Categories
Wagalatia

Wagalatia 2

Paulo Akubaliwa Na Mitume

1 Kisha, baada ya miaka kumi na minne, nilipanda tena kwenda Yerusalemu pamoja na Barnaba, nikamchukua na Tito ili awe pamoja nami.

2 Nilikwenda kwa sababu nilikuwa nimefunuliwa na Mungu, ili nikawaeleze kwa faragha wale walioonekana kuwa viongozi, ile Injili ninayoihubiri kwa watu wa Mataifa. Nilifanya hivyo kwa kuhofia kwamba nisije nikawa nilikuwa ninakimbia au nilikimbia bure.

3 Lakini hata Tito ambaye alikuwa Myunani, hakulazimika kutahiriwa.

4 Lakini kwa sababu ya ndugu wa uongo ambao walijiingiza kwa siri katikati yetu ili kupeleleza uhuru wetu tulio nao katika Kristo Yesu, wapate kututia utumwani,

5 hatukukubaliana nao hata dakika moja, ili kwamba ukweli wa Injili ubaki nanyi.

6 Kwa habari ya wale waliokuwa wakubaliwe kuwa viongozi (kwangu mimi sikujali vyeo vyao, maana Mungu hana upendeleo), wale watu hawakuniongezea chochote.

7 Badala yake walitambua kwamba nilikuwa nimekabidhiwa kazi ya kuhubiri Injili kwa watu wa Mataifa, kama vile Petro alivyokabidhiwa kuhubiri Injili kwa Wayahudi.

8 Kwa maana, Mungu aliyekuwa akitenda kazi katika huduma ya Petro kama mtume kwa Wayahudi, ndiye pia aliyekuwa anatenda kazi katika huduma yangu kama mtume kwa watu wa Mataifa.

9 Basi, Yakobo, Kefana Yohana, walioonekana kama nguzo za kanisa, walitupa mkono wa shirika, mimi na Barnaba walipotambua ile neema niliyopewa. Wakakubali kwamba sisi twende kwa watu wa Mataifa na wao waende kwa Wayahudi.

10 Walichotuomba ni kwamba tuendelee kuwakumbuka maskini, jambo ambalo ndilo nililokuwa na shauku ya kulifanya.

Paulo Ampinga Petro Huko Antiokia

11 Lakini Petro alipofika Antiokia, mimi nilimpinga ana kwa ana kwa sababu alikuwa amekosea kwa wazi.

12 Kabla baadhi ya watu waliotoka kwa Yakobo hawajafika, alikuwa akila pamoja na watu wa Mataifa. Lakini hao watu walipofika alianza kujiondoa na kujitenga na watu wa Mataifa kwa sababu aliwaogopa wale wa kundi la tohara.

13 Pia Wayahudi wengine waliungana naye katika unafiki huu, hata Barnaba naye akapotoshwa na unafiki wao.

14 Nilipoona kwamba hawatendi sawasawa na kweli ya Injili, nilimwambia Petro mbele ya wote, “Wewe ni Myahudi, nawe unaishi kama mtu wa Mataifa na wala si kama Myahudi. Imekuwaje basi, mnawalazimisha watu wa Mataifa kufuata desturi za Kiyahudi?

Wayahudi Na Watu Wa Mataifa Wanaokolewa Kwa Imani

15 “Sisi wenyewe ni Wayahudi kwa kuzaliwa na si watu wenye dhambi kama watu wa Mataifa,

16 bado tunajua ya kwamba mtu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria bali kwa njia ya imani katika Yesu Kristo. Hivyo sisi pia, tumemwamini Kristo Yesu ili tupate kuhesabiwa haki kwa njia ya imani katika Kristo, wala si kwa matendo ya sheria, kwa sababu kwa kushika sheria hakuna hata mtu mmoja atakayehesabiwa haki.

17 “Lakini tukitafuta kuhesabiwa haki katika Kristo, inakuwa dhahiri kwamba sisi ni wenye dhambi. Je, ina maana kwamba Kristo amekuwa mtumishi wa dhambi? La hasha!

18 Lakini ikiwa mimi ninajenga tena kile ambacho nimekwisha kukibomoa, basi ninaonyesha kwamba mimi ni mkosaji.

19 Kwa maana mimi kwa njia ya sheria, nimeifia sheria ili nipate kuishi kwa ajili ya Mungu.

20 Nimesulubiwa pamoja na Kristo, wala si mimi tena ninayeishi, bali Kristo ndiye aishiye ndani yangu. Uhai nilio nao sasa katika mwili, ninaishi kwa imani ya Mwana wa Mungu, aliyenipenda na kujitoa kwa ajili yangu.

