Categories
Yeremia

Yeremia 50

Ujumbe Kuhusu Babeli

1 Hili ndilo neno alilosemaBwanakupitia nabii Yeremia kuhusu Babeli na nchi ya Wakaldayo:

2 “Tangazeni na mhubiri katikati ya mataifa,

twekeni bendera na mkahubiri;

msiache kitu chochote, bali semeni,

‘Babeli utatekwa;

Beli ataaibishwa,

Merodaki atajazwa na hofu kuu.

Sanamu zake zitaaibishwa

na vinyago vyake vitajazwa hofu kuu.’

3 Taifa kutoka kaskazini litamshambulia,

na kuifanya nchi yake ukiwa.

Hakuna hata mmoja atakayeishi ndani yake,

watu na wanyama wataikimbia.

4 “Katika siku hizo, wakati huo,”

asemaBwana,

“watu wa Israeli pamoja na watu wa Yuda

wataenda wakilia ili kumtafutaBwanaMungu wao.

5 Wataiuliza njia iendayo Sayuni

na kuelekeza nyuso zao huko.

Watakuja na kuambatana naBwana

katika agano la milele

ambalo halitasahaulika.

6 “Watu wangu wamekuwa kondoo waliopotea;

wachungaji wao wamewapotosha

na kuwasababisha kuzurura

juu ya milima.

Walitangatanga juu ya mlima na kilima,

na kusahau mahali pao wenyewe pa kupumzikia.

7 Yeyote aliyewakuta aliwala;

adui zao walisema, ‘Sisi hatuna hatia,

kwa kuwa wao walitenda dhambi dhidi yaBwana, malisho yao halisi,

Bwana, aliye tumaini la baba zao.’

8 “Kimbieni kutoka Babeli;

ondokeni katika nchi ya Wakaldayo

tena kuweni kama mbuzi wale waongozao kundi.

9 Kwa maana nitaamsha na kuleta dhidi ya Babeli

muungano wa mataifa makubwa kutoka nchi ya kaskazini.

Watashika nafasi zao dhidi yake,

naye kutokea kaskazini atatekwa.

Mishale yao itakuwa kama mishale ya mashujaa walio hodari,

ambao hawawezi kurudi mikono mitupu.

10 Kwa hiyo Ukaldayo utatekwa nyara;

wote wamtekao nyara watapata za kutosha,”

asemaBwana.

11 “Kwa sababu hushangilia na kufurahi,

wewe utekaye urithi wangu,

kwa sababu unachezacheza kama mtamba anayepura nafaka,

na kulia kama farasi dume,

12 mama yako ataaibika mno,

yeye aliyekuzaa atatahayari.

Atakuwa mdogo kuliko mataifa mengine yote,

atakuwa nyika, nchi kame na jangwa.

13 Kwa sababu ya hasira yaBwanahatakaliwa na mtu,

lakini ataachwa ukiwa kabisa.

Wote watakaopita Babeli watatiwa hofu na kudhihaki

kwa sababu ya majeraha yake yote.

14 “Shikeni nafasi zenu kuzunguka Babeli,

enyi nyote mvutao upinde.

Mpigeni! Msibakize mshale wowote,

kwa kuwa ametenda dhambi dhidi yaBwana.

15 Piga kelele dhidi yake kila upande!

Anajisalimisha, minara yake inaanguka,

kuta zake zimebomoka.

Kwa kuwa hiki ni kisasi chaBwana,

mlipizeni kisasi;

mtendeeni kama alivyowatendea wengine.

16 Katilieni mbali mpanzi kutoka Babeli,

pamoja na mvunaji na mundu wake akivuna.

Kwa sababu ya upanga wa mdhalimu

kila mmoja na arejee kwa watu wake mwenyewe,

kila mmoja na akimbilie

kwenye nchi yake mwenyewe.

17 “Israeli ni kundi lililotawanyika

ambalo simba wamelifukuzia mbali.

