Categories
Waamuzi

Waamuzi Utangulizi

Utangulizi

Jina la kitabu hiki limetokana na viongozi waliojulikana kama Waamuzi ambao Mungu aliwainua kuongoza nchi ya Israeli. Hii ilitokana na kupotoka kwingi na kurudi nyuma kwa wana wa Israeli baada ya kifo cha Yoshua. Kwa sababu yeye alikuwa amewachagua kuwa watu wake, ambao kupitia kwao watu wote wangeweza kujua upendo wa Mungu, basi Mungu asingewaacha waanguke kabisa chini ya uonevu wa adui zao. Kitabu hiki kinaelezea habari za Waisraeli kwa kipindi kati ya kifo cha Yoshua na huduma ya Samweli.

Mungu alikuwa amewasaidia Waisraeli kuishinda na kuiteka Kanaani, ambako ndani yake yaliishi mataifa mengi maovu. Lakini walikuwa katika hatari ya kuipoteza hii Nchi ya Ahadi kwa sababu walianza kumwasi Mungu. Walipomrudia Mungu, naye Mungu aliwainulia Waamuzi wa kuwaokoa kutoka mikononi mwa adui zao, na kuwarudisha tena katika njia na kusudi lake, na kuwaongoza. Hivyo kipindi hiki kilijulikana kwa mashujaa walioitwa Waamuzi ambao ndio walioongoza makabila ya Israeli. Jumla ya waamuzi kumi na wanne wameorodheshwa kuwa waliiongoza Israeli katika kitabu hiki. Waliojulikana zaidi walikuwa Yefta, Debora, Gideoni na Samsoni.

Mataifa yaliyowaonea Waisraeli wakati wa kipindi hiki cha Waamuzi yalikuwa: Wakaldayo, Wamoabu, Wakanaani, Wamidiani, Waamoni na Wafilisti. Kipindi hiki cha Waamuzi kilidumu kwa miaka 410 kikitazamwa na vile matukio yalivyofuatana.

Mwandishi

Mwandishi wa kitabu hiki hajulikani ni nani, lakini mapokeo ya Kiyahudi yanasema ni Samweli.

Kusudi

Ni kuonyesha kwamba hukumu ya Mungu juu ya dhambi ni lazima, na pia kuwasamahe na kuwarudisha waliotubu katika uhusiano wake ni lazima.

Mahali

Nchi ya Kanaani ambayo baadaye iliitwa Israeli.

Tarehe

Wakati kitabu hiki kiliandikwa haujulikani.

Wahusika Wakuu

Othnieli, Ehudi, Debora, Gideoni, Abimeleki, Yefta, Samsoni na Delila.

Wazo Kuu

Baada ya Yoshua kufariki, Waisraeli walikuwa wakiinuka walipompata kiongozi na baada ya kiongozi huyo kufariki walipotoka na kuangukia mikononi mwa maadui zao. Walipomlilia Mungu aliwainulia mwamuzi, ambaye aliwaongoza na kuwapa ushindi.

Mambo Muhimu

Mambo mawili muhimu katika kitabu cha Waamuzi ni vile Waisraeli waligandamizwa na mataifa jirani kwa sababu ya kumwasi Mungu, na vile Mungu aliwakomboa kutoka kwa watesi wao baada ya kutubu na kumrudia.

Mgawanyo

Waisraeli kushindwa kuyafukuza kabisa mataifa yaliyokuwa nchi ya Kanaani (

1:1–3:6

)

Waamuzi kuwakomboa Waisraeli (

3:7–16:31

)

Waisraeli kuanguka kiroho, kimaadili na kisiasa (

17:1–21:25

).

Categories
Waamuzi

Waamuzi 1

Israeli Wapigana Na Wakanaani Waliobaki

1 Baada ya kifo cha Yoshua, Waisraeli wakamuulizaBwana, “Ni nani atakayetangulia kupanda mbele yetu kwa ajili ya kupigana na Wakanaani?”

2 Bwanaakajibu, “Yuda ndiye atakayetangulia; nimewapa hiyo nchi mikononi mwao.”

3 Ndipo watu wa Yuda wakawaambia Wasimeoni ndugu zao, “Pandeni pamoja nasi katika nchi tuliyopewa, ili tupate kupigana na Wakanaani. Sisi pia tutakwenda pamoja nanyi katika sehemu yenu mliyopewa.” Basi Wasimeoni wakaenda pamoja nao.

4 Yuda aliposhambulia,Bwanaakawatia Wakanaani na Waperizi mikononi mwao, nao wakawaua watu 10,000 huko Bezeki.

5 Huko ndiko walipomkuta huyo Adoni-Bezeki, nao wakapigana naye na kuwafanya Wakanaani na Waperizi wakimbie.

6 Adoni-Bezeki pia alikimbia, nao wakamfuata na kumkamata, wakamkata vidole vyake gumba vya mikono na vya miguu.

7 Ndipo Adoni-Bezeki akasema, “Nimewatendea wafalme sabini kama nilivyotendewa na kuwalisha makombo ya chakula chini ya meza yangu. Sasa Mungu amenilipa haya, kama yale niliyowatendea.” Wakamleta Yerusalemu, naye akafa huko.

8 Watu wa Yuda wakashambulia pia Yerusalemu na kuiteka. Wakaupiga mji kwa upanga na kuuchoma kwa moto.

9 Baada ya hayo, watu wa Yuda wakateremka kupigana na Wakanaani walioishi katika nchi ya vilima, yaani, Negebu na nchi chini ya vilima vya magharibi.

10 Yuda wakakabiliana na Wakanaani walioishi Hebroni (ambayo hapo kwanza iliitwa Kiriath-Arba) na kuwashinda Sheshai, Ahimani na Talmai.

11 Kutoka huko wakasonga mbele kukabiliana na watu walioishi Debiri (ambao hapo kwanza uliitwa Kiriath-Seferi.)

12 Kalebu akasema, “Nitamwoza binti yangu Aksa kwa mtu atakayeweza kupigana na kuteka Kiriath-Seferi.”

13 Basi Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa huyo Kalebu, akawashinda, kwa hiyo Kalebu akamtoa binti yake Aksa akaolewa naye.

14 Siku moja Aksa alipokuja kwa Othnieli, alimsihi Othnieli amwombe baba yake, Kalebu, shamba. Aksa aliposhuka kutoka juu ya punda wake, Kalebu akamuuliza, “Je, wataka nikufanyie nini?”

15 Akamjibu, “Naomba unifanyie jambo moja la hisani. Kwa kuwa umenipa ardhi huko Negebu, nipe pia chemchemi za maji.” Ndipo Kalebu akampa chemchemi za juu na za chini.

16 Wazao wa yule Mkeni, baba mkwe wa Mose, wakapanda pamoja na watu wa Yuda kutoka Mji wa Mitende,wakaenda kuishi miongoni mwa watu wa jangwa ya Yuda huko Negebu karibu na mji wa Aradi.

17 Basi watu wa Yuda wakaenda na Wasimeoni ndugu zao kushambulia Wakanaani waishio Sefathi, nao wakauangamiza huo mji kabisa. Kwa hiyo huo mji ukaitwa Horma

18 Watu wa Yuda wakatwaa pia Gaza, Ashkeloni na Ekroni, kila mji na vijiji vyake vinavyouzunguka.

19 Bwanaalikuwa pamoja na watu wa Yuda. Wakaimiliki nchi ya vilima, lakini hawakuweza kuwafukuza watu waliokaa katika hiyo tambarare, kwa sababu walikuwa na magari ya chuma.

20 Kama vile Mose alivyoahidi, Kalebu alipewa Hebroni, naye akawafukuza wana watatu wa Anaki.

21 Hata hivyo, Wabenyamini walishindwa kuwafukuza Wayebusi, waliokuwa wanaishi Yerusalemu; hivyo hadi leo Wayebusi huishi humo pamoja na Wabenyamini.

22 Basi nyumba ya Yosefu wakashambulia Betheli, nayeBwanaalikuwa pamoja nao.

23 Walipotuma watu kwenda kupeleleza Betheli (ambao hapo kwanza uliitwa Luzu),

24 wale wapelelezi wakaona mtu anatoka mjini, nao wakamwambia, “Tuonyeshe jinsi ya kuingia mjini nasi tutakutendea wema.”

