Categories
2 Wakorintho

2 Wakorintho Utangulizi

Utangulizi

Ingawa inaonekana kwamba waraka wa kwanza wa Paulo kwa Wakorintho uliwasaidia, bado mivutano na mashindano yalikuwa yakiendelea. Walimu wa uongo walikuwa wamejiingiza ndani ya kanisa, wakiwa wanapinga na hata kushambulia uadilifu wa Paulo mwenyewe, na mamlaka yake kama mtume. Wengine katika kanisa hawakutaka kutubu. Hivyo Paulo aliamua kutorudi huko hadi tabia zao zibadilike.

Paulo aliandika waraka huu kueleza hisia zake kuhusu wajibu, shauku na majukumu katika ushirika wa Wakorintho, na pia kujibu mashambulizi yaliyokuwa yameelekezwa kwake binafsi kama mtume. Katika kushughulikia matatizo hayo, Paulo alithibitisha mamlaka yake kama mtume.

Mwandishi

Mtume Paulo.

Kusudi

Kuthibitisha huduma ya Paulo, na kutetea uwezo wake kama mtume, na pia kuyakataa mafundisho ya uongo katika kanisa la Korintho.

Mahali

Makedonia.

Tarehe

Kati ya 55-57 B.K.

Wahusika Wakuu

Paulo, Tito, Timotheo, na walimu wa uongo.

Wazo Kuu

Maisha binafsi na utumishi wa Paulo: anaorodhesha mambo aliyoyapitia katika maisha yake kama mtumishi wa Kristo.

Mambo Muhimu

Jinsi tunavyoweza kupata ushindi katika mateso, na jinsi neema ya Mungu inavyotenda kazi kuleta mema kutokana na mateso. Paulo pia anatetea utume wake na kuwaonya wasiotii.

Mgawanyo

Salamu na utambulisho, faraja kwa Wakristo (

1:1–2:4

)

Msamaha kwa wale waliotubu (

2:5-17

)

Maelekezo kuhusu utumishi wa kweli wa Kikristo (

3:1–6:2

)

Habari za Paulo mwenyewe (

6:3–7:16

)

Neema ya utoaji na maelekezo kuhusu changizo (

8:1–9:15

)

Utetezi wa Paulo kuhusu huduma yake (

10:1–11:33

)

Maono ya Paulo na mwiba aliokuwa nao (

12:1–12:21

)

Maonyo ya mwisho, na salamu (

13:1-14

).

Categories
2 Wakorintho

2 Wakorintho 1

Salamu

1 Barua hii ni kutoka kwangu mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo ndugu yetu,

Kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, pamoja na watakatifu wote walioko Akaya yote:

2 Neema na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo iwe nanyi.

Mungu Wa Faraja Yote

3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa huruma na Mungu wa faraja yote.

4 Yeye hutufariji katika taabu zetu, ili tuweze kuwafariji walio katika taabu yoyote kwa faraja ambayo sisi wenyewe tumepokea kutoka kwa Mungu.

5 Kama vile mateso ya Kristo yanavyozidi ndani ya maisha yetu, hivyo ndivyo faraja yetu inavyofurika kwa njia ya Kristo.

6 Kama tunataabika, ni kwa ajili ya faraja na wokovu wenu; kama tukifarijiwa, ni kwa ajili ya faraja yenu, iwaleteayo saburi ya mateso yale yale yanayotupata.

7 Nalo tumaini letu kwenu ni thabiti, kwa sababu tunajua kwamba kama vile mnavyoshiriki mateso yetu, ndivyo pia mnavyoshiriki katika faraja yetu.

8 Ndugu wapendwa, hatutaki mkose kujua kuhusu zile taabu tulizopata huko Asia. Kwa maana tulilemewa na mizigo sana, kiasi cha kushindwa kuvumilia, hata tulikata tamaa ya kuishi.

9 Kwa kweli, mioyoni mwetu tulihisi tumekabiliwa na hukumu ya kifo, ili tusijitegemee sisi wenyewe bali tumtegemee Mungu afufuaye wafu.

10 Yeye aliyetuokoa kwenye hatari kubwa ya kifo na atatuokoa tena. Kwake yeye tumeweka tumaini letu kwamba ataendelea kutuokoa.

11 Kama vile mlivyoungana kusaidiana nasi katika maombi, hivyo wengi watatoa shukrani kwa niaba yetu kwa ajili ya baraka za neema tulizopata kwa majibu ya maombi ya wengi.

