Categories
1 Samweli

1 Samweli Utangulizi

Utangulizi

Katika andiko la Kiebrania, vitabu vya 1 Samweli na 2 Samweli vilikuwa kitabu kimoja. Kugawanyika na kuwa vitabu viwili kulifanyika katika tafsiri ya “Septuagint” (yaani Agano la Kale la Kiyunani), ambayo iliviita “Kitabu cha Kwanza na cha Pili cha Ufalme.” Kitabu cha 1 Samweli kinaanza kuelezea kuzaliwa kwa Samweli na mafundisho yake hekaluni. Kinaelezea jinsi alivyoiongoza Israeli kama nabii, kuhani na mwamuzi.

Wakati wana wa Israeli walitaka kuwa na mfalme, Samweli, kwa uongozi wa Mungu, alimtia Sauli mafuta kuwa mfalme wa kwanza wa Waisraeli. Lakini Sauli aliacha kumtii Mungu, naye Mungu akamkataa asiendelee kuwa mfalme. Kisha Mungu akamwongoza Samweli kumtia Daudi mafuta kwa siri kuwa mfalme badala ya Sauli. Sehemu ya kitabu hiki iliyobaki inaelezea mapambano kati ya Sauli na Daudi.

Mwandishi

Inawezekana ni Samweli hadi mahali kifo chake kimenakiliwa; pia maandishi ya manabii Nathani na Gadi yamejumuishwa.

Kusudi

Kitabu cha 1 Samweli kinaonyesha historia ya Israeli chini ya uongozi wa waamuzi, kuonyesha mabadiliko ya uongozi katika Israeli kutoka mfumo wa uongozi wa waamuzi kwenda kwa uongozi wa wafalme, na kuweka kumbukumbu za maisha ya watu ambao kupitia kwao Masiya angezaliwa.

Mahali

Katika nchi ya Israeli.

Tarehe

Wakati kitabu hiki kiliandikwa haujulikani.

Wahusika Wakuu

Eli, Hana, Samweli, Sauli, Yonathani, na Daudi.

Wazo Kuu

Kuanzishwa kwa ufalme wa Waisraeli, na vile huo ufalme uliendelea chini ya mfalme Sauli na Daudi.

Mambo Muhimu

Kitabu cha 1 Samweli kinaonyesha kumomonyoka kwa maadili kwa waamuzi wakati wa Samweli; mwanzo wa kushindwa kwa ufalme wakati wa Sauli; Daudi kutiwa mafuta na kujaribiwa kwa uzoefu wake; na pia, mwisho wa Sauli.

Mgawanyo

Eli, kuhani na mwamuzi, na Samweli (

1:1–7:17

)

Samweli na Sauli, kiongozi wa Israeli (

8:1–15:35

)

Mfalme Sauli, na Daudi (

16:1–31:13

).

Categories
1 Samweli

1 Samweli 1

Kuzaliwa Kwa Samweli

1 Kulikuwepo na mtu mmoja kutoka Rama, Msufi kutoka nchi ya vilima vya Efraimu, ambaye jina lake aliitwa Elikana mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu mwana wa Tohu, mwana wa Sufu, Mwefraimu.

2 Alikuwa na wake wawili, mmoja aliitwa Hana na mwingine Penina. Penina alikuwa na watoto, lakini Hana hakuwa na mtoto.

3 Kila mwaka mtu huyu alikwea kutoka mji wake ili kuabudu na kutoa dhabihu kwaBwanaMwenye Nguvu Zote huko Shilo, ambapo Hofni na Finehasi, wana wawili wa Eli, walikuwa makuhani waBwana.

4 Kila mara ilipofika siku ya Elikana kutoa dhabihu, aliwapa mafungu Penina mkewe na wanawe wote pamoja na binti zake.

5 Lakini alimpa Hana fungu maradufu kwa sababu alimpenda, ingawaBwanaalikuwa amemfunga tumbo.

6 Kwa sababuBwanaalikuwa amemfunga tumbo, mke mwenzake alikuwa anamchokoza ili kumuudhi.

7 Hili liliendelea mwaka baada ya mwaka. Kila mara Hana alipokwenda katika nyumba yaBwana, mke mwenzake alikuwa akimkasirisha mpaka analia na kushindwa kula.

8 Elikana mumewe akawa anamwambia, “Hana, kwa nini unalia? Kwa nini huli? Kwa nini kuvunjika moyo? Je, mimi si bora zaidi kwako kuliko watoto kumi?”

9 Siku moja walipokuwa wamemaliza kula na kunywa huko Shilo, Hana alisimama. Wakati huo kuhani Eli alikuwa ameketi kwenye kiti pembeni mwa mwimo wa mlango wa Hekalu laBwana.

10 Kwa uchungu wa rohoni Hana alilia sana na akamwombaBwana.

11 Naye akaweka nadhiri, akisema, “EeBwanaMwenye Nguvu Zote, laiti ungeangalia huzuni kuu ya mtumishi wako na kunikumbuka mimi, wala usimsahau mtumishi wako nawe ukampa mwana, basi huyo mwana nitamtoa kwaBwanakwa siku zote za maisha yake, wala wembe hautapita kichwani mwake.”

12 Alipokuwa anaendelea kumwombaBwana, Eli alichunguza kinywa chake.

13 Hana alikuwa akiomba moyoni mwake, midomo yake ikiwa inachezacheza lakini sauti haikusikika. Eli akafikiri alikuwa amelewa

14 naye akamwambia, “Utaendelea kulewa mpaka lini? Achilia mbali mvinyo wako.”

15 Hana akajibu, “Si hivyo bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye huzuni kubwa. Mimi sijanywa mvinyo wala kileo, nilikuwa ninaumimina moyo wangu kwaBwana.

16 Usimdhanie mtumishi wako kuwa mwanamke mwovu; nimekuwa nikiomba hapa katika wingi wa uchungu mkuu na huzuni.”

17 Eli akamjibu, “Nenda kwa amani, naye Mungu wa Israeli na akujalie kile ulichomwomba.”

18 Hana akasema, “Mtumishi wako na apate kibali machoni pako.” Kisha akaondoka zake na kula chakula, wala uso wake haukuwa na huzuni tena.

