Categories
Sefania

Sefania Utangulizi

Utangulizi

Maana ya Sefania ni “Aliyefichwa na Yehova.” Alikuwa wa ukoo wa Hezekia, mfalme wa Yuda. Nabii Sefania alihudumu wakati wa utawala wa Mfalme Yosia. Sefania alionya kwamba siku ya Bwana ingeleta hukumu kwa Yuda pamoja na Yerusalemu, hivyo akawashauri Wayahudi kumrudia Mungu. Uvamizi wa kuteka Yuda ulikuwa unakuja kutoka kaskazini, nao ungekumba pia mataifa yaliyowazunguka. Ingawa hukumu ya Yuda imeainishwa, ahadi ya kufanywa upya ni yakini. Mataifa yatahukumiwa na kutiishwa na mfalme wa Israeli, atakayetawala kutoka Sayuni.

Mwandishi

Sefania.

Kusudi

Kuwaonya watu wa Yuda waepukane na kuabudu sanamu na wamrudie Mungu wao.

Mahali

Yerusalemu.

Tarehe

Kati ya 640–621 K.K.

Wahusika Wakuu

Sefania, na watu wa Yuda.

Wazo Kuu

Sefania aliwapa watu matumaini kwamba Mungu angewarudisha watu wake nyumbani.

Mambo Muhimu

Hukumu juu ya Yuda na mataifa ya Wafilisti, Amoni na Moabu. Yerusalemu pia inatajwa kwa siku zijazo.

Mgawanyo

Kutangazwa kwa hukumu ya Mungu (

1:1–2:3

)

Hukumu dhidi ya mataifa (

2:4-15

)

Maisha ya baadaye ya Yerusalemu (

3:1-20

).

Categories
Sefania

Sefania 1

1 Neno laBwanalililomjia Sefania mwana wa Kushi, mwana wa Gedalia, mwana wa Amaria, mwana wa Hezekia, wakati wa utawala wa Yosia mwana wa Amoni mfalme wa Yuda:

Onyo La Maangamizi Yanayokuja

2 Bwanaasema,

“Nitafagia kila kitu

kutoka kwenye uso wa dunia.”

3 “Nitafagilia mbali watu na wanyama;

nitafagilia mbali ndege wa angani

na samaki wa baharini.

Wafanyao maovu watapata tu kokoto,

nami nitamkatilia mbali mwanadamu atoke katika dunia,”

asemaBwana.

Dhidi Ya Yuda

4 “Nitaiadhibu Yuda

na wote wakaao Yerusalemu.

Kutoka mahali hapa nitakatilia mbali

kila mabaki ya Baali,

majina ya wapagani na makuhani

waabuduo sanamu:

5 wale ambao husujudu juu ya mapaa

kuabudu jeshi la vitu vya angani,

wale ambao husujudu na kuapa kwaBwana

na ambao pia huapa kwa Malkamu,

6 wale wanaoacha kumfuataBwana,

wala hawamtafutiBwana

wala kutaka shauri lake.

7 Nyamazeni mbele zaBwanaMwenyezi,

kwa maana siku yaBwanaiko karibu.

Bwanaameandaa dhabihu,

amewaweka wakfu wale aliowaalika.

8 Katika siku ya dhabihu yaBwana

nitawaadhibu wakuu

na wana wa mfalme

na wale wote wanaovaa

nguo za kigeni.

9 Katika siku hiyo nitaadhibu wote ambao

hukwepa kukanyaga kizingiti,

ambao hujaza hekalu la miungu yao

kwa dhuluma na udanganyifu.”

10 Bwanaasema, “Katika siku hiyo

kilio kitapanda juu kutoka lango la Samaki,

maombolezo kutoka mtaa wa pili,

na mshindo mkubwa kutoka vilimani.

11 Ombolezeni, ninyi mnaoishi katika eneo la sokoni;

wafanyabiashara wenu wote wameangamizwa,

wote ambao wanafanya biashara ya fedha

wataangamizwa.

12 Wakati huo nitasaka mji wa Yerusalemu kwa taa,

na kuwaadhibu wale ambao

wanakaa katika hali ya kuridhika,

ambao ni kama divai

iliyobaki kwenye machicha,

ambao hudhani, ‘Bwanahatafanya lolote,

jema au baya.’

13 Utajiri wao utatekwa nyara,

nyumba zao zitabomolewa.

Watajenga nyumba,

lakini hawataishi ndani yake;

watapanda mizabibu

lakini hawatakunywa divai yake.

Siku Kubwa Ya Bwana

14 “Siku kubwa yaBwanaiko karibu:

iko karibu na inakuja haraka.

