Categories
1 Wafalme

1 Wafalme 20

Ben-Hadadi Aishambulia Samaria

1 Wakati huu, Ben-Hadadi mfalme wa Aramu akakusanya jeshi lake lote. Akifuatana na wafalme thelathini na wawili wakiwa na farasi na magari ya vita, akakwea kuuzingira kwa jeshi Samaria na kuishambulia.

2 Akawatuma wajumbe katika mji kwa Ahabu mfalme wa Israeli, kusema, “Hivi ndivyo asemavyo Ben-Hadadi:

3 ‘Fedha yako na dhahabu ni yangu, nao wake zako walio wazuri sana na watoto ni wangu.’ ”

4 Mfalme wa Israeli akajibu, “Iwe kama usemavyo, bwana wangu mfalme. Mimi na vyote nilivyo navyo ni mali yako.”

5 Wale wajumbe wakaja tena na kusema, “Hivi ndivyo asemavyo Ben-Hadadi: ‘Nimetuma kutaka fedha yako na dhahabu, wake zako na watoto wako.

6 Lakini kesho wakati kama huu, nitawatuma maafisa wangu kukagua jumba lako la kifalme na nyumba za maafisa wako. Watatwaa kitu unachokithamini nao watakichukua.’ ”

7 Mfalme wa Israeli akawaita wazee wote wa nchi na akawaambia, “Tazama jinsi mtu huyu anavyochokoza! Wakati alipotuma apelekewe wake zangu na watoto wangu, fedha zangu na dhahabu yangu, sikumkatalia.”

8 Wazee na watu wote wakajibu, “Usimsikilize, wala usiyakubali matakwa yake.”

9 Kwa hiyo akawajibu wajumbe wa Ben-Hadadi, “Mwambieni bwana wangu mfalme, ‘Mtumishi wako atafanya yote uliyoyadai mwanzoni, lakini dai hili la sasa siwezi kulitekeleza.’ ” Wakaondoka na kupeleka jibu kwa Ben-Hadadi.

10 Kisha Ben-Hadadi akatuma ujumbe mwingine kwa Ahabu, kusema “Miungu iniletee maafa, tena makubwa zaidi, ikiwa vumbi la Samaria litatosheleza konzi moja ya kila mtu ya wale wafuatanao nami.”

11 Mfalme wa Israeli akajibu, “Mwambieni, ‘Yule anayevaa mavazi ya vita asije akajisifu kama yule anayevua.’ ”

12 Ben-Hadadi alisikia ujumbe huu wakati ambapo yeye na wafalme walikuwa wanakunywa katika mahema yao, na akawaamuru watu wake, “Jiandaeni kushambulia.” Kwa hiyo wakajiandaa kuushambulia mji.

Ahabu Amshinda Ben-Hadadi

13 Wakati ule ule nabii akamjia Ahabu mfalme wa Israeli na kutangaza, “Hivi ndivyo asemavyoBwana: ‘Je, unaona jeshi hili kubwa? Nitalitia mkononi mwako leo, nawe ndipo utajua kwamba mimi ndimiBwana.’ ”

14 Ahabu akauliza, “Ni nani atakayefanya hili?”

Nabii akamjibu, “Hivi ndivyo asemavyoBwana: ‘Maafisa vijana majemadari wa majimbo watafanya hili.’ ”

Akauliza, “Ni nani atakayeanzisha vita?”

Nabii akamjibu, “Ni wewe.”

15 Kwa hiyo Ahabu akawaita maafisa vijana majemadari wa majimbo, wanaume 232. Kisha akawakusanya Waisraeli wote waliobaki, jumla yao 7,000.

16 Wakaondoka wakati wa adhuhuri, Ben-Hadadi na wale wafalme thelathini na wawili walioungana naye walipokuwa katika mahema yao wakilewa.

