Categories
Zaburi

Zaburi 44

Kuomba Ulinzi Wa Mungu

Kwa mwimbishaji. Utenzi wa wana wa Kora.

1 Ee Mungu, tumesikia kwa masikio yetu,

baba zetu wametueleza

yale uliyotenda katika siku zao,

siku za kale.

2 Kwa mkono wako uliwafukuza mataifa

na ukawapanda baba zetu,

uliangamiza mataifa

na kuwastawisha baba zetu.

3 Sio kwa upanga wao waliipata nchi,

wala si mkono wao uliwapatia ushindi;

ilikuwa ni kitanga cha mkono wako wa kuume,

na nuru ya uso wako,

kwa kuwa uliwapenda.

4 Wewe ni mfalme wangu na Mungu wangu,

unayeamuru ushindi kwa Yakobo.

5 Kwa uwezo wako tunawasukuma nyuma watesi wetu;

kwa jina lako tunawakanyaga adui zetu.

6 Siutumaini upinde wangu,

upanga wangu hauniletei ushindi;

7 bali wewe unatupa ushindi juu ya adui zetu,

unawaaibisha watesi wetu.

8 Katika Mungu wetu tunajivuna mchana kutwa,

nasi tutalisifu jina lako milele.

9 Lakini sasa umetukataa na kutudhili,

wala huendi tena na jeshi letu.

10 Umetufanya turudi nyuma mbele ya adui,

nao watesi wetu wametuteka nyara.

11 Umetuacha tutafunwe kama kondoo

na umetutawanya katika mataifa.

12 Umewauza watu wako kwa fedha kidogo,

wala hukupata faida yoyote kwa mauzo yao.

13 Umetufanya lawama kwa jirani zetu,

dharau na dhihaka kwa wale wanaotuzunguka.

14 Umetufanya kuwa mithali miongoni mwa mataifa,

mataifa hutikisa vichwa vyao.

15 Fedheha yangu iko mbele yangu mchana kutwa,

na uso wangu umejaa aibu tele,

16 kwa ajili ya dhihaka ya wale wanaonilaumu na kunitukana,

kwa sababu ya adui, ambaye anatamani kulipiza kisasi.

17 Hayo yote yametutokea,

ingawa tulikuwa hatujakusahau

wala hatujaenda kinyume na agano lako.

18 Mioyo yetu ilikuwa haijarudi nyuma;

nyayo zetu zilikuwa hazijaiacha njia yako.

19 Lakini ulituponda na kutufanya makao ya mbweha,

na ukatufunika kwa giza nene.

20 Kama tungalikuwa tumelisahau jina la Mungu wetu

au kunyooshea mikono yetu kwa mungu mgeni,

21 je, Mungu hangaligundua hili,

kwa kuwa anazijua siri za moyo?

22 Hata hivyo kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa;

tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.

23 Amka, EeBwana! Kwa nini unalala?

Zinduka! Usitukatae milele.

24 Kwa nini unauficha uso wako

na kusahau taabu na mateso yetu?

25 Tumeshushwa hadi mavumbini,

miili yetu imegandamana na ardhi.

26 Inuka na utusaidie,

utukomboe kwa sababu ya upendo wako usio na mwisho.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/44-54b75441df84580e0380dbf22b6a37c2.mp3?version_id=1627—

Categories
Zaburi

Zaburi 45

Wimbo Wa Arusi Ya Kifalme

Kwa mwimbishaji. Mtindo wa utenzi wa “Yungiyungi.” Utenzi wa wana wa Kora. Wimbo wa arusi.

1 Moyo wangu umesisimuliwa na jambo jema

ninapomsimulia mfalme mabeti yangu;

ulimi wangu ni kalamu ya mwandishi stadi.

2 Wewe ni bora kuliko watu wengine wote

na midomo yako imepakwa neema,

kwa kuwa Mungu amekubariki milele.

3 Jifunge upanga wako pajani mwako, ee mwenye nguvu,

jivike fahari na utukufu.

4 Katika fahari yako, songa mbele kwa ushindi,

kwa ajili ya kweli, unyenyekevu na haki,

mkono wako wa kuume na uonyeshe matendo ya kutisha.

5 Mishale yako mikali na ichome mioyo ya adui za mfalme,

mataifa na yaanguke chini ya nyayo zako.

6 Ee Mungu, kiti chako cha enzi

kitadumu milele na milele,

fimbo ya utawala wa haki

itakuwa fimbo ya utawala wa ufalme wako.

