Categories
Yuda

Yuda Utangulizi

Utangulizi

Mwandishi wa waraka huu ni Yuda, aliyekuwa nduguye Yakobo, yule aliyekuwa msimamizi wa baraza la Yerusalemu, na mwandishi wa waraka wa Yakobo. Alikuwa ndugu wa Yesu kwa kuzaliwa na Maria (

Marko 6:3

).

Muktadha wa waraka huu na yale yaliyomo kwenye waraka wa 2 Petro yanaashiria kuwa Yuda alikuwa amehamasishwa na ujumbe wa Petro. Yuda anaonyesha kuwa alikusudia kuandika kuhusu wokovu, lakini akabadili nasaha zake ili kukemea mtazamo wa watu fulani wenye tabia mbaya, waliokuwa wakizunguka miongoni mwa waumini wakipotosha neema ya Mungu.

Mwandishi

Yuda, ndugu yake Yesu.

Kusudi

Kukumbusha kanisa umuhimu wa kuitetea imani, na kulionya juu ya watu waovu wanaozunguka miongoni mwao wakipotosha imani.

Mahali

Hapajulikani.

Tarehe

Kama 65 B.K.

Wahusika Wakuu

Yuda, Yakobo, na Yesu.

Wazo Kuu

Yuda anasisitiza umuhimu wa kuitetea imani. Wapotovu na wazushi ni lazima waonyeshwe wazi kwamba sio wa kweli. Yuda anaonya kwamba hukumu ya Mungu itawafikia wale waliopotoka katika imani, kama vile ilivyowafikia Kaini, Kora, na Balaamu.

Mambo Muhimu

Kuweka wazi walimu wa uongo na kuwakemea vikali. Anamalizia ujumbe wake kwa kuonyesha wazi kwamba Mungu anaweza kumlinda muumini, ili aweze kuishi maisha yaliyonyooka, na hatimaye kufika mbele ya Mungu bila lawama wala mawaa.

Mgawanyo

Utangulizi (

1-4

)

Maonyo dhidi ya uongo (

5-16

)

Adibisho na hitimisho (

17-25

).

Categories
Yuda

Yuda 1

Salamu

1 Yuda, mtumwa wa Yesu Kristo na nduguye Yakobo:

Kwa wale walioitwa, wapendwa katika Mungu Baba na kuhifadhiwa salama ndani ya Yesu Kristo:

2 Rehema, amani na upendo viwe kwenu kwa wingi.

Dhambi Na Hukumu Ya Watu Wasiomcha Mungu

3 Wapendwa, ingawa nilikuwa ninatamani sana kuwaandikia kuhusu wokovu ambao tunaushiriki sisi sote, niliona imenipasa kuwaandikia na kuwasihi kwamba mwitetee imani iliyokabidhiwa watakatifu kwa nafasi moja itoshayo.

4 Kwa kuwa kuna watu waliojipenyeza kwa siri katikati yenu, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, waovu, wapotoshao neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi wakimkana yeye aliye Bwana wetu wa pekee, Bwana Yesu Kristo.

Hukumu Kwa Walimu Wa Uongo

5 Ingawa mmekwisha kujua haya yote, nataka niwakumbushe kuwa Bwana akiisha kuwaokoa watu wake kutoka nchi ya Misri, baadaye aliwaangamiza wale ambao hawakuamini.

6 Nao malaika ambao hawakulinda nafasi zao, lakini wakayaacha makao yao, hawa amewaweka katika giza, wakiwa wamefungwa kwa minyororo ya milele kwa ajili ya hukumu Siku ile kuu.

7 Vivyo hivyo, Sodoma na Gomora na pia ile miji iliyokuwa kandokando, ambayo kwa jinsi moja na hao, walijifurahisha kwa uasherati na kufuata tamaa za mwili zisizo za asili, waliwekwa wawe mfano kwa kuadhibiwa katika moto wa milele.

8 Vivyo hivyo, hawa waotao ndoto huutia mwili unajisi, hukataa kuwa chini ya mamlaka na kunena mabaya juu ya wenye mamlaka.

9 Lakini hata malaika mkuu Mikaeli alipokuwa anashindana na ibilisi juu ya mwili wa Mose, hakuthubutu kumlaumu, bali alimwambia, “Bwana na akukemee!”

10 Lakini watu hawa hunena mabaya dhidi ya mambo wasiyoyafahamu. Na katika mambo yale wanayoyafahamu kwa hisia kama wanyama wasio na akili, hayo ndiyo hasa yanayowaharibu.

11 Ole wao! Kwa kuwa wanaifuata njia ya Kaini, wamekimbilia faida katika kosa la Balaamu na kuangamia katika uasi wa Kora.