21 Siibatilishi neema ya Mungu, kwa maana kama haki ingeweza kupatikana kwa njia ya sheria, basi Kristo alikufa bure!”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/GAL/2-7872fb98b94c1694841c8c00bf7bd0f6.mp3?version_id=1627—

Categories
Wagalatia

Wagalatia 3

Imani Au Kushika Sheria?

1 Ninyi Wagalatia wajinga! Ni nani aliyewaroga? Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele yenu kwamba amesulubiwa.

2 Nataka nijifunze neno moja kutoka kwenu: Je, mlipokea Roho wa Mungu kwa kushika sheria, au kwa kuyaamini yale mliyosikia?

3 Je, ninyi ni wajinga kiasi hicho? Baada ya kuanza kwa Roho, je, sasa mwataka kumalizia katika mwili?

4 Je, mlipata mateso kiasi hicho bure? Ni kama kweli yalikuwa bure!

5 Je, Mungu huwapa Roho wake na kufanya miujiza katikati yenu kwa sababu mnatii sheria, au kwa sababu mnaamini kile mlichosikia?

6 Kama vile “Abrahamu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki.”

7 Fahamuni basi kwamba wale walio na imani, hao ndio watoto wa Abrahamu.

8 Maandiko yakitabiri kwamba Mungu angewahesabia haki watu wa Mataifa kwa imani, alitangulia kumtangazia Abrahamu Injili akisema kwamba, “Kwa kupitia kwako mataifa yote yatabarikiwa.”

9 Kwa sababu hii, wale wote wanaoamini wanabarikiwa pamoja na Abrahamu, mtu wa imani.

Sheria Na Laana

10 Kwa maana wote wanaotumainia matendo ya sheria wako chini ya laana, kwa kuwa imeandikwa, “Alaaniwe kila mtu asiyeshikilia kutii mambo yote yaliyoandikwa katika Kitabu cha Sheria.”

11 Basi ni dhahiri kwamba hakuna mtu anayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa kushikilia sheria, kwa maana, “Mwenye haki ataishi kwa imani.”

12 Lakini sheria haitegemei imani. Kinyume chake, “Mtu atendaye matendo hayo ataishi kwa hayo.”

13 Kristo alitukomboa kutoka laana ya sheria kwa kufanyika laana kwa ajili yetu, kwa maana imeandikwa, “Amelaaniwa yeye aangikwaye juu ya mti.”

14 Alitukomboa ili kwamba baraka aliyopewa Abrahamu ipate kuwafikia watu wa Mataifa kwa njia ya Kristo Yesu, ili kwa imani tupate kupokea ile ahadi ya Roho.

Sheria Na Ahadi

15 Ndugu zangu, nataka nitoe mfano kutoka maisha ya kila siku. Kama vile hakuna mtu awezaye kutangua au kuongeza kitu katika agano la mtu ambalo limekwisha kuthibitishwa, vivyo hivyo kwa hali kama hii.

16 Ahadi zilinenwa kwa Abrahamu na kwa mzao wake. Maandiko hayasemi “kwa wazao,” likimaanisha watu wengi, bali “kwa mzao wako,” yaani mtu mmoja, ndiye Kristo.

17 Ninachotaka kusema ni kwamba, sheria, ambayo ilitolewa miaka 430 baadaye, haitangui Agano lililothibitishwa na Mungu ili kuibatilisha ahadi ile.

18 Kwa maana kama urithi hupatikana kwa sheria, basi hautegemei tena ahadi, lakini Mungu kwa neema yake alimpa Abrahamu urithi kwa njia ya ahadi.

Kusudi La Sheria

19 Kwa nini basi iwepo sheria? Sheria iliwekwa kwa sababu ya makosa mpaka atakapokuja yule Mzao wa Abrahamu, ambaye alitajwa katika ile ahadi. Sheria iliamriwa na malaika kwa mkono wa mpatanishi.

20 Basi mpatanishi huhusisha zaidi ya upande mmoja, lakini Mungu ni mmoja.

21 Je basi, sheria inapingana na ahadi za Mungu? La hasha! Kwa maana kama sheria iliyotolewa ingeweza kuwapa watu uzima, basi haki ingepatikana kwa njia ya sheria.

22 Lakini Maandiko yamefanya vitu vyote vifungwe chini ya nguvu ya dhambi, ili yale yaliyoahidiwa kwa njia ya imani katika Yesu Kristo yapate kupewa wale wanaoamini.

23 Kabla imani hii haijaja tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ile imani ifunuliwe.

24 Hivyo, sheria ilikuwa kiongozi kutufikisha kwa Kristo, ili tupate kuhesabiwa haki kwa imani.

25 Lakini sasa kwa kuwa ile imani imekuja, hatusimamiwi tena na sheria.

Watoto Wa Mungu

26 Kwa maana ninyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu katika Kristo Yesu kwa njia ya imani.

27 Kwa maana wote mliobatizwa ndani ya Kristo, mmemvaa Kristo.

28 Wala hakuna tena Myahudi au Myunani, mtumwa au mtu huru, mwanaume wala mwanamke, maana nyote mmekuwa wamoja ndani ya Kristo Yesu.

