Categories
Kumbukumbu

Kumbukumbu 30

Mafanikio Baada Ya Kumgeukia Bwana

1 Wakati baraka hizi zote pamoja na laana nilizoziweka mbele yako zitakapokujia, nawe ukazitafakari moyoni popoteBwanaMungu wako atakapokutawanya miongoni mwa mataifa,

2 hapo wewe na watoto wako mtakapomrudiaBwanaMungu wako, na kumtii kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote kulingana na kila kitu ninachokuamuru leo,

3 ndipoBwanaMungu wako atakapokurudisha kutoka utumwani na kukuhurumia, naye atakukusanya tena kutoka mataifa yote kule alikutawanya.

4 Hata kama umefukuziwa katika nchi ya mbali kiasi gani chini ya mbingu, kutoka hukoBwanaMungu wako atakukusanya na kukurudisha.

5 YeyeBwanaatakurudisha katika nchi iliyokuwa mali ya baba zako, nawe utaimiliki. Naye atakufanya ufanikiwe sana na kukuzidisha kwa idadi kuliko baba zako.

6 BwanaMungu wako ataitahiri mioyo yenu na mioyo ya wazao wenu ili mweze kumpenda kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote ukaishi.

7 BwanaMungu wako ataweka laana hizi zote juu ya adui zako ambao wanakuchukia na kukutesa.

8 Utamtii tenaBwanana kuzishika amri zake zote ninazokupa leo.

9 NdipoBwanaMungu wako atakapokufanikisha sana katika kazi zote za mikono yako na katika uzao wa tumbo lako, wadogo wa mifugo yako na mazao ya nchi yako.Bwanaatakufurahia tena na kukufanikisha, kama alivyowafurahia baba zako,

10 kama ukimtiiBwanaMungu wako, na kuzishika amri zake na maagizo yake ambayo yameandikwa katika Kitabu hiki cha Sheria, na kumgeukiaBwanaMungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote.

Uzima Na Mauti

11 Ninachokuagiza leo sio kigumu sana kwako au usichokiweza.

12 Hakiko juu mbinguni, ili uulize, “Ni nani atakayepanda mbinguni kukileta na kututangazia ili tuweze kutii?”

13 Wala hakiko ngʼambo ya bahari, ili uulize, “Ni nani atakayevuka bahari kwenda kukichukua na kututangazia ili tupate kutii?”

14 La hasha! Lile neno liko karibu sana nawe; liko kinywani mwako na ndani ya moyo wako ili uweze kulitii.

15 Tazama, naweka mbele yako leo uzima na mafanikio, mauti na maangamizo.

16 Ninakuamuru leo kwamba umpendeBwanaMungu wako, utembee katika njia zake, na kutunza maagizo yake, amri na sheria zake; ndipo utakapoishi na kuongezeka, nayeBwanaMungu wako atakubariki katika nchi unayoingia kuimiliki.

17 Lakini kama moyo wako ukigeukia mbali ukawa huna utii, kama umevutwa kuisujudia miungu mingine na kuiabudu,

18 nakutangazia leo hii kwamba hakika utaangamizwa. Hutaishi maisha marefu katika nchi unayovuka Yordani kuiingia na kuimiliki.

19 Leo ninaziita mbingu na nchi kama mashahidi dhidi yako kwamba nimeweka mbele yako uzima na mauti, baraka na laana. Basi sasa chagueni uzima, ili wewe na watoto wako mpate kuishi,

20 na ili upate kumpendaBwanaMungu wako, uisikilize sauti yake na kuambatana naye. Kwa kuwaBwanandiye uzima wako, na atakupa wingi wa siku ili upate kuishi katika nchi aliyoapa kuwapa baba zako Abrahamu, Isaki na Yakobo.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/DEU/30-7e4558bdab08c84d5d0739a04ab37b77.mp3?version_id=1627—

Categories
Kumbukumbu

Kumbukumbu 31

Yoshua Kutawala Baada Ya Mose

1 Kisha Mose akaenda akasema maneno haya kwa Waisraeli wote:

2 “Sasa nina miaka mia moja na ishirini nami siwezi tena kuwaongoza.Bwanaameniambia, ‘Hutavuka Yordani.’

