Categories
Habakuki

Habakuki Utangulizi

Utangulizi

Habakuki maana yake ni “Kumbatia.” Alikuwa nabii wa Yuda wa kabila la Lawi, mmoja wa waimbaji katika Hekalu. Kitabu hiki kimeandikwa kwa mtindo wa mazungumzo kati ya Mungu na nabii. Habakuki hakuelewa jinsi gani Mungu angeweza kuwatumia Wakaldayo, waliokuwa waovu kuliko Wayahudi, kutekeleza hukumu dhidi ya watu waliokuwa wamechaguliwa na Mungu. Jibu la Mungu lilikuwa kwamba wenye haki wangeishi kwa imani kwa Mungu, na kwamba walikuwa na uhakika kwamba Mungu alikuwa anafanya lililo sahihi. Mungu alimwambia Habakuki kwamba punde si punde Wakaldayo wangehukumiwa, na kwamba hatimaye haki ingeshinda kwa ajili ya watu wa Mungu.

Mwandishi

Habakuki.

Kusudi

Kuonyesha kwamba bado Mungu anaitawala dunia. Hata kama tunaona uovu ukishamiri, kuna siku Mungu atahukumu na kuadhibu huo uovu, na hatimaye kuuangamiza kabisa, usiwepo tena.

Mahali

Yuda.

Tarehe

Kati ya 612–589 K.K.

Wahusika Wakuu

Habakuki, na Wakaldayo.

Wazo Kuu

Mungu anaweza kuwatumia waovu kuadhibu watu wake wanapotenda dhambi kwa nia ya kuwarudisha kwake. Lakini hao waovu wakiisha kutimiza kusudi la Mungu, wao nao huadhibiwa zaidi.

Mambo Muhimu

Mungu hutumia watu waovu kuwaadhibu watu wake wanapokosea. Imani na mamlaka ya Mungu ni uhakika kwamba Mungu ana haki katika njia zake zote.

Mgawanyo

Swali la Habakuki na jibu la Mungu (

1:1-11

)

Swali la pili la Habakuki na jibu la Mungu (

1:12–2:20

)

Maombi ya Habakuki (

3:1-19

).

Categories
Habakuki

Habakuki 1

1 Neno alilopokea nabii Habakuki.

Lalamiko La Habakuki

2 EeBwana, hata lini nitakuomba msaada,

lakini wewe husikilizi?

Au kukulilia, “Udhalimu!”

Lakini hutaki kuokoa?

3 Kwa nini unanifanya nitazame dhuluma?

Kwa nini unavumilia makosa?

Uharibifu na udhalimu viko mbele yangu;

kuna mabishano na mapambano kwa wingi.

4 Kwa hiyo sheria imepotoshwa,

nayo haki haipo kabisa.

Waovu wanawazunguka wenye haki,

kwa hiyo haki imepotoshwa.

Jibu La Bwana

5 “Yatazame mataifa,

uangalie na ushangae kabisa.

Kwa sababu katika siku zako nitafanya kitu

ambacho hungeamini,

hata kama ungeambiwa.

6 Nitawainua Wakaldayo,

watu hao wakatili na wenye haraka,

ambao hupita dunia yote

kuteka mahali pa kuishi pasipo pao wenyewe.

7 Ni watu wanoogopwa na wanaotisha;

wenyewe ndio sheria yao,

na huinua heshima yao wenyewe.

8 Farasi wao ni wepesi kuliko chui,

na wakali kuliko mbwa mwitu wakati wa machweo.

Askari wapanda farasi wao huenda mbio;

waendesha farasi wao wanatoka mbali.

Wanaruka kasi kama tai ili kurarua;

9 wote wanakuja tayari kwa fujo.

Makundi yao ya wajeuri yanasonga mbele

kama upepo wa jangwani,

na kukusanya wafungwa

kama mchanga.

10 Wanawabeza wafalme,

na kuwadhihaki watawala.

Wanaicheka miji yote iliyozungushiwa maboma;

wanafanya malundo ya udongo na kuiteka hiyo miji.

11 Kisha wanapita kasi kama upepo na kusonga mbele:

watu wenye hatia, ambao nguvu zao ndio mungu wao.”

Lalamiko La Pili La Habakuki

12 EeBwana, je, wewe sio wa tangu milele?

Mungu wangu, Uliye Mtakatifu wangu, hatutakufa.

EeBwana, umewachagua wao ili watekeleze hukumu;

Ee Mwamba, umewaamuru watuadhibu.

