Categories
Amosi

Amosi Utangulizi

Utangulizi

Amosi maana yake ni “Mchukua mzigo.” Yeye alikuwa mchunga wanyama na pia mtunza mikuyu kutoka Tekoa, kijiji kilicho karibu na Bethlehemu na kilomita 16 kutoka Yerusalemu. Mungu alimwita kuwa nabii katika Ufalme wa Kaskazini (Israeli). Wakati huo ufalme ulikuwa na utajiri mwingi. Ujumbe wa Amosi unaonyesha kwamba wakati huo ulikuwa wa mafanikio mengi kiuchumi na kisiasa katika Israeli kuliko nyakati zingine zote, isipokuwa zile za enzi ya Solomoni.

Amosi aliwalaumu watu vikali kwa kuliacha neno la Mungu, kukosa haki katika jamii na kwa maskini, kuwa wakatili, kutawaliwa na ubinafsi, na kufuata anasa na kuabudu sanamu. Uwajibikaji wa Israeli ulikuwa mkubwa kuliko wa mataifa mengine yaliyowazunguka kwa sababu walikuwa wamepewa upendeleo mkubwa zaidi. Katika maono matano mfululizo, Amosi aliona kuwa siku ya maangamizi ilikuwa karibu. Aliwaonya watu kwamba iliwapasa kujiandaa kukutana na Mungu. Kwa wale waliokuwa wanampenda Mungu, Amosi alikuwa na neno la kuwapa matumaini. Siku ilikuwa inakuja ambapo ufalme wa Daudi ungekomeshwa ghafula lakini wacha Mungu wangeishi salama.

Mwandishi

Amosi.

Kusudi

Kutangaza hukumu ya Mungu dhidi ya Israeli kwa kuishi katika hali ya kutosheka na kuridhika, kuabudu sanamu na kuwadhulumu maskini.

Mahali

Samaria, Betheli, Gilgali.

Tarehe

760–750 K.K.

Wahusika Wakuu

Amosi, Amazia, na Yeroboamu wa Pili.

Wazo Kuu

Amosi aliwashutumu watu vikali kwa kuwagandamiza maskini. Kutokana na haya, alitangaza hukumu ya Mungu dhidi yao kwa sababu walikuwa wamemwacha Mungu.

Mambo Muhimu

Amosi ametumia mifano ya maneno ya kusisimua kutokana na uzoefu wake wa ukulima na uchungaji wa wanyama: Simba angurumaye, kipande cha kondoo kilichopokonywa kinywani mwa simba, ngʼombe walioshiba, kapu la matunda, n.k.

Mgawanyo

Hukumu kwa majirani wa Israeli (

1:1–2:5

)

Hukumu kwa Israeli (

2:6-16

)

Uovu wa Israeli (

3:1–6:14

)

Maono matano (

7:1–9:10

)

Matengenezo ya Israeli (

9:11-15

).

Categories
Amosi

Amosi 1

1 Maneno ya Amosi, mmoja wa wachunga wanyama wa Tekoa: yale aliyoyaona kuhusu Israeli miaka miwili kabla ya tetemeko la ardhi, wakati Uzia alikuwa mfalme wa Yuda, na Yeroboamu mwana wa Yehoashi alikuwa mfalme wa Israeli.

2 Alisema:

“Bwanaananguruma toka Sayuni,

pia ananguruma kutoka Yerusalemu;

malisho ya wachunga wanyama yanakauka,

kilele cha Karmeli kinanyauka.”

Hukumu Juu Ya Majirani Wa Israeli

3 Hili ndilo asemaloBwana:

“Kwa dhambi tatu za Dameski,

hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu.

Kwa sababu aliipura Gileadi

kwa vyombo vya chuma vyenye meno.

4 Nitatuma moto juu ya nyumba ya Hazaeli

ambao utateketeza ngome za Ben-Hadadi.

5 Nitalivunja lango la Dameski;

nitamwangamiza mfalme aliyeko katika Bonde la Aveni,

na yeye ambaye anaishika fimbo ya utawala katika Beth-Edeni.

Watu wote wa Aramu watakwenda uhamishoni huko Kiri,”

asemaBwana.

6 Hili ndilo asemaloBwana:

“Kwa dhambi tatu za Gaza,

hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu.

Kwa sababu walichukua mateka jumuiya nzima

na kuwauza kwa Edomu,

7 nitatuma moto juu ya kuta za Gaza

ambao utateketeza ngome zake.

