Categories
Matendo

Matendo 10

Kornelio Amwita Petro

1 Katika mji wa Kaisaria palikuwa na mtu jina lake Kornelio, ambaye alikuwa jemadari wa kile kilichojulikana kama kikosi cha Kiitalia.

2 Yeye alikuwa mcha Mungu pamoja na wote wa nyumbani mwake. Aliwapa watu sadaka nyingi na kumwomba Mungu daima.

3 Siku moja alasiri, yapata saa tisa, aliona maono waziwazi, malaika wa Mungu akimjia na kumwambia, “Kornelio!”

4 Kornelio akamkazia macho kwa hofu akasema, “Kuna nini, Bwana?”

Malaika akamwambia, “Sala zako na sadaka zako kwa maskini zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.

5 Sasa tuma watu waende Yafa wakamwite mtu mmoja jina lake Simoni aitwaye Petro.

6 Yeye anaishi na Simoni mtengenezaji ngozi ambaye nyumba yake iko kando ya bahari.”

7 Yule malaika aliyekuwa akizungumza naye alipoondoka, Kornelio akawaita watumishi wake wawili pamoja na askari mmoja mcha Mungu aliyekuwa miongoni mwa wale waliomtumikia.

8 Akawaambia mambo yote yaliyotukia, kisha akawatuma waende Yafa.

Maono Ya Petro

9 Siku ya pili yake, walipokuwa wameukaribia mji, wakati wa adhuhuri, Petro alipanda juu ya nyumba kuomba.

10 Alipokuwa akiomba akahisi njaa, akatamani kupata chakula. Lakini wakati walikuwa wakiandaa chakula, akalala usingizi mzito sana.

11 Akaona mbingu zimefunguka na kitu kama nguo kubwa kikishushwa duniani kwa ncha zake nne.

12 Ndani yake walikuwepo aina zote za wanyama wenye miguu minne, nao watambaao nchini, na ndege wa angani.

13 Ndipo sauti ikamwambia “Petro, ondoka, uchinje na ule.”

14 Petro akajibu, “La hasha Bwana! Sijawahi kamwe kula kitu chochote kilicho najisi.”

15 Ile sauti ikasema naye mara ya pili, “Usikiite najisi kitu chochote Mungu alichokitakasa.”

16 Jambo hili lilitokea mara tatu na ghafula ile nguo ikarudishwa mbinguni.

17 Wakati Petro akiwa bado anajiuliza kuhusu maana ya maono haya, wale watu waliokuwa wametumwa na Kornelio wakaipata nyumba ya Simoni mtengenezaji wa ngozi wakawa wamesimama mbele ya lango.

18 Wakabisha hodi na kuuliza kama Simoni aliyeitwa Petro alikuwa anaishi hapo.

19 Wakati Petro akiwa anafikiria juu ya yale maono, Roho Mtakatifu akamwambia, “Simoni, wako watu watatu wanaokutafuta.

20 Inuka na ushuke, usisite kwenda nao kwa kuwa mimi nimewatuma.”

21 Petro akashuka na kuwaambia wale watu waliokuwa wametumwa kutoka kwa Kornelio, “Mimi ndiye mnayenitafuta. Mmekuja kwa sababu gani?”

22 Wale watu wakamjibu, “Tumetumwa na Kornelio yule jemadari. Yeye ni mtu mwema anayemcha Mungu, na anaheshimiwa na Wayahudi wote. Yeye ameagizwa na malaika mtakatifu akukaribishe nyumbani kwake, ili asikilize maneno utakayomwambia.”

23 Basi Petro akawakaribisha wakafuatana naye ndani, akawapa pa kulala. Kesho yake akaondoka pamoja nao, na baadhi ya ndugu kutoka Yafa wakafuatana naye.

Petro Nyumbani Mwa Kornelio

24 Siku iliyofuata wakawasili Kaisaria. Kornelio alikuwa akiwangoja pamoja na jamaa yake na marafiki zake wa karibu.

25 Petro alipokuwa akiingia ndani, Kornelio alikuja kumlaki, akaanguka miguuni pake kwa heshima.

26 Lakini Petro akamwinua akamwambia, “Simama, mimi ni mwanadamu tu.”

27 Petro alipokuwa akizungumza naye akaingia ndani na kukuta watu wengi wamekusanyika.

28 Akawaambia, “Mnajua kabisa kwamba ni kinyume cha sheria yetu Myahudi kuchangamana na mtu wa Mataifa au kumtembelea. Lakini Mungu amenionyesha kwamba nisimwite mtu yeyote kuwa najisi au asiye safi.

29 Ndiyo sababu ulipotuma niitwe nilikuja bila kupinga lolote. Basi sasa naomba unieleze kwa nini umeniita?”

30 Kornelio akajibu, “Siku nne zilizopita, nilikuwa nyumbani nikisali saa kama hii, saa tisa alasiri. Ghafula mtu aliyevaa nguo zilizongʼaa akasimama mbele yangu,

31 akasema, ‘Kornelio, maombi yako yamesikiwa na sadaka zako kwa maskini zimekumbukwa mbele za Mungu.

32 Basi tuma watu waende Yafa wakaulize mtu mmoja Simoni aitwaye Petro, yeye ni mgeni katika nyumba ya Simoni mtengenezaji ngozi, ambaye nyumba yake iko kando ya bahari.’

33 Nilituma watu kwako mara moja, nawe umefanya vyema kuja. Basi sasa sisi sote tuko hapa mbele za Mungu kuyasikiliza yote ambayo Bwana amekuamuru kutuambia.”

Hotuba Ya Petro

34 Ndipo Petro akafungua kinywa chake akasema, “Mungu hana upendeleo,

35 Lakini katika kila taifa, kila mtu amchaye na kutenda yaliyo haki hukubaliwa naye.

36 Ninyi mnajua ule ujumbe uliotumwa kwa Israeli, ukitangaza habari njema za amani kwa Yesu Kristo. Yeye ni Bwana wa wote.

37 Mnajua yale yaliyotukia katika Uyahudi wote kuanzia Galilaya baada ya mahubiri ya Yohana Mbatizaji:

38 Jinsi Mungu alivyomtia Yesu wa Nazareti mafuta katika Roho Mtakatifu na jinsi alivyokwenda huku na huko akitenda mema na kuponya wote waliokuwa wameonewa na nguvu za ibilisi, kwa sababu Mungu alikuwa pamoja naye.

39 “Sisi ni mashahidi wa mambo yote aliyoyafanya katika Uyahudi na Yerusalemu. Wakamuua kwa kumtundika msalabani.

40 Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu siku ya tatu na akamwezesha kuonekana na watu.

41 Hakuonekana kwa watu wote, lakini kwetu sisi tuliochaguliwa na Mungu kuwa mashahidi, ambao tulikula na kunywa naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu.

42 Naye alituamuru kuhubiri kwa watu wote na kushuhudia kwamba ndiye alitiwa mafuta na Mungu kuwa hakimu wa walio hai na wafu.

43 Manabii wote walishuhudia juu yake kwamba kila mtu amwaminiye hupokea msamaha wa dhambi katika Jina lake.”

Watu Wa Mataifa Wapokea Roho Mtakatifu

44 Wakati Petro alikuwa akisema maneno haya, Roho Mtakatifu aliwashukia wote waliokuwa wakisikiliza ule ujumbe.

45 Wale wa tohara walioamini waliokuja na Petro walishangaa kwa kuona kuwa kipawa cha Roho Mtakatifu kimemwagwa juu ya watu wa Mataifa.

46 Kwa kuwa waliwasikia wakinena kwa lugha mpya na kumwadhimisha Mungu.

Ndipo Petro akasema,

47 “Je, kuna mtu yeyote anayeweza kuzuia watu hawa wasibatizwe kwa maji? Wamempokea Roho Mtakatifu kama sisi tulivyompokea.”

48 Kwa hiyo akaamuru wabatizwe kwa jina la Yesu Kristo. Wakamsihi Petro akae nao kwa siku chache.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ACT/10-c8896942f2c2eda43f616429c090084c.mp3?version_id=1627—

Categories
Matendo

Matendo 11

Petro Aeleza Alivyotumwa Kwa Watu Wa Mataifa

1 Mitume na ndugu walioamini waliokuwa huko Uyahudi wakasikia kuwa watu wa Mataifa nao wamepokea neno la Mungu.

2 Hivyo Petro alipopanda Yerusalemu, wale wa tohara waliokuwa wameamini wakamshutumu,

3 wakisema, “Ulikwenda kwa watu wasiotahiriwa na kula pamoja nao.”

