Categories
Ayubu

Ayubu 7

Ayubu: Mateso Yangu Hayana Mwisho

1 “Je, mwanadamu hana kazi ngumu duniani?

Siku zake si kama zile za mtu aliyeajiriwa?

2 Kama mtumwa anavyovionea shauku vivuli vya jioni,

au mtu aliyeajiriwa anavyoungojea mshahara wake,

3 ndivyo nilivyogawiwa miezi ya ubatili,

nami nimeandikiwa huzuni usiku hata usiku.

4 Wakati nilalapo ninawaza, ‘Itachukua muda gani kabla sijaamka?’

Usiku huwa mrefu, nami najigeuzageuza hadi mapambazuko.

5 Mwili wangu umevikwa mabuu na uchafu,

ngozi yangu imetumbuka na kutunga usaha.

Ayubu Anamlilia Mungu

6 “Siku zangu zinapita upesi kuliko mtande wa kufuma,

nazo zinafikia mwisho wake bila matumaini.

7 Kumbuka, Ee Mungu, maisha yangu ni kama pumzi;

macho yangu kamwe hayataona tena raha.

8 Lile jicho linaloniona sasa halitaniona tena;

utanitafuta, wala sitakuwepo.

9 Kama vile wingu liondokavyo na kutoweka,

vivyo hivyo yeye ashukaye kaburiniharudi tena.

10 Kamwe harudi tena nyumbani mwake;

wala mahali pake hapatamjua tena.

11 “Kwa hiyo sitanyamaza;

nitanena kutokana na maumivu makuu ya roho yangu,

nitalalama kwa uchungu wa nafsi yangu.

12 Je, mimi ni bahari, au mnyama mkubwa mno akaaye vilindini,

hata uniweke chini ya ulinzi?

13 Ninapofikiri kwamba kitanda changu kitanifariji,

nacho kiti changu cha fahari kitapunguza malalamiko yangu,

14 ndipo wanitisha kwa ndoto

na kunitia hofu kwa maono,

15 hivyo ninachagua kujinyonga na kufa,

kuliko huu mwili wangu.

16 Ninayachukia maisha yangu; nisingetamani kuendelea kuishi.

Niache; siku zangu ni ubatili.

17 “Mwanadamu ni kitu gani hata umjali kiasi hiki,

kwamba unamtia sana maanani,

18 kwamba unamwangalia kila asubuhi

na kumjaribu kila wakati?

19 Je, hutaacha kamwe kunitazama,

au kuniacha japo kwa kitambo kidogo tu?

20 Ikiwa nimetenda dhambi, nimekufanyia nini,

Ewe mlinzi wa wanadamu?

Kwa nini umeniweka niwe shabaha yako?

Je, nimekuwa mzigo kwako?

21 Kwa nini husamehi makosa yangu

na kuachilia dhambi zangu?

Kwa kuwa hivi karibuni nitalala mavumbini;

nawe utanitafuta, wala sitakuwepo.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/7-b81b95687814edd432a2870bc7b0273f.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 8

Bildadi Anasema: Yampasa Ayubu Atubu

1 Kisha Bildadi Mshuhi akajibu:

2 “Hata lini wewe utasema mambo kama haya?

Maneno yako ni kama upepo mkuu.

3 Je, Mungu hupotosha hukumu?

Je, Mwenyezi hupotosha kile kilicho haki?

4 Watoto wako walipomtenda dhambi,

aliwapa adhabu ya dhambi yao.

5 Lakini ukimtafuta Mungu,

nawe ukamsihi Mwenyezi,

6 ikiwa wewe ni safi na mnyofu,

hata sasa atainuka mwenyewe kwa niaba yako,

na kukurudisha katika mahali pako pa haki.

7 Ijapokuwa mwanzo wako ulikuwa mdogo,

lakini mwisho wako utakuwa wa mafanikio.

8 “Ukaulize vizazi vilivyotangulia

na uone baba zao walijifunza nini,

9 kwa kuwa sisi tumezaliwa jana tu na hatujui lolote,

nazo siku zetu duniani ni kama kivuli tu.

