Categories
1 Wakorintho

1 Wakorintho Utangulizi

Utangulizi

Korintho ulikuwa mji uliojengwa pwani ya Mediterania (Bahari Kuu). Mji huu ulistawi kwani ulikuwa kituo kikuu cha biashara. Ulikuwa koloni la Kirumi, ukiwavutia wakazi wa mataifa mbalimbali, wakiwemo Warumi, Wayunani na Wayahudi kutoka sehemu zilizoizunguka Bahari Kuu. Mchanganyiko huu wa wakazi ulisababisha kuharibika na kuzorota kwa maadili.

Paulo alianzisha kanisa katika mji wa Korintho katika safari yake ya pili ya kitume, akakaa huko kwa muda wa mwaka mmoja na nusu. Aliondoka Korintho akifuatana na Prisila na Akila kwenda Efeso, na kutoka huko alitembelea kanisa la Yerusalemu, na baadaye akarudi Antiokia. Paulo alipokea habari kutoka kwa nyumba ya Kloe kwamba kanisa lilikuwa limegawanyika. Paulo aliona ni muhimu awaandikie waraka huu ili kujibu matatizo mengi yaliyojitokeza. Aliposhughulikia matatizo haya moja kwa moja, Paulo alifafanua misingi ya mafundisho ya Kikristo kuhusu imani na maadili.

Mwandishi

Mtume Paulo.

Kusudi

Kusahihisha makosa dhahiri katika kanisa la Korintho, na pia kuwaelimisha waumini jinsi ya kumtumikia Kristo katika jamii iliyokosa maadili.

Mahali

Efeso.

Tarehe

Kama mwaka wa 55 B.K.

Wahusika Wakuu

Paulo, Timotheo, nyumba ya Kloe, waumini wa Korintho.

Wazo Kuu

Umuhimu wa mwenendo wa Mkristo kufanana na Kristo.

Mambo Muhimu

Suluhisho za matatizo mbalimbali kama: ugomvi kanisani, uzinzi, kushtakiana, mabishano juu ya ndoa, chakula kilichotolewa kwa sanamu, hali ya Paulo kuwa mtume, matumizi mabaya ya Meza ya Bwana, ukweli kuhusu ufufuo, n.k. Lazima mwenendo wa Mkristo ufanane na ule wa Kristo; kukosa kufanya hivyo ni kumwaibisha Kristo na kanisa lake.

Mgawanyo

Salamu za Paulo (

1:1-9

)

Tatizo la mgawanyiko katika kanisa (

1:10–4:21

)

Tatizo la zinaa katika kanisa (

5:1-13

)

Tatizo la kushtakiana mahakamani (

6:1-11

)

Tatizo la uasherati (

6:12-20

)

Tatizo juu ya ndoa (

7:1-40

)

Matatizo kuhusu ibada za sanamu (

8:1–11:1

)

Matatizo kuhusu Meza ya Bwana na ibada (

11:2–14:40

)

Matatizo kuhusu ufufuo wa wafu (

15:1-58

)

Mawaidha ya mwisho (

16:1-24

).

Categories
1 Wakorintho

1 Wakorintho 1

Salamu

1 Paulo, niliyeitwa kwa mapenzi ya Mungu kuwa mtume wa Kristo Yesu, na Sosthene ndugu yetu.

2 Kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, kwa wale waliotakaswa katika Kristo Yesu na walioitwa kuwa watakatifu, pamoja na wale wote ambao kila mahali wanaliitia Jina la Kristo Yesu Bwana wetu, aliye Bwana wao na wetu pia:

3 Neema na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo iwe nanyi.

Shukrani

4 Ninamshukuru Mungu siku zote kwa ajili yenu kwa sababu ya neema yake mliyopewa katika Kristo Yesu.

5 Kwa kuwa katika Kristo mmetajirishwa kwa kila hali, katika kusema kwenu na katika maarifa yenu yote,

6 kwa sababu ushuhuda wetu kumhusu Kristo ulithibitishwa ndani yenu.

7 Kwa hiyo hamkupungukiwa na karama yoyote ya kiroho wakati mnangoja kwa shauku kudhihirishwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo.

8 Atawafanya imara mpaka mwisho, ili msiwe na hatia siku ile ya Bwana wetu Yesu Kristo.

9 Mungu ambaye mmeitwa naye ili mwe na ushirika na Mwanawe Yesu Kristo, Bwana wetu ni mwaminifu.

Mgawanyiko Ndani Ya Kanisa

10 Nawasihi ndugu zangu, katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi, ili pasiwepo na matengano katikati yenu na kwamba mwe na umoja kikamilifu katika nia na katika kusudi.

11 Ndugu zangu, nimepata habari kutoka kwa baadhi ya watu wa nyumbani mwa Kloe kwamba kuna magomvi katikati yenu.

12 Maana yangu ni kwamba: Mmoja wenu husema, “Mimi ni wa Paulo”; mwingine, “Mimi ni wa Apolo”; mwingine, “Mimi ni wa Kefa,”na mwingine, “Mimi ni wa Kristo.”

