Categories
Ayubu

Ayubu 27

Ayubu Anadumisha Uadilifu Wake

1 Ndipo Ayubu akaendelea na hoja yake, akasema:

2 “Hakika kama Mungu aishivyo, aliyeninyima haki yangu,

Mwenyezi ambaye amenifanya

nionje uchungu wa nafsi,

3 kwa muda wote nitakaokuwa na uhai ndani yangu,

nayo pumzi ya Mungu ikiwa puani mwangu,

4 midomo yangu haitanena uovu,

wala ulimi wangu hautatamka udanganyifu.

5 Sitakubaliana nanyi kabisa kuwa mko sahihi;

hadi nife, sitakana uadilifu wangu.

6 Nitadumisha haki yangu wala sitaiacha;

dhamiri yangu haitanisuta muda wote ninaoishi.

7 “Watesi wangu wawe kama waovu,

nao adui zangu wawe kama wasio haki!

8 Kwa maana mtu asiyemcha Mungu

analo tegemeo gani anapokatiliwa mbali,

Mungu anapouondoa uhai wake?

9 Je, Mungu husikiliza kilio chake,

shida zimjiapo?

10 Je, anaweza kumfurahia Mwenyezi?

Je, atamwita Mungu nyakati zote?

11 “Nitawafundisha juu ya uweza wa Mungu;

njia za Mwenyezi sitazificha.

12 Ninyi nyote mmeona hili wenyewe.

Ni ya nini basi mazungumzo haya yasiyo na maana?

13 “Hili ndilo fungu ambalo Mungu humpa mtu mwovu,

urithi ule mtu mdhalimu anapokea kutoka kwa Mwenyezi:

14 Hata kama watoto wake watakuwa wengi kiasi gani,

fungu lao ni kuuawa kwa upanga;

wazao wake hawatakuwa kamwe

na chakula cha kuwatosha.

15 Tauni itawazika wale watakaonusurika miongoni mwao,

nao wajane wao hawatawaombolezea.

16 Ajapokusanya fedha nyingi kama mavumbi,

na mavazi kama malundo ya udongo wa mfinyanzi,

17 yale yote mtu mwovu aliyojiwekea akiba, mwenye haki atayavaa,

naye asiye na hatia ataigawanya fedha yake.

18 Nyumba aijengayo ni kama utando wa buibui,

kama kibanda alichotengeneza mlinzi.

19 Yeye hulala akiwa tajiri, lakini ndiyo mara ya mwisho;

afunguapo macho yake, yote yametoweka.

20 Vitisho humjia kama mafuriko;

dhoruba humkumba ghafula usiku.

21 Upepo mkali wa mashariki humchukua, naye hutoweka;

humzoa kutoka mahali pake.

22 Humvurumisha bila huruma,

huku akikimbia kasi kukwepa nguvu zake.

23 Upepo humpigia makofi kwa dharau,

na kumfukuza atoke mahali pake.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/27-985e4b5f356b0b720aef18ddf5c178fe.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 28

Mapumziko: Imani Inakopatikana

1 “Kuna machimbo ya fedha,

na mahali dhahabu isafishwapo.

2 Chuma hupatikana ardhini,

nayo shaba huyeyushwa kutoka mawe ya madini.

3 Mwanadamu hukomesha giza;

huyatafuta hadi sehemu iliyo mbali,

kwa ajili ya kuchimbua mawe yenye madini

katika giza jeusi sana.

4 Huchimba shimo jembamba mbali na makao ya watu,

mahali paliposahaulika na nyayo za wanadamu;

mbali na wanadamu huningʼinia na kupembea kwa kamba.

5 Ardhi, ambako chakula hutoka,

chini hugeuzwa kwa moto;

6 yakuti samawi hutoka katika miamba yake,

nalo vumbi lake lina vipande vya dhahabu.

7 Hakuna ndege awindaye aijuaye njia ile iliyofichika,

wala hakuna jicho la mwewe lililoiona.

8 Wanyama wa porini wanaotamba hawajawahi kupakanyaga,

wala simba azungukaye huko.

9 Mikono ya mwanadamu hushambulia miamba migumu sana,

na kuiacha wazi mizizi ya milima.

10 Hutoboa shimo refu la kupenya chini kwa chini kwenye miamba;

macho yake huona hazina zake zote.

11 Hutafuta vyanzo vya mito

na kuvileta vitu vilivyofichika katika nuru.

12 “Lakini hekima inaweza kupatikana wapi?

Ufahamu unakaa wapi?

13 Mwanadamu hatambui thamani yake;

haiwezi kupatikana katika nchi ya walio hai.

14 Kilindi husema, ‘Haiko ndani yangu’;

bahari nayo husema, ‘Haiko pamoja nami.’