29 Nanyi mkiwa ni mali ya Kristo, basi ninyi ni wa uzao wa Abrahamu na warithi sawasawa na ile ahadi.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/GAL/3-c03f3a49d19911af5d993d60ec187ce0.mp3?version_id=1627—

Categories
Wagalatia

Wagalatia 4

1 Lile nisemalo ni kwamba wakati wote mrithi bado ni mtoto, hana tofauti na mtumwa, ingawa ndiye mmiliki wa mali yote.

2 Yeye huwa yuko chini ya uangalizi wa walezi na wadhamini mpaka ufike wakati uliowekwa na baba yake.

3 Vivyo hivyo na sisi, tulipokuwa bado watoto wadogo, tulikuwa utumwani chini ya taratibu za kawaida za ulimwengu.

4 Lakini ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe, ambaye alizaliwa na mwanamke, akazaliwa chini ya sheria,

5 kusudi awakomboe wale waliokuwa chini ya sheria, ili tupate kupokea zile haki kamili za kufanywa watoto wa Mungu.

6 Kwa sababu ninyi ni watoto wa Mungu, Mungu amemtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, anayelia, “Abba,Baba.”

7 Kwa hiyo, wewe si mtumwa tena, bali ni mtoto, kwa kuwa wewe ni mtoto, Mungu amekufanya wewe pia kuwa mrithi kwa kupitia Kristo.

Paulo Awashawishi Wagalatia

8 Zamani, mlipokuwa hammjui Mungu, mlikuwa watumwa wa viumbe ambavyo kwa asili si Mungu.

9 Lakini sasa kwa kuwa mmemjua Mungu, au zaidi mmejulikana na Mungu, inakuwaje mnarejea tena katika zile kanuni za kwanza zenye udhaifu na upungufu? Mnataka ziwafanye tena watumwa?

10 Mnaadhimisha siku maalum, miezi, nyakati na miaka!

11 Nina hofu juu yenu, kwamba kazi niliyofanya kwa ajili yenu inaweza kuwa nimejitaabisha bure.

12 Ndugu zangu, nawasihi mwe kama mimi, kwa sababu mimi nimekuwa kama ninyi. Hamkunitendea jambo lolote baya.

13 Ninyi mwajua kwamba ni kwa ajili ya udhaifu wangu niliwahubiria Injili.

14 Ingawa hali yangu iliwatia majaribuni, hamkunidharau wala kunidhihaki, bali mlinikaribisha kama malaika wa Mungu, kama vile Kristo Yesu.

15 Ile hali ya furaha mliyokuwa nayo imekwenda wapi? Naweza kushuhudia kwamba, kama ingewezekana mngengʼoa macho yenu na kunipa mimi.

16 Je, sasa nimekuwa adui yenu kwa kuwaambia kweli?

17 Hao wana shauku ya kuwapata lakini si kwa kusudi zuri. Wanachotaka ni kuwatenga mbali nasi, ili ninyi mpate kuwaonea wao shauku.

18 Ni vizuri wakati wote kuwa na shauku kwa ajili ya kusudi zuri, si wakati nikiwa pamoja nanyi tu.

19 Watoto wangu wapendwa, ambao kwa mara nyingine ninawaonea utungu, ninatamani kwamba Kristo aumbike ndani yenu.

20 Natamani kama ningekuwa pamoja nanyi sasa, pengine ningebadilisha sauti yangu. Kwa maana nina wasiwasi kwa ajili yenu.

Mfano Wa Hagari Na Sara

21 Niambieni, ninyi mnaotaka kuwa chini ya sheria, je, hamjui sheria inavyosema?

22 Kwa maana imeandikwa kwamba Abrahamu alikuwa na wana wawili, mmoja wa mwanamke mtumwa na wa pili wa mwanamke huru.

23 Lakini, mtoto wa mwanamke mtumwa alizaliwa kwa mapenzi ya mwili, na yule mwingine wa mwanamke huru alizaliwa kutokana na ahadi ya Mungu.

24 Mambo haya yanaweza kuchukuliwa kama mfano. Kwa maana hao wanawake wawili ni mfano wa maagano mawili: Agano la kwanza, ni lile lililofanyika katika Mlima Sinai, lizaalo watoto wa utumwa. Hili ndilo huyo Hagari.

25 Basi Hagari anawakilisha Mlima Sinai ulioko Arabuni, na unafanana na Yerusalemu ya sasa ambayo iko utumwani pamoja na watoto wake.

