Categories
Ayubu

Ayubu 17

1 Moyo wangu umevunjika,

siku zangu zimefupishwa,

kaburi linaningojea.

2 Hakika wenye mizaha wamenizunguka;

macho yangu yamebaki kutazama uadui wao.

Ayubu Anaomba Msaada

3 “Ee Mungu, nipe dhamana unayodai.

Ni nani mwingine atakayeweka dhamana kwa ajili yangu?

4 Umezifunga akili zao zisipate ufahamu,

kwa hiyo hutawaacha wapate ushindi.

5 Kama mtu akiwashutumu rafiki zake ili apate ujira,

macho ya watoto wake yatashindwa kuona.

6 “Mungu amenifanya kitu cha dhihaka kwa kila mtu,

mtu ambaye watu humtemea mate usoni.

7 Macho yangu yamefifia kwa ajili ya majonzi;

umbile langu lote ni kama kivuli.

8 Watu wanyofu wanatishwa na hili;

watu wasio na hatia wanasimama dhidi ya wasiomcha Mungu.

9 Hata hivyo, waadilifu watazishika njia zao,

nao wale wenye mikono safi wataendelea kupata nguvu.

10 “Lakini ninyi njooni, ninyi nyote, jaribuni tena!

Sitampata mtu mwenye hekima miongoni mwenu.

11 Siku zangu zimepita, mipango yangu imevunjika,

vivyo hivyo shauku za moyo wangu.

12 Watu hawa hufanya usiku kuwa mchana,

kwenye giza wao husema, ‘Mwanga u karibu.’

13 Kama nyumba pekee ninayoitarajia ni kaburi,

kama nikikitandika kitanda changu gizani,

14 kama nikiuambia uharibifu, ‘Wewe u baba yangu,’

na kuliambia buu, ‘Wewe u mama yangu’ au ‘Dada yangu,’

15 liko wapi basi tarajio langu?

Ni nani awezaye kuona tarajio lolote kwa ajili yangu?

16 Je, litashuka chini hadi kwenye malango ya mauti?

Je, tutashuka pamoja mavumbini?”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/17-4a8d58413b7361fd4ec108a991e584e0.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 18

Bildadi Anasema: Mungu Huwaadhibu Waovu

1 Bildadi Mshuhi akajibu:

2 “Je, ni lini utafika mwisho wa maneno haya?

Uwe mwenye busara, nasi ndipo tutakapoweza kuongea.

3 Kwa nini sisi tunafikiriwa kama wanyama,

na kuonekana wajinga machoni pako?

4 Wewe unayejirarua mwenyewe vipande vipande

katika hasira yako,

je, dunia iachwe kwa ajili yako wewe?

Au ni lazima miamba iondolewe mahali pake?

5 “Taa ya mwovu imezimwa,

nao mwali wa moto wake umezimika.

6 Mwanga hemani mwake umekuwa giza;

taa iliyo karibu naye imezimika.

7 Nguvu za hatua zake zimedhoofishwa;

shauri lake baya litamwangusha.

8 Miguu yake imemsukumia kwenye wavu,

naye anatangatanga kwenye matundu ya wavu.

9 Tanzi litamkamata kwenye kisigino;

mtego utamshikilia kwa nguvu.

10 Kitanzi kimefichwa ardhini kwa ajili yake;

mtego uko kwenye njia yake.

11 Vitisho vimemtia hofu kila upande,

na adui zake humwandama kila hatua.

12 Janga linamwonea shauku;

maafa yako tayari kwa ajili yake aangukapo.

13 Nayo yatakula sehemu ya ngozi yake;

mzaliwa wa kwanza wa mauti atakula maungo yake.

14 Atangʼolewa kutoka usalama wa hema lake,

na kupelekwa kwa mfalme wa vitisho.

15 Moto utakaa katika hema lake;

moto wa kiberiti utamwagwa juu ya makao yake.

16 Mizizi yake chini itakauka

na matawi yake juu yatanyauka.

17 Kumbukumbu lake litatoweka katika dunia,

wala hatakuwa na jina katika nchi.