3 BwanaMungu wenu, yeye mwenyewe atavuka mbele yenu. Ataangamiza mataifa haya mbele yenu, nanyi mtaimiliki nchi yao. Pia Yoshua atavuka mbele yenu, kamaBwanaalivyosema.

4 NayeBwanaatawafanyia watu hao kile alichowafanyia Sihoni na Ogu, wafalme wa Waamori, ambao aliwaangamiza pamoja na nchi yao.

5 Bwanaatawakabidhi kwenu, nanyi lazima mwatendee yale yote niliyowaamuru.

6 Kuweni imara na moyo wa ushujaa. Msiogope wala msifadhaike kwa sababu yao, kwa kuwaBwanaMungu wenu anakwenda pamoja nanyi; kamwe hatawaacha wala hatawatupa ninyi.”

7 Kisha Mose akamwita Yoshua na akamwambia mbele ya Israeli wote, “Uwe imara na moyo wa ushujaa, kwa kuwa ni lazima uende na watu hawa katika nchi ileBwanaaliyowaapia baba zao kuwapa, nawe ni lazima uwagawie kama urithi wao.

8 Bwanamwenyewe atakutangulia naye atakuwa pamoja nawe; kamwe hatakuacha wala hatakutupa. Usiogope, wala usifadhaike.”

Kusoma Sheria

9 Kwa hiyo Mose akaandika sheria hii na kuwapa makuhani, wana wa Lawi, waliochukua Sanduku la Agano laBwanana wazee wote wa Israeli.

10 Kisha Mose akawaamuru, akasema: “Mwishoni mwa kila miaka saba, katika mwaka wa kufuta madeni, wakati wa Sikukuu ya Vibanda,

11 Waisraeli wote wanapokuja mbele zaBwanaMungu wenu mahali atakapopachagua, utasoma sheria hii mbele yao masikioni mwao.

12 Kusanya watu wote, wanaume, wanawake, watoto na wageni wanaoishi katika miji yenu, ili waweze kusikia na kujifunza kumchaBwanaMungu wenu na kufuata kwa bidii maneno yote ya sheria hii.

13 Watoto wao, ambao hawaijui sheria hii, lazima waisikie na kujifunza kumchaBwanaMungu wenu kwa muda mtakaoishi katika nchi mnayovuka Yordani kuimiliki.”

Kuasi Kwa Waisraeli Kunatabiriwa

14 Bwanaakamwambia Mose, “Sasa siku ya kifo chako imekaribia. Mwite Yoshua, mkajihudhurishe katika Hema la Kukutania, mahali nitakapompa maagizo ya kazi.” Kwa hiyo Mose na Yoshua wakaja na kujihudhurisha kwenye Hema la Kukutania.

15 KishaBwanaakatokea katika Hema katika nguzo ya wingu, nalo wingu likasimama juu ya ingilio la Hema.

16 KishaBwanaakamwambia Mose: “Unakwenda kupumzika na baba zako, nao watu hawa hivi karibuni watazini na miungu migeni ya nchi wanayoingia. Wataniacha na kuvunja Agano nililofanya nao.

17 Siku hiyo nitawakasirikia na kuwaacha; nitawaficha uso wangu, nao wataangamizwa. Maafa mengi na shida nyingi zitakuja juu yao, nao siku hiyo watauliza, ‘Je, maafa haya hayakuja juu yetu kwa sababu Mungu wetu hayuko pamoja nasi?’

18 Nami hakika nitauficha uso wangu siku hiyo kwa sababu ya maovu yao yote kwa kugeukia miungu mingine.

19 “Sasa ujiandikie wimbo huu,uwafundishe Waisraeli na uwaamuru wauimbe, ili upate kuwa ushahidi wangu dhidi yao.

20 Nitakapokwisha kuwaingiza katika nchi itiririkayo maziwa na asali, nchi niliyowaahidi baba zao kwa kiapo, nao watakapokula wakashiba na kufanikiwa, watageukia miungu mingine na kuiabudu, wakinikataa mimi na kuvunja Agano langu.

