Categories
Isaya

Isaya 40

Faraja Kwa Watu Wa Mungu

1 Wafarijini, wafarijini watu wangu,

asema Mungu wenu.

2 Sema na Yerusalemu kwa upole,

umtangazie

kwamba kazi yake ngumu imekamilika,

kwamba dhambi yake imefanyiwa fidia,

kwamba amepokea kutoka mkononi mwaBwana

maradufu kwa ajili ya dhambi zake zote.

3 Sauti ya mtu aliaye:

“Itengenezeni jangwani njia yaBwana,

nyoosheni njia kuu nyikani

kwa ajili ya Mungu wetu.

4 Kila bonde litainuliwa,

kila mlima na kilima kitashushwa;

penye mabonde patanyooshwa,

napo palipoparuza patasawazishwa.

5 Utukufu waBwanautafunuliwa,

nao wanadamu wote watauona pamoja.

Kwa maana kinywa chaBwanakimenena.”

6 Sauti husema, “Piga kelele.”

Nami nikasema, “Nipige kelele gani?”

“Wanadamu wote ni kama majani,

nao utukufu wao wote

ni kama maua ya kondeni.

7 Majani hunyauka na maua huanguka,

kwa sababu pumzi yaBwanahuyapuliza.

Hakika wanadamu ni majani.

8 Majani hunyauka na maua huanguka,

lakini neno la Mungu wetu ladumu milele.”

9 Wewe uletaye habari njema Sayuni,

panda juu ya mlima mrefu.

Wewe uletaye habari njema Yerusalemu,

inua sauti yako kwa kupiga kelele,

inua sauti, usiogope;

iambie miji ya Yuda,

“Yuko hapa Mungu wenu!”

10 Tazameni,BwanaMwenyezi anakuja na nguvu,

nao mkono wake ndio utawalao kwa ajili yake.

Tazameni, ujira wake u pamoja naye,

nayo malipo yake yanafuatana naye.

11 Huchunga kundi lake kama mchungaji wa mifugo:

Hukusanya wana-kondoo katika mikono yake

na kuwachukua karibu na moyo wake,

huwaongoza taratibu wale wanyonyeshao.

12 Ni nani aliyepima maji ya bahari

kwenye konzi ya mkono wake,

au kuzipima mbingu kwa shibiriyake?

Ni nani aliyeyashika mavumbi ya dunia katika kikapu,

au kupima milima kwenye kipimio

na vilima kwenye mizani?

13 Ni nani aliyeyafahamu mawazo yaBwana,

au kumfundisha akiwa kama mshauri wake?

14 Ni nani ambayeBwanaametaka shauri kwake ili kumwelimisha,

naye ni nani aliyemfundisha njia iliyo sawa?

Ni nani aliyemfundisha maarifa

au kumwonyesha mapito ya ufahamu?

15 Hakika mataifa ni kama tone ndani ya ndoo,

ni kama vumbi jembamba juu ya mizani,

huvipima visiwa kana kwamba vilikuwa vumbi laini.

16 Lebanoni hautoshi kwa moto wa madhabahuni,

wala wanyama wake hawatoshi kwa sadaka za kuteketezwa.

17 Mbele yake mataifa yote ni kama si kitu,

yanaonekana yasio na thamani

na zaidi ya bure kabisa.

18 Basi, utamlinganisha Mungu na nani?

Utamlinganisha na kitu gani?

19 Kwa habari ya sanamu, fundi huisubu,

naye mfua dhahabu huifunika kwa dhahabu

na kuitengenezea mikufu ya fedha.

20 Mtu aliye maskini sana asiyeweza kuleta sadaka kama hii

huuchagua mti usiooza.

Humtafuta fundi stadi

wa kusimamisha sanamu ambayo haitatikisika.

21 Je, hujui?

Je, hujasikia?

Je, hujaambiwa tangu mwanzo?

Je, hujafahamu tangu kuumbwa kwa dunia?

22 Anakaa kwenye kiti cha enzi juu ya duara ya dunia,

nao watu wakaao ndani yake ni kama panzi.

Huzitandaza mbingu kama chandarua,

na kuzitandaza kama hema la kuishi.

23 Huwafanya wakuu kuwa si kitu,

na kuwashusha watawala wa dunia hii kuwa kitu bure.

24 Mara baada ya kupandwa,

mara baada ya kutiwa ardhini,

mara baada ya kutoa mizizi yao ardhini,

ndipo huwapulizia nao wakanyauka,

nao upepo wa kisulisuli

huwapeperusha kama makapi.

25 “Utanilinganisha mimi na nani?

Au ni nani anayelingana nami?” asema yeye Aliye Mtakatifu.

26 Inueni macho yenu mtazame mbinguni:

Ni nani aliyeumba hivi vyote?

Ni yeye aletaye nje jeshi la nyota moja baada ya nyingine

na kuziita kila moja kwa jina lake.

Kwa sababu ya uweza wake mkuu na nguvu zake kuu,

hakuna hata mojawapo inayokosekana.

27 Kwa nini unasema, ee Yakobo,

nanyi ee Israeli, kulalamika,

“Njia yangu imefichwaBwanaasiione,

Mungu wangu hajali shauri langu?”

28 Je wewe, hufahamu?

Je wewe, hujasikia?

Bwanani Mungu wa milele,

Muumba wa miisho ya dunia.

Hatachoka wala kulegea,

wala hakuna hata mmoja

awezaye kuupima ufahamu wake.

29 Huwapa nguvu waliolegea

na huongeza nguvu za wadhaifu.

30 Hata vijana huchoka na kulegea,

nao vijana wanaume hujikwaa na kuanguka,

31 bali wale wamtumainioBwana

atafanya upya nguvu zao.

Watapaa juu kwa mbawa kama tai;

watapiga mbio wala hawatachoka,

watatembea kwa miguu wala hawatazimia.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/40-3461f7e73668810625cba05ce7394d8c.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 41

Msaidizi Wa Israeli

1 “Nyamazeni kimya mbele zangu, enyi visiwa!

Mataifa na wafanye upya nguvu zao!

Wao na wajitokeze, kisha waseme,

tukutane pamoja mahali pa hukumu.

2 “Ni nani aliyemchochea mmoja kutoka mashariki,

akimwita katika haki kwa utumishi wake?

Huyatia mataifa mikononi mwake,

na kuwatiisha wafalme mbele zake.

Huwafanya kuwa mavumbi kwa upanga wake,

huwafanya makapi yapeperushwayo na upepo kwa upinde wake.