15 Haiwezi kununuliwa kwa dhahabu safi kuliko zote,

wala thamani yake haiwezi kupimwa kwa fedha.

16 Haiwezi kununuliwa kwa dhahabu ya Ofiri,

kwa shohamu ya thamani kubwa au yakuti samawi ya thamani kubwa.

17 Dhahabu wala mawe maangavu haviwezi kulinganishwa nayo,

wala haiwezi hubadilishwa na vito vya dhahabu.

18 Marijani na yaspi hazistahili kutajwa;

thamani ya hekima ni zaidi ya akiki nyekundu.

19 Yakuti manjano ipatikanayo Kushi haiwezi kulinganishwa nayo,

wala haiwezi kununuliwa kwa dhahabu safi.

20 “Ni wapi basi hekima itokako?

Ufahamu hukaa wapi?

21 Imefichika machoni pa kila kitu kilicho hai,

imesitiriwa hata kwa ndege wa angani.

22 Uharibifu na Mauti husema,

‘Ni uvumi wake tu uliotufikia masikioni mwetu.’

23 Mungu anaifahamu njia ya kuiendea hekima

na ndiye peke yake anayefahamu inakokaa,

24 kwa maana yeye huitazama miisho ya dunia

na huona kila kitu chini ya mbingu.

25 Alipofanyiza nguvu za upepo

na kuyapima maji,

26 alipofanya maagizo kwa ajili ya mvua

na njia kwa ajili ya umeme wa radi,

27 ndipo alipoitazama hekima na kuikadiria thamani yake,

akaithibitisha na kuihakikisha.

28 Naye Mungu akamwambia mwanadamu,

‘KumchaBwana: hiyo ndiyo hekima,

nako kujitenga na uovu ndio ufahamu.’ ”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/28-df51764e811b351b5adcaf1c2f63aecd.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 29

Ayubu Anamaliza Utetezi Wake

1 Ayubu akaendelea na hoja yake, akasema:

2 “Tazama jinsi ninavyoitamani miezi iliyopita,

zile siku ambazo Mungu alikuwa akinilinda,

3 wakati taa yake iliniangazia kichwani changu,

na kwa mwanga wake Mungu nikapita katikati ya giza!

4 Natamani siku zile nilizokuwa katika ustawi wangu,

wakati urafiki wa Mungu wa ndani ulipoibariki nyumba yangu,

5 wakati Mwenyezi alikuwa pamoja nami,

nao watoto wangu walikuwa wamenizunguka,

6 wakati njia yangu ilikuwa imenyweshewa siagi,

nao mwamba ukanimiminia vijito vya mafuta ya zeituni.

7 “Wakati nilipokwenda kwenye lango la mji

na kuketi katika kiwanja,

8 vijana waliniona wakakaa kando,

nao wazee walioketi wakasimama;

9 wakuu wakaacha kuzungumza

na kuziba vinywa vyao kwa mikono yao;

10 wenye vyeo wakanyamazishwa,

nazo ndimi zao zikagandamana na makaakaa ya vinywa vyao.

11 Yeyote aliyenisikia alinena mema juu yangu,

nao walioniona walinisifu,

12 kwa sababu nilimwokoa maskini aliyeomba msaada,

naye yatima aliyekuwa hana wa kumsaidia.

13 Mtu aliyekuwa karibu kufa alinibariki,

nami niliufanya moyo wa mjane kuimba.

14 Niliivaa haki kama vazi langu;

uadilifu ulikuwa joho langu na kilemba changu.

15 Nilikuwa macho ya kipofu

na miguu kwa kiwete.

16 Nilikuwa baba kwa mhitaji;

nilimtetea mgeni.

17 Niliyavunja meno makali ya waovu,

na kuwapokonya wahanga kwenye meno yao.

18 “Nikafikiri, ‘Nitafia katika nyumba yangu mwenyewe,

nazo siku zangu zitakuwa nyingi kama chembechembe za mchanga.

19 Mizizi yangu itafika mpaka kwenye maji,

nao umande utakaa juu ya matawi yangu usiku kucha.

20 Utukufu wangu utabakia kuwa mpya ndani yangu,

upinde wangu daima utaendelea kuwa mpya mkononi mwangu.’

21 “Watu walinisikiliza kwa tumaini,

wakingojea ushauri wangu kwa utulivu.

22 Baada ya mimi kuzungumza, hawakusema zaidi;

maneno yangu yaliingia masikioni mwao kwa makini.

23 Waliningojea kama manyunyu ya mvua

na kuyapokea maneno yangu

kama ardhi inyonyavyo mvua ya vuli.