25 Hivyo akawaonyesha, nao wakaupiga mji kwa upanga lakini wakamhifadhi hai yule mtu na jamaa yake yote.

26 Yule mtu akaenda hadi nchi ya Wahiti, ambapo aliujenga mji na kuuita Luzu, ambao ndio jina lake hadi leo.

27 Lakini Manase hawakuwafukuza watu wa Beth-Shani na vijiji vyake, au watu wa Taanaki na vijiji vyake, au watu wa Dori na vijiji vyake, au watu wa Ibleamu na vijiji vyake, au watu wa Megido na vijiji vyake, lakini Wakanaani waliazimu kuishi katika nchi ile.

28 Israeli walipopata nguvu, wakawatia Wakanaani katika kazi ya kulazimishwa, lakini kamwe hawakuwafukuza watoke kabisa.

29 Wala Efraimu hawakuwafukuza kabisa Wakanaani walioishi Gezeri, bali Wakanaani waliendelea kuishi humo miongoni mwao.

30 Vivyo hivyo Zabuloni hawakuwafukuza Wakanaani walioishi huko Kitroni, wala walioishi Nahaloli, ambao walibaki miongoni mwao; bali waliwatia katika kazi ya kulazimishwa.

31 Wala Asheri hawakuwafukuza wale walioishi huko Ako, Sidoni, Alabu, Akzibu, Helba, Afeki wala Rehobu

32 na kwa sababu ya jambo hili Waasheri wakaishi miongoni mwa Wakanaani, wenyeji wa nchi.

33 Wala Naftali hawakuwafukuza wale walioishi Beth-Shemeshi wala wale walioishi Beth-Anathi; lakini Naftali nao pia wakaishi miongoni mwa Wakanaani, wenyeji wa nchi, nao wale walioishi Beth-Shemeshi na Beth-Anathi wakawa watumishi wao katika kazi ya kulazimishwa.

34 Waamori wakawazuilia Wadani kwenye nchi ya vilima, kwa maana hawakuwaacha washuke kuingia kwenye sehemu tambarare.

35 Waamori pia wakaendelea kukaa katika Mlima Heresi, katika Aiyaloni na Shaalbimu, lakini mkono wa nyumba ya Yosefu ukawalemea, nao wakashindwa hata wakalazimika kuingia katika kazi ya kulazimishwa.

36 Mpaka wa Waamori ulikuwa kuanzia Genge la Akrabimu, kuendelea hadi Sela na kuelekea juu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JDG/1-22c681990a665b316a7d299bf06d47a5.mp3?version_id=1627—

Categories
Waamuzi

Waamuzi 2

Malaika Wa Bwana Huko Bokimu

1 Malaika waBwanaakakwea kutoka Gilgali hadi Bokimu, naye akasema, “Niliwapandisha kutoka Misri na kuwaingiza katika nchi niliyoapa kuwapa baba zenu. Nikasema, ‘Kamwe sitalivunja Agano langu nanyi.

2 Nanyi msifanye agano na watu wa nchi hii, bali mtazibomoa madhabahu yao.’ Lakini ninyi hamkunitii mimi. Kwa nini mmefanya jambo hili?

3 Sasa basi ninawaambia kuwa sitawafukuza watoke katikati yenu ila watakuwa miiba kwenu, nao miungu yao itakuwa tanzi kwenu.”

4 Malaika waBwanaalipomaliza kusema mambo haya kwa Waisraeli wote, watu wakalia kwa sauti kuu.

5 Wakapaita mahali pale Bokimu. Nao wakamtoleaBwanasadaka.

Kifo Cha Yoshua

6 Baada ya Yoshua kuwapa watu ruhusa waende zao, Waisraeli wakaenda kwenye urithi wao wenyewe ili kumiliki nchi yao.

7 Watu wakamtumikiaBwanasiku zote za maisha ya Yoshua, na za hao wazee walioishi baada ya Yoshua kufa, waliokuwa wameona mambo makuu ambayoBwanaalikuwa ametenda kwa ajili ya Israeli.

8 Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi waBwana, akafa akiwa na umri wa miaka 110.

9 Wakamzika katika nchi ya urithi wake, huko Timnath-Heresikatika nchi ya vilima ya Efraimu, kaskazini ya Mlima Gaashi.

10 Baada ya kizazi kile chote kukusanywa pamoja na baba zao, kikainuka kizazi kingine baada yao ambacho hakikumjuaBwana, wala matendo yale aliyokuwa ametenda kwa ajili ya Waisraeli.

11 Kwa hiyo Waisraeli wakatenda maovu machoni paBwanana kuwatumikia Mabaali.

12 WakamwachaBwana, Mungu wa baba zao, aliyekuwa amewatoa katika nchi ya Misri. Wakaifuata na kuiabudu miungu mbalimbali ya mataifa yanayowazunguka. WakamkasirishaBwana,

13 kwa sababu walimwacha na kutumikia Baali na Maashtorethi.

14 Hivyo hasira yaBwanaikawaka juu ya Israeli, naye akawatia mikononi mwa wavamizi waliowateka nyara. Akawauza katika mikono ya adui zao pande zote, hivyo hawakuweza tena kuwazuia adui zao.

15 Popote Israeli walipotoka kwenda kupigana, mkono waBwanaulikuwa kinyume nao ili kuwashinda, kama vile alivyokuwa amewaapia. Nao wakawa katika taabu kubwa.

16 NdipoBwanaakawainua waamuzi, ambao waliwaokoa katika mikono ya hao watu waliowashambulia.

17 Lakini hawakuwasikiliza hata waamuzi wao, bali walifanya uasherati kwa kuifuata miungu mingine na kuiabudu. Waligeuka mara na kuiacha njia ambayo baba zao waliiendea, yaani, njia ya kutii amri zaBwana.

18 Kila maraBwanaalipowainulia mwamuzi,Bwanaalikuwa pamoja na huyo mwamuzi, naye aliwaokoa kutoka mikononi mwa adui zao kwa kipindi chote alichoishi yule mwamuzi. Kwa kuwaBwanaaliwahurumia kwa sababu ya kilio chao cha huzuni kwa ajili ya wale waliokuwa wakiwatesa na kuwataabisha.

19 Lakini kila mara mwamuzi alipofariki, watu walirudia katika hali mbaya ya uovu zaidi kuliko baba zao, wakiifuata miungu mingine kuitumikia na kuiabudu. Walikataa kuacha matendo yao maovu na njia zao za ukaidi.

20 Kwa hiyoBwanaakawakasirikia sana Israeli na kusema, “Kwa kuwa taifa hili limevunja Agano lile nililofanya na baba zao na hawakunisikiliza,

21 mimi nami sitafukuza taifa lolote ambalo Yoshua aliliacha alipofariki.

22 Nitayatumia ili nipate kuwapima Israeli na kuona kama wataishika njia yaBwanana kuenenda katika hiyo kama njia baba zao walivyofanya.”

23 Bwanaalikuwa ameyaacha hayo mataifa yabaki; hakuyaondoa mara moja kwa kuyatia mikononi mwa Yoshua.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JDG/2-2c8fb430d3a9cedf1d755d1cac3f4efe.mp3?version_id=1627—

Categories
Waamuzi

Waamuzi 3

Mataifa Yaliyobaki Katika Ile Nchi

1 Haya ndiyo mataifaBwanaaliyoyaacha ili kuwajaribu Waisraeli wote ambao hawakujua vita vyovyote vya Kanaani

2 (alifanya hivi ili tu kuwafundisha wazao wa Waisraeli ambao hawakuwa wamejua vita hapo awali):

3 wafalme watano wa Wafilisti, Wakanaani wote, Wasidoni, Wahivi waishio katika milima ya Lebanoni kuanzia Mlima wa Baal-Hermoni hadi Lebo-Hamathi.

4 Waliachwa ili kuwajaribu Waisraeli kuona kama wangetii amri zaBwana, alizokuwa amewapa baba zao kwa mkono wa Mose.

5 Waisraeli wakaishi miongoni mwa Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi.

6 Wakawaoa binti zao, nao wakawatoa binti zao waolewe na wana wa hayo mataifa, na kuitumikia miungu yao.

Othnieli

7 Waisraeli wakafanya maovu machoni paBwana, wakamsahauBwanaMungu wao na kutumikia Mabaali na Maashera.

8 Hasira yaBwanaikawaka dhidi ya Israeli, hivyo akawauza na kuwatia mikononi mwa Kushan-Rishathaimu mfalme wa Aramu-Naharaimuambaye Israeli walikuwa chini yake wakimtumikia kwa muda wa miaka minane.

9 Waisraeli walipomliliaBwana, yeye akawainulia mwokozi, Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa Kalebu, ambaye aliwaokoa.

