Categories
Ayubu

Ayubu 30

1 “Lakini sasa watu wadogo kwa umri kuniliko wananidhihaki,

watu ambao baba zao ningekataa kwa dharau

kuwaweka pamoja na mbwa wangu wa kulinda kondoo.

2 Nguvu za mikono yao zingekuwa na faida gani kwangu,

kwa kuwa nguvu zao zilikuwa zimewaishia?

3 Wakiwa wamekonda kutokana na kupungukiwa na kwa njaa,

walizurura usiku katika nchi kame iliyo ukiwa.

4 Katika vichaka walikusanya mimea ya chumvi,

nacho chakula chao kilikuwa mizizi ya mti wa mfagio.

5 Walifukuzwa mbali na watu wao,

wakipigiwa kelele kama wevi.

6 Walilazimika kuishi katika mikondo ya vijito vilivyokauka,

kwenye majabali na mahandaki.

7 Kwenye vichaka walilia kama punda,

na walijisongasonga pamoja kwenye vichaka.

8 Wao ni watoto wa wapumbavu wenye asili ya ubaya,

waliofukuzwa watoke katika nchi.

9 “Nao sasa wana wao wananidhihaki katika nyimbo;

nimekuwa kitu cha dhihaka kwao.

10 Wananichukia sana na kujitenga nami,

wala hawasiti kunitemea mate usoni.

11 Sasa kwa kuwa Mungu ameilegeza kamba ya upinde wangu na kunitesa,

wamekuwa huru kunitendea waonavyo.

12 Kuume kwangu kundi linashambulia;

wao huitegea miguu yangu tanzi,

na kunizingira.

13 Huizuia njia yangu,

nao hufanikiwa katika kuniletea maafa,

nami sina yeyote wa kunisaidia.

14 Wananijia kama watu wapitao katika ufa mpana;

katikati ya magofu huja na kunishambulia.

15 Vitisho vimenifunika;

heshima yangu imetoweshwa kama kwa upepo,

salama yangu imetoweka kama wingu.

16 “Sasa maisha yangu yamefikia mwisho;

siku za mateso zimenikamata.

17 Usiku mifupa yangu inachoma;

maumivu yanayonitafuna hayatulii kamwe.

18 Kwa uwezo wake mkuu Mungu huwa kwangu kama nguo;

hushikamana nami kama ukosi wa vazi langu.

19 Yeye amenitupa kwenye matope,

nami nimekuwa kama mavumbi na majivu.

20 “EeBwana, ninakulilia wewe lakini hunijibu;

ninasimama, nawe unanitazama tu.

21 Wewe unanigeukia bila huruma;

unanishambulia kwa nguvu za mkono wako.

22 Unaninyakua na kunipeperusha kwa upepo;

umenirusha huku na huko kwenye dhoruba kali.

23 Ninajua utanileta mpaka kifoni,

mahali ambapo wenye uhai wote wamewekewa.

24 “Hakika hakuna yeyote amshambuliaye mhitaji,

anapoomba msaada katika shida yake.

25 Je, sikulia kwa ajili ya wale waliokuwa katika taabu?

Je, nafsi yangu haikusononeka kwa ajili ya maskini?

26 Lakini nilipotazamia mema, mabaya yalinijia;

nilipotafuta nuru, ndipo giza lilipokuja.

27 Kusukwasukwa ndani yangu kamwe hakutulii;

siku za mateso zinanikabili.

28 Ninazunguka nikiwa nimeungua, lakini si kwa jua;

ninasimama katika kusanyiko nikiomba msaada.

29 Nimekuwa ndugu wa mbweha,

rafiki wa mabundi.

30 Ngozi yangu imekuwa nyeusi nayo inachunika;

mifupa yangu inaungua kwa homa.

31 Kinubi changu kimegeuka kuwa maombolezo,

nayo filimbi yangu imekuwa sauti ya kilio.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/30-d655d6bc17ce8e3ebf55bd52cfb01282.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 31

1 “Nimefanya agano na macho yangu

yasimtazame msichana kwa kumtamani.

2 Kwa kuwa fungu la mwanadamu ni gani kutoka kwa Mungu juu,

urithi wake kutoka kwa Mungu Mwenye Nguvu Aliye juu?

3 Je, si uharibifu kwa watu waovu,

maangamizi kwa wale watendao mabaya?

4 Je, yeye hazioni njia zangu

na kuihesabu kila hatua yangu?

5 “Kama nimeishi katika uongo

au mguu wangu umekimbilia udanganyifu,

6 Mungu na anipime katika mizani za uaminifu,

naye atajua kwamba sina hatia:

7 kama hatua zangu zimepotoka kutoka kwenye njia,

kama moyo wangu umeongozwa na macho yangu,

au kama mikono yangu imetiwa unajisi,

8 basi wengine na wale nilichokipanda,

nayo yale yote niliyootesha na yangʼolewe.