24 Walipokata tamaa niliwaonyesha uso wa furaha;

nuru ya uso wangu ilikuwa ya thamani kwao.

25 Niliwachagulia njia na kukaa kama mkuu wao;

niliishi kama mfalme katikati ya majeshi yake;

nikawa kama yeye anayewafariji waombolezaji.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/29-6d71ac5ab2e4ddd690952a27673daf69.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 30

1 “Lakini sasa watu wadogo kwa umri kuniliko wananidhihaki,

watu ambao baba zao ningekataa kwa dharau

kuwaweka pamoja na mbwa wangu wa kulinda kondoo.

2 Nguvu za mikono yao zingekuwa na faida gani kwangu,

kwa kuwa nguvu zao zilikuwa zimewaishia?

3 Wakiwa wamekonda kutokana na kupungukiwa na kwa njaa,

walizurura usiku katika nchi kame iliyo ukiwa.

4 Katika vichaka walikusanya mimea ya chumvi,

nacho chakula chao kilikuwa mizizi ya mti wa mfagio.

5 Walifukuzwa mbali na watu wao,

wakipigiwa kelele kama wevi.

6 Walilazimika kuishi katika mikondo ya vijito vilivyokauka,

kwenye majabali na mahandaki.

7 Kwenye vichaka walilia kama punda,

na walijisongasonga pamoja kwenye vichaka.

8 Wao ni watoto wa wapumbavu wenye asili ya ubaya,

waliofukuzwa watoke katika nchi.

9 “Nao sasa wana wao wananidhihaki katika nyimbo;

nimekuwa kitu cha dhihaka kwao.

10 Wananichukia sana na kujitenga nami,

wala hawasiti kunitemea mate usoni.

11 Sasa kwa kuwa Mungu ameilegeza kamba ya upinde wangu na kunitesa,

wamekuwa huru kunitendea waonavyo.

12 Kuume kwangu kundi linashambulia;

wao huitegea miguu yangu tanzi,

na kunizingira.

13 Huizuia njia yangu,

nao hufanikiwa katika kuniletea maafa,

nami sina yeyote wa kunisaidia.

14 Wananijia kama watu wapitao katika ufa mpana;

katikati ya magofu huja na kunishambulia.

15 Vitisho vimenifunika;

heshima yangu imetoweshwa kama kwa upepo,

salama yangu imetoweka kama wingu.

16 “Sasa maisha yangu yamefikia mwisho;

siku za mateso zimenikamata.

17 Usiku mifupa yangu inachoma;

maumivu yanayonitafuna hayatulii kamwe.

18 Kwa uwezo wake mkuu Mungu huwa kwangu kama nguo;

hushikamana nami kama ukosi wa vazi langu.

19 Yeye amenitupa kwenye matope,

nami nimekuwa kama mavumbi na majivu.

20 “EeBwana, ninakulilia wewe lakini hunijibu;

ninasimama, nawe unanitazama tu.

21 Wewe unanigeukia bila huruma;

unanishambulia kwa nguvu za mkono wako.

22 Unaninyakua na kunipeperusha kwa upepo;

umenirusha huku na huko kwenye dhoruba kali.

23 Ninajua utanileta mpaka kifoni,

mahali ambapo wenye uhai wote wamewekewa.

24 “Hakika hakuna yeyote amshambuliaye mhitaji,

anapoomba msaada katika shida yake.

25 Je, sikulia kwa ajili ya wale waliokuwa katika taabu?

Je, nafsi yangu haikusononeka kwa ajili ya maskini?

26 Lakini nilipotazamia mema, mabaya yalinijia;

nilipotafuta nuru, ndipo giza lilipokuja.

27 Kusukwasukwa ndani yangu kamwe hakutulii;

siku za mateso zinanikabili.

28 Ninazunguka nikiwa nimeungua, lakini si kwa jua;

ninasimama katika kusanyiko nikiomba msaada.

29 Nimekuwa ndugu wa mbweha,

rafiki wa mabundi.

30 Ngozi yangu imekuwa nyeusi nayo inachunika;

mifupa yangu inaungua kwa homa.

31 Kinubi changu kimegeuka kuwa maombolezo,

nayo filimbi yangu imekuwa sauti ya kilio.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/30-d655d6bc17ce8e3ebf55bd52cfb01282.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 31

1 “Nimefanya agano na macho yangu

yasimtazame msichana kwa kumtamani.

2 Kwa kuwa fungu la mwanadamu ni gani kutoka kwa Mungu juu,

urithi wake kutoka kwa Mungu Mwenye Nguvu Aliye juu?

3 Je, si uharibifu kwa watu waovu,

maangamizi kwa wale watendao mabaya?

4 Je, yeye hazioni njia zangu

na kuihesabu kila hatua yangu?