8 Nitamwangamiza mfalme wa Ashdodi

na yeye aishikaye fimbo ya utawala katika Ashkeloni.

Nitaugeuza mkono wangu dhidi ya Ekroni,

hadi Mfilisti wa mwisho atakapokufa,”

asemaBwanaMwenyezi.

9 Hili ndilo asemaloBwana:

“Kwa dhambi tatu za Tiro,

hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu.

Kwa sababu ameuza jumuiya nzima ya mateka kwa Edomu,

na kutokujali mapatano ya undugu,

10 Nitatuma moto kwenye kuta za Tiro

ambao utateketeza ngome zake.”

11 Hili ndiloBwanaasemalo:

“Kwa dhambi tatu za Edomu,

hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu.

Kwa sababu alimfuatia ndugu yake kwa upanga,

alikataa kuonyesha huruma yoyote,

kwa sababu hasira yake kali iliendelea kupanda wakati wote

na ghadhabu iliwaka bila kuzuiliwa.

12 Nitatuma moto juu ya Temani

ambao utateketeza ngome za Bosra.”

13 Hili ndilo asemaloBwana:

“Kwa dhambi tatu za Amoni,

hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu.

Kwa sababu aliwatumbua wanawake wajawazito wa Gileadi

ili kuongeza mipaka yake.

14 Nitatuma moto kwenye kuta za Raba

ambao utateketeza ngome zake

katikati ya vilio vya vita katika siku ya mapigano,

katikati ya upepo mkali katika siku ya dhoruba.

15 Mfalme wake atakwenda uhamishoni,

yeye pamoja na maafisa wake,”

asemaBwana.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/AMO/1-bd20a9f8d7c7ee7f62bebeb1022c5061.mp3?version_id=1627—

Categories
Amosi

Amosi 2

1 Hili ndilo asemaloBwana:

“Kwa dhambi tatu za Moabu,

hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu.

Kwa sababu alichoma mifupa ya mfalme wa Edomu,

ikawa kama chokaa.

2 Nitatuma moto juu ya Moabu

ambao utateketeza ngome za Keriothi.

Moabu ataanguka kwa ghasia kubwa

katikati ya vilio vya vita na mlio wa tarumbeta.

3 Nitamwangamiza mtawala wake

na kuwaua maafisa wake wote pamoja naye,”

asemaBwana.

4 Hili ndilo asemaloBwana:

“Kwa dhambi tatu za Yuda,

hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu.

Kwa sababu wameikataa sheria yaBwana

na hawakuzishika amri zake,

kwa sababu wamepotoshwa na miungu ya uongo,

miungu ambayo babu zao waliifuata.

5 Nitatuma moto juu ya Yuda

ambao utateketeza ngome za Yerusalemu.”

Hukumu Juu Ya Israeli

6 Hili ndilo asemaloBwana:

“Kwa dhambi tatu za Israeli,

hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu.

Wanawauza wenye haki kwa fedha,

na maskini kwa jozi ya viatu.

7 Wanakanyaga juu ya vichwa vya maskini,

kama vile juu ya mavumbi ya nchi,

na kukataa haki kwa walioonewa.

Baba na mwanawe hushiriki msichana mmoja,

kwa hivyo hulinajisi Jina langu takatifu.

8 Watu hulala kando ya kila madhabahu

juu ya nguo zilizowekwa rehani.

Katika nyumba ya mungu wao hunywa mvinyo

ulionunuliwa kwa fedha walizotozwa watu.

9 “Nilimwangamiza Mwamori mbele yao,

ingawa alikuwa mrefu kama mierezi,

na mwenye nguvu kama mialoni.

Niliyaangamiza matunda yake juu

na mizizi yake chini.

10 “Niliwapandisha toka Misri,

na nikawaongoza miaka arobaini jangwani

niwape nchi ya Waamori.

11 Pia niliinua manabii kutoka miongoni mwa wana wenu

na Wanadhiri kutoka miongoni mwa vijana wenu.

Je, hii si kweli, enyi watu wa Israeli?”

asemaBwana.

12 “Lakini mliwafanya Wanadhiri kunywa mvinyo

na kuwaamuru manabii wasitoe unabii.

13 “Sasa basi, nitawaponda

kama gari lipondavyo wakati limejazwa nafaka.

