Categories
1 Samweli

1 Samweli 26

Daudi Amwacha Sauli Hai Tena

1 Hao Wazifu wakamwendea Sauli huko Gibea na kusema, “Je, Daudi hakujificha katika kilima cha Hakila, kinachotazamana na Yeshimoni?”

2 Hivyo Sauli akashuka kwenda katika Jangwa la Zifu, akiwa na watu wake 3,000 wa Israeli waliochaguliwa, kumsaka Daudi huko.

3 Sauli akapiga kambi yake kando ya barabara juu ya kilima cha Hakila kinachotazamana na Yeshimoni, lakini Daudi alikuwa anaishi huko jangwani. Alipoona kuwa Sauli amemfuata huko,

4 Daudi akatuma wapelelezi na akapata habari kwa hakika kwamba Sauli alikuwa amewasili.

5 Ndipo Daudi akaondoka, akaenda hadi mahali Sauli alikuwa amepiga kambi. Akaona mahali Sauli na Abneri mwana wa Neri, jemadari wa jeshi, walipokuwa wamelala. Sauli alikuwa amelala ndani ya kambi, jeshi likiwa limemzunguka.

6 Basi Daudi akamuuliza Ahimeleki Mhiti, na Abishai mwana wa Seruya, nduguye Yoabu, akisema, “Ni nani atakayeshuka pamoja nami kambini kwa Sauli?”

Abishai akajibu, “Nitakwenda pamoja nawe.”

7 Hivyo Daudi na Abishai wakaenda kwenye jeshi wakati wa usiku, tazama Sauli, alikuwa amelala ndani ya kambi na mkuki wake umekitwa ardhini karibu na kichwa chake. Abneri na askari walikuwa wamelala kumzunguka Sauli.

8 Abishai akamwambia Daudi, “Leo Mungu amemtia adui yako mikononi mwako. Sasa niruhusu nimchome mpaka ardhini kwa pigo moja la mkuki wangu; sitamchoma mara mbili.”

9 Lakini Daudi akamwambia Abishai, “Usimwangamize! Ni nani awezaye kutia mkono juu ya mpakwa mafuta waBwanana asiwe na hatia?”

10 Daudi akasema, “Hakika kama vileBwanaaishivyo,Bwanamwenyewe atampiga; au wakati wake utafika, naye atakufa, au atakwenda vitani na kuangamia.

11 Lakini Mungu na apishie mbali nisije nikainua mkono juu ya mpakwa mafuta waBwana. Sasa chukua huo mkuki na hilo gudulia la maji vilivyo karibu na kichwa chake, tuondoke.”

12 Hivyo Daudi akachukua huo mkuki na hilo gudulia la maji vilivyokuwa karibu na kichwa cha Sauli, nao wakaondoka. Hakuna yeyote aliyeona au kufahamu habari hii, wala hakuna hata mmoja aliyeamka usingizini. Wote walikuwa wamelala, kwa sababuBwanaalikuwa amewatia kwenye usingizi mzito.

13 Kisha Daudi akavuka upande mwingine na kusimama juu ya kilima mahali palipokuwa na nafasi pana kati yao.

14 Daudi akalipigia kelele jeshi na Abneri mwana wa Neri, akisema, “Je, Abneri, hutanijibu?”

Abneri akajibu, “Nani wewe umwitaye mfalme?”

15 Daudi akasema, “Wewe si ni mtu shujaa? Ni nani aliye kama wewe katika Israeli? Kwa nini basi hukumlinda mfalme bwana wako? Mtu mmoja alikuja kumwangamiza mfalme, bwana wako.

16 Ulichokifanya si kizuri. Kwa hakika kama aishivyoBwana, wewe na watu wako mnastahili kufa, kwa sababu hamkumlinda bwana wenu, mpakwa mafuta waBwana. Tazameni hapo mlipo. Uko wapi mkuki wa mfalme na gudulia la maji ambavyo vilikuwa karibu na kichwa chake?”

17 Sauli akatambua sauti ya Daudi, na kusema, “Je, hiyo ni sauti yako, Daudi mwanangu?”

Daudi akajibu, “Naam, hiyo ndiyo, bwana wangu mfalme.”

18 Pia akaongeza, “Kwa nini bwana wangu anamfuatia mtumishi wake? Nimefanya nini, nalo kosa langu ni lipi nililolifanya niwe na hatia?

19 Sasa mfalme bwana wangu na asikilize maneno ya mtumishi wake. KamaBwanaamekuchochea dhidi yangu, basi yeye na aipokee sadaka yangu. Lakini hata hivyo, kama ni wanadamu waliofanya hivyo, walaaniwe mbele zaBwana! Wao sasa wamenifukuza kutoka sehemu yangu katika urithi waBwanawangu wakisema, ‘Nenda ukatumikie miungu mingine.’

20 Basi usiache damu yangu imwagike kwenye ardhi mbali na uso waBwana. Mfalme wa Israeli ametoka kutafuta kiroboto, kama vile mtu awindavyo kware katika milima.”

21 Ndipo Sauli akasema, “Nimetenda dhambi. Rudi, Daudi mwanangu. Kwa kuwa uliyahesabu maisha yangu kuwa ya thamani leo, sitajaribu kukudhuru tena. Hakika nimetenda kama mpumbavu na nimekosa sana.”

22 Daudi akajibu, “Mkuki wa mfalme uko hapa. Mmoja wa vijana wako na avuke kuuchukua.

23 Bwanahumlipa kila mtu kwa ajili ya haki yake na uaminifu wake.Bwanaalikutia katika mikono yangu leo, lakini sikuinua mkono wangu juu ya mpakwa mafuta waBwana.

24 Kwa hakika kama vile maisha yako yalivyokuwa ya thamani kwangu leo, vivyo hivyo maisha yangu na yawe na thamani kwaBwanana kuniokoa kutoka taabu zote.”

