Categories
Marko

Marko Utangulizi

Utangulizi

Yohana Marko, mwandishi wa Injili hii, alitajwa na mababa wa kanisa la mwanzo, yaani Papiasi, Irenio na Klementi wa Iskanderia, kuwa mshirika wa karibu sana wa Mtume Petro. Yohana Marko alikuwa mtoto wa Maria, ambaye nyumba yake ilikuwa kituo kikuu cha Ukristo huko Yerusalemu. Hatimaye Marko aliishi Rumi ambako aliandika kumbukumbu za Mtume Petro.

Marko alisafiri na mjomba wake, Barnaba, kwenda Antiokia ya Syria walipofuatana na Paulo kwenye safari yake ya kwanza ya kitume. Hata hivyo Marko aliwaacha Barnaba na Paulo huko Kipro na kurudi Yerusalemu. Baadaye Barnaba na Marko walielekea Kipro wakati Paulo alienda Asia. Miaka kama kumi baadaye, Marko alikuwa pamoja na Paulo huko Rumi. Shabaha ya Marko ilikuwa kukusanya pamoja ujumbe wote wa Injili kwa kifupi.

Mwandishi

Yohana Marko.

Kusudi

Kumtambulisha Yesu, kazi, na mafundisho yake.

Mahali

Rumi.

Tarehe

Kati ya 55-65 B.K.

Wahusika Wakuu

Yesu Kristo na wanafunzi wake, Pilato, na viongozi wa dini ya Kiyahudi.

Wazo Kuu

Marko anamdhihirisha Bwana Yesu kuwa Mtumishi wa Mungu, na Mtu wa vitendo aliyekuja kuyatimiza mapenzi ya Mungu.

Mambo Muhimu

Marko anaanza kwa kueleza habari za huduma ya Bwana Yesu hadharani na mahubiri yake kuhusu Habari Njema za Ufalme wa Mungu. Kisha anatoa wazi unabii kuhusu matazamio ya kifo cha Bwana Yesu. Hatimaye anaeleza jinsi Bwana Yesu alivyosulubiwa msalabani kwa ajili ya dhambi za ulimwengu, na alivyofufuliwa kutoka kwa wafu; pia maneno na maagizo yake ya mwisho kwa wanafunzi wake.

Mgawanyo

Yohana Mbatizaji, na ubatizo wa Bwana Yesu (

1:1-13

)

Huduma ya Yesu huko Galilaya (

1:14–9:50

)

Safari ya kwenda Yerusalemu na kuingia mjini (

10:1–11:26

)

Matatizo mjini Yerusalemu (

11:27–12:44

)

Unabii kuhusu mambo yajayo (

13:1-37

)

Kufa na kufufuka kwa Yesu (

14:1–16:20

).

Categories
Marko

Marko 1

Mahubiri Ya Yohana Mbatizaji

1 Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.

2 Kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya:

“Tazama, nitamtuma mjumbe wangu mbele yako,

atakayetengeneza njia mbele yako”:

3 “sauti ya mtu aliaye nyikani.

‘Itengenezeni njia ya Bwana,

yanyoosheni mapito yake.’ ”

4 Yohana alikuja, akibatiza huko nyikani, akihubiri ubatizo wa toba kwa ajili ya msamaha wa dhambi.

5 Watu kutoka Uyahudi wote na sehemu zote za Yerusalemu walikuwa wakimwendea. Nao wakaziungama dhambi zao, akawabatiza katika Mto Yordani.

6 Yohana alivaa mavazi yaliyotengenezwa kwa singa za ngamia na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu.

7 Naye alihubiri akisema, “Baada yangu atakuja yeye aliye na uwezo kuniliko mimi, ambaye sistahili hata kuinama na kulegeza kamba za viatu vyake.

8 Mimi nawabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu.”

Ubatizo Wa Yesu

9 Wakati huo Yesu akaja kutoka Nazareti ya Galilaya, naye akabatizwa na Yohana katika Mto Yordani.

10 Yesu alipokuwa akitoka ndani ya maji, aliona mbingu zikifunguka na Roho akishuka juu yake kama hua.

11 Nayo sauti kutoka mbinguni ikasema, “Wewe ni Mwanangu mpendwa; nami nimependezwa nawe sana.”

Majaribu Ya Yesu

12 Wakati huo huo, Roho akamwongoza Yesu kwenda nyikani,

13 naye akawa huko nyikani kwa muda wa siku arobaini, akijaribiwa na Shetani. Alikaa na wanyama wa mwituni, nao malaika wakamhudumia.

Yesu Aanza Kuhubiri

14 Baada ya Yohana kukamatwa na kutiwa gerezani, Yesu aliingia Galilaya akaanza kuhubiri habari njema ya Mungu,

15 akisema, “Wakati umewadia, Ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari Njema.”

Yesu Awaita Wanafunzi Wanne

16 Yesu alipokuwa akitembea kando ya Bahari ya Galilaya, aliwaona Simoni na Andrea nduguye wakizitupa nyavu zao baharini, kwa kuwa wao walikuwa wavuvi.

17 Yesu akawaambia, “Njooni, nifuateni nami nitawafanya mwe wavuvi wa watu.”

18 Mara wakaacha nyavu zao, wakamfuata.

19 Alipokwenda mbele kidogo, akamwona Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye, wakiwa kwenye mashua yao wakizitengeneza nyavu zao.

20 Papo hapo akawaita, nao wakamwacha Zebedayo baba yao kwenye mashua pamoja na watumishi wa kuajiriwa, nao wakamfuata Yesu.

Yesu Amtoa Pepo Mchafu

21 Wakaenda mpaka Kapernaumu. Ilipofika siku ya Sabato, mara Yesu akaingia sinagogi, akaanza kufundisha.

22 Watu wakashangaa sana kwa mafundisho yake, kwa maana aliwafundisha kama yeye aliye na mamlaka, wala si kama walimu wa sheria.

23 Wakati huo huo katika sinagogi lao palikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu,

24 naye akapiga kelele akisema, “Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakujua wewe ni nani. Wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu!”

25 Lakini Yesu akamkemea, akamwambia, “Nyamaza kimya! Nawe umtoke!”

26 Yule pepo mchafu akamtikisatikisa huyo mtu kwa nguvu, kisha akamtoka akipiga kelele kwa sauti kubwa.

27 Watu wote wakashangaa, hata wakaulizana wao kwa wao, “Haya ni mambo gani? Ni mafundisho mapya, tena yenye mamlaka! Anaamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii!”

28 Sifa zake zikaanza kuenea haraka katika eneo lote la karibu na Galilaya.

Yesu Amponya Mama Mkwe Wa Simoni

29 Mara walipotoka katika sinagogi, walikwenda pamoja na Yakobo na Yohana hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea.

30 Mama mkwe wa Simoni alikuwa kitandani, ana homa, nao wakamweleza Yesu habari zake.

31 Hivyo Yesu akamwendea, akamshika mkono na kumwinua. Kisha homa ikamwacha, naye akaanza kuwahudumia.

Yesu Aponya Wengi

32 Jioni ile baada ya jua kutua, watu wakamletea Yesu wagonjwa wote na waliopagawa na pepo wachafu.

33 Mji wote ukakusanyika mbele ya nyumba hiyo.

34 Yesu akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa ya aina mbalimbali. Akawatoa pepo wachafu wengi, lakini hakuwaacha hao pepo wachafu waseme, kwa sababu walimjua yeye ni nani.

Yesu Aenda Galilaya

35 Alfajiri na mapema sana kulipokuwa bado kuna giza, Yesu akaamka, akaondoka, akaenda mahali pa faragha ili kuomba.

36 Simoni na wenzake wakaenda kumtafuta,

37 nao walipomwona, wakamwambia, “Kila mtu anakutafuta!”

