Categories
Waebrania

Waebrania Utangulizi

Utangulizi

Waraka kwa Waebrania unajulikana kama kitabu cha mambo yaliyo bora, kwa sababu unazungumzia ukuu wa Kristo na kumdhihirisha kama ufunuo wa mwisho wa Mungu. Unabii na ahadi zilizoandikwa katika Agano la Kale zimetimizwa katika Agano Jipya, Kristo akiwa Mpatanishi. Kristo pia athibitishwa kuwa mkuu zaidi ya manabii, malaika, na Mose (ambaye alikuwa mpatanishi wa agano la hapo awali).

Msomaji ameonywa asidharau wala kukataa wokovu mkuu uliotolewa kupitia kwake Kristo. Uwezekano mkubwa ni kwamba waraka huu ulielekezwa kwa Wakristo Wayahudi huko Palestina au Rumi, waliokuwa wanajaribiwa kugeukia tena dini ya Kiyahudi, au kuifanya Injili iwe yenye mfumo wa dini ya Kiyahudi.

Mwandishi

Ingawa waraka hauna jina la mwandishi, una ushahidi mwingi kwamba alikuwa mtu wa kizazi cha pili cha Wakristo aliyekuwa na ujuzi sana wa Agano la Kale.

Kusudi

Mwandishi anamwonyesha Yesu kuwa ndiye ukamilifu wa ufunuo ulionenwa kwanza na Mungu, na kisha na manabii wake.

Mahali

Rumi.

Tarehe

Kabla ya kuharibiwa kwa Hekalu la Yerusalemu mwaka wa 70 B.K.

Wahusika Wakuu

Yesu, Yoshua, Mose, Melkizedeki, Abrahamu, makuhani, malaika, na watu wenye imani wa Agano la Kale.

Wazo Kuu

Kiini cha Waebrania ni mamlaka na uweza wa Yesu Kristo kama Mjumbe wa neema ya Mungu. Kitabu hiki kinatoa sifa za majina ya heshima zaidi ya ishirini yaliyomtaja Yesu Kristo katika huduma ya ukuhani na ya ufalme.

Mambo Muhimu

Yesu Kristo ni mngʼao wa utukufu wa Mungu, na pia Kristo ni mkuu kuliko malaika, mkuu kuliko viongozi wote, na mkuu kuliko makuhani.

Mgawanyo

Mnenaji bora kwa ajili ya Mungu (

1:1–4:13

)

Mwombezi au Kuhani aliye bora (

4:14–7:28

)

Agano na Dhabihu iliyo bora (

8:1–10:18

)

Agizo la kuitunza na kuilinda imani (

11:1–12:29

)

Mwisho: Kanuni za maisha ya Kikristo, na maelezo ya binafsi (

13:1-25

).

Categories
Waebrania

Waebrania 1

Mwana Ni Mkuu Kuliko Malaika

1 Zamani Mungu alisema na baba zetu kwa njia ya manabii mara nyingi na kwa njia mbalimbali,

2 lakini katika siku hizi za mwisho anasema nasi kwa njia ya Mwanawe, ambaye amemweka kuwa mrithi wa vitu vyote, na ambaye kupitia kwake aliuumba ulimwengu.

3 Mwana ni mngʼao wa utukufu wa Mungu na mfano halisi wa nafsi yake, akivihifadhi vitu vyote kwa neno lake lenye uweza. Akiisha kufanya utakaso kwa ajili ya dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Aliye Mkuu huko mbinguni.

4 Kwa hiyo alifanyika bora kuliko malaika, kama jina alilorithi lilivyo bora kuliko lao.

5 Kwa maana ni malaika yupi ambaye wakati wowote Mungu alipata kumwambia,

“Wewe ni Mwanangu;

leo mimi nimekuzaa?”

Au tena,

“Mimi nitakuwa Baba yake,

naye atakuwa Mwanangu?”

6 Tena, Mungu amletapo mzaliwa wake wa kwanza ulimwenguni, anasema,

“Malaika wote wa Mungu na wamsujudu.”

7 Anenapo kuhusu malaika asema,

“Huwafanya malaika wake kuwa pepo,

watumishi wake kuwa miali ya moto.”

8 Lakini kwa habari za Mwana asema,

“Kiti chako cha enzi, Ee Mungu,

kitadumu milele na milele,

nayo haki itakuwa fimbo ya utawala

ya ufalme wako.

9 Umependa haki na kuchukia uovu;

kwa hiyo Mungu, Mungu wako,

amekuweka juu ya wenzako

kwa kukupaka mafuta ya furaha.”

