Categories
Warumi

Warumi 10

1 Ndugu zangu, shauku ya moyo wangu na maombi yangu kwa Mungu ni kwa ajili ya Waisraeli, kwamba waokolewe.

2 Kwa maana ninaweza nikashuhudia wazi kwamba wao wana juhudi kubwa kwa ajili ya Mungu, lakini juhudi yao haina maarifa.

3 Kwa kuwa hawakuijua haki itokayo kwa Mungu, wakatafuta kuweka haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya Mungu.

4 Kwa maana Kristo ni ukomo wa sheria ili kuwe na haki kwa kila mtu aaminiye.

Wokovu Ni Kwa Ajili Ya Wote

5 Mose anaandika kuhusu haki ile itokanayo na sheria, kwamba, “Mtu atendaye matendo hayo ataishi kwa hayo.”

6 Lakini ile haki itokanayo na imani husema hivi: “Usiseme moyoni mwako, ‘Ni nani atakayepanda mbinguni?’ ” (yaani ili kumleta Kristo chini)

7 “au ‘Ni nani atashuka kwenda kuzimu?’ ” (yaani ili kumleta Kristo kutoka kwa wafu.)

8 Lakini andiko lasemaje? “Lile neno liko karibu nawe, liko kinywani mwako na moyoni mwako,” yaani, lile neno la imani tunalolihubiri.

9 Kwa sababu kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba “Yesu ni Bwana,” na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka.

10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini na hivyo kuhesabiwa haki, tena kwa kinywa mtu hukiri na hivyo kupata wokovu.

11 Kama yasemavyo Maandiko, “Yeyote amwaminiye hataaibika kamwe.”

12 Kwa maana hakuna tofauti kati ya Myahudi na Myunani, yeye ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao.

13 Kwa maana, “Kila mtu atakayeliitia Jina la Bwana, ataokolewa.”

14 Lakini watamwitaje yeye ambaye hawajamwamini? Nao watawezaje kumwamini yeye ambaye hawajamsikia? Tena watamsikiaje bila mtu kuwahubiria?

15 Nao watahubirije wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, “Tazama jinsi ilivyo mizuri miguu yao wale wanaohubiri habari njema!”

16 Lakini si wote waliotii Habari Njema. Kwa maana Isaya asema, “Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?”

17 Basi, imani chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Kristo.

18 Lakini nauliza: Je, wao hawakusikia? Naam, wamesikia, kwa maana:

“Sauti yao imeenea duniani pote,

nayo maneno yao yameenea

hadi miisho ya ulimwengu.”

19 Nami nauliza tena: Je, Waisraeli hawakuelewa? Kwanza, Mose asema,

“Nitawafanya mwe na wivu

kwa watu wale ambao si taifa.

Nitawakasirisha kwa taifa

lile lisilo na ufahamu.”

20 Naye Isaya kwa ujasiri mwingi anasema,

“Nimeonekana na watu wale ambao hawakunitafuta.

Nilijifunua kwa watu

wale ambao hawakunitafuta.”

21 Lakini kuhusu Israeli anasema,

“Mchana kutwa nimewanyooshea

watu wakaidi na wasiotii mikono yangu.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ROM/10-0864d8898873b398cc4cf456076702ae.mp3?version_id=1627—

Categories
Warumi

Warumi 11

Mabaki Ya Israeli

1 Basi nauliza: Je, Mungu amewakataa watu wake? La, hasha! Mimi mwenyewe ni Mwisraeli, tena uzao wa Abrahamu kutoka kabila la Benyamini.

2 Mungu hajawakataa watu wake, ambao yeye aliwajua tangu mwanzo. Je, hamjui yale Maandiko yasemayo kuhusu Eliya, jinsi alivyomlalamikia Mungu kuhusu Israeli?