38 Yesu akawajibu, “Twendeni mahali pengine kwenye vijiji jirani, ili niweze kuhubiri huko pia, kwa sababu hicho ndicho nilichokuja kukifanya.”

39 Kwa hiyo akazunguka Galilaya kote, akihubiri katika masinagogi yao na kutoa pepo wachafu.

Yesu Amtakasa Mwenye Ukoma

40 Mtu mmoja mwenye ukoma alimjia Yesu, akamwomba akipiga magoti, akamwambia, “Ukitaka, waweza kunitakasa.”

41 Yesu, akiwa amejawa na huruma, akanyoosha mkono wake akamgusa, akamwambia, “Nataka. Takasika!”

42 Mara ukoma ukamtoka, naye akatakasika.

43 Baada ya Yesu kumwonya vikali, akamruhusu aende zake

44 akimwambia, “Hakikisha humwambii mtu yeyote habari hizi, bali nenda ukajionyeshe kwa kuhani, na ukatoe sadaka alizoagiza Mose kwa utakaso wako, ili kuwa ushuhuda kwao.”

45 Lakini yule mtu akaenda akaanza kutangaza habari za kuponywa kwake waziwazi. Kwa hiyo, Yesu hakuweza tena kuingia katika miji waziwazi lakini alikaa sehemu zisizo na watu. Hata hivyo watu wakamfuata huko kutoka kila upande.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/MRK/1-5ff4b3b32c76068a43d826c8b48a799e.mp3?version_id=1627—

Categories
Marko

Marko 2

Yesu Amponya Mtu Aliyepooza

1 Baada ya siku kadhaa Yesu alirudi Kapernaumu, watu wakasikia kwamba amerudi nyumbani.

2 Hivyo watu wengi wakakusanyika kiasi kwamba hapakubaki nafasi yoyote hata mlangoni! Naye akawahubiria Neno.

3 Ndipo baadhi ya watu wakaja wakamletea Yesu mtu aliyepooza, akiwa amebebwa na watu wanne.

4 Kwa kuwa walikuwa hawawezi kumfikisha kwa Yesu kwa ajili ya umati wa watu, walitoboa tundu kwenye paa mahali pale alipokuwa Yesu, wakamshusha yule aliyepooza kwa kitanda alichokuwa amelalia.

5 Yesu alipoiona imani yao, alimwambia yule mtu aliyepooza, “Mwanangu, dhambi zako zimesamehewa.”

6 Basi baadhi ya walimu wa sheria waliokuwa wameketi huko wakawaza mioyoni mwao,

7 “Kwa nini mtu huyu anasema hivi? Huyu anakufuru! Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?”

8 Mara moja Yesu akatambua rohoni mwake kile walichokuwa wanawaza mioyoni mwao, naye akawaambia, “Kwa nini mnawaza hivyo mioyoni mwenu?

9 Je, ni lipi lililo rahisi zaidi: kumwambia huyu aliyepooza, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uchukue mkeka wako, uende’?

10 Lakini ili mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani kusamehe dhambi…” Yesu akamwambia yule aliyepooza,

11 “Nakuambia, inuka, chukua mkeka wako, uende nyumbani kwako.”

12 Yule mtu aliyekuwa amepooza akasimama, akachukua mkeka wake, akatembea machoni pao wote! Jambo hili likawashangaza wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, “Hatujapata kuona jambo kama hili kamwe!”

Yesu Amwita Lawi

13 Yesu akaenda tena kandokando ya Bahari ya Galilaya. Umati mkubwa wa watu ukamfuata, naye akaanza kuwafundisha.

14 Alipokuwa akitembea, akamwona Lawi mwana wa Alfayo ameketi forodhani mahali pa kutoza ushuru, akamwambia, “Nifuate.” Lawi akaondoka, akamfuata Yesu.

15 Yesu alipokuwa akila chakula nyumbani mwa Lawi, watoza ushuru wengi pamoja na “wenye dhambi” walikuwa wakila pamoja naye na wanafunzi wake, kwa maana kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakimfuata.

16 Baadhi ya walimu wa sheria waliokuwa Mafarisayo walipomwona akila pamoja na watoza ushuru na “wenye dhambi,” wakawauliza wanafunzi wake: “Mbona Yesu anakula pamoja na watoza ushuru na ‘wenye dhambi’?”

17 Yesu aliposikia haya akawaambia, “Watu wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio wagonjwa. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”

Yesu Aulizwa Kuhusu Kufunga

18 Basi wanafunzi wa Yohana pamoja na Mafarisayo walikuwa wakifunga. Baadhi ya watu wakamjia Yesu na kumuuliza, “Mbona wanafunzi wa Yohana na wa Mafarisayo hufunga lakini wanafunzi wako hawafungi?”

19 Yesu akawajibu, “Wageni wa bwana arusi wawezaje kufunga wakati angali pamoja nao? Wakati bwana arusi bado yuko pamoja nao, hawawezi kufunga.

20 Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao. Siku hiyo ndipo watakapofunga.

21 “Hakuna mtu ashoneaye kiraka cha nguo mpya kwenye nguo iliyochakaa. Akifanya hivyo, kile kiraka kipya kitachanika kutoka ile nguo iliyochakaa, nayo itachanika zaidi.

22 Wala hakuna mtu awekaye divai mpya kwenye viriba vikuukuu. Akifanya hivyo, ile divai mpya itavipasua hivyo viriba, nayo hiyo divai itamwagika na viriba vitaharibika. Lakini divai mpya huwekwa kwenye viriba vipya.”

Bwana Wa Sabato

23 Siku moja ya Sabato, Yesu pamoja na wanafunzi wake walikuwa wakipita katikati ya mashamba ya nafaka. Walipokuwa wakitembea, wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke.

24 Mafarisayo wakamwambia, “Tazama, mbona wanafanya jambo lisilo halali kufanywa siku ya Sabato?”

25 Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma kamwe alivyofanya Daudi wakati yeye na wenzake walikuwa na njaa, wakahitaji chakula?

26 Daudi aliingia katika nyumba ya Mungu, wakati Abiathari alikuwa kuhani mkuu, akaila ile mikate iliyowekwa wakfu, ambayo ni halali kuliwa na makuhani peke yao. Naye pia akawapa wenzake.”

27 Kisha Yesu akawaambia, “Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, lakini si mwanadamu kwa ajili ya Sabato.

28 Hivyo, Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/MRK/2-133c114d435642dbff0d57776d3d79a6.mp3?version_id=1627—

Categories
Marko

Marko 3

Mtu Aliyepooza Mkono Aponywa

1 Yesu akaingia tena ndani ya sinagogi, na huko palikuwa na mtu aliyepooza mkono.

2 Wakawa wanamwangalia waone kama atamponya siku ya Sabato, ili wapate sababu ya kumshtaki.

3 Yesu akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Njoo hapa mbele ya watu wote.”

4 Kisha Yesu akawauliza, “Je, ni lipi lililo halali siku ya Sabato: Ni kutenda mema au kutenda mabaya? Ni kuokoa maisha au kuua?” Lakini wao wakanyamaza kimya.

5 Yesu akawatazama pande zote kwa hasira, akahuzunika sana kwa ajili ya ugumu wa mioyo yao. Akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, “Nyoosha mkono wako.” Akaunyoosha, nao ukaponywa kabisa!

6 Kisha Mafarisayo wakatoka nje, nao wakaanza kufanya shauri la kumuua Yesu wakiwa na Maherode.

Umati Wa Watu Wamfuata Yesu

7 Yesu pamoja na wanafunzi wake wakaondoka huko wakaenda baharini, nao umati mkubwa wa watu kutoka Galilaya ukamfuata.

8 Waliposikia mambo yote aliyokuwa akiyafanya, umati mkubwa wa watu ukamjia kutoka Uyahudi, Yerusalemu, Idumaya, na ngʼambo ya Yordani, pamoja na wale wa sehemu za karibu na Tiro na Sidoni.