7 Unaipenda haki na kuchukia uovu;

kwa hiyo Mungu, Mungu wako,

amekuweka juu ya wenzako,

kwa kukupaka mafuta ya furaha.

8 Mavazi yako yote yana harufu nzuri

ya manemane, udi na mdalasini;

kutoka kwenye majumba ya kifalme

yaliyopambwa kwa pembe za ndovu,

sauti za vinanda vya nyuzi

zinakufanya ufurahi.

9 Binti za wafalme ni miongoni mwa wanawake wako waheshimiwa;

kuume kwako yupo bibi arusi malkia aliyevaa dhahabu ya Ofiri.

10 Sikiliza, ewe binti, fikiri na utege sikio:

Sahau watu wako na nyumba ya baba yako.

11 Mfalme ameshangazwa na uzuri wako;

mheshimu, kwa kuwa yeye ni bwana wako.

12 Binti wa Tiro atakuletea zawadi,

watu wenye utajiri watatafuta upendeleo wako.

13 Utukufu wote una binti mfalme katika chumba chake;

vazi lake limefumwa kwa nyuzi za dhahabu.

14 Anaongozwa kwa mfalme, akiwa amevalia mavazi yaliyotariziwa,

mabikira wenzake wanamfuata

na wanaletwa kwako.

15 Wanaingizwa ndani kwa shangwe na furaha,

na kuingia katika jumba la mfalme.

16 Wana wenu watachukua nafasi za baba zenu,

mtawafanya wakuu katika nchi yote.

17 Nitadumisha kumbukumbu lako katika vizazi vyote,

kwa hiyo mataifa watakusifu milele na milele.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/45-1dff6e6f94c36fcf53e0a799560014ec.mp3?version_id=1627—

Categories
Zaburi

Zaburi 46

Mungu Yuko Pamoja Nasi

Kwa mwimbishaji. Zaburi ya wana wa Kora. Mtindo wa alamothi.

1 Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu,

msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.

2 Kwa hiyo hatutaogopa, hata kama dunia ikiondolewa

nayo milima ikiangukia moyoni mwa bahari.

3 Hata kama maji yake yatanguruma na kuumuka,

milima nayo ikitetemeka kwa mawimbi yake.

4 Kuna mto ambao vijito vyake vinaufurahisha mji wa Mungu,

mahali patakatifu ambako Aliye Juu Sana anaishi.

5 Mungu yuko katikati yake, hautaanguka,

Mungu atausaidia asubuhi na mapema.

6 Mataifa yanafanya ghasia, falme zinaanguka,

Yeye huinua sauti yake, dunia ikayeyuka.

7 BwanaMwenye Nguvu Zote yu pamoja nasi,

Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.

8 Njooni mkaone kazi zaBwana

jinsi alivyofanya ukiwa katika nchi.

9 Anakomesha vita hata miisho ya dunia,

anakata upinde na kuvunjavunja mkuki,

anateketeza ngao kwa moto.

10 “Tulieni, mjue ya kwamba mimi ndimi Mungu;

nitatukuzwa katikati ya mataifa,

nitatukuzwa katika dunia.”

11 BwanaMwenye Nguvu Zote yu pamoja nasi;

Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/46-2f02b0237beb5a914cb3b0cb7ee4c0f0.mp3?version_id=1627—

Categories
Zaburi

Zaburi 47

Mtawala Mwenye Enzi Yote

Kwa mwimbishaji. Zaburi ya wana wa Kora.

1 Pigeni makofi, enyi mataifa yote,

mpigieni Mungu kelele za shangwe!

2 Jinsi gani alivyo wa kutisha,BwanaAliye Juu Sana,

Mfalme mkuu juu ya dunia yote!

3 Ametiisha mataifa chini yetu

watu wengi chini ya miguu yetu.

4 Alituchagulia urithi wetu,

fahari ya Yakobo, aliyempenda.

5 Mungu amepaa kwa kelele za shangwe,

Bwanakwa sauti za tarumbeta.

6 Mwimbieni Mungu sifa, imbeni sifa,

mwimbieni sifa Mfalme wetu, imbeni sifa.

7 Kwa kuwa Mungu ni mfalme wa dunia yote,

mwimbieni zaburi za sifa.

8 Mungu anatawala juu ya mataifa,

Mungu ameketi juu ya kiti chake cha enzi kitakatifu.

9 Wakuu wa mataifa wanakusanyika

kama watu wa Mungu wa Abrahamu,

kwa kuwa wafalme wa dunia ni mali ya Mungu;

yeye ametukuka sana.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/47-e21b9683f9512765cfa2895d3ed9ceab.mp3?version_id=1627—

Categories
Zaburi

Zaburi 48

Sayuni, Mji Wa Mungu

Wimbo. Zaburi ya wana wa Kora.

