Categories
Isaya

Isaya 20

Unabii Dhidi Ya Misri Na Kushi

1 Katika mwaka ule ambao jemadari mkuu alitumwa na Mfalme Sargoni wa Ashuru, naye akaja mpaka Ashdodi, akaushambulia na kuuteka,

2 wakati uleBwanaalisema kwa kinywa cha Isaya mwana wa Amozi. Akamwambia, “Vua nguo ya gunia kutoka mwilini mwako na viatu kutoka miguuni mwako.” Naye akafanya hivyo, akatembea huku na huko uchi, bila viatu.

3 KishaBwanaakasema, “Kama vile mtumishi wangu Isaya alivyotembea uchi na bila viatu kwa miaka mitatu, kama ishara na dalili mbaya dhidi ya nchi ya Misri na Kushi,

4 vivyo hivyo mfalme wa Ashuru atawaongoza mateka wa Wamisri, na watu wa uhamisho wa Kushi, uchi na bila viatu, vijana hata wazee, wakiwa matako wazi, kwa aibu ya Wamisri.

5 Wale waliotegemea Kushi na kujivunia Misri wataogopa na kuaibika.

6 Katika siku ile watu wanaoishi katika pwani hii watasema, ‘Tazama lililowapata wale tuliowategemea, wale tuliowakimbilia kwa msaada na wokovu kutoka mikononi mwa mfalme wa Ashuru! Tutawezaje basi kupona?’ ”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/20-877f55b7e4e46243d495a2c18c32868d.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 21

Unabii Dhidi Ya Babeli

1 Neno kuhusu Jangwa kando ya Bahari:

Kama upepo wa kisulisuli unaopita katika nchi hadi kusini,

mshambuliaji anakuja kutoka jangwani,

kutoka nchi inayotisha.

2 Nimeonyeshwa maono ya kutisha:

Msaliti anasaliti, mteka nyara anateka nyara.

Elamu, shambulia! Umedi, izunguke kwa jeshi!

Nitakomesha huzuni zote alizosababisha.

3 Katika hili mwili wangu umeteswa na maumivu,

maumivu makali ya ghafula yamenishika,

kama yale ya mwanamke mwenye utungu wa kuzaa.

Nimeduwazwa na lile ninalolisikia,

nimeshangazwa na lile ninaloliona.

4 Moyo wangu unababaika,

woga unanifanya nitetemeke,

gizagiza la jioni nililolitamani sana,

limekuwa hofu kuu kwangu.

5 Wanaandaa meza,

wanatandaza mazulia,

wanakula, wanakunywa!

Amkeni, enyi maafisa,

zitieni ngao mafuta!

6 Hili ndilo Bwana analoniambia:

“Nenda, weka mlinzi,

na atoe taarifa ya kile anachokiona.

7 Anapoona magari ya vita

pamoja na kundi la farasi,

wapanda punda au wapanda ngamia,

na awe macho, awe macho kikamilifu.”

8 Naye mlinzi alipaza sauti,

“Mchana baada ya mchana, bwana wangu, ninasimama katika mnara wa ulinzi,

kila usiku ninakaa mahali pangu nilipoamriwa.

9 Tazama, yuaja mtu anayepanda gari la vita

pamoja na kundi la farasi.

Naye anajibu:

‘Babeli umeanguka, umeanguka!

Vinyago vyote vya miungu yake

vimelala chini vikiwa vimevunjwa!’ ”

10 Ee watu wangu, mliopondwa kwenye sakafu ya kupuria,

ninawaambia kile nilichokisikia

kutoka kwaBwanaMwenye Nguvu Zote,

kutoka kwa Mungu wa Israeli.

Unabii Dhidi Ya Edomu

11 Neno kuhusu Duma:

Mtu fulani ananiita kutoka Seiri,

“Mlinzi, usiku utaisha lini?

Mlinzi, usiku utaisha lini?”

12 Mlinzi anajibu,

“Asubuhi inakuja, lakini pia usiku.

Kama ungeliuliza, basi uliza;

bado na urudi tena.”

Unabii Dhidi Ya Arabia

13 Neno kuhusu Arabia:

Enyi misafara ya Wadedani,

mnaopiga kambi katika vichaka vya Arabia,

14 leteni maji kwa wenye kiu,

ninyi mnaoishi Tema,

leteni chakula kwa ajili ya wakimbizi.

15 Wanaukimbia upanga,

kutoka upanga uliochomolewa alani,

kutoka upinde uliopindwa,

na kutoka kwenye joto la vita.

16 Hili ndilo Bwana analoniambia: “Katika muda wa mwaka mmoja, kama vile mtumishi aliyefungwa na mkataba angeihesabu, majivuno yote ya Kedari yatafikia mwisho.

