Categories
Waefeso

Waefeso 5

Kuenenda Nuruni

1 Kwa hiyo, mfuateni Mungu kama watoto wapendwao,

2 mkiishi maisha ya upendo, kama vile Kristo alivyotupenda sisi akajitoa kwa ajili yetu kuwa sadaka yenye harufu nzuri na dhabihu kwa Mungu.

3 Lakini uasherati, usitajwe miongoni mwenu, wala uchafu wa aina yoyote, wala tamaa, kwa sababu mambo haya hayastahili miongoni mwa watakatifu.

4 Wala pasiwepo mazungumzo machafu ya aibu, au maneno ya upuzi au mzaha, ambayo hayafai, badala yake mshukuruni Mungu.

5 Kwa habari ya mambo haya mjue hakika kwamba: Msherati, wala mtu mwovu, wala mwenye tamaa mbaya, mtu kama huyo ni mwabudu sanamu, kamwe hataurithi Ufalme wa Kristo na wa Mungu.

6 Mtu yeyote na asiwadanganye kwa maneno matupu, kwa kuwa hasira ya Mungu huwaka kwa sababu ya mambo kama haya juu ya wale wasiomtii.

7 Kwa hiyo, msishirikiane nao.

8 Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, lakini sasa ninyi ni nuru katika Bwana. Enendeni kama watoto wa nuru

9 (kwa kuwa tunda la nuru hupatikana katika wema wote, haki na kweli),

10 nanyi tafuteni yale yanayompendeza Bwana.

11 Msishiriki matendo ya giza yasiyofaa, bali yafichueni.

12 Kwa maana ni aibu hata kutaja mambo yale ambayo wasiotii wanayafanya sirini.

13 Lakini kila kitu kilichowekwa nuruni, huonekana,

14 kwa kuwa nuru ndiyo hufanya kila kitu kionekane. Hii ndiyo sababu imesemekana:

“Amka, wewe uliyelala,

ufufuke kutoka kwa wafu,

naye Kristo atakuangazia.”

15 Kwa hiyo angalieni sana jinsi mnavyoenenda, si kama watu wasio na hekima, bali kama wenye hekima,

16 mkiukomboa wakati, kwa sababu nyakati hizi ni za uovu.

17 Kwa hiyo msiwe wajinga, bali mpate kujua nini mapenzi ya Bwana.

18 Pia msilewe kwa mvinyo, ambamo ndani yake mna upotovu, bali mjazwe Roho.

19 Msemezane ninyi kwa ninyi kwa zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, mkimwimbia na kumsifu Bwana mioyoni mwenu,

20 siku zote mkimshukuru Mungu Baba kwa kila jambo katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo.

21 Nyenyekeaneni ninyi kwa ninyi kwa heshima kwa ajili ya Kristo.

Mafundisho Kuhusu Wake Na Waume

22 Ninyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana.

23 Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe kama vile Kristo alivyo kichwa cha Kanisa, ambalo ni mwili wake, naye Kristo ni Mwokozi wake.

24 Basi, kama vile Kanisa linavyomtii Kristo, vivyo hivyo na wake nao imewapasa kuwatii waume zao kwa kila jambo.

25 Ninyi waume, wapendeni wake zenu, kama vile Kristo alivyolipenda Kanisa akajitoa kwa ajili yake

26 kusudi alifanye takatifu, akilitakasa kwa kuliosha kwa maji katika Neno lake,

27 apate kujiletea Kanisa tukufu lisilo na doa wala kunyanzi au waa lolote, bali takatifu na lisilo na hatia.

28 Vivyo hivyo imewapasa waume kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe.

29 Hakuna mtu anayeuchukia mwili wake mwenyewe, bali huulisha na kuutunza vizuri, kama Kristo anavyolitunza Kanisa lake.

30 Sisi tu viungo vya mwili wake.

31 “Kwa sababu hii, mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, naye ataambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja.”

32 Siri hii ni kubwa, bali mimi nanena kuhusu Kristo na Kanisa.

33 Hata hivyo, kila mmoja wenu ampende mkewe kama anavyoipenda nafsi yake mwenyewe, naye mke lazima amheshimu mumewe.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/EPH/5-fbf0b82424bfee2a26b8eef58e24dfc6.mp3?version_id=1627—

Categories
Waefeso

Waefeso 6

Mafundisho Kuhusu Watoto Na Wazazi

1 Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, kwa kuwa hili ni jema.

2 “Waheshimu baba yako na mama yako,” hii ndio amri ya kwanza yenye ahadi,

3 “upate baraka na uishi siku nyingi duniani.”

4 Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, bali waleeni kwa nidhamu na mafundisho ya Bwana.

Mafundisho Kuhusu Watumwa Na Mabwana

5 Ninyi watumwa, watiini hao walio mabwana zenu hapa duniani kwa heshima na kwa kutetemeka na kwa moyo mmoja, kama vile mnavyomtii Kristo.

