Categories
1 Samweli

1 Samweli 6

Sanduku La Mungu Larudishwa Israeli

1 Sanduku laBwanalilipokuwa limekaa katika nchi ya Wafilisti kwa miezi saba,

2 Wafilisti waliwaita makuhani wa Dagoni na waaguzi, na kuwaambia, “Tutafanya nini na hili Sanduku laBwana? Tuambieni jinsi tutakavyolirudisha mahali pake.”

3 Wakajibu, “Kama mtalirudisha Sanduku la Mungu wa Israeli, msilirudishe mikono mitupu bali kwa vyovyote mpelekeeni sadaka ya hatia. Kisha mtaponywa, nanyi mtafahamu kwa nini mkono wake haujaondolewa kwenu.”

4 Wafilisti wakawauliza, “Ni sadaka gani ya hatia tutakayompelekea?”

Wakajibu, “Majipu matano ya dhahabu na panya wa dhahabu watano, kulingana na idadi ya watawala wa Wafilisti, kwa sababu tauni iyo hiyo imewaua ninyi na watawala wenu.

5 Tengenezeni mifano ya majipu na ya panya wale wanaoharibu nchi yenu, nanyi mheshimuni Mungu wa Israeli. Labda ataondoa mkono wake kutoka kwenu na kwa miungu yenu na nchi yenu.

6 Kwa nini ninyi mnafanya mioyo yenu migumu kama Wamisri na Farao walivyofanya? Je, alipowatendea kwa ukali, hawakuwaachia Waisraeli wakaenda zao?

7 “Sasa basi, wekeni gari jipya la kukokotwa pamoja na ngʼombe wawili ambao wamezaa lakini ambao kamwe hawajafungwa nira. Fungieni hao ngʼombe hilo gari, lakini ondoeni ndama wao na mwaweke zizini.

8 Chukueni hilo Sanduku laBwanana mliweke juu ya gari la kukokotwa, na ndani ya kasha kando yake wekeni hivyo vitu vya dhahabu mnavyompelekeaBwanakama sadaka ya hatia. Lipelekeni,

9 lakini liangalieni kwa makini. Iwapo litakwenda katika nchi yake lenyewe, kuelekea Beth-Shemeshi, basi tutajua kwambaBwanandiye alileta haya maafa makubwa juu yetu. Lakini kama halikwenda, basi tutajua kwamba haukuwa mkono waBwanauliotupiga na kwamba iliyotokea kwetu ni ajali.”

10 Basi wakafanya hivyo. Wakachukua ngʼombe wawili wa aina hiyo, wakawafungia hilo gari la kukokotwa, nao ndama wao wakawekwa zizini.

11 Wakaliweka Sanduku laBwanajuu ya hilo gari la kukokotwa pamoja na lile kasha lenye ile mifano ya panya wa dhahabu na ya majipu ya dhahabu.

12 Kisha hao ngʼombe wakaenda moja kwa moja kuelekea Beth-Shemeshi, wakishuka bila kugeuka kuume au kushoto, huku wakilia njia yote. Watawala wa Wafilisti waliwafuata hao ngʼombe hadi mpakani mwa Beth-Shemeshi.

13 Wakati huu watu wa Beth-Shemeshi walikuwa wakivuna ngano yao huko bondeni, walipoinua macho yao na kuona lile Sanduku, wakafurahi kuliona.

14 Lile gari la kukokotwa lilikuja mpaka kwenye shamba la Yoshua wa Beth-Shemeshi, nalo likasimama kando ya mwamba mkubwa. Watu wakapasua mbao za lile gari la kukokotwa na kutoa dhabihu wale ngʼombe kama sadaka ya kuteketezwa kwaBwana.

15 Walawi walilishusha Sanduku laBwana, pamoja na lile kasha lililokuwa na vile vitu vya dhahabu na kuviweka juu ya ule mwamba mkubwa. Siku ile watu wa Beth-Shemeshi wakatoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu kwaBwana.

16 Wale watawala watano wa Wafilisti waliona haya yote, nao wakarudi siku ile ile mpaka Ekroni.

17 Haya ndiyo yale majipu ya dhahabu Wafilisti waliyotuma kama sadaka ya hatia kwaBwana, moja kwa ajili ya Ashdodi, moja kwa Gaza, moja kwa Ashkeloni, moja kwa Gathi, na moja kwa Ekroni.

18 Nayo hesabu ya wale panya wa dhahabu ilikuwa kulingana na idadi ya miji ya Wafilisti ya watawala watano wa Wafilisti: miji yao iliyozungukwa na maboma, pamoja na vijiji vya miji hiyo. Ule mwamba mkubwa, ambao juu yake waliliweka lile Sanduku laBwana, ni ushahidi hadi leo katika shamba la Yoshua wa Beth-Shemeshi.

19 Lakini Mungu aliwapiga baadhi ya watu wa Beth-Shemeshi, akiwaua watu sabini miongoni mwao kwa sababu walichungulia ndani ya Sanduku laBwana. Watu wakaomboleza kwa sababu ya pigo zito kutoka kwaBwana,

20 nao watu wa Beth-Shemeshi wakauliza, “Ni nani awezaye kusimama mbele zaBwana, huyu Mungu aliye mtakatifu? Sanduku litapanda kwenda kwa nani kutoka hapa?”

21 Kisha wakatuma wajumbe kwa watu wa Kiriath-Yearimu, wakisema, “Wafilisti wamerudisha Sanduku laBwana. Shukeni na mlipandishe huko kwenu.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1SA/6-1dedbf2c43bb98e39b5e3cfeeb80678b.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Samweli

1 Samweli 7

1 Kisha watu wa Kiriath-Yearimu wakaja na kulichukua Sanduku laBwana. Wakalipeleka katika nyumba ya Abinadabu juu kilimani na kumweka Eleazari mwanawe wakfu kulichunga Sanduku laBwana.

Samweli Awatiisha Wafilisti Huko Mispa

2 Sanduku laBwanalilibakia huko Kiriath-Yearimu kwa muda mrefu, yaani jumla ya miaka ishirini, nao watu wa Israeli wakaomboleza na kumtafutaBwana.