4 Ndipo Petro akaanza kuwaeleza kuhusu mambo yote yalivyotokea hatua kwa hatua akisema,

5 “Nilikuwa katika mji wa Yafa nikiomba, nami nikapitiwa na usingizi wa ghafula, nikaona maono. Kulikuwa na kitu kama nguo kubwa ikishuka kutoka mbinguni, ikishushwa kwa ncha zake nne, nayo ikanikaribia.

6 Nilipoangalia ndani yake kwa karibu niliona wanyama wenye miguu minne wa nchini, wanyama wa mwitu, watambaao na ndege wa angani.

7 Ndipo nikasikia sauti ikiniambia ‘Petro, ondoka uchinje na ule.’

8 “Nikajibu, ‘La hasha Bwana! Kitu chochote kilicho najisi hakijaingia kinywani mwangu.’

9 “Sauti ikasema kutoka mbinguni mara ya pili, ‘Usikiite najisi kitu chochote Mungu alichokitakasa.’

10 Jambo hili lilitokea mara tatu, ndipo kile kitu kikavutwa tena mbinguni.

11 “Wakati ule ule watu watatu, waliokuwa wametumwa kutoka Kaisaria waliwasili katika nyumba niliyokuwa nikikaa.

12 Roho Mtakatifu akaniambia niende nao bila kuwa na ubaguzi kati yao na sisi. Hawa ndugu sita pia walifuatana nami, nasi tukaingia nyumbani mwa huyo Kornelio.

13 Akatuambia jinsi alivyoona malaika aliyekuwa amesimama katika nyumba yake na kusema, ‘Tuma watu waende Yafa wakamlete Simoni aitwaye Petro.

14 Yeye atakupa ujumbe ambao kwa huo wewe na wa nyumbani mwako wote mtaokoka.’

15 “Nami nilipoanza kusema, Roho Mtakatifu akashuka juu yao kama vile alivyotushukia sisi hapo mwanzo.

16 Nami nikakumbuka neno la Bwana alivyosema, ‘Yohana alibatiza kwa maji, lakini ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu.’

17 Basi ikiwa Mungu aliwapa hawa watu kipawa kile kile alichotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo, mimi ni nani hata nifikirie kuwa ningeweza kumpinga Mungu?”

18 Waliposikia haya hawakuwa na la kupinga zaidi. Nao wakamwadhimisha Mungu wakisema, “Basi, Mungu amewapa hata watu wa Mataifa toba iletayo uzima wa milele.”

Kanisa La Antiokia

19 Basi wale waliotawanyika kwa ajili ya mateso yaliyotokana na kifo cha Stefano, wakasafiri hadi Foinike na Kipro na Antiokia. Nao hawakuhubiri lile Neno kwa mtu yeyote isipokuwa Wayahudi.

20 Lakini baadhi yao walikuwepo watu wa Kipro na Kirene, ambao walipokuja Antiokia walinena na Wayunani pia wakiwahubiria habari njema za Bwana Yesu.

21 Mkono wa Bwana ulikuwa pamoja nao, nayo idadi kubwa ya watu wakaamini na kumgeukia Bwana.

22 Habari hizi zilipofika masikioni mwa kanisa huko Yerusalemu, wakamtuma Barnaba aende Antiokia.

23 Alipofika na kuona madhihirisho ya neema ya Mungu, akafurahi na kuwatia moyo waendelee kuwa waaminifu kwa Bwana kwa mioyo yao yote.

24 Barnaba alikuwa mtu mwema, aliyejaa Roho Mtakatifu, mwenye imani, nayo idadi kubwa ya watu wakaongezeka kwa Bwana.

25 Kisha Barnaba akaenda Tarso kumtafuta Sauli,

26 naye alipompata akamleta Antiokia. Hivyo kwa mwaka mzima Barnaba na Sauli wakakutana na kanisa na kufundisha idadi kubwa ya watu. Ilikuwa ni katika kanisa la Antiokia kwa mara ya kwanza wanafunzi waliitwa Wakristo.

27 Wakati huo manabii walishuka toka Yerusalemu hadi Antiokia.

28 Mmoja wao, jina lake Agabo, akasimama akatabiri kwa uweza wa Roho Mtakatifu kwamba njaa kubwa itaenea ulimwengu mzima. Njaa hiyo ilitokea wakati wa utawala wa Klaudio.

29 Mitume wakaamua kwamba kila mtu, kulingana na uwezo alio nao, atoe msaada kwa ajili ya ndugu wanaoishi Uyahudi.

30 Wakafanya hivyo, misaada yao ikapelekwa kwa wazee kwa mikono ya Barnaba na Sauli.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ACT/11-87727ee766d3dfd4f4440eb53c560032.mp3?version_id=1627—

Categories
Matendo

Matendo 12

Yakobo Auawa, Petro Atiwa Gerezani

1 Wakati huo huo Mfalme Herode Agripa aliwakamata baadhi ya watu wa kanisa.

2 Akaamuru Yakobo, ndugu yake Yohana, auawe kwa upanga.

3 Alipoona jambo hilo limewapendeza Wayahudi, akaendelea, akamkamata pia Petro. Hii ilitokea wakati wa Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu.

4 Baada ya kumkamata alimtia gerezani, chini ya ulinzi wa vikundi vinne vya askari, vyenye askari wanne kila kimoja. Herode alikuwa amekusudia kumtoa na kumfanyia mashtaka mbele ya watu baada ya Pasaka.

5 Kwa hiyo Petro akawekwa gerezani, lakini kanisa lilikuwa likimwombea kwa Mungu kwa bidii.

6 Usiku ule kabla ya siku ambayo Herode Agripa alikuwa amekusudia kumtoa na kumfanyia mashtaka, Petro alikuwa amelala kati ya askari wawili, akiwa amefungwa kwa minyororo miwili. Nao walinzi wa zamu walikuwa wakilinda penye lango la gereza.

7 Ghafula malaika wa Bwana akatokea na nuru ikamulika mle ndani ya gereza. Yule malaika akampiga Petro ubavuni na kumwamsha, akisema, “Ondoka upesi!” Mara ile minyororo ikaanguka kutoka mikononi mwa Petro.

8 Yule malaika akamwambia, “Vaa nguo zako na viatu vyako.” Petro akafanya hivyo. Kisha akamwambia, “Jifunge vazi lako na unifuate.”

9 Petro akatoka mle gerezani akiwa amefuatana na yule malaika. Hakujua wakati huo kuwa yaliyokuwa yakitukia yalikuwa kweli. Alidhani kuwa anaona maono.

10 Wakapita lindo la kwanza na la pili, ndipo wakafika kwenye lango la chuma linaloelekea mjini. Lango likawafungukia lenyewe, nao wakapita hapo wakatoka nje. Baada ya kutembea umbali wa mtaa mmoja, ghafula yule malaika akamwacha Petro.

11 Ndipo Petro akarudiwa na fahamu, akasema, “Sasa ninajua bila shaka yoyote kuwa Bwana amemtuma malaika wake na kuniokoa kutoka makucha ya Herode Agripa na kutoka matazamio yote ya Wayahudi.”

12 Mara Petro alipotambua hili alikwenda nyumbani kwa Maria, mama yake Yohana aliyeitwa pia Marko, ambako watu wengi walikuwa wamekutana kwa maombi.

13 Petro alipobisha hodi kwenye lango la nje, mtumishi wa kike jina lake Roda, akaja kumfungulia.

14 Alipoitambua sauti ya Petro, alifurahi mno akarudi bila kufungua na kuwaeleza kwamba, “Petro yuko langoni!”

15 Wakamwambia yule mtumishi wa kike, “Umerukwa na akili.” Alipozidi kusisitiza kuwa ni kweli, wakasema, “Lazima awe ni malaika wake.”

16 Lakini Petro aliendelea kugonga langoni, nao walipofungua lango na kumwona Petro, walistaajabu sana.

17 Yeye akawaashiria kwa mkono wake wanyamaze kimya, akawaeleza jinsi Bwana alivyomtoa gerezani. Naye akaongeza kusema, “Waelezeni Yakobo na ndugu wengine habari hizi.” Kisha akaondoka akaenda sehemu nyingine.

18 Kulipokucha kukawa na fadhaa kubwa miongoni mwa wale askari kuhusu yaliyomtukia Petro.

19 Baada ya Herode kuamuru atafutwe kila mahali na bila kumpata, aliwahoji wale askari walinzi kisha akatoa amri wauawe. Basi Herode Agripa akatoka Uyahudi akaenda Kaisaria, akakaa huko kwa muda.