5 “Kama nimeishi katika uongo

au mguu wangu umekimbilia udanganyifu,

6 Mungu na anipime katika mizani za uaminifu,

naye atajua kwamba sina hatia:

7 kama hatua zangu zimepotoka kutoka kwenye njia,

kama moyo wangu umeongozwa na macho yangu,

au kama mikono yangu imetiwa unajisi,

8 basi wengine na wale nilichokipanda,

nayo yale yote niliyootesha na yangʼolewe.

9 “Kama moyo wangu umeshawishiwa na mwanamke,

au kama nimevizia mlangoni mwa jirani yangu,

10 basi mke wangu na asage nafaka ya mwanaume mwingine,

nao wanaume wengine walale naye.

11 Kwa kuwa hilo lingekuwa aibu,

naam, dhambi ya kuhukumiwa.

12 Ni moto uwakao kwa Uharibifu;

ungekuwa umengʼoa mavuno yangu.

13 “Kama ningewanyima haki watumishi wangu wanaume au vijakazi wangu,

walipokuwa na manungʼuniko dhidi yangu,

14 nitafanya nini Mungu atakaponikabili?

Nitamjibu nini nitakapoitwa kutoa hesabu?

15 Je, yeye aliyeniumba tumboni mwa mama yangu,

si ndiye aliwaumba?

Je, si ni yeye huyo mmoja aliyetuumba sote

ndani ya mama zetu?

16 “Ikiwa nimewanyima maskini haja zao,

au kuyaacha macho ya wajane yadhoofike,

17 kama nimekula chakula changu mwenyewe,

bila kuwashirikisha yatima;

18 lakini tangu ujana wangu nimemlea yatima kama ambavyo baba angefanya,

nami tangu kuzaliwa kwangu nimewaongoza wajane:

19 kama nilimwona yeyote akiteseka kwa kukosa nguo,

au mtu mhitaji asiye na mavazi

20 ambaye wala moyo wake haukunibariki

kwa kumpatia joto kwa mavazi ya manyoya ya kondoo zangu,

21 na kama nimeinua mkono wangu dhidi ya yatima,

nikijua kuwa nina ushawishi mahakamani,

22 basi mkono wangu na unyofoke toka begani mwangu,

nao na uvunjike kutoka kiungio chake.

23 Kwa kuwa niliogopa uharibifu kutoka kwa Mungu,

nami kwa kuuogopa utukufu wake sikuweza kufanya mambo kama hayo.

24 “Kama nimeweka tumaini langu kwenye dhahabu,

au kuiambia dhahabu safi, ‘Wewe ndiwe salama yangu,’

25 kama nimefurahia wingi wa utajiri wangu,

ustawi ambao mikono yangu ilikuwa imepata,

26 kama nimelitazama jua katika kungʼaa kwake

au mwezi ukienda kwa fahari yake,

27 hivyo moyo wangu kushawishiwa kwa siri,

au kubusu mkono wangu kwa kuviheshimu,

28 basi hiyo pia ingekuwa dhambi ya kuhukumiwa,

kwa kuwa ningekuwa si mwaminifu kwa Mungu aishiye juu sana.

29 “Kama nimeshangilia msiba wa adui yangu,

au kutazama kwa furaha taabu iliyomjia,

30 lakini sikuruhusu kinywa changu kufanya dhambi

kwa kuomba laana dhidi ya maisha yake;

31 kama watu wa nyumbani mwangu kamwe hawakusema,

‘Ni nani ambaye hajashibishwa na nyama ya Ayubu?’

32 Lakini hakuna mgeni aliyelala njiani,

kwa maana mlango wangu ulikuwa wazi kwa msafiri;

33 kama nimeifunika dhambi yangu kama wanadamu wengine wafanyavyo,

kwa kuficha hatia yangu moyoni mwangu,

34 kwa sababu ya kuogopa umati wa watu,

na hivyo kuwa na hofu ya kudharauliwa na jamaa,

nikanyamaza kimya nisitoke nje ya mlango:

35 (“Laiti kama angekuwepo mtu wa kunisikia!

Tazama sasa ninatia sahihi kwenye utetezi wangu:

Mwenyezi na anijibu;

mshtaki wangu na aweke mashtaka yake kwenye maandishi.

36 Hakika ningeyavaa begani mwangu,

ningeyavaa kama taji.

37 Ningempa hesabu ya kila hatua yangu,

ningemwendea kama mwana wa mfalme.)

38 “Kama nchi yangu inalia dhidi yangu,

na mifereji yake yote imelowana kwa machozi,

39 kama nimekula mazao yake bila malipo,

au kuvunja mioyo ya wapangaji wake,

40 basi miiba na iote badala ya ngano,

na magugu badala ya shayiri.”