3 Naye Samweli akawaambia nyumba yote ya Israeli, “Ikiwa mtamrudiaBwanakwa mioyo yenu yote, basi iacheni miungu migeni na Maashtorethi na kujitoa wenyewe kwaBwanana kumtumikia yeye peke yake, naye atawaokoa ninyi na mkono wa Wafilisti.”

4 Hivyo Waisraeli wakaweka mbali Mabaali yao na Maashtorethi, nao wakamtumikiaBwanapeke yake.

5 Kisha Samweli akasema, “Wakusanyeni Israeli wote huko Mispa, nami nitawaombea ninyi kwaBwana.”

6 Walipokwisha kukutanika huko Mispa, walichota maji na kuyamimina mbele zaBwana. Siku hiyo walifunga na wakaungama, wakisema, “Tumetenda dhambi dhidi yaBwana.” Naye Samweli alikuwa kiongoziwa Israeli huko Mispa.

7 Wafilisti waliposikia kwamba Israeli wamekusanyika huko Mispa, watawala wa Wafilisti wakapanda ili kuwashambulia. Waisraeli waliposikia habari hiyo, waliogopa kwa sababu ya Wafilisti.

8 Wakamwambia Samweli, “Usiache kumliliaBwana, Mungu wetu, kwa ajili yetu, ili apate kutuokoa na mikono ya Wafilisti.”

9 Kisha Samweli akamchukua mwana-kondoo anyonyaye na kumtoa mzima kama sadaka ya kuteketezwa kwaBwana. AkamliliaBwanakwa niaba ya Israeli, nayeBwanaakamjibu.

10 Samweli alipokuwa anatoa hiyo dhabihu ya kuteketezwa, Wafilisti wakasogea karibu ili kupigana vita na Israeli. Lakini siku ileBwanaalinguruma kwa ngurumo kubwa dhidi ya Wafilisti na kuwafanya wafadhaike na kutetemeka hivi kwamba walikimbizwa mbele ya Waisraeli.

11 Watu wa Israeli wakatoka mbio huko Mispa na kuwafuatia Wafilisti, wakiwachinja njiani hadi mahali chini ya Beth-Kari.

12 Ndipo Samweli akachukua jiwe na kulisimamisha kati ya Mispa na Sheni. Akaliita Ebenezeri,akisema, “Hata sasaBwanaametusaidia.”

13 Basi Wafilisti wakashindwa na hawakuvamia nchi ya Israeli tena.

Katika maisha yote ya Samweli, mkono waBwanaulikuwa dhidi ya Wafilisti.

14 Miji kuanzia Ekroni hadi Gathi, ile ambayo Wafilisti walikuwa wameiteka kutoka Israeli, ilirudishwa kwake, naye Israeli akazikomboa nchi jirani mikononi mwa Wafilisti. Kukawepo amani kati ya Israeli na Waamori.

15 Samweli akaendelea kama mwamuzi juu ya Israeli siku zote za maisha yake.

16 Mwaka hadi mwaka aliendelea kuzunguka kutoka Betheli mpaka Gilgali na Mispa, akiamua Israeli katika sehemu hizo zote.

17 Lakini kila mara alirudi Rama, kulikokuwa nyumbani kwake, huko pia aliwaamua Israeli. Naye huko alimjengeaBwanamadhabahu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1SA/7-8b441ad35427c44bf58cb20459f1bda5.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Samweli

1 Samweli 8

Israeli Waomba Mfalme

1 Samweli alipokuwa mzee, akaweka wanawe kuwa waamuzi wa Israeli.

2 Mzaliwa wa kwanza alikuwa Yoeli, na la wa pili lilikuwa Abiya, nao wakatumika huko Beer-Sheba.

3 Lakini wanawe hawakuenenda katika njia zake. Waliziacha wakageukia faida za udanganyifu nao wakapokea rushwa na kupotosha haki.

4 Basi wazee wote wa Israeli wakakusanyika pamoja na kumjia Samweli huko Rama.

5 Wakamwambia, “Wewe umekuwa mzee, nao wanao hawaenendi katika njia zako, sasa tuteulie mfalme wa kutuongoza, kama ilivyo kwa mataifa mengine yote.”

6 Lakini wao waliposema, “Tupe mfalme wa kutuongoza,” hili lilimchukiza Samweli, hivyo akamwombaBwana.

7 NayeBwanaakamwambia: “Sikiliza yale yote watu wanakuambia. Si wewe ambaye wamekukataa, bali wamenikataa mimi kuwa mfalme wao.

8 Kama vile walivyofanya tangu siku nilipowapandisha kutoka Misri mpaka siku hii ya leo; wakiniacha mimi na kutumikia miungu mingine, ndivyo wanavyokufanyia wewe.

9 Sasa wasikilize, lakini waonye kwa makini na uwafahamishe yale watakayotendewa na mfalme atakayewatawala.”

10 Samweli akawaambia wale watu waliokuwa wakiomba wapewe mfalme maneno yote yaBwana.

11 Akasema, “Hivi ndivyo atakavyowatendea mfalme atakayewatawala. Atawachukua wana wenu na kuwafanya watumike kwa magari yake ya vita na farasi, nao watakimbia mbele ya magari yake.

12 Baadhi yao atawaweka kuwa majemadari wa jeshi wa maelfu na majemadari wa jeshi wa hamsini, wengine kulima mashamba yake na kuvuna mavuno yake, pia na wengine kutengeneza silaha za vita na vifaa kwa ajili ya magari yake.

13 Atawachukua binti zenu kuwa watengeneza manukato, wapishi na waokaji.

14 Atayachukua mashamba yenu yaliyo mazuri, mashamba ya mizabibu na mashamba yenu ya mizeituni na kuwapa watumishi wake.

15 Ataichukua sehemu ya kumi ya nafaka yenu na ya zabibu zenu na kuwapa maafisa wake na watumishi wake.

16 Atawachukua watumishi wenu wa kiume na wa kike, na ngʼombe wenu walio wazuri sana na punda kwa matumizi yake mwenyewe.

