Categories
Ayubu

Ayubu 10

Ayubu: Nayachukia Maisha Yangu

1 “Nayachukia sana haya maisha yangu;

kwa hiyo nitatoa malalamiko yangu kwa wazi bila kujizuia,

nami nitanena kutokana na uchungu wa moyo wangu.

2 Nitamwambia Mungu: Usinihukumu,

bali niambie una mashtaka gani dhidi yangu.

3 Je, inakupendeza wewe kunionea,

kuikataa kwa dharau kazi ya mikono yako,

huku wewe ukitabasamu juu ya mipango ya waovu?

4 Je, wewe una macho ya kimwili?

Je, wewe huona kama mwanadamu aonavyo?

5 Je, siku zako ni kama zile za mwanadamu,

au miaka yako ni kama ile ya mtu,

6 ili kwamba utafute makosa yangu

na kuichunguza dhambi yangu;

7 ingawa wajua kuwa mimi sina hatia,

na hakuna awezaye kunitoa mkononi mwako?

8 “Mikono yako ndiyo iliyoniumba na kunifanya.

Je, sasa utageuka na kuniangamiza?

9 Kumbuka kuwa ulinifinyanga kama udongo wa mfinyanzi.

Je, sasa utanifanya kuwa mavumbi tena?

10 Je, wewe hukunimimina mimi kama maziwa,

na kunigandisha kama jibini,

11 ukanivika ngozi na nyama,

na kuniunga pamoja kwa mifupa na mishipa?

12 Umenipa uhai na kunitendea wema,

katika uangalizi wako umeilinda roho yangu.

13 “Lakini hili ndilo ulilolificha moyoni mwako,

nami ninajua kuwa hili lilikuwa katika nia yako:

14 Kama nilifanya dhambi, ungekuwa umeniona,

wala usingeacha kosa langu lipite bila kuadhibiwa.

15 Kama nina hatia, ole wangu!

Hata kama ningekuwa sina hatia,

siwezi kukiinua kichwa changu,

kwa kuwa nimejawa na aibu,

na kuzama katika mateso yangu.

16 Kama nikiinua kichwa changu juu, unaninyatia kama simba,

na kuonyesha tena uwezo wa kutisha dhidi yangu.

17 Wewe waleta mashahidi wapya dhidi yangu

na kuzidisha hasira yako juu yangu;

nazo nguvu zako zinanijia wimbi moja baada ya jingine.

18 “Kwa nini basi ulinitoa tumboni?

Ninatamani ningekufa kabla jicho lolote halijaniona.

19 Laiti nisingekuwako kamwe,

au ningekuwa nimechukuliwa moja kwa moja

kutoka tumboni kwenda kaburini!

20 Je, siku zangu chache si zimekaribia kuisha?

Niachie ili niweze kupata muda mfupi wa kufurahi

21 kabla sijaenda mahali ambapo hakuna kurudi tena,

katika nchi ya giza na uvuli wa mauti,

22 nchi ya giza kuu sana,

yenye uvuli wa giza na machafuko,

mahali ambapo hata nuru ni giza.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/10-caa0a02a1bea04be51fd6a62f5adaf51.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 11

Sofari Anasema: Hatia Ya Ayubu Inastahili Adhabu

1 Ndipo Sofari Mnaamathi akajibu:

2 “Je, maneno haya yote yapite bila kujibiwa?

Je, huyu mnenaji athibitishwe kuwa na haki?

3 Je, maneno yako ya upuzi yawafanye watu wanyamaze kimya?

Je, mtu asikukemee unapofanya dhihaka?

4 Unamwambia Mungu, ‘Imani yangu ni kamili

nami ni safi mbele zako.’

5 Aha! Laiti kwamba Mungu angesema,

kwamba angefungua midomo yake dhidi yako,

6 naye akufunulie siri za hekima,

kwa kuwa hekima ya kweli ina pande mbili.

Ujue hili: Mungu amesahau hata baadhi ya dhambi zako.

7 “Je, waweza kujua siri za Mungu?

Je, waweza kuyachunguza mambo yote kumhusu Mwenyezi?

8 Ni juu mno kuliko mbingu: waweza kufanya nini?

Kina chake ni kirefu kuliko kuzimu:

wewe waweza kujua nini?

9 Kipimo chake ni kirefu kuliko dunia,

nacho ni kipana kuliko bahari.

10 “Kama akija na kukufunga gerezani,

na kuitisha mahakama, ni nani awezaye kumpinga?