Paulo Aahirisha Ziara

12 Basi haya ndiyo majivuno yetu: Dhamiri yetu inatushuhudia kwamba tumeenenda katika ulimwengu na hasa katika uhusiano wetu na ninyi, katika utakatifu na uaminifu utokao kwa Mungu. Hatukufanya hivyo kwa hekima ya kidunia bali kwa neema ya Mungu.

13 Kwa maana hatuwaandikii mambo ambayo hamwezi kusoma au kuyaelewa. Natumaini kwamba,

14 kama vile mlivyotuelewa kwa sehemu, mtakuja kuelewa kwa ukamilifu ili mweze kujivuna kwa ajili yetu, kama na sisi tutakavyojivuna kwa ajili yenu katika siku ya Bwana Yesu.

15 Kwa kuwa nilikuwa na uhakika wa mambo haya, nilitaka nije kwenu kwanza, ili mpate faida mara mbili.

16 Nilipanga kuwatembelea nikiwa safarini kwenda Makedonia na kurudi tena kwenu nikitoka Makedonia, ili mnisafirishe katika safari yangu ya kwenda Uyahudi.

17 Nilipopanga jambo hili, je, nilikuwa kigeugeu? Au ninafanya mipango yangu kwa hali ya mwili, ili niseme, “Ndiyo, ndiyo” na “Siyo, siyo” wakati huo huo?

18 Hakika kama Mungu alivyo mwaminifu, maneno yetu kwenu hayajawa “Ndiyo na Siyo.”

19 Kwa kuwa Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, ambaye tulimhubiri kwenu: Mimi, Silvanona Timotheo, hakuwa “Ndiyo” na “Siyo,” bali kwake yeye siku zote ni “Ndiyo.”

20 Kwa maana ahadi zote za Mungu zilizo katika Kristo ni “Ndiyo.” Kwa sababu hii ni kwake yeye tunasema “Amen” kwa utukufu wa Mungu.

21 Basi ni Mungu atufanyaye sisi pamoja nanyi kusimama imara katika Kristo. Ametutia mafuta

22 kwa kututia muhuri wake na kutupa Roho wake mioyoni mwetu kuwa rehani kwa ajili ya kututhibitishia kile kijacho.

23 Mungu ni shahidi wangu kwamba ilikuwa ni kwa ajili ya kuwahurumia ninyi sikurudi Korintho.

24 Si kwamba tunatawala imani yenu, bali twatenda kazi pamoja nanyi kwa ajili ya furaha yenu, kwa sababu ni kwa imani mwasimama imara.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2CO/1-50c1c677c34a85ad1c599ed14c5e7ed2.mp3?version_id=1627—

Categories
2 Wakorintho

2 Wakorintho 2

1 Hivyo nilikusudia moyoni mwangu nisifanye ziara nyingine yenye kuwaumiza ninyi.

2 Kwa kuwa kama nikiwahuzunisha ninyi, ni nani aliyebaki wa kunifurahisha isipokuwa ninyi ambao nimewahuzunisha?

3 Niliandika hivyo kama nilivyofanya, ili nikija nisihuzunishwe na wale watu ambao wangenifanya nifurahi. Nina uhakika na ninyi nyote, kwamba wote mngeshiriki furaha yangu.

4 Kwa maana niliwaandikia kutokana na dhiki kubwa na kutaabika sana kwa moyo wangu tena kwa machozi mengi, shabaha yangu si ili niwasababishe mhuzunike bali kuwaonyesha kina cha upendo wangu kwenu.

Msamaha Kwa Mwenye Dhambi

5 Lakini ikiwa mtu yeyote amesababisha huzuni, kwa kiasi fulani hakunihuzunisha mimi kama vile alivyowahuzunisha ninyi nyote, ili nisiwe mkali kupita kiasi.

6 Adhabu hii aliyopewa na wengi inamtosha.

7 Basi sasa badala yake, inawapasa kumsamehe na kumfariji, ili asigubikwe na huzuni kupita kiasi.

8 Kwa hiyo, nawasihi, mpate kuuthibitisha tena upendo wenu kwa ajili yake.

9 Sababu ya kuwaandikia ni kuona kama mngeweza kushinda hilo jaribio na kutii katika kila jambo.

10 Kama ninyi mkimsamehe mtu yeyote, mimi pia nimemsamehe. Kile nilichosamehe, kama kulikuwa na kitu chochote cha kusamehe, nimekwisha kusamehe mbele ya Kristo kwa ajili yenu,

11 ili Shetani asitushinde. Kwa maana hatuachi kuzijua hila zake.