17 Maafisa vijana majemadari wa majimbo waliondoka kwanza.

Wakati huu Ben-Hadadi alikuwa amewatuma wapelelezi, ambao walileta taarifa kusema kwamba, “Askari wanasonga mbele kutoka Samaria.”

18 Akasema, “Ikiwa wamekuja kwa amani, wakamate wakiwa hai; ikiwa wamekuja kwa vita, wakamate wakiwa hai.”

19 Wale maafisa vijana majemadari wa majimbo wakatoka nje ya mji jeshi likiwa nyuma yao,

20 kila mmoja akamuua adui yake. Hii ilisababisha Waaramu kukimbia, huku Waisraeli wakiwafuatia. Lakini Ben-Hadadi mfalme wa Aramu akatoroka akiwa amepanda farasi wake pamoja na baadhi ya wapanda farasi wake.

21 Mfalme wa Israeli akasonga mbele na kushinda farasi na magari ya vita na kusababisha hasara kubwa kwa Waaramu.

22 Baadaye nabii akaja kwa mfalme wa Israeli na kusema, “Jiandae vizuri ufikirie la kufanya, kwa sababu mwakani mfalme wa Aramu atakuja kukushambulia tena.”

23 Wakati ule ule, maafisa wa mfalme wa Aramu wakamshauri, wakamwambia, “Miungu yao ni miungu ya vilimani. Ndiyo sababu walikuwa na nguvu sana kutuzidi. Lakini kama tukipigana nao katika nchi tambarare, hakika tutawashinda.

24 Fanya hivi: Waondoe hao wafalme wote thelathini na wawili kutoka nafasi zao na uweke maafisa wengine mahali pao.

25 Ni lazima pia uandae jeshi jingine kama lile ulilopoteza, farasi kwa farasi, gari la vita kwa gari la vita, ili tuweze kupigana na Israeli katika nchi tambarare. Kisha kwa hakika tutakuwa na nguvu kuliko wao.” Akakubaliana nao naye akashughulika ipasavyo.

26 Mwaka uliofuata, majira kama hayo, Ben-Hadadi akawakusanya Waaramu mpaka Afeki kupigana dhidi ya Israeli.

27 Baada ya Waisraeli kukusanywa na kupewa mahitaji, walikwenda kukabiliana nao. Waisraeli wakapiga kambi mkabala nao kama makundi mawili madogo ya mbuzi, wakati Waaramu walienea katika nchi yote.

28 Mtu wa Mungu akaja na kumwambia mfalme wa Israeli, “Hivi ndivyoBwanaasemavyo: ‘Kwa sababu Waaramu wanafikiriBwanani Mungu wa vilimani na sio Mungu wa mabondeni, nitatia jeshi hili kubwa mkononi mwako, nawe utajua kuwa mimi ndimiBwana.’ ”

29 Kwa siku saba walipiga kambi wakitazamana na siku ya saba vita vikaanza. Waisraeli wakawajeruhi askari wa miguu wa Waaramu 100,000 kwa siku moja.

30 Waliobaki wakatorokea katika mji wa Afeki, mahali ambapo watu 27,000 waliangukiwa na ukuta. Naye Ben-Hadadi akakimbilia mjini na kujificha kwenye chumba cha ndani.

31 Maafisa wake wakamwambia, “Tazama, tumesikia kwamba wafalme wa nyumba ya Israeli wana huruma. Twendeni kwa mfalme wa Israeli tukiwa tumevaa nguo za gunia viunoni mwetu na kamba kuzunguka vichwa vyetu. Huenda akakuacha hai.”

32 Wakiwa wamevaa nguo za gunia viunoni mwao na kamba kuzunguka vichwa vyao, walikwenda kwa mfalme wa Israeli na kusema, “Mtumishi wako Ben-Hadadi anasema: ‘Tafadhali, naomba uniache hai.’ ”

Mfalme akajibu, “Je, bado yuko hai? Yeye ni ndugu yangu.”