6 Watiini, si tu wakati wakiwaona ili mpate upendeleo wao, bali mtumike kama watumwa wa Kristo, mkifanya mapenzi ya Mungu kwa moyo.

7 Tumikeni kwa moyo wote, kama vile mnamtumikia Bwana na si wanadamu.

8 Mkijua kwamba Bwana atampa kila mtu thawabu kwa lolote jema alilotenda, kama yeye ni mtumwa au ni mtu huru.

9 Nanyi mabwana, watendeeni watumwa wenu kwa jinsi iyo hiyo. Msiwatishe, kwa kuwa mnajua ya kwamba yeye aliye Bwana wenu na Bwana wao yuko mbinguni, naye hana upendeleo.

Silaha Za Mungu

10 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake.

11 Vaeni silaha zote za Mungu ili kwamba mweze kuzipinga hila za ibilisi.

12 Kwa maana kushindana kwetu si juu ya nyama na damu, bali dhidi ya falme, mamlaka, dhidi ya wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.

13 Kwa hiyo vaeni silaha zote za Mungu ili mweze kushindana siku ya uovu itakapokuja nanyi mkiisha kufanya yote, simameni imara.

14 Kwa hiyo simameni imara mkiwa mmejifunga kweli kiunoni na kuvaa dirii ya haki kifuani,

15 nayo miguu yenu ifungiwe utayari tuupatao kwa Injili ya amani.

16 Zaidi ya haya yote, twaeni ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.

17 Vaeni chapeo ya wokovu na mchukue upanga wa Roho, ambao ni Neno la Mungu.

18 Mkiomba kwa Roho siku zote katika sala zote na maombi, mkikesha kila wakati mkiwaombea watakatifu wote.

19 Niombeeni na mimi pia, ili kila nifunguapo kinywa changu, nipewe maneno ya kusema, niweze kutangaza siri ya Injili kwa ujasiri,

20 ambayo mimi ni balozi wake katika vifungo. Ombeni ili nipate kuhubiri kwa ujasiri kama inipasavyo.

Salamu Za Mwisho

21 Tikiko, aliye ndugu mpendwa na mtumishi mwaminifu katika Bwana, atawaambia kila kitu, ili pia mpate kujua hali yangu na kile ninachofanya sasa.

22 Ninamtuma kwenu kwa ajili ya kusudi hili hasa, ili mpate kujua hali yetu, na awatie moyo.

23 Amani iwe kwa ndugu, na pendo pamoja na imani kutoka kwa Mungu Baba na Bwana Yesu Kristo.

24 Neema iwe na wote wampendao Bwana wetu Yesu Kristo kwa upendo wa dhati. Amen.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/EPH/6-ad13160cfa1b084b4fb41d5b64bc2c04.mp3?version_id=1627—

Categories
Wafilipi

Wafilipi Utangulizi

Utangulizi

Paulo alitembelea mji wa Filipi katika safari yake ya pili ya kitume, kutokana na maono aliyoyapata akiwa Troa kumwelezea aelekee Makedonia. Filipi hapakuwa na Sinagogi kwa sababu ya idadi ndogo ya Wayahudi. Kanisa la Filipi lilimpelekea Paulo msaada kupitia kwa Epafrodito. Pia alitumia nafasi hiyo kuelezea matatizo aliyopata huko Rumi. Waumini wote waliambiwa wawe na malengo ya juu kabisa katika maisha yao ya Kikristo, kwa maana Mungu angewatimizia mahitaji yao yote katika maisha. Paulo aliwakazia kufurahi nyakati zote.

Mwandishi

Mtume Paulo.

Kusudi

Kuwashukuru rafiki zake wapendwa waliokuwa wamempelekea msaada kwa ajili ya mahitaji yake. Kuwatia Wafilipi moyo na kuwataka kusimama imara, akiwahimiza wawe na unyenyekevu kama aliokuwa nao Kristo, na pia wawe na umoja.

Mahali

Rumi.

Tarehe

Kama mwaka wa 61 B.K.

Wahusika Wakuu

Paulo, Timotheo, Epafrodito, Euodia na Sintike.

Wazo Kuu

Paulo alisisitiza kuhusu furaha ya muumini katika Kristo.

Mambo Muhimu

Paulo anaagiza waumini kukataa kabisa mafundisho ya uongo na kuwahimiza wafurahi nyakati zote.

Mgawanyo

Paulo na matatizo yake huko Rumi (

1:1-30

)

Mfano wa utii wa Yesu (

2:1-30

)

Mafundisho kuhusu mwenendo wa Mkristo (

3:1-21

)

Amani ya Mungu, na jinsi Mungu anavyowatimizia waumini mahitaji yao (

4:1-23

).