10 Pia asema,

“Hapo mwanzo, Ee Bwana, uliweka misingi ya dunia,

nazo mbingu ni kazi ya mikono yako.

11 Hizo zitatoweka, lakini wewe utadumu;

zote zitachakaa kama vazi.

12 Utazikungʼutakungʼuta kama joho,

nazo zitachakaa kama vazi.

Lakini wewe hubadiliki,

nayo miaka yako haikomi kamwe.”

13 Je, ni kwa malaika yupi ambaye Mungu amepata kumwambia wakati wowote,

“Keti mkono wangu wa kuume,

hadi nitakapowaweka adui zako

chini ya miguu yako”?

14 Je, malaika wote si roho watumikao, waliotumwa kuwahudumia wale watakaourithi wokovu?

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/HEB/1-477941132c7f821e41229c8efd63f530.mp3?version_id=1627—

Categories
Waebrania

Waebrania 2

Wokovu Mkuu

1 Kwa hiyo, imetupasa kuwa waangalifu sana kuhusu kile tulichosikia, ili tusije tukakiacha.

2 Kwa kuwa kama ujumbe ulionenwa na malaika ulikuwa imara, na kila uasi na kutokutii kulipata adhabu ya haki,

3 je, sisi tutapaje kupona kama tusipojali wokovu mkuu namna hii? Wokovu huu, ambao mwanzo ulitangazwa na Bwana, ulithibitishwa kwetu na wale waliomsikia.

4 Pia Mungu aliushuhudia kwa ishara, maajabu na kwa miujiza mbalimbali, na karama za Roho Mtakatifu alizozigawa kulingana na mapenzi yake.

Yesu Alifananishwa Na Ndugu Zake

5 Mungu hakuuweka ulimwengu ujao ambao tunanena habari zake chini ya malaika.

6 Lakini kuna mahali mtu fulani ameshuhudia akisema:

“Mwanadamu ni kitu gani hata unamfikiria,

binadamu ni nani hata unamjali?

7 Umemfanya chini kidogo kuliko malaika;

ukamvika taji ya utukufu na heshima,

8 nawe umeweka vitu vyote chini ya miguu yake.”

Kwa kuweka vitu vyote chini yake, Mungu hakuacha kitu chochote ambacho hakukiweka chini ya mwanadamu. Lakini kwa sasa, hatuoni kwamba kila kitu kiko chini yake.

9 Lakini twamwona Yesu, aliyefanywa chini kidogo kuliko malaika, sasa akiwa amevikwa taji ya utukufu na heshima kwa sababu alistahimili mauti, ili kwamba kwa neema ya Mungu apate kuonja mauti kwa ajili ya kila mtu.

10 Ili kuwaleta wana wengi katika utukufu, ilifaa kwamba Mungu, ambaye ni kwa ajili yake na kupitia kwake kila kitu kimekuwepo, amkamilishe mwanzilishi wa wokovu wao kwa njia ya mateso.

11 Yeye awafanyaye watu kuwa watakatifu, pamoja na hao ambao hufanywa watakatifu, wote hutoka katika jamaa moja. Hivyo Yesu haoni aibu kuwaita ndugu zake.

12 Yeye husema,

“Nitalitangaza jina lako kwa ndugu zangu;

mbele ya kusanyiko nitaimba sifa zako.”

13 Tena,

“Nitaweka tumaini langu kwake.”

Tena anasema,

“Niko hapa, pamoja na watoto ambao Mungu amenipa.”

14 Basi kwa kuwa watoto wana nyama na damu, yeye pia alishiriki katika ubinadamu wao, ili kwa kifo chake, apate kumwangamiza huyo mwenye nguvu za mauti, yaani ibilisi,

15 na kuwaweka huru wale waliokuwa utumwani maisha yao yote kwa sababu ya kuogopa mauti.

16 Kwa kuwa ni dhahiri kwamba hakuja kusaidia malaika, bali uzao wa Abrahamu.

17 Kwa sababu hii ilibidi afanane na ndugu zake kwa kila hali, ili apate kuwa Kuhani Mkuu mwenye huruma na mwaminifu katika kumtumikia Mungu, ili pia apate kufanya upatanisho kwa ajili ya dhambi za watu.