17 Atachukua sehemu ya kumi ya makundi yenu ya kondoo na mbuzi, na ninyi wenyewe mtakuwa watumwa wake.

18 Siku ile itakapowadia, mtalia kwa kutaka msaada kutokana na mfalme mliyemchagua, nayeBwanahatawajibu.”

19 Lakini watu wakakataa kumsikiliza Samweli wakasema, “Hapana! Tunataka mfalme wa kututawala.

20 Kisha tutakuwa kama mataifa mengine yote, tukiwa na mfalme wa kutuongoza na kwenda mbele yetu na kutupigania vita vyetu.”

21 Samweli aliposikia yote watu waliyosema, akarudia kuyasema mbele zaBwana.

22 Bwanaakamjibu, “Wasikilize na uwape mfalme.”

Kisha Samweli akawaambia watu wa Israeli, “Kila mmoja arudi mjini kwake.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1SA/8-1a368e3a90d322c9e3439d482f5e4df4.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Samweli

1 Samweli 9

Samweli Anamtia Sauli Mafuta

1 Kulikuwako Mbenyamini mmoja, mtu maarufu, ambaye aliitwa Kishi mwana wa Abieli, mwana wa Serori, mwana wa Bekorathi, mwana wa Afia wa Benyamini.

2 Alikuwa na mwana aliyeitwa Sauli, kijana anayevutia sana, hakuwepo aliyelingana naye miongoni mwa Waisraeli, alikuwa mrefu kuliko wengine wote.

3 Basi punda wa Kishi baba yake Sauli walipotea, naye Kishi akamwambia mwanawe Sauli, “Mchukue mmoja wa watumishi mwende pamoja naye kuwatafuta punda.”

4 Hivyo akapita katika nchi ya vilima ya Efraimu na katika eneo la Shalisha, lakini hawakuwapata. Wakaendelea katika sehemu ya Shaalimu, lakini punda hawakuwepo huko. Kisha wakapita katika nchi ya Benyamini, lakini hawakuwapata.

5 Walipofika sehemu ya Sufu, Sauli akamwambia mtumishi aliyekuwa pamoja naye, “Njoo, sisi na turudi, au baba yangu ataacha kufikiria juu ya punda na kuanza kufadhaika kutuhusu sisi.”

6 Lakini mtumishi akajibu, “Tazama, katika mji huu yupo mtu wa Mungu, anayeheshimiwa sana na kila kitu asemacho hutokea kweli. Sasa na twende huko. Huenda atatuambia twende njia ipi.”

7 Sauli akamwambia mtumishi wake, “Kama tukienda, tutampa nini huyo mtu? Chakula kimekwisha kwenye mifuko yetu. Hatuna zawadi ya kumpelekea huyo mtu wa Mungu. Je tuna nini?”

8 Mtumishi akamjibu Sauli tena, akasema, “Tazama, nina fedha robo shekeli.Hiyo nitampa huyo mtu wa Mungu ili aweze kutuambia twende kwa njia ipi.”

9 (Zamani katika Israeli, kama mtu alikwenda kuuliza neno kwa Mungu, angalisema, “Njoo na twende kwa mwonaji,” kwa sababu nabii wa sasa alikuwa akiitwa mwonaji.)

10 Sauli akamwambia mtumishi wake, “Vyema, njoo na twende.” Basi wakaenda mjini alipokuwepo huyo mtu wa Mungu.

11 Walipokuwa wakipanda mlima kwenda mjini, wakakutana na baadhi ya wasichana wanakuja kuchota maji, nao wakawauliza, “Je, mwonaji yuko?”

12 Wakajibu, “Yuko, yu mbele yenu amewatangulia, sasa fanyeni haraka, ndiyo tu amekuja mjini kwetu leo, kwa kuwa watu wana dhabihu huko mahali pa juu.

13 Mara tu mwingiapo mjini, mtamkuta kabla hajapanda kwenda mahali pa juu kula. Watu hawataanza kula mpaka atakapofika kwa sababu ni lazima kwanza yeye abariki dhabihu, ndipo wale walioalikwa watakapokula. Pandeni sasa, mtamkuta kwa wakati huu.”

14 Wakapanda mjini, nao walipokuwa wakiingia mjini, tazama, Samweli alikuwa akija kuelekea walikokwenda mahali pa juu.

15 Basi siku moja kabla Sauli hajaja,Bwanaalikuwa amemfunulia Samweli jambo hili:

16 “Kesho wakati kama huu nitakupelekea mtu kutoka nchi ya Benyamini. Umtie mafuta awe kiongozi juu ya watu wangu Israeli, ndiye atakayewakomboa watu wangu na mkono wa Wafilisti. Nimewaangalia watu wangu, kwa kuwa kilio chao kimenifikia.”

17 Samweli alipomwona Sauli,Bwanaakamwambia, “Huyu ndiye mtu niliyekuambia habari zake, kwamba yeye atawatawala watu wangu.”

18 Sauli akamkaribia Samweli langoni na kumuuliza, “Tafadhali, je, waweza kuniambia mahali nyumba ya mwonaji ilipo?”

19 Samweli akamjibu Sauli, “Mimi ndiye mwonaji, panda utangulie mbele yangu mpaka mahali pa juu, kwa kuwa leo itakupasa kula pamoja nami na asubuhi nitakuruhusu uende na nitakuambia yale yote yaliyo moyoni mwako.

20 Kuhusu wale punda uliowapoteza siku tatu zilizopita, usifadhaike kwa habari yao; wamepatikana. Ni kwa nani ambaye shauku yote ya Israeli imeelekea, kama si kwako na jamaa yote ya baba yako?”

21 Sauli akajibu, “Je, mimi si Mbenyamini, kutoka kabila dogo kuliko yote ya Israeli, nao ukoo wangu si ndio mdogo kuliko koo zote za kabila la Benyamini? Kwa nini uniambie jambo la namna hiyo?”

22 Kisha Samweli akamleta Sauli na mtumishi wake ndani ukumbini na kuwaketisha mahali pa heshima zaidi miongoni mwa wale waliokuwa wamealikwa; jumla yao walikuwa kama watu thelathini.

