Categories
Ufunuo

Ufunuo 8

Lakiri Ya Saba Na Chetezo Cha Dhahabu

1 Mwana-Kondoo alipoivunja ile lakiri ya saba, pakawa kimya mbinguni kwa muda wa nusu saa.

2 Nami nikawaona wale malaika saba wanaosimama mbele za Mungu, nao wakapewa tarumbeta saba.

3 Malaika mwingine aliyekuwa na chetezo cha dhahabu, akaja na kusimama mbele ya madhabahu. Akapewa uvumba mwingi ili autoe pamoja na maombi ya watakatifu wote, juu ya yale madhabahu ya dhahabu yaliyo mbele ya kile kiti cha enzi.

4 Ule moshi wa uvumba pamoja na yale maombi ya watakatifu, vikapanda juu mbele za Mungu, kutoka mkononi mwa huyo malaika.

5 Kisha yule malaika akachukua kile chetezo, akakijaza moto kutoka kwa yale madhabahu, akautupa juu ya dunia. Pakatokea sauti za radi, ngurumo, umeme wa radi na tetemeko la ardhi.

Tarumbeta Ya Kwanza

6 Basi wale malaika saba waliokuwa na zile tarumbeta saba wakajiandaa kuzipiga.

7 Malaika wa kwanza akaipiga tarumbeta yake, pakatokea mvua ya mawe na moto uliochanganyika na damu, navyo vikatupwa kwa nguvu juu ya nchi. Na theluthi ya dunia ikateketea, theluthi ya miti ikateketea, na nyasi yote mbichi ikateketea.

Tarumbeta Ya Pili

8 Malaika wa pili akaipiga tarumbeta yake na kitu kama mlima mkubwa unaowaka moto kikatupwa baharini. Theluthi ya bahari ikawa damu,

9 theluthi ya viumbe vyenye uhai viishivyo baharini vikafa na theluthi ya meli zikaharibiwa.

Tarumbeta Ya Tatu

10 Malaika wa tatu akaipiga tarumbeta yake, na nyota kubwa iliyokuwa ikiwaka kama taa ikaanguka toka angani, ikaangukia theluthi ya mito na chemchemi za maji.

11 Nyota hiyo inaitwa Uchungu. Theluthi ya maji yakawa machungu na watu wengi wakafa kutokana na maji hayo kwa maana yalikuwa machungu.

Tarumbeta Ya Nne

12 Kisha malaika wa nne akaipiga tarumbeta yake, na theluthi ya jua, theluthi ya mwezi na theluthi ya nyota zikapigwa. Kwa hiyo theluthi moja ya mwanga ikawa giza. Theluthi ya mchana ikawa haina mwanga na pia theluthi ya usiku.

13 Nilipokuwa tena nikitazama, nikamsikia tai mmoja akipiga kelele kwa sauti kuu wakati akiruka katikati ya mbingu, akisema, “Ole! Ole! Ole wa watu waishio duniani, kwa sababu ya tarumbeta ambazo malaika hao wengine watatu wanakaribia kuzipiga!”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/REV/8-15812af24b0916e4120c5c42cd1394ab.mp3?version_id=1627—

Categories
Ufunuo

Ufunuo 9

Tarumbeta Ya Tano

1 Malaika wa tano akaipiga tarumbeta yake, nami nikaona nyota iliyokuwa imeanguka toka angani hadi ardhini. Nyota hiyo ilipewa ufunguo wa lile Shimo.

2 Alipolifungua hilo Shimo, moshi ukapanda kutoka humo kama moshi wa tanuru kubwa sana. Jua na anga vikatiwa giza na ule moshi uliotoka katika hilo Shimo.

3 Ndipo katika ule moshi wakatoka nzige wakaenda juu ya nchi, nao wakapewa nguvu kama zile za nge wa duniani.

4 Wakaambiwa wasidhuru nyasi ya nchi, wala mmea wala mti wowote, bali wawadhuru tu wale watu ambao hawana muhuri wa Mungu kwenye vipaji vya nyuso zao.

5 Wakaruhusiwa kuwatesa kwa muda wa miezi mitano, lakini wasiwaue. Uchungu wa kuuma kwao ulikuwa kama ule wa mtu aumwapo na nge.

6 Katika siku hizo watu watatafuta kifo lakini hawatakiona, watatamani kufa, lakini kifo kitawakimbia.

7 Wale nzige walikuwa na umbo kama la farasi waliotayarishwa kwa ajili ya vita. Kwenye vichwa vyao kulikuwa na kitu kama taji za dhahabu na nyuso zao zilikuwa kama za binadamu.

8 Walikuwa na nywele kama za wanawake, na meno yao yalikuwa kama ya simba.

9 Walikuwa na dirii kama za chuma, na sauti za mabawa yao zilikuwa kama ngurumo za farasi wengi na magari mengi yakikimbilia vitani.

