Categories
2 Yohana

2 Yohana Utangulizi

Utangulizi

Waraka wa pili wa Yohana uliandikwa kwa bibi mteule na watoto wake. Unaweza kuwa ulimhusu mtu binafsi na jamaa yake, au ulilihusu kanisa fulani. Msisitizo unawekwa katika umuhimu wa imani kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu katika umbo la mwanadamu. Inawapasa waumini wanaosoma kudumu katika pendo la Mungu, na kukataa mafundisho mapotovu yanayopinga imani ya kweli.

Yohana pia anaandika kuwaonya ili waweze kutambua walimu wa uongo waliosafiri huku na huko, wasije wakawaunga mkono na kuwasaidia. Yaani mtu yeyote asije akachangia kwenye kueneza mafundisho ya uongo badala ya yale ya kweli.

Mwandishi

Mtume Yohana.

Kusudi

Kuhimiza mwenendo wa muumini, na maonyo kuhusu wadanganyifu na mbinu zao.

Mahali

Efeso.

Tarehe

Kama mwaka wa 90 B.K.

Wahusika Wakuu

Yohana, bibi mteule na watoto wake.

Wazo Kuu

Mtume Yohana anaagiza watu kuenenda katika kweli na kumtii Mungu, wakijihadhari na udanganyifu, ili wapate kumpenda Mungu, na kupendana wao kwa wao.

Mambo Muhimu

Pendo la kweli ni kuwajali wengine. Tunatamani kupendwa na kuwapenda wengine, lakini tunaona mifano michache sana ya uhalisi katika jambo hili. Dunia imejaa ubinafsi, uchoyo na kujipenda mwenyewe.

Mgawanyo

Salamu (

1-3

)

Ushauri na maonyo (

4-11

)

Hitimisho (

12-13

).

Categories
2 Yohana

2 Yohana 1

Salamu

1 Mzee:

Kwa bibi mteule na watoto wake, niwapendao katika kweli, wala si mimi tu, bali na wale wote waijuayo kweli:

2 kwa sababu ya ile kweli ikaayo ndani yetu na ambayo itaendelea kukaa nasi milele:

3 Neema, rehema na amani itokayo kwa Mungu Baba na kwa Yesu Kristo, Mwanawe Baba, itakuwa pamoja nasi katika kweli na upendo.

Kweli Na Upendo

4 Imenipa furaha kuu kuona baadhi ya watoto wako wanaenenda katika kweli, kama vile Baba alivyotuagiza.

5 Sasa, bibi mpendwa, si kwamba ninakuandikia amri mpya, bali ile tuliyokuwa nayo tangu mwanzo. Tupendane kila mmoja na mwenzake.

6 Hili ndilo pendo, kwamba tuenende sawasawa na amri zake. Hii ndiyo amri yake kama vile mlivyosikia tangu mwanzo, kwamba mwenende katika upendo.

7 Wadanganyifu wengi, wasiokubali kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili, wametokea ulimwenguni. Mtu wa namna hiyo ni mdanganyifu na mpinga Kristo.

8 Jihadharini msije mkapoteza kile mlichokitenda, bali mpate kupewa thawabu kamilifu.

9 Mtu yeyote asiyedumu katika mafundisho ya Kristo, bali akayaacha, yeye hana Mungu. Yeyote anayedumu katika mafundisho ana Baba na Mwana pia.

10 Msimpokee mtu yeyote anayewajia ambaye hawaletei mafundisho haya, wala msimkaribishe nyumbani mwenu.

11 Yeyote amkaribishaye mtu wa namna hiyo anashiriki katika matendo maovu ya mtu huyo.

Salamu Za Mwisho

12 Ninayo mengi ya kuwaandikia, lakini sitaki kutumia karatasi na wino. Badala yake, nataraji kuja kwenu na kuongea nanyi ana kwa ana, ili furaha yetu ipate kuwa timilifu.

13 Watoto wa dada yako mteule wanakusalimu. Amen.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2JN/1-01922791e51083ee0d6d6cf6d4f3f655.mp3?version_id=1627—