Categories
3 Yohana

3 Yohana Utangulizi

Utangulizi

Waraka wa tatu wa Yohana uliandikiwa Gayo, ambaye alikuwa kiongozi muhimu katika kanisa. Alielekezwa kuwasaidia na kuwahudumia wale waliokuja kama wajumbe wa Mungu. Pia alipewa onyo kuhusu Deotrefe, juu ya tabia yake ya kukosa ushirikiano. Yohana alieleza tarajio lake la kuja na kushughulikia tatizo hili mwenyewe.

Mwandishi

Mtume Yohana.

Kusudi

Yohana anamwandikia Gayo akimpa onyo kuhusu Deotrefe, kwa tabia yake ya kukosa ushirikiano.

Mahali

Efeso.

Tarehe

Kama mwaka wa 90 B.K.

Wahusika Wakuu

Yohana, Gayo, Deotrefe, na Demetrio.

Wazo Kuu

Wajibu binafsi wa Gayo kuhusu watumishi wa kweli na wa uongo.

Mambo Muhimu

Yohana anamtakia Gayo kufanikiwa katika mambo yote, na pia anamwagiza asiige lililo baya bali aige lililo jema.

Mgawanyo

Salamu (

1-4

)

Kutiwa moyo kwa Gayo (

5-8

)

Kukemewa kwa Deotrefe (

9-10

)

Kusifiwa kwa Demetrio (

11-12

)

Hitimisho (

13-14

).

Categories
3 Yohana

3 Yohana 1

Salamu

1 Mzee:

Kwa Gayo rafiki yangu, nimpendaye katika kweli.

Gayo Anasifiwa Kwa Ajili Ya Ukarimu Wake

2 Mpendwa, naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya njema kama vile roho yako ifanikiwavyo.

3 Ilinifurahisha sana baadhi ya ndugu walipokuja na kutueleza juu ya uaminifu wako katika kweli na jinsi unavyoendelea kuenenda katika hiyo kweli.

4 Sina furaha kubwa kuliko hii, kusikia kwamba watoto wangu wanaenenda katika kweli.

5 Rafiki mpendwa, wewe ni mwaminifu kwa yale unayowatendea ndugu, ingawa wao ni wageni kwako.

6 Wameshuhudia kuhusu upendo wako mbele ya kanisa. Utafanya vyema ukiwasafirisha kama inavyostahili kwa Mungu.

7 Ilikuwa ni kwa ajili ya hilo Jina waliondoka, bila kukubali kupokea msaada wowote kutoka kwa watu wasioamini.

8 Kwa hiyo imetupasa sisi kuonyesha ukarimu kwa watu kama hao ili tuweze kutenda kazi pamoja kwa ajili ya kweli.

Deotrefe

9 Nililiandikia kanisa, lakini Deotrefe, yeye apendaye kujifanya wa kwanza, hakubali mamlaka yetu.

10 Hivyo kama nikija, nitakumbuka matendo yake atendayo, akitusingizia kwa maneno ya hila. Wala hatosheki na hayo anayotusingizia, bali pia hukataa kuwakaribisha ndugu, na hata huwazuia wale walio tayari kufanya hivyo na kuwafukuza watoke kanisani.

Demetrio

11 Rafiki mpendwa, usiige lile lililo baya bali lile lililo jema. Yeyote atendaye mema atoka kwa Mungu, bali atendaye mabaya hajamwona Mungu.

12 Kila mtu ameshuhudia mema kuhusu Demetrio, vivyo hivyo hata na hiyo kweli yenyewe. Sisi pia twashuhudia mema juu yake, nanyi mwajua kwamba ushuhuda wetu ni kweli.

Salamu Za Mwisho

13 Ninayo mambo mengi ya kukuandikia, lakini sipendi kuandika kwa kalamu na wino.

14 Badala yake, nataraji kukuona upesi, nasi tutaongea pamoja ana kwa ana.

Amani iwe kwako. Rafiki zetu walioko hapa wanakusalimu. Wasalimu hao rafiki zetu walioko huko, kila mmoja kwa jina lake.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/3JN/1-4387cdc648dbd7fbbedcd1fbc89ff6c1.mp3?version_id=1627—