Categories
Mwanzo

Mwanzo 20

Abrahamu Na Abimeleki

1 Basi Abrahamu akaendelea mbele kutoka huko hadi nchi ya Negebu na akaishi kati ya Kadeshi na Shuri. Kwa muda mfupi alikaa Gerari kama mgeni,

2 huko Abrahamu akasema kuhusu Sara mkewe, “Huyu ni dada yangu.” Kisha Abimeleki mfalme wa Gerari akatuma Sara aletwe, naye akamchukua.

3 Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto wakati wa usiku na kumwambia, “Wewe ni kama mfu kwa sababu ya huyu mwanamke uliyemchukua; yeye ni mke wa mtu.”

4 Wakati huo Abimeleki alikuwa bado hajamsogelea, kwa hiyo akasema, “Je, Bwana utaliharibu taifa lisilo na hatia?

5 Hakusema kwangu, ‘Huyu ni dada yangu,’ naye Sara pia hakusema, ‘Huyu ni kaka yangu’? Nimefanya haya kwa dhamiri njema na mikono safi.”

6 Kisha Mungu akamwambia katika ndoto, “Ndiyo, najua ya kwamba umefanya haya kwa dhamiri safi, kwa hiyo nimekuzuia usinitende dhambi. Ndiyo sababu sikukuacha umguse.

7 Sasa umrudishe huyo mke wa mtu, kwa maana ni nabii, naye atakuombea nawe utaishi. Lakini kama hutamrudisha, ujue kwa hakika kuwa wewe na watu wako wote mtakufa.”

8 Kesho yake asubuhi na mapema Abimeleki akawaita maafisa wake wote, na baada ya kuwaambia yote yaliyotokea, waliogopa sana.

9 Kisha Abimeleki akamwita Abrahamu na kumwambia, “Wewe umetufanyia nini? Nimekukosea nini hata ukaleta hatia kubwa namna hii juu yangu na ufalme wangu? Umenifanyia mambo ambayo hayakupasa kufanyika.”

10 Abimeleki akamuuliza Abrahamu, “Ulikuwa na kusudi gani kufanya hivi?”

11 Abrahamu akajibu, “Niliwaza kwamba, ‘Hakika hakuna hofu ya Mungu mahali hapa, nao wataniua kwa sababu ya mke wangu.’

12 Pamoja na hayo, ni kweli kwamba yeye ni dada yangu, binti wa baba yangu ingawa si mtoto wa mama yangu; basi akawa mke wangu.

13 WakatiBwanaaliponifanya nisafiri mbali na nyumbani mwa baba yangu, nilimwambia, ‘Hivi ndivyo utakavyoonyesha pendo lako kwangu: Kila mahali tutakapokwenda, kuhusu mimi sema, “Huyu ni kaka yangu.” ’ ”

14 Kisha Abimeleki akatwaa kondoo na ngʼombe, na watumwa wa kiume na wa kike akampa Abrahamu, akamrudisha Sara kwa mumewe.

15 Abimeleki akasema, “Nchi yangu iko mbele yako, ishi popote unapotaka.”

16 Akamwambia Sara, “Ninampa kaka yako shekeli elfu moja za fedha. Hii ni kufidia kosa lililofanyika dhidi yako mbele ya wote walio pamoja nawe; haki yako imethibitishwa kabisa.”

17 Kisha Abrahamu akamwomba Mungu, naye Mungu akamponya Abimeleki, mke wake, na watumwa wake wa kike kwamba waweze kupata watoto tena,

18 kwa kuwaBwanaalikuwa ameyafunga matumbo ya wote katika nyumba ya Abimeleki kwa sababu ya Sara, mke wa Abrahamu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/GEN/20-e60b3ec0343050cc0c82305af3bde6a0.mp3?version_id=1627—

Categories
Mwanzo

Mwanzo 21

Kuzaliwa Kwa Isaki

1 Wakati huuBwanaakamrehemu Sara kama alivyokuwa amesema, nayeBwanaakamtendea Sara kile alichokuwa ameahidi.

2 Sara akapata mimba, akamzalia Abrahamu mwana katika uzee wake, majira yale ya Mungu aliomwahidi.

3 Abrahamu akamwita Isaki yule mwana ambaye Sara alimzalia.

4 Isaki alipokuwa na umri wa siku nane, Abrahamu akamtahiri, kama Mungu alivyomwamuru.

5 Abrahamu alikuwa na miaka 100 wakati Isaki mwanawe alipozaliwa.

6 Sara akasema, “Mungu ameniletea kicheko, kila mmoja atakayesikia jambo hili atacheka pamoja nami.”

7 Akaongeza kusema, “Nani angemwambia Abrahamu kuwa Sara angenyonyesha watoto? Tena nimemzalia mwana katika uzee wake.”

Hagari Na Ishmaeli Wafukuzwa

8 Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya. Siku hiyo Isaki alipoachishwa kunyonya, Abrahamu alifanya sherehe kubwa.

9 Lakini Sara aliona kuwa mwana ambaye Hagari, Mmisri, aliyemzalia Abrahamu alikuwa anadhihaki,

10 Sara akamwambia Abrahamu, “Mwondoe mwanamke huyo mtumwa pamoja na mwanawe, kwa kuwa mwana wa mwanamke mtumwa kamwe hatarithi pamoja na mwanangu Isaki.”

11 Jambo hili lilimhuzunisha sana Abrahamu kwa sababu lilimhusu mwanawe.

12 Lakini Mungu akamwambia, “Usihuzunike hivyo kwa sababu ya kijana na mtumishi wako wa kike. Sikiliza lolote Sara analokuambia, kwa sababu uzao wako utahesabiwa kupitia kwake Isaki.

13 Nitamfanya huyu mwana wa mtumishi wako wa kike kuwa taifa pia, kwa sababu naye ni uzao wako.”

14 Kesho yake asubuhi na mapema, Abrahamu akachukua chakula na kiriba cha maji, akampa Hagari. Akaviweka mabegani mwa Hagari, akamwondoa pamoja na kijana. Hagari akashika njia, akatangatanga katika jangwa la Beer-Sheba.

15 Maji yalipokwisha kwenye kiriba, akamwacha kijana chini ya mojawapo ya vichaka.

16 Kisha akajiendea zake akaketi karibu, umbali wa kutupa mshale, akawaza, “Siwezi kumwangalia kijana akifa.” Ikawa alipokuwa ameketi pale karibu, akaanza kulia kwa huzuni.

17 Mungu akamsikia kijana akilia, malaika wa Mungu akamwita Hagari kutoka mbinguni na kumwambia, “Kuna nini Hagari? Usiogope, Mungu amesikia kijana analia akiwa amelala pale.

18 Mwinue kijana na umshike mkono, kwa maana nitamfanya kuwa taifa kubwa.”

19 Ndipo Mungu akamfumbua Hagari macho yake naye akaona kisima cha maji. Hivyo akaenda akajaza kiriba maji na kumpa kijana anywe.

20 Mungu akawa pamoja na huyu kijana alipokuwa akiendelea kukua. Aliishi jangwani na akawa mpiga upinde.

21 Alipokuwa akiishi katika Jangwa la Parani, mama yake akampatia mke kutoka Misri.

Mapatano Katika Beer-Sheba

22 Wakati huo Abimeleki na Fikoli mkuu wa majeshi yake wakamwambia Abrahamu, “Mungu yu pamoja nawe katika kila kitu unachofanya.

