Categories
Zaburi

Zaburi 4

Sala Ya Jioni Ya Kuomba Msaada

Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za muziki. Zaburi ya Daudi.

1 Nijibu nikuitapo,

Ee Mungu wangu mwenye haki!

Nipumzishe katika shida zangu;

nirehemu, usikie ombi langu.

2 Enyi watu, mtabadilisha utukufu wangu

kuwa aibu mpaka lini?

Mtapenda udanganyifu

na kufuata miungu ya uongo mpaka lini?

3 Fahamuni hakika kwambaBwanaamewatenga

wale wamchao kwa ajili yake;

Bwanaatanisikia nimwitapo.

4 Katika hasira yako, usitende dhambi.

Mkiwa vitandani mwenu, mtulie kimya

mkiichunguza mioyo yenu.

5 Toeni dhabihu zilizo haki;

mtegemeeniBwana.

6 Wengi wanauliza, “Ni nani awezaye

kutuonyesha jema lolote?”

EeBwana, tuangazie nuru ya uso wako.

7 Wewe umejaza moyo wangu kwa furaha kubwa

kuliko watu waliopata nafaka na divai kwa wingi.

8 Nitajilaza chini na kulala kwa amani,

kwa kuwa wewe peke yako, EeBwana,

waniwezesha kukaa kwa salama.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/4-d29771b2637e4953932c84584e8c7c0e.mp3?version_id=1627—

Categories
Zaburi

Zaburi 5

Sala Kwa Ajili Ya Ulinzi Wakati Wa Hatari

Kwa mwimbishaji. Kwa filimbi. Zaburi ya Daudi.

1 EeBwana, tegea sikio maneno yangu,

uangalie kupiga kite kwangu.

2 Sikiliza kilio changu ili unisaidie,

Mfalme wangu na Mungu wangu,

kwa maana kwako ninaomba.

3 Asubuhi, unasikia sauti yangu, EeBwana;

asubuhi naleta haja zangu mbele zako,

na kusubiri kwa matumaini.

4 Wewe si Mungu unayefurahia uovu,

kwako mtu mwovu hataishi.

5 Wenye kiburi hawawezi kusimama mbele yako,

unawachukia wote watendao mabaya.

6 Unawaangamiza wasemao uongo.

Bwanahuwachukia

wamwagao damu na wadanganyifu.

7 Lakini mimi, kwa rehema zako kuu,

nitakuja katika nyumba yako,

kwa unyenyekevu, nitasujudu

kuelekea Hekalu lako takatifu.

8 Niongoze katika haki yako, EeBwana,

kwa sababu ya adui zangu,

nyoosha njia yako mbele yangu.

9 Hakuna neno kinywani mwao linaloweza kuaminika,

mioyo yao imejaa maangamizi.

Koo lao ni kaburi lililo wazi,

kwa ndimi zao, wao hunena udanganyifu.

10 Uwatangaze kuwa wenye hatia, Ee Mungu!

Hila zao ziwe anguko lao wenyewe.

Wafukuzie mbali kwa sababu ya dhambi zao nyingi,

kwa kuwa wamekuasi wewe.

11 Lakini wote wakimbiliao kwako na wafurahi,

waimbe kwa shangwe daima.

Ueneze ulinzi wako juu yao,

ili wale wapendao jina lako

wapate kukushangilia.

12 Kwa hakika, EeBwana, unawabariki wenye haki,

unawazunguka kwa wema wako kama ngao.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/5-2a517cdb34986fc621a99e3f7cba50d4.mp3?version_id=1627—

Categories
Zaburi

Zaburi 6

Sala Kwa Ajili Ya Msaada Wakati Wa Taabu

Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za muziki. Mtindo wa sheminithi.

Zaburi ya Daudi.

1 EeBwana, usinikemee katika hasira yako,

wala usiniadhibu katika ghadhabu yako.

2 UnirehemuBwana,

kwa maana nimedhoofika;

EeBwana, uniponye,

kwa maana mifupa yangu

ina maumivu makali.

3 Nafsi yangu ina uchungu mwingi.

Mpaka lini, EeBwana, mpaka lini?

4 Geuka EeBwana, unikomboe,

uniokoe kwa sababu ya fadhili zako.

5 Hakuna mtu anayekukumbuka

akiwa amekufa.

Ni nani awezaye kukusifu

akiwa kuzimu?

