Categories
Luka

Luka 10

Yesu Awatuma Wale Sabini Na Wawili

1 Baada ya hayo, Bwana akawachagua wengine sabini na wawili, akawatuma wawili wawili katika kila mji na kila sehemu aliyokusudia kwenda baadaye.

2 Akawaambia, “Mavuno ni mengi, lakini watendakazi ni wachache. Kwa hiyo mwombeni Bwana wa mavuno, ili apeleke watendakazi katika shamba lake la mavuno.

3 Haya! nendeni. Ninawatuma kama wana-kondoo katikati ya mbwa mwitu.

4 Msichukue mkoba, wala mfuko, wala viatu, na msimsalimu mtu yeyote njiani.

5 “Mkiingia katika nyumba yoyote, kwanza semeni, ‘Amani iwe kwenu.’

6 Kama kuna mtu wa amani humo, basi amani yenu itakuwa juu yake. La sivyo, itawarudia.

7 Kaeni katika nyumba hiyo, mkila na kunywa kile watakachowapa, kwa sababu kila mtendakazi anastahili malipo yake. Msihamehame kutoka nyumba hadi nyumba.

8 “Mkienda katika mji na watu wake wakawakaribisha, kuleni chochote kiwekwacho mbele yenu,

9 waponyeni wagonjwa waliomo na waambieni: ‘Ufalme wa Mungu umekaribia.’

10 Lakini mkiingia katika mji, nao hawakuwakaribisha, tokeni mwende katika barabara zake mkaseme:

11 ‘Hata mavumbi ya mji wenu yaliyoshikamana na miguu yetu, tunayakungʼuta dhidi yenu. Lakini mjue kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia.’

12 Ninawaambia, itakuwa rahisi zaidi kwa Sodoma kustahimili katika siku ile kuliko mji ule.

Onyo Kwa Miji Isiyotubu

13 “Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingefanyika Tiro na Sidoni, miji hiyo ingekuwa imetubu zamani, kwa kuvaa magunia na kujipaka majivu.

14 Lakini itakuwa rahisi zaidi kwa Tiro na Sidoni kustahimili katika siku ya hukumu, kuliko ninyi.

15 Nawe, Kapernaumu, je, utainuliwa hadi mbinguni? La hasha, utashushwa mpaka kuzimu.”

16 “Yeye awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi; naye awakataaye ninyi amenikataa mimi. Lakini yeye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma.”

17 Wale sabini na wawili wakarudi kwa furaha, na kusema, “Bwana, hata pepo wachafu wanatutii kwa jina lako.”

18 Yesu akawaambia, “Nilimwona Shetani akianguka kutoka mbinguni kama umeme wa radi.

19 Tazama nimewapa mamlaka ya kukanyaga nyoka na nge na juu ya nguvu zote za adui; wala hakuna kitu chochote kitakachowadhuru.

20 Basi, msifurahi kwa kuwa pepo wachafu wanawatii, bali furahini kwa kuwa majina yenu yameandikwa mbinguni.”

Yesu Anashangilia

21 Wakati huo Yesu akashangilia katika Roho Mtakatifu, akasema, “Nakuhimidi Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa umewaficha mambo haya wenye hekima na wenye elimu, nawe ukawafunulia watoto wadogo. Naam, Baba, kwa kuwa hivyo ndivyo ilivyokupendeza.

22 “Nimekabidhiwa vitu vyote na Baba yangu. Hakuna mtu amjuaye Mwana ni nani ila Baba, wala hakuna amjuaye Baba ni nani ila Mwana na yeyote ambaye Mwana anapenda kumfunulia.”

23 Basi Yesu akawageukia wanafunzi wake akanena nao faraghani, akawaambia, “Heri macho yanayoona yale mambo mnayoyaona.

24 Kwa maana nawaambia, manabii wengi na wafalme walitamani kuona yale mnayoyaona lakini hawakuyaona, na walitamani kusikia yale mnayoyasikia lakini hawakuyasikia.”

Mfano Wa Msamaria Mwema

25 Wakati huo mtaalamu mmoja wa sheria alisimama ili kumjaribu Yesu, akamuuliza, “Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”

26 Yesu akamjibu, “Imeandikwaje katika Sheria? Kwani unasoma nini humo?”

27 Akajibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote’; tena, ‘Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.’ ”

28 Yesu akamwambia, “Umejibu vyema. Fanya hivyo nawe utaishi.”

29 Lakini yule mtaalamu wa sheria, akitaka kujionyesha kuwa mwenye haki, akamuuliza Yesu, “Jirani yangu ni nani?”

30 Yesu akamjibu akasema, “Mtu mmoja alikuwa akiteremka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko, naye akaangukia mikononi mwa wanyangʼanyi. Wakampiga, wakaondoka, wakamwacha akiwa karibu kufa.

31 Kuhani mmoja alikuwa akipitia njia ile, alipomwona huyo mtu, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani.

32 Vivyo hivyo, Mlawi mmoja naye alipofika mahali pale, alimwona, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani

33 Lakini Msamaria mmoja aliyekuwa akisafiri alipomwona, alimhurumia.

34 Akaenda alipokuwa na akasafisha majeraha yake kwa divai na mafuta, kisha akayafunga. Ndipo akampandisha kwenye punda wake, akampeleka mpaka kwenye nyumba ya wageni na kumtunza.

35 Kesho yake, yule Msamaria akachukua dinari mbiliakampa yule mwenye nyumba ya wageni na kusema, ‘Mtunze, nami nirudipo nitakulipa gharama yoyote ya ziada uliyotumia kwa ajili yake.’

36 “Ni yupi basi miongoni mwa hawa watatu wewe unadhani ni jirani yake yule mtu aliyeangukia mikononi mwa wanyangʼanyi?”

37 Yule mtaalamu wa sheria akajibu, “Ni yule aliyemhurumia.”

Ndipo Yesu akamwambia, “Nenda, ukafanye vivyo hivyo.”

Yesu Awatembelea Martha Na Maria

38 Ikawa Yesu na wanafunzi wake walipokuwa wakienda Yerusalemu, akaingia kwenye kijiji kimoja ambapo mwanamke mmoja aliyeitwa Martha alimkaribisha nyumbani kwake.

39 Martha alikuwa na mdogo wake aliyeitwa Maria, ambaye aliketi chini miguuni mwa Bwana akisikiliza yale aliyokuwa akisema.

40 Lakini Martha alikuwa akihangaika na maandalizi yote yaliyokuwa yafanyike. Martha akaja kwa Yesu na kumuuliza, “Bwana, hujali kwamba ndugu yangu ameniachia kazi zote mwenyewe? Basi mwambie anisaidie.”

41 Lakini Bwana akamjibu, “Martha, Martha, mbona unasumbuka na kuhangaika na mengi?

42 Lakini kunahitajika kitu kimoja tu. Maria amechagua kile kilicho bora, wala hakuna mtu atakayemwondolea.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/LUK/10-f3a38dcbd98e2f9503d5ed7407c6a358.mp3?version_id=1627—

Categories
Luka

Luka 11

Yesu Afundisha Wanafunzi Wake Kuomba

1 Siku moja, Yesu alikuwa mahali fulani akiomba. Alipomaliza kuomba, mmoja wa wanafunzi wake akamwambia, “Bwana, tufundishe kuomba, kama vile Yohana alivyowafundisha wanafunzi wake.”

2 Akawaambia, “Mnapoomba, semeni:

“ ‘Baba yetu (uliye mbinguni),

jina lako litukuzwe,

ufalme wako uje.

(Mapenzi yako yafanyike

hapa duniani kama huko mbinguni.)

3 Utupatie kila siku riziki yetu.

4 Utusamehe dhambi zetu,

kwa kuwa na sisi huwasamehe wote wanaotukosea.

Wala usitutie majaribuni

(bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu).’ ”

5 Kisha akawaambia, “Ni nani miongoni mwenu mwenye rafiki yake, naye akamwendea usiku wa manane na kumwambia, ‘Rafiki, nikopeshe mikate mitatu.

6 Kwa sababu rafiki yangu amekuja kutoka safarini, nami sina kitu cha kumpa.’

7 “Kisha yule aliyeko ndani amjibu, ‘Usinisumbue. Mlango umefungwa, nami na watoto wangu tumelala. Siwezi kuamka nikupe chochote.’

8 Nawaambia, ingawa huyo mtu hataamka na kumpa hiyo mikate kwa sababu ni rafiki yake, lakini kwa sababu ya kuendelea kwake kuomba, ataamka na kumpa kiasi anachohitaji.

9 “Kwa hiyo nawaambia: Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtapata; bisheni nanyi mtafunguliwa mlango.