12 Watu hawa ni dosari katika karamu zenu za upendo, wakila pamoja nanyi bila hofu, wakijilisha pasipo hofu. Wao ni mawingu yasiyokuwa na maji, yakichukuliwa na upepo, miti isiyo na matunda wakati wa mapukutiko, ambayo hunyauka, iliyokufa mara mbili na kungʼolewa kabisa.

13 Wao ni mawimbi makali ya bahari, yakitoa povu la aibu yao wenyewe, ni nyota zipoteazo, ambao weusi wa giza ndio akiba waliowekewa milele.

14 Enoki, mtu wa saba kuanzia Adamu alitoa unabii kuhusu watu hawa, akisema: “Tazama, Bwana anakuja pamoja na maelfu kwa maelfu ya watakatifu wake,

15 ili kumhukumu kila mmoja na kuwapatiliza wote wasiomcha Mungu kwa matendo yao yote ya uasi waliyoyatenda, pamoja na maneno yote ya kuchukiza ambayo wenye dhambi wamesema dhidi yake.”

16 Watu hawa ni wenye kunungʼunika na wenye kutafuta makosa; wao hufuata tamaa zao mbaya, hujisifu kwa maneno makuu kuhusu wao wenyewe na kuwasifu mno watu wenye vyeo kwa ajili ya kujipatia faida.

Maonyo Na Mausia

17 Lakini ninyi wapenzi, kumbukeni yale mitume wa Bwana Yesu Kristo waliyonena zamani.

18 Kwa kuwa waliwaambia, “Siku za mwisho kutakuwa na watu wenye kudhihaki, watakaofuata tamaa zao wenyewe za upotovu.”

19 Hawa ndio watu wanaowagawa ninyi, wafuatao tamaa zao za asili, wala hawana Roho.

20 Lakini ninyi wapendwa, jijengeni katika imani yenu iliyo takatifu sana tena ombeni katika Roho Mtakatifu.

21 Jilindeni katika upendo wa Mungu mkitazamia kwa furaha rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo ili awalete katika uzima wa milele.

22 Wahurumieni walio na mashaka;

23 wengine waokoeni kwa kuwanyakua kutoka kwenye moto; nao wengine wahurumieni mkiwa na hofu, mkichukia hata vazi lenye mawaa na kutiwa unajisi na mwili.

Dua Ya Kutakia Heri

24 Kwake yeye awezaye kuwalinda ninyi msianguke na kuwaleta mbele za utukufu wake mkuu bila dosari na kwa furaha ipitayo kiasi:

25 kwake yeye Mungu pekee Mwokozi wetu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu, utukufu, ukuu, uweza na mamlaka ni vyake tangu milele, sasa na hata milele! Amen.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JUD/1-078a97e1a0bac433e445382647c30e22.mp3?version_id=1627—

Categories
Ufunuo

Ufunuo Utangulizi

Utangulizi

Kitabu hiki kinazungumzia Ufunuo wa Yesu Kristo aliopewa na Mungu, ili awaonyeshe watumishi wake mambo ambayo yalitarajiwa kutukia karibuni. Ijapokuwa kitabu kimechukua jina la mwandishi, “Ufunuo wa Yohana,” ukweli ni kwamba hakimzungumzii Yohana wala hakimfunui yeye, bali kinamzungumzia na kumfunua Yesu Kristo. Yesu ndiye Mwana-Kondoo ambaye ameleta ukombozi. Yeye ndiye atakayehukumu na kushinda kabisa uovu, ili Ufalme wa milele ulio bora kabisa uthibitishwe.

Mwandishi

Mtume Yohana.

Kusudi

Kuwahimiza waumini kukataana na shinikizo la kumwabudu mfalme, na kusimama imara katika majaribu mpaka kifo.

Mahali

Kisiwa cha Patmo, karibu na pwani ya Uyunani (Ugiriki).

Tarehe

Kama 95 B.K.

Wahusika Wakuu

Yohana na Yesu.

Wazo Kuu

Kitabu hiki kinamwonyesha Yesu kuwa ndiye Mwana-Kondoo aliyechinjwa kwa ajili ya dhambi za ulimwengu, na akileta utawala wa haki milele na milele.

Mambo Muhimu

Kitabu hiki kinatumia lugha ya kiufunuo, yaani matumizi ya mifano, na majina ya kufananisha, ndoto, maono, matumizi makubwa ya tarakimu, na pia viumbe vya mbinguni na vya dunia vya kutisha. Kinaonyesha mambo yale Yohana aliyoyaona, yaani maono ya Yesu Kristo akiwa katikati ya kile kinara cha taa. Nayo mambo yaliyopo ina maana zile barua saba kwa makanisa saba katika Asia Ndogo. Nayo mambo ambayo hayana budi kutukia baada ya hayo inaweza kumaanisha matukio baada ya kunyakuliwa kwa kanisa.

