na kumfanya Yuda atende dhambi.

36 “Mnasema kuhusu mji huu, ‘Kwa upanga, njaa na tauni, mji utatiwa mkononi mwa mfalme wa Babeli,’ lakini hili ndiloBwana, Mungu wa Israeli asemalo:

37 Hakika nitawakusanya kutoka nchi zote nilizowafukuzia katika hasira yangu kali na ghadhabu yangu kuu, nitawarudisha mahali hapa na kuwaruhusu waishi kwa salama.

38 Watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao.

39 Nitawapa moyo mmoja na kutenda pamoja, ili kwamba waniche daima kwa mema yao wenyewe na kwa mema ya watoto wao baada yao.

40 Nitafanya nao agano la milele: Kamwe sitaacha kuwatendea mema, nami nitawavuvia kunicha mimi, ili kamwe wasigeukie mbali nami.

41 Nitafurahia kuwatendea mema, na kwa hakika nitawapanda katika nchi hii kwa moyo wangu wote na roho yangu yote.

42 “Hili ndilo asemaloBwana: Kama nilivyoleta maafa haya makubwa kwa watu hawa, ndivyo nitakavyowapa mafanikio niliyowaahidi.

43 Kwa mara nyingine tena mashamba yatanunuliwa katika nchi hii ambayo mlisema, ‘Imekuwa ukiwa, isiyofaa, isiyo na watu wala wanyama, kwa sababu imetiwa mikononi mwa Wakaldayo.’

44 Mashamba yatanunuliwa kwa fedha, na hati zitatiwa sahihi, zitatiwa muhuri na kushuhudiwa katika nchi ya Benyamini, katika vijiji vinavyoizunguka Yerusalemu, katika miji ya Yuda na katika miji ya nchi ya vilima, sehemu za magharibi katika miji ya tambarare na katika Negebu, kwa sababu nitarudisha tena mafanikio yao,asemaBwana.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JER/32-6c94f231c5d7297db41fee6303780ebd.mp3?version_id=1627—

Categories
Yeremia

Yeremia 33

Ahadi Ya Kurudishwa

1 Wakati Yeremia alipokuwa angali amefungwa kwenye ua wa walinzi, neno laBwanalilimjia mara ya pili kusema:

2 “Hili ndiloBwanaasemalo, yeye aliyeumba dunia,Bwanaaliyeifanya na kuithibitisha,Bwanandilo jina lake:

3 ‘Niite nami nitakuitika na kukuambia mambo makuu na yasiyochunguzika, usiyoyajua.’

4 Kwa maana hili ndiloBwana, Mungu wa Israeli, asemalo kuhusu nyumba katika mji huu na majumba ya kifalme ya Yuda yaliyobomolewa ili yatumiwe dhidi ya kule kuzungukwa na jeshi na upanga

5 katika kupigana na Wakaldayo: ‘Zitajazwa na maiti za watu nitakaowachinja katika hasira na ghadhabu yangu. Nitauficha uso wangu kwa sababu ya maovu yake yote.

6 “ ‘Hata hivyo, nitauletea afya na uponyaji, nitawaponya watu wangu na kuwafanya wafurahie amani tele na salama.

7 Nitawarudisha Yuda na Israeli kutoka nchi ya kutekwa kwao, na kuwajenga tena kama walivyokuwa hapo awali.

8 Nitawatakasa dhambi zote walizofanya dhidi yangu, na nitawasamehe dhambi zote za uasi dhidi yangu.

9 Kisha mji huu utaniletea utukufu, furaha, sifa na heshima mbele ya mataifa yote ya dunia yatakayosikia mambo yote mazuri ninayoufanyia. Nao watashangaa na kutetemeka kwa ajili ya wingi wa mafanikio na amani nitakayoupatia.’

10 “Hili ndilo asemaloBwana: ‘Mnasema kuhusu mahali hapa kwamba, “Ni mahali palipoachwa ukiwa, pasipo na wanadamu wala wanyama.” Lakini katika miji ya Yuda na barabara za Yerusalemu ambazo zimeachwa, ambazo hazikaliwi na wanadamu wala wanyama, huko kutasikika kwa mara nyingine

11 sauti za shangwe na furaha, sauti za bibi na bwana arusi, na sauti za wale waletao sadaka za shukrani katika nyumba yaBwana, wakisema,

“ ‘ “MshukuruniBwanaMwenye Nguvu Zote,

kwa maanaBwanani mwema;

upendo wake wadumu milele.”

Kwa kuwa nitairudishia nchi baraka kama zilivyokuwa hapo awali,’ asemaBwana.

12 “Hili ndilo asemaloBwanaMwenye Nguvu Zote: ‘Mahali hapa, ambapo ni ukiwa, pasipo na wanadamu wala wanyama: katika miji yake, patakuwepo tena malisho kwa ajili ya wachungaji kupumzisha makundi yao ya kondoo.

13 Katika miji ya nchi ya vilima, ya vilima vya magharibi na ya Negebu, katika nchi ya Benyamini, katika vijiji vinavyoizunguka Yerusalemu na katika miji ya Yuda, makundi ya kondoo yatapita tena chini ya mkono wa yeye ayahesabuye,’ asemaBwana.

14 “ ‘Siku zinakuja,’ asemaBwana, ‘wakati nitakapotimiza ahadi yangu ya rehema niliyoifanya kwa nyumba ya Israeli na kwa nyumba ya Yuda.

15 “ ‘Katika siku hizo na wakati huo

nitalifanya Tawi la haki lichipuke kutoka ukoo wa Daudi,

naye atafanya lile lililo haki na sawa

katika nchi.

16 Katika siku hizo, Yuda ataokolewa

na Yerusalemu ataishi salama.

Hili ndilo jina atakaloitwa:

BwanaHaki Yetu.’

