Categories
Zaburi

Zaburi 54

Kuomba Ulinzi Wa Mungu Kutokana Na Adui

Kwa mwimbishaji. Na ala za nyuzi za uimbaji. Utenzi wa Daudi. Wakati Wazifu walimwendea Sauli na kumjulisha, “Je, Daudi hajifichi miongoni mwetu?”

1 Ee Mungu uniokoe kwa jina lako,

unifanyie hukumu kwa uwezo wako.

2 Ee Mungu, sikia maombi yangu,

usikilize maneno ya kinywa changu.

3 Wageni wananishambulia,

watu wakatili wanayatafuta maisha yangu,

watu wasiomjali Mungu.

4 Hakika Mungu ni msaada wangu,

Bwana ndiye anayenitegemeza.

5 Mabaya na yawarudie wale wanaonisingizia,

kwa uaminifu wako uwaangamize.

6 Nitakutolea dhabihu za hiari;

EeBwana, nitalisifu jina lako

kwa kuwa ni vyema.

7 Kwa maana ameniokoa katika shida zangu zote,

na macho yangu yamewatazama adui zangu kwa ushindi.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/54-d49c4c9ba5831ca660230c77e7a26ee4.mp3?version_id=1627—

Categories
Zaburi

Zaburi 55

Maombi Ya Mtu Aliyesalitiwa Na Rafiki

Kwa mwimbishaji. Na ala za uimbaji. Utenzi wa Daudi.

1 Ee Mungu, sikiliza maombi yangu,

wala usidharau hoja yangu.

2 Nisikie na unijibu.

Mawazo yangu yananisumbua na nimehangaishwa

3 kwa sauti ya adui,

kwa kukaziwa macho na waovu,

kwa sababu wananiletea mateso juu yangu

na kunitukana kwa hasira zao.

4 Moyo wangu umejaa uchungu,

hofu ya kifo imenishambulia.

5 Woga na kutetemeka vimenizunguka,

hofu kuu imenigharikisha.

6 Nilisema, “Laiti ningekuwa na mbawa za njiwa!

Ningeruka niende mbali kupumzika.

7 Ningalitorokea mbali sana

na kukaa jangwani,

8 ningaliharakisha kwenda mahali pa salama,

mbali na tufani kali na dhoruba.”

9 EeBwana, uwatahayarishe waovu

na uwachanganyishie semi zao,

maana nimeona jeuri na ugomvi mjini.

10 Usiku na mchana wanazunguka juu ya kuta zake,

uovu na dhuluma vimo ndani yake.

11 Nguvu za uharibifu zinatenda kazi mjini,

vitisho na uongo haviondoki mitaani mwake.

12 Kama aliyenitukana ni adui yangu, ningevumilia,

kama mtu mwovu angejiinua dhidi yangu,

ningejificha asinione.

13 Kumbe ni wewe, mwenzangu,

mshiriki na rafiki yangu wa karibu,

14 ambaye awali tulifurahia ushirika mzuri,

tulipokuwa tukienda na umati hekaluni mwa Mungu.

15 Kifo na kiwajie adui zangu ghafula,

na washuke kuzimu wangali hai,

kwa maana uovu upo ndani yao.

16 Lakini ninamwita Mungu,

nayeBwanahuniokoa.

17 Jioni, asubuhi na adhuhuri

ninalia kwa huzuni,

naye husikia sauti yangu.

18 Huniokoa nikawa salama katika vita

vilivyopangwa dhidi yangu,

ingawa watu wengi hunipinga.

19 Mungu anayemiliki milele,

atawasikia na kuwaadhibu,

watu ambao hawabadilishi njia zao,

wala hawana hofu ya Mungu.

20 Mwenzangu hushambulia rafiki zake,

naye huvunja agano lake.

21 Mazungumzo yake ni laini kama siagi,

hata hivyo vita vimo moyoni mwake.

Maneno yake ni mororo kuliko mafuta,

hata hivyo ni upanga mkali uliofutwa.