3 Huwafuatia na kuendelea salama,

katika njia ambayo miguu yake haijawahi kupita.

4 Ni nani aliyefanya jambo hili na kulitimiliza,

akiita vizazi tangu mwanzo?

Mimi,Bwana, ni wa kwanza

nami nitakuwa pamoja na wa mwisho:

mimiBwanandiye.”

5 Visiwa vimeliona na kuogopa,

miisho ya dunia inatetemeka.

Wanakaribia na kuja mbele,

6 kila mmoja humsaidia mwingine

na kusema kwa ndugu yake, “Uwe hodari!”

7 Fundi humtia moyo sonara,

yeye alainishaye kwa nyundo

humhimiza yeye agongeaye kwenye fuawe,

Humwambia yeye aunganishaye, “Ni kazi njema.”

Naye huikaza sanamu kwa misumari ili isitikisike.

8 “Lakini wewe, ee Israeli, mtumishi wangu,

Yakobo, niliyemchagua,

ninyi wazao wa Abrahamu rafiki yangu,

9 nilikuchukua toka miisho ya dunia,

nilikuita kutoka pembe zake za mbali.

Nilisema, ‘Wewe ni mtumishi wangu’;

nimekuchagua, wala sikukukataa.

10 Hivyo usiogope, kwa maana niko pamoja nawe;

usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako.

Nitakutia nguvu na kukusaidia;

nitakutegemeza kwa mkono wa kuume wa haki yangu.

11 “Wote walioona hasira dhidi yako

hakika wataaibika na kutahayarika,

wale wakupingao

watakuwa kama vile si kitu, na kuangamia.

12 Ingawa utawatafuta adui zako,

hutawaona.

Wale wanaopigana vita dhidi yako

watakuwa kama vile si kitu kabisa.

13 Kwa maana Mimi ndimiBwana, Mungu wako,

nikushikaye mkono wako wa kuume

na kukuambia, Usiwe na hofu,

nitakusaidia.

14 Usiogope, ee Yakobo uliye mdudu,

ee Israeli uliye mdogo,

kwa kuwa Mimi mwenyewe nitakusaidia,” asemaBwana,

Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.

15 “Tazama, nitakufanya chombo cha kupuria,

kipya na chenye makali, chenye meno mengi.

Utaipura milima na kuiponda

na kuvifanya vilima kuwa kama makapi.

16 Utaipepeta, nao upepo utaichukua,

dhoruba itaipeperushia mbali.

Bali wewe utajifurahisha katikaBwana

na katika utukufu wa yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.

17 “Maskini na wahitaji wanatafuta maji,

lakini hayapo,

ndimi zao zimekauka kwa kiu.

Lakini MimiBwananitawajibu,

Mimi, Mungu wa Israeli, sitawaacha.

18 Nitaifanya mito itiririke juu ya vilima vilivyo kame,

nazo chemchemi ndani ya mabonde.

Nitaligeuza jangwa liwe mabwawa ya maji,

nayo ardhi iliyokauka kuwa chemchemi za maji.

19 Katika jangwa nitaotesha

mwerezi, mshita, mhadasi na mzeituni.

Nitaweka misunobari, mivinje na misanduku

pamoja huko nyikani,

20 ili kwamba watu wapate kuona na kujua,

wapate kufikiri na kuelewa,

kwamba mkono waBwanaumetenda hili,

kwamba yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli ndiye alilifanya.”

21 Bwanaasema, “Leta shauri lako.

Toa hoja yako,” asema Mfalme wa Yakobo.

22 “Leteni sanamu zenu zituambie

ni nini kitakachotokea.

Tuambieni mambo ya zamani yalikuwa nini,

ili tupate kuyatafakari

na kujua matokeo yake ya mwisho.

Au tutangazieni mambo yatakayokuja,

23 tuambieni ni nini kitakachotokea baadaye,

ili tupate kujua kuwa ninyi ni miungu.

Fanyeni jambo lolote zuri au baya,

ili tupate kutishika na kujazwa na hofu.

24 Lakini ninyi ni zaidi ya bure kabisa,

na kazi zenu hazifai kitu kabisa;

yeye awachaguaye ni chukizo sana.

25 “Nimemchochea mtu mmoja kutoka kaskazini,

naye yuaja, mmoja toka mawio ya jua aliitaye Jina langu.

Huwakanyaga watawala kana kwamba ni matope,

kama mfinyanzi akanyagavyo udongo wa kufinyangia.

26 Ni nani aliyenena hili tokea mwanzoni, ili tupate kujua,

au kabla, ili tuweze kusema, ‘Alikuwa sawa’?

Hakuna aliyenena hili,

hakuna aliyetangulia kusema hili,

hakuna yeyote aliyesikia maneno kutoka kwenu.

27 Nilikuwa wa kwanza kumwambia Sayuni,

‘Tazama, wako hapa!’

Nilimpa Yerusalemu mjumbe wa habari njema.

28 Ninatazama, lakini hakuna yeyote:

hakuna yeyote miongoni mwao awezaye kutoa shauri,

hakuna yeyote wa kutoa jibu wakati ninapowauliza.

29 Tazama, wote ni ubatili!

Matendo yao ni bure;

vinyago vyao ni upepo mtupu na machafuko.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/41-f33740067275a72627924a0505b905d0.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 42

Mtumishi Wa Bwana

1 “Huyu hapa mtumishi wangu, ninayemtegemeza,

mteule wangu, ambaye ninapendezwa naye;

nitaweka Roho yangu juu yake,

naye ataleta haki kwa mataifa.

2 Hatapaza sauti wala kupiga kelele,

wala hataiinua sauti yake barabarani.

3 Mwanzi uliopondeka hatauvunja,

na utambi unaofuka moshi hatauzima.

Kwa uaminifu ataleta haki,

4 hatazimia roho wala kukata tamaa,

mpaka atakaposimamisha haki juu ya dunia.

Visiwa vitaweka tumaini lao katika sheria yake.”

5 Hili ndilo asemalo Mungu,Bwana,

yeye aliyeziumba mbingu na kuzitanda,

aliyeitandaza dunia na vyote vitokavyo humo,

awapaye watu wake pumzi,

na uzima kwa wale waendao humo:

6 “Mimi,Bwana, nimekuita katika haki;

nitakushika mkono wako.

Nitakulinda na kukufanya

kuwa Agano kwa ajili ya watu

na nuru kwa Mataifa,

7 kuwafungua macho wale wasioona,

kuwaacha huru kutoka kifungoni waliofungwa jela,

na kuwafungua kutoka gerezani

wale wanaokaa gizani.