18 Ameondolewa nuruni na kusukumiwa gizani,

naye amefukuzwa mbali atoke duniani.

19 Hana mtoto wala mzao miongoni mwa watu wake,

wala aliyenusurika mahali alipoishi.

20 Watu wa magharibi watashangaa yaliyompata;

watu wa mashariki watapatwa na hofu.

21 Hakika ndivyo yalivyo makao ya mtu mwovu;

ndivyo palivyo mahali pake mtu asiyemjua Mungu.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/18-d89e2a1e195c1b0db89cbba5f1372856.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 19

Ayubu Anajibu: Najua Mkombozi Wangu Yu Hai

1 Ndipo Ayubu akajibu:

2 “Je, mtaendelea kunitesa mpaka lini,

na kuniponda kwa maneno yenu?

3 Mara kumi hizi mmenishutumu;

bila aibu mnanishambulia.

4 Kama ni kweli nimepotoka,

kosa langu ninabaki kuhusika nalo mwenyewe.

5 Kama kweli mngejitukuza wenyewe juu yangu,

na kutumia unyonge wangu dhidi yangu,

6 basi jueni kuwa Mungu amenitendea yaliyo mabaya,

naye amekokota wavu wake kunizunguka.

7 “Ingawa ninalia, ‘Nimetendewa mabaya!’ sipati jibu;

ingawa ninaomba msaada, hakuna haki.

8 Yeye ameizuia njia yangu hivyo siwezi kupita;

ameyafunika mapito yangu na giza.

9 Amenivua heshima yangu,

na kuniondolea taji kichwani pangu.

10 Amenibomoa kila upande hadi nimeisha;

amelingʼoa tegemeo langu kama mti.

11 Hasira yake imewaka juu yangu;

amenihesabu kuwa miongoni mwa adui zake.

12 Majeshi yake yananisogelea kwa nguvu;

yamenizingira,

yamepiga kambi kulizunguka hema langu.

13 “Amewatenga ndugu zangu mbali nami;

wale tunaojuana nao wamefarakana nami kabisa.

14 Watu wa jamaa yangu wamekwenda mbali;

rafiki zangu wamenisahau.

15 Wageni wangu na watumishi wangu wa kike wananiona kama mgeni;

wananitazama kama mgeni.

16 Namwita mtumishi wangu, wala haitiki,

ingawa namwomba kwa kinywa changu mwenyewe.

17 Pumzi ya kinywa changu ni kinyaa kwa mke wangu;

nimekuwa chukizo mno kwa ndugu zangu mwenyewe.

18 Hata watoto wadogo hunidhihaki;

ninapojitokeza, hunifanyia mzaha.

19 Rafiki zangu wa moyoni wote wananichukia kabisa;

wale niwapendao wamekuwa kinyume nami.

20 Mimi nimebaki mifupa na ngozi tu;

nimeponea nikiwa karibu kufa.

21 “Nihurumieni, rafiki zangu, kuweni na huruma,

kwa kuwa mkono wa Mungu umenipiga.

22 Kwa nini mnanifuatia kama Mungu afanyavyo?

Hamtosheki kamwe na mwili wangu?

23 “Laiti maneno yangu yangewekwa kwenye kumbukumbu,

laiti kwamba yangeandikwa kwenye kitabu,

24 kwamba yangechorwa kwenye risasi kwa kifaa cha chuma,

au kuyachonga juu ya mwamba milele!

25 Ninajua kwamba Mkomboziwangu yu hai,

naye kwamba mwishoni atasimama juu ya nchi.

26 Nami baada ya ngozi yangu kuharibiwa,

bado nikiwa na mwili huu nitamwona Mungu;

27 mimi nitamwona kwa macho yangu mwenyewe:

mimi, wala si mwingine.

Tazama jinsi moyo wangu unavyomtamani sana!