18 Kwa kuwa yeye mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wale wanaojaribiwa.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/HEB/2-78e98b66fd5465ac246ee7a9922b7933.mp3?version_id=1627—

Categories
Waebrania

Waebrania 3

Yesu Ni Mkuu Kuliko Mose

1 Kwa hiyo ndugu watakatifu, mnaoshiriki mwito wa mbinguni, mtafakarini Yesu, mtume na Kuhani Mkuu wa ukiri wetu.

2 Alikuwa mwaminifu kwa yeye aliyemweka, kama vile Mose alivyokuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu.

3 Yesu ameonekana anastahili heshima kubwa kuliko Mose, kama vile mjenzi wa nyumba alivyo wa heshima kubwa kuliko nyumba yenyewe.

4 Kwa kuwa kila nyumba hujengwa na mtu fulani, lakini Mungu ni mjenzi wa kila kitu.

5 Basi Mose kama mtumishi alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu, akishuhudia kwa yale ambayo yangetamkwa baadaye.

6 Lakini Kristo ni mwaminifu kama Mwana katika nyumba ya Mungu. Sisi ndio nyumba yake, kama tutashikilia sana ujasiri wetu na tumaini tunalojivunia.

Onyo Dhidi Ya Kutokuamini

7 Kwa hiyo, kama Roho Mtakatifu asemavyo:

“Leo, kama mkiisikia sauti yake,

8 msiifanye mioyo yenu migumu,

kama mlivyofanya katika uasi,

wakati ule wa kujaribiwa jangwani,

9 ambapo baba zenu walinijaribu na kunipima

ingawa kwa miaka arobaini

walikuwa wameyaona matendo yangu.

10 Hiyo ndiyo sababu nilikasirikia kizazi kile,

nami nikasema, ‘Siku zote mioyo yao imepotoka,

nao hawajazijua njia zangu.’

11 Hivyo nikatangaza kwa kiapo katika hasira yangu,

‘Kamwe hawataingia rahani mwangu.’ ”

12 Ndugu zangu, angalieni, asiwepo miongoni mwenu mtu mwenye moyo mwovu usioamini, unaojitenga na Mungu aliye hai.

13 Lakini mtiane moyo mtu na mwenzake kila siku, maadamu iitwapo Leo, ili asiwepo hata mmoja wenu mwenye kufanywa mgumu kwa udanganyifu wa dhambi.

14 Kwa kuwa tumekuwa washiriki wa Kristo, kama tukishikamana tu kwa uthabiti na tumaini letu la kwanza hadi mwisho.

15 Kama ilivyonenwa:

“Leo, kama mkiisikia sauti yake,

msiifanye mioyo yenu migumu

kama mlivyofanya wakati wa kuasi.”

16 Basi ni nani waliosikia lakini bado wakaasi? Je, si wale wote waliotoka Misri wakiongozwa na Mose?

17 Lakini ni nani aliowakasirikia miaka arobaini? Je, si wale waliofanya dhambi ambao miili yao ilianguka jangwani?

18 Ni nani hao ambao Mungu aliapa kuwa kamwe hawataingia rahani mwake isipokuwa ni wale waliokataa kutii?

19 Hivyo tunaona kwamba hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutokuamini kwao.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/HEB/3-3c941f65ae9207abfe401f52a09facf3.mp3?version_id=1627—

Categories
Waebrania

Waebrania 4

Pumziko Aliloahidi Mungu

1 Kwa hiyo, kwa kuwa bado ahadi ya kuingia rahani iko wazi, tujihadhari ili hata mmoja wenu asije akaikosa.

2 Kwa maana sisi pia tumesikia Injili iliyohubiriwa kwetu, kama nao walivyosikia; lakini ujumbe ule waliousikia haukuwa na maana kwao, kwa sababu wale waliousikia hawakuuchanganya na imani.

3 Sasa sisi ambao tumeamini tunaingia katika ile raha, kama vile Mungu alivyosema,

“Kwa hiyo nikaapa katika hasira yangu,

‘Kamwe hawataingia rahani mwangu.’ ”

Lakini kazi yake ilikamilika tangu kuumbwa kwa ulimwengu.

4 Kwa maana mahali fulani amezungumza kuhusu siku ya saba, akisema: “Katika siku ya saba Mungu alipumzika kutoka kazi zake zote.”

5 Tena hapo juu asema, “Kamwe hawataingia rahani mwangu.”

6 Kwa hiyo inabaki kuwa wazi kwa wengine kuingia, nao wale wa kwanza waliopokea Injili walishindwa kuingia kwa sababu ya kutokutii.

7 Kwa hiyo Mungu ameweka siku nyingine, akaiita Leo, akisema kwa kinywa cha Daudi baadaye sana, kwa maneno yaliyotangulia kunenwa:

“Leo, kama mkiisikia sauti yake,

msiifanye mioyo yenu migumu.”