8 “Mimi ndimiBwana; hilo ndilo Jina langu!

Sitampa mwingine utukufu wangu

wala sanamu sifa zangu.

9 Tazama, mambo ya kwanza yametokea,

nami natangaza mambo mapya;

kabla hayajatokea

nawatangazia habari zake.”

Wimbo Wa Kumsifu Bwana

10 MwimbieniBwanawimbo mpya,

sifa zake toka miisho ya dunia,

ninyi mshukao chini baharini,

na vyote vilivyomo ndani yake,

enyi visiwa na wote wakaao ndani yake.

11 Jangwa na miji yake na vipaze sauti zao;

makao anamoishi Kedari na yashangilie.

Watu wa Sela waimbe kwa furaha,

na wapige kelele kutoka vilele vya milima.

12 WampeBwanautukufu,

na kutangaza sifa zake katika visiwa.

13 Bwanaataenda kama mtu mwenye nguvu,

kama shujaa atachochea shauku yake,

kwa kelele ataamsha kilio cha vita,

naye atashinda adui zake.

14 “Kwa muda mrefu nimenyamaza kimya,

nimekaa kimya na kujizuia.

Lakini sasa, kama mwanamke wakati wa kujifungua,

ninapiga kelele, ninatweta na kushusha pumzi.

15 Nitaharibu milima na vilima

na kukausha mimea yako yote;

nitafanya mito kuwa visiwa

na kukausha mabwawa.

16 Nitawaongoza vipofu kwenye njia ambayo hawajaijua,

kwenye mapito wasiyoyazoea nitawaongoza;

nitafanya giza kuwa nuru mbele yao,

na kufanya mahali palipoparuza kuwa laini.

Haya ndiyo mambo nitakayofanya;

mimi sitawaacha.

17 Lakini wale wanaotumaini sanamu,

wanaoviambia vinyago, ‘Ninyi ndio miungu yetu,’

watarudishwa nyuma kwa aibu kubwa.

Israeli Kipofu Na Kiziwi

18 “Sikieni, enyi viziwi;

tazameni, enyi vipofu, mpate kuona!

19 Ni nani aliye kipofu isipokuwa mtumishi wangu,

na kiziwi kama mjumbe ninayemtuma?

Ni nani aliye kipofu kama yeye aliyejitoa kwangu,

aliye kipofu kama mtumishi waBwana?

20 Mmeona vitu vingi, lakini hamkuzingatia;

masikio yenu yako wazi, lakini hamsikii chochote.”

21 IlimpendezaBwana

kwa ajili ya haki yake

kufanya sheria yake kuwa kuu na tukufu.

22 Lakini hili ni taifa lililoibwa na kutekwa nyara,

wote wamenaswa katika mashimo,

au wamefichwa katika magereza.

Wamekuwa nyara,

wala hapana yeyote awaokoaye.

Wamefanywa mateka,

wala hapana yeyote asemaye, “Warudishe.”

23 Ni nani miongoni mwenu atakayesikiliza hili,

au atakayezingatia kwa makini katika wakati ujao?

24 Ni nani aliyemtoa Yakobo kuwa mateka,

na Israeli kwa wateka nyara?

Je, hakuwa yeye,Bwana,

ambaye tumetenda dhambi dhidi yake?

Kwa kuwa hawakufuata njia zake,

hawakutii sheria zake.

25 Hivyo akawamwagia hasira yake inayowaka,

ukali wa vita.

Iliwazunguka kwa miali ya moto, lakini hata hivyo hawakuelewa;

iliwateketeza, lakini hawakuyatia moyoni.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/42-788fb4b293f8b7e54626fd900a3a74bd.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 43

Mwokozi Pekee Wa Israeli

1 Lakini sasa hili ndilo asemaloBwana,

yeye aliyekuumba, ee Yakobo,

yeye aliyekuhuluku, ee Israeli:

“Usiogope kwa maana nimekukomboa,

nimekuita wewe kwa jina lako, wewe u wangu.

2 Unapopita kwenye maji makuu,

nitakuwa pamoja nawe,

unapopita katika mito ya maji,

hayatakugharikisha.

Utakapopita katika moto,

hutaungua,

miali ya moto haitakuunguza.

3 Kwa kuwa Mimi ndimiBwana, Mungu wako,

yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wako.

Ninaitoa Misri kuwa fidia yako,

Kushi na Seba badala yako.

4 Kwa kuwa wewe ni wa thamani na wa kuheshimiwa machoni pangu,

nami kwa kuwa ninakupenda,

nitatoa watu badala yako

na mataifa badala ya maisha yako.

5 Usiogope, kwa kuwa mimi nipo pamoja nawe,

nitawaleta watoto wako kutoka mashariki,

na kukukusanya kutoka magharibi.

6 Nitaiambia kaskazini, ‘Watoe!’

nayo kusini, ‘Usiwazuie.’

Walete wana wangu kutoka mbali,

na binti zangu kutoka miisho ya dunia:

7 kila mmoja ambaye ameitwa kwa Jina langu,

niliyemuumba kwa utukufu wangu,

niliyemhuluku na kumfanya.”

8 Uwaongoze wale wenye macho lakini hawaoni,

wenye masikio lakini hawasikii.

9 Mataifa yote yanakutanika pamoja,

na makabila yanakusanyika.

Ni nani miongoni mwao aliyetangulia kutuambia haya,

na kututangazia mambo yaliyopita?

Walete mashahidi wao ili kuwathibitisha kuwa walikuwa sahihi,

ili wengine waweze kusikia, waseme, “Ni kweli.”

10 “Ninyi ni mashahidi wangu,” asemaBwana,

“na mtumishi wangu niliyemchagua,

ili mpate kunijua na kuniamini,

na kutambua kwamba Mimi ndiye.

Kabla yangu hakuna mungu aliyefanyizwa,

wala hatakuwepo mwingine baada yangu.

11 Mimi, naam mimi, ndimiBwana,

zaidi yangu hakuna mwokozi.

12 Nimedhihirisha, kuokoa na kutangaza:

Mimi, wala si mungu mgeni katikati yenu.

Ninyi ni mashahidi wangu,” asemaBwana,

“kwamba Mimi ndimi Mungu.

13 Naam, tangu siku za kale, Mimi ndiye.

Hakuna hata mmoja awezaye kuokoa

kutoka mkononi wangu.

Mimi ninapotenda,

ni nani awezaye kutangua?”