Mwisho wa maneno ya Ayubu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/31-c99ad5dba81d4c9faaf00f3dce8a272b.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 32

Elihu Awakemea Rafiki Za Ayubu

1 Basi watu hawa watatu wakaacha kumjibu Ayubu, kwa kuwa alikuwa mwadilifu machoni pake mwenyewe.

2 Lakini Elihu mwana wa Barakeli, wa kabila la Buzi wa jamaa ya Ramu, akamkasirikia sana Ayubu, kwa sababu ya kujihesabia haki mwenyewe badala ya Mungu.

3 Pia aliwakasirikia hao rafiki watatu wa Ayubu, kwa sababu hawakuweza kupata njia ya kuthibitisha ya kuwa hayo maneno ya Ayubu hayakuwa ya kweli, nao bado walikuwa wamemlaumu.

4 Basi Elihu alikuwa amesubiri kwanza waongee na Ayubu kwa sababu walikuwa na umri mkubwa kumliko yeye.

5 Lakini alipoona watu hao watatu hawakuwa na kitu zaidi cha kusema, hasira yake ikaamka.

6 Basi Elihu mwana wa Barakeli wa kabila la Buzi akasema:

“Mimi ni mdogo kwa umri,

nanyi ni wazee;

ndiyo sababu niliogopa,

sikuthubutu kuwaambia kile ninachojua.

7 Nilifikiri, ‘Yafaa umri useme,

nao wingi wa miaka ungefundisha hekima.’

8 Lakini ni Roho iliyoko ndani ya mwanadamu,

pumzi ya Mwenyezi, ndiyo impayo yeye ufahamu.

9 Sio wazee peke yao walio na hekima,

sio wenye umri mkubwa peke yao wanaofahamu lililo sawa.

10 “Kwa hiyo nasema: Nisikilizeni mimi;

mimi nami nitawaambia lile ninalojua.

11 Nilingojea mlipokuwa mnaongea,

nilizisikiliza hoja zenu;

mlipokuwa mkitafuta maneno ya kusema,

12 niliwasikiliza kwa makini.

Lakini hakuna hata mmoja wenu

aliyethibitisha kwamba Ayubu amekosa;

hakuna hata mmoja wenu

aliyeweza kujibu hoja zake.

13 Msiseme, ‘Tumepata hekima;

Mungu na amthibitishe kuwa mwongo,

wala si mwanadamu.’

14 Lakini Ayubu hajayapanga maneno yake dhidi yangu,

nami sitamjibu kwa kutumia hoja zenu.

15 “Wametiwa hofu na hawana la zaidi la kusema;

maneno yamewaishia.

16 Je, ningoje sasa kwa sababu wamekuwa kimya,

kwa vile sasa wanasimama bila kuwa na la kujibu?

17 Mimi nami nitakuwa na la kusema;

mimi nami nitasema lile nilijualo.

18 Kwa kuwa nimejawa na maneno,

nayo Roho iliyomo ndani yangu yanisukuma;

19 ndani yangu niko kama chupa iliyojazwa divai,

kama kiriba kipya cha divai kilicho tayari kupasuka.

20 Ni lazima niseme ili niweze kutulia;

ni lazima nifumbue midomo yangu nipate kujibu.

21 Sitampendelea mtu yeyote,

wala sitajipendekeza kwa mtu yeyote;

22 kwa kuwa kama ningekuwa stadi wa kujipendekeza,

Muumba wangu angeniondolea mbali kwa upesi.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/32-06188589f097de19f345121b69023171.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 33

Elihu Anamkemea Ayubu

1 “Lakini Ayubu, sasa, sikiliza maneno yangu;

zingatia kila kitu nitakachosema.

2 Karibu nitafungua kinywa changu;

maneno yangu yapo katika ncha ya ulimi wangu.

3 Maneno yangu yanatoka katika moyo mnyofu;

midomo yangu hunena kwa uaminifu yale niyajuayo.

4 Roho wa Mungu ameniumba;

pumzi ya Mwenyezi hunipa uhai.

5 Unijibu basi, kama unaweza;

jiandae kunikabili mimi.

6 Mimi ni kama wewe mbele za Mungu;

mimi pia nimetolewa kwenye udongo.

7 Huna sababu ya kuniogopa,

wala mkono wangu haupaswi kukulemea.

8 “Lakini umesema nikiwa ninakusikia,

nami nilisikia maneno yenyewe:

9 ‘Mimi ni safi na sina dhambi;

mimi ni safi na sina hatia.

10 Lakini bado Mungu amepata dosari kwangu,

naye ananiona kama adui yake.

11 Ananifunga miguu kwa pingu,

tena anaziangalia njia zangu zote kwa karibu.’