8 Kwa maana kama Yoshua alikuwa amewapa raha, Mungu hangesema tena baadaye kuhusu siku nyingine.

9 Kwa hiyo basi, imebaki raha ya Sabato kwa ajili ya watu wa Mungu;

10 kwa kuwa kila mmoja aingiaye katika raha ya Mungu pia hupumzika kutoka kazi zake mwenyewe, kama vile Mungu alivyopumzika kutoka kazi zake.

11 Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha hiyo, ili kwamba asiwepo yeyote atakayeanguka kwa kufuata mfano wao wa kutokutii.

12 Kwa maana Neno la Mungu li hai tena lina nguvu. Lina makali kuliko upanga wowote wenye makali kuwili, hivyo linachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, viungo na mafuta yaliyo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.

13 Wala hakuna kiumbe chochote kilichofichika machoni pa Mungu. Kila kitu kimefunuliwa na kiko wazi machoni pake yeye ambaye kwake ni lazima tutatoa hesabu.

Yesu Kristo Kuhani Mkuu Kuliko Wote

14 Kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu kuliko wote ambaye ameingia mbinguni, Yesu Mwana wa Mungu, basi na tushikamane sana kwa uthabiti na ule ukiri wa imani yetu.

15 Kwa kuwa hatuna Kuhani Mkuu asiyeweza kuchukuliana na sisi katika udhaifu wetu, lakini tunaye mmoja ambaye alijaribiwa kwa kila namna, kama vile sisi tujaribiwavyo: lakini yeye hakutenda dhambi.

16 Basi na tukikaribie kiti cha rehema kwa ujasiri, ili tupewe rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/HEB/4-bea9946e8920fbc208b7fa3ba515811a.mp3?version_id=1627—

Categories
Waebrania

Waebrania 5

1 Kwa maana kila kuhani mkuu anayechaguliwa miongoni mwa wanadamu anawekwa kuwawakilisha kwa mambo yanayomhusu Mungu, ili apate kutoa matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi.

2 Kwa kuwa yeye mwenyewe ni dhaifu, aweza kuwachukulia kwa upole wale wasiojua na kupotoka.

3 Hii ndiyo sababu inampasa kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe na vivyo hivyo kwa ajili ya dhambi za watu.

4 Hakuna anayejitwalia heshima hii mwenyewe; ni lazima aitwe na Mungu, kama vile Aroni alivyoitwa.

5 Pia Kristo hakujitwalia utukufu yeye mwenyewe wa kuwa Kuhani Mkuu, bali Mungu alimwambia,

“Wewe ni Mwanangu;

leo mimi nimekuzaa.”

6 Pia mahali pengine asema,

“Wewe ni kuhani milele,

kwa mfano wa Melkizedeki.”

7 Katika siku za maisha ya Yesu hapa duniani, alimtolea maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, yeye awezaye kumwokoa na mauti, naye Mungu akamsikia kwa sababu ya kutii kwake kwa unyenyekevu.

8 Ingawa alikuwa Mwana, alijifunza utiifu kutokana na mateso aliyoyapata,

9 na akiisha kukamilishwa, akawa chanzo cha wokovu wa milele kwa wote wanaomtii.

10 Naye amewekwa na Mungu kuwa Kuhani Mkuu kwa mfano wa Melkizedeki.

Wito Wa Kukua Kiroho

11 Tunayo mengi ya kusema kuhusu habari ya ukuhani huu, lakini ni vigumu kuyaeleza, kwa sababu ninyi ni wazito wa kuelewa.

12 Kwa hakika, ingawa mpaka wakati huu ingewapasa kuwa walimu, bado mnahitaji mtu wa kuwafundisha tena hatua za awali za kweli ya Neno la Mungu. Mnahitaji maziwa, wala si chakula kigumu!

13 Kwa maana yeyote aishiye kwa kunywa maziwa bado yeye ni mtoto mchanga, hana ujuzi katika mafundisho kuhusu neno la haki.

14 Lakini chakula kigumu ni kwa ajili ya watu wazima, ambao kwa kujizoeza wamejifunza kupambanua kati ya mema na mabaya.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/HEB/5-889f21e3462b55b0e6311925acdd954c.mp3?version_id=1627—

Categories
Waebrania

Waebrania 6

Hatari Ya Kuanguka

1 Kwa hiyo, tukiachana na mafundisho yale ya awali kuhusu Kristo na tukisonga mbele ili tufikie utimilifu, sio kuweka tena msingi wa mafundisho ya kuzitubia kazi zisizo na uhai na imani katika Mungu,

2 mafundisho kuhusu aina za ubatizo, kuwekea watu mikono, ufufuo wa wafu, na hukumu ya milele.

