Categories
2 Samweli

2 Samweli 20

Sheba Aasi Dhidi Ya Daudi

1 Basi, kulikuwa na mtu mbaya sana aliyeitwa Sheba mwana wa Bikri, Mbenyamini, aliyekuwako huko. Akapiga tarumbeta na kupaza sauti,

“Hatuna fungu katika Daudi,

wala hatuna sehemu

katika mwana wa Yese!

Kila mtu aende hemani mwake,

enyi Israeli!”

2 Kwa hiyo watu wote wa Israeli wakamwacha Daudi na kumfuata Sheba mwana Bikri. Lakini watu wa Yuda wakawa karibu na mfalme wao katika safari yote kutoka Yordani mpaka Yerusalemu.

3 Daudi aliporudi katika jumba lake la kifalme huko Yerusalemu, aliwachukua wale masuria kumi aliokuwa amewaacha ili kuangalia jumba la kifalme na kuwaweka ndani ya nyumba chini ya ulinzi. Akawapa mahitaji yao lakini hakukutana nao kimwili. Waliwekwa kifungoni wakaishi kama wajane mpaka kifo chao.

4 Ndipo mfalme akamwambia Amasa, “Waite watu wa Yuda waje kwangu katika muda wa siku tatu, nawe mwenyewe uwepo hapa.”

5 Lakini Amasa alipokwenda kuwaita Yuda, alichukua muda mrefu zaidi ya ule mfalme aliokuwa amemwekea.

6 Daudi akamwambia Abishai, “Sasa Sheba mwana wa Bikri atatuletea madhara zaidi kuliko alivyofanya Absalomu. Wachukue watu wa bwana wako na umfuatie, la sivyo atapata mji wenye ngome na kututoroka.”

7 Hivyo watu wa Yoabu, na Wakerethi na Wapelethi, pamoja na wapiganaji mashujaa wote wakaondoka chini ya uongozi wa Abishai. Wakatoka Yerusalemu ili kumfuata Sheba mwana wa Bikri.

8 Wakati walikuwa kwenye mwamba mkubwa huko Gibeoni, Amasa alikuja kuwalaki. Yoabu alikuwa amevaa mavazi yake ya kijeshi; juu yake alifunga mkanda kwenye kiuno wenye upanga ndani ya ala. Alipokuwa akienda mbele, ule upanga ukaanguka kutoka kwenye ala.

9 Yoabu akamwambia Amasa, “U hali gani, ndugu yangu?” Kisha Yoabu akamshika Amasa ndevu kwa mkono wake wa kuume ili ambusu.

10 Amasa hakuona upanga uliokuwa mkononi mwa Yoabu, naye Yoabu akamchoma nao tumboni, nayo matumbo yake yakamwagika chini. Pasipo kuchomwa mara ya pili, Amasa akafa. Basi Yoabu na Abishai nduguye wakamfuatia Sheba mwana wa Bikri.

11 Mmoja wa watu wa Yoabu akasimama kando ya Amasa, akasema, “Yeyote ampendaye Yoabu na yeyote aliye upande wa Daudi, na amfuate Yoabu!”

12 Amasa alikuwa akigaagaa katika damu yake katikati ya barabara; mtu mmoja akaona kwamba vikosi vyote vilikuwa vinasimama pale. Huyo mtu alipotambua kwamba kila aliyefika pale Amasa alipokuwa alisimama, alimburuta Amasa kutoka barabarani mpaka kwenye shamba na kutupia nguo juu yake.

13 Baada ya Amasa kuondolewa kutoka barabarani, watu wote walienda pamoja na Yoabu kumfuatia Sheba mwana wa Bikri.

14 Sheba akapita katika makabila yote ya Israeli hadi Abel-Beth-Maaka na kupitia eneo lote la Waberi ambao walijikusanya pamoja na kumfuata.