Wa kwanza kumla alikuwa mfalme wa Ashuru,

wa mwisho kuponda mifupa yake

alikuwa Nebukadneza mfalme wa Babeli.”

18 Kwa hiyo hili ndiloBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo:

“Nitamwadhibu mfalme wa Babeli na nchi yake

kama nilivyomwadhibu mfalme wa Ashuru.

19 Lakini nitamrudisha Israeli katika malisho yake mwenyewe

naye atalisha huko Karmeli na Bashani;

njaa yake itashibishwa

juu ya vilima vya Efraimu na Gileadi.

20 Katika siku hizo, wakati huo,”

asemaBwana,

“uchunguzi utafanyika kwa ajili ya kosa la Israeli,

lakini halitakuwepo,

kwa ajili ya dhambi za Yuda,

lakini haitapatikana hata moja,

kwa kuwa nitawasamehe

mabaki nitakaowaacha.

21 “Shambulieni nchi ya Merathaimu

na wale waishio huko Pekodi.

Wafuatieni, waueni

na kuwaangamiza kabisa,”

asemaBwana.

“Fanyeni kila kitu nilichowaamuru.

22 Kelele ya vita iko ndani ya nchi,

kelele ya maangamizi makuu!

23 Tazama jinsi nyundo ya dunia yote

ilivyovunjika na kuharibika!

Tazama jinsi Babeli ilivyokuwa ukiwa

miongoni mwa mataifa!

24 Nimetega mtego kwa ajili yako, ee Babeli,

nawe ukakamatwa kabla haujafahamu;

ulipatikana na ukakamatwa

kwa sababu ulimpingaBwana.

25 Bwanaamefungua ghala lake la silaha

na kuzitoa silaha za ghadhabu yake,

kwa kuwaBwanaMwenyezi Mwenye Nguvu Zote

anayo kazi ya kufanya

katika nchi ya Wakaldayo.

26 Njooni dhidi yake kutoka mbali.

Zifungueni ghala zake za nafaka;

mlundikeni kama lundo la nafaka.

Mwangamizeni kabisa

na msimwachie mabaki yoyote.

27 Waueni mafahali wake wachanga wote;

waacheni washuke machinjoni!

Ole wao! Kwa kuwa siku yao imewadia,

wakati wao wa kuadhibiwa.

28 Wasikilizeni watoro na wakimbizi kutoka Babeli

wakitangaza katika Sayuni

jinsiBwana, Mungu wetu alivyolipiza kisasi,

kisasi kwa ajili ya Hekalu lake.

29 “Waiteni wapiga mishale dhidi ya Babeli,

wote wale wavutao upinde.

Pigeni kambi kumzunguka kabisa,

asitoroke mtu yeyote.

Mlipizeni kwa matendo yake;

mtendeeni kama alivyotenda.

Kwa kuwa alimdharauBwana,

yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.

30 Kwa hiyo, vijana wake wanaume wataanguka barabarani;

askari wake wote watanyamazishwa siku ile,”

asemaBwana.

31 “Tazama, niko kinyume nawe, ewe mwenye majivuno,”

asema Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote,

“kwa kuwa siku yako imewadia,

yaani, wakati wako wa kuadhibiwa.

32 Mwenye majivuno atajikwaa na kuanguka,

wala hakuna yeyote atakayemuinua;

nitawasha moto katika miji yake,

utakaowateketeza wote wanaomzunguka.”

33 Hili ndilo asemaloBwanaMwenye Nguvu Zote:

“Watu wa Israeli wameonewa,

nao watu wa Yuda pia.

Wote waliowateka wamewashikilia sana,

wanakataa kuwaachia waende.

34 Lakini Mkombozi wao ana nguvu;

BwanaMwenye Nguvu Zote ndilo jina lake.

Atatetea kwa nguvu shauri lao

ili alete raha katika nchi yao,

lakini ataleta msukosuko

kwa wale waishio Babeli.

