Categories
2 Timotheo

2 Timotheo 1

1 Paulo mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, kulingana na ile ahadi ya uzima uliomo ndani ya Kristo Yesu.

2 Kwa Timotheo, mwanangu mpendwa:

Neema, rehema na amani itokayo kwa Mungu Baba, na kwa Kristo Yesu Bwana wetu.

Shukrani Na Kutiwa Moyo

3 Ninamshukuru Mungu, ninayemtumikia kwa dhamiri safi, kama walivyofanya baba zangu, ninapokukumbuka usiku na mchana katika maombi yangu.

4 Nikiyakumbuka machozi yako, ninatamani sana kukuona ili nipate kujawa na furaha.

5 Nimekuwa nikiikumbuka imani yako ya kweli, waliokuwa nayo bibi yako Loisi na mama yako Eunike na ambayo mimi ninasadiki sasa wewe pia unayo.

6 Kwa sababu hii nakukumbusha uchochee ile karama ya Mungu, iliyowekwa ndani yako nilipokuwekea mikono yangu.

7 Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali roho ya nguvu, ya upendo na ya moyo wa kiasi.

8 Kwa hiyo usione haya kushuhudia kuhusu Bwana wetu, wala usinionee haya mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Bali uishiriki pamoja nami taabu ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu,

9 ambaye alituokoa na kutuita katika mwito mtakatifu: si kwa kadiri ya matendo yetu mema bali kwa sababu ya kusudi lake mwenyewe na neema yake. Neema hii tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele.

10 Lakini sasa imefunuliwa kwa kudhihirishwa kwake Mwokozi wetu, Kristo Yesu, ambaye amebatilisha mauti na kuleta uzima na kutokufa kwa njia ya Injili.

11 Nami nimewekwa kuwa mhubiri, mtume na mwalimu wa Injili hii.

12 Hii ndiyo sababu ninateseka namna hii, lakini sioni haya kwa maana ninamjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kuwa anaweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hadi siku ile.

13 Shika kwa uthabiti kielelezo cha mafundisho yenye uzima yale uliyoyasikia kwangu, pamoja na imani na upendo katika Kristo Yesu.

14 Ilinde ile amana uliyokabidhiwa kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu.

15 Unajua ya kuwa watu wote katika Asia wameniacha, miongoni mwao wamo Filego na Hermogene.

16 Bwana akawahurumie watu wa nyumbani mwa Onesiforo, kwa sababu aliniburudisha mara kwa mara wala hakuionea aibu minyororo yangu.

17 Badala yake, alipokuwa Rumi, alinitafuta kwa bidii mpaka akanipata.

18 Bwana na amjalie kupata rehema zake siku ile! Nawe unajua vyema jinsi alivyonisaidia huko Efeso.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2TI/1-ec4901cdc1fc953af51c13f643df0866.mp3?version_id=1627—

Categories
2 Timotheo

2 Timotheo 2

Askari Mwema Wa Kristo Yesu

1 Basi, wewe mwanangu, uwe hodari katika neema iliyo ndani ya Kristo Yesu.

2 Nayo mambo yale uliyonisikia nikiyasema mbele ya mashahidi wengi, uwakabidhi watu waaminifu watakaoweza kuwafundisha watu wengine vilevile.

3 Vumilia taabu pamoja nasi kama askari mwema wa Kristo Yesu.

4 Hakuna askari yeyote ambaye akiwa vitani hujishughulisha na mambo ya kawaida ya maisha haya kwa sababu nia yake ni kumpendeza yule aliyemwandika awe askari.

5 Vivyo hivyo, yeye ashindanaye katika michezo hawezi kupewa tuzo ya ushindi asiposhindana kulingana na kanuni za mashindano.

6 Mkulima mwenye bidii ya kazi ndiye anayestahili kuwa wa kwanza kupata fungu la mavuno.

7 Fikiri sana kuhusu haya nisemayo, kwa maana Bwana atakupa ufahamu katika mambo hayo yote.

8 Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuliwa kutoka kwa wafu, yeye aliye wa uzao wa Daudi. Hii ndiyo Injili yangu,

9 ambayo kwayo ninateseka hata kufikia hatua ya kufungwa minyororo kama mhalifu. Lakini neno la Mungu halifungwi.