13 Macho yako ni safi mno hata yasiweze kuutazama uovu,

wala huwezi kuvumilia makosa.

Kwa nini basi unawavumilia wadanganyifu?

Kwa nini unakuwa kimya wakati waovu

wanawameza wale wenye haki

kuliko wao wenyewe?

14 Umewafanya watu kama samaki baharini,

kama viumbe wa bahari wasio na mtawala.

15 Adui mwovu anawavuta wote kwa ndoana,

anawakamata katika wavu wake,

anawakusanya katika juya lake;

kwa hiyo anashangilia na anafurahi.

16 Kwa hiyo anatoa kafara kwa wavu wake,

na kuchoma uvumba kwa juya lake,

kwa kuwa kwa wavu wake anaishi kwa starehe,

na anafurahia chakula kizuri.

17 Je, aendelee kuwatoa walio katika wavu wake,

akiangamiza mataifa bila huruma?

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/HAB/1-2499ca2309f069f88b812cf56b5f222e.mp3?version_id=1627—

Categories
Habakuki

Habakuki 2

1 Nitasimama katika zamu yangu,

na kujiweka mwenyewe juu ya maboma;

nitatazama nione atakaloniambia,

na ni jibu gani nitakalotoa kuhusu lalamiko hili.

Jibu La Bwana

2 KishaBwanaakajibu:

“Andika ufunuo huu,

na ukaufanye wazi juu ya vibao,

ili mpiga mbiu akimbie nao.

3 Kwa kuwa ufunuo huu unasubiri wakati uliokubalika;

unazungumzia mambo ya mwisho,

na kamwe hautakosea.

Iwapo utakawia, wewe usubiri;

kwa hakika utakuja na hautachelewa.

4 “Tazama, amejaa majivuno;

anavyovitamani si vya unyofu:

lakini mwenye haki ataishi kwa imani yake:

5 hakika mvinyo humsaliti;

ni mwenye kiburi na hana amani.

Kwa sababu ni mlafi kama kuzimu

na kama kifo kamwe hatosheki;

anajikusanyia mataifa yote

na kuchukua watu wote mateka.

6 “Je, watu wote hawatamsuta kwa dhihaka na kumbeza, wakisema,

“ ‘Ole wake yeye akusanyaye bidhaa zilizoibwa

na kujifanyia utajiri kwa kutoza kwa nguvu!

Ataendelea hivi kwa muda gani?’

7 Je, wadai wako hawatainuka ghafula?

Je, hawataamka na kukufanya utetemeke?

Kisha utakuwa mhanga kwao.

8 Kwa kuwa umeteka nyara mataifa mengi,

watu waliobaki watakuteka nyara wewe.

Kwa kuwa umemwaga damu ya mtu;

umeharibu nchi na miji, na kila mmoja ndani yake.

9 “Ole wake yeye ajengaye milki yake kwa mapato ya udhalimu,

awekaye kiota chake juu,

ili kukimbia makucha ya uharibifu!

10 Umefanya shauri la maangamizi ya watu wengi,

ukiaibisha nyumba yako mwenyewe, na kupotewa na maisha yako.

11 Mawe ya kuta yatapiga kelele,

na mihimili ya kazi ya mbao itarudisha mwangwi wake.

12 “Ole wake yeye ajengaye mji kwa kumwaga

damu na kuusimamisha mji kwa uhalifu!

13 Je,BwanaMwenye Nguvu Zote hakuonyesha

kwamba kazi ya wanadamu ni mafuta tu kwa ajili ya moto,

na kwamba mataifa

yanajichosha bure?

14 Kwa kuwa dunia itajazwa na maarifa ya utukufu waBwana,

kama maji yaifunikavyo bahari.

15 “Ole wake yeye awapaye jirani zake kileo,

akiimimina kutoka kwenye kiriba

cha mvinyo mpaka wamelewa,

ili apate kutazama miili yao iliyo uchi.

16 Utajazwa na aibu badala ya utukufu.

Sasa ni zamu yako! Kunywa na ujifunue!

Kikombe kutoka kwenye mkono wa kuume waBwanakinakujia,

na aibu itafunika utukufu wako.

17 Ukatili ulioifanyia Lebanoni utakufunika,

na uharibifu uliowafanyia wanyama utakutisha.

Kwa sababu umemwaga damu ya mtu;

umeharibu nchi na miji na kila mmoja aliyeko ndani yake.