25 Ndipo Sauli akamwambia Daudi, “Mwanangu Daudi na ubarikiwe; utafanya mambo makubwa na hakika utashinda.”

Basi Daudi akaenda zake, naye Sauli akarudi nyumbani.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1SA/26-eb462046df9e3585198e172d8c7da599.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Samweli

1 Samweli 27

Daudi Miongoni Mwa Wafilisti

1 Daudi akasema moyoni mwake, “Katika mojawapo ya siku hizi nitaangamizwa kwa mkono wa Sauli. Jambo lililo bora ni kutorokea kwenye nchi ya Wafilisti. Hivyo Sauli atakata tamaa ya kunisaka popote katika Israeli, nami nitakuwa nimeponyoka mkononi mwake.”

2 Hivyo Daudi akaondoka na hao watu mia sita waliokuwa pamoja naye na kwenda kwa Akishi mwana wa Maoki mfalme wa Gathi.

3 Daudi na watu wake wakakaa huko Gathi pamoja na Akishi. Kila mtu alikuwa pamoja na jamaa yake, naye Daudi pamoja na wakeze wawili: yaani Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili wa Karmeli, mjane wa Nabali.

4 Sauli alipokuwa ameambiwa kwamba Daudi alikuwa amekimbilia Gathi, hakuendelea kumsaka tena.

5 Ndipo Daudi akamwambia Akishi, “Kama nimepata kibali machoni pako, unipe sehemu katika mojawapo ya miji katika nchi nikae huko. Kwa nini mtumwa wako akae pamoja nawe katika mji huu wa kifalme?”

6 Hivyo siku hiyo Akishi akampa Daudi mji wa Siklagi, nao Siklagi umekuwa mali ya wafalme wa Yuda tangu wakati huo.

7 Daudi akaishi katika nchi ya Wafilisti muda wa mwaka mmoja na miezi minne.

8 Basi Daudi na watu wake wakapanda na kuwashambulia Wageshuri, Wagirizi na Waamaleki. (Tangu zamani haya mataifa yalikuwa yameishi kwenye eneo lililotanda kuanzia Telemu katika njia iteremkayo Shuri hadi kufikia nchi ya Misri.)

9 Kila mara Daudi aliposhambulia eneo, hakubakiza hai mwanaume wala mwanamke, lakini alichukua kondoo na ngʼombe, punda na ngamia, na nguo. Kisha akarudi kwa Akishi.

10 Akishi alipomuuliza, “Je leo umeshambulia wapi?” Daudi humjibu, “Dhidi ya Negebu ya Yuda,” au wakati mwingine husema, “Dhidi ya Negebu ya Yerameeli,” au “Dhidi ya Negebu ya Wakeni.”

11 Daudi hakumwacha hai mwanaume au mwanamke ili apate kuletwa Gathi, kwa maana Daudi aliwaza, “Wanaweza kujulisha habari zetu na kusema, ‘Hivi ndivyo alivyofanya Daudi.’ ” Hii ndiyo ilikuwa desturi yake wakati wote aliishi katika nchi ya Wafilisti.

12 Akishi akamsadiki Daudi na kuwaza moyoni mwake, akasema, “Daudi amekuwa kitu cha kuchukiza kabisa kwa watu wake, Waisraeli, hivi kwamba atakuwa mtumishi wangu milele.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1SA/27-c627582a08a713ed23c056833ef9350f.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Samweli

1 Samweli 28

Sauli Na Mchawi Wa Endori

1 Siku zile Wafilisti wakakusanya majeshi yao ili kupigana vita dhidi ya Israeli. Akishi akamwambia Daudi, “Lazima ujue kuwa wewe pamoja na watu wako mtafuatana nami kwenda vitani.”

2 Daudi akasema, “Ndipo wewe mwenyewe utakapojionea jambo ambalo mtumishi wako anaweza kufanya.”

Akishi akamjibu Daudi, “Vyema sana, mimi nitakufanya uwe mlinzi wangu daima.”

3 Wakati huo Samweli alikuwa amekufa, nao Israeli wote walikuwa wamemwombolezea na kumzika kwenye mji wake mwenyewe huko Rama. Sauli alikuwa amewafukuza waaguzi na wachawi.

4 Wafilisti wakakusanyika na kupiga kambi yao huko Shunemu, naye Sauli akawakusanya Waisraeli wote na kupiga kambi yao huko Gilboa.

5 Sauli alipoona jeshi la Wafilisti, akaogopa; moyo wake ukajawa na hofu kuu.

6 Ndipo Sauli akauliza ushauri kwaBwana, lakiniBwanahakumjibu kwa ndoto, wala kwa Urimu,wala kwa njia ya manabii.

7 Basi Sauli akawaambia watumishi wake, “Nitafutieni mwanamke mwaguzi ili nimwendee, nipate kuuliza kwake.”

Watumishi wake wakamwambia, “Yuko mwanamke mmoja huko Endori.”

8 Hivyo Sauli akajigeuza kwa kuvaa mavazi mengine, naye usiku akiwa amefuatana na watu wawili wakaenda kwa huyo mwanamke. Akamwambia, “Nibashirie kwa uaguzi, unipandishie yule nitakayekutajia.”

9 Huyo mwanamke akamwambia, “Wewe unajua lile alilofanya Mfalme Sauli. Amewakatilia mbali waaguzi, wapiga ramli wote na wachawi katika nchi. Mbona umenitegea maisha yangu ili wapate kuniua?”

10 Sauli akamwapia huyo mwanamke kwa Jina laBwana, akasema, “Kwa hakika kamaBwanaaishivyo, hutaadhibiwa kwa ajili ya jambo hili.”

11 Ndipo yule mwanamke akauliza, “Je unataka nikupandishie nani?”

Sauli akasema, “Nipandishie Samweli.”

12 Yule mwanamke alipomwona Samweli, alipiga yowe kwa sauti kuu, naye akamuuliza Sauli, “Mbona umenidanganya? Wewe ndiwe Sauli.”

13 Mfalme akamwambia, “Usiogope. Unaona nini?”

Yule mwanamke akasema, “Naona mungu unapanda kutoka ardhini.”

14 Sauli akamuuliza, “Ni mfano wa nini?”

Yule mwanamke akasema, “Ni mwanaume mzee amevaa joho anayepanda.”

Ndipo Sauli akatambua kwamba ni Samweli. Sauli akasujudu kifudifudi, uso wake hadi ardhini.