10 Je, hawatakufundisha na kukueleza?

Je, hawataleta maneno kutoka kwenye kufahamu kwao?

11 Je, mafunjo yaweza kumea mahali pasipo na matope?

Matete yaweza kustawi bila maji?

12 Wakati bado yanaendelea kukua kabla ya kukatwa,

hunyauka haraka kuliko majani mengine.

13 Huu ndio mwisho wa watu wote wanaomsahau Mungu;

vivyo hivyo matumaini ya wasiomjali Mungu huangamia.

14 Lile analolitumainia huvunjika upesi;

lile analolitegemea ni utando wa buibui.

15 Huutegemea utando wake, lakini hausimami;

huungʼangʼania, lakini haudumu.

16 Yeye ni kama mti ulionyeshewa vizuri wakati wa jua,

ukieneza machipukizi yake bustanini;

17 huifunganisha mizizi yake kwenye lundo la mawe,

na kutafuta nafasi katikati ya mawe.

18 Unapongʼolewa kutoka mahali pake,

ndipo mahali pale huukana na kusema,

‘Mimi kamwe sikukuona.’

19 Hakika uhai wake hunyauka,

na kutoka udongoni mimea mingine huota.

20 “Hakika Mungu hamkatai mtu asiye na hatia,

wala kuitia nguvu mikono ya mtenda mabaya.

21 Bado atakijaza kinywa chako na kicheko,

na midomo yako na kelele za shangwe.

22 Adui zako watavikwa aibu,

nazo hema za waovu hazitakuwepo tena.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/8-8e5202493c50f57ae42df252e4d54581.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 9

Hakuna Mpatanishi

1 Kisha Ayubu akajibu:

2 “Naam, najua hili ni kweli.

Lakini mwanadamu awezaje kuwa mwadilifu mbele za Mungu?

3 Ingawa mtu angetaka kushindana naye,

asingaliweza kumjibu Mungu hata mara moja miongoni mwa elfu moja.

4 Hekima yake ni kubwa sana na ana uwezo mwingi mno.

Ni nani aliyempinga naye akawa salama?

5 Aiondoa milima bila yenyewe kujua

na kuipindua kwa hasira yake.

6 Aitikisa dunia kutoka mahali pake

na kuzifanya nguzo zake zitetemeke.

7 Husema na jua, nalo likaacha kuangaza;

naye huizima mianga ya nyota.

8 Yeye peke yake huzitandaza mbingu

na kuyakanyaga mawimbi ya bahari.

9 Yeye ndiye Muumba wa nyota za Dubu,na Orioni,

Kilimia,na makundi ya nyota za kusini.

10 Hutenda maajabu yasiyopimika,

miujiza isiyoweza kuhesabiwa.

11 Anapopita karibu nami, siwezi kumwona;

apitapo mbele yangu, simtambui.

12 Anapochukua kwa ghafula, ni nani awezaye kumzuia?

Ni nani awezaye kumwambia, ‘Unafanya nini?’

13 Mungu hataizuia hasira yake;

hata jeshi kubwa la Rahabulenye nguvu

linajikunyata miguuni pake.

14 “Ni vipi basi mimi nitaweza kubishana naye?

Nawezaje kupata maneno ya kuhojiana naye?

15 Ingawa sikuwa na hatia, sikuweza kumjibu;

ningeweza tu kumsihi Mhukumu wangu anihurumie.

16 Hata kama ningemwita kwenye shauri, naye akakubali,

siamini kama angenisikiliza.

17 Yeye angeniangamiza kwa dhoruba

na kuongeza majeraha yangu pasipo na sababu.

18 Asingeniacha nipumue

bali angenifunika kabisa na huzuni kuu.

19 Kama ni suala la nguvu, yeye ni mwenye nguvu!

Kama ni suala la haki, ni nani awezaye kumwita mahakamani?

20 Hata kama sikuwa na hatia, kinywa changu kingenihukumu;

kama sikuwa na kosa, kingenitangaza kuwa mwenye hatia.

21 “Ingawa mimi sina kosa,

haileti tofauti katika nafsi yangu;

nauchukia uhai wangu.