28 “Kama mkisema, ‘Tazama tutakavyomwinda,

maadamu mzizi wa tatizo uko ndani yake,’

29 ninyi wenyewe uogopeni upanga,

kwa kuwa ghadhabu italeta adhabu kwa upanga,

nanyi ndipo mtakapojua kwamba kuna hukumu.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/19-4d145c9095576af9b13d48707c468451.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 20

Sofari Anasema: Uovu Hupokea Malipo Ya Haki

1 Ndipo Sofari Mnaamathi akajibu:

2 “Mawazo yanayonisumbua yananisukuma kujibu,

kwa sababu nimehangaika sana.

3 Ninasikia makaripio ambayo yananivunjia heshima,

nao ufahamu wangu unanisukuma kujibu.

4 “Hakika unajua jinsi ilivyokuwa tangu zamani,

tangu zamani mwanadamu alipowekwa duniani,

5 macheko ya mtu mwovu ni ya muda mfupi,

nayo furaha ya wasiomcha Mungu hudumu kwa kitambo tu.

6 Ingawa kujikweza kwake hufikia mbinguni

na kichwa chake hugusa mawingu,

7 ataangamia milele kama mavi yake mwenyewe.

Wale waliomwona watauliza, ‘Yuko wapi?’

8 Kama ndoto hutoweka, wala hapatikani tena,

amefukuziwa mbali kama maono ya usiku.

9 Jicho lililomwona halitamwona tena;

mahali pake hapatamwona tena.

10 Watoto wake watalipa yote baba yao aliyowadhulumu maskini,

nayo mikono yake itarudisha mali yote aliyonyangʼanya watu.

11 Nguvu za ujana zilizoijaza mifupa yake,

zitalala naye mavumbini.

12 “Ingawa uovu ni mtamu kinywani mwake

naye huuficha chini ya ulimi wake,

13 ingawa hawezi kukubali kuuachia uende,

lakini huuweka kinywani mwake.

14 Hata hivyo chakula chake kitakuwa kichungu tumboni mwake,

nacho kitakuwa sumu kali ya nyoka ndani yake.

15 Atatema mali alizozimeza;

Mungu atalifanya tumbo lake kuzitapika.

16 Atanyonya sumu za majoka;

meno ya nyoka mwenye sumu kali yatamuua.

17 Hatafurahia vijito,

mito inayotiririsha asali na siagi.

18 Vile alivyovitaabikia atavirudisha bila kuvila;

hatafurahia faida itokanayo na biashara yake.

19 Kwa kuwa aliwaonea maskini na kuwaacha pasipo kitu;

amenyangʼanya kwa nguvu nyumba asizozijenga.

20 “Hakika hatakuwa na raha katika kutamani kwake sana;

hawezi kujiokoa mwenyewe kwa hazina zake.

21 Hakuna chochote kitakachosalia kwa ajili yake ili ale;

kufanikiwa kwake hakutadumu.

22 Katikati ya wingi wa ustawi wake, dhiki itampata;

taabu itamjia kwa nguvu zote.

23 Atakapokuwa amelijaza tumbo lake,

Mungu ataionyesha ghadhabu kali dhidi yake,

na kumnyeshea mapigo juu yake.

24 Ijapokuwa aikimbia silaha ya chuma,

mshale wa shaba utamchoma.

25 Atauchomoa katika mgongo wake,

ncha ingʼaayo kutoka ini lake.

Vitisho vitakuja juu yake;

26 giza nene linavizia hazina zake.

Moto usiopepewa na mtu utamteketeza,

na kuangamiza yaliyosalia nyumbani mwake.

27 Mbingu zitaweka wazi hatia yake,

nayo nchi itainuka kinyume chake.

28 Mafuriko yataichukua nyumba yake,

maji yaendayo kasi katika siku ya ghadhabu ya Mungu.

29 Hili ndilo fungu Mungu alilowagawia waovu,

urithi uliowekwa kwa ajili yao na Mungu.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/20-ac760fc64b5b2d89b62f0d88b39c61c4.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 21

Ayubu Anajibu: Waovu Mara Nyingi Huenda Bila Kuadhibiwa

1 Ndipo Ayubu akajibu:

2 “Yasikilizeni maneno yangu kwa makini;

hii na iwe faraja mnayonipa mimi.