15 Vikosi vyote vya Yoabu vikaja na kumhusuru Sheba mwana wa Bikri huko Abel-Beth-Maaka. Wakauzingira mji kwa kuweka vikosi vya askari, ili kukabiliana na ngome ya mji. Walipokuwa wanagongagonga ukuta ili kuubomoa na kuuangusha chini,

16 mwanamke mmoja mwenye busara akaita kutoka ndani ya mji, akisema, “Sikilizeni! Sikilizeni! Mwambieni Yoabu aje hapa ili niweze kuzungumza naye.”

17 Yoabu alikwenda mbele yake, akamuuliza, “Wewe ni Yoabu?”

Akamjibu, “Ndiye mimi.”

Yule mwanamke akamwambia, “Sikiliza kile mtumishi wako atakachokuambia.” Akamwambia, “Ninasikiliza.”

18 Huyo mwanamke akaendelea kusema, “Zamani za kale walikuwa wakisema, ‘Wakaulize ushauri huko Abeli,’ hivyo kulimaliza lile shauri.

19 Sisi ni watu wa amani na waaminifu katika Israeli. Wewe unajaribu kuharibu mji ambao ni mama katika Israeli. Kwa nini unataka kumeza urithi waBwana?”

20 Yoabu akajibu, “Hilo liwe mbali nami. Hilo liwe mbali nami kumeza au kuharibu.

21 Hivyo sivyo ilivyo. Mtu mmoja jina lake Sheba mwana wa Bikri, kutoka nchi ya vilima vya Efraimu, ameinua mkono wake dhidi ya mfalme, dhidi ya Daudi. Nikabidhini mtu huyu mmoja, nami nitajiondoa katika mji huu.”

Huyu mwanamke akamwambia Yoabu, “Kichwa chake mtatupiwa kupitia juu ya ukuta.”

22 Ndipo huyo mwanamke akaenda kwa watu wote akiwa na ushauri wake wa busara, nao wakakata kichwa cha Sheba mwana wa Bikri na kumtupia Yoabu. Kwa hiyo Yoabu akapiga tarumbeta, na watu wake wakatawanyika kutoka mjini, kila mmoja akirejea nyumbani kwake. Naye Yoabu akarudi kwa mfalme huko Yerusalemu.

23 Yoabu alikuwa jemadari wa jeshi lote la Israeli; Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa juu ya Wakerethi na Wapelethi;

24 Adoramu alikuwa kiongozi wa wale waliofanya kazi ya kulazimishwa; Yehoshafati mwana wa Ahiludi alikuwa mweka kumbukumbu;

25 Shevaalikuwa mwandishi; Sadoki na Abiathari walikuwa makuhani;

26 na Ira, Myairi, alikuwa kuhani wa Daudi.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2SA/20-08f49f6cf974d5c3a4940a80e19c4e38.mp3?version_id=1627—

Categories
2 Samweli

2 Samweli 21

Wagibeoni Walipiza Kisasi

1 Wakati wa utawala wa Daudi kulikuwa na njaa kwa miaka mitatu mfululizo, kwa hiyo Daudi akautafuta uso waBwana.Bwanaakasema, “Ni kwa sababu ya Sauli na nyumba yake iliyotiwa madoa ya damu, kwa sababu aliwaua Wagibeoni.”

2 Mfalme akawaita Wagibeoni na kuzumgumza nao. (Wagibeoni hawakuwa wa wana wa Israeli, ila walikuwa mabaki ya Waamori. Waisraeli walikuwa wameapa kuwaacha hai, lakini Sauli katika wivu wake kwa ajili ya Israeli na Yuda, alikuwa amejaribu kuwaangamiza.)

3 Daudi akawauliza Wagibeoni, “Niwatendee nini? Nitawaridhishaje ili mbariki urithi waBwana?”

4 Wagibeoni wakamjibu, “Hatuna haki ya kudai fedha wala dhahabu kutoka kwa Sauli au jamaa yake, wala hatuna haki ya kumuua mtu yeyote katika Israeli.”

Daudi akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?”

5 Wakamjibu mfalme, “Kwa habari ya mtu aliyetuangamiza na kufanya hila mbaya dhidi yetu ili kwamba tuangamizwe na tusiwe na yeyote katika Israeli,

6 tupatieni wazao wake saba wa kiume tuwaue hadharani mbele zaBwanahuko Gibea ya Sauli, aliyekuwa amechaguliwa naBwana.”