17 Kwa maana hili ndilo asemaloBwana: ‘Daudi kamwe hatakosa mtu wa kukalia kiti cha enzi cha nyumba ya Israeli,

18 wala hata makuhani, ambao ni Walawi, kamwe hawatakosa mtu wa kusimama mbele zangu daima ili kutoa sadaka za kuteketezwa, ili kuteketeza sadaka ya nafaka na kutoa dhabihu.’ ”

19 Neno laBwanalikamjia Yeremia kusema:

20 “Hili ndilo asemaloBwana: ‘Ikiwa mtaweza kuvunja agano langu kuhusu usiku na mchana, ili usiku na mchana visiwepo kwa nyakati zake,

21 basi agano langu na Daudi mtumishi wangu, na agano langu na Walawi ambao ni makuhani wanaohudumu mbele zangu, linaweza kuvunjwa, na Daudi hatakuwa tena na mzao wa kutawala katika kiti chake cha enzi.

22 Nitawafanya wazao wa Daudi mtumishi wangu na Walawi wanaohudumu mbele zangu wengi, wasioweza kuhesabika kama nyota za angani, tena wasiopimika kama mchanga wa ufuoni mwa bahari.’ ”

23 Neno laBwanalikamjia Yeremia kusema:

24 “Je, hujasikia kwamba watu hawa wanasema, ‘Bwanaamezikataa zile falme mbili alizozichagua?’ Kwa hiyo wamewadharau watu wangu, na hawawaoni tena kama taifa.

25 Hili ndilo asemaloBwana: ‘Kama sijathibitisha agano langu na usiku na mchana, na kuziweka wakfu sheria za mbingu na nchi,

26 basi nitawakataa wazao wa Yakobo na Daudi mtumishi wangu, na sitachagua mmoja wa wanawe kutawala juu ya wazao wa Abrahamu, Isaki na Yakobo. Kwa maana nitawarudisha kutoka nchi ya kutekwa kwao na kuwaonea huruma.’ ”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JER/33-2a1aedabc8ed086cc555318a1a07e42a.mp3?version_id=1627—

Categories
Yeremia

Yeremia 34

Onyo Kwa Sedekia

1 Wakati Nebukadneza mfalme wa Babeli na jeshi lake lote, pamoja na falme zote na mataifa katika himaya aliyotawala walipokuwa wakipigana dhidi ya Yerusalemu pamoja na miji yote inayoizunguka, neno hili lilimjia Yeremia kutoka kwaBwana:

2 “Hili ndilo asemaloBwana, Mungu wa Israeli, kusema: Nenda kwa Sedekia mfalme wa Yuda umwambie, ‘Hili ndilo asemaloBwana: Ninakaribia kuutia mji huu mikononi mwa mfalme wa Babeli, naye atauteketeza kwa moto.

3 Hutaweza kuepuka mkono wake, bali hakika utatekwa na kukabidhiwa kwake. Utamwona mfalme wa Babeli kwa macho yako mwenyewe, naye atazungumza nawe ana kwa ana. Nawe utakwenda Babeli.

4 “ ‘Lakini sikia ahadi yaBwana, ee Sedekia mfalme wa Yuda. Hili ndilo asemaloBwanakukuhusu: Hutakufa kwa upanga,

5 utakufa kwa amani. Kama vile watu walivyowasha moto wa maziko kwa heshima ya baba zako, wafalme waliokutangulia, ndivyo watu watakavyowasha moto kwa heshima yako na kuomboleza, wakisema: “Ole, EeBwana!” Mimi mwenyewe ninaweka ahadi hii, asemaBwana.’ ”

6 Ndipo nabii Yeremia akamwambia Sedekia mfalme wa Yuda mambo haya yote huko Yerusalemu,

7 wakati jeshi la mfalme wa Babeli lilipokuwa likipigana dhidi ya Yerusalemu na miji mingine ya Yuda ambayo bado ilikuwa imara, yaani Lakishi na Azeka. Hii ilikuwa miji pekee yenye ngome iliyobaki katika Yuda.

Uhuru Kwa Watumwa

8 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwaBwana, baada ya Mfalme Sedekia kufanya agano na watu wote huko Yerusalemu ili kutangaza uhuru kwa watumwa.

9 Kila mmoja alipaswa kuwaacha huru watumwa wake wa Kiebrania, wanawake na wanaume. Hakuna yeyote aliyeruhusiwa kumshikilia Myahudi mwenzake kama mtumwa.

10 Kwa hiyo maafisa wote na watu walioingia katika agano hili wakakubali kwamba watawaacha huru watumwa wao wa kiume na wa kike, na hawatawashikilia tena kama watumwa. Wakakubali na wakawaacha huru.

11 Lakini baadaye wakabadili mawazo yao, na kuwarudisha wale watumwa waliokuwa wamewaacha huru, wakawafanya tena watumwa.

12 Ndipo neno laBwanalikamjia Yeremia kusema:

13 “Hili ndilo asemaloBwana, Mungu wa Israeli: Nilifanya agano na baba zenu nilipowatoa Misri, kutoka nchi ya utumwa. Nilisema,

14 ‘Kila mwaka wa saba, kila mmoja wenu ni lazima amwache huru mtumwa ambaye ni Mwebrania mwenzenu aliyejiuza kwenu. Baada ya kukutumikia kwa miaka sita, ni lazima umwache huru aende zake.’ Hata hivyo baba zenu hawakunisikiliza wala kunijali.

15 Hivi karibuni tu mlitubu na kufanya yaliyo sawa machoni pangu: Kila mmoja wenu aliwatangazia uhuru Waebrania wake. Hata mlifanya agano mbele zangu ndani ya nyumba iitwayo kwa Jina langu.

16 Lakini sasa mmegeuka na kulinajisi jina langu. Kila mmoja wenu amemrudisha mtumwa wa kiume na wa kike ambao mlikuwa mmewaacha huru waende zao walikotaka. Mmewalazimisha kuwa watumwa wenu tena.

17 “Kwa hiyo, hili ndilo asemaloBwana: Hamkunitii mimi. Hamkutangaza uhuru kwa ndugu zenu. Hivyo sasa, ninawatangazia ninyi ‘uhuru,’ asemaBwana: ‘uhuru’ ili kuanguka kwa upanga, tauni na njaa. Nitawafanya mwe chukizo kwa falme zote za dunia.

18 Watu waliovunja agano langu, na ambao hawakutunza masharti ya agano walilofanya mbele zangu, nitawafanya kama ndama waliyemkata vipande viwili, kisha wakatembea kati ya vile vipande vya huyo ndama.