17 Wanaume wavutao pinde walionusurika, mashujaa wa Kedari, watakuwa wachache.”Bwana, Mungu wa Israeli, amesema.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/21-52a2530139a33f32d01ec23aad0d1ed7.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 22

Unabii Kuhusu Yerusalemu

1 Neno kuhusu Bonde la Maono:

Nini kinachokutaabisha sasa,

kwamba ninyi nyote mmepanda juu ya mapaa?

2 Ewe mji uliojaa ghasia,

ewe mji wa makelele na sherehe!

Watu wenu waliokufa hawakuuawa kwa upanga,

wala hawakufa vitani.

3 Viongozi wako wote wamekimbia pamoja,

wamekamatwa bila kutumia upinde.

Ninyi nyote mliokamatwa mlichukuliwa wafungwa pamoja,

mlikimbia wakati adui alipokuwa bado mbali.

4 Kwa hiyo nilisema, “Geukia mbali nami,

niache nilie kwa uchungu.

Usijaribu kunifariji

juu ya maangamizi ya watu wangu.”

5 Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote, anayo siku

ya ghasia, ya kukanyaga, na ya kuogofya

katika Bonde la Maono,

siku ya kuangusha kuta

na ya kupiga kelele mpaka milimani.

6 Elamu analichukua podo,

pamoja na waendesha magari ya vita na farasi.

Kiri anaifungua ngao.

7 Mabonde yako yaliyo mazuri sana yamejaa magari ya vita,

nao wapanda farasi wamewekwa kwenye malango ya mji;

8 ulinzi wa Yuda umeondolewa.

Nawe ulitazama siku ile

silaha katika Jumba la Kifalme la Mwituni,

9 mkaona kuwa Mji wa Daudi

una matundu mengi katika ulinzi wake,

mkaweka akiba ya maji

kwenye Bwawa la Chini.

10 Mlihesabu majengo katika Yerusalemu

nanyi mkabomoa nyumba ili kuimarisha ukuta.

11 Mlijenga bwawa la maji katikati ya kuta mbili

kwa ajili ya maji ya Bwawa la Zamani,

lakini hamkumtazama Yule aliyelitengeneza,

au kuwa na heshima kwa Yule aliyeubuni tangu zamani za kale.

12 Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote,

aliwaita siku ile

ili kulia na kuomboleza,

kungʼoa nywele zenu na kuvaa nguo ya gunia.

13 Lakini tazama, kuna furaha na sherehe,

kuchinja ngʼombe na kuchinja kondoo,

kula nyama na kunywa mvinyo!

Mnasema, “Tuleni na kunywa,

kwa kuwa kesho tutakufa!”

14 BwanaMwenye Nguvu Zote amelifunua hili nikiwa ninasikia: Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote, asema: “Mpaka siku ya kufa kwenu, dhambi hii haitafanyiwa upatanisho.”

15 Hili ndilo Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote, asemalo:

“Nenda ukamwambie huyu wakili Shebna,

ambaye ni msimamizi wa jumba la kifalme:

16 Unafanya nini hapa, na ni nani aliyekupa ruhusa

kujikatia kaburi lako mwenyewe,

ukichonga kaburi lako mahali palipo juu,

na kutoboa kwa patasi mahali pako pa kupumzikia katika mwamba?

17 “Jihadhari,Bwanayu karibu kukukamata thabiti,

na kukutupa mbali, ewe mtu mwenye nguvu.

18 Atakuvingirisha uwe kama mpira

na kukutupa katika nchi kubwa.

Huko ndiko utakakofia,

na huko ndiko magari yako ya vita ya fahari yatabakia,

wewe unayeifedhehesha nyumba ya bwana wako!

19 Nitakuondoa kutoka kazi yako,

nawe utaondoshwa kutoka nafasi yako.

20 “Katika siku ile, nitamwita mtumishi wangu, Eliakimu mwana wa Hilkia.

21 Nitamvika joho lako, nami nitamfunga mshipi wako kiunoni mwake, na kumkabidhi mamlaka yako. Yeye atakuwa baba kwa wale wanaoishi Yerusalemu na kwa nyumba ya Yuda.

22 Nitaweka mabegani mwake ufunguo wa nyumba ya Daudi. Kile afunguacho hakuna awezaye kufunga, na kile afungacho hakuna awezaye kufungua.

23 Nitamgongomea kama kigingi kilicho mahali palipo imara, naye atakuwa kiti cha enzi cha heshima kwa ajili ya nyumba ya baba yake.

24 Utukufu wote wa jamaa yake utakuwa juu yake: Watoto wa jamaa hiyo na machipukizi yake, vyombo vyake vyote vidogo, tangu bakuli hadi magudulia yote.”