Mgawanyo

Mwanzo wa maono kuhusu Yesu Kristo (

1:1-20

)

Barua saba kwa Makanisa saba (

2:1–3:22

)

Maono kuhusu Mungu na Mwana-Kondoo (

4:1–5:14

)

Lakiri saba za hukumu (

6:1–8:5

)

Tarumbeta saba za hukumu (

8:6–11:19

)

Maono kuhusu vita ya duniani na mbinguni (

12:1–14:20

)

Mabakuli saba ya hukumu (

15:1–16:21

)

Hukumu juu ya Kahaba Babeli (

17:1–19:21

)

Mwisho wa nyakati, na wakati ujao (

20:1–22:21

).

Categories
Ufunuo

Ufunuo 1

Utangulizi Na Salamu

1 Ufunuo wa Yesu Kristo aliopewa na Mungu ili awaonyeshe watumishi wake mambo ambayo ni lazima yatukie hivi karibuni. Alijulisha mambo haya kwa kumtuma malaika wake kwa Yohana mtumishi wake,

2 ambaye anashuhudia kuhusu kila kitu alichokiona, yaani, Neno la Mungu na ushuhuda wa Yesu Kristo.

3 Amebarikiwa yeye asomaye maneno ya unabii huu, na wamebarikiwa wale wanaoyasikia na kuyatia moyoni yale yaliyoandikwa humo, kwa sababu wakati umekaribia.

Salamu Kwa Makanisa Saba

4 Yohana, kwa makanisa saba yaliyoko Asia:

Neema na amani iwe kwenu kutoka kwake aliyeko, aliyekuwako na atakayekuja, na kutoka kwa wale roho saba walioko mbele ya kiti chake cha enzi,

5 na kutoka kwa Yesu Kristo ambaye ni yule shahidi mwaminifu, mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu, mtawala wa wafalme wa dunia.

Kwake yeye anayetupenda na ambaye ametuweka huru kutoka dhambi zetu kwa damu yake,

6 akatufanya sisi kuwa ufalme na makuhani, tumtumikie Mungu wake ambaye ni Baba yake. Utukufu na uwezo ni vyake milele na milele! Amen.

7 Tazama! Anakuja na mawingu,

na kila jicho litamwona,

hata wale waliomchoma;

na makabila yote duniani

yataomboleza kwa sababu yake.

Naam, ndivyo itakavyokuwa! Amen.

8 “Mimi ni Alfa na Omega,” asema Bwana Mungu, “aliyeko, aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi.”

Maono Ya Kristo

9 Mimi, Yohana, ndugu yenu ninayeshiriki pamoja nanyi mateso katika Yesu na katika ufalme na uvumilivu katika saburi, nilikuwa katika kisiwa cha Patmo kwa ajili ya neno la Mungu na ushuhuda wa Yesu.

10 Katika siku ya Bwana, nilikuwa katika Roho na nikasikia sauti kubwa kama ya baragumu nyuma yangu

11 ikisema, “Andika kwenye kitabu haya yote unayoyaona, kisha uyapeleke kwa makanisa saba, yaani: Efeso, Smirna, Pergamo, Thiatira, Sardi, Filadelfia na Laodikia.”

12 Ndipo nikageuka ili nione ni sauti ya nani iliyokuwa ikisema nami. Nami nilipogeuka, nikaona vinara saba vya taa vya dhahabu,

13 na katikati ya vile vinara vya taa, alikuwamo mtu kama Mwana wa Adamu, akiwa amevaa joho refu, na mkanda wa dhahabu ukiwa umefungwa kifuani mwake.

14 Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu, nyeupe kama theluji, nayo macho yake yalikuwa kama mwali wa moto.

15 Nyayo zake zilikuwa kama shaba inayongʼaa, katika tanuru ya moto, nayo sauti yake ilikuwa kama mugurumo ya maji mengi.

16 Katika mkono wake wa kuume alishika nyota saba, na kinywani mwake ulitoka upanga mkali wenye makali kuwili. Uso wake ulikuwa kama jua likingʼaa kwa nguvu zake zote.

17 Nilipomwona, nilianguka miguuni pake kama aliyekufa. Ndipo akauweka mkono wake wa kuume juu yangu na kusema: “Usiogope, Mimi ndiye wa Kwanza na wa Mwisho.

18 Mimi ni Yeye Aliye Hai, niliyekuwa nimekufa, na tazama, ni hai milele na milele! Nami ninazo funguo za mauti na kuzimu.

19 “Basi andika mambo uliyoyaona, yaliyopo na yale yatakayotukia baada ya haya.