14 Mkimbiaji hodari hatanusurika,

wenye nguvu wataishiwa nguvu zao,

na shujaa hataweza kuokoa maisha yake.

15 Mpiga upinde atakimbia,

askari wapiga mbio hawataweza kutoroka,

na mpanda farasi hataokoa maisha yake.

16 Hata askari walio mashujaa sana

siku hiyo watakimbia uchi,”

asemaBwana.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/AMO/2-6a9e6bcc6ff37c87f934430ef4f642f7.mp3?version_id=1627—

Categories
Amosi

Amosi 3

Mashahidi Waitwa Dhidi Ya Israeli

1 Sikilizeni neno hili alilosemaBwanadhidi yenu, enyi watu wa Israeli, dhidi ya jamaa nzima niliowapandisha toka Misri:

2 “Ni ninyi tu niliowachagua

kati ya jamaa zote za dunia;

kwa hiyo nitawaadhibu

kwa ajili ya dhambi zenu zote.”

3 Je, watu wawili hutembea pamoja

wasipokubaliana kufanya hivyo?

4 Je, simba hunguruma katika kichaka

wakati hana mawindo?

Aweza kuvuma katika pango

wakati ambao hajakamata chochote?

5 Je, ndege aweza kuanguka kwenye mtego ulio ardhini

ambapo hajategewa chambo?

Je, mtego unaweza kufyatuka toka ardhini

wakati ambapo hakuna chochote cha kunasa?

6 Je, tarumbeta inapopigwa mjini kujulisha hatari,

watu hawatetemeki?

Mji upatwapo na maafa,

je, siBwanaamesababisha?

7 HakikaBwanaMwenyezi hatafanya neno lolote

bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.

8 Simba amenguruma:

je, ni nani ambaye hataogopa?

BwanaMwenyezi ametamka:

je, ni nani awezaye kukosa kutoa unabii?

9 Tangazeni katika ngome za Ashdodi

na katika ngome za Misri:

“Kusanyikeni juu ya milima ya Samaria;

angalieni wingi wa wasiwasi ulio ndani yake,

na uonevu ulio miongoni mwa watu wake.”

10 Bwanaasema: “Hawajui kutenda lililo jema,

wale ambao hujilundikia nyara

na vitu vilivyotekwa katika ngome zao.”

11 Kwa hiyo hili ndilo asemaloBwanaMwenyezi:

“Adui ataizingira nchi;

ataangusha chini ngome zenu

na kuteka nyara maboma yenu.”

12 Hili ndilo asemaloBwana:

“Kama vile mchungaji aokoavyo kinywani mwa simba

vipande viwili tu vya mfupa wa mguu

au kipande cha sikio,

hivyo ndivyo Waisraeli watakavyookolewa,

wale wakaao Samaria

kwenye kingo za vitanda vyao,

na katika Dameski

kwenye viti vyao vya fahari.”

13 “Sikia hili na ushuhudie dhidi ya nyumba ya Yakobo,” asema Bwana,BwanaMungu Mwenye Nguvu Zote.

14 “Siku nitakapomwadhibu Israeli kwa sababu ya dhambi zake,

nitaharibu madhabahu za Betheli;

pembe za madhabahu zitakatiliwa mbali

na kuanguka chini.

15 Nitabomoa nyumba ya wakati wa masika,

pamoja na nyumba ya wakati wa kiangazi;

nyumba zilizonakshiwa kwa pembe za ndovu

na majumba makubwa ya fahari yatabomolewa,”

asemaBwana.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/AMO/3-ada4971a53a7543228046864d9aa670e.mp3?version_id=1627—

Categories
Amosi

Amosi 4

Israeli Hajarudi Kwa Mungu

1 Sikilizeni neno hili, ninyi ngʼombe wa Bashani

mlioko juu ya Mlima Samaria,

ninyi wanawake mnaowaonea maskini,

na kuwagandamiza wahitaji,

na kuwaambia wanaume wenu,

“Tuleteeni vinywaji!”

2 BwanaMwenyezi ameapa kwa utakatifu wake:

“Hakika wakati utakuja

mtakapochukuliwa na kulabu,

na wanaosalia kwa ndoana za samaki.

3 Nanyi mtakwenda moja kwa moja

kupitia mahali palipobomolewa kwenye ukuta,

nanyi mtatupwa nje kuelekea Harmoni,”

asemaBwana.

