Categories
Isaya

Isaya Utangulizi

Utangulizi

Jina Isaya maana yake ni “

Bwana

anaokoa.” Kufuatana na mapokeo, Isaya alitoa unabii wakati mmoja na Amosi, Hosea na Mika. Isaya alianza huduma yake mwaka wa 740 K.K. Isaya alikuwa ameoa, na akapata watoto wawili, Shear-Yashubu na Maher-Shalal-Hash-Bazi. Yamkini, Isaya alitumia wakati wake mwingi huko Yerusalemu wakati wa Mfalme Hezekia. Kufuatana na historia ya Kiyahudi, Isaya aliuawa kwa kupasuliwa vipande viwili chini ya utawala wa Manase, yule mwana mwovu wa Mfalme Hezekia, aliyetawala tangu 696–642 K.K.

Mwandishi

Isaya mwana wa Amozi.

Kusudi

Isaya anatoa wito kwa taifa la Yuda kumrudia Mungu, na pia anawatangazia wokovu wa Mungu kupitia kwa Masiya.

Mahali

Yerusalemu.

Tarehe

700–680 K.K.

Wahusika Wakuu

Isaya, wanawe wawili Shear-Yashubu na Maher-Shalal-Hash-Bazi, Mfalme Hezekia.

Wazo Kuu

Kuufanya ujumbe wa Mungu uwe wazi kwa Israeli, ili kuwaonya kuhusu hukumu ikiwa wataendelea kudumu katika dhambi. Pia kudhihirisha jinsi Mungu atakavyoshughulika nao katika kukamilisha kuwarejesha upya chini ya Masiya wao milele.

Mambo Muhimu

Mungu atamtuma Masiya ili kuokoa watu wake; atakuja kama Mwokozi na Bwana pekee, lakini atatenda kama mtumishi. Atakufa ili kuziondoa dhambi. Mungu anaahidi kutuma faraja, ukombozi na urejesho katika ufalme wake ujao. Masiya atatawala juu ya wafuasi wake wakati huo. Tumaini ni hakika kwa sababu Kristo yuaja.

Mgawanyo

Hukumu na matumaini ya matengenezo (

1:1–6:13

)

Matumaini kwa Ashuru au Mungu (

7:1–12:6

)

Unabii kuhusu mataifa (

13:1–23:18

)

Hukumu ya Israeli na ukombozi (

24:1–27:13

)

Maonyo, na Sayuni yatengenezwa (

28:1–35:10

)

Mfalme Hezekia awazuia Waashuru (

36:1–39:8

)

Ahadi za ukombozi wa Mungu (

40:1–56:8

)

Ufalme wa mwisho unasimamishwa (

56:9–66:24

).

Categories
Isaya

Isaya 1

1 Maono kuhusu Yuda na Yerusalemu ambayo Isaya mwana wa Amozi aliyaona wakati wa utawala wa Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda.

Taifa Asi

2 Sikieni, enyi mbingu! Sikilizeni, enyi dunia!

Kwa maanaBwanaamesema:

“Nimewalisha watoto na kuwalea,

lakini wameniasi mimi.

3 Ngʼombe anamjua bwana wake,

naye punda anajua hori la mmiliki wake,

lakini Israeli hajui,

watu wangu hawaelewi.”

4 Lo! Taifa lenye dhambi,

watu waliolemewa na uovu,

uzao wa watenda mabaya,

watoto waliozoelea upotovu!

WamemwachaBwana,

Wamemkataa kwa dharau

yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli

na kumgeuzia kisogo.

5 Kwa nini mzidi kupigwa?

Kwa nini kudumu katika uasi?

Kichwa chako chote kimejeruhiwa,

moyo wako wote ni mgonjwa.

6 Kutoka wayo wako wa mguu hadi kwenye utosi wa kichwa chako

hakuna uzima:

ni majeraha matupu na makovu

na vidonda vitokavyo damu,

havikusafishwa au kufungwa

wala kulainishwa kwa mafuta.

7 Nchi yenu imekuwa ukiwa,

miji yenu imeteketezwa kwa moto;

nchi yenu imeachwa tupu na wageni

mbele ya macho yenu,

imeharibiwa kama vile imepinduliwa na wageni.

8 Binti Sayuni ameachwa kama kipenu

katika shamba la mizabibu,

kama kibanda katika shamba la matikitimaji,

kama mji uliohusuriwa.

9 KamaBwanaMungu Mwenye Nguvu Zote

asingelituachia walionusurika,

tungelikuwa kama Sodoma,

tungelifanana na Gomora.

10 Sikieni neno laBwana,

ninyi watawala wa Sodoma;

sikilizeni sheria ya Mungu wetu,

enyi watu wa Gomora!

11 Bwanaanasema, “Wingi wa sadaka zenu,

ni kitu gani kwangu?

Ninazo sadaka za kuteketezwa nyingi kupita kiasi,

za kondoo dume na mafuta ya wanyama walionona.

Sipendezwi na damu za mafahali

wala za wana-kondoo na mbuzi.