9 “Kama moyo wangu umeshawishiwa na mwanamke,

au kama nimevizia mlangoni mwa jirani yangu,

10 basi mke wangu na asage nafaka ya mwanaume mwingine,

nao wanaume wengine walale naye.

11 Kwa kuwa hilo lingekuwa aibu,

naam, dhambi ya kuhukumiwa.

12 Ni moto uwakao kwa Uharibifu;

ungekuwa umengʼoa mavuno yangu.

13 “Kama ningewanyima haki watumishi wangu wanaume au vijakazi wangu,

walipokuwa na manungʼuniko dhidi yangu,

14 nitafanya nini Mungu atakaponikabili?

Nitamjibu nini nitakapoitwa kutoa hesabu?

15 Je, yeye aliyeniumba tumboni mwa mama yangu,

si ndiye aliwaumba?

Je, si ni yeye huyo mmoja aliyetuumba sote

ndani ya mama zetu?

16 “Ikiwa nimewanyima maskini haja zao,

au kuyaacha macho ya wajane yadhoofike,

17 kama nimekula chakula changu mwenyewe,

bila kuwashirikisha yatima;

18 lakini tangu ujana wangu nimemlea yatima kama ambavyo baba angefanya,

nami tangu kuzaliwa kwangu nimewaongoza wajane:

19 kama nilimwona yeyote akiteseka kwa kukosa nguo,

au mtu mhitaji asiye na mavazi

20 ambaye wala moyo wake haukunibariki

kwa kumpatia joto kwa mavazi ya manyoya ya kondoo zangu,

21 na kama nimeinua mkono wangu dhidi ya yatima,

nikijua kuwa nina ushawishi mahakamani,

22 basi mkono wangu na unyofoke toka begani mwangu,

nao na uvunjike kutoka kiungio chake.

23 Kwa kuwa niliogopa uharibifu kutoka kwa Mungu,

nami kwa kuuogopa utukufu wake sikuweza kufanya mambo kama hayo.

24 “Kama nimeweka tumaini langu kwenye dhahabu,

au kuiambia dhahabu safi, ‘Wewe ndiwe salama yangu,’

25 kama nimefurahia wingi wa utajiri wangu,

ustawi ambao mikono yangu ilikuwa imepata,

26 kama nimelitazama jua katika kungʼaa kwake

au mwezi ukienda kwa fahari yake,

27 hivyo moyo wangu kushawishiwa kwa siri,

au kubusu mkono wangu kwa kuviheshimu,

28 basi hiyo pia ingekuwa dhambi ya kuhukumiwa,

kwa kuwa ningekuwa si mwaminifu kwa Mungu aishiye juu sana.

29 “Kama nimeshangilia msiba wa adui yangu,

au kutazama kwa furaha taabu iliyomjia,

30 lakini sikuruhusu kinywa changu kufanya dhambi

kwa kuomba laana dhidi ya maisha yake;

31 kama watu wa nyumbani mwangu kamwe hawakusema,

‘Ni nani ambaye hajashibishwa na nyama ya Ayubu?’

32 Lakini hakuna mgeni aliyelala njiani,

kwa maana mlango wangu ulikuwa wazi kwa msafiri;

33 kama nimeifunika dhambi yangu kama wanadamu wengine wafanyavyo,

kwa kuficha hatia yangu moyoni mwangu,

34 kwa sababu ya kuogopa umati wa watu,

na hivyo kuwa na hofu ya kudharauliwa na jamaa,

nikanyamaza kimya nisitoke nje ya mlango:

35 (“Laiti kama angekuwepo mtu wa kunisikia!

Tazama sasa ninatia sahihi kwenye utetezi wangu:

Mwenyezi na anijibu;

mshtaki wangu na aweke mashtaka yake kwenye maandishi.

36 Hakika ningeyavaa begani mwangu,

ningeyavaa kama taji.

37 Ningempa hesabu ya kila hatua yangu,

ningemwendea kama mwana wa mfalme.)

38 “Kama nchi yangu inalia dhidi yangu,

na mifereji yake yote imelowana kwa machozi,

39 kama nimekula mazao yake bila malipo,

au kuvunja mioyo ya wapangaji wake,

40 basi miiba na iote badala ya ngano,

na magugu badala ya shayiri.”

Mwisho wa maneno ya Ayubu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/31-c99ad5dba81d4c9faaf00f3dce8a272b.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 32

Elihu Awakemea Rafiki Za Ayubu

1 Basi watu hawa watatu wakaacha kumjibu Ayubu, kwa kuwa alikuwa mwadilifu machoni pake mwenyewe.

2 Lakini Elihu mwana wa Barakeli, wa kabila la Buzi wa jamaa ya Ramu, akamkasirikia sana Ayubu, kwa sababu ya kujihesabia haki mwenyewe badala ya Mungu.

3 Pia aliwakasirikia hao rafiki watatu wa Ayubu, kwa sababu hawakuweza kupata njia ya kuthibitisha ya kuwa hayo maneno ya Ayubu hayakuwa ya kweli, nao bado walikuwa wamemlaumu.