4 “Nendeni Betheli mkatende dhambi;

nendeni Gilgali mkazidi kutenda dhambi.

Leteni dhabihu zenu kila asubuhi,

zaka zenu kila mwaka wa tatu.

5 Mchome mkate uliotiwa chachu kama sadaka ya shukrani,

jisifuni kuhusu sadaka zenu za hiari:

jigambeni kwa ajili ya sadaka hizo, enyi Waisraeli,

kwa kuwa hili ndilo mnalopenda kulitenda,”

asemaBwanaMwenyezi.

6 “Niliwapa njaa kwenye kila mji,

na ukosefu wa chakula katika kila mji,

hata hivyo bado hamjanirudia mimi,”

asemaBwana.

7 “Pia niliwazuilia ninyi mvua miezi mitatu

kabla ya kufikia mavuno.

Nilinyesha mvua kwenye mji mmoja,

lakini niliizuia mvua isinyeshe mji mwingine.

Shamba moja lilipata mvua,

na lingine halikupata, nalo likakauka.

8 Watu walitangatanga mji hata mji kutafuta maji,

lakini hawakupata ya kuwatosha kunywa,

hata hivyo hamjanirudia mimi,”

asemaBwana.

9 “Mara nyingi nilizipiga bustani zenu na mashamba ya mizabibu,

niliyapiga kwa kutu na ukungu.

Nzige walitafuna tini zenu na miti ya mizeituni,

hata hivyo hamjanirudia mimi,”

asemaBwana.

10 “Niliwapelekea tauni miongoni mwenu

kama nilivyofanya kule Misri.

Niliwaua vijana wenu wa kiume kwa upanga,

niliwachukua farasi wenu.

Nilijaza pua zenu kwa uvundo kutoka kwenye kambi zenu,

hata hivyo hamjanirudia mimi,”

asemaBwana.

11 “Niliwaangamiza baadhi yenu kama

nilivyoangamiza Sodoma na Gomora.

Mlikuwa kama kijiti kiwakacho kilichonyakuliwa motoni,

hata hivyo hamjanirudia,”

asemaBwana.

12 “Kwa hiyo hili ndilo nitakalowafanyia, Israeli,

na kwa sababu nitawafanyia hili,

jiandaeni kukutana na Mungu wenu, ee Israeli.”

13 Yeye ambaye hufanya milima, anaumba upepo,

na kufunua mawazo yake kwa mwanadamu,

yeye ageuzaye asubuhi kuwa giza,

na kukanyaga mahali pa juu pa nchi:

BwanaMungu Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/AMO/4-eae60c5bcb1e245043031d20a6d46ed3.mp3?version_id=1627—

Categories
Amosi

Amosi 5

Maombolezo Na Wito Wa Toba

1 Sikia neno hili, ee nyumba ya Israeli, ombolezo hili ninalifanya kuwahusu ninyi:

2 “Bikira Israeli ameanguka,

kamwe hatainuka tena,

ameachwa pweke katika nchi yake,

hakuna yeyote wa kumwinua.”

3 Hili ndiloBwanaMwenyezi asemalo:

“Wakati mmoja wa miji yako utakapopeleka watu elfu moja vitani kwa ajili ya Israeli,

mia moja tu watarudi;

wakati mji utakapopeleka mia moja,

kumi tu ndio watarudi hai.”

4 Hili ndiloBwanaasemalo kwa nyumba ya Israeli:

“Nitafuteni mpate kuishi;

5 msitafute Betheli,

msiende Gilgali,

msisafiri kwenda Beer-Sheba.

Kwa maana kwa hakika Gilgali itakwenda uhamishoni,

na Betheli itafanywa kuwa si kitu.”

6 MtafuteniBwanampate kuishi,

au atafagia nyumba ya Yosefu kama moto;

utawateketeza, nayo Betheli

haitakuwa na yeyote wa kuuzima.

7 Ninyi ambao mnageuza haki kuwa uchungu

na kuiangusha haki chini

8 (yeye ambaye alifanya Kilimia na Orioni,

ambaye hugeuza giza kuwa mapambazuko

na mchana kuwa usiku,

ambaye huyaita maji ya bahari

na kuyamwaga juu ya uso wa nchi:

Bwanandilo jina lake;

9 yeye hufanya maangamizo kwenye ngome

na kufanya mji uliozungushiwa ngome kuwa ukiwa),

10 mnamchukia yule akemeaye mahakamani,

na kumdharau yule ambaye husema kweli.