33 Wale watu wakalipokea jambo lile kama dalili nzuri nao wakawa wepesi kulichukua neno lake wakisema, “Ndiyo, yeye ni ndugu yako Ben-Hadadi!”

Mfalme akawaambia, “Nendeni mkamlete.” Ikawa Ben-Hadadi alipokuja, Ahabu akampandisha katika gari lake la vita.

Ben-Hadadi akajitolea, akisema,

34 “Nitairudisha ile miji ambayo baba yangu aliiteka kutoka kwa baba yako. Unaweza kuweka maeneo yako ya soko katika Dameski, kama baba yangu alivyofanya huko Samaria.”

Ahabu akasema, “Katika misingi ya mkataba, nitakuachilia huru.” Kwa hiyo akaweka mkataba naye, akamruhusu aende zake.

Nabii Amlaumu Ahabu

35 Kwa neno laBwana, mmoja wa wana wa manabii akamwambia mwenzake, “Nipige kwa silaha yako,” lakini yule mtu akakataa.

36 Kwa hiyo yule nabii akasema, “Kwa sababu hukumtiiBwana, mara tu tutakapoachana utauawa na simba.” Na baada ya yule mtu kuondoka, simba akatokea na kumuua.

37 Nabii akamkuta mtu mwingine na kumwambia, “Nipige tafadhali.” Kisha yule mtu akampiga na kumjeruhi.

38 Ndipo nabii akaenda na kusimama barabarani akimsubiri mfalme. Akajibadilisha kwa kushusha kitambaa cha kichwani mwake hadi kwenye macho.

39 Mfalme alipopita pale, yule nabii akamwita, “Mtumishi wako alikwenda vitani wakati vita vilipopamba moto, mtu mmoja akanijia na mateka akasema, ‘Mlinde mtu huyu. Kama akitoroka itakuwa uhai wako kwa uhai wake, ama vipande 3,000 vya fedha.’

40 Wakati mtumishi wako alipokuwa na shughuli nyingi hapa na pale, yule mtu akatoweka.”

Mfalme wa Israeli akasema, “Hiyo ndiyo hukumu yako. Wewe umeitaja mwenyewe.”

41 Kisha yule nabii akajifunua macho yake haraka, na mfalme wa Israeli akamtambua kama mmoja wa manabii.

42 Akamwambia mfalme, “Hivi ndivyoBwanaasemavyo: ‘Umemwacha huru mtu niliyekusudia afe. Kwa hiyo ni uhai wako kwa uhai wake, watu wako kwa watu wake.’ ”

43 Kwa uchungu na hasira, mfalme wa Israeli akaenda kwenye jumba lake la kifalme huko Samaria.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1KI/20-3053e0ad4a24967098ad8bc5803370f7.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Wafalme

1 Wafalme 21

Shamba La Mizabibu La Nabothi

1 Baada ya hayo, Nabothi, Myezreeli, alikuwa na shamba la mizabibu jirani na jumba la kifalme la Ahabu mfalme wa Samaria.

2 Ahabu akamwambia Nabothi, “Nipe shamba lako la mizabibu nilitumie kwa bustani ya mboga, kwa kuwa liko karibu na jumba langu la kifalme. Badala yake, nitakupa shamba jingine la mizabibu zuri zaidi au, kama utapenda, nitakulipa kiasi chochote unachoona ni thamani yake.”

3 Lakini Nabothi akamjibu, “Bwanana apishe mbali kukupa wewe urithi wa baba zangu.”

4 Basi Ahabu akaenda nyumbani, mwenye huzuni na hasira kwa sababu ya yale ambayo Nabothi, Myezreeli, alikuwa amesema, “Sitakupa urithi wa baba zangu.” Akajinyoosha juu ya kitanda akisononeka, na akakataa kula.