6 Nimechakaa kwa kulia kwa huzuni;

usiku kucha nafurikisha

kitanda changu kwa machozi;

nimelowesha viti vyangu vya fahari

kwa machozi.

7 Macho yangu yamedhoofika kwa kuhuzunika,

yamedhoofika kwa sababu ya adui zangu wote.

8 Kaeni mbali nami, ninyi nyote mtendao mabaya,

kwa maanaBwanaamesikia kulia kwangu.

9 Bwanaamesikia kilio changu kwa huruma,

Bwanaamekubali sala yangu.

10 Adui zangu wote wataaibika na kufadhaika,

watarudi nyuma kwa aibu ya ghafula.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/6-a9a79421fa300ef0aa37e5024d36f37d.mp3?version_id=1627—

Categories
Zaburi

Zaburi 7

Sala Ya Mtu Anayedhulumiwa

Ombolezo la Daudi kwa

Bwana

kwa sababu ya Kushi, Mbenyamini.

1 EeBwana, Mungu wangu, ninakukimbilia wewe,

uniokoe na kunikomboa na wote wanaonifuatia,

2 la sivyo watanirarua kama simba

na kunichana vipande vipande, asiwepo wa kuniokoa.

3 EeBwana, Mungu wangu, kama nimetenda haya

na kuna hatia mikononi mwangu,

4 au ikiwa nimemtenda uovu aliye na amani nami,

au nimemnyangʼanya adui yangu pasipo sababu,

5 basi adui anifuatie na kunipata,

auponde uhai wangu ardhini

na kunilaza mavumbini.

6 Amka kwa hasira yako, EeBwana,

inuka dhidi ya ghadhabu ya adui zangu.

Amka, Mungu wangu, uamue haki.

7 Kusanyiko la watu na likuzunguke.

Watawale kutoka juu.

8 Bwanana awahukumu kabila za watu.

Nihukumu EeBwana,

kwa kadiri ya haki yangu,

kwa kadiri ya uadilifu wangu,

Ewe Uliye Juu Sana.

9 Ee Mungu mwenye haki,

uchunguzaye mawazo na mioyo,

komesha ghasia za waovu

na ufanye wenye haki waishi kwa amani.

10 Ngao langu ni Mungu Aliye Juu Sana,

awaokoaye wanyofu wa moyo.

11 Mungu ni mwamuzi mwenye haki,

Mungu aghadhibikaye kila siku.

12 Kama hakutuhurumia,

atanoa upanga wake,

ataupinda na kuufunga uzi upinde wake.

13 Ameandaa silaha zake kali,

ameweka tayari mishale yake ya moto.

14 Yeye aliye na mimba ya uovu

na achukuaye mimba ya ghasia huzaa uongo.

15 Yeye achimbaye shimo na kulifukua

hutumbukia katika shimo alilochimba mwenyewe.

16 Ghasia azianzishazo humrudia mwenyewe,

ukatili wake humrudia kichwani.

17 NitamshukuruBwanakwa ajili ya haki yake,

na nitaliimbia sifa jina laBwanaAliye Juu Sana.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/7-9e53f9c428c3200c087bbe4527cde841.mp3?version_id=1627—

Categories
Zaburi

Zaburi 8

Utukufu Wa Mungu Na Heshima Ya Mwanadamu

Kwa mwimbishaji. Mtindo wa gitithi. Zaburi ya Daudi.

1 EeBwana, Bwana wetu,

tazama jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!

Umeuweka utukufu wako

juu ya mbingu.

2 Midomoni mwa watoto wachanga na wanyonyao

umeamuru sifa,

kwa sababu ya watesi wako,

kumnyamazisha adui na mlipiza kisasi.

3 Nikiziangalia mbingu zako,

kazi ya vidole vyako,

mwezi na nyota,

ulizoziratibisha,

4 mwanadamu ni kitu gani hata unamfikiria,

binadamu ni nani hata unamjali?

5 Umemfanya chini kidogo kuliko viumbe wa mbinguni,

ukamvika taji ya utukufu na heshima.

6 Umemfanya mtawala juu ya kazi za mikono yako;

umeweka vitu vyote chini ya miguu yake.

7 Mifugo na makundi yote pia,

naam, na wanyama wa kondeni,

8 ndege wa angani na samaki wa baharini,

naam, kila kiogeleacho katika njia za bahari.