Sikilizeni! Kilio katika siku yaBwana

kitakuwa kichungu,

hata shujaa atapiga kelele.

15 Siku ile ni siku ya ghadhabu,

siku ya fadhaa na dhiki,

siku ya uharibifu na ukiwa,

siku ya giza na utusitusi,

siku ya mawingu na giza nene,

16 siku ya tarumbeta na mlio wa vita

dhidi ya miji yenye ngome

na dhidi ya minara mirefu.

17 Nitawaletea watu dhiki,

nao watatembea kama vipofu,

kwa sababu wametenda dhambi

dhidi yaBwana.

Damu yao itamwagwa kama vumbi

na matumbo yao kama taka.

18 Fedha yao wala dhahabu yao

hazitaweza kuwaokoa

katika siku hiyo ya ghadhabu yaBwana.

Katika moto wa wivu wake

dunia yote itateketezwa,

kwa maana ataleta mwisho

wa wote wanaoishi katika dunia ghafula.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ZEP/1-7b0933800ffffe34ebb9fa5dcbd54cdb.mp3?version_id=1627—

Categories
Sefania

Sefania 2

1 Kusanyikeni pamoja, kusanyikeni pamoja,

enyi taifa lisilo na aibu,

2 kabla ya wakati ulioamriwa haujafika

na siku ile inayopeperusha kama makapi,

kabla hasira kali yaBwanahaijaja juu yenu,

kabla siku ya ghadhabu yaBwana

haijaja juu yenu.

3 MtafuteniBwana, enyi nyote wanyenyekevu wa nchi,

ninyi ambao hufanya lile analoamuru.

Tafuteni haki, tafuteni unyenyekevu;

labda mtahifadhiwa

siku ya hasira yaBwana.

Dhidi Ya Ufilisti

4 Gaza utaachwa

na Ashkeloni utaachwa magofu.

Wakati wa adhuhuri Ashdodi utaachwa mtupu

na Ekroni utangʼolewa.

5 Ole wenu ninyi ambao mnaishi kando ya bahari,

enyi Wakerethi;

neno laBwanaliko dhidi yenu,

ee Kanaani, nchi ya Wafilisti.

“Mimi nitawaangamiza,

na hakuna atakayebaki.”

6 Nchi kando ya bahari, mahali ambapo wanaishi Wakerethi,

patakuwa mahali pa wachungaji

na mazizi ya kondoo.

7 Itakuwa mali ya mabaki ya nyumba ya Yuda,

hapo watapata malisho.

Wakati wa jioni watajilaza chini

katika nyumba za Ashkeloni.

BwanaMungu wao atawatunza,

naye atawarudishia wafungwa wao.

Dhidi Ya Moabu Na Amoni

8 “Nimeyasikia matukano ya Moabu

nazo dhihaka za Waamoni,

ambao waliwatukana watu wangu

na kutoa vitisho dhidi ya nchi yao.

9 Hakika, kama niishivyo,”

asemaBwanaMwenye Nguvu Zote,

Mungu wa Israeli,

“hakika Moabu itakuwa kama Sodoma,

Waamoni kama Gomora:

mahali pa magugu na mashimo ya chumvi,

nchi ya ukiwa milele.

Mabaki ya watu wangu watawateka nyara;

mabaki ya taifa langu watarithi nchi yao.”

10 Hiki ndicho watarudishiwa kwa ajili ya kiburi chao,

kwa kutukana na kudhihaki

watu waBwanaMwenye Nguvu Zote.

11 Bwanaatakuwa wa kuhofisha kwao

atakapoangamiza miungu yote ya nchi.

Mataifa katika kila pwani yatamwabudu,

kila moja katika nchi yake.

Dhidi Ya Kushi

12 “Ninyi pia, ee Wakushi,

mtauawa kwa upanga wangu.”

Dhidi Ya Ashuru

13 Mungu atanyoosha mkono wake dhidi ya kaskazini

na kuangamiza Waashuru,

akiiacha Ninawi ukiwa

na pakame kama jangwa.

14 Makundi ya kondoo na ngʼombe yatajilaza pale,

viumbe vya kila aina.

Bundi wa jangwani na bundi waliao kwa sauti nyembamba

wataishi juu ya nguzo zake.

Mwangwi wa kuita kwao utapita madirishani,

kifusi kitakuwa milangoni,

boriti za mierezi zitaachwa wazi.

15 Huu ndio mji uliotukuka na kuishi kwa furaha

wakijisikia salama.

Ulisema moyoni mwako,

“Mimi ndimi, na wala hapana mwingine ila mimi.”