3 Alisema, “Bwana, wamewaua manabii wako na kuzibomoa madhabahu zako, nimebaki mimi peke yangu, nao wanataka kuniua?”

4 Je, Mungu alimjibuje? “Nimejibakizia watu elfu saba ambao hawajapiga magoti kumwabudu Baali.”

5 Vivyo hivyo pia, sasa wapo mabaki waliochaguliwa kwa neema ya Mungu.

6 Lakini ikiwa wamechaguliwa kwa neema, si tena kwa msingi wa matendo. Kama ingekuwa kwa matendo, neema isingekuwa neema tena.

7 Tuseme nini basi? Kile kitu ambacho Israeli alikitafuta kwa bidii hakukipata. Lakini waliochaguliwa walikipata. Waliobaki walifanywa wagumu,

8 kama ilivyoandikwa:

“Mungu aliwapa bumbuazi la mioyo,

macho ili wasiweze kuona,

na masikio ili wasiweze kusikia,

hadi leo.”

9 Naye Daudi anasema:

“Karamu zao na ziwe tanzi na mtego wa kuwanasa,

kitu cha kuwakwaza waanguke, na adhabu kwao.

10 Macho yao yatiwe giza ili wasiweze kuona,

nayo migongo yao iinamishwe daima.”

Matawi Yaliyopandikizwa

11 Hivyo nauliza tena: Je, Waisraeli walijikwaa ili waanguke na kuangamia kabisa? La, hasha! Lakini kwa sababu ya makosa yao, wokovu umewafikia watu wa Mataifa, ili kuwafanya Waisraeli waone wivu.

12 Basi ikiwa kukosa kwao kumekuwa utajiri mkubwa kwa ulimwengu, tena kama kuangamia kwao kumeleta utajiri kwa watu wa Mataifa, kurudishwa kwao kutaleta utajiri mkuu zaidi.

13 Sasa ninasema nanyi watu wa Mataifa. Maadamu mimi ni mtume kwa watu wa Mataifa, naitukuza huduma yangu

14 ili kuwafanya watu wangu waone wivu na hivyo kuwaokoa baadhi yao.

15 Kwa kuwa ikiwa kukataliwa kwao ni kupatanishwa kwa ulimwengu, kukubaliwa kwao si kutakuwa ni uhai baada ya kufa?

16 Kama sehemu ya donge la unga uliotolewa kuwa limbuko ni mtakatifu, basi unga wote ni mtakatifu, nalo shina kama ni takatifu, vivyo hivyo na matawi nayo.

17 Lakini kama baadhi ya matawi yalikatwa, nawe chipukizi la mzeituni mwitu ukapandikizwa mahali pao ili kushiriki unono pamoja na matawi mengine kutoka shina la mzeituni,

18 basi usijivune juu ya hayo matawi. Kama ukijivuna, kumbuka jambo hili: si wewe unayelishikilia shina, bali ni shina linalokushikilia wewe.

19 Basi utasema, “Matawi yale yalikatwa ili nipate kupandikizwa katika hilo shina.”

20 Hii ni kweli. Matawi hayo yalikatwa kwa sababu ya kutokuamini kwake, lakini wewe umesimama tu kwa sababu ya imani. Kwa hiyo usijivune, bali simama kwa kuogopa.

21 Kwa maana kama Mungu hakuyahurumia matawi ya asili, wala hatakuhurumia wewe.

22 Angalia basi wema na ukali wa Mungu: Kwa wale walioanguka, ukali, bali kwako wewe wema wa Mungu, kama utadumu katika wema wake. La sivyo, nawe utakatiliwa mbali.

23 Wao nao wasipodumu katika kutokuamini kwao, watapandikizwa tena kwenye shina, kwa maana Mungu anao uwezo wa kuwapandikiza tena kwenye hilo shina.

24 Ikiwa wewe ulikatwa kutoka kile ambacho kwa asili ni mzeituni mwitu na kupandikizwa kinyume cha asili kwenye mzeituni uliopandwa, si rahisi zaidi matawi haya ya asili kupandikizwa tena kwenye shina lake la mzeituni!