35 “Upanga dhidi ya Wakaldayo!”

asemaBwana,

“dhidi ya wale waishio Babeli

na dhidi ya maafisa wake na watu wenye busara!

36 Upanga dhidi ya manabii wake wa uongo!

Watakuwa wapumbavu.

Upanga dhidi ya mashujaa wake!

Watajazwa na hofu kuu

37 Upanga dhidi ya farasi na magari yake ya vita

pamoja na askari wake wote wa kigeni katika safu zake!

Wao watakuwa kama wanawake.

Upanga dhidi ya hazina zake!

Hizo zitatekwa nyara.

38 Ukame juu ya maji yake!

Nayo yatakauka.

Kwa kuwa ni nchi ya sanamu,

wao wanaenda wazimu kwa ajili ya sanamu.

39 “Kwa hiyo, viumbe vya jangwani na fisi wataishi humo,

nao bundi watakaa humo.

Kamwe haitakaliwa tena

wala watu hawataishi humo kutoka kizazi hadi kizazi.

40 Kama vile Mungu alivyoangamiza Sodoma na Gomora

pamoja na miji iliyokuwa jirani nayo,”

asemaBwana,

“vivyo hivyo hakuna mtu yeyote

atakayeishi humo.

Naam, hakuna mtu yeyote

atakayekaa humo.

41 “Tazama! Jeshi linakuja kutoka kaskazini;

taifa kubwa na wafalme wengi

wanaamshwa kutoka miisho ya dunia.

42 Wamejifunga pinde na mikuki;

ni wakatili na wasio na huruma.

Wanatoa sauti kama bahari inayonguruma

wanapoendesha farasi zao;

wanakuja kama watu waliojipanga tayari kwa vita

ili kukushambulia, ee Binti Babeli.

43 Mfalme wa Babeli amesikia habari kuwahusu,

nayo mikono yake imelegea.

Uchungu umemshika,

maumivu kama ya mwanamke katika utungu wa kuzaa.

44 Kama simba anayepanda kutoka vichaka vya Yordani

kuja kwenye nchi ya malisho mengi,

ndivyo nitamfukuza Babeli kutoka nchi yake ghafula.

Ni nani aliye mteule,

nitakayemweka kwa ajili ya jambo hili?

Ni nani aliye kama mimi,

na ni nani awezaye kunipinga?

Tena ni mchungaji yupi

awezaye kusimama kinyume nami?”

45 Kwa hiyo, sikia kileBwanaalichokipanga dhidi ya Babeli,

kile alichokusudia dhidi ya nchi ya Wakaldayo:

Aliye mchanga katika kundi ataburutwa mbali.

Yeye ataharibu kabisa malisho yao kwa sababu yao.

46 Kwa sauti ya kutekwa kwa Babeli, dunia itatetemeka;

kilio chake kitasikika pote miongoni mwa mataifa.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JER/50-5b601e05cff5714c3c5f4e4f3abb1384.mp3?version_id=1627—

Categories
Yeremia

Yeremia 51

1 Hili ndilo asemaloBwana:

“Tazama nitaamsha roho ya mwangamizi

dhidi ya Babeli na watu wakaao Leb-Kamai.

2 Nitawatuma wageni Babeli

kumpepeta na kuiharibu nchi yake;

watampinga kila upande

katika siku ya maafa yake.

3 Usimwache mpiga upinde afunge kamba upinde wake,

wala usimwache avae silaha zake.

Usiwaonee huruma vijana wake;

angamiza jeshi lake kabisa.

4 Wataanguka waliouawa katika Babeli,

wakiwa na majeraha ya kutisha barabarani zake.

5 Kwa maana Israeli na Yuda hawajaachwa

na Mungu wao,BwanaMwenye Nguvu Zote,

ingawa nchi yao imejaa uovu

mbele zake yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.

6 “Kimbieni kutoka Babeli!

Okoeni maisha yenu!