11 Mnamgandamiza maskini

na kumlazimisha awape nafaka.

Kwa hiyo, ingawa mmejenga majumba ya mawe ya fahari,

hamtaishi ndani yake;

ingawa mmepanda mashamba mazuri ya mizabibu,

hamtakunywa divai yake.

12 Kwa kuwa ninajua hesabu ya makosa yenu

na ukubwa wa dhambi zenu.

Mmewaonea wenye haki na kupokea rushwa

na kuzuia haki ya maskini mahakamani.

13 Kwa hiyo mtu mwenye busara hunyamaza kimya nyakati kama hizo,

kwa kuwa nyakati ni mbaya.

14 Tafuteni mema, wala si mabaya,

ili mpate kuishi.

NdipoBwanaMungu Mwenye Nguvu Zote atakuwa pamoja nanyi,

kama msemavyo yupo nanyi.

15 Yachukieni maovu, yapendeni mema;

dumisheni haki mahakamani.

YamkiniBwanaMungu Mwenye Nguvu Zote

atawahurumia mabaki ya Yosefu.

16 Kwa hiyo hili ndilo Bwana,BwanaMungu Mwenye Nguvu Zote, asemalo:

“Kutakuwepo maombolezo katika barabara zote

na vilio vya uchungu katika njia kuu zote.

Wakulima wataitwa kuja kulia,

na waombolezaji waje kuomboleza.

17 Kutakuwepo kuomboleza katika mashamba yote ya mizabibu,

kwa kuwa nitapita katikati yenu,”

asemaBwana.

Siku Ya Bwana

18 Ole wenu ninyi mnaoitamani

siku yaBwana!

Kwa nini mnaitamani siku yaBwana?

Siku hiyo itakuwa giza, si nuru.

19 Itakuwa kama vile mtu aliyemkimbia simba

kumbe akakutana na dubu,

kama vile mtu aliyeingia nyumbani mwake

na kuupumzisha mkono wake kwenye ukuta,

kumbe akaumwa na nyoka.

20 Je, siku yaBwanahaitakuwa giza, na si nuru:

giza nene, bila mwonzi wa mwanga?

21 “Ninachukia, ninazidharau sikukuu zenu za dini;

siwezi kuvumilia makusanyiko yenu.

22 Hata ingawa mnaniletea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka za nafaka,

sitazikubali.

Ingawa mnaniletea sadaka nzuri za amani,

sitazitambua.

23 Niondoleeni kelele za nyimbo zenu!

Sitasikiliza sauti za vinubi vyenu.

24 Lakini acheni haki itiririke kama mto,

na uadilifu uwe kama kijito kisichokauka!

25 “Je, mliniletea dhabihu na sadaka

kwa miaka arobaini kule jangwani,

ee nyumba ya Israeli?

26 Mmeyainua madhabahu ya mfalme wenu,

Sikuthi mungu wenu mtawala,

na Kiuni mungu wenu wa nyota,

ambao mliwatengeneza wenyewe.

27 Kwa sababu hiyo nitawapeleka uhamishoni mbali kupita Dameski,”

asemaBwana, ambaye jina lake ni Mungu Mwenye Nguvu Zote.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/AMO/5-ee752d29b5071367ece5f6ff3b14473b.mp3?version_id=1627—

Categories
Amosi

Amosi 6

Ole Kwa Wanaoridhika

1 Ole wenu ninyi mnaostarehe na kuridhika katika Sayuni,

na ninyi mnaojisikia salama juu ya Mlima Samaria,

ninyi watu mashuhuri wa taifa lililoendelea kuliko mataifa mengine,

ambao watu wa Israeli wanawategemea!

2 Nendeni Kalne mkaone kutoka huko;

mwende hadi Hamathi iliyo kuu,

kisha mshuke hadi Gathi ya Wafilisti.

Je, wao ni bora kuliko falme zenu mbili?

Je, nchi yao ni kubwa kuliko yenu?

3 Mnaiweka mbali siku iliyo mbaya

na kuleta karibu utawala wa kuogofya.

4 Ninyi mnalala juu ya vitanda vilivyofunikwa kwa pembe za ndovu,

na kujinyoosha juu ya viti vya fahari.