Israeli Wote Wataokolewa

25 Ndugu zangu, ili msije mkajidai kuwa wenye hekima kuliko mlivyo, nataka mfahamu siri hii: Ugumu umewapata Israeli kwa sehemu hadi idadi ya watu wa Mataifa watakaoingia itimie.

26 Hivyo Israeli wote wataokolewa. Kama ilivyoandikwa:

“Mkombozi atakuja kutoka Sayuni;

ataondoa kutokumcha Mungu katika Yakobo.

27 Hili ndilo agano langu nao

nitakapoziondoa dhambi zao.”

28 Kwa habari ya Injili, wao ni adui wa Mungu kwa ajili yenu, lakini kuhusu kule kuteuliwa kwao ni wapendwa, kwa ajili ya mababa zao wa zamani,

29 kwa maana akishawapa watu karama, Mungu haziondoi, wala wito wake.

30 Kama vile ninyi wakati fulani mlivyokuwa waasi kwa Mungu lakini sasa mmepata rehema kwa sababu ya kutokutii kwao,

31 hivyo nao Waisraeli wamekuwa waasi ili kwamba wao nao sasa waweze kupata rehema kwa ajili ya rehema za Mungu kwenu.

32 Kwa maana Mungu amewafunga wanadamu wote kwenye kuasi ili apate kuwarehemu wote.

Wimbo Wa Shukrani

33 Tazama jinsi kilivyo kina cha utajiri

wa hekima na maarifa ya Mungu!

Tazama jinsi ambavyo hukumu zake hazichunguziki,

na ambavyo njia zake zisivyotafutikana!

34 “Ni nani aliyeyafahamu mawazo ya Bwana?

Au ni nani ambaye amekuwa mshauri wake?”

35 “Au ni nani aliyempa chochote

ili arudishiwe?”

36 Kwa maana vitu vyote vyatoka kwake, viko kwake na kwa ajili yake.

Utukufu ni wake milele! Amen.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ROM/11-b1d98791aabb237f65b14fb331a3ce53.mp3?version_id=1627—

Categories
Warumi

Warumi 12

Maisha Mapya Katika Kristo

1 Kwa hiyo, ndugu zangu, nawasihi kwa rehema zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na inayompendeza Mungu, hii ndiyo ibada yenu yenye maana.

2 Msifuatishe tena mfano wa ulimwengu huu, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu. Ndipo mtaweza kuonja na kuhakikisha ni nini mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yanayopendeza machoni pake na ukamilifu.

3 Kwa ajili ya neema niliyopewa nawaambia kila mmoja miongoni mwenu, asijidhanie kuwa bora kuliko impasavyo, bali afikiri kwa busara kwa kulingana na kipimo cha imani Mungu aliyompa.

4 Kama vile katika mwili mmoja tulivyo na viungo vingi, navyo viungo vyote havina kazi moja,

5 vivyo hivyo na sisi tulio wengi, tu mwili mmoja katika Kristo, nasi kila mmoja ni kiungo cha mwenzake.

6 Tuna karama zilizotofautiana kila mmoja kutokana na neema tuliyopewa. Kama ni unabii na tutoe unabii kwa kadiri ya imani.

7 Kama ni kuhudumu na tuhudumu, mwenye kufundisha na afundishe,

8 kama ni kutia moyo na atie moyo, kama ni kuchangia kwa ajili ya mahitaji ya wengine na atoe kwa ukarimu, kama ni uongozi na aongoze kwa bidii, kama ni kuhurumia wengine na afanye hivyo kwa furaha.