20 Kuhusu siri ya zile nyota saba ulizoziona katika mkono wangu wa kuume na vile vinara saba vya taa vya dhahabu ni hii: Zile nyota saba ni malaika wa yale makanisa saba, navyo vile vinara saba ni hayo makanisa saba.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/REV/1-1b3e8e306581865c9d3e066dfca8cc01.mp3?version_id=1627—

Categories
Ufunuo

Ufunuo 2

Kwa Kanisa Lililoko Efeso

1 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso andika:

“Haya ndiyo maneno ya yule aliyezishika zile nyota saba katika mkono wake wa kuume na ambaye hutembea kati ya vile vinara saba vya taa vya dhahabu.

2 Nayajua matendo yako, bidii yako na saburi yako. Najua kuwa huwezi kuvumiliana na watu waovu na ya kwamba umewajaribu wale wanaojifanya kuwa mitume na kumbe sio, nawe umewatambua kuwa ni waongo.

3 Umevumilia na kustahimili taabu kwa ajili ya Jina langu, wala hukuchoka.

4 “Lakini nina neno dhidi yako: Umeuacha upendo wako wa kwanza.

5 Kumbuka basi ni wapi ulikoangukia! Tubu na ukafanye matendo yale ya kwanza. Kama usipotubu, nitakuja kwako na kukiondoa kinara chako cha taa kutoka mahali pake.

6 Lakini una jambo hili kwa upande wako: Unayachukia matendo ya Wanikolai, ambayo nami pia nayachukia.

7 “Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa haki ya kula matunda toka kwa mti wa uzima, ambao uko katika paradisoya Mungu.

Kwa Kanisa Lililoko Smirna

8 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Smirna andika:

“Haya ndiyo maneno yake yeye aliye wa Kwanza na wa Mwisho, aliyekufa kisha akafufuka.

9 Naijua dhiki yako na umaskini wako, lakini wewe ni tajiri! Nayajua masingizio ya wale wasemao kuwa ni Wayahudi lakini sio, bali wao ni sinagogi la Shetani.

10 Usiogope mateso yatakayokupata. Nakuambia ibilisi atawatia baadhi yenu gerezani ili kuwajaribu, nanyi mtapata dhiki kwa muda wa siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.

11 “Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatadhuriwa kamwe na mauti ya pili.

Kwa Kanisa Lililoko Pergamo

12 “Kwa malaika wa Kanisa lililoko Pergamo andika:

“Haya ndiyo maneno yake yeye aliye na upanga mkali wenye makali kuwili.

13 Ninajua unakoishi, ni kule ambako Shetani ana kiti chake cha enzi. Lakini umelishika Jina langu. Wala hukuikana imani yako kwangu hata katika siku za shahidi wangu mwaminifu Antipa, ambaye aliuawa katika mji mkuu wenu, ambako ndiko anakoishi Shetani.

14 “Hata hivyo, nina mambo machache dhidi yako: Unao watu wafuatao mafundisho ya Balaamu, yule aliyemfundisha Balaki kuwashawishi Waisraeli watende dhambi kwa kula vitu vilivyotolewa kafara kwa sanamu na kufanya uasherati.

15 Vivyo hivyo unao wale wayashikayo mafundisho ya Wanikolai.

16 Basi tubu! Ama sivyo, nitakuja kwako upesi na kupigana na watu hao kwa upanga wa kinywa changu.

17 “Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa. Nitampa pia jiwe jeupe ambalo juu yake limeandikwa jina jipya asilolijua mtu, isipokuwa yule anayelipokea.

Kwa Kanisa Lililoko Thiatira

18 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira andika:

“Haya ndiyo maneno ya Mwana wa Mungu, ambaye macho yake ni kama mwali wa moto na ambaye miguu yake ni kama shaba iliyosuguliwa sana.

19 Nayajua matendo yako, upendo wako na imani yako, huduma na saburi yako na kwamba matendo yako ya sasa yamezidi yale ya kwanza.

20 “Hata hivyo, nina neno dhidi yako: Unamvumilia yule mwanamke Yezebeli ambaye anajiita nabii, lakini anawafundisha na kuwapotosha watumishi wangu ili wafanye uasherati na kula vyakula vilivyotolewa kafara kwa sanamu.

21 Nimempa muda ili atubu kwa ajili ya uasherati wake, lakini hataki.

22 Kwa hiyo nitamtupa kwenye kitanda cha mateso, na nitawafanya hao wanaozini naye kupata mateso makali wasipotubia njia zake.

23 Nami nitawaua watoto wake. Nayo makanisa yote yatajua kwamba Mimi ndiye nichunguzaye mioyo na nia, na kwamba nitamlipa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake.