12 “Lakini mimi ninakuambia, katika jambo hili wewe una makosa,

kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mwanadamu.

13 Kwa nini unamlalamikia

kwamba yeye hamjibu mwanadamu?

14 Kwa kuwa Mungu husema, wakati huu kwa njia moja,

au wakati mwingine kwa njia nyingine,

ingawa mwanadamu anaweza asielewe.

15 Mungu husema na mwanadamu katika ndoto,

katika maono ya usiku,

wakati usingizi mzito uwaangukiapo

wanadamu wasinziapo vitandani mwao,

16 anaweza akasemea masikioni mwao,

na kuwatia hofu kwa maonyo,

17 ili kumgeuza mtu kutoka kwenye kutenda mabaya

na kumwepusha na kiburi,

18 kuiokoa nafsi yake na shimo,

uhai wake usiangamizwe kwa upanga.

19 Mtu anaweza kutiwa adabu kwa maumivu kitandani mwake,

kwa dhiki za mfululizo katika mifupa yake,

20 kiasi kwamba maisha yake yenyewe yanakataa chakula

nayo nafsi yake ikakichukia kabisa hata chakula kizuri.

21 Nyama ya mwili wake huisha kwa kukonda,

nayo mifupa yake ambayo mwanzoni ilikuwa imefichika,

sasa inatokeza nje.

22 Nafsi yake inakaribia kaburi,

nao uhai wake karibu na wajumbe wa kifo.

23 “Kama bado kuna malaika upande wake

kama mtetezi, mmoja miongoni mwa elfu,

wa kumwambia mwanadamu lililo jema kwake,

24 kumwonea huruma na kusema,

‘Mwokoe asije akatumbukia shimoni;

nimepata ukombozi kwa ajili yake’:

25 ndipo nyama ya mwili wake hufanywa mpya kama ya mtoto;

hurudishwa upya kama siku za ujana wake.

26 Humwomba Mungu, akapata kibali kwake,

huuona uso wa Mungu na kushangilia kwa furaha;

Mungu humrudisha katika hali yake ya uadilifu.

27 Ndipo huja mbele za watu na kusema,

‘Nilitenda dhambi na kupotosha kilichokuwa haki,

lakini sikuadhibiwa kama nilivyostahili.

28 Alinikomboa nafsi yangu nisitumbukie shimoni,

nami nitaishi ili kuufurahia mwanga.’

29 “Mungu hufanya haya yote kwa mwanadamu;

mara mbili hata mara tatu,

30 ili aigeuze nafsi yake toka shimoni,

ili nuru ya uzima imwangazie.

31 “Ayubu, zingatia, nisikilize mimi;

nyamaza, nami nitanena.

32 Kama unalo lolote la kusema, unijibu;

sema, kwa maana ninataka uonekane huna hatia.

33 Lakini kama huna la kusema, basi nisikilize mimi;

nyamaza, nami nitakufundisha hekima.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/33-8abc26d47a0a25480736b4429981e5f6.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 34

Elihu Anatangaza Haki Ya Mungu

1 Kisha Elihu akasema:

2 “Sikieni maneno yangu, enyi watu wenye hekima;

nisikilizeni mimi, ninyi watu wenye maarifa.

3 Kwa kuwa sikio huyajaribu maneno

kama vile ulimi uonjavyo chakula.

4 Tujichagulie wenyewe yaliyo sawa,

nasi tujifunze pamoja yaliyo mema.

5 “Ayubu anasema, ‘Mimi sina hatia,

lakini Mungu ameninyima haki yangu.

6 Ingawa niko sawa,

ninaonekana mwongo;

nami ingawa sina kosa,

kidonda changu hakiponi.’

7 Ni mtu gani aliye kama Ayubu,

anywaye dharau kama maji?

8 Ashirikianaye na watenda mabaya

na kuchangamana na watu waovu.

9 Kwa kuwa anasema, ‘Haimfaidi mwanadamu kitu chochote

anapojitahidi kumpendeza Mungu.’

10 “Hivyo nisikilizeni mimi, ninyi watu wenye ufahamu.

Kamwe Mungu hatendi uovu,

Mwenyezi hafanyi kosa.

11 Humlipa mwanadamu kwa ajili ya lile alilotenda;

huleta juu yake kile ambacho matendo yake yanastahili.

12 Ni jambo lisiloweza kufikiriwa kwamba Mungu angefanya makosa,

kwamba Mwenyezi angepotosha hukumu.

13 Je, ni nani aliyemtawaza juu ya dunia?

Ni nani aliyemweka kuwa mwangalizi wa ulimwengu wote?