12 Mnapokuja kujihudhurisha mbele zangu,

ni nani aliyewataka ninyi mfanye hivyo,

huku kuzikanyaga nyua zangu?

13 Acheni kuniletea sadaka zisizokuwa na maana!

Uvumba wenu ni chukizo kwangu.

Miandamo ya Mwezi, Sabato na makusanyiko ya ibada:

siwezi kuvumilia makusanyiko yenu maovu.

14 Sikukuu zenu za Miandamo ya Mwezi, na sikukuu zenu zilizoamriwa:

moyo wangu unazichukia.

Zimekuwa mzigo kwangu,

nimechoka kuzivumilia.

15 Mnaponyoosha mikono yenu katika maombi,

nitaficha macho yangu nisiwaone;

hata mkiomba maombi mengi

sitasikiliza.

Mikono yenu imejaa damu;

16 jiosheni na mkajitakase.

Yaondoeni matendo yenu maovu

mbele zangu!

Acheni kutenda mabaya,

17 jifunzeni kutenda mema!

Tafuteni haki,

watieni moyo walioonewa.

Teteeni shauri la yatima,

wateteeni wajane.

18 “Njooni basi tuhojiane,”

asemaBwana.

“Ingawa dhambi zenu ni kama rangi nyekundu,

zitakuwa nyeupe kama theluji;

ingawa ni nyekundu sana kama damu,

zitakuwa nyeupe kama sufu.

19 Kama mkikubali na kutii,

mtakula mema ya nchi,

20 lakini kama mkikataa na kuasi,

mtaangamizwa kwa upanga.”

Kwa kuwa kinywa chaBwanakimenena.

21 Tazama jinsi mji uliokuwa mwaminifu

umekuwa kahaba!

Mwanzoni ulikuwa umejaa unyofu,

haki ilikuwa inakaa ndani yake,

lakini sasa ni wauaji!

22 Fedha yenu imekuwa takataka,

divai yenu nzuri imechanganywa na maji.

23 Watawala wenu ni waasi,

rafiki wa wevi,

wote wanapenda rushwa

na kukimbilia hongo.

Hawatetei yatima,

shauri la mjane haliletwi mbele yao lisikilizwe.

24 Kwa hiyo Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote,

Mwenye Nguvu wa Israeli, asema hivi:

“Lo, nitapata faraja kutoka kwa adui zangu

na kujilipizia kisasi juu ya watesi wangu.

25 Nitauelekeza mkono wangu dhidi yenu,

nitawasafisha takataka zenu zote

na kuwaondolea unajisi wenu wote.

26 Nitawarudishia waamuzi wenu kama ilivyokuwa siku za zamani,

nao washauri wenu kama ilivyokuwa mwanzoni.

Baadaye utaitwa,

Mji wa Haki,

Mji Mwaminifu.”

27 Sayuni itakombolewa kwa haki,

wale waliomo ndani yake waliotubu kwa uaminifu.

28 Lakini waasi na wenye dhambi wote wataangamizwa,

nao wanaomwachaBwanawataangamia.

29 “Mtaaibika kwa sababu ya hiyo mialoni

ambayo mlifurahia,

mtafadhaika kwa sababu ya bustani

mlizozichagua.

30 Mtakuwa kama mwaloni wenye majani yanayonyauka,

kama bustani isiyokuwa na maji.

31 Mtu mwenye nguvu atatoweka kama majani makavu yawakayo moto,

na kazi yake kama cheche ya moto;

vyote vitaungua pamoja,

wala hakuna wa kuuzima huo moto.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/1-7f652a74bdea1a198249732ecbbf8fbe.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 2

Mlima Wa Bwana

1 Hili ndilo aliloliona Isaya mwana wa Amozi kuhusu Yuda na Yerusalemu:

2 Katika siku za mwisho

mlima wa Hekalu laBwanautaimarishwa

kama mlima mkuu miongoni mwa milima yote,

utainuliwa juu ya vilima,

na mataifa yote yatamiminika huko.

3 Mataifa mengi yatakuja na kusema,

“Njooni, twendeni mlimani mwaBwana,

kwenye nyumba ya Mungu wa Yakobo.

Atatufundisha njia zake,

ili tuweze kuenenda katika mapito yake.”

Sheria itatoka Sayuni,

neno laBwanalitatoka Yerusalemu.

4 Atahukumu kati ya mataifa

na ataamua migogoro ya mataifa mengi.

Watafua panga zao ziwe majembe,

na mikuki yao kuwa miundu ya kukata matawi.

Taifa halitainua upanga dhidi ya taifa jingine,

wala hawatajifunza vita tena.

5 Njooni, enyi nyumba ya Yakobo,

tutembeeni katika nuru yaBwana.

Siku Ya Bwana

6 Umewatelekeza watu wako,

nyumba ya Yakobo.

Wamejaa ushirikina utokao Mashariki,

wanapiga ramli kama Wafilisti

na wanashikana mikono na wapagani.

7 Nchi yao imejaa fedha na dhahabu,

hakuna mwisho wa hazina zao.

Nchi yao imejaa farasi,

hakuna mwisho wa magari yao.