23 Sasa niapie hapa mbele za Mungu kwamba hutanitenda hila mimi, watoto wangu wala wazao wangu. Nitendee mimi na nchi ambayo unaishi kama mgeni wema ule ule ambao nimekutendea.”

24 Abrahamu akasema, “Ninaapa hivyo.”

25 Ndipo Abrahamu akalalamika kwa Abimeleki kuhusu kisima cha maji ambacho watumishi wa Abimeleki walikuwa wamekinyangʼanya.

26 Lakini Abimeleki akasema, “Sijui ni nani ambaye amefanya hili. Hukuniambia, leo tu ndipo ninasikia habari zake.”

27 Hivyo Abrahamu akaleta kondoo na ngʼombe, akampa Abimeleki, nao watu hawa wawili wakafanya mapatano.

28 Abrahamu akatenga kondoo wa kike saba kutoka kwenye kundi,

29 Abimeleki akamuuliza Abrahamu, “Ni nini maana ya hawa kondoo wa kike saba uliowatenga peke yao?”

30 Abrahamu akamjibu, “Upokee hawa kondoo wa kike saba kutoka mkononi mwangu kama ushahidi kuwa nilichimba kisima hiki.”

31 Hivyo mahali pale pakaitwa Beer-Sheba, kwa sababu watu wawili waliapiana hapo.

32 Baada ya mapatano kufanyika huko Beer-Sheba, Abimeleki na Fikoli mkuu wa majeshi yake wakarudi katika nchi ya Wafilisti.

33 Abrahamu akapanda mti wa mkwaju huko Beer-Sheba, na hapo akaliitia jina laBwana, Mungu wa milele.

34 Naye Abrahamu akakaa katika nchi ya Wafilisti kwa muda mrefu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/GEN/21-4146966073bce336b0fbeac084cd1f2a.mp3?version_id=1627—

Categories
Mwanzo

Mwanzo 22

Kujua Uthabiti Wa Abrahamu

1 Baadaye Mungu akamjaribu Abrahamu. Akamwambia, “Abrahamu!”

Abrahamu akajibu, “Mimi hapa.”

2 Kisha Mungu akamwambia, “Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, Isaki umpendaye, uende katika nchi ya Moria. Mtoe huko kama sadaka ya kuteketezwa juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia.”

3 Abrahamu akaamka asubuhi na mapema siku iliyofuata, akamtayarisha punda wake. Akawachukua watumishi wake wawili pamoja na Isaki mwanawe. Baada ya kuchanja kuni za kutosha kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka kuelekea mahali Mungu alipokuwa amemwambia.

4 Siku ya tatu Abrahamu akainua macho, akapaona mahali pale kwa mbali.

5 Akawaambia watumishi wake, “Kaeni hapa pamoja na punda, wakati mimi na kijana tunakwenda kule. Tutakwenda kuabudu na kisha tutawarudia.”

6 Abrahamu akachukua kuni kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, akamtwika Isaki mwanawe, yeye mwenyewe akachukua moto na kisu. Walipokuwa wakienda pamoja,

7 Isaki akanena akamwambia Abrahamu baba yake, “Baba yangu!”

Abrahamu akaitika, “Mimi hapa, mwanangu.”

Isaki akasema, “Moto na kuni zipo, Je, yuko wapi mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa?”

8 Abrahamu akajibu, “Mwanangu, Mungu mwenyewe atajipatia mwana-kondoo kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa.” Nao hawa wawili wakaendelea mbele pamoja.

9 Walipofika mahali pale alipokuwa ameambiwa na Mungu, Abrahamu akajenga madhabahu hapo, akaziweka kuni juu yake. Akamfunga Isaki mwanawe na akamlaza kwenye madhabahu, juu ya zile kuni.

10 Kisha akanyoosha mkono wake na akachukua kisu ili amchinje mwanawe.

11 Lakini malaika waBwanaakamwita kutoka mbinguni, akamwambia, “Abrahamu! Abrahamu!”

Akajibu, “Mimi hapa.”

12 Akamwambia, “Usimdhuru kijana, wala usimtendee jambo lolote. Sasa ninajua kwamba unamcha Mungu, kwa sababu hukunizuilia mwanao, mwana wako wa pekee.”

13 Abrahamu akainua macho yake, akaona kondoo dume amenaswa pembe zake nyuma yake katika kichaka. Akaenda akamchukua huyo kondoo dume, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe.

14 Abrahamu akapaita mahali pale Yehova-Yire.Mpaka siku ya leo inasemekana, “Katika mlima waBwanaitapatikana.”

15 Basi malaika waBwanaakamwita Abrahamu kutoka mbinguni mara ya pili,

16 akasema, “Ninaapa kwa nafsi yangu, asemaBwana, kwamba kwa sababu umefanya jambo hili na hukunizuilia mwanao, mwana wako wa pekee,

17 hakika nitakubariki, na nitauzidisha uzao wako kama nyota za angani na kama mchanga ulioko pwani. Wazao wako watamiliki miji ya adui zao,

18 na kupitia uzao wako mataifa yote duniani yatabarikiwa, kwa sababu umenitii.”

19 Ndipo Abrahamu akawarudia watumishi wake, wakaondoka wakaenda wote pamoja mpaka Beer-Sheba. Abrahamu akaishi huko Beer-Sheba.

Wana Wa Nahori

20 Baada ya muda, Abrahamu akaambiwa, “Milka pia amepata watoto, amemzalia ndugu yako Nahori wana:

21 Usi mzaliwa wake wa kwanza, Buzi nduguye, Kemueli (baba wa Aramu),

22 Kesedi, Hazo, Pildashi, Yidlafu na Bethueli.”

23 Bethueli akamzaa Rebeka. Milka alimzalia Nahori nduguye Abrahamu hao wana wanane.

24 Suria wake Nahori aliyeitwa Reuma pia alikuwa na wana: Teba, Gahamu, Tahashi na Maaka.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/GEN/22-82dbfe1a03e13c70a748d1dba50033f8.mp3?version_id=1627—

Categories
Mwanzo

Mwanzo 23

Kifo Cha Sara

1 Sara aliishi akawa na umri wa miaka mia na ishirini na saba.

2 Sara akafa huko Kiriath-Arba (yaani Hebroni) katika nchi ya Kanaani, Abrahamu akamwombolezea na kumlilia Sara.

3 Ndipo Abrahamu akainuka kutoka pale penye maiti ya mke wake. Akazungumza na Wahiti, akasema,

4 “Mimi ni mpitaji na mgeni miongoni mwenu. Niuzieni sehemu ya ardhi yenu ili niweze kumzika maiti wangu.”

5 Wahiti wakamjibu Abrahamu,

6 “Bwana, tusikilize. Wewe ni mtawala mkuu sana miongoni mwetu. Zika maiti wako katika kaburi unalolipenda kati ya makaburi yetu. Hakuna mtu wa kwetu atakayekuzuia kaburi lake ili kuzika maiti wako.”

7 Abrahamu akainuka na akasujudu mbele ya wenyeji wa nchi, yaani Wahiti.

8 Akawaambia, “Kama mnaniruhusu kumzika maiti wangu, basi nisikilizeni mkamsihi Efroni mwana wa Sohari kwa niaba yangu

9 ili aniuzie pango la Makpela, lililo mali yake, nalo liko mwisho wa shamba lake. Mwambieni aniuzie kwa bei kamili atakayosema ili liwe mahali pangu pa kuzikia miongoni mwenu.”

