Categories
Ezekieli

Ezekieli 40

Eneo La Hekalu Jipya

1 Katika mwaka wa ishirini na tano wa uhamisho wetu, mwanzoni mwa huo mwaka, siku ya kumi ya mwezi, katika mwaka wa kumi na nne baada ya kuanguka kwa mji, siku hiyo hiyo mkono waBwanaulikuwa juu yangu, naye akanipeleka huko.

2 Nikiwa katika maono ya Mungu alinichukua mpaka nchi ya Israeli, naye akaniweka kwenye mlima mrefu sana, ambako upande wa kusini kulikuwepo baadhi ya majengo ambayo yalionekana kama mji.

3 Akanipeleka huko, nami nikamwona mtu ambaye kuonekana kwake kulikuwa kama kuonekana kwa shaba. Alikuwa amesimama kwenye lango akiwa na kamba ya kitani na ufito wa kupimia mkononi mwake.

4 Mtu huyo akaniambia, “Mwanadamu, angalia kwa macho yako na usikie kwa masikio yako nawe uzingatie kitu nitakachokuonyesha, kwa kuwa ndiyo sababu umeletwa hapa. Iambie nyumba ya Israeli kila kitu utakachoona.”

Lango La Mashariki Kuelekea Ukumbi Wa Nje

5 Nikaona ukuta uliozunguka eneo lote la Hekalu. Ule ufito wa kupimia uliokuwa mkononi mwa yule mtu ulikuwa na urefu wa dhiraa ndefu sita,yaani, dhiraa ndefu ni sawa na dhiraa na nyanda nne, akapima ule ukuta. Ukuta huo ulikuwa na unene wa dhiraa ndefu sita na kimo cha dhiraa ndefu sita.

6 Kisha akaenda kwenye lango linaloelekea mashariki. Akapanda ngazi zake akapima kizingiti cha lango, nacho kilikuwa na kina cha huo ufito.

7 Vyumba vya kupumzikia vya walinzi vilikuwa na urefu wa huo ufito mmoja na upana wa huo ufito, kuta zilizogawa vyumba hivyo vya mapumziko zilikuwa na unene wa dhiraa tano.Nacho kizingiti cha lango lililokuwa karibu na ukumbi unaoelekea hekaluni ulikuwa na kina cha huo ufito.

8 Kisha akapima baraza ya njia ya lango,

9 ambayo ilikuwa na kina cha dhiraa nanena miimo yake ilikuwa na unene wa dhiraa mbili.Baraza ya lango ilielekea Hekalu.

10 Ndani ya lango la mashariki kulikuwepo vyumba vitatu vya kupumzikia kila upande, vyote vitatu vilikuwa na vipimo vilivyo sawa, nazo nyuso za kuta zilizotenganisha kila upande zilikuwa na vipimo vilivyo sawa.

11 Kisha akapima upana wa ingilio la lango, ilikuwa dhiraa kumi na urefu wake ulikuwa dhiraa kumi na tatu.

12 Mbele ya kila chumba cha kupumzikia kulikuwepo ukuta uliokuwa na kimo cha dhiraa mojakwenda juu, navyo hivyo vyumba vilikuwa dhiraa sita mraba.

13 Kisha akapima njia ya lango kuanzia juu ya ukuta wa nyuma wa chumba kimoja cha kupumzikia hadi juu ya ukuta wa nyuma wa chumba upande wa pili; kukawa na nafasi ya dhiraa ishirini na tano kuanzia lango la ukuta mmoja hadi lango la ukuta uliokuwa upande mwingine.

14 Akapima pia ukumbi, urefu wa dhiraa ishirinina lango linalofuatia hiyo nguzo kila upande wa huo ukumbi.

15 Umbali kuanzia ingilio la njia ya lango hadi mwisho kabisa wa baraza yake ulikuwa dhiraa hamsini.

16 Kulikuwa na vidirisha kwenye hivyo vyumba vya walinzi na nguzo za hivyo vyumba zilikuwa kwenye mzunguko wa hilo lango, vivyo hivyo kulikuwa na madirisha yaliyozunguka kuelekeana na ua na juu ya kila nguzo kulikuwa na mapambo ya miti ya mitende.

Ukumbi Wa Nje

17 Kisha akanileta katika ukumbi wa nje. Huko nikaona vyumba vingine pamoja na njia iliyokuwa imejengwa kuzunguka ukumbi wote, kulikuwa na vyumba thelathini vimepangana kando ya hiyo njia.

18 Njia hii iliyojengwa iliambaa na lango, ikiwa na urefu sawa na lango, hii ilikuwa ni njia ya chini.

19 Kisha akapima umbali kutoka ndani ya lango la chini mpaka nje ya ukumbi wa ndani, nao ulikuwa dhiraa mia mojaupande wa mashariki na dhiraa mia moja upande wa kaskazini.

Lango La Kaskazini

20 Kisha akapima urefu na upana wa lango linaloelekea kaskazini, kukabili ukumbi wa nje.

21 Vyumba vyake vilikuwa vitatu kila upande, kuta zilizogawanya vyumba na baraza ilikuwa na vipimo sawa na zile kuta za lango la kwanza. Zilikuwa na urefu wa dhiraa hamsini na upana wa dhiraa ishirini na tano.

22 Madirisha yake, baraza yake na nakshi yake ya miti ya mitende vilikuwa na vipimo sawasawa na vile vya lango linaloelekea mashariki. Kulikuwa na ngazi saba za kupandia huko, pamoja na baraza yake mkabala nazo.

23 Kulikuwa na lango kwenye ukumbi wa ndani lililoelekea lile lango la kaskazini, kama vile ilivyokuwa ule upande wa mashariki. Akapima kutoka lango moja hadi lile lililo mkabala nalo, lilikuwa dhiraa mia moja.

Lango La Kusini

24 Ndipo akaniongoza mpaka upande wa kusini, nami nikaona lango linaloelekea kusini. Akaipima miimo yake na baraza yake, navyo vilikuwa na vipimo sawa kama hivyo vingine.

25 Lango na baraza yake vilikuwa na madirisha membamba pande zote, kama madirisha ya huko kwingine. Ilikuwa na urefu wa dhiraa hamsini na upana wake dhiraa ishirini na tano.

26 Kulikuwa na ngazi saba za kupandia huko, pamoja na baraza yake mkabala nazo. Ilikuwa na nakshi za miti ya mitende kwenye kuta zilizogawanya vyumba kila upande.

27 Ukumbi wa ndani pia ulikuwa na lango lililoelekea kusini. Naye akapima kutoka lango hili mpaka kwenye lango la nje upande wa kusini; ilikuwa dhiraa mia moja.

Malango Ya Kuelekea Ukumbi Wa Ndani

28 Kisha akanileta mpaka ukumbi wa ndani kwa kupitia lango la kusini, naye akapima lango la kusini, ambalo lilikuwa na vipimo sawa na yale mengine.

29 Vyumba vyake, kuta zilizogawanya vyumba na ukumbi wake zilikuwa na vipimo sawasawa na zile nyingine. Hilo lango na baraza yake vilikuwa na madirisha pande zote. Navyo vilikuwa na urefu wa dhiraa hamsini na upana wa dhiraa ishirini na tano.

30 (Baraza za malango zilizozunguka ukumbi wa ndani zilikuwa na upana wa dhiraa ishirini na tano na kina cha dhiraa tano.)

31 Baraza yake ilielekeana na ukumbi wa nje, miimo yake ilinakshiwa miti ya mitende, kulikuwa na ngazi nane za kupandia huko.

32 Kisha akanileta mpaka kwenye ukumbi wa ndani ulioko upande wa mashariki, naye akalipima lango hilo, lilikuwa na vipimo vilivyo sawasawa na yale mengine.