1 Bwanani mkuu, anayestahili kusifiwa sana,

katika mji wa Mungu wetu,

mlima wake mtakatifu.

2 Ni mzuri katika kuinuka kwake juu sana,

furaha ya dunia yote.

Kama vilele vya juu sana vya Safonini Mlima Sayuni,

mji wa Mfalme Mkuu.

3 Mungu yuko katika ngome zake;

amejionyesha mwenyewe kuwa ngome yake.

4 Wakati wafalme walipounganisha nguvu,

waliposonga mbele pamoja,

5 walimwona nao wakashangaa,

wakakimbia kwa hofu.

6 Kutetemeka kuliwashika huko,

maumivu kama ya mwanamke

mwenye utungu wa kuzaa.

7 Uliwaangamiza kama meli za Tarshishi

zilizovunjwa na upepo wa mashariki.

8 Kama tulivyokuwa tumesikia,

ndivyo tulivyoona

katika mji waBwanaMwenye Nguvu Zote,

katika mji wa Mungu wetu:

Mungu ataufanya uwe salama milele.

9 Ee Mungu, hekaluni mwako

tunatafakari upendo wako usiokoma.

10 Ee Mungu, kama jina lako lilivyo,

sifa zako zinafika hadi miisho ya dunia,

mkono wako wa kuume umejazwa na haki.

11 Mlima Sayuni unashangilia,

vijiji vya Yuda vinafurahi

kwa sababu ya hukumu zako.

12 Tembeeni katika Sayuni,

uzungukeni mji,

hesabuni minara yake;

13 yatafakarini vyema maboma yake,

angalieni ngome zake,

ili mpate kusimulia habari zake

kwa kizazi kijacho.

14 Kwa kuwa huyu Mungu ni Mungu wetu milele na milele;

atakuwa kiongozi wetu hata mwisho.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/48-e221b6e7706605fa6c85745014786c40.mp3?version_id=1627—

Categories
Zaburi

Zaburi 49

Upumbavu Wa Kutegemea Mali

Kwa mwimbishaji. Zaburi ya wana wa Kora.

1 Sikieni haya, enyi mataifa yote,

sikilizeni, ninyi wote mkaao dunia hii.

2 Wakubwa kwa wadogo,

matajiri na maskini pamoja:

3 Kinywa changu kitasema maneno ya hekima,

usemi wa moyo wangu utatoa ufahamu.

4 Nitatega sikio langu nisikilize mithali,

nitafafanua kitendawili kwa zeze:

5 Kwa nini niogope siku mbaya zinapokuja,

wakati wadanganyifu waovu wanaponizunguka,

6 wale wanaotegemea mali zao

na kujivunia utajiri wao mwingi?

7 Hakuna mwanadamu awaye yote

awezaye kuukomboa uhai wa mwingine,

au kumpa Mungu fidia kwa ajili yake.

8 Fidia ya uhai ni gharama kubwa,

hakuna malipo yoyote yanayotosha,

9 ili kwamba aishi milele

na asione uharibifu.

10 Wote wanaona kwamba watu wenye hekima hufa;

wajinga na wapumbavu vivyo hivyo huangamia

na kuwaachia wengine mali zao.

11 Makaburi yao yatabaki kuwa nyumba zao za milele,

makao yao vizazi vyote;

ingawa walikuwa na mashamba

na kuyaita kwa majina yao.

12 Lakini mwanadamu, licha ya utajiri wake, hadumu;

anafanana na mnyama aangamiaye.

13 Hii ndiyo hatima ya wale wanaojitumainia wenyewe,

pia ya wafuasi wao, waliothibitisha misemo yao.

14 Kama kondoo, wamewekewa kwenda kaburini,

nacho kifo kitawala.

Wanyofu watawatawala asubuhi,

maumbile yao yataozea kaburini,

mbali na majumba yao makubwa ya fahari.

15 Lakini Mungu atakomboa uhaiwangu na kaburi,

hakika atanichukua kwake.

16 Usitishwe mtu anapotajirika,

fahari ya nyumba yake inapoongezeka,

17 kwa maana hatachukua chochote atakapokufa,

fahari yake haitashuka pamoja naye.

18 Ingawa alipokuwa akiishi alijihesabu kuwa heri,

na wanadamu wanakusifu unapofanikiwa,

19 atajiunga na kizazi cha baba zake,

ambao hawataona kamwe nuru ya uzima.