3 Nivumilieni ninapozungumza,

nami nikishazungumza, endeleeni kunidhihaki.

4 “Je, kwani malalamiko yangu yanaelekezwa kwa mwanadamu?

Kwa nini nisikose subira?

5 Niangalieni mkastaajabu;

mkaweke mkono juu ya vinywa vyenu.

6 Ninapowaza juu ya hili, ninaogopa,

nao mwili wangu unatetemeka.

7 Kwa nini waovu wanaendelea kuishi,

wakifikia umri wa uzee na kuendelea kuwa na nguvu?

8 Huwaona watoto wao wakithibitika

wakiwa wamewazunguka,

wazao wao mbele za macho yao.

9 Nyumba zao zi salama wala hakuna hofu;

fimbo ya Mungu haiko juu yao.

10 Madume yao ya ngʼombe huvyaza bila kushindwa kamwe;

ngʼombe wao huzaa wala hawaharibu mimba.

11 Huwatoa watoto wao nje kama kundi;

wadogo wao huchezacheza.

12 Huimba nyimbo kwa matari na kwa kinubi,

nao huifurahia sauti ya filimbi.

13 Huitumia miaka yao katika mafanikio

nao hushuka kaburini kwa amani.

14 Lakini humwambia Mungu, ‘Tuache sisi!’

Hatuna haja ya kufahamu njia zako.

15 Mwenyezi ni nani hata tumtumikie?

Tutapata faida gani kumwomba?

16 Lakini kufanikiwa kwao hakupo mikononi mwao wenyewe,

hivyo najitenga mbali na shauri la waovu.

17 “Lakini ni mara ngapi taa ya waovu huzimwa?

Ni mara ngapi maafa huwajia,

yale yawapatayo ambayo Mungu

huwapangia katika hasira yake?

18 Ni mara ngapi huwa kama majani makavu mbele ya upepo,

kama makapi yachukuliwayo na dhoruba?

19 Imesemekana, ‘Mungu huiweka akiba adhabu ya mtu

kwa ajili ya wanawe.’

Mungu na amlipe mtu mwenyewe,

ili apate kulijua!

20 Macho yake mwenyewe na yaone maangamizi yake;

yeye na ainywe ghadhabu ya Mwenyezi.

21 Kwani anajali nini kuhusu jamaa anayoiacha nyuma,

miezi yake aliyopangiwa ifikapo mwisho?

22 “Je, yuko mtu yeyote awezaye kumfundisha Mungu maarifa,

iwapo yeye ndiye ahukumuye hata walio juu ya wote?

23 Mtu mmoja hufa akiwa na nguvu zake kamili,

akiwa salama na mwenye raha kamili,

24 mwili wake ukiwa umenawiri,

nayo mifupa yake ikiwa imejaa mafuta ndani yake.

25 Mtu mwingine hufa katika uchungu wa nafsi,

akiwa hajafurahia kamwe jambo lolote zuri.

26 Hao wote hulala mavumbini,

nao mabuu huwafunika wote.

27 “Ninayajua kikamilifu yale mnayoyafikiri,

mipango ambayo kwayo mngenitendea mabaya.

28 Mwasema, ‘Iko wapi sasa nyumba ya huyo mtu mkuu,

mahema ambayo watu waovu walikaa?’

29 Je, hamkuwahi kuwauliza hao wanaosafiri?

Je, hamkutafakari taarifa zao:

30 kwamba mtu mwovu huepushwa kutoka siku ya maafa,

kwamba huokolewa kutoka siku ya ghadhabu?

31 Ni nani hulaumu matendo yake mbele ya uso wake?

Ni nani ampatilizaye kwa yale aliyoyatenda?

32 Hupelekwa kaburini,

nao ulinzi ukawekwa kwenye kaburi lake.

33 Udongo ulio bondeni ni mtamu kwake;

watu wote watamfuata,

nao umati wa watu usiohesabika umemtangulia.

34 “Hivyo ninyi mnawezaje kunifariji kwa upuzi wenu?