13 Je, Kristo amegawanyika? Je, Paulo ndiye alisulubishwa kwa ajili yenu? Je, mlibatizwa kwa jina la Paulo?

14 Nashukuru kwamba sikumbatiza mtu yeyote isipokuwa Krispo na Gayo.

15 Kwa hiyo hakuna mtu yeyote anayeweza kusema kwamba alibatizwa kwa jina langu.

16 (Naam, niliwabatiza pia watu wa nyumbani mwa Stefana. Lakini zaidi ya hao sijui kama nilimbatiza mtu mwingine yeyote.)

17 Kwa maana Kristo hakunituma ili kubatiza bali kuhubiri Injili; sio kwa maneno ya hekima ya kibinadamu, ili msalaba wa Kristo usije ukakosa nguvu yake.

Kristo Ni Hekima Na Nguvu Ya Mungu

18 Kwa maana ujumbe wa msalaba kwa wale wanaopotea ni upuzi, lakini kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu.

19 Kwa maana imeandikwa:

“Nitaiharibu hekima ya wenye hekima,

na kubatilisha akili ya wenye akili.”

20 Yuko wapi mwenye hekima? Yuko wapi msomi? Yuko wapi mwanafalsafa wa nyakati hizi? Je, Mungu hakufanya hekima ya ulimwengu huu kuwa upumbavu?

21 Kwa kuwa katika hekima ya Mungu, ulimwengu kwa hekima yake haukumjua yeye, ilimpendeza Mungu kuwaokoa wale walioamini kwa upuzi wa lile neno lililohubiriwa.

22 Wayahudi wanadai ishara za miujiza na Wayunani wanatafuta hekima.

23 Lakini sisi tunamhubiri Kristo aliyesulubiwa: yeye kwa Wayahudi ni kikwazo na kwa Wayunani ni upuzi.

24 Lakini kwa wale ambao Mungu amewaita, Wayahudi na pia Wayunani, Kristo ndiye nguvu ya Mungu na pia hekima ya Mungu.

25 Kwa maana upumbavu wa Mungu una hekima zaidi kuliko hekima ya wanadamu, nao udhaifu wa Mungu una nguvu kuliko nguvu ya wanadamu.

26 Ndugu zangu, kumbukeni mlivyokuwa mlipoitwa. Kwa kipimo cha kibinadamu, si wengi wenu mliokuwa na hekima. Si wengi mliokuwa na ushawishi, si wengi mliozaliwa katika jamaa zenye vyeo.

27 Lakini Mungu alivichagua vitu vipumbavu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye hekima, Mungu alivichagua vitu dhaifu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye nguvu.

28 Alivichagua vitu vya chini na vinavyodharauliwa vya dunia hii, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko,

29 ili mtu yeyote asijisifu mbele zake.

30 Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanyika kwetu hekima itokayo kwa Mungu, yaani haki, na utakatifu na ukombozi.

31 Hivyo, kama ilivyoandikwa: “Yeye ajisifuye na ajisifu katika Bwana.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1CO/1-5f6dbac1c09057b91f50cfd908d59939.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Wakorintho

1 Wakorintho 2

Kumtangaza Kristo Aliyesulubiwa

1 Ndugu zangu nilipokuja kwenu, sikuja na maneno ya ushawishi wala hekima ya hali ya juu nilipowahubiria siri ya Mungu.

2 Kwa kuwa niliamua kutokujua kitu chochote wakati nikiwa nanyi isipokuwa Yesu Kristo aliyesulubiwa.

3 Mimi nilikuja kwenu nikiwa dhaifu na mwenye hofu na kwa kutetemeka sana.

4 Kuhubiri kwangu na ujumbe wangu haukuwa kwa hekima na maneno ya ushawishi bali kwa madhihirisho ya nguvu za Roho

5 ili imani yenu isiwe imejengwa katika hekima ya wanadamu bali katika nguvu za Mungu.

Hekima Ya Kweli Itokayo Kwa Mungu

6 Lakini miongoni mwa watu waliokomaa twanena hekima, wala si hekima ya ulimwengu huu au ya watawala wa dunia hii wanaobatilika.

7 Sisi tunanena hekima ya Mungu ambayo ni siri, tena iliyofichika, ambayo Mungu aliikusudia kabla ya ulimwengu kuwepo, kwa ajili ya utukufu wetu.

8 Hakuna hata mtawala mmoja wa nyakati hizi aliyeelewa jambo hili. Kwa maana kama wangelielewa, wasingemsulubisha Bwana wa utukufu.

9 Lakini ni kama ilivyoandikwa:

“Hakuna jicho limepata kuona,

wala sikio limepata kusikia,

wala hayakuingia moyoni wowote,

yale Mungu amewaandalia

wale wampendao”:

10 Lakini mambo haya Mungu ametufunulia kwa Roho wake.

Roho huchunguza kila kitu, hata mambo ya ndani sana ya Mungu.