33 Vyumba vyake, kuta zake na baraza yake vilikuwa na vipimo vilivyo sawa na vile vingine. Lile lango pamoja na baraza yake vilikuwa na madirisha pande zote. Urefu wake ulikuwa dhiraa hamsini na upana wake dhiraa ishirini na tano.

34 Baraza yake ilielekea ukumbi wa nje, miimo yake ilinakshiwa miti ya mitende pande zote. Kulikuwa na ngazi nane za kupandia huko.

35 Kisha akanileta mpaka kwenye lango la kaskazini na kulipima. Lilikuwa na vipimo sawa na yale mengine,

36 kama vile ilivyokuwa kwa vyumba, kuta zake na baraza yake, tena kulikuwa na madirisha pande zote. Ilikuwa na urefu wa dhiraa hamsini na upana wake dhiraa ishirini na tano.

37 Baraza yake ilielekeana na ukumbi wa nje, miimo yake ilinakshiwa miti ya mitende pande zote, kulikuwa na ngazi nane za kupandia huko.

Vyumba Vya Kutayarishia Dhabihu

38 Kulikuwa na chumba na mlango karibu na baraza katika kila njia ya ndani ya lango ambamo sadaka za kuteketezwa zilioshwa.

39 Kwenye baraza ya lile lango kulikuwepo meza mbili kila upande, ambako sadaka za kuteketezwa, sadaka za dhambi na sadaka za hatia zilichinjiwa.

40 Karibu na ukuta wa nje wa baraza ya lile lango karibu na ngazi kwenye ingilio kuelekea kaskazini kulikuwa na meza mbili, nako upande mwingine wa ngazi kulikuwepo na meza mbili.

41 Kwa hiyo kulikuwa na meza nne upande mmoja wa lango na nyingine nne upande mwingine, zote zilikuwa meza nane, ambapo dhabihu zilichinjiwa.

42 Pia kulikuwa na meza nne za mawe yaliyochongwa kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, kila meza ilikuwa na urefu wa dhiraa moja na nusu,upana wake dhiraa moja na nusu na kimo cha dhiraa moja. Juu ya meza hizo viliwekwa vyombo vya kuchinjia sadaka za kuteketezwa na dhabihu nyingine mbalimbali.

43 Kulikuwa na kulabu, urefu wake nyanda nne,zilikuwa zimeshikizwa ukutani pande zote. Meza zilikuwa kwa ajili ya nyama za sadaka.

Vyumba Kwa Ajili Ya Makuhani

44 Nje ya lango la ndani, kwenye ukumbi wa ndani, kulikuwa na vyumba viwili, kimoja upande wa lango la kaskazini nacho kilielekea kusini, kingine upande wa lango la kusini nacho kilielekea kaskazini.

45 Akaniambia, “Chumba kinachoelekea upande wa kusini ni kwa ajili ya makuhani ambao wana usimamizi wa hekaluni,

46 nacho chumba kinachoelekea upande wa kaskazini ni kwa ajili ya makuhani wenye usimamizi wa madhabahuni. Hawa ni wana wa Sadoki, ambao ndio Walawi pekee wanaoweza kumkaribiaBwanaili kuhudumu mbele zake.”

47 Ndipo alipopima ukumbi: nao ulikuwa mraba wa dhiraa mia moja urefu na upana. Madhabahu yalikuwa mbele ya Hekalu.

Hekalu

48 Akanileta mpaka kwenye baraza ya Hekalu naye akaipima miimo ya hiyo baraza, nayo ilikuwa na upana wa dhiraa tatukila upande. Upana wa ingilio ulikuwa dhiraa kumi na nnena kuta zake zilikuwa na upana wa dhiraa tatu kila upande.

49 Baraza ilikuwa na dhiraa ishirini kwenda juu na dhiraa kumi na mbilikuanzia mbele hadi nyuma. Kulikuwa na ngazi kumi za kupandia huko, pia kulikuwa na nguzo kwa kila upande wa miimo.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/EZK/40-90dfbba3fe1ad386d0ec90589fe487f2.mp3?version_id=1627—

Categories
Ezekieli

Ezekieli 41

1 Kisha yule mtu akanileta katika sehemu ya nje ya patakatifu, naye akaipima miimo; upana wake ulikuwa dhiraa sitakila upande.

2 Ingilio lilikuwa la upana wa dhiraa kumi na kuta zilizojitokeza kila upande zilikuwa na upana wa dhiraa tano. Pia akapima sehemu ya nje ya patakatifu, nayo ilikuwa na urefu wa dhiraa arobainina upana wa dhiraa ishirini.

3 Kisha akaingia sehemu takatifu ndani ya Hekalu na kupima miimo ya ingilio, kila mmoja ulikuwa na upana wa dhiraa mbili. Ingilio lilikuwa na upana wa dhiraa sita, na kuta zilizotokeza kila upande zilikuwa na upana wa dhiraa saba.

4 Naye akapima urefu wa sehemu takatifu ndani, nao ulikuwa dhiraa ishirini, na upana wake ulikuwa dhiraa ishirini hadi mwisho wa sehemu ya nje ya sehemu takatifu. Akaniambia, “Hapa ndipo Patakatifu pa Patakatifu.”

5 Kisha akapima ukuta wa Hekalu, nao ulikuwa na unene wa dhiraa sita, na kila chumba cha pembeni kuzunguka Hekalu kilikuwa na upana wa dhiraa nne.

6 Vyumba vya pembeni vilikuwa na ghorofa tatu, kimoja juu ya kingine, kila ghorofa ilikuwa na vyumba thelathini. Kulikuwa na boriti katika ukuta wote wa Hekalu ili kuimarisha vyumba vya pembeni, kwa hiyo boriti hizo hazikushikamanishwa kwenye ukuta wa Hekalu.

7 Vyumba vya pembeni vilivyozunguka Hekalu vilizidi kupanuka kulingana na sakafu zilivyokwenda juu. Ujenzi uliozunguka Hekalu ulijengwa kukwea juu, kwa hiyo vyumba vilipanuka kwa kadiri ya kila kimoja kilivyokwenda juu. Ngazi za kupandia zilianzia sakafu ya chini hadi sakafu ya juu kabisa kwa kupitia sakafu ya kati.

8 Nikaona pia kuwa Hekalu lilikuwa na kitako kilichoinuliwa pande zote, huu ulikuwa ndio msingi wa vile vyumba vya pembeni ambao ulikuwa na urefu wa ule ufito mmoja wa kupimia, yaani, dhiraa ndefu sita.

9 Ukuta wa nje wa vyumba vya pembeni ulikuwa na unene wa dhiraa tano. Eneo la wazi katikati ya vyumba vya pembeni vya Hekalu

10 na vyumba vya makuhani lilikuwa na upana wa dhiraa ishirini kuzunguka Hekalu pande zote.

11 Kulikuwa na maingilio kwenye vyumba vya pembeni kutokea eneo lililo wazi, moja upande wa kaskazini na lingine upande wa kusini, nao msingi uliounganisha lile eneo la wazi ulikuwa na upana wa dhiraa tano ukilizunguka lote.

12 Jengo lililoelekeana na ua wa Hekalu upande wa magharibi lilikuwa na upana wa dhiraa sabini. Ukuta wa jengo hilo ulikuwa na unene wa dhiraa tano, kulizunguka lote, urefu ulikuwa wa dhiraa tisini.

13 Kisha akapima Hekalu, lilikuwa na urefu wa dhiraa mia moja na ua wa Hekalu na jengo pamoja na kuta zake vilikuwa na urefu wa dhiraa mia moja pia.

14 Upana wa ua wa Hekalu upande wa mashariki, pamoja na upande wa mbele wa Hekalu ulikuwa dhiraa mia moja.

15 Kisha akapima urefu wa jengo linaloelekeana na ua upande wa nyuma wa Hekalu, pamoja na vyumba vyake kila upande, ilikuwa dhiraa mia moja.