10 Walikuwa na mikia yenye miiba ya kuumia kama nge. Nguvu yao ya kutesa watu kwa huo muda wa miezi mitano ilikuwa katika hiyo mikia yao.

11 Walikuwa na mfalme wao, ambaye ni malaika wa lile Shimo, ambaye jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kiyunani ni Apolioni.

12 Ole ya kwanza imepita, bado nyingine mbili zinakuja.

Tarumbeta Ya Sita

13 Malaika wa sita akaipiga tarumbeta yake, nami nikasikia sauti ikitoka katika zile pembe za madhabahu ya dhahabu iliyoko mbele za Mungu.

14 Ile sauti ikamwambia yule malaika wa sita mwenye tarumbeta, “Wafungulie wale malaika wanne waliofungwa kwenye ule mto mkubwa Frati.”

15 Basi wale malaika wanne, waliokuwa wamewekwa tayari kwa ajili ya saa hiyo, na siku hiyo, na mwezi huo, na mwaka huo ili wawaue theluthi ya wanadamu wakafunguliwa.

16 Idadi ya majeshi wapanda farasi ilikuwa 200,000,000. Nilisikia idadi yao.

17 Hivi ndivyo nilivyowaona hao farasi na wapanda farasi katika maono yangu: Wapanda farasi walivaa dirii vifuani zenye rangi nyekundu sana kama ya moto na yakuti samawi na kiberiti. Vichwa vya hao farasi vilikuwa kama vichwa vya simba, na moto, moshi na kiberiti vilitoka vinywani mwao.

18 Theluthi ya wanadamu wakauawa kwa mapigo hayo matatu, yaani, huo moto, moshi na kiberiti, vilivyotoka kwenye vinywa vya hao farasi.

19 Nguvu za hao farasi zilikuwa katika vinywa vyao na kwenye mikia yao, kwa sababu mikia yao ilikuwa kama nyoka, yenye vichwa ambayo waliitumia kudhuru.

20 Wanadamu waliosalia, ambao hawakuuawa katika mapigo hayo, bado walikataa kutubia kazi za mikono yao na hawakuacha kuabudu mashetani na sanamu za dhahabu, za fedha, za shaba, za mawe na za miti, ambazo haziwezi kuona, kusikia wala kutembea.

21 Wala hawakutubu na kuacha matendo yao ya uuaji, uchawi, uasherati wala wizi wao.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/REV/9-53de142a7e350b6300b149724819fa7b.mp3?version_id=1627—

Categories
Ufunuo

Ufunuo 10

Malaika Mwenye Kitabu Kidogo

1 Kisha nikamwona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni. Alikuwa amevikwa wingu na upinde wa mvua juu ya kichwa chake. Uso wake ulingʼaa kama jua na miguu yake ilikuwa kama nguzo za moto.

2 Mkononi mwake alikuwa ameshika kijitabu kilichokuwa kimefunguliwa. Akauweka mguu wake wa kuume juu ya bahari na mguu wake wa kushoto akauweka juu ya nchi kavu.

3 Naye akapiga kelele kwa sauti kuu kama simba anayenguruma. Alipopiga kelele, zile radi saba zikatoa ngurumo zake.

4 Nazo zile radi saba zilipotoa ngurumo, nilitaka kuanza kuandika, lakini nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Yatie muhuri hayo yaliyosemwa na hizo radi saba na usiyaandike.”

5 Kisha yule malaika niliyekuwa nimemwona akiwa amesimama juu ya bahari na juu ya nchi akainua mkono wake wa kuume kuelekea mbinguni.

6 Naye akaapa kwa Yule aishiye milele na milele, aliyeumba mbingu na vyote vilivyomo, dunia na vyote viijazavyo, pamoja na bahari na vyote vilivyomo ndani yake, akasema, “Hakuna kungoja tena!

7 Lakini katika siku zile ambazo huyo malaika wa saba atakapokaribia kuipiga hiyo tarumbeta yake, siri ya Mungu itatimizwa, kama vile alivyowatangazia watumishi wake manabii.”

8 Ndipo ile sauti niliyokuwa nimeisikia kutoka mbinguni ikasema nami tena ikaniambia, “Nenda, chukua kile kitabu kilichofunguliwa kilichoko mkononi mwa yule malaika aliyesimama juu ya bahari na juu ya nchi kavu.”

9 Basi nikamwendea nikamwomba yule malaika anipe kile kitabu kidogo. Akaniambia, “Chukua na ukile. Kitakuwa kichungu tumboni mwako, lakini kinywani mwako kitakuwa kitamu kama asali.”