Huruma Za Mungu, Na Kukosa Uaminifu Kwa Israeli

14 Hili ndiloBwanaasemalo,

Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli:

“Kwa ajili yenu nitatumana Babeli

na kuwaleta Wakaldayo wote kama wakimbizi,

katika meli walizozionea fahari.

15 Mimi ndimiBwana, yeye Aliye Mtakatifu wako,

Muumba wa Israeli, Mfalme wako.”

16 Hili ndilo asemaloBwana,

yeye aliyefanya njia baharini,

mahali pa kupita kwenye maji mengi,

17 aliyeyakokota magari ya vita na farasi,

jeshi pamoja na askari wa msaada,

nao wakalala huko, wala hawatainuka tena kamwe,

wakakomeshwa, na wakazimika kama utambi:

18 “Msiyakumbuke mambo yaliyopita,

wala msiyatafakari mambo ya zamani.

19 Tazama, nitafanya jambo jipya!

Sasa litachipuka, je, hamtalitambua?

Nitafanya njia jangwani

na vijito vya maji katika nchi kame.

20 Wanyama wa mwituni wataniheshimu,

mbweha na bundi,

kwa sababu ninawapatia maji jangwani,

na vijito katika nchi kame,

ili kuwapa watu wangu maji, wale niliowachagua,

21 watu wale niliowaumba kwa ajili yangu,

ili wapate kutangaza sifa zangu.

22 “Hata hivyo hukuniita mimi, ee Yakobo,

hujajitaabisha kwa ajili yangu, ee Israeli.

23 Hujaniletea kondoo kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa,

wala kuniheshimu kwa dhabihu zako.

Sikukulemea kwa sadaka za nafaka

wala kukuchosha kwa kuhitaji uvumba.

24 Hukuninunulia uvumba wowote wenye manukato,

wala hukunipa kwa ukarimu

mafuta ya wanyama wa dhabihu zako.

Lakini umenilemea kwa dhambi zako,

na kunitaabisha kwa makosa yako.

25 “Mimi, naam mimi, ndimi nizifutaye dhambi zako,

kwa ajili yangu mwenyewe,

wala sizikumbuki dhambi zako tena.

26 Tafakari mambo yaliyopita,

njoo na tuhojiane,

leta shauri lako uweze kupewa haki yako.

27 Baba yako wa kwanza alitenda dhambi,

wasemaji wako wameasi dhidi yangu.

28 Kwa hiyo nitawaaibisha wakuu wa Hekalu lako,

nami nitamtoa Yakobo aangamizwe,

na Israeli adhihakiwe.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/43-9fe976cb0192986d267c1965feb29cf4.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 44

Israeli Aliyechaguliwa

1 “Lakini sasa sikiliza, ee Yakobo, mtumishi wangu,

Israeli, niliyemchagua.

2 Hili ndilo asemaloBwana,

yeye aliyekuhuluku, aliyekuumba tumboni,

yeye atakayekusaidia:

Usiogope, ee Yakobo, mtumishi wangu,

Yeshuruni,niliyekuchagua.

3 Kwa maana nitamimina maji juu ya nchi yenye kiu,

na vijito vya maji juu ya ardhi iliyokauka;

nitamimina Roho wangu juu ya watoto wako,

nayo baraka yangu juu ya wazao wako.

4 Nao watachipua kama manyasi katika shamba la majani,

kama mierezi kando ya vijito vya maji yatiririkayo.

5 Mmoja atasema, ‘Mimi ni waBwana’;

mwingine atajiita kwa jina la Yakobo;

vilevile mwingine ataandika juu ya mkono wake, ‘WaBwana,’

na kujiita kwa jina la Israeli.

Ni Bwana, Siyo Sanamu

6 “Hili ndilo asemaloBwana,

Mfalme wa Israeli na Mkombozi,

BwanaMwenye Nguvu Zote:

Mimi ni wa kwanza na Mimi ni wa mwisho;

zaidi yangu hakuna Mungu.

7 Ni nani basi aliye kama mimi? Yeye na atangaze.

Yeye atangaze na kuweka mbele yangu

ni kitu gani kilichotokea tangu nilipoumba watu wangu wa kale,

tena ni nini kitakachotokea:

naam, yeye na atoe unabii ni nini kitakachokuja.

8 Msitetemeke, msiogope.

Je, sikutangaza hili, na kutoa unabii tangu zamani?

Ninyi ni mashahidi wangu.

Je, yuko Mungu zaidi yangu mimi?

Hasha, hakuna Mwamba mwingine;

mimi simjui mwingine.”

9 Wote wachongao sanamu ni ubatili,

navyo vitu wanavyovithamini havifai kitu.

Wale ambao wanazitetea ni vipofu,

ni wajinga, nao waaibika.

10 Ni nani atengenezaye mungu na kusubu sanamu,

ambayo haiwezi kumfaidia kitu chochote?

11 Yeye pamoja na wenziwe wa aina yake wataaibishwa,

mafundi wao si kitu ila ni wanadamu tu.

Wote wakusanyike pamoja na kuwa na msimamo wao,

watashushwa chini kwa hofu na kwa fedheha.

12 Muhunzi huchukua kifaa

na kukifanyia kazi kwenye makaa ya moto,

hutengeneza sanamu kwa nyundo,

huifanyiza kwa nguvu za mkono wake.

Huona njaa na kupoteza nguvu zake,

asipokunywa maji huzimia.

13 Seremala hupima kwa kutumia kamba

na huuchora mstari kwa kalamu;

huchonga kwa patasi

na kutia alama kwa bikari.

Huifanyiza katika umbo la binadamu,

la mwanadamu katika utukufu wake wote,

ili iweze kukaa katika sehemu yake ya ibada ya miungu.

14 Hukata miti ya mierezi,

huchukua mtiriza au mwaloni.

Huuacha ukue miongoni mwa miti ya msituni,

au hupanda msunobari, nayo mvua huufanya ukue.

15 Ni kuni ya binadamu:

yeye huchukua baadhi yake na kuota moto,

huwasha moto na kuoka mkate.

Lakini pia huutumia kumtengeneza mungu na akamwabudu,

huitengeneza sanamu na kuisujudia.

16 Sehemu ya kuni huziweka motoni,

akapikia chakula chake,

hubanika nyama na kula hadi ashibe.

Huota moto na kusema,

“Aha! Ninahisi joto, ninaona moto.”

17 Mabaki yake hutengeneza mungu, sanamu yake;

yeye huisujudia na kuiabudu.