19 Viongozi wa Yuda na Yerusalemu, maafisa wa mahakama, makuhani na watu wote wa nchi waliopita kati ya vile vipande vya ndama,

20 nitawatia mikononi mwa adui zao wanaotafuta uhai wao. Maiti zao zitakuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa nchi.

21 “Nitamtia Sedekia mfalme wa Yuda na maafisa wake mikononi mwa adui zao wanaotafuta uhai wao, kwa jeshi la mfalme wa Babeli, lililokuwa limeondoka kwenu.

22 Nitatoa amri, asemaBwana, nami nitawarudisha tena katika mji huu. Watapigana dhidi yake, wautwae na kuuteketeza kwa moto. Nami nitaiangamiza miji ya Yuda hivyo pasiwe na yeyote atakayeweza kuishi humo.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JER/34-708bbfd1d2edd2547a5530ab7fbdbe21.mp3?version_id=1627—

Categories
Yeremia

Yeremia 35

Warekabi Wasifiwa

1 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwaBwana, wakati wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda:

2 “Nenda kwa jamaa ya Warekabi, uwaalike waje kwenye moja ya vyumba vya pembeni vya nyumba yaBwana, na uwape divai wanywe.”

3 Basi nikaenda kumwita Yaazania mwana wa Yeremia, mwana wa Habazinia, na ndugu zake na wanawe wote, yaani jamaa nzima ya Warekabi.

4 Nikawaleta katika nyumba yaBwana, ndani ya chumba cha wana wa Hanani mwana wa Igdalia mtu wa Mungu. Kilikuwa karibu na chumba cha maafisa, ambacho kilikuwa juu ya kile cha Maaseya mwana wa Shalumu, aliyekuwa bawabu.

5 Kisha nikaweka mabakuli yaliyojaa divai na baadhi ya vikombe mbele ya watu wa jamaa ya Warekabi na kuwaambia, “Kunyweni divai.”

6 Lakini wao wakajibu, “Sisi hatunywi divai, kwa sababu baba yetu Yonadabu mwana wa Rekabu, alitupa agizo hili: ‘Ninyi wala wazao wenu kamwe msinywe divai.

7 Pia msijenge nyumba kamwe, wala kuotesha mbegu au kupanda mashamba ya mizabibu. Kamwe msiwe na kitu chochote katika hivi, lakini siku zote lazima muishi kwenye mahema. Ndipo mtakapoishi kwa muda mrefu katika nchi ambayo ninyi ni wahamiaji.’

8 Tumetii kila kitu ambacho baba yetu Yonadabu mwana wa Rekabu alituamuru. Sisi wenyewe wala wake zetu wala wana wetu na binti zetu kamwe hatujanywa divai

9 wala kujenga nyumba za kuishi au kuwa na mashamba ya mizabibu, mashamba au mazao.

10 Tumeishi katika mahema na tumetii kikamilifu kila kitu alichotuamuru baba yetu Yonadabu.

11 Lakini wakati Nebukadneza mfalme wa Babeli alipoivamia nchi hii, tulisema, ‘Njooni, lazima twende Yerusalemu ili kukimbia majeshi ya Wakaldayo na ya Washamu.’ Kwa hiyo tumeishi Yerusalemu.”

12 Ndipo neno laBwanalikamjia Yeremia kusema:

13 “Hili ndiloBwanaMwenye Nguvu Zote, aliye Mungu wa Israeli, asemalo: Nenda ukawaambie watu wa Yuda na watu wa Yerusalemu, ‘Je, hamwezi kujifunza kutoka kwa wana wa Rekabu, na kuyatii maneno yangu?’ asemaBwana.

14 ‘Yonadabu mwana wa Rekabu aliwaagiza wanawe wasinywe divai, na agizo hilo wamelishika mpaka leo hawanywi divai, kwa sababu wanatii amri ya baba yao. Lakini nimenena nanyi tena na tena, lakini hamkunitii mimi.

15 Tena na tena nimewatuma watumishi wangu wote manabii kwenu. Wakasema, “Kila mmoja wenu ni lazima ageuke na kuacha njia zake mbaya, na kuyatengeneza matendo yake. Msifuate miungu mingine ili kuitumikia. Ndipo mtakapoishi katika nchi niliyowapa ninyi na baba zenu.” Lakini hamkujali wala kunisikiliza.

16 Wazao wa Yonadabu mwana wa Rekabu walitimiza amri ambayo baba yao aliwapa, lakini watu hawa hawakunitii mimi.’

17 “Kwa hiyo, hili ndiloBwanaMungu Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Sikilizeni! Nitaleta juu ya Yuda na juu ya kila mmoja aishiye Yerusalemu kila aina ya maafa niliyotamka dhidi yao. Nilinena nao, lakini hawakusikiliza. Niliwaita, lakini hawakujibu.’ ”

18 Kisha Yeremia akaiambia jamaa ya Warekabi, “Hili ndilo asemaloBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: ‘Mmetii amri ya baba yenu Yonadabu, na mmefuata mafundisho yake yote na mmefanya kila kitu alichowaamuru.’

19 Kwa hiyo hili ndiloBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Yonadabu mwana wa Rekabu hatakosa kamwe kuwa na mtu wa kunitumikia mimi.’ ”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JER/35-7693612bbd58e667378b5d475304d49d.mp3?version_id=1627—

Categories
Yeremia

Yeremia 36

Yehoyakimu Achoma Kitabu Cha Yeremia

1 Katika mwaka wa nne wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, neno hili lilimjia nabii Yeremia kutoka kwaBwana, kusema:

2 “Chukua kitabu uandike ndani yake maneno yote niliyonena nawe kuhusu Israeli, Yuda na mataifa mengine yote, tangu nilipoanza kunena nawe wakati wa utawala wa Yosia hadi sasa.

3 Labda watu wa Yuda watakaposikia juu ya kila maafa ninayokusudia kuwapiga nayo, kila mmoja wao atageuka kutoka njia zake mbaya, kisha nitasamehe uovu wao na dhambi yao.”

4 Hivyo Yeremia akamwita Baruku mwana wa Neria, naye Yeremia alipokuwa akiyakariri maneno yote aliyoyasemaBwana, Baruku akayaandika katika kitabu.