3 Mungu akitujalia tutafanya hivyo.

4 Kwa kuwa ni vigumu kwa wale ambao wakati fulani walishapata nuru, ambao walishaonja kipawa cha mbinguni, ambao wamekwisha kushiriki katika Roho Mtakatifu,

5 ambao wameonja uzuri wa Neno la Mungu na nguvu za wakati ujao,

6 kisha wakianguka, kuwarejesha tena katika toba. Kwa kuwa wanamsulubisha Mwana wa Mungu mara ya pili na kumdhalilisha hadharani, nayo ikawa hasara kwao.

7 Ardhi ile ipokeayo mvua inyeshayo juu yake mara kwa mara hutoa mazao yanayowanufaisha wale ambao kwa ajili yao yalimwa, nayo nchi hiyo hupokea baraka kutoka kwa Mungu.

8 Lakini ardhi ikizaa miiba na mibaruti, haina thamani na iko hatarini ya kulaaniwa. Mwisho wake ni kuchomwa moto.

9 Ingawa tunasema hivi, ndugu zangu wapendwa, kwa upande wenu tuna hakika ya mambo mema zaidi, mambo yale yahusuyo wokovu.

10 Mungu si mdhalimu: yeye hataisahau kazi yenu na upendo ule mlioonyesha kwa ajili yake katika kuwahudumia watakatifu na hata sasa mnaendelea kuwahudumia.

11 Nasi twataka kila mmoja wenu aonyeshe bidii iyo hiyo ili mpate kujua uhakika kamili wa lile tumaini mpaka mwisho,

12 ili msije mkawa wavivu, bali mpate kuwaiga wale ambao kwa imani na saburi hurithi zile ahadi.

Uhakika Wa Ahadi Ya Mungu

13 Mungu alipompa Abrahamu ahadi yake, kwa kuwa hakuwepo mwingine aliyekuwa mkuu kuliko yeye ambaye angeweza kuapa kwa jina lake, aliapa kwa nafsi yake,

14 akisema, “Hakika nitakubariki na kukupa wazao wengi.”

15 Abrahamu naye, baada ya kungoja kwa saburi, alipokea kile kilichoahidiwa.

16 Wanadamu huapa kwa yeye aliye mkuu kuwaliko, nacho kiapo hicho huthibitisha kile kilichosemwa na hivyo humaliza mabishano yote.

17 Mungu alipotaka kuonyesha kwa udhahiri zaidi ile asili ya kutokubadilika kwa ahadi yake kwa warithi wa ahadi, aliithitibisha kwa kiapo.

18 Mungu alifanya hivyo ili kwa vitu viwili visivyobadilika, yaani ahadi yake na kiapo chake, ambavyo kwavyo Mungu hawezi kusema uongo, sisi ambao tumemkimbilia ili tulishike lile tumaini lililowekwa mbele yetu tuwe na faraja thabiti.

19 Tunalo tumaini hili kama nanga ya roho iliyo imara na thabiti. Tumaini hili huingia katika sehemu takatifu iliyopo nyuma ya pazia,

20 mahali ambapo Yesu mtangulizi wetu aliingia kwa niaba yetu. Yeye amekuwa Kuhani Mkuu milele, kwa mfano wa Melkizedeki.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/HEB/6-9c32152f6ae0491e330bc3ac47a5d53b.mp3?version_id=1627—

Categories
Waebrania

Waebrania 7

Kuhani Melkizedeki

1 Kwa kuwa huyu Melkizedeki alikuwa mfalme wa Salemu na kuhani wa Mungu Aliye Juu Sana. Alipokutana na Abrahamu akirudi kutoka kuwashinda hao wafalme, Melkizedeki alimbariki,

2 naye Abrahamu alimpa sehemu ya kumiya kila kitu. Kwanza, jina hilo Melkizedeki maana yake ni “mfalme wa haki.” Na pia “mfalme wa Salemu” maana yake ni “mfalme wa amani.”

3 Hana Baba wala mama, hana ukoo, hana mwanzo wala mwisho wa siku zake. Kama Mwana wa Mungu, yeye adumu akiwa kuhani milele.

4 Tazama jinsi alivyokuwa mkuu: Hata Abrahamu, baba yetu mkuu, alimpa sehemu ya kumi ya nyara zake.

5 Basi sheria inawaagiza wana wa Lawi ambao hufanyika makuhani kupokea sehemu ya kumi kutoka kwa watu ambao ni ndugu zao, ingawa ndugu zao ni wazao wa Abrahamu.