Huiomba na kusema,

“Niokoe; wewe ni mungu wangu.”

18 Hawajui chochote, hawaelewi chochote,

macho yao yamefungwa hata hawawezi kuona,

akili zao zimefungwa hata hawawezi kufahamu.

19 Hakuna anayefikiri,

hakuna mwenye maarifa wala ufahamu wa kusema,

“Sehemu yake nilitumia kwa kuni;

hata pia nilioka mkate juu ya makaa yake,

nikabanika nyama na kuila.

Je, nifanye machukizo kwa kile kilichobaki?

Je, nisujudie gogo la mti?”

20 Hujilisha kwa majivu, moyo uliodanganyika humpotosha;

hawezi kujiokoa mwenyewe, au kusema,

“Je, kitu hiki kilichoko katika mkono wangu wa kuume si ni uongo?”

21 “Ee Yakobo, kumbuka mambo haya,

ee Israeli, kwa kuwa wewe ni mtumishi wangu.

Nimekuumba wewe, wewe ni mtumishi wangu.

Ee Israeli, sitakusahau.

22 Nimeyafuta makosa yako kama wingu,

dhambi zako kama ukungu wa asubuhi.

Nirudie mimi,

kwa kuwa nimekukomboa wewe.”

23 Enyi mbingu, imbeni kwa furaha,

kwa maanaBwanaamefanya jambo hili.

Ee vilindi vya dunia, piga kelele.

Enyi milima, pazeni sauti kwa nyimbo,

enyi misitu na miti yenu yote,

kwa maanaBwanaamemkomboa Yakobo,

ameuonyesha utukufu wake katika Israeli.

Yerusalemu Kukaliwa

24 “Hili ndilo asemaloBwana,

Mkombozi wako, aliyekuumba tumboni:

“Mimi niBwana,

niliyeumba vitu vyote,

niliyezitanda mbingu peke yangu,

niliyeitandaza nchi mwenyewe,

25 “mimi huzipinga ishara za manabii wa uongo,

na kuwatia upumbavu waaguzi,

niyapinduaye maarifa ya wenye hekima,

na kuyafanya kuwa upuzi,

26 niyathibitishaye maneno ya watumishi wake,

na kutimiza utabiri wa wajumbe wake,

“niambiaye Yerusalemu, ‘Itakaliwa na watu,’

niambiaye miji ya Yuda kuwa, ‘Itajengwa,’

na kuhusu magofu yake, ‘Mimi nitayatengeneza,’

27 niambiaye kilindi cha maji, ‘Kauka,

nami nitakausha vijito vyako,’

28 nisemaye kuhusu Koreshi, ‘Yeye ni mchungaji wangu,

naye atatimiza yote yanipendezayo;

atauambia Yerusalemu, “Ukajengwe tena,”

na kuhusu Hekalu, “Misingi yake na iwekwe.” ’

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/44-b52439c0d00bf031343b941f4d9a938c.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 45

Koreshi Chombo Cha Mungu

1 “Hili ndilo asemaloBwanakwa mpakwa mafuta wake,

Koreshi, ambaye nimemshika mkono wake wa kuume

kutiisha mataifa mbele yake

na kuwavua wafalme silaha zao,

kufungua milango mbele yake

ili malango yasije yakafungwa:

2 Nitakwenda mbele yako

na kusawazisha milima;

nitavunjavunja malango ya shaba

na kukatakata mapingo ya chuma.

3 Nitakupa hazina za gizani,

mali zilizofichwa mahali pa siri,

ili upate kujua ya kwamba Mimi ndimiBwana,

Mungu wa Israeli, akuitaye kwa jina lako.

4 Kwa ajili ya Yakobo mtumishi wangu,

Israeli niliyemchagua,

nimekuita wewe kwa jina lako,

na kukupa jina la heshima,

ingawa wewe hunitambui.

5 Mimi ndimiBwana, wala hakuna mwingine,

zaidi yangu hakuna Mungu.

Nitakutia nguvu,

ingawa wewe hujanitambua,

6 ili kutoka mawio ya jua

mpaka machweo yake,

watu wapate kujua kwamba hakuna Mungu mwingine ila Mimi.

Mimi ndimiBwanawala hakuna mwingine.

7 Mimi ninaumba nuru na kuhuluku giza,

ninaleta mafanikio na kusababisha maafa.

Mimi,Bwana, huyatenda haya yote.

8 “Enyi mbingu juu, nyesheni haki,

mawingu na yaidondoshe.

Dunia na ifunguke sana,

wokovu na uchipuke,

haki na ikue pamoja nao.

Mimi,Bwana, ndiye niliyeiumba.

9 “Ole wake yeye ashindanaye na Muumba wake,

yeye ambaye ni kigae tu kati ya vigae juu ya ardhi.

Je, udongo wa kufinyangia humwambia mfinyanzi,

‘Unatengeneza nini wewe?’

Je, kazi yako husema,

‘Hana mikono’?

10 Ole wake amwambiaye baba yake,

‘Umezaa nini?’

Au kumwambia mama yake,

‘Umezaa kitu gani?’

11 “Hili ndilo asemaloBwana,

yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli na Muumba wake:

Kuhusu mambo yatakayokuja,

je, unaniuliza habari za watoto wangu,

au kunipa amri kuhusu kazi za mikono yangu?

12 Mimi ndiye niliyeumba dunia

na kumuumba mwanadamu juu yake.

Mikono yangu mwenyewe ndiyo iliyozitanda mbingu,

nikayapanga majeshi yake yote ya angani.

13 Mimi nitamwinua Koreshi katika haki yangu:

nitazinyoosha njia zake zote.

Yeye atajenga mji wangu upya,

na kuwaweka huru watu wangu walio uhamishoni,

lakini si kwa kulipiwa fedha wala kupewa zawadi,

asemaBwanaMwenye Nguvu Zote.”

14 Hili ndilo asemaloBwana:

“Mazao ya Misri na bidhaa za Kushi,

nao wale Waseba warefu,

watakujia na kuwa wako,

watakujia wakijikokota nyuma yako,

watakujia wamefungwa minyororo.

Watasujudu mbele yako

wakikusihi na kusema,

‘Hakika Mungu yu pamoja nawe,

wala hakuna mwingine;

hakuna Mungu mwingine.’ ”

15 Hakika wewe u Mungu unayejificha,

Ee Mungu na Mwokozi wa Israeli.

16 Wote watengenezao sanamu wataaibika na kutahayarika;

wataenda kutahayarika pamoja.

