Categories
Ayubu

Ayubu 20

Sofari Anasema: Uovu Hupokea Malipo Ya Haki

1 Ndipo Sofari Mnaamathi akajibu:

2 “Mawazo yanayonisumbua yananisukuma kujibu,

kwa sababu nimehangaika sana.

3 Ninasikia makaripio ambayo yananivunjia heshima,

nao ufahamu wangu unanisukuma kujibu.

4 “Hakika unajua jinsi ilivyokuwa tangu zamani,

tangu zamani mwanadamu alipowekwa duniani,

5 macheko ya mtu mwovu ni ya muda mfupi,

nayo furaha ya wasiomcha Mungu hudumu kwa kitambo tu.

6 Ingawa kujikweza kwake hufikia mbinguni

na kichwa chake hugusa mawingu,

7 ataangamia milele kama mavi yake mwenyewe.

Wale waliomwona watauliza, ‘Yuko wapi?’

8 Kama ndoto hutoweka, wala hapatikani tena,

amefukuziwa mbali kama maono ya usiku.

9 Jicho lililomwona halitamwona tena;

mahali pake hapatamwona tena.

10 Watoto wake watalipa yote baba yao aliyowadhulumu maskini,

nayo mikono yake itarudisha mali yote aliyonyangʼanya watu.

11 Nguvu za ujana zilizoijaza mifupa yake,

zitalala naye mavumbini.

12 “Ingawa uovu ni mtamu kinywani mwake

naye huuficha chini ya ulimi wake,

13 ingawa hawezi kukubali kuuachia uende,

lakini huuweka kinywani mwake.

14 Hata hivyo chakula chake kitakuwa kichungu tumboni mwake,

nacho kitakuwa sumu kali ya nyoka ndani yake.

15 Atatema mali alizozimeza;

Mungu atalifanya tumbo lake kuzitapika.

16 Atanyonya sumu za majoka;

meno ya nyoka mwenye sumu kali yatamuua.

17 Hatafurahia vijito,

mito inayotiririsha asali na siagi.

18 Vile alivyovitaabikia atavirudisha bila kuvila;

hatafurahia faida itokanayo na biashara yake.

19 Kwa kuwa aliwaonea maskini na kuwaacha pasipo kitu;

amenyangʼanya kwa nguvu nyumba asizozijenga.

20 “Hakika hatakuwa na raha katika kutamani kwake sana;

hawezi kujiokoa mwenyewe kwa hazina zake.

21 Hakuna chochote kitakachosalia kwa ajili yake ili ale;

kufanikiwa kwake hakutadumu.

22 Katikati ya wingi wa ustawi wake, dhiki itampata;

taabu itamjia kwa nguvu zote.

23 Atakapokuwa amelijaza tumbo lake,

Mungu ataionyesha ghadhabu kali dhidi yake,

na kumnyeshea mapigo juu yake.

24 Ijapokuwa aikimbia silaha ya chuma,

mshale wa shaba utamchoma.

25 Atauchomoa katika mgongo wake,

ncha ingʼaayo kutoka ini lake.

Vitisho vitakuja juu yake;

26 giza nene linavizia hazina zake.

Moto usiopepewa na mtu utamteketeza,

na kuangamiza yaliyosalia nyumbani mwake.

27 Mbingu zitaweka wazi hatia yake,

nayo nchi itainuka kinyume chake.

28 Mafuriko yataichukua nyumba yake,

maji yaendayo kasi katika siku ya ghadhabu ya Mungu.

29 Hili ndilo fungu Mungu alilowagawia waovu,

urithi uliowekwa kwa ajili yao na Mungu.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/20-ac760fc64b5b2d89b62f0d88b39c61c4.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 21

Ayubu Anajibu: Waovu Mara Nyingi Huenda Bila Kuadhibiwa

1 Ndipo Ayubu akajibu:

2 “Yasikilizeni maneno yangu kwa makini;

hii na iwe faraja mnayonipa mimi.

3 Nivumilieni ninapozungumza,

nami nikishazungumza, endeleeni kunidhihaki.

4 “Je, kwani malalamiko yangu yanaelekezwa kwa mwanadamu?

Kwa nini nisikose subira?

5 Niangalieni mkastaajabu;

mkaweke mkono juu ya vinywa vyenu.