15 Samweli akamuuliza Sauli, “Kwa nini unanitaabisha kwa kunipandisha juu?”

Sauli akasema, “Mimi ninasumbuka sana, kwa maana Wafilisti wanapigana vita dhidi yangu, naye Mungu ameniacha. Hanijibu tena wala kwa njia ya manabii wala kwa ndoto. Kwa hiyo nimekuita wewe ili unijulishe la kufanya.”

16 Samweli akamuuliza, “Kwa nini uniulize mimi, maadamuBwanaamekuacha na kuwa adui yako?

17 Bwanaametenda lile alilotangulia kusema kupitia kwangu.Bwanaameurarua ufalme kutoka mikononi mwako, naye amempa mmoja wa jirani zako, yaani Daudi.

18 Kwa sababu wewe hukumtiiBwana, wala hukumtimizia ghadhabu yake kali juu ya Waamaleki,Bwanaamekutendea mambo haya leo.

19 Zaidi ya hayo,Bwanaatawatia Israeli pamoja na wewe mikononi mwa Wafilisti, na kesho wewe na wanao mtakuwa pamoja nami.Bwanapia atalitia jeshi la Israeli mikononi mwa Wafilisti.”

20 Papo hapo Sauli akaanguka chini, akajinyoosha, akiwa amejawa na hofu kwa ajili ya maneno ya Samweli. Nguvu zake zikamwishia kwa maana alikuwa hajala chochote mchana ule wote na usiku.

21 Yule mwanamke alipomwendea Sauli na kumwona amepatwa na hofu, akamwambia, “Tazama, mimi mtumishi wako mwanamke nimekutii. Nimeweka maisha yangu hatarini kwa kufanya kile ulichoniagiza nifanye.

22 Sasa tafadhali isikilize sauti ya mtumishi wako, uniruhusu nikupatie chakula kidogo ule ili uwe na nguvu za kurejea ulikotoka.”

23 Akakataa, akisema, “Mimi sitaki kula.”

Lakini watumishi wake wakaungana na yule mwanamke wakamsihi ale, naye akakubali. Basi akainuka hapo chini, akaketi juu ya kitanda.

24 Yule mwanamke alikuwa na ndama aliyenona hapo nyumbani, akamchinja mara moja. Akachukua unga, akaukanda, akatengeneza mkate usio chachu.

25 Ndipo akamwandalia meza Sauli pamoja na watu wake, nao wakala. Usiku ule ule wakainuka na kwenda zao.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1SA/28-2b4949d038560d053f5f1ceaaa05e94b.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Samweli

1 Samweli 29

Akishi Amrudisha Daudi Huko Siklagi

1 Wafilisti wakakusanya majeshi yao yote huko Afeki, nao Waisraeli wakapiga kambi karibu na chemchemi iliyoko Yezreeli.

2 Watawala wa Wafilisti walipokuwa wakipita pamoja na vikosi vyao vya mamia na vya maelfu, Daudi na watu wake walikuwa wakitembea huko nyuma pamoja na Akishi.

3 Majemadari wa Wafilisti wakauliza, “Vipi kuhusu hawa Waebrania?”

Akishi akajibu, “Huyu si Daudi, aliyekuwa afisa wa Sauli mfalme wa Israeli? Ameshakuwa pamoja nami kwa zaidi ya mwaka, naye tangu alipomwacha Sauli hadi sasa, sikuona kosa lolote kwake.”

4 Lakini majemadari wa Wafilisti wakamkasirikia na kusema, “Mrudishe mtu huyu, apate kurudi mahali pale ulipompangia. Haimpasi kufuatana pamoja nasi vitani, asije akageuka, akawa kinyume chetu vitani. Ni kwa njia ipi bora zaidi angeweza kujipatia tena kibali kwa bwana wake, isipokuwa kwa vichwa vya watu wetu wenyewe?

5 Je, huyu si ndiye Daudi walioimba kumhusu katika ngoma zao, wakisema:

“ ‘Sauli amewaua elfu zake,

naye Daudi makumi elfu yake’?”

6 Basi Akishi akamwita Daudi na kumwambia, “Kama vileBwanaaishivyo, wewe umekuwa mtu mwaminifu, nami ningependa utumike pamoja nami katika jeshi. Tangu siku ile uliyofika kwangu hadi sasa, sijaona kosa lolote kwako, lakini hao watawala hawakukubali.

7 Rudi na uende kwa amani; usifanye chochote cha kuwakasirisha watawala wa Kifilisti.”

8 Daudi akamuuliza Akishi, “Lakini mimi nimefanya nini? Je, umeona nini kibaya juu ya mtumishi wako tangu siku ile niliyokuja kwako hadi leo? Kwa nini nisirudi na kupigana na adui za bwana wangu mfalme?”

9 Akishi akamjibu Daudi, “Mimi ninajua ya kuwa wewe umekuwa wa kupendeza machoni pangu kama vile malaika wa Mungu. Lakini hao majemadari wa Wafilisti wamesema, ‘Huyu haimpasi kwenda vitani pamoja nasi.’

10 Sasa amka mapema, pamoja na watumishi wa bwana wako waliofuatana nawe, nanyi ondokeni asubuhi mara kutakapopambazuka.”

11 Hivyo Daudi na watu wake wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda zao kurudi katika nchi ya Wafilisti, nao Wafilisti wakapanda kwenda Yezreeli.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1SA/29-dfc7a89459f785f2bd397fd9fea38ec9.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Samweli

1 Samweli 30

Daudi Aangamiza Waamaleki

1 Daudi na watu wake wakafika Siklagi siku ya tatu. Basi Waamaleki walikuwa wamevamia Negebu na Siklagi. Wakawa wameshambulia mji wa Siklagi na kuuteketeza kwa moto,

2 nao wakawa wamewachukua mateka wanawake pamoja na wote waliokuwamo humo, vijana na wazee. Hawakuua yeyote, bali waliwachukua wakaenda zao.

3 Daudi na watu wake walipofika Siklagi, wakakuta mji umeangamizwa kwa moto na wake zao pamoja na wana wao na binti zao wamechukuliwa mateka.