17 Lakini Israeli ataokolewa naBwana

kwa wokovu wa milele;

kamwe hutaaibika wala kutatahayarika,

milele yote.

18 Kwa kuwa hili ndilo asemaloBwana,

yeye aliyeumba mbingu,

ndiye Mungu;

yeye aliyeifanya dunia na kuiumba,

yeye ndiye aliiwekea misingi imara,

hakuiumba ili iwe tupu,

bali aliiumba ikaliwe na viumbe vyake.

Anasema:

“Mimi ndimiBwana,

wala hakuna mwingine.

19 Sijasema sirini,

kutoka mahali fulani katika nchi ya giza;

sijawaambia wazao wa Yakobo,

‘Nitafuteni bure.’

Mimi,Bwana, nasema kweli;

ninatangaza lililo sahihi.

20 “Kusanyikeni pamoja mje,

enyi wakimbizi kutoka mataifa.

Wale wabebao sanamu za mti ni watu wasio na akili,

wale waombao miungu isiyoweza kuokoa.

21 Tangazeni litakalokuwepo, lisemeni hilo,

wao na wafanye shauri pamoja.

Ni nani aliyetangulia kusema hili tangu zamani,

aliyetangaza tangu zamani za kale?

Je, haikuwa Mimi,Bwana?

Wala hapana Mungu mwingine

zaidi yangu mimi,

Mungu mwenye haki na Mwokozi;

hapana mwingine ila mimi.

22 “Nigeukieni mimi, nanyi mkaokolewe,

enyi miisho yote ya dunia;

kwa maana mimi ndimi Mungu,

wala hapana mwingine.

23 Nimeapa kwa nafsi yangu,

kinywa changu kimenena katika uadilifu wote

neno ambalo halitatanguka:

Kila goti litapigwa mbele zangu,

kwangu mimi kila ulimi utaapa.

24 Watasema kuhusu mimi,

‘KatikaBwanapeke yake

ndiko kuna haki na nguvu.’ ”

Wote ambao wamemkasirikia Mungu

watamjia yeye, nao watatahayarika.

25 Lakini katikaBwanawazao wote wa Israeli

wataonekana wenye haki na watashangilia.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/45-b9b962d8a5efc8e5b8c2437ec3e2c6a4.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 46

Miungu Ya Babeli

1 Beli anasujudu hadi nchi, Nebo anainama;

sanamu zao zabebwa na wanyama wa mizigo.

Vinyago hivi mnavyobeba kila mahali ni mzigo wa kulemea,

mzigo kwa waliochoka.

2 Vinyago pamoja na wale wanaovibeba wanainama chini;

hiyo miungu haiwezi kuwaokoa watu,

wote wanakwenda utumwani pamoja.

3 “Nisikilizeni mimi, ee nyumba ya Yakobo,

ninyi nyote mliobaki wa nyumba ya Israeli,

ninyi ambao nimewategemeza tangu mlipotungwa mimba,

nami nimewabeba tangu kuzaliwa kwenu.

4 Hata mpaka wakati wa uzee wenu na mvi, Mimi ndiye,

Mimi ndiye nitakayewasaidia ninyi.

Nimewahuluku, nami nitawabeba,

nitawasaidia ninyi na kuwaokoa.

5 “Mtanilinganisha na nani, au mtanihesabu kuwa sawa na nani?

Ni nani mtakayenifananisha naye ili tuweze kulinganishwa?

6 Wengine humwaga dhahabu kutoka kwenye mifuko yao,

na kupima fedha kwenye mizani;

huajiri mfua dhahabu kutengeneza mungu,

kisha huisujudia na kuiabudu.

7 Huiinua mabegani na kuichukua;

huiweka mahali pake, papo hapo ndipo isimamapo.

Wala haiwezi kusogea kutoka mahali pale.

Ingawa mtu huililia, haimjibu;

haiwezi kumwokoa kwenye taabu zake.

8 “Kumbukeni hili, litieni akilini,

liwekeni moyoni, enyi waasi.

9 Kumbukeni mambo yaliyopita, yale ya zamani za kale;

mimi ndimi Mungu, wala hakuna mwingine;

mimi ndimi Mungu,

wala hakuna mwingine aliye kama mimi.

10 Ni mimi nitangazaye mwisho tangu mwanzo,

naam, tangu zamani za kale,

mambo ambayo hayajatendeka.

Ninasema: Kusudi langu ndilo litakalosimama,

nami nitatenda mapenzi yangu yote.

11 Kutoka mashariki ninaita ndege awindaye;

kutoka nchi ya mbali,

mtu atakayetimiza kusudi langu.

Lile ambalo nimelisema, ndilo nitakalolitimiza;

lile nililolipanga, ndilo nitakalolitenda.

12 Nisikilizeni, ninyi wenye mioyo migumu,

ninyi mlio mbali na haki.

13 Ninaleta haki yangu karibu,

haiko mbali;

wala wokovu wangu hautachelewa.

Nitawapa Sayuni wokovu,

Israeli utukufu wangu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/46-eac1d24dd960b072cef119ad4ac2543f.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 47

Anguko La Babeli

1 “Shuka uketi mavumbini,

ee Bikira Binti Babeli;

keti chini pasipo na kiti cha enzi,

ee binti wa Wakaldayo.

Hutaitwa tena mwororo wala wa kupendeza.

2 Chukua mawe ya kusagia, usage unga,

vua shela yako.

Pandisha mavazi yako, ondoa viatu vyako,

vuka vijito kwa shida.

3 Uchi wako utafunuliwa

na aibu yako itaonekana.

Nitalipa kisasi;

sitamhurumia hata mmoja.”

4 Mkombozi wetu:BwanaMwenye Nguvu Zote ndilo jina lake;

ndiye yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.

5 “Keti kimya, ingia gizani,

Binti wa Wakaldayo,

hutaitwa tena malkia wa falme.

6 Niliwakasirikia watu wangu

na kuaibisha urithi wangu;

niliwatia mikononi mwako,

nawe hukuwaonea huruma.

Hata juu ya wazee

uliweka nira nzito sana.

7 Ukasema, ‘Nitaendelea

kuwa malkia milele!’

Lakini hukutafakari mambo haya

wala hukuwaza juu ya kile kingeweza kutokea.

8 “Sasa basi, sikiliza, ewe kiumbe mpenda anasa,

ukaaye mahali pako pa salama,

na kujiambia mwenyewe,

‘Mimi ndiye, wala hakuna mwingine zaidi yangu.