26 Lakini Yerusalemu wa juu ni huru, nayo ndiye mama yetu.

27 Kwa maana imeandikwa:

“Furahi, ewe mwanamke tasa,

wewe usiyezaa;

paza sauti, na kuimba kwa furaha,

wewe usiyepatwa na utungu wa kuzaa;

kwa maana watoto wa mwanamke aliyeachwa ukiwa ni wengi

kuliko wa mwanamke mwenye mume.”

28 Basi, sisi ndugu zangu, ni kama Isaki, tu watoto wa ahadi.

29 Lakini, kama vile ilivyokuwa siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomchokoza yule aliyezaliwa kwa Roho, ndivyo ilivyo hata sasa.

30 Lakini Maandiko yasemaje? “Mwondoe mwanamke mtumwa pamoja na mwanawe, kwa sababu mwana wa mwanamke mtumwa kamwe hatarithi pamoja na mwana wa aliye huru.”

31 Kwa hiyo ndugu zangu, sisi si watoto wa mwanamke mtumwa, bali wa yule aliye huru.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/GAL/4-84e7bdaec3a31f486347619ea2b12d16.mp3?version_id=1627—

Categories
Wagalatia

Wagalatia 5

Uhuru Ndani Ya Kristo

1 Kristo alitupa uhuru, akataka tubaki huru. Hivyo simameni imara wala msikubali tena kulemewa na kongwa la utumwa.

2 Sikilizeni! Mimi, Paulo, nawaambieni kwamba kama mkikubali kutahiriwa, basi Kristo hatawafaidia chochote.

3 Namshuhudia tena kila mtu anayekubali kutahiriwa kwamba inampasa kushika sheria yote.

4 Ninyi mnaotafuta kuhesabiwa haki kwa njia ya sheria mmetengwa na Kristo, mko mbali na neema ya Mungu.

5 Kwa maana, kwa njia ya Roho kwa imani, tunangojea kwa shauku tumaini la haki.

6 Kwa maana ndani ya Kristo Yesu, kutahiriwa au kutokutahiriwa hakuleti tofauti, bali lililo muhimu ni imani itendayo kazi kwa njia ya upendo.

7 Mlikuwa mkipiga mbio vizuri. Ni nani aliyewazuia msiitii kweli?

8 Ushawishi wa namna hiyo haukutokana na yule anayewaita.

9 “Chachu kidogo huchachua donge zima.”

10 Nina hakika katika Bwana kwamba hamtakuwa na msimamo mwingine. Mtu anayewachanganya anastahili adhabu, hata awe nani.

11 Lakini ndugu zangu, kama mimi bado ninahubiri kuhusu kutahiriwa, kwa nini bado ninateswa? Katika hiyo hali basi, kwazo la msalaba limeondolewa.

12 Laiti hao wanaowavuruga wangejihasi wao wenyewe!

13 Ndugu zangu, ninyi mliitwa ili mwe huru, hivyo msitumie uhuru wenu kama fursa ya kufuata tamaa za mwili, bali tumikianeni ninyi kwa ninyi kwa upendo.

14 Kwa maana sheria yote hukamilika katika amri moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.”

15 Kama mkiumana na kutafunana, angalieni, msije mkaangamizana.

Maisha Ya Kiroho

16 Kwa hiyo nasema, enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.

17 Kwa maana mwili hutamani yale yaliyo kinyume na Roho, naye Roho hutamani yale yaliyo kinyume na mwili. Roho na mwili hupingana na kwa sababu hiyo hamwezi kufanya mnayotaka.

18 Lakini kama mkiongozwa na Roho, hamko chini ya sheria.

19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi,

20 kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,

21 husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi Ufalme wa Mungu.

22 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,

23 upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria.

24 Wote walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili na shauku zake pamoja na tamaa zake.

25 Kwa kuwa tunaishi kwa Roho, basi, tuenende kwa Roho.

26 Tusijisifu bure, tukichokozana na kuoneana wivu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/GAL/5-0a09bd629b94c9a5d7636f4632568b9f.mp3?version_id=1627—

Categories
Wagalatia

Wagalatia 6

Chukulianeni Mizigo

1 Ndugu zangu, ikiwa mtu ameghafilika akatenda dhambi, basi ninyi mlio wa rohoni, mrejesheni upya mtu huyo kwa roho ya upole. Lakini jihadharini, ili ninyi wenyewe msije mkajaribiwa.

2 Chukulianeni mizigo ninyi kwa ninyi, nanyi kwa njia hii mtatimiza sheria ya Kristo.

3 Kama mtu yeyote akijiona kuwa yeye ni bora na kumbe sivyo, basi mtu huyo anajidanganya mwenyewe.

4 Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo aweze kujisifu, bila kujilinganisha na mtu mwingine.