4 Basi Elihu alikuwa amesubiri kwanza waongee na Ayubu kwa sababu walikuwa na umri mkubwa kumliko yeye.

5 Lakini alipoona watu hao watatu hawakuwa na kitu zaidi cha kusema, hasira yake ikaamka.

6 Basi Elihu mwana wa Barakeli wa kabila la Buzi akasema:

“Mimi ni mdogo kwa umri,

nanyi ni wazee;

ndiyo sababu niliogopa,

sikuthubutu kuwaambia kile ninachojua.

7 Nilifikiri, ‘Yafaa umri useme,

nao wingi wa miaka ungefundisha hekima.’

8 Lakini ni Roho iliyoko ndani ya mwanadamu,

pumzi ya Mwenyezi, ndiyo impayo yeye ufahamu.

9 Sio wazee peke yao walio na hekima,

sio wenye umri mkubwa peke yao wanaofahamu lililo sawa.

10 “Kwa hiyo nasema: Nisikilizeni mimi;

mimi nami nitawaambia lile ninalojua.

11 Nilingojea mlipokuwa mnaongea,

nilizisikiliza hoja zenu;

mlipokuwa mkitafuta maneno ya kusema,

12 niliwasikiliza kwa makini.

Lakini hakuna hata mmoja wenu

aliyethibitisha kwamba Ayubu amekosa;

hakuna hata mmoja wenu

aliyeweza kujibu hoja zake.

13 Msiseme, ‘Tumepata hekima;

Mungu na amthibitishe kuwa mwongo,

wala si mwanadamu.’

14 Lakini Ayubu hajayapanga maneno yake dhidi yangu,

nami sitamjibu kwa kutumia hoja zenu.

15 “Wametiwa hofu na hawana la zaidi la kusema;

maneno yamewaishia.

16 Je, ningoje sasa kwa sababu wamekuwa kimya,

kwa vile sasa wanasimama bila kuwa na la kujibu?

17 Mimi nami nitakuwa na la kusema;

mimi nami nitasema lile nilijualo.

18 Kwa kuwa nimejawa na maneno,

nayo Roho iliyomo ndani yangu yanisukuma;

19 ndani yangu niko kama chupa iliyojazwa divai,

kama kiriba kipya cha divai kilicho tayari kupasuka.

20 Ni lazima niseme ili niweze kutulia;

ni lazima nifumbue midomo yangu nipate kujibu.

21 Sitampendelea mtu yeyote,

wala sitajipendekeza kwa mtu yeyote;

22 kwa kuwa kama ningekuwa stadi wa kujipendekeza,

Muumba wangu angeniondolea mbali kwa upesi.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/32-06188589f097de19f345121b69023171.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 33

Elihu Anamkemea Ayubu

1 “Lakini Ayubu, sasa, sikiliza maneno yangu;

zingatia kila kitu nitakachosema.

2 Karibu nitafungua kinywa changu;

maneno yangu yapo katika ncha ya ulimi wangu.

3 Maneno yangu yanatoka katika moyo mnyofu;

midomo yangu hunena kwa uaminifu yale niyajuayo.

4 Roho wa Mungu ameniumba;

pumzi ya Mwenyezi hunipa uhai.

5 Unijibu basi, kama unaweza;

jiandae kunikabili mimi.

6 Mimi ni kama wewe mbele za Mungu;

mimi pia nimetolewa kwenye udongo.

7 Huna sababu ya kuniogopa,

wala mkono wangu haupaswi kukulemea.

8 “Lakini umesema nikiwa ninakusikia,

nami nilisikia maneno yenyewe:

9 ‘Mimi ni safi na sina dhambi;

mimi ni safi na sina hatia.

10 Lakini bado Mungu amepata dosari kwangu,

naye ananiona kama adui yake.

11 Ananifunga miguu kwa pingu,

tena anaziangalia njia zangu zote kwa karibu.’

12 “Lakini mimi ninakuambia, katika jambo hili wewe una makosa,

kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mwanadamu.

13 Kwa nini unamlalamikia

kwamba yeye hamjibu mwanadamu?

14 Kwa kuwa Mungu husema, wakati huu kwa njia moja,

au wakati mwingine kwa njia nyingine,

ingawa mwanadamu anaweza asielewe.

15 Mungu husema na mwanadamu katika ndoto,

katika maono ya usiku,

wakati usingizi mzito uwaangukiapo

wanadamu wasinziapo vitandani mwao,

16 anaweza akasemea masikioni mwao,

na kuwatia hofu kwa maonyo,

17 ili kumgeuza mtu kutoka kwenye kutenda mabaya

na kumwepusha na kiburi,

18 kuiokoa nafsi yake na shimo,

uhai wake usiangamizwe kwa upanga.

19 Mtu anaweza kutiwa adabu kwa maumivu kitandani mwake,

kwa dhiki za mfululizo katika mifupa yake,

20 kiasi kwamba maisha yake yenyewe yanakataa chakula

nayo nafsi yake ikakichukia kabisa hata chakula kizuri.