5 Yezebeli mke wake akaingia na akamuuliza, “Kwa nini unahuzunika hivi? Kwa nini huli chakula?”

6 Akamjibu, “Kwa sababu nilimwambia Nabothi, Myezreeli, ‘Niuzie shamba lako la mizabibu, au kama ukipenda, nitakupa shamba jingine la mizabibu badala yake.’ Lakini akasema, ‘Sitakupa shamba langu la mizabibu.’ ”

7 Yezebeli mke wake akasema, “Hivi ndivyo unavyofanya, nawe ni mfalme katika Israeli yote? Inuka na ule! Changamka. Nitakupatia shamba la mizabibu la Nabothi, Myezreeli.”

8 Kwa hiyo akaandika barua kwa jina la Ahabu akaweka muhuri wake juu ya hizo barua, akazipeleka kwa wazee na kwa watu wenye cheo walioishi katika mji pamoja na Nabothi.

9 Katika barua hizo aliandika:

“Tangazeni siku ya watu kufunga na mkamketishe Nabothi mahali pa wazi miongoni mwa watu.

10 Lakini waketisheni watu wawili wabaya kabisa mkabala naye, nao washuhudie kuwa yeye amemlaani Mungu na mfalme. Kisha mtoeni nje na kumpiga kwa mawe hadi afe.”

11 Hivyo wazee na watu wenye cheo walioishi katika mji wa Nabothi wakafanya kama Yezebeli alivyoelekeza katika barua aliyowaandikia.

12 Wakatangaza mfungo na kumketisha Nabothi mahali pa wazi miongoni mwa watu.

13 Kisha watu wawili wabaya kabisa wakaja wakaketi mkabala naye, nao wakaleta mashtaka dhidi ya Nabothi mbele ya watu, wakisema, “Nabothi amemlaani Mungu na mfalme.” Kwa hiyo wakamtoa nje na kumpiga kwa mawe hadi akafa.

14 Kisha wakatuma ujumbe kwa Yezebeli, kusema, “Nabothi amepigwa mawe na amekufa.”

15 Mara tu Yezebeli aliposikia kwamba Nabothi amepigwa mawe na amekufa, akamwambia Ahabu, “Amka na uchukue lile shamba la mizabibu la Nabothi, Myezreeli, ambalo alikataa kukuuzia. Hayuko hai tena, bali amekufa.”

16 Ahabu aliposikia Nabothi amekufa, akainuka na kushuka ili kulichukua shamba la mizabibu la Nabothi.

17 Kisha neno laBwanalikamjia Eliya, Mtishbi:

18 “Shuka ukakutane na Ahabu mfalme wa Israeli, anayetawala Samaria. Sasa yuko katika shamba la mizabibu la Nabothi, ambapo amekwenda alimiliki.

19 Umwambie, ‘Hivi ndivyoBwanaasemavyo: Je, hujamuua mtu na kuitwaa mali yake?’ Kisha umwambie, ‘Hivi ndivyo asemavyoBwana: Mahali ambapo mbwa waliramba damu ya Nabothi, mbwa watairamba damu yako, naam, yako wewe!’ ”

20 Ahabu akamwambia Eliya, “Kwa hiyo umenipata, wewe adui yangu!”

Akajibu, “Ndiyo, nimekupata. Kwa sababu umejiuza mwenyewe kufanya uovu mbele ya macho yaBwana.

21 ‘Nitaleta maafa juu yako. Nitaangamiza uzao wako na kukatilia mbali kutoka kwa Ahabu kila mzaliwa wa mwisho wa kiume katika Israeli, wa mtumwa au wa mtu huru.

22 Nitaifanya nyumba yako kama ile ya Yeroboamu mwana wa Nebati na ile ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa sababu umenighadhibisha kwa kuwa umesababisha Israeli kutenda dhambi.’

23 “Pia kwa habari ya YezebeliBwanaanasema, ‘Mbwa watamla Yezebeli karibu na ukuta wa Yezreeli.’

24 “Mbwa watawala wale wa nyumba ya Ahabu watakaofia mjini, nao wale watakaofia mashambani wataliwa na ndege wa angani.”

