Categories
Nehemia

Nehemia 12

Makuhani Na Walawi Waliorudi Na Zerubabeli

1 Hawa wafuatao walikuwa makuhani na Walawi ambao walirudi na Zerubabeli mwana wa Shealtieli pamoja na Yeshua:

Seraya, Yeremia, Ezra,

2 Amaria, Maluki, Hatushi,

3 Shekania, Rehumu, Meremothi,

4 Ido, Ginethoni, Abiya,

5 Miyamini, Moadia, Bilga,

6 Shemaya, Yoyaribu, Yedaya,

7 Salu, Amoki, Hilkia na Yedaya.

Hawa walikuwa viongozi wa makuhani na wenzao wakati wa Yeshua.

8 Walawi walikuwa Yeshua, Binui, Kadmieli, Sherebia, Yuda, na pia Matania, ambaye pamoja na wenzake, alikuwa kiongozi wa nyimbo za shukrani.

9 Bakbukia na Uni, wenzao, walisimama mkabala nao wakati wa ibada.

10 Yeshua alikuwa baba wa Yoyakimu, Yoyakimu alikuwa baba wa Eliashibu, Eliashibu alikuwa baba wa Yoyada,

11 Yoyada alikuwa baba wa Yonathani, na Yonathani alikuwa baba wa Yadua.

12 Katika siku za Yoyakimu, kulikuwa na wakuu wa jamaa za kikuhani:

wa jamaa ya Seraya, Meraya;

wa jamaa ya Yeremia, Hanania;

13 wa jamaa ya Ezra, Meshulamu;

wa jamaa ya Amaria, Yehohanani;

14 wa jamaa ya Maluki, Yonathani;

wa jamaa ya Shebania, Yosefu;

15 wa jamaa ya Harimu, Adna;

wa jamaa ya Meremothi, Helkai;

16 wa jamaa ya Ido, Zekaria;

wa jamaa ya Ginethoni, Meshulamu;

17 wa jamaa ya Abiya, Zikri;

wa jamaa ya Miniamini na ya Maazia, Piltai;

18 wa jamaa ya Bilgai, Shamua;

wa jamaa ya Shemaya, Yehonathani;

19 wa jamaa ya Yoyaribu, Matenai;

wa jamaa ya Yedaya, Uzi;

20 wa jamaa ya Salu, Kalai;

wa jamaa ya Amoki, Eberi;

21 wa jamaa ya Hilkia, Hashabia;

wa jamaa ya Yedaya, Nethaneli.

22 Wakuu wa jamaa za Walawi katika siku za Eliashibu, Yoyada, Yohanani na Yadua, pia wale jamaa za makuhani, waliandikishwa wakati wa utawala wa Dario, Mwajemi.

23 Wakuu wa jamaa miongoni mwa wazao wa Lawi hadi wakati wa Yohanani mwana wa Eliashibu waliandikishwa katika kitabu cha kumbukumbu.

24 Viongozi wa Walawi walikuwa: Hashabia, Sherebia, Yeshua mwana wa Kadmieli na wenzao, waliosimama mkabala nao kusifu na kushukuru, sehemu moja ikipokezana na nyingine kama ilivyoagizwa na Daudi mtu wa Mungu.

25 Mabawabu waliokuwa wakilinda kwenye malango ya ghala ni: Matania, Bakbukia, Obadia, Meshulamu, Talmoni na Akubu.

26 Walihudumu siku za Yoyakimu mwana wa Yeshua, mwana wa Yosadaki, na katika siku za mtawala Nehemia, na za Ezra kuhani na mwandishi.

Kuwekwa Wakfu Ukuta Wa Yerusalemu

27 Wakati wa kuwekwa wakfu ukuta wa Yerusalemu, Walawi walitafutwa kule walikokuwa wakiishi, nao wakaletwa Yerusalemu kuadhimisha kwa shangwe huko kuweka wakfu kwa nyimbo za shukrani na kwa uimbaji wakitumia matoazi, vinubi na zeze.

28 Pia waimbaji walikusanywa pamoja kutoka maeneo yaliyozunguka Yerusalemu, kutoka vijiji vya Wanetofathi,

29 kutoka Beth-Gilgali, na kutoka eneo la Geba na Azmawethi, kwa kuwa waimbaji walikuwa wamejijengea vijiji kuzunguka Yerusalemu.

30 Wakati makuhani na Walawi walipokuwa wamekwisha kujitakasa kwa kufuatana na desturi, waliwatakasa watu, malango na ukuta.

31 Niliwaagiza viongozi wa Yuda wapande juu ya ukuta. Pia niliagiza makundi mawili makubwa ya waimbaji waimbe nyimbo za kumshukuru Mungu. Kundi moja lilipanda juu ya ukuta upande wa kuume, kuelekea Lango la Samadi.

32 Hoshaya na nusu ya viongozi wa Yuda wakawafuata,

33 pamoja na Azaria, Ezra, Meshulamu,

34 Yuda, Benyamini, Shemaya, Yeremia,

35 pamoja na baadhi ya makuhani wenye tarumbeta, na pia walikuwa na Zekaria mwana wa Yonathani, mwana wa Shemaya, mwana wa Matania, mwana wa Mikaya, mwana wa Zakuri, mwana wa Asafu,

36 pamoja na wenzake, Shemaya, Azareli, Milalai, Gilalai, Maai, Nethaneli, Yuda na Hanani, wakiwa na vyombo vya uimbaji, kama ilivyoagizwa na Daudi mtu wa Mungu. Mwandishi Ezra aliongoza maandamano.

37 Kwenye Lango la Chemchemi waliendelea moja kwa moja mpaka kwenye ngazi za Mji wa Daudi, kwenye mwinuko wa ukuta, na kupitia juu ya nyumba ya Daudi mpaka kwenye Lango la Maji upande wa mashariki.