Wasiwasi Wa Paulo Huko Troa

12 Basi nilipofika Troa kuhubiri Injili ya Kristo na kukuta kwamba Bwana alikuwa amenifungulia mlango,

13 bado nilikuwa sina utulivu akilini mwangu kwa sababu sikumkuta ndugu yangu Tito huko. Hivyo niliagana nao nikaenda Makedonia.

14 Lakini Mungu ashukuriwe, yeye ambaye siku zote hutufanya tuandamane kwa ushindi tukiwa ndani ya Kristo. Naye kupitia kwetu hueneza kila mahali harufu nzuri ya kumjua yeye.

15 Kwa maana sisi kwa Mungu ni harufu nzuri ya manukato ya Kristo miongoni mwa wale wanaookolewa na kwa wale wanaopotea.

16 Kwa wale wanaopotea, sisi ni harufu ya mauti iletayo mauti; lakini kwa wale wanaookolewa, sisi ni harufu nzuri iletayo uzima. Ni nani awezaye mambo hayo?

17 Tofauti na watu wengine wengi, sisi hatufanyi biashara na Neno la Mungu kwa ajili ya kupata faida. Kinyume chake, katika Kristo tunalisema Neno la Mungu kwa unyoofu, kama watu tuliotumwa kutoka kwa Mungu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2CO/2-4b7999417f41f999a86db19e88a21f84.mp3?version_id=1627—

Categories
2 Wakorintho

2 Wakorintho 3

Wahudumu Wa Agano Jipya

1 Je, tunaanza tena kujisifu wenyewe? Au tunahitaji kupata barua za utambulisho kwenu au kutoka kwenu, kama watu wengine?

2 Ninyi wenyewe ndio barua yetu iliyoandikwa katika mioyo yetu, inayojulikana na kusomwa na kila mtu.

3 Nanyi mwadhihirisha wazi kwamba ninyi ni barua itokayo kwa Kristo, matokeo ya huduma yetu, ambayo haikuandikwa kwa wino bali kwa Roho wa Mungu aliye hai, si katika vibao vya mawe, bali katika vibao ambavyo ni mioyo ya wanadamu.

4 Hili ndilo tumaini tulilo nalo mbele za Mungu kwa njia ya Kristo.

5 Si kwamba sisi tunafikiri kuwa tunaweza kufanya jambo lolote wenyewe, lakini nguvu yetu inatoka kwa Mungu.

6 Ndiye alituwezesha sisi kuwa wahudumu wa Agano Jipya: si wa andiko, bali wa Roho; kwa kuwa andiko huua bali Roho hutia uzima.

Utukufu Wa Agano Jipya

7 Basi ikiwa ile huduma iliyoleta mauti, iliyoandikwa kwa herufi juu ya jiwe ilikuja kwa utukufu, hata Waisraeli wakawa hawawezi kuutazama uso wa Mose kwa sababu ya ule utukufu wake ingawa ulikuwa ni wa kufifia,

8 je, huduma ya Roho haitakuwa na utukufu zaidi?

9 Ikiwa huduma ile inayowahukumu wanadamu ina utukufu, je, ile huduma iletayo haki haitakuwa ya utukufu zaidi?

10 Kwa maana kile kilichokuwa na utukufu sasa hakina utukufu ukilinganisha na huu utukufu unaozidi wa Agano Jipya.

11 Ikiwa kile kilichokuwa kinafifia kilikuja kwa utukufu, je, si zaidi utukufu wa kile kinachodumu?

12 Kwa hiyo, kwa kuwa tunalo tumaini hili, tuna ujasiri sana.

13 Sisi si kama Mose, ambaye ilimpasa kuweka utaji ili kufunika uso wake ili Waisraeli wasiuone ule mngʼao uliokuwa juu yake hadi ulipofifia na hatimaye kutoweka.

14 Lakini akili zao zilipumbazwa, kwa maana mpaka leo utaji ule ule hufunika wakati Agano la Kale linasomwa. Huo utaji haujaondolewa, kwa maana ni katika Kristo peke yake unaondolewa.