21 Nyama ya mwili wake huisha kwa kukonda,

nayo mifupa yake ambayo mwanzoni ilikuwa imefichika,

sasa inatokeza nje.

22 Nafsi yake inakaribia kaburi,

nao uhai wake karibu na wajumbe wa kifo.

23 “Kama bado kuna malaika upande wake

kama mtetezi, mmoja miongoni mwa elfu,

wa kumwambia mwanadamu lililo jema kwake,

24 kumwonea huruma na kusema,

‘Mwokoe asije akatumbukia shimoni;

nimepata ukombozi kwa ajili yake’:

25 ndipo nyama ya mwili wake hufanywa mpya kama ya mtoto;

hurudishwa upya kama siku za ujana wake.

26 Humwomba Mungu, akapata kibali kwake,

huuona uso wa Mungu na kushangilia kwa furaha;

Mungu humrudisha katika hali yake ya uadilifu.

27 Ndipo huja mbele za watu na kusema,

‘Nilitenda dhambi na kupotosha kilichokuwa haki,

lakini sikuadhibiwa kama nilivyostahili.

28 Alinikomboa nafsi yangu nisitumbukie shimoni,

nami nitaishi ili kuufurahia mwanga.’

29 “Mungu hufanya haya yote kwa mwanadamu;

mara mbili hata mara tatu,

30 ili aigeuze nafsi yake toka shimoni,

ili nuru ya uzima imwangazie.

31 “Ayubu, zingatia, nisikilize mimi;

nyamaza, nami nitanena.

32 Kama unalo lolote la kusema, unijibu;

sema, kwa maana ninataka uonekane huna hatia.

33 Lakini kama huna la kusema, basi nisikilize mimi;

nyamaza, nami nitakufundisha hekima.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/33-8abc26d47a0a25480736b4429981e5f6.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 34

Elihu Anatangaza Haki Ya Mungu

1 Kisha Elihu akasema:

2 “Sikieni maneno yangu, enyi watu wenye hekima;

nisikilizeni mimi, ninyi watu wenye maarifa.

3 Kwa kuwa sikio huyajaribu maneno

kama vile ulimi uonjavyo chakula.

4 Tujichagulie wenyewe yaliyo sawa,

nasi tujifunze pamoja yaliyo mema.

5 “Ayubu anasema, ‘Mimi sina hatia,

lakini Mungu ameninyima haki yangu.

6 Ingawa niko sawa,

ninaonekana mwongo;

nami ingawa sina kosa,

kidonda changu hakiponi.’

7 Ni mtu gani aliye kama Ayubu,

anywaye dharau kama maji?

8 Ashirikianaye na watenda mabaya

na kuchangamana na watu waovu.

9 Kwa kuwa anasema, ‘Haimfaidi mwanadamu kitu chochote

anapojitahidi kumpendeza Mungu.’

10 “Hivyo nisikilizeni mimi, ninyi watu wenye ufahamu.

Kamwe Mungu hatendi uovu,

Mwenyezi hafanyi kosa.

11 Humlipa mwanadamu kwa ajili ya lile alilotenda;

huleta juu yake kile ambacho matendo yake yanastahili.

12 Ni jambo lisiloweza kufikiriwa kwamba Mungu angefanya makosa,

kwamba Mwenyezi angepotosha hukumu.

13 Je, ni nani aliyemtawaza juu ya dunia?

Ni nani aliyemweka kuwa mwangalizi wa ulimwengu wote?

14 Kama lilikuwa kusudi la Mungu,

naye akaiondoa Roho yake na pumzi yake,

15 wanadamu wote wangeliangamia kwa pamoja,

na mtu angerudi mavumbini.

16 “Kama ninyi mnaufahamu, sikieni hili;

sikilizeni hili nisemalo.

17 Je, yeye aichukiaye haki aweza kutawala?

Je, utamhukumu mwenye haki, Aliye na Nguvu Zote?

18 Je, si ni yeye awaambiaye wafalme, ‘Ninyi hamfai kitu,’

nao watu mashuhuri, ‘Ninyi ni waovu,’

19 yeye asiyependelea wakuu,

wala haonyeshi upendeleo kwa matajiri kuliko maskini,

kwa kuwa wote ni kazi ya mikono yake?

20 Wanakufa ghafula, usiku wa manane;

watu wanatikiswa nao hupita;

wenye nguvu huondolewa

bila mkono wa mwanadamu.

21 “Macho yake yanazitazama njia za wanadamu;

anaona kila hatua yao.

22 Hakuna mahali penye giza nene, wala uvuli mkubwa,

ambapo watenda mabaya wanaweza kujificha.

23 Mungu hana haja ya kumchunguza mtu sana,

ili apate kuja mbele zake kwa hukumu.

24 Bila kuuliza huwapondaponda wenye nguvu nyingi

na kuwaweka wengine mahali pao.