Categories
Wafilipi

Wafilipi 1

Salamu

1 Waraka wa Paulo na Timotheo, watumishi wa Kristo Yesu:

Kwa watakatifu wote katika Kristo Yesu walioko Filipi, pamoja na waangalizi na mashemasi:

2 Neema na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi.

Shukrani Na Maombi

3 Ninamshukuru Mungu wangu kila niwakumbukapo ninyi.

4 Katika maombi yangu yote daima nimekuwa nikiwaombea ninyi nyote kwa furaha,

5 kwa sababu ya kushiriki kwenu katika kueneza Injili, tangu siku ya kwanza hadi leo.

6 Nina hakika kwamba yeye aliyeianza kazi njema mioyoni mwenu, ataiendeleza na kuikamilisha hata siku ya Kristo Yesu.

7 Ni haki na ni wajibu wangu kufikiri hivi juu yenu nyote, kwa sababu ninyi mko moyoni mwangu. Ikiwa nimefungwa au nikiwa ninaitetea na kuithibitisha Injili, ninyi nyote mnashiriki neema ya Mungu pamoja nami.

8 Mungu ni shahidi wangu jinsi ninavyowaonea shauku ninyi nyote kwa huruma ya Kristo Yesu.

9 Haya ndiyo maombi yangu: kwamba upendo wenu uongezeke zaidi na zaidi katika maarifa na ufahamu wote,

10 ili mpate kutambua yale yaliyo mema, mkawe safi, wasio na hatia hadi siku ya Kristo,

11 mkiwa mmejawa na matunda ya haki yapatikanayo kwa njia ya Yesu Kristo, kwa utukufu na sifa za Mungu.

Kufungwa Kwa Paulo Kwaieneza Injili

12 Basi, ndugu zangu, nataka mjue kwamba mambo yale yaliyonipata kwa kweli yamesaidia sana kueneza Injili.

13 Matokeo yake ni kwamba imejulikana wazi kwa walinzi wote wa jumba la kifalme na kwa wengine wote kuwa nimefungwa kwa ajili ya Kristo.

14 Kwa sababu ya vifungo vyangu, ndugu wengi katika Bwana wametiwa moyo kuhubiri neno la Mungu kwa ujasiri zaidi na bila woga.

15 Ni kweli kwamba wengine wanamhubiri Kristo kutokana na wivu na kwa kutaka kushindana, lakini wengine wanamhubiri Kristo kwa nia njema.

16 Hawa wa mwisho wanamhubiri Kristo kwa moyo wa upendo, wakifahamu kwamba nimo humu gerezani kwa ajili ya kuitetea Injili.

17 Hao wa kwanza wanamtangaza Kristo kutokana na tamaa zao wenyewe wala si kwa moyo mweupe, bali wanakusudia kuongeza mateso yangu katika huku kufungwa kwangu.

18 Lakini inadhuru nini? Jambo la muhimu ni kwamba kwa kila njia, ikiwa ni kwa nia mbaya au njema, Kristo anahubiriwa. Nami kwa ajili ya jambo hilo ninafurahi.

Naam, nami nitaendelea kufurahi,

19 kwa maana ninajua kwamba kwa maombi yenu na kwa msaada unaotolewa na Roho wa Yesu Kristo, yale yaliyonipata mimi yatageuka kuwa wokovu wangu.

20 Ninatarajia kwa shauku kubwa na kutumaini kwamba sitaaibika kwa njia yoyote, bali nitakuwa na ujasiri wa kutosha ili sasa kama wakati mwingine wowote, Kristo atukuzwe katika mwili wangu, ikiwa ni kwa kuishi au kwa kufa.

21 Kwa maana kwangu mimi, kuishi ni Kristo, na kufa ni faida.

22 Kama nitaendelea kuishi katika mwili, kwangu hili ni kwa ajili ya matunda ya kazi. Lakini sijui nichague lipi? Mimi sijui!

23 Ninavutwa kati ya mambo mawili: Ninatamani kuondoka nikakae pamoja na Kristo, jambo hilo ni bora zaidi.

24 Lakini kwa sababu yenu ni muhimu zaidi mimi nikiendelea kuishi katika mwili.

25 Kwa kuwa nina matumaini haya, ninajua kwamba nitaendelea kuwepo na kuwa pamoja nanyi nyote, ili mpate kukua na kuwa na furaha katika imani.

26 Ili kwamba furaha yenu iwe nyingi katika Kristo Yesu kwa ajili yangu kwa kule kuja kwangu kwenu tena.

Kuenenda Ipasavyo Injili

27 Lakini lolote litakalotukia, mwenende kama ipasavyo Injili ya Kristo, ili kwamba nikija na kuwaona au ikiwa sipo, nipate kusikia haya juu yenu: Kuwa mnasimama imara katika roho moja, mkiishindania imani ya Injili kwa umoja,

28 wala msitishwe na wale wanaowapinga. Hii ni ishara kwao kuwa wataangamia, lakini ninyi mtaokolewa, na hii ni kazi ya Mungu.