10 Efroni Mhiti alikuwa ameketi miongoni mwa watu wake, akamjibu Abrahamu mbele ya Wahiti wote waliokuwepo katika lango la mji.

11 “La hasha, bwana wangu, nisikilize, nakupa shamba, pia nakupa pango lililomo ndani yake. Nakupa mbele ya watu wangu. Uzike maiti wako.”

12 Abrahamu akasujudu tena, mbele ya wenyeji wa nchi,

13 akamwambia Efroni wale watu wakiwa wanasikia, “Tafadhali nisikilize. Nitakulipa fedha za hilo shamba. Kubali kuzipokea ili niweze kumzika maiti wangu.”

14 Efroni akamjibu Abrahamu,

15 “Nisikilize, bwana wangu, thamani ya ardhi hiyo ni shekeli 400 za fedha,lakini hiyo ni nini kati yako na mimi? Mzike maiti wako.”

16 Abrahamu akakubali masharti ya Efroni, akampimia ile fedha aliyotaja masikioni mwa Wahiti: Shekeli 400 za fedha kulingana na viwango vya uzito vilivyokuwa vikitumika wakati huo na wafanyabiashara.

17 Hivyo shamba la Efroni huko Makpela karibu na Mamre, yaani shamba pamoja na pango lililokuwamo, nayo miti yote iliyokuwamo ndani ya mipaka ya shamba hilo, vilikabidhiwa,

18 kwa Abrahamu kuwa mali yake mbele ya Wahiti wote waliokuwa wamekuja kwenye lango la mji.

19 Baada ya hayo Abrahamu akamzika Sara mkewe kwenye pango ndani ya shamba la Makpela karibu na Mamre (huko Hebroni) katika nchi ya Kanaani.

20 Hivyo Wahiti wakamkabidhi Abrahamu shamba pamoja na pango lililokuwa humo kuwa mahali pa kuzikia.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/GEN/23-0efe194da9756d5b560376b94a464b13.mp3?version_id=1627—

Categories
Mwanzo

Mwanzo 24

Isaki Na Rebeka

1 Wakati huu Abrahamu alikuwa mzee mwenye miaka mingi, nayeBwanaalikuwa amembariki katika kila njia.

2 Akamwambia mtumishi wake mkuu wa vitu vyote katika nyumba yake, yule aliyekuwa msimamizi wa vitu vyote alivyokuwa navyo, “Weka mkono wako chini ya paja langu,

3 Ninataka uape kwaBwana, Mungu wa mbingu na Mungu wa nchi, kwamba hutamtwalia mwanangu mke kutoka binti za Wakanaani, ambao ninaishi miongoni mwao,

4 bali utakwenda katika nchi yangu na jamaa zangu umpatie Isaki mwanangu mke.”

5 Yule mtumishi akamuuliza, “Je, kama huyo mwanamke atakataa kuja nami katika nchi hii? Je, nimpeleke mwanao katika hiyo nchi uliyotoka?”

6 Abrahamu akasema, “Hakikisha kwamba hutamrudisha mwanangu huko.

7 Bwana, Mungu wa mbingu, aliyenitoa nyumbani kwa baba yangu na nchi yangu niliyozaliwa na aliyesema nami na akaniahidi kwa kiapo, akisema, ‘Nitawapa watoto wako nchi hii,’ atatuma malaika wake akutangulie ili umpatie mwanangu mke kutoka huko.

8 Kama huyo mwanamke asipokubali kufuatana nawe, basi utafunguliwa kutoka kiapo nilichokuapisha. Ila usimrudishe mwanangu huko.”

9 Basi yule mtumishi akaweka mkono wake chini ya paja la bwana wake Abrahamu akamwapia kuhusu shauri hili.

10 Ndipo huyo mtumishi akachukua ngamia kumi miongoni mwa ngamia za bwana wake, akaondoka, akiwa amechukua aina zote za vitu vizuri kutoka kwa bwana wake. Akaelekea Aramu-Naharaimuna kushika njia kwenda mji wa Nahori.

11 Akawapigisha ngamia magoti karibu na kisima cha maji nje ya mji, ilikuwa inaelekea jioni, wakati ambapo wanawake wanakuja kuteka maji.

12 Kisha akaomba, “EeBwana, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, nipatie ushindi leo, uonyeshe huruma kwa bwana wangu Abrahamu.

13 Tazama, nimesimama karibu na kisima hiki cha maji, nao binti za watu wa mji huu wanakuja kuteka maji.

14 Basi na iwe hivi, nitakapomwambia binti mmojawapo, ‘Tafadhali tua mtungi wako nipate kunywa maji,’ naye akisema, ‘Kunywa, nitawanywesha na ngamia wako pia.’ Basi na awe ndiye uliyemchagua kwa ajili ya mtumishi wako Isaki. Kwa hili nitajua umemhurumia bwana wangu.”

15 Ikawa kabla hajamaliza kuomba, Rebeka akatokea akiwa na mtungi begani mwake. Alikuwa binti wa Bethueli. Bethueli alikuwa mwana wa Milka aliyekuwa mke wa Nahori ndugu wa Abrahamu.

16 Huyu msichana alikuwa mzuri sana wa sura, bikira, ambaye hakuna mtu aliyekuwa amekutana naye kimwili. Aliteremka kisimani, akajaza mtungi wake akapanda juu.

17 Ndipo yule mtumishi akaharakisha kukutana naye akamwambia, “Tafadhali nipe maji kidogo katika mtungi wako.”

18 Yule msichana akasema, “Kunywa, bwana wangu.” Akashusha kwa haraka mtungi mkononi mwake na akampa, akanywa.

19 Baada ya kumpa yule mtumishi yale maji, akamwambia, “Nitateka maji kwa ajili ya ngamia zako pia mpaka wote watosheke.”

20 Akafanya haraka kumimina maji kwenye birika ya kunyweshea wanyama, akakimbia kisimani kuteka maji mengine na akateka ya kuwatosha ngamia wake wote.

21 Pasipo kusema neno, yule mtumishi akamtazama kwa makini aone kamaBwanaameifanikisha safari yake, au la.

22 Ikawa ngamia walipokwisha kunywa wote, yule mtumishi akampa huyo msichana pete ya puani ya dhahabu yenye uzito wa beka mojana bangili mbili za dhahabu zenye uzito wa shekeli kumi.

23 Kisha akamuuliza, “Wewe ni binti wa nani? Tafadhali uniambie, je, kuna nafasi katika nyumba ya baba yako tutakapoweza kulala?”

24 Yule msichana akamjibu, “Mimi ni binti wa Bethueli, mwana wa Milka aliyemzalia Nahori.”

25 Akaendelea kusema, “Kwetu kuna majani mengi na malisho, tena kuna nafasi kwa ajili yenu kulala.”

26 Yule mtumishi akasujudu na kumwabuduBwana,

27 akisema, “AtukuzweBwana, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, ambaye hakuondoa wema na uaminifu wake kwa bwana wangu. Mimi nami,Bwanaameniongoza safarini akanifikisha nyumbani kwa jamaa za bwana wangu.”

28 Yule msichana akakimbia akawaeleza watu wa nyumbani mwa mama yake kuhusu mambo haya.

29 Rebeka alikuwa na kaka aliyeitwa Labani, huyo akaharakisha kukutana na yule mtumishi kule kisimani.

30 Mara alipoiona ile pete puani, na bangili mikononi mwa dada yake na kusikia yale maneno Rebeka aliyoambiwa na huyo mtumishi, alimwendea huyo mtumishi, akamkuta amesimama karibu na ngamia wake pale karibu na kisima.