25 (Hapajapata kamwe kuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza mwenyewe kutenda uovu machoni mwaBwana, akiwa anachochewa na Yezebeli mkewe.

26 Alitenda kwa uovu sana katika kuabudu sanamu, kama wale Waamori ambaoBwanaaliowafukuza mbele ya Israeli.)

27 Ahabu aliposikia maneno haya, akararua nguo zake, akavaa nguo za gunia na kufunga. Akalala na kujifunika nguo za gunia na kwenda kwa unyenyekevu.

28 Ndipo neno laBwanalilipomjia Eliya Mtishbi kusema,

29 “Umeona jinsi Ahabu alivyojinyenyekeza mbele zangu? Kwa kuwa amejishusha mwenyewe, sitaleta maafa haya wakati akiwa hai, lakini nitayaleta juu ya nyumba yake katika siku za mwanawe.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1KI/21-f9959196a38fb35c665b433f11f02ff6.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Wafalme

1 Wafalme 22

Mikaya Anatabiri Dhidi Ya Ahabu

1 Kwa miaka mitatu hapakuwa na vita kati ya Aramu na Israeli.

2 Lakini katika mwaka wa tatu Yehoshafati mfalme wa Yuda akashuka kwenda kumwona mfalme wa Israeli.

3 Mfalme wa Israeli alikuwa amewaambia maafisa wake, “Je, hamjui Ramoth-Gileadi ni mali yetu na bado hatufanyi chochote kuirudisha kwetu kutoka kwa mfalme wa Aramu?”

4 Kwa hiyo akamuuliza Yehoshafati, “Je, utakwenda pamoja nami kupigana dhidi ya Ramoth-Gileadi?”

Yehoshafati akamjibu mfalme wa Israeli, “Mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, farasi wangu ni kama farasi wako.”

5 Lakini Yehoshafati pia akamwambia mfalme wa Israeli, “Kwanza tafuta shauri laBwana.”

6 Kwa hiyo mfalme wa Israeli akawaleta pamoja manabii wanaume wapatao mia nne, akawauliza, “Je, niende vitani dhidi ya Ramoth-Gileadi, au niache?”

Wakajibu, “Naam, nenda, kwa kuwa Bwana ataiweka Ramoth-Gileadi mkononi mwa mfalme.”

7 Lakini Yehoshafati akauliza, “Je, hayuko nabii waBwanahapa ambaye tunaweza kumuuliza?”

8 Mfalme wa Israeli akamjibu Yehoshafati, “Bado yupo mtu mmoja ambaye kupitia yeye twaweza kumuuliza shauri laBwana, lakini namchukia kwa sababu huwa hatabiri jambo lolote jema kunihusu mimi, lakini kila mara hunitabiria mabaya tu. Yeye ni Mikaya mwana wa Imla.”

Yehoshafati akajibu, “Mfalme hapaswi kusema hivyo.”

9 Kwa hiyo mfalme wa Israeli akamwita mmoja wa maafisa wake na kusema, “Mlete Mikaya mwana wa Imla mara moja.”

10 Wakiwa wamevalia majoho yao ya kifalme, mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wameketi juu ya viti vyao vya kifalme katika sakafu ya kupuria, kwenye ingilio la lango la Samaria, pamoja na manabii wote wakiwa wakitabiri mbele yao.

11 Wakati huu Sedekia mwana wa Kenaana alikuwa ametengeneza pembe za chuma, akatangaza, “Hivi ndivyoBwanaasemavyo, ‘Kwa hizi pembe utawapiga na kuwarudisha Waaramu nyuma mpaka wameangamizwa.’ ”

12 Manabii wengine wote walikuwa wanatabiri kitu hicho hicho wakisema, “Ishambulie Ramoth-Gileadi na uwe mshindi. Kwa kuwaBwanaataitia mkononi mwa mfalme.”