29 Kwa maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, bali pia kuteswa kwa ajili yake,

30 kwa kuwa mnashiriki mashindano yale yale mliyoyaona nikiwa nayo na ambayo hata sasa mnasikia kuwa bado ninayo.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PHP/1-b7aafafa48e28b75ebb7020107e60715.mp3?version_id=1627—

Categories
Wafilipi

Wafilipi 2

Kuiga Unyenyekevu Wa Kristo

1 Kama kukiwa na jambo lolote la kutia moyo katika kuunganishwa na Kristo, kukiwa faraja yoyote katika upendo wake, kukiwa na ushirika wowote na Roho, kukiwa na wema wowote na huruma,

2 basi ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na nia moja, mkiwa na upendo huo moja, mkiwa wa roho na kusudi moja.

3 Msitende jambo lolote kwa nia ya kujitukuza wala kujivuna, bali kwa unyenyekevu kila mtu amhesabu mwingine bora kuliko nafsi yake.

4 Kila mmoja wenu asiangalie faida yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine.

5 Kuweni na nia ile ile aliyokuwa nayo Kristo Yesu:

6 Yeye, ingawa alikuwa na asili ya Mungu hasa,

hakuona kule kuwa sawa na Mungu

kuwa kitu cha kushikilia,

7 bali alijifanya si kitu,

akachukua hali hasa na mtumwa,

naye akazaliwa katika umbo la mwanadamu.

8 Naye akiwa na umbo la mwanadamu,

alijinyenyekeza, akatii hata mauti:

naam, mauti ya msalaba!

9 Kwa hiyo, Mungu alimtukuza juu sana,

na kumpa Jina lililo kuu kuliko kila jina,

10 ili kwa Jina la Yesu, kila goti lipigwe,

la vitu vya mbinguni, na vya duniani,

na vya chini ya nchi,

11 na kila ulimi ukiri ya kwamba

Yesu Kristo ni Bwana,

kwa utukufu wa Mungu Baba.

Ngʼaeni Kama Mianga Katika Ulimwengu

12 Kwa hiyo, wapenzi wangu, kama vile ambavyo mmekuwa mkitii siku zote, si tu wakati nikiwa pamoja nanyi, bali sasa zaidi sana nisipokuwepo, utimizeni wokovu wenu kwa kuogopa na kutetemeka,

13 kwa maana Mungu ndiye atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu kwa kulitimiza kusudi lake jema.

14 Fanyeni mambo yote bila kunungʼunika wala kushindana,

15 ili msiwe na lawama wala hatia, bali mwe wana wa Mungu wasio na kasoro katika kizazi chenye ukaidi na kilichopotoka, ambacho ndani yake ninyi mnangʼaa kama mianga ulimwenguni.

16 Mkilishika neno la uzima, ili nipate kuona fahari siku ya Kristo kwamba sikupiga mbio wala kujitaabisha bure.

17 Lakini hata kama nikimiminwa kama sadaka ya kinywaji kwenye dhabihu na huduma itokayo katika imani yenu, mimi ninafurahi na kushangilia pamoja nanyi nyote.

18 Vivyo hivyo, ninyi nanyi imewapasa kufurahi na kushangilia pamoja nami.

Paulo Amsifu Timotheo

19 Natumaini katika Bwana Yesu kumtuma Timotheo hivi karibuni aje kwenu, ili nipate kufarijika moyo nitakapopata habari zenu.

20 Sina mtu mwingine kama yeye, ambaye ataangalia hali yenu kwa halisi.

21 Kwa maana kila mmoja anajishughulisha zaidi na mambo yake mwenyewe wala si yale ya Yesu Kristo.

22 Lakini ninyi wenyewe mnajua jinsi Timotheo alivyojithibitisha mwenyewe, kwa maana ametumika pamoja nami kwa kazi ya Injili, kama vile mwana kwa baba yake.

23 Kwa hiyo, ninatumaini kumtuma kwenu upesi mara nitakapojua mambo yangu yatakavyokuwa.

24 Nami mwenyewe ninatumaini katika Bwana kwamba nitakuja kwenu hivi karibuni.

Paulo Amsifu Epafrodito

25 Lakini nadhani ni muhimu kumtuma tena kwenu Epafrodito, ndugu yangu na mtendakazi pamoja nami, aliye askari mwenzangu, ambaye pia ni mjumbe wenu mliyemtuma ili ashughulike na mahitaji yangu.

26 Kwa maana amekuwa akiwaonea sana shauku ninyi nyote, akiwa na wasiwasi kwa kuwa mlisikia kwamba alikuwa mgonjwa.

27 Kweli alikuwa mgonjwa, tena karibu ya kufa. Lakini Mungu alimhurumia, wala si yeye tu, bali hata na mimi alinihurumia, nisipatwe na huzuni juu ya huzuni.

28 Kwa hiyo mimi ninafanya bidii kumtuma kwenu ili mtakapomwona kwa mara nyingine, mpate kufurahi, nami wasiwasi wangu upungue.