Hakuna kilichosalia cha majibu yenu isipokuwa uongo!”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/21-c28fa39ae554b3852a4b8086edbd1817.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 22

Elifazi Anasema: Uovu Wa Ayubu Ni Mkubwa

1 Ndipo Elifazi Mtemani akajibu:

2 “Je, mwanadamu aweza kuwa wa faida kwa Mungu?

Je, hata mtu mwenye hekima aweza kumfaidi?

3 Je, Mwenyezi angefurahia nini

kama ungekuwa mwadilifu?

Au je, yeye angepata faida gani

kama njia zako zingekuwa kamilifu?

4 “Je, ni kwa ajili ya utaua wako ndiyo maana anakukemea

na kuleta mashtaka dhidi yako?

5 Je, uovu wako si mkuu?

Dhambi zako si hazina mwisho?

6 Umedai dhamana kwa ndugu zako bila sababu;

umewavua watu nguo zao, ukawaacha uchi.

7 Hukumpa maji aliyechoka,

nawe ulimnyima chakula mwenye njaa,

8 ingawa ulikuwa mtu mwenye uwezo ukimiliki nchi:

mtu uliyeheshimiwa, ukiishi ndani yake.

9 Umewafukuza wajane mikono mitupu

na kuzivunja nguvu za yatima.

10 Ndiyo sababu mitego imekuzunguka pande zote,

hatari ya ghafula inakutia hofu,

11 ndiyo sababu ni giza sana huwezi kuona,

tena ndiyo sababu mafuriko ya maji yamekufunika.

12 “Je, Mungu hayuko katika mbingu za juu?

Juu kuliko nyota zilizo juu sana!

13 Hivyo wewe wasema, ‘Mungu anajua nini?’

Je, yeye huhukumu katika giza kama hilo?

14 Mawingu mazito ni pazia lake, hivyo hatuoni sisi

atembeapo juu ya anga la dunia.

15 Je, utaifuata njia ya zamani,

ambayo watu waovu waliikanyaga?

16 Waliondolewa kabla ya wakati wao,

misingi yao ikachukuliwa na mafuriko.

17 Walimwambia Mungu, ‘Tuache sisi!

Huyo Mwenyezi aweza kutufanyia nini?’

18 Lakini ndiye alizijaza nyumba zao na vitu vizuri,

hivyo ninajitenga mbali na mashauri ya waovu.

19 “Wenye haki wanaona maangamizi yao na kufurahi,

nao wasio na hatia huwadhihaki, wakisema,

20 ‘Hakika adui zetu wameangamizwa,

nao moto umeteketeza mali zao.’

21 “Mjue sana Mungu ili uwe na amani,

ndipo mema yatakapokujia.

22 Uyapokee mafundisho toka kinywani mwake,

na maneno yake uyaweke moyoni mwako.

23 Kama ukimrudia Mwenyezi, utarudishwa upya:

Kama ukiuondoa uovu uwe mbali na hema lako,

24 kama dhahabu yako ukiihesabu kama mavumbi,

dhahabu yako ya Ofiri kama miamba ya mabondeni,

25 ndipo Mwenyezi atakuwa dhahabu yako,

naye atakuwa fedha yako iliyo bora.

26 Hakika ndipo utakapojifurahisha kwa Mwenyezi,

nawe utamwinulia Mungu uso wako.

27 Utamwomba yeye, naye atakusikia,

nawe utazitimiza nadhiri zako.

28 Utakusudia jambo nalo litatendeka,

nao mwanga utaangazia njia zako.

29 Watu watakaposhushwa, nawe ukasema, ‘Wainue!’

ndipo atamwokoa aliyevunjika moyo.

30 Atamwokoa hata yule ambaye ana hatia,

ataokolewa kwa sababu ya usafi wa mikono yako.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/22-2f1754ba7ee89cebc08299eed153fe31.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 23

Ayubu Anajibu: Kulalamika Kwangu Ni Uchungu

1 Ndipo Ayubu akajibu:

2 “Hata leo malalamiko yangu ni chungu;

mkono wake ni mzito juu yangu hata nikiugua.

3 Laiti ningefahamu mahali pa kumwona;

laiti ningeweza kwenda mahali akaapo!