Alama Za Mkristo Wa Kweli

9 Upendo lazima usiwe na unafiki. Chukieni lililo ovu, shikamaneni na lililo jema.

10 Pendaneni ninyi kwa ninyi kwa upendo wa ndugu. Waheshimuni na kuwatanguliza wengine.

11 Msiwe wavivu, bali mwe na bidii katika roho mkimtumikia Bwana.

12 Kuweni na furaha katika tumaini, katika dhiki kuweni na saburi, dumuni katika maombi.

13 Changieni katika mahitaji ya watakatifu, wakaribisheni wageni.

14 Wabarikini wale wanaowatesa, barikini wala msilaani.

15 Furahini pamoja na wenye kufurahi, lieni pamoja na wale waliao.

16 Kaeni kwa amani ninyi kwa ninyi. Msijivune, bali mwe tayari kushirikiana na wanyonge. Wala msiwe watu wenye kujivuna kwamba mnajua kila kitu.

17 Msimlipe mtu yeyote ovu kwa ovu. Jitahidini ili mtende yaliyo mema machoni pa watu wote.

18 Kama ikiwezekana, kwa upande wenu kaeni kwa amani na watu wote.

19 Wapendwa, msilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu, maana imeandikwa: “Ni juu yangu kulipiza kisasi, nitalipiza,” asema Bwana.

20 Badala yake:

“Kama adui yako ana njaa, mlishe;

kama ana kiu, mpe kinywaji.

Kwa kufanya hivyo,

unaweka makaa ya moto yanayowaka kichwani pake.”

21 Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ROM/12-9debfb689fdc0715f082d1c879de661f.mp3?version_id=1627—

Categories
Warumi

Warumi 13

Kutii Mamlaka

1 Kila mtu na atii mamlaka inayotawala, kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu, nazo mamlaka zilizopo zimewekwa na Mungu.

2 Kwa hiyo yeye anayeasi dhidi ya mamlaka inayotawala anaasi dhidi ya kile kilichowekwa na Mungu, nao wale wafanyao hivyo watajiletea hukumu juu yao wenyewe.

3 Kwa kuwa watawala hawawatishi watu wale wanaotenda mema bali wale wanaotenda mabaya. Je, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Basi tenda lile lililo jema naye atakusifu.

4 Kwa maana mwenye mamlaka ni mtumishi wa Mungu kwa ajili ya mema. Lakini kama ukitenda mabaya, basi ogopa, kwa kuwa hauinui upanga bila sababu. Yeye ni mtumishi wa Mungu, mjumbe wa Mungu wa kutekeleza adhabu juu ya watenda mabaya.

5 Kwa hiyo ni lazima kutii wenye mamlaka, si kwa sababu ya kuogopa adhabu iwezayo kutolewa, bali pia kwa ajili ya dhamiri.

6 Kwa sababu hii mnalipa kodi, kwa maana watawala ni watumishi wa Mungu, ambao hutumia muda wao wote kutawala.

7 Mlipeni kila mtu kile mnachodaiwa. Kama mnadaiwa kodi lipeni kodi, kama ni ushuru, lipeni ushuru, astahiliye hofu, mhofu, astahiliye heshima, mheshimu.

Kupendana Kila Mmoja Na Mwingine

8 Msidaiwe kitu na mtu yeyote, isipokuwa kupendana, kwa maana yeye ampendaye mwenzake, ameitimiza sheria.

9 Kwa kuwa amri hizi zisemazo, “Usizini,” “Usiue,” “Usiibe,” “Usitamani,” na amri nyingine zote, zinajumlishwa katika amri hii moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.”

10 Upendo haumfanyii jirani jambo baya. Kwa hiyo upendo ndio utimilifu wa sheria.

11 Nanyi fanyeni hivi, mkiutambua wakati tulio nao. Saa ya kuamka kutoka usingizini imewadia, kwa maana sasa wokovu wetu umekaribia zaidi kuliko hapo kwanza tulipoamini.

12 Usiku umeendelea sana, mapambazuko yamekaribia. Kwa hiyo tuyaweke kando matendo ya giza na tuvae silaha za nuru.

13 Basi na tuenende kwa adabu kama inavyopasa wakati wa mchana, si kwa kufanya karamu za ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu.