Sehemu takatifu ya nje, sehemu takatifu ya ndani, pamoja na baraza inayoelekeana na ukumbi,

16 pamoja na vizingiti, madirisha membamba na vyumba vyote vitatu, kila kimoja pamoja na kizingiti vilifunikwa kwa mbao. Sakafu, ukuta mpaka kwenye madirisha na madirisha yenyewe vilifunikwa kwa mbao.

17 Katika nafasi iliyokuwa juu ya upande wa nje wa ingilio la sehemu takatifu ya ndani, na katika kuta zilizozunguka sehemu takatifu ya ndani na sehemu takatifu ya nje, kwa nafasi zilizo sawa,

18 kulinakshiwa makerubi na miti ya mitende. Miti ya mitende ilikuwa kati ya kerubi na kerubi. Kila kerubi alikuwa na nyuso mbili:

19 upande mmoja uso wa mwanadamu kuelekea mti wa mtende na upande mwingine uso wa simba ukielekea mti mwingine wa mtende. Ilinakshiwa kuzunguka Hekalu lote.

20 Kuanzia sakafu mpaka eneo lililo juu ya ingilio, palinakshiwa makerubi na miti ya mitende pamoja na kwenye ukuta wa nje wa patakatifu.

21 Mahali patakatifu pa nje palikuwa na miimo ya mlango uliokuwa mraba na ule uliokuwa katika Patakatifu Pa Patakatifu ulikuwa unafanana na huo mwingine.

22 Kulikuwa na madhabahu ya mbao kimo chake dhiraa tatu na ilikuwa dhiraa mbili mraba pande zote, tako lake na pande zake zilikuwa za mbao. Yule mtu akaniambia, “Hii ni meza ambayo iko mbele zaBwana.”

23 Mahali patakatifu pa nje na Patakatifu Pa Patakatifu zilikuwa na milango miwili.

24 Kila mlango ulikuwa na vipande viwili, vipande viwili vilivyoshikwa na bawaba vyenye kufunguka kwa kila mlango.

25 Juu ya hiyo milango ya Patakatifu palinakshiwa makerubi na miti ya mitende kama yale yaliyonakshiwa kwenye kuta, na kulikuwa na ubao ulioningʼinia mbele ya baraza kwa nje.

26 Katika kuta za pembeni za ukumbi kulikuwa na madirisha membamba yaliyonakshiwa miti ya mitende kila upande. Vyumba vya pembeni vya Hekalu pia vilikuwa vimefunikwa kwa mbao.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/EZK/41-80e6aeb20c415ab3db57fd246c32c901.mp3?version_id=1627—

Categories
Ezekieli

Ezekieli 42

Vyumba Vya Makuhani

1 Ndipo yule mtu akaniongoza kuelekea kaskazini mpaka kwenye ua wa nje na kunileta mpaka kwenye vyumba vinavyoelekeana na ua wa Hekalu na kuelekeana na ukuta wa nje upande wa kaskazini.

2 Jengo ambalo mlango wake ulielekea kaskazini lilikuwa na urefu wa dhiraa mia moja na upana wa dhiraa hamsini.

3 Mbele ya zile dhiraa ishirini za ule ua wa ndani unaoelekeana na ile njia ya ua wa nje, kuliinuka vyumba virefu kimoja baada ya kingine vya ghorofa tatu.

4 Mbele ya hivi vyumba kulikuwa na njia ya ndani yenye upana wa dhiraa kumi na urefu wa dhiraa mia moja. Milango yake ilikuwa upande wa kaskazini.

5 Basi vyumba vya juu vilikuwa vyembamba zaidi, kwa kuwa ujiaulichukua nafasi zaidi ndani yake kuliko katika vyumba vya sakafu ya chini na vya katikati ya jengo.

6 Vyumba katika ghorofa ya tatu havikuwa na nguzo, kama kumbi zilivyokuwa nazo, kwa hiyo eneo la sakafu ya vyumba vya juu lilikuwa ni dogo kuliko la sakafu ya chini na ya kati.

7 Kulikuwa na ukuta wa nje uliokuwa sambamba na vile vyumba na ukumbi wa nje, ulitokeza urefu wa dhiraa hamsini.

8 Wakati safu ya vyumba katika ua wa nje vilikuwa na urefu wa dhiraa hamsini, vile vyumba vilivyokuwa karibu zaidi na Hekalu vilikuwa na urefu wa dhiraa mia moja.

9 Vyumba vya chini vilikuwa na ingilio upande wa mashariki unapoingia kutoka ukumbi wa nje.

10 Upande wa kusini kufuata urefu wa ukuta wa ukumbi wa nje, unaopakana na ukumbi wa Hekalu na kuelekeana na ukuta wa nje, kulikuwa na vyumba

11 vyenye ujia unayopita mbele yake. Hivi vilifanana na vile vyumba vya upande wa kaskazini, vilikuwa na urefu na upana ulio sawa, mahali pa kutokea na vipimo vyake vilikuwa sawa. Kama ilivyokuwa milango ya upande wa kaskazini,

12 ndivyo ilivyokuwa milango ya vyumba vya upande wa kusini. Kulikuwa na ingilio kuanzia mwanzo wa njia ambao ulikuwa sambamba na ukuta wa pili uliokuwa upande wa mashariki, ambako ndiko kwa kuingia vyumbani.

13 Kisha akaniambia, “Vyumba vya upande wa kaskazini na vya upande wa kusini ambavyo vinaelekeana na ukumbi wa Hekalu ni vyumba vya makuhani, mahali ambapo wale makuhani ambao humkaribiaBwanawatakula zile sadaka takatifu sana. Huko ndiko watakakoweka zile sadaka takatifu sana, yaani, sadaka za nafaka, sadaka za dhambi na sadaka za hatia, kwa kuwa mahali ni patakatifu.

14 Mara makuhani waingiapo mahali patakatifu, hawaruhusiwi kwenda kwenye ukumbi wa nje mpaka wayaache mavazi ambayo walivaa wakiwa wanahudumu, kwa kuwa hayo mavazi ni matakatifu. Inawapasa kuvaa mavazi mengine kabla hawajakaribia eneo lililo wazi kwa ajili ya watu.”

15 Alipomaliza kupima vile vilivyokuwa katika eneo la ndani la Hekalu, akanitoa nje kupitia lango la upande wa mashariki na kupima eneo lote linalozunguka:

16 Akapima upande wa mashariki kwa ule ufito wa kupimia, nao ulikuwa dhiraa 500

17 Akapima upande wa kaskazini, nao ulikuwa dhiraa 500 kwa ufito ule wa kupimia.

18 Tena akapima upande wa kusini, nao ulikuwa dhiraa 500 kwa ufito ule wa kupimia.

19 Kisha akageukia upande wa magharibi na kuupima, ulikuwa dhiraa 500 kwa ufito ule wa kupimia.

20 Hivyo akapima eneo katika pande zote nne. Lilikuwa na ukuta kulizunguka wenye urefu wa dhiraa 500 na upana wa dhiraa 500, uliotenganisha mahali Patakatifu na eneo la watu wote.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/EZK/42-ed6d53e7c715407ff1430b43634e1865.mp3?version_id=1627—

Categories
Ezekieli

Ezekieli 43

Utukufu Warudi Hekaluni

1 Kisha yule mtu akanileta kwenye lango linaloelekea upande wa mashariki,

2 nami nikaona utukufu wa Mungu wa Israeli ukija kutoka upande wa mashariki. Sauti yake ilikuwa kama ya ngurumo ya maji yaendayo kasi, nayo nchi ikangʼaa kwa utukufu wake.

3 Maono niliyoyaona yalikuwa kama maono yale niliyokuwa nimeyaona wakati Mungu alipokuja kuangamiza mji na kama maono niliyokuwa nimeyaona kando ya Mto wa Kebari, nami nikaanguka kifudifudi.