8 Nchi yao imejaa sanamu,

wanasujudia kazi za mikono yao,

vitu vile vidole vyao vimevitengeneza.

9 Kwa hiyo mwanadamu atashushwa

na binadamu atanyenyekezwa:

usiwasamehe.

10 Ingieni kwenye miamba,

jificheni ardhini

kutokana na utisho waBwana

na utukufu wa enzi yake!

11 Macho ya mtu mwenye majivuno yatanyenyekezwa

na kiburi cha wanadamu kitashushwa,

Bwanapeke yake ndiye atakayetukuzwa siku hiyo.

12 BwanaMwenye Nguvu Zote anayo siku aliyoiweka akiba

kwa wote wenye kujivuna na wenye kiburi,

kwa wote wanaojikweza

(nao watanyenyekezwa),

13 kwa mierezi yote ya Lebanoni iliyo mirefu sana,

na mialoni yote ya Bashani,

14 kwa milima yote mirefu

na vilima vyote vilivyoinuka,

15 kwa kila mnara ulio mrefu sana

na kila ukuta wenye ngome,

16 kwa kila meli ya biashara,

na kila chombo cha baharini cha fahari.

17 Majivuno ya mwanadamu yatashushwa,

na kiburi cha wanadamu kitanyenyekezwa,

Bwanapeke yake ndiye atatukuzwa siku hiyo,

18 nazo sanamu zitatoweka kabisa.

19 Watu watakimbilia kwenye mapango ndani ya miamba,

na kwenye mahandaki ardhini

kutokana na utisho waBwana

na utukufu wa enzi yake,

ainukapo kuitikisa dunia.

20 Siku ile, watu watawatupia

panya na popo

sanamu zao za fedha na za dhahabu,

walizozitengeneza ili waziabudu.

21 Watakimbilia kwenye mapango miambani

na kwenye nyufa za miamba

kutokana na utisho waBwana

na utukufu wa enzi yake,

ainukapo kuitikisa dunia.

22 Acheni kumtumainia mwanadamu,

ambaye hana kitu ila pumzi katika pua zake.

Yeye ana thamani gani?

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/2-fe1cc94206caa8ad1921991cf7dd89f7.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 3

Hukumu Juu Ya Yerusalemu Na Yuda.

1 Tazama sasa, Bwana,

BwanaMwenye Nguvu Zote,

yu karibu kuwaondolea Yerusalemu na Yuda

upatikanaji wa mahitaji na misaada,

upatikanaji wote wa chakula na tegemeo lote la maji,

2 shujaa na mtu wa vita,

mwamuzi na nabii,

mwaguzi na mzee,

3 jemadari wa kikosi cha watu hamsini

na mtu mwenye cheo, mshauri,

fundi stadi na mlozi mjanja.

4 Nitawafanya wavulana wawe maafisa wao,

watoto ndio watakaowatawala.

5 Watu wataoneana wao kwa wao:

mtu dhidi ya mtu, na jirani dhidi ya jirani yake.

Kijana atainuka dhidi ya mzee,

mtu mnyonge dhidi ya mtu mwenye heshima.

6 Mtu atamkamata mmoja wa ndugu zake

katika nyumba ya baba yake na kusema,

“Unalo joho, sasa uwe kiongozi wetu,

tawala lundo hili la magofu!”

7 Lakini siku hiyo atapiga kelele akisema,

“Sina uponyaji.

Sina chakula wala mavazi katika nyumba yangu,

msinifanye niwe kiongozi wa watu.”

8 Yerusalemu inapepesuka,

Yuda inaanguka;

maneno yao na matendo yao ni kinyume naBwana,

wakiudharau uwepo wake uliotukuka.

9 Nyuso zao zinavyoonekana zinashuhudia dhidi yao,

hujivunia dhambi yao kama Sodoma,

wala hawaifichi.

Ole wao!

Wamejiletea maafa juu yao wenyewe.

10 Waambie wanyofu itakuwa heri kwao,

kwa kuwa watafurahia tunda la matendo yao.

11 Ole kwa watu waovu! Maafa yapo juu yao!

Watalipwa kwa ajili ya yale mikono yao iliyotenda.

12 Vijana wanawatesa watu wangu,

wanawake wanawatawala.

Enyi watu wangu, viongozi wenu wanawapotosha,

wanawapoteza njia.

13 Bwanaanachukua nafasi yake mahakamani,

anasimama kuhukumu watu.

14 Bwanaanaingia katika hukumu

dhidi ya wazee na viongozi wa watu wake:

“Ninyi ndio mlioharibu shamba langu la mizabibu,

mali zilizonyangʼanywa maskini zimo nyumbani mwenu.

15 Mnamaanisha nini kuwaponda watu wangu

na kuzisaga nyuso za maskini?”

asema Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote.

16 Bwanaasema,

“Wanawake wa Sayuni wana kiburi,

wanatembea na shingo ndefu,

wakikonyeza kwa macho yao,

wanatembea kwa hatua za madaha,

wakiwa na mapambo ya njuga kwenye vifundo vya miguu yao.