4 Hivyo Daudi na watu wake wakapiga yowe mpaka wakaishiwa na nguvu za kulia.

5 Wake wawili wa Daudi walikuwa wametekwa: yaani Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili, mjane wa Nabali wa Karmeli.

6 Daudi alihuzunika sana kwa sababu watu walikuwa wakisemezana juu ya kumpiga kwa mawe. Kila mmoja alikuwa na uchungu rohoni kwa sababu ya wanawe na binti zake. Lakini Daudi akajitia nguvu katikaBwana, Mungu wake.

7 Kisha Daudi akamwambia kuhani Abiathari mwana wa Ahimeleki, “Niletee kisibau.” Abiathari akamletea,

8 naye Daudi akamuulizaBwana, “Je, nifuatie kundi hili la wavamizi? Je, nitawapata?”

Bwanaakajibu, “Wafuatie. Hakika utawapata na utafanikiwa kuwaokoa.”

9 Daudi pamoja na watu wake 600 wakafika kwenye Bonde la Besori, mahali ambapo wengine waliachwa nyuma,

10 kwa kuwa watu 200 walikuwa wamechoka sana kuweza kuvuka hilo bonde. Lakini Daudi pamoja na watu 400 wakaendelea kufuatia.

11 Wakamkuta Mmisri katika shamba fulani, nao wakamleta kwa Daudi. Wakampa huyo Mmisri maji ya kunywa na chakula;

12 kipande cha andazi la tini na andazi la zabibu zilizokaushwa. Akala naye akapata nguvu, kwa kuwa hakuwa amekula chakula chochote wala kunywa maji kwa siku tatu usiku na mchana.

13 Daudi akamuuliza, “Wewe ni wa nani, na umetoka wapi?”

Akajibu, “Mimi ni Mmisri, mtumwa wa Mwamaleki. Bwana wangu alinitelekeza nilipougua siku tatu zilizopita.

14 Tulivamia Negebu ya Wakerethi, na nchi ya Yuda, na Negebu ya Kalebu. Nasi tulichoma moto Siklagi.”

15 Daudi akamuuliza, “Je, unaweza kuniongoza kufikia kundi hili la uvamizi?”

Akajibu, “Niapie mbele ya Mungu kwamba hutaniua wala kunikabidhi mikononi mwa bwana wangu, nami nitakupeleka hadi waliko.”

16 Akamwongoza Daudi mpaka mahali walipokuwa, nao walikuwa wametawanyika eneo lote, wakila, wakinywa na wakifanya karamu kwa sababu ya nyara nyingi walizochukua kutoka nchi ya Wafilisti na kutoka Yuda.

17 Daudi akapigana nao kuanzia machweo ya jua hadi kesho yake jioni, na hakuna yeyote miongoni mwao aliyetoroka, isipokuwa vijana wanaume 400 waliopanda ngamia na kutoroka.

18 Daudi akarudisha kila kitu Waamaleki walikuwa wamechukua, pamoja na wake zake wawili.

19 Hakuna chochote kilichopotea: kijana au mzee, mvulana au msichana, nyara au kitu kingine chochote walichokuwa wamechukua. Daudi akarudisha kila kitu.

20 Akachukua makundi yote ya kondoo, mbuzi na ngʼombe, nao watu wake wakawaswaga wanyama hao mbele ya wanyama wengine wa kufugwa, wakisema, “Hizi ni nyara za Daudi.”

21 Kisha Daudi akafika kwa wale watu 200 waliokuwa wamechoka sana kumfuata na ambao waliachwa nyuma kwenye Bonde la Besori. Wakatoka kwenda kumlaki Daudi na wale watu aliokuwa nao. Daudi na watu wake walipowakaribia, akawasalimu.

22 Lakini watu wote waovu na wakorofi miongoni mwa wafuasi wa Daudi wakasema, “Kwa sababu hawakwenda pamoja nasi, hatutagawana nao nyara tulizorudisha. Lakini, kila mtu aweza kuchukua mkewe na watoto wake na kuondoka.”

23 Daudi akajibu, “La hasha, ndugu zangu, kamwe hamwezi kufanya hivyo kwa kile ambachoBwanaametupatia. Yeye ametulinda na kuweka mikononi mwetu majeshi yale yaliyokuja kupigana dhidi yetu.

24 Ni nani atasikiliza yale mnayosema? Fungu la mtu aliyekaa na vyombo litakuwa sawa na la yule aliyekwenda vitani. Wote watashiriki sawa.”

25 Daudi akafanya hili liwe amri na agizo kwa Israeli kutoka siku ile hata leo.

26 Daudi alipofika Siklagi, akatuma baadhi ya nyara kwa wazee wa Yuda, waliokuwa rafiki zake, akasema, “Tazama, hapa kuna zawadi kwa ajili yenu kutoka nyara za adui zaBwana.”

27 Akazituma kwa wale waliokuwa Betheli, Ramoth-Negebu na Yatiri;

28 kwa wale walioko Aroeri, Sifmothi, Eshtemoa

29 na Rakali; kwa wale waliokuwa katika miji ya Wayerameeli na ya Wakeni;

30 na kwa wale walioko Horma, Bori-Ashani, Athaki,

31 na kwa wakazi wa Hebroni; na kwa wale waliokuwa mahali pengine pote ambako Daudi na watu wake walitembelea.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1SA/30-70ddc46f23f590e3c943c4e8f1909cba.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Samweli

1 Samweli 31

Sauli Ajiua

1 Basi Wafilisti wakapigana na Israeli. Waisraeli wakawakimbia, na wengi wakauawa katika Mlima Gilboa.

2 Wafilisti wakawafuatia kwa bidii Sauli na wanawe, wakawaua Yonathani, Abinadabu na Malki-Shua.

3 Mapigano yakawa makali sana kumzunguka Sauli, nao wapiga upinde wakampata na kumjeruhi vibaya.

4 Sauli akamwambia mbeba silaha wake, “Futa upanga wako unichome nao, la sivyo hawa watu wasiotahiriwa watakuja wanichome na kunidhalilisha.”

Lakini mbeba silaha wake akaogopa sana wala hakuweza kufanya hivyo. Kwa hiyo Sauli akachukua upanga wake mwenyewe na kuuangukia.