25 BwanaMwenye Nguvu Zote asema, “Katika siku ile, kigingi kilichogongomewa mahali imara kitaachia njia. Kitakatwa, nacho kitaanguka na mzigo ulioningʼinia juu yake utaanguka chini.”Bwanaamesema.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/22-adb9150a718fe6572b0ba7194db44151.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 23

Unabii Kuhusu Tiro

1 Neno kuhusu Tiro:

Ombolezeni, enyi meli za Tarshishi!

Kwa kuwa Tiro imeangamizwa,

imeachwa bila nyumba wala bandari.

Kuanzia nchi ya Kitimu

neno limewajia.

2 Nyamazeni kimya, enyi watu wa kisiwani,

pia ninyi wafanyabiashara wa Sidoni,

ambao mabaharia wamewatajirisha.

3 Kwenye maji makuu

nafaka za Shihori zilikuja;

mavuno ya Naili yalikuwa mapato ya Tiro,

naye akawa soko la mataifa.

4 Uaibishwe ee Sidoni, nawe ee ngome la bahari,

kwa kuwa bahari imesema:

“Sijapata kuwa na uchungu wa kuzaa wala sijapata kuzaa,

wala sijapata kulea wana wala kutunza mabinti.”

5 Habari ifikapo Misri,

watakuwa katika maumivu makuu kwa ajili ya taarifa kutoka Tiro.

6 Vukeni mpaka Tarshishi,

ombolezeni, enyi watu wa kisiwani.

7 Je, huu ndio mji wenu uliojaa sherehe,

mji wa zamani, zamani kabisa

ambao miguu yake imeuchukua

kufanya makao nchi za mbali sana?

8 Ni nani amepanga hili dhidi ya Tiro,

mji utoao mataji,

ambao wafanyabiashara wake ni wana wa mfalme

na wachuuzi wake ni watu mashuhuri wa dunia?

9 BwanaMwenye Nguvu Zote ndiye alipanga jambo hili,

ili kukishusha kiburi cha utukufu wote

na kuwanyenyekesha wale wote

ambao ni mashuhuri duniani.

10 Ee Binti Tarshishi,

pita katika nchi yako kama vile Mto Naili

kwa kuwa huna tena bandari.

11 Bwanaamenyoosha mkono wake juu ya bahari

na kuzifanya falme zake zitetemeke.

Ametoa amri kuhusu Kanaani

kwamba ngome zake ziangamizwe.

12 Alisema, “Usizidi kufurahi,

ee Bikira Binti Sidoni, sasa umepondwa!

“Simama, vuka uende Kitimu;

hata huko hutapata pumziko.”

13 Tazama katika nchi ya Wakaldayo,

watu hawa ambao sasa hawaonekani kama wapo!

Waashuru wameifanya nchi hiyo

kuwa mahali pa viumbe wa jangwani.

Wamesimamisha minara yao ya vita kuuzunguka,

wameziteka ngome zake na kuziacha tupu

na kuufanya kuwa magofu.

14 Ombolezeni, enyi meli za Tarshishi;

ngome yenu imeangamizwa!

15 Wakati huo Tiro utasahauliwa kwa miaka sabini, muda wa maisha ya mfalme. Lakini mwisho wa miaka hiyo sabini, itakuwa kwa Tiro kama ilivyo katika wimbo wa kahaba:

16 “Twaa kinubi, tembea mjini kote,

ewe kahaba uliyesahauliwa;

piga kinubi vizuri, imba nyimbo nyingi,

ili upate kukumbukwa.”

17 Mwishoni mwa miaka sabini,Bwanaatashughulika na Tiro. Naye atarudia ajira yake ya ukahaba, na atafanya biashara yake na falme zote juu ya uso wa dunia.

18 Lakini faida na mapato yake yatawekwa wakfu kwaBwana; hayatahifadhiwa wala kufichwa. Faida zake zitakwenda kwa wale wakaao mbele zaBwanakwa ajili ya chakula tele na mavazi mazuri.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/23-000a34f833cc6a05893a007dcd8cc273.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 24

Dunia Kuharibiwa Upesi

1 Tazama,Bwanaataifanya dunia kuwa ukiwa

na kuiharibu,

naye atauharibu uso wake

na kutawanya wakaao ndani yake:

2 ndivyo itakavyokuwa

kwa makuhani na kwa watu,

kwa bwana na kwa mtumishi,

kwa bibi na kwa mtumishi wake wa kike,

kwa muuzaji na kwa mnunuzi,

kwa mkopaji na kwa mkopeshaji,

kwa mdaiwa na kwa mdai.

3 Dunia itaharibiwa kabisa

na kutekwa nyara kabisa.

Bwanaamesema neno hili.

4 Dunia inakauka na kunyauka,

dunia inanyongʼonyea na kunyauka,

waliotukuzwa wa dunia wananyongʼonyea.

5 Dunia imetiwa unajisi na watu wake;

wameacha kutii sheria,

wamevunja amri

na kuvunja agano la milele.