Mnajilisha kwa wana-kondoo wazuri

na ndama walionenepeshwa.

5 Ninyi mnapiga vinubi kama Daudi,

huku mkitunga nyimbo za vinanda mbalimbali.

6 Mnakunywa mvinyo kwa bakuli zilizojazwa,

na mnajipaka mafuta mazuri,

lakini hamhuzuniki kwa maangamizi ya Yosefu.

7 Kwa hiyo mtakuwa miongoni mwa watu wa kwanza kwenda uhamishoni;

karamu zenu na kustarehe kutakoma.

Bwana Anachukia Kiburi Cha Israeli

8 BwanaMwenyezi ameapa kwa nafsi yake mwenyewe:BwanaMungu Mwenye Nguvu Zote asema:

“Nachukia kiburi cha Yakobo,

nachukia ngome zake;

nitautoa mji wao na kila kitu

kilichomo ndani mwake.”

9 Kama watu kumi watabaki katika nyumba moja, wao pia watakufa.

10 Kama jamaa ambaye atachoma miili akija ili kuitoa nje ya nyumba, na kumuuliza yeyote ambaye bado anajificha humo, “Je, yuko mtu yeyote pamoja nawe?” Naye akisema, “Hapana,” ndipo atakaposema, “Nyamaza kimya! Haturuhusiwi kutaja jina laBwana.”

11 Kwa kuwaBwanaameamuru,

naye atabomoa jumba kubwa vipande vipande

na nyumba ndogo vipande vidogo vidogo.

12 Je, farasi waweza kukimbia kwenye miamba mikali?

Je, aweza mtu kulima huko kwa maksai?

Lakini mmegeuza haki kuwa sumu

na matunda ya uadilifu kuwa uchungu:

13 ninyi mnaoshangilia kushindwa kwa Lo-Debari

na kusema, “Je, hatukuteka Karnaimu kwa nguvu zetu wenyewe?”

14 MaanaBwanaMungu Mwenye Nguvu Zote asema,

“Nitainua taifa dhidi yenu, ee nyumba ya Israeli,

nalo litawatesa kuanzia Lebo-Hamathi

hadi Bonde la Araba.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/AMO/6-02314229646042210bd02661e6e1c8e8.mp3?version_id=1627—

Categories
Amosi

Amosi 7

Maono Ya Kwanza: Nzige

1 Hili ndilo alilonionyeshaBwanaMwenyezi katika maono: Alikuwa anaandaa makundi ya nzige baada ya kuvunwa fungu la mfalme na wakati ule tu mimea ya pili ilipokuwa ikichipua.

2 Wakati nzige walikuwa wamekula mimea yote ya nchi, nililia kwa sauti kuu, “BwanaMwenyezi, samehe! Je, Yakobo atawezaje kuendelea kuishi? Yeye ni mdogo sana!”

3 Kwa hiyoBwanaakaghairi.

KishaBwanaakasema, “Hili halitatokea.”

Maono Ya Pili: Moto

4 Hili ndiloBwanaMwenyezi alilonionyesha katika maono:BwanaMwenyezi alikuwa akiita hukumu ya moto; nao ulikausha vilindi vikuu, ukateketeza nchi.

5 Ndipo nikalia, “BwanaMwenyezi, nakusihi, zuia! Je, Yakobo atawezaje kuendelea kuishi? Yeye ni mdogo sana!”

6 Kwa hiyoBwanaakaghairi.

BwanaMwenyezi akasema, “Hili nalo halitatokea.”

Maono Ya Tatu: Timazi

7 Hili ndilo alilonionyesha katika maono: Bwana alikuwa amesimama karibu na ukuta ambao ulikuwa umejengwa kwa timazi, akiwa na uzi wa timazi mkononi mwake.

8 NayeBwanaakaniuliza, “Je, Amosi unaona nini?”

Nikamjibu, “Uzi wa timazi.”

Kisha Bwana akasema, “Tazama, ninaweka uzi wa timazi miongoni mwa watu wangu Israeli; sitawahurumia tena.

9 “Mahali pa Isaki pa juu pa kuabudia miungu pataangamizwa,

na mahali patakatifu pa Israeli pa kuabudia pataharibiwa;

kwa upanga wangu nitainuka

dhidi ya nyumba ya Yeroboamu.”