4 Utukufu waBwanaukaingia hekaluni kwa kupitia lango linaloelekea upande wa mashariki.

5 Kisha Roho akanichukua na kunileta katika ule ua wa ndani, nao utukufu waBwanaulilijaza Hekalu.

6 Wakati yule mtu akiwa amesimama kando yangu, nilisikia mtu mmoja akisema nami kutoka ndani ya Hekalu.

7 Akasema, “Mwanadamu, hapa ni mahali pa kiti changu cha enzi na mahali pa kuweka nyayo za miguu yangu. Hapa ndipo nitakapoishi miongoni mwa Waisraeli milele. Kamwe nyumba ya Israeli hawatalinajisi tena Jina langu takatifu, yaani, wao wala wafalme wao, kwa ukahaba wao na kwa sanamu zao zisizokuwa na uhai za wafalme wao katika mahali pao pa juu pa kuabudia miungu.

8 Walipoweka kizingiti chao karibu na kizingiti changu na miimo yao ya milango karibu na miimo yangu, pakiwa na ukuta tu kati yangu na wao, walilinajisi Jina langu takatifu kwa matendo yao ya machukizo. Kwa sababu hiyo niliwaangamiza kwa hasira yangu.

9 Basi sasa na waweke mbali nami ukahaba wao na sanamu za wafalme wao zisizo na uhai, nami nitakaa miongoni mwao milele.

10 “Mwanadamu, elezea hilo Hekalu kwa watu wa Israeli, ili wapate kuona aibu kwa ajili ya dhambi zao. Wao na wapime hicho kielelezo.

11 Wakishaona aibu kwa ajili ya yale yote waliyotenda, wafahamishe kielelezo cha hilo Hekalu, yaani mpangilio wake, maingilio yake ya kutoka na kuingia, kielelezo chake chote, na masharti yake yote na sheria zake zote. Yaandike haya mbele yao ili wapate kuwa waaminifu kwa hicho kielelezo chake na kufuata masharti yake yote.

12 “Hii ndiyo sheria ya Hekalu: Eneo lote linalozunguka Hekalu juu ya mlima litakuwa takatifu kuliko yote. Hii ndiyo sheria ya Hekalu.

Madhabahu

13 “Hivi ndivyo vipimo vya madhabahu kwa dhiraa ndefu, yaani, dhiraa moja na nyanda nne:Tako lake liwe na kina cha hiyo dhiraa moja na upana wa hiyo dhiraa moja, ikiwa na ukingo wa shibiri mojakuizunguka pembeni. Hiki kitakuwa ndicho kimo cha madhabahu:

14 Kimo cha msingi kuanzia usawa wa ardhi mpaka kwenye mfereji sehemu ya chini kimo chake ni dhiraa mbili na upana wake ni dhiraa moja na kuanzia kwenye ukingo mdogo hadi kwenye ukingo mpana kimo chake ni dhiraa nne na upana wake ni dhiraa moja.

15 Pale pawashwapo moto madhabahuni kimo chake kitakuwa dhiraa nne, na pembe nne zinazoelekeza juu kutoka pale pawashwapo moto.

16 Pale pawashwapo moto pa madhabahu ni mraba, urefu wake ni dhiraa kumi na mbilina upana wa dhiraa kumi na mbili.

17 Pia sehemu ya juu ni mraba, urefu wake dhiraa kumi na nne na upana wa dhiraa kumi na nne, ikiwa na ukingo wa nusu dhiraa na mfereji kuizunguka madhabahu. Ngazi za kupandia madhabahuni zitaelekea upande wa mashariki.”

18 Kisha akaniambia, “Mwanadamu, hili ndiloBwanaMwenyezi asemalo: Haya ndiyo yatakayokuwa masharti ya kutoa dhabihu za kuteketezwa na kunyunyiza damu juu ya madhabahu itakapokuwa imejengwa.

19 Utatoa fahali mchanga kuwa sadaka ya dhambi kwa makuhani, ambao ni Walawi, wa jamaa ya Sadoki, ndio watakaonikaribia kuhudumu mbele zangu, asemaBwanaMwenyezi.

20 Itakupasa kuchukua baadhi ya hiyo damu ya mnyama huyo na kuiweka juu ya hizo pembe nne za madhabahu na juu ya ncha zake nne za sehemu ya juu kuzunguka ukingo wote, ili kuitakasa madhabahu na kufanya upatanisho kwa ajili yake.

21 Itakupasa kumchukua huyo fahali mchanga kwa ajili ya sadaka ya dhambi na kumteketeza mahali palipoagizwa katika eneo la Hekalu nje ya mahali Patakatifu.

22 “Siku ya pili yake utamtoa beberu asiye na dosari kwa ajili ya sadaka ya dhambi, nayo madhabahu itatakaswa kama ilivyotakaswa kwa yule fahali.

23 Utakapokuwa umemaliza kazi ya kuitakasa, utamtoa fahali mchanga pamoja na kondoo dume toka kwenye kundi, wote wawe hawana dosari.

24 Utawatoa mbele zaBwana, nao makuhani watanyunyizia chumvi juu yao na kuwatoa kuwa sadaka ya kuteketezwa kwaBwana.

25 “Kwa siku saba itakupasa kutoa beberu kila siku kwa ajili ya sadaka ya dhambi, pia itakupasa kutoa fahali mchanga na kondoo dume kutoka zizini, wote wawe hawana dosari.

26 Kwa siku saba itawapasa kufanya upatanisho kwa ajili ya madhabahu na kuitakasa na hivyo ndivyo watakavyoiweka wakfu.

27 Mwishoni mwa hizi siku saba, kuanzia siku ya nane na kuendelea, itawapasa makuhani kutoa sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka za amani juu ya madhabahu. Kisha nitawakubali ninyi, asemaBwanaMwenyezi.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/EZK/43-d0abc399774505642729302e3f2b8aca.mp3?version_id=1627—

Categories
Ezekieli

Ezekieli 44

Mkuu, Walawi, Makuhani

1 Ndipo yule mtu akanirudisha mpaka kwenye lango la nje la mahali Patakatifu, lile linaloelekea upande wa mashariki, nalo lilikuwa limefungwa.

2 Bwanaakaniambia, “Lango hili litabaki limefungwa. Haliruhusiwi kufunguliwa, wala hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kuingilia kwenye lango hili. Litabaki limefungwa kwa sababuBwana, Mungu wa Israeli, ameingia kwa kupitia lango hili.

3 Yeye aliye mkuu peke yake ndiye anayeweza kukaa penye njia ya hilo lango na kula chakula mbele zaBwana. Itampasa aingie kwa njia hiyo ya lango la ukumbini na kutokea njia iyo hiyo.”

4 Kisha yule mtu akanileta kwa njia ya lango la kaskazini mpaka mbele ya Hekalu. Nikatazama nami nikauona utukufu waBwanaukilijaza Hekalu laBwana, nami nikaanguka kifudifudi.

5 Bwanaakaniambia, “Mwanadamu, angalia kwa uangalifu, usikilize kwa bidii na uzingatie kila kitu ninachokuambia kuhusu masharti yote yanayohusu Hekalu laBwana. Uwe mwangalifu kuhusu wale wanaoruhusiwa hekaluni na wale wasioruhusiwa kuingia mahali patakatifu.

6 Iambie nyumba ya kuasi ya Israeli, ‘Hili ndiloBwanaMwenyezi asemalo: Matendo yenu ya machukizo yatosha, ee nyumba ya Israeli!

7 Zaidi ya matendo yenu yote ya machukizo, mmewaleta wageni wasiotahiriwa mioyo na miili katika patakatifu pangu, mkilinajisi Hekalu langu, huku mkinitolea chakula, mafuta ya wanyama na damu, nanyi mmevunja Agano langu.