29 Kwa hiyo mpokeeni katika Bwana kwa furaha kubwa, nanyi wapeni heshima watu kama hawa,

30 kwa sababu alikaribia kufa kwa ajili ya kazi ya Kristo, akihatarisha maisha yake ili aweze kunihudumia vile ninyi hamkuweza.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PHP/2-c4c4f604b469dca9baebdfea358fe437.mp3?version_id=1627—

Categories
Wafilipi

Wafilipi 3

Hakuna Tumaini Katika Mwili

1 Hatimaye, ndugu zangu, furahini katika Bwana! Mimi kuwaandikia mambo yale yale hakuniudhi, kwa maana ni kinga kwa ajili yenu.

2 Jihadharini na mbwa, wale watenda maovu, jihadharini na wale wajikatao miili yao, wasemao ili kuokoka ni lazima kutahiriwa.

3 Kwa maana sisi ndio tulio tohara, sisi tumwabuduo Mungu katika Roho, tunaona fahari katika Kristo Yesu, ambao hatuweki tumaini letu katika mwili,

4 ingawa mimi mwenyewe ninazo sababu za kuutumainia mwili.

Kama mtu yeyote akidhani anazo sababu za kuutumainia mwili, mimi zaidi.

5 Nilitahiriwa siku ya nane, mimi ni Mwisraeli wa kabila la Benyamini, Mwebrania wa Waebrania. Kwa habari ya sheria, ni Farisayo,

6 kwa habari ya juhudi, nilikuwa nalitesa kanisa, kuhusu haki ipatikanayo kwa sheria, mimi nilikuwa sina hatia.

7 Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, sasa nayahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo.

8 Zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara tupu nikiyalinganisha na faida kubwa ipitayo kiasi cha kumjua Kristo Yesu Bwana wangu, ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote, nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nimpate Kristo.

9 Nami nionekane mbele zake bila kuwa na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu kwa njia ya imani.

10 Nataka nimjue Kristo na uweza wa kufufuka kwake na ushirika wa mateso yake, ili nifanane naye katika mauti yake,

11 ili kwa njia yoyote niweze kufikia ufufuo wa wafu.

Kukaza Mwendo Ili Kufikia Lengo

12 Si kwamba nimekwisha kufikia, au kwamba nimekwisha kuwa mkamilifu, la hasha! Bali nakaza mwendo ili nipate kile ambacho kwa ajili yake, nimeshikwa na Kristo Yesu.

13 Ndugu zangu, sijihesabu kuwa nimekwisha kushika. Lakini ninafanya jambo moja: Ninasahau mambo yale yaliyopita, nakaza mwendo kufikia yale yaliyo mbele.

14 Nakaza mwendo nifikie ile alama ya ushindi iliyowekwa ili nipate tuzo ya mwito mkuu wa Mungu ambao nimeitiwa huko juu mbinguni katika Kristo Yesu.

15 Hivyo sisi sote tuliokuwa kiroho tuwaze jambo hili, hata mkiwaza mengine katika jambo lolote, Mungu ataliweka wazi hilo nalo.

16 Lakini na tushike sana lile ambalo tumekwisha kulifikia.

17 Ndugu zangu, kwa pamoja fuateni mfano wangu na kuwatazama wale wanaofuata kielelezo tulichowawekea.

18 Kwa maana, kama nilivyokwisha kuwaambia mara nyingi kabla, nami sasa nasema tena hata kwa machozi, watu wengi wanaishi kama adui wa msalaba wa Kristo.

19 Mwisho wa watu hao ni maangamizi, Mungu wao ni tumbo, na utukufu wao ni aibu, na mawazo yao yamo katika mambo ya dunia.

20 Lakini uenyeji wetu uko mbinguni. Nasi tunamngoja kwa shauku Mwokozi kutoka huko, yaani, Bwana Yesu Kristo,

21 atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, ili upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote chini yake.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PHP/3-945354f8780b4743617c17627c857b09.mp3?version_id=1627—

Categories
Wafilipi

Wafilipi 4

1 Kwa hiyo, ndugu zangu, ninaowapenda na ambao ninawaonea shauku, ninyi mlio furaha yangu na taji yangu, hivi ndivyo iwapasavyo kusimama imara katika Bwana, ninyi wapenzi wangu.

Mausia

2 Nawasihi Euodia na Sintike wawe na nia moja katika Bwana.

3 Naam, nakusihi wewe pia, mwenzangu mwaminifu, uwasaidie hawa wanawake, kwa sababu walijitaabisha katika kazi ya Injili pamoja nami bega kwa bega, wakiwa pamoja na Klementi na watendakazi wenzangu ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima.

4 Furahini katika Bwana siku zote, tena nasema furahini!

5 Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu.

6 Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.

7 Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.