15 Hata leo Sheria ya Mose inaposomwa, utaji hufunika mioyo yao.

16 Lakini wakati wowote mtu anapomgeukia Bwana, utaji unaondolewa.

17 Basi Bwana ndiye Roho. Mahali alipo Roho wa Bwana hapo pana uhuru.

18 Nasi sote, tukiwa na nyuso zisizotiwa utaji tunadhihirisha utukufu wa Bwana, kama kwenye kioo. Nasi tunabadilishwa ili tufanane naye, toka utukufu hadi utukufu mkuu zaidi, utokao kwa Bwana, ambaye ndiye Roho.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2CO/3-5de02adfa7c0bebf39de62a416f664d5.mp3?version_id=1627—

Categories
2 Wakorintho

2 Wakorintho 4

Hazina Ya Mbinguni Katika Vyombo Vya Udongo

1 Kwa hiyo, kwa kuwa tuna huduma hii kwa rehema za Mungu, hatukati tamaa.

2 Tumekataa mambo ya siri na ya aibu, wala hatufuati njia za udanganyifu, tukichanganya Neno la Mungu na uongo. Kinyume cha hayo, tunadhihirisha kweli waziwazi na kujitambulisha wenyewe kwenye dhamiri ya kila mtu mbele za Mungu.

3 Hata nayo Injili yetu kama imetiwa utaji, ni kwa wale tu wanaopotea.

4 Kwa habari yao, mungu wa dunia hii amepofusha akili za wasioamini, ili wasione nuru ya Injili ya utukufu wa Kristo, aliye sura ya Mungu.

5 Kwa maana hatujihubiri sisi wenyewe ila tunamhubiri Yesu Kristo kuwa ni Bwana na sisi ni watumishi wenu kwa ajili ya Yesu.

6 Kwa kuwa Mungu, yeye aliyesema, “Nuru na ingʼae gizani,” ameifanya nuru yake ingʼae mioyoni mwetu ili kutupatia nuru ya maarifa ya utukufu wa Mungu katika uso wa Kristo.

7 Lakini tunayo hazina hii katika vyombo vya udongo, ili ijulikane wazi kwamba uwezo huu wa ajabu unatoka kwa Mungu wala si kwetu.

8 Twataabika kila upande lakini hatuangamizwi; twaona wasiwasi lakini hatukati tamaa;

9 twateswa lakini hatuachwi; twatupwa chini lakini hatupondwi.

10 Siku zote twachukua katika mwili kufa kwake Yesu ili kwamba uzima wa Yesu uweze kudhihirika katika miili yetu.

11 Kwa maana sisi tulio hai siku zote tumetolewa tufe kwa ajili ya Yesu, ili kwamba uzima wake upate kudhihirishwa katika mwili wetu upatikanao na mauti.

12 Hivyo basi, mauti inatenda kazi ndani yetu, bali uzima unatenda kazi ndani yenu.

13 Imeandikwa, “Niliamini, kwa hiyo nimesema.” Kwa roho yule yule wa imani pia tuliamini na hivyo tunasema,

14 kwa sababu tunajua kwamba yeye aliyemfufua Bwana Yesu kutoka kwa wafu, atatufufua sisi pia pamoja na Yesu na kutuleta sisi pamoja nanyi mbele zake.

15 Haya yote ni kwa faida yenu, ili kwamba neema ile inavyowafikia watu wengi zaidi na zaidi, ipate kusababisha shukrani nyingi kwa utukufu wa Mungu.

16 Kwa hiyo, hatukati tamaa. Ingawa utu wetu wa nje unachakaa, utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku.

17 Kwa maana dhiki yetu nyepesi iliyo ya kitambo inatutayarisha kwa ajili ya utukufu wa milele unaozidi kuwa mwingi kupita kiasi,

18 kwa sababu hatuangalii yale yanayoweza kuonekana bali yale yasiyoweza kuonekana. Kwa maana yale yanayoweza kuonekana ni ya kitambo tu, bali yale yasiyoweza kuonekana ni ya milele.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2CO/4-085c3200424f863af00219dd2c593434.mp3?version_id=1627—

Categories
2 Wakorintho

2 Wakorintho 5

Makao Yetu Ya Mbinguni

1 Kwa maana twajua kama hema yetu ya dunia tunayoishi ikiharibiwa, tunalo jengo kutoka kwa Mungu, nyumba iliyo ya milele kule mbinguni, isiyojengwa kwa mikono ya wanadamu.

2 Katika hema hii twalia kwa uchungu, tukitamani kuvikwa makao yetu ya mbinguni,

3 kwa kuwa tukiisha kuvikwa hatutaonekana tena kuwa uchi.

4 Kwa kuwa tukiwa bado katika hema hii twalia kwa uchungu na kulemewa, kwa sababu hatutaki kuvuliwa bali kuvikwa makao yetu ya mbinguni ili kwamba kile kipatikanacho na mauti kimezwe na uzima.