10 Kwa hiyo ninavumilia mambo yote kwa ajili ya wateule wa Mungu, kusudi wao nao wapate wokovu ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele.

11 Hili ni neno la kuaminiwa:

Kwa maana kama tumekufa pamoja naye,

tutaishi pia pamoja naye.

12 Kama tukistahimili,

pia tutatawala pamoja naye.

Kama tukimkana yeye,

naye atatukana sisi.

13 Kama tusipoamini,

yeye hudumu kuwa mwaminifu,

kwa maana hawezi kujikana mwenyewe.

Mfanyakazi Aliyekubaliwa Na Mungu

14 Endelea kuwakumbusha mambo haya ukiwaonya mbele za Bwana waache kushindana kwa maneno ambayo hayana faida yoyote bali huwaangamiza tu wale wanaoyasikia.

15 Jitahidi kujionyesha kwa Mungu kuwa umekubaliwa naye, mtendakazi asiye na sababu ya kuona aibu, ukilitumia kwa usahihi neno la kweli.

16 Jiepushe na maneno mabaya, yasiyo na maana, yasiyo ya utauwa, kwa maana hayo huzidi kuwatosa watu katika kukosa heshima kwa Mungu.

17 Mafundisho yao yataenea kama kidonda kisichopona. Miongoni mwao wamo Himenayo na Fileto

18 ambao wameiacha kweli, wakisema kwamba ufufuo wa wafu umekwisha kuwako, nao huharibu imani ya baadhi ya watu.

19 Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, ukiwa na muhuri wenye maandishi haya: “Bwana anawajua walio wake”; tena, “Kila alitajaye jina la Bwana, na auache uovu.”

20 Katika nyumba kubwa si kwamba kuna vyombo vya dhahabu na fedha tu, bali pia vimo vyombo vya miti na vya udongo; vingine kwa matumizi maalum, na vingine kwa matumizi ya kawaida.

21 Basi ikiwa mtu amejitakasa na kujitenga na hayo niliyoyataja, atakuwa chombo maalum, kilichotengwa na ambacho kinamfaa mwenye nyumba, kimeandaliwa tayari kwa kila kazi njema.

22 Zikimbie tamaa mbaya za ujana, ufuate haki, imani, upendo na amani pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi.

23 Jiepushe na mabishano ya kipumbavu na yasiyo na maana, kwa kuwa wajua ya kwamba hayo huzaa magomvi.

24 Tena haimpasi mtumishi wa Bwana kuwa mgomvi, bali inampasa awe mwema kwa kila mtu, awezaye kufundisha, tena mvumilivu.

25 Inampasa kuwaonya kwa upole wale wanaopingana naye, kwa matumaini kwamba Mungu atawajalia kutubu na kuijua kweli,

26 ili fahamu zao ziwarudie tena, nao waponyoke katika mtego wa ibilisi ambaye amewateka wapate kufanya mapenzi yake.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2TI/2-f743a3b49b28b62e6c3be3269b9f94cf.mp3?version_id=1627—

Categories
2 Timotheo

2 Timotheo 3

Hatari Za Siku Za Mwisho

1 Lakini yakupasa ufahamu jambo hili, kwamba siku za mwisho kutakuwa na nyakati za hatari.

2 Kwa maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kumkufuru Mungu, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio watakatifu,

3 wasio na upendo, wasiopenda kupatanishwa, wasingiziaji, wasiozuia tamaa zao, wakatili, wasiopenda mema,

4 wasaliti, wakaidi, waliojaa majivuno, wapendao anasa zaidi kuliko kumpenda Mungu:

5 wakiwa na mfano wa utauwa kwa nje, lakini wakizikana nguvu za Mungu. Jiepushe na watu wa namna hiyo.

6 Miongoni mwao wamo wale wajiingizao katika nyumba za watu na kuwachukua mateka wanawake wajinga, waliolemewa na dhambi zao na kuyumbishwa na aina zote za tamaa mbaya.

7 Wakijifunza siku zote lakini kamwe wasiweze kufikia ujuzi wa kweli.

8 Kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Mose, vivyo hivyo watu hawa hupingana na ile kweli. Hawa ni watu wenye akili zilizopotoka, ambao wamekataliwa kwa mambo ya imani.