22 MtwikeBwanafadhaa zako,

naye atakutegemeza,

hatamwacha kamwe mwenye haki wake aanguke.

23 Lakini wewe, Ee Mungu,

utawashusha waovu katika shimo la uharibifu.

Wenye kiu ya kumwaga damu na wenye hila,

hawataishi nusu ya siku zao.

Lakini mimi ninakutumaini wewe.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/55-3175e503e9a8a5521761076cc2711731.mp3?version_id=1627—

Categories
Zaburi

Zaburi 56

Kumtumaini Mungu

Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Njiwa mkimya wa mbali.” Utenzi wa Daudi. Baada ya kukamatwa na Wafilisti huko Gathi.

1 Ee Mungu unihurumie, maana watu wananifuatia vikali;

mchana kutwa wanazidisha mashambulizi yao.

2 Wasingiziaji wangu wananifuatia mchana kutwa,

wengi wananishambulia kwa kiburi chao.

3 Wakati ninapoogopa,

nitakutumaini wewe.

4 Katika Mungu, ambaye neno lake ninalisifu,

katika Mungu ninatumaini; sitaogopa.

Mwanadamu apatikanaye na kufa,

atanitenda nini?

5 Mchana kutwa wanayageuza maneno yangu,

siku zote wanapanga shauri la kunidhuru.

6 Wananifanyia hila, wanajificha,

wanatazama hatua zangu,

wakiwa na shauku ya kuutoa uhai wangu.

7 Wasiepuke kwa vyovyote,

Ee Mungu, katika hasira yako yaangushe mataifa.

8 Andika maombolezo yangu,

orodhesha machozi yangu katika gombo lako:

je, haya hayapo katika kumbukumbu zako?

9 Ndipo adui zangu watarudi nyuma

ninapoita msaada.

Kwa hili nitajua kwamba Mungu

yuko upande wangu.

10 Katika Mungu, ambaye neno lake ninalisifu,

katikaBwana, ambaye neno lake ninalisifu,

11 katika Mungu ninatumaini, sitaogopa.

Mwanadamu anaweza kunitenda nini?

12 Ee Mungu, nina nadhiri kwako,

nitakutolea wewe sadaka zangu za shukrani.

13 Kwa kuwa umeniokoa toka kwenye mauti

na miguu yangu kwenye kujikwaa,

ili niweze kuenenda mbele za Mungu

katika nuru ya uzima.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/56-f0003c24e12c7c001b28418bb94b4285.mp3?version_id=1627—

Categories
Zaburi

Zaburi 57

Kuomba Msaada

Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Usiharibu!” Utenzi wa Daudi. Baada ya kumponyoka Sauli pangoni.

1 Unihurumie, Ee Mungu, unihurumie,

kwa maana nafsi yangu inakukimbilia.

Chini ya uvuli wa mbawa zako nitakimbilia

mpaka maafa yapite.

2 Namlilia Mungu Aliye Juu Sana,

Mungu atimizaye makusudi yake kwangu.

3 Hutumana kutoka mbinguni na kuniokoa,

akiwakemea wale wanaonifuatilia vikali;

Mungu huutuma upendo wake na uaminifu wake.

4 Niko katikati ya simba,

nimelala katikati ya wanyama wenye njaa kuu:

watu ambao meno yao ni mikuki na mishale,

ambao ndimi zao ni panga kali.

5 Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu,

utukufu wako na uenee duniani kote.

6 Waliitegea miguu yangu nyavu,

nikainamishwa chini na dhiki.

Wamechimba shimo katika njia yangu,

lakini wametumbukia humo wao wenyewe.

7 Ee Mungu, moyo wangu ni thabiti;

nitaimba na kusifu kwa moyo wangu wote.

8 Amka, nafsi yangu!

Amka, kinubi na zeze!

Nitayaamsha mapambazuko.

9 Nitakusifu wewe, EeBwana, katikati ya mataifa;

nitaimba habari zako, katikati ya jamaa za watu.