25 Kwa sababu huyaangalia matendo yao yote,

huwaondoa usiku, nao wakaangamia.

26 Anawaadhibu kwa ajili ya uovu wao

mahali ambapo kila mmoja ataweza kuwaona,

27 kwa sababu wameacha kumfuata Mungu,

nao hawakuiheshimu njia yake hata moja.

28 Wamesababisha kilio cha maskini kifike mbele zake,

hivyo akasikia kilio cha wahitaji.

29 Lakini kama akinyamaza kimya,

ni nani awezaye kumhukumu?

Kama akiuficha uso wake,

ni nani awezaye kumwona?

Ikiwa ni taifa au mtu mmoja, kwake ni sawa,

30 ili kumzuia mtu mwovu kutawala,

au wale ambao huwategea watu mitego.

31 “Kama mwanadamu akimwambia Mungu,

‘Nimekosa lakini sitatenda dhambi tena.

32 Nifundishe nisichoweza kuona;

kama nimekukosea, sitafanya hivyo tena.’

33 Je basi, Mungu atakulipa kwa masharti yako,

wakati wewe umekataa kutubu?

Yakupasa wewe uamue, wala si mimi;

sasa niambie lile ulijualo.

34 “Wanadamu wenye ufahamu husema,

wenye hekima wanaonisikia huniambia,

35 ‘Ayubu huongea bila maarifa;

maneno yake hayana busara.’

36 Laiti Ayubu angejaribiwa hadi kikomo cha mwisho,

kwa sababu anajibu kama mtu mwovu!

37 Kwenye dhambi yake huongeza uasi;

kwa dharau hupiga makofi miongoni mwetu,

na kuzidisha maneno yake dhidi ya Mungu.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/34-95a833a22622be8b51f604d546339a58.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 35

Elihu Analaumu Mtu Kujiona Kuwa Mwenye Haki

1 Ndipo Elihu akasema:

2 “Je, unadhani hili ni haki?

Wewe unasema, ‘Nina haki mbele za Mungu.’

3 Bado unamuuliza, ‘Ni faida gani nimepata,

na imenifaidi nini kwa kutokutenda dhambi?’

4 “Ningependa nikujibu wewe

pamoja na marafiki zako walio pamoja nawe.

5 Tazama juu mbinguni ukaone;

yaangalie mawingu yaliyo juu sana juu yako.

6 Je, ukitenda dhambi, inamdhuruje Mungu?

Kama dhambi zako zikiwa nyingi,

hilo linamfanyia nini Mungu?

7 Kama wewe ni mwadilifu, unampa nini,

au yeye anapokea nini mkononi kwako?

8 Uovu wako unamdhuru tu mtu mwingine kama wewe,

nayo haki yako inawafaa wanadamu tu.

9 “Wanadamu hulia kwa kulemewa na mateso;

huomba msaada kutoka mkono wenye nguvu.

10 Lakini hakuna asemaye, ‘Yuko wapi Mungu Muumba wangu,

yeye anifanyaye niimbe usiku,

11 yeye atufundishaye sisi zaidi kuliko wanyama wa dunia,

na kutufanya wenye hekima kuliko ndege wa angani?’

12 Yeye hajibu wakati watu waliapo

kwa sababu ya kiburi cha watu waovu.

13 Naam, Mungu hasikilizi maombi yao ya ubatili;

Mwenyezi hayazingatii.

14 Si zaidi sana kwamba hatakusikiliza

wewe usemapo humwoni,

tena ya kwamba shauri lako liko mbele zake

na wewe lazima umngojee,

15 pia zaidi, kwamba hasira yake kamwe haiadhibu

wala haangalii uovu hata kidogo?

16 Hivyo Ayubu hufumbua kinywa chake kwa maneno yasiyo na maana;

anaongea maneno mengi bila maarifa.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/35-9d717b87ee5a7272fadc496a6c03cdb7.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 36

Elihu Atukuza Wema Wa Mungu

1 Elihu akaendelea kusema:

2 “Nivumilie kidogo zaidi nami nitakuonyesha

kwamba yako mengi zaidi ya kusemwa kwa ajili ya Mungu.

3 Ninayapata maarifa yangu kutoka mbali,

nami nitamhesabia haki Muumba wangu.

4 Uwe na hakika kwamba maneno yangu si ya uongo;

mmoja aliye mkamilifu katika maarifa yuko pamoja na wewe.

5 “Mungu ni mwenye nguvu, lakini hamdharau mwanadamu;

ni mwenye nguvu, naye ni thabiti katika shauri lake.

6 Hawaachi waovu waendelee kuishi,

bali huwapa walioteswa haki yao.

7 Yeye haondoi macho yake kwa wenye haki;

huwaketisha penye viti vya enzi pamoja na wafalme

na kuwatukuza milele.

8 Lakini ikiwa watu wamefungwa kwenye minyororo,

wakiwa wameshikiliwa na kamba za mateso,

9 huwaonyesha yale waliyoyatenda,

kwamba wametenda dhambi kwa majivuno.