5 Mchukua silaha wake alipoona Sauli amekufa, naye pia akaangukia upanga wake akafa pamoja naye.

6 Basi Sauli, wanawe watatu, mbeba silaha wake na watu wake wote wakafa pamoja siku ile ile.

7 Waisraeli waliokuwa kandokando ya bonde na wale waliokuwa ngʼambo ya Yordani walipoona kuwa jeshi la Waisraeli limekimbia na kwamba Sauli na wanawe wamekufa, wakaacha miji yao na kukimbia. Nao Wafilisti wakaja na kukaa humo.

8 Kesho yake Wafilisti walipokuja kuwavua maiti silaha, walimkuta Sauli na wanawe watatu wameanguka katika Mlima Gilboa.

9 Wakamkata Sauli kichwa na kumvua silaha zake, nao wakatuma wajumbe katika nchi yote ya Wafilisti kutangaza habari katika hekalu la sanamu zao na miongoni mwa watu wao.

10 Wakaweka silaha zake katika hekalu la Maashtorethi, na kukifunga kiwiliwili chake katika ukuta wa Beth-Shani.

11 Watu wa Yabeshi-Gileadi waliposikia yale Wafilisti walichomfanyia Sauli,

12 mashujaa wao wote wakaenda usiku hadi Beth-Shani. Wakauchukua mwili wa Sauli na miili ya wanawe kutoka kwenye ukuta wa Beth-Shani na kurudi hadi Yabeshi, mahali ambapo waliiteketeza kwa moto.

13 Kisha wakachukua mifupa yao na kuizika chini ya mti wa mkwaju huko Yabeshi, nao wakafunga siku saba.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1SA/31-5a13f618e2a33b51f5e785f2c130dd9c.mp3?version_id=1627—

Categories
2 Samweli

2 Samweli Utangulizi

Utangulizi

Kitabu cha 2 Samweli kinaendeleza historia ya kuanzishwa kwa ufalme katika Israeli. Kinaanza na kifo cha Sauli, na kuendelea na habari za kutawazwa kwa Daudi kukalia kiti cha ufalme cha Israeli, na pia kipindi chote cha utawala wake. Kinaweka kumbukumbu ya vita na matukio mengine ya wakati wa utawala wa Daudi kama vile kutekwa kwa mji wa Yerusalemu (

5:6-16

), dhambi ya Daudi na Bathsheba (

11:1-27

), na uasi wa Absalomu (

13:1-20

).

Mwandishi

Haijulikani kwa uhakika. Wengine wamesema inawezekana ikawa ni Zabudi, mwanawe Nathani; pia kitabu kina habari zilizoandikwa na Nathani na Gadi.

Kusudi

Kitabu hiki kinamwonyesha Daudi kama mtu muhimu ambaye chini ya uongozi wake taifa la Israeli lilifikia kilele cha umoja na nguvu kuliko nyakati nyingine zote katika historia lake.

Mahali

Katika nchi ya Israeli chini ya utawala wa Mfalme Daudi.

Tarehe

Kitabu hiki kinadhaniwa kiliandikwa mwaka wa 930 K.K.

Wahusika Wakuu

Daudi, Yoabu, Bathsheba, Nathani na Absalomu.

Wazo Kuu

Kitabu hiki kinashughulika zaidi na miaka arobaini ya utawala wa Mfalme Daudi, kikionyesha jinsi ambavyo ustawi wa watu wote kifamilia na kitaifa umefungwa katika hali ya kiroho na ya kimaadili ya kiongozi wao. Uadilifu au upotovu wa kiongozi huamua ustawi au kudidimia kwa jamii au taifa.

Mambo Muhimu

Kukua kwa ufalme wa Israeli na utawala wa Mfalme Daudi.

Mgawanyo

Daudi mfalme wa Yuda (

1:1–4:12

)

Daudi anaiunganisha Israeli (

5:1–24:25

).

Categories
2 Samweli

2 Samweli 1

Daudi Afahamishwa Kifo Cha Sauli

1 Baada ya kifo cha Sauli, Daudi alipokuwa amerudi kutoka kuwashinda Waamaleki, Daudi alikaa siku mbili huko Siklagi.

2 Siku ya tatu akaja mtu mwenye nguo zilizoraruka na mavumbi kichwani mwake kutoka kwenye kambi ya Sauli. Alipomjia Daudi, akajitupa chini ili kumpa heshima.

3 Daudi akamuuliza, “Wewe umetoka wapi?”

Akamjibu, “Nimetoroka kutoka kambi ya Waisraeli.”

4 Daudi akamuuliza, “Ni nini kilichotokea? Niambie.”

Akasema, “Watu walikimbia kutoka vitani. Wengi wao walianguka na kufa. Naye Sauli na Yonathani mwanawe wamekufa.”

5 Ndipo Daudi akamwambia huyo kijana aliyemletea taarifa, “Je, umefahamuje kwamba Sauli na Yonathani mwanawe wamekufa?”

6 Yule kijana akasema, “Nilijipata huko Mlima Gilboa, naye Sauli alikuwa huko akiegemea mkuki wake, na magari ya vita na wapanda farasi wa upande wa adui wakawa wamemkaribia sana.

7 Alipogeuka na kuniona, akaniita, nami nikasema, ‘Je, nifanye nini?’

8 “Akaniuliza, ‘Wewe ni nani?’

“Nikamjibu, ‘Mimi ni Mwamaleki.’

9 “Kisha akaniambia, ‘Nikaribie mimi na uniue! Niko katika maumivu makali ya kifo, lakini bado ningali hai.’

10 “Kwa hiyo nikamkaribia nikamuua, kwa sababu nilijua kwamba baada ya kuanguka hangeweza kupona. Nami nikachukua lile taji lililokuwa kichwani mwake na utepe uliokuwa mkononi mwake nami nimevileta hapa kwa bwana wangu.”

11 Ndipo Daudi pamoja na watu wote waliokuwa pamoja naye wakazishika nguo zao na kuzirarua.

12 Wakaomboleza, wakalia pia na kufunga mpaka jioni kwa ajili ya Sauli na Yonathani mwanawe, kwa ajili ya jeshi laBwanana nyumba ya Israeli, kwa sababu wameanguka kwa upanga.