10 Roho waBwanaakaja juu yake, hivyo akawa mwamuzi wa Israeli, akaenda vitani.Bwanaakamtia Kushan-Rishathaimu mfalme wa Aramu mikononi mwa Othnieli, naye akamshinda.

11 Hivyo nchi ikawa na amani kwa muda wa miaka arobaini, mpaka Othnieli mwana wa Kenazi alipofariki.

Ehudi

12 Waisraeli wakafanya maovu mbele zaBwanatena, kwa kuwa walifanya maovu hayoBwanaakamtia nguvu Egloni mfalme wa Moabu dhidi ya Israeli.

13 Egloni akawataka Waamoni na Waamaleki waungane naye, akaja kuishambulia Israeli, nao wakatwaa Mji wa Mitende

14 Waisraeli wakawa chini ya Egloni mfalme wa Moabu kwa muda wa miaka kumi na minane.

15 Waisraeli wakamlilia tenaBwana, naye akawapa mwokozi: Ehudi, mtu wa shoto, mwana wa Gera, Mbenyamini. Waisraeli wakatuma kwa Egloni mfalme wa Moabu ushuru kwa mkono wa Ehudi.

16 Basi Ehudi alikuwa ametengeneza upanga wenye ukatao kuwili, urefu wake ni kama dhiraa moja,akaufunga upanga huo ndani ya nguo yake kwenye paja lake la mkono wa kuume.

17 Akamkabidhi ushuru Egloni mfalme wa Moabu, ambaye alikuwa mtu mnene sana.

18 Baada ya Ehudi kumkabidhi ule ushuru, wale watu waliokuwa wameubeba huo ushuru aliwaruhusu waende zao.

19 Yeye mwenyewe akafuatana nao hadi kwenye sanamu ya kuchora kwenye mawe karibu na Gilgali, ndipo yeye akarudi, akafika kwa Egloni na kusema, “Ee Mfalme, ninao ujumbe wa siri kwa ajili yako.”

Mfalme akasema, “Nyamazeni kimya!” Nao wale waliomhudumia wote wakamwacha, wakatoka nje.

20 Ndipo Ehudi akamsogelea alipokuwa ameketi peke yake kwenye chumba cha juu cha jumba lake la kifalme la majira ya kiangazi, na kusema, “Ninao ujumbe kutoka kwa Mungu kwa ajili yako.” Mfalme alipokuwa anainuka kutoka kwenye kiti chake,

21 Ehudi akaunyoosha mkono wake wa kushoto na kuufuta ule upanga aliokuwa ameufunga kwenye paja lake la kulia, akamdunga Mfalme Egloni tumboni mwake.

22 Hata mpini nao ukazama tumboni pamoja na upanga wenyewe, nao upanga ukatokea mgongoni mwake. Ehudi hakuuchomoa huo upanga, nayo mafuta yakashikamana juu ya upanga.

23 Ehudi akatoka nje barazani; akamfungia milango ya chumba cha juu na kuifunga kwa funguo.

24 Baada ya kuondoka, watumishi wakaja na kukuta milango ya chumba cha juu imefungwa kwa funguo. Wakasema, “Bila shaka amejipumzisha kwenye chumba cha ndani cha nyumba yake ya majira ya kiangazi.”

25 Wakangoja hata wakawa na fadhaa, basi wakati hakufungua milango ya chumba, wakachukua funguo na kuifungua. Tazama wakaona bwana wao amelala sakafuni, amekufa.

26 Walipokuwa wangali wanangoja, Ehudi akatoroka, akapita hapo kwenye sanamu ya kuchora kwenye mawe na kukimbilia Seira.

27 Alipofika huko, akapiga tarumbeta katika nchi ya vilima ya Efraimu, nao Waisraeli wakateremka pamoja naye kutoka vilimani, yeye akiwa anawaongoza.

28 Akawaagiza, “Nifuateni, kwa kuwaBwanaamewatia Moabu, adui zenu, mikononi mwenu.” Kwa hiyo wakateremka wakamfuata, wakavishika vivuko vya Yordani kuelekea Moabu, wala hawakuacha mtu yeyote kuvuka.

29 Wakati huo wakawaua Wamoabu watu waume wapatao 10,000 ambao wote walikuwa wenye nguvu na mashujaa; hakuna mtu yeyote aliyetoroka.

30 Siku ile Moabu wakashindwa na Israeli, nayo nchi ikawa na amani kwa miaka themanini.

Shamgari

31 Baada ya Ehudi akaja Shamgari mwana wa Anathi, aliyewapiga Wafilisti 600 kwa fimbo iliyochongoka ya kuongozea ngʼombe. Naye pia akawaokoa Waisraeli.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JDG/3-c18a0782f94d8effb4cc5ff79b00e745.mp3?version_id=1627—

Categories
Waamuzi

Waamuzi 4

Debora

1 Baada ya Ehudi kufa, Waisraeli wakafanya tena maovu machoni paBwana.

2 HivyoBwanaakawatia mikononi mwa Yabini, mfalme wa Kanaani, aliyetawala huko Hazori. Jemadari wa jeshi lake alikuwa Sisera, aliyeishi huko Haroshethi-Hagoyimu

3 Kwa kuwa Sisera alikuwa na magari ya chuma yapatayo 900, naye alikuwa amewatesa Waisraeli kwa ukatili kwa muda wa miaka ishirini, Waisraeli wakamliliaBwanawakaomba msaada.

4 Debora, nabii mwanamke, mkewe Lapidothi, ndiye alikuwa anaamua Israeli wakati ule.

5 Debora alikuwa akiketi chini ya Mtende wa Debora uliokuwa kati ya Rama na Betheli katika nchi ya vilima ya Efraimu, nao Waisraeli wakaja kwake ili awaamue.

6 Akatuma wamwite Baraka mwana wa Abinoamu kutoka Kedeshi huko Naftali na kumwambia, “Bwana, Mungu wa Israeli, anakuagiza: ‘Nenda, chukua wanaume 10,000 toka Naftali na Zabuloni, mwende Mlima Tabori.

7 Nitamshawishi Sisera, jemadari wa jeshi la Yabini, pamoja na magari yake na jeshi lake, hadi Mto Kishoni na kumtia mikononi mwako.’ ”

8 Baraka akamwambia, “Ukienda pamoja nami nitakwenda, lakini usipokwenda pamoja nami, sitakwenda.”

9 Debora akamwambia, “Hakika nitakwenda pamoja nawe, lakini njia unayoiendea haitakupa heshima wewe, kwa kuwaBwanaatamtia Sisera mikononi mwa mwanamke.” Hivyo Debora akaenda pamoja na Baraka mpaka Kedeshi,

10 mahali ambapo Baraka aliwaita Zabuloni na Naftali. Watu 10,000 wakamfuata Baraka, na Debora pia akaenda pamoja naye.

11 Basi Heberi, Mkeni, alikuwa amejitenga na Wakeni wengine, yaani, wazao wa Hobabu, mkwewe Mose, naye akapiga hema lake karibu na ule mti mkubwa wa mwaloni ulioko Saananimu, karibu na Kedeshi.

12 Sisera alipoambiwa kuwa Baraka mwana wa Abinoamu alikuwa amepanda Mlima Tabori,

13 Sisera akakusanya pamoja magari yake yote 600 ya chuma na watu wote waliokuwa pamoja naye, kuanzia Haroshethi-Hagoyimu mpaka Mto wa Kishoni.

14 Ndipo Debora akamwambia Baraka, “Nenda! Hii ndiyo siku ambayoBwanaamemtia Sisera mikononi mwako. Je,Bwanahakukutangulia mbele yako?” Hivyo Baraka akashuka kutoka Mlima Tabori, akifuatwa na watu 10,000.

15 Bwanaakamfadhaisha Sisera na magari yake yote, pamoja na jeshi lake lote kwa upanga mbele ya Baraka, naye Sisera akaliacha gari lake na kukimbia kwa miguu.

16 Lakini Baraka akafuata magari pamoja na jeshi mpaka Haroshethi-Hagoyimu. Jeshi lote la Sisera likaanguka kwa upanga, wala hakuna hata mtu mmoja aliyesalia.

17 Sisera, hata hivyo, akakimbia kwa miguu mpaka kwenye hema la Yaeli, mkewe Heberi, Mkeni, kwa sababu palikuwa na uhusiano wa kirafiki kati ya Yabini mfalme wa Hazori na ukoo wa Heberi, Mkeni.