9 Kwa sababu ya umati mkubwa wa watu, aliwaambia wanafunzi wake waweke tayari mashua ndogo kwa ajili yake, ili kuwazuia watu kumsonga.

10 Kwa kuwa alikuwa amewaponya wagonjwa wengi, wale wenye magonjwa walikuwa wanasukumana ili wapate kumgusa.

11 Kila mara pepo wachafu walipomwona, walianguka chini mbele yake na kupiga kelele wakisema, “Wewe ndiwe Mwana wa Mungu.”

12 Lakini aliwaonya wasimseme yeye ni nani.

Yesu Achagua Mitume Kumi Na Wawili

13 Yesu akapanda mlimani na kuwaita wale aliowataka, nao wakamjia.

14 Akawachagua kumi na wawili, ambao aliwaita mitume, ili wapate kuwa pamoja naye, na awatume kwenda kuhubiri

15 na kuwa na mamlaka ya kutoa pepo wachafu.

16 Hawa ndio wale kumi na wawili aliowachagua: Simoni (ambaye alimwita Petro);

17 Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohana nduguye (ambao aliwaita Boanerge, maana yake Wana wa Ngurumo);

18 Andrea, Filipo, Bartholomayo, Mathayo, Tomaso, Yakobo mwana wa Alfayo, Thadayo, Simoni Mkananayo,

19 na Yuda Iskariote aliyemsaliti Yesu.

Yesu Na Beelzebuli

20 Kisha Yesu aliporudi nyumbani, umati wa watu ukakusanyika tena, kiasi kwamba yeye na wanafunzi wake hawakuweza kula chakula.

21 Ndugu zake walipopata habari wakaja ili kumchukua kwa maana watu walikuwa wakisema, “Amerukwa na akili.”

22 Walimu wa sheria walioteremka kutoka Yerusalemu walisema, “Amepagawa na Beelzebuli!Anatoa pepo wachafu kwa kutumia mkuu wa pepo wachafu!”

23 Basi Yesu akawaita na kuzungumza nao kwa mifano akasema: “Shetani awezaje kumtoa Shetani?

24 Kama ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe, ufalme huo hauwezi kusimama.

25 Nayo nyumba kama ikigawanyika dhidi yake yenyewe, nyumba hiyo haiwezi kusimama.

26 Naye Shetani kama akijipinga mwenyewe na awe amegawanyika, hawezi kusimama bali mwisho wake umewadia.

27 Hakuna mtu yeyote awezaye kuingia kwenye nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka nyara mali zake asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu. Ndipo ataweza kuteka nyara mali zake.

28 Amin, nawaambia, dhambi zote na makufuru yote ya wanadamu watasamehewa.

29 Lakini yeyote anayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa kamwe, atakuwa na hatia ya dhambi ya milele.”

30 Yesu alisema hivi kwa sababu walikuwa wanasema, “Ana pepo mchafu.”

Mama Na Ndugu Zake Yesu

31 Kisha wakaja ndugu zake Yesu pamoja na mama yake. Wakasimama nje, wakamtuma mtu kumwita.

32 Umati wa watu ulikuwa umeketi kumzunguka, nao wakamwambia, “Mama yako na ndugu zako wako nje, wanakutafuta.”

33 Akawauliza, “Mama yangu na ndugu zangu ni nani?”

34 Kisha akawatazama wale watu waliokuwa wameketi kumzunguka pande zote, akasema, “Hawa ndio mama yangu na ndugu zangu.

35 Mtu yeyote anayetenda mapenzi ya Mungu, huyo ndiye ndugu yangu, na dada yangu na mama yangu.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/MRK/3-69d5e075b3d87913941228fcda2cdb33.mp3?version_id=1627—

Categories
Marko

Marko 4

Mfano Wa Mpanzi

1 Yesu akaanza kufundisha tena kando ya bahari. Umati wa watu uliokuwa umekusanyika kumzunguka ulikuwa mkubwa, kiasi kwamba ilimbidi Yesu aingie kwenye mashua iliyokuwa baharini na kuketi humo, nao watu wote walikuwa ufuoni mwa bahari.

2 Akawafundisha mambo mengi kwa mifano, naye katika mafundisho yake akasema:

3 “Sikilizeni! Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake.

4 Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia, nao ndege wakaja na kuzila.

5 Nyingine zilianguka kwenye ardhi yenye mwamba isiyo na udongo wa kutosha. Zikaota haraka, kwa kuwa udongo ulikuwa haba.

6 Lakini jua lilipozidi, mimea ikanyauka na kukauka kwa kuwa mizizi yake haikuwa na kina.

7 Mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo miiba hiyo ikakua, ikaisonga hiyo mimea, hivyo haikutoa mazao.

8 Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri, zikaota vizuri na kukua, zikatoa mazao, moja mara thelathini, nyingine mara sitini, na nyingine mara mia moja.”

9 Kisha Yesu akasema, “Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”

Sababu Za Mifano

10 Alipokuwa peke yake, watu waliokuwepo naye pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili wakamuuliza kuhusu mifano yake.

11 Naye akawaambia, “Ninyi mmepewa kujua siri ya Ufalme wa Mungu. Lakini kwa wale walioko nje, kila kitu husemwa kwao kwa mifano,

12 ili,

“ ‘daima waone lakini wasitambue,

daima wasikie lakini wasielewe;

wasije wakageuka, wakatubu na kusamehewa!’ ”

Yesu Afafanua Maana Ya Mfano Wa Mbegu

13 Kisha Yesu akawauliza, “Hamwelewi maana ya mfano huu? Basi mtaelewaje mifano mingine?

14 Yule mpanzi hupanda neno.

15 Hawa ndio wale walio kando ya njia ambako neno lilipandwa. Walisikiapo neno, Shetani huja mara na kulinyakua lile neno lililopandwa ndani yao.

16 Nazo zile mbegu zilizoanguka kwenye udongo wenye miamba, ni wale wanaolisikia neno, na mara hulipokea kwa furaha.

17 Lakini kwa kuwa hawana mizizi, wao hudumu kwa muda mfupi tu. Kisha dhiki au mateso yanapoinuka kwa ajili ya lile neno, mara wao huiacha imani.

18 Lakini wengine, kama mbegu iliyopandwa kwenye miiba, hulisikia lile neno;

19 lakini masumbufu ya maisha haya, na udanganyifu wa mali na tamaa ya mambo mengine huja na kulisonga lile neno na kulifanya lisizae.

20 Wengine, kama mbegu iliyopandwa kwenye udongo mzuri, hulisikia lile neno, wakalipokea na kuzaa mazao. Wao huzaa mara thelathini, au mara sitini, au mara mia ya mbegu iliyopandwa.”

Mfano Wa Taa

21 Akawaambia, “Je, taa huwashwa na kufunikwa chini ya kikapu au mvunguni mwa kitanda? Je, haiwashwi na kuwekwa juu ya kinara chake?

22 Kwa kuwa hakuna kilichofichika ambacho hakitafunuliwa, wala hakuna jambo lolote la siri ambalo halitaletwa nuruni.

23 Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”

24 Naye akawaambia, “Kuweni waangalifu na yale mnayosikia. Kipimo kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa ninyi, hata na zaidi.

25 Kwa maana kila mtu aliye na kitu atapewa zaidi, naye atakuwa navyo tele. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyangʼanywa.”