9 Lakini hawataendelea sana, kwa sababu upumbavu wao utakuwa dhahiri kwa watu wote, kama ulivyokuwa dhahiri upumbavu wa hao watu wawili.

Paulo Amwagiza Timotheo

10 Lakini wewe umeyajua mafundisho yangu, mwenendo, makusudi, imani, uvumilivu, upendo, ustahimilivu,

11 mateso na taabu, yaani mambo yote yaliyonipata huko Antiokia, Ikonio na Listra, mateso yote niliyostahimili, lakini Bwana aliniokoa katika hayo yote.

12 Naam, yeyote anayetaka kuishi maisha ya utauwa ndani ya Kristo Yesu atateswa.

13 Lakini watu waovu na wadanganyaji watazidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika.

14 Bali wewe, udumu katika yale uliyojifunza na kuyaamini kwa uthabiti, ukitambua ya kuwa ulijifunza hayo kutoka kwa nani,

15 na jinsi ambavyo tangu utoto umeyajua Maandiko matakatifu, ambayo yanaweza kukuhekimisha upate wokovu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu.

16 Kila Andiko limevuviwa na Mungu na lafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, kwa kuwaongoza na kwa kuwafundisha katika haki,

17 ili mtu wa Mungu awe amekamilishwa, apate kutenda kila kazi njema.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2TI/3-ce0abd464658ffcfdc67abde5aeb638c.mp3?version_id=1627—

Categories
2 Timotheo

2 Timotheo 4

Maagizo Ya Mwisho

1 Nakuagiza mbele za Mungu na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu watu walio hai na waliokufa wakati wa kuja kwake na ufalme wake, kwamba:

2 Hubiri Neno; kuwa tayari wakati ufaao na wakati usiofaa; karipia, kemea na utie moyo kwa uvumilivu wote na kwa mafundisho mazuri.

3 Maana wakati utakuja watu watakapokataa kuyakubali mafundisho yenye uzima. Badala yake, ili kutimiza tamaa zao wenyewe, watajikusanyia idadi kubwa ya walimu wapate kuwaambia yale ambayo masikio yao yanayowasha yanatamani kuyasikia.

4 Watakataa kusikiliza kweli na kuzigeukia hadithi za uongo.

5 Kwa habari yako wewe, vumilia mateso, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiza wajibu wote wa huduma yako.

6 Kwa maana mimi sasa ni tayari kumiminwa kama sadaka ya kinywaji, nayo saa yangu ya kuondoka imetimia.

7 Nimevipiga vita vizuri, mashindano nimeyamaliza, imani nimeilinda.

8 Sasa nimewekewa taji ya haki ambayo Bwana, mwamuzi wa haki, atanitunukia siku ile: wala si mimi tu, bali pia wote ambao wamengoja kwa shauku kudhihirishwa kwake.

Maelekezo Ya Binafsi

9 Jitahidi kuja kwangu upesi

10 kwa sababu Dema, kwa kuupenda ulimwengu, ameniacha na amekwenda Thesalonike. Kreske amekwenda Galatia na Tito amekwenda Dalmatia.

11 Ni Luka peke yake aliye hapa pamoja nami. Mtafute Marko uje naye kwa sababu ananifaa sana katika huduma yangu.

12 Nimemtuma Tikiko huko Efeso.

13 Utakapokuja, niletee lile joho nililoliacha kwa Karpo huko Troa na vile vitabu vyangu, hasa vile vya ngozi.

14 Aleksanda yule mfua chuma alinitendea ubaya mkubwa. Bwana atamlipa kwa ajili ya yale aliyotenda.

15 Wewe pia ujihadhari naye kwa sababu aliyapinga sana maneno yetu.

16 Katika utetezi wangu wa mara ya kwanza, hakuna hata mmoja aliyeniunga mkono, bali kila mmoja aliniacha. Namwomba Mungu wasihesabiwe hatia kwa jambo hilo.

17 Lakini Bwana alisimama upande wangu akanitia nguvu, ili kupitia kwangu lile Neno lihubiriwe kwa ukamilifu, watu wote Mataifa wapate kulisikia. Mimi niliokolewa kutoka kinywa cha simba.