5 Kwa maana, kila mtu atauchukua mzigo wake mwenyewe.

6 Basi, yeye afundishwaye katika neno na amshirikishe mwalimu wake mema yote.

7 Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi. Kwa kuwa kile apandacho mtu ndicho atakachovuna.

8 Apandaye kwa mwili, katika mwili wake atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye katika Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele.

9 Hivyo, tusichoke katika kutenda mema, kwa kuwa tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa.

10 Kwa hiyo, kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, hasa wale wa jamaa ya waaminio.

Si Kutahiriwa Bali Kuwa Kiumbe Kipya

11 Angalieni herufi kubwa nitumiazo ninapowaandikia kwa mkono wangu mwenyewe!

12 Wale wanaotaka kuonekana wazuri kwa mambo ya mwili wanataka wawalazimishe kutahiriwa. Sababu pekee ya kufanya hivyo ni kuepuka kuteswa kwa ajili ya msalaba wa Kristo.

13 Hata wale waliotahiriwa wenyewe hawaitii sheria, lakini wanataka ninyi mtahiriwe ili wapate kujivuna kwa habari ya miili yenu.

14 Mungu apishie mbali nisije nikajivunia kitu chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye ulimwengu umesulubiwa kwangu, nami nimesulubiwa kwa ulimwengu.

15 Kwa maana katika Kristo Yesu, kutahiriwa au kutokutahiriwa si kitu, bali kule kuwa kiumbe kipya ni kila kitu!

16 Amani na rehema viwe na wote wanaofuata kanuni hii, na juu ya Israeli wa Mungu.

17 Hatimaye, tangu sasa mtu yeyote asinitaabishe, kwa maana nachukua katika mwili wangu chapa zake Yesu.

18 Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja na roho zenu. Amen.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/GAL/6-d9677d634dbb0670988eeccdee00c81a.mp3?version_id=1627—

Categories
Waefeso

Waefeso Utangulizi

Utangulizi

Paulo aliandika waraka huu akiwa gerezani huko Rumi ili kuwatia moyo waumini wa Asia. Waraka huu ulikuwa kama mwongozo uliokusudiwa kwa makanisa kadhaa. Zaidi ya hayo, kwenye waraka huu hakuna salamu za watu binafsi, wala hakuna matatizo maalum. Paulo alielezea kwamba kanisa lilianzishwa na Mungu, akiwaelezea mpango wa Mungu wa tangu awali wa kuwaokoa watu wake kwa njia ya Kristo kwa imani. Mpango huu ulikuwako hata kabla ya ulimwengu kuumbwa. Mwenendo wa maisha mapya upo kinyume kabisa na ule wa maisha ya kale bila Kristo.

Mwandishi

Mtume Paulo.

Kusudi

Kuwaimarisha waumini katika imani yao ya Kikristo kwa kueleza asili na kusudi la kanisa, ambalo ni mwili wa Kristo.

Mahali

Rumi.

Tarehe

Kama mwaka wa 60 B.K.

Wahusika Wakuu

Paulo, Tikiko, na waumini wa Efeso.

Wazo Kuu

Mpango wa Mungu wa milele wa kuuokoa ulimwengu ulitimizwa kwa njia ya Kristo katika mwili wake.

Mambo Muhimu

Umoja katika Kristo na maisha mapya katika Kristo (

2:4-6

), na umoja katika mwili wa Kristo. Pia maisha Wakristo wanayopaswa kuishi kuhusu ndoa, tabia, mwenendo, wazazi na watoto, watumishi na mabwana zao.

Mgawanyo

Mpango wa Mungu, na wokovu wa wote wamwaminio (

1:1–2:22

)

Siri ya Injili (

3:1-21

)

Maisha ya Mkristo duniani (

4:1–5:21

)

Jinsi Wakristo wapaswavyo kuhusiana (

5:22–6:9

)

Kupigana na uovu (

6:10-24

).

Categories
Waefeso

Waefeso 1

Salamu

1 Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu:

Kwa watakatifu walioko Efeso, walio waaminifu katika Kristo Yesu:

2 Neema na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi.

Baraka Za Kiroho Katika Kristo Yesu

3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki sisi kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho ndani ya Kristo.

4 Kwa maana alituchagua katika yeye kabla ya kuumbwa ulimwengu ili tuwe watakatifu na bila lawama mbele zake. Kwa upendo

5 alitangulia kutuchagua tuwe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo kwa furaha yake na mapenzi yake mwenyewe.

6 Kwa hiyo tunamsifu Mungu kwa huruma zake kuu alizotumiminia sisi katika Mwanawe Mpendwa.

7 Ndani yake tunao ukombozi kwa njia ya damu yake, yaani, msamaha wa dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake

8 aliyotumiminia kwa wingi, kwa hekima yote na maarifa yote.