6 Ninapowaza juu ya hili, ninaogopa,

nao mwili wangu unatetemeka.

7 Kwa nini waovu wanaendelea kuishi,

wakifikia umri wa uzee na kuendelea kuwa na nguvu?

8 Huwaona watoto wao wakithibitika

wakiwa wamewazunguka,

wazao wao mbele za macho yao.

9 Nyumba zao zi salama wala hakuna hofu;

fimbo ya Mungu haiko juu yao.

10 Madume yao ya ngʼombe huvyaza bila kushindwa kamwe;

ngʼombe wao huzaa wala hawaharibu mimba.

11 Huwatoa watoto wao nje kama kundi;

wadogo wao huchezacheza.

12 Huimba nyimbo kwa matari na kwa kinubi,

nao huifurahia sauti ya filimbi.

13 Huitumia miaka yao katika mafanikio

nao hushuka kaburini kwa amani.

14 Lakini humwambia Mungu, ‘Tuache sisi!’

Hatuna haja ya kufahamu njia zako.

15 Mwenyezi ni nani hata tumtumikie?

Tutapata faida gani kumwomba?

16 Lakini kufanikiwa kwao hakupo mikononi mwao wenyewe,

hivyo najitenga mbali na shauri la waovu.

17 “Lakini ni mara ngapi taa ya waovu huzimwa?

Ni mara ngapi maafa huwajia,

yale yawapatayo ambayo Mungu

huwapangia katika hasira yake?

18 Ni mara ngapi huwa kama majani makavu mbele ya upepo,

kama makapi yachukuliwayo na dhoruba?

19 Imesemekana, ‘Mungu huiweka akiba adhabu ya mtu

kwa ajili ya wanawe.’

Mungu na amlipe mtu mwenyewe,

ili apate kulijua!

20 Macho yake mwenyewe na yaone maangamizi yake;

yeye na ainywe ghadhabu ya Mwenyezi.

21 Kwani anajali nini kuhusu jamaa anayoiacha nyuma,

miezi yake aliyopangiwa ifikapo mwisho?

22 “Je, yuko mtu yeyote awezaye kumfundisha Mungu maarifa,

iwapo yeye ndiye ahukumuye hata walio juu ya wote?

23 Mtu mmoja hufa akiwa na nguvu zake kamili,

akiwa salama na mwenye raha kamili,

24 mwili wake ukiwa umenawiri,

nayo mifupa yake ikiwa imejaa mafuta ndani yake.

25 Mtu mwingine hufa katika uchungu wa nafsi,

akiwa hajafurahia kamwe jambo lolote zuri.

26 Hao wote hulala mavumbini,

nao mabuu huwafunika wote.

27 “Ninayajua kikamilifu yale mnayoyafikiri,

mipango ambayo kwayo mngenitendea mabaya.

28 Mwasema, ‘Iko wapi sasa nyumba ya huyo mtu mkuu,

mahema ambayo watu waovu walikaa?’

29 Je, hamkuwahi kuwauliza hao wanaosafiri?

Je, hamkutafakari taarifa zao:

30 kwamba mtu mwovu huepushwa kutoka siku ya maafa,

kwamba huokolewa kutoka siku ya ghadhabu?

31 Ni nani hulaumu matendo yake mbele ya uso wake?

Ni nani ampatilizaye kwa yale aliyoyatenda?

32 Hupelekwa kaburini,

nao ulinzi ukawekwa kwenye kaburi lake.

33 Udongo ulio bondeni ni mtamu kwake;

watu wote watamfuata,

nao umati wa watu usiohesabika umemtangulia.

34 “Hivyo ninyi mnawezaje kunifariji kwa upuzi wenu?

Hakuna kilichosalia cha majibu yenu isipokuwa uongo!”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/21-c28fa39ae554b3852a4b8086edbd1817.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 22

Elifazi Anasema: Uovu Wa Ayubu Ni Mkubwa

1 Ndipo Elifazi Mtemani akajibu:

2 “Je, mwanadamu aweza kuwa wa faida kwa Mungu?

Je, hata mtu mwenye hekima aweza kumfaidi?

3 Je, Mwenyezi angefurahia nini

kama ungekuwa mwadilifu?

Au je, yeye angepata faida gani

kama njia zako zingekuwa kamilifu?