10 Kwa maana upendo wako ni mkuu, waenea hadi mbinguni,

uaminifu wako unazifikia anga.

11 Ee Mungu, utukuzwe juu mbinguni,

utukufu wako na uwe duniani pote.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/57-1a616b85bc55b04c8c07c200ab7055be.mp3?version_id=1627—

Categories
Zaburi

Zaburi 58

Mungu Kuwaadhibu Waovu

Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Usiharibu!” Utenzi wa Daudi.

1 Enyi watawala, je, kweli mwanena kwa haki?

Je, mnahukumu kwa unyofu miongoni mwa watu?

2 La, mioyoni mwenu mnatunga udhalimu,

na mikono yenu hupima jeuri duniani.

3 Waovu ni wapotovu tangu kuzaliwa kwao,

toka tumboni mwa mama zao

ni wakaidi na husema uongo.

4 Sumu yao ni kama sumu ya nyoka,

kama ile ya fira ambaye ameziba masikio yake,

5 ambaye hatasikia sauti ya kutumbuiza ya mwaguzi,

hata kama mganga angecheza kwa ustadi kiasi gani.

6 Ee Mungu, yavunje meno katika vinywa vyao;

EeBwana, vunja meno makali ya hao simba!

7 Na watoweke kama maji yapitayo kwa kasi,

wavutapo pinde zao, mishale yao na iwe butu.

8 Kama konokono ayeyukavyo akitembea,

kama mtoto aliyezaliwa akiwa mfu,

wasilione jua.

9 Kabla vyungu vyenu havijapata moto wa kuni za miiba,

zikiwa mbichi au kavu,

waovu watakuwa

wamefagiliwa mbali.

10 Wenye haki watafurahi waonapo wakilipizwa kisasi,

watakapochovya nyayo zao katika damu ya waovu.

11 Ndipo wanadamu watasema,

“Hakika utulivu wa wenye haki bado una thawabu,

hakika kuna Mungu ahukumuye dunia.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/58-08ae4a791ab7ffb065875e6c58cfcf43.mp3?version_id=1627—

Categories
Zaburi

Zaburi 59

Kuomba Ulinzi Wa Mungu

Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Usiharibu!” Utenzi wa Daudi. Wakati Sauli alipotuma wapelelezi nyumbani mwa Daudi ili wamuue.

1 Ee Mungu, uniokoe na adui zangu,

unilinde kutokana na hao wanaoinuka dhidi yangu.

2 Uniponye na watu watendao mabaya,

uniokoe kutokana na wamwagao damu.

3 Tazama wanavyonivizia!

Watu wakali wananifanyia hila,

ingawa EeBwana, mimi sijakosea

wala kutenda dhambi.

4 Sijatenda kosa; hata hivyo wako tayari kunishambulia.

Inuka unisaidie, uone hali yangu mbaya!

5 EeBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli!

Zinduka uyaadhibu mataifa yote,

usionyeshe huruma kwa wasaliti.

6 Hurudi wakati wa jioni,

wakibweka kama mbwa,

wakiuzurura mji.

7 Tazama yale wanayotema kutoka vinywa vyao,

hutema upanga kutoka midomo yao,

nao husema, “Ni nani atakayetusikia?”

8 Lakini wewe,Bwana, uwacheke;

unayadharau mataifa hayo yote.

9 Ee nguvu yangu, ninakutazama wewe,

wewe, Ee Mungu, ndiwe ngome yangu,

10 Mungu wangu unipendaye.

Mungu atanitangulia,

naye atanifanya niwachekelee

wale wanaonisingizia.

11 Lakini usiwaue, EeBwana, ngao yetu,

au sivyo watu wangu watasahau.

Katika uwezo wako wafanye watangetange

na uwashushe chini.

12 Kwa ajili ya dhambi za vinywa vyao,

kwa ajili ya maneno ya midomo yao,

waache wanaswe katika kiburi chao.