6 Kwa hiyo laana inaiteketeza dunia,

watu wake lazima waichukue hatia yao.

Kwa hiyo wakazi wa dunia wameteketezwa,

nao waliosalia ni wachache sana.

7 Divai mpya inakauka na mzabibu unanyauka,

watu wote wafurahishao wanalia kwa huzuni.

8 Furaha ya matoazi imekoma,

kelele za wenye furaha zimekoma,

shangwe za kinubi zimenyamaza.

9 Hawanywi tena mvinyo pamoja na wimbo,

kileo ni kichungu kwa wanywaji wake.

10 Mji ulioharibiwa umekuwa ukiwa,

mlango wa kila nyumba umefungwa.

11 Barabarani wanalilia kupata mvinyo,

furaha yote imegeuka kuwa majonzi,

furaha yote imefukuziwa mbali na dunia.

12 Mji umeachwa katika uharibifu,

lango lake limevunjwa vipande.

13 Ndivyo itakavyokuwa duniani

na miongoni mwa mataifa,

kama vile wakati mzeituni upigwavyo,

au kama vile wakati masazo yabakiavyo baada ya zabibu kuvunwa.

14 Wanainua sauti zao, wanapiga kelele kwa furaha,

kutoka magharibi wanasifu kwa ukelele utukufu waBwana.

15 Kwa hiyo upande wa mashariki mpeniBwanautukufu,

liadhimisheni jina laBwana, Mungu wa Israeli,

katika visiwa vya bahari.

16 Kutoka miisho ya dunia tunasikia uimbaji:

“Utukufu kwa Yule Mwenye Haki.”

Lakini nilisema, “Ninadhoofika, ninadhoofika!

Ole wangu!

Watenda hila wanasaliti!

Kwa hila watenda hila wanasaliti!”

17 Hofu, shimo na mtego vinakungojea,

ewe mtu ukaaye duniani.

18 Kila akimbiaye asikiapo sauti ya hofu

atatumbukia shimoni,

naye yeyote apandaye kutoka shimoni,

atanaswa kwenye mtego.

Malango ya gharika ya mbinguni yamefunguliwa,

misingi ya dunia inatikisika.

19 Dunia imepasuka,

dunia imechanika,

dunia imetikiswa kabisa.

20 Dunia inapepesuka kama mlevi,

inayumbayumba kama kibanda kwenye upepo;

imelemewa sana na mzigo wa hatia ya uasi wake

na ikianguka kamwe haitainuka tena.

21 Katika siku ileBwanaataadhibu

nguvu zilizoko mbinguni juu,

na wafalme walioko duniani chini.

22 Watakusanywa pamoja

kama wafungwa waliofungwa gerezani,

watafungiwa gerezani

na kuadhibiwa baada ya siku nyingi.

23 Mwezi utatiwa haya, nalo jua litaaibishwa;

kwa maanaBwanaMwenye Nguvu Zote atawala

juu ya Mlima Sayuni na katika Yerusalemu,

tena mbele ya wazee wake kwa utukufu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/24-8dc01515934c24aa4e99b6094af8ed27.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 25

Msifuni Bwana

1 EeBwana, wewe ni Mungu wangu,

nitakutukuza na kulisifu jina lako,

kwa maana katika ukamilifu wa uaminifu

umetenda mambo ya ajabu,

mambo yaliyokusudiwa tangu zamani.

2 Umeufanya mji kuwa lundo la kifusi,

mji wenye ngome kuwa magofu,

ngome imara ya wageni kuwa si mji tena,

wala hautajengwa tena kamwe.

3 Kwa hiyo mataifa yenye nguvu yatakuheshimu,

miji ya mataifa katili itakuheshimu wewe.

4 Umekuwa kimbilio la watu maskini,

kimbilio la mhitaji katika taabu yake,

hifadhi wakati wa dhoruba

na kivuli wakati wa hari.

Kwa maana pumzi ya wakatili

ni kama dhoruba ipigayo ukuta

5 na kama joto la jangwani.

Wewe wanyamazisha makelele ya wageni;

kama vile hari ipunguzwavyo na kivuli cha wingu,

ndivyo wimbo wa wakatili unyamazishwavyo.

6 Juu ya mlima huuBwanaMwenye Nguvu Zote ataandaa

karamu ya vinono kwa mataifa yote,

karamu ya mvinyo wa zamani,

nyama nzuri sana na divai zilizo bora sana.

7 Juu ya mlima huu ataharibu

sitara ihifadhiyo mataifa yote,

kile kifuniko kifunikacho mataifa yote,

8 yeye atameza mauti milele.

BwanaMwenyezi atafuta machozi katika nyuso zote;

ataondoa aibu ya watu wake duniani kote.

Bwanaamesema hili.

9 Katika siku ile watasema,

“Hakika huyu ndiye Mungu wetu;

tulimtumaini, naye akatuokoa.