24 Basi nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, ninyi ambao hamyafuati mafundisho ya Yezebeli, wala hamkujifunza hayo yanayoitwa mambo ya ndani sana ya Shetani (sitaweka mzigo mwingine wowote juu yenu):

25 Lakini shikeni sana mlicho nacho, mpaka nitakapokuja.

26 “Atakayeshinda na kutenda mapenzi yangu mpaka mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa:

27 “ ‘Atawatawala kwa fimbo ya chuma,

atawavunja vipande vipande

kama chombo cha udongo’:

kama vile mimi nilivyopokea mamlaka kutoka kwa Baba yangu.

28 Nami nitampa pia ile nyota ya asubuhi.

29 Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/REV/2-3da260843ae4c59492025e2d9db423ce.mp3?version_id=1627—

Categories
Ufunuo

Ufunuo 3

Kwa Kanisa Lililoko Sardi

1 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi andika:

“Haya ndiyo maneno ya aliye na zile Roho sabaza Mungu na zile nyota saba. Nayajua matendo yako, kwamba una sifa ya kuwa hai, lakini umekufa.

2 Amka! Nawe uyaimarishe yale yaliyosalia na yaliyo karibu kufa, kwa maana sikuona kwamba kazi zako zimekamilika machoni pa Mungu wangu.

3 Kumbuka basi yale uliyoyapokea na kuyasikia, yatii na ukatubu. Lakini usipoamka, nitakuja kama mwizi wala hutajua saa nitakayokuja kwako.

4 “Lakini bado una watu wachache katika Sardi ambao hawajayachafua mavazi yao. Wao wataenda pamoja nami, wakiwa wamevaa mavazi meupe, kwa maana wanastahili.

5 Yeye ashindaye atavikwa vazi jeupe kama wao. Sitafuta jina lake kutoka kitabu cha uzima, bali nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu na mbele za malaika wake.

6 Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa.

Kwa Kanisa Lililoko Filadelfia

7 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika:

“Haya ndiyo maneno yake yeye aliye mtakatifu na wa kweli, yeye aliye na ufunguo wa Daudi. Anachokifungua hakuna awezaye kukifunga, wala anachokifunga hakuna awezaye kukifungua.

8 Nayajua matendo yako. Tazama, nimeweka mbele yako mlango uliofunguliwa, wala hakuna awezaye kuufunga. Ninajua kwamba una nguvu kidogo lakini umelishika neno langu wala hukulikana Jina langu.

9 Nitawafanya wale wa sinagogi la Shetani, wale ambao husema kuwa ni Wayahudi lakini sio, bali ni waongo, nitawafanya waje wapige magoti miguuni pako, na wakiri ya kwamba nimekupenda.

10 Kwa kuwa umeshika amri yangu ya kuvumilia katika saburi, nitakulinda katika saa ya kujaribiwa inayokuja ulimwenguni pote, ili kuwajaribu wote wakaao duniani.

11 “Ninakuja upesi. Shika sana ulicho nacho, ili mtu asije akaichukua taji yako.

12 Yeye ashindaye nitamfanya kuwa nguzo katika hekalu la Mungu wangu, wala hatatoka humo kamwe. Nitaandika juu yake Jina la Mungu wangu na jina la mji mkubwa wa Mungu wangu, Yerusalemu mpya, ambao unashuka kutoka mbinguni kwa Mungu wangu. Nami pia nitaandika juu yake Jina langu jipya.

13 Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa.

Kwa Kanisa Lililoko Laodikia

14 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika:

“Haya ndiyo maneno yake yeye aliye Amen, shahidi mwaminifu na wa kweli, mtawala wa uumbaji wote wa Mungu.

15 Nayajua matendo yako, ya kwamba wewe si baridi wala si moto. Afadhali ungelikuwa moja au lingine.

16 Hivyo kwa kuwa u vuguvugu, si baridi wala moto, nitakutapika utoke kinywani mwangu.

17 Kwa maana unasema: ‘Mimi ni tajiri, nimejilimbikizia mali, wala sihitaji kitu chochote.’ Lakini hutambui ya kwamba wewe ni mnyonge, wa kuhurumiwa, maskini, kipofu, tena uliye uchi.

18 Nakushauri ununue kutoka kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, ili upate kuwa tajiri, na mavazi meupe ili uyavae upate kuficha aibu ya uchi wako, na mafuta ya kupaka macho yako ili upate kuona.

19 “Wale niwapendao, ninawakemea na kuwaadibisha. Hivyo uwe na bidii ukatubu.

20 Tazama! Nasimama mlangoni nabisha. Kama mtu yeyote akisikia sauti yangu na kufungua mlango, nitaingia ndani na kula pamoja naye, naye pamoja nami.

21 “Yeye ashindaye nitampa haki ya kuketi pamoja nami kwenye kiti changu cha enzi, kama vile mimi nilivyoshinda na nikaketi pamoja na Baba yangu kwenye kiti chake cha enzi.