Basi mfalme akasema, “Nitawakabidhi kwenu.”

7 Mfalme akamhifadhi Mefiboshethi mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli, kwa sababu ya kile kiapo mbele zaBwanakati ya Daudi na Yonathani.

8 Lakini mfalme akamchukua Armoni na Mefiboshethi, wana wawili wa Rispa binti Aiya, ambao alikuwa amemzalia Sauli, pamoja na wana watano wa Merabu binti Sauli, aliokuwa amemzalia Adrieli mwana wa Barzilai, Mmeholathi.

9 Akawakabidhi kwa Wagibeoni, ambao waliwaua na kuwaweka wazi juu ya kilima mbele zaBwana. Wote saba walianguka kwa pamoja; waliuawa katika siku za kwanza za mavuno, mara tu uvunaji wa shayiri ulipokuwa unaanza.

10 Rispa binti Aiya akachukua nguo ya gunia, akajitandikia juu ya mwamba. Kuanzia mwanzo wa mavuno mpaka mvua ziliponyesha juu ya miili ya hao waliouawa, Rispa hakuruhusu ndege wa angani kuwagusa wakati wa mchana, wala wanyama wa mwitu wakati wa usiku.

11 Daudi alipoambiwa kile Rispa binti Aiya, suria wa Sauli, alichokuwa amekifanya,

12 alikwenda akachukua mifupa ya Sauli na mwanawe Yonathani kutoka kwa watu wa Yabeshi-Gileadi. (Walikuwa wameichukua kwa siri kutoka uwanja wa watu wote huko Beth-Shani, mahali ambapo Wafilisti walikuwa wamewatundika baada ya kumuua Sauli huko Gilboa.)

13 Daudi akaileta mifupa ya Sauli na ya mwanawe Yonathani kutoka huko, pia mifupa ya wale waliokuwa wameuawa na kutupwa ilikusanywa.

14 Wakazika mifupa ya Sauli na ya mwanawe Yonathani katika kaburi la Kishi, babaye Sauli, huko Sela katika nchi ya Benyamini, nao wakafanya kila kitu mfalme alichoagiza. Baada ya hayo, Mungu akajibu maombi kwa ajili ya nchi.

Vita Dhidi Ya Wafilisti

15 Kwa mara nyingine tena kulikuwa na vita kati ya Wafilisti na Israeli. Daudi akashuka pamoja na watu wake ili kupigana dhidi ya Wafilisti, naye akawa amechoka sana.

16 Naye Ishbi-Benobu, mmoja wa wazao wa Warefai,ambaye mkuki wake ulikuwa na uzito wa shekeli 300 za shaba,alikuwa amejifunga upanga mpya, naye alisema angemuua Daudi.

17 Lakini Abishai mwana wa Seruya akaja kumwokoa Daudi; akampiga huyo Mfilisti, akamwangusha chini na kumuua. Ndipo watu wakamwapia Daudi, wakisema, “Kamwe hutakwenda tena nasi vitani, ili kwamba taa ya Israeli isije ikazimwa.”

18 Baada ya muda, kukawa na vita nyingine na Wafilisti, huko Gobu. Wakati huo Sibekai, Mhushathi, akamuua Safu, mmoja wa wazao wa Warefai.

19 Katika vita vingine na Wafilisti huko Gobu, Elhanani mwana wa Yaare-Oregimu, Mbethlehemu, alimuua nduguye Goliathi, Mgiti, ambaye mkuki wake ulikuwa na mpini kama mti wa mfumaji.

20 Katika vita vingine tena, vilivyopiganwa huko Gathi, kulikuwako na mtu mmoja mkubwa mwenye vidole sita katika kila mkono na vidole sita kila mguu, jumla vidole ishirini na vinne. Yeye alikuwa pia mzao wa Mrefai.

