Categories
Nahumu

Nahumu Utangulizi

Utangulizi

Nahumu ambaye jina lake linamaanisha “Faraja” alikuwa mwenyeji wa Elikoshi. Alihudumu wakati mmoja na Sefania, Yeremia na Habakuki. Katika ujumbe wake alizungumzia kuanguka kwa Thebesi mwaka wa 663 K.K. na kuanguka kwa Ninawi mnamo mwaka wa 612 K.K. Nahumu anaeleza kwa wazi juu ya uonevu na udhalimu wa kikatili wa Ashuru, na jinsi walivyosonga mbele na kushinda taifa moja baada ya lingine.

Ukatili huo usiokuwa na chembe cha huruma usingeweza kuvumiliwa na Mungu mwenye haki aliye mtakatifu pasipo kikomo. Katika unabii huu Nahumu anaelezea vizuri na kuonyesha kuzingirwa na kuanguka kwa Ninawi kuwa ndio mwisho wa huu ufalme wenye nguvu wa Ashuru, ambao ndio ulikuwa unakalia sehemu zenye rutuba kwa zaidi ya karne nzima. Kwa nasaha fupi kwa watu wa Yuda, Nahumu anawashauri watu wake kuzitii sikukuu zao za kidini, kwa kuwa Waashuru wasingeliishambulia tena Yerusalemu.

Mwandishi

Nahumu.

Kusudi

Kutamka hukumu ya Mungu dhidi ya Waashuru na kuwafariji Yuda.

Tarehe

Kati ya 663–612 K.K.

Mahali

Ninawi.

Wahusika Wakuu

Waninawi.

Wazo Kuu

Yehova ni Mungu mwenye wivu ambaye mapatilizo yake kwa hakika lazima yawapate adui zake, lakini yeye ni ngome kwa wale wanaomtumaini.

Mambo Muhimu

Nahumu anaeleza kukaribia kwa hukumu ya Ninawi na jinsi itakavyokuwa kwa lugha ya wazi. Anaorodhesha kwa kifupi dhambi za Ninawi na kutamka kwamba Mungu ni mwenye haki katika hukumu zake. Anamalizia kwa kuiona hukumu iliyokamilika. Hiki ndicho kitabu cha Agano la Kale kinachotoa unabii wake waziwazi juu ya ukatili wa Waashuru.

Mgawanyo

Hasira ya Mungu dhidi ya Ninawi (

1:1-15

)

Kuanguka kwa Ninawi (

2:1-13

)

Ukiwa kwa Ninawi (

3:1-19

).

Categories
Nahumu

Nahumu 1

1 Neno alilosema Mungu kuhusu Ninawi. Kitabu cha maono cha Nahumu, Mwelkoshi.

Hasira Ya Mungu Dhidi Ya Ninawi

2 Bwanani mwenye wivu na Mungu mlipiza kisasi;

Bwanahulipiza kisasi na amejaa ghadhabu.

Bwanahulipiza kisasi juu ya watesi wake,

naye anadumisha ghadhabu yake dhidi ya adui zake.

3 Bwanasi mwepesi wa hasira naye ni mwenye nguvu,

Bwanahataacha kuadhibu wenye hatia.

Njia yake ipo katika kisulisuli na tufani,

na mawingu ni vumbi la miguu yake.

4 Anakemea bahari na kuikausha,

anafanya mito yote kukauka.

Bashani na Karmeli zinanyauka

na maua ya Lebanoni hukauka.

5 Milima hutikisika mbele yake

na vilima huyeyuka.

Nchi hutetemeka mbele yake,

dunia na wote waishio ndani yake.

6 Ni nani awezaye kuzuia hasira yake yenye uchungu?

Nani awezaye kuvumilia hasira yake kali?

Ghadhabu yake imemiminwa kama moto,

na miamba inapasuka mbele zake.

7 Bwanani Mwema,

kimbilio wakati wa taabu.

Huwatunza wale wanaomtegemea,

8 lakini kwa mafuriko makubwa,

ataangamiza Ninawi;

atafuatilia adui zake hadi gizani.

9 Shauri baya lolote wapangalo dhidi yaBwana

yeye atalikomesha;

taabu haitatokea mara ya pili.