4 Ningeliweka shauri langu mbele zake,

na kukijaza kinywa changu na hoja.

5 Ningejua kwamba angenijibu nini,

na kuelewa lile ambalo angelisema.

6 Je, angenipinga kwa nguvu nyingi?

La, asingenigandamiza.

7 Hapo mtu mwadilifu angeweka shauri lake mbele zake,

nami ningeokolewa milele na mhukumu wangu.

8 “Lakini nikienda mashariki, hayupo;

nikienda magharibi, simpati.

9 Anapokuwa kazini pande za kaskazini, simwoni;

akigeukia kusini, nako simwoni hata kidogo.

10 Lakini anaijua njia niiendeayo;

akiisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu.

11 Nyayo zangu zimefuata hatua zake kwa karibu;

nimeishika njia yake bila kukengeuka.

12 Sijaziacha amri zilizotoka midomoni mwake;

nimeyathamini maneno ya kinywa chake kuliko chakula changu cha kila siku.

13 “Lakini yeye husimama peke yake; ni nani awezaye kumpinga?

Yeye hufanya lolote atakalo.

14 Hutimiliza maagizo yake dhidi yangu,

na bado anayo mipango mingi kama hiyo ambayo ameiweka akiba.

15 Hiyo ndiyo sababu ninaingiwa na hofu mbele zake;

nifikiriapo haya yote ninamwogopa.

16 Mungu ameufanya moyo wangu kuzimia;

yeye Mwenyezi amenitia hofu.

17 Hata hivyo sijanyamazishwa na giza,

wala kwa giza nene linalofunika uso wangu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/23-141a9b0fd288b09e7b73418d07072958.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 24

Ayubu Analalamikia Jeuri Duniani

1 “Kwa nini Mwenyezi asiweke nyakati kwa ajili ya hukumu?

Kwa nini wale wamjuao wazitafute siku kama hizo bila mafanikio?

2 Watu husogeza mawe ya mpaka;

huchunga makundi ya wanyama waliyonyangʼanya kwa nguvu.

3 Huwanyangʼanya yatima punda wao,

na kumchukua rehani fahali wa mjane.

4 Humsukuma mhitaji kutoka njia,

na kuwafanya maskini wote wa nchi kulazimika kujificha.

5 Kama punda-mwitu jangwani,

maskini huzunguka katika kazi zao za kutafuta chakula;

mahali palipo jangwa

huwapa chakula cha watoto wao.

6 Hukusanya chakula mashambani na kuokota masazo

katika mashamba ya mizabibu ya waovu.

7 Kwa kukosa nguo, usiku kucha hukaa uchi;

hawana chochote cha kujifunika baridi.

8 Hutota kwa mvua za mlimani,

nao huikumbatia miamba kwa ajili ya kukosa pa kujisitiri.

9 Mtoto yatima hupokonywa matitini;

mtoto wachanga wa maskini hunyakuliwa kwa ajili ya deni.

10 Kwa kukosa nguo, hutembea uchi;

hubeba miganda ya ngano, lakini huwa na njaa.

11 Hukamua zeituni katika mawe ya kusagia;

hukanyaga mashinikizo, lakini wanaona kiu.

12 Kilio cha huzuni cha wanaokufa kinapaa kutoka mjini,

nazo nafsi za waliojeruhiwa zinalilia msaada.

Lakini Mungu hamlaumu mtu yeyote

kwa kutenda mabaya.

13 “Wako wale wanaoiasi nuru,

wasiofahamu njia zake

wala hawakai katika mapito yake.

14 Wakati mwanga wa mchana unapotoweka, muuaji huinuka

naye huwaua maskini na mhitaji;

wakati wa usiku hunyemelea kama mwizi.

15 Jicho la mzinzi hungojea wakati wa giza,

naye hufikiri, ‘Hakuna jicho litakaloniona,’

naye huuficha uso wake.

16 Katika giza, huvunja majumba,

lakini wakati wa mchana hujifungia ndani;

hawataki kufanya lolote nuruni.