11 Hakika anawatambua watu wadanganyifu;

naye aonapo uovu, je, haangalii?

12 Mpumbavu aweza kuwa mwenye hekima,

endapo mtoto wa punda-mwitu atazaliwa mwanadamu.

13 “Hata sasa ukiutoa moyo wako kwake

na kumwinulia mikono yako,

14 ukiiondolea mbali ile dhambi iliyo mkononi mwako

wala usiuruhusu uovu ukae hemani mwako,

15 ndipo utainua uso wako bila aibu;

utasimama imara bila hofu.

16 Hakika utaisahau taabu yako,

utaikumbuka tu kama maji yaliyokwisha kupita.

17 Maisha yako yatangʼaa kuliko adhuhuri,

nalo giza litakuwa kama alfajiri.

18 Utakuwa salama, kwa kuwa lipo tumaini;

utatazama pande zote na kupumzika kwa salama.

19 Utalala, wala hakuna atakayekuogofya,

naam, wengi watajipendekeza kwako.

20 Bali macho ya waovu hayataona,

wokovu utawaepuka;

tarajio lao litakuwa ni hangaiko

la mtu anayekata roho.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/11-303367365150fb670b22e76b200c264b.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 12

Ayubu Anajibu: Mimi Ni Mtu Wa Kuchekwa

1 Ndipo Ayubu akajibu:

2 “Bila shaka ninyi ndio watu,

nayo hekima itakoma mtakapokufa!

3 Lakini mimi ninao ufahamu kama ninyi;

mimi si duni kwenu.

Ni nani asiyejua mambo haya yote?

4 “Nimekuwa mtu wa kuchekwa na rafiki zangu,

ingawa nilimwita Mungu naye akanijibu:

mimi ni mtu wa kuchekwa tu,

ingawa ni mwadilifu na nisiye na hatia!

5 Wanadamu wakiwa katika utulivu huwa na dharau kwa wale wenye msiba

kana kwamba ndiyo haki ya wale ambao miguu yao inateleza.

6 Hema za wanyangʼanyi hazisumbuliwi,

wale wanaomghadhibisha Mungu wako salama:

wale wamchukuao mungu wao mikononi mwao.

7 “Lakini ulizeni wanyama, nao watawafundisha,

au ndege wa angani, nao watawaambia;

8 au zungumzeni na dunia, nayo itawafundisha,

au acheni samaki wa baharini wawape taarifa.

9 Ni nani miongoni mwa hawa wote asiyejua

kwamba mkono waBwanandio uliofanya hili?

10 Mkononi mwake kuna uhai wa kila kiumbe,

na pumzi ya wanadamu wote.

11 Je, sikio haliyajaribu maneno

kama vile ulimi uonjavyo chakula?

12 Je, hekima haipatikani katikati ya wazee?

Je, maisha marefu hayaleti ufahamu?

13 “Hekima na nguvu ni vya Mungu;

shauri na ufahamu ni vyake yeye.

14 Kile anachokibomoa hakiwezi kujengeka tena;

mtu aliyefungiwa naye hawezi kufunguliwa.

15 Akizuia maji, huwa pana ukame;

akiyaachia maji, huharibu nchi.

16 Kwake kuna nguvu na ushindi;

adanganywaye na adanganyaye, wote wawili ni wake.

17 Yeye huwaondoa washauri wakiwa wametekwa nyara,

naye huwapumbaza wanaotoa maamuzi.

18 Huondoa pingu zilizofungwa na wafalme,

na kuwafunga mishipi ya kiunoni.

19 Huwaondoa makuhani wakiwa wametekwa nyara,

na kuwaangusha waliojiimarisha muda mrefu.

20 Hunyamazisha midomo ya washauri wanaoaminika,

na kuondoa busara ya wazee.

21 Huwamwagia dharau wanaoheshimika,

na kuwavua silaha wenye nguvu.

22 Hufunua mambo ya ndani ya gizani,

na kuyaleta nuruni yale yaliyositirika sana.

23 Huyafanya mataifa yatukuke na kuyaangamiza;

hufanya mataifa kuwa makubwa, naye huyatawanya.

24 Huwaondolea viongozi wa nchi akili zao;

huwapeleka watangetange nyikani pasipo na njia.