6 Huyu Melkizedeki, ingawa hakufuatia ukoo wake kutoka kwa Lawi, lakini alipokea sehemu ya kumi kutoka kwa Abrahamu na kumbariki yeye aliyekuwa na zile ahadi.

7 Wala hakuna shaka kwamba mdogo hubarikiwa na aliye mkuu kumliko yeye.

8 Kwa upande mmoja, sehemu ya kumi hupokelewa na wale ambao hupatikana na kufa; lakini kwa upande mwingine hupokelewa na yeye ambaye hushuhudiwa kuwa yu hai.

9 Mtu anaweza hata kusema kwamba Lawi, ambaye hupokea sehemu ya kumi, alitoa hiyo sehemu ya kumi kupitia kwa Abrahamu,

10 kwa sababu Melkizedeki alipokutana na Abrahamu, Lawi alikuwa bado katika viuno vya baba yake wa zamani.

Yesu Mfano Wa Melkizedeki

11 Kama ukamilifu ungeweza kupatikana kwa njia ya ukuhani wa Walawi (kwa kuwa katika msingi huo, sheria ilitolewa kwa watu), kwa nini basi imekuwepo haja ya kuja kuhani mwingine: kuhani kwa mfano wa Melkizedeki, wala si kwa mfano wa Aroni?

12 Kwa kuwa yanapotokea mabadiliko ya ukuhani, pia lazima yawepo mabadiliko ya sheria.

13 Yeye ambaye mambo haya yanasemwa alikuwa wa kabila lingine, na hakuna mtu wa kabila hilo aliyewahi kuhudumu katika madhabahu.

14 Kwa maana ni dhahiri kwamba Bwana wetu alitoka katika uzao wa Yuda, tena kuhusu kabila hilo Mose hakusema lolote kwa habari za makuhani.

15 Tena hayo tuliyosema yako wazi zaidi kama akitokea kuhani mwingine kama Melkizedeki,

16 yeye ambaye amefanyika kuhani si kwa misingi ya sheria kama ilivyokuwa kwa baba zake, bali kwa misingi ya uwezo wa uzima usioharibika.

17 Kwa maana imeshuhudiwa kwamba:

“Wewe ni kuhani milele,

kwa mfano wa Melkizedeki.”

18 Kwa upande mmoja, ile amri ya mwanzo isiyofaa na dhaifu imebatilishwa

19 (kwa maana sheria haikufanya kitu chochote kuwa kikamilifu). Kwa upande mwingine, tumeletewa tumaini lililo bora zaidi ambalo linatuleta karibu na Mungu.

20 Nalo tumaini hilo halikutolewa pasipo kiapo! Wengine walikuwa makuhani pasipo kiapo chochote,

21 lakini Yesu alifanywa kuhani kwa kiapo wakati Mungu alimwambia:

“Bwanaameapa

naye hatabadilisha mawazo yake:

‘Wewe ni kuhani milele.’ ”

22 Kwa ajili ya kiapo hiki, Yesu amekuwa mdhamini wa agano lililo bora zaidi.

23 Basi pamekuwepo na makuhani wengi wa aina hiyo, kwa kuwa kifo kiliwazuia kuendelea na huduma yao ya ukuhani.

24 Lakini kwa sababu Yesu anaishi milele, anao ukuhani wa kudumu.

25 Kwa hiyo anaweza kuwaokoa kabisa wale wanaomjia Mungu kupitia kwake, kwa sababu yeye adumu daima kuomba kwa ajili yao.

26 Kwa kuwa ilitupasa tuwe na Kuhani Mkuu wa namna hii, yaani, aliye mtakatifu, asiye na lawama, asiye na dosari, aliyetengwa na wenye dhambi na kuinuliwa juu ya mbingu.

27 Yeye hahitaji kutoa dhabihu siku kwa siku kwa ajili ya dhambi, kwanza kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za watu kama wale makuhani wakuu wengine. Yeye alitoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zao mara moja tu, alipojitoa mwenyewe.

28 Kwa kuwa sheria huwaweka makuhani wakuu watu ambao ni dhaifu; lakini lile neno la kiapo, lililokuja baada ya sheria, lilimweka Mwana, ambaye amefanywa kuwa mkamilifu milele.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/HEB/7-f144e85acd4bddbb9e7842805e3327e0.mp3?version_id=1627—

Categories
Waebrania

Waebrania 8

Kuhani Mkuu Wa Agano Jipya

1 Basi jambo tunalotaka kulisema ni hili: Tunaye Kuhani Mkuu ambaye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Aliye Mkuu mbinguni,

2 yeye ahudumuye katika patakatifu, hema la kweli lililowekwa na Bwana, wala si na mwanadamu.