4 “Je, ni kwa ajili ya utaua wako ndiyo maana anakukemea

na kuleta mashtaka dhidi yako?

5 Je, uovu wako si mkuu?

Dhambi zako si hazina mwisho?

6 Umedai dhamana kwa ndugu zako bila sababu;

umewavua watu nguo zao, ukawaacha uchi.

7 Hukumpa maji aliyechoka,

nawe ulimnyima chakula mwenye njaa,

8 ingawa ulikuwa mtu mwenye uwezo ukimiliki nchi:

mtu uliyeheshimiwa, ukiishi ndani yake.

9 Umewafukuza wajane mikono mitupu

na kuzivunja nguvu za yatima.

10 Ndiyo sababu mitego imekuzunguka pande zote,

hatari ya ghafula inakutia hofu,

11 ndiyo sababu ni giza sana huwezi kuona,

tena ndiyo sababu mafuriko ya maji yamekufunika.

12 “Je, Mungu hayuko katika mbingu za juu?

Juu kuliko nyota zilizo juu sana!

13 Hivyo wewe wasema, ‘Mungu anajua nini?’

Je, yeye huhukumu katika giza kama hilo?

14 Mawingu mazito ni pazia lake, hivyo hatuoni sisi

atembeapo juu ya anga la dunia.

15 Je, utaifuata njia ya zamani,

ambayo watu waovu waliikanyaga?

16 Waliondolewa kabla ya wakati wao,

misingi yao ikachukuliwa na mafuriko.

17 Walimwambia Mungu, ‘Tuache sisi!

Huyo Mwenyezi aweza kutufanyia nini?’

18 Lakini ndiye alizijaza nyumba zao na vitu vizuri,

hivyo ninajitenga mbali na mashauri ya waovu.

19 “Wenye haki wanaona maangamizi yao na kufurahi,

nao wasio na hatia huwadhihaki, wakisema,

20 ‘Hakika adui zetu wameangamizwa,

nao moto umeteketeza mali zao.’

21 “Mjue sana Mungu ili uwe na amani,

ndipo mema yatakapokujia.

22 Uyapokee mafundisho toka kinywani mwake,

na maneno yake uyaweke moyoni mwako.

23 Kama ukimrudia Mwenyezi, utarudishwa upya:

Kama ukiuondoa uovu uwe mbali na hema lako,

24 kama dhahabu yako ukiihesabu kama mavumbi,

dhahabu yako ya Ofiri kama miamba ya mabondeni,

25 ndipo Mwenyezi atakuwa dhahabu yako,

naye atakuwa fedha yako iliyo bora.

26 Hakika ndipo utakapojifurahisha kwa Mwenyezi,

nawe utamwinulia Mungu uso wako.

27 Utamwomba yeye, naye atakusikia,

nawe utazitimiza nadhiri zako.

28 Utakusudia jambo nalo litatendeka,

nao mwanga utaangazia njia zako.

29 Watu watakaposhushwa, nawe ukasema, ‘Wainue!’

ndipo atamwokoa aliyevunjika moyo.

30 Atamwokoa hata yule ambaye ana hatia,

ataokolewa kwa sababu ya usafi wa mikono yako.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/22-2f1754ba7ee89cebc08299eed153fe31.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 23

Ayubu Anajibu: Kulalamika Kwangu Ni Uchungu

1 Ndipo Ayubu akajibu:

2 “Hata leo malalamiko yangu ni chungu;

mkono wake ni mzito juu yangu hata nikiugua.

3 Laiti ningefahamu mahali pa kumwona;

laiti ningeweza kwenda mahali akaapo!

4 Ningeliweka shauri langu mbele zake,

na kukijaza kinywa changu na hoja.

5 Ningejua kwamba angenijibu nini,

na kuelewa lile ambalo angelisema.

6 Je, angenipinga kwa nguvu nyingi?

La, asingenigandamiza.

7 Hapo mtu mwadilifu angeweka shauri lake mbele zake,

nami ningeokolewa milele na mhukumu wangu.

8 “Lakini nikienda mashariki, hayupo;

nikienda magharibi, simpati.

9 Anapokuwa kazini pande za kaskazini, simwoni;

akigeukia kusini, nako simwoni hata kidogo.

10 Lakini anaijua njia niiendeayo;

akiisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu.