Kwa ajili ya laana na uongo wanaotamka,

13 wateketeze katika ghadhabu,

wateketeze hadi wasiwepo tena.

Ndipo itakapofahamika katika miisho ya dunia

kwamba Mungu anatawala juu ya Yakobo.

14 Hurudi jioni,

wakibweka kama mbwa,

wakiuzurura mji.

15 Wanatangatanga wakitafuta chakula,

wasipotosheka hubweka kama mbwa.

16 Lakini mimi nitaziimba nguvu zako,

asubuhi nitaimba juu ya upendo wako;

kwa maana wewe ndiwe ngome yangu

na kimbilio langu wakati wa shida.

17 Ee uliye Nguvu zangu, ninakuimbia sifa.

Wewe, Ee Mungu, ndiwe ngome yangu,

Mungu unipendaye.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/59-00e3ed39a1437da771044d392663d592.mp3?version_id=1627—

Categories
Zaburi

Zaburi 60

Kuomba Kuokolewa

Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Shushani Eduthi.” Utenzi wa Daudi wa kufundisha. Wakati alipopigana na Waaramu kutoka Aramu-Naharaimu na Aramu-Soba, naye Yoabu akarudi nyuma na kuwaua Waedomu 12,000 katika Bonde la Chumvi.

1 Ee Mungu, umetukataa na kutokea ghafula juu yetu,

umekasirika: sasa turejeshe upya!

2 Umetetemesha nchi na kuipasua;

uiponye mavunjiko yake, kwa maana inatetemeka.

3 Umewaonyesha watu wako nyakati za kukata tamaa;

umetunywesha mvinyo unaotuyumbisha.

4 Kwa wale wanaokucha wewe,

umewainulia bendera,

ili iweze kutwekwa dhidi ya upinde.

5 Tuokoe na utusaidie kwa mkono wako wa kuume,

ili wale uwapendao wapate kuokolewa.

6 Mungu amenena kutoka patakatifu pake:

“Nitaigawa Shekemu kwa ushindi

na kulipima Bonde la Sukothi.

7 Gileadi ni yangu na Manase ni yangu;

Efraimu ni kofia yangu ya chuma,

nayo Yuda ni fimbo yangu ya utawala.

8 Moabu ni sinia langu la kunawia,

juu ya Edomu natupa kiatu changu;

nashangilia kwa kushindwa kwa Ufilisti.”

9 Ni nani atakayenipeleka hadi mji wenye ngome?

Ni nani atakayeniongoza hadi nifike Edomu?

10 Ee Mungu, si ni wewe uliyetukataa sisi,

na hutoki tena na majeshi yetu?

11 Tuletee msaada dhidi ya adui,

kwa maana msaada wa mwanadamu haufai kitu.

12 Kwa msaada wa Mungu tutapata ushindi,

naye atawaponda adui zetu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/60-1f5cd29a55f6c20cc05ab78c548a317c.mp3?version_id=1627—

Categories
Zaburi

Zaburi 61

Kuomba Ulinzi

Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za uimbaji. Zaburi ya Daudi.

1 Ee Mungu, sikia kilio changu,

usikilize maombi yangu.

2 Kutoka miisho ya dunia ninakuita,

ninaita huku moyo wangu unadhoofika;

uniongoze kwenye mwamba

ule ulio juu kuliko mimi.

3 Kwa kuwa umekuwa kimbilio langu,

ngome imara dhidi ya adui.

4 Natamani kukaa hemani mwako milele,

na kukimbilia chini ya uvuli wa mbawa zako.

5 Ee Mungu, kwa kuwa umesikia nadhiri zangu,

umenipa urithi wa wale wanaoliogopa jina lako.

6 Mwongezee mfalme siku za maisha yake,

miaka yake kwa vizazi vingi.

7 Yeye na atawazwe kwenye kiti cha enzi mbele za Mungu milele;

amuru upendo wako na uaminifu wako vimlinde.