5 Kisha Yeremia akamwambia Baruku, “Nimezuiliwa, mimi siwezi kuingia katika Hekalu laBwana.

6 Basi wewe nenda katika nyumba yaBwanasiku ya kufunga, uwasomee watu maneno yaBwanakutoka kitabu hiki yale uliyoyaandika kutoka kinywani mwangu. Wasomee watu wote wa Yuda waliofika kutoka miji yao.

7 Labda wataomba na kusihi mbele zaBwanana kila mmoja akageuka kutoka njia zake mbaya, kwa sababu hasira na ghadhabu zilizotamkwa dhidi ya watu hawa naBwanani kubwa.”

8 Baruku mwana wa Neria akafanya kila kitu nabii Yeremia alichomwambia kufanya. Alisoma maneno yaBwanakatika Hekalu laBwanakutoka kile kitabu.

9 Katika mwezi wa tisa, mnamo mwaka wa tano wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, wakati wa kufunga mbele zaBwana, ilitangazwa kwa watu wote walioko Yerusalemu, na wale wote waliokuwa wamekuja kutoka miji ya Yuda.

10 Kutoka chumba cha Gemaria mwana wa Shafani mwandishi, kilichokuwa katika ua wa juu kwenye ingilio la Lango Jipya la Hekalu, Baruku akawasomea watu wote waliokuwa katika Hekalu laBwanamaneno ya Yeremia kutoka kwenye kile kitabu.

11 Basi Mikaya mwana wa Gemaria, mwana wa Shafani, aliposikia maneno yote yaBwanakutoka kwenye kile kitabu,

12 alishuka hadi kwenye chumba cha mwandishi kwenye jumba la kifalme, mahali walipokuwa wameketi maafisa wote: yaani Elishama mwandishi, Delaya mwana wa Shemaya, Elnathani mwana wa Akbori, Gemaria mwana wa Shafani, Sedekia mwana wa Hanania, na maafisa wengine wote.

13 Baada ya Mikaya kuwaambia kila kitu ambacho alikuwa amesikia Baruku akiwasomea watu kutoka kwenye kile kitabu,

14 maafisa wote wakamtuma Yehudi mwana wa Nethania, mwana wa Shelemia, mwana wa Kushi, kumwambia Baruku, “Leta hicho kitabu ambacho umewasomea watu, nawe mwenyewe uje.” Ndipo Baruku mwana wa Neria akawaendea akiwa na hicho kitabu mkononi mwake.

15 Wakamwambia, “Tafadhali, keti na utusomee hicho kitabu.”

Ndipo Baruku akawasomea kile kitabu.

16 Walipoyasikia maneno hayo yote, wakatazamana wao kwa wao kwa woga na kumwambia Baruku, “Lazima tutoe taarifa ya maneno haya yote kwa mfalme.”

17 Kisha wakamuuliza Baruku, “Tuambie, uliandikaje haya yote? Je, yalitoka kinywani mwa Yeremia?”

18 Baruku akajibu, “Ndiyo, maneno haya yote yalitoka kinywani mwa Yeremia, nami nikayaandika kwa wino katika hiki kitabu.”

19 Ndipo wale maafisa wakamwambia Baruku, “Wewe na Yeremia nendeni mkajifiche. Mtu yeyote asijue mahali mlipo.”

20 Baada ya kuhifadhi kile kitabu ndani ya chumba cha Elishama mwandishi, wakamwendea mfalme katika ua wa nje na kumwarifu kila kitu.

21 Mfalme akamtuma Yehudi akachukue kile kitabu. Yehudi akakileta hicho kitabu kutoka kwenye chumba cha Elishama mwandishi, na akakisoma mbele ya mfalme na maafisa wakiwa wamesimama kando ya mfalme.

22 Ulikuwa mwezi wa tisa, na mfalme alikuwa ameketi chumba cha wakati wa baridi akiota moto.

23 Hata ikawa kila wakati Yehudi alipomaliza kusoma kurasa tatu au nne za hicho kitabu, mfalme alizikata kwa kisu cha mwandishi na kuzitupia motoni, hadi kitabu chote kikateketea.

24 Mfalme na watumishi wake wote waliosikia yote yaliyosomwa hawakuonyesha hofu yoyote, wala hawakuyararua mavazi yao.

25 Hata ingawa Elnathani, Delaya na Gemaria walimsihi mfalme asikichome kile kitabu, yeye hakuwasikiliza.

26 Badala yake, mfalme akamwamuru Yerameeli, mwana wa mfalme, Seraya mwana wa Azrieli, na Shelemia mwana wa Abdeeli kuwakamata mwandishi Baruku na nabii Yeremia. LakiniBwanaalikuwa amewaficha.

27 Baada ya mfalme kuchoma kile kitabu kilichokuwa na yale maneno Baruku aliyokuwa ameyaandika kutoka kinywani mwa Yeremia, neno laBwanalilimjia Yeremia likisema:

28 “Chukua kitabu kingine na uandike juu yake maneno yote yaliyokuwa katika kile kitabu cha kwanza, ambacho Yehoyakimu mfalme wa Yuda amekiteketeza kwa moto.

29 Mwambie pia Yehoyakimu mfalme wa Yuda, ‘Hili ndilo asemaloBwana: Ulikiteketeza kile kitabu ukasema, “Kwa nini uliandika kwenye kitabu kwamba kwa hakika mfalme wa Babeli angekuja na kuangamiza nchi hii, na kuwakatilia mbali watu na wanyama kutoka humo?”

30 Kwa hiyo, hili ndilo asemaloBwanakuhusu Yehoyakimu mfalme wa Yuda: Hatakuwa na mtu yeyote atakayekalia kiti cha enzi cha Daudi; maiti yake itatupwa nje kwenye joto wakati wa mchana na kupigwa na baridi wakati wa usiku.