38 Kundi la pili la waimbaji lilielekea upande wa kushoto. Niliwafuata juu ya ukuta, pamoja na nusu ya watu kupitia Mnara wa Tanuru mpaka kwenye Ukuta Mpana,

39 juu ya Lango la Efraimu, Lango la Yeshana, Lango la Samaki, Mnara wa Hananeli, na Mnara wa Mia, mpaka kwenye Lango la Kondoo. Walipofika kwenye Lango la Ulinzi wakasimama.

40 Kisha yale makundi mawili ya waimbaji yaliyoshukuru yakachukua nafasi zao katika nyumba ya Mungu. Nami pia nikafanya hivyo, pamoja na nusu ya maafisa,

41 na makuhani wafuatao: Eliakimu, Maaseya, Miniamini, Mikaya, Elioenai, Zekaria na Hanania wakiwa na tarumbeta zao,

42 na pia Maaseya, Shemaya, Eleazari, Uzi, Yehohanani, Malkiya, Elamu na Ezeri. Makundi haya yaliimba chini ya uongozi wa Yezrahia.

43 Siku hiyo watu walitoa dhabihu nyingi, wakishangilia kwa sababu Mungu aliwapa furaha kuu. Wanawake na watoto walishangilia pia. Sauti ya kushangilia huko Yerusalemu iliweza kusikika mbali sana.

44 Wakati huo watu walichaguliwa kuwa wasimamizi wa vyumba vya ghala kwa ajili ya matoleo, malimbuko na zaka. Kutoka kwenye yale mashamba yaliyozunguka miji walipaswa walete kwenye ghala mafungu kama sheria ilivyoamuru kwa ajili ya makuhani na Walawi, kwa kuwa Yuda alifurahishwa na huduma ya makuhani na Walawi.

45 Walifanya ibada ya Mungu wao na ibada ya utakaso, nao waimbaji na walinzi wa lango wakafanya hivyo pia, kufuatana na amri za Daudi na Solomoni mwanawe.

46 Muda mrefu uliopita, katika siku za Daudi na Asafu, walikuwepo viongozi wa waimbaji na wa nyimbo za sifa na za kumshukuru Mungu.

47 Kwa hiyo katika siku za Zerubabeli na za Nehemia, Israeli wote walitoa mafungu kila siku kwa ajili ya waimbaji na mabawabu. Pia walitenga fungu kwa ajili ya Walawi wengine, nao Walawi walitenga fungu kwa ajili ya wazao wa Aroni.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/NEH/12-66d363585c6d3fe335271bf2ee34be25.mp3?version_id=1627—

Categories
Nehemia

Nehemia 13

Nehemia Afanya Matengenezo Ya Mwisho

1 Siku hiyo, Kitabu cha Mose kilisomwa kwa sauti kuu, na watu wote wakasikia. Humo ilionekana imeandikwa kwamba hakuna Mwamoni wala Mmoabu atakayeruhusiwa katika kusanyiko la watu wa Mungu,

2 kwa sababu hawakuwalaki Waisraeli kwa chakula na maji. Badala yake walimwajiri Balaamu kuwalaani (lakini hata hivyo Mungu wetu aligeuza laana kuwa baraka).

3 Watu waliposikia sheria hii, waliwatenga watu wote wasio Waisraeli waliokuwa wa uzao wa kigeni.

4 Kabla ya hili, kuhani Eliashibu alikuwa amewekwa kuwa msimamizi wa vyumba vya ghala ya nyumba ya Mungu wetu. Alikuwa na uhusiano wa karibu na Tobia,

5 naye alikuwa amempa Tobia chumba kikubwa ambacho mwanzo kilikuwa kikitumika kuweka sadaka za nafaka, uvumba na vyombo vya Hekalu, pamoja na zaka za nafaka, divai mpya na mafuta waliyoagizwa Waisraeli kwa ajili ya Walawi, waimbaji na mabawabu wa lango, pamoja na matoleo kwa makuhani.

6 Lakini wakati haya yote yalipokuwa yakitendeka, sikuwa Yerusalemu, kwa kuwa katika mwaka wa thelathini na mbili wa utawala wa Artashasta mfalme wa Babeli nilikuwa nimerudi kwa mfalme. Baadaye nilimwomba ruhusa,

7 nikarudi Yerusalemu. Hapo niligundua jambo la uovu alilofanya Eliashibu kwa kumpa Tobia chumba katika nyua za nyumba ya Mungu.

8 Nilikasirika sana na nikavitupa nje vyombo vyote vya Tobia.

9 Nilitoa amri kutakasa vyumba, kisha nikavirudisha vifaa vya nyumba ya Mungu, pamoja na sadaka za nafaka na uvumba.

10 Pia niligundua kuwa mafungu yaliyopangwa kupewa Walawi hawakuwa wamepewa, nao Walawi wote na waimbaji waliowajibika kwa huduma walikuwa wamerudi katika mashamba yao.

11 Basi niliwakemea maafisa na kuwauliza, “Kwa nini nyumba ya Mungu imepuuzwa?” Kisha niliwaita pamoja na kuwaweka kwenye nafasi zao.

12 Yuda wote walileta zaka za nafaka, divai mpya na mafuta kwenye ghala.

13 Nikamweka kuhani Shelemia, mwandishi Sadoki, na Mlawi aliyeitwa Pedaya kuwa wasimamizi wa ghala, na kumfanya Hanani mwana wa Zakuri, mwana wa Matania kuwa msaidizi wao, kwa sababu watu hawa walionekana kuwa waaminifu. Walipewa wajibu wa kugawa mahitaji kwa ndugu zao.

14 Ee Mungu wangu, unikumbuke kwa hili, wala usifute kile nilichokifanya kwa uaminifu kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu na kwa ajili ya huduma yake.

15 Siku hizo nikaona watu katika Yuda wakikanyaga mashinikizo ya divai siku ya Sabato na kuleta nafaka wakiwapakiza punda, pamoja na divai, zabibu, tini na aina nyingine za mizigo. Nao walikuwa wakileta haya yote Yerusalemu siku ya Sabato. Kwa hiyo niliwaonya dhidi ya kuuza vyakula siku hiyo.