Amosi Na Amazia

10 Kisha Amazia kuhani wa Betheli akatuma ujumbe kwa Yeroboamu mfalme wa Israeli, akisema: “Amosi analeta fitina juu yako katikati ya Israeli. Nchi haiwezi kuvumilia maneno yake yote.

11 Kwa kuwa hili ndilo Amosi analosema:

“ ‘Yeroboamu atakufa kwa upanga,

na kwa hakika Israeli watakwenda uhamishoni,

mbali na nchi yao.’ ”

12 Kisha Amazia akamwambia Amosi, “Nenda zako, ewe mwonaji! Urudi katika nchi ya Yuda. Ujipatie riziki yako huko na kutoa unabii wako.

13 Usiendelee kutoa unabii katika Betheli, kwa sababu hapa ni mahali pa mfalme pa kuabudia na Hekalu la ufalme huu.”

14 Amosi akamjibu Amazia, “Mimi sikuwa nabii wala mwana wa nabii, lakini nilikuwa mchungaji wa kondoo na mtunza mikuyu.

15 LakiniBwanaakanitoa kutoka kuchunga kondoo na kuniambia, ‘Nenda, ukawatabirie watu wangu Israeli.’

16 Sasa basi, sikieni neno laBwana. Ninyi mnasema,

“ ‘Usitabiri dhidi ya Israeli,

na uache kuhubiri dhidi ya nyumba ya Isaki.’

17 “Kwa hiyo hili ndilo asemaloBwana:

“ ‘Mke wako atakuwa kahaba mjini,

nao wana wako na binti zako watauawa kwa upanga.

Shamba lako litapimwa na kugawanywa,

na wewe mwenyewe utafia katika nchi ya kipagani.

Nayo Israeli kwa hakika itakwenda uhamishoni,

mbali na nchi yao.’ ”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/AMO/7-3357b256954d11cd203e6401872f6212.mp3?version_id=1627—

Categories
Amosi

Amosi 8

Maono Ya Nne: Kikapu Cha Matunda Yaliyoiva

1 Hili ndilo alilonionyeshaBwanaMwenyezi katika maono: kikapu cha matunda yaliyoiva.

2 Akaniuliza, “Amosi, unaona nini?”

Nikajibu, “Kikapu chenye matunda yaliyoiva.”

NdipoBwanaakaniambia, “Wakati umewadia kwa watu wangu Israeli; sitawahurumia zaidi.”

3 BwanaMwenyezi asema, “Katika siku ile, nyimbo katika Hekalu zitageuka kuwa maombolezo. Miili mingi, mingi sana: itatupwa kila mahali! Kimya!”

4 Lisikieni hili, ninyi ambao mnawagandamiza wahitaji,

na kuwaonea maskini wa nchi,

5 mkisema,

“Ni lini Mwezi Mwandamo utakapopita

ili tupate kuuza nafaka,

na Sabato itakwisha lini

ili tuweze kuuza ngano?”

Mkipunguza vipimo,

na kuongeza bei,

na kudanganya kwa mizani zisizo sawa,

6 mkiwanunua maskini kwa fedha,

na wahitaji kwa jozi ya viatu,

na mkiuza hata takataka za ngano

pamoja na ngano.

7 Bwanaameapa kwake mwenyewe, aliye Kiburi cha Yakobo: “Kamwe sitasahau chochote ambacho wamefanya.

8 “Je, nchi haitatetemeka kwa ajili ya hili,

nao wote waishio ndani mwake hawataomboleza?

Nchi yote itainuka kama Naili;

itapanda na kushuka kama mto wa Misri.

9 “Katika siku ile,” asemaBwanaMwenyezi,

“Nitalifanya jua litue alasiri na kuifanya dunia

iwe giza wakati wa mchana mwangavu.

10 Nitageuza sikukuu zenu za kidini kuwa maombolezo,

na kuimba kwenu kote kuwe kilio.

Nitawafanya ninyi nyote mvae nguo ya gunia

na kunyoa nywele zenu.

Nitaufanya wakati ule uwe kama wa kuombolezea mwana wa pekee,

na mwisho wake kama siku ya uchungu.

11 “Siku zinakuja,” asemaBwanaMwenyezi,

“wakati nitakapotuma njaa katika nchi yote:

si njaa ya chakula wala kiu ya maji,

lakini njaa ya kusikia maneno yaBwana.