22 Hayo yote ni sawa; ndiyo sababu nasema,

‘Yeye huwaangamiza wasio na makosa pamoja na waovu.’

23 Wakati pigo liletapo kifo cha ghafula,

yeye hudhihaki kule kukata tamaa kwa yule asiye na kosa.

24 Wakati nchi inapoangukia mikononi mwa waovu,

yeye huwafunga macho mahakimu wake.

Kama si yeye, basi ni nani?

25 “Siku zangu zapita mbio kuliko mkimbiaji;

zinapita upesi bila kuona furaha hata kidogo.

26 Zinapita upesi kama mashua ya mafunjo,

mfano wa tai ayashukiaye mawindo kwa ghafula.

27 Kama nikisema, ‘Nitayasahau malalamiko yangu,

nitabadili sura ya uso wangu na kutabasamu,’

28 bado ninahofia mateso yangu yote,

kwa kuwa ninajua hutanihesabu kuwa sina hatia.

29 Kwa kuwa nimeonekana mwenye hatia,

kwa nini basi nitaabishwe bure?

30 Hata kama ningejiosha kwa sabuni

na kutakasa mikono yangu kwa magadi,

31 wewe ungenitupa kwenye shimo la utelezi

kiasi kwamba hata nguo zangu zingenichukia sana.

32 “Yeye si mwanadamu kama mimi ili niweze kumjibu,

ili kwamba tuweze kushindana naye mahakamani.

33 Laiti angelikuwepo mtu wa kutupatanisha kati yetu,

aweke mkono wake juu yetu sote wawili,

34 mtu angeliiondoa fimbo ya Mungu juu yangu,

ili utisho wake usiendelee kunitia hofu.

35 Ndipo ningenena naye, bila kumwogopa,

lakini kama ilivyo kwangu sasa, sitaweza.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/9-13876cc46d0e381c17459d52de98778f.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 10

Ayubu: Nayachukia Maisha Yangu

1 “Nayachukia sana haya maisha yangu;

kwa hiyo nitatoa malalamiko yangu kwa wazi bila kujizuia,

nami nitanena kutokana na uchungu wa moyo wangu.

2 Nitamwambia Mungu: Usinihukumu,

bali niambie una mashtaka gani dhidi yangu.

3 Je, inakupendeza wewe kunionea,

kuikataa kwa dharau kazi ya mikono yako,

huku wewe ukitabasamu juu ya mipango ya waovu?

4 Je, wewe una macho ya kimwili?

Je, wewe huona kama mwanadamu aonavyo?

5 Je, siku zako ni kama zile za mwanadamu,

au miaka yako ni kama ile ya mtu,

6 ili kwamba utafute makosa yangu

na kuichunguza dhambi yangu;

7 ingawa wajua kuwa mimi sina hatia,

na hakuna awezaye kunitoa mkononi mwako?

8 “Mikono yako ndiyo iliyoniumba na kunifanya.

Je, sasa utageuka na kuniangamiza?

9 Kumbuka kuwa ulinifinyanga kama udongo wa mfinyanzi.

Je, sasa utanifanya kuwa mavumbi tena?

10 Je, wewe hukunimimina mimi kama maziwa,

na kunigandisha kama jibini,

11 ukanivika ngozi na nyama,

na kuniunga pamoja kwa mifupa na mishipa?

12 Umenipa uhai na kunitendea wema,

katika uangalizi wako umeilinda roho yangu.

13 “Lakini hili ndilo ulilolificha moyoni mwako,

nami ninajua kuwa hili lilikuwa katika nia yako:

14 Kama nilifanya dhambi, ungekuwa umeniona,

wala usingeacha kosa langu lipite bila kuadhibiwa.

15 Kama nina hatia, ole wangu!

Hata kama ningekuwa sina hatia,

siwezi kukiinua kichwa changu,

kwa kuwa nimejawa na aibu,

na kuzama katika mateso yangu.

16 Kama nikiinua kichwa changu juu, unaninyatia kama simba,

na kuonyesha tena uwezo wa kutisha dhidi yangu.