31 Nitamwadhibu yeye, watoto wake na watumishi wake kwa ajili ya uovu wao. Nitaleta juu yao na wote waishio Yerusalemu na watu wa Yuda kila maafa niliyoyasema dhidi yao, kwa sababu hawajasikiliza.’ ”

32 Kisha Yeremia akachukua kitabu kingine na kumpa mwandishi Baruku mwana wa Neria, naye kama Yeremia alivyosema, Baruku akaandika juu yake maneno yote ya kile kitabu ambacho Yehoyakimu mfalme wa Yuda alikuwa amekichoma moto, na maneno mengine mengi yaliyofanana na hayo yaliyoongezewa humo.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JER/36-2fda8ecc95aeb8e760099e8bb2aca80c.mp3?version_id=1627—

Categories
Yeremia

Yeremia 37

Yeremia Gerezani

1 Sedekia mwana wa Yosia akafanywa kuwa mfalme wa Yuda na Nebukadneza mfalme wa Babeli, naye akatawala mahali pa Yehoyakinimwana wa Yehoyakimu.

2 Lakini sio Sedekia, wala watumishi wake, wala watu wa nchi walisikiliza maneno yaBwanaaliyonena kupitia kwa nabii Yeremia.

3 Hata hivyo, Mfalme Sedekia akamtuma Yehukali mwana wa Shelemia, pamoja na kuhani Sefania mwana wa Maaseya kwa nabii Yeremia na ujumbe huu: “Tafadhali utuombee kwaBwana, Mungu wetu.”

4 Wakati huu Yeremia alikuwa huru kuingia na kutoka katikati ya watu, kwa sababu alikuwa bado hajatiwa gerezani.

5 Jeshi la Farao lilikuwa limetoka Misri, nao Wakaldayo waliokuwa wameuzunguka Yerusalemu kwa majeshi waliposikia taarifa kuhusu jeshi hilo walijiondoa Yerusalemu.

6 Ndipo neno laBwanalikamjia nabii Yeremia kusema:

7 “Hili ndilo asemaloBwana, Mungu wa Israeli: Mwambie mfalme wa Yuda aliyekutuma uniulize mimi, ‘Jeshi la Farao lililotoka kuja kukusaidia litarudi katika nchi yake yenyewe, yaani Misri.

8 Kisha Wakaldayo watarudi na kushambulia mji huu, watauteka na kuuchoma moto.’

9 “Hili ndiloBwanaasemalo: Msijidanganye wenyewe mkifikiri, ‘Hakika Wakaldayo watatuacha na kwenda zao.’ Hakika hawatawaacha!

10 Hata kama mngelishinda jeshi lote la Wakaldayo linalowashambulia ninyi, na wakawa ni watu waliojeruhiwa tu waliobaki kwenye mahema yao, wangetoka na kuuchoma mji huu moto.”

11 Baada ya jeshi la Wakaldayo kujiondoa kutoka Yerusalemu kwa sababu ya jeshi la Farao,

12 Yeremia akaanza kuondoka mjini ili kwenda nchi ya Benyamini ili akapate sehemu yake ya milki miongoni mwa watu huko.

13 Lakini alipofika kwenye Lango la Benyamini, mkuu wa walinzi, ambaye jina lake lilikuwa Iriya mwana wa Shelemia mwana wa Hanania, akamkamata Yeremia na kusema, “Wewe unakwenda kujiunga na Wakaldayo!”

14 Yeremia akasema, “Hiyo si kweli, mimi sijiungi na Wakaldayo.” Lakini Iriya hakumsikiliza; badala yake, akamkamata Yeremia na kumpeleka kwa maafisa.

15 Wakamkasirikia Yeremia, wakaamuru apigwe, na akafungwa katika nyumba ya Yonathani mwandishi waliyokuwa wameifanya gereza.

16 Yeremia akawekwa kwenye chumba kilichofukuliwa chini, kilichojengwa kwa zege ndani ya gereza chini ya ngome, akakaa huko kwa muda mrefu.

17 Kisha Mfalme Sedekia akatumana aletwe katika jumba la kifalme, mahali alipomuuliza kwa siri, “Je, kuna neno lolote kutoka kwaBwana?”

Yeremia akajibu, “Ndiyo, utatiwa mikononi mwa mfalme wa Babeli.”

18 Kisha Yeremia akamwambia Mfalme Sedekia, “Nimefanya kosa gani dhidi yako na maafisa wako au watu hawa, hata ukanitia gerezani?

19 Wako wapi manabii wako waliokutabiria wakisema, ‘Mfalme wa Babeli hatakushambulia wewe wala nchi hii?’

20 Lakini sasa, bwana wangu mfalme, tafadhali sikiliza. Niruhusu nilete maombi yangu mbele yako, usinirudishe kwenye nyumba ya Yonathani mwandishi, nisije nikafia humo.”

21 Ndipo Mfalme Sedekia akatoa maagizo Yeremia awekwe katika ua wa walinzi, na apewe mkate kutoka mitaa ya waokaji kila siku mpaka mikate yote katika mji itakapokwisha. Kwa hiyo Yeremia akabaki katika ua wa walinzi.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JER/37-5b5fbaef301f5b47a1a458dfc81aca3f.mp3?version_id=1627—

Categories
Yeremia

Yeremia 38

Yeremia Atupwa Kwenye Kisima

1 Shefatia mwana wa Matani, na Gedalia mwana wa Pashuri, na Yehukali mwana wa Shelemia, na Pashuri mwana wa Malkiya wakasikia kile Yeremia alichokuwa akiwaambia watu wote wakati aliposema,

2 “Hili ndilo asemaloBwana: ‘Yeyote akaaye ndani ya mji huu atakufa kwa upanga, njaa au tauni, lakini yeyote atakayejisalimisha kwa Wakaldayo ataishi. Atakayeyatoa maisha yake kama nyara, ataishi.’

3 Tena hili ndilo asemaloBwana: ‘Mji huu kwa hakika utatiwa mikononi mwa jeshi la mfalme wa Babeli, ambaye atauteka.’ ”

4 Ndipo maafisa wakamwambia mfalme, “Mtu huyu imempasa kuuawa. Anawakatisha tamaa askari waliobaki katika mji huu, vivyo hivyo na watu wote pia, kwa ajili ya mambo anayowaambia. Mtu huyu hawatakii mema watu hawa, bali maangamizi yao.”