21 Alipowadhihaki Israeli, Yonathani mwana wa Shimea, nduguye Daudi, akamuua.

22 Hawa wanne walikuwa wazao wa Warefai huko Gathi, nao walianguka kwa mikono ya Daudi na watu wake.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2SA/21-6722a002e0e884041c77ac5b23437da0.mp3?version_id=1627—

Categories
2 Samweli

2 Samweli 22

Wimbo Wa Daudi Wa Sifa

1 Daudi alimwimbiaBwanamaneno ya wimbo huu wakatiBwanaalipomwokoa mikononi mwa adui zake wote, na pia mkononi mwa Sauli.

2 Akasema:

“Bwanani mwamba wangu,

ngome yangu na mwokozi wangu,

3 Mungu wangu ni mwamba wangu,

ambaye kwake ninakimbilia,

ngao yangu na pembe ya wokovu wangu.

Yeye ni ngome yangu, kimbilio langu

na mwokozi wangu,

huniokoa kutoka kwa watu wenye jeuri.

4 NinamwitaBwana, anayestahili kusifiwa,

nami ninaokolewa kutoka kwa adui zangu.

5 “Mawimbi ya mauti yalinizunguka,

mafuriko ya maangamizi yalinilemea.

6 Kamba za kuzimuzilinizunguka,

mitego ya mauti ilinikabili.

7 Katika shida yangu nalimwitaBwana,

nilimlilia Mungu wangu.

Kutoka Hekaluni mwake alisikia sauti yangu,

kilio changu kikafika masikioni mwake.

8 “Dunia ilitetemeka na kutikisika,

misingi ya mbingu ikatikisika,

vilitetemeka kwa sababu

alikuwa amekasirika.

9 Moshi ukapanda kutoka puani mwake,

moto uteketezao ukatoka kinywani mwake,

makaa ya moto yawakayo

yakatoka ndani mwake.

10 Akazipasua mbingu akashuka chini,

mawingu meusi yalikuwa chini ya miguu yake.

11 Alipanda juu ya kerubi akaruka,

akapaa juu kwa mbawa za upepo.

12 Alifanya giza hema lake la kujifunika:

mawingu meusi ya mvua ya angani.

13 Kutokana na mwanga wa uwepo wake

mawingu yalisogea,

ikanyesha mvua ya mawe

na umeme wa radi.

14 Bwanaalinguruma kutoka mbinguni,

sauti ya Aliye Juu Sana ilisikika.

15 Aliipiga mishale na kutawanya adui,

umeme wa radi na kuwafukuza.

16 Mabonde ya bahari yalifunuliwa,

na misingi ya dunia ikawa wazi

kwa kukaripia kwakeBwana,

kwa uvumi wa pumzi kutoka puani mwake.

17 “Alinyoosha mkono kutoka juu na kunishika;

alinitoa kutoka kilindi cha maji makuu.

18 Aliniokoa kutoka adui wangu mwenye nguvu nyingi,

kutoka adui zangu waliokuwa na nguvu nyingi kuliko mimi.

19 Walinikabili siku ya msiba wangu,

lakiniBwanaalikuwa msaada wangu.

20 Alinileta nje mahali penye nafasi tele,

akaniokoa kwa kuwa alipendezwa nami.

21 “Bwanaalinitendea sawasawa na uadilifu wangu;

sawasawa na usafi wa mikono yangu amenilipa.

22 Kwa maana nimezishika njia zaBwana;

sijatenda ubaya nikamwacha Mungu wangu.

23 Sheria zake zote zi mbele yangu,

wala sijayaacha maagizo yake.

24 Nimekuwa sina hatia mbele zake,

nami nimejilinda nisitende dhambi.

25 Bwanaamenilipa sawasawa na uadilifu wangu,

sawasawa na usafi wangu machoni pake.

26 “Kwa yeye aliye mwaminifu unajionyesha kuwa mwaminifu,

kwa asiye na hatia unajionyesha kutokuwa na hatia,

27 kwa aliye mtakatifu unajionyesha kuwa mtakatifu,

lakini kwa aliyepotoka unajionyesha kuwa mkaidi.

28 Wewe huwaokoa wanyenyekevu,

lakini macho yako ni juu ya wenye kiburi

ili uwashushe.