17 Wewe waleta mashahidi wapya dhidi yangu

na kuzidisha hasira yako juu yangu;

nazo nguvu zako zinanijia wimbi moja baada ya jingine.

18 “Kwa nini basi ulinitoa tumboni?

Ninatamani ningekufa kabla jicho lolote halijaniona.

19 Laiti nisingekuwako kamwe,

au ningekuwa nimechukuliwa moja kwa moja

kutoka tumboni kwenda kaburini!

20 Je, siku zangu chache si zimekaribia kuisha?

Niachie ili niweze kupata muda mfupi wa kufurahi

21 kabla sijaenda mahali ambapo hakuna kurudi tena,

katika nchi ya giza na uvuli wa mauti,

22 nchi ya giza kuu sana,

yenye uvuli wa giza na machafuko,

mahali ambapo hata nuru ni giza.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/10-caa0a02a1bea04be51fd6a62f5adaf51.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 11

Sofari Anasema: Hatia Ya Ayubu Inastahili Adhabu

1 Ndipo Sofari Mnaamathi akajibu:

2 “Je, maneno haya yote yapite bila kujibiwa?

Je, huyu mnenaji athibitishwe kuwa na haki?

3 Je, maneno yako ya upuzi yawafanye watu wanyamaze kimya?

Je, mtu asikukemee unapofanya dhihaka?

4 Unamwambia Mungu, ‘Imani yangu ni kamili

nami ni safi mbele zako.’

5 Aha! Laiti kwamba Mungu angesema,

kwamba angefungua midomo yake dhidi yako,

6 naye akufunulie siri za hekima,

kwa kuwa hekima ya kweli ina pande mbili.

Ujue hili: Mungu amesahau hata baadhi ya dhambi zako.

7 “Je, waweza kujua siri za Mungu?

Je, waweza kuyachunguza mambo yote kumhusu Mwenyezi?

8 Ni juu mno kuliko mbingu: waweza kufanya nini?

Kina chake ni kirefu kuliko kuzimu:

wewe waweza kujua nini?

9 Kipimo chake ni kirefu kuliko dunia,

nacho ni kipana kuliko bahari.

10 “Kama akija na kukufunga gerezani,

na kuitisha mahakama, ni nani awezaye kumpinga?

11 Hakika anawatambua watu wadanganyifu;

naye aonapo uovu, je, haangalii?

12 Mpumbavu aweza kuwa mwenye hekima,

endapo mtoto wa punda-mwitu atazaliwa mwanadamu.

13 “Hata sasa ukiutoa moyo wako kwake

na kumwinulia mikono yako,

14 ukiiondolea mbali ile dhambi iliyo mkononi mwako

wala usiuruhusu uovu ukae hemani mwako,

15 ndipo utainua uso wako bila aibu;

utasimama imara bila hofu.

16 Hakika utaisahau taabu yako,

utaikumbuka tu kama maji yaliyokwisha kupita.

17 Maisha yako yatangʼaa kuliko adhuhuri,

nalo giza litakuwa kama alfajiri.

18 Utakuwa salama, kwa kuwa lipo tumaini;

utatazama pande zote na kupumzika kwa salama.

19 Utalala, wala hakuna atakayekuogofya,

naam, wengi watajipendekeza kwako.

20 Bali macho ya waovu hayataona,

wokovu utawaepuka;

tarajio lao litakuwa ni hangaiko

la mtu anayekata roho.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/11-303367365150fb670b22e76b200c264b.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 12

Ayubu Anajibu: Mimi Ni Mtu Wa Kuchekwa

1 Ndipo Ayubu akajibu:

2 “Bila shaka ninyi ndio watu,

nayo hekima itakoma mtakapokufa!

3 Lakini mimi ninao ufahamu kama ninyi;

mimi si duni kwenu.

Ni nani asiyejua mambo haya yote?

4 “Nimekuwa mtu wa kuchekwa na rafiki zangu,

ingawa nilimwita Mungu naye akanijibu:

mimi ni mtu wa kuchekwa tu,

ingawa ni mwadilifu na nisiye na hatia!