Kifo Cha Herode Agripa

20 Basi Herode Agripa alikuwa amekasirishwa sana na watu wa Tiro na Sidoni. Hivyo watu wa miji hiyo miwili wakaungana pamoja wakatafuta kukutana naye. Wakiisha kuungwa mkono na Blasto, mtumishi maalum wa Mfalme Herode Agripa aliyeaminika, wakaomba mapatano ya amani maana nchi zao zilitegemea nchi ya huyo mfalme kwa mahitaji yao ya chakula.

21 Katika siku iliyochaguliwa Herode Agripa akavaa mavazi yake ya kifalme, akaketi kwenye kiti chake cha enzi na kuwahutubia watu.

22 Watu waliokuwa wamekusanyika wakapiga kelele, wakisema, “Hii si sauti ya mwanadamu, bali ni ya Mungu.”

23 Ghafula, kwa kuwa Herode hakumpa Mungu utukufu, malaika wa Bwana akampiga, naye akaliwa na chango, akafa.

24 Lakini neno la Mungu likaendelea mbele na kuenea, nao wengi wakaambatana nalo.

25 Barnaba na Sauli walipomaliza ile huduma yao iliyowapeleka, wakarudi Yerusalemu wakiwa pamoja na Yohana aitwaye Marko.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ACT/12-5762c9302133399f9cb12c8a53be000f.mp3?version_id=1627—

Categories
Matendo

Matendo 13

Barnaba Na Sauli Wanatumwa

1 Katika kanisa huko Antiokia ya Shamu walikuwako manabii na walimu, yaani: Barnaba, Simeoni aitwaye Nigeri, Lukio Mkirene, Manaeni aliyekuwa amelelewa pamoja na Mfalme Herode Agripa, na Sauli.

2 Walipokuwa wakimwabudu Bwana na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, “Nitengeeni Sauli na Barnaba kwa kazi ile maalum niliyowaitia.”

3 Ndipo baada ya kufunga na kuomba, wakawawekea mikono yao na wakawatuma waende zao.

Barnaba Na Sauli Waenda Kipro

4 Hivyo, wakiwa wametumwa na Roho Mtakatifu, wakashuka kwenda Seleukia na kutoka huko wakasafiri baharini mpaka kisiwa cha Kipro.

5 Walipowasili katika mji wa Salami, wakahubiri neno la Mungu katika sinagogi la Wayahudi. Pia walikuwa na Yohana Marko kuwa msaidizi wao.

6 Walipokwisha kupita katika nchi zote hizo wakafika Pafo, ambapo walikutana na Myahudi mmoja mchawi aliyekuwa nabii wa uongo, jina lake Bar-Yesu.

7 Mtu huyu alikuwa pamoja na Sergio Paulo, mtu mwenye hekima aliyekuwa msaidizi wa mwakilishi wa mtawala wa kile kisiwa. Sergio Paulo akawaita Sauli na Barnaba akitaka kusikia neno la Mungu.

8 Lakini Elima yule mchawi (hii ndiyo maana ya jina lake), aliwapinga Barnaba na Sauli na kujaribu kumpotosha yule mkuu wa kile kisiwa aiache imani.

9 Ndipo Sauli, ambaye pia aliitwa Paulo, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu, akamkazia macho Elima huyo mchawi,

10 akamwambia, “Ewe mwana wa ibilisi, wewe ni adui wa kila kilicho haki! Umejaa kila aina ya udanganyifu na ulaghai. Je, hutaacha kuzipotosha njia za Bwana zilizonyooka?

11 Nawe sasa sikiliza, mkono wa Bwana u dhidi yako. Utakuwa kipofu, wala hutaona jua kwa muda.”

Mara ukungu na giza vikamfunika, naye akaenda huku na huko akitafuta mtu wa kumshika mkono ili amwonyeshe njia.

12 Yule mkuu wa kile kisiwa alipoona yaliyotukia, akaamini kwa sababu alistaajabishwa na mafundisho kuhusu Bwana.

Paulo Na Barnaba Huko Antiokia Ya Pisidia

13 Kisha Paulo na wenzake wakasafiri toka Pafo wakafika Perga huko Pamfilia. Lakini, Yohana Marko akawaacha huko, akarejea Yerusalemu.

14 Kutoka Perga wakaendelea hadi Antiokia ya Pisidia. Siku ya Sabato wakaingia ndani ya sinagogi, wakaketi.

15 Baada ya Sheria ya Mose na Kitabu cha Manabii kusomwa, viongozi wa sinagogi wakawatumia ujumbe wakisema, “Ndugu, kama mna neno la kuwafariji watu hawa, tafadhali lisemeni.”

16 Paulo akasimama, akawapungia mkono na kusema: “Enyi wanaume wa Israeli na ninyi nyote mnaomcha Mungu.

17 Mungu wa watu hawa wa Israeli aliwachagua baba zetu, akawafanya kustawi walipokuwa huko Misri, kwa uwezo mwingi akawaongoza na kuwatoa katika nchi ile.

18 Kwa muda wa miaka arobaini alivumilia matendo yao walipokuwa jangwani.

19 Naye baada ya kuyaangamiza mataifa saba waliokuwa wakiishi katika nchi ya Kanaani, akawapa Waisraeli nchi yao iwe urithi wao.

20 Haya yote yalichukua kama muda wa miaka 450.

“Baada ya haya, Mungu akawapa waamuzi mpaka wakati wa nabii Samweli.

21 Ndipo watu wakaomba wapewe mfalme, naye Mungu akawapa Sauli mwana wa Kishi wa kabila la Benyamini, aliyetawala kwa miaka arobaini.

22 Baada ya kumwondoa Sauli katika ufalme, akawainulia Daudi kuwa mfalme wao. Mungu pia alimshuhudia, akisema, ‘Nimemwona Daudi mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayetimiza mapenzi yangu yote.’

23 “Kutoka uzao wa mtu huyu, Mungu amewaletea Israeli Mwokozi Yesu, kama alivyoahidi.

24 Kabla ya kuja kwa Yesu, Yohana alihubiri toba na ubatizo kwa watu wote wa Israeli.

25 Yohana alipokuwa anakamilisha kazi yake, alisema: ‘Ninyi mnadhani mimi ni nani? Mimi si yeye. La hasha, lakini yeye yuaja baada yangu, ambaye mimi sistahili kufungua kamba za viatu vya miguu yake.’

26 “Ndugu zangu, wana wa Abrahamu, nanyi watu wa Mataifa mnaomcha Mungu, ujumbe huu wa wokovu umeletwa kwetu.

27 Kwa sababu wakaao Yerusalemu na viongozi wao hawakumtambua wala kuelewa maneno ya manabii yasomwayo kila Sabato, bali waliyatimiza maneno hayo kwa kumhukumu yeye.

28 Ijapokuwa hawakupata sababu yoyote ya kumhukumu kifo, walimwomba Pilato aamuru auawe.

29 Walipokwisha kufanya yale yote yaliyoandikwa kumhusu, walimshusha kutoka msalabani na kumzika kaburini.

30 Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu.

31 Naye kwa siku nyingi akawatokea wale waliokuwa pamoja naye kuanzia Galilaya hadi Yerusalemu. Nao sasa wamekuwa mashahidi wake kwa watu wetu.

32 “Nasi tunawaletea habari njema, kwamba yale Mungu aliyowaahidi baba zetu

33 sasa ameyatimiza kwetu sisi watoto wao, kwa kumfufua Yesu, kama ilivyoandikwa katika Zaburi ya pili:

“ ‘Wewe ni Mwanangu;

leo mimi nimekuzaa.’

34 Kwa kuwa Mungu alimfufua kutoka kwa wafu asioze kamwe, alitamka maneno haya:

“ ‘Nitakupa wewe baraka takatifu zilizo za hakika

nilizomwahidi Daudi.’

35 Kama ilivyosemwa mahali pengine katika Zaburi,

“ ‘Hutamwacha Aliye Mtakatifu wako kuona uharibifu.’

36 “Kwa maana Daudi akiisha kulitumikia kusudi la Mungu katika kizazi chake, alilala; akazikwa pamoja na baba zake na mwili wake ukaoza.

37 Lakini yule ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu hakuona uharibifu.

38 “Kwa hiyo ndugu zangu, nataka ninyi mjue kwamba kwa kupitia huyu Yesu msamaha wa dhambi unatangazwa kwenu.