11 Kwa maana ni nani anayejua mawazo ya mtu isipokuwa roho iliyo ndani ya huyo mtu? Vivyo hivyo hakuna mtu ajuaye mawazo ya Mungu isipokuwa Roho wa Mungu.

12 Basi hatukupokea roho ya dunia bali Roho atokaye kwa Mungu, ili tuweze kuelewa kile kipawa ambacho Mungu ametupatia bure.

13 Haya ndiyo tusemayo, si kwa maneno tuliyofundishwa kwa hekima ya wanadamu bali kwa maneno tuliyofundishwa na Roho, tukifafanua kweli za kiroho kwa maneno ya kiroho.

14 Mtu ambaye hana Roho hawezi kupokea mambo yatokayo kwa Roho wa Mungu, kwa kuwa ni upuzi kwake, naye hawezi kuyaelewa kwa sababu hayo yanaeleweka tu kwa upambanuzi wa rohoni.

15 Mtu wa kiroho hubainisha mambo yote, lakini yeye mwenyewe habainishwi na mtu yeyote.

16 “Kwa maana ni nani aliyefahamu mawazo ya Bwana

ili apate kumfundisha?”

Lakini sisi tunayo mawazo ya Kristo.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1CO/2-019a5eb9aac018c4124ae9e76d9aafcf.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Wakorintho

1 Wakorintho 3

Kuhusu Mgawanyiko Katika Kanisa

1 Ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama watu wa kiroho, bali kama watu wa mwilini, kama watoto wachanga katika Kristo.

2 Naliwanywesha maziwa, wala si chakula kigumu, kwa kuwa hamkuwa tayari kwa hicho chakula. Naam, hata sasa hamko tayari.

3 Ninyi bado ni watu wa mwilini. Kwa kuwa bado kuna wivu na magombano miongoni mwenu, je, ninyi si watu wa mwilini? Je, si mwaendelea kama watu wa kawaida?

4 Kwa maana mmoja anaposema, “Mimi ni wa Paulo,” na mwingine, “Mimi ni wa Apolo,” je, ninyi si wanadamu wa kawaida?

5 Kwani, Apolo ni nani? Naye Paulo ni nani? Ni watumishi tu ambao kupitia wao mliamini, kama vile Bwana alivyompa kila mtu huduma yake.

6 Mimi nilipanda mbegu, Apolo akatia maji, lakini Mungu ndiye aliikuza.

7 Hivyo mwenye kupanda na mwenye kutia maji si kitu, bali Mungu peke yake ambaye huifanya ikue.

8 Apandaye mbegu ana lengo sawa na yule atiaye maji na kila mmoja atalipwa kulingana na kazi yake.

9 Kwa kuwa sisi tu watendakazi pamoja na Mungu. Ninyi ni shamba la Mungu, jengo la Mungu.

10 Kwa neema Mungu aliyonipa, niliweka msingi kama mjenzi stadi na mtu mwingine anajenga juu yake. Lakini kila mmoja inampasa awe mwangalifu jinsi anavyojenga.

11 Kwa maana hakuna mtu yeyote awezaye kuweka msingi mwingine wowote isipokuwa ule uliokwisha kuwekwa, ambao ni Yesu Kristo.

12 Kama mtu yeyote akijenga juu ya msingi huu kwa kutumia dhahabu, fedha, vito vya thamani, miti, majani au nyasi,

13 kazi yake itaonekana ilivyo, kwa kuwa Siku ile itaidhihirisha. Itadhihirishwa kwa moto, nao moto utapima ubora wa kazi ya kila mtu.

14 Kama kile alichojenga kitabaki, atapokea thawabu yake.

15 Kama kazi kitateketea, atapata hasara, ila yeye mwenyewe ataokolewa, lakini tu kama mtu aliyenusurika kwenye moto.

16 Je, hamjui ya kwamba ninyi wenyewe ni hekalu la Mungu na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?

17 Kama mtu yeyote akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamwangamiza; kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, na ninyi ndiyo hilo hekalu.

18 Msijidanganye. Kama mtu yeyote miongoni mwenu akidhani kuwa ana hekima kwa viwango vya dunia hii, inampasa awe mjinga ili apate kuwa na hekima.

19 Kwa maana hekima ya ulimwengu huu ni upuzi mbele za Mungu. Kama ilivyoandikwa: “Mungu huwanasa wenye hekima katika hila yao,”

20 tena, “Bwana anajua kwamba mawazo ya wenye hekima ni ubatili.”

21 Hivyo basi, mtu asijivune kuhusu wanadamu! Vitu vyote ni vyenu,

22 ikiwa ni Paulo au Apolo au Kefaau dunia au uzima au mauti, au wakati uliopo au wakati ujao, haya yote ni yenu

23 na ninyi ni wa Kristo, naye Kristo ni wa Mungu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1CO/3-460093c974171613041a242f57f32e09.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Wakorintho

1 Wakorintho 4

Mawakili Wa Siri Za Mungu

1 Basi, watu na watuhesabu sisi kuwa tu watumishi wa Kristo na mawakili wa siri za Mungu.

2 Tena, litakiwalo ni mawakili waonekane kuwa waaminifu.

3 Lakini kwangu mimi ni jambo dogo sana kwamba nihukumiwe na ninyi au na mahakama yoyote ya kibinadamu. Naam, hata mimi mwenyewe sijihukumu.