8 Badala ya kutimiza wajibu wenu kuhusiana na vitu vyangu vitakatifu, mmeweka watu wengine kuwa viongozi katika patakatifu pangu.

9 Hili ndiloBwanaMwenyezi asemalo: Hakuna mgeni asiyetahiriwa moyo na mwilini anayeruhusiwa kuingia patakatifu pangu, wala hata wageni wanaoishi miongoni mwa Waisraeli.

10 “ ‘Walawi walioniacha wakati Waisraeli walipopotoka wakatoka kwangu na kutangatanga kwa kufuata sanamu zao, watachukua adhabu ya dhambi zao.

11 Wanaweza wakatumika katika mahali patakatifu pangu, wakiwa na uangalizi wa malango ya Hekalu, nao watachinja sadaka za kuteketezwa na dhabihu kwa ajili ya watu na kusimama mbele ya watu ili kuwahudumia.

12 Lakini kwa sababu waliwatumikia watu mbele ya sanamu zao na kuifanya nyumba ya Israeli ianguke kwenye dhambi, kwa hiyo nimeapa kwa mkono ulioinuliwa kwamba ni lazima wachukue matokeo ya dhambi yao, asemaBwanaMwenyezi.

13 Hawaruhusiwi kukaribia ili kunitumikia kama makuhani wala kukaribia chochote changu kilicho kitakatifu au sadaka iliyo takatifu kupita zote, bali watachukua aibu ya matendo yao ya kuchukiza.

14 Lakini nitawaweka katika uangalizi wa Hekalu na kazi zote zile zinazotakiwa kufanyika ndani yake.

15 “ ‘Lakini makuhani, ambao ni Walawi na wazao wa Sadoki, ambao walitimiza wajibu wao kwa uaminifu katika patakatifu pangu wakati Waisraeli walipopotoka, watakaribia ili kutumika mbele zangu. Itawapasa wasimame mbele zangu ili kutoa dhabihu za mafuta ya wanyama na damu, asemaBwanaMwenyezi.

16 Wao peke yao ndio wenye ruhusa ya kuingia mahali patakatifu pangu. Wao peke yao ndio watakaokaribia meza yangu ili kuhudumu mbele zangu na kufanya utumishi wangu.

17 “ ‘Watakapoingia kwenye malango ya ukumbi wa ndani, watavaa nguo za kitani safi, hawaruhusiwi kamwe kuvaa mavazi ya sufu wakati wanapokuwa wakihudumu kwenye malango ya ukumbi wa ndani wala ndani ya Hekalu.

18 Watavaa vilemba vya kitani safi vichwani mwao na nguo za ndani za kitani safi viunoni mwao. Hawatavaa chochote kitakachowafanya kutoa jasho.

19 Watakapotoka ili kuingia katika ukumbi wa nje mahali watu walipo, watavua nguo walizokuwa wakihudumu nazo na wataziacha katika vyumba vitakatifu nao watavaa nguo nyingine, ili kwamba wasije wakaambukiza watu utakatifu kwa njia ya mavazi yao.

20 “ ‘Hawatanyoa nywele za vichwa vyao wala kuziacha ziwe ndefu, bali watazipunguza.

21 Kuhani yeyote asinywe mvinyo aingiapo katika ukumbi wa ndani.

22 Wasioe wanawake wajane wala walioachika, inawapasa kuoa wanawake bikira wenye heshima wa Israeli au wajane wa makuhani.

23 Watawafundisha watu wangu tofauti kati ya vitu vitakatifu na vitu vya kawaida na kuwaonyesha jinsi ya kupambanua kati ya vitu najisi na vitu safi.

24 “ ‘Katika magombano yoyote, makuhani watatumika kama mahakimu na kuamua hilo jambo kufuatana na sheria zangu. Watazishika sheria zangu na maagizo yangu katika sikukuu zangu zote zilizoamriwa, nao watatakasa Sabato zangu.

25 “ ‘Kuhani asijitie unajisi kwa kukaribia maiti, lakini, kama mtu aliyekufa alikuwa baba yake au mama yake, mwana au binti yake, ndugu yake au dada ambaye hajaolewa, basi aweza kujitia unajisi kwa hao.

26 Baada ya kujitakasa, atakaa hali hiyo kwa muda wa siku saba.

27 Siku atakapoingia katika ukumbi wa ndani wa mahali patakatifu ili kuhudumu, atatoa sadaka ya dhambi kwa ajili yake mwenyewe, asemaBwanaMwenyezi.

28 “ ‘Mimi nitakuwa ndio urithi pekee walio nao makuhani katika Israeli. Msiwape wao milki, mimi nitakuwa milki yao.

29 Wao watakula sadaka za nafaka, sadaka za dhambi na sadaka za hatia na kila kitu kitakachotolewa kwaBwanakatika Israeli kitakuwa chao.

30 Yote yaliyo bora ya malimbuko ya vitu vyote na matoleo yenu maalum vitakuwa vya makuhani. Inawapasa kuwapa malimbuko ya kwanza ya unga wenu ili kwamba baraka ipate kuwa katika nyumba zenu.

31 Makuhani hawaruhusiwi kula chochote, ikiwa ni ndege au mnyama, aliyekutwa akiwa amekufa au aliyeraruliwa na wanyama pori.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/EZK/44-e04fe73cdf5e32e3ae40081a84dfc016.mp3?version_id=1627—

Categories
Ezekieli

Ezekieli 45

Mgawanyo Wa Nchi

1 “ ‘Mtakapogawa nchi kuwa urithi, mtaitoa sehemu ya nchi kwaBwanakuwa eneo takatifu, urefu wake dhiraa 25,000,upana wake dhiraa 20,000eneo hili lote litakuwa takatifu.

2 Katika hiyo, itakuwepo sehemu mraba ambayo ni mahali patakatifu kila upande dhiraa 500 ikiwa imezungukwa na eneo la wazi lenye upana wa dhiraa hamsini.

3 Katika eneo takatifu, pima sehemu yenye urefu wa dhiraa 25,000 na upana wa dhiraa 10,000.Ndani ya hilo eneo kutakuwa mahali patakatifu, Patakatifu pa Patakatifu.

4 Itakuwa sehemu takatifu ya nchi kwa ajili ya makuhani, wale wanaohudumu ndani ya mahali patakatifu na ambao hukaribia ili kuhudumu mbele zaBwana. Patakuwa mahali pa nyumba zao pamoja na sehemu kwa ajili ya mahali patakatifu.

5 Eneo la urefu wa dhiraa 25,000 na upana wa dhiraa 10,000 litakuwa la Walawi wale wanaotumika hekaluni, kama milki yao kwa ajili ya miji ya kuishi.

6 “ ‘Utatoa mji kama mali yao wenye upana wa dhiraa 5,000na urefu wa dhiraa 25,000, karibu na sehemu takatifu, itakuwa mali ya nyumba yote ya Israeli.

7 “ ‘Mkuu anayetawala atakuwa na lile eneo linalopakana na lile eneo lililowekwa wakfu upande huu na upande huu na eneo la mji. Eneo la mji litaenea upande wa magharibi kuanzia upande wa magharibi na upande wa mashariki kuanzia upande wa mashariki, likiendelea kwa urefu kutoka magharibi hadi mpaka wa mashariki sambamba na mojawapo ya sehemu za makabila.

8 Nchi hii itakuwa milki yake katika Israeli. Nao wakuu wangu hawataonea tena watu wangu bali watairuhusu nyumba ya Israeli kuimiliki nchi kulingana na makabila yao.

9 “ ‘Hili ndiloBwanaMwenyezi asemalo: Yatosha, enyi wakuu wa Israeli! Acheni mbali ukatili wenu na uonevu wenu mkafanye lile lililo haki na sawa. Acheni kuwatoza watu wangu isivyo haki, asemaBwanaMwenyezi.