12 Wanaume watayumbayumba kutoka bahari hadi bahari

na kutangatanga kutoka kaskazini mpaka mashariki,

wakitafuta neno laBwana,

lakini hawatalipata.

13 “Katika siku ile

“wasichana wazuri na vijana wanaume wenye nguvu

watazimia kwa sababu ya kiu.

14 Wale waapao kwa aibu ya Samaria,

au kusema, ‘Hakika kama miungu yenu iishivyo, ee Dani,’

au ‘Hakika kama mungu wa Beer-Sheba aishivyo’:

wataanguka, wala hawatasimama tena.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/AMO/8-9d2d11d415c7d57d34be47cf2f3a8d11.mp3?version_id=1627—

Categories
Amosi

Amosi 9

Israeli Kuangamizwa

1 Nilimwona Bwana akiwa amesimama kando ya madhabahu, naye akasema:

“Piga vichwa vya nguzo

ili vizingiti vitikisike.

Viangushe juu ya vichwa vya watu wote;

na wale watakaosalia nitawaua kwa upanga.

Hakuna awaye yote atakayekimbia,

hakuna atakayetoroka.

2 Wajapojichimbia chini mpaka kwenye vina vya kuzimu,

kutoka huko mkono wangu utawatoa.

Wajapopanda juu hadi kwenye mbingu,

kutoka huko nitawashusha.

3 Wajapojificha juu ya kilele cha Karmeli,

huko nitawawinda na kuwakamata.

Wajapojificha kutoka kwenye uso wangu

katika vilindi vya bahari,

huko nako nitaamuru joka kuwauma.

4 Wajapopelekwa uhamishoni na adui zao,

huko nako nitaamuru upanga uwaue.

Nitawakazia macho yangu kwa mabaya

wala si kwa mazuri.”

5 Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote,

yeye agusaye dunia nayo ikayeyuka,

na wote wakaao ndani mwake wakaomboleza:

nayo nchi yote huinuka kama Naili,

kisha hushuka kama mto wa Misri;

6 yeye ambaye hujenga jumba lake la kifalme katika mbingu

na kuisimika misingi yake juu ya dunia,

yeye aitaye maji ya bahari

na kuyamwaga juu ya uso wa nchi:

Bwanandilo jina lake.

7 “Je, Waisraeli,

ninyi si sawa kwangu kama Wakushi?”

asemaBwana.

“Je, sikuleta Israeli kutoka Misri,

Wafilisti kutoka Kaftori,

na Washamu kutoka Kiri?

8 “Hakika macho yaBwanaMwenyezi

yako juu ya ufalme wenye dhambi.

Nami nitauangamiza

kutoka kwenye uso wa dunia:

hata hivyo sitaiangamiza kabisa

nyumba ya Yakobo,”

asemaBwana.

9 “Kwa kuwa nitatoa amri,

na nitaipepeta nyumba ya Israeli

miongoni mwa mataifa yote,

kama vile nafaka ipepetwavyo katika ungo,

na hakuna hata punje moja itakayoanguka chini.

10 Watenda dhambi wote miongoni mwa watu wangu

watauawa kwa upanga,

wale wote wasemao,

‘Maafa hayatatupata wala kutukuta.’

Kurejezwa Kwa Israeli

11 “Katika siku ile nitaisimamisha

hema ya Daudi iliyoanguka.

Nitakarabati mahali palipobomoka

na kujenga upya magofu yake,

na kuijenga kama ilivyokuwa awali,

12 ili wapate kuyamiliki mabaki ya Edomu,

na mataifa yote yale yanayobeba Jina langu,”

asemaBwanaambaye atafanya mambo haya.

13 “Siku zinakuja,” asemaBwana,

“wakati mvunaji atatanguliwa na mkulima,

naye mpanzi atatanguliwa na yeye akamuaye zabibu.

Divai mpya itadondoka kutoka milimani,

na kutiririka kutoka vilima vyote.

14 Nitawarejesha tena watu wangu Israeli waliohamishwa;

wataijenga tena miji iliyoachwa magofu,

nao wataishi ndani mwake.

Watapanda mizabibu na kunywa divai yake;

watalima bustani na kula matunda yake.

15 Nitaipanda Israeli katika nchi yao wenyewe,

hawatangʼolewa tena

kutoka nchi ambayo nimewapa,”

asemaBwanaMungu wenu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/AMO/9-45ce86977450217474ac40ec61b497d3.mp3?version_id=1627—