4 Dhamiri yangu ni safi, lakini hilo halinihesabii kuwa asiye na hatia. Bwana ndiye anihukumuye.

5 Kwa hiyo msihukumu jambo lolote kabla ya wakati wake. Ngojeni mpaka Bwana atakapokuja. Yeye atayaleta nuruni mambo yale yaliyofichwa gizani, na kuweka wazi nia za mioyo ya wanadamu. Wakati huo kila mmoja atapokea sifa anayostahili kutoka kwa Mungu.

6 Basi ndugu zangu, mambo haya nimeyafanya kwangu binafsi na Apolo kwa faida yenu, ili mweze kujifunza kutoka kwetu maana ya ule usemi usemao, “Msivuke zaidi ya yale yaliyoandikwa.” Hivyo hamtajivunia mtu fulani na kumdharau mwingine.

7 Kwa maana ni nani aliyewafanya kuwa tofauti na wengine? Ni nini mlicho nacho ambacho hamkupokea? Nanyi kama mlipokea, kwa nini mnajivuna kama vile hamkupokea?

8 Sasa tayari mnayo yale yote mnayohitaji! Tayari mmekwisha kuwa matajiri! Mmekuwa wafalme, tena bila sisi! Laiti mngekuwa wafalme kweli ili na sisi tupate kuwa wafalme pamoja nanyi!

9 Kwa maana ninaona kwamba Mungu ametuweka sisi mitume katika nafasi ya mwisho kabisa, kama watu waliohukumiwa kufa kwenye uwanja wa tamasha, kwa sababu tumefanywa kuwa maonyesho kwa ulimwengu wote, kwa malaika na kwa wanadamu pia.

10 Kwa ajili ya Kristo sisi ni wajinga, lakini ninyi mna hekima sana ndani ya Kristo. Sisi tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu. Tunadharauliwa, lakini ninyi mnaheshimiwa.

11 Mpaka saa hii tuna njaa na kiu, tu uchi, tumepigwa na hatuna makao.

12 Tunafanya kazi kwa bidii kwa mikono yetu wenyewe. Tunapolaaniwa, tunabariki, tunapoteswa, tunastahimili,

13 tunaposingiziwa, tunajibu kwa upole. Mpaka sasa tumekuwa kama takataka ya dunia na uchafu wa ulimwengu.

14 Siwaandikii mambo haya ili kuwaaibisha, bali ili kuwaonya, kama wanangu wapendwa.

15 Hata kama mnao walimu 10,000 katika Kristo, lakini hamna baba wengi. Mimi nilikuwa baba yenu katika Kristo Yesu kwa kuwaletea Injili.

16 Basi nawasihi igeni mfano wangu.

17 Kwa sababu hii ninamtuma Timotheo, mwanangu mpendwa na mwaminifu katika Bwana. Yeye atawakumbusha kuhusu njia za maisha yangu katika Kristo Yesu, ambayo yanakubaliana na mafundisho yangu ninayofundisha katika kila kanisa.

18 Baadhi yenu mmekuwa na jeuri mkidhani kuwa sitafika kwenu.

19 Lakini kama Bwana akipenda, nitafika kwenu mapema, nami nitapenda kujua, si tu kile wanachosema hawa watu jeuri, bali pia kujua nguvu yao.

20 Kwa kuwa Ufalme wa Mungu si maneno matupu tu bali ni nguvu.

21 Ninyi amueni. Je, nije kwenu na fimbo, au nije kwa upendo na kwa roho ya upole?

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1CO/4-62bb6e9537f1f502f485c8872c8c1a9b.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Wakorintho

1 Wakorintho 5

Mwasherati Atengwe

1 Yamkini habari imeenea ya kuwa miongoni mwenu kuna uzinzi ambao haujatokea hata miongoni mwa watu wasiomjua Mungu: Kwamba mtu anaishi na mke wa baba yake.

2 Nanyi mwajivuna! Je, haiwapasi kuhuzunika na kumtenga na ushirika wenu mtu huyo aliyefanya mambo hayo?

3 Hata kama siko pamoja nanyi katika mwili, niko nanyi katika roho. Nami nimekwisha kumhukumu mtu huyo aliyetenda jambo hili, kama vile ningekuwepo.

4 Mnapokutana katika Jina la Bwana wetu Yesu nami nikiwepo pamoja nanyi katika roho na uweza wa Bwana Yesu ukiwepo,

5 mkabidhini mtu huyu kwa Shetani, ili mwili wake uharibiwe, ili roho yake iokolewe katika siku ya Bwana.