Jinsi gani umekuwa gofu,

mahali pa kulala wanyama pori!

Wote wanaopita kando yake wanauzomea

na kutikisa mkono kwa dharau.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ZEP/2-1b18ca38d2ccf242c0429323ed47e58d.mp3?version_id=1627—

Categories
Sefania

Sefania 3

Hatima Ya Yerusalemu

1 Ole mji wa wadhalimu,

waasi na waliotiwa unajisi!

2 Hautii mtu yeyote,

haukubali maonyo.

HaumtumainiBwana,

haukaribii karibu na Mungu wake.

3 Maafisa wake ni simba wangurumao,

watawala wake ni mbwa mwitu wa jioni,

ambao hawabakizi chochote

kwa ajili ya asubuhi.

4 Manabii wake ni wenye kiburi,

ni wadanganyifu.

Makuhani wake hunajisi patakatifu

na kuihalifu sheria.

5 Bwanaaliye ndani yake ni mwenye haki,

hafanyi kosa.

Asubuhi kwa asubuhi hutoa haki yake,

kila kukipambazuka huitimiza,

bali mtu dhalimu hana aibu.

6 “Nimeyafutilia mbali mataifa,

ngome zao zimebomolewa.

Nimeziacha barabara ukiwa,

hakuna anayepita humo.

Miji yao imeharibiwa;

hakuna mmoja atakayeachwa:

hakuna hata mmoja.

7 Niliuambia huo mji,

‘Hakika utaniogopa na kukubali maonyo!’

Ndipo makao yake hayatafutiliwa mbali,

wala adhabu zangu zote hazitakuja juu yake.

Lakini walikuwa bado na shauku

kutenda kwa upotovu katika yote waliyofanya.”

8 Bwanaanasema,

“Kwa hiyo ningojee mimi,

siku nitakayosimama kuteka nyara.

Nimeamua kukusanya mataifa,

kukusanya falme

na kumimina ghadhabu yangu juu yao,

hasira yangu kali yote.

Dunia yote itateketezwa

kwa moto wa wivu wa hasira yangu.

9 “Ndipo nitatakasa midomo ya mataifa,

kwamba wote waweze kuliitia jina laBwana

na kumtumikia kwa pamoja.

10 Kutoka ngʼambo ya mito ya Kushi

watu wangu wanaoniabudu,

watu wangu waliotawanyika,

wataniletea sadaka.

11 Siku hiyo hutaaibishwa

kwa ajili ya makosa yote ulionitendea,

kwa sababu nitawaondoa kutoka mji huu

wale wote wanaoshangilia

katika kiburi chao.

Kamwe hutajivuna tena

katika kilima changu kitakatifu.

12 Lakini nitakuachia ndani yako

wapole na wanyenyekevu,

ambao wanatumaini jina laBwana.

13 Mabaki ya Israeli hayatafanya kosa;

hawatasema uongo,

wala udanganyifu hautakuwa

katika vinywa vyao.

Watakula na kulala

wala hakuna yeyote

atakayewaogopesha.”

14 Imba, ee Binti Sayuni;

paza sauti, ee Israeli!

Furahi na kushangilia kwa moyo wako wote,

ee Binti Yerusalemu!

15 Bwanaamekuondolea adhabu yako,

amewarudisha nyuma adui zako.

Bwana, Mfalme wa Israeli, yu pamoja nawe;

kamwe hutaogopa tena madhara yoyote.

16 Katika siku hiyo watauambia Yerusalemu,

“Usiogope, ee Sayuni;

usiiache mikono yako ilegee.

17 BwanaMungu wako yu pamoja nawe,

yeye ni mwenye nguvu kuokoa.

Atakufurahia kwa furaha kubwa,

atakutuliza kwa pendo lake,

atakufurahia kwa kuimba.”

18 “Huzuni katika sikukuu zilizoamriwa

nitaziondoa kwenu;

hizo ni mzigo na fedheha kwenu.

19 Wakati huo nitawashughulikia

wote waliokudhulumu;

nitaokoa vilema na kukusanya

wale ambao wametawanywa.

Nitawapa sifa na heshima

katika kila nchi ambayo waliaibishwa.

20 Wakati huo nitawakusanya;

wakati huo nitawaleta nyumbani.

Nitawapa sifa na heshima

miongoni mwa mataifa yote ya dunia

wakati nitakapowarudishia mateka yenu

mbele ya macho yenu hasa,”

asemaBwana.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ZEP/3-f093c4ce0bcf69b438670c034e31a7bd.mp3?version_id=1627—