10 Kwa kuwa kila aombaye hupewa; naye kila atafutaye hupata; na kila abishaye hufunguliwa mlango.

11 “Je, kuna yeyote miongoni mwenu ambaye mtoto wake akimwomba samaki, atampa nyoka badala yake?

12 Au mtoto akimwomba yai atampa nge?

13 Basi ikiwa ninyi mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa Roho Mtakatifu wale wamwombao!”

Yesu Na Beelzebuli

14 Basi Yesu alikuwa anamtoa pepo mchafu kutoka kwa mtu aliyekuwa bubu. Yule pepo mchafu alipomtoka yule mtu aliyekuwa bubu, akaanza kuongea, nao umati wa watu ukashangaa.

15 Lakini wengine wakasema, “Anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa Beelzebuli,yule mkuu wa pepo wachafu wote.”

16 Wengine ili kumjaribu wakataka awaonyeshe ishara kutoka mbinguni.

17 Yesu akajua mawazo yao, naye akawaambia, “Kila ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe huangamia. Nayo nyumba iliyogawanyika dhidi yake yenyewe itaanguka.

18 Kama Shetani amegawanyika mwenyewe, ufalme wake utasimamaje? Nawaambia haya kwa sababu ninyi mnadai ya kuwa mimi ninatoa pepo wachafu kwa uwezo wa Beelzebuli.

19 Kama mimi natoa pepo wachafu kwa nguvu za Beelzebuli, wafuasi wenu nao je, wao hutoa pepo wachafu kwa uwezo wa nani? Hivyo basi, wao ndio watakaowahukumu.

20 Lakini kama mimi ninatoa pepo wachafu kwa kidole cha Mungu, basi Ufalme wa Mungu umewajia.

21 “Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha anapoilinda nyumba yake, mali yake iko salama.

22 Lakini mtu mwenye nguvu zaidi kumliko akimshambulia na kumshinda, yeye humnyangʼanya silaha zake zote alizozitegemea, na kuchukua nyara.

23 “Mtu asiyekuwa pamoja nami yu kinyume nami, na mtu ambaye hakusanyi pamoja nami, hutawanya.

Kurudi Kwa Pepo Mchafu

24 “Pepo mchafu amtokapo mtu, hutangatanga katika sehemu zisizo na maji akitafuta mahali pa kupumzika, lakini hapati. Ndipo husema, ‘Nitarudi kwenye nyumba yangu nilikotoka.’

25 Naye arudipo na kuikuta ile nyumba imefagiliwa na kupangwa vizuri,

26 ndipo huenda na kuchukua pepo wachafu wengine saba wabaya kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo. Nayo hali ya mwisho ya yule mtu huwa ni mbaya kuliko ile ya kwanza.”

27 Ikawa Yesu alipokuwa akisema hayo, mwanamke mmoja katikati ya ule umati wa watu akapaza sauti akasema, “Limebarikiwa tumbo lililokuzaa na matiti uliyonyonya!”

28 Yesu akajibu, “Wamebarikiwa zaidi wale wanaolisikia neno la Mungu na kulitii.”

Ishara Ya Yona

29 Umati wa watu ulipokuwa unazidi kuongezeka, Yesu akaendelea kusema, “Hiki ni kizazi kiovu. Kinatafuta ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ile ya Yona.

30 Kwa maana kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa watu wa Ninawi, ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa ishara kwa kizazi hiki.

31 Malkia wa Kusini atasimama wakati wa hukumu na kuwahukumu watu wa kizazi hiki. Kwa kuwa yeye alikuja kutoka miisho ya dunia ili kuisikiliza hekima ya Solomoni. Na hapa yupo aliye mkuu kuliko Solomoni.

32 Siku ya hukumu, watu wa Ninawi watasimama pamoja na kizazi hiki na kukihukumu; kwa maana wao walitubu waliposikia mahubiri ya Yona. Na tazama, hapa yupo yeye aliye mkuu kuliko Yona.

Taa Ya Mwili

33 “Hakuna mtu yeyote awashaye taa na kuiweka mahali palipofichika au kuifunikia chini ya bakuli. Badala yake huiweka juu ya kinara chake, ili watu wote wanaoingia waone nuru.

34 Jicho lako ni taa ya mwili wako. Kama jicho lako ni zima, mwili wako wote pia umejaa nuru. Lakini kama jicho ni bovu, mwili wako wote pia umejaa giza.

35 Kwa hiyo, hakikisha kwamba nuru iliyoko ndani yako isiwe giza.

36 Basi ikiwa mwili wako wote umejaa nuru, bila sehemu yake yoyote kuwa gizani, basi utakuwa na nuru kama vile taa ikuangazavyo kwa nuru yake.”

Yesu Awashutumu Mafarisayo Na Wanasheria

37 Yesu alipomaliza kuzungumza, Farisayo mmoja alimwalika nyumbani mwake kwa chakula. Yesu akaingia na kuketi katika sehemu yake mezani.

38 Yule Farisayo akashangaa kwamba Yesu hakunawa kwanza kabla ya kula.

39 Ndipo Bwana akamwambia, “Sasa, enyi Mafarisayo, mnasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani mmejaa unyangʼanyi na uovu.

40 Enyi wapumbavu! Hamjui kuwa yeye aliyetengeneza nje ndiye alitengeneza na ndani pia?

41 Basi toeni sadaka ya vile mlivyo navyo, na tazama, vitu vyote vitakuwa safi kwenu.

42 “Lakini ole wenu, Mafarisayo, kwa maana mnampa Mungu zaka za mnanaa, mchicha na kila aina ya mboga, lakini mnapuuza haki na upendo wa Mungu. Iliwapasa kufanya haya ya pili bila kupuuza hayo ya kwanza.

43 “Ole wenu Mafarisayo, kwa sababu ninyi mnapenda kukalia viti vya mbele katika masinagogi, na kusalimiwa kwa heshima masokoni.

44 “Ole wenu, kwa sababu ninyi ni kama makaburi yasiyokuwa na alama, ambayo watu huyakanyaga pasipo kujua.”

45 Mtaalamu mmoja wa sheria akamjibu, akasema, “Mwalimu, unaposema mambo haya, unatutukana na sisi pia.”

46 Yesu akamjibu, “Nanyi wataalamu wa sheria, ole wenu, kwa sababu mnawatwika watu mizigo mizito ambayo hawawezi kubeba, wala ninyi wenyewe hamwinui hata kidole kimoja kuwasaidia.

47 “Ole wenu, kwa sababu ninyi mnajenga makaburi ya manabii waliouawa na baba zenu.

48 Hivyo ninyi mwashuhudia na mnathibitisha kile baba zenu walichofanya. Wao waliwaua manabii, nanyi mnawajengea makaburi.

49 Kwa sababu ya jambo hili, Mungu katika hekima yake alisema, ‘Tazama, nitatuma kwao manabii na mitume, nao watawaua baadhi yao na wengine watawatesa.’

50 Kwa hiyo kizazi hiki kitawajibika kwa ajili ya damu ya manabii iliyomwagwa tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu,

51 tangu damu ya Abeli mpaka damu ya Zekaria, aliyeuawa kati ya madhabahu na mahali patakatifu. Naam, nawaambia, kizazi hiki kitawajibika kwa haya yote.

52 “Ole wenu ninyi wataalamu wa sheria, kwa sababu mmeuondoa ufunguo wa maarifa. Ninyi wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wanaingia mkawazuia.”

53 Yesu alipoondoka huko, walimu wa sheria na Mafarisayo wakaanza kumpinga vikali na kumsonga kwa maswali,

54 wakivizia kumkamata kwa kitu atakachosema ili wamshtaki.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/LUK/11-a66d3e7d1fd97cdc08310a982c7537ca.mp3?version_id=1627—

Categories
Luka

Luka 12

Maonyo Dhidi Ya Unafiki

1 Wakati huo, umati mkubwa wa watu maelfu, walipokuwa wamekusanyika hata wakawa wanakanyagana, Yesu akaanza kuzungumza kwanza na wanafunzi wake, akawaambia: “Jihadharini na chachu ya Mafarisayo, yaani, unafiki wao.

2 Hakuna jambo lolote lililositirika ambalo halitafunuliwa, au lililofichwa ambalo halitajulikana.

3 Kwa hiyo, lolote mlilosema gizani litasikiwa nuruni. Na kile mlichonongʼona masikioni mkiwa kwenye vyumba vya ndani, kitatangazwa juu ya paa.

4 “Nawaambieni rafiki zangu, msiwaogope wale wauao mwili, lakini baada ya hilo hawawezi kufanya lolote zaidi.

5 Lakini nitawaambia nani wa kumwogopa: Mwogopeni yule ambaye baada ya kuua mwili, ana mamlaka ya kuwatupa motoni. Naam, nawaambia, mwogopeni huyo!