10 Watasongwa katikati ya miiba

na kulewa kwa mvinyo wao.

Watateketezwa kama mabua makavu.

11 Ee Ninawi, kutoka kwako amejitokeza mmoja,

ambaye anapanga shauri baya

dhidi yaBwana

na kushauri uovu.

12 Hili ndilo asemaloBwana:

“Ingawa wana muungano nao ni wengi sana,

watakatiliwa mbali na kuangamia.

Ingawa nimekutesa wewe, ee Yuda,

sitakutesa tena.

13 Sasa nitavunja nira zao kutoka shingo yako,

nami nitazivunjilia mbali pingu zako.”

14 Hii ndiyo amriBwanaaliyoitoa kukuhusu wewe, Ninawi:

“Hutakuwa na wazao

watakaoendeleza jina lako.

Nitaharibu sanamu za kuchonga na sanamu za kuyeyusha

ambazo zipo katika hekalu la miungu yenu.

Nitaandaa kaburi lako,

kwa maana wewe ni mwovu kabisa.”

15 Tazama, huko juu milimani,

miguu ya huyo mmoja aletaye habari njema,

ambaye anatangaza amani!

Ee Yuda, sherehekea sikukuu zako,

nawe utimize nadhiri zako.

Waovu hawatakuvamia tena;

wataangamizwa kabisa.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/NAM/1-e7b3a0bd3e138a8d3423ddb036387da5.mp3?version_id=1627—

Categories
Nahumu

Nahumu 2

Ninawi Kuanguka

1 Mshambuliaji anasogea dhidi yako, Ninawi.

Linda ngome,

chunga barabara,

jitieni nguvu wenyewe,

kusanya nguvu zako zote!

2 Bwanaatarudisha fahari ya Yakobo,

kama fahari ya Israeli,

ingawa waangamizi wamewaacha ukiwa

na wameharibu mizabibu yao.

3 Ngao za askari wake ni nyekundu,

mashujaa wamevaa nguo nyekundu.

Chuma kwenye magari ya vita chametameta,

katika siku aliyoyaweka tayari,

mikuki ya mierezi inametameta.

4 Magari ya vita yanafanya msukosuko barabarani,

yakikimbia nyuma na mbele uwanjani.

Yanaonekana kama mienge ya moto;

yanakwenda kasi kama umeme.

5 Anaita vikosi vilivyochaguliwa,

lakini bado wanajikwaa njiani.

Wanakimbilia haraka kwenye ukuta wa mji,

ile ngao ya kuwakinga imetayarishwa.

6 Malango ya mto yamefunguliwa wazi,

na jumba la kifalme limeanguka.

7 Imeagizwa kwamba mji uchukuliwe

na upelekwe uhamishoni.

Vijakazi wake wanaomboleza kama hua

na kupigapiga vifua vyao.

8 Ninawi ni kama dimbwi,

nayo maji yake yanakauka.

Wanalia, “Simama! Simama!”

Lakini hakuna anayegeuka nyuma.

9 Chukueni nyara za fedha!

Chukueni nyara za dhahabu!

Wingi wake hauna mwisho,

utajiri kutoka hazina zake zote!

10 Ameharibiwa, ametekwa nyara, ameachwa uchi!

Mioyo inayeyuka, magoti yanalegea,

miili inatetemeka,

na kila uso umebadilika rangi.

11 Liko wapi sasa pango la simba,

mahali ambapo waliwalisha watoto wao,

ambapo simba dume na simba jike walikwenda

na ambapo wana simba walikwenda

bila kuogopa chochote?

12 Simba aliua mawindo ya kutosha watoto wake,

alinyonga mawindo kwa ajili ya mwenzi wake,

akijaza makao yake kwa alivyoua

na mapango yake kwa mawindo.

13 BwanaMwenye Nguvu Zote anatangaza,

“Mimi ni kinyume na ninyi.

Magari yenu ya vita nitayateketeza kwa moto,

na upanga utakula wana simba wako.

Sitawaachia mawindo juu ya nchi.