21 Maafa na shida zitakapokuja juu yao, wimbo huu utashuhudia dhidi yao, kwa sababu hautasahauliwa na wazao wao. Ninajua lile wanaloandaa kufanya, hata kabla sijawaingiza katika nchi niliyowaahidi kwa kiapo.”

22 Hivyo Mose akaandika wimbo huu siku ile na akawafundisha Waisraeli.

23 Bwanaakampa Yoshua mwana wa Nuni agizo hili: “Uwe hodari na shujaa, kwa kuwa utawaleta Waisraeli katika nchi niliyowaahidi kwa kiapo, nami mwenyewe nitakuwa pamoja nawe.”

24 Baada ya Mose kumaliza kuandika kwenye kitabu maneno ya sheria hii kutoka mwanzo hadi mwisho,

25 akawapa Walawi wale waliolibeba Sanduku la Agano laBwanaagizo hili, akawaambia:

26 “Chukueni Kitabu hiki cha Sheria mkakiweke kando ya Sanduku la Agano laBwanaMungu wenu. Hapo ndipo kitakapokaa kama shahidi dhidi yenu.

27 Kwa kuwa ninajua jinsi mlivyo waasi na mlivyo na shingo ngumu. Kama mmekuwa mkiasi dhidi yaBwananikiwa bado niko hai na nikiwa pamoja nanyi, mtaasi mara ngapi baada ya kufa kwangu!

28 Kusanyeni mbele yangu wazee wote wa makabila yenu na maafisa wenu wote, ili nipate kusema maneno haya masikioni mwao na kuziita mbingu na nchi ili kushuhudia dhidi yao.

29 Kwa kuwa ninajua baada ya kifo changu hakika mtakuwa waovu kabisa na kugeuka kutoka njia niliyowaamuru ninyi. Katika siku zijazo, maafa yatawapata kwa sababu mtafanya maovu mbele ya macho yaBwana, na kuchochea hasira yake kwa yale mikono yenu itakayokuwa imefanya.”

Wimbo Wa Mose

30 Mose akayasoma maneno ya wimbo huu kutoka mwanzo hadi mwisho katika masikio ya kusanyiko lote la Israeli:

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/DEU/31-352d8c8e6fa80c4366c1ca104f0630c5.mp3?version_id=1627—

Categories
Kumbukumbu

Kumbukumbu 32

1 Sikilizeni, enyi mbingu, nami nitasema;

sikia, ee nchi, maneno ya kinywa changu.

2 Mafundisho yangu na yanyeshe kama mvua,

na maneno yangu na yashuke kama umande,

kama manyunyu juu ya majani mabichi,

kama mvua tele juu ya mimea myororo.

3 Nitalitangaza jina laBwana.

Naam, sifuni ukuu wa Mungu wetu!

4 Yeye ni Mwamba, kazi zake ni kamilifu,

njia zake zote ni haki.

Mungu mwaminifu ambaye hakosei,

yeye ni mnyofu na mwenye haki.

5 Wamefanya mambo ya upotovu mbele zake;

kwa aibu yao, wao si watoto wake tena,

lakini ni kizazi kilicho kiovu na kilichopotoka.

6 Je, hii ndiyo njia ya kumlipaBwana,

enyi watu wajinga na wasio na busara?

Je, yeye siye Baba yenu, Muumba wenu,

aliyewafanya ninyi na kuwaumba?

7 Kumbuka siku za kale;

tafakari vizazi vya zamani vilivyopita.

Uliza baba yako, naye atakuambia,

wazee wako, nao watakueleza.

8 Aliye Juu Sana alipowapa mataifa urithi wao,

alipogawanya wanadamu wote,

aliweka mipaka kwa ajili ya mataifa

sawasawa na hesabu ya wana wa Israeli.

9 Kwa kuwa fungu laBwanani watu wake,

Yakobo kura yake ya urithi.

10 Katika nchi ya jangwa alimkuta,

katika nyika tupu ivumayo upepo.