Huyu ndiyeBwana, tuliyemtumaini;

sisi tushangilie na kufurahia katika wokovu wake.”

10 Mkono waBwanautatulia juu ya mlima huu,

bali Moabu atakanyagwa chini

kama majani makavu yakanyagwavyo kwenye shimo la mbolea.

11 Watakunjua mikono yao katikati yake,

kama vile mwogeleaji akunjuavyo mikono yake ili aogelee.

Mungu atashusha kiburi chao

licha ya ujanja wa mikono yao.

12 Atabomoa kuta ndefu za maboma yako

na kuziangusha chini,

atazishusha chini ardhini,

mpaka mavumbini kabisa.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/25-cd29ea3c711afef4cf9519ee40cb09d5.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 26

Wimbo Wa Ushindi

1 Katika siku ile, wimbo huu utaimbwa katika nchi ya Yuda:

Tuna mji ulio na nguvu,

Mungu huufanya wokovu kuwa kuta zake na maboma yake.

2 Fungua malango ili taifa lenye haki lipate kuingia,

taifa lile lidumishalo imani.

3 Utamlinda katika amani kamilifu

yeye ambaye moyo wake ni thabiti

kwa sababu anakutumaini wewe.

4 MtumainiBwanamilele,

kwa kuwaBwana,Bwana, ni Mwamba wa milele.

5 Huwashusha wale wajikwezao,

huushusha chini mji wenye kiburi,

huushusha hadi ardhini

na kuutupa chini mavumbini.

6 Miguu huukanyaga chini,

miguu ya hao walioonewa,

hatua za hao maskini.

7 Mapito ya wenye haki yamenyooka.

Ewe uliye Mwenye Haki,

waisawazisha njia ya mtu mnyofu.

8 Naam,Bwana, tukienenda katika sheria zako,

twakungojea wewe,

jina lako na sifa zako

ndizo shauku za mioyo yetu.

9 Nafsi yangu yakutamani wakati wa usiku,

wakati wa asubuhi roho yangu yakuonea shauku.

Wakati hukumu zako zinapokuja juu ya dunia,

watu wa ulimwengu hujifunza haki.

10 Ingawa neema yaonyeshwa kwa waovu,

hawajifunzi haki,

hata katika nchi ya unyofu huendelea kutenda mabaya

wala hawazingatii utukufu waBwana.

11 EeBwana, mkono wako umeinuliwa juu,

lakini hawauoni.

Wao na waone wivu wako kwa ajili ya watu wako tena waaibishwe,

moto uliowekwa akiba kwa ajili ya adui zako na uwateketeze.

12 Bwana, unaamuru amani kwa ajili yetu,

yale yote tuliyoweza kuyakamilisha ni wewe uliyetenda kwa ajili yetu.

13 EeBwana, Mungu wetu, mabwana wengine zaidi ya wewe wametutawala,

lakini jina lako pekee ndilo tunaloliheshimu.

14 Wao sasa wamekufa, wala hawako tena hai,

roho za waliokufa hazitarudi tena.

Uliwaadhibu na kuwaangamiza,

umefuta kumbukumbu lao lote.

15 Umeliongeza hilo taifa, EeBwana,

umeliongeza hilo taifa.

Umejipatia utukufu kwa ajili yako mwenyewe,

umepanua mipaka yote ya nchi.

16 Bwana, walikujia katika taabu yao,

wewe ulipowarudi,

waliweza kuomba kwa kunongʼona tu.

17 Kama mwanamke mwenye mimba aliyekaribia kuzaa

anavyogaagaa na kulia kwa ajili ya maumivu yake,

ndivyo tulivyokuwa mbele zako, EeBwana.

18 Tulikuwa na mimba, tuligaagaa kwa maumivu,

lakini tulizaa upepo.

Hatukuleta wokovu duniani,

hatujazaa watu katika ulimwengu huu.

19 Lakini wafu wenu wataishi,

nayo miili yao itafufuka.

Ninyi mnaokaa katika mavumbi,

amkeni mkapige kelele kwa furaha.

Umande wenu ni kama umande wa asubuhi,

dunia itawazaa wafu wake.

20 Nendeni, watu wangu, ingieni vyumbani mwenu

na mfunge milango nyuma yenu,

jificheni kwa kitambo kidogo

mpaka ghadhabu yake ipite.

21 Tazama,Bwanaanakuja kutoka makao yake

ili kuwaadhibu watu wa dunia kwa ajili ya dhambi zao.

Dunia itadhihirisha umwagaji damu juu yake,

wala haitaendelea kuwaficha watu wake waliouawa.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/26-5e3fa261bb59ab57eddae9a43d7103c3.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 27

Wokovu Kwa Ajili Ya Israeli

1 Katika siku ile,

Bwanaataadhibu kwa upanga wake,

upanga wake mkali, mkubwa na wenye nguvu,

ataadhibu Lewiathaniyule nyoka apitaye kwa mwendo laini,

Lewiathani yule nyoka mwenye kujipinda;

atamuua joka huyo mkubwa sana wa baharini.