10 Hivyo nikakichukua kile kitabu kidogo kutoka mkononi mwa yule malaika nikakila. Kilikuwa kitamu kama asali kinywani mwangu, lakini baada ya kukila, tumbo langu likatiwa uchungu.

11 Kisha nikaambiwa, “Imekupasa kutoa unabii tena kuhusu makabila mengi, mataifa, lugha na wafalme.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/REV/10-78b78836d7a2b6fcffe1a2c3f63deed8.mp3?version_id=1627—

Categories
Ufunuo

Ufunuo 11

Mashahidi Wawili

1 Ndipo nikapewa mwanzi uliokuwa kama ufito wa kupimia, nikaambiwa, “Nenda ukapime hekalu la Mungu pamoja na madhabahu, nawe uwahesabu wale waabuduo humo.

2 Lakini usiupime ua wa nje wa Hekalu, uache, kwa sababu ua huo wamepewa watu wa Mataifa. Hao wataukanyagakanyaga mji mtakatifu kwa muda wa miezi arobaini na miwili.

3 Nami nitawapa mashahidi wangu wawili uwezo, nao watoe unabii kwa muda wa siku 1,260, wakiwa wamevaa nguo za gunia.”

4 Hawa ndio ile mizeituni miwili na vile vinara viwili vya taa visimamavyo mbele za Bwana Mungu wa dunia yote.

5 Kama mtu yeyote akitaka kuwadhuru, moto hutoka vinywani mwao na kuwateketeza adui zao. Hivi ndivyo impasavyo kufa mtu yeyote atakayetaka kuwadhuru.

6 Watu hawa wanao uwezo wa kufunga anga ili mvua isinyeshe wakati wote watakapokuwa wanatoa unabii wao. Nao watakuwa na uwezo wa kuyabadili maji kuwa damu na kuipiga dunia kwa kila aina ya mapigo mara kwa mara kama watakavyo.

7 Basi watakapokuwa wamemaliza ushuhuda wao, yule mnyama atokaye katika lile Shimo atapigana nao vita, atawashinda na kuwaua.

8 Maiti zao zitabaki katika barabara ya mji mkubwa,ambao kwa fumbo unaitwa Sodoma na Misri,ambapo pia Bwana wao alisulubiwa.

9 Kwa muda wa siku tatu na nusu, watu wa kila kabila, jamaa, lugha na taifa wataziangalia hizo maiti zao na hawataruhusu wazikwe.

10 Watu waishio duniani watazitazama kwa furaha maiti za hao manabii wawili na kushangilia kwa kupeana zawadi kwa sababu hao manabii waliwatesa watu waishio duniani.

11 Lakini baada ya zile siku tatu na nusu, pumzi ya uhai kutoka kwa Mungu ikawaingia, nao wakasimama kwa miguu yao na wote waliowaona wakaingiwa na hofu kuu.

12 Kisha wale manabii wawili wakasikia sauti kuu kutoka mbinguni ikiwaambia, “Njooni huku juu!” Nao wakapaa mbinguni katika wingu, wakati adui zao wakiwa wanawatazama.

13 Saa iyo hiyo, kukatokea tetemeko kubwa la nchi na sehemu ya kumi ya mji ikaanguka. Watu elfu saba wakauawa katika tetemeko hilo, nao walionusurika wakaogopa sana, wakamtukuza Mungu wa mbinguni.

14 Ole ya pili imekwisha kupita, tazama ole ya tatu inakuja upesi.

Tarumbeta Ya Saba

15 Yule malaika wa saba akaipiga tarumbeta yake, pakawa na sauti kubwa mbinguni iliyosema:

“Ufalme wa ulimwengu umekuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo wake,

naye atatawala milele na milele.”

16 Nao wale wazee ishirini na wanne, waliokuwa wameketi mbele za Mungu, kwenye viti vyao vya enzi, wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu Mungu,

17 wakisema:

“Tunakushukuru,BwanaMungu Mwenyezi,

uliyeko na uliyekuwako,

kwa kuwa umetwaa uweza wako mkuu

na ukaanza kutawala.

18 Mataifa walikasirika nao

wakati wa ghadhabu yako umewadia.

Wakati umewadia wa kuwahukumu waliokufa

na kuwapa thawabu watumishi wako manabii

na watakatifu wako pamoja na wale wote

wanaoliheshimu Jina lako,

wakubwa kwa wadogo:

na kuwaangamiza wale wanaoiangamiza dunia.”

19 Ndipo hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa, na sanduku la agano lake likaonekana humo ndani. Kukatokea mianga ya umeme wa radi, ngurumo, sauti za radi, tetemeko la nchi na mvua kubwa ya mawe.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/REV/11-eab956d93de83483e6b6c4ee767577fd.mp3?version_id=1627—

Categories
Ufunuo

Ufunuo 12

Mwanamke Na Joka

1 Kukaonekana ishara kuu mbinguni: Palikuwa na mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi ukiwa chini ya miguu yake, na taji ya nyota kumi na mbili ilikuwa kichwani mwake.