3 Kila kuhani mkuu huwekwa ili atoe sadaka na dhabihu. Vivyo hivyo, ilikuwa jambo muhimu kwa huyu Kuhani naye awe na kitu cha kutoa.

4 Kama angekuwa duniani, hangekuwa kuhani, kwa sababu tayari wapo watu watoao sadaka kama ilivyoelekezwa na sheria.

5 Wanahudumu katika patakatifu palipo mfano na kivuli cha mambo ya mbinguni. Hii ndiyo sababu Mose alionywa alipokaribia kujenga hema, akiambiwa: “Hakikisha kuwa unavitengeneza vitu vyote kwa mfano ulioonyeshwa kule mlimani.”

6 Lakini huduma aliyopewa Yesu ni bora zaidi kuliko yao, kama vile agano ambalo yeye ni mpatanishi wake lilivyo bora zaidi kuliko lile la zamani, nalo limewekwa misingi wa ahadi zilizo bora zaidi.

7 Kwa maana kama hapakuwa na kasoro katika lile agano la kwanza, pasingekuwa na haja ya kutafuta nafasi kwa ajili ya jingine.

8 Lakini Mungu aliona kosa kwa watu, naye akasema:

“Siku zinakuja, asema Bwana,

nitakapofanya agano jipya

na nyumba ya Israeli

na nyumba ya Yuda.

9 Agano langu halitakuwa kama lile

nililofanya na baba zao

nilipowashika mkono

kuwaongoza watoke nchi ya Misri,

kwa sababu hawakuendelea kuwa waaminifu katika agano langu,

nami nikawaacha,

asema Bwana.

10 Hili ndilo agano nitakalofanya na nyumba ya Israeli

baada ya siku zile, asema Bwana.

Nitaziweka sheria zangu katika nia zao

na kuziandika mioyoni mwao.

Nitakuwa Mungu wao,

nao watakuwa watu wangu.

11 Mtu hatamfundisha tena jirani yake,

wala mtu kumfundisha ndugu yake akisema, ‘Mjue Bwana,’

kwa sababu wote watanijua mimi,

tangu aliye mdogo kabisa kwao, hadi aliye mkuu sana.

12 Kwa sababu nitasamehe uovu wao,

wala sitazikumbuka dhambi zao tena!”

13 Kwa kuliita agano hili “jipya,” Mungu amefanya lile agano la kwanza kuwa kuukuu; nacho kitu kinachoanza kuchakaa na kuwa kikuukuu kiko karibu kutoweka.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/HEB/8-da391403df16dc980a95b56a1ce4abd0.mp3?version_id=1627—

Categories
Waebrania

Waebrania 9

Ibada Katika Hema La Kidunia

1 Basi agano lile la kwanza lilikuwa na kanuni zake za kuabudu na pia patakatifu pake pa kidunia.

2 Hema ilitengenezwa. Katika sehemu yake ya kwanza kulikuwa na kinara cha taa, meza na mikate iliyowekwa wakfu; hii sehemu iliitwa Mahali Patakatifu.

3 Nyuma ya pazia la pili, palikuwa na sehemu iliyoitwa Patakatifu pa Patakatifu,

4 ambapo palikuwa na yale madhabahu ya dhahabu ya kufukizia uvumba, na lile Sanduku la Agano lililofunikwa kwa dhahabu. Sanduku hili lilikuwa na gudulia la dhahabu lenye mana, ile fimbo ya Aroni iliyochipuka, na vile vibao vya mawe vya Agano.

5 Juu ya lile Sanduku kulikuwa na makerubi ya Utukufu yakitilia kivuli kile kifuniko ambacho ndicho kiti cha rehema. Lakini hatuwezi kueleza vitu hivi kwa undani sasa.

6 Basi vitu hivi vilipokuwa vimepangwa, makuhani waliingia daima katika sehemu ya kwanza ya hema ili kufanya taratibu zao za ibada.

7 Lakini ni kuhani mkuu peke yake aliyeingia ndani ya sehemu ya pili ya hema. Tena hii ilikuwa mara moja tu kwa mwaka, na hakuingia kamwe bila damu, ambayo alitoa kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya dhambi za watu walizotenda bila kukusudia.