18 Yaeli akaenda kumlaki Sisera na kumwambia, “Karibu, bwana wangu, karibu ingia ndani kabisa. Usiogope.” Basi Sisera akaingia ndani ya hema ya Yaeli, naye akamfunika kwa blanketi nene.

19 Akamwambia, “Nina kiu, tafadhali nipe maji ya kunywa.” Ndipo akafungua kiriba cha maziwa na kumpa akanywa, kisha akamfunika.

20 Naye Sisera akamwambia, “Simama mlangoni pa hema na mtu yeyote akija na kukuuliza, ‘Je, kuna mtu yeyote hapa?’ sema, ‘Hapana.’ ”

21 Ndipo Yaeli, mkewe Heberi, akatwaa kigingi cha hema, akachukua nyundo mkononi mwake, akamwendea polepole, akiwa amelala usingizi, akiwa amechoka. Akakigongomea kile kigingi kwenye paji la uso wake, kikapenya hata kuingia ardhini, naye akafa.

22 Baraka akakaribia akimfuatia Sisera, Yaeli akatoka kumlaki. Akamwambia, “Njoo, nitakuonyesha mtu unayemtafuta.” Hivyo wakaingia ndani ya hema wakiwa wamefuatana na tazama Sisera alikuwa amelala humo, akiwa amekufa, na hicho kigingi cha hema kikiwa kimegongomewa kupitia paji la uso wake.

23 Basi siku ile Mungu akamshinda Yabini, mfalme wa Kanaani, mbele ya Israeli.

24 Nao mkono wa Waisraeli ukaendelea kuwa na nguvu zaidi na zaidi dhidi ya Yabini, mfalme wa Kanaani, mpaka wakamwangamiza.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JDG/4-907911f3bebd3a265a18811b90486689.mp3?version_id=1627—

Categories
Waamuzi

Waamuzi 5

Wimbo Wa Debora

1 Ndipo Debora na Baraka mwana wa Abinoamu wakaimba wimbo huu:

2 “Wakuu katika Israeli wanapoongoza,

wakati watu wanapojitoa

kwa hiari yao wenyewe:

mhimidiniBwana!

3 “Sikieni hili, enyi wafalme!

Sikilizeni, enyi watawala!

NitamwimbiaBwana, nitaimba;

kwa wimbo nitamhimidiBwana,

Mungu wa Israeli.

4 “EeBwana, ulipotoka katika Seiri,

ulipopita katika mashamba ya Edomu,

nchi ilitetemeka, mbingu nazo zikamwaga,

naam, mawingu yakamwaga maji.

5 Milima ilitetemeka mbele zaBwana,

hata ule wa Sinai,

mbele zaBwana,

Mungu wa Israeli.

6 “Katika siku za Shamgari mwana wa Anathi,

katika siku za Yaeli,

barabara kuu hazikuwa na watu;

wasafiri walipita njia za kando.

7 Mashujaa walikoma katika Israeli,

walikoma mpaka mimi, Debora, nilipoinuka,

nilipoinuka kama mama katika Israeli.

8 Walipochagua miungu migeni,

vita vilikuja katika malango ya mji,

hapakuonekana ngao wala mkuki

miongoni mwa mashujaa 40,000 katika Israeli.

9 Moyo wangu u pamoja na wakuu wa Israeli,

pamoja na wale wanaojitoa wenyewe

kwa hiari yao miongoni mwa watu.

MhimidiniBwana!

10 “Nanyi mpandao punda weupe,

mkiketi juu ya matandiko ya thamani,

nanyi mtembeao barabarani,

fikirini

11 juu ya sauti za waimbaji

mahali pa kunyweshea maji.

Wanasimulia matendo ya haki yaBwana,

matendo ya haki ya mashujaa wake

katika Israeli.

“Ndipo watu waBwana

walipoteremka malangoni pa mji.

12 ‘Amka, amka! Debora!

Amka, amka, uimbe!

Ee Baraka! Inuka,

chukua mateka wako uliowateka,

ee mwana wa Abinoamu.’

13 “Ndipo mabaki ya watu

wakashuka dhidi ya wenye nguvu,

watu waBwana,

wakashuka dhidi ya mashujaa wenye nguvu.

14 Kutoka Efraimu wakaja watu, ambao chimbuko lao ni Amaleki;

Benyamini akiwa miongoni

mwa watu waliokufuata.

Kutoka Makiri wakashuka viongozi,

na kutoka Zabuloni wale washikao

fimbo ya jemadari.

15 Wakuu wa Isakari walikuwa pamoja na Debora;

naam, Isakari alikuwa pamoja na Baraka,

wakija nyuma yake kwa mbio

wakielekea bondeni.

Katika jamaa za Reubeni,

palikuwa na kujihoji kukubwa moyoni.

16 Kwa nini ulikaa katikati ya mazizi ya kondoo

kusikiliza sauti ya filimbi zinazoita makundi?

Kwa jamaa za Reubeni,

palikuwa na kujihoji kukubwa moyoni.

17 Gileadi alikaa ngʼambo ya Yordani.

Naye Dani, kwa nini alikaa

kwenye merikebu siku nyingi?

Asheri alikaa kwa utulivu ufuoni mwa bahari,

akikaa kwenye ghuba zake ndogo.

18 Watu wa Zabuloni walihatarisha maisha yao,

vilevile nao watu wa Naftali.

19 “Wafalme walikuja na kufanya vita;

wafalme wa Kanaani walipigana

huko Taanaki karibu na maji ya Megido,

lakini hawakuchukua fedha wala nyara.

20 Kutoka mbinguni nyota zilipigana,

nyota kutoka njia zake

zilipigana na Sisera.

21 Mto wa Kishoni uliwasomba,

ule mto wa zamani, mto wa Kishoni.

Songa mbele, ee nafsi yangu,

kwa ujasiri!

22 Ndipo kwato za farasi zikafanya mshindo:

farasi wake wenye nguvu

huenda mbio kwa kurukaruka.

23 Malaika waBwanaakasema, ‘Merozi alaaniwe.

Walaaniwe watu wake kwa uchungu,

kwa kuwa hawakuja kumsaidiaBwana,

kumsaidiaBwanadhidi ya hao wenye nguvu.’

24 “Yaeli abarikiwe kuliko wanawake wote,

mkewe Heberi, Mkeni,

abarikiwe kuliko wanawake wote

waishio kwenye mahema.

25 Aliomba maji, naye akampa maziwa;

kwenye bakuli la heshima

akamletea maziwa mgando.

26 Akanyoosha mkono wake

akashika kigingi cha hema,

mkono wake wa kuume

ukashika nyundo ya fundi.

Akampiga Sisera kwa nyundo,

akamponda kichwa chake,

akamvunjavunja na kumtoboa

paji lake la uso.

27 Aliinama miguuni pa Yaeli,

akaanguka; akalala hapo.

Pale alipoinama miguuni pake,

alianguka;

pale alipoinamia, ndipo alipoanguka,

akiwa amekufa.

28 “Kupitia dirishani mamaye Sisera alichungulia;

nyuma ya dirisha alilia, akasema,

‘Mbona gari lake linachelewa kufika?

Mbona vishindo vya magari yake

vimechelewa?’

29 Wanawake wenye busara

kuliko wengine wote wakamjibu;

naam, husema moyoni mwake,

30 ‘Je, hawapati na kugawanya nyara:

msichana mmoja au wawili kwa kila mtu,

mavazi ya rangi mbalimbali kwa Sisera kuwa nyara,

mavazi ya rangi mbalimbali yaliyotariziwa,

mavazi yaliyotariziwa vizuri kwa ajili ya shingo yangu:

yote haya yakiwa nyara?’

31 “Adui zako wote na waangamie, EeBwana!

Bali wote wakupendao na wawe kama jua

lichomozavyo kwa nguvu zake.”

Hivyo nchi ikawa na amani kwa miaka arobaini.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JDG/5-54532687ea068db9b0f4449cc384bb0a.mp3?version_id=1627—

Categories
Waamuzi

Waamuzi 6

Gideoni

1 Waisraeli wakafanya tena yaliyo maovu mbele zaBwana, naye kwa miaka sabaBwanaakawatia mikononi mwa Wamidiani.

2 Mkono wa Midiani ukawa na nguvu dhidi ya Israeli na kwa ajili ya Wamidiani, Waisraeli wakajitengenezea mahali pa kujificha milimani, kwenye mapango na ngome.

3 Kila wakati Waisraeli walipopanda mazao mashambani, Wamidiani, Waamaleki na mataifa mengine ya mashariki walivamia nchi yao.