18 Bwana ataniokoa katika kila shambulio baya na kunileta salama katika Ufalme wake wa mbinguni. Atukuzwe yeye milele na milele. Amen.

Salamu Za Mwisho

19 Wasalimu Prisilana Akila, na wote wa nyumbani kwa Onesiforo.

20 Erasto alibaki Korintho. Nami nikamwacha Trofimo huko Mileto akiwa mgonjwa.

21 Jitahidi ufike huku kabla ya majira ya baridi. Eubulo anakusalimu, vivyo hivyo Pude, Lino, Klaudia na ndugu wote.

22 Bwana awe pamoja na roho yako. Neema iwe pamoja nanyi. Amen.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2TI/4-1888fb73fa92f723aeccf484ba9d66dd.mp3?version_id=1627—

Categories
Tito

Tito Utangulizi

Utangulizi

Tito, kama vile Timotheo, alikuwa mshirika na rafiki wa karibu wa Paulo katika huduma yake. Alikuwa muumini asiyetahiriwa, mtu wa Mataifa kutoka Antiokia. Kama alifuatana na Paulo na Barnaba kuhudhuria baraza la Yerusalemu. Paulo alimwandikia Tito waraka huu muda mfupi tu baada ya kumwachia wajibu wa kuliangalia na kuliimarisha kanisa la Krete. Tito alikuwa na wajibu wa kuwateua wazee wa kanisa, kuwaweka wakfu, na kuwafundisha kushika misingi ya imani ya Kikristo.

Waraka huu unaonyesha kuwa kanisa la Krete halikuwa na mpangilio mahsusi. Ilimbidi Paulo aeleze kwa kina kuhusu sifa za wazee wa kanisa, na pia kutoa mafundisho kwa waumini. Paulo aligusia juu ya matatizo yanayowapata watumishi wa Mungu, na jinsi matatizo hayo yanavyoweza kutatuliwa.

Mwandishi

Mtume Paulo.

Kusudi

Kumshauri Tito kuhusu wajibu wake wa uangalizi wa makanisa katika kisiwa cha Krete.

Mahali

Pengine ni Korintho.

Tarehe

Mwaka wa 64 B.K.

Wahusika Wakuu

Paulo na Tito.

Wazo Kuu

Ingawa katika maisha yetu hapa duniani tumezungukwa na uovu na chuki, hatuna budi maisha yetu kuwa kielelezo jinsi neema ya Mungu inatupatia ushindi.

Mambo Muhimu

Kuweka mpango na uangalizi wa makanisa, na jinsi ya kufanya kazi hiyo. Mkazo wa barua hii ni kuhusu kuishi maisha matakatifu katika Kristo katikati ya uovu ulioko duniani. Paulo anarudia mara kwa mara kusisitiza kudumisha matendo mema.

Mgawanyo

Salamu (

1:1-4

)

Sifa za wazee wa kanisa (

1:5-16

)

Maelezo ya jumla kuhusu waumini (

2:1-15

)

Maagizo kuhusu maisha yawapasayo Wakristo (

3:1-15

).

Categories
Tito

Tito 1

1 Paulo, mtumishi wa Mungu na mtume wa Yesu Kristo kwa ajili ya imani ya wateule wa Mungu na kuijua kweli iletayo utauwa:

2 imani na ujuzi ulioko katika tumaini la uzima wa milele, ambao Mungu, asiyesema uongo, aliahidi hata kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu,

3 naye kwa wakati wake aliouweka alilidhihirisha neno lake kwa njia ya mahubiri ambayo mimi nimewekewa amana kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu:

4 Kwa Tito, mwanangu hasa katika imani tunayoshiriki sote:

Neema iwe kwako na amani itokayo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Mwokozi wetu.

Kazi Ya Tito Huko Krete

5 Sababu ya mimi kukuacha huko Krete ni ili uweke utaratibu mambo yale yaliyosalia na kuwaweka wazee wa kanisa katika kila mji, kama nilivyokuagiza.

6 Mzee wa kanisa asiwe na lawama, awe mume wa mke mmoja, mtu ambaye watoto wake ni waaminio na wala hawashtakiwi kwa ufisadi.