17 Kwa hiyo Bwana ataleta majipu kwenye vichwa vya wanawake wa Sayuni;

Bwanaatazifanya ngozi za vichwa vyao kuwa vipara.”

18 Katika siku ile Bwana atawanyangʼanya uzuri wao: bangili, tepe za kichwani, mikufu yenye alama za mwezi mwandamo,

19 vipuli, vikuku, shela,

20 vilemba, mikufu ya vifundo vya miguu, mshipi, chupa za manukato na hirizi,

21 pete zenye muhuri, pete za puani,

22 majoho mazuri, mitandio, mavazi, kifuko cha kutilia fedha,

23 vioo, mavazi ya kitani, taji na shali.

24 Badala ya harufu ya manukato kutakuwa na uvundo;

badala ya mishipi, ni kamba;

badala ya nywele zilizotengenezwa vizuri, ni upara;

badala ya mavazi mazuri, ni nguo za magunia;

badala ya uzuri, ni alama ya aibu kwa chuma cha moto.

25 Wanaume wako watauawa kwa upanga,

nao mashujaa wako watauawa vitani.

26 Malango ya Sayuni yataomboleza na kulia,

ataketi mavumbini akiwa fukara.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/3-97337bf7bbab98858f9a6194f2663a83.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 4

1 Katika siku ile wanawake saba

watamshika mwanaume mmoja

wakisema, “Tutakula chakula chetu wenyewe

na kuvaa nguo zetu wenyewe,

ila wewe uturuhusu tu tuitwe kwa jina lako.

Utuondolee aibu yetu!”

Tawi La Bwana

2 Katika siku ile Tawi laBwanalitakuwa zuri na lenye utukufu, nalo tunda la nchi litakuwa fahari na utukufu wa wale Waisraeli watakaonusurika.

3 Wale watakaoachwa Sayuni, watakaobaki Yerusalemu, wataitwa watakatifu, wale wote ambao wameorodheshwa miongoni mwa walio hai huko Yerusalemu.

4 Bwana atausafisha uchafu wa wanawake wa Sayuni, atatakasa madoa ya damu kutoka Yerusalemu kwa Roho ya hukumu na Roho ya moto.

5 KishaBwanaataumba juu ya Mlima wote wa Sayuni, na juu ya wale wote wanaokusanyika hapo, wingu la moshi wakati wa mchana, na kungʼaa kwa miali ya moto wakati wa usiku, nako juu ya huo utukufu wote kutatanda kifuniko cha ulinzi.

6 Utakuwa sitara na kivuli kutokana na joto la mchana, na kuwa mahali pa kujificha kutokana na dhoruba na mvua.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/4-29a0f8ff5e4f3c8fcfb5d73edd660c18.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 5

Wimbo Wa Shamba La Mizabibu

1 Nitaimba wimbo kwa ajili ya mmoja nimpendaye,

kuhusu shamba lake la mizabibu:

Mpendwa wangu alikuwa na shamba la mizabibu

kwenye kilima chenye rutuba.

2 Alililima na kuondoa mawe

na akaliotesha mizabibu bora sana.

Akajenga mnara wa ulinzi ndani yake,

na kutengeneza shinikizo la kukamulia divai pia.

Kisha akatazamia kupata mazao ya zabibu nzuri,

lakini lilizaa matunda mabaya tu.

3 “Basi enyi wakazi wa Yerusalemu na watu wa Yuda,

hukumuni kati yangu na shamba langu la mizabibu.

4 Ni nini zaidi ambacho kingeweza kufanyika kwa shamba langu la mizabibu

kuliko yale niliyofanya?

Nilipotazamia kupata zabibu nzuri,

kwa nini lilizaa zabibu mbaya tu?

5 Sasa nitawaambia lile nitakalolitendea

shamba langu la mizabibu:

Nitaondoa uzio wake,

nalo litaharibiwa,

nitabomoa ukuta wake,

nalo litakanyagwa.

6 Nitalifanya nchi ya ukiwa isiyokaliwa na watu,

halitakatiwa matawi wala kulimwa,

nayo michongoma na miiba itamea huko,

nitaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake.”

7 Shamba la mzabibu laBwanaMwenye Nguvu Zote

ni nyumba ya Israeli,

na watu wa Yuda

ni bustani yake ya kumpendeza.

Alitazamia haki, lakini akaona umwagaji damu,

alitazamia uadilifu, lakini akasikia vilio vya taabu.

Ole Na Hukumu

8 Ole wenu mnaoongeza nyumba baada ya nyumba

na kuunganisha mashamba baada ya mashamba

hadi hakuna nafasi iliyobaki,

nanyi mnaishi peke yenu katika nchi.

9 BwanaMwenye Nguvu Zote amesema nikisikia:

“Hakika nyumba kubwa zitakuwa ukiwa,

nayo majumba ya fahari yatabaki bila kukaliwa.

10 Shamba la mizabibu la eka kumi

litatoa bathimoja ya divai,

na homeriya mbegu zilizopandwa

itatoa efamoja tu ya nafaka.”