13 Daudi akamwambia yule kijana aliyemletea taarifa, “Wewe ni mwenyeji wa wapi?”

Akamjibu, “Mimi ni mwana wa mgeni, Mwamaleki.”

14 Daudi akamuuliza, “Kwa nini hukuogopa kuinua mkono wako ili kumwangamiza mpakwa mafuta waBwana?”

15 Kisha Daudi akamwita mmoja wa watu wake na kumwambia, “Nenda ukamuue!” Kwa hiyo akampiga, naye akafa.

16 Kwa maana Daudi alikuwa amemwambia, “Damu yako iwe juu ya kichwa chako mwenyewe. Kinywa chako mwenyewe kimeshuhudia dhidi yako uliposema, ‘Nilimuua mpakwa mafuta waBwana.’ ”

Ombolezo La Daudi Kwa Ajili Ya Sauli Na Yonathani

17 Daudi akafanya maombolezo haya kuhusu Sauli na Yonathani mwanawe,

18 naye akaagiza kwamba watu wa Yuda wafundishwe ombolezo hili la upinde (ambalo limeandikwa katika Kitabu cha Yashari):

19 “Walio fahari yako, ee Israeli, wameuawa juu ya mahali pako palipoinuka.

Jinsi wenye nguvu walivyoanguka!

20 “Msilisimulie hili katika Gathi,

msilitangaze hili katika

barabara za Ashkeloni,

binti za Wafilisti wasije wakafurahia,

binti za hao wasiotahiriwa

wasije wakashangilia.

21 “Enyi milima ya Gilboa,

msipate umande wala mvua,

wala mashamba yazaayo sadaka ya nafaka.

Kwa maana huko ndiko ngao ya mwenye nguvu iliponajisiwa,

ngao ya Sauli haitapakwa tena mafuta.

22 Kutokana na damu ya waliouawa,

kutokana na miili ya wenye nguvu,

ule upinde wa Yonathani haukugeuka nyuma.

Upanga wa Sauli haukurudi bure.

23 “Sauli na Yonathani,

maishani walipendwa na kuneemeka,

na katika kifo hawakutengana.

Walikuwa wepesi kuliko tai,

walikuwa na nguvu kuliko simba.

24 “Enyi binti za Israeli,

lieni kwa ajili ya Sauli,

ambaye aliwavika nguo

nyekundu na maridadi,

ambaye aliremba mavazi yenu

kwa mapambo ya dhahabu.

25 “Tazama jinsi mashujaa

walivyoanguka vitani!

Yonathani ameuawa

mahali pako palipoinuka.

26 Nahuzunika kwa ajili yako,

Yonathani ndugu yangu,

kwangu ulikuwa mpendwa sana.

Upendo wako kwangu ulikuwa wa ajabu,

wa ajabu zaidi kuliko ule wa wanawake.

27 “Tazama jinsi mashujaa walivyoanguka!

Silaha za vita zimeangamia!”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2SA/1-38adc8e82f3885fc096407d8cee04f58.mp3?version_id=1627—

Categories
2 Samweli

2 Samweli 2

Daudi Atiwa Mafuta Kuwa Mfalme Wa Yuda

1 Ikawa baada ya mambo haya, Daudi akamuulizaBwana, “Je, nipande kwenda katika mojawapo ya miji ya Yuda?”

Bwanaakasema, “Panda.”

Daudi akauliza, “Je, niende wapi?”

Bwanaakajibu, “Nenda Hebroni.”

2 Basi Daudi akakwea kwenda huko pamoja na wake zake wawili, Ahinoamu wa Yezreeli na Abigaili, mjane wa Nabali wa Karmeli.

3 Pia Daudi akawachukua watu waliokuwa pamoja naye, kila mmoja na jamaa yake, nao wakaishi huko Hebroni na miji yake.

4 Ndipo watu wa Yuda wakaja Hebroni, huko wakamtia Daudi mafuta awe mfalme juu ya nyumba ya Yuda.

Daudi alipoambiwa kuwa ni watu wa Yabeshi-Gileadi waliomzika Sauli,

5 akatuma wajumbe kwa watu wa Yabeshi-Gileadi kuwaambia, “Bwanaawabariki kwa kuonyesha wema huu kwa kumzika Sauli bwana wenu.

6 SasaBwanana awaonyeshe wema na uaminifu, nami pia nitawaonyesha wema ule ule kwa kuwa mmefanya jambo hili.

7 Sasa basi, kuweni hodari na mashujaa, kwa maana bwana wenu Sauli amekufa, nayo nyumba ya Yuda imenitia mafuta niwe mfalme juu yao.”

Vita Kati Ya Nyumba Ya Daudi Na Sauli

8 Wakati huo Abneri mwana wa Neri, jemadari wa jeshi la Sauli, alikuwa amemchukua Ish-Boshethi mwana wa Sauli na kumleta hadi Mahanaimu.

9 Akamweka awe mfalme juu ya nchi ya Gileadi, Waasheri,Yezreeli, Efraimu, Benyamini na Israeli yote.

10 Ish-Boshethimwana wa Sauli alikuwa na umri wa miaka arobaini alipoanza kutawala Israeli, naye akatawala miaka miwili. Hata hivyo, nyumba ya Yuda ikamfuata Daudi.

11 Muda ambao Daudi alikuwa mfalme juu ya nyumba ya Yuda huko Hebroni ilikuwa miaka saba na miezi sita.

12 Abneri mwana wa Neri, pamoja na watu wa Ish-Boshethi mwana wa Sauli, wakatoka Mahanaimu kwenda Gibeoni.

13 Yoabu mwana wa Seruya na watu wa Daudi wakatoka na kukutana nao kwenye bwawa la Gibeoni. Kikundi kimoja kiliketi upande mmoja wa bwawa, na kikundi kingine upande wa pili.

14 Ndipo Abneri akamwambia Yoabu, “Tuwaweke baadhi ya vijana wasimame na wapigane ana kwa ana mbele yetu.”

Yoabu akasema, “Sawa, na wafanye hivyo.”

15 Kwa hiyo vijana wakasimama, wakahesabiwa: watu wa Benyamini na wa Ish-Boshethi mwana wa Sauli kumi na wawili, na upande wa Daudi kumi na wawili.