23 Samweli akamwambia mpishi, “Leta ile sehemu ya nyama niliyokupa, ile niliyokuambia iweke kando.”

24 Hivyo mpishi akachukua mguu pamoja na kile kilichokuwa juu yake akaiweka mbele ya Sauli. Samweli akasema, “Hiki ndicho ambacho kimewekwa kwa ajili yako. Ule, kwa sababu kilitengwa kwa ajili yako kwa tukio hili, tangu niliposema, ‘Nimewaalika wageni.’ ” Naye Sauli akala pamoja na Samweli siku ile.

25 Baada ya kushuka kutoka mahali pa juu na kufika mjini, Samweli alizungumza na Sauli juu ya dari ya nyumba yake.

26 Walipoamka mapema alfajiri, Samweli akamwita Sauli darini, akamwambia, “Jiandae, nami nitakuaga uende zako.” Sauli alipokuwa tayari yeye na Samweli wakatoka nje pamoja.

27 Hata walipokuwa wakiteremka kuelekea mwisho wa mji, Samweli akamwambia Sauli, “Mwambie mtumishi atangulie mbele yetu.” Naye mtumishi akafanya hivyo. “Lakini subiri hapa kwa kitambo kidogo, ili nipate kukupa ujumbe kutoka kwa Mungu.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1SA/9-b9ee713094a5de06d961451e2a0ba8e4.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Samweli

1 Samweli 10

1 Ndipo Samweli akachukua chupa ndogo ya mafuta na kuyamimina juu ya kichwa cha Sauli, akambusu, akisema, “Je,Bwanahakukutia mafuta uwe kiongozi juu ya watu wake Israeli?

2 Utakapoondoka kwangu leo, utakutana na watu wawili karibu na kaburi la Raheli, huko Selsa kwenye mpaka wa Benyamini. Watakuambia, ‘Punda wale uliotoka kwenda kuwatafuta, wamekwisha kupatikana. Sasa baba yako ameacha kufikiri kuhusu punda na sasa ana hofu kukuhusu wewe. Anauliza, “Nitafanyaje kuhusu mwanangu?” ’

3 “Kisha utakwenda mbele kutoka hapa mpaka uufikie mwaloni wa Tabori. Watu watatu wanaopanda kwa Mungu huko Betheli watakutana nawe hapo. Mmoja atakuwa amechukua wana-mbuzi watatu, mwingine mikate mitatu, na mwingine kiriba cha divai.

4 Watakusalimu na kukupa mikate miwili, ambayo utaipokea kutoka kwao.

5 “Baada ya hayo utakwenda Gibea ya Mungu, ambapo hapo kuna kambi ya Wafilisti. Unapokaribia mji utakutana na kundi la manabii wakiteremka kutoka mahali pa juu wakiwa na vinubi, matari, filimbi na zeze vikipigwa mbele yao, nao watakuwa wakitoa unabii.

6 Roho waBwanaatakuja juu yako kwa nguvu, nawe utatoa unabii pamoja nao; nawe utageuzwa kuwa mtu wa tofauti.

7 Mara ishara hizi zitakapotimizwa, fanya lolote mkono wako upasao kufanya, kwa kuwa Mungu yu pamoja nawe.

8 “Tangulia kushuka mbele yangu mpaka Gilgali. Hakika nami nitateremka nikujie ili kutoa dhabihu za sadaka za kuteketezwa na dhabihu za amani, lakini lazima ungoje kwa siku saba hata nitakapokujia na kukuambia likupasalo kufanya.”

Sauli Afanywa Mfalme

9 Ikawa Sauli alipogeuka kumwacha Samweli, Mungu aliubadilisha moyo wa Sauli, na ishara hizi zote zikatimizwa siku ile.

10 Walipofika Gibea, akakutana na kundi la manabii. Roho wa Mungu akaja juu yake kwa nguvu, naye akajiunga nao katika kutoa unabii kwao.

11 Ikawa wale wote waliomfahamu hapo mwanzo walipomwona akitoa unabii pamoja na manabii, wakaulizana, “Ni nini hiki kilichomtokea mwana wa Kishi? Je, Sauli naye pia yumo miongoni mwa manabii?”

12 Mtu mmoja ambaye aliishi huko akajibu, “Je, naye baba yao ni nani?” Basi ikawa mithali, kusema, “Je, Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?”

13 Baada ya Sauli kumaliza kutoa unabii, alikwenda mahali pa juu.

14 Basi babaye mdogo akamuuliza Sauli na mtumishi wake, “Je, mlikuwa wapi?”

Akajibu, “Tulikuwa tukiwatafuta punda. Lakini tulipoona hawapatikani, tulikwenda kwa Samweli.”

15 Babaye mdogo Sauli akasema, “Niambie Samweli amekuambia nini.”

16 Sauli akajibu, “Alituhakikishia kwamba punda wamepatikana.” Lakini hakumwambia babaye mdogo kila kitu Samweli alichomwambia kuhusu ufalme.

17 Samweli akawaita watu wa Israeli kuja kwaBwanahuko Mispa,

18 naye akawaambia, “Hili ndilo asemaloBwana, Mungu wa Israeli: ‘Niliwatoa Israeli kutoka Misri, nami niliwaokoa toka nguvu za Misri na falme zote zilizowaonea.’

19 Lakini sasa mmemkataa Mungu wenu, ambaye anawaokoa toka katika maafa yenu yote na taabu zenu zote. Nanyi mmesema, ‘Hapana, tuteulie mfalme atutawale.’ Sasa basi, jihudhurisheni wenyewe mbele zaBwanakwa kabila zenu na kwa koo zenu.”

20 Samweli alipoyasogeza makabila yote ya Israeli, kabila la Benyamini likachaguliwa.

21 Kisha akalisogeza mbele kabila la Benyamini, ukoo kwa ukoo, nao ukoo wa Matri ukachaguliwa. Mwishoni Sauli mwana wa Kishi akachaguliwa. Lakini walipomtafuta, hakuonekana.

22 Wakazidi kuuliza kwaBwana, “Je, huyo mtu amekwisha kufika hapa?”

NayeBwanaakasema, “Ndiyo, amejificha katikati ya mizigo.”

23 Wakakimbia na kumleta kutoka huko, naye aliposimama katikati ya watu, alikuwa mrefu kuliko watu wengine wote.

24 Samweli akawaambia watu wote, “Je, mnamwona mtu ambayeBwanaamemchagua? Hayupo aliye kama yeye miongoni mwa watu wote.”