39 Kwa kupitia yeye, kila mtu amwaminiye anahesabiwa haki kwa kila kitu ambacho asingeweza kuhesabiwa haki kwa sheria ya Mose.

40 Kwa hiyo jihadharini ili yale waliyosema manabii yasiwapate:

41 “ ‘Angalieni, enyi wenye dhihaka,

mkastaajabu, mkaangamie,

kwa maana nitatenda jambo wakati wenu

ambalo hamtasadiki,

hata kama mtu akiwaambia.’ ”

42 Paulo na Barnaba walipokuwa wakitoka nje ya sinagogi, watu wakawaomba wazungumze tena mambo hayo Sabato iliyofuata.

43 Baada ya kusanyiko la Sinagogi kutawanyika, wengi wa Wayahudi na waongofu wa dini ya Kiyahudi wakawafuata Paulo na Barnaba, wakazungumza nao na kuwahimiza wadumu katika neema ya Mungu.

44 Sabato iliyofuata, karibu watu wote wa mji walikuja kusikiliza neno la Bwana.

45 Lakini Wayahudi walipoona ule umati mkubwa wa watu walijawa na wivu, wakayakanusha maneno Paulo aliyokuwa akisema.

46 Ndipo Paulo na Barnaba wakawajibu kwa ujasiri, wakisema, “Ilitupasa kunena nanyi neno la Mungu kwanza. Lakini kwa kuwa mmelikataa, mkajihukumu wenyewe kuwa hamstahili uzima wa milele, sasa tunawageukia watu wa Mataifa.

47 Kwa maana hili ndilo Bwana alilotuamuru:

“ ‘Nimewafanya ninyi kuwa nuru kwa watu wa Mataifa,

ili mpate kuuleta wokovu hadi miisho ya dunia.’ ”

48 Watu wa Mataifa waliposikia haya wakafurahi na kulitukuza neno la Bwana; nao wote waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini.

49 Neno la Bwana likaenea katika eneo lile lote.

50 Lakini Wayahudi wakawachochea wanawake wenye kumcha Mungu, wenye vyeo pamoja na watu maarufu katika mji, wakachochea mateso dhidi ya Paulo na Barnaba na kuwafukuza kutoka eneo hilo.

51 Hivyo Paulo na Barnaba wakakungʼuta mavumbi ya miguu yao ili kuwapinga, nao wakaenda Ikonio.

52 Wanafunzi wakajawa na furaha na Roho Mtakatifu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ACT/13-6396e13b7cf5190488969c575fd12493.mp3?version_id=1627—

Categories
Matendo

Matendo 14

Paulo Na Barnaba Huko Ikonio

1 Huko Ikonio Paulo na Barnaba waliingia pamoja katika sinagogi la Wayahudi kama ilivyokuwa desturi yao. Huko wakahubiri kwa uwezo mkubwa kiasi kwamba Wayahudi pamoja na watu wa Mataifa wakaamini.

2 Lakini wale Wayahudi waliokataa kuamini, wakawachochea watu wa Mataifa, wakatia chuki ndani ya mioyo yao dhidi ya wale walioamini.

3 Hivyo Paulo na Barnaba wakakaa huko kwa muda wa kutosha wakihubiri kwa ujasiri juu ya Bwana, ambaye alithibitisha ujumbe wa neema yake kwa kuwawezesha kufanya ishara na miujiza.

4 Lakini watu wa mji ule waligawanyika, wengine wakakubaliana na Wayahudi na wengine na mitume.

5 Watu wa Mataifa na Wayahudi wakajiunga na baadhi ya viongozi, wakafanya mpango wa kuwatendea mitume mabaya na kuwapiga mawe.

6 Lakini mitume walipopata habari hizi wakakimbilia Listra na Derbe, miji ya Likaonia na sehemu zilizopakana nayo.

7 Huko wakaendelea kuhubiri habari njema.

Paulo Na Barnaba Huko Listra

8 Katika mji wa Listra, alikuwako kiwete, ambaye alikuwa amelemaa tangu kuzaliwa na hakuwa ametembea kamwe.

9 Alimsikiliza Paulo alipokuwa akihubiri. Paulo alipomtazama akaona ana imani ya kuponywa.

10 Paulo akapaza sauti, “Simama kwa miguu yako!” Mara yule mtu akasimama upesi akaanza kutembea!

11 Ule umati wa watu ulipoona yaliyokuwa yamefanywa na Paulo, wakapiga kelele kwa lugha yao ya Kilikaonia wakasema, “Miungu imetushukia katika umbo la binadamu!”

12 Wakamwita Barnaba Zeu na Paulo wakamwita Herme kwa kuwa ndiye alikuwa msemaji mkuu.

13 Kuhani wa Zeu, ambaye hekalu lake lilikuwa nje kidogo tu ya mji, akaleta mafahali na mashada ya maua penye lango la mji kwa sababu yeye na ule umati wa watu walitaka kuwatolea dhabihu.

14 Lakini mitume Paulo na Barnaba waliposikia haya, wakararua nguo zao, wakawaendea wale watu kwa haraka, wakawapigia kelele, wakisema,

15 “Enyi watu, kwa nini mnafanya mambo haya? Sisi ni wanadamu tu kama ninyi! Tunawaletea habari njema, tukiwaambia kwamba mgeuke mtoke katika mambo haya yasiyofaa, mmwelekee Mungu aliye hai, aliyeziumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo.

16 Zamani aliwaachia mataifa waishi walivyotaka.

17 Lakini hakuacha kuwaonyesha watu uwepo wake: Ameonyesha wema kwa kuwanyeshea mvua toka mbinguni na kuwapa mazao kwa majira yake, naye amewapa chakula tele na kuijaza mioyo yenu na furaha.”

18 Hata kwa maneno haya yote, ilikuwa vigumu kuuzuia ule umati wa watu kuwatolea dhabihu.

19 Ndipo wakaja baadhi ya Wayahudi kutoka Antiokia na Ikonio wakawashawishi wale watu, wakampiga Paulo kwa mawe, wakamburuta hadi nje ya mji, wakidhani amekufa.

20 Lakini baada ya wanafunzi kukusanyika akainuka na kurudi mjini. Kesho yake yeye na Barnaba wakaondoka kwenda Derbe.

Paulo Na Barnaba Warudi Antiokia Huko Syria

21 Wakahubiri habari njema katika mji huo na kupata wanafunzi wengi. Kisha wakarudi Listra, Ikonio na Antiokia,

22 wakiwaimarisha wanafunzi na kuwatia moyo waendelee kudumu katika imani. Wakawaonya wakisema, “Imetupasa kuingia katika Ufalme wa Mungu kwa kupitia katika taabu nyingi.”

23 Nao baada ya kuwateua wazee katika kila kanisa, kwa kufunga na kuomba wakawakabidhi kwa Bwana waliyemwamini.

24 Kisha wakapitia Pisidia wakafika Pamfilia.

25 Baada ya kuhubiri neno la Mungu huko Perga, wakateremkia Atalia.

26 Kutoka Atalia wakasafiri baharini wakarudi Antiokia, ambako walikuwa wamesifiwa kwa ajili ya neema ya Mungu kutokana na ile huduma waliyokuwa wameikamilisha.

27 Walipowasili Antiokia wakaliita kanisa pamoja na kutoa taarifa ya yale yote Mungu aliyokuwa ametenda kupitia kwao na jinsi alivyokuwa amefungua mlango wa imani kwa ajili ya watu wa Mataifa.

28 Nao wakakaa huko pamoja na wanafunzi kwa muda mrefu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ACT/14-b9f7eb01847dfe0441f2f02685350dac.mp3?version_id=1627—

Categories
Matendo

Matendo 15

Baraza La Yerusalemu

1 Baadhi ya watu wakashuka Antiokia kutoka Uyahudi, nao wakawa wanawafundisha wandugu: “Msipotahiriwa kufuatana na desturi aliyofundisha Mose, hamwezi kuokoka.”

2 Baada ya Paulo na Barnaba kutokubaliana nao kukawa na mabishano makali, Paulo na Barnaba na baadhi ya wengine miongoni mwao wakachaguliwa kwenda Yerusalemu ili kujadiliana jambo hili na mitume na wazee.

3 Hivyo wakasafirishwa na kanisa, wakiwa njiani wakapitia nchi ya Foinike na Samaria, wakawaeleza jinsi watu wa Mataifa walivyookoka. Habari hizi zikaleta furaha kubwa kwa ndugu wote.