19 Kesho yake asubuhi na mapema waliamka wakaabudu mbele zaBwanana kisha wakarudi nyumbani kwao huko Rama. Elikana akakutana kimwili na mkewe Hana, nayeBwanaakamkumbuka.

20 Hivyo wakati ulipotimia, Hana akapata mimba na akamzaa mwana. Hana akamwita jina lake Samweli, akasema, “Kwa kuwa nilimwomba kwaBwana.”

Hana Anamweka Samweli Wakfu

21 Wakati huyo mtu Elikana alipanda pamoja na jamaa yake yote kutoa dhabihu ya mwaka kwaBwanana kutimiza nadhiri yake,

22 Hana hakwenda. Alimwambia mume wake, “Baada ya mtoto kuachishwa kunyonya, nitamchukua na kumpeleka mbele zaBwana, naye ataishi huko wakati wote.”

23 Elikana mumewe akamwambia, “Fanya lile unaloona ni bora zaidi kwako. Ukae hapa mpaka utakapomwachisha kunyonya,Bwanana akujalie kutimiza nadhiri yako.” Hivyo huyo mwanamke akakaa nyumbani na kumnyonyesha mwanawe mpaka alipomwachisha kunyonya.

24 Baada ya mtoto kuachishwa kunyonya, Hana akamchukua huyo mtoto, akiwa mdogo hivyo hivyo, pamoja na fahali wa miaka mitatu, efa ya ungana kiriba cha divai, naye akamleta mtoto kwenye nyumba yaBwanahuko Shilo.

25 Walipokwisha kumchinja yule fahali, wakamleta mtoto kwa Eli,

26 naye Hana akamwambia Eli, “Hakika kama uishivyo, bwana wangu, mimi ndiye yule mama ambaye alisimama hapa karibu nawe akiomba kwaBwana.

27 Niliomba mtoto huyu, nayeBwanaamenijalia kile nilichomwomba.

28 Hivyo sasa ninamtoa kwaBwana. Kwa maana maisha yake yote atakuwa ametolewa kwaBwana.” Naye akamwabuduBwanahuko.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1SA/1-944348c2e6fc8a34714eb69026225c44.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Samweli

1 Samweli 2

Maombi Ya Hana

1 Kisha Hana akaomba na kusema:

“Moyo wangu wamshangiliaBwana,

katikaBwanapembe yangu imeinuliwa juu.

Kinywa changu chajisifu juu ya adui zangu,

kwa kuwa naufurahia wokovu wako.

2 “Hakuna yeyote aliye mtakatifu kamaBwana,

hakuna mwingine zaidi yako;

hakuna Mwamba kama Mungu wetu.

3 “Msiendelee kusema kwa kiburi hivyo

wala msiache vinywa vyenu kunena kwa kiburi,

kwa kuwaBwanandiye Mungu ajuaye,

na kwa yeye matendo hupimwa.

4 “Pinde za mashujaa zimevunjika,

lakini wale wanaojikwaa wamevikwa nguvu.

5 Wale waliokuwa na chakula tele wamejikodisha wenyewe

ili kupata chakula,

lakini wale waliokuwa na njaa

hawana njaa tena.

Mwanamke yule aliyekuwa tasa

amezaa watoto saba,

lakini yule ambaye alikuwa na wana wengi

amedhoofika.

6 “Bwanahuua na huleta uhai,

hushusha chini mpaka kaburinina hufufua.

7 Bwanahumfanya mtu maskini naye hutajirisha,

hushusha na hukweza.

8 Humwinua maskini kutoka mavumbini

na humwinua mhitaji kutoka lundo la majivu;

huwaketisha pamoja na wakuu

na kuwafanya warithi kiti cha enzi cha heshima.

“Kwa kuwa misingi ya dunia ni yaBwana;

juu yake ameuweka ulimwengu.

9 Yeye atailinda miguu ya watakatifu wake,

lakini waovu watanyamazishwa kwenye giza.

“Si kwa nguvu mtu hushinda;

10 wale wampingaoBwana

wataharibiwa kabisa.

Atapiga radi dhidi yao kutoka mbinguni;

Bwanaataihukumu miisho ya dunia.

“Atampa nguvu mfalme wake,

na kuitukuza pembe

ya mpakwa mafuta wake.”

11 Kisha Elikana akaenda nyumbani Rama, lakini mtoto akahudumu mbele zaBwanachini ya kuhani Eli.

Wana Waovu Wa Eli

12 Wana wa Eli walikuwa watu wabaya kabisa, hawakumheshimuBwana.

13 Basi ilikuwa desturi ya makuhani pamoja na watu kwamba kila mara yeyote anapotoa dhabihu na huku nyama ikiwa inachemshwa, mtumishi wa kuhani angalikuja na uma wenye meno matatu mkononi mwake.

14 Angeutumbukiza huo uma kwenye sufuria au birika au sufuria kubwa au chungu, naye kuhani angalijichukulia mwenyewe chochote ambacho uma ungekileta. Hivi ndivyo walivyowatendea Waisraeli wote waliokuja Shilo.

15 Lakini hata kabla mafuta ya mnyama hayajachomwa, mtumishi wa kuhani angalikuja na kusema kwa mtu ambaye alikuwa akitoa dhabihu, “Mpe kuhani nyama akaoke, kwani hatapokea nyama iliyochemshwa kutoka kwako, ila iliyo mbichi tu.”

16 Kama mtu akimwambia, “Mafuta ya mnyama na yachomwe kwanza, ndipo uchukue chochote unachotaka,” mtumishi angalijibu, “Hapana, nipe sasa, kama huwezi nitaichukua kwa nguvu.”