6 Majivuno yenu si mazuri. Je, hamjui ya kwamba chachu kidogo huchachusha donge zima la unga?

7 Ondoeni chachu ya kale ili mpate kuwa donge jipya lisilotiwa chachu, kama vile mlivyo. Kwa maana Kristo, Mwana-Kondoo wetu wa Pasaka amekwisha tolewa kuwa dhabihu.

8 Kwa hiyo, tusiiadhimishe sikukuu hii, kwa chachu ya zamani, chachu ya nia mbaya na uovu, bali kwa mkate usiotiwa chachu, ndio weupe wa moyo na kweli.

9 Niliwaandikia katika waraka wangu kuwa msishirikiane na wazinzi.

10 Sina maana kwamba msishirikiane na wazinzi wa ulimwengu huu, au wenye tamaa mbaya, wanyangʼanyi au waabudu sanamu. Kwa kufanya hivyo ingewalazimu mtoke ulimwenguni humu.

11 Lakini sasa nawaandikia kwamba msishirikiane na mtu yeyote anayejiita ndugu, hali akiwa ni mzinzi, au mwenye tamaa mbaya, mwabudu sanamu au msingiziaji, mlevi au mdhalimu. Mtu kama huyo hata msile naye.

12 Yanihusu nini kuwahukumu wale watu walio nje ya kanisa? Je, si mnapaswa kuwahukumu hao walio ndani?

13 Mungu atawahukumu hao walio nje. “Ninyi mwondoeni huyo mtu mwovu miongoni mwenu.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1CO/5-644ab093b6c61743e90dea0d28969c66.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Wakorintho

1 Wakorintho 6

Kushtakiana Miongoni Mwa Waumini

1 Kama mtu yeyote wa kwenu ana ugomvi na mwenzake, anathubutuje kuupeleka kwa wasiomcha Mungu ili kuamuliwa badala ya kuupeleka kwa watakatifu?

2 Je, hamjui kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Nanyi kama mtauhukumu ulimwengu, je, hamwezi kuamua mambo madogo madogo?

3 Hamjui kwamba tutawahukumu malaika? Je, si zaidi mambo ya maisha haya?

4 Kwa hiyo kama kuna ugomvi miongoni mwenu kuhusu mambo kama haya, chagueni kuwa waamuzi, watu ambao wanaonekana hata sio wa heshima katika kanisa.

5 Nasema hivi ili mwone aibu. Je, inawezekana kuwa miongoni mwenu hakuna mtu mwenye hekima ya kutosha kuamua ugomvi kati ya waaminio?

6 Badala yake ndugu mmoja anampeleka mwenzake mahakamani, tena mbele ya watu wasioamini!

7 Huko kuwa na mashtaka miongoni mwenu ina maana kwamba tayari ni kushindwa kabisa. Kwa nini msikubali kutendewa mabaya? Kwa nini msikubali kunyangʼanywa?

8 Badala yake, ninyi wenyewe mwadanganya na kutenda mabaya, tena mwawatendea ndugu zenu.

9 Je, hamjui kwamba wasio haki hawataurithi Ufalme wa Mungu? Msidanganyike: Waasherati, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wahanithi, wala walawiti,

10 wala wezi, wala wenye tamaa mbaya, wala walevi, wala wanaodhihaki, wala wanyangʼanyi hawataurithi Ufalme wa Mungu.

11 Baadhi yenu mlikuwa kama hao. Lakini mlioshwa, mlitakaswa, mlihesabiwa haki kwa jina la Bwana Yesu Kristo na katika Roho wa Mungu wetu.

Dhambi Za Zinaa

12 “Vitu vyote ni halali kwangu”: lakini si vitu vyote vyenye faida. “Vitu vyote ni halali kwangu”: lakini sitatawaliwa na kitu chochote.

13 “Chakula ni cha tumbo, na tumbo ni la chakula”: lakini Mungu ataviangamiza vyote viwili. Mwili haukuumbwa kwa ajili ya zinaa bali kwa ajili ya Bwana na Bwana kwa ajili ya mwili.

14 Naye Mungu aliyemfufua Bwana kutoka kwa wafu atatufufua sisi pia kwa uweza wake.

15 Je, hamjui kwamba miili yenu ni viungo vya Kristo mwenyewe? Je, nichukue viungo vya mwili wa Kristo na kuviunganisha na mwili wa kahaba? La hasha!

16 Hamjui kwamba aliyeungwa na kahaba anakuwa mwili mmoja naye? Kwa kuwa imenenwa, “Hao wawili watakuwa mwili mmoja.”

17 Lakini mtu aliyeungwa na Bwana anakuwa roho moja naye.

18 Ikimbieni zinaa. Dhambi zingine zote atendazo mtu ziko nje ya mwili wake, lakini yeye aziniye hutenda dhambi ndani ya mwili wake mwenyewe.