5 Basi Mungu ndiye alitufanya kwa ajili ya jambo lilo hilo naye ametupa Roho Mtakatifu kuwa amana, akituhakikishia ahadi ya kile kijacho.

6 Kwa hiyo siku zote tunalo tumaini, hata ingawa tunajua kwamba wakati tukiwa katika mwili huu, tuko mbali na Bwana,

7 kwa maana twaenenda kwa imani wala si kwa kuona.

8 Naam, tunalo tumaini na ingekuwa bora zaidi kuuacha mwili huu na kwenda kukaa na Bwana.

9 Kwa hiyo, kama tuko katika mwili huu au tuko mbali nao, lengo letu ni kumpendeza Bwana.

10 Kwa kuwa sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mmoja apate kulipwa kwa ajili ya yale ambayo yametendwa katika mwili wake, yakiwa mema au mabaya.

Huduma Ya Upatanisho

11 Basi, kwa kuwa tunajua kumcha Bwana, tunajitahidi kuwavuta wengine. Lakini Mungu anatufahamu dhahiri, nami natumaini kwamba tu dhahiri katika dhamiri zenu pia.

12 Sio kwamba tunajaribu kujistahilisha kwenu tena, lakini tunataka kuwapa nafasi ili mwone fahari juu yetu mweze kuwajibu hao wanaoona fahari juu ya mambo yanayoonekana badala ya mambo yaliyo moyoni.

13 Kama tumerukwa na akili, ni kwa ajili ya Mungu; kama tuna akili timamu, ni kwa ajili yenu.

14 Kwa kuwa upendo wa Kristo unatutia nguvu, kwa sababu tunasadiki kuwa mmoja alikufa kwa ajili ya wote, kwa hiyo wote walikufa.

15 Naye alikufa kwa ajili ya watu wote, ili kwamba wote wanaoishi wasiishi tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa na kufufuliwa tena kwa ajili yao.

16 Hivyo tangu sasa hatumwangalii mtu yeyote kwa mtazamo wa kibinadamu. Ingawa wakati fulani tulimwangalia Kristo kwa namna ya kibinadamu, hatumwangalii tena hivyo.

17 Kwa hiyo kama mtu akiwa ndani ya Kristo, amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita, tazama, yamekuwa mapya.

18 Haya yote yanatokana na Mungu, ambaye ametupatanisha sisi na nafsi yake kwa njia ya Yesu Kristo na kutupata sisi huduma ya upatanisho:

19 Kwamba Mungu alikuwa ndani ya Kristo akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake mwenyewe, akiwa hawahesabii watu dhambi zao. Naye ametukabidhi sisi ujumbe huu wa upatanisho.

20 Kwa hiyo sisi ni mabalozi wa Kristo, kana kwamba Mungu anawasihi kupitia kwa vinywa vyetu. Nasi twawaomba sana ninyi kwa niaba ya Kristo, mpatanishwe na Mungu.

21 Kwa maana Mungu alimfanya yeye asiyekuwa na dhambi kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kufanywa haki ya Mungu kwake yeye.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2CO/5-78bab55573c4900c4f912b8c8bac56b9.mp3?version_id=1627—

Categories
2 Wakorintho

2 Wakorintho 6

1 Kama watendakazi pamoja na Mungu, tunawasihi msipokee neema ya Mungu bure.

2 Kwa maana asema:

“Wakati wangu uliokubalika nilikusikia,

siku ya wokovu nilikusaidia.”

Tazama, wakati uliokubalika ndio huu, siku ya wokovu ndiyo sasa.

Taabu Za Paulo

3 Hatuweki kitu cha kukwaza katika njia ya mtu yeyote, ili huduma yetu isionekane kuwa na lawama.

4 Bali kama watumishi wa Mungu tuonyeshe kwa kila njia: katika saburi nyingi; katika dhiki, katika misiba, na katika shida;

5 katika kupigwa, katika kufungwa gerezani na katika ghasia; katika kazi ngumu, katika kukesha na katika kufunga;

6 katika utakatifu, katika ufahamu, katika uvumilivu, na katika utu wema; katika Roho Mtakatifu na upendo wa kweli;

7 katika maneno ya kweli na katika nguvu za Mungu, kwa silaha za haki za mkono wa kuume na za mkono wa kushoto;

8 katika utukufu na katika kudharauliwa; katika sifa mbaya na katika sifa nzuri; tukiwa kama wadanganyaji, lakini tukiwa wakweli;

9 tukiwa maarufu, lakini tukihesabiwa kama tusiojulikana; tukiwa kama wanaokufa, lakini tunaishi; tukipigwa, lakini hatuuawi;

10 tukiwa kama wenye huzuni, lakini siku zote tukifurahi; tukionekana maskini, lakini tukitajirisha wengi; tukiwa kama wasio na kitu, lakini tuna vitu vyote.