4 Walipofika Yerusalemu, walipokelewa na kanisa na mitume pamoja na wazee, ndipo Paulo na Barnaba wakawaarifu kila kitu Mungu alichokuwa amefanya kupitia kwao.

5 Ndipo baadhi ya walioamini wa madhehebu ya Mafarisayo wakasimama na kusema, “Hao watu wa Mataifa lazima watahiriwe na waagizwe kutii sheria ya Mose.”

6 Mitume na wazee wakakutana pamoja ili kufikiri jambo hili.

7 Baada ya majadiliano mengi, Petro akasimama na kusema, “Ndugu zangu, mnajua kwamba siku za kwanza Mungu alinichagua ili kwa midomo yangu watu wa Mataifa wapate kusikia ujumbe wa Injili na kuamini.

8 Mungu, yeye ajuaye mioyo, alionyesha kwamba anawakubali kwa kuwapa Roho Mtakatifu kama vile alivyotupa sisi.

9 Mungu hakutofautisha kati yetu na wao, bali alitakasa mioyo yao kwa imani.

10 Sasa basi, mbona mnataka kumjaribu Mungu kwa kuweka kongwa shingoni mwa wanafunzi ambalo baba zetu wala sisi hatukuweza kulibeba?

11 Lakini sisi tunaamini ya kuwa tunaokolewa kwa neema ya Bwana Yesu Kristo, kama wao wanavyookolewa.”

12 Kusanyiko lote likakaa kimya, wakawasikiliza Paulo na Barnaba wakieleza jinsi Mungu alivyowatumia kutenda ishara na maajabu kwa watu wa Mataifa.

13 Walipomaliza kunena, Yakobo akasema, “Ndugu zangu, nisikilizeni.

14 Simoni amekwisha kutueleza jinsi Mungu, kwa mara ya kwanza alivyoonyesha kuhusika kwa kujichagulia watu kutoka watu wa Mataifa kwa ajili ya Jina lake.

15 Maneno ya manabii yanakubaliana na jambo hili, kama ilivyoandikwa:

16 “ ‘Baada ya mambo haya nitarudi,

nami nitajenga upya

nyumba ya Daudi iliyoanguka.

Nitajenga tena magofu yake

na kuisimamisha,

17 ili wanadamu wengine wote

wapate kumtafuta Bwana,

hata wale watu wa Mataifa wote

ambao wanaitwa kwa Jina langu,

asema Bwana, afanyaye mambo haya’

18 ambayo yamejulikana tangu zamani.

19 “Kwa hivyo uamuzi wangu ni kwamba, tusiwataabishe watu wa Mataifa wanaomgeukia Mungu.

20 Badala yake, tuwaandikie kwamba wajiepushe na vyakula vilivyonajisiwa kwa kutolewa sanamu, wajiepushe na uasherati, au kula mnyama aliyenyongwa, na damu.

21 Kwa maana katika kila mji kwa vizazi vilivyopita, Mose amekuwa na wale wanaotangaza sheria yake kwa kuwa imekuwa ikisomwa kwa sauti kubwa katika masinagogi kila Sabato.”

Barua Kwa Waumini Wa Mataifa

22 Mitume na wazee pamoja na kanisa lote, wakaamua kuwachagua baadhi ya watu wao na kuwatuma Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba. Wakamchagua Yuda aitwaye Barsaba pamoja na Sila, watu wawili waliokuwa viongozi miongoni mwa ndugu.

23 Wakatumwa na barua ifuatayo:

Sisi mitume na wazee, ndugu zenu,

Kwa ndugu Mataifa mlioamini mlioko Antiokia, Shamu na Kilikia:

Salamu.

24 Tumesikia kwamba kuna baadhi ya watu waliokuja huko kutoka kwetu bila ruhusa yetu na kuwasumbua, wakiyataabisha mawazo yenu.

25 Hivyo tumekubaliana wote kuwachagua baadhi ya watu na kuwatuma kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo,

26 watu ambao wamehatarisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo.

27 Kwa hiyo tunawatuma Yuda na Sila, kuthibitisha kwa maneno ya mdomo mambo haya tunayowaandikia.

28 Kwa maana imempendeza Roho Mtakatifu na sisi tusiwatwike mzigo wowote mkubwa zaidi ya mambo haya yafuatayo ambayo ni ya lazima:

29 Kwamba mjiepushe na vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, au kula nyama ya mnyama aliyenyongwa, na mjiepushe na uasherati. Mkiyaepuka mambo haya, mtakuwa mmefanya vyema.

Kwaherini.

30 Hivyo wakaagwa, wakashuka kwenda Antiokia. Baada ya kulikusanya kanisa pamoja, wakawapa ile barua.

31 Nao hao watu wakiisha kuisoma, wakafurahishwa sana kwa ujumbe wake wa kutia moyo.

32 Yuda na Sila, ambao wenyewe walikuwa manabii, wakanena maneno mengi ya kuwatia moyo na kuwajenga katika imani wale ndugu walioamini.

33 Baada ya kukaa huko Antiokia kwa muda, wakaagwa kwa amani na wale ndugu ili waende kwa wale waliowatuma. [

34 Lakini Sila bado akaendelea kukaa huko.]

35 Lakini Paulo na Barnaba walibaki Antiokia ambako wao pamoja na wengine wengi walifundisha na kuhubiri neno la Bwana.

Paulo Na Barnaba Wagawanyika

36 Baada ya muda, Paulo akamwambia Barnaba, “Turudi tukawatembelee ndugu katika miji yote tuliyohubiri neno la Bwana tuone jinsi wanavyoendelea.”

37 Barnaba alitaka wamchukue Yohana aitwaye Marko waende naye.

38 Lakini Paulo aliona si vyema kwa sababu aliwahi kuwaacha walipokuwa huko Pamfilia, hakutaka kuendelea kufanya kazi naye.

39 Pakatokea ubishi mkali kati ya Paulo na Barnaba kuhusu jambo hili, hivyo wakagawanyika. Barnaba akamchukua Yohana Marko wakasafiri baharini kwenda Kipro.

40 Lakini Paulo akamchagua Sila na akaondoka baada ya ndugu kuwatakia neema ya Bwana.

41 Akapitia Shamu na Kilikia, akiimarisha makanisa ya huko.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ACT/15-c0379c3f6e22eca653595eb16801ced6.mp3?version_id=1627—

Categories
Matendo

Matendo 16

Timotheo Aungana Na Paulo Na Sila

1 Paulo akafika Derbe na kisha Listra, ambako kulikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, ambaye mama yake alikuwa Myahudi aliyeamini, lakini baba yake alikuwa Myunani.

2 Alikuwa amesifiwa sana na wale ndugu waliokuwa wameamini huko Listra na Ikonio

3 Paulo alitaka Timotheo afuatane naye, hivyo akamchukua na kumtahiri kwa sababu ya Wayahudi waliokuwa wanaishi eneo lile kwa maana wote walimjua baba yake ni Myunani.

4 Walipokuwa wakienda mji kwa mji, wakawa wanawapa maamuzi yaliyotolewa na mitume na wazee huko Yerusalemu ili wayafuate.

5 Hivyo makanisa yakawa imara katika imani na kuongezeka kiidadi kila siku.

6 Paulo pamoja na wenzake wakasafiri sehemu za Frigia na Galatia, kwa kuwa Roho Mtakatifu hakuwaruhusu kulihubiri neno huko Asia.

7 Walipofika mpaka wa Misia, wakajaribu kuingia Bithinia lakini Roho wa Yesu hakuwaruhusu.

8 Kwa hiyo wakapita Misia, wakafika Troa.

9 Wakati wa usiku Paulo akaona maono, mtu wa Makedonia amesimama akimsihi, “Vuka uje huku Makedonia utusaidie.”

10 Baada ya Paulo kuona maono haya, tulijiandaa kwa haraka kuondoka kwenda Makedonia tukiwa tumesadiki kuwa Mungu alikuwa ametuita kuhubiri habari njema huko.

Kuokoka Kwa Lidia

11 Tukasafiri kwa njia ya bahari kutoka Troa na kwenda moja kwa moja hadi Samothrake, kesho yake tukafika Neapoli.

12 Kutoka huko tukasafiri hadi Filipi, mji mkuu wa jimbo hilo la Makedonia, uliokuwa koloni ya Warumi. Nasi tukakaa huko siku kadhaa.