Ndipo watu wakapiga kelele, wakasema, “Mfalme na aishi maisha marefu.”

25 Samweli akawaeleza watu madaraka ya ufalme. Akayaandika kwenye kitabu na kuweka mbele zaBwana. Kisha Samweli akawaruhusu watu, kila mmoja aende nyumbani kwake.

26 Sauli pia akaenda nyumbani kwake huko Gibea, akisindikizwa na watu hodari ambao Mungu alikuwa amegusa mioyo yao.

27 Lakini baadhi ya watu wakorofi walisema, “Huyu mtu atawezaje kutuokoa?” Wakamdharau na wala hawakumletea zawadi. Lakini Sauli akanyamaza kimya.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1SA/10-a1a214764e2ddb39b0d9bff20cdea391.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Samweli

1 Samweli 11

Sauli Aukomboa Mji Wa Yabeshi

1 Nahashi yule Mwamoni, akakwea kuuzunguka kwa jeshi mji wa Yabeshi-Gileadi. Watu wote wa Yabeshi wakamwambia, “Fanya mkataba na sisi, na tutakuwa chini yako.”

2 Lakini Nahashi yule Mwamoni akajibu, “Nitafanya mkataba na ninyi tu kwa sharti kwamba nitangʼoa jicho la kulia la kila mmoja wenu, na hivyo kuleta aibu juu ya Israeli yote.”

3 Viongozi wa Yabeshi wakamwambia, “Tupe siku saba ili tuweze kutuma wajumbe katika Israeli yote, kama hakuna hata mmoja anayekuja kutuokoa, tutajisalimisha kwako.”

4 Wajumbe walipofika Gibea ya Sauli na kutoa taarifa juu ya masharti haya kwa watu, wote walilia kwa sauti kubwa.

5 Wakati huo huo Sauli alikuwa anarudi kutoka mashambani, akiwa nyuma ya maksai wake, naye akauliza, “Watu wana nini? Mbona wanalia?” Ndipo wakamweleza jinsi watu wa Yabeshi walivyokuwa wamesema.

6 Sauli aliposikia maneno yao, Roho wa Mungu akaja juu yake kwa nguvu, naye akawaka hasira.

7 Akachukua jozi ya maksai na kuwakata vipande vipande, naye kuvituma hivyo vipande kupitia wajumbe katika Israeli yote, wakitangaza, “Hivi ndivyo itakavyofanyika kwa maksai wa kila mmoja ambaye hatamfuata Sauli na Samweli.” Kisha hofu yaBwanaikawaangukia watu, nao wakatoka kama mtu mmoja.

8 Sauli alipowakusanya huko Bezeki, watu wa Israeli walikuwa 300,000 na watu wa Yuda 30,000.

9 Wakawaambia wale wajumbe waliokuwa wamekuja, “Waambieni watu wa Yabeshi-Gileadi, ‘Kesho kabla jua halijawa kali, mtaokolewa.’ ” Wajumbe walipokwenda na kutoa taarifa hii kwa watu wa Yabeshi, wakafurahi.

10 Wakawaambia Waamoni, “Kesho tutajisalimisha kwenu, nanyi mtaweza kututendea chochote mnachoona chema kwenu.”

11 Kesho yake Sauli alitenganisha watu wake katika vikosi vitatu; wakati wa zamu ya mwisho ya usiku wakaingia katika kambi ya Waamoni na kuwachinja mpaka mchana. Wale walionusurika wakasambaa, kiasi kwamba hawakusalia watu wawili pamoja.

Sauli Athibitishwa Kuwa Mfalme

12 Kisha watu wakamwambia Samweli, “Ni nani yule aliyeuliza, ‘Je, Sauli atatawala juu yetu?’ Tuletee hawa watu, nasi tutawaua.”

13 Lakini Sauli akasema, “Hakuna hata mmoja atakayeuawa leo, kwa kuwa siku hiiBwanaameokoa Israeli.”

14 Ndipo Samweli akawaambia watu, “Njooni, twendeni Gilgali na huko tuthibitishe ufalme.”

15 Kwa hiyo watu wote wakaenda Gilgali na kumthibitisha Sauli kuwa mfalme mbele zaBwana. Huko wakatoa dhabihu za sadaka za amani mbele zaBwana, naye Sauli na Waisraeli wote wakafanya karamu kubwa.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1SA/11-298a1807a441dda23ff60d05c0613f8b.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Samweli

1 Samweli 12

Hotuba Ya Samweli Ya Kuaga

1 Samweli akawaambia Israeli wote, “Nimesikiliza kila kitu mlichoniambia nami nimewawekea mfalme juu yenu.

2 Sasa mnaye mfalme kama kiongozi wenu. Lakini kwa habari yangu mimi ni mzee na nina mvi, nao wanangu wapo hapa pamoja nanyi. Nimekuwa kiongozi wenu tangu ujana wangu mpaka siku hii ya leo.

3 Mimi ninasimama hapa. Shuhudieni juu yangu mbele zaBwanana mpakwa mafuta wake. Nimechukua maksai wa nani? Nimechukua punda wa nani? Ni nani nimepata kumdanganya? Ni nani nimepata kumwonea? Ni kutoka kwenye mkono wa nani nimepokea rushwa ili kunifanya nifumbe macho yangu? Kama nimefanya chochote katika hivi, mimi nitawarudishia.”

4 Wakajibu, “Hujatudanganya wala kutuonea. Hujapokea chochote kutoka kwenye mkono wa mtu awaye yote.”

5 Samweli akawaambia, “Bwanani shahidi juu yenu, pia mpakwa mafuta wake ni shahidi siku hii ya leo, kwamba hamkukuta chochote mkononi mwangu.”

Wakasema, “Yeye ni shahidi.”

6 Kisha Samweli akawaambia watu, “Bwanandiye alimchagua Mose na Aroni, na kuwaleta baba zenu akiwapandisha kutoka Misri.

7 Sasa basi, simameni hapa, kwa sababu nitakabiliana nanyi kwa ushahidi mbele zaBwanawa matendo yote ya haki yaliyofanywa naBwanakwenu na kwa baba zenu.