Msiangamizwe kwa sababu ya dhambi zake.

Ni wakati wa kisasi chaBwana,

atamlipa kile anachostahili.

7 Babeli alikuwa kikombe cha dhahabu katika mkono waBwana;

aliufanya ulimwengu wote ulewe.

Mataifa walikunywa mvinyo wake;

kwa hiyo sasa wameingiwa na wazimu.

8 Babeli ataanguka ghafula na kuvunjika.

Mwombolezeni!

Tafuteni zeri ya kutuliza maumivu yake,

labda anaweza kupona.

9 “ ‘Tungemponya Babeli,

lakini hawezi kuponyeka;

tumwacheni, na kila mmoja wetu aende nchi yake mwenyewe,

kwa kuwa hukumu yake inafika angani,

inapanda juu hadi mawinguni.’

10 “ ‘Bwanaamethibitisha haki yetu;

njooni, tutangaze katika Sayuni

kitu ambachoBwanaMungu wetu amefanya.’

11 “Noeni mishale,

chukueni ngao!

Bwanaamewaamsha wafalme wa Wamedi,

kwa sababu nia yake ni kuangamiza Babeli.

Bwanaatalipiza kisasi,

kisasi kwa ajili ya Hekalu lake.

12 Twekeni bendera juu ya kuta za Babeli!

Imarisheni ulinzi,

wekeni walinzi,

andaeni waviziao!

Bwanaatatimiza kusudi lake,

amri yake juu ya watu wa Babeli.

13 Wewe uishiye kando ya maji mengi

na uliye na wingi wa hazina,

mwisho wako umekuja,

wakati wako wa kukatiliwa mbali.

14 BwanaMwenye Nguvu Zote

ameapa kwa nafsi yake mwenyewe:

‘Hakika nitakujaza na watu, kama kundi la nzige,

nao watapiga kelele za ushindi juu yako.’

15 “Aliiumba dunia kwa uweza wake;

akaweka misingi ya ulimwengu kwa hekima yake

na akazitandaza mbingu kwa ufahamu wake.

16 Atoapo sauti yake, maji yaliyo katika mbingu hunguruma,

huyafanya mawingu yainuke kutoka miisho ya dunia.

Hupeleka umeme wa radi pamoja na mvua,

naye huuleta upepo kutoka ghala zake.

17 “Kila mtu ni mjinga na hana maarifa;

kila sonara ameaibishwa na sanamu zake.

Vinyago vyake ni vya udanganyifu,

havina pumzi ndani yavyo.

18 Havifai kitu, ni vitu vya kufanyia mzaha,

hukumu yavyo itakapowadia, vitaangamia.

19 Yeye Aliye Fungu la Yakobo sivyo alivyo,

kwani ndiye Muumba wa vitu vyote,

pamoja na kabila la urithi wake:

BwanaMwenye Nguvu Zote ndilo jina lake.

20 “Wewe ndiwe rungu langu la vita,

silaha yangu ya vita:

kwa wewe navunjavunja mataifa,

kwa wewe naangamiza falme,

21 kwa wewe navunjavunja

farasi na mpanda farasi,

kwa wewe navunjavunja

gari la vita na mwendeshaji wake,

22 kwa wewe napondaponda

mwanaume na mwanamke,

kwa wewe napondaponda

mzee na kijana,

kwa wewe napondaponda

kijana wa kiume na mwanamwali,

23 kwa wewe nampondaponda

mchungaji na kundi,

kwa wewe nampondaponda

mkulima na maksai,

kwa wewe nawapondaponda

watawala na maafisa.

24 “Mbele ya macho yako nitamlipiza Babeli na wote waishio Ukaldayo kwa ajili ya makosa yote waliyofanya katika Sayuni,” asemaBwana.

25 “Mimi niko kinyume nawe, ee mlima unaoharibu,

wewe uangamizaye dunia yote,”

asemaBwana.