31 Akamwambia, “Karibu nyumbani wewe uliyebarikiwa naBwana, kwa nini unasimama huko nje? Mimi nimekuandalia nyumba na mahali kwa ajili ya ngamia.”

32 Hivyo yule mtumishi akaenda nyumbani, mizigo ikaondolewa juu ya ngamia. Majani na malisho yakaletwa kwa ajili ya ngamia na maji kwa ajili yake na watu wake ili kunawa miguu.

33 Ndipo chakula kikaandaliwa kwa ajili yake, lakini akasema, “Sitakula mpaka niwe nimewaambia yale niliyo nayo ya kusema.”

Labani akasema, “Basi tuambie.”

34 Hivyo akasema, “Mimi ni mtumishi wa Abrahamu.

35 Bwanaamembariki sana bwana wangu, amekuwa tajiri. Amempa kondoo na ngʼombe, fedha na dhahabu, watumishi wa kiume na wa kike, ngamia na punda.

36 Sara mkewe bwana wangu amemzalia mwana katika uzee wake, naye amempa kila kitu alichokuwa nacho.

37 Naye bwana wangu ameniapisha na akasema, ‘Kamwe usimtwalie mwanangu mke katika binti za Wakanaani, ambao ninaishi katika nchi yao,

38 ila uende mpaka kwa jamaa ya baba yangu na ukoo wangu mwenyewe, ukamtwalie mwanangu mke huko.’

39 “Kisha nikamuuliza bwana wangu, ‘Je, kama huyo mwanamke hatakubali kurudi nami?’

40 “Akanijibu, ‘Bwanaambaye nimetembea mbele zake, atatuma malaika wake pamoja nawe, na kuifanikisha safari yako, ili uweze kupata mke kwa ajili ya mwanangu katika ukoo wangu na kutoka jamaa ya baba yangu.

41 Kisha, utakapokwenda kwenye ukoo wangu, utakuwa umefunguliwa kutoka kiapo changu hata kama wakikataa kukupa huyo binti, utakuwa umefunguliwa kutoka kiapo changu.’

42 “Nilipokuja kisimani leo nilisema, ‘EeBwana, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, ikikupendeza, naomba uifanikishe safari niliyoijia.

43 Tazama, ninasimama kando ya kisima hiki, kama mwanamwali akija kuteka maji nami nikimwambia, tafadhali niruhusu ninywe maji kidogo kutoka kwenye mtungi wako,

44 naye kama akiniambia, “Kunywa, nami nitateka maji kwa ajili ya ngamia wako pia,” basi huyo awe ndiye mke ambayeBwanaamemchagulia mwana wa bwana wangu.’

45 “Kabla sijamaliza kuomba moyoni mwangu, Rebeka akatokea, amebeba mtungi begani mwake. Akashuka kisimani akateka maji, nami nikamwambia, ‘Tafadhali nipe maji ninywe.’

46 “Akafanya haraka kushusha mtungi wake begani na kusema, ‘Kunywa na nitawanywesha ngamia wako pia,’ basi nikanywa, akawanywesha na ngamia pia.

47 “Nikamuuliza, ‘Wewe ni binti wa nani?’

“Akasema, ‘Mimi ni binti wa Bethueli, mwana wa Nahori, Milka aliyemzalia.’

“Ndipo nilipotia pete puani mwake na bangili mikononi mwake,

48 nikasujudu na nikamwabuduBwana. NikamtukuzaBwana, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, aliyeniongoza katika njia sahihi ili nimtwalie mwana na bwana wangu mke katika jamaa zake.

49 Ikiwa mtaonyesha wema na uaminifu kwa bwana wangu, mniambie, la sivyo, mniambie, ili niweze kujua njia ya kugeukia.”

50 Labani na Bethueli wakajibu, “Jambo hili limetoka kwaBwana, hatuwezi kukuambia jambo lolote baya au jema.

51 Rebeka yuko hapa, mchukue na uende, awe mke wa mwana wa bwana wako, sawasawa naBwanaalivyoongoza.”

52 Ikawa huyo mtumishi wa Abrahamu aliposikia waliyosema, alisujudu mpaka nchi mbele zaBwana.

53 Ndipo huyo mtumishi akatoa vitu vilivyotengenezwa kwa dhahabu na kwa fedha pamoja na mavazi, akampa Rebeka, pia akawapa zawadi za thamani kubwa nduguye na mamaye.

54 Kisha yeye na wale watu waliokuwa pamoja naye wakala, wakanywa na kulala palepale.

Walipoamka asubuhi, yule mtumishi, akasema, “Nipeni ruhusa nirudi kwa bwana wangu.”

55 Lakini ndugu yake Rebeka pamoja na mama yake wakajibu, “Acha binti akae kwetu siku kumi au zaidi, ndipo mwondoke.”

56 Lakini yule mtumishi akawaambia, “Msinicheleweshe, kwa kuwaBwanaamefanikisha safari yangu, nipeni ruhusa nirudi kwa bwana wangu.”

57 Ndipo wakasema, “Acha tumwite huyo binti tumuulize, tusikie atakavyosema.”

58 Kwa hiyo wakamwita Rebeka na kumuuliza, “Je, utakwenda na mtu huyu?”

Akasema, “Nitakwenda.”

59 Hivyo wakamwaga ndugu yao Rebeka aondoke, pamoja na mjakazi wake, mtumishi wa Abrahamu na watu wake.

60 Wakambariki Rebeka, wakamwambia,

“Ndugu yetu, uwe wewe kumi elfu,

mara elfu nyingi,

nao wazao wako wamiliki

malango ya adui zao.”

61 Rebeka na vijakazi wake wakajiandaa, wakapanda ngamia zao wakafuatana na yule mtu. Hivyo yule mtumishi akamchukua Rebeka akaondoka.

62 Basi Isaki alikuwa ametoka Beer-Lahai-Roi, kwa kuwa alikuwa anaishi nchi ya Negebu.

63 Isaki akatoka kwenda shambani kutafakari wakati wa jioni, alipoinua macho yake, akaona ngamia wanakuja.

64 Rebeka pia akainua macho akamwona Isaki. Akashuka kutoka kwenye ngamia wake

65 na akamuuliza yule mtumishi, “Ni nani mtu yule aliye kule shambani anayekuja kutulaki?”

Yule mtumishi akajibu, “Huyu ndiye bwana wangu.” Hivyo Rebeka akachukua shela yake akajifunika.

66 Kisha yule mtumishi akamweleza Isaki mambo yote aliyoyatenda.

67 Ndipo Isaki akamwingiza Rebeka katika hema la Sara mama yake, Isaki akamchukua Rebeka, hivyo akawa mke wake. Isaki akampenda, akafarijika baada ya kifo cha mama yake.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/GEN/24-74c526e8f7d99d61c83521a078b9a7ac.mp3?version_id=1627—

Categories
Mwanzo

Mwanzo 25

Kifo Cha Abrahamu

1 Abrahamu alioa mke mwingine, ambaye jina lake aliitwa Ketura.

2 Huyu alimzalia Zimrani, Yokshani, Medani, Midiani, Ishbaki na Shua.

3 Yokshani alikuwa baba wa Sheba na Dedani, wazao wa Dedani walikuwa Waashuri, Waletushi na Waleumi.

4 Wana wa Midiani walikuwa Efa, Eferi, Hanoki, Abida na Eldaa. Hawa wote walikuwa uzao wa Ketura.

5 Abrahamu akamwachia Isaki kila kitu alichokuwa nacho.

6 Lakini Abrahamu alipokuwa bado hai, akawapa watoto wa masuria wake zawadi, kisha akawaondoa waende kuishi pande za mashariki mbali na mwanawe Isaki.