11 Nyayo zangu zimefuata hatua zake kwa karibu;

nimeishika njia yake bila kukengeuka.

12 Sijaziacha amri zilizotoka midomoni mwake;

nimeyathamini maneno ya kinywa chake kuliko chakula changu cha kila siku.

13 “Lakini yeye husimama peke yake; ni nani awezaye kumpinga?

Yeye hufanya lolote atakalo.

14 Hutimiliza maagizo yake dhidi yangu,

na bado anayo mipango mingi kama hiyo ambayo ameiweka akiba.

15 Hiyo ndiyo sababu ninaingiwa na hofu mbele zake;

nifikiriapo haya yote ninamwogopa.

16 Mungu ameufanya moyo wangu kuzimia;

yeye Mwenyezi amenitia hofu.

17 Hata hivyo sijanyamazishwa na giza,

wala kwa giza nene linalofunika uso wangu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/23-141a9b0fd288b09e7b73418d07072958.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 24

Ayubu Analalamikia Jeuri Duniani

1 “Kwa nini Mwenyezi asiweke nyakati kwa ajili ya hukumu?

Kwa nini wale wamjuao wazitafute siku kama hizo bila mafanikio?

2 Watu husogeza mawe ya mpaka;

huchunga makundi ya wanyama waliyonyangʼanya kwa nguvu.

3 Huwanyangʼanya yatima punda wao,

na kumchukua rehani fahali wa mjane.

4 Humsukuma mhitaji kutoka njia,

na kuwafanya maskini wote wa nchi kulazimika kujificha.

5 Kama punda-mwitu jangwani,

maskini huzunguka katika kazi zao za kutafuta chakula;

mahali palipo jangwa

huwapa chakula cha watoto wao.

6 Hukusanya chakula mashambani na kuokota masazo

katika mashamba ya mizabibu ya waovu.

7 Kwa kukosa nguo, usiku kucha hukaa uchi;

hawana chochote cha kujifunika baridi.

8 Hutota kwa mvua za mlimani,

nao huikumbatia miamba kwa ajili ya kukosa pa kujisitiri.

9 Mtoto yatima hupokonywa matitini;

mtoto wachanga wa maskini hunyakuliwa kwa ajili ya deni.

10 Kwa kukosa nguo, hutembea uchi;

hubeba miganda ya ngano, lakini huwa na njaa.

11 Hukamua zeituni katika mawe ya kusagia;

hukanyaga mashinikizo, lakini wanaona kiu.

12 Kilio cha huzuni cha wanaokufa kinapaa kutoka mjini,

nazo nafsi za waliojeruhiwa zinalilia msaada.

Lakini Mungu hamlaumu mtu yeyote

kwa kutenda mabaya.

13 “Wako wale wanaoiasi nuru,

wasiofahamu njia zake

wala hawakai katika mapito yake.

14 Wakati mwanga wa mchana unapotoweka, muuaji huinuka

naye huwaua maskini na mhitaji;

wakati wa usiku hunyemelea kama mwizi.

15 Jicho la mzinzi hungojea wakati wa giza,

naye hufikiri, ‘Hakuna jicho litakaloniona,’

naye huuficha uso wake.

16 Katika giza, huvunja majumba,

lakini wakati wa mchana hujifungia ndani;

hawataki kufanya lolote nuruni.

17 Kwa wote hawa, giza nene ndiyo asubuhi yao;

hujifanya rafiki na vitisho vya gizani.

18 “Lakini wao ni povu juu ya maji;

sehemu yao juu ya nchi imelaaniwa,

hivyo hakuna hata mmoja

aendaye kwenye shamba la mizabibu.

19 Kama vile joto na hari vinyakuavyo theluji iliyoyeyuka,

ndivyo kuzimu kuwanyakuavyo waliotenda dhambi.

20 Tumbo lililowazaa huwasahau,

nao huwa karamu ya mabuu;

watu waovu hawakumbukwi tena,

lakini huvunjika kama mti.

21 Huwafanya mawindo wanawake tasa na wasio na watoto,

nao hawaonyeshi huruma kwa wajane.

22 Lakini Mungu huwakokota wenye nguvu kwa uwezo wake;

ingawa wamestawi, hawana hakika ya maisha.