14 Bali jivikeni Bwana Yesu Kristo, wala msifikiri jinsi mtakavyotimiza tamaa za miili yenu yenye asili ya dhambi.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ROM/13-a99c95b3f20bfd209712046088710c0b.mp3?version_id=1627—

Categories
Warumi

Warumi 14

Msiwahukumu Wengine

1 Mkaribisheni yeye ambaye imani yake ni dhaifu, lakini si kwa kugombana na kubishana juu ya mawazo yake.

2 Mtu mmoja imani yake inamruhusu kula kila kitu, lakini mwingine ambaye imani yake ni dhaifu, hula mboga tu.

3 Yeye alaye kila kitu asimdharau yeye asiyekula. Wala yeye asiyekula kila kitu asimhukumu yule alaye kila kitu, kwa maana Mungu amemkubali.

4 Wewe ni nani hata umhukumu mtumishi wa mtu mwingine? Kwa bwana wake tu anasimama au kuanguka. Naye atasimama kwa sababu Bwana anaweza kumsimamisha.

5 Mtu mmoja anaitukuza siku fulani kuwa ni bora kuliko nyingine, na mwingine anaona kuwa siku zote ni sawa. Basi kila mmoja awe na hakika na yale anayoamini.

6 Yeye anayehesabu siku moja kuwa takatifu kuliko nyingine, hufanya hivyo kwa kumheshimu Bwana. Naye alaye nyama hula kwa Bwana, kwa maana humshukuru Mungu, naye akataaye kula nyama hufanya hivyo kwa Bwana na humshukuru Mungu.

7 Kwa kuwa hakuna hata mmoja wetu anayeishi kwa ajili yake mwenyewe, wala hakuna hata mmoja wetu afaye kwa ajili yake mwenyewe.

8 Kama tunaishi, tunaishi kwa Bwana, nasi pia tukifa tunakufa kwa Bwana. Kwa hiyo basi, kama tukiishi au kama tukifa, sisi ni mali ya Bwana.

9 Kwani kwa sababu hii hasa, Kristo alikufa na akawa hai tena kusudi apate kuwa Bwana wa wote, yaani, waliokufa na walio hai.

10 Basi kwa nini wewe wamhukumu ndugu yako? Au kwa nini wewe unamdharau ndugu yako? Kwa kuwa sote tutasimama mbele ya kiti cha Mungu cha hukumu.

11 Kwa kuwa imeandikwa:

“ ‘Kama vile niishivyo,’ asema Bwana,

‘kila goti litapigwa mbele zangu,

na kila ulimi utakiri kwa Mungu.’ ”

12 Hivyo basi kila mmoja wetu atatoa habari zake mwenyewe kwa Mungu.

Usimfanye Ndugu Yako Ajikwae

13 Kwa hiyo tusiendelee kuhukumiana: Badala yake mtu asiweke kamwe kikwazo au kizuizi katika njia ya ndugu mwingine.

14 Ninajua tena nimehakikishiwa sana katika Bwana Yesu kwamba hakuna kitu chochote ambacho ni najisi kwa asili yake. Lakini kama mtu anakiona kitu kuwa ni najisi, basi kwake huyo kitu hicho ni najisi.

15 Kama ndugu yako anahuzunishwa kwa sababu ya kile unachokula, basi huenendi tena katika upendo. Usiruhusu kile unachokula kiwe sababu ya kumwangamiza ndugu yako ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake.

16 Usiruhusu kile ambacho unakiona kuwa chema kisemwe kuwa ni kiovu.

17 Kwa maana Ufalme wa Mungu si kula na kunywa, bali ni haki, amani na furaha katika Roho Mtakatifu.

18 Kwa sababu mtu yeyote anayemtumikia Kristo kwa jinsi hii, anampendeza Mungu na kukubaliwa na wanadamu.

19 Kwa hiyo na tufanye bidii kutafuta yale yaletayo amani na kujengana sisi kwa sisi.

20 Usiiharibu kazi ya Mungu kwa ajili ya chakula. Hakika vyakula vyote ni safi, lakini ni kosa kula kitu chochote kinachomsababisha ndugu yako ajikwae.