17 Hii Dhambi ya hawa vijana ilikuwa kubwa sana machoni paBwana, kwa kuwa waliitendea dhabihu yaBwanakwa dharau.

18 Lakini Samweli alikuwa akihudumu mbele zaBwana, kijana akivaa kisibau cha kitani.

19 Kila mwaka mama yake alimshonea joho dogo na kumchukulia wakati alipokwea pamoja na mumewe kutoa dhabihu ya mwaka.

20 Eli alikuwa akiwabariki Elikana na mkewe, akisema, “Bwanana akupe watoto kwa mwanamke huyu ili kuchukua nafasi ya yule aliyekuwa amemwomba na akamtoa kwaBwana.” Kisha wakawa wanakwenda nyumbani.

21 Bwanaakawa mwenye neema kwa Hana, naye akapata mimba akazaa wana watatu na binti wawili. Wakati huo, kijana Samweli akaendelea kukua mbele zaBwana.

22 Basi Eli, ambaye alikuwa mzee sana, alisikia kuhusu kila kitu ambacho wanawe walikuwa wakiwafanyia Israeli wote na jinsi walivyokutana kimwili na wanawake waliohudumu kwenye ingilio la Hema la Kukutania.

23 Hivyo akawaambia, “Kwa nini mmefanya mambo kama haya? Nimesikia kutoka kwa watu wote juu ya haya matendo yenu maovu.

24 Sivyo, wanangu, hii si habari nzuri ambayo ninasikia ikienea miongoni mwa watu waBwana.

25 Kama mtu akifanya dhambi dhidi ya mtu mwenzake, mtu mwingine aweza kumwombea kwa Mungu, lakini kama mtu akimfanyia Mungu dhambi, ni nani atakayemwombea?” Hata hivyo wanawe hawakusikia maonyo ya baba yao, kwa sababuBwanaalitaka kuwaua.

26 Naye kijana Samweli akaendelea kukua katika kimo, akimpendezaBwanana wanadamu.

Unabii Dhidi Ya Nyumba Ya Eli

27 Basi mtu wa Mungu akaja kwa Eli na kumwambia, “Hivi ndivyo asemavyoBwana: ‘Je, sikujifunua waziwazi kwa nyumba ya baba yako wakati walikuwa huko Misri chini ya Farao?

28 Nilimchagua baba yako kati ya makabila yote ya Israeli kuwa kuhani wangu, kukwea kwenye madhabahu yangu, kufukiza uvumba na kuvaa kisibau mbele yangu. Pia niliwapa nyumba ya baba yako sadaka zote zilizotolewa kwa moto na Waisraeli.

29 Kwa nini unadharau dhabihu zangu na sadaka zile nilizoziamuru kwa ajili ya makao yangu? Kwa nini unawaheshimu wanao kuliko mimi kwa kujinenepesha wenyewe kwa kula sehemu zilizo bora za kila sadaka zinazotolewa na watu wangu wa Israeli?’

30 “Kwa hiyo,Bwana, Mungu wa Israeli asema: ‘Niliahidi kuwa nyumba yako na nyumba ya baba yako wangehudumu mbele zangu milele.’ Lakini sasaBwanaanasema: ‘Jambo hili na liwe mbali nami! Wale wanaoniheshimu nitawaheshimu, wale wanaonidharau mimi watadharauliwa.

31 Wakati unakuja nitakapozipunguza nguvu zenu na nguvu ya nyumba ya baba yenu, ili pasiwepo mtu katika mbari yenu atakayeishi kuuona uzee

32 nanyi mtaona huzuni katika makao yangu. Ingawa Israeli watafanyiwa mema, katika mbari yenu kamwe hapatakuwepo mtu atakayeishi hadi kuwa mzee.

33 Kila mmoja wenu ambaye sitamkatilia mbali kutoka madhabahuni pangu atabakizwa tu kupofusha macho yenu kwa machozi na kuihuzunisha mioyo yenu, nao wazao wenu wote watakufa watakapokuwa wamefikia umri wa kustawi.

34 “ ‘Kile kitakachotokea kwa wanao wawili, Hofni na Finehasi, kitakuwa ishara kwako. Wote wawili watakufa katika siku moja.

35 Mimi mwenyewe nitajiinulia kuhani mwaminifu, ambaye atafanya sawasawa na kile kilichoko moyoni mwangu na akilini mwangu. Nitaifanya nyumba yake kuwa imara, naye atahudumu mbele ya mpakwa mafuta wangu daima.

36 Kisha kila mmoja aliyeachwa katika mbari yenu atakuja na kusujudu mbele yake kwa ajili ya kipande cha fedha na ganda la mkate akisema, “Niteue katika baadhi ya ofisi ya ukuhani ili niweze kupata chakula.” ’ ”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1SA/2-db4aa0a373ca3bc53bf1058ef3c18d27.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Samweli

1 Samweli 3

Bwana Amwita Samweli

1 Kijana Samweli alihudumu mbele zaBwanachini ya Eli. Katika siku zile neno la Mungu lilikuwa adimu, hapakuwepo na maono mengi.

2 Usiku mmoja Eli, ambaye macho yake yalikuwa yamefifia sana kiasi kwamba aliona kwa shida sana, alikuwa amelala mahali pake pa kawaida.

3 Taa ya Mungu bado ilikuwa haijazimika, na Samweli alikuwa amelala HekalunimwaBwana, ambapo Sanduku la Mungu lilikuwako.

4 KishaBwanaakamwita Samweli.

Samweli akajibu, “Mimi hapa.”

5 Naye akakimbia kwa Eli na kumwambia, “Mimi hapa, kwa kuwa umeniita.”

Lakini Eli akasema, “Sikukuita; rudi ukalale.” Hivyo akaenda kulala.

6 Bwanaakaita tena, “Samweli!” Naye Samweli akaamka, kwenda kwa Eli na kusema, “Mimi hapa, kwa kuwa umeniita.”

Eli akasema, “Mwanangu, sikukuita, rudi ukalale.”

7 Wakati huu Samweli alikuwa bado hajamjuaBwana. Neno laBwanalilikuwa bado halijafunuliwa kwake.

8 Bwanaakamwita Samweli mara ya tatu, naye Samweli akaamka kwenda kwa Eli na kusema, “Mimi hapa, kwa kuwa umeniita.”

Ndipo Eli akatambua kuwaBwanaalikuwa akimwita kijana.