6 Mnajua kwamba shomoro watano huuzwa kwa senti mbili? Lakini Mungu hamsahau hata mmoja wao.

7 Naam, hata nywele za vichwa vyenu zote zimehesabiwa. Hivyo msiogope, kwa maana ninyi ni wa thamani kubwa kuliko shomoro wengi.

8 “Ninawaambia kwamba yeyote atakayenikiri mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkiri mbele za malaika wa Mungu.

9 Lakini yeye atakayenikana mimi mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkana mbele ya malaika wa Mungu.

10 Naye kila atakayenena neno baya dhidi ya Mwana wa Adamu atasamehewa, lakini yeyote atakayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa.

11 “Watakapowapeleka katika masinagogi, na mbele ya watawala na wenye mamlaka, msiwe na wasiwasi kuhusu namna mtakavyojitetea au mtakavyosema.

12 Kwa maana Roho Mtakatifu atawafundisha wakati huo huo mnachopaswa kusema.”

Mfano Wa Tajiri Mpumbavu

13 Mtu mmoja katika umati wa watu akamwambia Yesu, “Mwalimu, mwambie ndugu yangu tugawane naye urithi wetu.”

14 Lakini Yesu akamwambia, “Rafiki, ni nani aliyeniweka mimi kuwa hakimu wenu au msuluhishi juu yenu?”

15 Ndipo Yesu akawaambia, “Jihadharini! Jilindeni na aina zote za choyo. Kwa maana maisha ya mtu hayatokani na wingi wa mali alizo nazo.”

16 Kisha akawaambia mfano huu: “Shamba la mtu mmoja tajiri lilizaa sana.

17 Akawaza moyoni mwake, ‘Nifanye nini? Sina mahali pa kuhifadhi mavuno yangu.’

18 “Ndipo huyo tajiri akasema, ‘Nitafanya hivi: Nitabomoa ghala zangu za nafaka na kujenga nyingine kubwa zaidi na huko nitayahifadhi mavuno yangu yote na vitu vyangu.

19 Nami nitaiambia nafsi yangu, “Nafsi, unavyo vitu vingi vizuri ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi. Pumzika; kula, unywe, ufurahi.” ’

20 “Lakini Mungu akamwambia, ‘Mpumbavu wewe! Usiku huu uhai wako unatakiwa. Sasa hivyo vitu ulivyojiwekea akiba vitakuwa vya nani?’

21 “Hivyo ndivyo ilivyo kwa wale wanaojiwekea mali lakini hawajitajirishi kwa Mungu.”

Msiwe Na Wasiwasi

22 Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake: “Kwa hiyo nawaambia, msisumbukie maisha yenu kwamba mtakula nini; au msumbukie miili yenu kwamba mtavaa nini.

23 Maisha ni zaidi ya chakula, na mwili ni zaidi ya mavazi.

24 Fikirini ndege! Wao hawapandi wala hawavuni, hawana ghala wala popote pa kuhifadhi nafaka; lakini Mungu huwalisha. Ninyi ni wa thamani zaidi kuliko ndege!

25 Ni nani miongoni mwenu ambaye kwa kujitaabisha kwake anaweza kujiongezea hata saa moja zaidi katika maisha yake?

26 Kama hamwezi kufanya jambo dogo kama hilo, kwa nini basi kuyasumbukia hayo mengine?

27 “Angalieni maua jinsi yameavyo: Hayafanyi kazi wala hayafumi. Lakini nawaambia, hata Solomoni katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo maua.

28 Basi ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya shambani, ambayo leo yapo, na kesho yanatupwa motoni, si atawavika ninyi vizuri zaidi, enyi wa imani haba!

29 Wala msisumbuke mioyoni mwenu mtakula nini au mtakunywa nini. Msiwe na wasiwasi juu ya haya.

30 Watu wa mataifa ya duniani husumbuka sana kuhusu vitu hivi vyote, lakini Baba yenu anafahamu kuwa mnahitaji haya yote.

31 Bali utafuteni Ufalme wa Mungu, na haya yote atawapa pia.

Utajiri Wa Mbinguni

32 “Msiogope enyi kundi dogo, kwa maana Baba yenu ameona vyema kuwapa ninyi Ufalme.

33 Uzeni mali zenu mkawape maskini. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, mkajiwekee hazina mbinguni isiyokwisha, mahali ambapo mwizi hakaribii wala nondo haharibu.

34 Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo moyo wako utakapokuwa pia.

Kukesha

35 “Kuweni tayari mkiwa mmevikwa kwa ajili ya huduma na taa zenu zikiwa zinawaka,

36 kama watumishi wanaomngojea bwana wao arudi kutoka kwenye karamu ya arusi, ili ajapo na kubisha mlango waweze kumfungulia mara.

37 Heri wale watumishi ambao bwana wao atakapokuja atawakuta wakiwa wanakesha. Amin, nawaambia, atajifunga mkanda wake na kuwaketisha ili wale, naye atakuja na kuwahudumia.

38 Itakuwa heri kwa watumwa hao ikiwa bwana wao atakapokuja atawakuta wamekesha hata kama atakuja mnamo usiku wa manane, au karibu na mapambazuko.

39 Lakini fahamuni jambo hili: Kama mwenye nyumba angalijua saa mwizi atakuja, asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa.

40 Ninyi nanyi hamna budi kuwa tayari, kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja saa msiyotazamia.”

Mtumishi Mwaminifu Na Yule Asiye Mwaminifu

41 Ndipo Petro akamuuliza, “Bwana, mfano huu unatuambia sisi peke yetu au watu wote?”

42 Yesu akamjibu, “Ni yupi basi wakili mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake atamfanya msimamizi juu ya watumishi wake wote, ili awape watumishi wengine chakula chao wakati unaofaa?

43 Heri mtumishi yule ambaye bwana wake atakaporudi atamkuta akifanya hivyo.

44 Amin nawaambia, atamweka mtumishi huyo kuwa msimamizi wa mali yake yote.

45 Lakini kama yule mtumishi atasema moyoni mwake, ‘Bwana wangu anakawia kurudi,’ kisha akaanza kuwapiga wale watumishi wa kiume na wa kike, na kula na kunywa na kulewa.

46 Basi bwana wa mtumishi huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyoijua. Atamkata vipande vipande na kumweka katika sehemu moja pamoja na wale wasioamini.

47 “Yule mtumishi anayefahamu vyema mapenzi ya bwana wake na asijiandae wala kufanya kama apendavyo bwana wake, atapigwa kwa mapigo mengi.

48 Lakini yeyote ambaye hakujua naye akafanya yale yastahiliyo kupigwa, atapigwa kidogo. Yeyote aliyepewa vitu vingi, atadaiwa vingi; na yeyote aliyekabidhiwa vingi, kwake vitatakiwa vingi.

Yesu Kuleta Mafarakano

49 “Nimekuja kuleta moto duniani; laiti kama ungekuwa tayari umewashwa!

50 Lakini ninao ubatizo ambao lazima nibatizwe, nayo dhiki yangu ni kuu mpaka ubatizo huo ukamilike!

51 Mnadhani nimekuja kuleta amani duniani? La, nawaambia sivyo, nimekuja kuleta mafarakano.

52 Kuanzia sasa, kutakuwa na watu watano katika nyumba moja, watatu dhidi ya wawili, na wawili dhidi ya watatu.

53 Watafarakana baba dhidi ya mwanawe na mwana dhidi ya babaye, mama dhidi ya bintiye na binti dhidi ya mamaye, naye mama mkwe dhidi ya mkwewe na mkwe dhidi ya mama mkwe wake.”

Kutambua Majira

54 Pia Yesu akauambia ule umati wa watu, “Mwonapo wingu likitokea magharibi, mara mwasema, ‘Mvua itanyesha,’ nayo hunyesha.

55 Nanyi mwonapo upepo wa kusini ukivuma, ninyi husema, ‘Kutakuwa na joto,’ na huwa hivyo.

56 Enyi wanafiki! Mnajua jinsi ya kutambua kuonekana kwa dunia na anga. Inakuwaje basi kwamba mnashindwa kutambua wakati huu wa sasa?

57 “Kwa nini hamwamui wenyewe lililo haki?

58 Uwapo njiani na mshtaki wako kwenda kwa hakimu, jitahidi kupatana naye mkiwa njiani. La sivyo, atakupeleka kwa hakimu, naye hakimu atakukabidhi kwa afisa, naye afisa atakutupa gerezani.