7 Kwa jumla, Abrahamu aliishi miaka 175.

8 Ndipo Abrahamu akapumua pumzi ya mwisho na akafa akiwa mwenye umri mzuri, mzee aliyeshiba siku, naye akakusanywa pamoja na watu wake.

9 Watoto wake Isaki na Ishmaeli wakamzika katika pango la Makpela karibu na Mamre, katika shamba lililokuwa la Efroni mwana wa Sohari Mhiti,

10 Shamba ambalo Abrahamu alilinunua kwa Wahiti. Hapo ndipo Abrahamu alipozikwa pamoja na mkewe Sara.

11 Baada ya kifo cha Abrahamu, Mungu akambariki mwanawe Isaki, ambaye baadaye aliishi karibu na Beer-Lahai-Roi.

Wana Wa Ishmaeli

12 Hivi ndivyo vizazi vya Ishmaeli mtoto wa Abrahamu, ambaye mjakazi wake Sara, Hagari Mmisri, alimzalia Abrahamu.

13 Haya ndiyo majina ya wana wa Ishmaeli, yaliyoorodheshwa kulingana na jinsi walivyozaliwa: Mzaliwa wa kwanza wa Ishmaeli ni Nebayothi, akafuatia Kedari, Adbeeli, Mibsamu,

14 Mishma, Duma, Masa,

15 Hadadi, Tema, Yeturi, Nafishi na Kedema.

16 Hawa walikuwa wana wa Ishmaeli na haya ni majina ya viongozi wa makabila kumi na mawili kulingana na makao yao na kambi zao.

17 Kwa jumla Ishmaeli aliishi miaka 137. Akapumua pumzi ya mwisho, akafa, naye akakusanywa pamoja na watu wake.

18 Wazao wa Ishmaeli waliishi kuanzia nchi ya Havila hadi Shuri, karibu na mpaka wa Misri, unapoelekea Ashuru. Hao waliishi kwa uhasama na ndugu zao wote.

Yakobo Na Esau

19 Hivi ndivyo vizazi vya Isaki mwana wa Abrahamu.

Abrahamu akamzaa Isaki,

20 Isaki alikuwa na umri wa miaka arobaini alipomwoa Rebeka binti Bethueli Mwaramu kutoka Padan-Aramu, nduguye Labani Mwaramu.

21 Isaki akamwombaBwanakwa ajili ya mke wake, kwa sababu alikuwa tasa.Bwanaakajibu maombi yake na Rebeka mkewe akapata mimba.

22 Watoto wakashindana tumboni mwake, akasema, “Kwa nini haya yanatokea kwangu?” Kwa hiyo akaenda kumuulizaBwana.

23 Bwanaakamjibu,

“Mataifa mawili yamo tumboni mwako,

na mataifa hayo mawili

kutoka ndani yako watatenganishwa.

Mmoja atakuwa na nguvu zaidi kuliko mwingine,

na yule mkubwa atamtumikia yule mdogo.”

24 Wakati wake wa kujifungua ulipotimia, walikuwepo mapacha wa kiume tumboni mwake.

25 Wa kwanza kuzaliwa alikuwa mwekundu, mwili wake wote ulikuwa kama mtu aliyevaa vazi lenye nywele; wakamwita jina lake Esau.

26 Baadaye, ndugu yake akatoka, mkono wake ukiwa umemshika Esau kisigino; akaitwa jina lake Yakobo.Isaki alikuwa mwenye miaka sitini Rebeka alipowazaa.

27 Watoto wakakua, naye Esau akakuwa mwindaji hodari, mtu wa mbugani, wakati Yakobo alikuwa mtu mtulivu, mwenye kukaa nyumbani.

28 Isaki, ambaye alikuwa anapendelea zaidi nyama za porini, alimpenda Esau, bali Rebeka alimpenda Yakobo.

29 Siku moja Yakobo alipika mchuzi wa dengu, Esau akarudi kutoka porini akiwa na njaa kali.

30 Esau akamwambia Yakobo, “Haraka, nipe huo mchuzi mwekundu! Nina njaa kali sana!” (Hii ndiyo sababu pia aliitwa Edomu.)

31 Yakobo akamjibu, “Niuzie kwanza haki yako ya mzaliwa wa kwanza.”

32 Esau akasema, “Tazama, mimi niko karibu ya kufa, itanifaa nini haki ya mzaliwa wa kwanza?”

33 Yakobo akamwambia, “Niapie kwanza.” Hivyo Esau akamwapia, akamuuzia Yakobo haki yake ya kuzaliwa.

34 Ndipo Yakobo akampa Esau mkate na ule mchuzi wa dengu. Akala na kunywa, kisha akainuka akaenda zake.

Kwa hiyo Esau alidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/GEN/25-f1f72cece546ea2e9991c4d15a030565.mp3?version_id=1627—

Categories
Mwanzo

Mwanzo 26

Isaki Na Abimeleki

1 Basi njaa kubwa ikawa katika nchi hiyo, kuliko ile njaa iliyotangulia iliyotokea wakati wa Abrahamu. Isaki akamwendea Abimeleki mfalme wa Wafilisti huko Gerari.

2 Bwanaakamtokea Isaki, akamwambia, “Usiende Misri, bali ukae katika nchi nitakayokuambia.

3 Kaa katika nchi hii kwa kitambo, mimi nitakuwa pamoja na wewe na nitakubariki. Kwa maana nitakupa wewe na uzao wako nchi hizi zote na nitatimiza kiapo nilichomwapia Abrahamu baba yako.

4 Nitafanya wazao wako kuwa wengi kama nyota za angani, nami nitawapa nchi hizi zote na kutokana na uzao wako mataifa yote yatabarikiwa,

5 kwa sababu Abrahamu alinitii mimi akatunza kanuni zangu na maagizo yangu, amri zangu pamoja na sheria zangu.”

6 Hivyo Isaki akaishi huko Gerari.

7 Watu wa mahali pale walipomuuliza habari za mke wake, akasema, “Huyu ni dada yangu,” kwa sababu aliogopa kusema, “Huyu ni mke wangu.” Alifikiri, “Watu wa mahali pale wataweza kumuua kwa sababu ya Rebeka, kwa kuwa alikuwa mzuri wa sura.”

8 Wakati Isaki alipokuwa amekaa huko siku nyingi, Abimeleki mfalme wa Wafilisti akachungulia dirishani, akaona jinsi Isaki alivyomkumbatia Rebeka mke wake.

9 Abimeleki akamwita Isaki akamwambia, “Hakika huyu ni mke wako! Mbona uliniambia, ‘Huyu ni dada yangu?’ ”

Isaki akamjibu, “Kwa sababu nilifikiri ningeweza kuuawa kwa sababu yake.”

10 Ndipo Abimeleki akamjibu, “Ni nini hiki ulichotufanyia? Ingewezekana mtu yeyote akawa amekutana kimwili na mke wako, nawe ungeleta hatia juu yetu.”