Alimhifadhi na kumtunza;

akamlinda kama mboni ya jicho lake,

11 kama tai avurugaye kiota chake,

na kurukaruka juu ya makinda yake,

ambaye hutanda mabawa yake kuwadaka,

na huwachukua kwenye mabawa yake.

12 Bwanapeke yake alimwongoza;

hakuwepo mungu mgeni pamoja naye.

13 Akamfanya apande sehemu zilizoinuka za nchi,

akamlisha kwa mavuno ya mashamba.

Akamlea kwa asali toka mwambani,

na kwa mafuta kutoka mwamba mgumu,

14 kwa jibini na maziwa kutoka makundi ya ngʼombe

na kutoka makundi ya mbuzi,

kwa mafuta ya wana-kondoo na mbuzi,

kwa kondoo dume wazuri wa Bashani,

na kwa ngano nzuri.

Ukanywa damu ya zabibu inayotoa povu.

15 Yeshurunialinenepa na kupiga teke;

alikuwa na chakula tele,

akawa mzito na akapendeza sana.

Akamwacha Mungu aliyemuumba,

na kumkataa Mwamba Mwokozi wake.

16 Wakamfanya Mungu kuwa na wivu kwa miungu yao migeni,

na kumkasirisha kwa sanamu zao

za machukizo.

17 Wakatoa dhabihu kwa pepo, ambao si Mungu:

miungu wasiyoijua,

miungu iliyojitokeza siku za karibuni,

miungu ambayo baba zenu hawakuiogopa.

18 Mkamwacha Mwamba, aliyewazaa ninyi;

mkamsahau Mungu aliyewazaa.

19 Bwanaakaona hili, akawakataa,

kwa sababu alikasirishwa

na wanawe na binti zake.

20 Akasema, “Nitawaficha uso wangu,

nami nione mwisho wao utakuwa nini,

kwa kuwa wao ni kizazi kilichopotoka,

watoto ambao si waaminifu.

21 Wamenifanya niwe na wivu

kwa kile ambacho si mungu,

na kunikasirisha kwa sanamu zao

zisizokuwa na thamani.

Nitawafanya wawaonee wivu wale ambao si taifa.

Nitawafanya wakasirishwe

na taifa lile lisilo na ufahamu.

22 Kwa maana moto umewashwa kwa hasira yangu,

ule uwakao hadi kwenye vina vya mauti.

Utateketeza dunia pamoja na mazao yake,

na kuwasha moto katika misingi ya milima.

23 “Nitalundika majanga juu yao

na kutumia mishale yangu dhidi yao.

24 Nitatuma njaa kali dhidi yao maradhi mabaya,

yateketezayo na tauni ya kufisha;

nitawapelekea meno makali ya wanyama mwitu,

na sumu ya nyoka wale watambaao mavumbini.

25 Barabarani upanga utawakosesha watoto;

nyumbani mwao hofu itatawala.

Vijana wao wa kiume na wa kike wataangamia,

pia watoto wachanga na wazee wenye mvi.

26 Nilisema ningewatawanya

na kufuta kumbukumbu lao

katika mwanadamu.

27 Lakini nilihofia dhihaka za adui,

adui asije akashindwa kuelewa,

na kusema, ‘Mikono yetu imeshinda;

Bwanahakufanya yote haya.’ ”

28 Wao ni taifa lisilo na akili,

hakuna busara ndani yao.

29 Laiti wangekuwa na hekima wangefahamu hili,

na kutambua mwisho wao utakuwa aje!

30 Mtu mmoja angewezaje kufukuza elfu moja,

au wawili kufukuza elfu kumi,

kama si kwamba Mwamba wao amewauza,

kama si kwambaBwanaamewaacha?

31 Kwa kuwa mwamba wao si kama Mwamba wetu,

sawasawa na vile adui zetu wanavyokiri.

32 Mzabibu wao unatoka kwenye mzabibu wa Sodoma,

na kutoka kwenye mashamba ya Gomora.

Zabibu zake zimejaa sumu,

na vishada vyake vimejaa uchungu.

33 Mvinyo wao ni sumu ya nyoka,

sumu yenye kufisha ya swila.