8 Hatimaye, ndugu zangu, mambo yote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo na sifa njema, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote ya kupendeza, yoyote yenye staha, ukiwepo uzuri wowote, pakiwepo chochote kinachostahili kusifiwa, tafakarini mambo hayo.

9 Mambo yote mliyojifunza au kuyapokea au kuyasikia kutoka kwangu, au kuyaona kwangu, yatendeni hayo. Naye Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.

Shukrani Kwa Matoleo Yenu

10 Nina furaha kubwa katika Bwana kwamba hatimaye mmeanza upya kushughulika tena na maisha yangu. Kweli mmekuwa mkinifikiria lakini mlikuwa hamjapata nafasi ya kufanya hivyo.

11 Sisemi hivyo kwa vile nina mahitaji, la! Kwa maana nimejifunza kuridhika katika hali yoyote.

12 Ninajua kupungukiwa, pia ninajua kuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuridhika katika kila hali, wakati wa kushiba na wakati wa kuona njaa, wakati wa kuwa na vingi na wakati wa kupungukiwa.

13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.

14 Lakini, mlifanya vyema kushiriki nami katika taabu zangu.

15 Zaidi ya hayo, ninyi Wafilipi mnajua kwamba siku za kwanza nilipoanza kuhubiri Injili, nilipoondoka Makedonia, hakuna kanisa jingine lililoshiriki nami katika masuala ya kutoa na kupokea isipokuwa ninyi.

16 Kwa maana hata nilipokuwa huko Thesalonike, mliniletea msaada kwa ajili ya mahitaji yangu zaidi ya mara moja.

17 Si kwamba natafuta sana yale matoleo, bali natafuta sana ile faida itakayozidi sana kwa upande wenu.

18 Nimelipwa kikamilifu hata na zaidi; nimetoshelezwa kabisa sasa, kwa kuwa nimepokea kutoka kwa Epafrodito vile vitu mlivyonitumia, sadaka yenye harufu nzuri, dhabihu inayokubalika na ya kumpendeza Mungu.

19 Naye Mungu wangu atawajaza ninyi na kila mnachohitaji kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu ndani ya Kristo Yesu.

20 Mungu wetu aliye Baba yetu apewe utukufu milele na milele. Amen.

Salamu Za Mwisho

21 Msalimuni kila mtakatifu katika Kristo Yesu. Ndugu walioko pamoja nami wanawasalimu.

22 Watakatifu wote wanawasalimu, hasa wale watu wa nyumbani mwa Kaisari.

23 Neema ya Bwana Yesu Kristo iwe pamoja na roho zenu. Amen.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PHP/4-14544951b0432ee787978db780199908.mp3?version_id=1627—

Categories
Wakolosai

Wakolosai Utangulizi

Utangulizi

Nyaraka za Waefeso na Wakolosai zinaitwa pacha kwa sababu mambo yaliyomo yanafanana. Timotheo alishirikiana na Paulo huko Rumi katika kuandika nyaraka hizi mbili. Hivyo Wakolosai ni mojawapo ya nyaraka za gerezani. Tikiko ndiye alipeleka waraka huu huko Kolosai.

Mji wa Kolosai ulikuwa umejengwa kama kilomita 160 kutoka Efeso kwenye Bonde la Lika, karibu na Hierapoli na Laodikia. Kwa kadiri ionekanavyo, Paulo alikuwa hajautembelea mji wa Kolosai, ila mji huu ulihubiriwa Injili na Epafra wakati Paulo alikuwa Efeso. Paulo alipata kuwafahamu waumini hawa akiwa Efeso katika safari yake ya pili ya kueneza Injili. Sasa alikuwa na wasiwasi kwa sababu alisikia kuwa mafundisho ya Unostiki yalikuwa yameingia katika kanisa hilo. Mafundisho haya yalikuwa yakiuelekeza ujumbe wa Injili hatarini.

Mwandishi

Mtume Paulo.

Kusudi

Kupinga mafundisho ya uzushi katika kanisa, na kuwaonyesha waumini kwamba wana kila kitu wanachokihitaji katika Kristo.

Mahali

Rumi.

Tarehe

Kama 60 B.K.

Wahusika Wakuu

Paulo, Timotheo, Tikiko, Onesimo, Aristarko, Marko, na Epafra.

Wazo Kuu

Kuthibitisha utoshelevu wa Kristo, ukilinganishwa na utupu wa filosofia ya mwanadamu.

Mambo Muhimu

Mambo yaliyokuwa yakiwasumbua Wakolosai: Mchanganyiko wa elimu ya nyota, uchawi, na mafundisho ya Unostiki ambayo yalisema kwamba Kristo alikuwa sawa na malaika.

Mgawanyo

Salamu na shukrani za Paulo (

1:1-8

)

Yesu Kristo na waumini (

1:9–2:7

)

Hatari kuhusu mafundisho ya uongo (

2:8-23

)

Mafundisho kuhusu maisha ya Kikristo (

3:1–4:1

)

Maagizo kuhusu kuomba, na mausia ya mwisho (

4:2-18

).