11 Ole wao wale waamkao asubuhi na mapema

wakikimbilia kunywa vileo,

wale wakawiao sana mpaka usiku,

mpaka wamewaka kwa mvinyo.

12 Wana vinubi na zeze kwenye karamu zao,

matari, filimbi na mvinyo,

lakini hawayajali matendo yaBwana,

wala hawana heshima kwa ajili ya kazi ya mikono yake.

13 Kwa hiyo watu wangu watakwenda uhamishoni

kwa sababu ya kukosa ufahamu,

watu wao wenye vyeo watakufa kwa njaa

na watu wao wengi watakauka kwa kiu.

14 Kwa hiyo kaburilimeongeza hamu yake

na kupanua mdomo wake bila kikomo,

ndani mwake watashuka wakuu wao na wingi wa watu,

pamoja na wagomvi wao, na wafanyao sherehe wote.

15 Hivyo mwanadamu atashushwa,

na binadamu kunyenyekezwa,

macho ya wenye majivuno yatanyenyekezwa.

16 LakiniBwanaMwenye Nguvu Zote atatukuzwa

kwa ajili ya haki yake,

naye Mungu Mtakatifu atajionyesha mwenyewe

kuwa mtakatifu kwa haki yake.

17 Kondoo watajilisha kwenye malisho yao wenyewe,

wana-kondoo watajilisha katika magofu ya matajiri.

18 Ole wao wanaovuta dhambi kwa kamba za udanganyifu

na uovu kama kwa kamba za mkokoteni,

19 kwa wale wanaosema, “Mungu na afanye haraka,

aharakishe kazi yake ili tupate kuiona.

Huo mpango wa Aliye Mtakatifu wa Israeli na ukamilike,

tena udhihirike ili tupate kuujua.”

20 Ole wao wanaoita ubaya ni wema,

na wema ni ubaya,

wawekao giza badala ya nuru,

na nuru badala ya giza,

wawekao uchungu badala ya utamu,

na utamu badala ya uchungu.

21 Ole wao walio na hekima machoni pao wenyewe,

na kujiona wenye akili machoni pao wenyewe.

22 Ole wao walio mashujaa kwa kunywa mvinyo,

nao walio hodari katika kuchanganya vileo,

23 wale wanaoachilia wenye hatia kwa kupokea hongo,

lakini huwanyima haki wasio na hatia.

24 Kwa hiyo, kama ndimi za moto zirambavyo nyasi,

na kama vile majani makavu yazamavyo katika miali ya moto,

ndivyo mizizi yao itakavyooza

na maua yao yatakavyopeperushwa kama mavumbi;

kwa kuwa wameikataa sheria yaBwanaMwenye Nguvu Zote

na kulisukumia mbali neno la Aliye Mtakatifu wa Israeli.

25 Kwa hiyo hasira yaBwanainawaka dhidi ya watu wake,

mkono wake umeinuliwa na anawapiga.

Milima inatetemeka,

maiti ni kama takataka kwenye barabara.

Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali,

mkono wake bado umeinuliwa juu.

26 Yeye anainua bendera kwa ajili ya mataifa yaliyo mbali,

anapiga filimbi kwa ajili ya wale walio kwenye miisho ya dunia.

Tazama wamekuja,

kwa kasi na kwa haraka!

27 Hakuna hata mmoja wao anayechoka wala kujikwaa,

hakuna hata mmoja anayesinzia wala kulala,

hakuna mkanda uliolegezwa kiunoni,

hakuna gidamu ya kiatu iliyokatika.

28 Mishale yao ni mikali,

pinde zao zote zimevutwa,

kwato za farasi wao ziko kama jiwe la gumegume,

magurudumu ya magari yao ya vita ni kama upepo wa kisulisuli.

29 Ngurumo yao ni kama ile ya simba,

wananguruma kama wana simba,

wanakoroma wanapokamata mawindo yao,

na kuondoka nayo pasipo yeyote wa kuokoa.

30 Katika siku ile watanguruma juu yake

kama ngurumo za bahari.

Kama mtu akiitazama nchi,

ataona giza na dhiki;

hata nuru itatiwa giza kwa mawingu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/5-9bfcdfb609100a4924e8bba32be4ad0b.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 6

Agizo Kwa Isaya

1 Katika mwaka ule Mfalme Uzia alikufa, nilimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu na kilichotukuzwa sana, nalo pindo la joho lake likajaza Hekalu.

2 Juu yake walikuwepo maserafi, kila mmoja alikuwa na mabawa sita: Kwa mabawa mawili walifunika nyuso zao, kwa mengine mawili walifunika miguu yao, na kwa mawili walikuwa wakiruka.

3 Nao walikuwa wakiitana kila mmoja na mwenzake:

“Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu

niBwanaMwenye Nguvu Zote;

dunia yote imejaa utukufu wake.”

4 Kwa sauti zao, miimo ya milango na vizingiti vilitikisika, nalo Hekalu likajaa moshi.

5 Ndipo nikalia, “Ole wangu! Nimeangamia! Kwa kuwa mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninaishi katikati ya watu wenye midomo michafu, nayo macho yangu yamemwona Mfalme,BwanaMwenye Nguvu Zote.”