Mfano Wa Mbegu Inayoota

26 Pia akawaambia, “Ufalme wa Mungu unafanana na mtu apandaye mbegu shambani.

27 Akiisha kuzipanda, usiku na mchana, akiwa amelala au ameamka, mbegu huota na kukua pasipo yeye kujua ikuavyo.

28 Udongo huifanya iote kuwa mche, halafu suke, kisha nafaka kamili kwenye suke.

29 Lakini nafaka inapokuwa imekomaa, mara mkulima huingia shambani na mundu wa kuvunia, maana mavuno yamekuwa tayari.”

Mfano Wa Mbegu Ya Haradali

30 Akawaambia tena, “Tuufananishe Ufalme wa Mungu na nini? Au tutumie mfano gani ili kuueleza?

31 Ni kama punje ya haradali, ambayo ni mbegu ndogo sana kuliko mbegu zote zinazopandwa ardhini.

32 Lakini ikishaota, hukua ikawa mmea mkubwa kuliko yote ya bustanini, ikawa na matawi makubwa hata ndege wa angani wanaweza kujenga viota kwenye matawi yake.”

33 Kwa mifano mingine mingi kama hii Yesu alinena nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulielewa.

34 Hakusema nao neno lolote pasipo mfano. Lakini alipokuwa na wanafunzi wake, aliwafafanulia kila kitu.

Yesu Atuliza Dhoruba

35 Siku hiyo ilipokaribia jioni, aliwaambia wanafunzi wake, “Tuvukeni twende mpaka ngʼambo.”

36 Wakauacha ule umati wa watu, na wakamchukua vile alivyokuwa kwenye mashua. Palikuwa pia na mashua nyingine nyingi pamoja naye.

37 Kukawa na dhoruba kali, nayo mawimbi yakaipiga ile mashua hata ikawa karibu kujaa maji.

38 Yesu alikuwa katika shetri, akiwa analala juu ya mto. Wanafunzi wake wakamwamsha, wakamwambia, “Mwalimu, hujali kama tunazama?”

39 Akaamka, akaukemea ule upepo, akayaambia yale mawimbi, “Uwe kimya! Tulia!” Ule upepo ukatulia, kukawa shwari kabisa.

40 Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kwa nini mnaogopa hivyo? Je, bado hamna imani?”

41 Nao wakawa wameogopa sana, wakaulizana, “Ni nani huyu ambaye hata upepo na mawimbi vinamtii?”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/MRK/4-74f4defb3384b67a4beb90520b4a556b.mp3?version_id=1627—

Categories
Marko

Marko 5

Yesu Amponya Mtu Mwenye Pepo

1 Wakafika upande wa pili wa ziwa wakaingia katika nchi ya Wagerasi.

2 Yesu alipotoka kwenye mashua, mara mtu mmoja mwenye pepo mchafu akatoka makaburini akakutana naye.

3 Mtu huyu aliishi makaburini, wala hakuna aliyeweza kumzuia hata kwa kumfunga minyororo.

4 Kwa kuwa mara kwa mara alikuwa amefungwa minyororo mikononi na miguuni, lakini akaikata hiyo minyororo na kuzivunja zile pingu miguuni mwake. Hapakuwa na mtu yeyote aliyekuwa na nguvu za kumzuia.

5 Usiku na mchana alikuwa makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikatakata kwa mawe.

6 Alipomwona Yesu kwa mbali, alimkimbilia, akapiga magoti mbele yake.

7 Akapiga kelele kwa nguvu akisema, “Una nini nami, Yesu, Mwana wa Mungu Aliye Juu Sana? Ninakusihi kwa jina la Mungu, usinitese!”

8 Kwa kuwa Yesu alikuwa amemwambia, “Mtoke mtu huyu, wewe pepo mchafu!”

9 Yesu akamuuliza, “Jina lako ni nani?”

Akamjibu, “Jina langu ni Legioni,kwa kuwa tuko wengi.”

10 Akamsihi Yesu sana asiwapeleke nje ya nchi ile.

11 Palikuwa na kundi kubwa la nguruwe lililokuwa likilisha karibu kando ya kilima.

12 Wale pepo wachafu wakamsihi Yesu wakisema, “Tuamuru twende kwenye wale nguruwe. Turuhusu tuwaingie.”

13 Basi Yesu akawaruhusu, nao wale pepo wachafu wakatoka, wakawaingia hao nguruwe. Lile kundi lilikuwa na nguruwe wapatao 2,000, nao wote wakateremkia gengeni kwa kasi, nao wakatumbukia ziwani na kuzama.

14 Wale watu waliokuwa wakichunga hao nguruwe wakakimbilia mjini na vijijini kueleza yaliyotukia. Watu wakatoka kwenda kuona hayo yaliyokuwa yametukia.

15 Walipofika kwa Yesu, wakamwona yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu legioni akiwa ameketi hapo, amevaa nguo na mwenye akili timamu. Wakaogopa.

16 Wale walioyaona mambo hayo wakawaeleza watu wengine yaliyomtokea yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu, na habari za lile kundi la nguruwe pia.

17 Basi watu wakaanza kumwomba Yesu aondoke katika nchi yao.

18 Yesu alipokuwa anaingia kwenye mashua, yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu akamsihi Yesu waende pamoja.

19 Yesu hakumruhusu, bali alimwambia, “Nenda nyumbani kwa jamaa yako ukawaeleze mambo makuu aliyokutendea Bwana, na jinsi alivyokuhurumia.”

20 Yule mtu akaenda zake, akaanza kutangaza katika Dekapoli mambo makuu Yesu aliyomtendea. Nao watu wote wakastaajabu.

Mwanamke Aponywa

21 Yesu alipokwisha kuvuka tena na kufika ngʼambo, umati mkubwa wa watu ukamzunguka yeye akiwa hapo kando ya bahari.

22 Kisha mmoja wa viongozi wa sinagogi aliyeitwa Yairo akafika pale. Naye alipomwona Yesu, akapiga magoti miguuni pake,

23 akamsihi akisema, “Binti yangu mdogo ni mgonjwa mahututi. Tafadhali nakusihi, njoo uweke mikono yako juu yake ili apate kupona, naye atakuwa hai.”

24 Hivyo Yesu akaenda pamoja naye.

Umati mkubwa wa watu ukamfuata, nao watu wakawa wanamsonga.

25 Hapo palikuwa na mwanamke aliyekuwa amesumbuliwa na tatizo la kutokwa damu kwa miaka kumi na miwili.

26 Mwanamke huyu alikuwa ameteseka sana kwa mikono ya matabibu wengi, na kutumia kila kitu alichokuwa nacho. Lakini badala ya kupona, hali yake ilizidi kuwa mbaya.

27 Alikuwa amesikia habari za Yesu, naye akaja kwa nyuma yake kwenye umati wa watu, akaligusa vazi lake,

28 kwa maana alisema moyoni mwake, “Kama nikiweza kuligusa vazi lake tu, nitaponywa.”

29 Mara kutoka damu kwake kukakoma, naye akajisikia mwilini mwake amepona kabisa.

30 Ghafula Yesu akatambua kuwa nguvu zimemtoka. Akaugeukia ule umati wa watu na kuuliza, “Ni nani aliyegusa mavazi yangu?”

31 Wanafunzi wake wakamjibu, “Unaona jinsi umati wa watu unavyokusonga. Wawezaje kuuliza, ‘Ni nani aliyenigusa?’ ”

32 Lakini Yesu akaangalia pande zote ili aone ni nani aliyemgusa.

33 Yule mwanamke, akijua kilichomtokea, akaja, akaanguka miguuni pake akitetemeka kwa hofu, akamweleza ukweli wote.

34 Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako.”

Yesu Amfufua Binti Yairo

35 Alipokuwa bado anaongea, watu wakafika kutoka nyumbani kwa Yairo. Wakamwambia, “Binti yako amekufa. Kwa nini kuendelea kumsumbua Mwalimu?”