16 Watu kutoka Tiro waliokuwa wakiishi Yerusalemu walileta samaki na aina nyingi za bidhaa na kuziuza Yerusalemu siku ya Sabato kwa watu wa Yuda.

17 Niliwakemea wakuu wa Yuda na kuwaambia, “Ni uovu gani huu mnaofanya wa kuinajisi siku ya Sabato?

18 Je, baba zenu hawakufanya mambo kama haya, hata wakamsababisha Mungu wetu kuleta maafa haya yote juu yetu na juu ya mji huu? Sasa bado mnazidi kuchochea ghadhabu yake dhidi ya Israeli kwa kuinajisi Sabato.”

19 Wakati vivuli vya jioni vilipoangukia juu ya malango ya Yerusalemu kabla ya Sabato, niliamuru milango ifungwe, wala isifunguliwe mpaka Sabato iishe. Nikawaweka baadhi ya watu wangu mwenyewe kwenye malango ili pasiwepo mzigo utakaoingizwa ndani siku ya Sabato.

20 Mara moja au mbili wachuuzi na wauzaji wa bidhaa za aina zote walilala usiku nje ya mji wa Yerusalemu.

21 Lakini niliwaonya na kuwaambia, “Kwa nini mnalala karibu na ukuta? Kama mkifanya hivi tena, nitawaadhibu.” Kuanzia wakati ule hawakuja tena siku ya Sabato.

22 Kisha nikawaamuru Walawi kujitakasa na kwenda kulinda malango ili kutunza Sabato iwe takatifu.

Ee Mungu wangu, unikumbuke kwa ajili ya hili pia, nawe unionyeshe wema wako sawasawa na upendo wako mkuu.

23 Zaidi ya hayo, niliona Wayahudi waliokuwa wameoa wanawake kutoka Ashdodi, Amoni na Moabu.

24 Nusu ya watoto wao walizungumza lugha ya Kiashidodi au lugha ya watu wengine, bali hawakuweza kuzungumza Kiyahudi.

25 Niliwakemea na kuwalaani. Niliwapiga baadhi ya watu na kungʼoa nywele zao. Niliwaapisha kwa jina la Mungu na kusema: “Msiwaoze binti zenu kwa wana wao, wala binti zao wasiolewe na wana wenu wala ninyi wenyewe.

26 Je, Solomoni hakutenda dhambi kwa sababu ya wanawake wa namna hiyo? Miongoni mwa mataifa mengi hapakuwepo mfalme kama yeye. Alipendwa na Mungu wake. Naye Mungu alimweka kuwa mfalme juu ya Israeli yote, lakini hata yeye, wanawake wa mataifa mengine walimfanya atende dhambi.

27 Je, tulazimike sasa kusikia kwamba ninyi pia mmefanya uovu huu mkubwa na kutokuwa waaminifu kwa Mungu wetu kwa kuoa wanawake wa kigeni?”

28 Mmoja wa wana wa Yoyada mwana wa Eliashibu kuhani mkuu alikuwa mkwewe Sanbalati Mhoroni. Nami nilimfukuza mbele yangu.

29 Ee Mungu wangu, uwakumbuke, kwa sababu wamenajisi ukuhani, na agano la kikuhani na la Walawi.

30 Kwa hiyo niliwatakasa makuhani na Walawi kutokana na chochote kilichokuwa cha kigeni, na kuwapa wajibu, kila mmoja katika kazi yake.

31 Pia nilihakikisha kwamba matoleo ya kuni yaliletwa kwa wakati unaopaswa, na malimbuko kwa wakati wake.

Ee Mungu wangu, unikumbuke, unitendee mema.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/NEH/13-64e882dd6740d1962afcb87f89876d45.mp3?version_id=1627—

Categories
Esta

Esta Utangulizi

Utangulizi

Kitabu hiki kinachukua jina la mhusika wake mkuu, Esta. Jina hili limetokana na neno la Kiajemi ambalo maana yake ni “Nyota.” Jina la Esta la Kiebrania ni “Hadassah,” maana yake “Mhadasi” ambayo ni aina ya miti iliyokuwa inastawi milimani karibu na Yerusalemu, na ilikuwa inatumika kujengea vibanda wakati wa Sikukuu ya Vibanda. Kitabu hiki kinaelezea kisa cha msichana mzuri wa Kiyahudi ambaye Mfalme Ahasuero wa Kwanza alimchagua awe malkia wake.

Matukio yaliyowapata Wayahudi yanayoelezewa kwenye kitabu hiki yalitukia huko Shushani, uliokuwa mji mkuu wa Uajemi wakati wa Mfalme Ahasuero, aliyetawala Uajemi kuanzia 486–465 K.K. Kule kuokolewa kwa Wayahudi kwa ajabu wakati wa Mfalme Ahasuero baadaye kuliadhimishwa kila mwaka kama Sikukuu ya Puri; wakati huu, kitabu cha Esta husomwa hadharani.

Mwandishi

Ingawa mwandishi hajulikani kwa wazi, inawezekana akawa Mordekai. Wengine hudhani ni Ezra au Nehemia kwa sababu ya mtindo wa kuandika.

Kusudi

Kuonyesha ukuu wa Mungu, na upendo wake kwa watu wake.

Mahali

Katika jumba la kifalme huko Shushani, mji mkuu wa Uajemi.

Tarehe

Kinadhaniwa kuandikwa mwaka wa 470 K.K.

Wahusika Wakuu

Esta, Mordekai, Mfalme Ahasuero, na Hamani.

Wazo Kuu

Mungu aliwaokoa Wayahudi katika maangamizi yaliyopangwa na Hamani. Mungu aligeuza mabaya yaliyokusudiwa dhidi ya Wayahudi yakawapata adui zao katika utawala wote wa Mfalme Ahasuero, baada ya Esta na watu wake kumwomba Mungu.