10 Tumieni mizani sahihi na vipimo sahihi vya efana bathi.

11 Efa na bathi viwe sawa, bathi iwe sehemu ya kumi ya homeri na efa iwe sehemu ya kumi ya homeri, homeri itakuwa ndicho kiwango cha kukubalika kwa vyote viwili.

12 Shekeli moja itakuwa gera ishirini.Shekeli ishirini, jumlisha na shekeli ishirini na tano, jumlisha na shekeli kumi na tano zitakuwa mina moja.

Sadaka Na Siku Takatifu

13 “ ‘Hili ndilo toleo maalum mtakalotoa: moja ya sita ya efa kutoka kila homeri ya ngano na moja ya sita ya efa kutoka kila homeri ya shayiri.

14 Sehemu ya mafuta iliyoamriwa, yaliyopimwa kwa bathi, ni sehemu ya kumi ya bathi kutoka kila kori moja(ambayo ina bathi kumi au homeri moja.)

15 Pia kondoo mmoja atachukuliwa kutoka kwenye kila kundi la kondoo mia mbili kutoka kwenye malisho yaliyonyeshewa vizuri ya Israeli. Hivi vitatumika kwa ajili ya sadaka ya nafaka, sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani ili kufanya upatanisho kwa ajili ya watu, asemaBwanaMwenyezi.

16 Watu wote wa nchi wataungana pamoja na mkuu anayetawala Israeli ili kutoa hii sadaka maalum.

17 Huu utakuwa ndio wajibu wa mkuu anayetawala kutoa sadaka ya kuteketezwa, sadaka ya nafaka na sadaka ya kinywaji kwenye sikukuu, Mwezi Mwandamo na Sabato, kwenye sikukuu zote zilizoamriwa za nyumba ya Israeli. Atatoa sadaka za dhambi, sadaka za nafaka, sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nyumba ya Israeli.

18 “ ‘Hili ndiloBwanaMwenyezi asemalo: Katika mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya huo mwezi utamchukua fahali mchanga asiye na dosari na kutakasa mahali patakatifu.

19 Kuhani itampasa achukue sehemu ya hiyo damu ya sadaka ya dhambi na kuipaka kwenye miimo ya Hekalu, kwenye pembe nne za juu za ukingo wa hayo madhabahu na juu ya miimo ya lango la ukumbi wa ndani.

20 Itakupasa kufanya vivyo hivyo katika siku ya saba ya mwezi huo kwa ajili ya mtu yeyote ambaye hutenda dhambi bila kukusudia au bila kujua, hivyo utafanya upatanisho kwa ajili ya Hekalu.

21 “ ‘Katika mwezi wa kwanza siku ya kumi na nne utaadhimisha Pasaka. Sikukuu itaendelea kwa siku saba, wakati huo wa hizo siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu.

22 Katika siku hiyo mkuu anayetawala atatoa fahali kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya watu wote wa nchi.

23 Kila siku wakati wa hizo siku saba za sikukuu atatoa mafahali saba na kondoo dume saba wasio na dosari kuwa sadaka ya kuteketezwa kwaBwanana beberu kwa ajili ya sadaka ya dhambi.

24 Pia atatoa sadaka ya nafaka efa moja kwa kila fahali na efa moja kwa kila kondoo dume, pamoja na hini mojaya mafuta kwa kila efa.

25 “ ‘Wakati wa hizo siku saba za sikukuu, ambayo huanza katika mwezi wa saba kwenye siku ya kumi na tano, mkuu anayetawala atatoa mahitaji yale yale kwa ajili ya sadaka za dhambi, sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka na mafuta.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/EZK/45-2d6ce2a5485b62a15f54344cd88bc98d.mp3?version_id=1627—

Categories
Ezekieli

Ezekieli 46

Sheria Nyingine Mbalimbali

1 “ ‘Hili ndiloBwanaMwenyezi asemalo: Lango la ukumbi wa ndani linaloelekea upande wa mashariki litakuwa linafungwa kwa siku sita za juma, ila siku ya Sabato na siku ya Mwezi Mwandamo litafunguliwa.

2 Mkuu anayetawala ataingia kupitia baraza ya njia ya lango la ukumbi na kusimama karibu na nguzo ya lango. Makuhani watatoa sadaka za mkuu anayetawala za kuteketezwa na sadaka za amani. Mkuu anayetawala atasujudu kwenye kizingiti cha njia ya lango, kisha atatoka nje, lakini lango halitafungwa mpaka jioni.

3 Siku za Sabato na za Mwezi mwandamo watu wote wa nchi wataabudu mbele zaBwanapenye lile ingilio la ile njia.

4 Sadaka ya kuteketezwa aletazo mkuu anayetawala kwaBwanasiku ya Sabato itakuwa ni wana-kondoo sita na kondoo dume mmoja, wote wasiwe na dosari.

5 Sadaka ya nafaka inayotolewa pamoja na huyo kondoo dume itakuwa efa moja na sadaka ya nafaka inayotolewa na hao wana-kondoo itakuwa kiasi apendacho mtu pamoja na hini ya mafuta kwa kila efa.

6 Siku ya mwezi mwandamo atatoa fahali mchanga, wana-kondoo sita na kondoo dume, wote wasiwe na dosari.

7 Atatoa kuwa sadaka ya nafaka efa moja pamoja na fahali mmoja, efa moja na kondoo dume mmoja na pamoja na wana-kondoo kama atakavyo kutoa, pamoja na hini ya mafuta kwa kila efa.

8 Wakati mkuu anayetawala aingiapo, atapitia kwenye baraza ya njia ya lango, naye atatoka nje kwa njia hiyo hiyo.

9 “ ‘Wakati watu wa nchi wanapokuja mbele zaBwanakatika sikukuu zilizoamriwa, yeyote aingiaye kwa lango la kaskazini kuabudu atatoka nje kwa lango la kusini na yeyote aingiaye kwa lango la kusini atatoka nje kwa lango la kaskazini. Hakuna mtu yeyote atakayerudi kwa kupitia lango lile aliloingilia, lakini kila mmoja atatoka nje kwa lango linalokabili lile aliloingilia.

10 Mkuu anayetawala atakuwa miongoni mwao, akiingia nao ndani wanapoingia, naye atatoka nao nje wanapotoka.

11 “ ‘Kwenye sikukuu na kwenye sikukuu zilizoamriwa, sadaka ya nafaka itakuwa efa moja pamoja na fahali mmoja, efa moja pamoja na kondoo dume mmoja, pamoja na idadi ya wana-kondoo kama mtu apendavyo kutoa, pamoja na hini ya mafuta kwa kila efa.

12 Mkuu anayetawala anapotoa sadaka ya hiari kwaBwana, ikiwa ni sadaka ya kuteketezwa au sadaka ya amani, lango linaloelekea mashariki litafunguliwa kwa ajili yake. Atatoa sadaka yake ya kuteketezwa au sadaka yake ya amani kama afanyavyo katika siku ya Sabato. Kisha atatoka nje, naye akiisha kutoka nje, lango litafungwa.

13 “ ‘Kila siku utamtoa mwana-kondoo wa mwaka mmoja asiyekuwa na dosari kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa kwaBwana, utaitoa kila siku asubuhi.

14 Pia kila siku asubuhi pamoja na hiyo sadaka utatoa sadaka ya nafaka, ikiwa na sehemu ya sita ya efa pamoja na theluthi moja ya hiniya mafuta ya kuchanganya na ule unga. Utoaji wa sadaka hii ya nafaka kwaBwanani amri ya daima.

15 Kwa hiyo mwana-kondoo na sadaka ya nafaka na mafuta vitatolewa kila siku asubuhi kwa ajili ya sadaka ya daima ya kuteketezwa.

16 “ ‘Hili ndiloBwanaMwenyezi asemalo: Ikiwa mkuu atawalaye atatoa zawadi kutoka kwenye urithi wake na kumpa mmoja wa wanawe, hiyo zawadi itakuwa pia kwa wazao wake, itakuwa mali yao kwa urithi.