13 Siku ya Sabato tukaenda nje ya lango la mji kando ya mto, mahali ambapo tulitarajia tungepata mahali pa kufanyia maombi. Tukaketi, tukaanza kuongea na baadhi ya wanawake waliokuwa wamekusanyika huko.

14 Mmoja wa wale wanawake waliotusikiliza aliitwa Lidia, mfanyabiashara wa nguo za zambarau, mwenyeji wa mji wa Thiatira, aliyekuwa mcha Mungu. Bwana akaufungua moyo wake akaupokea ujumbe wa Paulo.

15 Basi alipokwisha kubatizwa yeye na watu wa nyumba yake, alitukaribisha nyumbani kwake akisema, “Kama mmeona kweli mimi nimemwamini Bwana, karibuni mkae nyumbani mwangu.” Naye akatushawishi.

Paulo Na Sila Watiwa Gerezani

16 Siku moja, tulipokuwa tukienda mahali pa kusali, tulikutana na mtumwa mmoja wa kike ambaye alikuwa na pepo wa uaguzi. Naye alikuwa amewapa mabwana zake mapato makubwa ya fedha kwa ubashiri.

17 Huyu msichana alikuwa akimfuata Paulo na sisi akipiga kelele, “Watu hawa ni watumishi wa Mungu Aliye Juu Sana, wao wanawatangazieni njia ya wokovu.”

18 Akaendelea kufanya hivi kwa siku nyingi, lakini Paulo akiwa ameudhika sana, akageuka na kumwambia yule pepo mchafu, “Ninakuamuru katika jina la Yesu Kristo, umtoke!” Yule pepo mchafu akamtoka saa ile ile.

19 Basi mabwana wa yule mtumwa wa kike walipoona kuwa tumaini lao la kuendelea kujipatia fedha limetoweka, wakawakamata Paulo na Sila wakawaburuta mpaka sokoni mbele ya viongozi wa mji.

20 Baada ya kuwafikisha mbele ya mahakimu wakawashtaki wakisema, “Hawa watu wanaleta ghasia katika mji wetu, nao ni Wayahudi.

21 Wanafundisha desturi ambazo sisi raiya wa Kirumi hatuwezi kuzikubali au kuzitimiza.”

22 Umati wa watu waliokuwepo wakajiunga katika kuwashambulia Paulo na Sila na wale mahakimu wakaamuru wavuliwe nguo zao na wachapwe viboko.

23 Baada ya kuwachapa sana, wakawatupa gerezani na kumwagiza mkuu wa gereza awalinde kikamilifu.

24 Kufuata maelekezo haya, yule mkuu wa gereza akawaweka katika chumba cha ndani sana mle gerezani, na akawafunga miguu yao kwa minyororo.

25 Ilipokaribia usiku wa manane, Paulo na Sila walikuwa wakiomba na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, nao wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza.

26 Ghafula pakatokea tetemeko kubwa la ardhi, hata msingi wa gereza ukatikisika. Mara milango ya gereza ikafunguka na ile minyororo iliyowafunga kila mmoja ikafunguka.

27 Yule mkuu wa gereza alipoamka na kuona milango ya gereza iko wazi, akachomoa upanga wake akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wote wametoroka.

28 Lakini Paulo akapiga kelele kwa sauti kubwa, akasema, “Usijidhuru kwa maana sisi sote tuko hapa!”

29 Yule askari wa gereza akaagiza taa ziletwe, akaingia ndani ya kile chumba cha gereza, akapiga magoti akitetemeka mbele ya Paulo na Sila.

30 Kisha akawaleta nje akisema, “Bwana zangu, nifanye nini nipate kuokoka?”

31 Wakamjibu, “Mwamini Bwana Yesu Kristo, nawe utaokoka, pamoja na watu wa nyumbani mwako.”

32 Wakamwambia neno la Bwana yeye pamoja na wote waliokuwako nyumbani mwake.

33 Wakati ule ule, yule mkuu wa gereza akawachukua, akawaosha majeraha yao, kisha akabatizwa yeye pamoja na wote waliokuwa nyumbani mwake bila kuchelewa.

34 Akawapandisha nyumbani mwake akawaandalia chakula, yeye pamoja na nyumba yake yote wakafurahi sana kwa kuwa sasa walikuwa wamemwamini Mungu.

35 Kulipopambazuka wale mahakimu wakawatuma maafisa wao kwa mkuu wa gereza wakiwa na agizo linalosema, “Wafungue wale watu, waache waende zao.”

36 Mkuu wa gereza akamwambia Paulo “Mahakimu wameagiza niwaache huru, kwa hiyo tokeni na mwende zenu kwa amani.”

37 Lakini Paulo akawaambia wale maafisa, “Wametupiga hadharani bila kutufanyia mashtaka na kutuhoji, nao wakatutupa gerezani, hata ingawa sisi ni raiya wa Rumi. Nao sasa wanataka kututoa gerezani kwa siri? Hapana! Wao na waje wenyewe watutoe humu gerezani.”

38 Wale maafisa wakarudi na kuwaambia wale mahakimu maneno haya, wakaogopa sana walipofahamu kuwa Paulo na Sila ni raiya wa Rumi.

39 Kwa hiyo wakaja wakawaomba msamaha, wakawatoa gerezani, wakawaomba waondoke katika ule mji.

40 Baada ya Paulo na Sila kutoka gerezani walikwenda nyumbani kwa Lidia, ambapo walikutana na wale ndugu walioamini, wakawatia moyo, ndipo wakaondoka.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ACT/16-0cec2393049e2d3d913162ac52be00c6.mp3?version_id=1627—

Categories
Matendo

Matendo 17

Ghasia Huko Thesalonike

1 Wakasafiri kupitia Amfipoli na Apolonia wakafika Thesalonike, ambako kulikuwa na sinagogi la Wayahudi.

2 Kama desturi yake, Paulo aliingia ndani ya sinagogi, na kwa muda wa Sabato tatu akawa anahojiana nao kutoka kwenye Maandiko,

3 akidhihirisha wazi na kuthibitisha kwamba ilikuwa lazima Kristoateswe na afufuke kutoka kwa wafu. Akasema, “Huyu Yesu ninayewaambia habari zake, ndiye Kristo.”

4 Baadhi ya Wayahudi wakasadiki, wakaungana na Paulo na Sila, wakiwepo idadi kubwa ya Wayunani waliomcha Mungu na wanawake wengi mashuhuri.

5 Lakini Wayahudi ambao hawakuwa wameamini wakawa na wivu, wakawakodi watu waovu kutoka sokoni, wakakutanisha umati wa watu, wakaanzisha ghasia mjini. Wakaenda mbio nyumbani kwa Yasoni wakiwatafuta Paulo na Sila ili kuwaleta nje penye ule umati wa watu.

6 Lakini walipowakosa wakamburuta Yasoni na ndugu wengine mbele ya maafisa wa mji, wakipiga kelele: “Watu hawa ni wale walioupindua ulimwengu wamekuja huku,

7 naye Yasoni amewakaribisha nyumbani mwake. Hawa wote wanaasi amri za Kaisari wakisema yuko mfalme mwingine aitwaye Yesu.”

8 Waliposikia haya, ule umati wa watu na maafisa wa mji wakaongeza ghasia.

9 Nao baada ya kuchukua dhamana kwa ajili ya Yasoni na wenzake wakawaacha waende zao.

Paulo Na Sila Huko Beroya

10 Usiku ule ule, wale ndugu walioamini wakawapeleka Paulo na Sila waende zao Beroya. Walipowasili huko wakaenda kwenye sinagogi la Wayahudi.

11 Hawa Waberoya walikuwa waungwana zaidi kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa waliupokea ule ujumbe kwa shauku kubwa na kuyachunguza Maandiko kila siku ili kuona kama yale Paulo aliyosema yalikuwa kweli.

12 Wayahudi wengi wakaamini pamoja na wanawake na wanaume wa Kiyunani wa tabaka la juu.

13 Lakini wale Wayahudi wa Thesalonike waliposikia kuwa Paulo anahubiri neno la Mungu huko Beroya, wakaenda huko ili kuwashawishi watu na kuwachochea.

14 Mara hiyo, wale ndugu wakamsafirisha Paulo hadi pwani, lakini Sila na Timotheo wakabaki Beroya.

15 Wale waliomsindikiza Paulo wakaenda naye mpaka Athene, kisha wakarudi Beroya wakiwa na maagizo kutoka kwa Paulo kuhusu Sila na Timotheo kwamba wamfuate upesi iwezekanavyo.