29 Wewe ni taa yangu, EeBwana.

Bwanahulifanya giza langu

kuwa mwanga.

30 Kwa msaada wako naweza kushinda jeshi,

nikiwa pamoja na Mungu wangu

nitaweza kuruka ukuta.

31 “Kuhusu Mungu, njia yake ni kamilifu;

neno laBwanahalina dosari.

Yeye ni ngao kwa wote

wanaokimbilia kwake.

32 Kwa maana ni nani aliye Mungu

zaidi yaBwana?

Ni nani aliye Mwamba

isipokuwa Mungu wetu?

33 Mungu ndiye anivikaye nguvu

na kufanya njia yangu kuwa kamilifu.

34 Huifanya miguu yangu kama miguu ya kulungu,

huniwezesha kusimama mahali palipo juu.

35 Huifundisha mikono yangu kupigana vita;

mikono yangu inaweza kupinda upinde wa shaba.

36 Hunipa ngao yako ya ushindi,

unajishusha chini ili kuniinua.

37 Huyapanua mapito yangu,

ili miguu yangu isiteleze.

38 “Niliwafuatia adui zangu na nikawaseta,

sikurudi nyuma mpaka walipoangamizwa.

39 Niliwaseta kabisa, nao hawakuweza kuinuka tena;

walianguka chini ya miguu yangu.

40 Ulinivika nguvu kwa ajili ya kupigana vita;

uliwafanya adui zangu wasujudu miguuni pangu.

41 Uliwafanya adui zangu wageuke na kukimbia,

nami nikawaangamiza adui zangu.

42 Walipiga yowe, lakini hapakuwepo na yeyote wa kuwaokoa;

walimliliaBwana, lakini hakuwajibu.

43 Niliwaponda kama mavumbi ya nchi;

niliwaponda na kuwakanyaga kama tope barabarani.

44 “Umeniokoa kutokana na mashambulizi ya watu wangu;

umenihifadhi mimi kama kiongozi wa mataifa.

Watu ambao sikuwajua wananitumikia,

45 nao wageni huja wakininyenyekea,

mara wanisikiapo, hunitii.

46 Wote wanalegea,

wanatoka katika ngome zao wakitetemeka.

47 “Bwanayu hai! Sifa ni kwa Mwamba wangu!

Atukuzwe Mungu,

Mwamba, Mwokozi wangu!

48 Yeye ndiye Mungu anilipiziaye kisasi,

ayawekaye mataifa chini yangu,

49 aniwekaye huru toka kwa adui zangu.

Uliniinua juu ya adui zangu;

uliniokoa toka kwa watu wajeuri.

50 Kwa hiyo nitakusifu, EeBwana,

katikati ya mataifa;

nitaliimbia sifa jina lako.

51 Humpa mfalme wake ushindi mkuu;

huonyesha fadhili zake kwa mpakwa mafuta wake,

kwa Daudi na wazao wake milele.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2SA/22-29f734b8edeca81bc9fa9c69b32334a4.mp3?version_id=1627—

Categories
2 Samweli

2 Samweli 23

Maneno Ya Mwisho Ya Daudi

1 Haya ni maneno ya mwisho ya Daudi:

“Neno la Daudi mwana wa Yese,

neno la mtu aliyeinuliwa na Aliye Juu Sana,

mtu aliyepakwa mafuta na Mungu wa Yakobo,

mwimbaji wa nyimbo wa Israeli:

2 “Roho waBwanaalinena kupitia kwangu,

neno lake lilikuwa ulimini mwangu.

3 Mungu wa Israeli alinena,

mwamba wa Israeli akaniambia:

‘Mtu anatawala watu kwa haki,

wakati anapotawala

akiwa na hofu ya Mungu,

4 yeye ni kama mwanga wa asubuhi jua lichomozapo

asubuhi isiyo na mawingu,

kama mwanga baada ya mvua

uchipuzao majani kutoka ardhini.’

5 “Je, si hivyo ilivyo nyumba yangu

mbele za Mungu?