“Nitanyoosha mkono wangu dhidi yako,

nikuvingirishe kutoka kwenye kilele cha mwamba,

na kukufanya mlima ulioteketezwa kwa moto.

26 Hakuna jiwe litakalochukuliwa kutoka kwako

kwa ajili ya kufanywa jiwe la pembeni,

wala jiwe lolote kwa ajili ya msingi,

kwa maana utakuwa ukiwa milele,”

asemaBwana.

27 “Twekeni bendera katika nchi!

Pigeni tarumbeta katikati ya mataifa!

Andaeni mataifa kwa ajili ya vita dhidi yake,

iteni falme hizi dhidi yake:

Ararati, Mini na Ashkenazi.

Wekeni jemadari dhidi yake,

pelekeni farasi wengi kama kundi la nzige.

28 Andaeni mataifa kwa ajili ya vita dhidi yake,

wafalme wa Wamedi,

watawala wao na maafisa wao wote,

pamoja na nchi zote wanazotawala.

29 Nchi inatetemeka na kugaagaa,

kwa kuwa makusudi yaBwanadhidi ya Babeli yanasimama:

yaani, kuangamiza nchi ya Babeli

ili pasiwe na yeyote atakayeishi humo.

30 Mashujaa wa Babeli wameacha kupigana,

wamebaki katika ngome zao.

Nguvu zao zimekwisha,

wamekuwa kama wanawake.

Makazi yake yameteketezwa kwa moto,

makomeo ya malango yake yamevunjika.

31 Tarishi mmoja humfuata mwingine,

na mjumbe humfuata mjumbe,

kumtangazia mfalme wa Babeli

kwamba mji wake wote umetekwa,

32 Vivuko vya mito vimekamatwa,

mabwawa yenye mafunjo yametiwa moto,

nao askari wameingiwa na hofu kuu.”

33 Hili ndiloBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo:

“Binti Babeli ni kama sakafu ya kupuria

wakati inapokanyagwa;

wakati wa kumvuna utakuja upesi.”

34 “Nebukadneza mfalme wa Babeli ametula,

ametufanya tuchangayikiwe,

ametufanya tuwe gudulia tupu.

Kama nyoka ametumeza

na kujaza tumbo lake kwa vyakula vyetu vizuri,

kisha akatutapika.

35 Jeuri iliyofanyiwa miili yetuna iwe juu ya Babeli,”

ndivyo wasemavyo wakaao Sayuni.

“Damu yetu na iwe juu ya wale waishio Babeli,”

asema Yerusalemu.

36 Kwa hiyo, hili ndiloBwanaasemalo:

“Tazama, nitatetea shauri lako

na kulipiza kisasi kwa ajili yako;

nitaikausha bahari yake

na kuzikausha chemchemi zake.

37 Babeli utakuwa lundo la magofu

na makao ya mbweha,

kitu cha kutisha na kudharauliwa,

mahali asipoishi mtu.

38 Watu wake wote wananguruma kama simba wadogo,

wanakoroma kama wana simba.

39 Lakini wakati wakiwa wameamshwa,

nitawaandalia karamu

na kuwafanya walewe,

ili wapige kelele kwa kicheko,

kisha walale milele na wasiamke,”

asemaBwana.

40 “Nitawateremsha kama wana-kondoo waendao machinjoni,

kama kondoo dume na mbuzi.

41 “Tazama jinsi Sheshakiatakamatwa,

majivuno ya dunia yote yatakavyonyakuliwa.

Babeli atakuwa mwenye hofu kiasi gani

kati ya mataifa!

42 Bahari itainuka juu ya Babeli;

mawimbi yake yenye kunguruma yatamfunika.

43 Miji yake itakuwa ukiwa,

kame na jangwa,

nchi ambayo hakuna yeyote anayeishi ndani yake,

ambayo hakuna mtu anayepita humo.

44 Nitamwadhibu Beli katika Babeli,

na kumfanya atapike kile alichokimeza.