Mambo Muhimu

Esta kuchaguliwa kuwa malkia badala ya Vashti aliyekuwa malkia mbele yake, na vile Mungu alivyobadilisha makusudi ya Hamani dhidi ya Wayahudi.

Mgawanyo

Esta afanywa malkia (

1:1–2:23

)

Hila ya Hamani kuwaangamiza Wayahudi (

3:1–5:14

)

Ushindi wa Wayahudi (

6:1–10:3

).

Categories
Esta

Esta 1

Malkia Vashti Aondolewa

1 Hili ndilo lililotokea wakati wa utawala wa Mfalme Ahasuero, yule aliyetawala juu ya majimbo mia na ishirini na saba tangu Bara Hindi hadi Kushi.

2 Wakati huo Mfalme Ahasuero alitawala katika kiti chake cha enzi katika ngome ya mji wa Shushani.

3 Katika mwaka wa tatu wa utawala wake, alifanya karamu kwa ajili ya wakuu wake wote pamoja na maafisa. Akawaalika viongozi wa jeshi wa Uajemi na Umedi, wana wa wafalme na wakuu wa majimbo.

4 Kwa siku zote 180 mfalme alionyesha utajiri mwingi wa ufalme wake, fahari na utukufu wa enzi yake.

5 Siku hizo zilipopita, mfalme alifanya karamu kwa muda wa siku saba, katika bustani ya ndani katika jumba la kifalme, kwa ajili ya watu wote kuanzia mdogo hadi mkubwa, waliokuwa katika ngome ya mji wa Shushani.

6 Bustani ilikuwa na mapazia ya kitani nyeupe na buluu, yaliyofungiwa kamba za kitani nyeupe na kitambaa cha zambarau, kwenye pete za fedha juu ya nguzo za marmar. Kulikuwepo viti vya dhahabu na vya fedha vilivyokuwa vimewekwa kwenye ile sakafu iliyotengenezwa kwa mawe ya rangi, marmar, lulumizi na mawe mengine ya thamani.

7 Vyombo vya dhahabu vilitumika kwa watu kunywea mvinyo, kila kimoja tofauti na kingine, naye mfalme akatoa mvinyo kwa wingi kwa kadiri ya ukarimu wake.

8 Kwa amri ya mfalme kila mgeni aliruhusiwa kunywa alichotaka, kwa kuwa mfalme alitoa maagizo kwa watumishi wote wa kuhudumu mvinyo kumhudumia kila mtu kwa jinsi alivyotaka.

9 Malkia Vashti pia akawafanyia wanawake karamu katika jumba la kifalme la Mfalme Ahasuero.

10 Siku ya saba, wakati Mfalme Ahasuero alikuwa amesisimka roho yake kwa mvinyo, aliamuru matowashi saba waliokuwa wakimhudumia, yaani, Mehumani, Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari na Karkasi,

11 kumleta Malkia Vashti mbele ya mfalme akiwa amevaa taji lake la kifalme, ili aonyeshe uzuri wake kwa watu na wakuu, kwa kuwa alikuwa ni mzuri wa kupendeza.

12 Lakini wakati watumishi walipotoa amri ya mfalme, Malkia Vashti alikataa kuja. Ndipo mfalme alighadhibika, na hasira yake ikawaka.

13 Kwa kuwa ilikuwa desturi ya mfalme kupata ushauri kwa wataalamu katika mambo ya sheria na haki, alizungumza na watu wenye busara, ambao walijua nyakati,

14 nao waliokuwa karibu na mfalme ni Karshena, Shethari, Admatha, Tarshishi, Meresi, Marsena na Memukani, wakuu saba wa Uajemi na Umedi waliokuwa na nafasi ya pekee kwa mfalme nao walikuwa na vyeo vya juu kabisa katika utawala wake.

15 Mfalme akauliza, “Kulingana na sheria, Malkia Vashti anapaswa kutendewa nini? Malkia hakutii amri ya Mfalme Ahasuero ambayo matowashi walimpelekea.”

16 Kisha Memukani akajibu mbele ya mfalme na wakuu, “Malkia Vashti si kwamba amemkosea mfalme tu bali pia amewakosea wakuu wote na watu wa himaya yote ya Mfalme Ahasuero.

17 Kwa maana tendo hili la malkia litajulikana kwa wanawake wote, kwa hiyo watawadharau waume zao na kusema, ‘Mfalme Ahasuero aliagiza Malkia Vashti aletwe mbele yake, lakini alikataa.’

18 Leo hii wanawake wa wakuu wa Uajemi na Umedi ambao wamesikia juu ya tabia ya malkia watawatendea wakuu wote wa mfalme vivyo hivyo. Hapatakuwepo na mwisho wa dharau na magomvi.

19 “Kwa hiyo, kama itampendeza mfalme, atoe amri ya kifalme na iandikwe katika sheria ya Uajemi na Umedi, ambayo haitabadilika, kwamba Vashti kamwe asije tena mbele ya Mfalme Ahasuero. Pia mfalme na atoe hiyo nafasi yake ya umalkia kwa mwanamke mwingine aliye bora kumliko yeye.

20 Kisha mbiu hii ya mfalme itakapotangazwa katika himaya yake iliyo kubwa sana, wanawake wote watawaheshimu waume zao, kuanzia mdogo hadi mkubwa.”

21 Mfalme na wakuu wake walipendezwa na shauri hili, hivyo basi mfalme akafanya kama Memukani alivyopendekeza.

22 Alipeleka barua katika sehemu zote za ufalme wake, kwa kila jimbo kwa maandishi yake mwenyewe na kwa kila watu katika lugha yao wenyewe, akitangaza kwa msemo wa kila watu kwamba inampasa kila mwanaume kuwa mtawala wa nyumba yake mwenyewe.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/EST/1-0266356e88d9c1ec20e94ae51896bee8.mp3?version_id=1627—

Categories
Esta

Esta 2

Esta Afanywa Malkia

1 Baadaye, wakati hasira ya Mfalme Ahasuero ilikuwa imetulia, alimkumbuka Vashti na kile alichokuwa amekifanya na alilokuwa ameamuru juu yake.