9 EeBwana, Bwana wetu,

tazama jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/8-9b9688e20a06c6dd7f5a4839406532c4.mp3?version_id=1627—

Categories
Zaburi

Zaburi 9

Shukrani Kwa Mungu Kwa Ajili Ya Haki Yake

Kwa mwimbishaji. Mtindo wa muth-labeni.

Zaburi ya Daudi.

1 EeBwana, nitakutukuza kwa moyo wangu wote,

nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu.

2 Nitafurahi na kushangilia ndani yako.

Nitaliimbia sifa jina lako, Ewe Uliye Juu Sana.

3 Adui zangu wamerudi nyuma,

wamejikwaa na kuangamia mbele zako.

4 Kwa maana umetetea haki yangu na msimamo wangu;

umeketi kwenye kiti chako cha enzi,

ukihukumu kwa haki.

5 Umekemea mataifa na kuwaangamiza waovu;

umeyafuta majina yao milele na milele.

6 Uharibifu usiokoma umempata adui,

umeingʼoa miji yao;

hata kumbukumbu lao limetoweka.

7 Bwanaanatawala milele,

ameweka kiti chake cha enzi apate kuhukumu.

8 Mungu atahukumu ulimwengu kwa haki,

atatawala mataifa kwa haki.

9 Bwanani kimbilio la watu wanaoonewa,

ni ngome imara wakati wa shida.

10 Wote wanaolijua jina lako watakutumaini wewe,

kwa maana weweBwana,

hujawaacha kamwe wakutafutao.

11 MwimbieniBwanasifa, amefanywa mtawala Sayuni,

tangazeni miongoni mwa mataifa, yale aliyoyatenda.

12 Kwa maana yeye alipizaye kisasi cha damu hukumbuka,

hapuuzi kilio cha wanaoonewa.

13 EeBwana, tazama jinsi walivyo wengi adui zangu wanaonitesa!

Nihurumie, uniinue kutoka malango ya mauti,

14 ili niweze kutangaza sifa zako

katika malango ya Binti Sayuni

na huko niushangilie wokovu wako.

15 Mataifa wameanguka kwenye shimo walilolichimba,

miguu yao imenaswa kwenye wavu waliouficha.

16 Bwanaanajulikana kwa haki yake,

waovu wamenaswa katika kazi za mikono yao.

17 Waovu wataishia kuzimu,

naam, mataifa yote wanaomsahau Mungu.

18 Lakini mhitaji hatasahaulika siku zote,

wala matumaini ya walioonewa hayatapotea.

19 EeBwana, inuka, usimwache binadamu ashinde.

Mataifa na yahukumiwe mbele zako.

20 EeBwana, wapige kwa hofu,

mataifa na yajue kuwa wao ni watu tu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/9-0f5efef9c3685c2abd60fe6eb0bef333.mp3?version_id=1627—

Categories
Zaburi

Zaburi 10

Sala Kwa Ajili Ya Haki

1 Kwa nini, EeBwana, unasimama mbali?

Kwa nini unajificha wakati wa shida?

2 Katika kiburi chake, mwovu humtesa maskini,

waovu na wanaswe katika hila wanazozitunga.

3 Hujivunia tamaa za moyo wake;

humbariki mlafi na kumtukanaBwana.

4 Katika kiburi chake, mwovu hamtafuti Mungu,

katika mawazo yake yote

hakuna nafasi ya Mungu.

5 Njia zake daima hufanikiwa;

hujivuna na amri zako ziko mbali naye,

huwacheka kwa dharau adui zake wote.

6 Anajisemea mwenyewe, “Hakuna kitakachonitikisa,

daima nitakuwa na furaha,

kamwe sitakuwa na shida.”

7 Kinywa chake kimejaa laana, uongo na vitisho;

shida na ubaya viko chini ya ulimi wake.

8 Huvizia karibu na vijiji;

kutoka mafichoni huwanasa wasio na hatia,

akivizia wapitaji.

9 Huvizia kama simba aliye mawindoni;

huvizia kumkamata mnyonge,

huwakamata wanyonge na kuwaburuza

katika wavu wake.

10 Mateka wake hupondwa, huzimia;

wanaanguka katika nguvu zake.

11 Anajisemea mwenyewe, “Mungu amesahau,

huficha uso wake na haoni kabisa.”

12 InukaBwana! Inua mkono wako, Ee Mungu.

Usiwasahau wanyonge.