Je, hajafanya Agano la milele nami,

lililopangwa na kuimarishwa

kila sehemu?

Je, hatanifanya niufurahie wokovu wangu

na kunijalia matakwa yangu yote?

6 Lakini watu waovu wote

watatupwa kando kama miiba,

ambayo haikusanywi kwa mkono.

7 Yeyote agusaye miiba

hutumia chombo cha chuma

au mpini wa mkuki,

nayo huchomwa pale ilipo.”

Mashujaa Wa Daudi

8 Haya ndiyo majina ya mashujaa wa Daudi:

Yosheb-Bashebethi,Mtahkemoni, alikuwa kiongozi wa wale Watatu; yeye aliinua mkuki wake dhidi ya watu 800, ambao aliwaua katika pambano moja.

9 Wa pili wake alikuwa Eleazari mwana wa Dodai,Mwahohi. Akiwa mmojawapo wa wale mashujaa watatu, alikuwa pamoja na Daudi wakati waliwadhihaki Wafilisti waliokuwa wamekusanyika huko Pas-Damimu kwa ajili ya vita. Kisha watu wa Israeli wakarudi nyuma,

10 lakini yeye alisimama imara akawaua Wafilisti hadi mkono wake ukachoka na ukagandamana na upanga.Bwanaakawapa ushindi mkubwa siku ile. Vikosi vikarudi kwa Eleazari, kuteka tu nyara za waliokufa.

11 Aliyefuata alikuwa Shama mwana wa Agee, Mharari. Wafilisti walipokusanyika pamoja mahali palipokuwa shamba lililojaa dengu, vikosi vya Israeli viliwakimbia.

12 Lakini Shama akasimama imara katikati ya lile shamba. Akalitetea na kuwaua Wafilisti, nayeBwanaakawapa ushindi mkubwa.

13 Wakati wa mavuno, viongozi watatu kati ya viongozi thelathini walishuka, wakamwendea Daudi katika pango la Adulamu, wakati kikundi cha Wafilisti kilikuwa kimepiga kambi katika Bonde la Warefai.

14 Wakati huo Daudi alikuwa katika ngome, na kambi ya Wafilisti ilikuwa huko Bethlehemu.

15 Daudi akatamani maji, akasema, “Laiti mtu angenipatia maji ya kunywa kutoka kisima kilicho karibu na lango la Bethlehemu!”

16 Basi mashujaa hao watatu wakapenya katikati ya Wafilisti, wakaenda kuchota maji kutoka kwa kisima kilicho karibu na lango la Bethlehemu, wakamletea Daudi. Lakini Daudi akakataa kuyanywa. Badala yake, aliyamimina mbele zaBwana.

17 Akasema, “Iwe mbali nami, EeBwana, kufanya kitu hiki. Je, hii si damu ya watu ambao walikwenda kwa kuhatarisha maisha yao?” Naye Daudi hakuyanywa.

Haya yalifanywa na hao mashujaa watatu.

18 Abishai ndugu yake Yoabu mwana wa Seruya ndiye alikuwa kiongozi wa hao Watatu. Aliinua mkuki wake dhidi ya watu 300 ambao aliwaua, kwa hiyo naye akawa na sifa kama hao Watatu.

19 Je, hakupata heshima kubwa zaidi kuliko hao Watatu? Alikuwa jemadari wao, ingawa hakuhesabiwa miongoni mwao.

20 Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa mpiganaji hodari kutoka Kabseeli ambaye alifanya mambo makubwa ya ujasiri. Aliwaua mashujaa wawili waliokuwa hodari kuliko wote wa Moabu. Pia alishuka shimoni kulipokuwa na theluji na kumuua simba.

21 Pia alimuua Mmisri mrefu mkubwa. Ingawa Mmisri alikuwa na mkuki mkononi mwake, Benaya alimwendea akiwa na rungu. Alipokonya mkuki kutoka mkononi mwa Mmisri na kumuua kwa mkuki wake mwenyewe.