9 Hivyo Eli akamwambia Samweli, “Nenda ukalale, na kama akikuita, sema, ‘NenaBwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikiliza.’ ” Hivyo Samweli akaenda na kulala mahali pake.

10 Bwanaakaja akasimama hapo, akiita kama mara zile nyingine, “Samweli! Samweli!”

Kisha Samweli akasema, “NenaBwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikiliza.”

11 NayeBwanaakamwambia Samweli: “Tazama, nipo karibu kufanya kitu katika Israeli ambacho kitafanya masikio ya kila mmoja atakayesikia yawashe.

12 Wakati huo nitatimiza dhidi ya Eli kila kitu nilichonena dhidi ya jamaa yake, kuanzia mwanzo mpaka mwisho.

13 Kwa kuwa nilimwambia kwamba ningehukumu jamaa yake milele kwa sababu ya dhambi aliyoijua, wanawe kumkufuru Mungu, naye akashindwa kuwazuia.

14 Kwa hiyo, nikaapa kuhusu nyumba ya Eli, ‘Hatia ya nyumba ya Eli kamwe haitaweza kufidiwa kwa dhabihu au sadaka.’ ”

15 Samweli akalala mpaka asubuhi, kisha akafungua milango ya nyumba yaBwana. Aliogopa kumwambia Eli yale maono,

16 lakini Eli akamwita na kumwambia, “Samweli mwanangu.”

Samweli akamjibu, “Mimi hapa.”

17 Eli akamuuliza, “Ni nini alichokuambia? Usinifiche.Bwanana ashughulike nawe, tena kwa ukali, kama utanificha chochote alichokuambia.”

18 Kwa hiyo Samweli akamwambia kila kitu, bila kumficha chochote. Ndipo Eli akasema, “Yeye niBwana; na afanye lile lililo jema machoni pake!”

19 Bwanaalikuwa pamoja na Samweli alipokuwa akikua, na hakuacha hata moja ya maneno yake lianguke chini.

20 Nao Israeli wote kuanzia Dani hadi Beer-Sheba wakatambua kuwa Samweli amethibitishwa kuwa nabii waBwana.

21 Bwanaakaendelea kutokea huko Shilo, na huko kujidhihirisha kwa Samweli kwa njia ya neno lake.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1SA/3-361bf88a206e6f8392e895de002b749f.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Samweli

1 Samweli 4

1 Nalo neno la Samweli likaja kwa Israeli yote.

Wafilisti Wateka Sanduku La Mungu

Basi Waisraeli walitoka kwenda kupigana dhidi ya Wafilisti. Waisraeli wakapiga kambi huko Ebenezeri, nao Wafilisti wakapiga kambi huko Afeki.

2 Wafilisti wakapanga safu za majeshi yao kupambana na Israeli, wakati vita vilipoenea, Israeli wakashindwa na Wafilisti, ambao waliwaua askari wa Israeli wapatao 4,000 kwenye uwanja wa vita.

3 Askari waliporudi kambini, wazee wa Israeli wakawauliza, “Kwa niniBwanaameruhusu leo tushindwe mbele ya Wafilisti? Tuleteni Sanduku la Agano laBwanakutoka Shilo, ili lipate kwenda pamoja nasi, na kutuokoa kutoka mikono ya adui zetu.”

4 Hivyo wakawatuma watu huko Shilo, nao wakalichukua Sanduku la Agano laBwanaMwenye Nguvu Zote, aliyekaa kwenye kiti chake cha enzi kati ya makerubi. Nao wale wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, walikuwako huko pamoja na Sanduku la Agano la Mungu.

5 Wakati Sanduku la Agano laBwanalilikuja kambini, Waisraeli wote wakapiga kelele kwa sauti kuu hata ardhi ikatikisika.

6 Wafilisti waliposikia makelele wakauliza, “Ni nini makelele haya yote katika kambi ya Waebrania?”

Walipofahamu kuwa Sanduku laBwanalimekuja kambini,

7 Wafilisti wakaogopa, wakasema, “Mungu amekuja kambini, ole wetu. Halijatokea jambo kama hili tangu hapo.

8 Ole wetu! Ni nani atakayetuokoa kutoka mikononi mwa miungu hii yenye nguvu? Ni miungu ile iliyowapiga Wamisri kwa mapigo ya aina zote huko jangwani.

9 Tuweni hodari, enyi Wafilisti! Tuweni wanaume, la sivyo mtakuwa watumwa wa Waebrania, kama wao walivyokuwa kwenu. Kuweni wanaume, mpigane!”

10 Basi Wafilisti wakapigana, nao Waisraeli wakashindwa na kila mtu akakimbilia hemani mwake. Mauaji yalikuwa makubwa sana, Israeli wakapoteza askari 30,000 waendao kwa miguu.

11 Sanduku la Mungu likatekwa, na hao wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, wakauawa.

Kifo Cha Eli

12 Siku ile ile mtu mmoja wa kabila la Benyamini akakimbia kutoka kwenye uwanja wa vita na kwenda Shilo, nguo zake zikiwa zimeraruka na akiwa na mavumbi kichwani mwake.

13 Alipofika, Eli alikuwa ameketi juu ya kiti chake kando ya barabara akiangalia, kwa sababu moyo wake ulikuwa na hofu kwa ajili ya Sanduku la Mungu. Mtu yule alipoingia mjini na kueleza kilichokuwa kimetokea, mji wote ukalia.

14 Eli akasikia kelele za kilio, naye akauliza, “Ni nini maana ya makelele haya?”

Yule mtu akafanya haraka kwenda kwa Eli,

15 wakati huu Eli alikuwa na miaka tisini na minane nayo macho yake yalikuwa yamepofuka na hakuweza kuona.

16 Akamwambia Eli, “Mimi nimetoka vitani sasa hivi, nimekimbia kutoka huko leo hii.”

Eli akamuuliza, “Je, mwanangu, ni nini kimetokea huko?”