59 Nakuambia, hautatoka humo hadi uwe umelipa senti ya mwisho.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/LUK/12-40aae8bdd940f94e810371a998b38991.mp3?version_id=1627—

Categories
Luka

Luka 13

Tubu, La Sivyo Utaangamia

1 Wakati huo huo, kulikuwa na watu waliomwambia Yesu habari za Wagalilaya ambao Pilato aliwaua, na damu ya hao watu akaichanganya na dhabihu yao waliyokuwa wanatoa.

2 Yesu akawauliza, “Mnadhani kwamba hawa Wagalilaya ambao walikufa kifo cha namna hiyo walikuwa na dhambi kuwazidi Wagalilaya wengine wote?

3 La hasha! Ninyi nanyi msipotubu, mtaangamia vivyo hivyo.

4 Au wale watu kumi na wanane waliokufa walipoangukiwa na mnara huko Siloamu: mnadhani wao walikuwa waovu kuliko watu wote waliokuwa wanaishi Yerusalemu?

5 Nawaambia, la hasha! Ninyi nanyi msipotubu, wote mtaangamia vivyo hivyo.”

Mfano Wa Mti Usiozaa Matunda

6 Kisha Yesu akawaambia mfano huu: “Mtu mmoja alikuwa na mtini uliopandwa katika shamba lake la mizabibu, akaja ili kutafuta tini kwenye mti huo, lakini hakupata hata moja.

7 Hivyo akamwambia mtunza shamba: ‘Tazama, kwa muda wa miaka mitatu sasa nimekuwa nikija kutafuta matunda kwenye mtini huu, nami sikupata hata moja. Ukate! Kwa nini uendelee kuharibu ardhi?’

8 “Yule mtunza shamba akamjibu, ‘Bwana, uache tena kwa mwaka mmoja zaidi, nami nitaupalilia na kuuwekea mbolea.

9 Kama ukizaa matunda mwaka ujao, vyema, la sivyo uukate.’ ”

Yesu Amponya Mwanamke Kilema Siku Ya Sabato

10 Basi Yesu alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo siku ya Sabato.

11 Wakati huo huo akaja mwanamke mmoja aliyekuwa na pepo mchafu, naye alikuwa amepinda mgongo kwa muda wa miaka kumi na minane, wala alikuwa hawezi kunyooka wima.

12 Yesu alipomwona, akamwita, akamwambia, “Mwanamke, uwe huru, umepona ugonjwa wako.”

13 Yesu alipomwekea mikono yake, mara akasimama wima akaanza kumtukuza Mungu.

14 Lakini kiongozi wa sinagogi akakasirika kwa sababu Yesu alikuwa ameponya mtu siku ya Sabato. Akaambia ule umati wa watu, “Kuna siku sita ambazo watu wanapaswa kufanya kazi. Katika siku hizo, njooni mponywe, lakini si katika siku ya Sabato.”

15 Lakini Bwana akamjibu, “Enyi wanafiki! Je, kila mmoja wenu hamfungulii ngʼombe wake au punda wake kutoka zizini akampeleka kumnywesha maji siku ya Sabato?

16 Je, huyu mwanamke, ambaye ni binti wa Abrahamu, aliyeteswa na Shetani akiwa amemfunga kwa miaka yote hii kumi na minane, hakustahili kufunguliwa kutoka kifungo hicho siku ya Sabato?”

17 Aliposema haya, wapinzani wake wakaaibika, lakini watu wakafurahi kwa ajili ya mambo ya ajabu aliyoyafanya.

Mfano Wa Punje Ya Haradali

18 Kisha Yesu akauliza, “Ufalme wa Mungu unafanana na nini? Nitaufananisha na nini?

19 Umefanana na punje ya haradali ambayo mtu aliichukua na kuipanda katika shamba lake. Nayo ikakua, ikawa mti nao ndege wa angani wakatengeneza viota vyao kwenye matawi yake.”

Mfano Wa Chachu

20 Yesu akauliza tena, “Nitaufananisha Ufalme wa Mungu na nini?

21 Unafanana na chachu ambayo mwanamke aliichukua akaichanganya katika kiasi kikubwa cha unga mpaka wote ukaumuka.”

Mlango Mwembamba

22 Yesu akapita katika miji na vijiji, akifundisha wakati alisafiri kwenda Yerusalemu.

23 Mtu mmoja akamuuliza, “Bwana, ni watu wachache tu watakaookolewa?”

24 Yesu akawaambia, “Jitahidini sana kuingia kupitia mlango mwembamba, kwa maana nawaambia wengi watajaribu kuingia, lakini hawataweza.

25 Wakati mwenye nyumba atakapoondoka na kufunga mlango, mtasimama nje mkibisha mlango na kusema, ‘Bwana! Tufungulie mlango!’

“Lakini yeye atawajibu, ‘Siwajui ninyi, wala mtokako.’

26 “Ndipo mtamjibu, ‘Tulikula na kunywa pamoja nawe, tena ulifundisha katika mitaa yetu.’

27 “Lakini yeye atawajibu, ‘Siwajui ninyi, wala mtokako. Ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu!’

28 “Ndipo kutakuwako kilio na kusaga meno, mtakapowaona Abrahamu, Isaki, Yakobo na manabii wote wakiwa katika Ufalme wa Mungu, lakini ninyi mkiwa mmetupwa nje.

29 Watu watatoka mashariki na magharibi, kaskazini na kusini, nao wataketi kwenye sehemu walizoandaliwa karamuni katika Ufalme wa Mungu.

30 Tazama, kunao walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, nao wa kwanza watakaokuwa wa mwisho.”

Yesu Aomboleza Kwa Ajili Ya Yerusalemu

31 Wakati huo huo baadhi ya Mafarisayo wakamwendea Yesu na kumwambia, “Ondoka hapa uende mahali pengine kwa maana Herode anataka kukuua.”

32 Yesu akawajibu, “Nendeni mkamwambie yule mbweha, ‘Ninafukuza pepo wachafu na kuponya wagonjwa leo na kesho, nami siku ya tatu nitaikamilisha kazi yangu.’

33 Sina budi kuendelea na safari yangu leo, kesho na kesho kutwa: kwa maana haiwezekani nabii kufa mahali pengine isipokuwa Yerusalemu.

34 “Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako! Mara ngapi nimetamani kuwakusanya watoto wako pamoja, kama vile kuku akusanyavyo vifaranga wake chini ya mabawa yake, lakini hukutaka!

35 Tazama nyumba yenu imeachwa ukiwa. Ninawaambia, hamtaniona tena mpaka wakati ule mtakaposema, ‘Amebarikiwa yeye ajaye kwa jina la Bwana.’ ”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/LUK/13-e32a47fa9b8ef3d34ec26811cb21ec5d.mp3?version_id=1627—

Categories
Luka

Luka 14

Yesu Nyumbani Mwa Farisayo

1 Ikawa siku moja Yesu alipokuwa amekwenda kula chakula kwa mmoja wa viongozi wa Mafarisayo siku ya Sabato, watu walikuwa wakimchunguza kwa bidii.

2 Papo hapo mbele yake palikuwa na mtu mmoja mwenye ugonjwa wa kuvimba mwili.

3 Yesu akawauliza wale Mafarisayo na walimu wa sheria, “Je, ni halali kuponya watu siku ya Sabato au la?”

4 Wakakaa kimya. Hivyo Yesu akamshika yule mgonjwa mkono na kumponya, akamruhusu aende zake.

5 Kisha akawauliza, “Kama mmoja wenu angekuwa na mtoto au ngʼombe wake aliyetumbukia katika kisima siku ya Sabato, je, hamtamvuta mara moja na kumtoa?”

6 Nao hawakuwa na la kusema.

Unyenyekevu Na Ukarimu

7 Alipoona jinsi wageni walivyokuwa wanachagua mahali pa heshima wakati wa kula, akawaambia mfano huu:

8 “Mtu akikualika arusini, usikae mahali pa mgeni wa heshima kwa kuwa inawezekana amealikwa mtu mheshimiwa kuliko wewe.

9 Kama mkifanya hivyo yule aliyewaalika ninyi wawili atakuja na kukuambia, ‘Mpishe huyu mtu kiti chako.’ Ndipo kwa aibu utalazimika kukaa katika nafasi ya chini kabisa.

10 Badala yake, unapoalikwa, chagua nafasi ya chini, ili yule mwenyeji wako atakapokuona atakuja na kukuambia, ‘Rafiki yangu, nenda kwenye nafasi iliyo bora zaidi.’ Kwa jinsi hii utakuwa umepewa heshima mbele ya wageni wenzako wote.