2 Alikuwa na mimba naye akilia kwa uchungu kwa kuwa alikuwa anakaribia kuzaa.

3 Kisha ishara nyingine ikaonekana mbinguni: Likaonekana joka kubwa jekundu lenye vichwa saba na pembe kumi na taji saba katika vichwa vyake.

4 Mkia wake ukakokota theluthi ya nyota zote angani na kuziangusha katika nchi. Ndipo lile joka likasimama mbele ya yule mwanamke aliyekuwa karibu kuzaa ili lipate kumla huyo mtoto mara tu atakapozaliwa.

5 Yule mwanamke akazaa mtoto mwanaume, atakayeyatawala mataifa yote kwa fimbo yake ya utawala ya chuma. Lakini huyo mtoto akanyakuliwa na kupelekwa kwa Mungu kwenye kiti chake cha enzi.

6 Yule mwanamke akakimbilia jangwani, ambako Mungu alikuwa amemtayarishia mahali ili apate kutunzwa huko kwa muda wa siku 1,260.

Malaika Mikaeli Amshinda Yule Joka

7 Basi palikuwa na vita mbinguni: Mikaeli na malaika zake wakapigana na hilo joka, nalo joka pamoja na malaika zake likapigana nao.

8 Lakini joka na malaika zake wakashindwa, na hapakuwa tena na nafasi yao huko mbinguni.

9 Lile joka kuu likatupwa chini, yule nyoka wa zamani aitwaye ibilisi au Shetani, aupotoshaye ulimwengu wote. Akatupwa chini duniani, yeye pamoja na malaika zake.

Ushindi Mbinguni Watangazwa

10 Kisha nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema:

“Sasa wokovu na uweza na Ufalme wa Mungu wetu umekuja

na mamlaka ya Kristo wake.

Kwa kuwa ametupwa chini

mshtaki wa ndugu zetu,

anayewashtaki mbele za Mungu

usiku na mchana.

11 Nao wakamshinda

kwa damu ya Mwana-Kondoo

na kwa neno la ushuhuda wao.

Wala wao hawakuyapenda maisha yao

hata kufa.

12 Kwa hiyo, furahini ninyi mbingu

na wote wakaao humo!

Lakini ole wenu nchi na bahari,

kwa maana huyo ibilisi ameshuka kwenu,

akiwa amejaa ghadhabu,

kwa sababu anajua ya kuwa

muda wake ni mfupi!”

13 Lile joka lilipoona kuwa limetupwa chini duniani, lilimfuatilia yule mwanamke aliyekuwa amezaa mtoto mwanaume.

14 Lakini huyo mwanamke akapewa mabawa mawili ya tai mkubwa, kusudi aweze kuruka mpaka mahali palipotayarishwa kwa ajili yake huko jangwani, ambako atatunzwa kwa wakati na nyakati na nusu,ya wakati ambako yule joka hawezi kufika.

15 Ndipo lile joka likamwaga maji kama mto kutoka kinywani mwake, ili kumfikia huyo mwanamke na kumkumba kama mafuriko.

16 Lakini nchi ikamsaidia huyo mwanamke kwa kufungua kinywa na kuumeza huo mto ambao huyo joka alikuwa ameutoa kinywani mwake.

17 Kisha lile joka likapatwa na hasira kali kwa ajili ya huyo mwanamke na likaondoka ili kupigana vita na watoto waliosalia wa huyo mwanamke, yaani, wale wanaozitii amri za Mungu na kuushika ushuhuda wa Yesu Kristo. Lile joka likasimama kwenye mchanga wa bahari.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/REV/12-ac1302b27797bf067ba61a0c115d7adf.mp3?version_id=1627—

Categories
Ufunuo

Ufunuo 13

1 Yule joka akajikita katika mchanga ulioko ufuoni mwa bahari.

Mnyama Kutoka Baharini

Nami nikamwona mnyama akitoka ndani ya bahari. Mnyama huyo alikuwa na pembe kumi na vichwa saba, akiwa na taji kumi kwenye hizo pembe zake, na juu ya kila kichwa kulikuwa na jina la kukufuru.

2 Mnyama yule niliyemwona alifanana na chui, lakini miguu yake ilikuwa kama ya dubu na kichwa chake kama cha simba. Lile joka likampa huyo mnyama nguvu zake, kiti chake cha enzi na mamlaka makubwa.

3 Kimojawapo ya vichwa vya huyo mnyama kilikuwa kama kilichokwisha kupata jeraha la mauti, lakini jeraha hilo la mauti likapona. Ulimwengu wote ukashangaa ukamfuata huyo mnyama.