25 Hupapasa gizani pasipokuwa na mwanga;

huwafanya wapepesuke kama walevi.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/12-1a7d2e9f5e33539ac126e3c024589272.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 13

1 “Macho yangu yameona hili lote,

masikio yangu yamesikia na kulielewa.

2 Hayo mnayoyajua mimi pia ninayajua;

mimi si mtu duni kuliko ninyi.

3 Lakini ninayo shauku ya kuzungumza na Mwenyezi

na kuhojiana shauri langu na Mungu.

4 Ninyi, hata hivyo, hunipakaza uongo;

ninyi ni matabibu wasiofaa kitu, ninyi nyote!

5 Laiti wote mngenyamaza kimya!

Kwa kuwa kwenu hilo lingekuwa hekima.

6 Sikieni sasa hoja yangu;

sikilizeni kusihi kwangu.

7 Je, mtazungumza kwa uovu kwa niaba ya Mungu?

Je, mtazungumza kwa udanganyifu kwa niaba yake?

8 Mtamwonyesha upendeleo?

Mtamtetea Mungu kwenye mashtaka yake?

9 Je, ingekuwa vyema Mungu akiwahoji ninyi?

Je, mngeweza kumdanganya kama ambavyo mngeweza kuwadanganya wanadamu?

10 Hakika angewakemea

kama mkiwapendelea watu kwa siri.

11 Je, huo ukuu wake haungewatisha ninyi?

Je, hofu yake isingewaangukia ninyi?

12 Maneno yenu ni mithali za majivu;

utetezi wenu ni ngome za udongo wa mfinyanzi.

13 “Nyamazeni kimya nipate kusema;

kisha na yanipate yatakayonipata.

14 Kwa nini nijiweke mwenyewe kwenye hatari

na kuyaweka maisha yangu mikononi mwangu?

15 Ingawa ataniua, bado nitamtumaini;

hakika nitazitetea njia zangu mbele zake.

16 Naam, hili litanigeukia kuwa wokovu wangu,

kwa maana hakuna mtu asiyemcha Mungu

atakayethubutu kuja mbele yake!

17 Sikilizeni maneno yangu kwa makini;

nayo masikio yenu yaingize kile nisemacho.

18 Sasa kwamba nimekwisha kutayarisha mambo yangu,

ninajua mimi nitahesabiwa kuwa na haki.

19 Je, kuna yeyote anayeweza kuleta mashtaka dhidi yangu?

Kama ndivyo, nitanyamaza kimya na nife.

20 “Ee Mungu, unijalie tu mimi haya mambo mawili,

nami sitajificha uso wako:

21 Ondoa mkono wako uwe mbali nami,

nawe uache kuniogofya kwa hofu zako kuu.

22 Niite kwenye shauri nami nitajibu,

au niache niseme, nawe upate kujibu.

23 Ni makosa na dhambi ngapi nilizotenda?

Nionyeshe kosa langu na dhambi yangu.

24 Kwa nini kuuficha uso wako

na kunihesabu mimi kuwa adui yako?

25 Je, utaliadhibu jani lipeperushwalo na upepo?

Je, utayasaka makapi makavu?

26 Kwa kuwa unaandika mambo machungu dhidi yangu

na kunifanya nizirithi dhambi za ujana wangu.

27 Umeifunga miguu yangu kwenye pingu.

Unazichunga kwa makini njia zangu zote

kwa kutia alama kwenye nyayo za miguu yangu.

28 “Hivyo mwanadamu huangamia kama kitu kilichooza,

kama vazi lililoliwa na nondo.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/13-d28d26816e8ade5518d2bc6f04ca3c2f.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 14

1 “Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke

siku zake ni chache nazo zimejaa taabu.

2 Huchanua kama ua kisha hunyauka;

huwa kama kivuli kipitacho upesi, wala hadumu.

3 Je, unamwekea jicho lako mtu kama huyo?

Je, utamleta mbele yako katika hukumu?

4 Ni nani awezaye kutoa kitu safi kutoka kitu najisi?

Hakuna awezaye!

5 Siku za mwanadamu zimewekewa mpaka;

umekwisha kutangaza idadi ya miezi yake

na kuweka mpaka ambao hawezi kuuvuka.

6 Hivyo angalia mbali umwache,

hadi awe amekamilisha muda wake

kama mtu aliyeajiriwa.

7 “Kwa maana lipo tumaini kwa mti;

kama ukikatwa utachipuka tena,

nayo machipukizi yake mapya hayatakoma.