7 Kwa kuwa mwangalizi, kama wakili wa Mungu, imempasa kuwa mtu asiye na lawama, asiwe mwenye majivuno au mwepesi wa hasira, wala mlevi, wala asiwe mtu mwenye tamaa ya mapato yasiyo ya halali.

8 Bali awe mkarimu, anayependa mema, mwenye kiasi, mwenye haki, mwadilifu, mnyofu, mtakatifu na mwenye kuitawala nafsi yake.

9 Inampasa alishike kwa uthabiti lile neno la imani kama lilivyofundishwa, kusudi aweze kuwaonya wengine kwa mafundisho manyofu na kuwakanusha wale wanaopingana nayo.

Walimu Wa Uongo

10 Kwa maana wako wengi wasiotii, wenye maneno yasiyo na maana, hasa wale wa kikundi cha tohara.

11 Hao ni lazima wanyamazishwe, kwa sababu wanaharibu watu wa nyumba nzima wakifundisha mambo yasiyowapasa kufundisha. Wanafanya hivyo kwa ajili ya kujipatia mapato ya udanganyifu.

12 Hata mmojawapo wa manabii wao mwenyewe amesema, “Wakrete ni waongo siku zote, wanyama wabaya, walafi, wavivu.”

13 Ushuhuda huu ni kweli. Kwa hiyo, uwakemee kwa ukali wapate kuwa wazima katika imani,

14 ili wasiendelee kuangalia hadithi za Kiyahudi au maagizo ya wale watu wanaoikataa kweli.

15 Kwa wale walio safi, kila kitu ni safi kwao. Lakini kwa wale waliopotoka na wasioamini, hakuna chochote kilicho safi. Kwa kweli nia zao na dhamiri zao zimepotoka.

16 Wanadai kumjua Mungu, lakini kwa matendo yao wanamkana. Hao watu ni chukizo, wasiotii, wasiofaa kwa jambo lolote jema.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/TIT/1-7befd35d637fee5a973428fe6b9ae05c.mp3?version_id=1627—

Categories
Tito

Tito 2

Fundisha Mafundisho Manyofu

1 Inakupasa kufundisha itikadi sahihi.

2 Wafundishe wazee kuwa na kiasi, wastahivu, wenye busara na wanyofu katika imani, upendo na saburi.

3 Vivyo hivyo, wafundishe wanawake wazee kuwa na mwenendo wa utakatifu, wala wasiwe wasingiziaji au walevi, bali wafundishe yale yaliyo mema,

4 ili waweze kuwafundisha wanawake vijana kuwa na kiasi, wawapende waume zao na kuwapenda watoto wao,

5 wawe waaminifu, watakatifu, wakitunza vyema nyumba zao, wema, watiifu kwa waume zao, ili mtu yeyote asije akalikufuru neno la Mungu.

6 Vivyo hivyo, himiza vijana wawe na kiasi.

7 Katika kila jambo uwe kielelezo kwa kutenda mema. Katika mafundisho yako uonyeshe uadilifu, utaratibu,

8 na usemi sahihi usio na lawama, ili wanaokupinga watahayari, wakose neno lolote baya la kusema juu yetu.

9 Wafundishe watumwa kuwatii mabwana zao katika kila jambo, wakijitahidi kuwapendeza wala wasijibizane nao,

10 wala wasiwaibie, bali waonyeshe kuwa wanaweza kuaminika kabisa, ili kwa kila namna wayafanye mafundisho ya Mungu Mwokozi wetu yawe ya kuvutia.

11 Kwa maana neema ya Mungu ambayo inawaokoa wanadamu wote imefunuliwa.

12 Nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia, ili tupate kuishi maisha ya kiasi, ya haki na ya utaua katika ulimwengu huu wa sasa,

13 huku tukilitazamia tumaini lenye baraka na ufunuo wa utukufu wa Mungu wetu Mkuu, aliye Mwokozi wetu Yesu Kristo.

14 Ndiye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe kutoka uovu wote na kujisafishia watu kuwa mali yake Mwenyewe, yaani, wale walio na juhudi katika kutenda mema.