11 Kwa maana kila mtu ajikwezaye atashushwa, naye ajishushaye atakwezwa.”

12 Kisha Yesu akamwambia yule aliyewaalika, “Uandaapo karamu ya chakula cha mchana au cha jioni, usialike rafiki zako au ndugu zako au jamaa zako au majirani zako walio matajiri tu. Ukifanya hivyo, wao nao wanaweza kukualika kwao, nawe ukawa umelipwa kile ulichofanya na kupata thawabu yako.

13 Bali ufanyapo karamu, waalike maskini, vilema na vipofu,

14 nawe utabarikiwa kwa sababu hawa hawana uwezo wa kukulipa. Mungu atakulipa wakati wa ufufuo wa wenye haki.”

Mfano Wa Karamu Kuu

15 Mmoja wa wale waliokuwa pamoja naye mezani aliposikia hivi akamwambia Yesu, “Amebarikiwa mtu yule atakayekula katika karamu ya Ufalme wa Mungu!”

16 Yesu akamjibu, “Mtu mmoja alikuwa anaandaa karamu kubwa, akaalika watu wengi.

17 Wakati wa karamu ulipofika, akamtuma mtumishi wake akawaambie wale walioalikwa, ‘Karibuni, kila kitu ki tayari sasa.’

18 “Lakini wote, kila mmoja, wakaanza kutoa udhuru: Wa kwanza akasema, ‘Nimenunua shamba, lazima niende kuliona. Tafadhali niwie radhi.’

19 “Mwingine akasema, ‘Ndipo tu nimenunua jozi tano za ngʼombe wa kulimia, nami ninakwenda kuwajaribu, tafadhali niwie radhi.’

20 Naye mwingine akasema, ‘Nimeoa mke, kwa hiyo siwezi kuja.’

21 “Yule mtumishi akarudi, akampa bwana wake taarifa. Ndipo yule mwenye nyumba akakasirika, akamwagiza yule mtumishi wake, akisema, ‘Nenda upesi kwenye mitaa na vichochoro vya mjini uwalete maskini, vilema, vipofu na viwete.’

22 “Yule mtumishi akamwambia, ‘Bwana, yale uliyoniagiza nimefanya, lakini bado ipo nafasi.’

23 “Ndipo yule bwana akamwambia mtumishi wake, ‘Nenda kwenye barabara na vijia vilivyoko nje ya mji na uwalazimishe watu waingie ili nyumba yangu ipate kujaa.

24 Kwa maana nawaambia, hakuna hata mmoja wa wale walioalikwa atakayeionja karamu yangu.’ ”

Gharama Ya Kuwa Mwanafunzi

25 Umati mkubwa wa watu ulikuwa ukisafiri pamoja na Yesu, naye akageuka, akawaambia,

26 “Mtu yeyote anayekuja kwangu hawezi kuwa mwanafunzi wangu kama hatanipenda mimi zaidi ya baba yake na mama yake, mke wake na watoto wake, ndugu zake na dada zake, naam, hata maisha yake mwenyewe.

27 Yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

28 “Ni nani miongoni mwenu ambaye kama anataka kujenga nyumba, hakai kwanza chini na kufanya makisio ya gharama aone kama ana fedha za kutosha kukamilisha?

29 La sivyo, akiisha kuweka msingi, naye akiwa hana uwezo wa kuikamilisha, wote waionao wataanza kumdhihaki,

30 wakisema, ‘Mtu huyu alianza kujenga lakini hakuweza kukamilisha.’

31 “Au ni mfalme gani atokaye kwenda kupigana vita na mfalme mwingine, ambaye hakai chini kwanza na kufikiri iwapo akiwa na jeshi la watu 10,000 ataweza kupigana na yule anayekuja na jeshi la watu 20,000?

32 Kama hawezi, basi wakati yule mwingine akiwa bado yuko mbali, yeye hutuma ujumbe wa watu na kuomba masharti ya amani.

33 Vivyo hivyo, yeyote miongoni mwenu ambaye hawezi kuacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

Chumvi Isiyofaa

34 “Chumvi ni nzuri, lakini chumvi ikiwa imepoteza ladha yake, itafanywaje ili iweze kukolea tena?

35 Haifai ardhi wala kwa lundo la mbolea, bali hutupwa nje.

“Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/LUK/14-852ddf10c94fcd0e935166d3470a7140.mp3?version_id=1627—

Categories
Luka

Luka 15

Mfano Wa Kondoo Aliyepotea

1 Basi watoza ushuru na wenye dhambi wote walikuwa wanakusanyika ili wapate kumsikiliza Yesu.

2 Lakini Mafarisayo na walimu wa sheria wakanungʼunika wakisema, “Huyu mtu anawakaribisha wenye dhambi na kula nao.”

3 Ndipo Yesu akawaambia mfano huu:

4 “Ikiwa mmoja wenu ana kondoo mia moja, naye akapoteza mmoja wao, je, hawaachi wale tisini na tisa nyikani na kwenda kumtafuta huyo aliyepotea mpaka ampate?

5 Naye akishampata, humbeba mabegani mwake kwa furaha

6 na kwenda nyumbani. Kisha huwaita rafiki zake na majirani, na kuwaambia, ‘Furahini pamoja nami; nimempata kondoo wangu aliyepotea.’

7 Nawaambieni, vivyo hivyo kutakuwa na furaha zaidi mbinguni kwa sababu ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa wenye haki tisini na tisa ambao hawana haja ya kutubu.”

Mfano Wa Sarafu Iliyopotea

8 “Au ikiwa mwanamke ana sarafu za fedha kumi, naye akapoteza moja, je, hawashi taa na kufagia nyumba na kuitafuta kwa bidii mpaka aipate?

9 Naye akiisha kuipata, huwaita rafiki zake na majirani na kuwaambia, ‘Furahini pamoja nami; nimeipata ile sarafu yangu ya fedha iliyopotea.’

10 Vivyo hivyo, nawaambia, kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu juu ya mwenye dhambi mmoja atubuye.”

Mfano Wa Mwana Mpotevu

11 Yesu akaendelea kusema: “Kulikuwa na mtu mmoja aliyekuwa na wana wawili.

12 Yule mdogo akamwambia baba yake, ‘Baba, nipe urithi wangu.’ Hivyo akawagawia wanawe mali yake.

13 “Baada ya muda mfupi, yule mdogo akakusanya vitu vyote alivyokuwa navyo, akaenda nchi ya mbali, na huko akaitapanya mali yake kwa maisha ya anasa.

14 Baada ya kutumia kila kitu alichokuwa nacho, kukawa na njaa kali katika nchi ile yote, naye akawa hana chochote.

15 Kwa hiyo akaenda akaajiriwa na mwenyeji mmoja wa nchi ile ambaye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe.

16 Akatamani kujishibisha kwa maganda waliyokula wale nguruwe, wala hakuna mtu aliyempa chochote.

17 “Lakini alipozingatia moyoni mwake, akasema, ‘Ni watumishi wangapi walioajiriwa na baba yangu ambao wana chakula cha kuwatosha na kusaza, bali mimi hapa nakufa kwa njaa!

18 Nitaondoka na kurudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimetenda dhambi mbele za Mungu na mbele yako.

19 Sistahili tena kuitwa mwanao; nifanye kama mmoja wa watumishi wako.’

20 Basi akaondoka, akaenda kwa baba yake.

“Lakini alipokuwa bado yuko mbali, baba yake akamwona, moyo wake ukajawa na huruma. Akamkimbilia mwanawe, akamkumbatia na kumbusu.

21 “Yule mwana akamwambia baba yake, ‘Baba, nimekosa mbele za Mungu na mbele yako. Sistahili kuitwa mwanao tena.’

22 “Lakini baba yake akawaambia watumishi, ‘Leteni upesi joho lililo bora sana, tieni pete kidoleni mwake na viatu miguuni mwake.

23 Leteni ndama aliyenona, mkamchinje ili tuwe na karamu, tule na kufurahi.

24 Kwa maana huyu mwanangu alikuwa amekufa na sasa yu hai tena; alikuwa amepotea na sasa amepatikana!’ Nao wakaanza kufanya tafrija.

25 “Wakati huo, yule mwana mkubwa alikuwa shambani. Alipokaribia nyumbani, akasikia sauti ya nyimbo na watu wakicheza.

26 Akamwita mmoja wa watumishi na kumuuliza, ‘Kuna nini?’

27 Akamwambia, ‘Ndugu yako amekuja, naye baba yako amemchinjia ndama aliyenona kwa sababu mwanawe amerudi nyumbani akiwa salama na mzima.’

28 “Yule mwana mkubwa akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi baba yake akatoka nje na kumsihi.

29 Lakini yeye akamjibu baba yake, ‘Tazama! Miaka yote hii nimekutumikia na hata siku moja sijaacha kutii amri zako, lakini hujanipa hata mwana-mbuzi ili nifurahi na rafiki zangu.