11 Hivyo Abimeleki akatoa amri kwa watu wote, akisema, “Yeyote atakayemnyanyasa mtu huyu au mkewe hakika atauawa.”

12 Isaki akapanda mazao katika nchi hiyo, kwa mwaka huo huo, akavuna mara mia, kwa sababuBwanaalimbariki.

13 Isaki akawa tajiri, mali zake zikaendelea kuongezeka mpaka akawa tajiri sana.

14 Akawa na mifugo ya kondoo na ngʼombe, na watumishi wengi sana, kiasi kwamba Wafilisti wakamwonea wivu.

15 Kwa hiyo visima vyote vilivyochimbwa na watumishi wakati wa Abrahamu baba yake, Wafilisti wakavifukia, wakavijaza udongo.

16 Ndipo Abimeleki akamwambia Isaki, “Ondoka kwetu, kwa maana umetuzidi nguvu sana.”

17 Basi Isaki akatoka huko akajenga kambi katika Bonde la Gerari, akaishi huko.

18 Ndipo Isaki akavichimbua tena vile visima vya maji ambavyo vilichimbwa siku zile za Abrahamu baba yake, ambavyo Wafilisti walivifukia baada ya kufa Abrahamu, akavipa majina yale yale ambayo baba yake alikuwa amevipa.

19 Watumishi wa Isaki wakachimba katika lile bonde wakagundua huko kisima chenye maji safi.

20 Lakini wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaki wakisema, “Maji haya ni yetu!” Ndipo akakiita kile kisima Eseki,kwa sababu waligombana naye.

21 Kisha wakachimba kisima kingine, lakini hata hicho pia wakakigombania, akakiita Sitna.

22 Akaondoka huko, akachimba kisima kingine, wala hakuna yeyote aliyekigombania. Akakiita Rehobothi,akisema, “SasaBwanaametufanyia nafasi, nasi tutastawi katika nchi.”

23 Kutoka pale akaenda Beer-Sheba.

24 Usiku uleBwanaakamtokea, akamwambia, “Mimi ndimi Mungu wa Abrahamu baba yako. Usiogope, kwa maana mimi niko pamoja nawe, nitakubariki na kuongeza idadi ya wazao wako kwa ajili ya Abrahamu mtumishi wangu.”

25 Isaki akajenga madhabahu huko, akaliitia jina laBwana. Akapiga hema lake huko, nao watumishi wake wakachimba kisima.

26 Wakati huo, Abimeleki alikuwa amemjia kutoka Gerari, akifuatana na Ahuzathi mshauri wake, pamoja na Fikoli jemadari wa majeshi yake.

27 Isaki akawauliza, “Mbona mmekuja kwangu na ninyi mlinichukia na kunifukuza?”

28 Wakamjibu, “Tuliona wazi kuwaBwanaalikuwa pamoja nawe, kwa hiyo tukasema, ‘Inabidi kuwe na kiapo cha mapatano kati yetu, kati yetu na wewe. Na tufanye mkataba pamoja nawe

29 kwamba hutatudhuru, kama jinsi nasi hatukuwanyanyasa bali tuliwatendea mema wakati wote na kuwaondoa kwetu kwa amani. Tena sasa umebarikiwa naBwana.’ ”

30 Basi Isaki akawaandalia karamu, nao wakala na kunywa.

31 Kesho yake asubuhi na mapema, wakaapizana wao kwa wao. Kisha Isaki akawaruhusu waende zao, wakamwacha Isaki kwa amani.

32 Siku hiyo watumishi wa Isaki wakaja wakampa habari kuhusu kisima walichokuwa wamekichimba, wakamwambia, “Tumepata maji!”

33 Naye akakiita Shiba,mpaka leo mji huo unaitwa Beer-Sheba.

34 Esau alipokuwa na umri wa miaka arobaini, akamwoa Yudithi binti Beeri Mhiti, kisha akamwoa Basemathi binti Eloni Mhiti.

35 Hawa walikuwa chanzo cha huzuni ya Isaki na Rebeka.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/GEN/26-594434aee43f6597886a8ffca93a4760.mp3?version_id=1627—

Categories
Mwanzo

Mwanzo 27

Yakobo Anaipata Baraka Ya Isaki

1 Isaki alipokuwa mzee na macho yake yalipokuwa yamekosa nguvu asiweze kuona tena, akamwita Esau mwanawe mkubwa, akamwambia, “Mwanangu.”

Akajibu, “Mimi hapa.”

2 Isaki akasema, “Mimi sasa ni mzee na sijui siku ya kifo changu.

3 Sasa basi, chukua silaha zako, podo na upinde, uende nyikani, ukawinde nyama pori kwa ajili yangu.

4 Uniandalie aina ya chakula kitamu nikipendacho uniletee nile, ili niweze kukubariki kabla sijafa.”

5 Basi Rebeka alikuwa akisikiliza Isaki alipokuwa akizungumza na mwanawe Esau. Esau alipoondoka kwenda nyikani kuwinda nyama pori na kuleta,

6 Rebeka akamwambia Yakobo mwanawe, “Tazama, nimemsikia baba yako akimwambia ndugu yako Esau,

7 ‘Niletee mawindo, kisha ukaniandalie chakula kitamu nile, ili niweze kukubariki mbele zaBwanakabla sijafa.’

8 Sasa, mwanangu, nisikilize kwa makini na ufanye yale ninayokuambia:

9 Nenda sasa katika kundi ukaniletee wana-mbuzi wawili wazuri, ili niandalie chakula kitamu kwa ajili ya baba yako, kama vile anavyopenda.

10 Kisha umpelekee baba yako ale, ili apate kukubariki kabla hajafa.”

11 Yakobo akamwambia Rebeka mama yake, “Lakini ndugu yangu Esau ana nywele mwilini, mimi nina ngozi nyororo.

12 Itakuwaje kama baba yangu akinigusa? Itaonekana kwake kama niliyemfanyia ujanja na kuleta laana juu yangu badala ya baraka.”

13 Mama yake akamwambia, “Mwanangu, laana na iwe juu yangu. Fanya tu ninalokuambia, nenda ukaniletee hao wana-mbuzi.”

14 Kwa hiyo alikwenda akawaleta, akampa mama yake, akaandaa chakula kitamu, kama vile alivyopenda baba yake.

15 Kisha Rebeka akachukua nguo nzuri za Esau mwanawe wa kwanza, alizokuwa nazo nyumbani, akamvika Yakobo mwanawe mdogo.

16 Pia akamfunika mikononi na sehemu laini ya shingo kwa ngozi za mbuzi.

17 Hatimaye akampa Yakobo hicho chakula kitamu pamoja na mkate aliouoka.

18 Akamwendea baba yake akasema, “Baba yangu.”

Akajibu, “Naam, mwanangu, wewe ni nani?”

19 Yakobo akamwambia baba yake, “Mimi ni Esau mzaliwa wako wa kwanza. Nimefanya kama ulivyoniambia. Tafadhali uketi, ule sehemu ya mawindo yangu ili uweze kunibariki.”

20 Isaki akamuuliza mwanawe. “Umepataje haraka namna hii, mwanangu?”

Akajibu, “BwanaMungu wako amenifanikisha.”

21 Kisha Isaki akamwambia Yakobo, “Mwanangu tafadhali sogea karibu nami ili nikupapase, nione kama hakika ndiwe Esau mwanangu, au la.”

22 Yakobo akasogea karibu na baba yake Isaki, ambaye alimpapasa na kusema, “Sauti ni ya Yakobo, bali mikono ni ya Esau.”

23 Hakumtambua, kwa sababu mikono yake ilikuwa na nywele kama ya ndugu yake Esau, kwa hiyo akambariki.

24 Akamuuliza, “Hivi kweli wewe ni mwanangu Esau?”

Akajibu, “Mimi ndiye.”