15 Basi wewe fundisha mambo haya. Onya na kukaripia kwa mamlaka yote. Mtu yeyote asikudharau.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/TIT/2-fe35cb1eed1fb802510fac447899d919.mp3?version_id=1627—

Categories
Tito

Tito 3

Kutenda Mema

1 Wakumbushe watu kuwanyenyekea watawala na kuwatii wenye mamlaka, wawe tayari kutenda kila lililo jema.

2 Wasimnenee mtu yeyote mabaya, wasiwe wagomvi, bali wawe wapole, wakionyesha unyenyekevu kwa watu wote.

3 Maana sisi wenyewe wakati fulani tulikuwa wajinga, wasiotii, tukiwa watumwa wa tamaa mbaya na anasa za kila aina. Tuliishi katika uovu na wivu, tukichukiwa na kuchukiana sisi kwa sisi.

4 Lakini wema na upendo wa Mungu Mwokozi wetu ulipofunuliwa,

5 alituokoa, si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyotenda, bali kwa sababu ya rehema zake. Alituokoa kwa kutuosha kwa kuzaliwa mara ya pili na kwa kufanywa wapya kwa njia ya Roho Mtakatifu,

6 ambaye Mungu alitumiminia kwa wingi kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu,

7 ili kwamba, tukiisha kuhesabiwa haki kwa neema yake, tupate kuwa warithi tukiwa na tumaini la uzima wa milele.

8 Hili ni neno la kuaminiwa. Nami nataka uyasisitize mambo haya, ili wale ambao wamemwamini Mungu wapate kuwa waangalifu kujitoa kwa ajili ya kutenda mema wakati wote. Mambo haya ni mazuri tena ya manufaa kwa kila mtu.

9 Lakini jiepushe na maswali ya kipuzi, mambo ya koo, mabishano na ugomvi kuhusu sheria, kwa sababu hayana faida, tena ni ubatili.

10 Mtu anayesababisha mafarakano, mwonye mara ya kwanza, kisha mwonye mara ya pili. Baada ya hapo, usihusike naye tena.

11 Kwa kuwa unajua kwamba mtu kama huyo amepotoka na tena ni mwenye dhambi. Yeye amejihukumu mwenyewe.

Maneno Ya Mwisho Na Kumtamkia Baraka

12 Mara nitakapomtuma Artema au Tikiko kwako, jitahidi kuja unione huko Nikopoli, kwa sababu nimeamua kukaa huko wakati wa majira ya baridi.

13 Fanya kila uwezalo uwasafirishe Zena yule mwanasheria na Apolo na uhakikishe kwamba wana kila kitu wanachohitaji katika safari yao.

14 Watu wetu hawana budi kujifunza kutenda mema, ili waweze kuyakimu mahitaji ya kila siku, wasije wakaishi maisha yasiyokuwa na matunda.

15 Wote walio pamoja nami wanakusalimu. Wasalimu wale wanaotupenda katika imani.

Neema iwe nanyi nyote. Amen.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/TIT/3-80400f3cf64f758a550f4806e59753d1.mp3?version_id=1627—

Categories
Filemoni

Filemoni Utangulizi

Utangulizi

Waraka huu mfupi umeainishwa na nyaraka za Waefeso, Wakolosai na Wafilipi kama mojawapo wa nyaraka Paulo alizoandika akiwa gerezani. Aliandikia Filemoni, Afia mwanamke Mkristo (ambaye huenda alikuwa mkewe Filemoni), na Arkipo, na kanisa lililokuwa likikusanyika nyumbani kwa Filemoni.

Onesimo alikuwa mtumwa aliyetoroka kutoka kwa Filemoni huko Kolosai akaenda Rumi, ambako aliokoka. Onesimo, kama mtumwa, alikuwa mali ya Filemoni kisheria.

Mwandishi

Mtume Paulo.

Kusudi

Kumhimiza Filemoni amsamehe Onesimo, mtumwa aliyemtoroka, na amkubali kama ndugu Mkristo katika imani.

Mahali

Rumi.

Tarehe

Kama mwaka wa 60 B.K.

Wahusika Wakuu

Paulo, Filemoni, na Onesimo.

Wazo Kuu

Paulo alimwandikia Filemoni kumshawishi amkubali Onesimo kurudi kwake, na amsamehe aliyomkosea.