11 Tumesema nanyi wazi, enyi Wakorintho na kuwafungulieni mioyo yetu wazi kabisa.

12 Sisi hatujizuii kuwapenda, bali ninyi mmeuzuia upendo wenu kwetu.

13 Sasa nasema, kama na watoto wangu: Ninyi pia ifungueni mioyo yenu kabisa.

Msifungiwe Nira Pamoja Na Wasioamini

14 Msifungiwe nira pamoja na watu wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa, kwa maana pana uhusiano gani kati ya haki na uovu? Au kuna ushirika gani kati ya nuru na giza?

15 Kuna mapatano gani kati ya Kristo na Beliari?Yeye aaminiye ana sehemu gani na yeye asiyeamini?

16 Kuna mapatano gani kati ya Hekalu la Mungu na sanamu? Kwa kuwa sisi tu Hekalu la Mungu aliye hai. Kama Mungu alivyosema: “Nitakaa pamoja nao na kutembea katikati yao, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.”

17 “Kwa hiyo tokeni miongoni mwao,

mkatengwe nao,

asema Bwana.

Msiguse kitu chochote kilicho najisi,

nami nitawakaribisha.”

18 “Mimi nitakuwa Baba kwenu,

nanyi mtakuwa wanangu na binti zangu,

asema Bwana Mwenyezi.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2CO/6-5a25b68d5d369fa2494ad0f73ea721b9.mp3?version_id=1627—

Categories
2 Wakorintho

2 Wakorintho 7

1 Wapenzi, kwa kuwa tunazo ahadi hizi, basi na tujitakase nafsi zetu kutokana na kila kitu kitiacho mwili na roho unajisi, tukitimiza utakatifu kwa kumcha Mungu.

Furaha Ya Paulo

2 Tupatieni nafasi mioyoni mwenu. Hatujamkosea mtu yeyote, hatujampotosha mtu yeyote, wala hatujamdhulumu mtu yeyote.

3 Sisemi haya ili kuwahukumu, kwa kuwa nilisema mwanzo, kwamba ninyi mko mioyoni mwetu hata kwa kufa pamoja au kuishi pamoja.

4 Mara nyingi najivuna kwa ajili yenu; naona fahari juu yenu. Nimejawa na faraja. Nina furaha kupita kiasi katika mateso yetu yote.

5 Kwa maana hata tulipoingia Makedonia, miili yetu haikuwa na raha. Tulisumbuliwa kila upande, kwa nje kulikuwa na mapigano na mioyoni mwetu tulikuwa na hofu.

6 Bali Mungu, yeye awafarijie wenye huzuni, alitufariji kwa kufika kwake Tito.

7 Lakini si kule kuja kwa Tito tu, bali pia kwa faraja mliyompa. Alitueleza jinsi mlivyonionea shauku, huzuni yenu kubwa na juhudi yenu kwa ajili yangu, ili kwamba furaha yangu ipate kuwa kubwa kuliko wakati wowote.

8 Hata kama niliwahuzunisha kwa barua yangu, sijutii. Ingawa nilijuta kwa muda mfupi, kwa kuwa najua kwamba barua yangu iliwaumiza, lakini ni kwa kitambo tu,

9 lakini sasa nina furaha, si kwa sababu mlihuzunika, bali kwa kuwa huzuni hiyo iliwafanya mtubu. Kwa maana mlihuzunishwa kama Mungu alivyokusudia watu wahuzunike na hivyo sisi hatukuwadhuru kwa njia yoyote.

10 Kwa maana huzuni ya kimungu huleta toba iletayo wokovu na wala haina majuto. Lakini huzuni ya kidunia husababisha mauti.

11 Tazameni jinsi huzuni hii ya kimungu ilivyoleta faida ndani yenu: bidii mliyo nayo, juhudi mliyofanya kujitetea, uchungu wenu, hofu yenu, upendo wenu, shauku yenu na jinsi mlivyokuwa tayari kutoa adhabu inayostahili. Kwa kila njia mmejithibitisha kuwa safi katika jambo hilo.