13 Mjumbe aliyekuwa amekwenda kumwita Mikaya akamwambia, “Tazama, manabii wote kama mtu mmoja wanatabiri ushindi kwa mfalme. Neno lako na likubaliane na lao, nawe unene mema kuhusu mfalme.”

14 Lakini Mikaya akasema, “Hakika kamaBwanaaishivyo, nitamwambia kile tuBwanaatakachoniambia.”

15 Alipofika, mfalme akamuuliza, “Mikaya, je, twende vitani dhidi ya Ramoth-Gileadi au niache?”

Akamjibu, “Shambulia na ushinde, kwa kuwaBwanaatawatia mkononi mwa mfalme.”

16 Mfalme akamwambia, “Je, ni mara ngapi nitakuapisha ili usiniambie kitu chochote ila kweli tu kwa jina laBwana?”

17 Ndipo Mikaya akajibu, “Niliona Israeli wote wametawanyika vilimani kama kondoo wasio na mchungaji, nayeBwanaakasema, ‘Watu hawa hawana bwana. Mwache kila mmoja aende nyumbani kwa amani.’ ”

18 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Sikukuambia kwamba huwa hatabiri jambo lolote jema kunihusu, bali mabaya tu?”

19 Mikaya akaendelea, “Kwa hiyo lisikie neno laBwana: NilimwonaBwanaameketi juu ya kiti chake cha enzi pamoja na jeshi lote la mbinguni likiwa limesimama kumzunguka upande wa kulia na wa kushoto.

20 NayeBwanaakasema, ‘Ni nani atakayemshawishi Ahabu ili aishambulie Ramoth-Gileadi na kukiendea kifo chake huko?’

“Mmoja akapendekeza hili na mwingine lile.

21 Mwishoni, pepo mchafu akajitokeza, akasimama mbele zaBwanana kusema, ‘Nitamshawishi.’

22 “Bwanaakauliza, ‘Kwa njia gani?’

“Akasema, ‘Nitakwenda na kuwa roho ya uongo katika vinywa vya manabii wake wote.’

“Bwanaakasema, ‘Utafanikiwa katika kumshawishi. Nenda ukafanye hivyo.’

23 “Kwa hiyo sasaBwanaameweka roho ya kudanganya ndani ya vinywa vya hawa manabii wako wote.Bwanaameamuru maafa kwa ajili yako.”

24 Kisha Sedekia mwana wa Kenaana akatoka na kumpiga Mikaya kofi usoni. Akauliza, “Huyo Roho kutoka kwaBwanaalipita njia gani alipotoka kwangu ili kusema nawe?”

25 Mikaya akajibu, “Utagundua siku hiyo utakapokwenda kujificha kwenye chumba cha ndani.”

26 Kisha mfalme wa Israeli akaagiza, “Mchukueni na mkamrudishe kwa Amoni mtawala wa mji na kwa Yoashi mwana wa mfalme.

27 Mkaseme, ‘Hivi ndivyo asemavyo mfalme: Mwekeni mtu huyu gerezani na asipewe chochote ila mkate na maji mpaka nitakaporudi salama.’ ”

28 Mikaya akasema, “Kama utarudi salama, basiBwanahajanena kupitia kwangu.” Kisha akaongeza kusema, “Zingatieni maneno yangu, enyi watu wote!”

Ahabu Auawa Ramoth-Gileadi

29 Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda wakaenda Ramoth-Gileadi.

30 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Nitaingia vitani nikiwa nimejibadilisha, lakini wewe uvae majoho yako ya kifalme.” Kwa hiyo mfalme wa Israeli akajibadilisha na kwenda vitani.

31 Wakati huu, mfalme wa Aramu alikuwa amewaagiza majemadari thelathini na wawili wa magari ya vita, “Msipigane na yeyote, mdogo au mkubwa, isipokuwa mfalme wa Israeli.”

32 Wakati wale majemadari wa magari ya vita walipomwona Yehoshafati wakafikiri, “Hakika huyu ndiye mfalme wa Israeli.” Kwa hiyo wakageuka ili wamshambulie, lakini Yehoshafati akapiga kelele,

33 wale majemadari wakaona kwamba hakuwa mfalme wa Israeli, nao wakaacha kumfuatilia.