22 Haya yalikuwa mambo ya ushujaa ya Benaya mwana wa Yehoyada; naye pia alikuwa maarufu kama wale mashujaa watatu.

23 Yeye aliheshimiwa zaidi ya wale Thelathini, lakini hakujumuishwa miongoni mwa wale Watatu. Daudi akamweka kuwa kiongozi wa walinzi wake.

24 Miongoni mwa wale Thelathini walikuwepo:

Asaheli ndugu wa Yoabu;

Elhanani mwana wa Dodo kutoka Bethlehemu;

25 Shama, Mharodi;

Elika, Mharodi;

26 Helesi, Mpalti;

Ira mwana wa Ikeshi kutoka Tekoa;

27 Abiezeri kutoka Anathothi;

Mebunai, Mhushathi;

28 Salmoni, Mwahohi;

Maharai, Mnetofathi;

29 Heledi mwana wa Baana, Mnetofathi;

Itai mwana wa Ribai kutoka Gibea ya Benyamini;

30 Benaya Mpirathoni;

Hidai kutoka mabonde ya Gaashi;

31 Abi-Alboni, Mwaribathi;

Azmawethi, Mbarhumi;

32 Eliaba, Mshaalboni;

wana wa Yasheni;

Yonathani

33 mwana wa Shama, Mharari;

Ahiamu mwana wa Sharari, Mharari;

34 Elifeleti mwana wa Ahasbai, Mmaakathi;

Eliamu mwana wa Ahithofeli, Mgiloni;

35 Hezro, Mkarmeli;

Paarai, Mwarbi;

36 Igali mwana wa Nathani kutoka Soba;

Bani, Mgadi;

37 Seleki, Mwamoni;

Naharai, Mbeerothi, aliyekuwa mbeba silaha za Yoabu mwana wa Seruya;

38 Ira, Mwithiri;

Garebu, Mwithiri;

39 na Uria, Mhiti.

Jumla yao wote walikuwa watu thelathini na saba.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2SA/23-1c34637ed3ddd6c0e20b9a7fc9ee6bca.mp3?version_id=1627—

Categories
2 Samweli

2 Samweli 24

Daudi Ahesabu Wapiganaji

1 Hasira yaBwanaikawaka tena dhidi ya Israeli, naye akamchochea Daudi dhidi yao, akisema, “Nenda ukawahesabu Israeli na Yuda.”

2 Kwa hiyo mfalme akamwambia Yoabu, pamoja na majemadari wa jeshi aliokuwa nao, “Nendeni kwa makabila yote ya Israeli kuanzia Dani hadi Beer-Sheba na mwandikishe watu wapiganaji, ili niweze kujua idadi yao.”

3 Lakini Yoabu akamjibu mfalme, “BwanaMungu wako na azidishe jeshi mara mia, nayo macho ya bwana wangu mfalme na yaone hili. Lakini kwa nini bwana wangu mfalme anataka kufanya kitu cha namna hii?”

4 Hata hivyo, neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu pamoja na majemadari wa jeshi, kwa hiyo wakaondoka mbele ya mfalme kuandikisha wapiganaji wa Israeli.

5 Baada ya kuvuka Yordani, walipiga kambi karibu na Aroeri, kusini ya mji ulioko kwenye bonde jembamba, ndipo wakipitia Gadi, wakaenda hadi Yazeri.

6 Walikwenda hadi Gileadi na pia eneo la Tahtimu-Hodshi, wakaendelea hadi Dani-Yaani na kuzunguka kuelekea Sidoni.

7 Kisha wakaenda kuelekea ngome ya Tiro pamoja na miji yote ya Wahivi na ya Wakanaani. Mwishoni, walikwenda mpaka Beer-Sheba katika Negebu ya Yuda.

8 Baada ya kupita katika nchi nzima, walirudi Yerusalemu baada ya miezi tisa na siku ishirini.

9 Yoabu akatoa hesabu ya wapiganaji kwa mfalme: Katika Israeli kulikuwako watu 800,000 wenye uwezo wa kupigana, na katika Yuda watu 500,000.