36 Aliposikia hayo waliyosema, Yesu akamwambia huyo kiongozi wa sinagogi, “Usiogope. Amini tu.”

37 Hakumruhusu mtu mwingine yeyote amfuate isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana, nduguye Yakobo.

38 Walipofika nyumbani kwa yule kiongozi wa sinagogi, Yesu akaona ghasia, watu wakilia na kuomboleza kwa sauti kubwa.

39 Alipokwisha kuingia ndani, akawaambia, “Kwa nini mnafanya ghasia na kulia? Mtoto hajafa, bali amelala tu.”

40 Wale watu wakamcheka kwa dharau.

Lakini yeye akawatoa wote nje, akawachukua baba na mama wa yule mtoto, pamoja na wale wanafunzi aliokuwa nao. Wakaingia ndani mpaka pale alipokuwa yule mtoto.

41 Akamshika mtoto mkono, akamwambia, “Talitha koum!”(maana yake ni, “Msichana, nakuambia: amka!”)

42 Mara yule msichana akasimama, akaanza kutembea (alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili). Walipoona haya, wakastaajabu sana.

43 Yesu akawaagiza kwa ukali wasimweleze mtu yeyote jambo hilo, naye akawaambia wampe yule msichana chakula.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/MRK/5-d7305734c75087550fefe4722ed44c12.mp3?version_id=1627—

Categories
Marko

Marko 6

Nabii Hana Heshima Kwao

1 Yesu akaondoka huko na kwenda mji wa kwao, akiwa amefuatana na wanafunzi wake.

2 Ilipofika siku ya Sabato, akaanza kufundisha katika sinagogi, na wengi waliomsikia wakashangaa.

Nao wakauliza, “Mtu huyu ameyapata wapi mambo haya yote? Tazama ni hekima ya namna gani hii aliyopewa? Tazama matendo ya miujiza ayafanyayo kwa mikono yake!

3 Huyu si yule seremala, mwana wa Maria? Na ndugu zake si Yakobo, Yose,Yuda na Simoni? Dada zake wote si tuko nao hapa kwetu?” Nao wakachukizwa sana kwa ajili yake, wakakataa kumwamini.

4 Yesu akawaambia, “Nabii hakosi heshima isipokuwa katika mji wake mwenyewe, na miongoni mwa jamaa na ndugu zake, na nyumbani kwake.”

5 Hakufanya miujiza yoyote huko isipokuwa kuweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache na kuwaponya.

6 Naye akashangazwa sana kwa jinsi wasivyokuwa na imani.

Yesu Awatuma Wale Kumi Na Wawili

Kisha Yesu akawa anakwenda kutoka kijiji kimoja hadi kingine akifundisha.

7 Akawaita wale kumi na wawili, akawatuma wawili wawili, na kuwapa mamlaka kutoa pepo wachafu.

8 Akawaagiza akisema, “Msichukue chochote kwa ajili ya safari isipokuwa fimbo tu. Msichukue mkate, wala mkoba, wala fedha kwenye mikanda yenu.

9 Vaeni viatu, lakini msivae nguo ya ziada.”

10 Akawaambia, “Mkiingia kwenye nyumba yoyote, kaeni humo hadi mtakapoondoka katika mji huo.

11 Kama mahali popote hawatawakaribisha wala kuwasikiliza, mtakapoondoka huko, kungʼuteni mavumbi kutoka kwenye miguu yenu ili kuwa ushuhuda dhidi yao.”

12 Kwa hiyo wakatoka na kuhubiri kwamba inawapasa watu kutubu na kuacha dhambi.

13 Wakatoa pepo wachafu wengi, wakawapaka wagonjwa wengi mafuta na kuwaponya.

Yohana Mbatizaji Akatwa Kichwa

14 Mfalme Herode akasikia habari hizi, kwa maana jina la Yesu lilikuwa limejulikana sana. Watu wengine walikuwa wakisema, “Yohana Mbatizaji amefufuliwa kutoka kwa wafu, ndiyo sababu nguvu za kutenda miujiza zinafanya kazi ndani yake.”

15 Wengine wakasema, “Yeye ni Eliya.”

Nao wengine wakasema, “Yeye ni nabii, kama mmojawapo wa wale manabii wa zamani.”

16 Lakini Herode aliposikia habari hizi, akasema, “Huyo ni Yohana Mbatizaji, niliyemkata kichwa, amefufuliwa kutoka kwa wafu!”

17 Kwa kuwa Herode alikuwa ameagiza kwamba Yohana Mbatizaji akamatwe, afungwe na kutiwa gerezani. Alifanya hivi kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake, ambaye Herode alikuwa amemwoa.

18 Yohana alikuwa amemwambia Herode, “Si halali kwako kuwa na mke wa ndugu yako.”

19 Kwa hiyo Herodia alikuwa amemwekea Yohana kinyongo akataka kumuua. Lakini hakuweza,

20 kwa sababu Herode alimwogopa Yohana akijua kwamba ni mtu mwenye haki na mtakatifu, hivyo akamlinda. Herode alifadhaika sana alipomsikia Yohana, lakini bado alipenda kumsikiliza.

21 Mfalme Herode alifanya karamu kubwa wakati wa sikukuu ya kuzaliwa kwake. Akawaalika maafisa wake wakuu, majemadari wa jeshi na watu mashuhuri wa Galilaya. Hatimaye Herodia alipata wasaa aliokuwa akiutafuta.

22 Binti yake Herodia alipoingia na kucheza, akamfurahisha Herode pamoja na wageni wake walioalikwa chakulani.

Mfalme Herode akamwambia yule binti, “Niombe kitu chochote utakacho, nami nitakupa.”

23 Tena akamwahidi kwa kiapo, akamwambia, “Chochote utakachoomba nitakupa, hata kama ni nusu ya ufalme wangu.”

24 Yule binti akatoka nje, akaenda kumuuliza mama yake, “Niombe nini?”

Mama yake akamjibu, “Omba kichwa cha Yohana Mbatizaji.”

25 Yule binti akarudi haraka kwa mfalme, akamwambia, “Nataka unipe sasa hivi kichwa cha Yohana Mbatizaji kwenye sinia.”

26 Mfalme akasikitika sana, lakini kwa sababu alikuwa ameapa viapo mbele ya wageni wake, hakutaka kumkatalia.

27 Mara mfalme akatuma askari mmojawapo wa walinzi wake kukileta kichwa cha Yohana. Akaenda na kumkata Yohana kichwa humo gerezani,

28 akakileta kichwa chake kwenye sinia na kumpa yule msichana, naye yule msichana akampa mama yake.

29 Wanafunzi wa Yohana walipopata habari hizi, wakaja na kuuchukua mwili wake, wakauzika kaburini.

Yesu Awalisha Wanaume 5,000

30 Wale mitume wakakusanyika kwa Yesu na kumpa taarifa ya mambo yote waliyokuwa wamefanya na kufundisha.

31 Basi kwa kuwa watu wengi mno walikuwa wakija na kutoka, hata wakawa hawana nafasi ya kula, Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Twendeni peke yetu mahali pa faragha, mpate kupumzika.”

32 Hivyo wakaondoka kwa mashua peke yao, wakaenda mahali pasipo na watu.

33 Lakini watu wengi waliowaona wakiondoka, wakawatambua, nao wakaenda haraka kwa miguu kutoka miji yote, nao wakatangulia kufika.

34 Yesu alipofika kando ya bahari, aliona makutano makubwa ya watu, akawahurumia kwa maana walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. Kwa hiyo akaanza kuwafundisha mambo mengi.