5 Wanadamu wakiwa katika utulivu huwa na dharau kwa wale wenye msiba

kana kwamba ndiyo haki ya wale ambao miguu yao inateleza.

6 Hema za wanyangʼanyi hazisumbuliwi,

wale wanaomghadhibisha Mungu wako salama:

wale wamchukuao mungu wao mikononi mwao.

7 “Lakini ulizeni wanyama, nao watawafundisha,

au ndege wa angani, nao watawaambia;

8 au zungumzeni na dunia, nayo itawafundisha,

au acheni samaki wa baharini wawape taarifa.

9 Ni nani miongoni mwa hawa wote asiyejua

kwamba mkono waBwanandio uliofanya hili?

10 Mkononi mwake kuna uhai wa kila kiumbe,

na pumzi ya wanadamu wote.

11 Je, sikio haliyajaribu maneno

kama vile ulimi uonjavyo chakula?

12 Je, hekima haipatikani katikati ya wazee?

Je, maisha marefu hayaleti ufahamu?

13 “Hekima na nguvu ni vya Mungu;

shauri na ufahamu ni vyake yeye.

14 Kile anachokibomoa hakiwezi kujengeka tena;

mtu aliyefungiwa naye hawezi kufunguliwa.

15 Akizuia maji, huwa pana ukame;

akiyaachia maji, huharibu nchi.

16 Kwake kuna nguvu na ushindi;

adanganywaye na adanganyaye, wote wawili ni wake.

17 Yeye huwaondoa washauri wakiwa wametekwa nyara,

naye huwapumbaza wanaotoa maamuzi.

18 Huondoa pingu zilizofungwa na wafalme,

na kuwafunga mishipi ya kiunoni.

19 Huwaondoa makuhani wakiwa wametekwa nyara,

na kuwaangusha waliojiimarisha muda mrefu.

20 Hunyamazisha midomo ya washauri wanaoaminika,

na kuondoa busara ya wazee.

21 Huwamwagia dharau wanaoheshimika,

na kuwavua silaha wenye nguvu.

22 Hufunua mambo ya ndani ya gizani,

na kuyaleta nuruni yale yaliyositirika sana.

23 Huyafanya mataifa yatukuke na kuyaangamiza;

hufanya mataifa kuwa makubwa, naye huyatawanya.

24 Huwaondolea viongozi wa nchi akili zao;

huwapeleka watangetange nyikani pasipo na njia.

25 Hupapasa gizani pasipokuwa na mwanga;

huwafanya wapepesuke kama walevi.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/12-1a7d2e9f5e33539ac126e3c024589272.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 13

1 “Macho yangu yameona hili lote,

masikio yangu yamesikia na kulielewa.

2 Hayo mnayoyajua mimi pia ninayajua;

mimi si mtu duni kuliko ninyi.

3 Lakini ninayo shauku ya kuzungumza na Mwenyezi

na kuhojiana shauri langu na Mungu.

4 Ninyi, hata hivyo, hunipakaza uongo;

ninyi ni matabibu wasiofaa kitu, ninyi nyote!

5 Laiti wote mngenyamaza kimya!

Kwa kuwa kwenu hilo lingekuwa hekima.

6 Sikieni sasa hoja yangu;

sikilizeni kusihi kwangu.

7 Je, mtazungumza kwa uovu kwa niaba ya Mungu?

Je, mtazungumza kwa udanganyifu kwa niaba yake?

8 Mtamwonyesha upendeleo?

Mtamtetea Mungu kwenye mashtaka yake?

9 Je, ingekuwa vyema Mungu akiwahoji ninyi?

Je, mngeweza kumdanganya kama ambavyo mngeweza kuwadanganya wanadamu?

10 Hakika angewakemea

kama mkiwapendelea watu kwa siri.

11 Je, huo ukuu wake haungewatisha ninyi?

Je, hofu yake isingewaangukia ninyi?

12 Maneno yenu ni mithali za majivu;

utetezi wenu ni ngome za udongo wa mfinyanzi.

13 “Nyamazeni kimya nipate kusema;

kisha na yanipate yatakayonipata.

14 Kwa nini nijiweke mwenyewe kwenye hatari

na kuyaweka maisha yangu mikononi mwangu?