23 Aweza akawaacha wakapumzika wakijihisi salama,

lakini macho yake yanaona njia zao.

24 Kwa kitambo kidogo hutukuka, hatimaye hutoweka;

hushushwa na kukusanywa kama wengine wote,

hukatwa kama masuke ya nafaka.

25 “Kama hili sivyo, ni nani awezaye kunithibitisha kuwa mwongo,

na kuyafanya maneno yangu kuwa si kitu?”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/24-371672903050fe2165c24e426b3d26df.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 25

Bildadi Anasema: Mwanadamu Awezaje Kuwa Mwadilifu Mbele Za Mungu?

1 Ndipo Bildadi Mshuhi akajibu:

2 “Mamlaka na kuheshimiwa ni vyake Mungu;

yeye huthibitisha amani katika mbingu juu.

3 Je, majeshi yake yaweza kuhesabika?

Ni nani asiyeangaziwa na nuru yake?

4 Mtu awezaje kuwa mwadilifu mbele za Mungu?

Awezaje mtu aliyezaliwa na mwanamke kuwa safi?

5 Ikiwa hata mwezi sio mwangavu

nazo nyota si safi machoni pake,

6 sembuse mtu ambaye ni funza:

mwanadamu ambaye ni buu tu!”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/25-d9dbc23a05f445282c5d246614f53c82.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 26

Ayubu Anajibu: Utukufu Wa Mungu Hauchunguziki

1 Kisha Ayubu akajibu:

2 “Tazama jinsi ulivyomsaidia mtu asiye na uwezo!

Jinsi ulivyouokoa mkono ulio dhaifu!

3 Ni shauri gani ulilompa yeye asiye na hekima?

Nayo ni busara gani kubwa uliyoonyesha!

4 Ni nani aliyekusaidia kutamka maneno hayo?

Nayo ni roho ya nani iliyosema kutoka kinywani mwako?

5 “Wafu wako katika maumivu makuu,

wale walio chini ya maji na wale waishio ndani yake.

6 Mautiiko wazi mbele za Mungu;

Uharibifuhaukufunikwa.

7 Hutandaza anga la kaskazini mahali patupu;

naye huiningʼiniza dunia mahali pasipo na kitu.

8 Huyafungia maji kwenye mawingu yake,

hata hivyo mawingu hayapasuki kwa uzito wake.

9 Huufunika uso wa mwezi mpevu,

akitandaza mawingu juu yake.

10 Amechora mstari wa upeo juu ya uso wa maji,

ameweka mpaka wa nuru na giza.

11 Nguzo za mbingu nazo zatetemeka,

zinatishika anapozikemea.

12 Kwa nguvu zake aliisukasuka bahari;

kwa hekima yake alimkata Rahabuvipande vipande.

13 Aliisafisha anga kwa pumzi yake;

kwa mkono wake alimchoma joka aendaye mbio.

14 Haya ni mambo madogo tu katika matendo yake;

tazama jinsi ulivyo mdogo mnongʼono tunaousikia kumhusu!

Ni nani basi awezaye kuelewa

ngurumo za nguvu zake?”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/26-ed6bf60e96ef1425fcbc6bacd9e922ae.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 27

Ayubu Anadumisha Uadilifu Wake

1 Ndipo Ayubu akaendelea na hoja yake, akasema:

2 “Hakika kama Mungu aishivyo, aliyeninyima haki yangu,

Mwenyezi ambaye amenifanya

nionje uchungu wa nafsi,

3 kwa muda wote nitakaokuwa na uhai ndani yangu,

nayo pumzi ya Mungu ikiwa puani mwangu,

4 midomo yangu haitanena uovu,

wala ulimi wangu hautatamka udanganyifu.

5 Sitakubaliana nanyi kabisa kuwa mko sahihi;

hadi nife, sitakana uadilifu wangu.

6 Nitadumisha haki yangu wala sitaiacha;

dhamiri yangu haitanisuta muda wote ninaoishi.

7 “Watesi wangu wawe kama waovu,

nao adui zangu wawe kama wasio haki!

8 Kwa maana mtu asiyemcha Mungu

analo tegemeo gani anapokatiliwa mbali,

Mungu anapouondoa uhai wake?

9 Je, Mungu husikiliza kilio chake,

shida zimjiapo?