4 Wakapiga kambi katika mashamba yao na kuharibu mazao ya nchi yote hadi kufikia Gaza, wala hawakuacha kiumbe chochote kilicho hai kwa Waisraeli, iwe kondoo au ngʼombe au punda.

5 Walipanda na mifugo yao na mahema yao, mfano wa makundi ya nzige. Ilikuwa haiwezekani kuwahesabu watu na ngamia zao; wakavamia nchi ili kuiharibu.

6 Waisraeli wakafanywa kuwa maskini sana na Wamidiani, hata Israeli wakamliliaBwanakuomba msaada.

7 Waisraeli walipomliliaBwanakwa sababu ya Wamidiani,

8 Bwanaakawapelekea nabii, ambaye aliwaambia, “Hili ndiloBwana, Mungu wa Israeli, asemalo: Niliwapandisha mtoke Misri, toka nchi ya utumwa.

9 Nikawanyakua kutoka mikononi mwa Wamisri na kutoka mikononi mwa watesi wenu wote. Nikawafukuza watoke mbele yenu nami nikawapa ninyi nchi yao.

10 Nikawaambia, ‘Mimi ndimiBwanaMungu wenu; msiiabudu miungu ya Waamori, ambayo mnakaa katika nchi yao!’ Lakini ninyi hamkuitii sauti yangu.”

11 Malaika waBwanaakaja akaketi chini ya mti wa mwaloni huko Ofra, ambao ulikuwa mali ya Yoashi, Mwabiezeri, ambako Gideoni mwanawe alikuwa akipepeta ngano penye shinikizo la kukamulia zabibu, ili kuificha Wamidiani wasiione.

12 Malaika waBwanaalipomtokea Gideoni, akamwambia, “Bwanayu pamoja nawe, Ewe shujaa mwenye nguvu.”

13 Gideoni akajibu, “Ee Bwana wangu, kamaBwanayu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametutokea? Yako wapi basi yale matendo yake makuu baba zetu waliyotusimulia juu yake waliposema, ‘Je,Bwanahakutupandisha kutoka Misri?’ Lakini sasaBwanaametuacha na kututia katika mkono wa Midiani.”

14 Bwanaakamgeukia na kusema “Enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli kutoka mikononi mwa Wamidiani. Je, si mimi ninayekutuma wewe?”

15 Gideoni akauliza, “Ee Bwana wangu, nitawezaje kuwaokoa Israeli? Ukoo wangu ndio dhaifu kuliko zote katika Manase, nami ndiye mdogo wa wote katika jamaa yangu.”

16 Bwanaakamjibu, “Nitakuwa pamoja nawe, nawe utawapiga Wamidiani kana kwamba walikuwa ni mtu mmoja.”

17 Gideoni akajibu, “Kama basi nimepata kibali machoni pako, nipe ishara kuonyesha kweli kwamba ni wewe unayesema nami.

18 Tafadhali ninakuomba usiondoke hapa mpaka nitakaporudi na kukuletea sadaka yangu na kuiweka mbele yako.”

NayeBwanaakamwambia, “Nitangoja mpaka utakaporudi.”

19 Gideoni akaingia ndani ya nyumba yake na kuandaa mwana-mbuzi pamoja na kuoka mikate isiyotiwa chachu kutokana na efa mojaya unga. Akaweka nyama kwenye kikapu na mchuzi kwenye chungu, akamletea huyo malaika hapo nje chini ya mti wa mwaloni na kumpa.

20 Malaika wa Mungu akamwambia, “Itwae nyama na mikate isiyotiwa chachu, uviweke juu ya mwamba huu na umimine huo mchuzi juu yake.” Gideoni akafanya hivyo.

21 Malaika waBwanaakainyoosha fimbo iliyokuwa mkononi mwake, ncha yake ikagusa ile nyama na ile mikate isiyotiwa chachu, nao moto ukatoka kwenye mwamba ukateketeza ile nyama na ile mikate. Malaika waBwanaakatoweka kutoka machoni pake.

22 Gideoni alipotambua kuwa ni malaika waBwana, akapiga kelele kwa mshangao, akasema, “Ole wangu,BwanaMwenyezi! Kwa kuwa nimemwona malaika waBwanauso kwa uso!”

23 LakiniBwanaakamwambia, “Amani iwe kwako! Usiogope. Hutakufa.”

24 Hivyo Gideoni akamjengeaBwanamadhabahu mahali pale na kupaita, Yehova-Shalom.Mpaka leo ingalipo imesimama huko Ofra ya Waabiezeri.

25 Usiku ule uleBwanaakamwambia, “Mchukue ngʼombe dume wa baba yako, yaani, yule wa pili mwenye miaka saba, na ubomoe madhabahu ya Baali aliyo nayo baba yako, na ukaikate Ashera iliyo karibu nayo.

26 Kisha mjengeeBwanaMungu wako, madhabahu halisi, kwa taratibu zake, juu ya huu mwamba. Kwa kutumia kuni za hiyo nguzo ya Ashera uliyoikatakata, mtoe sadaka huyo dume wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa.”

27 Basi Gideoni akawachukua watumishi wake kumi na kufanya kamaBwanaalivyomwambia. Lakini kwa kuwa aliwaogopa jamaa yake na watu wa mji, akafanya haya usiku badala ya mchana.

28 Watu wa mji walipoamka asubuhi, tazama madhabahu ya Baali imebomolewa na nguzo ya Ashera iliyokuwa karibu nayo imekatwakatwa na yule ngʼombe wa pili ametolewa sadaka juu ya madhabahu yaliyojengwa upya!

29 Wakaulizana, “Ni nani aliyetenda mambo haya?”

Walipochunguza kwa makini, wakaambiwa, “Ni Gideoni mwana wa Yoashi, ndiye alitenda hivi.”

30 Watu wa mji wakamwambia Yoashi, “Mlete mwanao hapa. Ni lazima afe, kwa sababu amebomoa madhabahu ya Baali na kukatakata nguzo ya Ashera iliyokuwa karibu nayo.”

31 Lakini Yoashi akauambia ule umati uliokuwa umezunguka ukiwa kinyume naye, “Je, ninyi mtamtetea Baali? Mnajaribu kumwokoa? Yeyote mwenye kumpigania atauawa kufikia kesho asubuhi! Kama Baali ni mungu kweli, anaweza kujitetea mwenyewe wakati mtu anapobomoa madhabahu yake.”

32 Basi siku ile wakamwita Gideoni “Yerub-Baali,” yaani, “Baali na ashindane naye,” kwa sababu alibomoa madhabahu yake.

33 Basi Wamidiani wote, Waamaleki na mataifa mengine ya mashariki wakaunganisha majeshi yao, wakavuka ngʼambo ya Yordani na kupiga kambi katika Bonde la Yezreeli.

34 Ndipo Roho waBwanaakamjia Gideoni, akapiga tarumbeta, akiwaita Waabiezeri ili wamfuate.

35 Akatuma wajumbe waende katika Manase yote, akiwataka wachukue silaha na pia katika Asheri, Zabuloni na Naftali, nao wakakwea ili kukutana nao.

36 Gideoni akamwambia Mungu, “Kama utawaokoa Waisraeli kwa mkono wangu, kama ulivyoahidi:

37 tazama, nitaweka ngozi ya kondoo kwenye kiwanja cha kupuria nafaka, na kama utakuwepo umande juu ya ngozi tu, nayo ardhi yote ikiwa kavu, ndipo nitakapojua kuwa utaokoa Israeli kwa mkono wangu, kama ulivyosema.”

38 Hivyo ndivyo ilivyotokea. Gideoni akaamka asubuhi na mapema kesho yake, akaikamua ile ngozi, umande ukatoka, maji ya kujaa bakuli.

39 Kisha Gideoni akamwambiaBwana, “Usinikasirikie. Ninaomba nifanye ombi moja lingine. Niruhusu nifanye jaribio jingine moja kwa ngozi hii. Wakati huu uifanye ngozi hii kavu na ardhi yote ifunikwe na umande.”

40 Usiku ule Mungu akafanya hivyo. Ngozi ile ilikuwa kavu, nayo ardhi yote ikafunikwa na umande.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JDG/6-2b4effce819ff9f4eabfd4b77b6bef3a.mp3?version_id=1627—

Categories
Waamuzi

Waamuzi 7

Gideoni Awashinda Wamidiani

1 Ndipo Yerub-Baali (yaani Gideoni) na lile jeshi lililokuwa pamoja naye, wakaondoka asubuhi na mapema na kupiga kambi kando ya chemchemi ya Harodi. Kambi ya Wamidiani ilikuwa kaskazini yao katika bonde karibu na kilima cha More.