2 Katika siku ile:

“Imbeni kuhusu shamba la mizabibu lililozaa:

3 Mimi,Bwana, ninalitunza,

nalinyweshea maji mfululizo.

Ninalichunga usiku na mchana

ili mtu yeyote asije akalidhuru.

4 Mimi sijakasirika.

Licha pangekuwepo michongoma na miiba kunikabili!

Ningepambana dhidi yake katika vita,

ningeliichoma moto yote.

5 Au niwaache waje kwangu kwa ajili ya kupata kimbilio,

wao na wafanye amani nami,

naam, wafanye amani nami.”

6 Katika siku zijazo, Yakobo atatia mizizi,

Israeli atatoa chipukizi na kuchanua maua,

naye atajaza ulimwengu wote kwa matunda.

7 Je,Bwanaamempiga

vile alivyowapiga wale waliompiga?

Je, yeye ameuawa

vile walivyouawa wale waliomuua yeye?

8 Kwa vita na kwa kumfukuza unapingana naye:

kwa mshindo wake mkali anamfukuza,

kama siku ile uvumapo upepo wa mashariki.

9 Kwa hili, basi, hatia ya Yakobo itafanyiwa upatanisho,

nalo hili litakuwa matunda ya utimilizo wa kuondolewa kwa dhambi yake:

Wakati atakapoyafanya mawe yote ya madhabahu

kuwa kama mawe ya chokaa yaliyopondwa vipande vipande,

hakuna nguzo za Ashera au madhabahu za kufukizia uvumba

zitakazobaki zimesimama.

10 Mji ulio na boma umebaki ukiwa,

makao yaliyotelekezwa, yaliyoachwa kama jangwa.

Huko ndama hulisha,

huko hujilaza,

wanakwanyua matawi yake.

11 Wakati vijiti vyake vimekauka, huvunjwa

nao wanawake huja na kuwasha navyo moto.

Kwa kuwa hili ni taifa lisilo na ufahamu,

kwa hiyo yeye aliyewafanya hana huruma juu yao,

Muumba wao hawaonyeshi fadhili.

12 Katika siku ileBwanaatapura kutoka matiririko ya Mto Frati hadi Kijito cha Misri, nanyi ee Waisraeli, mtakusanywa mmoja mmoja.

13 Katika siku ile tarumbeta kubwa italia. Wale waliokuwa wakiangamia katika nchi ya Ashuru, nao wale waliokuwa uhamishoni katika nchi ya Misri watakuja na kumwabuduBwanakatika mlima mtakatifu huko Yerusalemu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/27-11d9a8e1a22a0bf89939a171a02d608c.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 28

Ole Wa Efraimu

1 Ole kwa lile taji la maua, kiburi cha walevi wa Efraimu,

kwa ua linalosinyaa, uzuri wa utukufu wake,

uliowekwa kwenye kichwa cha bonde lenye rutuba:

kwa ule mji, kiburi cha wale walioshushwa na mvinyo!

2 Tazama, Bwana anaye mmoja aliye na uwezo na nguvu.

Kama dhoruba ya mvua ya mawe na upepo uharibuo,

kama mvua inyeshayo kwa nguvu na mafuriko yashukayo,

atakiangusha chini kwa nguvu.

3 Lile taji la maua, kiburi cha walevi cha Efraimu,

kitakanyagwa chini ya nyayo.

4 Lile ua linalosinyaa, uzuri wa utukufu wake,

uliowekwa kwenye kichwa cha bonde lenye rutuba,

litakuwa kama tini iliyoiva kabla ya mavuno:

mara mtu aionapo, huichuma na kuila.

5 Katika siku ile,BwanaMwenye Nguvu Zote

atakuwa taji la utukufu,

taji zuri la maua

kwa mabaki ya watu wake.

6 Atakuwa roho ya haki

kwa yeye aketiye katika kiti cha hukumu,

chanzo cha nguvu

kwa wale wazuiao vita langoni.

7 Hawa pia wanapepesuka kwa sababu ya mvinyo,

wanayumbayumba kwa sababu ya kileo:

Makuhani na manabii wanapepesuka kwa sababu ya kileo,

wanachanganyikiwa kwa sababu ya mvinyo;

wanapepesuka wanapoona maono,

wanajikwaa wanapotoa maamuzi.

8 Meza zote zimejawa na matapishi

wala hakuna sehemu hata ndogo

isiyokuwa na uchafu.

9 “Yeye anajaribu kumfundisha nani?

Yeye anamwelezea nani ujumbe wake?

Je, ni kwa watoto walioachishwa kunyonya?