30 Lakini huyu mwanao ambaye ametapanya mali yako kwa makahaba aliporudi nyumbani, wewe umemchinjia ndama aliyenona!’

31 “Baba yake akamjibu, ‘Mwanangu, umekuwa nami siku zote na vyote nilivyo navyo ni vyako.

32 Lakini ilitubidi tufurahi na kushangilia kwa sababu huyu ndugu yako alikuwa amekufa na sasa yu hai; alikuwa amepotea naye amepatikana.’ ”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/LUK/15-e579d12e34698ff550faf587dc0db4c8.mp3?version_id=1627—

Categories
Luka

Luka 16

Mfano Wa Msimamizi Mjanja

1 Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Palikuwa na tajiri mmoja na msimamizi wake. Ilisemekana kwamba huyo msimamizi alikuwa anatumia vibaya mali ya tajiri yake.

2 Hivyo huyo tajiri akamwita na kumuuliza, ‘Ni mambo gani haya ninayoyasikia kukuhusu? Toa taarifa ya usimamizi wako, kwa sababu huwezi kuendelea kuwa msimamizi.’

3 “Yule msimamizi akawaza moyoni mwake, ‘Nitafanya nini sasa? Bwana wangu ananiondoa katika kazi yangu. Sina nguvu za kulima, nami ninaona aibu kuombaomba.

4 Najua nitakalofanya ili nikiachishwa kazi yangu hapa, watu wanikaribishe nyumbani kwao.’

5 “Kwa hiyo akawaita wadeni wote wa bwana wake, mmoja mmoja. Akamuuliza wa kwanza, ‘Deni lako kwa bwana wangu ni kiasi gani?’

6 “Akajibu, ‘Galoni 800za mafuta ya mizeituni.’

“Msimamizi akamwambia, ‘Chukua hati ya deni lako, ibadilishe upesi, uandike galoni 400.’

7 “Kisha akamuuliza wa pili, ‘Wewe deni lako ni kiasi gani?’

“Akajibu, ‘Vipimo 1,000vya ngano.’

“Yule msimamizi akamwambia, ‘Chukua hati yako, andika vipimo 800!’

8 “Yule bwana akamsifu yule msimamizi dhalimu kwa jinsi alivyotumia ujanja. Kwa maana watu wa dunia hii wana ujanja zaidi wanapojishughulisha na mambo ya dunia kuliko watu wa nuru.

9 Nawaambia, tumieni mali ya kidunia kujipatia marafiki, ili itakapokwisha, mkaribishwe katika makao ya milele.

10 “Yeyote aliye mwaminifu katika mambo madogo, pia ni mwaminifu hata katika mambo makubwa, naye mtu ambaye si mwaminifu katika mambo madogo pia si mwaminifu katika mambo makubwa.

11 Ikiwa hamkuwa waaminifu katika mali ya kidunia, ni nani atakayewaaminia mali ya kweli?

12 Nanyi kama hamkuwa waaminifu na mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe?

13 “Hakuna mtumishi awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Kwa kuwa atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali.”

14 Mafarisayo, waliokuwa wapenda fedha, waliyasikia hayo yote na wakamcheka kwa dharau.

15 Yesu akawaambia, “Ninyi mnajionyesha kuwa wenye haki mbele za wanadamu, lakini Mungu anaijua mioyo yenu. Kwa maana vile vitu ambavyo wanadamu wanavithamini sana, kwa Mungu ni machukizo.

Sheria Na Ufalme Wa Mungu

16 “Sheria na Manabii vilihubiriwa mpaka kuja kwa Yohana Mbatizaji. Tangu wakati huo habari njema za Ufalme wa Mungu zinahubiriwa, na kila mmoja hujiingiza kwa nguvu.

17 Lakini ni rahisi zaidi mbingu na dunia kupita kuliko hata herufi moja kuondoka katika Sheria.

18 “Mtu yeyote amwachaye mkewe na kumwoa mwanamke mwingine anazini, naye mwanaume amwoaye mwanamke aliyetalikiwa anazini.

Tajiri Na Lazaro

19 “Palikuwa na mtu mmoja tajiri aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, ambaye aliishi kwa anasa kila siku.

20 Hapo penye mlango wake aliishi maskini mmoja, jina lake Lazaro, mwenye vidonda mwili mzima.

21 Huyo Lazaro alitamani kujishibisha kwa makombo yaliyoanguka kutoka mezani kwa yule tajiri. Hata mbwa walikuwa wakija na kuramba vidonda vyake.

22 “Wakati ukafika yule maskini akafa, nao malaika wakamchukua akae pamoja na Abrahamu. Yule tajiri naye akafa na akazikwa.

23 Kule kuzimu alipokuwa akiteseka, alitazama juu, akamwona Abrahamu kwa mbali, naye Lazaro alikuwa karibu yake.

24 Hivyo yule tajiri akamwita, ‘Baba Abrahamu, nihurumie na umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake ndani ya maji aupoze ulimi wangu, kwa sababu nina maumivu makuu kwenye moto huu.’

25 “Lakini Abrahamu akamjibu, ‘Mwanangu, kumbuka kwamba wakati wa uhai wako ulipata mambo mazuri, lakini Lazaro alipata mambo mabaya. Lakini sasa anafarijiwa hapa na wewe uko katika maumivu makuu.

26 Zaidi ya hayo, kati yetu na ninyi huko kumewekwa shimo kubwa, ili wale wanaotaka kutoka huku kuja huko wasiweze, wala mtu yeyote asiweze kuvuka kutoka huko kuja kwetu.’

27 “Akasema, ‘Basi, nakuomba, umtume Lazaro aende nyumbani kwa baba yangu,

28 maana ninao ndugu watano. Awaonye, ili wasije nao wakafika mahali hapa pa mateso.’

29 “Abrahamu akamjibu, ‘Ndugu zako wana Maandiko ya Mose na Manabii, wawasikilize hao.’

30 “Yule tajiri akasema, ‘Hapana, baba Abrahamu, lakini mtu kutoka kwa wafu akiwaendea, watatubu.’

31 “Abrahamu akamwambia, ‘Kama wasipowasikiliza Mose na Manabii, hawataweza kushawishika hata kama mtu akifufuka kutoka kwa wafu.’ ”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/LUK/16-e47c0cc05bb4bd5e39a7c02eec781c02.mp3?version_id=1627—

Categories
Luka

Luka 17

Yesu Afundisha Kuhusu Majaribu, Dhambi Na Imani

1 Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Mambo yanayosababisha watu watende dhambi hayana budi kutukia. Lakini ole wake mtu yule anayeyasababisha.

2 Ingekuwa heri kama mtu huyo angefungiwa jiwe la kusagia shingoni na kutoswa baharini, kuliko kumsababisha mmojawapo wa hawa wadogo kutenda dhambi.

3 Kwa hiyo, jilindeni.

“Kama ndugu yako akikukosea mwonye, naye akitubu, msamehe.

4 Kama akikukosea mara saba kwa siku moja na mara saba kwa siku moja akaja kwako akisema, ‘Ninatubu,’ msamehe.”

Imani

5 Mitume wake wakamwambia Bwana, “Tuongezee imani.”

6 Bwana akawajibu, “Kama mkiwa na imani ndogo kama punje ya haradali, mngeweza kuuambia mti huu wa mkuyu, ‘Ngʼoka ukaote baharini,’ nao ungewatii.

Wajibu Wa Mtumishi

7 “Ikiwa mmoja wenu ana mtumishi anayelima shambani au anayechunga kondoo, je, mtumishi huyo arudipo atamwambia, ‘Karibu hapa keti ule chakula?’

8 Je, badala yake, hatamwambia, ‘Niandalie chakula, nile, jifunge unitumikie ninapokula na kunywa; baadaye waweza kula na kunywa?’

9 Je, huyo mtu atamshukuru mtumishi huyo kwa kutimiza yale aliyoamriwa?

10 Vivyo hivyo nanyi mkiisha kufanya mliyoagizwa, semeni, ‘Sisi tu watumishi tusiostahili; tumefanya tu yale tuliyopaswa kufanya.’ ”

Yesu Atakasa Wakoma Kumi

11 Yesu alipokuwa njiani akienda Yerusalemu, alipitia mpakani mwa Samaria na Galilaya.

12 Alipokuwa akiingia kwenye kijiji kimoja, watu kumi waliokuwa na ukoma wakakutana naye. Wakasimama mbali,

13 wakapaza sauti, wakasema, “Yesu, Bwana, tuhurumie!”