9 Naye alitujulisha siri ya mapenzi yake sawasawa na uradhi wa mapenzi yake, ambayo alikusudia katika Kristo,

10 ili yapate kutimizwa wakati mkamilifu utakapowadia, yaani, kuvitia vitu vyote vya mbinguni na vya duniani pamoja, chini ya kiongozi mmoja, ndiye Kristo.

11 Katika Kristo sisi nasi tumepata urithi, tukisha kuchaguliwa sawasawa na kusudi la Mungu, yeye ambaye hufanya mambo yote kulingana na kusudi la mapenzi yake,

12 ili kwamba, sisi tuliokuwa wa kwanza kuweka tumaini katika Kristo, tupate kuishi kwa sifa ya utukufu wake.

13 Ninyi pia mliingia ndani ya Kristo mliposikia Neno la kweli, Injili ya wokovu wenu. Mkiisha kuamini, ndani yake mlitiwa muhuri, yaani, Roho Mtakatifu mliyeahidiwa,

14 yeye ambaye ni amana yetu akituhakikishia urithi wetu hadi ukombozi wa wale walio milki ya Mungu kwa sifa ya utukufu wake.

Shukrani Na Maombi

15 Kwa sababu hii, tangu niliposikia juu ya imani yenu katika Bwana Yesu na upendo wenu kwa watakatifu wote,

16 sijaacha kumshukuru Mungu kwa ajili yenu, nikiwakumbuka katika maombi yangu.

17 Nazidi kumwomba Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awajalieni ninyi roho ya hekima na ya ufunuo, ili mpate kumjua zaidi.

18 Ninaomba pia kwamba macho ya mioyo yenu yatiwe nuru ili mpate kujua tumaini mliloitiwa, utajiri wa urithi wa utukufu wake kwa watakatifu

19 na uweza wake mkuu usiolinganishwa kwa ajili yetu sisi tuaminio. Uweza huo unaofanya kazi ndani yetu, ni sawa na ile nguvu kuu mno

20 aliyoitumia katika Kristo alipomfufua kutoka kwa wafu, na akamketisha mkono wake wa kuume huko mbinguni,

21 juu sana kuliko falme zote na mamlaka, enzi na milki, na juu ya kila jina litajwalo, si katika ulimwengu huu tu, bali katika ule ujao pia.

22 Naye Mungu ameweka vitu vyote viwe chini ya miguu yake na amemfanya yeye awe kichwa cha vitu vyote kwa ajili ya Kanisa,

23 ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake yeye aliye yote katika yote.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/EPH/1-a5456c701fa7166a4fa174ed32de3765.mp3?version_id=1627—

Categories
Waefeso

Waefeso 2

Tumefanywa Kuwa Hai Ndani Ya Kristo

1 Kwa habari zenu, mlikuwa wafu katika makosa na dhambi zenu,

2 ambazo mlizitenda mlipofuatisha namna ya ulimwengu huu na za yule mtawala wa ufalme wa anga, yule roho atendaye kazi sasa ndani ya wale wasiotii.

3 Sisi sote pia tuliishi katikati yao hapo zamani, tukitimiza tamaa za asili yetu ya dhambi na kufuata tamaa zake na mawazo yake. Nasi kwa asili tulikuwa wana wa ghadhabu, kama mtu mwingine yeyote.

4 Lakini Mungu kwa upendo wake mwingi kwetu sisi, ambaye ni mwingi wa rehema,

5 hata tulipokuwa wafu kwa ajili ya makosa yetu, alitufanya tuwe hai pamoja na Kristo Yesu, yaani, mmeokolewa kwa neema.

6 Mungu alitufufua pamoja na Kristo na kutuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho katika Kristo Yesu,

7 ili katika ule ulimwengu ujao apate kuonyesha wingi wa neema yake isiyopimika, iliyodhihirishwa kwetu kwa wema wake ndani ya Kristo Yesu.

8 Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, wala si kwa matendo yenu mema. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu,

9 si kwa matendo, ili mtu yeyote asije akajisifu.

10 Kwa maana sisi ni kazi ya mikono ya Mungu, tulioumbwa katika Kristo Yesu, ili tupate kutenda matendo mema, ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa tupate kuishi katika hayo.

Wamoja Katika Kristo

11 Kwa hiyo kumbukeni kwamba ninyi ambao hapo awali mlikuwa watu wa Mataifa kwa kuzaliwa na kuitwa “wasiotahiriwa” na wale wanaojiita “waliotahiriwa” (yaani tohara ifanyikayo katika mwili kwa mikono ya wanadamu),

12 kumbukeni kwamba wakati ule mlikuwa mbali na Kristo, mkiwa mmetengwa kutoka jumuiya ya Israeli, na mkiwa wageni katika yale maagano ya ahadi, nanyi mkiwa hamna tumaini wala Mungu duniani.