2 Kisha watumishi waliomhudumia mfalme walipendekeza, “Na ufanyike utafiti kwa ajili ya wanawali mabikira wazuri wa sura kwa ajili ya mfalme.

3 Mfalme na ateue maafisa katika kila jimbo la himaya yake kuwaleta hao wanawali wote wazuri wa sura katika nyumba ya wanawake katika ngome ya mji wa Shushani. Kisha wawekwe chini ya utunzaji wa Hegai, towashi wa mfalme, msimamizi wa wanawake; na wapewe matunzo yote ya urembo.

4 Kisha yule ambaye atampendeza mfalme na awe malkia badala ya Vashti.” Shauri hili likampendeza mfalme, naye akalifuata.

5 Basi katika mji wa ngome ya Shushani palikuwa na Myahudi wa kabila ya Benyamini, jina lake Mordekai mwana wa Yairi, mwana wa Shimei, mwana wa Kishi,

6 ambao walichukuliwa uhamishoni kutoka Yerusalemu na Mfalme Nebukadneza wa Babeli, wakiwa miongoni mwa waliochukuliwa mateka pamoja na Mfalme Yekonia wa Yuda.

7 Mordekai alikuwa na binamu yake msichana aliyeitwa Hadasa, ambaye alimlea kwa kuwa hakuwa na baba wala mama. Msichana huyu, ambaye pia alijulikana kwa jina la Esta, alikuwa na umbo na sura ya kupendeza, naye Mordekai alimtunza kama binti yake mwenyewe baada ya baba yake na mama yake kufariki.

8 Wakati agizo na amri ya mfalme lilitangazwa, wanawali wengi waliletwa kwenye ngome ya mji wa Shushani na kuwekwa chini ya uangalizi wa Hegai. Pia Esta alipelekwa katika jumba la mfalme na akakabidhiwa Hegai, aliyekuwa mkuu wa nyumba ya wanawake.

9 Msichana huyu alimpendeza na kupata kibali mbele zake. Mara moja akaanza kumpa matunzo ya uzuri na chakula maalum. Alimpa Esta vijakazi saba waliochaguliwa kutoka jumba la kifalme, na kumhamishia yeye pamoja na vijakazi wake katika sehemu bora zaidi katika nyumba ya wanawake.

10 Esta alikuwa hajadhihirisha uraia wala kabila lake, kwa sababu Mordekai alikuwa amemkataza.

11 Kila siku Mordekai alikuwa akitembeatembea karibu na ua wa nyumba ya wanawake kujua Esta alivyoendelea na kuona yaliyokuwa yakitendeka kwake.

12 Kabla zamu ya msichana haijafika ya kwenda kwa Mfalme Ahasuero, ilimbidi atimize miezi kumi na miwili ya matunzo ya urembo kama ilivyokuwa imepangwa. Kwa miezi sita walikuwa wajipake mafuta ya manemane, na miezi sita kujipaka manukato na vipodozi.

13 Basi hivi ndivyo ambavyo msichana angeingia kwa mfalme: Kila kitu alichohitaji aliruhusiwa kuchukua kutoka nyumba ya wanawake na kwenda navyo katika jumba la mfalme.

14 Jioni angekwenda pale na asubuhi kurudi sehemu nyingine ya nyumba ya wanawake katika utunzaji wa Shaashgazi, towashi wa mfalme ambaye alikuwa mkuu wa masuria. Hangeweza kurudi kwa mfalme mpaka apendezwe naye na kuagiza aitwe kwa jina lake.

15 Zamu ya Esta ilipofika kwenda kwa mfalme (msichana ambaye Mordekai alikuwa amemlea, binti wa Abihaili mjomba wake), Esta hakutaka vitu zaidi ya vile ambavyo Hegai, towashi wa mfalme aliyekuwa mkuu wa nyumba ya wanawake alivyokuwa amemshauri. Naye Esta alipata kibali kwa kila mtu aliyemwona.

16 Esta alipelekwa kwa Mfalme Ahasuero katika makao ya mfalme mwezi wa kumi, yaani mwezi wa Tebethi, katika mwaka wake wa saba wa kutawala.

17 Basi ikawa mfalme alivutiwa na Esta kuliko wanawake wengine wote, naye akapata upendeleo na kibali kuliko mabikira wengine. Kisha akamvika taji la kifalme kichwani mwake na kumfanya malkia badala ya Vashti.

18 Mfalme akafanya karamu kubwa, karamu ya Esta, kwa wakuu wake wote na maafisa. Mfalme alitangaza mapumziko katika majimbo yake yote na kugawa zawadi kwa ukarimu wa kifalme.

Mordekai Afunua Hila

19 Wakati mabikira walikusanyika mara ya pili, Mordekai alikuwa ameketi katika lango la mfalme.

20 Lakini Esta alikuwa ameficha siri ya kabila lake na uraia wake, kama Mordekai alivyokuwa amemwambia, kwa maana aliendelea kufuata maelekezo ya Mordekai kama alivyokuwa akifanya alipokuwa akimlea.

21 Wakati Mordekai alikuwa ameketi kwenye lango la mfalme, Bigthana na Tereshi, maafisa wawili wa mfalme waliokuwa walinzi wa lango, walikasirika na kupanga njama ya kumuua Mfalme Ahasuero.

22 Lakini Mordekai aligundua hila hii na kumwambia Malkia Esta, ambaye baadaye alimwarifu mfalme, huku akimsifu Mordekai.