21 Ni afadhali kutokula nyama wala kunywa divai au kufanya jambo lingine lolote litakalomsababisha ndugu yako ajikwae.

22 Je, wewe unayo imani? Ile imani uliyo nayo, uwe nayo nafsini mwako mbele za Mungu. Heri mtu yule asiye na sababu ya kujihukumu nafsi yake kwa ajili ya kile anachokifanya.

23 Lakini kama mtu ana shaka kuhusu kile anachokula, amehukumiwa, kwa sababu hakula kwa imani. Kwa kuwa chochote kinachofanywa pasipo imani ni dhambi.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ROM/14-9f0688f7d0e4128d08a0ad65b0b5a4f4.mp3?version_id=1627—

Categories
Warumi

Warumi 15

Usijipendeze Mwenyewe, Bali Wapendeze Wengine

1 Sisi tulio na nguvu, hatuna budi kuchukuliana na kushindwa kwa wale walio dhaifu wala si kujipendeza nafsi zetu wenyewe.

2 Kila mmoja wetu inampasa kumpendeza jirani yake kwa mambo mema, ili kumjenga katika imani.

3 Kwa maana hata Kristo hakujipendeza mwenyewe, bali kama ilivyoandikwa: “Matukano yao wale wanaokutukana wewe yalinipata mimi.”

4 Kwa maana kila kitu kilichoandikwa zamani, kiliandikwa kutufundisha, ili kwamba kwa saburi na faraja tunayopata katika Maandiko tuwe na tumaini.

5 Mungu atoaye saburi na faraja, awajalie ninyi roho ya umoja miongoni mwenu mnapomfuata Kristo Yesu,

6 ili kwa moyo mmoja mpate kumtukuza Mungu aliye Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo.

Injili Sawa Kwa Wayahudi Na Kwa Watu Wa Mataifa

7 Karibishaneni ninyi kwa ninyi kama Kristo alivyowakaribisha ninyi ili kumletea Mungu utukufu.

8 Kwa maana nawaambia kwamba, Kristo amekuwa mtumishi kwa wale waliotahiriwa ili kuonyesha kweli ya Mungu na kuthibitisha zile ahadi walizopewa baba zetu wa zamani,

9 pia ili watu wa Mataifa wamtukuze Mungu kwa rehema zake. Kama ilivyoandikwa:

“Kwa hiyo nitakutukuza katikati ya watu wa Mataifa;

nitaliimbia sifa jina lako.”

10 Tena yasema,

“Enyi watu wa Mataifa, furahini

pamoja na watu wa Mungu.”

11 Tena,

“Msifuni Bwana, ninyi watu wa Mataifa wote,

na kumwimbia sifa, enyi watu wote.”

12 Tena Isaya anasema,

“Shina la Yese litachipuka,

yeye atakayeinuka ili kutawala juu ya mataifa.

Watu wa Mataifa watamtumaini.”

13 Mungu wa tumaini awajaze ninyi furaha yote na amani katika kumwamini, ili mpate kujawa na tumaini tele kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.

Paulo Mhudumu Wa Watu Wa Mataifa

14 Ndugu zangu, mimi mwenyewe ninasadiki kwamba mmejaa wema na ufahamu wote, tena mnaweza kufundishana ninyi kwa ninyi.

15 Nimewaandikia kwa ujasiri vipengele kadha wa kadha katika waraka huu kama kuwakumbusha tena kwa habari ya ile neema Mungu aliyonipa,

16 ili kuwa mhudumu wa Kristo Yesu kwa watu wa Mataifa nikiwa na huduma ya kikuhani ya kutangaza Injili ya Mungu, ili watu wa Mataifa wapate kuwa dhabihu inayokubaliwa na Mungu, iliyotakaswa na Roho Mtakatifu.