10 Dhamiri ya Daudi ilishtuka baada ya kuwahesabu wapiganaji, naye akamwambiaBwana, “Nimefanya dhambi kubwa kwa kufanya jambo hili. EeBwana, sasa ninakusihi, ondoa hatia ya mtumishi wako. Nimefanya jambo la kipumbavu sana.”

11 Kabla Daudi hajaamka kesho yake asubuhi, neno laBwanalilikuwa limemjia Gadi nabii, aliyekuwa mwonaji wa Daudi, kusema:

12 “Nenda ukamwambie Daudi, ‘Hivi ndivyo asemavyoBwana: Ninakupa wewe uchaguzi wa mambo matatu. Nichagulie mojawapo nitakalotenda dhidi yako.’ ”

13 Basi Gadi akaenda kwa Daudi na kumwambia, “Je, ije njaa ya miaka mitatu katika nchi yako? Au miezi mitatu ya kukimbia adui zako wakikufuatia? Au siku tatu za tauni katika nchi yako? Basi sasa, fikiri juu ya hilo na uamue jinsi nitakavyomjibu huyo aliyenituma.”

14 Daudi akamjibu Gadi, “Nitataabika sana. Afadhali tuangukie mikononi mwaBwana, kwa maana rehema zake ni kuu, lakini usiniache nianguke mikononi mwa wanadamu.”

15 BasiBwanaakatuma tauni katika Israeli kuanzia asubuhi mpaka mwisho wa muda ulioamriwa, wakafa watu 70,000 kuanzia Dani hadi Beer-Sheba.

16 Malaika aliponyoosha mkono wake ili kuangamiza Yerusalemu,Bwanaakahuzunika kwa sababu ya maafa, akamwambia yule malaika aliyekuwa anawadhuru watu, “Yatosha! Rudisha mkono wako.” Wakati huo malaika waBwanaalikuwa kwenye sakafu ya kupuria ya Arauna,Myebusi.

17 Ikawa Daudi alipomwona huyo malaika aliyekuwa akiwaua watu, akamwambiaBwana, “Mimi ndiye niliyetenda dhambi na kukosa. Hawa ni kondoo tu. Wamefanya nini? Mkono wako uwe juu yangu na nyumba yangu.”

Daudi Ajenga Madhabahu

18 Siku hiyo Gadi akamwendea Daudi na kumwambia, “Panda ukamjengeeBwanamadhabahu kwenye sakafu ya kupuria ya Arauna Myebusi.”

19 Kwa hiyo Daudi akakwea kama vileBwanaalivyokuwa ameamuru kwa kinywa cha Gadi.

20 Arauna alipotazama na kumwona mfalme na watu wake wakija kumwelekea, alitoka nje na kusujudu mbele ya mfalme kifudifudi, akiuinamisha uso wake ardhini.

21 Arauna akasema, “Mbona bwana wangu mfalme amekuja kwa mtumishi wake?”

Daudi akajibu, “Kununua sakafu yako ya kupuria, ili niweze kumjengeaBwanamadhabahu, ili tauni iliyo katika watu iondolewe.”

22 Arauna akamwambia Daudi, “Bwana wangu mfalme na achukue chochote kinachompendeza na akitoe sadaka. Hapa kuna maksai kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, pia kuna miti ya kupuria na nira za ngʼombe kwa ajili ya kuni.

23 Ee mfalme, Arauna anatoa vyote hivi kwa mfalme.” Pia Arauna akamwambia mfalme, “BwanaMungu wako na akukubali.”

24 Lakini mfalme akamjibu Arauna, “La hasha, nasisitiza kuvilipia. Sitatoa sadaka ya kuteketezwa kwaBwanaMungu wangu isiyonigharimu chochote.”

Kwa hiyo Daudi akanunua ile sakafu ya kupuria nafaka na maksai, akazilipia shekeli hamsini za fedha.

25 Kisha Daudi akamjengeaBwanamadhabahu mahali hapo, na kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. KishaBwanaakajibu kwa ajili ya nchi, nayo tauni ikakoma katika Israeli.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2SA/24-5ca31c9044d4e6473c118c288a2e9c90.mp3?version_id=1627—