4 Watu wakaliabudu lile joka kwa sababu lilikuwa limempa huyo mnyama mamlaka yake, pia wakamwabudu huyo mnyama na kuuliza, “Ni nani aliye kama huyu mnyama? Ni nani awezaye kupigana vita naye?”

5 Huyo mnyama akapewa kusema maneno ya kiburi na kukufuru na kutumia mamlaka yake kwa muda wa miezi arobaini na miwili.

6 Akafungua kinywa chake ili kumkufuru Mungu, akilitukana Jina lake na mahali aishipo na wale wakaao mbinguni.

7 Pia akaruhusiwa kufanya vita na watakatifu na kuwashinda. Akapewa uwezo juu ya watu wa kila kabila, jamaa, lugha na taifa.

8 Nao watu wote waishio duniani watamwabudu huyo mnyama, yaani, wale wote ambao majina yao hayakuandikwa kwenye kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo aliyechinjwa tangu kuumbwa kwa ulimwengu.

9 Yeye aliye na sikio na asikie.

10 Ikiwa mtu ni wa kuchukuliwa mateka,

atachukuliwa mateka.

Ikiwa mtu ni wa kuuawa kwa upanga,

atauawa kwa upanga.

Hapa ndipo penye wito wa subira na imani ya watakatifu.

Mnyama Kutoka Dunia

11 Kisha nikamwona mnyama mwingine, akipanda juu kutoka dunia. Alikuwa na pembe mbili kama mwana-kondoo, lakini akanena kama joka.

12 Akatumia mamlaka yote ya yule mnyama wa kwanza kwa niaba yake, naye akawafanya wote wakaao duniani kumwabudu yule mnyama wa kwanza, ambaye jeraha lake la mauti lilipona.

13 Naye akafanya ishara kuu na za ajabu, hata kusababisha moto kushuka toka mbinguni kuja duniani watu wakiona waziwazi.

14 Kwa sababu ya zile ishara alizokuwa amepewa uwezo wa kuzifanya kwa niaba ya yule mnyama wa kwanza, akawadanganya wakaao duniani. Akawaamuru wasimamishe sanamu kwa heshima ya yule mnyama aliyekuwa amejeruhiwa kwa upanga lakini akaishi.

15 Akapewa uwezo wa kuipa pumzi ile sanamu ya yule mnyama wa kwanza, ili iweze kusema na kuwasababisha wale wote waliokataa kuiabudu hiyo sanamu kuuawa.

16 Pia alimlazimisha kila mmoja, mdogo na mkubwa, tajiri na maskini, mtu huru na mtumwa, atiwe chapa kwenye mkono wake wa kuume au kwenye kipaji chake cha uso,

17 ili kwamba mtu yeyote asiweze kununua wala kuuza isipokuwa amekuwa na hiyo chapa, ambayo ni jina la huyo mnyama au tarakimu za jina lake.

18 Hapa ndipo penye hekima. Yeye aliye na ufahamu na ahesabu tarakimu za huyo mnyama, kwa maana ni tarakimu za kibinadamu. Tarakimu zake ni 666.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/REV/13-f1139f2ea8b9e65e8d55840879066ddd.mp3?version_id=1627—

Categories
Ufunuo

Ufunuo 14

Mwana-Kondoo Na Wale 144,000

1 Kisha nikatazama na hapo mbele yangu alikuwepo Mwana-Kondoo, akiwa amesimama juu ya Mlima Sayuni. Pamoja naye walikuwa wale 144,000 wenye Jina la Mwana-Kondoo na Jina la Baba yake likiwa limeandikwa kwenye vipaji vya nyuso zao.

2 Nami nikasikia sauti kutoka mbinguni kama sauti ya maji mengi yaendayo kwa kasi na sauti kama ngurumo ya radi. Sauti hiyo niliyoisikia ilikuwa kama sauti ya wapiga vinubi wakipiga vinubi vyao.

3 Nao wakaimba wimbo mpya mbele ya hicho kiti cha enzi na mbele ya wale viumbe wanne wenye uhai na wale wazee. Hakuna mtu yeyote aliyeweza kujifunza wimbo huo isipokuwa hao 144,000 waliokuwa wamekombolewa kutoka duniani.

4 Hawa ndio wale ambao hawakujitia unajisi kwa wanawake, kwa kuwa wao ni bikira. Wao humfuata Mwana-Kondoo kila aendako. Hawa wamekombolewa kutoka miongoni mwa wanadamu wakawa malimbuko kwa Mungu na kwa Mwana-Kondoo.