17 Hata hivyo, kama atatoa zawadi kutoka urithi wake na kumpa mmoja wa watumishi wake, mtumishi anaweza kuiweka mpaka mwaka wa uhuru, kisha itarudishwa kwa mkuu anayetawala. Urithi wake ni wa wanawe peke yao, ni mali yao.

18 Mkuu anayetawala hana ruhusa kuchukua urithi wowote wa watu na kuwaondoa kwenye mali zao. Mkuu atawalaye atawapa wanawe urithi wao, kutoka kwenye mali zake mwenyewe, ili kwamba pasiwe na mtu wangu yeyote atakayetengwa na urithi wake.’ ”

19 Kisha mtu yule akanileta kwa kupitia kwenye ingilio lililokuwa kando ya lango mpaka kwenye vyumba vitakatifu vinavyoelekea kaskazini, ambavyo ni vya makuhani, naye akanionyesha mahali fulani upande wa mwisho wa magharibi.

20 Akaniambia, “Mahali hapa ndipo makuhani watakapotokosea sadaka ya hatia na sadaka ya dhambi na kuoka sadaka ya nafaka, kuepuka kuzileta katika ukumbi wa nje na kushirikisha utakatifu kwa watu.”

21 Baada ya hapo akanileta kwenye ukumbi wa nje na kunizungusha kwenye pembe zake nne, nami nikaona katika kila pembe ya huo ukumbi kulikuwa na ukumbi mwingine.

22 Katika pembe nne za huo ukumbi wa nje kulikuwa na kumbi nyingine, zenye urefu wa dhiraa arobaini na upana wake dhiraa thelathini, ambapo hizo kumbi kwenye hizo pembe nne zilikuwa na vipimo vilivyo sawa.

23 Mzunguko wa ndani wa hizo kumbi nne ulikuwa na ukingo wa jiwe, zikiwa na sehemu zilizojengwa kwa ajili ya moto kuzunguka chini ya huo ukingo.

24 Akaniambia, “Hizi ndizo sehemu za kupikia ambazo wale wanaohudumu kwenye Hekalu watatokosea dhabihu za watu.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/EZK/46-2670619042ff791d89347c9c9e183386.mp3?version_id=1627—

Categories
Ezekieli

Ezekieli 47

Mto Kutoka Hekaluni

1 Yule mtu akanirudisha mpaka kwenye ingilio la Hekalu, nami nikaona maji yakitoka chini ya kizingiti cha Hekalu yakitiririkia upande wa mashariki (kwa maana upande wa mbele wa Hekalu ulielekea mashariki). Maji yalikuwa yakitoka chini upande wa kusini wa Hekalu, kusini mwa madhabahu.

2 Ndipo akanitoa nje kupitia lango la kaskazini na kunizungusha mpaka kwenye lango la nje linaloelekea mashariki, nayo maji yalikuwa yakitiririka kutoka upande wa kusini.

3 Mtu yule alipokwenda upande wa mashariki akiwa na kamba ya kupimia mkononi mwake, akapima dhiraa 1,000kisha akanipitisha kwenye hayo maji ambayo yalifika kwenye vifundo vya miguu.

4 Akapima dhiraa 1,000 nyingine na kunipitisha kwenye hayo maji ambayo yalifika magotini. Akapima dhiraa nyingine 1,000 na kunipitisha kwenye hayo maji ambayo yalifika kiunoni.

5 Akapima tena dhiraa 1,000 nyingine, lakini wakati huu yalikuwa mto ambao sikuweza kuvuka, kwa kuwa maji yalikuwa na kina kirefu ambacho ni cha kuogelea, mto ambao hakuna mtu yeyote ambaye angeweza kuvuka.

6 Akaniuliza, “Je, mwanadamu, unaona hili?”

Kisha akanirudisha mpaka kwenye ukingo wa huo mto.

7 Nilipofika pale, nikaona idadi kubwa ya miti kila upande wa ule mto.

8 Akaniambia, “Haya maji yanatiririka kuelekea nchi ya mashariki na kushuka mpaka Araba,ambapo huingia Baharini. Yanapomwagikia kwenye hiyo Bahari,maji yaliyoko humo huponywa na kuwa safi.

9 Popote mto huu uendapo kila kiumbe hai kinachoyaparamia hayo maji kitaishi, nako kutakuwa na samaki wengi mno, mara maji haya yafikapo huko. Maji hayo yatakuwa hai na kila kitu kitakachoishi kule mto uendako.

10 Wavuvi watasimama kando ya bahari, kuanzia En-Gedi hadi En-Eglaimu huko patakuwa mahali pa kutandaza nyavu za kuvulia samaki. Samaki watakuwa wa aina nyingi, kama samaki wa Bahari Kuu

11 Lakini madimbwi yake na mabwawa yake hayatakuwa na maji yanayofaa kunywa, bali yatabakia kuwa maji ya chumvi.

12 Miti ya matunda ya kila aina itaota kwenye kingo zote mbili za mto huu. Majani yake hayatanyauka wala haitaacha kuwa na matunda katika matawi yake. Kila mwezi kutakuwa na matunda, kwa sababu maji yatokayo patakatifu yanaitiririkia. Matunda yake yatakuwa chakula na majani yake yatakuwa dawa.”

Mipaka Mipya Ya Nchi

13 Hili ndiloBwanaMwenyezi asemalo: “Hii ndiyo mipaka ambayo kwayo mtagawanya hiyo nchi kuwa urithi miongoni mwa hayo makabila kumi na mawili ya Israeli, pamoja na mafungu mawili ya Yosefu.

14 Mtagawa kwa usawa miongoni mwao. Kwa sababu niliapa kwa mkono ulioinuliwa kuwapa baba zenu, nchi hii itakuwa urithi wenu.

15 “Huu ndio utakuwa mpaka wa hiyo nchi:

“Upande wa kaskazini utaanzia Bahari Kuu kwa njia ya Hethloni kupitia Lebo-Hamathi hadi maingilio ya Sedadi.

16 Berotha na Sibraimu (ambao uko kwenye mpaka kati ya Dameski na Hamathi), hadi kufikia Haser-Hatikoni, ambao uko katika mpaka wa Haurani.

17 Hivyo mpaka utaendelea kuanzia Baharini hadi Hasar-Enoni, ukiambaa na mpaka wa kaskazini wa Dameski, pamoja na mpaka wa Hamathi upande wa kaskazini. Huu utakuwa ndio mpaka wa kaskazini.

18 Upande wa mashariki mpaka utapita kati ya Haurani na Dameski, kuambaa Yordani na kati ya Gileadi na nchi ya Israeli, hadi bahari ya masharikina kufika Tamari. Huu utakuwa ndio mpaka wa mashariki.

19 Upande wa kusini utaanzia Tamari hadi kufikia maji ya Meriba-Kadeshi, kisha utaambaa na Kijito cha Misri hadi Bahari Kuu. Huu utakuwa ndio mpaka wa kusini.

20 Upande wa magharibi, Bahari Kuu itakuwa ndio mpaka hadi kwenye sehemu mkabala na Lebo-Hamathi. Huu utakuwa ndio mpaka wa magharibi.

21 “Mtagawanya nchi hii miongoni mwenu kufuatana na makabila ya Israeli.

22 Mtaigawanya kuwa urithi kwa ajili yenu na kwa ajili ya wageni wanaoishi miongoni mwenu na ambao wana watoto. Wao watakuwa kwenu kama wenyeji wazawa wa Israeli, pamoja na ninyi watagawiwa urithi miongoni mwa makabila ya Israeli.