35 Mchana ulipokuwa umeendelea sana, wanafunzi wake walienda kwake, wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, nazo saa zimekwenda sana.

36 Waage watu ili waende mashambani na vijijini jirani, wakajinunulie chakula.”

37 Lakini Yesu akawajibu, “Ninyi wapeni chakula.”

Wakamwambia, “Je, twende tukanunue mikate ya dinari 200ili tuwape watu hawa wale?”

38 Akawauliza, “Kuna mikate mingapi? Nendeni mkaangalie.”

Walipokwisha kujua wakarudi, wakamwambia, “Kuna mikate mitano na samaki wawili.”

39 Kisha Yesu akawaamuru wawaketishe watu makundi makundi kwenye majani,

40 nao wakaketi kwenye makundi ya watu mia mia na wengine hamsini hamsini.

41 Yesu akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akainua macho yake akatazama mbinguni, akavibariki na kuimega ile mikate. Kisha akawapa wanafunzi wake ili wawagawie wale watu wote. Pia akawagawia wote wale samaki wawili.

42 Watu wote wakala, wakashiba.

43 Nao wanafunzi wake wakakusanya vipande vilivyosalia vya mikate na samaki, wakajaza vikapu kumi na viwili.

44 Idadi ya wanaume waliokula walikuwa 5,000.

Yesu Atembea Juu Ya Maji

45 Mara Yesu akawaambia wanafunzi wake waingie kwenye mashua watangulie kwenda Bethsaida, wakati yeye alikuwa akiwaaga wale makutano.

46 Baada ya kuwaaga wale watu, akaenda mlimani kuomba.

47 Ilipofika jioni, ile mashua ilikuwa imefika katikati ya bahari, na Yesu alikuwa peke yake katika nchi kavu.

48 Akawaona wanafunzi wake wanahangaika na kupiga makasia kwa nguvu, kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho. Wakati wa zamu ya nne ya usiku, Yesu akawaendea wanafunzi wake, akiwa anatembea juu ya maji. Alikuwa karibu kuwapita,

49 lakini walipomwona akitembea juu ya maji, wakadhani ni mzimu. Wakapiga yowe,

50 kwa sababu wote walipomwona waliogopa.

Mara Yesu akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Msiogope!”

51 Akapanda ndani ya mashua nao, na ule upepo ukakoma! Wakashangaa kabisa,

52 kwa kuwa walikuwa hawajaelewa kuhusu ile mikate. Mioyo yao ilikuwa migumu.

53 Walipokwisha kuvuka, wakafika nchi ya Genesareti, wakatia nanga.

54 Mara waliposhuka kutoka mashua yao, watu wakamtambua Yesu.

55 Wakaenda katika vijiji vyote upesi, wakawabeba wagonjwa kwenye mikeka ili kuwapeleka mahali popote waliposikia kuwa Yesu yupo.

56 Kila mahali Yesu alipokwenda, iwe vijijini, mijini au mashambani, watu waliwaweka wagonjwa wao masokoni. Wakamwomba awaruhusu hao wagonjwa waguse japo upindo wa vazi lake. Nao wote waliomgusa waliponywa.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/MRK/6-6c9770ed2bdb5cff6a5f180b2ee16308.mp3?version_id=1627—

Categories
Marko

Marko 7

Kilicho Safi Na Kilicho Najisi

1 Mafarisayo na baadhi ya walimu wa sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu wakakusanyika mbele ya Yesu.

2 Wakawaona baadhi ya wanafunzi wake wakila chakula kwa mikono iliyo najisi, yaani, bila kunawa kama ilivyotakiwa na sheria ya dini ya Wayahudi.

3 Kwa kuwa Mafarisayo na Wayahudi wote hawali chakula pasipo kunawa kwa kufuata desturi za wazee wao.

4 Wanapotoka sokoni hawawezi kula pasipo kunawa. Pia kuna desturi nyingine nyingi wanazofuata kama vile jinsi ya kuosha vikombe, vyungu na vyombo vya shaba.

5 Kwa hiyo wale Mafarisayo na walimu wa sheria wakamuuliza Yesu, “Mbona wanafunzi wako hawafuati desturi za wazee, na badala yake wanakula kwa mikono najisi?”

6 Yesu akawajibu, “Nabii Isaya alisema ukweli alipotabiri juu yenu, ninyi wanafiki. Kama ilivyoandikwa:

“ ‘Watu hawa huniheshimu kwa midomo yao,

lakini mioyo yao iko mbali nami.

7 Huniabudu bure,

nayo mafundisho yao ni maagizo ya wanadamu tu.’

8 Ninyi mmeziacha amri za Mungu na kushika desturi za watu.”

9 Naye akawaambia, “Ninyi mnayo njia nzuri ya kukataa amri za Mungu ili mpate kuyashika mapokeo yenu!

10 Kwa mfano, Mose alisema, ‘Waheshimu baba yako na mama yako,’ na, ‘Yeyote amtukanaye baba yake au mama yake, na auawe.’

11 Lakini ninyi mwafundisha kwamba mtu akimwambia baba yake au mama yake, ‘Kile ambacho ningeweza kukusaidia ni Korbani’ (yaani kimewekwa wakfu kwa Mungu),

12 basi hawajibiki tena kumsaidia baba yake au mama yake.

13 Kwa njia hiyo ninyi mnabatilisha neno la Mungu kwa mapokeo yenu mliyojiwekea. Nanyi mnafanya mambo mengi ya aina hiyo.”

14 Yesu akaita tena ule umati wa watu, akawaambia, “Nisikilizeni, kila mmoja wenu na mwelewe jambo hili.

15 Hakuna kitu kinachomwingia mtu kimtiacho unajisi, lakini kile kimtokacho ndicho kimtiacho unajisi. [

16 Kama mtu yeyote ana masikio ya kusikia na asikie.]”

17 Akiisha kuuacha ule umati wa watu na kuingia ndani, wanafunzi wake wakamuuliza maana ya mfano ule.

18 Akawajibu, “Je, hata nanyi hamwelewi? Je, hamfahamu kwamba kitu kimwingiacho mtu hakimtii unajisi?

19 Mtu akila kitu hakiingii moyoni mwake bali tumboni, na baadaye hutolewa nje ya mwili wake.” (Kwa kusema hivi, Yesu alivihalalisha vyakula vyote kuwa ni “safi.”)

20 Akaendelea kusema, “Kile kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi.

21 Kwa maana kutoka ndani ya moyo wa mtu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, uzinzi,

22 tamaa mbaya, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, matukano, kiburi na upumbavu.

23 Maovu haya yote hutoka ndani ya mtu, nayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi.”

Imani Ya Mwanamke Msirofoinike

24 Ndipo Yesu akaondoka hapo akaenda sehemu za Tiro. Akaingia katika nyumba moja, naye hakutaka mtu yeyote ajue kwamba yuko humo. Lakini hakuweza kujificha.

25 Mara mwanamke mmoja, ambaye binti yake mdogo alikuwa na pepo mchafu, akaja na kumpigia magoti miguuni pake.

26 Basi huyo mwanamke alikuwa Myunani, aliyezaliwa Foinike ya Siria.Akamsihi Yesu amtoe binti yake huyo pepo mchafu.

27 Yesu akamwambia, “Waache watoto washibe kwanza, kwa maana si vyema kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.”

28 Lakini yule mwanamke akamjibu, “Bwana, hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya chakula cha watoto.”

29 Ndipo Yesu akamjibu, “Kwa sababu ya jibu lako, nenda zako nyumbani; yule pepo mchafu amemtoka binti yako.”

30 Akaenda zake nyumbani akamkuta binti yake amelala kitandani, yule pepo mchafu akiwa amemtoka.

Yesu Amponya Mtu Aliyekuwa Kiziwi Na Bubu

31 Kisha Yesu akaondoka sehemu za Tiro, akapita katikati ya Sidoni, hadi Bahari ya Galilaya na kuingia eneo la Dekapoli.

32 Huko, watu wakamletea Yesu mtu mmoja kiziwi, ambaye pia alikuwa na kigugumizi, wakamwomba aweke mkono wake juu ya huyo mtu na amponye.