10 Je, anaweza kumfurahia Mwenyezi?

Je, atamwita Mungu nyakati zote?

11 “Nitawafundisha juu ya uweza wa Mungu;

njia za Mwenyezi sitazificha.

12 Ninyi nyote mmeona hili wenyewe.

Ni ya nini basi mazungumzo haya yasiyo na maana?

13 “Hili ndilo fungu ambalo Mungu humpa mtu mwovu,

urithi ule mtu mdhalimu anapokea kutoka kwa Mwenyezi:

14 Hata kama watoto wake watakuwa wengi kiasi gani,

fungu lao ni kuuawa kwa upanga;

wazao wake hawatakuwa kamwe

na chakula cha kuwatosha.

15 Tauni itawazika wale watakaonusurika miongoni mwao,

nao wajane wao hawatawaombolezea.

16 Ajapokusanya fedha nyingi kama mavumbi,

na mavazi kama malundo ya udongo wa mfinyanzi,

17 yale yote mtu mwovu aliyojiwekea akiba, mwenye haki atayavaa,

naye asiye na hatia ataigawanya fedha yake.

18 Nyumba aijengayo ni kama utando wa buibui,

kama kibanda alichotengeneza mlinzi.

19 Yeye hulala akiwa tajiri, lakini ndiyo mara ya mwisho;

afunguapo macho yake, yote yametoweka.

20 Vitisho humjia kama mafuriko;

dhoruba humkumba ghafula usiku.

21 Upepo mkali wa mashariki humchukua, naye hutoweka;

humzoa kutoka mahali pake.

22 Humvurumisha bila huruma,

huku akikimbia kasi kukwepa nguvu zake.

23 Upepo humpigia makofi kwa dharau,

na kumfukuza atoke mahali pake.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/27-985e4b5f356b0b720aef18ddf5c178fe.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 28

Mapumziko: Imani Inakopatikana

1 “Kuna machimbo ya fedha,

na mahali dhahabu isafishwapo.

2 Chuma hupatikana ardhini,

nayo shaba huyeyushwa kutoka mawe ya madini.

3 Mwanadamu hukomesha giza;

huyatafuta hadi sehemu iliyo mbali,

kwa ajili ya kuchimbua mawe yenye madini

katika giza jeusi sana.

4 Huchimba shimo jembamba mbali na makao ya watu,

mahali paliposahaulika na nyayo za wanadamu;

mbali na wanadamu huningʼinia na kupembea kwa kamba.

5 Ardhi, ambako chakula hutoka,

chini hugeuzwa kwa moto;

6 yakuti samawi hutoka katika miamba yake,

nalo vumbi lake lina vipande vya dhahabu.

7 Hakuna ndege awindaye aijuaye njia ile iliyofichika,

wala hakuna jicho la mwewe lililoiona.

8 Wanyama wa porini wanaotamba hawajawahi kupakanyaga,

wala simba azungukaye huko.

9 Mikono ya mwanadamu hushambulia miamba migumu sana,

na kuiacha wazi mizizi ya milima.

10 Hutoboa shimo refu la kupenya chini kwa chini kwenye miamba;

macho yake huona hazina zake zote.

11 Hutafuta vyanzo vya mito

na kuvileta vitu vilivyofichika katika nuru.

12 “Lakini hekima inaweza kupatikana wapi?

Ufahamu unakaa wapi?

13 Mwanadamu hatambui thamani yake;

haiwezi kupatikana katika nchi ya walio hai.

14 Kilindi husema, ‘Haiko ndani yangu’;

bahari nayo husema, ‘Haiko pamoja nami.’

15 Haiwezi kununuliwa kwa dhahabu safi kuliko zote,

wala thamani yake haiwezi kupimwa kwa fedha.

16 Haiwezi kununuliwa kwa dhahabu ya Ofiri,

kwa shohamu ya thamani kubwa au yakuti samawi ya thamani kubwa.

17 Dhahabu wala mawe maangavu haviwezi kulinganishwa nayo,

wala haiwezi hubadilishwa na vito vya dhahabu.

18 Marijani na yaspi hazistahili kutajwa;

thamani ya hekima ni zaidi ya akiki nyekundu.

19 Yakuti manjano ipatikanayo Kushi haiwezi kulinganishwa nayo,

wala haiwezi kununuliwa kwa dhahabu safi.