Sauti za wajumbe wako

hazitasikika tena.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/NAM/2-a38be8b5316b20df831b93932f1e5efe.mp3?version_id=1627—

Categories
Nahumu

Nahumu 3

Ole Wa Ninawi

1 Ole wa mji umwagao damu,

uliojaa uongo,

umejaa nyara,

usiokosa kuwa na vitu vya kuteka nyara.

2 Kelele za mijeledi,

vishindo vya magurudumu,

farasi waendao mbio

na mshtuo wa magari ya vita!

3 Wapanda farasi wanaenda mbio,

panga zinameremeta,

na mikuki inangʼaa!

Majeruhi wengi,

malundo ya maiti,

idadi kubwa ya miili isiyohesabika,

watu wanajikwaa juu ya mizoga:

4 yote haya kwa sababu ya wingi wa tamaa za kahaba,

anayeshawishi, bibi wa mambo ya uchawi,

anayewatia utumwani mataifa kwa ukahaba wake

na pia jamaa za watu kwa ulozi wake.

5 BwanaMwenye Nguvu Zote anasema,

“Mimi ni kinyume na ninyi.

Nitafunika uso wako kwa gauni lako.

Nitaonyesha mataifa uchi wako

na falme aibu yako.

6 Nitakutupia uchafu,

nitakufanyia dharau

na kukufanya kioja.

7 Wote wanaokuona watakukimbia na kusema,

‘Ninawi ipo katika kuangamia:

ni nani atakayeomboleza kwa ajili yake?’

Nitampata wapi yeyote wa kukufariji?”

8 Je, wewe ni bora kuliko No-Amoni,

uliopo katika Mto Naili,

uliozungukwa na maji?

Mto ulikuwa kinga yake,

nayo maji yalikuwa ukuta wake.

9 Kushina Misri walikuwa nguvu zake zisizo na mpaka;

Putu na Libia walikuwa miongoni mwa wale walioungana naye.

10 Hata hivyo alichukuliwa mateka

na kwenda uhamishoni.

Watoto wake wachanga walivunjwa vunjwa vipande

kwenye mwanzo wa kila barabara.

Kura zilipigwa kwa watu wake wenye heshima,

na watu wake wote wakuu walifungwa kwa minyororo.

11 Wewe pia utalewa;

utakwenda mafichoni

na kutafuta kimbilio kutoka kwa adui.

12 Ngome zako zote ni kama mitini

yenye matunda yake ya kwanza yaliyoiva;

wakati inapotikiswa,

tini huanguka kwenye kinywa chake alaye.

13 Tazama vikosi vyako:

wote ni wanawake!

Malango ya nchi yako

yamekuwa wazi kwa adui zako;

moto umeteketeza mapingo yake.

14 Teka maji kwa ajili ya kuzingirwa kwako,

imarisha ulinzi wako,

Ufanyie udongo wa mfinyanzi kazi,

yakanyage matope,

karabati tanuru la kuchomea matofali!

15 Huko moto utakuteketeza,

huko upanga utakuangusha chini

na kama vile panzi, watakumaliza.

Ongezeka kama panzi,

ongezeka kama nzige!

16 Umeongeza idadi ya wafanyabiashara wako

mpaka wamekuwa wengi kuliko nyota za angani,

lakini kama nzige wanaacha nchi tupu

kisha huruka na kwenda zake.

17 Walinzi wako ni kama nzige,

maafisa wako ni kama makundi ya nzige

watuao kwenye kuta wakati wa siku ya baridi:

lakini wakati jua linapotokea wanaruka kwenda zao,

na hakuna ajuaye waendako.

18 Ee mfalme wa Ashuru, wachungaji wako wanasinzia;

wakuu wako wanalala chini mavumbini kupumzika.

Watu wako wametawanyika juu ya milima

bila kuwa na mtu yeyote wa kuwakusanya.

19 Hakuna kitu kinachoweza kuponya jeraha lako;

jeraha lako ni la kukuua.

Kila anayesikia habari zako,

hupiga makofi kwa kuanguka kwako,

kwa kuwa ni nani ambaye hajaguswa

na ukatili wako usio na mwisho?

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/NAM/3-042fb57d52bd9f9110981ba6bbb7d98c.mp3?version_id=1627—