8 “Baada ya Yakobo kuingia Misri, walimliliaBwanakwa ajili ya msaada, nayeBwanaakawatuma Mose na Aroni, ambao waliwatoa baba zenu kutoka Misri na kuwakalisha mahali hapa.

9 “Lakini wakamsahauBwanaMungu wao, hivyo Mungu akawauza katika mkono wa Sisera, jemadari wa jeshi la Hazori na katika mikono ya Wafilisti na mfalme wa Moabu, ambaye alipigana dhidi yao.

10 WakamliliaBwanana kusema, ‘Tumetenda dhambi; tumemwachaBwanana kutumikia Mabaali na Maashtorethi. Lakini sasa tuokoe kutoka mikono ya adui zetu, nasi tutakutumikia.’

11 NdipoBwanaakawatuma Yerub-Baali,Baraka, Yefta na Samweli, naye akawaokoa kutoka mikononi mwa adui zenu kila upande, ili ninyi mpate kukaa salama.

12 “Lakini mlipomwona yule Nahashi mfalme wa Waamoni anakuja dhidi yenu, mliniambia, ‘Hapana, tunataka mfalme atutawale,’ hata ingawaBwanaMungu wenu alikuwa mfalme wenu.

13 Sasa huyu hapa ndiye mfalme mliyemchagua, yule mliyeomba; tazameni,Bwanaamemweka mfalme juu yenu.

14 Kama mkimchaBwanana kumtumikia na kumtii nanyi msipoasi dhidi ya amri zake, ninyi pamoja na mfalme anayetawala juu yenu mkimfuataBwana, Mungu wenu, mambo yatakuwa mema kwenu!

15 Lakini kama hamkumtiiBwana, nanyi kama mkiasi dhidi ya amri zake, mkono wake utakuwa dhidi yenu, kama ulivyokuwa dhidi ya baba zenu.

16 “Sasa basi, simameni kimya mkaone jambo hili kubwa ambaloBwanaanakwenda kulifanya mbele ya macho yenu!

17 Je, sasa si mavuno ya ngano? NitamwombaBwanaili alete ngurumo na mvua. Nanyi mtatambua jambo hili lilivyo baya mlilolifanya mbele za macho yaBwanamlipoomba mfalme.”

18 Kisha Samweli akamwombaBwana, na siku ile ileBwanaakatuma ngurumo na mvua. Hivyo watu wote wakamwogopa sanaBwanana Samweli.

19 Watu wote wakamwambia Samweli, “MwombeBwanaMungu wako kwa ajili ya watumishi wako, ili tusije tukafa, kwa kuwa tumeongeza uovu juu ya dhambi zetu nyingine kwa kuomba mfalme.”

20 Samweli akajibu, “Msiogope, mmefanya uovu huu wote; hata hivyo msimwacheBwana, bali mtumikieniBwanakwa moyo wenu wote.

21 Msigeukie sanamu zisizofaa. Haziwezi kuwatendea jema, wala haziwezi kuwaokoa kwa sababu hazina maana.

22 Kwa ajili ya jina lake kuuBwanahatawakataa watu wake, kwa sababu ilimpendezaBwanakuwafanya kuwa wake mwenyewe.

23 Kwa habari yangu, iwe mbali nami kutenda dhambi dhidi yaBwanakwa kushindwa kuwaombea. Mimi nitawafundisha njia iliyo njema na ya kunyooka.

24 Lakini hakikisheni mnamchaBwanana kumtumikia kwa uaminifu kwa moyo wenu wote; tafakarini mambo makubwa aliyoyatenda kwa ajili yenu.

25 Hata hivyo mkiendelea kufanya uovu, ninyi na mfalme wenu mtafutiliwa mbali!”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1SA/12-3d7adcdded84140c77aa14094ce7e3b8.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Samweli

1 Samweli 13

Samweli Amkemea Sauli

1 Sauli alikuwa na miaka thelathini, alipokuwa mfalme, akatawala Israeli miaka arobaini na miwili.

2 Sauli alichagua watu 3,000 kutoka Israeli; miongoni mwa hao watu 2,000 walikuwa pamoja naye huko Mikmashi na katika nchi ya vilima ya Betheli, nao watu 1,000 walikuwa pamoja na Yonathani huko Gibea ya Benyamini. Watu waliosalia aliwarudisha nyumbani mwao.

3 Yonathani akashambulia ngome ya Wafilisti huko Geba, nao Wafilisti wakapata habari hizo. Kisha Sauli akaamuru tarumbeta ipigwe nchi yote na kusema, “Waebrania na wasikie!”

4 Hivyo Israeli wote wakasikia habari kwamba: “Sauli ameshambulia ngome ya Wafilisti, nao sasa Israeli wamekuwa harufu mbaya kwa Wafilisti.” Basi watu waliitwa kuungana na Sauli huko Gilgali.

5 Wafilisti wakakusanyika ili kupigana na Israeli, wakiwa na magari ya vita 3,000, waendesha magari ya vita 6,000 na askari wa miguu wengi kama mchanga wa ufuoni mwa bahari. Walipanda na kupiga kambi huko Mikmashi, mashariki ya Beth-Aveni.

6 Watu wa Israeli walipoona kuwa hali yao ni ya hatari na kuwa jeshi lao limesongwa sana, wakajificha katika mapango na katika vichaka, katikati ya miamba, kwenye mashimo na kwenye mahandaki.

7 Hata baadhi ya Waebrania wakavuka Yordani mpaka nchi ya Gadi na Gileadi.

Sauli akabaki huko Gilgali, navyo vikosi vyote vilivyokuwa pamoja naye vilikuwa vikitetemeka kwa hofu.

8 Akangoja kwa siku saba, muda uliowekwa na Samweli; lakini Samweli hakuja Gilgali, nao watu wa Sauli wakaanza kutawanyika.

9 Basi akasema, “Nileteeni hapa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani.” Naye Sauli akatoa sadaka ya kuteketezwa.