22 Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/REV/3-47298f51be8a257e39d9a63c209e5019.mp3?version_id=1627—

Categories
Ufunuo

Ufunuo 4

Kiti Cha Enzi Kilichoko Mbinguni

1 Baada ya mambo hayo nilitazama, nami nikaona mbele yangu mlango uliokuwa wazi mbinguni. Nayo ile sauti niliyokuwa nimeisikia hapo mwanzo ikisema nami kama tarumbeta ikasema, “Njoo, huku, nami nitakuonyesha yale ambayo hayana budi kutokea baada ya haya.”

2 Ghafula nilikuwa katika Roho, na hapo mbele yangu kilikuwepo kiti cha enzi mbinguni, kikiwa kimekaliwa na mtu.

3 Aliyekuwa amekikalia alikuwa anaonekana kama yaspi na akiki. Kukizunguka kile kiti cha enzi palikuwa na upinde wa mvua ulioonekana kama zumaridi.

4 Kukizunguka hicho kiti cha enzi palikuwa na viti vingine vya enzi ishirini na vinne, na juu ya hivyo viti walikuwa wameketi wazee ishirini na wanne. Walivaa mavazi meupe, na walikuwa na taji za dhahabu vichwani mwao.

5 Kwenye kile kiti cha enzi palikuwa panatoka miali ya umeme wa radi, ngurumo na sauti za radi. Mbele ya kiti cha enzi, taa saba zilikuwa zinawaka. Hizi ndizo roho sabaza Mungu.

6 Pia mbele ya kiti cha enzi palikuwa na kile kilichoonekana kama bahari ya kioo, iliyokuwa angavu kama bilauri.

Katikati, kukizunguka kile kiti cha enzi, kulikuwa na viumbe wanne wenye uhai, wakiwa wamejawa na macho mbele na nyuma.

7 Kiumbe wa kwanza mwenye uhai alikuwa kama simba, wa pili alikuwa kama ngʼombe dume, wa tatu alikuwa na uso kama wa mwanadamu, na wa nne alikuwa kama tai anayeruka.

8 Kila mmoja wa hawa viumbe wanne wenye uhai alikuwa na mabawa sita, na kujawa na macho pande zote hadi chini ya mabawa. Usiku na mchana hawaachi kusema:

“Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,

niBwanaMungu Mwenyezi,

aliyekuwako, aliyeko na atakayekuja.”

9 Kila mara viumbe hao wanne wenye uhai wanapomtukuza, kumheshimu na kumshukuru yeye aketiye kwenye kile kiti cha enzi, tena aishiye milele na milele,

10 wale wazee ishirini na wanne huanguka mbele zake aketiye kwenye kiti cha enzi na kumwabudu yeye aliye hai milele na milele. Huziweka taji zao mbele ya kiti cha enzi, wakisema:

11 “Bwana wetu na Mungu wetu,

wewe unastahili kupokea utukufu

na heshima na uweza,

kwa maana ndiwe uliyeviumba vitu vyote,

na kwa mapenzi yako viliumbwa

na vimekuwako.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/REV/4-937f7ca6d3e9708cbb1096b059c882bd.mp3?version_id=1627—

Categories
Ufunuo

Ufunuo 5

Kitabu Na Mwana-Kondoo

1 Kisha nikaona katika mkono wake wa kuume wa yule aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi, kitabu kilichoandikwa ndani na upande wa nje, kikiwa kimefungwa kwa lakiri saba.

2 Nami nikamwona malaika mwenye nguvu akitangaza kwa sauti kuu, akisema, “Ni nani anayestahili kuzivunja hizo lakiri na kukifungua kitabu?”

3 Lakini hapakuwa na yeyote mbinguni wala duniani au chini ya dunia aliyeweza kukifungua hicho kitabu wala hata kutazama ndani yake.

4 Nikalia sana sana kwa sababu hakuonekana yeyote anayestahili kukifungua hicho kitabu wala kutazama ndani yake.

5 Kisha, mmoja wa wale wazee akaniambia, “Usilie! Tazama, Simba wa kabila la Yuda, wa Uzao wa Daudi, ameshinda. Yeye ndiye anayeweza kukifungua hicho kitabu na kuvunja hizo lakiri zake saba.”

6 Ndipo nikaona katikati ya kile kiti cha enzi na wale viumbe wenye uhai wanne na miongoni mwa wale wazee, Mwana-Kondoo amesimama, akiwa kama amechinjwa. Alikuwa na pembe saba na macho saba, ambazo ndizo zile Roho sabaza Mungu zilizotumwa duniani pote.

7 Huyo Mwana-Kondoo akaja na kukitwaa kile kitabu kutoka kwenye mkono wa kuume wa yule aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi.

8 Alipokwisha kukitwaa kile kitabu, wale viumbe wenye uhai wanne pamoja na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele ya yule Mwana-Kondoo. Kila mmoja wao alikuwa na kinubi, nao walikuwa wameshika mabakuli ya dhahabu yaliyojaa uvumba, ambayo ni maombi ya watakatifu.