17 Yule mtu aliyeleta habari akajibu, “Israeli amekimbia mbele ya Wafilisti, nalo jeshi limepata hasara kubwa. Pia wana wako wawili, Hofni na Finehasi, wamekufa, na Sanduku la Mungu limetekwa.”

18 Mara alipotaja Sanduku la Mungu, Eli alianguka kutoka kwenye kiti chake kwa nyuma kando ya lango. Shingo yake ikavunjika naye akafa, kwa kuwa alikuwa mzee tena mzito. Alikuwa amewaongoza Israeli kwa miaka arobaini.

19 Mkwewe, mke wa Finehasi, alikuwa mjamzito na karibu wakati wa kujifungua. Aliposikia habari kwamba Sanduku la Mungu limetekwa na ya kuwa baba mkwe wake na mumewe wamekufa, akapata utungu naye akajifungua lakini akazidiwa na utungu.

20 Alipokuwa akifa, wanawake waliokuwa wanamhudumia wakamwambia, “Usikate tamaa, umemzaa mwana.” Lakini hakujibu wala kuweka maanani.

21 Alimwita yule mtoto Ikabodi,akisema, “Utukufu umeondoka katika Israeli,” kwa sababu ya kutekwa kwa Sanduku la Mungu na vifo vya baba mkwe na mumewe.

22 Akasema, “Utukufu umeondoka katika Israeli, kwa kuwa Sanduku la Mungu limetekwa.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1SA/4-3e2ae0d5a7799679163b177c4df8e321.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Samweli

1 Samweli 5

Sanduku La Agano Huko Ashdodi Na Ekroni

1 Baada ya Wafilisti kuteka Sanduku la Mungu, walilichukua kutoka Ebenezeri mpaka Ashdodi.

2 Kisha wakaliingiza lile Sanduku ndani ya hekalu la Dagoni na kuliweka kando ya huyo Dagoni.

3 Watu wa Ashdodi walipoamka asubuhi na mapema kesho yake, kumbe, wakamkuta Dagoni ameanguka chini kifudifudi mbele ya Sanduku laBwana! Wakamwinua Dagoni na kumrudisha mahali pake.

4 Lakini asubuhi iliyofuata, walipoamka kumbe, walimkuta huyo Dagoni ameanguka chini kifudifudi mbele ya Sanduku laBwana! Kichwa chake na mikono vilikuwa vimevunjwa navyo vimelala kizingitini, ni kiwiliwili chake tu kilichokuwa kimebaki.

5 Ndiyo sababu mpaka leo makuhani wa Dagoni wala wengine waingiao katika hekalu la Dagoni huko Ashdodi hawakanyagi kizingiti.

6 Mkono waBwanaulikuwa mzito juu ya watu wa Ashdodi na vijiji jirani, akaleta uharibifu juu yao na kuwatesa kwa majipu.

7 Watu wa Ashdodi walipoona kile kilichokuwa kikitokea, wakasema, “Sanduku la Mungu wa Israeli kamwe lisikae hapa pamoja na sisi, kwa sababu mkono wake ni mzito juu yetu na juu ya Dagoni mungu wetu.”

8 Basi wakawaita watawala wote wa Wafilisti pamoja na kuwauliza, “Tutafanya nini na hili Sanduku la Mungu wa Israeli?”

Wakajibu, “Sanduku la Mungu wa Israeli na liende Gathi.” Basi wakalihamisha Sanduku la Mungu wa Israeli.

9 Lakini baada ya kulihamisha, mkono waBwanaulikuwa dhidi ya huo mji wa Gathi, akiuweka katika fadhaa kuu. Mungu akawatesa watu wa huo mji, vijana kwa wazee, kwa kuwaletea majipu.

10 Basi wakapeleka Sanduku la Mungu Ekroni.

Wakati Sanduku la Mungu lilipokuwa linaingia Ekroni, watu wa Ekroni walilia wakisema “Wamelileta Sanduku la Mungu wa Israeli kwetu ili kutuua sisi na watu wetu.”

11 Basi wakawaita watawala wote wa Wafilisti pamoja na kusema, “Liondoeni Sanduku la Mungu wa Israeli na lirudishwe mahali pake, la sivyo litatuua sisi na watu wetu.” Kwa kuwa kifo kilikuwa kimeujaza mji hofu; kwani mkono wa Mungu ulikuwa mzito sana juu yake.

12 Wale ambao hawakufa walipatwa na majipu, na kilio cha mji kilikwenda juu hadi mbinguni.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1SA/5-ec28e10fe674ac2c5eb7b839a8737e43.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Samweli

1 Samweli 6

Sanduku La Mungu Larudishwa Israeli

1 Sanduku laBwanalilipokuwa limekaa katika nchi ya Wafilisti kwa miezi saba,

2 Wafilisti waliwaita makuhani wa Dagoni na waaguzi, na kuwaambia, “Tutafanya nini na hili Sanduku laBwana? Tuambieni jinsi tutakavyolirudisha mahali pake.”

3 Wakajibu, “Kama mtalirudisha Sanduku la Mungu wa Israeli, msilirudishe mikono mitupu bali kwa vyovyote mpelekeeni sadaka ya hatia. Kisha mtaponywa, nanyi mtafahamu kwa nini mkono wake haujaondolewa kwenu.”

4 Wafilisti wakawauliza, “Ni sadaka gani ya hatia tutakayompelekea?”

Wakajibu, “Majipu matano ya dhahabu na panya wa dhahabu watano, kulingana na idadi ya watawala wa Wafilisti, kwa sababu tauni iyo hiyo imewaua ninyi na watawala wenu.

5 Tengenezeni mifano ya majipu na ya panya wale wanaoharibu nchi yenu, nanyi mheshimuni Mungu wa Israeli. Labda ataondoa mkono wake kutoka kwenu na kwa miungu yenu na nchi yenu.

6 Kwa nini ninyi mnafanya mioyo yenu migumu kama Wamisri na Farao walivyofanya? Je, alipowatendea kwa ukali, hawakuwaachia Waisraeli wakaenda zao?