19 Je, hamjui ya kwamba miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu akaaye ndani yenu, ambaye mmepewa na Mungu? Ninyi si mali yenu wenyewe,

20 kwa maana mmenunuliwa kwa gharama. Kwa hiyo mtukuzeni Mungu katika miili yenu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1CO/6-f2eb8bcc6623ec8de949f95d94963db8.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Wakorintho

1 Wakorintho 7

Kuhusu Ndoa

1 Basi kuhusu mambo yale mliyoyaandika: Ni vyema mwanaume asimguse mwanamke.

2 Lakini ili kuepuka zinaa, kila mwanaume na awe na mke wake mwenyewe na kila mwanamke awe na mume wake mwenyewe.

3 Mume atimize wajibu wake wa ndoa kwa mkewe, naye vivyo hivyo mke kwa mumewe.

4 Mwanamke hana mamlaka juu ya mwili wake bali mumewe, wala mume hana mamlaka juu ya mwili wake bali mkewe.

5 Msinyimane, isipokuwa mmekubaliana kufanya hivyo kwa muda fulani ili mweze kujitoa kwa maombi, kisha mrudiane tena ili Shetani asije akapata nafasi ya kuwajaribu kwa sababu ya kutokuwa na kiasi.

6 Nasema haya kama ushauri na si amri.

7 Laiti watu wangekuwa kama mimi nilivyo. Lakini kila mtu amepewa kipawa chake kutoka kwa Mungu, mmoja ana kipawa cha namna hii na mwingine ana cha namna ile.

8 Kwa wale wasiooa na kwa wajane, nasema hivi, ingekuwa vizuri wasioe.

9 Lakini kama hawawezi kujizuia, basi waoe na kuolewa, kwa maana ni afadhali kuoa au kuolewa kuliko kuwaka tamaa.

10 Kwa wale waliooana nawapa amri (si mimi ila ni Bwana): Mke asitengane na mumewe.

11 Lakini akitengana, ni lazima akae bila kuolewa, ama sivyo apatane tena na mumewe. Wala mume asimpe mkewe talaka.

12 Lakini kwa wengine nasema (si Bwana ila ni mimi): Kama ndugu ana mke asiyeamini, naye huyo mke anakubali kuishi pamoja naye, basi asimwache.

13 Naye mwanamke aaminiye kama ameolewa na mwanaume asiyeamini na huyo mume anakubali kuishi naye, basi huyo mwanamke asimwache.

14 Kwa maana huyo mume asiyeamini anatakaswa kupitia mkewe, naye mke asiyeamini anatakaswa kupitia mumewe anayeamini. Kama isingalikuwa hivyo watoto wenu wangalikuwa si safi, lakini ilivyo sasa wao ni watakatifu.

15 Lakini kama yule asiyeamini akijitenga, basi afanye hivyo. Katika hali kama hiyo mwanamke au mwanaume aaminiye hafungwi, kwa sababu Mungu ametuita tuishi kwa amani.

16 Wewe mke, unajuaje kama utamwokoa mumeo? Au wewe mume unajuaje kama utamwokoa mkeo?

Kuishi Kama Alivyoagiza Bwana

17 Lakini kila mtu na aishi maisha aliyopangiwa na Bwana, yale Mungu aliyomwitia. Hii ni sheria ninayoiweka kwa makanisa yote.

18 Je, mtu alikuwa tayari ametahiriwa alipoitwa? Asijifanye asiyetahiriwa. Je, mtu alikuwa hajatahiriwa alipoitwa? Asitahiriwe.

19 Kutahiriwa si kitu, na kutokutahiriwa si kitu. Lakini kuzitii amri za Mungu ndilo jambo muhimu.

20 Basi kila mmoja wenu na abaki katika hali aliyoitwa nayo.

21 Je, wewe ulipoitwa ulikuwa mtumwa? Jambo hilo lisikusumbue. Ingawaje unaweza kupata uhuru, tumia nafasi uliyo nayo sasa kuliko wakati mwingine wowote.

22 Kwa maana yeyote aliyeitwa katika Bwana akiwa mtumwa yeye ni mtu huru kwa Bwana, kama vile yeyote aliyekuwa huru alipoitwa yeye ni mtumwa wa Kristo.

23 Mlinunuliwa kwa gharama; msiwe watumwa wa wanadamu.

24 Ndugu zangu, kama kila mtu alivyoitwa, akae katika wito wake alioitiwa na Mungu.

Wajane Na Wasioolewa

25 Basi, kuhusu wale walio bikira, mimi sina amri kutoka kwa Bwana, lakini mimi natoa shauri kama mtu ambaye ni mwaminifu kwa rehema za Bwana.

26 Kwa sababu ya shida iliyoko kwa sasa, naona ni vyema mkibaki kama mlivyo.

27 Je, umeolewa? Basi usitake talaka. Je, hujaoa? Usitafute mke.

28 Lakini kama ukioa, hujatenda dhambi; na kama bikira akiolewa, hajatenda dhambi. Lakini wale wanaooa watakabiliana na matatizo mengi katika maisha haya, nami nataka kuwazuilia hayo.