25 Kisha akasema, “Mwanangu, niletee sehemu ya mawindo yako nile, ili nipate kukubariki.”

Yakobo akamletea naye akala, akamletea na divai akanywa.

26 Kisha Isaki baba yake akamwambia, “Njoo hapa, mwanangu, unibusu.”

27 Kwa hiyo akamwendea akambusu. Isaki aliposikia harufu ya nguo zake, akambariki, akasema,

“Aha, harufu ya mwanangu

ni kama harufu ya shamba

ambaloBwanaamelibariki.

28 Mungu na akupe umande kutoka mbinguni

na utajiri wa duniani:

wingi wa nafaka na divai mpya.

29 Mataifa na yakutumikie

na mataifa yakusujudie.

Uwe bwana juu ya ndugu zako,

na wana wa mama yako wakusujudie.

Walaaniwe wale wakulaanio,

nao wale wakubarikio wabarikiwe.”

30 Baada ya Isaki kumaliza kumbariki na baada tu ya Yakobo kuondoka kwa baba yake, ndugu yake Esau akaingia kutoka mawindoni.

31 Naye pia akaandaa chakula kitamu akamletea baba yake. Kisha akamwambia, “Baba yangu, keti ule sehemu ya mawindo yangu, ili upate kunibariki.”

32 Isaki baba yake akamuuliza, “Wewe ni nani?”

Akajibu, “Mimi ni mwanao, mzaliwa wako wa kwanza, Esau.”

33 Isaki akatetemeka kwa nguvu sana, akasema, “Alikuwa nani basi, ambaye aliwinda mawindo akaniletea? Nilikula kabla tu hujaja na nikambariki, naye hakika atabarikiwa!”

34 Esau aliposikia maneno haya ya baba yake, akalia sauti kubwa na ya uchungu, na kumwambia baba yake, “Nibariki mimi, mimi pia, baba yangu!”

35 Lakini akasema, “Ndugu yako amekuja kwa udanganyifu na akachukua baraka yako.”

36 Esau akasema, “Si ndiyo sababu anaitwa Yakobo? Amenidanganya mara hizi mbili: Alichukua haki yangu ya kuzaliwa na sasa amechukua baraka yangu!” Kisha akauliza, “Hukubakiza hata baraka moja kwa ajili yangu?”

37 Isaki akamjibu Esau, “Nimemfanya yeye kuwa bwana juu yako, pia nimewafanya ndugu zako wote kuwa watumishi wake, nimemtegemeza kwa nafaka na divai mpya. Sasa nitaweza kukufanyia nini, mwanangu?”

38 Esau akamwambia baba yake, “Je, baba yangu una baraka moja tu? Unibariki mimi pia, baba yangu!” Kisha Esau akalia kwa sauti kubwa.

39 Baba yake Isaki akamjibu, akamwambia,

“Makao yako yatakuwa

mbali na utajiri wa dunia,

mbali na umande wa mbinguni juu.

40 Utaishi kwa upanga,

nawe utamtumikia ndugu yako,

lakini wakati utakapokuwa umejikomboa,

utatupa nira yake

kutoka shingoni mwako.”

Yakobo Anakimbilia Kwa Labani

41 Esau akawa na kinyongo dhidi ya Yakobo kwa ajili ya baraka ambazo baba yake alikuwa amembariki. Akasema moyoni mwake, “Siku za kuomboleza kwa ajili ya baba yangu zimekaribia, ndipo nitamuua ndugu yangu Yakobo.”

42 Rebeka alipokwisha kuambiwa yale aliyoyasema Esau mwanawe mkubwa, alimwita Yakobo mwanawe mdogo, akamwambia, “Ndugu yako Esau anajifariji kwa wazo la kukuua.

43 Sasa basi, mwanangu, fanya nisemalo: Kimbilia haraka kwa Labani ndugu yangu kule Harani.

44 Ukae naye kwa muda mpaka ghadhabu ya ndugu yako itulie.

45 Wakati ndugu yako atakapokuwa hana hasira nawe tena na amesahau uliyomtendea, nitakupelekea ujumbe urudi. Kwa nini niwapoteze wote wawili kwa siku moja?”

46 Kisha Rebeka akamwambia Isaki, “Nimechukia kuishi kwa sababu ya hawa wanawake wa Kihiti. Ikiwa Yakobo ataoa mke miongoni mwa wanawake wa nchi hii, wanawake wa Kihiti kama hawa, sitakuwa na faida kuendelea kuishi.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/GEN/27-177403a3692550942c4595eb42391977.mp3?version_id=1627—

Categories
Mwanzo

Mwanzo 28

1 Basi Isaki akamwita Yakobo, akambariki na akamwamuru, akisema, “Usioe mwanamke wa Kikanaani.

2 Nenda mara moja mpaka Padan-Aramu, kwenye nyumba ya Bethueli baba wa mama yako. Uchukue mke kati ya binti za Labani ambaye ni ndugu wa mama yako.

3 Mungu Mwenyezina akubariki uwe na uzao uongezeke idadi yako upate kuwa jamii kubwa ya watu.

4 Na akupe wewe na uzao wako baraka aliyopewa Abrahamu, upate kumiliki nchi unayoishi sasa kama mgeni, nchi ambayo Mungu alimpa Abrahamu.”

5 Kisha Isaki akamuaga Yakobo, naye akaenda Padan-Aramu, kwa Labani mwana wa Bethueli Mwaramu, ndugu wa Rebeka, aliyekuwa mama wa Yakobo na Esau.

6 Sasa Esau akajua kuwa Isaki amembariki Yakobo na kumtuma kwenda Padan-Aramu ili achukue mke huko na kwamba alipombariki alimwamuru akisema, “Usioe mke katika binti za Wakanaani,”

7 tena kwamba Yakobo amewatii baba yake na mama yake naye amekwenda Padan-Aramu.

8 Esau akatambua jinsi ambavyo baba yake Isaki anavyowachukia binti za Wakanaani.

9 Ndipo Esau akaenda kwa Ishmaeli, akamwoa Mahalati, ndugu wa Nebayothi na binti wa Ishmaeli mwana wa Abrahamu, kuongezea wale wake wengine aliokuwa nao.

Ndoto Ya Yakobo Huko Betheli

10 Yakobo akatoka Beer-Sheba kwenda Harani.

11 Alipofika mahali fulani, akalala hapo kwa sababu jua lilikuwa limetua. Akachukua jiwe moja la mahali pale, akaliweka chini ya kichwa chake akajinyoosha akalala usingizi.

12 Akaota ndoto ambayo aliona ngazi imesimamishwa juu ya ardhi, ncha yake ikiwa imefika mbinguni na malaika wa Mungu wakawa wakipanda na kushuka juu yake.

13 Juu yake alisimamaBwana, akasema, “Mimi niBwana, Mungu wa baba yako Abrahamu na Mungu wa Isaki. Nchi ambayo umelala juu yake, nitakupa wewe na uzao wako.

14 Uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi na mashariki, kaskazini na kusini. Kupitia wewe na uzao wako mataifa yote ya duniani yatabarikiwa.

15 Niko pamoja nawe nami nitakulinda kila uendako na nitakurudisha katika nchi hii. Sitakuacha mpaka nitakapofanya hayo niliyokuahidi.”