33 Baadaye Yesu akampeleka yule kiziwi kando mbali na watu, Yesu akatia vidole vyake masikioni mwa yule mtu. Kisha akatema mate na kuugusa ulimi wa yule mtu.

34 Ndipo Yesu akatazama mbinguni, akavuta hewa ndani kwa nguvu akamwambia, “Efatha!” Yaani, “Funguka!”

35 Mara masikio yake yakafunguka na ulimi wake ukaachiliwa, akaanza kuongea sawasawa.

36 Yesu akawaamuru wasimwambie mtu yeyote habari hizi. Lakini kadiri alivyowazuia, ndivyo walivyozidi kutangaza kwa bidii.

37 Walistaajabu mno. Wakasema, “Amefanya mambo yote vizuri mno! Amewawezesha viziwi wasikie na bubu waseme!”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/MRK/7-1d73435573c4112f154ccd8e010579c0.mp3?version_id=1627—

Categories
Marko

Marko 8

Yesu Alisha Wanaume 4,000

1 Katika siku hizo, umati mkubwa wa watu ulikusanyika tena. Kwa kuwa walikuwa hawana chakula, Yesu akawaita wanafunzi wake akawaambia,

2 “Ninauhurumia huu umati wa watu, kwa sababu sasa wamekuwa nami kwa muda wa siku tatu na hawana chakula.

3 Nikiwaaga waende nyumbani bila kula, watazimia njiani kwa sababu baadhi yao wametoka mbali.”

4 Wanafunzi wake wakamjibu, “Lakini hapa nyikani tutapata wapi mikate ya kutosha kuwalisha?”

5 Yesu akawauliza, “Mna mikate mingapi?”

Wakajibu, “Tuna mikate saba.”

6 Akawaambia watu waketi chini. Akiisha kuichukua mikate saba na kushukuru, akaimega na kuwapa wanafunzi wake ili wawagawie watu. Wanafunzi wake wakafanya hivyo.

7 Walikuwa pia na visamaki vichache, Yesu akavibariki, akawaamuru wanafunzi wake wawagawie watu.

8 Wale watu walikula na kutosheka. Baadaye wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu saba.

9 Watu waliokula walikuwa wapata 4,000. Akiisha kuwaaga,

10 aliingia kwenye mashua pamoja na wanafunzi wake, akaenda sehemu za Dalmanutha.

Mafarisayo Waomba Ishara

11 Mafarisayo wakaja, wakaanza kumhoji Yesu. Ili kumtega, wakamwomba awaonyeshe ishara kutoka mbinguni.

12 Akahuzunika moyoni, akawaambia, “Kwa nini kizazi hiki kinataka ishara? Amin nawaambieni, hakitapewa ishara yoyote.”

13 Kisha akawaacha, akarudi kwenye mashua, akavuka hadi ngʼambo.

Chachu Ya Mafarisayo Na Ya Herode

14 Wanafunzi walikuwa wamesahau kuchukua mikate ya kutosha. Walikuwa na mkate mmoja tu kwenye mashua.

15 Yesu akawaonya: “Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na ya Herode.”

16 Wakajadiliana wao kwa wao, na kusema, “Anasema hivi kwa sababu hatukuleta mikate.”

17 Yesu, akifahamu majadiliano yao, akawauliza: “Mbona mnajadiliana kuhusu kutokuwa na mikate? Je, bado hamtambui wala hamwelewi? Je, mbona mioyo yenu ni migumu kiasi hicho?

18 Je, mna macho lakini mnashindwa kuona, na mna masikio lakini mnashindwa kusikia? Je, hamkumbuki?

19 Nilipoimega ile mikate mitano kuwalisha watu 5,000, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa vya masazo?”

Wakamjibu, “Kumi na viwili.”

20 “Je, nilipoimega ile mikate saba kuwalisha watu 4,000, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa vya masazo?”

Wakamjibu, “Saba.”

21 Ndipo akawauliza, “Je, bado hamwelewi?”

Yesu Amponya Kipofu Huko Bethsaida

22 Wakafika Bethsaida na baadhi ya watu wakamleta mtu mmoja kipofu wakamsihi Yesu amguse.

23 Yesu akamshika mkono huyo kipofu akampeleka nje ya kijiji. Baada ya kuyatemea mate macho ya yule kipofu na kumwekea mikono, Yesu akamuuliza, “Unaona chochote?”

24 Yule kipofu akaangalia, akasema, “Ninaona watu, wanaonekana kama miti inayotembea.”

25 Yesu akamwekea tena mikono machoni. Kisha macho yake yakafunguka, kuona kwake kukarejea naye akaona kila kitu dhahiri.

26 Yesu akamuaga aende nyumbani kwake, akimwambia, “Hata kijijini usiingie.”

Petro Amkiri Yesu Kuwa Ndiye Kristo

27 Yesu na wanafunzi wake wakaondoka kwenda katika vijiji vya Kaisaria-Filipi. Walipokuwa njiani, Yesu akawauliza, “Watu husema mimi ni nani?”

28 Wakamjibu, “Baadhi husema wewe ni Yohana Mbatizaji, wengine husema ni Eliya, na bado wengine husema wewe ni mmojawapo wa manabii.”

29 Akawauliza, “Je, ninyi mnasema mimi ni nani?”

Petro akajibu, “Wewe ndiwe Kristo.”

30 Yesu akawaonya wasimwambie mtu yeyote habari zake.

Yesu Atabiri Kifo Chake

31 Ndipo akaanza kuwafundisha wanafunzi wake kuwa Mwana wa Adamu lazima atapata mateso mengi na kukataliwa na wazee, viongozi wa makuhani, na walimu wa sheria, na kwamba itampasa auawe lakini baada ya siku tatu afufuke.

32 Aliyasema haya waziwazi, ndipo Petro akamchukua kando na akaanza kumkemea.

33 Lakini Yesu alipogeuka na kuwaangalia wanafunzi wake, akamkemea Petro. Akasema, “Rudi nyuma yangu, Shetani! Moyo wako hauwazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”

34 Ndipo akauita ule umati wa watu pamoja na wanafunzi wake, akasema, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate.

35 Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili atayaokoa.

36 Je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake?

37 Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?

38 Mtu yeyote akinionea aibu mimi na maneno yangu katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu naye atamwonea aibu wakati atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/MRK/8-7ce75f79a9969e587597c7701faaa16c.mp3?version_id=1627—

Categories
Marko

Marko 9

1 Yesu akaendelea kuwaambia, “Amin, nawaambia, kuna watu waliosimama hapa ambao hawataonja mauti kabla ya kuuona Ufalme wa Mungu ukija kwa nguvu.”

Yesu Ageuka Sura

2 Baada ya siku sita, Yesu akawachukua Petro, Yakobo na Yohana, akawapeleka juu ya mlima mrefu, mahali walipokuwa faraghani. Huko, Yesu akageuka sura mbele yao.

3 Mavazi yake yakawa na weupe wa kuzima macho, meupe kuliko ambavyo mtu yeyote duniani angaliweza kuyangʼarisha.

4 Mose na Eliya wakawatokea, wakawa wanazungumza na Yesu.

5 Petro akamwambia Yesu, “Rabi, ni vyema sisi tukae hapa. Turuhusu tujenge vibanda vitatu: kimoja chako, kingine cha Mose na kingine cha Eliya.”