23 Taarifa hiyo ilipochunguzwa na kuonekana kuwa kweli, maafisa hao wawili waliangikwa juu ya miti ya kunyongea. Haya yote yaliandikwa katika kitabu cha kumbukumbu mbele ya mfalme.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/EST/2-a8dec7e2535eab1bd32f41a689873e2d.mp3?version_id=1627—

Categories
Esta

Esta 3

Hila Ya Hamani Kuwaangamiza Wayahudi

1 Baada ya matukio haya, Mfalme Ahasuero alimheshimu Hamani mwana wa Hamedatha, Mwagagi, akampandisha na kumpa kiti chake cha heshima cha juu sana kuliko wakuu wengine wote.

2 Maafisa wote wa mfalme waliokaa langoni mwa mfalme walipiga magoti na kumpa Hamani heshima, kwa kuwa mfalme alikuwa ameamuru hili kuhusu Hamani. Lakini Mordekai hakumpigia magoti wala kumheshimu.

3 Kisha maafisa wa mfalme waliokuwa langoni mwa mfalme walimuuliza Mordekai, “Kwa nini hutii agizo la mfalme?”

4 Siku baada ya siku walizungumza naye lakini hakukubali. Kwa hiyo walimweleza Hamani kuona kama tabia ya Mordekai itaweza kuvumiliwa, kwa maana alikuwa amewaambia kuwa yeye ni Myahudi.

5 Wakati Hamani alipoona kuwa Mordekai hampigii magoti wala kumpa heshima alighadhibika.

6 Hata hivyo baada ya kujulishwa watu wa Mordekai ni akina nani, alibadili wazo la kumuua Mordekai peke yake. Badala yake Hamani alitafuta njia ya kuwaangamiza watu wote wa Mordekai, yaani, Wayahudi, walio katika ufalme wote wa Ahasuero.

7 Katika mwaka wa kumi na mbili wa utawala wa Mfalme Ahasuero, katika mwezi wa kwanza uitwao Nisani, walipiga puri (yaani kura) mbele ya Hamani ili kuchagua siku na mwezi. Kura ikaangukia kwenye mwezi wa kumi na mbili, yaani Adari.

8 Kisha Hamani akamwambia Mfalme Ahasuero, “Wako watu fulani wameenea na kutawanyika miongoni mwa watu katika majimbo yote ya ufalme wako, ambao desturi zao ni tofauti na zile za watu wengine wote, nao hawatii sheria za mfalme. Haifai mfalme kuwavumilia watu hawa.

9 Kama inampendeza mfalme, itolewe amri kuwaangamiza, nami nitaweka talanta 10,000za fedha katika hazina ya mfalme kwa ajili ya watu watakaoshughulikia jambo hili.”

10 Basi mfalme alichukua pete yake ya muhuri kutoka kwenye kidole chake na kumpa Hamani mwana wa Hamedatha, Mwagagi, adui wa Wayahudi.

11 Mfalme akamwambia Hamani, “Baki na fedha yako na uwatendee hao watu utakavyo.”

12 Kisha siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kwanza waandishi wa mfalme waliitwa. Wakaandika barua kwa kila jimbo na katika kila lugha ya watu kama agizo la Hamani lilivyotoka kwa mfalme, kwa watawala wa majimbo mbalimbali, na wakuu wa watu mbalimbali. Hizi ziliandikwa kwa jina la Mfalme Ahasuero mwenyewe na kutiwa muhuri wa pete yake mwenyewe.

13 Barua zilipelekwa na tarishi katika majimbo yote ya mfalme zikiwa na amri ya kuharibu, kuua na kuangamiza Wayahudi wote, wadogo kwa wakubwa, wanawake na watoto wadogo, siku moja, yaani siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari, na pia kuteka nyara vitu vyao.

14 Nakala ya andiko la amri ilipaswa kutolewa kama sheria katika kila jimbo, na kufahamishwa kwa watu wa kila taifa ili waweze kuwa tayari kwa siku ile.

15 Kwa kuharakishwa na amri ya mfalme, matarishi walikwenda na andiko lilitolewa katika mji wa ngome ya Shushani. Mfalme na Hamani waliketi na kunywa, lakini mji wa Shushani ulifadhaika.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/EST/3-23ed20a0f6d821ef9f1d8123c27b17f1.mp3?version_id=1627—

Categories
Esta

Esta 4

Mordekai Amshawishi Esta Kusaidia

1 Mordekai alipojua yote yaliyokwisha kufanyika, alirarua mavazi yake na kuvaa nguo za magunia na kujipaka majivu, akaenda mjini, akiomboleza kwa sauti na kwa uchungu.

2 Alikwenda akasimama nje ya lango la mfalme, kwa sababu hakuna yeyote aliyeruhusiwa kuingia akiwa amevaa nguo za magunia.

3 Katika kila jimbo ambapo amri na agizo la mfalme lilifika, kulikuwa na maombolezo makuu miongoni mwa Wayahudi pamoja na kufunga, kulia na kuomboleza. Watu wengi wakalala juu ya nguo za magunia na majivu.

4 Wajakazi wa Esta na matowashi walipokuja na kumwambia kuhusu Mordekai, alipatwa na huzuni kuu. Alimtumia nguo avae badala ya nguo za magunia, lakini Mordekai hakuzikubali.

5 Ndipo Esta akamwita Hathaki, mmojawapo wa matowashi wa mfalme ambaye alikuwa amewekwa kumhudumia Esta, akamwagiza kutafuta ni nini kilikuwa kikimtaabisha Mordekai na ni kwa nini.

6 Basi Hathaki alitoka nje kumwendea Mordekai kwenye uwanja ulio wazi wa mji mbele ya lango la mfalme.

7 Mordekai akamwambia kila kitu ambacho kimempata, pamoja na hesabu kamili ya fedha ambazo Hamani aliahidi kulipa katika hazina ya mfalme kwa ajili ya maangamizi ya Wayahudi.