13 Lakini sasa katika Kristo Yesu, ninyi ambao hapo kwanza mlikuwa mbali na Mungu, sasa mmeletwa karibu kwa njia ya damu ya Kristo.

14 Kwa maana yeye mwenyewe ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi tuliokuwa wawili, yaani, Wayahudi na watu wa Mataifa, tuwe wamoja kwa kuvunja kizuizi na kubomoa ule ukuta wa uadui uliokuwa kati yetu,

15 kwa kuibatilisha ile sheria pamoja na amri zake na maagizo yake alipoutoa mwili wake, ili apate kufanya ndani yake mtu mmoja mpya badala ya hao wawili, hivyo akifanya amani,

16 naye katika mwili huu mmoja awapatanishe wote wawili na Mungu kupitia msalaba, ili kwa huo msalaba akaangamiza uadui wao.

17 Alikuja na kuhubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali na pia akahubiri amani kwao waliokuwa karibu.

18 Kwa maana kwa kupitia kwake, sisi sote tunaweza kumkaribia Baba katika Roho mmoja.

19 Hivyo basi, ninyi sasa si wageni tena wala wapitaji, bali mmekuwa wenyeji pamoja na watakatifu na pia jamaa wa nyumbani mwake Mungu.

20 Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ndiye jiwe kuu la pembeni.

21 Ndani yake jengo lote limeshikamanishwa pamoja na kusimamishwa ili kuwa Hekalu takatifu katika Bwana.

22 Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja ili mpate kuwa makao ambayo Mungu anaishi ndani yake kwa njia ya Roho wake.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/EPH/2-e23a39884fd17de61de72e94b73333b5.mp3?version_id=1627—

Categories
Waefeso

Waefeso 3

Huduma Ya Paulo Kwa Watu Wa Mataifa

1 Kwa sababu hii, mimi Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu kwa ajili yenu ninyi watu wa Mataifa:

2 Kwa hakika mmekwisha kusikia kuhusu ile huduma ya neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu,

3 yaani, ile siri iliodhihirishwa kwangu kwa njia ya ufunuo, kama nilivyotangulia kuandika kwa kifupi.

4 Kwa kusoma haya, basi mtaweza kuelewa ufahamu wangu katika siri ya Kristo.

5 Siri hii haikudhihirishwa kwa wanadamu katika vizazi vingine kama vile sasa ilivyodhihirishwa na Roho kwa mitume na manabii watakatifu wa Mungu.

6 Siri hii ni kwamba, kwa njia ya Injili, watu wa Mataifa ni warithi pamoja na Israeli, viungo vya mwili mmoja na washiriki pamoja wa ahadi katika Kristo Yesu.

7 Nimekuwa mtumishi wa Injili hii kwa kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa nguvu yake itendayo kazi.

8 Ingawa mimi ni mdogo kuliko aliye mdogo kabisa miongoni mwa watakatifu wote, nilipewa neema hii: ili niwahubirie watu wa Mataifa kuhusu utajiri usiopimika ulio ndani ya Kristo,

9 na kuweka wazi kwa kila mtu siri hii iliyokuwa imefichwa tangu zamani katika Mungu, aliyeumba vitu vyote.

10 Ili sasa kwa njia ya Kanisa, hekima yote ya Mungu ipate kujulikana kwa watawala na wenye mamlaka katika ulimwengu wa roho,

11 sawasawa na kusudi lake la milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.

12 Ndani yake na kwa njia ya imani katika yeye twaweza kumkaribia Mungu kwa uhuru na kwa ujasiri.

13 Kwa hiyo, nawaomba msikate tamaa kwa sababu ya mateso yangu kwa ajili yenu, hayo ni utukufu wenu.

Maombi Ya Paulo Kwa Waefeso

14 Kwa sababu hii nampigia Baba magoti,

15 ambaye ubaba wote wa kila jamaa za mbinguni na za duniani unatokana naye.

16 Namwomba Mungu awaimarishe kwa kuwatia nguvu mioyo yenu kwa njia ya Roho wake kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake,

17 ili kwamba, Kristo apate kukaa mioyoni mwenu kwa njia ya imani. Nami ninaomba kwamba ninyi mkiwa wenye mizizi tena imara katika msingi wa upendo,

18 mwe na uwezo wa kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, urefu, kimo na kina upendo wa Kristo,

19 na kujua upendo huu unaopita fahamu, ili mpate kujazwa na kufikia kipimo cha ukamilifu wote wa Mungu.