10 Huwafanya wao kusikia maonyo,

na huwaagiza kutubu uovu wao.

11 Kama wakitii na kumtumikia,

wataishi siku zao zilizobaki katika mafanikio,

na miaka yao katika utoshelevu.

12 Lakini wasiposikiliza,

wataangamia kwa upanga,

nao watakufa pasipo maarifa.

13 “Wasiomcha Mungu moyoni mwao huficha chuki;

hata anapowafunga, hawamwombi msaada.

14 Wanakufa wangali vijana,

miongoni mwa wanaume hanithi wa mahali pa kuabudia miungu.

15 Bali wao wanaoteseka huwaokoa katika mateso yao,

na kuzungumza nao katika dhiki zao.

16 “Yeye anakubembeleza utoke katika mataya ya dhiki,

ili kukuweka mahali palipo na nafasi mbali na kizuizi,

hadi kwenye meza yako ya faraja iliyojaa vyakula vizuri.

17 Lakini sasa umelemewa na hukumu kwa ajili ya uovu;

hukumu na haki vimekukamata.

18 Uwe mwangalifu ili yeyote asikushawishi kwa utajiri;

usipotoshwe kwa fungu kubwa la rushwa.

19 Je, utajiri wako hata nguvu zako nyingi

vinaweza kukusaidia usiingie kwenye dhiki?

20 Usiutamani usiku uje,

ili uwaburute watu mbali na nyumba zao.

21 Jihadhari usigeukie uovu,

ambao unaupenda zaidi kuliko mateso.

22 “Mungu ametukuzwa katika nguvu zake.

Ni nani aliye mwalimu kama yeye?

23 Ni nani aliyemwelekeza katika njia zake,

au kumwambia, ‘Wewe umetenda yasiyo sawa’?

24 Kumbuka kuzitukuza kazi zake,

ambazo watu wamezisifu katika wimbo.

25 Wanadamu wote wameiona;

watu wanaikazia macho kwa mbali.

26 Tazama jinsi Mungu alivyo mkuu,

kupita ufahamu wetu!

Hesabu ya miaka yake haitafutiki.

27 “Yeye huvuta juu matone ya maji,

ayachujayo kama mvua kutoka kwenye vijito;

28 mawingu huangusha chini maji yake,

nayo mvua nyingi huwanyeshea wanadamu.

29 Ni nani ajuaye jinsi ayatandazavyo mawingu,

jinsi angurumavyo kutoka hemani mwake.

30 Tazama jinsi anavyotandaza umeme wa radi kumzunguka,

naye huvifunika vilindi vya bahari.

31 Hivi ndivyo atawalavyo mataifa,

na kuwapa chakula kwa wingi.

32 Huujaza mkono wake kwa umeme wa radi,

na kuuagiza kulenga shabaha yake.

33 Ngurumo zake hutangaza dhoruba inayokuja;

hata mifugo hujulisha kukaribia kwake.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/36-9dfe7bb9c67e7d2f7e4b2305978f90e7.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 37

1 “Kwa hili moyo wangu unatetemeka,

nao unaruka kutoka mahali pake.

2 Sikiliza! Sikiliza ngurumo ya sauti yake,

sauti ya ngurumo itokayo kinywani mwake.

3 Huuachilia umeme wake wa radi chini ya mbingu yote

na kuupeleka hata miisho ya dunia.

4 Baada ya hayo huja sauti ya ngurumo yake;

Mungu hunguruma kwa sauti yake ya fahari.

Wakati sauti yake ingurumapo tena,

huuachilia umeme wake wa radi.

5 Sauti ya Mungu hunguruma kwa namna za ajabu;

yeye hutenda mambo makuu kupita ufahamu wetu.

6 Huiambia theluji, ‘Anguka juu ya dunia,’

nayo manyunyu ya mvua, ‘Uwe mvua ya nguvu.’

7 Ili wanadamu wote aliowaumba wapate kujua kazi zake,

yeye humzuilia kila mtu shughuli zake.

8 Wanyama hujificha;

hubakia kwenye mapango yao.

9 Dhoruba hutoka katika chumba chake,

baridi hutoka katika upepo uendao kasi.

10 Pumzi ya Mungu hutoa barafu,

eneo kubwa la maji huganda.

11 Huyasheheneza mawingu kwa maji,

naye husambaza umeme wake wa radi kupitia hayo.

12 Nayo mawingu huzungukazunguka pande zote kwa amri yake,

juu ya uso wa dunia yote,

kufanya lolote ayaamuruyo.

13 Huleta mawingu ili kuadhibu wanadamu,

au kuinyeshea dunia yake na kuonyesha upendo wake.

14 “Ayubu, sikiliza hili;

nyamaza na uyafikiri maajabu ya Mungu.

15 Je, unajua jinsi Mungu anavyoyaongoza mawingu,

na kufanya umeme wake wa radi utoe mwanga?