8 Akampa nakala ya andiko la amri kwa ajili ya maangamizi yao, lililokuwa limechapishwa huko Shushani, kumwonyesha Esta na kumwelezea. Mordekai akamwambia towashi amshawishi Esta kwenda mbele ya mfalme kuomba rehema na kumsihi kwa ajili ya watu wake.

9 Hathaki akarudi kwa Esta na kumwarifu alilolisema Mordekai.

10 Kisha Esta akamwamuru Hathaki amweleze Mordekai,

11 “Maafisa wote wa mfalme na watu wa majimbo ya ufalme wanajua kuwa mwanaume au mwanamke yeyote ambaye ataingia kumwona mfalme katika ua wa ndani bila kuitwa, mfalme ana sheria moja tu: Atauawa. Njia pekee kinyume na hili ni mfalme kumnyooshea fimbo ya dhahabu ili aishi. Lakini siku thelathini zimepita tangu nilipoitwa kwenda kwa mfalme.”

12 Wakati Mordekai aliarifiwa maneno ya Esta,

13 Mordekai alirudisha jibu hili: “Usifikiri kwamba kwa sababu uko katika nyumba ya mfalme wewe pekee katika Wayahudi wote utapona.

14 Kwa kuwa kama utakaa kimya wakati huu, msaada na ukombozi kwa Wayahudi utatoka mahali pengine, lakini wewe na jamaa ya baba yako mtaangamia. Nani ajuaye kwamba hukuja kwenye nafasi ya mamlaka kwa ajili ya wakati kama huu?”

15 Kisha Esta alituma jibu hili kwa Mordekai:

16 “Nenda, kusanya pamoja Wayahudi wote walioko Shushani, nanyi mfunge kwa ajili yangu. Msile wala kunywa kwa siku tatu, usiku na mchana. Mimi na wajakazi wangu tutafunga kama mnavyofanya. Baada ya kufanyika hili, nitakwenda kwa mfalme, hata ingawa ni kinyume cha sheria. Ikiwa ni kuangamia na niangamie.”

17 Kwa hiyo Mordekai alikwenda zake na kutekeleza maagizo yote ya Esta.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/EST/4-07010ffad0a1842a0d8892c2aa42319d.mp3?version_id=1627—

Categories
Esta

Esta 5

Ombi La Esta Kwa Mfalme

1 Siku ya tatu, Esta alivaa mavazi yake ya kimalkia, naye akasimama katika ua wa ndani wa jumba la mfalme, mbele ya ukumbi wa mfalme. Naye mfalme alikuwa akiketi katika kiti chake cha kifalme katika ukumbi, akielekea langoni.

2 Alipomwona Malkia Esta amesimama uani alipendezwa naye, akamnyooshea fimbo ya utawala ya dhahabu ile iliyokuwa mkononi mwake. Kwa hiyo Esta alikaribia na kuigusa ncha ya fimbo ya mfalme.

3 Kisha mfalme aliuliza, “Malkia Esta, ni nini? Ombi lako ni nini? Hata kama ni nusu ya ufalme, utapewa.”

4 Esta akajibu, “Kama itampendeza mfalme, mfalme pamoja na Hamani waje leo katika karamu ambayo nimeiandaa kwa ajili yake.”

5 Mfalme akasema, “Mleteni Hamani mara moja, ili tupate kufanya lile Esta analoomba.”

Kwa hiyo mfalme na Hamani walihudhuria karamu aliyoiandaa Esta.

6 Walipokuwa wakinywa mvinyo mfalme akamuuliza Esta tena, “Sasa haja yako ni nini? Utapewa. Ombi lako ni nini? Hata nusu ya ufalme, utapewa.”

7 Esta akajibu, “Haja yangu na ombi langu ni hili:

8 Kama mfalme ameona vyema, nami nimepata kibali kwake na kama ikimpendeza mfalme kunipa ombi langu na kunitimizia haja yangu, mfalme na Hamani waje kwangu kesho katika karamu nitakayowaandalia. Kisha nitajibu swali la mfalme.”

Ghadhabu Ya Hamani Dhidi Ya Mordekai

9 Hamani alitoka siku hiyo kwa furaha na moyo mchangamfu. Lakini alipomwona Mordekai langoni mwa mfalme na kuona kwamba hakusimama wala hakuonyesha hofu mbele yake, alijawa na ghadhabu dhidi ya Mordekai.

10 Hata hivyo, Hamani alijizuia akaenda zake nyumbani.

Akawaita pamoja rafiki zake na Zereshi, mkewe.

11 Hamani akajisifia kwao juu ya utajiri wake mwingi, wanawe wengi na kwa njia zote ambazo mfalme amemheshimu kwazo na jinsi alivyomweka juu ya wakuu na maafisa wengine.

12 Hamani akaongeza, “Si hayo tu. Mimi ndiye mtu pekee ambaye Malkia Esta amemwalika kumsindikiza mfalme kwenye karamu aliyomwandalia. Naye amenialika pamoja na mfalme kesho.

13 Lakini haya yote hayanipi kuridhika iwapo ninaendelea kumwona yule Myahudi Mordekai akiketi kwenye lango la mfalme.”

14 Zereshi mkewe na rafiki zake wote wakamwambia, “Tengeneza mahali pa kuangika watu kimo chake dhiraa hamsini,kisha kesho asubuhi mwombe mfalme Mordekai aangikwe juu yake. Ndipo uende na mfalme kwenye karamu kwa furaha.” Shauri hili lilimpendeza Hamani, naye akajenga mahali pa kuangika watu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/EST/5-f5c94411dad1d569eb16740f3abff92c.mp3?version_id=1627—

Categories
Esta

Esta 6

Mordekai Anapewa Heshima

1 Usiku ule mfalme hakupata usingizi, hivyo akaagiza aletewe kitabu cha kumbukumbu za matukio ya utawala wake, asomewe.

2 Kitabu hicho kilikutwa na kumbukumbu kwamba Mordekai alikuwa amefichua jinsi Bigthana na Tereshi, waliokuwa maafisa wawili wa mfalme, walinzi wa lango walivyokuwa wamepanga hila ya kumuua Mfalme Ahasuero.