9 Nao wakaimba wimbo mpya, wakisema:

“Wewe unastahili kukitwaa kitabu

na kuzivunja lakiri zake,

kwa sababu ulichinjwa

na kwa damu yako ukamnunulia Mungu watu

kutoka kila kabila, kila lugha,

kila jamaa na kila taifa.

10 Wewe umewafanya hawa wawe ufalme na makuhani

wa kumtumikia Mungu wetu,

nao watatawala duniani.”

11 Kisha nikatazama, nikasikia sauti za malaika wengi wakiwa wamekizunguka kile kiti cha enzi, pamoja na wale viumbe wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne. Idadi yao ilikuwa kumi elfu mara kumi elfu na maelfu ya maelfu.

12 Nao waliimba kwa sauti kuu, wakisema:

“Anastahili Mwana-Kondoo, yeye aliyechinjwa,

kupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu

na heshima na utukufu na sifa!”

13 Kisha nikasikia kila kiumbe mbinguni na duniani, chini ya nchi na baharini na vyote vilivyomo ndani yake vikiimba:

“Sifa na heshima na utukufu na uweza

ni vyake yeye aketiye juu ya hicho kiti cha enzi

na kwa Mwana-Kondoo,

milele na milele!”

14 Wale viumbe wenye uhai wanne wakasema, “Amen!” Nao wale wazee ishirini na wanne wakaanguka kifudifudi wakaabudu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/REV/5-959fdf8919d949a4dcb65436c8dcb771.mp3?version_id=1627—

Categories
Ufunuo

Ufunuo 6

Mwana-Kondoo Avunja Lakiri Saba

1 Kisha nikaangalia wakati Mwana-Kondoo akivunja ile lakiri ya kwanza miongoni mwa zile saba. Ndipo nikasikia mmoja wa wale viumbe wanne wenye uhai akisema kwa sauti kama ya radi: “Njoo!”

2 Nikatazama, na hapo mbele yangu alikuwepo farasi mweupe! Yeye aliyempanda alikuwa na upinde, naye akapewa taji, akampanda akatoka akiwa kama mshindi aelekeaye katika kushinda.

3 Alipoivunja ile lakiri ya pili, nikamsikia yule kiumbe wa pili mwenye uhai akisema, “Njoo!”

4 Ndipo akatokea farasi mwingine mwekundu sana. Yeye aliyempanda akapewa uwezo wa kuondoa amani duniani na kuwafanya watu wauane. Yeye akapewa upanga mkubwa.

5 Mwana-kondoo alipoivunja ile lakiri ya tatu, nikamsikia yule kiumbe wa tatu mwenye uhai akisema, “Njoo!” Nikatazama, na mbele yangu alikuwepo farasi mweusi! Yeye aliyempanda alikuwa na mizani mkononi mwake.

6 Ndipo nikasikia kile kilichokuwa kama sauti katikati ya wale viumbe wanne wenye uhai ikisema, “Kipimo kimojacha ngano kwa mshahara wa kibarua wa siku moja,na vipimo vitatu vya shayiri kwa mshahara wa kibarua cha siku moja. Lakini usiharibu mafuta wala divai!”

7 Alipovunja ile lakiri ya nne, nikasikia sauti ya yule kiumbe wa nne mwenye uhai ikisema, “Njoo!”

8 Nikatazama, na hapo mbele yangu alikuwepo farasi mwenye rangi ya kijivujivu! Yeye aliyempanda aliitwa Mauti, naye Kuzimualikuwa akimfuata nyuma yake kwa karibu. Wakapewa mamlaka juu ya robo ya dunia, kuua kwa upanga, njaa, tauni na kwa wanyama wakali wa dunia.

9 Mwana-kondoo alipoivunja ile lakiri ya tano, nikaona chini ya madhabahu, roho za wale waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu na kwa ajili ya ushuhuda walioutunza.

10 Wakalia kwa sauti kuu, wakisema, “Hata lini, Ee Bwana Mwenyezi, uliye mtakatifu na mwaminifu, hutawahukumu na kulipiza kisasi juu ya watu waishio duniani kwa ajili ya damu yetu?”

11 Kisha kila mmoja wao akapewa joho jeupe na wakaambiwa wangoje kwa muda kidogo zaidi, mpaka idadi ya ndugu zao na watumishi wenzao watakaouawa kama wao walivyouawa, itakapotimia.

12 Nikatazama akiivunja ile lakiri ya sita. Pakatokea tetemeko kuu la nchi, na jua likawa jeusi kama nguo ya gunia iliyotengenezwa kwa singa za mbuzi, na mwezi wote ukawa mwekundu kama damu.