2 Bwanaakamwambia Gideoni, “Jeshi lililo pamoja nawe ni kubwa sana kwa mimi kuwatia Wamidiani mikononi mwao. Ili kwamba Israeli asije akajisifu juu yangu akisema, ‘Mkono wangu ndio ulioniokoa,

3 kwa hiyo sasa tangaza jeshi lote likiwa linasikia, kwamba: Yeyote anayeogopa na kutetemeka, yeye na arudi nyumbani, aondoke katika Mlima Gileadi.’ ” Hivyo watu 22,000 walirudi, wakabaki 10,000.

4 LakiniBwanaakamwambia Gideoni, “Idadi ya jeshi bado ni kubwa. Wapeleke chini katika maji nami nitawajaribu huko kwa ajili yako. Kama nikikuambia, ‘Huyu atakwenda pamoja nawe,’ yeye atakwenda; lakini kama nikisema, ‘Huyu hatakwenda pamoja nawe,’ yeye hatakwenda.”

5 Hivyo Gideoni akalileta lile jeshi chini kwenye maji nayeBwanaakamwambia Gideoni, “Watenge upande mmoja wale wote wanywao maji kwa ulimi, kama vile mbwa anywavyo, wale wote wapigao magoti ili kunywa wakipeleka mikono yao vinywani mwao, waweke upande mwingine.”

6 Idadi ya wale waliokunywa kwa kuramba ramba walikuwa 300, lakini wengine wote katika jeshi walipiga magoti ili kunywa.

7 Bwanaakamwambia Gideoni, “Kwa hao watu 300 walioramba maji nitawaokoa ninyi, nami nitawatia Wamidiani mkononi mwako. Waache hao watu wengine wote warudi kila mmoja nyumbani mwake.”

8 Hivyo Gideoni akawaacha wale Waisraeli wengine kila mmoja aende kwenye hema yake. Akabakia na wale 300, ambao walichukua vyakula na tarumbeta za wale wenzao.

Basi kambi ya Wamidiani ilikuwa chini yake bondeni.

9 Usiku ule uleBwanaakamwambia Gideoni, “Ondoka, ushuke kambini, kwa kuwa nimeitia mkononi mwako.

10 Lakini kama unaogopa kushambulia, shuka kambini pamoja na mtumishi wako Pura,

11 nawe sikiliza wanayosema. Hatimaye, utatiwa moyo kushambulia kambi.” Basi yeye na Pura mtumishi wake wakashuka na kufikia walinzi wa mbele wenye silaha waliokuwa mle kambini.

12 Wamidiani, Waamaleki na mataifa mengine yote ya mashariki walikaa bondeni, nao walikuwa mfano wa nzige kwa wingi wao. Ngamia zao hazikuhesabika, wingi wao ulikuwa kama mchanga wa ufuoni mwa bahari.

13 Gideoni alifika wakati huo huo kukiwa na mtu mmoja aliyekuwa anamweleza mwenzake ndoto yake, akisema, “Niliota ndoto: Tazama mkate wa shayiri ulioviringana ulianguka katika kambi moja ya Wamidiani, ukaipiga na ikaanguka nao ukaipindua juu chini na hema ikaporomoka chini.”

14 Rafiki yake akamjibu, “Habari hii si kitu kingine zaidi ya upanga wa Gideoni mwana wa Yoashi, Mwisraeli. Mungu amewatia Wamidiani na jeshi lote mkononi mwake.”

15 Gideoni alipoisikia hiyo ndoto na tafsiri yake, akamwabudu Mungu. Akarudi kwenye kambi ya Israeli na kusema, “Inukeni!Bwanaamelitia jeshi la Wamidiani mikononi mwenu.”

16 Akawagawa wale watu 300 katika makundi matatu, akawakabidhi tarumbeta mikononi mwao wote na mitungi isiyokuwa na maji yenye mienge ndani yake.

17 Akawaambia, “Nitazameni, fanyeni kama nitakavyofanya, nitakapofika mwisho wa kambi mfanye kama nitakavyofanya.

18 Wakati mimi na wale walio pamoja nami wote, tutakapopiga tarumbeta zetu, ninyi nanyi pigeni tarumbeta pande zote za kambi na mpige kelele, mseme, ‘Upanga waBwanana wa Gideoni.’ ”

19 Gideoni na wale watu 100 waliokuwa pamoja naye wakafika mwisho wa kambi usiku mwanzoni mwa zamu ya kati, mara tu walipokuwa wamebadili zamu. Wakapiga zile tarumbeta zao na kuvunja ile mitungi iliyokuwa mikononi mwao.

20 Yale makundi matatu yakapiga tarumbeta na kuvunja mitungi. Wakashika mienge kwa mikono yao ya kushoto na katika mikono yao ya kuume tarumbeta ili kuzipiga, wakapaza sauti zao, “Upanga waBwanana wa Gideoni!”

21 Wakasimama kila mtu mahali pake kuizunguka kambi pande zote, Wamidiani wote wakakimbia, huku wakipiga kelele.

22 Walipozipiga zile tarumbeta 300,Bwanaakafanya watu katika kambi yote kugeuziana upanga kila mmoja na mwenziwe. Jeshi likakimbia mpaka Beth-Shita kuelekea Sererahadi mpakani mwa Abel-Mehola karibu na Tabathi.

23 Watu wa Israeli wakaitwa kutoka Naftali, Asheri na Manase, wakawafuatia Wamidiani.

24 Gideoni akatuma wajumbe katika nchi yote ya vilima vya Efraimu akisema, “Teremkeni dhidi ya Wamidiani na mkazuie vivuko vya maji mbele yao hadi Beth-Bara na pia Yordani.”

Hivyo watu wote wa Efraimu wakakutanika pamoja na kuzingira mto wa Yordani hadi Beth-Bara.

25 Wakawakamata wakuu wawili wa Midiani, Orebu na Zeebu. Wakamuulia Orebu pale penye mwamba wa Orebu, na Zeebu wakamuulia penye shinikizo la kukamulia divai la Zeebu. Wakawafuatia Wamidiani na kuleta vichwa vya Orebu na Zeebu kwa Gideoni, huko ngʼambo ya Yordani.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JDG/7-547f543df542832b22099206ba613afe.mp3?version_id=1627—

Categories
Waamuzi

Waamuzi 8

Ushindi Wa Gideoni Na Kulipiza Kisasi

1 Basi Waefraimu wakamuuliza Gideoni, “Mbona mmetutenda hivi? Kwa nini hukutuita ulipokwenda kupigana na Wamidiani?” Wakawalaumu kwa ukali sana.

2 Gideoni akawajibu, “Nilichofanya mimi ni nini kulinganisha na kile ninyi mlichofanya? Je, kuokoa masazo ya zabibu za Efraimu si bora kuliko mavuno kamili ya zabibu ya Abiezeri?

3 Mungu amewatia Orebu na Zeebu, hao viongozi wa Wamidiani, mikononi mwenu. Je, mimi niliweza kufanya nini kulinganisha na mlichofanya ninyi?” Aliposema hili, hasira yao dhidi yake ikatulia.

4 Gideoni akiwa pamoja na wale watu 300 waliofuatana naye, wakiwa wamechoka na wenye njaa lakini bado wakiwafuatia, wakafika Yordani na kuuvuka.

5 Akawaambia watu wa Sukothi, “Tafadhali lipatieni jeshi langu mikate, kwa maana wamechoka, nami ningali ninawafuatia Zeba na Salmuna, wafalme wa Midiani.”

6 Lakini maafisa wa Sukothi wakasema, “Je, mikono ya Zeba na Salmuna tayari mnayo sasa ili tuweze kulipatia jeshi lako mikate?”

7 Gideoni akajibu, “Kwa ajili ya hilo tu,Bwanaatakapowatia Zeba na Salmuna mkononi mwangu, nitaichana nyama ya miili yenu kwenye miiba ya nyikani na kwenye michongoma.”

8 Kutoka hapo alikwea mpaka Penieli na kutoa ombi lile lile, lakini nao watu wa Penieli wakamjibu kama watu wa Sukothi walivyokuwa wamemjibu.