14 Alipowaona akawaambia, “Nendeni mkajionyeshe kwa makuhani.” Nao walipokuwa njiani wakienda, wakatakasika.

15 Mmoja wao alipoona kwamba amepona, akarudi kwa Yesu, akimsifu Mungu kwa sauti kuu.

16 Akajitupa miguuni mwa Yesu akamshukuru. Yeye alikuwa Msamaria.

17 Yesu akauliza, “Je, hawakutakaswa wote kumi? Wako wapi wale wengine tisa?

18 Hakuna hata mmoja aliyeonekana kurudi ili kumshukuru Mungu isipokuwa huyu mgeni?”

19 Yesu akamwambia, “Inuka na uende zako, imani yako imekuponya.”

Kuja Kwa Ufalme Wa Mungu

20 Yesu alipoulizwa na Mafarisayo Ufalme wa Mungu utakuja lini, yeye akawajibu, “Ufalme wa Mungu hauji kwa kuchunguza kwa bidii,

21 wala watu hawatasema, ‘Huu hapa,’ au ‘Ule kule,’ kwa maana Ufalme wa Mungu umo ndani yenu.”

22 Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Wakati utafika ambapo mtatamani kuiona moja ya siku ya Mwana wa Adamu, lakini hamtaiona.

23 Watu watawaambia, ‘Yule kule!’ Au, ‘Huyu hapa!’ Msiwakimbilie.

24 Kwa maana kama vile umeme wa radi umulikavyo katika anga kuanzia mwisho mmoja hadi mwingine, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu katika siku yake.

25 Lakini kwanza itampasa kuteseka katika mambo mengi na kukataliwa na kizazi hiki.

26 “Kama ilivyokuwa siku za Noa, ndivyo itakavyokuwa katika siku za Mwana wa Adamu.

27 Watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka siku ile Noa alipoingia katika safina. Ndipo gharika ikaja na kuwaangamiza wote.

28 “Ndivyo ilivyokuwa katika siku za Loti: Watu walikuwa wakila na kunywa, wakinunua na kuuza, wakilima na kujenga.

29 Lakini siku ile Loti alipoondoka Sodoma, ikanyesha mvua ya moto na kiberiti kutoka mbinguni ukawaangamiza wote.

30 “Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile Mwana wa Adamu atakapofunuliwa.

31 Siku hiyo, mtu yeyote aliye juu ya dari ya nyumba yake, hata vitu vyake vikiwa ndani ya hiyo nyumba, asishuke kuvichukua. Vivyo hivyo mtu aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua chochote.

32 Mkumbukeni mke wa Loti!

33 Mtu yeyote anayejaribu kuyaokoa maisha yake atayapoteza, na yeyote atakayeyapoteza maisha yake atayaokoa.

34 Nawaambia, usiku huo watu wawili watakuwa wamelala kitanda kimoja; naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa.

35 Wanawake wawili watakuwa wanasaga nafaka pamoja; naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa. [

36 Wanaume wawili watakuwa wanafanya kazi pamoja shambani; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.]”

37 Kisha wakamuuliza, “Haya yatatukia wapi Bwana?”

Akawaambia, “Pale ulipo mzoga, huko ndiko tai watakapokusanyika.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/LUK/17-e85f1183335dd051ee2ce15c5f64859e.mp3?version_id=1627—

Categories
Luka

Luka 18

Mfano Wa Mjane Asiyekata Tamaa

1 Kisha Yesu akawapa wanafunzi wake mfano ili kuwaonyesha kuwa yawapasa kuomba pasipo kukata tamaa.

2 Akawaambia, “Katika mji mmoja alikuwepo hakimu ambaye hakumwogopa Mungu wala kumjali mtu.

3 Katika mji huo alikuwako mjane mmoja ambaye alikuwa akija kwake mara kwa mara akimwomba, ‘Tafadhali nipatie haki kati yangu na adui yangu.’

4 “Kwa muda mrefu yule hakimu alikataa. Lakini hatimaye akasema moyoni mwake, ‘Ijapokuwa simwogopi Mungu wala simjali mwanadamu,

5 lakini kwa kuwa huyu mjane ananisumbuasumbua, nitahakikisha amepata haki yake ili asiendelee kunichosha kwa kunijia mara kwa mara!’ ”

6 Bwana akasema, “Sikilizeni asemavyo huyu hakimu dhalimu.

7 Je, Mungu hatawatendea haki wateule wake wanaomlilia usiku na mchana? Je, atakawia kuwasaidia?

8 Ninawaambia, atawapatia haki upesi. Lakini je, Mwana wa Adamu atakapokuja ataikuta imani duniani?”

Mfano Wa Farisayo Na Mtoza Ushuru

9 Yesu akatoa mfano huu kwa wale waliojiamini kuwa wao ni wenye haki na kuwadharau wengine:

10 “Watu wawili walikwenda Hekaluni kusali, mmoja wao alikuwa Farisayo na mwingine alikuwa mtoza ushuru.

11 Yule Farisayo, akasimama, akasali hivi na kuomba kwake mwenyewe: ‘Mungu, nakushukuru kwa sababu mimi si kama watu wengine ambao ni wanyangʼanyi, wadhalimu, na wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru.

12 Mimi nafunga mara mbili kwa juma, na natoa sehemu ya kumi ya mapato yangu.’

13 “Lakini yule mtoza ushuru akasimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua uso wake kutazama mbinguni, bali alijipigapiga kifuani na kusema: ‘Mungu, nihurumie, mimi mwenye dhambi.’

14 “Nawaambia, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amehesabiwa haki mbele za Mungu zaidi ya yule Farisayo. Kwa maana yeyote ajikwezaye atashushwa, na yeyote ajishushaye atakwezwa.”

Yesu Awabariki Watoto Wadogo

15 Pia, watu walikuwa wakimletea Yesu watoto wachanga ili awaguse. Wanafunzi wake walipoona hivyo, wakawakemea.

16 Lakini Yesu akawaita wale watoto waje kwake, akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni wa wale walio kama hawa.

17 Amin, nawaambia, mtu yeyote asiyeupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hatauingia kamwe.”

Mtawala Tajiri

18 Mtawala mmoja akamuuliza Yesu, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”

19 Yesu akamjibu, “Mbona unaniita mwema? Hakuna yeyote aliye mwema ila Mungu peke yake.

20 Unazijua amri: ‘Usizini, usiue, usiibe, usishuhudie uongo, waheshimu baba yako na mama yako.’ ”

21 Akajibu, “Amri hizi zote nimezishika tangu nikiwa mtoto.”

22 Yesu aliposikia haya, akamwambia, “Bado kuna jambo moja ulilopungukiwa. Nenda ukauze kila kitu ulicho nacho, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”

23 Aliposikia jambo hili, alisikitika sana kwa maana alikuwa mtu mwenye mali nyingi.

24 Yesu akamtazama, akasema, “Tazama jinsi ilivyo vigumu kwa tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu!

25 Hakika ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.”

26 Wale waliosikia haya wakauliza, “Ni nani basi awezaye kuokoka?”

27 Yesu akajibu, “Yasiyowezekana kwa wanadamu yanawezekana kwa Mungu.”

28 Ndipo Petro akamjibu, “Tazama, tumeacha vyote tulivyokuwa navyo tukakufuata!”

29 Yesu akajibu, “Amin, nawaambia, hakuna hata mtu aliyeacha nyumba yake, au mke, au ndugu, au wazazi au watoto kwa ajili ya Ufalme wa Mungu

30 ambaye hatapewa mara nyingi zaidi ya hivyo katika maisha haya, na hatimaye kupata uzima wa milele ujao.”

Yesu Atabiri Kifo Chake Mara Ya Tatu

31 Yesu akawachukua wale wanafunzi wake kumi na wawili kando na kuwaambia, “Tunapanda kwenda Yerusalemu, na kila kitu kilichoandikwa na manabii kumhusu Mwana wa Adamu kitatimizwa.

32 Kwa kuwa atatiwa mikononi mwa watu wasiomjua Mungu, nao watamdhihaki, watamtukana na kumtemea mate, watampiga mijeledi na kumuua.

33 Naye siku ya tatu atafufuka.”

34 Wanafunzi wake hawakuelewa mambo haya, kwa kuwa maana yake ilikuwa imefichika kwao, nao hawakujua Yesu alikuwa anazungumzia nini.

Yesu Amponya Kipofu Karibu Na Yeriko

35 Yesu alipokuwa anakaribia Yeriko, kipofu mmoja alikuwa ameketi kando ya njia akiomba msaada.

36 Kipofu huyo aliposikia umati wa watu ukipita, akauliza, “Kuna nini?”

37 Wakamwambia, “Yesu wa Nazareti anapita.”

38 Akapaza sauti, akasema, “Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie!”

39 Wale waliokuwa wametangulia mbele wakamkemea, wakamwambia akae kimya. Lakini yeye akapaza sauti zaidi, “Mwana wa Daudi, nihurumie!”