20 Basi kwa yeye awezaye kutenda mambo ya ajabu yasiyopimika kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya uweza wake ule utendao kazi ndani yetu,

21 yeye atukuzwe katika kanisa na katika Kristo Yesu kwa vizazi vyote, milele na milele. Amen.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/EPH/3-864e88cbc9a15e6af5877450826f39f8.mp3?version_id=1627—

Categories
Waefeso

Waefeso 4

Umoja Katika Mwili Wa Kristo

1 Basi, mimi niliye mfungwa wa Bwana, nawasihi mwenende kama inavyostahili wito wenu mlioitiwa.

2 Kwa unyenyekevu wote na upole, mkiwa wavumilivu, mkichukuliana kwa upendo.

3 Jitahidini kudumisha umoja wa Roho katika kifungo cha amani.

4 Kuna mwili mmoja na Roho mmoja, kama vile mlivyoitwa katika tumaini moja.

5 Tena kuna Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja,

6 Mungu mmoja ambaye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote, katika yote na ndani ya yote.

7 Lakini kila mmoja wetu amepewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa cha Kristo.

8 Kwa hiyo husema:

“Alipopaa juu zaidi,

aliteka mateka,

akawapa wanadamu vipawa.”

9 (Asemapo “alipaa juu,” maana yake nini isipokuwa ni kusema pia kwamba Kristo alishuka pande za chini sana za dunia?

10 Yeye aliyeshuka ndiye alipaa juu zaidi kupita mbingu zote, ili apate kuujaza ulimwengu wote.)

11 Ndiye aliweka wengine kuwa mitume, wengine kuwa manabii, wengine kuwa wainjilisti, wengine kuwa wachungaji na walimu,

12 kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu kwa ajili ya kazi za huduma, ili kwamba mwili wa Kristo upate kujengwa

13 mpaka sote tutakapoufikia umoja katika imani na katika kumjua sana Mwana wa Mungu na kuwa watu wazima kwa kufikia kimo cha ukamilifu wa Kristo.

14 Ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwatupwa huku na huku na kuchukuliwa na kila upepo wa mafundisho kwa hila za watu, kwa ujanja, kwa kufuata njia zao za udanganyifu.

15 Badala yake, tukiambiana kweli kwa upendo, katika mambo yote tukue, hata tumfikie yeye aliye kichwa, yaani, Kristo.

16 Kutoka kwake, mwili wote ukiwa umeungamanishwa na kushikamanishwa pamoja kwa msaada wa kila kiungo, hukua na kujijenga wenyewe katika upendo, wakati kila kiungo kinafanya kazi yake.

Maisha Ya Zamani Na Maisha Mapya

17 Hivyo nawaambia hivi, nami nasisitiza katika Bwana kwamba, msiishi tena kama watu wa Mataifa waishivyo, katika ubatili wa mawazo yao.

18 Watu hao akili zao zimetiwa giza na wametengwa mbali na uzima wa Mungu kwa sababu ya ujinga wao kutokana na ugumu wa mioyo yao.

19 Wakiisha kufa ganzi, wamejitia katika mambo ya ufisadi na kupendelea kila aina ya uchafu, wakiendelea kutamani zaidi.

20 Lakini ninyi, hivyo sivyo mlivyojifunza Kristo.

21 Kama hivyo ndivyo ilivyo, ninyi mmemsikia, tena mmefundishwa naye, vile kweli ilivyo katika Yesu.

22 Mlifundishwa kuuvua mwenendo wenu wa zamani, utu wenu wa kale, ulioharibiwa na tamaa zake za udanganyifu,

23 ili mfanywe upya roho na nia zenu,

24 mkajivike utu mpya, ulioumbwa sawasawa na mfano wa Mungu katika haki yote na utakatifu.

Kanuni Za Maisha Mapya

25 Kwa hiyo kila mmoja wenu avue uongo na kuambiana kweli mtu na jirani yake, kwa maana sisi sote tu viungo vya mwili mmoja.

26 Mkikasirika, msitende dhambi, wala jua lisichwe mkiwa bado mmekasirika,

27 wala msimpe ibilisi nafasi.

28 Yeye ambaye amekuwa akiiba, asiibe tena, lakini lazima ajishughulishe, afanye kitu kifaacho kwa mikono yake mwenyewe, ili awe na kitu cha kuwagawia wahitaji.

29 Maneno mabaya yasitoke vinywani mwenu, bali yale yafaayo kwa ajili ya kuwajenga wengine kulingana na mahitaji yao, ili yawafae wale wasikiao.

30 Wala msimhuzunishe Roho Mtakatifu wa Mungu, ambaye kwake mlitiwa muhuri kwa ajili ya siku ya ukombozi.

31 Ondoeni kabisa uchungu, ghadhabu, hasira, makelele na masingizio pamoja na kila aina ya uovu.

32 Kuweni wafadhili na wenye kuhurumiana ninyi kwa ninyi, mkisameheana, kama vile naye Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/EPH/4-2263790e73751ef16d256801284c812f.mp3?version_id=1627—