8 Mizizi yake yaweza kuchakaa ardhini

na kisiki chake kufa udongoni,

9 lakini kwa kupata dalili ya maji utachipua

na kutoa machipukizi kama mche.

10 Lakini mwanadamu hufa, na huo ndio mwisho wake;

hutoa pumzi ya mwisho, naye hayuko tena!

11 Kama vile maji yatowekavyo katika bahari,

au mkondo wa mto ukaushwavyo na kuwa mkavu,

12 ndivyo mwanadamu alalavyo chini asiamke;

hadi mbingu zitakapokuwa hazipo tena,

wanadamu hawataamka au kuamshwa

kutoka kwenye usingizi wao.

13 “Laiti kama ungenificha kaburini,

na kunisitiri hadi hasira yako ipite!

Laiti ungeniwekea wakati,

na kisha ukanikumbuka!

14 Je, kama mtu akifa, aweza kuishi tena?

Siku zote za kazi zangu ngumu

nitangojea kufanywa upya kwangu.

15 Utaniita nami nitakuitika;

utakionea shauku kiumbe ambacho mikono yako ilikiumba.

16 Hakika ndipo utakapozihesabu hatua zangu,

lakini hutazifuatia dhambi zangu.

17 Makosa yangu yatafungiwa kwa lakiri kwenye mfuko,

nawe utazifunika dhambi zangu.

18 “Lakini kama mlima umomonyokavyo na kufikichika

na kama vile mwamba uondolewavyo mahali pake,

19 kama maji yamalizavyo mawe,

na mafuriko yachukuavyo udongo,

ndivyo unavyoharibu tegemeo la mwanadamu.

20 Humshinda mara moja kwa daima, naye hutoweka;

waibadilisha sura yake na kumwondoa.

21 Kama wanawe wakipewa heshima, yeye hafahamu;

kama wakidharauliwa, yeye haoni.

22 Yeye hasikii kingine isipokuwa maumivu ya mwili wake mwenyewe,

naye huomboleza kwa ajili yake mwenyewe.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/14-f497accccff8d70b94db306801bbf2f5.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 15

Elifazi Anaongea: Ayubu Anadhoofisha Imani

1 Kisha Elifazi Mtemani akajibu:

2 “Je, mtu mwenye hekima hujibu kwa mawazo matupu,

au kujaza tumbo lake kwa upepo wenye joto wa mashariki?

3 Je, aweza kubishana juu ya maneno yasiyofaa,

kwa hotuba zisizo na maana?

4 Lakini unadhoofisha hata uchaji wa Mungu

na kuzuia ibada mbele za Mungu.

5 Dhambi yako inasukuma kinywa chako,

nawe umechagua ulimi wa hila.

6 Kinywa chako mwenyewe kinakuhukumu, wala si changu;

midomo yako mwenyewe inashuhudia dhidi yako.

7 “Je, wewe ni mtu wa kwanza kuzaliwa?

Ulizaliwa kabla ya vilima?

8 Je, wewe husikiliza mashauri ya siri ya Mungu?

Je, wewe unaizuia hekima iwe yako mwenyewe?

9 Wewe unajua kitu gani tusichokijua sisi?

Unafahamu kitu gani tusichokifahamu sisi?

10 Wale wenye mvi na wazee wako upande wetu,

watu ambao ni wazee hata kuliko baba yako.

11 Je, faraja za Mungu hazikutoshi,

au maneno yaliyosemwa kwako kwa upole si kitu?

12 Kwa nini moyo wako unakudanganya,

na kwa nini macho yako yanangʼaa,

13 ili kwamba upate kutoa hasira yako dhidi ya Mungu,

na kumwaga maneno kama hayo kutoka kinywani mwako?

14 “Mwanadamu ni kitu gani, hata aweze kuwa safi,

au yeye aliyezaliwa na mwanamke, hata aweze kuwa mwadilifu?

15 Kama Mungu hawaamini watakatifu wake,

kama hata mbingu zenyewe si safi machoni pake,

16 sembuse mwanadamu ambaye ni mwovu na mpotovu,

ambaye hunywa uovu kama anywavyo maji!

17 “Nisikilize mimi nami nitakueleza,

acha nikuambie yale niliyoyaona,

18 ambayo watu wenye hekima wameyanena,

bila kuficha lolote walilopokea toka kwa baba zao

19 (wakati ambao wao peke yao ndio walipewa nchi,

hakuna mgeni aliyepita miongoni mwao):

20 Mtu mwovu siku zake zote hupata mateso,

miaka yote aliwekewa mkorofi.