5 Mfalme Sedekia akajibu, “Yeye yuko mikononi mwenu! Mfalme hawezi kufanya lolote kuwapinga ninyi.”

6 Basi wakamchukua Yeremia na kumtia kwenye kisima cha Malkiya, mwana wa mfalme, kilichokuwa katika ua wa walinzi. Wakamteremsha Yeremia kwa kamba ndani ya kisima. Hakikuwa na maji ndani yake, ila tope tu, naye Yeremia akazama ndani ya matope.

7 Lakini Ebed-Meleki Mkushi, aliyekuwa afisa katika jumba la kifalme, akasikia kuwa walikuwa wamemtia Yeremia ndani ya kisima. Wakati mfalme alipokuwa ameketi katika Lango la Benyamini,

8 Ebed-Meleki akatoka nje ya jumba la kifalme na kumwambia,

9 “Mfalme bwana wangu, watu hawa wamefanya uovu kwa yote waliomtendea nabii Yeremia. Wamemtupa ndani ya kisima, mahali ambapo atakufa kwa njaa wakati ambapo hakuna chakula popote katika mji.”

10 Basi mfalme akamwamuru Ebed-Meleki Mkushi, akisema, “Chukua watu thelathini kutoka hapa pamoja nawe, mkamtoe nabii Yeremia huko kwenye kisima kabla hajafa.”

11 Basi Ebed-Meleki akawachukua watu pamoja naye, wakaenda mpaka kwenye chumba kilichoko chini ya hazina ndani ya jumba la kifalme. Akachukua matambaa makuukuu pamoja na nguo zilizochakaa kutoka huko, na kumshushia Yeremia kwa kamba ndani ya kisima.

12 Ebed-Meleki Mkushi akamwambia Yeremia, “Weka haya matambaa makuukuu na hizo nguo zilizochakaa makwapani ili kuzuia kamba.” Yeremia akafanya hivyo,

13 nao wakamvuta juu kwa kamba na kumtoa katika kisima. Yeremia akakaa katika ua wa walinzi.

Sedekia Amhoji Yeremia Tena

14 Ndipo Mfalme Sedekia akatuma watu wamwitie nabii Yeremia wamlete kwake kwenye ingilio la tatu la Hekalu laBwana. Mfalme akamwambia Yeremia, “Ninataka kukuuliza jambo fulani, usinifiche kitu chochote.”

15 Yeremia akamwambia Sedekia, “Nikikupa jibu, je, hutaniua? Hata kama nikikupa shauri, wewe hutanisikiliza.”

16 Lakini Mfalme Sedekia akamwapia Yeremia kiapo hiki kwa siri, akisema, “Hakika kama aishivyoBwana, ambaye ametupa pumzi, sitakuua wala sitakutia mikononi mwa wale wanaotafuta uhai wako.”

17 Kisha Yeremia akamwambia Sedekia, “Hili ndilo asemaloBwanaMungu Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: ‘Ikiwa utajisalimisha kwa maafisa wa mfalme wa Babeli, maisha yako yatasalimika, na mji huu hautateketezwa kwa moto. Pia wewe na jamaa yako mtaishi.

18 Lakini ikiwa hutajisalimisha kwa maafisa wa mfalme wa Babeli, mji huu utatiwa mikononi mwa Wakaldayo na watauteketeza kwa moto, nawe mwenyewe hutaweza kujiokoa mikononi mwao.’ ”

19 Mfalme Sedekia akamwambia Yeremia, “Ninawaogopa Wayahudi ambao wamekimbilia kwa Wakaldayo, kwa kuwa Wakaldayo wanaweza kunitia mikononi mwao, nao wakanitenda vibaya.”

20 Yeremia akajibu, “Hawatakutia mikononi mwao. MtiiBwanakwa kufanya kile ninachokuambia. Kisha utafanikiwa na maisha yako yatakuwa salama.

21 Lakini ukikataa kujisalimisha, hili ndiloBwanaalilonifunulia:

22 Wanawake wote walioachwa katika jumba la kifalme la mfalme wa Yuda wataletwa mbele ya maafisa wa mfalme wa Babeli. Wanawake hao watakuambia:

“ ‘Walikupotosha na kukushinda,

wale rafiki zako uliowaamini.

Miguu yako imezama matopeni;

rafiki zako wamekuacha.’

23 “Wake zako wote na watoto wataletwa na kutiwa mikononi mwa Wakaldayo. Wewe mwenyewe hutaweza kujiokoa mikononi mwao. Lakini utatekwa na mfalme wa Babeli, na mji huu utateketezwa kwa moto.”

24 Kisha Sedekia akamwambia Yeremia, “Usiruhusu mtu yeyote ajue kuhusu haya mazungumzo, la sivyo utakufa.

25 Maafisa wakisikia kwamba nimezungumza nawe, nao wakakujia na kusema, ‘Tuambie kile ulichozungumza na mfalme na kile mfalme alichokuambia, usitufiche au sivyo tutakuua,’

26 basi waambie, ‘Nilikuwa ninamsihi mfalme asinirudishe kwenye nyumba ya Yonathani nisije nikafia humo.’ ”

27 Maafisa wote wakamjia Yeremia na kumuuliza, naye Yeremia akawaambia kila kitu mfalme alichomwagiza kusema. Kisha hawakusema lolote zaidi na Yeremia kwa sababu hakuna yeyote aliyesikia mazungumzo yake na mfalme.

28 Naye Yeremia akabaki katika ua wa walinzi hadi siku Yerusalemu ilipotekwa.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JER/38-d77bf7850fbfaa60d21dd26098288fd9.mp3?version_id=1627—

Categories
Yeremia

Yeremia 39

Anguko La Yerusalemu

1 Hivi ndivyo Yerusalemu ilivyotwaliwa: Katika mwaka wa tisa wa utawala wa Mfalme Sedekia wa Yuda, katika mwezi wa kumi, Nebukadneza mfalme wa Babeli akiwa na jeshi lake lote alifanya vita dhidi ya Yerusalemu na akauzunguka mji.

2 Katika siku ya tisa ya mwezi wa nne wa mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Sedekia, ukuta wa mji ulibomolewa.