Paulo Huko Athene

16 Paulo alipokuwa akiwasubiri huko Athene, alisumbuka sana moyoni mwake kuona vile mji huo ulivyojaa sanamu.

17 Hivyo akahojiana kwenye sinagogi na Wayahudi pamoja na Wayunani waliomcha Mungu, na pia sokoni kila siku na watu aliopatana nao huko.

18 Kisha baadhi ya Waepikureo na Wastoiko wenye falsafa wakakutana naye. Baadhi yao wakasema, “Je, huyu mpayukaji anajaribu kusema nini?” Wengine wakasema, “Inaonekana anasema habari za miungu ya kigeni.” Walisema haya kwa sababu Paulo alikuwa anahubiri habari njema kuhusu Yesu na ufufuo wa wafu.

19 Hivyo wakamchukua na kumleta kwenye mkutano wa Areopago, walikomwambia, “Je, tunaweza kujua mafundisho haya mapya unayofundisha ni nini?

20 Wewe unaleta mambo mapya masikioni mwetu, hivyo tungetaka kujua maana yake ni nini.”

21 (Waathene na wageni wote walioishi humo hawakutumia muda wao kufanya chochote kingine isipokuwa kueleza au kusikia mambo mapya).

22 Ndipo Paulo akasimama katikati ya Areopago akasema, “Enyi watu wa Athene! Ninaona kwamba katika kila jambo ninyi ni watu wa dini sana.

23 Kwa kuwa nilipokuwa nikitembea mjini na kuangalia kwa bidii vitu vyenu vya kuabudiwa, niliona huko madhabahu moja iliyoandikwa:Kwa Mungu Asiyejulikana. Basi sasa kile ambacho mmekuwa mkikiabudu kama kisichojulikana, ndicho ninachowahubiria.

24 “Mungu aliyeumba dunia na vyote vilivyomo ndani yake, yeye ndiye Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika mahekalu yaliyojengwa kwa mikono ya wanadamu.

25 Wala hatumikiwi na mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji chochote, kwa sababu yeye mwenyewe ndiye awapaye watu wote uhai na pumzi na vitu vyote.

26 Kutoka kwa mtu mmoja, yeye aliumba mataifa yote ya wanadamu ili waikalie dunia yote, naye akaweka nyakati za kuishi.

27 Mungu alifanya hivyo ili wanadamu wamtafute na huenda wakamfikia ingawa kwa kupapasapapasa ijapokuwa kwa kweli hakai mbali na kila mmoja wetu.

28 ‘Kwa kuwa katika yeye tunaishi, tunatembea na kuwa na uzima wetu.’ Kama baadhi ya watunga mashairi wenu walivyosema, ‘Sisi ni watoto wake.’

29 “Kwa kuwa sisi ni watoto wa Mungu, haitupasi kudhani kuwa uungu ni kama sanamu ya dhahabu au ya fedha au ya jiwe, mfano uliotengenezwa kwa ubunifu na ustadi wa mwanadamu.

30 Zamani wakati wa ujinga, Mungu alijifanya kama haoni, lakini sasa anawaamuru watu wote kila mahali watubu.

31 Kwa kuwa ameweka siku ambayo atauhukumu ulimwengu kwa haki akimtumia mtu aliyemchagua. Amewahakikishia watu wote mambo haya kwa kumfufua Kristo kutoka kwa wafu.”

32 Waliposikia habari za ufufuo wa wafu, baadhi yao wakadhihaki, lakini wengine wakasema, “Tunataka kukusikia tena ukizungumza juu ya jambo hili.”

33 Kwa hiyo Paulo akaondoka katikati yao.

34 Lakini baadhi yao wakaungana naye wakaamini. Kati yao alikuwepo Dionisio, Mwareopago na mwanamke mmoja aliyeitwa Damari na wengine wengi.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ACT/17-50b13e9b92ad3a5eb08c1cdcde730e8e.mp3?version_id=1627—

Categories
Matendo

Matendo 18

Paulo Huko Korintho

1 Baada ya haya, Paulo akaondoka Athene akaenda Korintho.

2 Huko akakutana na Myahudi mmoja jina lake Akila, mwenyeji wa Ponto, ambaye alikuwa amewasili karibuni kutoka Italia pamoja na mkewe Prisila, kwa sababu Klaudio alikuwa ameamuru Wayahudi wote waondoke Rumi. Paulo akaenda kuwaona,

3 naye kwa kuwa alikuwa mtengeneza mahema kama wao, akakaa na kufanya kazi pamoja nao.

4 Kila Sabato Paulo alikuwa akihojiana nao katika sinagogi, akijitahidi kuwashawishi Wayahudi na Wayunani.

5 Sila na Timotheo walipowasili kutoka Makedonia, walimkuta Paulo akiwa amejitolea muda wake wote katika kuhubiri, akiwashuhudia Wayahudi kwamba Yesu ndiye Kristo

6 Wayahudi walipompinga Paulo na kukufuru, yeye aliyakungʼuta mavazi yakef, akawaambia, “Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu! Mimi sina hatia, nimetimiza wajibu wangu. Kuanzia sasa nitawaendea watu wa Mataifa.”

7 Kisha akaondoka mle kwenye sinagogi, akaenda nyumbani kwa mtu mmoja jina lake Tito Yusto, aliyekuwa mcha Mungu. Nyumba yake ilikuwa karibu na sinagogi.

8 Kiongozi wa hilo sinagogi, aliyeitwa Krispo, akamwamini Bwana, yeye pamoja na watu wote wa nyumbani mwake. Nao Wakorintho wengi waliomsikia Paulo pia wakaamini na kubatizwa.

9 Usiku mmoja Bwana akamwambia Paulo katika maono, “Usiogope, lakini endelea kusema wala usinyamaze,

10 kwa maana mimi niko pamoja nawe, wala hakuna mtu atakayeweza kukushambulia ili kukudhuru, kwa kuwa ninao watu wengi katika mji huu ambao ni watu wangu.”

11 Hivyo Paulo akakaa huko kwa muda wa mwaka mmoja na nusu, akiwafundisha neno la Mungu.

12 Lakini wakati Galio alipokuwa msaidizi wa mwakilishi wa mtawala huko Akaya, Wayahudi waliungana kumshambulia Paulo, wakamkamata na kumpeleka mahakamani.

13 Wakamshtaki wakisema, “Mtu huyu anawashawishi watu wamwabudu Mungu kinyume cha sheria.”

14 Paulo alipotaka kujitetea, Galio akawaambia Wayahudi, “Kama ninyi Wayahudi mlikuwa mkilalamika kuhusu makosa makubwa ya uhalifu ingekuwa haki kwangu kuwasikiliza.

15 Lakini kwa kuwa linahusu maneno, majina na sheria yenu, amueni ninyi wenyewe. Mimi sitakuwa mwamuzi wa mambo haya.”

16 Akawafukuza kutoka mahakamani.

17 Ndipo wote wakamkamata Sosthene kiongozi wa sinagogi, wakampiga mbele ya mahakama, lakini Galio hakujali kitendo chao hata kidogo.

Paulo Arudi Antiokia

18 Baada ya kukaa Korintho kwa muda, Paulo akaagana na wale ndugu walioamini, akasafiri kwa njia ya bahari kwenda Shamu akiwa amefuatana na Prisila na Akila. Walipofika Kenkrea, Paulo alinyoa nywele zake kwa kuwa alikuwa ameweka nadhiri.

19 Walipofika Efeso, Paulo aliwaacha Prisila na Akila huko, lakini yeye akaingia kwenye sinagogi akawa anajadiliana na Wayahudi.

20 Walipomwomba akae nao kwa muda mrefu zaidi hakukubali.

21 Lakini alipokuwa akiondoka, akaahidi, “Nitarudi kama Mungu akipenda.” Kisha akasafiri kwa njia ya bahari kutoka Efeso.

22 Alitia nanga Kaisaria, akaenda Yerusalemu na kulisalimu kanisa, kisha akaenda Antiokia.

23 Baada ya kukaa huko kwa muda, akaondoka na kwenda sehemu moja hadi nyingine huko Galatia na Frigia, akiwaimarisha wanafunzi wote.

Huduma Ya Apolo Huko Efeso Na Korintho

24 Basi akaja Efeso Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mwenyeji wa Iskanderia. Yeye alikuwa na elimu kubwa, pia alikuwa hodari katika Maandiko.