23 Katika kabila lolote mgeni atakapoishi hapo ndipo mtakapompatia urithi wake,” asemaBwanaMwenyezi.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/EZK/47-d3f55158735d6aa2e920f380f131826c.mp3?version_id=1627—

Categories
Ezekieli

Ezekieli 48

Mgawanyo Wa Nchi

1 “Haya ndiyo majina ya makabila na sehemu zao: Kwenye mpaka wa kaskazini, Dani atakuwa na sehemu moja, mpaka huo utafuata barabara ya Hethloni hadi Lebo-Hamathi, Hasar-Enani hata mpaka wa kaskazini wa Dameski karibu na Hamathi utakuwa sehemu ya huo mpaka wake kuanzia upande wa mashariki hadi upande wa magharibi.

2 “Asheri atakuwa na sehemu moja, itapakana na nchi ya Dani kuanzia mashariki hadi upande wa magharibi.

3 “Naftali atakuwa na sehemu moja, itapakana na nchi ya Asheri kuanzia mashariki hadi magharibi.

4 “Manase atakuwa na sehemu moja, itapakana na nchi ya Naftali kuanzia mashariki hadi magharibi.

5 “Efraimu atakuwa na sehemu moja, itapakana na nchi ya Manase kuanzia mashariki hadi magharibi.

6 “Reubeni atakuwa na sehemu moja, itapakana na nchi ya Efraimu kuanzia mashariki hadi magharibi.

7 “Yuda atakuwa na sehemu moja, itapakana na nchi ya Reubeni kuanzia mashariki hadi magharibi.

8 “Kupakana na nchi ya Yuda kuanzia mashariki mpaka magharibi itakuwa ndiyo sehemu utakayoitoa ili kuwa toleo maalum. Itakuwa na upana wa dhiraa 25,000na urefu wake kuanzia mashariki mpaka magharibi utakuwa ule ule wa sehemu moja ya kabila, mahali patakatifu patakuwa katikati ya eneo hilo.

9 “Hiyo sehemu maalum mtakayotoa kwaBwanaitakuwa na urefu wa dhiraa 25,000 na upana wa dhiraa 10,000

10 Hii itakuwa ni sehemu takatifu kwa ajili ya makuhani. Itakuwa na urefu wa dhiraa 25,000 upande wa kaskazini, upana wa dhiraa 10,000 upande wa magharibi, dhiraa 10,000 upande wa mashariki na urefu wa dhiraa 25,000 upande wa kusini. Katikati yake patakuwa mahali patakatifu paBwana.

11 Hii itakuwa kwa ajili ya makuhani waliowekwa wakfu, Wasadoki, waliokuwa waaminifu katika kunitumikia nao hawakupotoka kama Walawi walivyofanya wakati Waisraeli walipopotoka.

12 Itakuwa toleo maalum kwao kutoka sehemu takatifu ya nchi, yaani, sehemu takatifu sana, inayopakana na nchi ya Walawi.

13 “Kando ya nchi ya makuhani, Walawi watakuwa na mgawo wa urefu wa dhiraa 25,000 na upana wa dhiraa 10,000. Urefu wake utakuwa jumla dhiraa 25,000 na upana wa dhiraa 10,000.

14 Hawataruhusiwa kuuza wala kuibadilisha hata mojawapo. Hii ndiyo sehemu nzuri ya nchi kuliko nyingine zote, hivyo haitakuwa mikononi mwa watu wengine, kwa sababu ni takatifu kwaBwana.

15 “Eneo linalobaki lenye upana wa dhiraa 5,000na urefu wa dhiraa 25,000, litakuwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya mji, kwa ajili ya ujenzi wa nyumba na malisho. Mji utakuwa katikati yake

16 nao utakuwa na vipimo hivi: upande wa kaskazini dhiraa 4,500,upande wa kusini dhiraa 4,500, upande wa mashariki dhiraa 4,500 na upande wa magharibi dhiraa 4,500.

17 Sehemu ya malisho kwa ajili ya mji itakuwa na eneo la dhiraa 250upande wa kaskazini, dhiraa 250 upande wa kusini, dhiraa 250 upande wa mashariki na dhiraa 250 upande wa magharibi.

18 Eneo linalobaki, linalopakana na sehemu takatifu likiwa na urefu sawa nalo, litakuwa dhiraa 10,000 upande wa mashariki na dhiraa 10,000 upande wa magharibi. Mazao yake yatawapa watumishi wa mji chakula.

19 Watumishi wa mji wanaolima shamba hili watatoka katika makabila yote ya Israeli.

20 Eneo lote la hiyo sehemu litakuwa mraba, yaani, dhiraa 25,000 kila upande. Kama toleo maalum mtatenga sehemu takatifu, pamoja na milki ya mji.

21 “Eneo linalobaki pande zote za eneo linalofanya sehemu takatifu na milki ya mji litakuwa mali ya mkuu atawalaye. Eneo hili litaenea upande wa mashariki kuanzia kwenye dhiraa 25,000 za sehemu takatifu hadi mpaka wa mashariki na kuelekea upande wa magharibi kuanzia kwenye dhiraa 25,000 hadi mpaka wa magharibi. Maeneo yote haya mawili yanayoenda sambamba na urefu wa sehemu za makabila yatakuwa ya mkuu anayetawala, na sehemu ile takatifu pamoja na mahali patakatifu pa Hekalu itakuwa katikati yake.

22 Kwa hiyo milki ya Walawi na milki ya mji vitakuwa katikati ya eneo lile ambalo ni mali ya mkuu anayetawala. Eneo la mkuu anayetawala litakuwa kati ya mpaka wa Yuda na mpaka wa Benyamini.

23 “Kuhusu makabila yaliyobaki: Benyamini atakuwa na sehemu moja, itakayoanzia upande wa mashariki hadi upande wa magharibi.

24 “Simeoni atakuwa na sehemu moja, itakayopakana na nchi ya Benyamini kuanzia mashariki hadi magharibi.

25 “Isakari atakuwa na sehemu moja, itakayopakana na nchi ya Simeoni kuanzia mashariki hadi magharibi.

26 “Zabuloni atakuwa na sehemu moja, itakayopakana na nchi ya Isakari kuanzia mashariki hadi magharibi.

27 “Gadi atakuwa na sehemu moja, itakayopakana na nchi ya Zabuloni kuanzia mashariki hadi magharibi.

28 “Mpaka wa kusini wa Gadi utapita kusini kuanzia Tamari hadi maji ya Meriba-Kadeshi, kisha kupitia upande wa Kijito cha Misri hadi Bahari Kuu.

29 “Hii ndiyo nchi mtakayogawanya kuwa urithi kwa makabila ya Israeli, nazo zitakuwa sehemu zao,” asemaBwanaMwenyezi.

Malango Ya Mji

30 “Haya yatakuwa ndiyo malango ya mji ya kutokea: Kuanzia upande wa kaskazini, ambayo urefu wake ni dhiraa 4,500, utakuwa na malango matatu,

31 malango hayo ya mji yatapewa majina ya makabila ya Israeli. Malango hayo matatu ya upande wa kaskazini moja litakuwa lango la Reubeni, lango la Yuda na lango la Lawi.

32 “Upande wa mashariki, wenye urefu wa dhiraa 4,500, utakuwa na malango matatu: lango la Yosefu, lango la Benyamini na lango la Dani.

33 “Upande wa kusini, wenye urefu wa dhiraa 4,500, utakuwa na malango matatu: lango la Simeoni, lango la Isakari na lango la Zabuloni.

34 “Upande wa magharibi, wenye urefu wa dhiraa 4,500, utakuwa na malango matatu: lango la Gadi, lango la Asheri na lango la Naftali.

35 “Urefu wote kuzunguka utakuwa dhiraa 18,000.

“Nalo jina la mji huo kuanzia wakati huo na kuendelea litakuwa:

Bwana yupo hapa.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/EZK/48-5cec6eda75021edc2158555d445f17bc.mp3?version_id=1627—