6 Ndipo mmoja wa wale maserafi akaruka kunijia akiwa na kaa la moto linalowaka mkononi mwake, ambalo alikuwa amelichukua kwa koleo kutoka madhabahuni.

7 Akanigusa nalo kinywa changu na kusema, “Tazama, hili limegusa midomo yako, uovu wako umeondolewa, nayo dhambi yako imesamehewa.”

8 Kisha nikasikia sauti ya Bwana ikisema, “Nimtume nani? Ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu?”

Nami nikasema, “Mimi hapa. Nitume mimi!”

9 Akasema, “Nenda ukawaambie watu hawa:

“ ‘Mtaendelea daima kusikiliza,

lakini kamwe hamtaelewa;

mtaendelea daima kutazama,

lakini kamwe hamtatambua.’

10 Fanya mioyo ya watu hawa kuwa migumu,

fanya masikio yao yasisikie,

na upofushe macho yao.

Wasije wakaona kwa macho yao,

na wakasikiliza kwa masikio yao,

wakaelewa kwa mioyo yao,

nao wakageuka, nikawaponywa.”

11 Ndipo nikasema, “Hadi lini, Ee Bwana?”

Naye akanijibu:

“Hadi miji iwe imeachwa magofu

na bila wakazi,

hadi nyumba zitakapobaki bila watu,

na mashamba yatakapoharibiwa na kuangamizwa,

12 hadiBwanaatakapokuwa amekwisha kumpeleka kila mmoja mbali sana,

na nchi itakapokuwa imeachwa kabisa.

13 Hata kama sehemu ya kumi ya watu watabaki katika nchi,

itaharibiwa tena.

Lakini kama vile mvinje na mwaloni

ibakizavyo visiki inapokatwa,

ndivyo mbegu takatifu

itakavyokuwa kisiki katika nchi.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/6-477c55de37f264094758a353be047415.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 7

Ishara Ya Imanueli

1 Wakati Ahazi mwana wa Yothamu, mwana wa Uzia, alipokuwa mfalme wa Yuda, Mfalme Resini wa Aramu,na Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli walipanda kupigana dhidi ya Yerusalemu, lakini hawakuweza kuushinda.

2 Wakati huu nyumba ya Daudi iliambiwa, “Aramu wameungana na Efraimu.” Kwa hiyo mioyo ya Ahazi na watu wake ilitikiswa, kama miti ya msituni inavyotikiswa na upepo.

3 NdipoBwanaakamwambia Isaya, “Toka uende, wewe na mwanao Shear-Yashubu,mkutane na Ahazi huko mwisho wa mfereji wa Bwawa la Juu, kwenye barabara iendayo Shamba la Dobi.

4 Mwambie, ‘Uwe mwangalifu, utulie na usiogope. Usife moyo kwa ajili ya watu hawa wawili walio kama visiki vya kuni vifukavyo moshi, kwa ajili ya hasira kali ya Resini na Aramu na ya mwana wa Remalia.

5 Aramu, Efraimu na mwana wa Remalia wamepanga shauri baya ili wakuangamize, wakisema,

6 “Tuishambulie Yuda, naam, tuirarue vipande vipande na kuigawa miongoni mwetu, na kumtawaza mwana wa Tabeeli awe mfalme juu yake.”

7 LakiniBwanaMwenyezi asema hivi:

“ ‘Jambo hili halitatendeka,

halitatokea,

8 kwa kuwa kichwa cha Aramu ni Dameski,

na kichwa cha Dameski ni Resini peke yake.

Katika muda wa miaka sitini na mitano,

Efraimu atakuwa ameharibiwa

kiasi kwamba hataweza tena kuwa taifa.

9 Kichwa cha Efraimu ni Samaria,

na kichwa cha Samaria

ni mwana wa Remalia peke yake.

Kama hamtasimama thabiti katika imani yenu,

hamtaimarika kamwe.’ ”

10 Bwanaakasema na Ahazi tena,

11 “MwombeBwanaMungu wako ishara, iwe kwenye vina virefu sana, au kwenye vimo virefu sana.”

12 Lakini Ahazi akasema, “Sitaomba; sitamjaribuBwana.”

13 Ndipo Isaya akasema, “Sikia sasa, ewe nyumba ya Daudi! Je, haitoshi kujaribu uvumilivu wa wanadamu? Je, mtaujaribu uvumilivu wa Mungu wangu pia?

14 Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara: Bikira atachukua mimba, naye atamzaa mwana, na ataitwa Imanueli.

15 Atakula jibini na asali atakapokuwa ameweza kukataa mabaya na kuchagua mema.

16 Lakini kabla mtoto hajajua kukataa mabaya na kuchagua mema, nchi ya wafalme hao wawili unaowaogopa itafanywa ukiwa.

17 Bwanaataleta juu yako, juu ya watu wako, na juu ya nyumba ya baba yako wakati ambao haujawahi kuwako tangu Efraimu alipojitenga na Yuda: yeye atawaleteeni mfalme wa Ashuru.”