21 Sauti za kutisha hujaa masikioni mwake;

katika kufanikiwa kwake, wanyangʼanyi humshambulia.

22 Hukata tamaa kuokoka gizani;

amewekwa kwa ajili ya upanga.

23 Hutangatanga, akitafuta chakula;

anajua kwamba siku ya giza iko karibu.

24 Taabu na maumivu makuu vinamtia hofu;

humshinda kama mfalme aliye tayari kwa vita,

25 kwa sababu amemkunjia Mungu ngumi yake

na kujigamba dhidi ya Mwenyezi,

26 kwa kiburi akishambulia dhidi ya Mungu

akiwa na ngao nene, iliyo imara.

27 “Ingawa uso wake umefunikwa na mafuta kwa unene

na kiuno chake kimevimba kwa kunenepa,

28 ataishi katika miji ya magofu,

na katika nyumba ambazo haziishi mwanadamu yeyote,

nyumba zinazokuwa vifusi.

29 Hatatajirika tena, nao utajiri wake hautadumu,

wala mali zake hazitakuwa nyingi juu ya nchi.

30 Hatatoka gizani;

mwali wa moto utanyausha machipukizi yake,

nayo pumzi ya kinywa cha Mungu itamwondolea mbali.

31 Asijidanganye mwenyewe kutumainia ubatili,

kwa kuwa hatapata malipo yoyote.

32 Atakuwa amelipwa kikamilifu kabla ya wakati wake,

nayo matawi yake hayatastawi.

33 Atafanana na mzabibu uliopukutishwa matunda yake kabla hayajaiva,

kama mzeituni unaodondosha maua yake.

34 Kwa kuwa jamii ya wasiomcha Mungu watakuwa tasa,

nao moto utateketeza hema za wale wanaopenda rushwa.

35 Hutunga mimba ya madhara na kuzaa uovu;

matumbo yao huumba udanganyifu.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/15-aef311f80c8e5b773ddf423a5371ae7c.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 16

Ayubu Anathibitisha Tena Hali Yake Ya Kutokuwa Na Hatia

1 Kisha Ayubu akajibu:

2 “Nimepata kusikia mambo mengi kama haya,

nanyi nyote ni wafariji wenye kutaabisha!

3 Je, maneno yenu mengi yasiyo na maana hayana mwisho?

Mna nini hata mwendelee kushindana kwa maneno?

4 Mimi pia ningeweza kuzungumza kama ninyi,

kama mngekuwa katika hali yangu;

ningeweza kutoa hotuba nzuri dhidi yenu,

na kuwatikisia ninyi kichwa changu.

5 Lakini kinywa changu kingewatia moyo;

faraja kutoka midomoni mwangu, ingewaletea nafuu.

6 “Lakini kama nikisema, maumivu yangu bado hayatulizwi;

nami kama nikijizuia, wala hayaondoki.

7 Ee Mungu, hakika umenichakaza;

umewaangamiza kabisa watu wa nyumbani mwangu wote.

8 Umenikunjakunja, nalo limekuwa ushahidi;

nako kukonda kwangu kumeongezeka sana na kushuhudia dhidi yangu.

9 Mungu amenishambulia na kunirarua katika hasira yake,

na kunisagia meno yake;

adui yangu hunikazia macho yake makali.

10 Watu wamenifumbulia vinywa vyao kunidhihaki;

hunipiga shavuni mwangu kwa dharau,

na kuungana pamoja dhidi yangu.

11 Mungu amenigeuzia kwa watu wabaya,

na kunitupa katika makucha ya waovu.

12 Mambo yote yalikuwa mazuri, lakini alinivunjavunja;

amenikamata shingo na kuniponda.

Amenifanya mimi kuwa shabaha yake;

13 wapiga upinde wake wananizunguka.

Bila huruma, huchoma figo zangu,

na kuimwaga nyongo yangu juu ya nchi.

14 Huniponda tena na tena;

hunishambulia kama shujaa wa vita.

15 “Nimejishonea nguo ya gunia juu ya mwili wangu

nami nimekizika kipaji cha uso wangu kwenye vumbi.

16 Uso wangu umekuwa mwekundu kwa kulia,

macho yangu yamepigwa na giza kuu.

17 Hata hivyo mikono yangu haijafanya jeuri,

na maombi yangu ni safi.