40 Yesu akasimama, akawaamuru wamlete huyo mtu kwake. Alipokaribia, Yesu akamuuliza,

41 “Unataka nikufanyie nini?”

Akajibu, “Bwana, nataka kuona.”

42 Yesu akamwambia, “Basi upate kuona. Imani yako imekuponya.”

43 Akapata kuona saa ile ile, akamfuata Yesu, huku akimsifu Mungu. Watu wote walipoona mambo hayo, nao wakamsifu Mungu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/LUK/18-d1f12901b554265eb700b70f240e5a09.mp3?version_id=1627—

Categories
Luka

Luka 19

Zakayo Mtoza Ushuru

1 Yesu akaingia Yeriko, naye alikuwa anapita katikati ya huo mji.

2 Tazama, palikuwa na mtu mmoja mkuu wa watoza ushuru naye alikuwa tajiri, jina lake Zakayo.

3 Yeye alikuwa akijitahidi kumwona Yesu ni mtu wa namna gani. Lakini kutokana na umati mkubwa wa watu hakuweza kwa sababu alikuwa mfupi wa kimo.

4 Kwa hiyo akatangulia mbio mbele ya umati wa watu akapanda juu ya mkuyu ili amwone Yesu, kwa sababu angeipitia njia ile.

5 Yesu alipofika pale chini ya huo mkuyu, akatazama juu, akamwambia, “Zakayo, shuka upesi, kwa maana leo nitakuwa mgeni nyumbani kwako!”

6 Hivyo Zakayo akashuka upesi, akamkaribisha Yesu nyumbani kwake kwa furaha kubwa.

7 Watu wote walipoona hivyo, wakaanza kunungʼunika wakisema, “Amekwenda kuwa mgeni wa ‘mtu mwenye dhambi.’ ”

8 Lakini Zakayo akasimama na kumwambia Bwana, “Tazama, Bwana! Sasa hivi nusu ya mali yangu ninawapa maskini, nami kama nimemdhulumu mtu yeyote kitu chochote, nitamrudishia mara nne ya hicho kiwango.”

9 Ndipo Yesu akamwambia, “Leo, wokovu umeingia nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Abrahamu.

10 Kwa maana Mwana wa Adamu amekuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.”

Mfano Wa Fedha

11 Walipokuwa wanasikiliza haya, Yesu akaendelea kuwaambia mfano, kwa sababu alikuwa anakaribia Yerusalemu na watu walikuwa wakidhani ya kuwa Ufalme wa Mungu ulikuwa unakuja saa iyo hiyo.

12 Hivyo akawaambia: “Mtu mmoja mwenye cheo kikubwa alisafiri kwenda nchi ya mbali ili akapokee madaraka ya kuwa mfalme, kisha arudi.

13 Hivyo akawaita kumi miongoni mwa watumishi wake, na akawapa kila mmoja fungu la fedha. Akawaambia, ‘Fanyeni biashara na fedha hizi mpaka nitakaporudi.’

14 “Lakini raiya wa nchi yake walimchukia wakapeleka ujumbe na kusema, ‘Hatutaki huyu mtu awe mfalme wetu.’

15 “Hata hivyo alirudi akiwa amekwisha kupokea mamlaka ya ufalme, akawaita wale watumishi wake aliokuwa amewaachia fedha, ili afahamu ni faida kiasi gani kila mmoja wao aliyopata kwa kufanya biashara.

16 “Wa kwanza akaja na kusema, ‘Bwana, kutokana na fedha uliyoniachia, nimepata faida mara kumi zaidi.’

17 “Yule bwana akamjibu, ‘Umefanya vizuri mtumishi mwema! Kwa sababu umekuwa mwaminifu katika wajibu mdogo sana, nakupa mamlaka juu ya miji kumi.’

18 “Wa pili naye akaja. Akasema, ‘Bwana, fedha yako imeleta faida mara tano zaidi.’

19 “Bwana wake akajibu, ‘Nakupa mamlaka juu ya miji mitano.’

20 “Kisha akaja yule mtumishi mwingine, akasema, ‘Bwana, hii hapa fedha yako. Niliitunza vizuri kwenye kitambaa.

21 Nilikuogopa, kwa sababu wewe ni mtu mgumu. Unachukua ambapo hukuweka kitu, na unavuna mahali ambapo hukupanda kitu.’

22 “Bwana wake akamjibu, ‘Nitakuhukumu kwa maneno yako mwenyewe, wewe mtumishi mwovu! Kama ulifahamu kwamba mimi ni mtu mgumu, nichukuaye mahali ambapo sikuweka kitu na kuvuna mahali ambapo sikupanda,

23 kwa nini basi hukuweka fedha zangu kwa watoa riba, ili nitakaporudi nichukue iliyo yangu na riba yake?’

24 “Ndipo akawaambia wale waliokuwa wamesimama karibu, ‘Mnyangʼanyeni fungu lake la fedha, mkampe yule mwenye kumi.’

25 “Wakamwambia, ‘Bwana, mbona; tayari anayo mafungu kumi!’

26 “Akawajibu, ‘Nawaambia kwamba kila aliye na kitu, ataongezewa. Lakini yule asiye na kitu, hata alicho nacho atanyangʼanywa.

27 Lakini wale adui zangu ambao hawakutaka mimi niwe mfalme juu yao. Waleteni hapa mkawaue mbele yangu.’ ”

Yesu Aingia Yerusalemu Kwa Ushindi

28 Baada ya Yesu kusema haya, alitangulia kupanda kwenda Yerusalemu.

29 Naye alipokaribia Bethfage na Bethania kwenye mlima uitwao Mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili, akawaambia,

30 “Nendeni katika kijiji kilichoko mbele yenu. Na mtakapokuwa mnaingia kijijini, mtamkuta mwana-punda amefungwa hapo, ambaye hajapandwa na mtu bado. Mfungueni, mkamlete hapa.

31 Kama mtu akiwauliza, ‘Mbona mnamfungua?’ Mwambieni, ‘Bwana anamhitaji.’ ”

32 Wale waliotumwa wakaenda, wakakuta kila kitu kama vile Yesu alivyokuwa amewaambia.

33 Walipokuwa wanamfungua yule mwana-punda, wenyewe wakawauliza, “Mbona mnamfungua huyo mwana-punda?”

34 Wale wanafunzi wakajibu, “Bwana anamhitaji.”

35 Wakamleta kwa Yesu, nao baada ya kutandika mavazi yao juu ya huyo mwana-punda, wakampandisha Yesu juu yake.

36 Alipokuwa akienda akiwa amempanda, watu wakatandaza mavazi yao barabarani.

37 Alipokaribia mahali yanapoanzia materemko ya Mlima wa Mizeituni, umati wote wa wafuasi wake wakaanza kumsifu Mungu kwa furaha kwa sauti kuu kwa ajili ya matendo yote ya miujiza waliyoyaona. Wakasema:

38 “Amebarikiwa Mfalme ajaye kwa Jina la Bwana!”

“Amani mbinguni na utukufu huko juu sana.”

39 Baadhi ya Mafarisayo waliokuwamo miongoni mwa ule umati wa watu wakamwambia, “Mwalimu, waamuru wanafunzi wako wanyamaze.”

40 Yesu akawajibu, “Nawaambia ninyi, kama hawa wakinyamaza, mawe yatapiga kelele.”

Yesu Anaulilia Mji Wa Yerusalemu

41 Alipokaribia Yerusalemu na kuuona mji, aliulilia,

42 akisema, “Laiti ungalijua hata wewe leo yale ambayo yangeleta amani, lakini sasa yamefichika machoni pako.

43 Hakika siku zinakujia, ambazo adui zako watakuzingira, nao watakuzunguka pande zote na kukuzuilia ndani.

44 Watakuponda chini, wewe na watoto walioko ndani ya kuta zako. Nao hawataacha hata jiwe moja juu ya jingine, kwa sababu hukutambua wakati wa kujiliwa kwako.”

Yesu Atakasa Hekaluni

45 Ndipo akaingia eneo la Hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza vitu humo.

46 Naye akawaambia, “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala,’ lakini ninyi mmeifanya kuwa ‘pango la wanyangʼanyi.’ ”

47 Kila siku alikuwa akifundisha Hekaluni. Lakini viongozi wa makuhani, walimu wa sheria na viongozi wa watu walikuwa wakitafuta njia ili kumuua.

48 Lakini hawakupata nafasi kwa sababu watu wote walimfuata wakiyasikiliza maneno yake kwa usikivu mwingi.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/LUK/19-09a2322e78ac839a7cf7b0ebfc17ee02.mp3?version_id=1627—