6 Petro hakujua aseme nini kwa maana yeye na wenzake walikuwa wameogopa sana.

7 Ndipo pakatokea wingu, likawafunika, nayo sauti kutoka lile wingu ikasema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa. Msikieni yeye.”

8 Mara walipotazama huku na huku, hawakuona tena mtu mwingine yeyote pamoja nao isipokuwa Yesu.

9 Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, Yesu akawakataza wasimwambie mtu yeyote mambo waliyoona, mpaka Mwana wa Adamu atakapokuwa amefufuka kutoka kwa wafu.

10 Wakalihifadhi jambo hilo wao wenyewe, lakini wakawa wanajiuliza, “Huku kufufuka kwa wafu maana yake nini?”

11 Wakamuuliza, “Kwa nini walimu wa sheria husema kwamba ni lazima Eliya aje kwanza?”

12 Yesu akawajibu, “Ni kweli, Eliya yuaja kwanza ili kutengeneza mambo yote. Mbona basi imeandikwa kwamba Mwana wa Adamu ni lazima ateseke sana na kudharauliwa?

13 Lakini ninawaambia, Eliya amekwisha kuja, nao wakamtendea walivyopenda, kama ilivyoandikwa kumhusu yeye.”

Mvulana Mwenye Pepo Mchafu Aponywa

14 Walipowafikia wale wanafunzi wengine, wakawakuta wamezungukwa na umati mkubwa wa watu na baadhi ya walimu wa sheria wakibishana nao.

15 Mara wale watu walipomwona Yesu, wakastaajabu sana, wakamkimbilia ili kumsalimu.

16 Akawauliza wanafunzi wake, “Mnabishana nao kuhusu nini?”

17 Mtu mmoja miongoni mwa ule umati wa watu akajibu, “Mwalimu, nilimleta kwako mwanangu ambaye ana pepo mchafu anayemfanya asiweze kuongea.

18 Kila mara huyo pepo mchafu ampagaapo mwanangu, humwangusha chini na kumfanya atokwe povu mdomoni na kusaga meno, kisha mwili wake hukauka. Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo mchafu, lakini hawakuweza.”

19 Yesu akawaambia, “Enyi kizazi kisicho na imani! Nitakuwa pamoja nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni mvulana kwangu.”

20 Nao wakamleta yule mvulana. Yule pepo mchafu alipomwona Yesu, mara akamtia yule mvulana kifafa, akaanguka, akagaagaa chini huku akitokwa na povu kinywani.

21 Yesu akamuuliza baba yake, “Mwanao amekuwa katika hali hii tangu lini?”

Akamjibu, “Tangu utoto wake.

22 Mara kwa mara huyo pepo mchafu amekuwa akimwangusha kwenye moto au kwenye maji ili kumwangamiza. Lakini kama unaweza kufanya jambo lolote, tafadhali tuhurumie utusaidie.”

23 Yesu akamwambia, “Kama ukiweza kuamini, yote yawezekana kwake yeye aaminiye.”

24 Mara baba yake yule mvulana akapiga kelele akisema, “Ninaamini. Nisaidie kutokuamini kwangu!”

25 Yesu alipoona kwamba umati wa watu unakusanyika pamoja mbio, akamkemea yule pepo mchafu, akimwambia, “Wewe pepo bubu na kiziwi, nakuamuru umtoke, wala usimwingie tena!”

26 Yule pepo mchafu akiisha kupiga kelele, akamtia kifafa kwa nguvu, na akamtoka. Yule mvulana alikuwa kama maiti, hivyo watu wengi wakasema, “Amekufa.”

27 Lakini Yesu akamshika mkono, akamwinua, naye akasimama.

28 Baada ya Yesu kuingia ndani ya nyumba, wanafunzi wake wakamuuliza wakiwa peke yao, “Mbona sisi hatukuweza kumtoa huyo pepo mchafu?”

29 Yesu akawajibu, “Hali hii haiwezi kutoka isipokuwa kwa kuomba na kufunga.”

Yesu Atabiri Tena Kifo Chake Na Ufufuo

30 Wakaondoka huko, wakapitia Galilaya. Yesu hakutaka mtu yeyote afahamu mahali walipo,

31 kwa maana alikuwa anawafundisha wanafunzi wake. Akawaambia, “Mwana wa Adamu atasalitiwa na kutiwa mikononi mwa watu. Nao watamuua, lakini siku tatu baada ya kuuawa atafufuka.”

32 Lakini wao hawakuelewa kile alimaanisha, nao waliogopa kumuuliza maana yake.

Mabishano Kuhusu Aliye Mkuu Zaidi

33 Basi wakafika Kapernaumu na baada ya kuingia nyumbani akawauliza, “Mlikuwa mnabishana nini kule njiani?”

34 Lakini hawakumjibu, kwa sababu njiani walikuwa wakibishana kuhusu nani miongoni mwao alikuwa mkuu zaidi ya wote.

35 Akaketi chini, akawaita wote kumi na wawili, akawaambia: “Kama mtu yeyote akitaka kuwa wa kwanza, hana budi kuwa wa mwisho na mtumishi wa wote.”

36 Kisha akamchukua mtoto mdogo, akamsimamisha katikati yao. Akamkumbatia, akawaambia,

37 “Mtu yeyote amkaribishaye mmoja wa hawa watoto wadogo kwa Jina langu, anikaribisha mimi. Naye anikaribishaye mimi, amkaribisha Baba yangu aliyenituma.”

Yeyote Asiye Kinyume Nasi Yuko Upande Wetu

38 Yohana akamwambia, “Mwalimu, tumemwona mtu akitoa pepo wachafu kwa jina lako, nasi tukamkataza, kwa sababu yeye si mmoja wetu.”

39 Yesu akasema, “Msimkataze, kwa kuwa hakuna yeyote atendaye miujiza kwa Jina langu ambaye baada ya kitambo kidogo aweza kunena lolote baya dhidi yangu.

40 Kwa maana yeyote asiye kinyume chetu, yuko upande wetu.

41 Amin, nawaambia, yeyote awapaye ninyi kikombe cha maji kwa Jina langu kwa sababu ninyi ni mali ya Kristo, hakika hataikosa thawabu yake.”

Kusababisha Kutenda Dhambi

42 “Kama mtu yeyote akimsababisha mmojawapo wa wadogo hawa wanaoniamini kutenda dhambi, ingekuwa bora kwake afungiwe jiwe kubwa la kusagia shingoni mwake, na kutoswa baharini.

43 Kama mkono wako ukikusababisha kutenda dhambi, ukate. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa na mkono mmoja, kuliko kuwa na mikono miwili lakini ukaingia jehanamu, mahali ambako moto hauzimiki. [

44 Mahali ambako funza wake hawafi wala moto wake hauzimiki.]

45 Kama mguu wako ukikusababisha kutenda dhambi, ukate. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa kiwete, kuliko kuwa na miguu miwili lakini ukaingia jehanamu. [

46 Mahali ambako funza wake hawafi wala moto hauzimiki.]

47 Nalo jicho lako likikusababisha kutenda dhambi, lingʼoe. Ni afadhali kwako kuingia katika Ufalme wa Mungu ukiwa na jicho moja, kuliko kuwa na macho mawili lakini ukatupwa jehanamu,

48 mahali ambako

“ ‘funza wake hawafi,

wala moto wake hauzimiki.’

49 Kila mmoja atatiwa chumvi kwa moto.

50 “Chumvi ni nzuri, lakini ikipoteza ladha yake utaifanyaje ili iweze kukolea tena? Mwe na chumvi ndani yenu, mkaishi kwa amani, kila mmoja na mwenzake.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/MRK/9-f009a19c2ad7844af1d3beb07da297a9.mp3?version_id=1627—