16 Kisha kila mtu akakamatana na mpinzani wake kichwani na kuchomana kwa upanga, nao wakaanguka chini pamoja. Kwa hiyo mahali pale katika Gibeoni pakaitwa Helkath-Hasurimu.

17 Siku hiyo vita vilikuwa vikali sana, naye Abneri na watu wa Israeli wakashindwa na watu wa Daudi.

18 Wana watatu wa Seruya walikuwako huko: nao ni Yoabu, Abishai na Asaheli. Basi huyo Asaheli alikuwa na mbio kama paa.

19 Asaheli akamfukuza Abneri, pasipo kugeuka kulia wala kushoto wakati akimfuata.

20 Abneri akaangalia nyuma na kumuuliza, “Ni wewe, Asaheli?”

Akamjibu, “Ndiyo.”

21 Ndipo Abneri akamwambia, “Geuka upande wa kulia au kushoto. Mchukue mmoja wa vijana wa kiume na umvue silaha zake.” Lakini Asaheli hakuacha kumfukuza.

22 Abneri akamwonya tena Asaheli akimwambia, “Acha kunifukuza! Kwa nini nikuue? Je, nitawezaje kumtazama ndugu yako Yoabu usoni?”

23 Lakini Asaheli alikataa kuacha kumfuatia, kwa hiyo Abneri akamchoma Asaheli tumboni kwa ncha butu ya mkuki wake, mkuki ukamtoboa ukatokea mgongoni mwake. Akaanguka na kufa papo hapo. Ikawa kila mtu alisimama alipofika mahali pale Asaheli alipoanguka na kufa.

24 Lakini Yoabu na Abishai walimfuata Abneri, na jua lilipokuwa linatua, wakafika kwenye kilima cha Ama, karibu na Gia kwenye njia ya kuelekea kwenye nyika ya Gibeoni.

25 Ndipo watu wa kabila la Benyamini wakakusanyika tena nyuma ya Abneri. Wakaunda kikosi na kujiimarisha juu ya kilima.

26 Abneri akamwita Yoabu, akamwambia, “Je, ni lazima upanga uendelee kuangamiza milele? Hutambui kwamba jambo hili litaishia katika uchungu? Utaacha kuwaagiza watu wako waache kuwafuatilia ndugu zao hata lini?”

27 Yoabu akajibu, “Hakika kama aishivyo Mungu, kama hukusema, hawa watu wangeendelea kuwafuatia ndugu zao mpaka asubuhi.”

28 Basi Yoabu akapiga tarumbeta, nao watu wote wakasimama, hawakuwafuata Israeli tena, wala hawakuwapiga tena.

29 Usiku ule wote Abneri na watu wake wakatembea kupitia Araba. Wakavuka Mto Yordani, wakaendelea wakipitia nchi yote ya Bithroni wakafika Mahanaimu.

30 Basi Yoabu akarudi kutoka kumfuatia Abneri, na kuwakusanya watu wake wote. Pamoja na Asaheli, watu kumi na tisa wa Daudi walikuwa wamepotea.

31 Lakini watu wa Daudi walikuwa wamewaua watu wa kabila la Benyamini 360 waliokuwa pamoja na Abneri.

32 Wakamchukua Asaheli, wakamzika katika kaburi la baba yake huko Bethlehemu. Kisha Yoabu na watu wake wakatembea usiku kucha na kufika huko Hebroni wakati wa mapambazuko.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2SA/2-3c23f89d43c2a6f812f792aed3940788.mp3?version_id=1627—

Categories
2 Samweli

2 Samweli 3

1 Vita kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi vilidumu kwa muda mrefu. Daudi akaendelea kuwa imara zaidi na zaidi, wakati nyumba ya Sauli iliendelea kudhoofika zaidi na zaidi.

2 Wana walizaliwa kwa Daudi huko Hebroni:

Mzaliwa wake wa kwanza alikuwa Amnoni mwana wa Ahinoamu wa Yezreeli;

3 mzaliwa wake wa pili alikuwa Danielimwana wa Abigaili, mjane wa Nabali wa Karmeli;

wa tatu, Absalomu mwana wa Maaka, binti Talmai mfalme wa Geshuri;

4 wa nne, Adoniya mwana wa Hagithi;

wa tano, Shefatia mwana wa Abitali;

5 wa sita, Ithreamu mwana wa Egla, mkewe Daudi.

Hawa ndio waliozaliwa kwa Daudi huko Hebroni.

Abneri Anamwendea Daudi

6 Wakati wa vita kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi, Abneri alikuwa anajiimarisha katika nafasi yake kwenye nyumba ya Sauli.

7 Basi Sauli alikuwa amekuwa na suria, jina lake Rispa binti wa Aiya. Naye Ish-Boshethi akamwambia Abneri, “Kwa nini umekutana kimwili na suria wa baba yangu?”

8 Abneri akakasirika sana kwa sababu ya kile Ish-Boshethi alichosema, naye akamjibu, “Je, mimi ni kichwa cha mbwa, kwa upande wa Yuda? Siku hii ya leo mimi ni mtiifu kwa nyumba ya baba yako Sauli, kwa jamaa yake na rafiki zake. Sijakukabidhi kwa Daudi, lakini bado unanilaumu kwa kosa la kuhusika na huyu mwanamke!

9 Mungu na amshughulikie Abneri, tena kwa ukali, ikiwa sitafanya kwa ajili ya Daudi kileBwanaalichomwahidi kwa kiapo,

10 na kuuhamisha ufalme kutoka kwenye nyumba ya Sauli na kuimarisha kiti cha ufalme cha Daudi juu ya Israeli na Yuda kuanzia Dani mpaka Beer-Sheba.”

11 Ish-Boshethi hakuthubutu kusema neno jingine kwa Abneri, kwa sababu alimwogopa Abneri.

12 Ndipo Abneri akatuma wajumbe kwa niaba yake kwa Daudi, kumwambia, “Nchi hii ni ya nani? Fanya mapatano na mimi, nami nitakusaidia kuiweka Israeli yote juu yako.”