Je, ni wale ambao ndipo tu wametolewa matitini?

10 Kwa maana ni:

Amri juu ya amri, amri juu ya amri,

kanuni juu ya kanuni, kanuni juu ya kanuni;

hapa kidogo, kule kidogo.”

11 Sawa kabisa, kwa midomo migeni

na kwa lugha ngeni,

Mungu atasema na watu hawa,

12 wale ambao aliwaambia,

“Hapa ni mahali pa kupumzika,

waliochoka na wapumzike,”

na, “Hapa ni mahali pa mapumziko,”

lakini hawakutaka kusikiliza.

13 Hivyo basi, neno laBwanakwao litakuwa:

Amri juu ya amri, amri juu ya amri,

kanuni juu ya kanuni, kanuni juu ya kanuni,

hapa kidogo, kule kidogo:

ili waende na kuanguka chali,

wakijeruhiwa, wakinaswa na kukamatwa.

14 Kwa hiyo sikieni neno laBwana, enyi watu wenye dharau

mnaotawala watu hawa wa Yerusalemu.

15 Ninyi mnajisifu, “Tumefanya agano na mauti,

tumefanya mapatano na kuzimu.

Wakati pigo lifurikalo litakapopita,

haliwezi kutugusa sisi,

kwa kuwa tumefanya uongo kuwa kimbilio letu

na miungu ya uongo kuwa mahali petu pa kujificha.”

16 Kwa hiyo hivi ndivyoBwanaMwenyezi asemavyo:

“Tazama, ninaweka jiwe katika Sayuni,

jiwe lililojaribiwa,

jiwe la pembeni la thamani kwa ajili ya msingi thabiti.

Yeye atumainiye kamwe hatatiwa hofu.

17 Nitaifanya haki kuwa kamba ya kupimia

na uadilifu kuwa timazi;

mvua ya mawe itafagia kimbilio lenu, huo uongo,

nayo maji yatafurikia mahali penu pa kujificha.

18 Agano lenu na kifo litabatilishwa,

patano lenu na kuzimu halitasimama.

Wakati pigo lifurikalo litakapowakumba,

litawaangusha chini.

19 Kila mara lijapo litawachukua,

asubuhi baada ya asubuhi,

wakati wa mchana na wakati wa usiku,

litawakumba tangu mwanzo hadi mwisho.”

Kuuelewa ujumbe huu

utaleta hofu tupu.

20 Kitanda ni kifupi mno kujinyoosha juu yake,

nguo ya kujifunikia ni nyembamba mno

mtu hawezi kujifunikia.

21 Bwanaatainuka kama alivyofanya kwenye Mlima Perasimu,

ataghadhibika kama alivyofanya katika Bonde la Gibeoni:

ili kufanya kazi yake, kazi yake ya ajabu,

ili kutimiza kazi yake, kazi yake ngeni.

22 Sasa acheni dharau zenu,

la sivyo minyororo yenu itakuwa mizito zaidi.

Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote, ameniambia

habari za maangamizi yaliyoamriwa dhidi ya nchi yote.

23 Sikilizeni msikie sauti yangu,

tegeni masikio na msikie niyasemayo.

24 Wakati mkulima alimapo ili apande,

je, hulima siku zote?

Je, huendelea kubomoa ardhi

na kusawazisha udongo?

25 Akiisha kusawazisha shamba,

je, hatapanyi mbegu za bizari na kutawanya jira?

Je, hapandi ngano katika sehemu yake,

shayiri katika eneo lake,

na nafaka nyingine katika shamba lake?

26 Mungu wake humwelekeza

na kumfundisha njia iliyo sahihi.

27 Iliki haipurwi kwa nyundo,

wala gurudumu la gari halivingirishwi juu ya jira;

iliki hupurwa kwa fimbo,

na jira kwa ufito.

28 Nafaka lazima isagwe ili kutengeneza mkate,

kwa hiyo mtu haendelei kuipura daima.

Ingawa huendesha magurudumu ya gari lake la kupuria juu yake,

farasi wake hawasagi.

29 Haya yote pia hutoka kwaBwanaMwenye Nguvu Zote,

mwenye mashauri ya ajabu, na anayepita wote kwa hekima.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/28-5e666061cae65be3720839d2b88c5b6d.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 29

Ole Wa Mji Wa Daudi

1 Ole wako, wewe Arieli, Arieli,

mji alimokaa Daudi!

Ongezeni mwaka kwa mwaka,

na mzunguko wa sikukuu zenu uendelee.

2 Hata hivyo nitauzunguka Arieli kwa jeshi,

utalia na kuomboleza,

utakuwa kwangu kama mahali

pa kuwashia moto madhabahuni.

3 Nitapiga kambi pande zote dhidi yako,

nitakuzunguka kwa minara

na kupanga mazingirwa yangu dhidi yako.