20 Mwanadamu mwenye utajiri bila ufahamu

ni kama wanyama waangamiao.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/49-4c002caae8dd81754a149ad4bb43413d.mp3?version_id=1627—

Categories
Zaburi

Zaburi 50

Ibada Ya Kweli

Zaburi ya Asafu.

1 Mwenye Nguvu, Mungu,Bwana,

asema na kuiita dunia,

tangu mawio ya jua

hadi mahali pake liendapo kutua.

2 Kutoka Sayuni, penye uzuri mkamilifu,

Mungu anaangaza.

3 Mungu wetu anakuja na hatakaa kimya,

moto uteketezao unamtangulia,

akiwa amezungukwa na tufani kali.

4 Anaziita mbingu zilizo juu,

na nchi, ili aweze kuwahukumu watu wake:

5 “Nikusanyieni watu wangu waliowekwa wakfu,

waliofanya agano nami kwa dhabihu.”

6 Nazo mbingu zinatangaza haki yake,

kwa maana Mungu mwenyewe ni hakimu.

7 “Sikieni, enyi watu wangu, nami nitasema,

ee Israeli, nami nitashuhudia dhidi yenu:

Mimi ndimi Mungu, Mungu wenu.

8 Sikukemei kwa sababu ya dhabihu zako,

au sadaka zako za kuteketezwa,

ambazo daima ziko mbele zangu.

9 Sina haja ya fahali wa banda lako,

au mbuzi wa zizi lako.

10 Kwa maana kila mnyama wa msituni ni wangu,

na pia makundi ya mifugo juu ya vilima elfu.

11 Ninamjua kila ndege mlimani,

nao viumbe wa kondeni ni wangu.

12 Kama ningekuwa na njaa, nisingewaambia ninyi,

kwa maana ulimwengu ni wangu,

pamoja na vyote vilivyomo ndani yake.

13 Je, mimi hula nyama ya mafahali

au kunywa damu ya mbuzi?

14 Toa sadaka za shukrani kwa Mungu,

timiza nadhiri zako kwake Yeye Aliye Juu Sana,

15 na uniite siku ya taabu;

nami nitakuokoa, nawe utanitukuza.”

16 Lakini kwake mtu mwovu, Mungu asema:

“Una haki gani kunena sheria zangu

au kuchukua agano langu midomoni mwako?

17 Unachukia mafundisho yangu

na kuyatupa maneno yangu nyuma yako.

18 Unapomwona mwizi, unaungana naye,

unapiga kura yako pamoja na wazinzi.

19 Unakitumia kinywa chako kwa mabaya

na kuuongoza ulimi wako kwa hila.

20 Wanena daima dhidi ya ndugu yako

na kumsingizia mwana wa mama yako.

21 Mambo haya unayafanya, nami nimekaa kimya,

ukafikiri Mimi nami ni kama wewe.

Lakini nitakukemea

na kuweka mashtaka mbele yako.

22 “Yatafakarini haya, ninyi mnaomsahau Mungu,

ama sivyo nitawararua vipande vipande,

wala hapatakuwepo na yeyote wa kuwaokoa:

23 Atoaye dhabihu za shukrani ananiheshimu mimi,

naye aiandaa njia yake

ili nimwonyeshe wokovu wa Mungu.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/50-ce8e48aa383d466ec190c7d8544492a7.mp3?version_id=1627—

Categories
Zaburi

Zaburi 51

Kuomba Msamaha

Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Baada ya kukemewa na nabii Nathani kwa kuzini na Bathsheba.

1 Ee Mungu, unihurumie,

kwa kadiri ya upendo wako usiokoma,

kwa kadiri ya huruma yako kuu,

uyafute makosa yangu.

2 Unioshe na uovu wangu wote

na unitakase dhambi yangu.

3 Kwa maana ninajua makosa yangu,

na dhambi yangu iko mbele yangu daima.

4 Dhidi yako, wewe peke yako, nimetenda dhambi

na kufanya yaliyo mabaya machoni pako,

ili uthibitike kuwa wa kweli unenapo,

na kuwa na haki utoapo hukumu.

5 Hakika mimi nilizaliwa mwenye dhambi,

mwenye dhambi tangu nilipotungwa mimba kwa mama yangu.

6 Hakika wewe wapendezwa na kweli itokayo moyoni,

ndani sana ya moyo wangu wanifundisha hekima.

7 Nioshe kwa hisopo, nami nitakuwa safi,

unisafishe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji.

8 Unipe kusikia furaha na shangwe,

mifupa uliyoiponda na ifurahi.