Kamwe sitakuwa mjane,

wala sitafiwa na watoto.’

9 Haya mawili yatakupata, kufumba na kufumbua,

katika siku moja:

kufiwa na watoto, na ujane.

Yote yatakupata kwa kipimo kikamilifu,

ijapokuwa uchawi wako ni mwingi,

na uaguzi wako ni mwingi.

10 Umeutegemea uovu wako,

nawe umesema, ‘Hakuna yeyote anionaye.’

Hekima yako na maarifa yako vinakupoteza

unapojiambia mwenyewe,

‘Mimi ndiye, wala hakuna mwingine zaidi yangu.’

11 Maafa yatakujia,

nawe hutaweza kuyaondoa kwa uaguzi.

Janga litakuangukia,

wala hutaweza kulikinga kwa fidia;

msiba mkuu usioweza kuutabiri

utakujia ghafula.

12 “Endelea basi na uaguzi wako,

na wingi wa uchawi wako,

ambao umeutumikia tangu utoto wako.

Labda utafanikiwa,

labda unaweza ukasababisha hofu kuu.

13 Ushauri wote uliopokea umekuchosha bure!

Wanajimu wako na waje mbele,

wale watazama nyota watabiriao mwezi baada ya mwezi,

wao na wawaokoe na lile linalokuja juu yenu.

14 Hakika wako kama mabua makavu;

moto utawateketeza.

Hawawezi hata kujiokoa wao wenyewe

kutokana na nguvu za mwali wa moto.

Hapa hakuna makaa ya kumtia mtu yeyote joto;

hapa hakuna moto wa kuota.

15 Hayo ndiyo yote wanayoweza kuwatendea ninyi,

hawa ambao umetaabika nao

na kufanya nao biashara tangu utoto.

Kila mmoja atatoroka;

hakuna yeyote awezaye kukuokoa.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/47-c3e227e8184bc18015f56aa605c72ec6.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 48

Israeli Mkaidi

1 “Sikilizeni hili, ee nyumba ya Yakobo,

ninyi mnaoitwa kwa jina la Israeli,

na mnaotoka katika ukoo wa Yuda,

ninyi mnaoapa kwa jina laBwana,

mnaomwomba Mungu wa Israeli,

lakini si katika kweli au kwa haki;

2 ninyi mnaojiita raiya wa mji mtakatifu,

na kumtegemea Mungu wa Israeli,

BwanaMwenye Nguvu Zote ndilo jina lake:

3 Nilitoa unabii mambo ya kwanza tangu zamani,

kinywa changu kiliyatangaza na kuyafanya yajulikane;

kisha ghafula nikayatenda, nayo yakatokea.

4 Kwa kuwa nalijua jinsi ulivyokuwa mkaidi;

mishipa ya shingo yako ilikuwa chuma,

kipaji chako cha uso kilikuwa shaba.

5 Kwa hiyo nilikuambia mambo haya tangu zamani,

kabla hayajatokea nilikutangazia

ili usije ukasema,

‘Sanamu zangu zilifanya hayo;

kinyago changu cha mti na mungu wangu wa chuma aliyaamuru.’

6 Umesikia mambo haya; yaangalie hayo yote.

Je, hutayakubali?

“Kuanzia sasa na kuendelea nitakueleza mambo mapya,

juu ya mambo yaliyofichika usiyoyajua.

7 Yameumbwa sasa, wala si tangu zamani;

hukupata kuyasikia kabla ya siku ya leo.

Hivyo huwezi kusema,

‘Naam, niliyajua hayo.’

8 Hujayasikia wala kuyaelewa,

tangu zamani sikio lako halikufunguka.

Ninafahamu vyema jinsi ulivyo mdanganyifu,

uliitwa mwasi tangu kuzaliwa kwako.

9 Kwa ajili ya Jina langu mwenyewe

ninaichelewesha ghadhabu yangu,

kwa ajili ya sifa zangu nimeizuia isikupate,

ili nisije nikakukatilia mbali.

10 Tazama, nimekusafisha, ingawa si kama fedha,

nimekujaribu katika tanuru ya mateso.

11 Kwa ajili yangu mwenyewe,

kwa ajili yangu mwenyewe, nafanya hili.

Jinsi gani niliache Jina langu lichafuliwe?

Sitautoa utukufu wangu kwa mwingine.

Israeli Anawekwa Huru

12 “Ee Yakobo, nisikilize mimi,

Israeli, ambaye nimekuita:

Mimi ndiye;

mimi ndimi mwanzo na mwisho.

13 Mkono wangu mwenyewe uliweka misingi ya dunia,

nao mkono wangu wa kuume umezitanda mbingu;

niziitapo, zote husimama pamoja.

14 “Kusanyikeni, ninyi nyote, msikilize:

Ni ipi miongoni mwa hizo sanamu

ambayo imetabiri vitu hivi?

Watu waBwanawaliochaguliwa na kuungana

watatimiza kusudi lake dhidi ya Babeli;

mkono wa Mungu utakuwa dhidi ya Wakaldayo.

15 Mimi, naam, Mimi, nimenena;

naam, nimemwita yeye.

Nitamleta,

naye atafanikiwa katika lile nililomtuma.

16 “Nikaribieni na msikilize hili:

“Tangu tangazo la kwanza sikusema kwa siri;

wakati litokeapo, nitakuwako hapo.”

SasaBwanaMwenyezi amenituma,

kwa Roho wake.

17 Hili ndilo asemaloBwana,

Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli:

“Mimi niBwana, Mungu wako,

nikufundishaye ili upate faida,

nikuongozaye katika njia ikupasayo kuiendea.

18 Laiti ungesikiliza kwa makini maagizo yangu,

amani yako ingekuwa kama mto,

haki yako kama mawimbi ya bahari.

19 Wazao wako wangekuwa kama mchanga,

watoto wako kama chembe zake zisizohesabika;

kamwe jina lao lisingefutiliwa mbali,

wala kuangamizwa kutoka mbele zangu.”

20 Tokeni huko Babeli,

kimbieni kutoka kwa Wakaldayo!

Tangazeni hili kwa kelele za shangwe

na kulihubiri.

Lipelekeni mpaka miisho ya dunia;

semeni, “Bwanaamemkomboa

mtumishi wake Yakobo.”

21 Hawakuona kiu alipowaongoza kupita jangwani;

alifanya maji yatiririke kutoka kwenye mwamba kwa ajili yao;

akapasua mwamba

na maji yakatoka kwa nguvu.