25 Alikuwa amefundishwa katika njia ya Bwana, naye alikuwa na bidii katika roho, akafundisha kwa usahihi juu ya Yesu, ingawa alijua tu ubatizo wa Yohana.

26 Apolo alianza kunena kwa ujasiri mkubwa katika sinagogi. Lakini Prisila na Akila walipomsikia, walimchukua kando na kumweleza njia ya Mungu kwa ufasaha zaidi.

27 Naye Apolo alipotaka kwenda Akaya, ndugu wa Efeso walimtia moyo, wakawaandikia wanafunzi huko ili wamkaribishe. Alipofika huko, aliwasaidia sana wale ambao, kwa neema ya Mungu, walikuwa wameamini.

28 Kwa uwezo mkubwa aliwakanusha hadharani Wayahudi waliokuwa wakipinga, akionyesha kwa njia ya Maandiko kwamba Yesu ndiye Kristo.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ACT/18-569898ba70fe739ab78724de15b5fd0f.mp3?version_id=1627—

Categories
Matendo

Matendo 19

Paulo Huko Efeso

1 Apolo alipokuwa huko Korintho, Paulo alisafiri sehemu za bara, akafika Efeso. Huko akawakuta wanafunzi kadhaa,

2 akawauliza, “Je, mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini?”

Wakajibu, “Hapana, hata hatukusikia kuwa kuna Roho Mtakatifu.”

3 Ndipo Paulo akawauliza, “Je, mlibatizwa kwa ubatizo gani?” Wakajibu, “Kwa ubatizo wa Yohana.”

4 Paulo akasema, “Ubatizo wa Yohana ulikuwa wa toba, aliwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja baada yake, yaani, Yesu.”

5 Waliposikia haya, wakabatizwa katika jina la Bwana Yesu.

6 Paulo alipoweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akawashukia, nao wakanena kwa lugha mpya na kutabiri.

7 Walikuwa kama wanaume kumi na wawili.

8 Paulo akaingia katika sinagogi na kunena humo kwa ujasiri kwa muda wa miezi mitatu, akijadiliana na watu na kuwashawishi katika mambo ya Ufalme wa Mungu.

9 Lakini baadhi yao walikaidi. Walikataa kuamini, na wakakashifu ujumbe wake mbele ya umati wa watu. Basi Paulo aliachana nao. Akawachukua wanafunzi naye, akahojiana nao kila siku katika darasa la Tirano.

10 Jambo hili likaendelea kwa muda wa miaka miwili, kiasi kwamba Wayahudi na Wayunani wote walioishi huko Asia wakawa wamesikia neno la Bwana.

Wana Wa Skewa Wajaribu Kutoa Pepo Mchafu

11 Mungu akafanya miujiza mingi isiyo ya kawaida kwa mkono wa Paulo,

12 hivi kwamba leso au vitambaa vilivyokuwa vimegusa mwili wa Paulo viliwekwa juu ya wagonjwa, nao wakapona magonjwa yao, na pepo wachafu wakawatoka.

13 Basi baadhi ya Wayahudi wenye kutangatanga huku na huko wakitoa pepo wachafu wakajaribu kutumia jina la Bwana Yesu wale wenye pepo wakisema, “Kwa jina la Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo, nakuamuru utoke.”

14 Wana saba wa Skewa, Myahudi aliyekuwa kiongozi wa makuhani, walikuwa wanafanya hivyo.

15 Lakini pepo mchafu akawajibu, “Yesu namjua na Paulo pia namjua, lakini ninyi ni nani?”

16 Kisha yule mtu aliyekuwa na pepo mchafu akawarukia, akawashambulia vikali, akawashinda nguvu wote, wakatoka ndani ya ile nyumba wakikimbia wakiwa uchi na wenye majeraha.

17 Habari hii ikajulikana kwa Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawajaa wote, nalo jina la Bwana Yesu likaheshimiwa sana.

18 Wengi wa wale waliokuwa wameamini wakati huu wakaja na kutubu waziwazi kuhusu matendo yao maovu.

19 Idadi kubwa ya wale waliofanya mambo ya uganga wakaleta vitabu vyao na kuviteketeza kwa moto hadharani. Walipofanya hesabu ya thamani ya vitabu vilivyoteketezwa ilikuwa drakma 50,000za fedha.

20 Hivyo neno la Bwana likaenea sana na kuwa na nguvu.

21 Baada ya mambo haya kutukia, Paulo akakusudia rohoni kwenda Yerusalemu kupitia Makedonia na Akaya. Akasema, “Baada ya kufika huko, yanipasa pia kwenda Rumi.”

22 Hivyo akatuma wasaidizi wake wawili, Timotheo na Erasto, waende Makedonia, wakati yeye mwenyewe alibaki kwa muda kidogo huko Asia.

Ghasia Huko Efeso

23 Wakati huo huo pakatokea dhiki kubwa kwa sababu ya Njia ile ya Bwana.

24 Mtu mmoja jina lake Demetrio mfua fedha aliyekuwa akitengeneza vinyago vya fedha vya Artemi na kuwapatia mafundi wake biashara kubwa,

25 aliwaita pamoja watu wengine waliofanya kazi ya ufundi kama yake na kusema, “Enyi watu, mnajua ya kuwa utajiri wetu unatokana na biashara hii!

26 Pia ninyi mmeona na kusikia jinsi ambavyo si huku Efeso peke yake lakini ni karibu Asia yote, huyu Paulo amewashawishi na kuvuta idadi kubwa ya watu kwa kusema kuwa miungu iliyotengenezwa na watu si miungu.

27 Kwa hiyo kuna hatari si kwa kazi yetu kudharauliwa tu, bali pia hata hekalu la mungu mke Artemi, aliye mkuu, anayeabudiwa Asia yote na ulimwengu wote, litakuwa limepokonywa fahari yake ya kiungu.”

28 Waliposikia maneno haya, wakaghadhibika, wakaanza kupiga kelele, “Artemi wa Waefeso ni mkuu!”

29 Mara mji wote ukajaa ghasia. Wakawakamata Gayo na Aristarko, watu wa Makedonia waliokuwa wakisafiri pamoja na Paulo, na watu wakakimbilia katika ukumbi wa michezo kama mtu mmoja.

30 Paulo akataka kuingia katikati ya umati huo, lakini wanafunzi hawakumruhusu.

31 Hata baadhi ya viongozi wa sehemu ile, waliokuwa rafiki zake Paulo, wakatuma watu wakitamani asiingie katika ule ukumbi.

32 Ule umati ulikuwa na taharuki. Wengine walikuwa wakipiga kelele, hawa wakisema hili na wengine lile. Idadi kubwa ya watu hawakujua hata ni kwa nini walikuwa wamekusanyika huko.

33 Wayahudi wakamsukumia Aleksanda mbele na baadhi ya watu kwenye ule umati wakampa maelekezo. Akawaashiria kwa mkono ili watulie aweze kujitetea mbele ya watu.

34 Lakini walipotambua kwamba alikuwa Myahudi, wote wakapiga kelele kwa sauti moja kwa karibu muda wa saa mbili, wakisema, “Artemi wa Efeso ni mkuu!”

35 Baadaye karani wa mji akaunyamazisha ule umati wa watu na kusema, “Enyi watu wa Efeso, je, ulimwengu wote haujui ya kuwa mji wa Efeso ndio unaotunza hekalu la Artemi aliye mkuu na ile sanamu yake iliyoanguka kutoka mbinguni?

36 Kwa hiyo, kwa kuwa mambo haya hayakanushiki, inawapasa mnyamaze na wala msifanye lolote kwa haraka.

37 Kwa kuwa mmewaleta hawa watu hapa, ingawa hawajaiba hekaluni wala kumkufuru huyu mungu wetu wa kike.

38 Basi, ikiwa Demetrio na mafundi wenzake wana jambo zito dhidi ya mtu yeyote, mahakama ziko wazi na wasaidizi wa mwakilishi wa mtawala. Wanaweza kufungua mashtaka.

39 Lakini kama kuna jambo jingine lolote zaidi mnalotaka kulileta, itabidi lisuluhishwe katika kusanyiko halali.

40 Kama ilivyo sasa, tuko hatarini kushtakiwa kwa kufanya ghasia kwa sababu ya tukio la leo. Kwa kuwa hakuna sababu tutakayoweza kutoa kuhalalisha msukosuko huu.”

41 Baada ya kusema haya akavunja mkutano.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ACT/19-91ace03528c5a213e2d2c189f40ab9df.mp3?version_id=1627—