7 “Sasa basi, wekeni gari jipya la kukokotwa pamoja na ngʼombe wawili ambao wamezaa lakini ambao kamwe hawajafungwa nira. Fungieni hao ngʼombe hilo gari, lakini ondoeni ndama wao na mwaweke zizini.

8 Chukueni hilo Sanduku laBwanana mliweke juu ya gari la kukokotwa, na ndani ya kasha kando yake wekeni hivyo vitu vya dhahabu mnavyompelekeaBwanakama sadaka ya hatia. Lipelekeni,

9 lakini liangalieni kwa makini. Iwapo litakwenda katika nchi yake lenyewe, kuelekea Beth-Shemeshi, basi tutajua kwambaBwanandiye alileta haya maafa makubwa juu yetu. Lakini kama halikwenda, basi tutajua kwamba haukuwa mkono waBwanauliotupiga na kwamba iliyotokea kwetu ni ajali.”

10 Basi wakafanya hivyo. Wakachukua ngʼombe wawili wa aina hiyo, wakawafungia hilo gari la kukokotwa, nao ndama wao wakawekwa zizini.

11 Wakaliweka Sanduku laBwanajuu ya hilo gari la kukokotwa pamoja na lile kasha lenye ile mifano ya panya wa dhahabu na ya majipu ya dhahabu.

12 Kisha hao ngʼombe wakaenda moja kwa moja kuelekea Beth-Shemeshi, wakishuka bila kugeuka kuume au kushoto, huku wakilia njia yote. Watawala wa Wafilisti waliwafuata hao ngʼombe hadi mpakani mwa Beth-Shemeshi.

13 Wakati huu watu wa Beth-Shemeshi walikuwa wakivuna ngano yao huko bondeni, walipoinua macho yao na kuona lile Sanduku, wakafurahi kuliona.

14 Lile gari la kukokotwa lilikuja mpaka kwenye shamba la Yoshua wa Beth-Shemeshi, nalo likasimama kando ya mwamba mkubwa. Watu wakapasua mbao za lile gari la kukokotwa na kutoa dhabihu wale ngʼombe kama sadaka ya kuteketezwa kwaBwana.

15 Walawi walilishusha Sanduku laBwana, pamoja na lile kasha lililokuwa na vile vitu vya dhahabu na kuviweka juu ya ule mwamba mkubwa. Siku ile watu wa Beth-Shemeshi wakatoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu kwaBwana.

16 Wale watawala watano wa Wafilisti waliona haya yote, nao wakarudi siku ile ile mpaka Ekroni.

17 Haya ndiyo yale majipu ya dhahabu Wafilisti waliyotuma kama sadaka ya hatia kwaBwana, moja kwa ajili ya Ashdodi, moja kwa Gaza, moja kwa Ashkeloni, moja kwa Gathi, na moja kwa Ekroni.

18 Nayo hesabu ya wale panya wa dhahabu ilikuwa kulingana na idadi ya miji ya Wafilisti ya watawala watano wa Wafilisti: miji yao iliyozungukwa na maboma, pamoja na vijiji vya miji hiyo. Ule mwamba mkubwa, ambao juu yake waliliweka lile Sanduku laBwana, ni ushahidi hadi leo katika shamba la Yoshua wa Beth-Shemeshi.

19 Lakini Mungu aliwapiga baadhi ya watu wa Beth-Shemeshi, akiwaua watu sabini miongoni mwao kwa sababu walichungulia ndani ya Sanduku laBwana. Watu wakaomboleza kwa sababu ya pigo zito kutoka kwaBwana,

20 nao watu wa Beth-Shemeshi wakauliza, “Ni nani awezaye kusimama mbele zaBwana, huyu Mungu aliye mtakatifu? Sanduku litapanda kwenda kwa nani kutoka hapa?”

21 Kisha wakatuma wajumbe kwa watu wa Kiriath-Yearimu, wakisema, “Wafilisti wamerudisha Sanduku laBwana. Shukeni na mlipandishe huko kwenu.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1SA/6-1dedbf2c43bb98e39b5e3cfeeb80678b.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Samweli

1 Samweli 7

1 Kisha watu wa Kiriath-Yearimu wakaja na kulichukua Sanduku laBwana. Wakalipeleka katika nyumba ya Abinadabu juu kilimani na kumweka Eleazari mwanawe wakfu kulichunga Sanduku laBwana.

Samweli Awatiisha Wafilisti Huko Mispa

2 Sanduku laBwanalilibakia huko Kiriath-Yearimu kwa muda mrefu, yaani jumla ya miaka ishirini, nao watu wa Israeli wakaomboleza na kumtafutaBwana.

3 Naye Samweli akawaambia nyumba yote ya Israeli, “Ikiwa mtamrudiaBwanakwa mioyo yenu yote, basi iacheni miungu migeni na Maashtorethi na kujitoa wenyewe kwaBwanana kumtumikia yeye peke yake, naye atawaokoa ninyi na mkono wa Wafilisti.”

4 Hivyo Waisraeli wakaweka mbali Mabaali yao na Maashtorethi, nao wakamtumikiaBwanapeke yake.

5 Kisha Samweli akasema, “Wakusanyeni Israeli wote huko Mispa, nami nitawaombea ninyi kwaBwana.”

6 Walipokwisha kukutanika huko Mispa, walichota maji na kuyamimina mbele zaBwana. Siku hiyo walifunga na wakaungama, wakisema, “Tumetenda dhambi dhidi yaBwana.” Naye Samweli alikuwa kiongoziwa Israeli huko Mispa.

7 Wafilisti waliposikia kwamba Israeli wamekusanyika huko Mispa, watawala wa Wafilisti wakapanda ili kuwashambulia. Waisraeli waliposikia habari hiyo, waliogopa kwa sababu ya Wafilisti.

8 Wakamwambia Samweli, “Usiache kumliliaBwana, Mungu wetu, kwa ajili yetu, ili apate kutuokoa na mikono ya Wafilisti.”

9 Kisha Samweli akamchukua mwana-kondoo anyonyaye na kumtoa mzima kama sadaka ya kuteketezwa kwaBwana. AkamliliaBwanakwa niaba ya Israeli, nayeBwanaakamjibu.