3 Mfalme akauliza, “Je, ni heshima na shukrani gani Mordekai alipokea kwa ajili ya jambo hili?”

Watumishi wake wakajibu, “Hakuna lolote alilofanyiwa.”

4 Mfalme akasema, “Ni nani yuko uani?” Wakati huo huo Hamani alikuwa ameingia ua wa nje wa jumba la mfalme kusema na mfalme kuhusu kumwangika Mordekai katika mahali pa kuangikia watu alipokuwa amepajenga kwa ajili yake.

5 Watumishi wake wakamjibu, “Hamani amesimama uani.”

Mfalme akaamuru, “Mleteni ndani.”

6 Hamani alipoingia, mfalme alimuuliza, “Afanyiwe nini mtu ambaye mfalme apenda kumheshimu?”

Basi Hamani akawaza moyoni mwake, “Ni nani mwingine ambaye mfalme angemheshimu kuliko mimi?”

7 Kwa hiyo akamjibu mfalme, “Kwa mtu ambaye mfalme apenda kumheshimu,

8 aletewe joho la kifalme ambalo mfalme ameshalivaa na farasi ambaye mfalme alishampanda, ambaye amevikwa taji ya kifalme kichwani mwake.

9 Kisha joho na farasi vikabidhiwe kwa mmojawapo wa wakuu wa mfalme anayeheshimika sana. Nao wamvike mtu yule ambaye mfalme anapenda kumheshimu, na aongozwe akiwa juu ya farasi kupitia barabara za mji, wakitangaza mbele yake, ‘Hivi ndivyo anavyofanyiwa mtu ambaye mfalme apenda kumheshimu!’ ”

10 Mfalme akamwamuru Hamani, “Nenda mara moja, chukua joho na farasi na ufanye kama vile ulivyopendekeza kwa Mordekai Myahudi, akaaye langoni mwa mfalme. Usipuuze kufanya kitu chochote ulichoshauri.”

11 Hivyo Hamani akachukua joho na farasi.

Akamvika Mordekai, na kumpandisha juu ya farasi akamtembeza katika barabara za mji akitangaza mbele yake, “Hivi ndivyo anavyofanyiwa mtu ambaye mfalme anapenda kumheshimu!”

12 Baadaye Mordekai akarudi kwenye lango la mfalme. Lakini Hamani akakimbia nyumbani, akiwa amejaa huzuni,

13 naye akamweleza Zereshi mkewe pamoja na rafiki zake wote kila kitu ambacho kimempata.

Washauri wake pamoja na Zereshi mkewe wakamwambia, “Kwa kuwa Mordekai, ambaye mbele yake umeanza kuanguka ni wa asili ya Kiyahudi, huwezi kushindana naye; kwa hakika utaanguka!”

14 Walipokuwa bado wakizungumza naye, matowashi wa mfalme wakaja na kumharakisha Hamani aende katika karamu aliyoiandaa Esta.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/EST/6-79038e557bb764dad115669cd9945cfe.mp3?version_id=1627—

Categories
Esta

Esta 7

Hamani Aangikwa

1 Basi mfalme na Hamani wakaenda kula chakula pamoja na Malkia Esta.

2 Walipokuwa wakinywa mvinyo katika siku ya pili, mfalme akauliza tena, “Malkia Esta, ni nini haja yako? Utapewa. Ombi lako ni nini? Hata nusu ya ufalme, utapewa.”

3 Kisha Malkia Esta akajibu, “Kama nimepata kibali kwako, ee mfalme, tena kama inapendeza utukufu wako, nijalie maisha yangu, hii ndiyo haja yangu. Pia uokoe watu wangu, hili ndilo ombi langu.

4 Kwa kuwa mimi na watu wangu tumeuzwa kwa kuangamizwa, kuchinjwa na kuharibiwa. Kama tungalikuwa tumeuzwa tu kuwa watumwa wa kiume na wa kike, ningalinyamaza kimya, kwa sababu shida kama hii isingalitosha kumsumbua mfalme.”

5 Mfalme Ahasuero akamuuliza Malkia Esta, “Ni nani huyu? Yuko wapi mtu huyu aliyethubutu kufanya jambo kama hili?”

6 Esta akasema, “Mtesi na adui ni huyu mwovu Hamani.”

Hamani alifadhaika mbele ya mfalme na malkia.

7 Mfalme akainuka kwa ghadhabu, akaacha mvinyo wake, akaenda kwenye bustani ya jumba la kifalme. Lakini Hamani, akitambua kwamba mfalme ameshaamua hatima yake, alibaki nyuma kumsihi Malkia Esta aokoe maisha yake.

8 Mara mfalme aliporudi kutoka bustani ya jumba la kifalme na kuja kwenye ukumbi wa karamu, Hamani alikuwa akijitupa juu ya kiti mahali ambapo Esta alikuwa akiegemea.

Mfalme akasema kwa nguvu, “Je, atamdhalilisha malkia hata huku nyumbani akiwa pamoja nami!”

Mara neno lilipotoka kinywani mwa mfalme, walifunika uso wa Hamani.

9 Kisha Harbona, mmoja wa matowashi wanaomtumikia mfalme, akasema, “Mahali pa kuangika watu penye urefu wa mita ishirini na mbili pako nyumbani mwa Hamani. Alikuwa amepatengeneza kwa ajili ya Mordekai, ambaye alizungumza ili kumsaidia mfalme.”

Mfalme akasema, “Mwangikeni juu yake!”

10 Kwa hiyo wakamtundika Hamani mahali alipokuwa ameandaa kwa ajili ya Mordekai. Ndipo ghadhabu ya mfalme ikatulia.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/EST/7-b23ad2022149248e69d083e0c9e94d4c.mp3?version_id=1627—