14 Kama lilikuwa kusudi la Mungu,

naye akaiondoa Roho yake na pumzi yake,

15 wanadamu wote wangeliangamia kwa pamoja,

na mtu angerudi mavumbini.

16 “Kama ninyi mnaufahamu, sikieni hili;

sikilizeni hili nisemalo.

17 Je, yeye aichukiaye haki aweza kutawala?

Je, utamhukumu mwenye haki, Aliye na Nguvu Zote?

18 Je, si ni yeye awaambiaye wafalme, ‘Ninyi hamfai kitu,’

nao watu mashuhuri, ‘Ninyi ni waovu,’

19 yeye asiyependelea wakuu,

wala haonyeshi upendeleo kwa matajiri kuliko maskini,

kwa kuwa wote ni kazi ya mikono yake?

20 Wanakufa ghafula, usiku wa manane;

watu wanatikiswa nao hupita;

wenye nguvu huondolewa

bila mkono wa mwanadamu.

21 “Macho yake yanazitazama njia za wanadamu;

anaona kila hatua yao.

22 Hakuna mahali penye giza nene, wala uvuli mkubwa,

ambapo watenda mabaya wanaweza kujificha.

23 Mungu hana haja ya kumchunguza mtu sana,

ili apate kuja mbele zake kwa hukumu.

24 Bila kuuliza huwapondaponda wenye nguvu nyingi

na kuwaweka wengine mahali pao.

25 Kwa sababu huyaangalia matendo yao yote,

huwaondoa usiku, nao wakaangamia.

26 Anawaadhibu kwa ajili ya uovu wao

mahali ambapo kila mmoja ataweza kuwaona,

27 kwa sababu wameacha kumfuata Mungu,

nao hawakuiheshimu njia yake hata moja.

28 Wamesababisha kilio cha maskini kifike mbele zake,

hivyo akasikia kilio cha wahitaji.

29 Lakini kama akinyamaza kimya,

ni nani awezaye kumhukumu?

Kama akiuficha uso wake,

ni nani awezaye kumwona?

Ikiwa ni taifa au mtu mmoja, kwake ni sawa,

30 ili kumzuia mtu mwovu kutawala,

au wale ambao huwategea watu mitego.

31 “Kama mwanadamu akimwambia Mungu,

‘Nimekosa lakini sitatenda dhambi tena.

32 Nifundishe nisichoweza kuona;

kama nimekukosea, sitafanya hivyo tena.’

33 Je basi, Mungu atakulipa kwa masharti yako,

wakati wewe umekataa kutubu?

Yakupasa wewe uamue, wala si mimi;

sasa niambie lile ulijualo.

34 “Wanadamu wenye ufahamu husema,

wenye hekima wanaonisikia huniambia,

35 ‘Ayubu huongea bila maarifa;

maneno yake hayana busara.’

36 Laiti Ayubu angejaribiwa hadi kikomo cha mwisho,

kwa sababu anajibu kama mtu mwovu!

37 Kwenye dhambi yake huongeza uasi;

kwa dharau hupiga makofi miongoni mwetu,

na kuzidisha maneno yake dhidi ya Mungu.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/34-95a833a22622be8b51f604d546339a58.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 35

Elihu Analaumu Mtu Kujiona Kuwa Mwenye Haki

1 Ndipo Elihu akasema:

2 “Je, unadhani hili ni haki?

Wewe unasema, ‘Nina haki mbele za Mungu.’

3 Bado unamuuliza, ‘Ni faida gani nimepata,

na imenifaidi nini kwa kutokutenda dhambi?’

4 “Ningependa nikujibu wewe

pamoja na marafiki zako walio pamoja nawe.

5 Tazama juu mbinguni ukaone;

yaangalie mawingu yaliyo juu sana juu yako.

6 Je, ukitenda dhambi, inamdhuruje Mungu?

Kama dhambi zako zikiwa nyingi,

hilo linamfanyia nini Mungu?

7 Kama wewe ni mwadilifu, unampa nini,

au yeye anapokea nini mkononi kwako?

8 Uovu wako unamdhuru tu mtu mwingine kama wewe,

nayo haki yako inawafaa wanadamu tu.

9 “Wanadamu hulia kwa kulemewa na mateso;

huomba msaada kutoka mkono wenye nguvu.

10 Lakini hakuna asemaye, ‘Yuko wapi Mungu Muumba wangu,

yeye anifanyaye niimbe usiku,

11 yeye atufundishaye sisi zaidi kuliko wanyama wa dunia,

na kutufanya wenye hekima kuliko ndege wa angani?’

12 Yeye hajibu wakati watu waliapo

kwa sababu ya kiburi cha watu waovu.

13 Naam, Mungu hasikilizi maombi yao ya ubatili;

Mwenyezi hayazingatii.