16 Je, wajua jinsi mawingu yanavyokaa yakiwa yametulia,

hayo maajabu yake yeye aliye mkamilifu katika maarifa?

17 Wewe unayeshindwa na joto katika nguo zako

wakati nchi imenyamazishwa kimya bila upepo wa kusini,

18 je, waweza kuungana naye katika kuzitandaza anga,

zilizo ngumu kama kioo cha shaba ya kuyeyushwa?

19 “Tuambieni yatupasayo kumwambia;

hatuwezi kutayarisha shauri letu kwa sababu ya ujinga wetu.

20 Je, aambiwe kwamba nataka kuongea?

Je, yuko mtu ambaye angeomba kumezwa?

21 Basi hakuna awezaye kulitazama jua,

jinsi linavyongʼaa angani,

upepo ukishafagia mawingu.

22 Kutoka kaskazini yeye huja na fahari kuu;

Mungu huja katika utukufu wa kutisha.

23 Yeye Mwenyezi hatuwezi kumfikia, naye ametukuzwa katika uweza;

katika hukumu zake na haki yake kuu, hataonea.

24 Kwa hiyo, wanadamu mheshimuni,

kwa kuwa yeye hamstahi yeyote anayejidhania kuwa ana hekima.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/37-1ce551230e0e6b77be709801a1c6dde5.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 38

Bwana Anamjibu Ayubu

1 KishaBwanaakamjibu Ayubu kutoka upepo wa kisulisuli. Akasema:

2 “Nani huyu atiaye mashauri yangu giza

kwa maneno yasiyo na maarifa?

3 Jikaze kama mwanaume;

nitakuuliza swali,

nawe unijibu.

4 “Ulikuwa wapi nilipoweka misingi ya dunia?

Niambie, kama unafahamu.

5 Ni nani aliyeweka alama vipimo vyake?

Hakika wewe unajua!

Ni nani aliyenyoosha kamba ya kupimia juu yake?

6 Je, misingi yake iliwekwa juu ya nini,

au ni nani aliyeweka jiwe la pembeni,

7 wakati nyota za asubuhi zilipoimba pamoja,

na malaika wote walipokuwa wakipiga kelele kwa furaha?

8 “Ni nani aliyeifungia bahari milango

ilipopasuka kutoka tumbo,

9 nilipoyafanya mawingu kuwa vazi lake,

na kuyafungia katika giza nene,

10 nilipoamuru mipaka yake,

na kuiweka milango yake na makomeo mahali pake,

11 niliposema, ‘Unaweza kufika mpaka hapa wala si zaidi;

hapa ndipo mawimbi yako yenye kiburi yatakapokomea’?

12 “Umepata kuiamrisha asubuhi ipambazuke,

au kuyaonyesha mapambazuko mahali pake,

13 yapate kushika miisho ya dunia,

na kuwakungʼuta waovu waliomo?

14 Dunia hubadilika kama udongo wa mfinyanzi chini ya lakiri;

sura yake hukaa kama ile ya vazi.

15 Waovu huzuiliwa nuru yao,

nao mkono wao ulioinuliwa huvunjwa.

16 “Je, umepata kufika kwenye chemchemi za bahari?

Au kutembea mahali pa ndani pa vilindi?

17 Umewahi kuonyeshwa malango ya mauti?

Umewahi kuiona milango ya uvuli wa mauti?

18 Je, wewe unafahamu ukubwa wa dunia?

Niambie kama unajua haya yote.

19 “Njia ya kufika kwenye makao ya nuru ni ipi?

Nako maskani mwa giza ni wapi?

20 Je, unaweza kuvirudisha kwenye makao yake?

Unajua njia za kufika maskani mwake?

21 Hakika unajua, kwa kuwa ulikuwa umeshazaliwa!

Kwani umeishi miaka mingi!

22 “Je, umeshawahi kuingia katika ghala za theluji,

au kuona ghala za mvua ya mawe,

23 ambazo nimeziweka akiba kwa ajili ya wakati wa taabu,

na kwa ajili ya wakati wa vita na mapigano?

24 Ni ipi njia iendayo mahali umeme wa radi unapotawanyiwa,

au mahali upepo wa mashariki unaposambaziwa juu ya dunia?

25 Ni nani aliyepasua mifereji kwa ajili ya maji mengi ya mvua yaendayo kasi

na njia ya umeme wa radi,

26 ili kusababisha mvua kunyeshea mahali pasipokaliwa na mtu,

jangwa lisilo na yeyote ndani yake,

27 ili kuitosheleza nchi ya ukiwa na jangwa,

na majani yaanze kumea ndani yake?

28 Je, mvua ina baba?

Ni nani baba azaaye matone ya umande?

29 Barafu inatoka tumbo la nani?

Ni nani azaaye ukungu kutoka mbinguni,

30 wakati maji yawapo magumu kama jiwe,

wakati uso wa vilindi vya maji unapoganda?

31 “Je, waweza kuufunga mnyororo wa Kilimia?

Waweza kulegeza kamba za Orioni?