16 Yakobo alipoamka kutoka usingizini, akawaza, “HakikaBwanayuko mahali hapa, wala mimi sikujua.”

17 Kwa hiyo akaogopa, akasema, “Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka hapa ndipo nyumba ya Mungu ilipo, hili ni lango la mbinguni.”

18 Asubuhi yake na mapema, Yakobo akalichukua lile jiwe aliloliweka chini ya kichwa chake, akalisimamisha kama nguzo na kumimina mafuta juu yake.

19 Mahali pale akapaita Betheli,ingawa mji ule hapo kwanza uliitwa Luzu.

20 Kisha Yakobo akaweka nadhiri, akisema, “Kama Mungu akiwa pamoja nami na kunilinda katika safari niendayo, akinipa chakula nile na nguo nivae

21 na nirudi salama nyumbani kwa baba yangu, hapo ndipoBwanaatakuwa Mungu wangu,

22 nalo jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu na katika yote utakayonipa nitakutolea wewe sehemu ya kumi.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/GEN/28-195626fd5de30f2cdedc043f4e7e178f.mp3?version_id=1627—

Categories
Mwanzo

Mwanzo 29

Yakobo Awasili Padan-Aramu

1 Kisha Yakobo akaendelea na safari yake na akafika kwenye nchi za mataifa ya mashariki.

2 Huko akaona kisima katika shamba, pamoja na makundi matatu ya kondoo yamelala karibu na kisima hicho kwa sababu walikuwa wanakunywa maji kutoka kwenye kisimani hicho. Jiwe lililokuwa mdomoni mwa kisima lilikuwa kubwa.

3 Wakati kondoo wanapokuwa wamekusanyika hapo, wachungaji huvingirisha jiwe hilo kutoka kwenye mdomo wa kisima na kunywesha kondoo. Kisha hulirudisha jiwe mahali pake juu ya mdomo wa kisima.

4 Yakobo aliwauliza wachungaji, “Ndugu zangu, ninyi mmetoka wapi?”

Wakamjibu, “Tumetoka Harani.”

5 Aliwaambia, “Je, mnamjua Labani, mjukuu wa Nahori?”

Wakamjibu, “Ndiyo, tunamfahamu.”

6 Kisha Yakobo akawauliza, “Je, yeye ni mzima?”

Wakasema, “Ndiyo, ni mzima, na hapa yuaja Raheli binti yake akiwa na kondoo.”

7 Akasema, “Tazama, jua bado liko juu, si wakati wa kukusanya mifugo. Nywesheni kondoo na mwarudishe malishoni.”

8 Walijibu, “Haiwezekani, mpaka kondoo wote wakusanyike na jiwe liwe limevingirishwa kutoka mdomo wa kisima. Ndipo tutanywesha kondoo.”

9 Alipokuwa akizungumza nao, Raheli akaja pamoja na kondoo wa baba yake, kwa maana alikuwa mchunga kondoo.

10 Yakobo alipomwona Raheli binti Labani, ndugu wa mama yake, pamoja na kondoo wa Labani, alikwenda na kulivingirisha jiwe kutoka mdomoni mwa kisima na kuwanywesha kondoo wa mjomba wake.

11 Kisha Yakobo akambusu Raheli na akaanza kulia kwa sauti.

12 Yakobo alikuwa amemwambia Raheli kuwa yeye alikuwa jamaa ya baba yake, na kwamba ni mwana wa Rebeka. Basi Raheli alikimbia na kumweleza baba yake.

13 Mara Labani aliposikia habari kuhusu Yakobo, mwana wa ndugu yake, aliharakisha kwenda kumlaki. Akamkumbatia na kumbusu, halafu akamleta nyumbani kwake, kisha Yakobo akamwambia mambo yote.

14 Ndipo Labani akamwambia, “Wewe ni nyama yangu na damu yangu mwenyewe.”

Yakobo Awaoa Lea Na Raheli

Baada ya Yakobo kukaa kwa Labani mwezi mzima,

15 Labani akamwambia, “Kwa vile wewe ni jamaa yangu, ndiyo sababu unifanyie kazi bila ujira? Niambie ujira wako utakuwa nini.”

16 Labani alikuwa na binti wawili, binti mkubwa aliitwa Lea na binti mdogo aliitwa Raheli.

17 Lea alikuwa na macho dhaifu, lakini Raheli alikuwa na umbo la kupendeza na mzuri wa sura.

18 Yakobo akampenda Raheli, akamwambia Labani, “Nitakutumikia kwa miaka saba kwa ajili ya kumpata Raheli binti yako mdogo.”

19 Labani akasema, “Ni bora zaidi nikupe Raheli kuliko kumpa mtu mwingine yeyote. Kaa pamoja na mimi hapa.”

20 Kwa hiyo Yakobo akatumika miaka saba ili kumpata Raheli, lakini ilionekana kwake kama siku chache tu kwa sababu ya upendo wake kwa Raheli.

21 Ndipo Yakobo akamwambia Labani, “Nipe mke wangu. Muda wangu umekamilika, nami nataka nikutane naye kimwili.”

22 Basi Labani akaalika watu wote wa mahali pale na akafanya karamu.

23 Lakini ilipofika jioni, akamchukua Lea binti yake akampa Yakobo, naye Yakobo akakutana naye kimwili.

24 Naye Labani akamtoa Zilpa, mtumishi wake wa kike, kuwa mtumishi wa Lea, binti yake.

25 Kesho yake asubuhi, Yakobo akagundua kuwa amepewa Lea! Basi Yakobo akamwambia Labani, “Ni jambo gani hili ulilonitendea? Nilikutumikia kwa ajili ya Raheli, sivyo? Kwa nini umenidanganya?”

26 Labani akajibu, “Si desturi yetu kumwoza binti mdogo kabla ya kumwoza binti mkubwa.

27 Maliza juma la arusi ya binti huyu, kisha pia nitakupa huyu binti mdogo, kwa kutumika miaka mingine saba.”

28 Naye Yakobo akafanya hivyo. Akamaliza juma na Lea, kisha Labani akampa Raheli binti yake kuwa mke wake.

29 Labani akamtoa Bilha mtumishi wake wa kike kwa Raheli ili kuwa mtumishi wake.

30 Pia Yakobo akakutana na Raheli kimwili, naye akampenda Raheli zaidi kuliko Lea. Yakobo akamtumikia Labani kwa miaka mingine saba.

Wana Wa Yakobo

31 Bwanaalipoona kwamba Lea hapendwi, akampa watoto, lakini Raheli alikuwa tasa.

32 Lea akapata mimba akazaa mwana. Akamwita Reubeni,kwa maana alisema, “Ni kwa sababuBwanaameona huzuni yangu. Hakika mume wangu sasa atanipenda.”

33 Akapata tena mimba, naye alipozaa mwana, akasema, “Kwa sababuBwanaalisikia kwamba sipendwi, amenipa tena huyu mwana.” Kwa hiyo akamwita Simeoni.

34 Akapata tena mimba, naye alipozaa mwana, akasema, “Sasa afadhali mume wangu ataambatana na mimi, kwa sababu nimemzalia wana watatu.” Kwa hiyo akamwita Lawi.

35 Akapata tena mimba, naye alipozaa mwana, akasema, “Wakati huu nitamsifuBwana.” Kwa hiyo akamwita Yuda.Kisha akaacha kuzaa watoto.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/GEN/29-a118ef4ca1b24e58f29da74250466b09.mp3?version_id=1627—