9 Hivyo akawaambia watu wa Penieli, “Nitakaporudi baada ya kushinda, nitaubomoa mnara huu.”

10 Wakati huu Zeba na Salmuna walikuwa Karkori wakiwa na jeshi lenye watu wapatao 15,000 wale wote waliokuwa wamesalia wa mataifa ya mashariki, kwa kuwa watu wapatao 120,000 wenye panga walikuwa wameuawa.

11 Basi Gideoni akakwea kwa njia ya wasafiri mashariki ya Noba na Yogbeha na kulishambulia jeshi ambalo halikushuku lolote.

12 Zeba na Salmuna, hao wafalme wawili wa Midiani, wakakimbia lakini yeye Gideoni akawafuata na kuwakamata, akalishinda hilo jeshi lao lote.

13 Gideoni mwana wa Yoashi akarudi kutoka vitani kwa kupitia Mwinuko wa Heresi.

14 Akamkamata kijana mmoja wa Sukothi na kumuuliza maswali, naye yule kijana akamwandikia majina ya maafisa sabini wa Sukothi, ambao ni viongozi wa mji.

15 Ndipo Gideoni akaja na kuwaambia watu wa Sukothi, “Tazama, hapa wapo Zeba na Salmuna mlionisimanga kwa ajili yao mkisema, ‘Je, mikono ya Zeba na Salmuna tayari mnayo sasa ili tuweze kulipatia jeshi lako mikate?’ ”

16 Akawachukua hao viongozi wa mji na kuwafundisha watu wa Sukothi somo kwa kuwaadhibu kwa miiba na michongoma ya nyikani.

17 Pia akaubomoa mnara wa Penieli na kuwaua watu wa mji.

18 Kisha akawauliza Zeba na Salmuna, “Ni watu wa aina gani mliowaua huko Tabori?”

Wakajibu, “Ni watu kama wewe, kila mmoja wao akiwa na nafasi ya uana wa mfalme.”

19 Gideoni akajibu, “Hao walikuwa ndugu zangu, wana wa mama yangu hasa. Hakika kama aishivyoBwana, kama mngekuwa mmewaacha hai, mimi nisingewaua ninyi.”

20 Akamgeukia Yetheri, mwanawe mzaliwa wa kwanza, akasema, “Waue hawa!” Lakini Yetheri hakuufuta upanga wake, kwa sababu aliogopa, kwa kuwa alikuwa bado kijana mdogo tu.

21 Zeba na Salmuna wakasema, “Njoo ufanye hivyo wewe mwenyewe. ‘Alivyo mtu, ndivyo zilivyo nguvu zake.’ ” Hivyo Gideoni akatoka mbele na kuwaua, naye akayaondoa mapambo kwenye shingo za ngamia zao.

Kisibau Cha Gideoni

22 Waisraeli wakamwambia Gideoni, “Ututawale, wewe, wanao na wana wa wana wako, kwa kuwa umetuokoa kutoka mikononi mwa Wamidiani.”

23 Lakini Gideoni akawaambia, “Mimi sitatawala juu yenu, wala wanangu hawatatawala juu yenu.Bwanandiye atakayetawala juu yenu ninyi.”

24 Naye akasema, “Ninalo ombi moja, kwamba kila mmoja wenu anipatie kipuli kutoka kwenye fungu lake la nyara.” (Ilikuwa desturi ya Waishmaeli kuvaa vipuli vya dhahabu.)

25 Wakajibu, “Tutafurahi kuvitoa.” Hivyo wakatanda vazi chini na kila mwanaume akatupia juu yake pete kutoka kwenye fungu lake la nyara.

26 Uzito wa pete za dhahabu alizoomba zilifikia shekeli 1,700,bila kuhesabu mapambo mengine, pete za masikio na mavazi ya zambarau yaliyovaliwa na wafalme wa Midiani, au mikufu iliyokuwa kwenye shingo za ngamia zao.

27 Gideoni akatengeneza kisibau kwa kutumia ile dhahabu, ambacho alikiweka katika mji wake, yaani, Ofra. Waisraeli wote wakafanya uasherati kwa kukiabudu huko, nacho kikawa mtego kwa Gideoni na jamaa yake.

28 Hivyo Midiani ikashindwa mbele ya Israeli nayo haikuinua kichwa chake tena. Wakati wa siku za uhai wa Gideoni, nchi ikafurahia amani miaka arobaini.

Kifo Cha Gideoni

29 Yerub-Baali mwana wa Yoashi akarudi kwenda kuishi katika nyumba yake.

30 Alikuwa na wana sabini wa kwake mwenyewe, kwa kuwa alikuwa na wake wengi.

31 Suria wake, aliyekuwa anaishi huko Shekemu, pia alimzalia mwana, ambaye alimwita Abimeleki.

32 Gideoni mwana wa Yoashi akafa akiwa na umri mzuri wa uzee, na akazikwa katika kaburi la Yoashi baba yake huko Ofra ya Waabiezeri.

33 Mara tu alipofariki Gideoni, Waisraeli wakarudia hali ya uovu na kufanya uasherati kwa kuabudu Mabaali. Wakamsimamisha Baal-Berithi kuwa mungu wao na

34 wala hawakumkumbukaBwanaMungu wao, aliyewaokoa kutoka mikononi mwa adui zao wote kutoka kila upande.

35 Pia wakashindwa kuitendea mema jamaa ya Yerub-Baali (yaani Gideoni) kwa ajili ya mambo yote mema aliyokuwa amefanya kwa ajili yao.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JDG/8-1c71e4d8db41e4b0698a5c80f0ffe2af.mp3?version_id=1627—

Categories
Waamuzi

Waamuzi 9

Abimeleki Ajaribu Kuanzisha Ufalme

1 Siku moja Abimeleki mwana wa Yerub-Baali akaenda kwa ndugu ya mama yake huko Shekemu na kuwaambia yeye na ukoo wote wa mama yake,

2 “Waulizeni watu wote wa Shekemu, ‘Lipi lililo bora kwenu: Kutawaliwa na wana wote sabini wa Yerub-Baali, au mtu mmoja peke yake?’ Kumbukeni kwamba, mimi ni mfupa wenu nyama yenu hasa.”

3 Ndugu za mama yake walipowaeleza watu wote wa Shekemu, wakaelekea kumkubali Abimeleki, kwa kuwa walisema, “Yeye ni ndugu yetu.”

4 Wakampa shekeli sabiniza fedha kutoka hekalu la Baal-Berithi, naye Abimeleki akaitumia kuajiri watu ovyo wasiojali, wakawa ndio wafuasi wake.

5 Akaenda nyumbani kwa baba yake huko Ofra, na juu ya jiwe moja wakawaua ndugu zake sabini, ambao ni wana wa Yerub-Baali. Lakini Yothamu, mwana mdogo wa wote wa Yerub-Baali, akaokoka kwa kujificha.

6 Ndipo watu wote wa Shekemu na Beth-Milo wakakusanyika pamoja chini ya mti mkubwa wa mwaloni penye nguzo iliyoko Shekemu wakamvika Abimeleki taji kuwa mfalme.

7 Yothamu alipoambiwa hayo, akapanda juu ya kilele cha mlima Gerizimu, akawapazia sauti yake akawaambia, “Nisikilizeni enyi watu wa Shekemu, ili Mungu naye apate kuwasikiliza ninyi.

8 Siku moja miti ilitoka ili kwenda kujitawazia mfalme. Ikauambia mzeituni, ‘Wewe uwe mfalme wetu.’

9 “Lakini mzeituni ukaijibu, ‘Je, niache kutoa mafuta yangu ambayo kwake miungu na wanadamu huheshimiwa, ili nikawe juu ya miti?’

10 “Kisha miti ikauambia mtini, ‘Njoo na uwe mfalme wetu!’

11 “Lakini mtini ukaijibu, ‘Je, niache kutoa matunda yangu mazuri na matamu, ili niende nikawe juu ya miti?’

12 “Ndipo miti ikauambia mzabibu, ‘Njoo na uwe mfalme wetu.’

13 “Lakini mzabibu ukaijibu, ‘Je, niache kutoa divai yangu inayofurahisha miungu na wanadamu ili nikawe juu ya miti?’

14 “Mwishoni miti yote ikauambia mti wa miiba, ‘Njoo na uwe mfalme wetu.’

15 “Nao mti wa miiba ukaijibu, ‘Kama kweli mnataka niwe mfalme wenu, basi njooni mpate kupumzika chini ya kivuli changu. Lakini kama sivyo, moto na utoke kwenye mti wa miiba ukateketeze mierezi ya Lebanoni!’

