Categories
Hagai

Hagai Utangulizi

Utangulizi

Hagai ni moja ya vitabu vitatu vya kinabii vya Agano la Kale vilivyoandikwa baada ya uhamisho. Hagai na Zekaria ndio waliowatia moyo watu waliorudi kutoka uhamishoni kujenga upya Hekalu baada ya Mfalme Dario kupitisha amri kuwaruhusu Wayahudi kurudi Yerusalemu.

Kundi la kwanza la Wayahudi liliporudi Yerusalemu liliweka msingi wa Hekalu jipya wakiwa na furaha na matumaini makubwa. Hata hivyo, Wasamaria na majirani wengine walipinga ujenzi huo kwa nguvu nyingi na kuwakatisha tamaa wafanyakazi, na hata kuufanya ujenzi huo usimame. Watu wakageukia ujenzi wa nyumba zao wenyewe. Ujumbe wa Hagai ulikuwa kwamba ni wakati wa kujenga nyumba ya Mungu.

Mwandishi

Hagai.

Kusudi

Kuwahimiza watu kujenga upya Hekalu la

Bwana

, na kuwahamasisha kuyatengeneza maisha yao upya na Mungu ili waweze kupata baraka zake.

Mahali

Yerusalemu.

Tarehe

520 K.K.

Wahusika Wakuu

Hagai, Zerubabeli, Yoshua.

Wazo Kuu

Hagai aliwaambia watu kwamba utukufu wa Hekalu walilokuwa wanajenga ungekuwa mkubwa kuliko ule wa Hekalu lililotangulia, ingawaje halingekuwa imara kama la kwanza. Hili Hekalu lingekuwa bora zaidi kwa sababu Mungu angelijaza utukufu wake ndani yake.

Mambo Muhimu

Kuwaita watu kujenga upya Hekalu la Yerusalemu lililobomolewa, na ahadi ya Mungu ya kuwabariki kama wangemtii.

Mgawanyo

Wito wa kujenga Hekalu (

1:1-15

)

Matumaini ya Hekalu jipya (

2:1-9

)

Baraka zilizoahidiwa (

2:10-19

)

Ushindi wa mwisho wa Mungu (

2:20-23

).

Categories
Hagai

Hagai 1

Wito Wa Kuijenga Nyumba Ya Bwana

1 Katika mwaka wa pili wa utawala wa Mfalme Dario wa Uajemi, katika siku ya kwanza ya mwezi wa sita, neno laBwanalilikuja kupitia kwa nabii Hagai kwenda kwa Zerubabeli mwana wa Shealtieli, mtawala wa Yuda na kwa Yoshuamwana wa kuhani mkuu Yehosadaki:

2 Hivi ndivyo asemavyoBwanaMwenye Nguvu Zote: “Hawa watu husema, ‘Wakati haujawadia wa kujenga nyumba yaBwana.’ ”

3 Kisha neno laBwanalikaja kupitia kwa nabii Hagai:

4 “Je, ni wakati wenu ninyi wa kuishi katika nyumba zenu zilizojengwa vizuri, wakati hii nyumba ikibaki, gofu?”

5 Sasa hili ndilo asemaloBwanaMwenye Nguvu Zote: “Zitafakarini vyema njia zenu.

6 Mmepanda vingi, lakini mmevuna haba. Mnakula lakini hamshibi, mnakunywa, lakini hamtosheki. Mnavaa nguo, lakini hamsikii joto. Mnapata mishahara, lakini inatoweka kama imewekwa kwenye mfuko uliotobokatoboka.”

7 Hili ndilo asemaloBwanaMwenye Nguvu Zote: “Zitafakarini vyema njia zenu.

8 Pandeni milimani mkalete miti na kujenga nyumba, ili nipate kuifurahia, na nitukuzwe,” asemaBwana.

9 “Mlitarajia mengi, kumbe, yametokea kidogo. Ulichokileta nyumbani nilikipeperusha. Kwa nini?” asemaBwanaMwenye Nguvu Zote. “Ni kwa sababu ya nyumba yangu, inayobaki katika hali ya magofu, wakati kila mmoja wenu anajishughulisha na nyumba yake mwenyewe.

10 Kwa hiyo, kwa sababu yenu mbingu zimezuia umande wake na ardhi mavuno yake.

11 Niliita ukame mashambani na milimani, kwenye nafaka, mvinyo mpya, mafuta pamoja na chochote kinachozalishwa na ardhi, juu ya watu na ngʼombe, pamoja na kazi za mikono yenu.”

12 Kisha Zerubabeli mwana wa Shealtieli, Yoshua kuhani mkuu mwana wa Yehosadaki, pamoja na mabaki yote ya watu wakaitii sauti yaBwanaMungu wao pamoja na ujumbe wa nabii Hagai, kwa sababu alikuwa ametumwa naBwanaMungu wao. Watu walimwogopaBwana.