32 Waweza kuyaongoza makundi ya nyota kwa majira yake,

au kuongoza Dubu na watoto wake?

33 Je, unajua sheria zinazotawala mbingu?

Waweza kuweka utawala wa Mungu duniani?

34 “Waweza kuiinua sauti yako mpaka mawinguni,

na kujifunika mwenyewe na gharika ya maji?

35 Je, wewe hutuma umeme wa radi kwenye njia zake?

Je, hutoa taarifa kwako kukuambia, ‘Sisi tuko hapa’?

36 Ni nani aliyeujalia moyo hekima

au kuzipa akili ufahamu?

37 Nani mwenye hekima ya kuyahesabu mawingu?

Ni nani awezaye kuinamisha magudulia ya mbinguni

38 wakati mavumbi yawapo magumu,

na mabonge ya udongo kushikamana pamoja?

39 “Je, utamwindia simba jike mawindo,

na kuwashibisha simba wenye njaa

40 wakati wao wamejikunyata mapangoni mwao,

au wakivizia kichakani?

41 Ni nani ampaye kunguru chakula

wakati makinda yake yanamlilia Mungu,

yakizungukazunguka kwa ajili ya kukosa chakula?

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/38-7c604a5e83e01c6fdafe8560184cbdb2.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 39

1 “Je, wajua ni wakati gani mbuzi wa mlimani wanapozaa?

Je, watambua ni wakati gani kulungu jike azaapo mtoto wake?

2 Je, waweza kuhesabu miezi hadi wazaapo?

Je, unajua majira yao ya kuzaa?

3 Wao hujiinamisha na kuzaa watoto wao;

utungu wa kuzaa unakoma.

4 Watoto wao hustawi na kuongezeka nguvu nyikani;

huenda zao wala hawarudi tena.

5 “Ni nani aliyemwachia punda-mwitu awe huru?

Ni nani aliyezifungua kamba zake?

6 Nimempa nchi isiyokaliwa na watu kuwa masikani yake,

nchi ya chumvi kuwa makao yake.

7 Huzicheka ghasia za mji,

wala hasikii kelele za mwendesha gari.

8 Huzunguka vilimani kwa ajili ya malisho

na kutafuta kila kitu kibichi.

9 “Je, nyati atakubali kukutumikia?

Atakaa karibu na hori lako usiku?

10 Je, waweza kumfungia kwenye matuta kwa kamba?

Je, atalima mabonde nyuma yako?

11 Je, utamtumainia kwa ajili ya nguvu zake nyingi?

Utamwachia yeye kazi zako nzito?

12 Utaweza kumwamini akuletee nafaka yako nyumbani

kutoka shambani na kuikusanya kwenye sakafu yako ya kupuria?

13 “Mbuni hupigapiga mabawa yake kwa furaha,

lakini hayawezi kulinganishwa

na mabawa na manyoya ya korongo.

14 Huyataga mayai yake juu ya ardhi,

na kuyaacha yapate joto mchangani,

15 bila kujali kuwa mguu waweza kuyaponda,

kwamba baadhi ya wanyama wa porini wanaweza kuyakanyaga.

16 Yeye huyafanyia makinda yake ukatili kama vile si yake;

hajali kwamba taabu yake inaweza ikawa bure,

17 kwa kuwa Mungu hakumjalia hekima,

wala hakumpa fungu la akili njema.

18 Lakini akunjuapo mabawa yake kukimbia,

humcheka farasi pamoja na yeye aliyempanda.

19 “Je, wewe humpa farasi nguvu

au kuivika shingo yake manyoya marefu?

20 Je, wewe humfanya farasi aruke kama nzige,

akistaajabisha kwa tishio la mlio wake wa majivuno?

21 Huparapara bila woga, akizifurahia nguvu zake,

husonga mbele kukabiliana na silaha.

22 Huicheka hofu, haogopi chochote,

wala haukimbii upanga.

23 Podo hutoa sauti kando yake,

pamoja na mkuki unaongʼaa na fumo.

24 Bila woga na kwa ghadhabu huimeza nchi,

wala tarumbeta iliapo yeye hawezi kusimama.

25 Asikiapo sauti ya baragumu yeye hulia, ‘Aha!’

Hunusa harufu ya vita toka mbali,

sauti ya mtoa amri na ukelele wa vita.

26 “Je, mwewe huruka kwa hekima yako

na kuyakunjua mabawa yake kuelekea kusini?

27 Je, tai hupaa juu kwa amri yako

na kujenga kiota chake mahali pa juu?

28 Huishi juu ya miamba mirefu na kukaa huko usiku;

majabali yenye ncha kali ndiyo ngome yake.

29 Kutoka huko hutafuta chakula chake;

macho yake hukiona kutoka mbali.

30 Makinda yake hujilisha damu,

na pale palipo na machinjo, ndipo yeye alipo.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/39-3de4d0f9a36a733ce63a94621bf3cc7a.mp3?version_id=1627—