8 Kwa njia hii, Roho Mtakatifu alikuwa anaonyesha kwamba, maadamu ile hema ya kwanza ilikuwa bado imesimama, njia ya kuingia Patakatifu pa Patakafifu ilikuwa bado haijafunguliwa.

9 Huu ulikuwa mfano kwa ajili ya wakati wa sasa, kuonyesha kwamba sadaka na dhabihu zilizokuwa zikitolewa hazikuweza kusafisha dhamiri ya mtu anayeabudu.

10 Lakini hizi zilishughulika tu na vyakula na vinywaji, pamoja na taratibu mbalimbali za kunawa kwa nje, kanuni kwa ajili ya mwili zilizowekwa hadi wakati utimie wa matengenezo mapya.

Damu Ya Kristo

11 Kristo alipokuja akiwa Kuhani Mkuu wa mambo mema ambayo tayari yameshawasili, alipitia kwenye hema iliyo kuu zaidi na bora zaidi, ambayo haikutengenezwa kwa mikono ya binadamu, hii ni kusema, ambayo si sehemu ya uumbaji huu.

12 Hakuingia kwa njia ya damu ya mbuzi na ya ndama; lakini aliingia Patakatifu pa Patakatifu mara moja tu kwa damu yake mwenyewe, akiisha kupata ukombozi wa milele.

13 Damu ya mbuzi na ya mafahali, na majivu ya mitamba walivyonyunyiziwa wale waliokuwa najisi kwa taratibu za kiibada viliwatakasa, hata kuwaondolea uchafu wa nje.

14 Basi ni zaidi aje damu ya Kristo, ambaye kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na waa, itatusafisha dhamiri zetu kutokana na matendo yaletayo mauti, ili tupate kumtumikia Mungu aliye hai!

15 Kwa sababu hii Kristo ni mpatanishi wa agano jipya, ili kwamba wale walioitwa waweze kupokea ile ahadi ya urithi wa milele: kwa vile yeye alikufa awe ukombozi wao kutoka kwa dhambi walizozitenda chini ya agano la kwanza.

16 Kwa habari ya wosia,ni muhimu kuthibitisha kifo cha yule aliyeutoa,

17 kwa sababu wosia huwa na nguvu tu wakati mtu ameshakufa; kamwe hauwezi kutumika wakati yule aliyeuandika bado yuko hai.

18 Hii ndiyo sababu hata lile agano la kwanza halikuweza kutekelezwa pasipo damu.

19 Mose alipotangaza kila amri kwa watu wote, alichukua damu ya ndama na ya mbuzi, pamoja na maji, sufu nyekundu na matawi ya mti wa hisopo, akanyunyizia kile kitabu na watu wote.

20 Alisema, “Hii ndiyo damu ya agano, ambalo Mungu amewaamuru kulitii.”

21 Vivyo hivyo alinyunyizia damu hiyo kwenye ile hema pamoja na kila kifaa kilichotumika ndani yake kwa taratibu za ibada.

22 Kwa kweli sheria hudai kwamba, karibu kila kitu kitakaswe kwa damu, wala pasipo kumwaga damu, hakuna msamaha wa dhambi.

23 Kwa hiyo, ilikuwa muhimu kwa nakala za vitu vile vya mbinguni vitakaswe kwa dhabihu hizi, lakini vitu halisi vya mbinguni vilihitaji dhabihu bora kuliko hizi.

24 Kwa maana Kristo hakuingia kwenye patakatifu palipofanywa kwa mikono ya mwanadamu, ambao ni mfano wa kile kilicho halisi. Yeye aliingia mbinguni penyewe, ili sasa aonekane mbele za Mungu kwa ajili yetu.

25 Wala hakuingia mbinguni ili apate kujitoa mwenyewe mara kwa mara, kama vile kuhani mkuu aingiavyo Patakatifu pa Patakatifu kila mwaka kwa damu ambayo si yake mwenyewe.

26 Ingekuwa hivyo, ingempasa Kristo kuteswa mara nyingi tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Lakini sasa ametokea mara moja tu katika mwisho wa nyakati aiondoe dhambi kwa kujitoa mwenyewe kuwa dhabihu.

27 Kama vile mwanadamu alivyowekewa kufa mara moja tu na baada ya kufa akabili hukumu,

28 vivyo hivyo Kristo alitolewa mara moja tu kuwa dhabihu ili azichukue dhambi za watu wengi. Naye atakuja mara ya pili, sio kuchukua dhambi, bali kuwaletea wokovu wale wanaomngoja kwa shauku.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/HEB/9-f44d655b87c155325a0281f316f39de8.mp3?version_id=1627—