17 Kwa hiyo ninajisifu katika Kristo Yesu, kwenye utumishi wangu kwa Mungu.

18 Kwa maana sitathubutu kusema kitu chochote zaidi ya kile ambacho Kristo amefanya kwa kunitumia mimi katika kuwaongoza watu wa Mataifa wamtii Mungu kwa yale niliyosema na kufanya,

19 kwa nguvu za ishara na miujiza, kwa uweza wa Roho wa Mungu, hivyo kuanzia Yerusalemu hadi maeneo yote ya kandokando yake mpaka Iliriko, nimekwisha kuihubiri Injili ya Kristo kwa ukamilifu.

20 Hivyo ni nia yangu kuhubiri Habari Njema, si pale ambapo Kristo amekwisha kujulikana, ili nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine.

21 Lakini kama ilivyoandikwa:

“Wale ambao hawajahubiriwa habari zake wataona,

nao wale ambao hawajazisikia watafahamu.”

22 Hii ndiyo sababu nimezuiliwa mara nyingi nisiweze kuja kwenu.

Paulo Apanga Kwenda Rumi

23 Lakini sasa kwa kuwa hakuna nafasi zaidi kwa ajili yangu katika sehemu hii, ninatamani kuja kwenu kama ambavyo nimekuwa na shauku kwa miaka mingi.

24 Nimekusudia kufanya hivyo nitakapokuwa njiani kwenda Hispania. Natarajia kuwaona katika safari yangu na kusafirishwa nanyi mpaka huko, baada ya kufurahia ushirika wenu kwa kitambo kidogo.

25 Sasa, niko njiani kuelekea Yerusalemu kwa ajili ya kuwahudumia watakatifu huko.

26 Kwa kuwa imewapendeza watu wa Makedonia na Akaya kufanya changizo kwa ajili ya maskini walioko miongoni mwa watakatifu huko Yerusalemu.

27 Imewapendeza kufanya hivyo, naam, kwani ni wadeni wao. Kwa maana ikiwa watu wa Mataifa wameshiriki baraka za rohoni za Wayahudi, wao ni wadeni wa Wayahudi, ili Wayahudi nao washiriki baraka zao za mambo ya mwilini.

28 Kwa hiyo baada ya kukamilisha kazi hii na kuhakikisha kuwa wamepokea kila kitu kilichokusanywa, nitapitia kwenu nikiwa njiani kwenda Hispania.

29 Ninajua kwamba nitakapokuja kwenu, nitakuja na wingi wa baraka za Kristo.

30 Basi, ndugu zangu, nawasihi kwa Jina la Bwana wetu Yesu Kristo na kwa upendo wa Roho Mtakatifu, kujiunga nami katika taabu zangu mkiniombea kwa Mungu.

31 Ombeni ili nipate kuokolewa mikononi mwa wale wasioamini walioko Uyahudi, na kwamba utumishi wangu upate kukubaliwa na watakatifu wa huko Yerusalemu,

32 ili kwa mapenzi ya Mungu niweze kuja kwenu kwa furaha, nami niburudishwe pamoja nanyi.

33 Mungu wa amani na awe pamoja nanyi nyote. Amen.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ROM/15-6d1ac9c8fb537f5de196c0e8410e19ea.mp3?version_id=1627—

Categories
Warumi

Warumi 16

Salamu Kwa Watu Binafsi

1 Napenda kumtambulisha kwenu dada yetu Foibe, mtumishi katika kanisa la Kenkrea.

2 Naomba mpokeeni katika Bwana ipasavyo watakatifu na kumpa msaada wowote atakaohitaji kutoka kwenu, kwa maana yeye amekuwa msaada kwa watu wengi, mimi nikiwa miongoni mwao.

3 Wasalimuni Prisilana Akila, watumishi wenzangu katika Kristo Yesu.

4 Wao walihatarisha maisha yao kwa ajili yangu; wala si mimi tu ninayewashukuru bali pia makanisa yote ya watu wa Mataifa.