16 “Basi ikiwa mmetenda kwa uaminifu na heshima kumfanya Abimeleki kuwa mfalme, na kama mmetendea vyema Yerub-Baali na jamaa yake kama ilivyostahili:

17 kwa kuwa baba yangu aliwapigania ninyi na kuhatarisha nafsi yake na kuwaokoa ninyi kutoka mikononi mwa Wamidiani

18 (lakini leo mmeasi dhidi ya jamaa ya baba yangu, na kuwaua wanawe sabini juu ya jiwe moja, nanyi mkamfanya Abimeleki mwana wa mwanamke mtumwa kuwa mfalme juu ya Shekemu, kwa kuwa yeye ni ndugu yenu),

19 nanyi kama basi mmemtendea Yerub-Baali na jamaa yake kwa heshima na uaminifu, basi Abimeleki na awe furaha yenu, nanyi mwe furaha yake pia!

20 Lakini kama sivyo, moto na utoke kwa Abimeleki na uwateketeze, ninyi watu wa Shekemu na Beth-Milo, nao moto utoke kwenu, watu wa Shekemu na Beth-Milo umteketeze Abimeleki!”

21 Ndipo Yothamu akakimbia, akatoroka akaenda Beeri, akaishi huko, kwa sababu alimwogopa ndugu yake Abimeleki.

22 Baada ya Abimeleki kutawala Israeli kwa muda wa miaka mitatu,

23 Mungu akaruhusu roho mbaya kati ya Abimeleki na watu wa Shekemu, nao watu wa Shekemu wakamtendea Abimeleki kwa hila.

24 Hili lilitokea ili ule ukatili waliotendewa hao wana sabini wa Yerub-Baali upatilizwe, na damu yao iwe juu ya Abimeleki ndugu yao aliyewaua, na pia iwe juu ya watu wa Shekemu, ambao walimsaidia kuua ndugu zake.

25 Hivyo, kutokana na uadui juu yake watu wa Shekemu wakaweka watu wa kumvizia katika vilele vya milima. Wakawanyangʼanya watu wote waliopita karibu nao, nayo haya yakaarifiwa kwa Abimeleki.

26 Basi Gaali mwana wa Ebedi akaenda pamoja na ndugu zake wakaingia Shekemu, nao watu wa huko wakamtumainia yeye.

27 Wakaenda mashambani mwao kuvuna zabibu na kuzisindika hizo zabibu, wakafanya sikukuu katika hekalu la mungu wao. Wakati wakila na kunywa, wakamlaani Abimeleki.

28 Gaali mwana wa Ebedi akasema, “Abimeleki ni nani, na Shekemu ni nani, hata tumtumikie? Je, yeye si mwana wa Yerub-Baali? Naye Zebuli si ndiye msaidizi wake? Basi watumikieni watu wa Hamori, babaye Shekemu. Kwa nini tumtumikie Abimeleki?

29 Laiti watu hawa wangekuwa chini ya amri yangu! Basi mimi ningemwondoa huyo Abimeleki. Ningemwambia Abimeleki, ‘Ondoa jeshi lako lote.’ ”

30 Zebuli aliyekuwa mtawala wa mji aliposikia aliyosema Gaali mwana wa Ebedi, akakasirika sana.

31 Akatuma ujumbe uende kwa Abimeleki kwa siri na kusema, “Gaali mwana wa Ebedi na ndugu zake wamekuja Shekemu, na wanauchochea mji huu kinyume chako.

32 Sasa, basi, usiku huu wewe uondoke na watu wako ili mje kuwavizia mashambani.

33 Kisha asubuhi wakati wa kuchomoza jua, amka mapema na ujipange dhidi ya huo mji. Wakati yeye na jeshi lililo pamoja naye watakapotoka kukabiliana nanyi, mwaweza kuwatendea kwa kadiri mnavyoweza.”

34 Kwa hiyo Abimeleki pamoja na jeshi lake lote wakaondoka usiku na kujificha karibu na Shekemu wakiwa vikosi vinne.

35 Basi Gaali mwana wa Ebedi alikuwa ametoka nje akawa amesimama katika ingilio la mji wakati ule ule ambao Abimeleki na watu wake walipokuwa wanatoka sehemu zao za maficho.

36 Gaali alipowaona, akamwambia Zebuli, “Tazama, watu wanashuka kutoka kwenye vilele vya milima!”

Zebuli akajibu, “Wewe unaona vivuli vya milima kana kwamba ni watu.”

37 Lakini Gaali akasema tena, “Tazama, watu wanashuka kutoka katikati ya nchi na kikosi kimoja kinakuja kutoka Tabur-Ezeri na kikosi kingine kutoka upande wa Elon-Meonenimu.”

38 Ndipo Zebuli akamwambia, “Kuko wapi kujivuna kwako sasa, wewe uliyesema, ‘Huyo Abimeleki ni nani hata tumtumikie?’ Hawa si wale watu uliowadharau? Toka nje sasa ukapigane nao!”

39 Basi Gaali akatoka akawaongoza watu wa Shekemu kupigana na Abimeleki.

40 Abimeleki akamfukuza, watu wengi wakajeruhiwa katika kukimbia huko, njia nzima hadi kwenye ingilio la lango.

41 Abimeleki akakaa Aruma, naye Zebuli akawafukuza Gaali na ndugu zake watoke Shekemu.

42 Kesho yake watu wa Shekemu wakatoka wakaenda mashambani, Abimeleki akaambiwa juu ya jambo hili.

43 Hivyo akawachukua watu wake, akawagawanya katika vikosi vitatu na kuwaweka waviziao huko mashambani. Alipowaona watu wanatoka kwenda nje ya mji, akainuka dhidi yao na kuwashambulia.

44 Abimeleki pamoja na vile vikosi wakaharakisha kwenda mbele kwenye nafasi, mahali pa ingilio la lango la mji. Vile vikosi viwili vikawawahi wale waliokuwa mashambani na kuwaua.

45 Siku hiyo nzima Abimeleki akazidisha mashambulizi yake dhidi ya mji hadi akawa ameuteka na kuwaua watu wa huo mji. Kisha akauangamiza mji na kusambaza chumvi juu yake.

46 Kwa kusikia jambo hili watu wote katika mnara wa Shekemu, wakaingia kwenye ngome ya hekalu la El-Berithi.

47 Abimeleki aliposikia kuwa wamekusanyika huko,

48 yeye na watu wake wote wakakwea kwenye Mlima Salmoni. Abimeleki akachukua shoka, akakata baadhi ya matawi, ambayo aliyachukua mabegani. Akawaagiza wale watu waliokuwa pamoja naye kuwa, “Fanyeni kile mlichoona mimi nikifanya!”

49 Basi watu wote wakakata matawi na kumfuata Abimeleki. Wakayakusanya hayo matawi juu ya ngome na kuitia moto ili kuwachoma wale watu wote waliokuwa ndani yake. Hivyo watu wote katika mnara wa Shekemu, karibia watu 1,000 waume kwa wake, pia wakafa.

50 Baadaye Abimeleki akaenda Thebesi na kuuzingira kwa jeshi na kuuteka.

51 Hata hivyo, ndani ya huo mji kulikuwa na mnara imara, ambako watu wote wa mji wanaume na wanawake, watu wote wa mji, walikimbilia ndani yake. Wakajifungia ndani yake na kupanda juu ya paa la mnara.

52 Abimeleki akaja kwenye ule mnara na kuushambulia, lakini alipokaribia kwenye ingilio la mnara ili kuuchoma kwa moto,

53 mwanamke mmoja akaangusha sehemu ya juu ya jiwe la kusagia juu ya kichwa cha Abimeleki, likapasua fuvu la kichwa chake.

54 Akamwita kwa haraka kijana yule aliyechukua silaha zake, na kumwambia, “Chukua upanga wako na uniue, watu wasije wakasema kwamba, ‘Mwanamke amemuua.’ ” Basi yule kijana akamchoma upanga, naye akafa.

55 Waisraeli walipoona kuwa Abimeleki amekufa, kila mtu akaenda nyumbani kwake.

56 Hivyo ndivyo Mungu alivyolipiza uovu ule ambao Abimeleki alikuwa ameutenda kwa baba yake kwa kuwaua ndugu zake sabini.

57 Mungu akawapatiliza watu wa Shekemu uovu wao juu ya vichwa vyao, na juu yao ikaja laana ya Yothamu mwana wa Yerub-Baali.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JDG/9-0a11864ae71ad68f82ef33a30f511c7e.mp3?version_id=1627—