5 Vinywani mwao hapakuonekana uongo, wala hawakuwa na hatia yoyote.

Malaika Watatu

6 Kisha nikamwona malaika mwingine akiruka juu angani, naye alikuwa na Injili ya milele ya kuwatangazia wale waishio duniani, yaani, kwa kila taifa, kabila, lugha na jamaa.

7 Akasema kwa sauti kubwa, “Mcheni Mungu na kumpa utukufu, kwa maana saa ya hukumu yake imewadia. Mwabuduni yeye aliyeziumba mbingu, dunia, bahari na chemchemi za maji.”

8 Malaika wa pili akafuata akisema, “Umeanguka! Umeanguka Babeli Mkuu, ule uliyafanya mataifa yote kulewa kwa mvinyo wa ghadhabu ya uasherati wake.”

9 Malaika wa tatu akawafuata hao wawili akisema kwa sauti kubwa, “Kama mtu yeyote anamwabudu huyo mnyama na sanamu yake na kutiwa chapa yake kwenye kipaji chake cha uso au kwenye mkono wake,

10 yeye pia atakunywa mvinyo wa hasira kali ya Mungu ambayo imemiminwa katika kikombe cha ghadhabu yake pasipo kuchanganywa na maji. Naye atateswa kwa moto uwakao na kiberiti mbele ya malaika watakatifu na mbele za Mwana-Kondoo.

11 Nao moshi wa mateso yao hupanda juu milele na milele. Hakuna mapumziko, mchana wala usiku, kwa wale wamwabuduo huyo mnyama na sanamu yake, au kwa yeyote anayepokea chapa ya jina lake.”

12 Hapa ndipo penye wito wa subira na uvumilivu wa watakatifu; wale wanaozishika amri za Mungu na kudumu katika uaminifu kwa Yesu.

13 Kisha nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Andika: Wamebarikiwa wafu wafao katika Bwana tangu sasa.”

“Naam,” asema Roho, “watapumzika kutoka taabu zao, kwa kuwa matendo yao yatawafuata.”

Kuvuna Mavuno Ya Dunia

14 Nikatazama, hapo mbele yangu palikuwa na wingu jeupe, na aliyekuwa ameketi juu ya hilo wingu alikuwa “kama Mwana wa Adamu” mwenye taji ya dhahabu kichwani mwake na mundu mkali mkononi mwake.

15 Kisha malaika mwingine akaja kutoka hekaluni naye akamwita kwa sauti kubwa yule aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu akasema, “Chukua mundu wako ukavune kwa kuwa wakati wa mavuno umewadia, kwa maana mavuno ya dunia yamekomaa.”

16 Hivyo yule aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu akauzungusha mundu wake duniani, nayo dunia ikavunwa.

17 Malaika mwingine akatoka katika hekalu lililoko mbinguni, naye pia alikuwa na mundu mkali.

18 Kisha malaika mwingine, aliyekuwa na mamlaka juu ya moto, akatoka kwenye madhabahu, naye akamwita yule malaika mwenye mundu mkali kwa sauti kubwa, akisema, “Chukua mundu wako mkali ukakusanye vichala vya mizabibu ya dunia, maana zabibu zake zimeiva.”

19 Hivyo yule malaika akauzungusha mundu wake duniani na kukusanya zabibu za dunia na kuzitupa kwenye shinikizo kubwa la ghadhabu ya Mungu.

20 Lile shinikizo likakanyagwa nje ya mji, nayo damu ikatiririka kama mafuriko kutoka hilo shinikizo kufikia kimo cha hatamu za farasi,kwa umbali wa maili 200.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/REV/14-3e645b069769645022c709ecdf94e8c6.mp3?version_id=1627—

Categories
Ufunuo

Ufunuo 15

Malaika Saba Na Mapigo Saba

1 Ndipo nikaona ishara nyingine kubwa ya ajabu mbinguni: malaika saba wenye yale mapigo saba ya mwisho, kwa sababu kwa mapigo hayo ghadhabu ya Mungu ilikuwa imekamilika.

2 Nikaona kile kilichoonekana kama bahari ya kioo iliyochanganyikana na moto. Kando ya hiyo bahari, walikuwa wamesimama wale watu waliomshinda yule mnyama na sanamu yake pamoja na tarakimu ya jina lake. Mikononi mwao walikuwa wameshika vinubi walivyopewa na Mungu.

3 Nao wakaimba wimbo wa Mose, mtumishi wa Mungu, na wimbo wa Mwana-Kondoo, wakisema:

“BwanaMungu Mwenyezi,

matendo yako ni makuu na ya ajabu.

Njia zako wewe ni za haki na za kweli,

Mfalme wa nyakati zote!

4 Ni nani ambaye hatakuogopa wewe Bwana

na kulitukuza jina lako?

Kwa kuwa wewe peke yako ndiwe mtakatifu.