13 Daudi akasema, “Vyema, nitafanya mapatano nawe. Lakini nahitaji jambo moja kwako: Usije mbele yangu mpaka umemleta Mikali binti Sauli wakati utakapokuja kuniona.”

14 Kisha Daudi akapeleka wajumbe kwa Ish-Boshethi mwana wa Sauli, kudai, “Nipe Mikali mke wangu, ambaye nilimposa mwenyewe kwa mahari ya magovi 100 ya Wafilisti.”

15 Kwa hiyo Ish-Boshethi akatoa amri kwamba Mikali achukuliwe kutoka kwa Paltieli mumewe, mwana wa Laishi.

16 Hata hivyo, mumewe alikwenda pamoja naye, akilia nyuma ya mkewe njia yote hadi Bahurimu. Ndipo Abneri akamwambia Paltieli, “Rudi nyumbani!” Kwa hiyo akarudi.

17 Abneri akafanya shauri pamoja na wazee wa Israeli, akasema, “Muda mrefu mmetaka kumfanya Daudi mfalme wenu.

18 Sasa fanyeni hivyo! Kwa maanaBwanaalimwahidi Daudi akisema, ‘Kwa kupitia Daudi mtumishi wangu nitawaokoa watu wangu Israeli kutoka mikononi mwa Wafilisti na kutoka mikononi mwa adui zako wote.’ ”

19 Pia Abneri mwenyewe akazungumza na kabila la Benyamini. Kisha akaenda mpaka Hebroni kumwambia Daudi kila kitu ambacho Israeli na nyumba yote ya Benyamini walichotaka kufanya.

20 Wakati Abneri aliyekuwa na watu ishirini pamoja naye, alipokuja kwa Daudi huko Hebroni, Daudi akamwandalia karamu pamoja na watu wake.

21 Ndipo Abneri akamwambia Daudi, “Niache niende mara moja nikakusanye Israeli yote kwa ajili ya mfalme bwana wangu, ili waweze kufanya mapatano na wewe, ili kwamba uweze kutawala juu ya yote yale ambayo moyo wako unaonea shauku.” Basi Daudi akamuaga Abneri, naye akaenda kwa amani.

Yoabu Amuua Abneri

22 Wakati huo huo, watu wa Daudi na Yoabu walirudi kutoka kwenye kushambulia, nao wakarudi na nyara nyingi mno. Lakini Abneri hakuwa tena pamoja na Daudi huko Hebroni, kwa sababu Daudi alikuwa amemruhusu aende zake, naye akaenda kwa amani.

23 Yoabu na askari wote aliokuwa nao walipowasili, aliambiwa kwamba Abneri mwana wa Neri alikuwa amekuja kwa mfalme na kwamba mfalme alikuwa amemruhusu aende zake, na kwamba alikwisha ondoka kwa amani.

24 Basi Yoabu alikwenda kwa mfalme na kumwambia, “Ni nini hiki ulichofanya? Tazama, Abneri alikuja kwako. Kwa nini ukamwacha aende? Sasa amekwenda!

25 Wajua Abneri mwana wa Neri alikuja kukudanganya na kuchunguza nyendo zako na kupata kila kitu unachokifanya.”

26 Ndipo Yoabu akamwacha Daudi na kutuma wajumbe wamfuate Abneri, nao wakamrudisha kutoka kisima cha Sira. Lakini Daudi hakufahamu jambo hili.

27 Basi Abneri aliporudi Hebroni, Yoabu akamchukua kando ndani ya lango, kama vile kuzungumza naye faraghani. Ili kulipiza kisasi damu ya nduguye Asaheli, Yoabu akamchoma mkuki tumboni palepale, naye akafa.

28 Baadaye, Daudi aliposikia kuhusu jambo hili, akasema, “Mimi na ufalme wangu kamwe hatuna hatia mbele zaBwanakuhusu damu ya Abneri mwana wa Neri.

29 Damu yake na iwe juu ya kichwa cha Yoabu na juu ya nyumba yote ya baba yake! Kamwe asikosekane yeyote katika nyumba ya Yoabu mwenye kidonda chenye usaha, au ukoma au mwenye kuegemea fimbo au aangukaye kwa upanga au kupungukiwa na chakula.”

30 (Yoabu na Abishai ndugu yake walimuua Abneri kwa sababu alikuwa amemuua Asaheli ndugu yao katika vita huko Gibeoni.)

31 Kisha Daudi akamwambia Yoabu na watu wote aliokuwa pamoja nao, “Rarueni nguo zenu na mvae nguo za gunia na mtembee mkiomboleza mbele ya Abneri.” Mfalme Daudi mwenyewe akatembea nyuma ya jeneza.

32 Wakamzika Abneri huko Hebroni, naye mfalme akalia kwa sauti kwenye kaburi la Abneri. Pia watu wote wakalia.

33 Mfalme akaimba ombolezo hili kwa ajili ya Abneri:

“Je, ilipasa Abneri afe kama afavyo mpumbavu?

34 Mikono yako haikufungwa,

miguu yako haikufungwa pingu.

Ulianguka kama yeye aangukaye

mbele ya watu waovu.”

Nao watu wote wakamlilia tena.

35 Kisha watu wote wakaja kumsihi Daudi ale chochote kulipokuwa kungali bado mchana; lakini Daudi akaapa, akisema, “Mungu na anishughulikie, tena kwa ukali, kama nikionja mkate au kitu kingine chochote kabla ya jua kutua!”

36 Watu wote wakaona hilo nao ikawapendeza; naam, kila kitu mfalme alichofanya kiliwapendeza.

37 Kwa hiyo siku ile watu wote na Israeli yote wakajua kwamba mfalme hakushiriki katika mauaji ya Abneri mwana wa Neri.

38 Kisha mfalme akawaambia watu wake, “Je, hamfahamu kwamba mkuu na mtu mashuhuri ameanguka katika Israeli leo?

39 Nami leo ingawa ni mfalme mpakwa mafuta, mimi ni dhaifu, nao hawa wana wa Seruya wananizidi nguvu.Bwanana amlipize mtenda maovu sawasawa na matendo yake maovu!”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2SA/3-f8bba0ddcb4ab4165fc943314c0a994a.mp3?version_id=1627—