14 Si zaidi sana kwamba hatakusikiliza

wewe usemapo humwoni,

tena ya kwamba shauri lako liko mbele zake

na wewe lazima umngojee,

15 pia zaidi, kwamba hasira yake kamwe haiadhibu

wala haangalii uovu hata kidogo?

16 Hivyo Ayubu hufumbua kinywa chake kwa maneno yasiyo na maana;

anaongea maneno mengi bila maarifa.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/35-9d717b87ee5a7272fadc496a6c03cdb7.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 36

Elihu Atukuza Wema Wa Mungu

1 Elihu akaendelea kusema:

2 “Nivumilie kidogo zaidi nami nitakuonyesha

kwamba yako mengi zaidi ya kusemwa kwa ajili ya Mungu.

3 Ninayapata maarifa yangu kutoka mbali,

nami nitamhesabia haki Muumba wangu.

4 Uwe na hakika kwamba maneno yangu si ya uongo;

mmoja aliye mkamilifu katika maarifa yuko pamoja na wewe.

5 “Mungu ni mwenye nguvu, lakini hamdharau mwanadamu;

ni mwenye nguvu, naye ni thabiti katika shauri lake.

6 Hawaachi waovu waendelee kuishi,

bali huwapa walioteswa haki yao.

7 Yeye haondoi macho yake kwa wenye haki;

huwaketisha penye viti vya enzi pamoja na wafalme

na kuwatukuza milele.

8 Lakini ikiwa watu wamefungwa kwenye minyororo,

wakiwa wameshikiliwa na kamba za mateso,

9 huwaonyesha yale waliyoyatenda,

kwamba wametenda dhambi kwa majivuno.

10 Huwafanya wao kusikia maonyo,

na huwaagiza kutubu uovu wao.

11 Kama wakitii na kumtumikia,

wataishi siku zao zilizobaki katika mafanikio,

na miaka yao katika utoshelevu.

12 Lakini wasiposikiliza,

wataangamia kwa upanga,

nao watakufa pasipo maarifa.

13 “Wasiomcha Mungu moyoni mwao huficha chuki;

hata anapowafunga, hawamwombi msaada.

14 Wanakufa wangali vijana,

miongoni mwa wanaume hanithi wa mahali pa kuabudia miungu.

15 Bali wao wanaoteseka huwaokoa katika mateso yao,

na kuzungumza nao katika dhiki zao.

16 “Yeye anakubembeleza utoke katika mataya ya dhiki,

ili kukuweka mahali palipo na nafasi mbali na kizuizi,

hadi kwenye meza yako ya faraja iliyojaa vyakula vizuri.

17 Lakini sasa umelemewa na hukumu kwa ajili ya uovu;

hukumu na haki vimekukamata.

18 Uwe mwangalifu ili yeyote asikushawishi kwa utajiri;

usipotoshwe kwa fungu kubwa la rushwa.

19 Je, utajiri wako hata nguvu zako nyingi

vinaweza kukusaidia usiingie kwenye dhiki?

20 Usiutamani usiku uje,

ili uwaburute watu mbali na nyumba zao.

21 Jihadhari usigeukie uovu,

ambao unaupenda zaidi kuliko mateso.

22 “Mungu ametukuzwa katika nguvu zake.

Ni nani aliye mwalimu kama yeye?

23 Ni nani aliyemwelekeza katika njia zake,

au kumwambia, ‘Wewe umetenda yasiyo sawa’?

24 Kumbuka kuzitukuza kazi zake,

ambazo watu wamezisifu katika wimbo.

25 Wanadamu wote wameiona;

watu wanaikazia macho kwa mbali.

26 Tazama jinsi Mungu alivyo mkuu,

kupita ufahamu wetu!

Hesabu ya miaka yake haitafutiki.

27 “Yeye huvuta juu matone ya maji,

ayachujayo kama mvua kutoka kwenye vijito;

28 mawingu huangusha chini maji yake,

nayo mvua nyingi huwanyeshea wanadamu.

29 Ni nani ajuaye jinsi ayatandazavyo mawingu,

jinsi angurumavyo kutoka hemani mwake.

30 Tazama jinsi anavyotandaza umeme wa radi kumzunguka,

naye huvifunika vilindi vya bahari.

31 Hivi ndivyo atawalavyo mataifa,

na kuwapa chakula kwa wingi.

32 Huujaza mkono wake kwa umeme wa radi,

na kuuagiza kulenga shabaha yake.

33 Ngurumo zake hutangaza dhoruba inayokuja;

hata mifugo hujulisha kukaribia kwake.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/36-9dfe7bb9c67e7d2f7e4b2305978f90e7.mp3?version_id=1627—