13 Kwa nini mtu mwovu anamtukana Mungu?

Kwa nini anajiambia mwenyewe,

“Hataniita nitoe hesabu?”

14 Lakini wewe, Ee Mungu, unaona shida na huzuni,

umekubali kuyapokea mkononi mwako.

Mhanga anajisalimisha kwako,

wewe ni msaada wa yatima.

15 Vunja mkono wa mtu mwovu na mbaya,

mwite atoe hesabu ya maovu yake

ambayo yasingejulikana.

16 Bwanani Mfalme milele na milele,

mataifa wataangamia watoke nchini mwake.

17 Unasikia, EeBwana, shauku ya wanaoonewa,

wewe huwatia moyo, na kusikiliza kilio chao,

18 ukiwatetea yatima na walioonewa,

ili mwanadamu, ambaye ni udongo, asiogopeshe tena.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/10-754824ce0d2c446f4f9a8c6e83c222fa.mp3?version_id=1627—

Categories
Zaburi

Zaburi 11

Kumtumaini Bwana

Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.

1 KwaBwananinakimbilia,

unawezaje basi kuniambia:

“Ruka kama ndege kwenye mlima wako.

2 Hebu tazama, waovu wanapinda pinde zao,

huweka mishale kwenye uzi wake,

wakiwa gizani ili kuwapiga

wale wanyofu wa moyo.

3 Wakati misingi imeharibiwa,

mwenye haki anaweza kufanya nini?”

4 Bwanayuko ndani ya Hekalu lake takatifu;

Bwanayuko kwenye kiti chake cha enzi mbinguni.

Huwaangalia wana wa watu,

macho yake yanawajaribu.

5 Bwanahuwajaribu wenye haki,

lakini waovu na wanaopenda jeuri,

nafsi yake huwachukia.

6 Atawanyeshea waovu makaa ya moto mkali

na kiberiti kinachowaka,

upepo wenye joto kali ndio fungu lao.

7 Kwa kuwaBwanani mwenye haki,

yeye hupenda haki.

Wanyofu watauona uso wake.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/11-5c07d8f7f91202ea2f0e5f2cfada8510.mp3?version_id=1627—

Categories
Zaburi

Zaburi 12

Kuomba Msaada

Kwa mwimbishaji. Mtindo wa sheminithi. Zaburi ya Daudi.

1 Bwanatusaidie, kwa kuwa wacha Mungu wametoweka;

waaminifu wametoweka miongoni mwa wanadamu.

2 Kila mmoja humwambia jirani yake uongo;

midomo yao ya hila huzungumza kwa udanganyifu.

3 Bwanana akatilie mbali midomo yote ya hila

na kila ulimi uliojaa majivuno,

4 ule unaosema, “Kwa ndimi zetu tutashinda;

midomo ni mali yetu, bwana wetu ni nani?”

5 “Kwa sababu ya uonevu wa wanyonge

na kulia kwa uchungu kwa wahitaji,

nitainuka sasa,” asemaBwana.

“Nitawalinda kutokana na wale

wenye nia mbaya juu yao.”

6 Maneno yaBwanani safi,

kama fedha iliyosafishwa katika tanuru,

iliyosafishwa mara saba.

7 EeBwana, utatuweka salama

na kutulinda na kizazi hiki milele.

8 Watu waovu huenda wakiringa kila mahali

wakati ambapo yule aliye mbaya sana

ndiye anayeheshimiwa miongoni mwa watu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/12-78f49a641ddd6c81699450d676c86446.mp3?version_id=1627—

Categories
Zaburi

Zaburi 13

Sala Ya Kuomba Msaada

Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.

1 Mpaka lini, EeBwana? Je, utanisahau milele?

Utanificha uso wako mpaka lini?

2 Nitapambana na mawazo yangu mpaka lini,

na kila siku kuwa na majonzi moyoni mwangu?

Adui zangu watanishinda mpaka lini?

3 Nitazame, unijibu, EeBwanaMungu wangu.

Yatie nuru macho yangu,

ama sivyo nitalala usingizi wa mauti.

4 Adui yangu atasema, “Nimemshinda,”

nao adui zangu watashangilia nitakapoanguka.

5 Lakini ninategemea upendo wako usiokoma;

moyo wangu unashangilia katika wokovu wako.

6 NitamwimbiaBwana,

kwa kuwa amekuwa mwema kwangu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/PSA/13-e4324ab50d31ef0ba6d185a93f9159ae.mp3?version_id=1627—