10 Samweli alipokuwa anatoa hiyo dhabihu ya kuteketezwa, Wafilisti wakasogea karibu ili kupigana vita na Israeli. Lakini siku ileBwanaalinguruma kwa ngurumo kubwa dhidi ya Wafilisti na kuwafanya wafadhaike na kutetemeka hivi kwamba walikimbizwa mbele ya Waisraeli.

11 Watu wa Israeli wakatoka mbio huko Mispa na kuwafuatia Wafilisti, wakiwachinja njiani hadi mahali chini ya Beth-Kari.

12 Ndipo Samweli akachukua jiwe na kulisimamisha kati ya Mispa na Sheni. Akaliita Ebenezeri,akisema, “Hata sasaBwanaametusaidia.”

13 Basi Wafilisti wakashindwa na hawakuvamia nchi ya Israeli tena.

Katika maisha yote ya Samweli, mkono waBwanaulikuwa dhidi ya Wafilisti.

14 Miji kuanzia Ekroni hadi Gathi, ile ambayo Wafilisti walikuwa wameiteka kutoka Israeli, ilirudishwa kwake, naye Israeli akazikomboa nchi jirani mikononi mwa Wafilisti. Kukawepo amani kati ya Israeli na Waamori.

15 Samweli akaendelea kama mwamuzi juu ya Israeli siku zote za maisha yake.

16 Mwaka hadi mwaka aliendelea kuzunguka kutoka Betheli mpaka Gilgali na Mispa, akiamua Israeli katika sehemu hizo zote.

17 Lakini kila mara alirudi Rama, kulikokuwa nyumbani kwake, huko pia aliwaamua Israeli. Naye huko alimjengeaBwanamadhabahu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1SA/7-8b441ad35427c44bf58cb20459f1bda5.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Samweli

1 Samweli 8

Israeli Waomba Mfalme

1 Samweli alipokuwa mzee, akaweka wanawe kuwa waamuzi wa Israeli.

2 Mzaliwa wa kwanza alikuwa Yoeli, na la wa pili lilikuwa Abiya, nao wakatumika huko Beer-Sheba.

3 Lakini wanawe hawakuenenda katika njia zake. Waliziacha wakageukia faida za udanganyifu nao wakapokea rushwa na kupotosha haki.

4 Basi wazee wote wa Israeli wakakusanyika pamoja na kumjia Samweli huko Rama.

5 Wakamwambia, “Wewe umekuwa mzee, nao wanao hawaenendi katika njia zako, sasa tuteulie mfalme wa kutuongoza, kama ilivyo kwa mataifa mengine yote.”

6 Lakini wao waliposema, “Tupe mfalme wa kutuongoza,” hili lilimchukiza Samweli, hivyo akamwombaBwana.

7 NayeBwanaakamwambia: “Sikiliza yale yote watu wanakuambia. Si wewe ambaye wamekukataa, bali wamenikataa mimi kuwa mfalme wao.

8 Kama vile walivyofanya tangu siku nilipowapandisha kutoka Misri mpaka siku hii ya leo; wakiniacha mimi na kutumikia miungu mingine, ndivyo wanavyokufanyia wewe.

9 Sasa wasikilize, lakini waonye kwa makini na uwafahamishe yale watakayotendewa na mfalme atakayewatawala.”

10 Samweli akawaambia wale watu waliokuwa wakiomba wapewe mfalme maneno yote yaBwana.

11 Akasema, “Hivi ndivyo atakavyowatendea mfalme atakayewatawala. Atawachukua wana wenu na kuwafanya watumike kwa magari yake ya vita na farasi, nao watakimbia mbele ya magari yake.

12 Baadhi yao atawaweka kuwa majemadari wa jeshi wa maelfu na majemadari wa jeshi wa hamsini, wengine kulima mashamba yake na kuvuna mavuno yake, pia na wengine kutengeneza silaha za vita na vifaa kwa ajili ya magari yake.

13 Atawachukua binti zenu kuwa watengeneza manukato, wapishi na waokaji.

14 Atayachukua mashamba yenu yaliyo mazuri, mashamba ya mizabibu na mashamba yenu ya mizeituni na kuwapa watumishi wake.

15 Ataichukua sehemu ya kumi ya nafaka yenu na ya zabibu zenu na kuwapa maafisa wake na watumishi wake.

16 Atawachukua watumishi wenu wa kiume na wa kike, na ngʼombe wenu walio wazuri sana na punda kwa matumizi yake mwenyewe.

17 Atachukua sehemu ya kumi ya makundi yenu ya kondoo na mbuzi, na ninyi wenyewe mtakuwa watumwa wake.

18 Siku ile itakapowadia, mtalia kwa kutaka msaada kutokana na mfalme mliyemchagua, nayeBwanahatawajibu.”

19 Lakini watu wakakataa kumsikiliza Samweli wakasema, “Hapana! Tunataka mfalme wa kututawala.

20 Kisha tutakuwa kama mataifa mengine yote, tukiwa na mfalme wa kutuongoza na kwenda mbele yetu na kutupigania vita vyetu.”

21 Samweli aliposikia yote watu waliyosema, akarudia kuyasema mbele zaBwana.

22 Bwanaakamjibu, “Wasikilize na uwape mfalme.”

Kisha Samweli akawaambia watu wa Israeli, “Kila mmoja arudi mjini kwake.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1SA/8-1a368e3a90d322c9e3439d482f5e4df4.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Samweli

1 Samweli 9

Samweli Anamtia Sauli Mafuta

1 Kulikuwako Mbenyamini mmoja, mtu maarufu, ambaye aliitwa Kishi mwana wa Abieli, mwana wa Serori, mwana wa Bekorathi, mwana wa Afia wa Benyamini.

2 Alikuwa na mwana aliyeitwa Sauli, kijana anayevutia sana, hakuwepo aliyelingana naye miongoni mwa Waisraeli, alikuwa mrefu kuliko wengine wote.