34 “Je, hili sikuliweka akiba

na kulifungia kwenye vyumba vyangu vya hazina?

35 Ni juu yangu kulipiza kisasi; nitalipiza.

Wakati utakapowadia, mguu wao utateleza;

siku yao ya maafa ni karibu,

na maangamizo yao yanawajia haraka.”

36 Bwanaatawahukumu watu wake,

na kuwahurumia watumishi wake

atakapoona nguvu zao zimekwisha

wala hakuna yeyote aliyebaki,

mtumwa au aliye huru.

37 Atasema: “Sasa iko wapi miungu yao,

mwamba walioukimbilia,

38 miungu wale waliokula mafuta ya dhabihu zao

na kunywa mvinyo wa sadaka zao za vinywaji?

Wainuke basi, wawasaidie!

Wawapeni basi ulinzi!

39 “Tazama basi, Mimi mwenyewe, Mimi Ndiye!

Hakuna mungu mwingine ila Mimi.

Mimi ninaua na Mimi ninafufua,

Mimi nimejeruhi na Mimi nitaponya,

wala hakuna awezaye kuokoa kutoka mkononi mwangu.

40 Ninainua mkono wangu kuelekea mbinguni na kusema:

Hakika kama niishivyo milele,

41 wakati ninapounoa upanga wangu unaometameta

na mkono wangu unapoushika ili kutoa hukumu,

nitalipiza kisasi juu ya adui zangu

na kuwalipiza wale wanaonichukia.

42 Nitailevya mishale yangu kwa damu,

wakati upanga wangu ukitafuna nyama:

damu ya waliochinjwa pamoja na mateka,

vichwa vya viongozi wa adui.”

43 Furahini, enyi mataifa, pamoja na watu wake,

kwa kuwa atailipiza damu ya watumishi wake,

atalipiza kisasi juu ya adui zake

na kufanya upatanisho

kwa ajili ya nchi na watu wake.

44 Mose na Yoshuamwana wa Nuni wakaja, wakanena maneno yote ya wimbo watu wakiwa wanasikia.

45 Mose alipomaliza kuyasoma maneno haya yote kwa Israeli wote,

46 akawaambia, “Yawekeni moyoni maneno yote ambayo nimewatangazia kwa makini siku hii ya leo, ili kwamba mpate kuwaagiza watoto wenu wayatii kwa bidii maneno yote ya sheria hii.

47 Siyo maneno matupu tu kwenu, bali ni uzima wenu. Kwa hayo mtaishi maisha marefu katika nchi mnayovuka Yordani kuimiliki.”

Mose Aelezwa Kuhusu Kifo Chake

48 Siku hiyo hiyoBwanaakamwambia Mose,

49 “Kwea katika mapangano ya Mlima Abarimu hadi kilima cha Nebo kilichoko Moabu, ngʼambo ya Yeriko, na uitazame Kanaani, nchi ninayowapa Waisraeli kama milki yao wenyewe.

50 Utafia kwenye mlima huo unaokwea na kukusanyika pamoja na watu wako, kama ndugu yako Aroni alivyofia juu ya Mlima Hori naye akakusanyika kwa watu wake.

51 Hii ni kwa sababu ninyi wawili mlivunja uaminifu nami mbele ya Waisraeli kwenye maji ya Meriba-Kadeshi katika Jangwa la Sini, na kwa sababu hamkuuinua utakatifu wangu miongoni mwa Waisraeli.

52 Kwa hiyo, utaiona tu nchi kwa mbali; wewe hutaingia nchi ninayowapa watu wa Israeli.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/DEU/32-58ef675860feeb6b511494e672a545f8.mp3?version_id=1627—

Categories
Kumbukumbu

Kumbukumbu 33

Mose Anayabariki Makabila

1 Hii ndiyo baraka Mose mtu wa Mungu aliyotamka kwa Waisraeli kabla ya kifo chake.

2 Alisema:

“Bwanaalikuja kutoka Mlima Sinai,

akachomoza kama jua juu yao

kutoka Mlima Seiri,

akaangaza kutoka Mlima Parani.