5 Lisalimuni pia kanisa linalokutana nyumbani mwao.

Msalimuni rafiki yangu mpendwa Epaineto, aliyekuwa mtu wa kwanza kumwamini Kristo huko Asia.

6 Msalimuni Maria, aliyefanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu.

7 Wasalimuni Androniko na Yunia, jamaa zangu ambao wamekuwa gerezani pamoja nami. Wao ni maarufu miongoni mwa mitume, nao walikuwa katika Kristo kabla yangu.

8 Msalimuni Ampliato, yeye nimpendaye katika Bwana.

9 Msalimuni Urbano, mtendakazi mwenzetu katika Kristo, pamoja na rafiki yangu mpendwa Stakisi.

10 Msalimuni Apele aliyejaribiwa na akaithibitisha imani yake katika Kristo.

Wasalimuni wote walio nyumbani mwa Aristobulo.

11 Msalimuni ndugu yangu Herodioni.

Wasalimuni wote walio nyumbani mwa Narkisi walio katika Bwana.

12 Wasalimuni Trifaina na Trifosa, wale wanawake wanaofanya kazi kwa bidii katika Bwana.

Msalimuni rafiki yangu mpendwa Persisi, mwanamke mwingine aliyefanya kazi kwa bidii katika Bwana.

13 Msalimuni Rufo, mteule katika Bwana, pamoja na mama yake, ambaye amekuwa mama kwangu pia.

14 Wasalimuni Asinkrito, Flegoni, Herme, Patroba, Herma na ndugu wote walio pamoja nao.

15 Wasalimuni Filologo, Yulia, Nerea na dada yake, na Olimpa na watakatifu wote walio pamoja nao.

16 Salimianeni ninyi kwa ninyi kwa busu takatifu.

Makanisa yote ya Kristo yanawasalimu.

Maelekezo Ya Mwisho

17 Ndugu zangu, nawasihi mjihadhari na kujiepusha na wale watu waletao matengano na kuweka vikwazo mbele yenu dhidi ya mafundisho mliyojifunza.

18 Kwa maana watu kama hao hawamtumikii Bwana Kristo, bali wanatumikia tamaa zao wenyewe. Kwa kutumia maneno laini na ya kubembeleza, hupotosha mioyo ya watu wajinga.

19 Kila mtu amesikia juu ya utii wenu, nami nimejawa na furaha tele kwa ajili yenu. Lakini nataka mwe na hekima katika mambo mema na bila hatia katika mambo maovu.

20 Mungu wa amani atamponda Shetani chini ya miguu yenu upesi.

Neema ya Bwana wetu Yesu iwe nanyi. Amen.

21 Timotheo, mtendakazi mwenzangu anawasalimu. Vivyo hivyo Lukio, Yasoni, na Sosipatro, ndugu zangu.

22 Mimi, Tertio, niliye mwandishi wa waraka huu, nawasalimu katika Bwana.

23 Gayo, ambaye ni mwenyeji wangu na wa kanisa lote, anawasalimu.

Erasto, mweka hazina wa mji huu, pamoja na Kwarto ndugu yetu pia wanawasalimu.

[

24 Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja nanyi nyote. Amen.]

Maneno Ya Mwisho Ya Kumsifu Mungu

25 Sasa atukuzwe yeye awezaye kuwafanya ninyi imara kwa Injili yangu na kuhubiriwa kwa Yesu Kristo, kutokana na kufunuliwa siri zilizofichika tangu zamani za kale.

26 Lakini sasa siri hiyo imefunuliwa na kujulikana kupitia maandiko ya kinabii kutokana na amri ya Mungu wa milele, ili mataifa yote yaweze kumwamini na kumtii

27 Mungu aliye pekee, mwenye hekima, ambaye kwa njia ya Yesu Kristo utukufu ni wake milele na milele! Amen.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ROM/16-1c31ad45264650f46d6ec3d62bf50cff.mp3?version_id=1627—