9 Ufiche uso wako usizitazame dhambi zangu,

na uufute uovu wangu wote.

10 Ee Mungu, uniumbie moyo safi,

uifanye upya roho ya uthabiti ndani yangu.

11 Usinitupe kutoka mbele zako

wala kuniondolea Roho wako Mtakatifu.

12 Unirudishie tena furaha ya wokovu wako,

unipe roho ya utii, ili initegemeze.

13 Ndipo nitakapowafundisha wakosaji njia zako,

na wenye dhambi watakugeukia wewe.

14 Ee Mungu, Mungu uniokoaye,

niokoe na hatia ya kumwaga damu,

nao ulimi wangu utaimba juu ya haki yako.

15 EeBwana, fungua midomo yangu,

na kinywa changu kitatangaza sifa zako.

16 Wewe hupendezwi na dhabihu, au ningaliileta,

hufurahii sadaka za kuteketezwa.

17 Bali dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika,

moyo uliovunjika wenye toba,

Ee Mungu, hutaudharau.

18 Kwa wema wa radhi yako uifanye Sayuni istawi,

ukazijenge upya kuta za Yerusalemu.

19 Hapo ndipo kutakapokuwa na dhabihu za haki,

sadaka nzima za kuteketezwa za kukupendeza sana,

pia mafahali watatolewa

madhabahuni mwako.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/51-d7e86911e361376b39ce500423ad55e4.mp3?version_id=1627—

Categories
Zaburi

Zaburi 52

Hukumu Ya Mungu

Kwa mwimbishaji. Utenzi wa Daudi. Baada ya Doegi, Mwedomu kumwendea Sauli na kumjulisha kuwa: “Daudi amekwenda nyumbani kwa Ahimeleki.”

1 Ewe jitu, mbona unajivunia ubaya?

Kwa nini unajivuna mchana kutwa,

wewe ambaye ni fedheha mbele za Mungu?

2 Ulimi wako hupanga mashauri mabaya ya maangamizi.

Ni kama wembe mkali, ninyi mfanyao hila.

3 Unapenda mabaya kuliko mema,

uongo kuliko kusema kweli.

4 Unapenda kila neno lenye kudhuru,

ewe ulimi wenye hila!

5 Hakika Mungu atakushusha chini

kwa maangamizi ya milele:

atakunyakua na kukuondoa kwa nguvu

kutoka hema yako,

atakungʼoa kutoka nchi ya walio hai.

6 Wenye haki wataona na kuogopa,

watamcheka, wakisema,

7 “Huyu ni yule mtu ambaye

hakumfanya Mungu kuwa ngome yake,

bali alitumainia wingi wa utajiri wake,

na akawa hodari kwa kuwaangamiza wengine!”

Neema Ya Mungu

8 Lakini mimi ni kama mti wa mzeituni

unaostawi katika nyumba ya Mungu,

nautegemea upendo wa Mungu usiokoma

milele na milele.

9 Nitakusifu milele kwa yale uliyoyatenda,

nitatumaini jina lako, kwa kuwa jina lako ni jema.

Nitakusifu mbele ya watakatifu wako.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/52-866b48522de5e9ba80791781fd94b645.mp3?version_id=1627—

Categories
Zaburi

Zaburi 53

Uovu Wa Wanadamu

Kwa mwimbishaji. Mtindo wa mahalathi. Utenzi wa Daudi.

1 Mpumbavu anasema moyoni mwake,

“Hakuna Mungu.”

Wameharibika, na njia zao ni za uovu kabisa,

hakuna hata mmoja atendaye mema.

2 Mungu anawachungulia wanadamu chini

kutoka mbinguni

aone kama wako wenye akili,

wowote wanaomtafuta Mungu.

3 Kila mmoja amegeukia mbali,

wameharibika wote pamoja,

hakuna atendaye mema.

Naam, hakuna hata mmoja!

4 Je, watendao mabaya kamwe hawatajifunza:

wale ambao huwala watu wangu

kama watu walavyo mkate,

hao ambao hawamwiti Mungu?

5 Hapo waliingiwa na hofu kuu,

ambapo hapakuwa cha kutetemesha.

Mungu alitawanya mifupa ya wale waliokushambulia;

uliwaaibisha, kwa sababu Mungu aliwadharau.

6 Laiti wokovu wa Israeli ungalikuja kutoka Sayuni!

Wakati Mungu arejeshapo wafungwa wa watu wake,

Yakobo na ashangilie, Israeli na afurahi!

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/53-b53885ea57ed4462561650e8e252af99.mp3?version_id=1627—