Categories
Wakolosai

Wakolosai 1

Salamu

1 Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo ndugu yetu:

2 Kwa ndugu watakatifu na waaminifu katika Kristo, waishio Kolosai:

Neema na amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu ziwe nanyi.

Shukrani Na Maombi

3 Siku zote tunamshukuru Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, tunapowaombea ninyi,

4 kwa sababu tumesikia kuhusu imani yenu katika Kristo Yesu, na upendo wenu mlio nao kwa watakatifu wote:

5 imani na upendo ule utokao katika tumaini mlilowekewa akiba mbinguni, na ambalo mmesikia habari zake katika neno la kweli, yaani, ile Injili

6 iliyowafikia ninyi. Duniani kote Injili hii inazaa matunda na kuenea kama ilivyokuwa kwenu tangu siku ile mlipoisikia na kuielewa neema ya Mungu katika kweli yote.

7 Mlijifunza habari zake kutoka kwa Epafra, mtumishi mwenzetu mpendwa, yeye aliye mhudumu mwaminifu wa Kristo kwa ajili yenu,

8 ambaye pia ametuambia kuhusu upendo wenu katika Roho.

9 Kwa sababu hii, tangu siku ile tuliposikia habari zenu, hatujakoma kuomba kwa ajili yenu na kumsihi Mungu awajaze ninyi maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote ya kiroho na ufahamu.

10 Nasi tunaomba haya ili mpate kuishi maisha yanayostahili mbele za Bwana, na mpate kumpendeza kwa kila namna: mkizaa matunda kwa kila kazi njema, mkikua katika kumjua Mungu,

11 mkiwa mmetiwa nguvu kwa uwezo wote kwa kadiri ya nguvu yake yenye utukufu, ili mpate kuwa na wingi wa saburi na uvumilivu. Nanyi kwa furaha

12 mkimshukuru Baba, ambaye amewastahilisha kushiriki katika urithi wa watakatifu katika ufalme wa nuru.

13 Kwa maana ametuokoa kutoka ufalme wa giza na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wake mpendwa,

14 ambaye katika yeye tunao ukombozi, yaani msamaha wa dhambi.

Ukuu Wa Kristo

15 Yeye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.

16 Kwake yeye vitu vyote vilivyoko mbinguni na juu ya nchi viliumbwa: vitu vinavyoonekana na visivyoonekana, viwe ni viti vya enzi au falme, au wenye mamlaka au watawala; vitu vyote viliumbwa na yeye na kwa ajili yake.

17 Yeye alikuwepo kabla ya vitu vyote, na katika yeye vitu vyote vinashikamana pamoja.

18 Yeye ndiye kichwa cha mwili, yaani kanisa, naye ndiye mwanzo na mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu, ili yeye awe mkuu katika vitu vyote.

19 Kwa kuwa ilimpendeza Mungu kwamba utimilifu wake wote ukae ndani yake,

20 na kwa njia yake aweze kuvipatanisha vitu vyote na yeye mwenyewe, viwe ni vitu vilivyo duniani au vilivyo mbinguni, kwa kufanya amani kwa damu yake, iliyomwagika msalabani.

21 Hapo kwanza mlikuwa mmetengana na Mungu, na mlikuwa adui zake katika nia zenu kwa sababu ya mienendo yenu mibaya.

22 Lakini sasa Mungu amewapatanisha ninyi kwa njia ya mwili wa Kristo kupitia mauti, ili awalete mbele zake mkiwa watakatifu, bila dosari wala lawama,

23 ikiwa mnaendelea katika imani yenu mkiwa imara na thabiti, pasipo kuliacha tumaini lililoahidiwa katika Injili. Hii ndiyo ile Injili mliyoisikia, ambayo imehubiriwa kwa kila kiumbe chini ya mbingu, na ambayo mimi Paulo nimekuwa mtumwa wake.

Taabu Ya Paulo Kwa Ajili Ya Kanisa

24 Sasa nafurahia kule kuteseka kwangu kwa ajili yenu, na katika mwili wangu ninatimiliza yale yaliyopungua katika mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake, ambao ni kanisa.

25 Mimi nimekuwa mtumishi wa kanisa kwa wajibu alionipa Mungu ili kuwaletea ninyi Neno la Mungu kwa ukamilifu:

26 Hii ni siri iliyokuwa imefichika tangu zamani na kwa vizazi vingi, lakini sasa imefunuliwa kwa watakatifu.

27 Kwao, Mungu amechagua kujulisha miongoni mwa watu wa Mataifa utukufu wa utajiri wa siri hii, ambayo ni Kristo ndani yenu, tumaini la utukufu.

28 Yeye ndiye tunayemtangaza, tukimwonya kila mtu na kumfundisha kila mtu kwa hekima yote ili tuweze kumleta kila mmoja akiwa amekamilika katika Kristo.