Mataifa yote yatakuja

na kuabudu mbele zako,

kwa kuwa matendo yako ya haki

yamedhihirishwa.”

5 Baada ya haya nikatazama, nalo hekalu, la hema la Ushuhuda, lilikuwa limefunguliwa mbinguni.

6 Ndani ya lile hekalu wakatoka malaika saba wakiwa na mapigo saba. Walikuwa wamevaa nguo safi za kitani ingʼaayo na kufungwa mikanda ya dhahabu vifuani mwao.

7 Ndipo mmoja wa wale viumbe wanne wenye uhai akawapa wale malaika saba mabakuli saba ya dhahabu yaliyojaa ghadhabu ya Mungu, yeye aishiye milele na milele.

8 Nalo lile hekalu lilijawa na moshi uliotokana na utukufu wa Mungu na uweza wake, wala hakuna yeyote aliyeweza kuingia mle hekaluni mpaka yale mapigo saba ya wale malaika saba yalipomalizika.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/REV/15-3ec0b7ac9fb05e65ff21005342ee7cc5.mp3?version_id=1627—

Categories
Ufunuo

Ufunuo 16

Mabakuli Saba Ya Ghadhabu Ya Mungu

1 Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka mle Hekaluni ikiwaambia wale malaika saba, “Nendeni, mkayamwage duniani hayo mabakuli saba ya ghadhabu ya Mungu.”

2 Malaika wa kwanza akaenda akalimwaga hilo bakuli lake juu ya nchi. Majipu mabaya yenye maumivu makali yakawapata wale watu wote waliokuwa na chapa ya yule mnyama na walioabudu sanamu yake.

3 Malaika wa pili akalimwaga bakuli lake baharini, nayo ikabadilika kuwa damu kama ya mtu aliyekufa na kila kiumbe hai kilichokuwa ndani ya bahari kikafa.

4 Malaika wa tatu akalimwaga bakuli lake katika mito na chemchemi za maji, nazo zikawa damu.

5 Ndipo nikamsikia malaika msimamizi wa maji akisema:

“Wewe una haki katika hukumu hizi ulizotoa,

wewe uliyeko, uliyekuwako, Uliye Mtakatifu,

kwa sababu umehukumu hivyo;

6 kwa kuwa walimwaga damu ya watakatifu wako

na manabii wako,

nawe umewapa damu wanywe

kama walivyostahili.”

7 Nikasikia madhabahu ikiitikia,

“Naam,BwanaMungu Mwenyezi,

hukumu zako ni kweli na haki.”

8 Malaika wa nne akamimina bakuli lake kwenye jua, nalo likapewa nguvu za kuwaunguza watu kwa moto.

9 Watu wakaunguzwa na hilo joto kali, wakalaani Jina la Mungu, aliyekuwa na uwezo juu ya mapigo haya, tena wakakataa kutubu na kumtukuza Mungu.

10 Malaika wa tano akamimina bakuli lake kwenye kiti cha enzi cha yule mnyama, nao ufalme wake ukagubikwa na giza. Watu wakatafuna ndimi zao kwa ajili ya maumivu,

11 wakamlaani Mungu wa mbinguni kwa sababu ya maumivu na majeraha yao, wala hawakutubu kwa ajili ya matendo yao maovu.

12 Malaika wa sita akamimina bakuli lake kwenye mto mkubwa Frati, maji yake yakakauka ili kutayarisha njia kwa ajili ya wafalme watokao Mashariki.

13 Kisha nikaona roho wachafu watatu waliofanana na vyura wakitoka katika kinywa cha lile joka na katika kinywa cha yule mnyama na katika kinywa cha yule nabii wa uongo.

14 Hizo ndizo roho za pepo wachafu zitendazo miujiza. Nazo huwaendea wafalme wa ulimwengu wote na kuwakusanya tayari kwa ajili ya vita katika siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi.

15 “Tazama, naja kama mwizi! Amebarikiwa yeye akeshaye na kuziweka tayari nguo zake ili asiende uchi na kuonekana aibu yake.”

16 Ndipo wakawakusanya wafalme pamoja mahali paitwapo Armagedonikwa Kiebrania.

17 Malaika wa saba akamimina bakuli lake angani na sauti kubwa ikatoka mle hekaluni katika kile kiti cha enzi, ikisema, “Imekwisha kuwa!”

18 Kukawa na mianga ya umeme wa radi, ngurumo, radi na tetemeko kubwa la ardhi. Hapajawa kamwe na tetemeko la ardhi kama hilo tangu mwanadamu awepo duniani, hivyo lilikuwa tetemeko kubwa ajabu.

19 Ule mji mkubwa ukagawanyika katika sehemu tatu, nayo miji ya mataifa ikaanguka. Mungu akaukumbuka Babeli Mkuu na kumpa kikombe kilichojaa mvinyo wa ghadhabu ya hasira yake.