18 “Sanamu ina thamani gani,

kwani mwanadamu ndiye alichonga?

Ama kinyago kinachofundisha uongo?

Kwa kuwa yeye aliyekitengeneza

hutegemea kazi ya mikono yake mwenyewe;

hutengeneza sanamu zisizoweza kuzungumza.

19 Ole wake yeye auambiaye mti, ‘Uwe hai!’

Ama asemaye na jiwe lisilo na uhai, ‘Amka!’

Je, linaweza kuongoza?

Limefunikwa kwa dhahabu na fedha;

hakuna pumzi ndani yake.

20 LakiniBwanayuko katika Hekalu lake takatifu;

dunia yote na inyamaze mbele yake.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/HAB/2-04979c73066568b41ab1d6b764839675.mp3?version_id=1627—

Categories
Habakuki

Habakuki 3

Maombi Ya Habakuki

1 Sala ya nabii Habakuki iliyoimbwa kwa shigionothi.

2 Bwana, nimezisikia sifa zako;

nami naogopa kwa matendo yako, EeBwana.

Fufua kazi yako katikati ya miaka,

katikati ya miaka tangaza habari yako;

katika ghadhabu kumbuka rehema.

3 Mungu alitoka Temani,

yeye Aliye Mtakatifu kutoka Mlima Parani.

Utukufu wake ulifunika mbingu,

na sifa zake zikaifunika dunia.

4 Mngʼao wake ulikuwa kama jua lichomozalo;

mionzi ilimulika kutoka mkononi mwake,

ambako nguvu zake zilifichwa.

5 Tauni ilimtangulia;

maradhi ya kuambukiza yalifuata nyayo zake.

6 Alisimama, akaitikisa dunia;

alitazama, na kuyafanya mataifa yatetemeke.

Milima ya zamani iligeuka mavumbi

na vilima vilivyozeeka vikaanguka.

Njia zake ni za milele.

7 Niliona watu wa Kushani katika dhiki,

na makazi ya Midiani katika maumivu makali.

8 EeBwana, uliikasirikia mito?

Je, ghadhabu yako ilikuwa dhidi ya vijito?

Je, ulighadhibikia bahari

ulipoendesha farasi wako

na magari yako ya ushindi?

9 Uliufunua upinde wako

na kuita mishale mingi.

Uliigawa dunia kwa mito;

10 milima ilikuona ikatetemeka.

Mafuriko ya maji yakapita huko;

vilindi vilinguruma

na kuinua mawimbi yake juu.

11 Jua na mwezi vilisimama kimya mbinguni

katika mngʼao wa mishale yako inayoruka,

na katika mngʼao wa mkuki wako umeremetao.

12 Kwa ghadhabu ulipita juu ya dunia,

na katika hasira ulikanyaga mataifa.

13 Ulikuja kuwaokoa watu wako,

kumwokoa uliyemtia mafuta.

Ulimponda kiongozi wa nchi ya uovu,

ukamvua toka kichwani hadi wayo.

14 Kwa mkuki wake mwenyewe ulitoboa kichwa chake

wakati mashujaa wake walifurika nje kwa kishindo kututawanya,

wakifurahi kama walio karibu kutafuna

wale wanyonge waliokuwa mafichoni.

15 Ulikanyaga bahari kwa farasi wako,

ukisukasuka maji makuu.

16 Nilisikia na moyo wangu ukagonga kwa nguvu,

midomo yangu ikatetemeka kwa hofu niliposikia sauti;

uchakavu ukanyemelea mifupa yangu,

na miguu yangu ikatetemeka.

Hata hivyo nitasubiri kwa uvumilivu siku ya maafa

kuyajilia mataifa yaliyotuvamia.

17 Ingawa mtini hauchanui maua

na hakuna zabibu juu ya mizabibu,

ingawaje mzeituni hauzai,

na hata mashamba hayatoi chakula,

iwapo hakuna kondoo katika banda,

wala ngʼombe katika zizi,

18 hata hivyo nitashangilia katikaBwana,

nitamfurahia Mungu Mwokozi wangu.

19 BwanaMwenyezi ni nguvu yangu;

huifanya miguu yangu kama miguu ya ayala,

huniwezesha kupita juu ya vilima.

Kwa kiongozi wa uimbaji. Kwa vinanda vyangu vya nyuzi.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/HAB/3-bec1d4175c363e1dfe8d2d3391793194.mp3?version_id=1627—