13 Kisha Hagai, mjumbe waBwana, akawapa watu ujumbe huu waBwana: “Mimi niko pamoja nanyi,” asemaBwana.

14 Kwa hiyoBwanaakachochea roho ya Zerubabeli mwana wa Shealtieli, mtawala wa Yuda, na roho ya kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki, pamoja na roho za mabaki yote ya watu. Walikuja wakaanza kufanya kazi katika nyumba yaBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wao,

15 katika siku ya ishirini na nne mwezi wa sita, katika mwaka wa pili wa utawala wa Mfalme Dario.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/HAG/1-69a75d53ced7552db5a3c2fe4a8597fc.mp3?version_id=1627—

Categories
Hagai

Hagai 2

Utukufu Ulioahidiwa Wa Nyumba Mpya

1 Katika siku ya ishirini na moja ya mwezi wa saba, neno laBwanalilikuja kupitia nabii Hagai, kusema:

2 “Sema na Zerubabeli mwana wa Shealtieli, mtawala wa Yuda, kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki, na mabaki ya watu. Uwaulize,

3 ‘Ni nani miongoni mwenu aliyebaki ambaye aliiona hii nyumba katika utukufu wake wa mwanzo? Sasa inaonekanaje kwenu? Je, haionekani kwenu kama si kitu?

4 Lakini sasa uwe imara, ee Zerubabeli,’ asemaBwana. ‘Kuwa imara, ee kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki. Mwe imara, enyi watu wote wa nchi,’ asemaBwana, ‘na mfanye kazi. Kwa kuwa mimi nipo pamoja nanyi,’ asemaBwanaMwenye Nguvu Zote.

5 ‘Hili ndilo nililoagana nanyi mlipotoka katika nchi ya Misri. Pia Roho wangu anadumu katikati yenu. Msiogope.’

6 “Hili ndilo asemaloBwanaMwenye Nguvu Zote: ‘Baada ya muda kidogo kwa mara nyingine nitazitikisa mbingu na nchi, bahari na nchi kavu.

7 Nitatikisa mataifa yote, nacho kile kinachotamaniwa na mataifa yote kitakuja, nami nitaujaza utukufu katika nyumba hii,’ asemaBwanaMwenye Nguvu Zote.

8 ‘Fedha ni mali yangu na dhahabu ni mali yangu,’ asemaBwanaMwenye Nguvu Zote.

9 ‘Utukufu wa nyumba hii ya sasa utakuwa mkubwa kuliko utukufu wa ile nyumba ya mwanzoni,’ asemaBwanaMwenye Nguvu Zote. ‘Na mahali hapa nitawapa amani,’ asemaBwanaMwenye Nguvu Zote.”

Baraka Kwa Watu Waliotiwa Unajisi

10 Katika siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, katika mwaka wa pili wa utawala wa Mfalme Dario, neno laBwanalilikuja kwa nabii Hagai:

11 “Hili ndilo asemaloBwanaMwenye Nguvu Zote: ‘Ulizeni makuhani jinsi sheria inavyosema:

12 Kama mtu akibeba nyama iliyowekwa wakfu katika pindo la vazi lake, kisha lile pindo likagusa mkate au mchuzi, divai, mafuta au chakula kingine, je, kitu hicho kitakuwa kimewekwa wakfu?’ ”

Makuhani wakajibu, “La hasha.”

13 Kisha Hagai akasema, “Je, kama mtu aliyetiwa unajisi kwa kugusa maiti akigusa mojawapo ya vitu hivi, kitu hicho kitakuwa kimetiwa unajisi?”

Makuhani wakajibu, “Ndiyo, huwa kimenajisiwa.”

14 Kisha Hagai akasema, “ ‘Basi ndivyo walivyo machoni pangu hawa watu na taifa hili,’ asemaBwana. ‘Lolote wafanyalo na chochote watoacho hapo ni najisi.

15 “ ‘Sasa fikirini kwa uangalifu kuanzia leo na kuendelea: tafakarini jinsi mambo yalivyokuwa kabla halijawekwa jiwe moja juu ya lingine katika Hekalu laBwana.

16 Wakati mtu alipoendea lundo la nafaka la vipimo ishirini, kulikuwa na vipimo kumi tu. Wakati mtu alipoendea pipa la mvinyo ili kuchota vipimo hamsini, kulikuwa na vipimo ishirini tu.

17 Kazi zenu zote za mikono nilizipiga kwa ukame, ukungu na mvua ya mawe, lakini hata hivyo, hamkunigeukia mimi,’ asemaBwana.

18 ‘Tangu leo na kuendelea, kuanzia siku hii ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, tafakarini siku ambayo msingi wa Hekalu laBwanauliwekwa. Tafakarini:

19 Je, bado kuna mbegu iliyobakia ghalani? Mpaka sasa, hakuna mzabibu au mtini, mkomamanga wala mzeituni uliozaa tunda.

“ ‘Kuanzia leo na kuendelea, nitawabariki.’ ”

Zerubabeli Pete Ya Muhuri Ya Bwana

20 Neno laBwanalikamjia Hagai kwa mara ya pili katika siku ya ishirini na nne ya mwezi kusema:

21 “Mwambie Zerubabeli mtawala wa Yuda kwamba nitazitikisa mbingu na nchi.

22 Nitapindua viti vya enzi vya falme, na kuziharibu kabisa nguvu za falme za kigeni. Nitapindua magari ya vita pamoja na waendeshaji wake; farasi na wapanda farasi wataanguka, kila mmoja kwa upanga wa ndugu yake.

23 “ ‘Katika siku ile,’ asemaBwanaMwenye Nguvu Zote, ‘nitakuchukua wewe, mtumishi wangu Zerubabeli mwana wa Shealtieli,’ asemaBwana. ‘Nitakufanya kama pete yangu ya muhuri, kwa kuwa nimekuchagua,’ asemaBwanaMwenye Nguvu Zote.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/HAG/2-26cce82c34d9eebd11892eb101f1a27b.mp3?version_id=1627—