29 Kwa ajili ya jambo hili, ninajitaabisha, nikijitahidi kwa kadiri ya nguvu zake ambazo hutenda kazi ndani yangu kwa uweza mwingi.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/COL/1-5e7586a32e83046f918bf14979237821.mp3?version_id=1627—

Categories
Wakolosai

Wakolosai 2

1 Nataka mjue jinsi ninavyojitaabisha kwa ajili yenu na kwa ajili ya wale walioko Laodikia, na pia kwa ajili ya wote ambao hawajapata kuniona mimi binafsi.

2 Kusudi langu ni watiwe moyo na kuunganishwa katika upendo, ili wapate ule utajiri wa ufahamu mkamilifu, ili waijue siri ya Mungu, yaani, Kristo mwenyewe,

3 ambaye ndani yake kumefichwa hazina zote za hekima na maarifa.

4 Nawaambia mambo haya ili mtu yeyote asiwadanganye kwa maneno ya kuwashawishi.

5 Kwa kuwa ingawa mimi siko pamoja nanyi kimwili, lakini niko pamoja nanyi kiroho, nami nafurahi kuuona utaratibu wenu na jinsi uthabiti wa imani yenu katika Kristo ulivyo.

Ukamilifu Wa Maisha Katika Kristo

6 Hivyo basi, kama vile mlivyompokea Kristo Yesu kuwa Bwana, endeleeni kukaa ndani yake,

7 mkiwa na mizizi, na mmejengwa ndani yake, mkiimarishwa katika imani kama mlivyofundishwa, na kufurika kwa wingi wa shukrani.

8 Angalieni mtu yeyote asiwafanye ninyi mateka kwa elimu batili na madanganyo matupu yanayotegemea mapokeo ya wanadamu na mafundisho ya ulimwengu badala ya Kristo.

9 Maana ukamilifu wote wa Uungu umo ndani ya Kristo katika umbile la mwili wa kibinadamu,

10 nanyi mmepewa ukamilifu ndani ya Kristo, ambaye ndiye mkuu juu ya kila enzi na kila mamlaka.

11 Katika Kristo pia mlitahiriwa kwa kutengwa mbali na asili ya dhambi, si kwa tohara inayofanywa kwa mikono ya wanadamu, bali kwa ile tohara iliyofanywa na Kristo,

12 mkiwa mmezikwa pamoja naye katika ubatizo, na kufufuliwa pamoja naye kwa njia ya imani yenu katika uweza wa Mungu, aliyemfufua kutoka kwa wafu.

13 Mlipokuwa wafu katika dhambi zenu na kutokutahiriwa katika asili yenu ya dhambi, Mungu aliwafanya mwe hai pamoja na Kristo. Alitusamehe dhambi zetu zote,

14 akiisha kuifuta ile hati yenye mashtaka yaliyokuwa yanatukabili, pamoja na maagizo yake. Aliiondoa isiwepo tena, akiigongomea kwenye msalaba wake.

15 Mungu akiisha kuzivua enzi na mamlaka, alizifanya kuwa kitu cha fedheha hadharani kwa kuziburura kwa ujasiri, akizishinda katika msalaba wa Kristo.

16 Kwa hiyo mtu asiwahukumu ninyi kuhusu vyakula au vinywaji, au kuhusu kuadhimisha sikukuu za dini, au Sikukuu za Mwezi Mwandamo au siku ya Sabato.

17 Hizi zilikuwa kivuli cha mambo ambayo yangekuja, lakini ile iliyo halisi imo ndani ya Kristo.

18 Mtu yeyote asiwaondolee thawabu yenu kwa kusisitiza kunyenyekea kwake na kuabudu malaika. Mtu kama huyo hudumu katika maono yake, akijivuna bila sababu katika mawazo ya kibinadamu.

19 Yeye amepoteza ushirikiano na Kichwa, ambaye kutoka kwake mwili wote unalishwa na kushikamanishwa pamoja kwa viungo na mishipa, nao hukua kwa ukuaji utokao kwa Mungu.

Maonyo Dhidi Ya Walimu Wa Uongo

20 Kwa kuwa mlikufa pamoja na Kristo, mkayaacha yale mafundisho ya msingi ya ulimwengu huu, kwa nini bado mnaishi kama ninyi ni wa ulimwengu? Kwa nini mnajitia chini ya amri:

21 “Msishike! Msionje! Msiguse!”?

22 Haya yote mwisho wake ni kuharibika yanapotumiwa, kwa sababu msingi wake ni katika maagizo na mafundisho ya wanadamu.

23 Kwa kweli amri kama hizo huonekana kama zina hekima, katika namna za ibada walizojitungia wenyewe, na unyenyekevu wa uongo na kuutawala mwili kwa ukali, lakini hayafai kitu katika kuzuia tamaa za mwili.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/COL/2-984a4793f812cb1e7c5e7330e2a37cc8.mp3?version_id=1627—