15 Ingawa ataniua, bado nitamtumaini;

hakika nitazitetea njia zangu mbele zake.

16 Naam, hili litanigeukia kuwa wokovu wangu,

kwa maana hakuna mtu asiyemcha Mungu

atakayethubutu kuja mbele yake!

17 Sikilizeni maneno yangu kwa makini;

nayo masikio yenu yaingize kile nisemacho.

18 Sasa kwamba nimekwisha kutayarisha mambo yangu,

ninajua mimi nitahesabiwa kuwa na haki.

19 Je, kuna yeyote anayeweza kuleta mashtaka dhidi yangu?

Kama ndivyo, nitanyamaza kimya na nife.

20 “Ee Mungu, unijalie tu mimi haya mambo mawili,

nami sitajificha uso wako:

21 Ondoa mkono wako uwe mbali nami,

nawe uache kuniogofya kwa hofu zako kuu.

22 Niite kwenye shauri nami nitajibu,

au niache niseme, nawe upate kujibu.

23 Ni makosa na dhambi ngapi nilizotenda?

Nionyeshe kosa langu na dhambi yangu.

24 Kwa nini kuuficha uso wako

na kunihesabu mimi kuwa adui yako?

25 Je, utaliadhibu jani lipeperushwalo na upepo?

Je, utayasaka makapi makavu?

26 Kwa kuwa unaandika mambo machungu dhidi yangu

na kunifanya nizirithi dhambi za ujana wangu.

27 Umeifunga miguu yangu kwenye pingu.

Unazichunga kwa makini njia zangu zote

kwa kutia alama kwenye nyayo za miguu yangu.

28 “Hivyo mwanadamu huangamia kama kitu kilichooza,

kama vazi lililoliwa na nondo.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/13-d28d26816e8ade5518d2bc6f04ca3c2f.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 14

1 “Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke

siku zake ni chache nazo zimejaa taabu.

2 Huchanua kama ua kisha hunyauka;

huwa kama kivuli kipitacho upesi, wala hadumu.

3 Je, unamwekea jicho lako mtu kama huyo?

Je, utamleta mbele yako katika hukumu?

4 Ni nani awezaye kutoa kitu safi kutoka kitu najisi?

Hakuna awezaye!

5 Siku za mwanadamu zimewekewa mpaka;

umekwisha kutangaza idadi ya miezi yake

na kuweka mpaka ambao hawezi kuuvuka.

6 Hivyo angalia mbali umwache,

hadi awe amekamilisha muda wake

kama mtu aliyeajiriwa.

7 “Kwa maana lipo tumaini kwa mti;

kama ukikatwa utachipuka tena,

nayo machipukizi yake mapya hayatakoma.

8 Mizizi yake yaweza kuchakaa ardhini

na kisiki chake kufa udongoni,

9 lakini kwa kupata dalili ya maji utachipua

na kutoa machipukizi kama mche.

10 Lakini mwanadamu hufa, na huo ndio mwisho wake;

hutoa pumzi ya mwisho, naye hayuko tena!

11 Kama vile maji yatowekavyo katika bahari,

au mkondo wa mto ukaushwavyo na kuwa mkavu,

12 ndivyo mwanadamu alalavyo chini asiamke;

hadi mbingu zitakapokuwa hazipo tena,

wanadamu hawataamka au kuamshwa

kutoka kwenye usingizi wao.

13 “Laiti kama ungenificha kaburini,

na kunisitiri hadi hasira yako ipite!

Laiti ungeniwekea wakati,

na kisha ukanikumbuka!

14 Je, kama mtu akifa, aweza kuishi tena?

Siku zote za kazi zangu ngumu

nitangojea kufanywa upya kwangu.

15 Utaniita nami nitakuitika;

utakionea shauku kiumbe ambacho mikono yako ilikiumba.

16 Hakika ndipo utakapozihesabu hatua zangu,

lakini hutazifuatia dhambi zangu.

17 Makosa yangu yatafungiwa kwa lakiri kwenye mfuko,

nawe utazifunika dhambi zangu.