Mataifa hayatamiminika tena kwake.

Nao ukuta wa Babeli utaanguka.

45 “Tokeni ndani yake, enyi watu wangu!

Okoeni maisha yenu!

Ikimbieni hasira kali yaBwana.

46 Msikate tamaa wala msiogope tetesi

zitakaposikika katika nchi;

tetesi moja inasikika mwaka huu,

nyingine mwaka unaofuata;

tetesi juu ya jeuri katika nchi,

na ya mtawala dhidi ya mtawala.

47 Kwa kuwa hakika wakati utawadia

nitakapoziadhibu sanamu za Babeli;

nchi yake yote itatiwa aibu,

na watu wake wote waliouawa

wataangukia ndani yake.

48 Ndipo mbingu na dunia na vyote vilivyomo ndani yake

vitapiga kelele za shangwe juu ya Babeli,

kwa kuwa kutoka kaskazini

waharabu watamshambulia,”

asemaBwana.

49 “Babeli ni lazima aanguke kwa sababu ya kuwaua Waisraeli,

kama vile waliouawa duniani kote

walivyoanguka kwa sababu ya Babeli.

50 Wewe uliyepona upanga,

ondoka wala usikawie!

MkumbukeBwanaukiwa katika nchi ya mbali,

na utafakari juu ya Yerusalemu.”

51 “Tumetahayari, kwa maana tumetukanwa

na aibu imefunika nyuso zetu,

kwa sababu wageni wameingia

mahali patakatifu pa nyumba yaBwana.”

52 “Lakini siku zinakuja,” asemaBwana,

“nitakapoadhibu sanamu zake,

na katika nchi yake yote

waliojeruhiwa watalia kwa maumivu makali.

53 Hata kama Babeli ikifika angani

na kuziimarisha ngome zake ndefu,

nitatuma waharabu dhidi yake,”

asemaBwana.

54 “Sauti ya kilio inasikika kutoka Babeli,

sauti ya uharibifu mkuu

kutoka nchi ya Wakaldayo.

55 Bwanaataiangamiza Babeli,

atanyamazisha makelele ya kishindo chake.

Mawimbi ya adui yatanguruma kama maji makuu,

ngurumo ya sauti zao itavuma.

56 Mharabu atakuja dhidi ya Babeli,

mashujaa wake watakamatwa,

nazo pinde zao zitavunjwa.

Kwa kuwaBwanani Mungu wa kisasi,

yeye atalipiza kikamilifu.

57 Nitawafanya maafisa wake na wenye busara walewe,

watawala wao, maafisa, pamoja na wapiganaji wao;

watalala milele na hawataamka,”

asema Mfalme, ambaye jina lake niBwanaMwenye Nguvu Zote.

58 Hili ndiloBwanaMwenye Nguvu Zote asemalo:

“Ukuta mnene wa Babeli utasawazishwa,

na malango yaliyoinuka yatateketezwa kwa moto;

mataifa yanajichosha bure,

taabu ya mataifa ni nishati tu ya miali ya moto.”

59 Huu ndio ujumbe Yeremia aliompa afisa Seraya mwana wa Neria mwana wa Maaseya, alipokwenda Babeli pamoja na Sedekia mfalme wa Yuda, katika mwaka wa nne wa utawala wake.

60 Yeremia alikuwa ameandika ndani ya kitabu kuhusu maafa yote yatakayoipata Babeli, yaani yote yaliyokuwa yameandikwa kuhusu Babeli.

61 Yeremia akamwambia Seraya, “Utakapofika Babeli, hakikisha kwamba umesoma maneno haya yote kwa sauti kubwa.

62 Kisha sema, ‘EeBwana, umesema utaangamiza mahali hapa ili mtu wala mnyama asiishi ndani yake, napo patakuwa ukiwa milele.’