Alikuja pamoja na watakatifu makumi elfu

kutoka kusini,

kutoka materemko ya mlima wake.

3 Hakika ni wewe ambaye huwapenda watu,

watakatifu wako wote wamo mkononi mwako.

Miguuni pako wote wanasujudu

na kutoka kwako wanapokea mafundisho,

4 sheria ile Mose aliyotupa sisi,

tulio milki ya kusanyiko la Yakobo.

5 Alikuwa mfalme juu ya Yeshuruni

wakati viongozi wa watu walipokusanyika,

pamoja na makabila ya Israeli.

6 “Reubeni na aishi, asife,

wala watu wake wasiwe wachache.”

7 Akasema hili kuhusu Yuda:

“EeBwana, sikia kilio cha Yuda,

mlete kwa watu wake.

Kwa mikono yake mwenyewe hujitetea.

Naam, uwe msaada wake

dhidi ya adui zake!”

8 Kuhusu Lawi alisema:

“Thumimu yako na Urimuyako ulimpa,

mtu yule uliyemfadhili.

Ulimjaribu huko Masa

na kushindana naye

kwenye maji ya Meriba.

9 Alinena hivi kuhusu baba yake na mama yake,

‘Mimi siwahitaji kamwe.’

Akawasahau jamaa zake,

asiwatambue hata watoto wake,

lakini akaliangalia neno lako

na kulilinda Agano lako.

10 Humfundisha Yakobo mausia yako

na Israeli sheria yako.

Hufukiza uvumba mbele zako

na sadaka nzima za kuteketezwa

juu ya madhabahu yako.

11 EeBwana, bariki ustadi wake wote,

nawe upendezwe na kazi ya mikono yake.

Vipige viuno vya wale wainukao dhidi yake;

wapige adui zake hata wasiinuke tena.”

12 Kuhusu Benyamini akasema:

“Mwache mpenzi waBwana

apumzike salama kwake,

kwa maana humkinga mchana kutwa,

na yuleBwanaampendaye

hupumzika kati ya mabega yake.”

13 Kuhusu Yosefu akasema:

“Bwanana aibariki nchi yake

kwa umande wa thamani

kutoka mbinguni juu,

na vilindi vya maji

vilivyotulia chini;

14 pamoja na vitu vilivyo bora sana

viletwavyo na jua,

na vitu vizuri sana vinavyoweza

kutolewa na mwezi;

15 pamoja na zawadi bora sana

za milima ya zamani

na kwa wingi wa baraka

za vilima vya milele;

16 pamoja na baraka nzuri mno

za ardhi na ukamilifu wake,

na upendeleo wake yeye

aliyeishi kwenye kichaka

kilichokuwa kinawaka moto.

Hivi vyote na vikae juu ya kichwa cha Yosefu,

juu ya paji la uso la aliye mkuu

miongoni mwa ndugu zake.

17 Katika fahari yeye ni kama fahali mzaliwa wa kwanza;

pembe zake ni pembe za nyati,

na kwa pembe hizo atapiga mataifa,

hata yaliyo miisho ya dunia.

Hivyo ndivyo yalivyo makumi elfu ya Efraimu;

hivyo ndivyo yalivyo maelfu ya Manase.”

18 Kuhusu Zabuloni akasema:

“Shangilia, Zabuloni, wakati wa kutoka nje,

nawe Isakari, katika mahema yako.

19 Watawaita mataifa kwenye mlima,

na huko mtatoa dhabihu za haki;

watajifurahisha kwa wingi uliojaza bahari,

kwa hazina zilizofichwa mchangani.”

20 Kuhusu Gadi akasema:

“Atabarikiwa yeye aongezaye milki ya Gadi!

Gadi huishi huko kama simba,

akirarua kwenye mkono au kichwa.

21 Alijichagulia nchi nzuri kuliko zote

kwa ajili yake mwenyewe;

fungu la kiongozi lilikuwa limehifadhiwa

kwa ajili yake.

Viongozi wa watu walipokusanyika,

alitimiza haki ya mapenzi yaBwana,

na hukumu zake kuhusu Israeli.”