10 Mara alipomaliza kutoa hiyo sadaka, Samweli akatokea, naye Sauli akaondoka kwenda kumlaki.

11 Samweli akamuuliza, “Umefanya nini?”

Sauli akajibu, “Nilipoona kwamba watu wanatawanyika, na kwamba hukuja wakati uliopangwa na kwamba Wafilisti walikuwa wakikusanyika huko Mikmashi,

12 nikawaza, ‘Sasa Wafilisti watateremka dhidi yangu huko Gilgali nami sijaomba kibali kwaBwana.’ Hivyo nikalazimika kutoa sadaka ya kuteketezwa.”

13 Samweli akasema, “Umetenda kwa upumbavu. Hukuyashika maagizo yaBwanaMungu wako aliyokupa. Kama ungelitii, angeudumisha ufalme wako juu ya Israeli kwa wakati wote.

14 Lakini sasa ufalme wako hautadumu;Bwanaamemtafuta mtu aupendezaye moyo wake, na amemchagua awe kiongozi wa watu wake, kwa sababu hukuyatii maagizo yaBwana.”

15 Kisha Samweli akaondoka Gilgali, akapanda Gibea ya Benyamini, naye Sauli akawahesabu watu aliokuwa nao. Jumla yao walikuwa watu 600.

Israeli Bila Silaha

16 Sauli, mwanawe Yonathani na watu waliokuwa pamoja nao walikuwa wakiishi huko Gibea ya Benyamini, wakati Wafilisti wakiwa wamepiga kambi huko Mikmashi.

17 Makundi ya wavamiaji walikuja kutoka kambi ya Wafilisti katika vikosi vitatu. Kikosi kimoja kilielekea Ofra karibu na Shuali,

18 kikosi kingine kilielekea Beth-Horoni, nacho kikosi cha tatu kilielekea kwenye nchi ya mpakani ielekeayo Bonde la Seboimu linalotazamana na jangwa.

19 Hapakuwa na mhunzi ambaye angeweza kupatikana katika nchi yote ya Israeli, kwa sababu Wafilisti walikuwa wamesema, “Waebrania wasije wakatengeneza panga au mikuki!”

20 Hivyo Waisraeli wote huteremka kwa Wafilisti ili kunoa majembe ya plau, majembe ya mkono, mashoka na miundu.

21 Bei ilikuwa fedha theluthi mbili za shekelikunoa majembe ya plau na majembe ya mkono, na theluthi moja ya shekelikwa nyuma, mashoka na michokoo.

22 Kwa hiyo siku ya vita hakuna askari yeyote aliyekuwa kambini na Sauli na Yonathani ambaye alikuwa na upanga wala mkuki mkononi mwake; Sauli tu na mwanawe Yonathani ndio waliokuwa navyo.

Yonathani Awashambulia Wafilisti

23 Basi kikosi cha Wafilisti kilikuwa kimetoka kuelekea njia iendayo Mikmashi.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1SA/13-5f3b1c4d79870f43961422b9b508a4d9.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Samweli

1 Samweli 14

1 Siku moja Yonathani mwana wa Sauli akamwambia kijana mbeba silaha wake, akasema, “Njoo, tuwavukie Wafilisti kwenye doria upande ule mwingine.” Lakini hakumwambia baba yake.

2 Sauli alikuwa akikaa kwenye viunga vya Gibea chini ya mkomamanga huko Migroni. Alikuwa pamoja na watu kama 600,

3 miongoni mwao alikuwepo Ahiya, ambaye alikuwa amevaa kisibau. Alikuwa mwana wa Ikabodi, nduguye Ahitubu mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani waBwanahuko Shilo. Hakuna yeyote aliyekuwa na habari kwamba Yonathani alikuwa ameondoka.

4 Kila upande wa njia ambayo Yonathani alikusudia kupita ili kuvuka kufikia doria ya Wafilisti kulikuwepo na jabali; moja lilikuwa linaitwa Bosesi, na jingine Sene.

5 Jabali moja lilisimama kaskazini kuelekea Mikmashi na jingine upande wa kusini kuelekea Geba.

6 Yonathani akamwambia kijana wake mbeba silaha, “Njoo, tuvukie doria ya wale jamaa wasiotahiriwa. HuendaBwanaatatenda kwa ajili yetu. Hakuna chochote kitakachoweza kumzuiaBwanakuokoa, kwamba ni kwa wingi au kwa uchache.”

7 Mbeba silaha wake akamwambia, “Fanya yale yote uliyo nayo katika moyo wako. Songa mbele; moyo wangu na roho yangu viko pamoja nawe.”

8 Yonathani akasema, “Basi njoo; tutavuka kuwaelekea hao watu na kuacha watuone.

9 Kama wakituambia, ‘Subirini hapo mpaka tuje kwenu,’ tutakaa pale tulipo na hatutakwea kwao.

10 Lakini kama watasema, ‘Pandeni mje kwetu,’ tutakwea, kwa sababu hiyo itakuwa ishara yetu kwambaBwanaamewatia mikononi mwetu.”

11 Basi wote wawili wakajionyesha kwa doria ya Wafilisti. Wafilisti wakasema, “Tazama! Waebrania wanatambaa toka mashimoni walimokuwa wamejificha.”

12 Watu wa kwenye doria wakawapigia kelele Yonathani na mbeba silaha wake, wakisema, “Njooni, pandeni kwetu nasi tutawakomesha.”

Basi Yonathani akamwambia mbeba silaha wake, “Panda nyuma yangu;Bwanaamewatia mikononi mwa Israeli.”

13 Yonathani akapanda juu, akitumia mikono yake na miguu, pamoja na mbeba silaha wake papo hapo nyuma yake. Wafilisti wakaanguka mbele ya Yonathani, naye mbeba silaha wake akamfuata akiwaua nyuma yake.

14 Katika hilo shambulio la kwanza, Yonathani na mbeba silaha wake waliua kama watu ishirini kwenye eneo kama la nusu eka.

Israeli Wawafukuza Wafilisti

15 Kisha fadhaa ikawapata jeshi lote, wale waliokuwa kambini na shambani, wale waliokuwa katika doria na makundi ya washambuliaji, nayo nchi ilitetemeka. Ilikuwa ni hofu ya ghafula iliyotumwa na Mungu.