20 Kila kisiwa kikatoweka wala milima haikuonekana.

21 Mvua kubwa ya mawe yenye uzito wa talanta mojaikashuka kutoka mbinguni, ikawaangukia wanadamu. Nao wanadamu wakamlaani Mungu kwa ajili ya hayo mapigo ya mvua ya mawe, kwa sababu pigo hilo lilikuwa la kutisha.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/REV/16-cacbcd1969f59e1688038a0d7a81d5de.mp3?version_id=1627—

Categories
Ufunuo

Ufunuo 17

Kahaba Mkuu Na Mnyama

1 Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na yale mabakuli saba akaja akaniambia, “Njoo, nitakuonyesha adhabu ya yule kahaba mkuu, aketiye juu ya maji mengi.

2 Yule ambaye wafalme wa dunia walizini naye na watu wakaao duniani walilewa kwa mvinyo wa uzinzi wake.”

3 Kisha yule malaika akanichukua katika Roho akanipeleka jangwani. Huko nikamwona mwanamke mmoja ameketi juu ya mnyama mwekundu aliyejaa majina ya kumkufuru Mungu mwili mzima. Mnyama huyo alikuwa na vichwa saba na pembe kumi.

4 Huyo mwanamke alikuwa amevaa mavazi ya rangi ya zambarau na nyekundu, akimetameta kwa dhahabu, vito vya thamani na lulu. Mkononi mwake alikuwa ameshika kikombe cha dhahabu kilichojaa mambo ya machukizo na uchafu wa uzinzi wake.

5 Kwenye kipaji chake cha uso palikuwa pameandikwa jina:

“Siri,

Babeli Mkuu,

Mama wa makahaba

na wa machukizo ya dunia.”

6 Nikaona kuwa huyo mwanamke alikuwa amelewa kwa damu ya watakatifu, yaani, damu ya wale watu waliouawa kwa ushuhuda wa Yesu.

Nilipomwona huyo mwanamke, nilistaajabu sana.

7 Ndipo yule malaika akaniambia, “Kwa nini unastaajabu? Nitakufafanulia siri ya huyo mwanamke na huyo mnyama aliyempanda, mwenye vichwa saba na pembe kumi.

8 Huyo mnyama ambaye ulimwona, wakati fulani alikuwepo, lakini sasa hayupo, naye atapanda kutoka lile Shimo na kwenda kwenye maangamizo yake. Watu waishio duniani ambao majina yao hayakuandikwa kwenye kitabu cha uzima tangu kuumbwa kwa ulimwengu watastaajabu kumwona huyo mnyama, kwa maana alikuwepo wakati fulani, na sasa hayupo, lakini atakuwepo.

9 “Hapa ndipo penye wito wa akili pamoja na hekima. Vile vichwa saba ni vilima saba ambavyo huyo mwanamke amevikalia.

10 Pia hivyo vichwa saba ni wafalme saba ambao miongoni mwao watano wamekwisha kuanguka, yupo mwingine hajaja bado, lakini atakapokuja, atalazimika kukaa kwa muda mfupi.

11 Yule mnyama aliyekuwepo wakati fulani na ambaye sasa hayupo, yeye ni mfalme wa nane. Ni miongoni mwa wale saba, naye anakwenda kwenye maangamizi yake.

12 “Zile pembe kumi ulizoziona ni wafalme kumi ambao bado hawajapokea ufalme, lakini watapokea mamlaka kuwa wafalme kwa saa moja pamoja na yule mnyama.

13 Hawa wana nia moja, nao watamwachia yule mnyama nguvu zao na mamlaka yao.

14 Watafanya vita na Mwana-Kondoo, lakini Mwana-Kondoo atawashinda kwa sababu yeye ni Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme. Yeye atakuwa pamoja na watu wake walioitwa ambao ni wateule wake na wafuasi wake waaminifu.”

15 Kisha yule malaika akaniambia, “Yale maji uliyoyaona yule kahaba akiwa ameketi juu yake ni jamaa, makutano, mataifa na lugha.

16 Zile pembe kumi ulizoziona, pamoja na huyo mnyama, watamchukia huyo kahaba, watamfilisi na kumwacha uchi, watamla nyama yake na kumteketeza kwa moto.

17 Kwa maana Mungu ameweka mioyoni mwao kutimiza kusudi lake kwa kukubali kumpa yule mnyama mamlaka yao ya utawala mpaka maneno ya Mungu yatakapotimia.

18 Yule mwanamke uliyemwona ni ule mji mkubwa unaotawala juu ya wafalme wa dunia.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/REV/17-8b6cb27aa61599aa7c16fc16f7a2a204.mp3?version_id=1627—