4 Utakaposhushwa, utanena kutoka ardhini,

utamumunya maneno yako kutoka mavumbini.

Sauti yako itatoka katika nchi kama vile ya mzimu,

utanongʼona maneno yako toka mavumbini.

5 Lakini adui zako wengi watakuwa kama vumbi laini,

kundi la wakatili watakuwa

kama makapi yapeperushwayo.

Naam, ghafula, mara moja,

6 BwanaMwenye Nguvu Zote atakuja

na ngurumo, tetemeko la ardhi, na kwa sauti kuu,

atakuja na dhoruba, tufani na miali ya moto iteketezayo.

7 Kisha makundi ya mataifa yote yale yapiganayo dhidi ya Arieli,

yale yanayomshambulia yeye na ngome zake, na kumzunguka kwa jeshi,

watakuwa kama ilivyo ndoto,

kama maono wakati wa usiku:

8 kama vile mtu aliye na njaa aotavyo kuwa anakula,

lakini huamka, bado njaa yake ingalipo,

kama vile mtu mwenye kiu aotavyo kuwa anakunywa maji,

lakini huamka akiwa anazimia, akiwa bado angali ana kiu.

Hivyo ndivyo itakavyokuwa kwa makundi yote ya mataifa

yanayopigana dhidi ya Mlima Sayuni.

9 Duwaeni na kushangaa,

jifanyeni vipofu wenyewe na msione,

leweni, lakini si kwa mvinyo,

pepesukeni lakini si kwa kileo.

10 Bwanaamewaleteeni usingizi mzito:

Ameziba macho yenu (ninyi manabii);

amefunika vichwa vyenu (ninyi waonaji).

11 Kwa maana kwenu ninyi, maono haya yote si kitu ila maneno yaliyotiwa lakiri katika kitabu. Kama mkimpa mtu yeyote awezaye kusoma kitabu hiki, nanyi mkamwambia, “Tafadhali kisome,” yeye atajibu, “Mimi siwezi, kwa kuwa kimetiwa lakiri.”

12 Au kama mkimpa mtu yeyote kitabu hiki asiyeweza kusoma na kumwambia, “Tafadhali kisome,” atajibu, “Mimi sijui kusoma.”

13 Bwana anasema:

“Watu hawa hunikaribia kwa vinywa vyao

na kuniheshimu kwa midomo yao,

lakini mioyo yao iko mbali nami.

Ibada yao kwangu inatokana na maagizo

waliyofundishwa na wanadamu.

14 Kwa hiyo mara nyingine tena nitawashangaza watu hawa,

kwa ajabu juu ya ajabu.

Hekima ya wenye hekima itapotea,

nayo akili ya wenye akili itatoweka.”

15 Ole kwa wale wanaokwenda kwenye vilindi virefu

kumfichaBwanamipango yao,

wafanyao kazi zao gizani na kufikiri,

“Ni nani anayetuona? Ni nani atakayejua?”

16 Mnapindua mambo juu chini,

kana kwamba mfinyanzi aweza kufikiriwa kuwa kama udongo wa mfinyanzi!

Je, kile kilichofinyangwa chaweza kumwambia yule aliyekifinyanga,

“Wewe hukunifinyanga mimi?”

Je, chungu kinaweza kumwambia mfinyanzi,

“Wewe hujui chochote?”

17 Kwa muda mfupi sana, je, Lebanoni haitageuzwa kuwa shamba lenye rutuba,

na shamba lenye rutuba liwe kama msitu?

18 Katika siku ile viziwi watasikia maneno ya kitabu,

na katika utusitusi na giza

macho ya kipofu yataona.

19 Mara nyingine tena wanyenyekevu watafurahi katikaBwana,

wahitaji watafurahi katika yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.

20 Wakatili watatoweka na wenye kudhihaki watatokomea,

nao wote wenye jicho la uovu watakatiliwa mbali,

21 wale ambao kwa neno humfanya mtu kuwa mwenye hatia,

wamtegeao mtego mtetezi katika mahakama,

na kwa ushuhuda wa uongo humnyima haki

yeye asiye na hatia.

22 Kwa hiyo hili ndiloBwana, aliyemkomboa Abrahamu, analosema kwa nyumba ya Yakobo:

“Yakobo hataaibishwa tena,

wala nyuso zao hazitabadilika sura tena.

23 Wakati watakapoona watoto wao miongoni mwao,

kazi ya mikono yangu,

watalitakasa Jina langu takatifu;

wataukubali utakatifu wa yeye Aliye Mtakatifu wa Yakobo,

nao watamcha Mungu wa Israeli.

24 Wale wanaopotoka rohoni watapata ufahamu,

nao wale wanaolalamika watayakubali mafundisho.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/29-25bc0f6f04f24099dd6bf61881500972.mp3?version_id=1627—