3 Kisha maafisa wote wa mfalme wa Babeli wakaja na kuketi kwenye Lango la Kati, nao ni: Nergal-Shareza wa Samgari, Nebo-Sarsekimu afisa mkuu, Nergal-Shareza afisa mwenye cheo cha juu, na maafisa wengine wote wa mfalme wa Babeli.

4 Mfalme Sedekia wa Yuda na askari wote walipowaona, wakakimbia na kuondoka mjini usiku kwa njia ya bustani ya mfalme, kupitia lango lililokuwa kati ya kuta mbili, wakaelekea Araba.

5 Lakini jeshi la Wakaldayo likawafuatia na kumpata Sedekia katika sehemu tambarare za Yeriko. Wakamkamata na kumpeleka kwa Nebukadneza mfalme wa Babeli huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, mahali ambapo alimtangazia hukumu.

6 Huko Ribla, mfalme wa Babeli aliwachinja wana wa Sedekia mbele ya macho yake, na pia akawaua wakuu wote wa Yuda.

7 Kisha akayangʼoa macho ya Sedekia na kumfunga kwa pingu za shaba na kumpeleka Babeli.

8 Jeshi la Wakaldayo likachoma moto jumba la kifalme na nyumba za watu, na kuzibomoa kuta za Yerusalemu.

9 Nebuzaradani kiongozi wa walinzi wa mfalme akawachukua na kuwapeleka uhamishoni Babeli watu waliokuwa wamebaki ndani ya mji, pamoja na wale waliokuwa wamejisalimisha kwake, na watu wengine wote.

10 Lakini Nebuzaradani kiongozi wa walinzi aliwabakiza baadhi ya watu maskini katika nchi ya Yuda, ambao hawakuwa na kitu. Naye wakati huo akawapa mashamba ya mizabibu na mashamba mengine.

11 Basi, Nebukadneza mfalme wa Babeli alikuwa ametoa maagizo kuhusu Yeremia kupitia Nebuzaradani kiongozi wa walinzi wa mfalme akisema:

12 “Mchukue umtunze. Usimdhuru, lakini umfanyie chochote anachotaka.”

13 Basi Nebuzaradani kiongozi wa walinzi, Nebushazbani afisa mkuu, Nergal-Shareza afisa wa cheo cha juu, na maafisa wengine wote wa mfalme wa Babeli

14 wakatuma watu kumwondoa Yeremia kutoka ua wa walinzi. Wakamkabidhi kwa Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani, ili amrudishe nyumbani kwake. Kwa hiyo akabaki miongoni mwa watu wake mwenyewe.

15 Wakati Yeremia alipokuwa amezuiliwa katika ua wa walinzi, neno laBwanalilimjia kusema:

16 “Nenda ukamwambie Ebed-Meleki Mkushi, ‘Hili ndiloBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: Ninakaribia kutimiza maneno yangu dhidi ya mji huu kwa njia ya maafa, wala si kwa kuwafanikisha. Wakati huo hayo yatatimizwa mbele ya macho yako.

17 Lakini siku hiyo nitakuokoa, asemaBwana; hutatiwa mikononi mwa wale unaowaogopa.

18 Nitakuokoa; hutaanguka kwa upanga, lakini maisha yako yatakuwa salama, kwa sababu unanitumaini, asemaBwana.’ ”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JER/39-1d95a259deec49a150ec6dac7bd0af60.mp3?version_id=1627—

Categories
Yeremia

Yeremia 40

Yeremia Aachiwa Huru

1 Neno likamjia Yeremia kutoka kwaBwanabaada ya Nebuzaradani kiongozi wa walinzi wa mfalme kumfungua huko Rama. Alikuwa amemkuta Yeremia akiwa amefungwa kwa minyororo miongoni mwa mateka wote kutoka Yerusalemu na Yuda waliokuwa wakipelekwa uhamishoni Babeli.

2 Kiongozi wa walinzi alipomwona Yeremia, akamwambia, “BwanaMungu wako aliamuru maafa haya kwa mahali hapa.

3 SasaBwanaameyaleta haya, amefanya sawasawa na vile alivyosema angefanya. Yote haya yametokea kwa sababu ninyi mlifanya dhambi dhidi yaBwanana hamkumtii.

4 Lakini leo ninakufungua minyororo iliyo kwenye viwiko vya mikono yako. Twende pamoja mpaka Babeli ikiwa unataka, nami nitakutunza. Lakini kama hutaki, basi usije. Tazama, nchi yote iko mbele yako, nenda kokote unakotaka.”

5 Lakini kabla Yeremia hajageuka kuondoka, Nebuzaradani akaongeza kusema, “Rudi kwa Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani, ambaye mfalme wa Babeli amemchagua awe juu ya miji ya Yuda, ukaishi naye miongoni mwa watu, au uende popote panapokupendeza.”

Kisha huyo kiongozi akampa posho yake na zawadi, akamwacha aende zake.

6 Kwa hiyo Yeremia akaenda kwa Gedalia mwana wa Ahikamu huko Mispa, na kuishi naye miongoni mwa watu walioachwa katika nchi.

Gedalia Auawa

7 Maafisa wote wa jeshi na watu wao waliokuwa bado wapo kwenye eneo la wazi waliposikia kwamba mfalme wa Babeli amemteua Gedalia mwana wa Ahikamu kuwa mtawala wa nchi, na amemweka kuwa kiongozi wa wanaume, wanawake na watoto waliokuwa maskini zaidi katika nchi ambao hawakuchukuliwa kwenda uhamishoni Babeli,

8 wakamjia Gedalia huko Mispa. Hawa walikuwa Ishmaeli mwana wa Nethania, Yohanani na Yonathani wana wa Karea, Seraya mwana wa Tanhumethi, wana wa Efai Mnetofathi, na Yezania mwana wa Mmaaka, pamoja na watu wao.

9 Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani akaapa ili kuwatia moyo wao na watu wao. Akasema: “Msiogope kuwatumikia Wakaldayo. Kaeni katika nchi na kumtumikia mfalme wa Babeli, na itakuwa vyema kwenu.

10 Mimi mwenyewe nitakaa Mispa ili kuwawakilisha mbele ya Wakaldayo wanaotujia, lakini ninyi mtavuna divai, matunda ya kiangazi na mafuta, nanyi mtaweka katika vyombo vyenu vya kuhifadhia, na kuishi katika miji mliyojitwalia.”