Mambo Muhimu

Barua hii ni kielelezo cha ukarimu wa Kikristo. Paulo alishukuru kwa moyo wa ukarimu ambao tayari Filemoni alikuwa ameonyesha kwa Wakristo wenzake. Paulo kwa mamlaka yake ya kitume katika kanisa angeweza kumtaka afanye hivyo kwa Onesimo. Badala yake Paulo aliomba kwa upendo Filemoni ampokee Onesimo.

Mgawanyo

Salamu (

1-3

)

Kuhusika kwa Paulo, na upendo wake (

4-7

)

Paulo kumwombea Onesimo (

8-22

)

Kuagana (

23-25

).

Categories
Filemoni

Filemoni 1

1 Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu, pamoja na Timotheo ndugu yetu:

Kwa Filemoni rafiki yetu mpendwa na mtendakazi mwenzetu,

2 kwa dada yetu mpendwa Afia, kwa Arkipo askari mwenzetu na kwa kanisa lile likutanalo nyumbani mwako:

3 Neema iwe nanyi na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.

Shukrani Na Maombi

4 Siku zote ninamshukuru Mungu ninapokukumbuka katika maombi yangu,

5 kwa sababu ninasikia juu ya imani yako katika Bwana Yesu na upendo wako kwa watakatifu wote.

6 Naomba utiwe nguvu katika kuishuhudia imani yako, ili upate kuwa na ufahamu mkamilifu juu ya kila kitu chema tulicho nacho ndani ya Kristo.

7 Upendo wako umenifurahisha mno na kunitia moyo, kwa sababu wewe ndugu, umeiburudisha mioyo ya watakatifu.

Maombi Ya Paulo Ya Kumtetea Onesimo

8 Hata hivyo, ingawa katika Kristo ningeweza kuwa na ujasiri na kukuagiza yale yakupasayo kutenda,

9 lakini ninakuomba kwa upendo, mimi Paulo, mzee na pia sasa nikiwa mfungwa wa Kristo Yesu,

10 nakuomba kwa ajili ya mwanangu Onesimo,aliyefanyika mwanangu nilipokuwa kwenye minyororo.

11 Mwanzoni alikuwa hakufai, lakini sasa anakufaa sana wewe na mimi pia.

12 Namtuma kwako, yeye aliye moyo wangu hasa.

13 Ningependa nikae naye ili ashike nafasi yako ya kunisaidia wakati huu nikiwa kifungoni kwa ajili ya Injili.

14 Lakini sikutaka kufanya lolote bila idhini yako, ili wema wowote uufanyao usiwe wa lazima, bali wa hiari.

15 Huenda sababu ya yeye kutengwa nawe kwa kitambo kidogo ni ili uwe naye daima.

16 Si kama mtumwa, bali bora kuliko mtumwa, kama ndugu mpendwa. Yeye ni mpendwa sana kwangu na hata kwako zaidi, yeye kama mwanadamu na kama ndugu katika Bwana.

17 Hivyo kama unanihesabu mimi kuwa mshirika wako, mkaribishe kama vile ungenikaribisha mimi mwenyewe.

18 Kama amekukosea lolote au kama unamdai chochote, nidai mimi.

19 Ni mimi Paulo, ninayeandika waraka huu kwa mkono wangu mwenyewe. Nitakulipa. Sitaji kwamba nakudai hata nafsi yako.

20 Ndugu yangu, natamani nipate faida kwako katika Bwana, uuburudishe moyo wangu katika Kristo.

21 Nikiwa na hakika ya utii wako, nakuandikia, nikijua kwamba utafanya hata zaidi ya yale ninayokuomba.

22 Jambo moja zaidi: Niandalie chumba cha wageni, kwa kuwa nataraji kurudishwa kwenu kama jibu la maombi yenu.

Salamu Za Mwisho Na Dua Ya Kuwatakia Heri

23 Epafra, aliye mfungwa mwenzangu katika Kristo Yesu, anakusalimu.

24 Vivyo hivyo Marko, Aristarko, Dema na Luka, watendakazi wenzangu wanakusalimu.

25 Neema ya Bwana Yesu Kristo iwe pamoja na roho zenu. Amen.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PHM/1-c02c81872025eb392b63e975d28ecde5.mp3?version_id=1627—