8 Ndipo daima nitaliimbia sifa jina lako

na kuzitimiza nadhiri zangu siku baada ya siku.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/61-3ac274c7c3493b29ad55324abf7cd5cb.mp3?version_id=1627—

Categories
Zaburi

Zaburi 62

Mungu Kimbilio La Pekee

Kwa mwimbishaji. Mtindo wa Yeduthuni. Zaburi ya Daudi.

1 Kwa Mungu peke yake nafsi yangu inapata pumziko;

wokovu wangu watoka kwake.

2 Yeye peke yake ndiye mwamba wangu na wokovu wangu;

yeye ni ngome yangu, sitatikisika kamwe.

3 Mtamshambulia mtu hata lini?

Je, ninyi nyote mtamtupa chini,

ukuta huu ulioinama na uzio huu unaotikisika?

4 Walikusudia kikamilifu kumwangusha

toka mahali pake pa fahari;

wanafurahia uongo.

Kwa vinywa vyao hubariki,

lakini ndani ya mioyo yao hulaani.

5 Ee nafsi yangu, upumzike, kwa Mungu peke yake,

tumaini langu latoka kwake.

6 Yeye peke yake ndiye mwamba wangu na wokovu wangu;

ndiye ngome yangu, sitatikisika.

7 Wokovu wangu na heshima yangu viko kwa Mungu,

ndiye mwamba wangu wenye nguvu

na kimbilio langu.

8 Enyi watu, mtumainini yeye wakati wote,

miminieni mioyo yenu kwake,

kwa kuwa Mungu ni kimbilio letu.

9 Binadamu wa ngazi ya chini ni pumzi tu,

nao wa ngazi ya juu ni uongo tu;

wakipimwa kwenye mizani, si chochote;

wote kwa pamoja ni pumzi tu.

10 Usitumainie vya udhalimu

wala usijivune kwa vitu vya wizi;

ingawa utajiri wako utaongezeka,

usiviwekee moyo wako.

11 Jambo moja Mungu amelisema,

mambo mawili nimeyasikia:

kwamba, Ee Mungu,

wewe una nguvu,

12 na kwamba, EeBwana,

wewe ni mwenye upendo.

Hakika utampa kila mtu thawabu

kwa kadiri ya alivyotenda.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/62-a950032ccaebbb5077ac681c630c0766.mp3?version_id=1627—

Categories
Zaburi

Zaburi 63

Shauku Kwa Ajili Ya Uwepo Wa Mungu

Zaburi ya Daudi. Wakati alipokuwa katika Jangwa la Yuda.

1 Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu,

nakutafuta kwa moyo wote;

nafsi yangu inakuonea kiu,

mwili wangu unakuonea wewe shauku,

katika nchi kame na iliyochoka

mahali ambapo hapana maji.

2 Nimekuona katika mahali patakatifu

na kuuona uwezo wako na utukufu wako.

3 Kwa sababu upendo wako ni bora kuliko uhai,

midomo yangu itakuadhimisha.

4 Nitakusifu siku zote za maisha yangu,

na kwa jina lako nitainua mikono yangu.

5 Nafsi yangu itatoshelezwa

kama kwa wingi wa vyakula;

kwa midomo iimbayo

kinywa changu kitakusifu wewe.

6 Kitandani mwangu ninakukumbuka wewe,

ninawaza juu yako makesha yote ya usiku.

7 Kwa sababu wewe ndiwe msaada wangu,

chini ya uvuli wa mbawa zako naimba.

8 Nafsi yangu inaambatana nawe,

mkono wako wa kuume hunishika.

9 Wale wanaotafuta uhai wangu wataharibiwa,

watakwenda chini kwenye vilindi vya dunia.

10 Watatolewa wafe kwa upanga,

nao watakuwa chakula cha mbweha.

11 Bali mfalme atafurahi katika Mungu,

wale wote waapao kwa jina la Mungu watamsifu,

bali vinywa vya waongo vitanyamazishwa.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/63-bb48ec067525b38ebabf85dc1e30c3ea.mp3?version_id=1627—