17 Kwa wote hawa, giza nene ndiyo asubuhi yao;

hujifanya rafiki na vitisho vya gizani.

18 “Lakini wao ni povu juu ya maji;

sehemu yao juu ya nchi imelaaniwa,

hivyo hakuna hata mmoja

aendaye kwenye shamba la mizabibu.

19 Kama vile joto na hari vinyakuavyo theluji iliyoyeyuka,

ndivyo kuzimu kuwanyakuavyo waliotenda dhambi.

20 Tumbo lililowazaa huwasahau,

nao huwa karamu ya mabuu;

watu waovu hawakumbukwi tena,

lakini huvunjika kama mti.

21 Huwafanya mawindo wanawake tasa na wasio na watoto,

nao hawaonyeshi huruma kwa wajane.

22 Lakini Mungu huwakokota wenye nguvu kwa uwezo wake;

ingawa wamestawi, hawana hakika ya maisha.

23 Aweza akawaacha wakapumzika wakijihisi salama,

lakini macho yake yanaona njia zao.

24 Kwa kitambo kidogo hutukuka, hatimaye hutoweka;

hushushwa na kukusanywa kama wengine wote,

hukatwa kama masuke ya nafaka.

25 “Kama hili sivyo, ni nani awezaye kunithibitisha kuwa mwongo,

na kuyafanya maneno yangu kuwa si kitu?”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/24-371672903050fe2165c24e426b3d26df.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 25

Bildadi Anasema: Mwanadamu Awezaje Kuwa Mwadilifu Mbele Za Mungu?

1 Ndipo Bildadi Mshuhi akajibu:

2 “Mamlaka na kuheshimiwa ni vyake Mungu;

yeye huthibitisha amani katika mbingu juu.

3 Je, majeshi yake yaweza kuhesabika?

Ni nani asiyeangaziwa na nuru yake?

4 Mtu awezaje kuwa mwadilifu mbele za Mungu?

Awezaje mtu aliyezaliwa na mwanamke kuwa safi?

5 Ikiwa hata mwezi sio mwangavu

nazo nyota si safi machoni pake,

6 sembuse mtu ambaye ni funza:

mwanadamu ambaye ni buu tu!”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/25-d9dbc23a05f445282c5d246614f53c82.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 26

Ayubu Anajibu: Utukufu Wa Mungu Hauchunguziki

1 Kisha Ayubu akajibu:

2 “Tazama jinsi ulivyomsaidia mtu asiye na uwezo!

Jinsi ulivyouokoa mkono ulio dhaifu!

3 Ni shauri gani ulilompa yeye asiye na hekima?

Nayo ni busara gani kubwa uliyoonyesha!

4 Ni nani aliyekusaidia kutamka maneno hayo?

Nayo ni roho ya nani iliyosema kutoka kinywani mwako?

5 “Wafu wako katika maumivu makuu,

wale walio chini ya maji na wale waishio ndani yake.

6 Mautiiko wazi mbele za Mungu;

Uharibifuhaukufunikwa.

7 Hutandaza anga la kaskazini mahali patupu;

naye huiningʼiniza dunia mahali pasipo na kitu.

8 Huyafungia maji kwenye mawingu yake,

hata hivyo mawingu hayapasuki kwa uzito wake.

9 Huufunika uso wa mwezi mpevu,

akitandaza mawingu juu yake.

10 Amechora mstari wa upeo juu ya uso wa maji,

ameweka mpaka wa nuru na giza.

11 Nguzo za mbingu nazo zatetemeka,

zinatishika anapozikemea.

12 Kwa nguvu zake aliisukasuka bahari;

kwa hekima yake alimkata Rahabuvipande vipande.

13 Aliisafisha anga kwa pumzi yake;

kwa mkono wake alimchoma joka aendaye mbio.

14 Haya ni mambo madogo tu katika matendo yake;

tazama jinsi ulivyo mdogo mnongʼono tunaousikia kumhusu!

Ni nani basi awezaye kuelewa

ngurumo za nguvu zake?”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/26-ed6bf60e96ef1425fcbc6bacd9e922ae.mp3?version_id=1627—