63 Utakapomaliza kusoma hiki kitabu, kifungie jiwe kisha ukitupe ndani ya Mto Frati.

64 Kisha sema, ‘Hivi ndivyo Babeli utakavyozama na usiinuke tena, kwa sababu ya maafa nitakayoleta juu yake. Nao watu wake wataanguka.’ ”

Maneno ya Yeremia yanaishia hapa.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JER/51-4d833f0116381e8ad748c9778b3ebe9b.mp3?version_id=1627—

Categories
Yeremia

Yeremia 52

Anguko La Yerusalemu

1 Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka kumi na mmoja. Jina la mama yake aliitwa Hamutali binti Yeremia, kutoka Libna.

2 Alifanya maovu machoni paBwana, kama alivyofanya Yehoyakimu.

3 Ilikuwa ni kwa sababu ya hasira yaBwanahaya yote yalitokea Yerusalemu na Yuda, naye mwishoni akawaondoa mbele zake.

Basi, Sedekia akaasi dhidi ya mfalme wa Babeli.

4 Hivyo katika mwaka wa tisa wa utawala wa Sedekia, katika siku ya kumi ya mwezi wa kumi, Nebukadneza mfalme wa Babeli akiwa na jeshi lake lote alifanya vita dhidi ya Yerusalemu. Wakapiga kambi nje ya mji na kuuzunguka mji pande zote.

5 Mji ulizungukwa na jeshi mpaka mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Mfalme Sedekia.

6 Ilipowadia siku ya tisa ya mwezi wa nne, njaa ikazidi kuwa kali sana ndani ya mji, hadi hapakuwa na chakula kwa ajili ya watu.

7 Kisha ukuta wa mji ukavunjwa na jeshi lote likakimbia. Wakaondoka mjini usiku kupitia lango lililokuwa kati ya kuta mbili karibu na bustani ya mfalme, ingawa Wakaldayo walikuwa wameuzunguka mji. Wakakimbia kuelekea Araba.

8 Lakini jeshi la Wakaldayo likamfuatia Mfalme Sedekia na kumpata katika sehemu tambarare za Yeriko. Askari wake wote wakatengwa naye na kutawanyika,

9 naye akakamatwa.

Akapelekwa kwa mfalme wa Babeli huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, mahali ambapo alimtangazia hukumu.

10 Huko Ribla mfalme wa Babeli aliwachinja wana wa Sedekia mbele ya macho yake. Pia akawaua maafisa wote wa Yuda.

11 Kisha akayangʼoa macho ya Sedekia, akamfunga kwa pingu za shaba na kumpeleka Babeli, alipomweka gerezani mpaka siku ya kifo chake.

12 Mnamo siku ya kumi ya mwezi wa tano, katika mwaka wa kumi na tisa wa utawala wa Nebukadneza mfalme wa Babeli, Nebuzaradani jemadari wa askari walinzi wa mfalme, aliyemtumikia mfalme wa Babeli, alikuja Yerusalemu.

13 Alichoma moto Hekalu laBwana, jumba la kifalme, na nyumba zote za Yerusalemu. Aliteketeza kila jengo muhimu.

14 Jeshi lote la Wakaldayo chini ya jemadari wa askari walinzi wa mfalme walivunja kuta zote zilizoizunguka Yerusalemu.

15 Nebuzaradani, jemadari wa askari walinzi, akawapeleka uhamishoni baadhi ya watu maskini sana na wale waliobaki katika mji, pamoja na mabaki ya watu wa kawaida, na wale waliojisalimisha kwa mfalme wa Babeli.

16 Lakini Nebuzaradani akawaacha mabaki ya wale watu maskini kabisa ili watunze mashamba ya mizabibu na mashamba mengine.

17 Wakaldayo walivunja vipande zile nguzo za shaba, vile vishikilio vya shaba vilivyohamishika, na ile Bahari ya shaba, ambavyo vyote vilikuwa katika Hekalu laBwana. Hivyo wakaichukua hiyo shaba yote na kuipeleka Babeli.