11 Wayahudi wote waliokuwa Moabu, Amoni, Edomu na nchi nyingine zote waliposikia kwamba mfalme wa Babeli ameacha mabaki ya watu katika Yuda na amemweka Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani kuwa mtawala wao,

12 wakarudi wote katika nchi ya Yuda kwa Gedalia huko Mispa, kutoka nchi zote ambazo walikuwa wametawanywa. Nao wakavuna divai na matunda tele wakati wa kiangazi.

13 Yohanani mwana wa Karea pamoja na maafisa wote wa jeshi waliokuwa bado wapo kwenye eneo la wazi wakamjia Gedalia huko Mispa

14 na kumwambia, “Je, hujui kwamba Baalisi mfalme wa Waamoni amemtuma Ishmaeli mwana wa Nethania akuue?” Lakini Gedalia mwana wa Ahikamu hakuwaamini.

15 Kisha Yohanani mwana wa Karea akamwambia Gedalia kwa siri huko Mispa, “Acha niende nikamuue Ishmaeli mwana wa Nethania, wala hakuna atakayejua. Kwa nini akuue na kusababisha Wayahudi wote waliokuzunguka watawanyike, na mabaki wa Yuda waangamie?”

16 Lakini Gedalia mwana wa Ahikamu akamwambia Yohanani mwana wa Karea, “Usifanye jambo kama hilo! Unalosema kuhusu Ishmaeli si kweli.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JER/40-2b41241e28fda5b61839539c135b76e0.mp3?version_id=1627—

Categories
Yeremia

Yeremia 41

1 Katika mwezi wa saba Ishmaeli mwana wa Nethania mwana wa Elishama, aliyekuwa wa uzao wa mfalme na pia alikuwa mmoja wa maafisa wa mfalme, akaja pamoja na watu kumi kwa Gedalia mwana wa Ahikamu huko Mispa. Walipokuwa wakila pamoja huko,

2 Ishmaeli mwana wa Nethania pamoja na wale watu kumi waliokuwa pamoja naye waliinuka na kumuua Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani kwa upanga, wakamuua yule ambaye mfalme wa Babeli alikuwa amemteua awe mtawala wa nchi.

3 Ishmaeli akawaua pia Wayahudi wote waliokuwa na Gedalia huko Mispa, pamoja na askari wa Kikaldayo waliokuwa huko.

4 Siku moja baada ya kuuawa kwa siri kwa Gedalia, kabla mtu yeyote hajafahamu jambo hilo,

5 watu themanini waliokuwa wamenyoa ndevu zao, waliorarua nguo zao na kujikatakata walikuja kutoka Shekemu, Shilo na Samaria wakileta sadaka za nafaka na uvumba katika nyumba yaBwana.

6 Ishmaeli mwana wa Nethania akaondoka Mispa ili kwenda kuwalaki, huku akilia alipokuwa akienda. Alipokutana nao, akasema, “Karibuni kwa Gedalia mwana wa Ahikamu.”

7 Walipoingia mjini, Ishmaeli mwana wa Nethania na wale watu waliokuwa pamoja naye wakawachinja na kuwatupa ndani ya kisima.

8 Lakini watu kumi miongoni mwao wakamwambia Ishmaeli, “Sisi usituue! Tuna ngano na shayiri, mafuta na asali, vilivyofichwa katika shamba.” Kwa hiyo akawaacha na hakuwaua pamoja na wale wengine.

9 Basi kile kisima ambacho alitupa zile maiti za watu aliowaua pamoja na Gedalia kilikuwa ni kile kisima ambacho Mfalme Asa alikifanya sehemu ya ulinzi wake dhidi ya Baasha mfalme wa Israeli. Ishmaeli mwana wa Nethania akakijaza kisima hicho kwa maiti.

10 Ishmaeli akawafanya mateka watu wote ambao Nebuzaradani kiongozi wa walinzi wa mfalme alikuwa amewaacha huko Mispa na kumweka Gedalia mwana wa Ahikamu juu yao: walikuwa binti za mfalme pamoja na watu wote aliokuwa amewaacha huko. Ishmaeli mwana wa Nethania akawachukua mateka na kuondoka nao, akavuka kwenda kwa Waamoni.

11 Yohanani mwana wa Karea na maafisa wote wa jeshi waliokuwa pamoja naye waliposikia juu ya uhalifu wote ambao Ishmaeli mwana wa Nethania alikuwa ameufanya,

12 waliwachukua watu wao wote kwenda kupigana na Ishmaeli mwana wa Nethania. Wakakutana naye karibu na bwawa kubwa huko Gibeoni.

13 Ikawa watu wote waliokuwa na Ishmaeli walipomwona Yohanani mwana wa Karea pamoja na maafisa wa jeshi waliokuwa pamoja naye, wakafurahi.

14 Watu wote ambao Ishmaeli alikuwa amewachukua mateka huko Mispa wakageuka na kumfuata Yohanani mwana wa Karea.

15 Lakini Ishmaeli mwana wa Nethania pamoja na watu wake wanane wakamtoroka Yohanani na kukimbilia kwa Waamoni.

Kukimbilia Misri

16 Ndipo Yohanani mwana wa Karea pamoja na maafisa wote wa jeshi waliokuwa pamoja naye wakawaongoza wote walionusurika kutoka Mispa, ambao walipona kutoka mikononi mwa Ishmaeli mwana wa Nethania baada yake kumuua Gedalia mwana wa Ahikamu: walikuwa askari, wanawake, watoto na matowashi aliowaleta kutoka Gibeoni.

17 Kisha wakaenda mbele na kutua Geruth-Kimhamu karibu na Bethlehemu wakiwa njiani kwenda Misri

18 ili kuwatoroka Wakaldayo. Waliwaogopa kwa sababu Ishmaeli mwana wa Nethania alikuwa amemuua Gedalia mwana wa Ahikamu, ambaye alikuwa amewekwa na mfalme wa Babeli kuwa mtawala wa nchi.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JER/41-ccd8f5f9bab8a17c7046626013160691.mp3?version_id=1627—