22 “Hakuna amani kwa waovu,” asemaBwana.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/48-ef9faba49d1e960ff4a6402c1f9b7397.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 49

Mtumishi Wa Bwana

1 Nisikilizeni, enyi visiwa, sikieni hili,

ninyi mataifa mlio mbali:

Kabla sijazaliwa,Bwanaaliniita,

tangu kuzaliwa kwangu, amelitaja jina langu.

2 Akafanya kinywa changu kuwa kama upanga ulionolewa,

katika uvuli wa mkono wake akanificha;

akanifanya kuwa mshale uliosuguliwa,

na kunificha katika podo lake.

3 Akaniambia, “Wewe u mtumishi wangu,

Israeli, ambaye katika yeye

nitaonyesha utukufu wangu.”

4 Lakini nilisema, “Nimetumika bure,

nimetumia nguvu zangu bure bila faida.

Hata hivyo linalonistahili liko mkononi mwaBwana,

nao ujira wangu uko kwa Mungu wangu.”

5 SasaBwanaasema:

yeye aliyeniumba tumboni kuwa mtumishi wake,

kumrudisha tena Yakobo kwake

na kumkusanyia Israeli,

kwa maana nimepata heshima machoni paBwana,

naye Mungu wangu amekuwa nguvu yangu;

6 yeye asema:

“Je, ni jambo dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu

ili kurejeza makabila ya Yakobo,

na kuwarudisha wale Waisraeli niliowahifadhi?

Pia nitakufanya uwe nuru kwa ajili ya watu wa Mataifa,

ili upate kuleta wokovu wangu hata miisho ya dunia.”

7 Hili ndilo asemaloBwana,

yeye Mkombozi na Aliye Mtakatifu wa Israeli,

kwake yeye aliyedharauliwa na kuchukiwa na taifa,

kwa mtumishi wa watawala:

“Wafalme watakuona na kusimama,

wakuu wataona na kuanguka kifudifudi,

kwa sababu yaBwana, aliye mwaminifu,

yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, aliyekuchagua wewe.”

Kurejezwa Kwa Israeli

8 Hili ndilo asemaloBwana:

“Wakati wangu uliokubalika nitakujibu,

nami katika siku ya wokovu nitakusaidia;

nitakuhifadhi, nami nitakufanya

kuwa agano kwa ajili ya watu,

ili kurudisha nchi

na kugawanyia urithi tena wale waliokuwa ukiwa,

9 kuwaambia mateka, ‘Tokeni nje,’

nao wale walio gizani, ‘Kuweni huru!’

“Watajilisha kando ya barabara

na kupata malisho yao juu ya kila kilima kilicho kitupu.

10 Hawataona njaa wala kuona kiu,

wala hari ya jangwani au jua halitawapiga.

Yeye mwenye huruma juu yao atawaonyesha njia,

na kuwaongoza kando ya chemchemi za maji.

11 Nitaifanya milima yangu yote kuwa barabara,

na njia kuu zangu zitainuliwa.

12 Tazama, watakuja kutoka mbali:

wengine kutoka kaskazini, wengine kutoka magharibi,

wengine kutoka nchi ya Sinimu.”

13 Pigeni kelele kwa furaha, enyi mbingu;

furahi, ee dunia;

pazeni sauti kwa kuimba, enyi milima!

Kwa maanaBwanaanawafariji watu wake,

naye atakuwa na huruma kwa watu wake walioumizwa.

14 Lakini Sayuni alisema, “Bwanaameniacha,

Bwana amenisahau.”

15 “Je, mama aweza kumsahau mtoto

aliyeko matitini mwake akinyonya,

wala asiwe na huruma

juu ya mtoto aliyemzaa?

Ingawa anaweza kusahau,

mimi sitakusahau wewe!

16 Tazama, nimekuchora kama muhuri

katika vitanga vya mikono yangu,

kuta zako zi mbele yangu daima.

17 Wana wako wanaharakisha kurudi,

nao wale waliokuteka wanaondoka kwako.

18 Inua macho yako ukatazame pande zote:

wana wako wote wanakusanyika na kukujia.

Kwa hakika kama vile niishivyo,

utawavaa wote kama mapambo,

na kujifunga nao kama bibi arusi,”

asemaBwana.

19 “Ingawa uliangamizwa na kufanywa ukiwa,

na nchi yako ikaharibiwa,

sasa nafasi itakuwa finyu kwa ajili ya watu wako,

nao wale waliokuangamiza watakuwa mbali sana.

20 Watoto waliozaliwa wakati wa msiba wako

bado watakuambia,

‘Mahali hapa ni finyu sana kwetu,

tupe eneo kubwa zaidi la kuishi.’

21 Ndipo utasema moyoni mwako,

‘Ni nani aliyenizalia hawa?

Nilikuwa nimefiwa, tena tasa;

nilikuwa nimehamishwa na kukataliwa.

Ni nani aliyewalea hawa?

Niliachwa peke yangu,

lakini hawa wametoka wapi?’ ”

22 Hili ndilo asemaloBwanaMwenyezi:

“Tazama, nitawaashiria watu wa Mataifa,

nitainua bendera yangu kwa mataifa;

watawaleta wana wako mikononi yao,

na kuwabeba binti zenu juu ya mabega yao.

23 Wafalme watakuwa baba zenu wa kuwalea,

na malkia wao watakuwa mama zenu wa kuwalea.

Watasujudu mbele yako nyuso zao zikigusa ardhi;

wataramba mavumbi yaliyo miguuni mwako.

Ndipo utajua ya kuwa Mimi ndimiBwana;

wale wanaonitumaini mimi hawataaibika.”

24 Je, nyara zaweza kuchukuliwa kutoka kwa mashujaa wa vita,

au mateka kuokolewa kutoka kwa watu wakali?

25 Lakini hili ndilo asemaloBwana:

“Naam, mateka watachukuliwa kutoka kwa mashujaa,

na nyara zitapokonywa kutoka kwa watu wakali.

Nitashindana na wale wanaoshindana nawe,

nami nitawaokoa watoto wako.

26 Nitawafanya wale wanaokuonea kula nyama yao wenyewe,

watalewa kwa damu yao wenyewe,

kama vile kwa mvinyo.

Ndipo wanadamu wote watajua

ya kuwa Mimi,Bwana, ni Mwokozi wako,

Mkombozi wako, niliye Mwenye Nguvu wa Yakobo.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/49-3756dc0655b9545f1a78eec34c6ba2cd.mp3?version_id=1627—