20 “Ni wapi basi hekima itokako?

Ufahamu hukaa wapi?

21 Imefichika machoni pa kila kitu kilicho hai,

imesitiriwa hata kwa ndege wa angani.

22 Uharibifu na Mauti husema,

‘Ni uvumi wake tu uliotufikia masikioni mwetu.’

23 Mungu anaifahamu njia ya kuiendea hekima

na ndiye peke yake anayefahamu inakokaa,

24 kwa maana yeye huitazama miisho ya dunia

na huona kila kitu chini ya mbingu.

25 Alipofanyiza nguvu za upepo

na kuyapima maji,

26 alipofanya maagizo kwa ajili ya mvua

na njia kwa ajili ya umeme wa radi,

27 ndipo alipoitazama hekima na kuikadiria thamani yake,

akaithibitisha na kuihakikisha.

28 Naye Mungu akamwambia mwanadamu,

‘KumchaBwana: hiyo ndiyo hekima,

nako kujitenga na uovu ndio ufahamu.’ ”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/28-df51764e811b351b5adcaf1c2f63aecd.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 29

Ayubu Anamaliza Utetezi Wake

1 Ayubu akaendelea na hoja yake, akasema:

2 “Tazama jinsi ninavyoitamani miezi iliyopita,

zile siku ambazo Mungu alikuwa akinilinda,

3 wakati taa yake iliniangazia kichwani changu,

na kwa mwanga wake Mungu nikapita katikati ya giza!

4 Natamani siku zile nilizokuwa katika ustawi wangu,

wakati urafiki wa Mungu wa ndani ulipoibariki nyumba yangu,

5 wakati Mwenyezi alikuwa pamoja nami,

nao watoto wangu walikuwa wamenizunguka,

6 wakati njia yangu ilikuwa imenyweshewa siagi,

nao mwamba ukanimiminia vijito vya mafuta ya zeituni.

7 “Wakati nilipokwenda kwenye lango la mji

na kuketi katika kiwanja,

8 vijana waliniona wakakaa kando,

nao wazee walioketi wakasimama;

9 wakuu wakaacha kuzungumza

na kuziba vinywa vyao kwa mikono yao;

10 wenye vyeo wakanyamazishwa,

nazo ndimi zao zikagandamana na makaakaa ya vinywa vyao.

11 Yeyote aliyenisikia alinena mema juu yangu,

nao walioniona walinisifu,

12 kwa sababu nilimwokoa maskini aliyeomba msaada,

naye yatima aliyekuwa hana wa kumsaidia.

13 Mtu aliyekuwa karibu kufa alinibariki,

nami niliufanya moyo wa mjane kuimba.

14 Niliivaa haki kama vazi langu;

uadilifu ulikuwa joho langu na kilemba changu.

15 Nilikuwa macho ya kipofu

na miguu kwa kiwete.

16 Nilikuwa baba kwa mhitaji;

nilimtetea mgeni.

17 Niliyavunja meno makali ya waovu,

na kuwapokonya wahanga kwenye meno yao.

18 “Nikafikiri, ‘Nitafia katika nyumba yangu mwenyewe,

nazo siku zangu zitakuwa nyingi kama chembechembe za mchanga.

19 Mizizi yangu itafika mpaka kwenye maji,

nao umande utakaa juu ya matawi yangu usiku kucha.

20 Utukufu wangu utabakia kuwa mpya ndani yangu,

upinde wangu daima utaendelea kuwa mpya mkononi mwangu.’

21 “Watu walinisikiliza kwa tumaini,

wakingojea ushauri wangu kwa utulivu.

22 Baada ya mimi kuzungumza, hawakusema zaidi;

maneno yangu yaliingia masikioni mwao kwa makini.

23 Waliningojea kama manyunyu ya mvua

na kuyapokea maneno yangu

kama ardhi inyonyavyo mvua ya vuli.

24 Walipokata tamaa niliwaonyesha uso wa furaha;

nuru ya uso wangu ilikuwa ya thamani kwao.

25 Niliwachagulia njia na kukaa kama mkuu wao;

niliishi kama mfalme katikati ya majeshi yake;

nikawa kama yeye anayewafariji waombolezaji.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/29-6d71ac5ab2e4ddd690952a27673daf69.mp3?version_id=1627—