29 Lakini ndugu zangu, nina maana kwamba muda uliobaki ni mfupi. Tangu sasa wale waliooa waishi kama wasio na wake;

30 nao wanaoomboleza, kama ambao hawaombolezi; wenye furaha kama wasiokuwa nayo; wale wanaonunua, kama vile vitu walivyonunua si mali yao;

31 nao wale wanaoshughulika na vitu vya dunia hii, kama ambao hawahusiki navyo. Kwa maana dunia hii kama tunavyoiona sasa inapita.

32 Ningetaka msiwe na masumbufu. Mwanaume ambaye hajaoa anajishughulisha na mambo ya Bwana, jinsi ya kumpendeza Bwana.

33 Lakini mwanaume aliyeoa anajishughulisha na mambo ya dunia, jinsi ya kumfurahisha mkewe,

34 na mawazo yake yamegawanyika. Mwanamke asiyeolewa hujishughulisha na mambo ya Bwana: lengo lake ni awe mtakatifu kimwili na kiroho. Lakini yule aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia, jinsi atakavyoweza kumfurahisha mumewe.

35 Ninasema haya kwa faida yenu wenyewe, sio ili kuwawekea vizuizi bali mpate kuishi kwa jinsi ilivyo vyema bila kuvutwa pengine katika kujitoa kwenu kwa Bwana.

36 Kama mtu yeyote anadhani kwamba hamtendei ilivyo sawa mwanamwali ambaye amemposa, naye akiwa umri wake unazidi kuendelea na mtu huyo anajisikia kwamba inampasa kuoa, afanye kama atakavyo. Yeye hatendi dhambi. Yawapasa waoane.

37 Lakini mwanaume ambaye ameamua moyoni mwake kutooa bila kulazimishwa na mtu yeyote, bali anaweza kuzitawala tamaa zake kutomwoa huyo mwanamwali, basi anafanya ipasavyo.

38 Hivyo basi, mwanaume amwoaye mwanamwali afanya vyema, lakini yeye asiyemwoa afanya vyema zaidi.

39 Mwanamke aliyeolewa amefungwa na sheria maadamu mumewe yu hai. Lakini mumewe akifa, basi mwanamke huyo yuko huru kuolewa na mume mwingine ampendaye, lakini lazima awe katika Bwana.

40 Lakini kwa maoni yangu, angekuwa na furaha zaidi akibaki alivyo. Nami nadhani pia nina Roho wa Mungu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1CO/7-5ac4c955c1a23ab3bedca62b743e7739.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Wakorintho

1 Wakorintho 8

Chakula Kilichotolewa Sadaka Kwa Sanamu

1 Sasa kuhusu chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu, tunajua kwamba “sisi sote tuna ujuzi.” Lakini ujuzi hujivuna, bali upendo hujenga.

2 Mtu yeyote anayedhani kwamba anajua kitu, bado hajui kama impasavyo kujua.

3 Lakini mtu ampendaye Mungu, hujulikana naye Mungu.

4 Hivyo basi, kuhusu kula chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu: Tunajua kwamba “Sanamu si kitu chochote kabisa duniani,” na kwamba “Kuna Mungu mmoja tu.”

5 Kwa kuwa hata kama wapo hao wanaoitwa miungu, kama wakiwa mbinguni au duniani (kama ilivyo kweli wapo “miungu” wengi na “mabwana” wengi),

6 kwetu sisi yuko Mungu mmoja, aliye Baba, ambaye vitu vyote vyatoka kwake na kwa ajili yake sisi twaishi; na kuna Bwana mmoja tu, Yesu Kristo, ambaye kwa yeye vitu vyote vimekuwepo na kwa yeye tunaishi.

7 Lakini si wote wanaojua jambo hili. Baadhi ya watu bado wamezoea sanamu kuwa halisi hivi kwamba wanapokula chakula kama hicho wanadhani kimetolewa sadaka kwa sanamu na kwa kuwa dhamiri zao ni dhaifu, dhamiri yao inanajisika.

8 Lakini chakula hakituleti karibu na Mungu, wala hatupotezi chochote tusipokula, wala hatuongezi chochote kama tukila.

9 Lakini angalieni jinsi mnavyotumia uhuru wenu usije ukawa kikwazo kwao walio dhaifu.

10 Kwa maana kama mtu yeyote mwenye dhamiri dhaifu akiwaona ninyi wenye ujuzi huu mkila katika hekalu la sanamu, je, si atatiwa moyo kula chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu?

11 Kwa njia hiyo, huyo ndugu mwenye dhamiri dhaifu, ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake, ataangamia kwa sababu ya ujuzi wenu.

12 Mnapotenda dhambi dhidi ya ndugu zenu kwa njia hii na kujeruhi dhamiri zao zilizo dhaifu, mnamkosea Kristo.

13 Kwa hiyo, kama kile ninachokula kitamfanya ndugu yangu aanguke katika dhambi, sitakula nyama kamwe, nisije nikamfanya ndugu yangu aanguke.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1CO/8-dbe16e0054998ff3928509dcec9b4180.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Wakorintho

1 Wakorintho 9

Haki Za Mtume

1 Je, mimi si huru? Je, mimi si mtume? Je, mimi sikumwona Yesu, Bwana wetu? Je, ninyi si matunda ya kazi yangu katika Bwana?