22 Kuhusu Dani akasema:

“Dani ni mwana simba,

akiruka kutoka Bashani.”

23 Kuhusu Naftali akasema:

“Naftali amejaa tele upendeleo waBwana,

naye amejaa baraka yake;

atarithi magharibi na kusini.”

24 Kuhusu Asheri akasema:

“Aliyebarikiwa zaidi sana katika wana ni Asheri;

yeye na apate upendeleo kwa ndugu zake,

yeye na anawe miguu yake kwenye mafuta.

25 Makomeo ya malango yako yawe chuma na shaba,

nazo nguvu zako zitakuwa sawa na siku zako.

26 “Hakuna mwingine kama Mungu wa Yeshuruni,

ambaye hupanda juu ya mbingu ili akusaidie,

na juu ya mawingu katika utukufu wake.

27 Mungu wa milele ni kimbilio lako,

na chini kuna mikono ya milele.

Atamfukuza adui yako mbele yako,

akisema, ‘Mwangamize yeye!’

28 Hivyo Israeli ataishi salama peke yake.

Mzao wa Yakobo ni salama

katika nchi ya nafaka na divai mpya,

mahali ambapo mbingu

hudondosha umande.

29 Ee Israeli, wewe umebarikiwa!

Ni nani kama wewe,

taifa lililookolewa naBwana?

Yeye ni ngao yako na msaada wako,

na upanga wako uliotukuka.

Adui zako watatetemeka mbele yako,

nawe utapakanyaga

mahali pao pa juu.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/DEU/33-a6c4e364662300629ffa031e84f19aaf.mp3?version_id=1627—

Categories
Kumbukumbu

Kumbukumbu 34

Kifo Cha Mose

1 Kisha Mose akaupanda mlima Nebo kutoka tambarare za Moabu mpaka kilele cha Pisga, ngʼambo ya Yeriko. HukoBwanaakamwonyesha nchi yote: kutoka Gileadi mpaka Dani,

2 Naftali yote, nchi ya Efraimu na Manase, nchi yote ya Yuda mpaka bahari ya magharibi,

3 Negebu na nchi yote kuanzia Bonde la Yeriko, Mji wa Mitende, hadi Soari.

4 KishaBwanaakamwambia, “Hii ndiyo nchi niliyomwahidi Abrahamu na Isaki na Yakobo kwa kiapo niliposema, ‘Nitawapa wazao wako.’ Nimekuruhusu uione kwa macho yako, lakini hutavuka kuingia.”

5 Naye Mose mtumishi waBwanaakafa huko Moabu, kamaBwanaalivyokuwa amesema.

6 Mungu akamzika huko Moabu, katika bonde mkabala na Beth-Peori, lakini hakuna ajuaye kaburi lake lilipo mpaka leo.

7 Mose alikuwa na umri wa miaka mia moja na ishirini alipofariki; hata hivyo nguvu ya macho yake haikufifia wala mwili wake haukudhoofika.

8 Waisraeli wakaomboleza kwa ajili ya Mose kwenye tambarare za Moabu kwa siku thelathini, mpaka wakati wa kulia na kuomboleza ulipopita.

9 Basi Yoshua mwana wa Nuni alijazwa roho ya hekima kwa sababu Mose alikuwa ameweka mikono yake juu yake. Kwa hiyo Waisraeli wakamsikiliza na wakafanya yale ambayoBwanaalikuwa amemwagiza Mose.

10 Tangu wakati huo, katika Israeli hajainuka nabii mwingine kama Mose, ambayeBwanaalimjua uso kwa uso,

11 aliyetenda ishara zote zile za miujiza na maajabu ambayoBwanaalimtuma kuyatenda huko Misri, yaani kwa Farao na maafisa wake wote na nchi yake yote.

12 Kwa kuwa hakuna mtu yeyote aliyewahi kuonyesha nguvu nyingi ama kutenda matendo ya kutisha ambayo Mose aliwahi kuyafanya mbele ya Israeli yote.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/DEU/34-e0154b8f805c9e884caee9fc493f73d2.mp3?version_id=1627—