18 Wakachukua pia vyungu, masepetu, mikasi ya kusawazishia tambi, mabakuli ya kunyunyizia, sahani na vyombo vyote vya shaba vilivyotumika katika huduma ya Hekalu.

19 Jemadari wa askari walinzi wa mfalme akachukua yale masinia, vile vyetezo, yale mabakuli ya kunyunyizia, zile sufuria, vile vinara vya taa, zile sahani na yale mabakuli yaliyotumika kwa sadaka za vinywaji, vitu vyote vile vilivyokuwa vimetengenezwa kwa dhahabu safi au fedha.

20 Shaba iliyotokana na zile nguzo mbili, ile Bahari na wale mafahali kumi na mawili wa shaba waliokuwa chini yake, pamoja na vile vishikilio vilivyohamishika, ambavyo Mfalme Solomoni alikuwa ametengeneza kwa ajili ya Hekalu laBwana, ilikuwa na uzito usioweza kupimika.

21 Kila nguzo ilikuwa na urefu wa dhiraa kumi na nane, kimo chake na mzunguko dhiraa kumi na mbili, na unene wa nyanda nne, na zote zilikuwa wazi ndani.

22 Sehemu ya shaba juu ya ile nguzo moja ilikuwa na urefu wa dhiraa tano, na ilikuwa imepambwa kwa wavu na makomamanga ya shaba kuizunguka kote. Ile nguzo nyingine pamoja na makomamanga yake ilifanana na hiyo ya kwanza.

23 Kulikuwa na makomamanga tisini na sita pembeni; jumla ya makomamanga juu ya wavu uliokuwa umezunguka yalikuwa mia moja.

24 Yule jemadari wa askari walinzi akawachukua kama wafungwa Seraya kuhani mkuu, kuhani Sefania aliyefuata kwa cheo, na mabawabu watatu.

25 Miongoni mwa wale watu waliokuwa wamesalia katika mji, alimchukua afisa kiongozi wa wapiganaji, na washauri saba wa mfalme. Akamchukua pia mwandishi aliyesimamia uandikishaji wa watu wa nchi, pamoja na watu wake sitini waliopatikana ndani ya mji.

26 Nebuzaradani jemadari akawachukua hao wote na kuwapeleka kwa mfalme wa Babeli huko Ribla.

27 Huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, mfalme wa Babeli akaamuru wanyongwe.

Hivyo Yuda wakaenda utumwani, mbali na nchi yao.

28 Hii ndiyo hesabu ya watu ambao Nebukadneza aliwachukua kwenda uhamishoni:

katika mwaka wa saba,

Wayahudi 3,023;

29 katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Nebukadneza,

watu 832 kutoka Yerusalemu;

30 katika mwaka wa ishirini na tatu wa utawala wake,

Wayahudi 745 walichukuliwa kwenda uhamishoni na Nebuzaradani jemadari wa askari walinzi wa mfalme.

Jumla ya watu wote walikuwa 4,600.

Yehoyakini Anaachiwa Huru

31 Katika mwaka wa thelathini na saba tangu Yehoyakini mfalme wa Yuda apelekwe uhamishoni, katika mwaka ule ambao Evil-Merodakialifanyika mfalme wa Babeli, alimwacha huru Yehoyakini mfalme wa Yuda, na kumfungua kutoka gerezani siku ya ishirini na tano ya mwezi wa kumi na mbili.

32 Alizungumza naye kwa upole na kumpa kiti cha heshima zaidi kuliko wale wafalme wengine aliokuwa nao huko Babeli.

33 Hivyo Yehoyakini akayavua mavazi yake ya mfungwa, na siku zote za maisha yake zilizobaki alikula mezani mwa mfalme.

34 Siku kwa siku mfalme wa Babeli alimpa Yehoyakini posho siku zote za maisha yake, hadi siku ya kifo chake.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JER/52-c2b86b923a92dc454bdb791d63c04e8c.mp3?version_id=1627—