2 Hata kama mimi si mtume kwa wengine, hakika mimi ni mtume kwenu, kwa maana ninyi ni mhuri wa utume wangu katika Bwana.

3 Huu ndio utetezi wangu kwa hao wanaokaa kunihukumu.

4 Je, hatuna haki ya kula na kunywa?

5 Je, hatuna haki ya kusafiri na mke anayeamini, kama wanavyofanya mitume wengine na ndugu zake Bwana na Kefa?

6 Au ni mimi na Barnaba tu inatubidi kufanya kazi ili tuweze kupata mahitaji yetu?

7 Ni askari yupi aendaye vitani kwa gharama zake mwenyewe? Ni nani apandaye shamba la mizabibu na asile matunda yake? Ni nani achungaye kundi na asipate maziwa yake.

8 Je, nasema mambo haya katika mtazamo wa kibinadamu tu? Je, sheria haisemi vivyo hivyo?

9 Kwa maana imeandikwa katika Sheria ya Mose: “Usimfunge maksai kinywa apurapo nafaka.” Je, Mungu hapa anahusika na ngʼombe?

10 Je, Mungu hasemi haya hasa kwa ajili yetu? Hakika yameandikwa kwa ajili yetu, kwa sababu mtu anapolima na mpuraji akapura nafaka, wote wanapaswa kufanya hivyo wakiwa na tumaini la kushiriki mavuno.

11 Je, ikiwa sisi tulipanda mbegu ya kiroho miongoni mwenu, itakuwa ni jambo kubwa iwapo tutavuna vitu vya mwili kutoka kwenu?

12 Kama wengine wana haki ya kupata msaada kutoka kwenu, isingepasa tuwe na haki hiyo hata zaidi?

Lakini sisi hatukutumia haki hii. Kinyume chake, tunavumilia kila kitu ili tusije tukazuia Injili ya Kristo.

13 Je, hamjui kwamba, watu wafanyao kazi hekaluni hupata chakula chao kutoka hekaluni, nao wale wahudumiao madhabahuni hushiriki kile kitolewacho madhabahuni?

14 Vivyo hivyo, Bwana ameamuru kwamba wale wanaohubiri Injili wapate riziki yao kutokana na Injili.

15 Lakini sijatumia hata mojawapo ya haki hizi. Nami siandiki haya nikitumaini kwamba mtanifanyia mambo hayo. Heri nife kuliko mtu yeyote kuninyima huku kujisifu kwangu.

16 Lakini ninapohubiri Injili siwezi kujisifu maana ninalazimika kuhubiri. Ole wangu nisipoihubiri Injili!

17 Nikihubiri kwa hiari, ninayo thawabu. Lakini kama si kwa hiari, basi ninachofanya ni kutekeleza tu uwakili niliowekewa.

18 Basi je, thawabu yangu ni nini? Thawabu yangu ni hii: Ya kwamba katika kuhubiri Injili niitoe bila gharama, bila kutumia kwa utimilifu uwezo wangu nilio nao katika Injili.

19 Ingawa mimi ni huru, wala si mtumwa wa mtu yeyote, nimejifanya kuwa mtumwa wa kila mtu, ili niweze kuwavuta wengi kadri iwezekanavyo.

20 Kwa Wayahudi, nilikuwa kama Myahudi, ili niwapate Wayahudi. Kwa watu wale walio chini ya sheria, nilikuwa kama aliye chini ya sheria (ingawa mimi siko chini ya sheria), ili niweze kuwapata wale walio chini ya sheria.

21 Kwa watu wasio na sheria nilikuwa kama asiye na sheria (ingawa siko huru mbali na sheria ya Mungu, bali niko chini ya sheria ya Kristo), ili niweze kuwapata wale wasio na sheria.

22 Kwa walio dhaifu nilikuwa dhaifu, ili niweze kuwapata walio dhaifu. Nimekuwa mtu wa hali zote kwa watu wote ili kwa njia yoyote niweze kuwaokoa baadhi yao.

23 Nafanya haya yote kwa ajili ya Injili, ili nipate kushiriki baraka zake.

24 Je, hamjui kwamba katika mashindano ya mbio wote wanaoshindana hukimbia, lakini ni mmoja wao tu apewaye tuzo? Kwa hiyo kimbieni katika mashindano kwa jinsi ambavyo mtapata tuzo.

25 Kila mmoja anayeshiriki katika mashindano hufanya mazoezi makali. Wao hufanya hivyo ili wapokee taji isiyodumu, lakini sisi tunafanya hivyo ili kupata taji idumuyo milele.

26 Kwa hiyo mimi sikimbii kama mtu akimbiaye bila lengo, sipigani kama mtu anayepiga hewa,

27 la, bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha ili nikiisha kuwahubiria wengine, mimi nisiwe mtu wa kukataliwa.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1CO/9-dbd225cdb0b3c985857d920bedd822de.mp3?version_id=1627—