18 Katika siku ileBwanaatawapigia filimbi mainzi kutoka vijito vya mbali vya Misri, na nyuki kutoka nchi ya Ashuru.

19 Wote watakuja na kukaa kwenye mabonde yenye miteremko, na kwenye nyufa za miamba, kwenye vichaka vyote vyenye miiba, na kwenye mashimo yote ya maji.

20 Katika siku ile Bwana atatumia wembe ulioajiriwa kutoka ngʼambo ya Mto,yaani mfalme wa Ashuru, kunyoa nywele za kichwa chako na malaika ya miguu yako, na kuziondoa ndevu zako pia.

21 Katika siku ile, mtu atahifadhi hai ndama mmoja na kondoo wawili.

22 Kwa ajili ya wingi wa maziwa watakayotoa, atapata jibini ya kula. Wote watakaobakia katika nchi watakula jibini na asali.

23 Katika siku ile, kila mahali palipokuwa na mizabibu elfu moja yenye thamani ya shekeli 1,000za fedha, patakuwa na michongoma na miiba tu.

24 Watu watakwenda huko wakiwa na upinde na mshale, kwa maana nchi itafunikwa na michongoma na miiba.

25 Kuhusu vilima vyote vilivyokuwa vikilimwa kwa jembe, hamtakwenda huko tena kwa ajili ya hofu ya michongoma na miiba. Patakuwa mahali ambapo ngʼombe wataachiwa huru, na kondoo kukimbia kimbia.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/7-788558f4b6838b26743b6aa0c4b84b55.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 8

Ashuru, Chombo Cha Bwana

1 Bwanaakaniambia, “Chukua gombo kubwa, uandike juu yake kwa kalamu ya kawaida jina: Maher-Shalal-Hash-Bazi.

2 Nami nitawaita kuhani Uria, na Zekaria mwana wa Yeberekia kama mashahidi wangu waaminifu.”

3 Kisha nikaenda kwa nabii mke, naye akapata mimba, akazaa mwana. KishaBwanaakaniambia, “Mwite huyo mtoto Maher-Shalal-Hash-Bazi.

4 Kabla mtoto hajaweza kusema ‘Baba yangu’ au ‘Mama yangu,’ utajiri wa Dameski na nyara za Samaria zitachukuliwa na mfalme wa Ashuru.”

5 Bwanaakasema nami tena:

6 “Kwa sababu watu hawa wamekataa maji ya Shilo yatiririkayo taratibu

wakamfurahia Resini na mwana wa Remalia,

7 kwa hiyo Bwana yu karibu kuleta dhidi yao

mafuriko makubwa ya Mto:

yaani mfalme wa Ashuru na fahari yake yote.

Yatafurika juu ya mifereji yake yote,

yatamwagikia juu ya kingo zake zote,

8 na kufika hadi Yuda, yakizunguka kwa kasi juu yake,

yakipita katikati na yakifika hadi shingoni.

Mabawa yake yaliyokunjuliwa

yatafunika upana wa nchi yako,

Ee Imanueli!”

9 Inueni kilio cha vita, enyi mataifa,

na mkavunjwevunjwe!

Sikilizeni, enyi nyote nchi za mbali.

Jiandaeni kwa vita, nanyi mkavunjwevunjwe!

Jiandaeni kwa vita, nanyi mkavunjwevunjwe!

10 Wekeni mikakati yenu, lakini itashindwa;

fanyeni mipango yenu, lakini haitafanikiwa,

kwa maana Mungu yu pamoja nasi.

Mwogope Mungu

11 Bwanaalisema nami mkono wake wenye nguvu ukiwa juu yangu, akinionya nisifuate njia za taifa hili. Akasema:

12 “Usiite fitina kila kitu ambacho watu hawa hukiita fitina,

usiogope kile wanachokiogopa,

wala usikihofu.

13 BwanaMwenye Nguvu Zote ndiye peke yake

ikupasaye kumheshimu kuwa mtakatifu,

ndiye peke yake utakayemwogopa,

ndiye peke yake utakayemhofu,

14 naye atakuwa mahali patakatifu;

lakini kwa nyumba zote mbili za Israeli atakuwa

jiwe lile linalosababisha watu kujikwaa

na mwamba wa kuwaangusha.

Kwa watu wa Yerusalemu,

atakuwa mtego na tanzi.

15 Wengi wao watajikwaa;

wataanguka na kuvunjika,

watategwa na kunaswa.”

16 Funga ushuhuda na kutia muhuri sheria

miongoni mwa wanafunzi wangu.

17 NitamngojeaBwana,

ambaye ameificha nyumba ya Yakobo uso wake.

Nitaliweka tumaini langu kwake.

18 Niko hapa, pamoja na watoto ambaoBwanaamenipa. Sisi ni ishara na mfano wake katika Israeli, kutoka kwaBwanaMwenye Nguvu Zote, anayeishi juu ya Mlima Sayuni.

19 Wakati watu wanapowaambia ninyi kutafuta ushauri kwa waaguzi na wenye kuongea na mizimu, ambao hunongʼona na kunungʼunika, je, watu wasingeuliza kwa Mungu wao? Kwa nini watake shauri kwa wafu kwa ajili ya walio hai?