13 Nyota zilizo angani zikaanguka ardhini kama vile matunda ya mtini yasiyokomaa yaangukavyo wakati mti wake unapotikiswa na upepo mkali.

14 Anga ikatoweka kama vile karatasi isokotwavyo, na kila mlima na kila kisiwa kikaondolewa mahali pake.

15 Ndipo wafalme wa dunia, wakuu wote, majemadari, matajiri, wenye nguvu na kila mtu, mtumwa na mtu huru, wakajificha katika mapango na kwenye miamba ya milima.

16 Wakaiita milima na miamba wakisema, “Tuangukieni, mkatufiche na uso wake yeye aketiye kwenye kiti cha enzi, na mkatuepushe na ghadhabu ya Mwana-Kondoo!

17 Kwa maana siku ile kuu ya ghadhabu yao imewadia. Je, ni nani awezaye kustahimili?”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/REV/6-f94a7c1e47564abb8380bde59e06230d.mp3?version_id=1627—

Categories
Ufunuo

Ufunuo 7

Waisraeli 144,000 Watiwa Muhuri

1 Baada ya hili nikaona malaika wanne wakiwa wamesimama katika pembe nne za dunia, wakizuia hizo pepo nne za dunia, ili kwamba pasiwe na upepo utakaovuma juu ya nchi au juu ya bahari au juu ya mti wowote.

2 Nikaona malaika mwingine akipanda kutoka mawio ya jua akiwa na muhuri wa Mungu aliye hai. Akawaita kwa sauti kubwa wale malaika wanne waliokuwa wamepewa mamlaka ya kuidhuru nchi na bahari, akisema,

3 “Msiidhuru nchi wala bahari, wala miti, hadi tuwe tumetia muhuri kwenye vipaji vya nyuso za watumishi wa Mungu wetu.”

4 Ndipo nikasikia idadi ya wale waliotiwa muhuri: yaani 144,000 kutoka makabila yote ya Israeli.

5 Kutoka kabila la Yuda 12,000 walitiwa muhuri,

kutoka kabila la Reubeni 12,000,

kutoka kabila la Gadi 12,000,

6 kutoka kabila la Asheri 12,000,

kutoka kabila la Naftali 12,000,

kutoka kabila la Manase 12,000,

7 kutoka kabila la Simeoni 12,000,

kutoka kabila la Lawi 12,000,

kutoka kabila la Isakari 12,000,

8 kutoka kabila la Zabuloni 12,000,

kutoka kabila la Yosefu 12,000,

na kutoka kabila la Benyamini 12,000.

Umati Mkubwa Wa Watu Kutoka Mataifa Yote

9 Baada ya hili nikatazama na hapo mbele yangu palikuwa na umati mkubwa wa watu ambao hakuna yeyote awezaye kuuhesabu, kutoka kila taifa, kila kabila, kila jamaa na kila lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi na mbele ya Mwana-Kondoo. Walikuwa wamevaa mavazi meupe na wakiwa wameshika matawi ya mitende mikononi mwao.

10 Nao walikuwa wakipiga kelele kwa sauti kubwa wakisema:

“Wokovu una Mungu wetu,

yeye aketiye kwenye kiti cha enzi,

na Mwana-Kondoo!”

11 Malaika wote walikuwa wamesimama kukizunguka kile kiti cha enzi na wale wazee ishirini na wanne na wale viumbe wanne wenye uhai. Wakaanguka kifudifudi mbele ya hicho kiti cha enzi na kumwabudu Mungu,

12 wakisema:

“Amen!

Sifa na utukufu

na hekima na shukrani na heshima

na uweza na nguvu

viwe kwa Mungu wetu milele na milele.

Amen!”

13 Kisha mmoja wa wale wazee ishirini na wanne akaniuliza, “Ni nani hawa waliovaa mavazi meupe, nao wametoka wapi?”

14 Nikamjibu, “Bwana, wewe wajua.”

Naye akasema, “Hawa ni wale waliotoka katika ile dhiki kuu, nao wamefua mavazi yao katika damu ya Mwana-Kondoo na kuyafanya meupe kabisa.

15 Kwa hiyo,

“Wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu

na kumtumikia usiku na mchana

katika hekalu lake;

naye aketiye katika kile kiti cha enzi

atatanda hema yake juu yao.

16 Kamwe hawataona njaa

wala kiu tena.

Jua halitawapiga

wala joto lolote liunguzalo.

17 Kwa maana Mwana-Kondoo

aliyeko katikati ya kile kiti cha enzi

atakuwa Mchungaji wao;

naye atawaongoza kwenda

kwenye chemchemi za maji yaliyo hai.

Naye Mungu atafuta kila chozi

kutoka macho yao.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/REV/7-8b7013eb05bcff29f19be4256b6999e8.mp3?version_id=1627—