18 “Ee nchi, usiifunike damu yangu,

nacho kilio changu kisinyamazishwe kamwe.

19 Hata sasa shahidi wangu yuko mbinguni;

wakili wangu yuko juu.

20 Mwombezi wangu ni rafiki yangu

macho yangu yamwagapo machozi kwa Mungu;

21 kwa niaba ya mtu anamsihi Mungu

kama mtu anavyosihi kwa ajili ya rafiki yake.

22 “Ni miaka michache tu itapita

kabla sijaenda safari ambayo sitarudi.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/16-7cf39d0e2a2171affc3179a7712bb812.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 17

1 Moyo wangu umevunjika,

siku zangu zimefupishwa,

kaburi linaningojea.

2 Hakika wenye mizaha wamenizunguka;

macho yangu yamebaki kutazama uadui wao.

Ayubu Anaomba Msaada

3 “Ee Mungu, nipe dhamana unayodai.

Ni nani mwingine atakayeweka dhamana kwa ajili yangu?

4 Umezifunga akili zao zisipate ufahamu,

kwa hiyo hutawaacha wapate ushindi.

5 Kama mtu akiwashutumu rafiki zake ili apate ujira,

macho ya watoto wake yatashindwa kuona.

6 “Mungu amenifanya kitu cha dhihaka kwa kila mtu,

mtu ambaye watu humtemea mate usoni.

7 Macho yangu yamefifia kwa ajili ya majonzi;

umbile langu lote ni kama kivuli.

8 Watu wanyofu wanatishwa na hili;

watu wasio na hatia wanasimama dhidi ya wasiomcha Mungu.

9 Hata hivyo, waadilifu watazishika njia zao,

nao wale wenye mikono safi wataendelea kupata nguvu.

10 “Lakini ninyi njooni, ninyi nyote, jaribuni tena!

Sitampata mtu mwenye hekima miongoni mwenu.

11 Siku zangu zimepita, mipango yangu imevunjika,

vivyo hivyo shauku za moyo wangu.

12 Watu hawa hufanya usiku kuwa mchana,

kwenye giza wao husema, ‘Mwanga u karibu.’

13 Kama nyumba pekee ninayoitarajia ni kaburi,

kama nikikitandika kitanda changu gizani,

14 kama nikiuambia uharibifu, ‘Wewe u baba yangu,’

na kuliambia buu, ‘Wewe u mama yangu’ au ‘Dada yangu,’

15 liko wapi basi tarajio langu?

Ni nani awezaye kuona tarajio lolote kwa ajili yangu?

16 Je, litashuka chini hadi kwenye malango ya mauti?

Je, tutashuka pamoja mavumbini?”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/17-4a8d58413b7361fd4ec108a991e584e0.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 18

Bildadi Anasema: Mungu Huwaadhibu Waovu

1 Bildadi Mshuhi akajibu:

2 “Je, ni lini utafika mwisho wa maneno haya?

Uwe mwenye busara, nasi ndipo tutakapoweza kuongea.

3 Kwa nini sisi tunafikiriwa kama wanyama,

na kuonekana wajinga machoni pako?

4 Wewe unayejirarua mwenyewe vipande vipande

katika hasira yako,

je, dunia iachwe kwa ajili yako wewe?

Au ni lazima miamba iondolewe mahali pake?

5 “Taa ya mwovu imezimwa,

nao mwali wa moto wake umezimika.

6 Mwanga hemani mwake umekuwa giza;

taa iliyo karibu naye imezimika.

7 Nguvu za hatua zake zimedhoofishwa;

shauri lake baya litamwangusha.

8 Miguu yake imemsukumia kwenye wavu,

naye anatangatanga kwenye matundu ya wavu.

9 Tanzi litamkamata kwenye kisigino;

mtego utamshikilia kwa nguvu.

10 Kitanzi kimefichwa ardhini kwa ajili yake;

mtego uko kwenye njia yake.

11 Vitisho vimemtia hofu kila upande,

na adui zake humwandama kila hatua.

12 Janga linamwonea shauku;

maafa yako tayari kwa ajili yake aangukapo.

13 Nayo yatakula sehemu ya ngozi yake;

mzaliwa wa kwanza wa mauti atakula maungo yake.

14 Atangʼolewa kutoka usalama wa hema lake,

na kupelekwa kwa mfalme wa vitisho.

15 Moto utakaa katika hema lake;

moto wa kiberiti utamwagwa juu ya makao yake.