18 “Lakini kama mlima umomonyokavyo na kufikichika

na kama vile mwamba uondolewavyo mahali pake,

19 kama maji yamalizavyo mawe,

na mafuriko yachukuavyo udongo,

ndivyo unavyoharibu tegemeo la mwanadamu.

20 Humshinda mara moja kwa daima, naye hutoweka;

waibadilisha sura yake na kumwondoa.

21 Kama wanawe wakipewa heshima, yeye hafahamu;

kama wakidharauliwa, yeye haoni.

22 Yeye hasikii kingine isipokuwa maumivu ya mwili wake mwenyewe,

naye huomboleza kwa ajili yake mwenyewe.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/14-f497accccff8d70b94db306801bbf2f5.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 15

Elifazi Anaongea: Ayubu Anadhoofisha Imani

1 Kisha Elifazi Mtemani akajibu:

2 “Je, mtu mwenye hekima hujibu kwa mawazo matupu,

au kujaza tumbo lake kwa upepo wenye joto wa mashariki?

3 Je, aweza kubishana juu ya maneno yasiyofaa,

kwa hotuba zisizo na maana?

4 Lakini unadhoofisha hata uchaji wa Mungu

na kuzuia ibada mbele za Mungu.

5 Dhambi yako inasukuma kinywa chako,

nawe umechagua ulimi wa hila.

6 Kinywa chako mwenyewe kinakuhukumu, wala si changu;

midomo yako mwenyewe inashuhudia dhidi yako.

7 “Je, wewe ni mtu wa kwanza kuzaliwa?

Ulizaliwa kabla ya vilima?

8 Je, wewe husikiliza mashauri ya siri ya Mungu?

Je, wewe unaizuia hekima iwe yako mwenyewe?

9 Wewe unajua kitu gani tusichokijua sisi?

Unafahamu kitu gani tusichokifahamu sisi?

10 Wale wenye mvi na wazee wako upande wetu,

watu ambao ni wazee hata kuliko baba yako.

11 Je, faraja za Mungu hazikutoshi,

au maneno yaliyosemwa kwako kwa upole si kitu?

12 Kwa nini moyo wako unakudanganya,

na kwa nini macho yako yanangʼaa,

13 ili kwamba upate kutoa hasira yako dhidi ya Mungu,

na kumwaga maneno kama hayo kutoka kinywani mwako?

14 “Mwanadamu ni kitu gani, hata aweze kuwa safi,

au yeye aliyezaliwa na mwanamke, hata aweze kuwa mwadilifu?

15 Kama Mungu hawaamini watakatifu wake,

kama hata mbingu zenyewe si safi machoni pake,

16 sembuse mwanadamu ambaye ni mwovu na mpotovu,

ambaye hunywa uovu kama anywavyo maji!

17 “Nisikilize mimi nami nitakueleza,

acha nikuambie yale niliyoyaona,

18 ambayo watu wenye hekima wameyanena,

bila kuficha lolote walilopokea toka kwa baba zao

19 (wakati ambao wao peke yao ndio walipewa nchi,

hakuna mgeni aliyepita miongoni mwao):

20 Mtu mwovu siku zake zote hupata mateso,

miaka yote aliwekewa mkorofi.

21 Sauti za kutisha hujaa masikioni mwake;

katika kufanikiwa kwake, wanyangʼanyi humshambulia.

22 Hukata tamaa kuokoka gizani;

amewekwa kwa ajili ya upanga.

23 Hutangatanga, akitafuta chakula;

anajua kwamba siku ya giza iko karibu.

24 Taabu na maumivu makuu vinamtia hofu;

humshinda kama mfalme aliye tayari kwa vita,

25 kwa sababu amemkunjia Mungu ngumi yake

na kujigamba dhidi ya Mwenyezi,

26 kwa kiburi akishambulia dhidi ya Mungu

akiwa na ngao nene, iliyo imara.

27 “Ingawa uso wake umefunikwa na mafuta kwa unene

na kiuno chake kimevimba kwa kunenepa,

28 ataishi katika miji ya magofu,

na katika nyumba ambazo haziishi mwanadamu yeyote,

nyumba zinazokuwa vifusi.