12 Hivyo ingawa niliwaandikia, haikuwa kwa sababu ya huyo aliyekosa au huyo aliyekosewa. Lakini nilitaka ninyi wenyewe mwone, mbele za Mungu, jinsi mlivyojitoa kwa ajili yetu.

13 Kwa ajili ya haya tumefarijika.

Zaidi ya kule sisi kutiwa moyo, tulifurahi sana kumwona Tito alivyo na furaha, kwa sababu roho yake imeburudishwa na ninyi nyote.

14 Nilikuwa nimewasifu ninyi kwake, nanyi hamkuniaibisha. Lakini kila kitu tulichowaambia ninyi, kilikuwa kweli, hivyo kule kujisifu kwetu kwa Tito kuwahusu ninyi kumethibitishwa kuwa kweli pia.

15 Upendo wake kwenu unaongezeka sana anapokumbuka jinsi mlivyokuwa watiifu, na kumpokea kwa hofu na kutetemeka.

16 Nafurahi kwamba ninaweza kuwatumaini ninyi kabisa.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2CO/7-ee01df6f73bfcd00096b70d6c901b279.mp3?version_id=1627—

Categories
2 Wakorintho

2 Wakorintho 8

Kutoa Kwa Ukarimu

1 Basi sasa ndugu, nataka ninyi mjue kuhusu ile neema ambayo Mungu amewapa makanisa ya Makedonia.

2 Pamoja na majaribu makali na taabu walizopata, furaha waliyokuwa nayo ilikuwa kubwa, ingawa walikuwa maskini kupindukia, kwa upande wao walifurika kwa wingi wa ukarimu.

3 Kwa maana nashuhudia kwamba wao walitoa kwa kadiri wawezavyo, hata na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe,

4 wakitusihi kwa bidii wapewe fursa ya kushiriki katika huduma hii ya kuwasaidia watakatifu.

5 Wala hawakufanya tulivyotazamia, bali walijitoa wao wenyewe kwa Bwana kwanza na ndipo wakajitoa kwa ajili yetu, kufuatana na mapenzi ya Mungu.

6 Kwa hiyo tulimsihi Tito, kwa kuwa ndiye alianzisha jambo hili, akamilishe tendo hili la neema kwa upande wenu.

7 Lakini kama vile mlivyo mbele sana katika yote: Katika imani, katika usemi, katika maarifa, katika uaminifu wote na katika upendo wenu kwetu sisi, vivyo hivyo tunataka pia mzidi katika neema hii ya kutoa.

8 Siwaamrishi, lakini nataka kujaribu unyofu wa upendo wenu kwa kuulinganisha na bidii ya wengine.

9 Kwa maana mnajua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba ingawa alikuwa tajiri, kwa ajili yenu alikubali kuwa maskini, ili kwa umaskini wake ninyi mpate kuwa matajiri.

10 Ushauri wangu kuhusu lile lililo bora kwenu juu ya jambo hili ni huu: Mwaka uliopita ninyi mlikuwa wa kwanza si tu kutoa lakini pia mlikuwa na shauku ya kufanya hivyo.

11 Sasa ikamilisheni kazi hii kwa shauku kama mlivyoanza, jitoleeni kulingana na uwezo wenu.

12 Kwa kuwa kama nia ya kutoa ipo, kitolewacho kinakubalika kulingana na kile mtu alicho nacho, wala si kwa kile ambacho hana.

13 Nia yetu si kwamba wengine wasaidike wakati ninyi mnateseka, bali pawe na uwiano.

14 Kwa wakati huu, wingi wa vitu mlivyo navyo usaidie kutosheleza mahitaji yao, ili wakati wao watakapokuwa na wingi wa vitu, nao wapate kutosheleza mahitaji yenu.

15 Ndipo patakuwa na usawa, kama ilivyoandikwa: “Aliyekusanya zaidi hakuwa na ziada, wala aliyekusanya kidogo hakupungukiwa.”

Tito Atumwa Korintho

16 Ninamshukuru Mungu ambaye amemtia Tito moyo wa kuwajali ninyi kama mimi ninavyowajali.

17 Si kwamba Tito amekubali tu ombi letu, bali anakuja kwenu akiwa na shauku kuliko wakati mwingine, tena kwa hiari yake mwenyewe.

18 Nasi tunamtuma pamoja naye ndugu ambaye anasifiwa na makanisa yote kwa huduma yake ya kuhubiri Injili.

19 Zaidi ya hayo, alichaguliwa na makanisa ili asafiri pamoja nasi tulipokuwa tunapeleka matoleo ya ukarimu, kwa ajili ya utukufu wa Bwana mwenyewe, na ili kuonyesha hisani yetu kuwasaidia.