16 Mizizi yake chini itakauka

na matawi yake juu yatanyauka.

17 Kumbukumbu lake litatoweka katika dunia,

wala hatakuwa na jina katika nchi.

18 Ameondolewa nuruni na kusukumiwa gizani,

naye amefukuzwa mbali atoke duniani.

19 Hana mtoto wala mzao miongoni mwa watu wake,

wala aliyenusurika mahali alipoishi.

20 Watu wa magharibi watashangaa yaliyompata;

watu wa mashariki watapatwa na hofu.

21 Hakika ndivyo yalivyo makao ya mtu mwovu;

ndivyo palivyo mahali pake mtu asiyemjua Mungu.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/18-d89e2a1e195c1b0db89cbba5f1372856.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 19

Ayubu Anajibu: Najua Mkombozi Wangu Yu Hai

1 Ndipo Ayubu akajibu:

2 “Je, mtaendelea kunitesa mpaka lini,

na kuniponda kwa maneno yenu?

3 Mara kumi hizi mmenishutumu;

bila aibu mnanishambulia.

4 Kama ni kweli nimepotoka,

kosa langu ninabaki kuhusika nalo mwenyewe.

5 Kama kweli mngejitukuza wenyewe juu yangu,

na kutumia unyonge wangu dhidi yangu,

6 basi jueni kuwa Mungu amenitendea yaliyo mabaya,

naye amekokota wavu wake kunizunguka.

7 “Ingawa ninalia, ‘Nimetendewa mabaya!’ sipati jibu;

ingawa ninaomba msaada, hakuna haki.

8 Yeye ameizuia njia yangu hivyo siwezi kupita;

ameyafunika mapito yangu na giza.

9 Amenivua heshima yangu,

na kuniondolea taji kichwani pangu.

10 Amenibomoa kila upande hadi nimeisha;

amelingʼoa tegemeo langu kama mti.

11 Hasira yake imewaka juu yangu;

amenihesabu kuwa miongoni mwa adui zake.

12 Majeshi yake yananisogelea kwa nguvu;

yamenizingira,

yamepiga kambi kulizunguka hema langu.

13 “Amewatenga ndugu zangu mbali nami;

wale tunaojuana nao wamefarakana nami kabisa.

14 Watu wa jamaa yangu wamekwenda mbali;

rafiki zangu wamenisahau.

15 Wageni wangu na watumishi wangu wa kike wananiona kama mgeni;

wananitazama kama mgeni.

16 Namwita mtumishi wangu, wala haitiki,

ingawa namwomba kwa kinywa changu mwenyewe.

17 Pumzi ya kinywa changu ni kinyaa kwa mke wangu;

nimekuwa chukizo mno kwa ndugu zangu mwenyewe.

18 Hata watoto wadogo hunidhihaki;

ninapojitokeza, hunifanyia mzaha.

19 Rafiki zangu wa moyoni wote wananichukia kabisa;

wale niwapendao wamekuwa kinyume nami.

20 Mimi nimebaki mifupa na ngozi tu;

nimeponea nikiwa karibu kufa.

21 “Nihurumieni, rafiki zangu, kuweni na huruma,

kwa kuwa mkono wa Mungu umenipiga.

22 Kwa nini mnanifuatia kama Mungu afanyavyo?

Hamtosheki kamwe na mwili wangu?

23 “Laiti maneno yangu yangewekwa kwenye kumbukumbu,

laiti kwamba yangeandikwa kwenye kitabu,

24 kwamba yangechorwa kwenye risasi kwa kifaa cha chuma,

au kuyachonga juu ya mwamba milele!

25 Ninajua kwamba Mkomboziwangu yu hai,

naye kwamba mwishoni atasimama juu ya nchi.

26 Nami baada ya ngozi yangu kuharibiwa,

bado nikiwa na mwili huu nitamwona Mungu;

27 mimi nitamwona kwa macho yangu mwenyewe:

mimi, wala si mwingine.

Tazama jinsi moyo wangu unavyomtamani sana!

28 “Kama mkisema, ‘Tazama tutakavyomwinda,

maadamu mzizi wa tatizo uko ndani yake,’

29 ninyi wenyewe uogopeni upanga,

kwa kuwa ghadhabu italeta adhabu kwa upanga,

nanyi ndipo mtakapojua kwamba kuna hukumu.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/19-4d145c9095576af9b13d48707c468451.mp3?version_id=1627—