3 Basi punda wa Kishi baba yake Sauli walipotea, naye Kishi akamwambia mwanawe Sauli, “Mchukue mmoja wa watumishi mwende pamoja naye kuwatafuta punda.”

4 Hivyo akapita katika nchi ya vilima ya Efraimu na katika eneo la Shalisha, lakini hawakuwapata. Wakaendelea katika sehemu ya Shaalimu, lakini punda hawakuwepo huko. Kisha wakapita katika nchi ya Benyamini, lakini hawakuwapata.

5 Walipofika sehemu ya Sufu, Sauli akamwambia mtumishi aliyekuwa pamoja naye, “Njoo, sisi na turudi, au baba yangu ataacha kufikiria juu ya punda na kuanza kufadhaika kutuhusu sisi.”

6 Lakini mtumishi akajibu, “Tazama, katika mji huu yupo mtu wa Mungu, anayeheshimiwa sana na kila kitu asemacho hutokea kweli. Sasa na twende huko. Huenda atatuambia twende njia ipi.”

7 Sauli akamwambia mtumishi wake, “Kama tukienda, tutampa nini huyo mtu? Chakula kimekwisha kwenye mifuko yetu. Hatuna zawadi ya kumpelekea huyo mtu wa Mungu. Je tuna nini?”

8 Mtumishi akamjibu Sauli tena, akasema, “Tazama, nina fedha robo shekeli.Hiyo nitampa huyo mtu wa Mungu ili aweze kutuambia twende kwa njia ipi.”

9 (Zamani katika Israeli, kama mtu alikwenda kuuliza neno kwa Mungu, angalisema, “Njoo na twende kwa mwonaji,” kwa sababu nabii wa sasa alikuwa akiitwa mwonaji.)

10 Sauli akamwambia mtumishi wake, “Vyema, njoo na twende.” Basi wakaenda mjini alipokuwepo huyo mtu wa Mungu.

11 Walipokuwa wakipanda mlima kwenda mjini, wakakutana na baadhi ya wasichana wanakuja kuchota maji, nao wakawauliza, “Je, mwonaji yuko?”

12 Wakajibu, “Yuko, yu mbele yenu amewatangulia, sasa fanyeni haraka, ndiyo tu amekuja mjini kwetu leo, kwa kuwa watu wana dhabihu huko mahali pa juu.

13 Mara tu mwingiapo mjini, mtamkuta kabla hajapanda kwenda mahali pa juu kula. Watu hawataanza kula mpaka atakapofika kwa sababu ni lazima kwanza yeye abariki dhabihu, ndipo wale walioalikwa watakapokula. Pandeni sasa, mtamkuta kwa wakati huu.”

14 Wakapanda mjini, nao walipokuwa wakiingia mjini, tazama, Samweli alikuwa akija kuelekea walikokwenda mahali pa juu.

15 Basi siku moja kabla Sauli hajaja,Bwanaalikuwa amemfunulia Samweli jambo hili:

16 “Kesho wakati kama huu nitakupelekea mtu kutoka nchi ya Benyamini. Umtie mafuta awe kiongozi juu ya watu wangu Israeli, ndiye atakayewakomboa watu wangu na mkono wa Wafilisti. Nimewaangalia watu wangu, kwa kuwa kilio chao kimenifikia.”

17 Samweli alipomwona Sauli,Bwanaakamwambia, “Huyu ndiye mtu niliyekuambia habari zake, kwamba yeye atawatawala watu wangu.”

18 Sauli akamkaribia Samweli langoni na kumuuliza, “Tafadhali, je, waweza kuniambia mahali nyumba ya mwonaji ilipo?”

19 Samweli akamjibu Sauli, “Mimi ndiye mwonaji, panda utangulie mbele yangu mpaka mahali pa juu, kwa kuwa leo itakupasa kula pamoja nami na asubuhi nitakuruhusu uende na nitakuambia yale yote yaliyo moyoni mwako.

20 Kuhusu wale punda uliowapoteza siku tatu zilizopita, usifadhaike kwa habari yao; wamepatikana. Ni kwa nani ambaye shauku yote ya Israeli imeelekea, kama si kwako na jamaa yote ya baba yako?”

21 Sauli akajibu, “Je, mimi si Mbenyamini, kutoka kabila dogo kuliko yote ya Israeli, nao ukoo wangu si ndio mdogo kuliko koo zote za kabila la Benyamini? Kwa nini uniambie jambo la namna hiyo?”

22 Kisha Samweli akamleta Sauli na mtumishi wake ndani ukumbini na kuwaketisha mahali pa heshima zaidi miongoni mwa wale waliokuwa wamealikwa; jumla yao walikuwa kama watu thelathini.

23 Samweli akamwambia mpishi, “Leta ile sehemu ya nyama niliyokupa, ile niliyokuambia iweke kando.”

24 Hivyo mpishi akachukua mguu pamoja na kile kilichokuwa juu yake akaiweka mbele ya Sauli. Samweli akasema, “Hiki ndicho ambacho kimewekwa kwa ajili yako. Ule, kwa sababu kilitengwa kwa ajili yako kwa tukio hili, tangu niliposema, ‘Nimewaalika wageni.’ ” Naye Sauli akala pamoja na Samweli siku ile.

25 Baada ya kushuka kutoka mahali pa juu na kufika mjini, Samweli alizungumza na Sauli juu ya dari ya nyumba yake.

26 Walipoamka mapema alfajiri, Samweli akamwita Sauli darini, akamwambia, “Jiandae, nami nitakuaga uende zako.” Sauli alipokuwa tayari yeye na Samweli wakatoka nje pamoja.

27 Hata walipokuwa wakiteremka kuelekea mwisho wa mji, Samweli akamwambia Sauli, “Mwambie mtumishi atangulie mbele yetu.” Naye mtumishi akafanya hivyo. “Lakini subiri hapa kwa kitambo kidogo, ili nipate kukupa ujumbe kutoka kwa Mungu.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1SA/9-b9ee713094a5de06d961451e2a0ba8e4.mp3?version_id=1627—