29 Hatatajirika tena, nao utajiri wake hautadumu,

wala mali zake hazitakuwa nyingi juu ya nchi.

30 Hatatoka gizani;

mwali wa moto utanyausha machipukizi yake,

nayo pumzi ya kinywa cha Mungu itamwondolea mbali.

31 Asijidanganye mwenyewe kutumainia ubatili,

kwa kuwa hatapata malipo yoyote.

32 Atakuwa amelipwa kikamilifu kabla ya wakati wake,

nayo matawi yake hayatastawi.

33 Atafanana na mzabibu uliopukutishwa matunda yake kabla hayajaiva,

kama mzeituni unaodondosha maua yake.

34 Kwa kuwa jamii ya wasiomcha Mungu watakuwa tasa,

nao moto utateketeza hema za wale wanaopenda rushwa.

35 Hutunga mimba ya madhara na kuzaa uovu;

matumbo yao huumba udanganyifu.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/15-aef311f80c8e5b773ddf423a5371ae7c.mp3?version_id=1627—

Categories
Ayubu

Ayubu 16

Ayubu Anathibitisha Tena Hali Yake Ya Kutokuwa Na Hatia

1 Kisha Ayubu akajibu:

2 “Nimepata kusikia mambo mengi kama haya,

nanyi nyote ni wafariji wenye kutaabisha!

3 Je, maneno yenu mengi yasiyo na maana hayana mwisho?

Mna nini hata mwendelee kushindana kwa maneno?

4 Mimi pia ningeweza kuzungumza kama ninyi,

kama mngekuwa katika hali yangu;

ningeweza kutoa hotuba nzuri dhidi yenu,

na kuwatikisia ninyi kichwa changu.

5 Lakini kinywa changu kingewatia moyo;

faraja kutoka midomoni mwangu, ingewaletea nafuu.

6 “Lakini kama nikisema, maumivu yangu bado hayatulizwi;

nami kama nikijizuia, wala hayaondoki.

7 Ee Mungu, hakika umenichakaza;

umewaangamiza kabisa watu wa nyumbani mwangu wote.

8 Umenikunjakunja, nalo limekuwa ushahidi;

nako kukonda kwangu kumeongezeka sana na kushuhudia dhidi yangu.

9 Mungu amenishambulia na kunirarua katika hasira yake,

na kunisagia meno yake;

adui yangu hunikazia macho yake makali.

10 Watu wamenifumbulia vinywa vyao kunidhihaki;

hunipiga shavuni mwangu kwa dharau,

na kuungana pamoja dhidi yangu.

11 Mungu amenigeuzia kwa watu wabaya,

na kunitupa katika makucha ya waovu.

12 Mambo yote yalikuwa mazuri, lakini alinivunjavunja;

amenikamata shingo na kuniponda.

Amenifanya mimi kuwa shabaha yake;

13 wapiga upinde wake wananizunguka.

Bila huruma, huchoma figo zangu,

na kuimwaga nyongo yangu juu ya nchi.

14 Huniponda tena na tena;

hunishambulia kama shujaa wa vita.

15 “Nimejishonea nguo ya gunia juu ya mwili wangu

nami nimekizika kipaji cha uso wangu kwenye vumbi.

16 Uso wangu umekuwa mwekundu kwa kulia,

macho yangu yamepigwa na giza kuu.

17 Hata hivyo mikono yangu haijafanya jeuri,

na maombi yangu ni safi.

18 “Ee nchi, usiifunike damu yangu,

nacho kilio changu kisinyamazishwe kamwe.

19 Hata sasa shahidi wangu yuko mbinguni;

wakili wangu yuko juu.

20 Mwombezi wangu ni rafiki yangu

macho yangu yamwagapo machozi kwa Mungu;

21 kwa niaba ya mtu anamsihi Mungu

kama mtu anavyosihi kwa ajili ya rafiki yake.

22 “Ni miaka michache tu itapita

kabla sijaenda safari ambayo sitarudi.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JOB/16-7cf39d0e2a2171affc3179a7712bb812.mp3?version_id=1627—