20 Tunataka kuepuka lawama yoyote kuhusu jinsi tunavyosimamia matoleo haya ya ukarimu.

21 Kwa kuwa tunakusudia kufanya kile kilicho haki si machoni mwa Bwana peke yake, bali pia machoni mwa watu wengine.

22 Pamoja nao, tunamtuma ndugu yetu ambaye mara kwa mara ametuthibitishia kwa njia nyingi kwamba ana shauku, naam, zaidi sana sasa kwa sababu analo tumaini kuu kwenu.

23 Kwa habari ya Tito, yeye ni mwenzangu na mtendakazi pamoja nami miongoni mwenu. Kwa habari za ndugu zetu, wao ni wawakilishi wa makanisa, na utukufu kwa Kristo.

24 Kwa hiyo waonyesheni wazi hawa ndugu uthibitisho wa upendo wenu na sababu inayotufanya tujivune kwa ajili yenu, mbele ya makanisa, ili yapate kuona.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2CO/8-7dfa9218cbb988bf678b0483c6c19c43.mp3?version_id=1627—

Categories
2 Wakorintho

2 Wakorintho 9

Wasaidieni Wakristo Wenzenu

1 Hakuna haja yangu kuwaandikia kuhusu huduma hii itolewayo kwa ajili ya watakatifu.

2 Kwa kuwa ninajua mlivyo na shauku ya kusaidia, nami nimekuwa nikijivuna kwa ajili ya jambo hilo kwa watu wa Makedonia, nikiwaambia kuwa ninyi wa Akaya mmekuwa tayari kutoa tangu mwaka jana na shauku yenu imewachochea wengi wao katika kutoa.

3 Lakini sasa nawatuma hawa ndugu ili kujivuna kwetu kuhusu mchango wenu kusiwe maneno matupu, bali mpate kuwa tayari kama nilivyosema mngekuwa tayari.

4 Kwa maana kama nikija na Mmakedonia yeyote na kuwakuta hamjawa tayari, tutaona aibu kusema chochote juu yenu katika matoleo.

5 Kwa hivyo niliona ni muhimu niwahimize hawa ndugu watangulie kuja huko kwenu kabla yangu, wafanye mipango ya hayo matoleo ya ukarimu mliyokuwa mmeahidi, ili yawe tayari kama matoleo ya hiari wala si kama ya kutozwa kwa nguvu.

Kupanda Kwa Ukarimu

6 Kumbukeni kwamba: Yeyote apandaye kwa uchache pia atavuna kwa uchache, naye apandaye kwa ukarimu pia atavuna kwa ukarimu.

7 Kila mtu atoe kama anavyokusudia moyoni mwake, si kwa uchoyo au kwa kulazimishwa, kwa maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo mkunjufu.

8 Naye Mungu aweza kuwapa kila baraka kwa wingi, ili katika mambo yote kila wakati, mwe na kila kitu mnachohitaji, ili mweze kushiriki kwa wingi katika kila kazi njema.

9 Kama ilivyoandikwa:

“Ametawanya vipawa vyake kwa ukarimu

akawapa maskini;

haki yake hudumu milele.”

10 Yeye ampaye mpanzi mbegu kwa ajili ya kupanda na mkate kuwa chakula, atawapa na kuzizidisha mbegu zenu za kupanda na kuongeza mavuno ya haki yenu.

11 Mtatajirishwa kwa kila namna ili mpate kuwa wakarimu kila wakati, na kupitia kwetu, ukarimu wenu utamletea Mungu shukrani.

12 Huduma hii mnayofanya si tu kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya watakatifu, bali huzidi sana kwa shukrani nyingi apewazo Mungu.

13 Kwa sababu ya huduma ambayo mmejithibitisha wenyewe, watu watamtukuza Mungu kwa ajili ya utiifu ufuatanao na ukiri wenu wa Injili ya Kristo, na kwa ukarimu wenu wa kushiriki pamoja nao na pia wengine wote.

14 Nao katika maombi yao kwenu mioyo yao itawaonea shauku kwa sababu ya neema ipitayo kiasi mliyopewa na Mungu.

15 Ashukuriwe Mungu kwa karama yake isiyoelezeka.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2CO/9-81d751a0e9effc3a1acf18fca42f3c82.mp3?version_id=1627—