20 Kwa sheria na kwa ushuhuda! Kama hawatasema sawasawa na neno hili, hawana mwanga wa mapambazuko.

21 Watazunguka katika nchi yote, wakiwa na dhiki na njaa. Watakapotaabika kwa njaa, watapatwa na hasira kali, nao, wakiwa wanatazama juu, watamlaani mfalme wao na Mungu wao.

22 Kisha wataangalia duniani na kuona tu dhiki na giza, hofu na huzuni tupu, nao watasukumiwa kwenye giza nene kabisa.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/8-6787976f18db72f78a8c589a8c126486.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 9

Kwa Ajili Yetu Mtoto Amezaliwa

1 Hata hivyo, hapatakuwepo huzuni tena kwa wale waliokuwa katika dhiki. Wakati uliopita aliidhili nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, lakini katika siku zijazo ataiheshimu Galilaya ya Mataifa, karibu na njia ya bahari, kando ya Yordani:

2 Watu wanaotembea katika giza

wameona nuru kuu,

wale wanaoishi katika nchi ya uvuli wa mauti,

nuru imewazukia.

3 Umelikuza taifa,

na kuzidisha furaha yao,

wanafurahia mbele zako,

kama watu wanavyofurahia wakati wa mavuno,

kama watu wafurahivyo

wagawanyapo nyara.

4 Kama vile siku ya kushindwa kwa Wamidiani,

umevunja nira iliyowalemea,

ile gongo mabegani mwao na

fimbo yake yeye aliyewaonea.

5 Kila kiatu cha askari kilichotumiwa vitani,

na kila vazi lililovingirishwa katika damu

vitawekwa kwa ajili ya kuchomwa,

vitakuwa kuni za kuwasha moto.

6 Kwa maana, kwa ajili yetu mtoto amezaliwa,

tumepewa mtoto mwanaume,

nao utawala utakuwa mabegani mwake.

Naye ataitwa

Mshauri wa Ajabu, Mungu Mwenye Nguvu,

Baba wa Milele, Mfalme wa Amani.

7 Kuongezeka kwa utawala wake na amani

hakutakuwa na mwisho.

Atatawala katika kiti cha enzi cha Daudi

na juu ya ufalme wake,

akiuthibitisha na kuutegemeza

kwa haki na kwa adili,

tangu wakati huo na hata milele.

Wivu waBwanaMwenye Nguvu Zote

utatimiza haya.

Hasira Ya Bwana Dhidi Ya Israeli

8 Bwana ametuma ujumbe dhidi ya Yakobo,

utamwangukia Israeli.

9 Watu wote watajua hili:

Efraimu na wakazi wa Samaria,

wanaosema kwa kiburi

na majivuno ya mioyo,

10 “Matofali yameanguka chini,

lakini tutajenga tena kwa mawe yaliyochongwa,

mitini imeangushwa,

lakini tutapanda mierezi badala yake.”

11 LakiniBwanaamemtia nguvu adui wa Resini dhidi yao

na kuchochea watesi wao.

12 Waashuru kutoka upande wa mashariki

na Wafilisti kutoka upande wa magharibi

wameila Israeli kwa kinywa kilichopanuliwa.

Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali,

mkono wake bado umeinuliwa juu.

13 Lakini watu hawajamrudia yeye aliyewapiga,

wala hawajamtafutaBwanaMwenye Nguvu Zote.

14 Kwa hiyoBwanaatakatilia mbali kutoka Israeli kichwa na mkia,

tawi la mtende na tete katika siku moja.

15 Wazee na watu mashuhuri ndio vichwa,

nao manabii wanaofundisha uongo ndio mkia.

16 Wale wanaowaongoza watu hawa wanawapotosha,

nao wale wanaoongozwa wamepotoka.

17 Kwa hiyo Bwana hatawafurahia vijana,

wala hatawahurumia yatima na wajane,

kwa kuwa kila mmoja wao hamchi Mungu, nao ni waovu,

na kila kinywa kinanena upotovu.

Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali,

mkono wake bado umeinuliwa juu.

18 Hakika uovu huwaka kama moto;

huteketeza michongoma na miiba,

huwasha moto vichaka vya msituni,

hujiviringisha kuelekea juu kama nguzo ya moshi.

19 Kwa hasira yaBwanaMwenye Nguvu Zote

nchi itachomwa kwa moto,

nao watu watakuwa kuni za kuchochea moto.

Hakuna mtu atakayemhurumia ndugu yake.

20 Upande wa kuume watakuwa wakitafuna,

lakini bado wataona njaa;

upande wa kushoto watakuwa wakila,

lakini hawatashiba.

Kila mmoja atajilisha kwa nyama ya mtoto wake mwenyewe:

21 Manase atamla Efraimu,

naye Efraimu atamla Manase;

nao pamoja watakuwa kinyume na Yuda.

Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali,

mkono wake bado umeinuliwa juu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/9-6adfeab4b4b730c340c8e2b1ad422194.mp3?version_id=1627—