34 Lakini mtu fulani akavuta upinde pasipo lengo na kumpiga mfalme wa Israeli katikati ya kiungio cha mavazi yake ya chuma. Mfalme akamwambia mwendesha gari lake, “Geuza gari na uniondoe mimi katika mapigano, nimejeruhiwa.”

35 Vita vikaendelea mchana kutwa, naye Mfalme Ahabu akategemezwa ndani ya gari kuelekea Waaramu. Damu kutoka kwenye jeraha lake ikachuruzika ndani ya gari na jioni yake akafa.

36 Jua lilipokuwa linazama, mbiu ikaenea katika jeshi lote: “Kila mtu aende mjini kwake, na kila mtu shambani kwake!”

37 Basi mfalme akafa na akaletwa Samaria, nao wakamzika huko.

38 Wakasafisha lile gari la vita katika bwawa la Samaria (mahali makahaba walipooga), na mbwa wakaramba damu yake, sawasawa na neno laBwanalilivyokuwa limesema.

39 Kwa matukio mengine ya utawala wa Ahabu, pamoja na yote aliyoyafanya, jumba la kifalme alilojenga na kupambwa kwa pembe za ndovu, nayo miji aliyoijengea maboma, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?

40 Ahabu akalala pamoja na baba zake. Naye Ahazia mwanawe akawa mfalme baada yake.

Yehoshafati Mfalme Wa Yuda

41 Yehoshafati mwana wa Asa akawa mfalme wa Yuda katika mwaka wa nne wa Ahabu mfalme wa Israeli.

42 Yehoshafati alikuwa na umri wa miaka thelathini na mitano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka ishirini na mitano. Jina la mama yake aliitwa Azuba binti Shilhi.

43 Katika kila jambo alitembea katika njia za Asa baba yake wala hakwenda kinyume chake. Alifanya yaliyo mema machoni paBwana. Hata hivyo mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa. Watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko.

44 Yehoshafati pia alikuwa na amani na mfalme wa Israeli.

45 Kwa habari ya matukio mengine ya utawala wa Yehoshafati, mafanikio aliyokuwa nayo na uhodari wake katika vita, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?

46 Aliondolea mbali katika nchi mahanithi wa mahali pa kuabudia miungu waliobaki huko hata baada ya utawala wa baba yake Asa.

47 Tangu hapo hapakuwepo na mfalme katika Edomu, naibu ndiye alitawala.

48 Wakati huu Yehoshafati akaunda merikebu nyingi za biasharaili kwenda Ofiri kuchukua dhahabu, lakini kamwe hazikusafiri, kwa maana zilivunjika huko Esion-Geberi.

49 Wakati ule, Ahazia mwana wa Ahabu akamwambia Yehoshafati, “Waache watu wangu wasafiri baharini pamoja na watu wako,” lakini Yehoshafati akakataa.

50 Kisha Yehoshafati akalala na baba zake, akazikwa pamoja nao katika mji wa Daudi baba yake. Mwanawe Yehoramu akawa mfalme baada yake.

Ahazia Mfalme Wa Israeli

51 Ahazia mwana wa Ahabu akawa mfalme wa Israeli huko Samaria katika mwaka wa kumi na saba wa Yehoshafati mfalme wa Yuda, naye alitawala katika Israeli kwa miaka miwili.

52 Akafanya maovu machoni mwaBwanakwa sababu alienenda katika njia za baba yake na mama yake na katika njia za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambaye alisababisha Israeli itende dhambi.

53 Alimtumikia na kumwabudu Baali na kumghadhibishaBwana, Mungu wa Israeli, kama vile baba yake alivyokuwa amefanya.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1KI/22-3851d230159079ac1b2ab098a23a7123.mp3?version_id=1627—