16 Wapelelezi wa Sauli huko Gibea ya Benyamini wakaona jeshi likitokomea pande zote.

17 Ndipo Sauli akawaambia watu wale waliokuwa pamoja naye, “Kagueni jeshi mkaone ni nani ameondoka katikati yetu.” Walipokagua, akawa ni Yonathani na mbeba silaha wake ambao hawakuwepo.

18 Sauli akamwambia Ahiya, “Leta Sanduku la Mungu.” (Wakati huo lilikuwa kwa Waisraeli.)

19 Wakati Sauli alipokuwa akisema na kuhani, makelele katika kambi ya Wafilisti yakaongezeka zaidi na zaidi. Hivyo Sauli akamwambia kuhani, “Rudisha mkono wako.”

20 Kisha Sauli na watu wake wote wakakusanyika na kwenda vitani. Wakawakuta Wafilisti wakiwa wamechanganyikiwa kabisa, wakitiana panga kila mmoja na wenzake.

21 Wale Waebrania ambao walishakuwa pamoja na Wafilisti, na waliokuwa wamepanda pamoja nao katika kambi zao, wakaenda upande wa Waisraeli waliokuwa pamoja na Sauli na Yonathani.

22 Waisraeli wote waliokuwa wamejificha katika nchi ya milima ya Efraimu waliposikia kuwa Wafilisti wamekimbia, wakajiunga vitani na kuwafuata kwa bidii.

23 HivyoBwanaakawaokoa Waisraeli siku ile, navyo vita vilienea hadi kupita Beth-Aveni.

Yonathani Ala Asali

24 Basi watu wa Israeli walikuwa katika dhiki siku ile, kwa sababu Sauli alikuwa amewafunga watu kwa kiapo, akisema, “Alaaniwe mtu yeyote ambaye atakula chakula kabla ya jioni, kabla sijalipiza kisasi juu ya adui zangu!” Kwa hiyo hakuna mtu yeyote katika jeshi aliyeonja chakula.

25 Jeshi lote liliingia mwituni, na huko kulikuwepo na asali ardhini.

26 Walipoingia mwituni, wakaona asali ikitiririka, hata hivyo hakuna mtu yeyote aliyetia mkono wake kinywani, kwa sababu waliogopa kiapo.

27 Lakini Yonathani alikuwa hajasikia kuwa baba yake alikuwa amewafunga watu kwa kiapo, hivyo akainyoosha ncha ya fimbo iliyokuwa mkononi mwake na kuichovya katika sega la asali. Akainua mkono wake na kuutia kinywani mwake, nayo macho yake yakawa maangavu.

28 Kisha mmoja wa askari wake akamwambia, “Baba yako alilifunga jeshi kwa kiapo kikali, akisema, ‘Alaaniwe mtu yeyote alaye chakula leo!’ Ndiyo sababu watu wanalegea.”

29 Yonathani akasema, “Baba yangu ameitaabisha nchi. Ona jinsi nilivyopata nguvu mpya nilipoonja asali hii kidogo.

30 Ingekuwa bora zaidi mara ngapi kama watu wangalikula leo baadhi ya nyara walizoteka kutoka kwa adui zao. Je, mauaji ya Wafilisti yasingekuwa makubwa zaidi?”

31 Siku ile baada ya Waisraeli kuwaua Wafilisti kutoka Mikmashi mpaka Aiyaloni, walikuwa wamechoka.

32 Watu wakarukia zile nyara, wakichukua kondoo, ngʼombe na ndama, wakawachinja hapo juu ya nchi na kuwala, pamoja na damu.

33 Kisha mtu mmoja akamwambia Sauli, “Tazama, watu wanatenda dhambi dhidi yaBwanakwa kula nyama yenye damu.”

Akasema, “Mmevunja uaminifu. Livingirisheni jiwe kubwa hapa mara moja.”

34 Kisha Sauli akasema, “Nendeni miongoni mwa watu, mwaambie, ‘Kila mmoja wenu aniletee ngʼombe wake na kondoo, mwachinjie hapa na mle. Msitende dhambi dhidi yaBwanakwa kula nyama ikiwa na damu ndani yake.’ ”

Hivyo kila mmoja akaleta ngʼombe wake jioni ile na kumchinja hapo.

35 Ndipo Sauli akamjengeaBwanamadhabahu, na ndiyo ilivyokuwa mara yake ya kwanza kujenga madhabahu.

36 Sauli akasema, “Tuteremke tufuatie Wafilisti usiku na kuwateka nyara mpaka mapambazuko, nasi tusiache hata mmoja wao hai.”

Wakajibu, “Fanya lolote lile uonalo jema zaidi kwako.”

Lakini kuhani akasema, “Tuulize kwa Mungu mahali hapa.”

37 Basi Sauli akamuuliza Mungu, akisema, “Je, niteremke kuwafuatia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwa Israeli?” Lakini Mungu hakumjibu siku ile.

38 Kwa hiyo Sauli akasema, “Njooni hapa, ninyi nyote ambao ni viongozi wa jeshi, na tutafute ni dhambi gani imefanywa leo.

39 Kwa hakika kamaBwanaaiokoaye Israeli aishivyo, hata kama itakuwa juu ya mwana wangu Yonathani, ni lazima afe.” Lakini hakuna mtu yeyote aliyesema neno.

40 Kisha Sauli akawaambia Waisraeli wote, “Ninyi simameni huko; mimi na mwanangu Yonathani tutasimama hapa.”

Watu wakajibu, “Fanya lile unaloona jema zaidi kwako.”

41 Kisha Sauli akamwombaBwana, Mungu wa Israeli, akisema, “Nipe jibu lililo sawa.” Yonathani na Sauli wakatolewa kwa kura, nao watu wakawa salama.

42 Sauli akasema, “Pigeni kura kati yangu na mwanangu Yonathani.” Kura ikamwangukia Yonathani.

43 Basi Sauli akamwambia Yonathani, “Niambie ni nini ulichokifanya.”

Hivyo Yonathani akamwambia, “Nilionja tu asali kidogo kwa ncha ya fimbo yangu. Je, sasa ni lazima nife?”

44 Sauli akasema, “Mungu na anishughulikie kwa ukali zaidi kama wewe Yonathani hutakufa.”

45 Lakini watu wakamwambia Sauli, “Je, Yonathani atakufa, yeye ambaye ameleta wokovu huu mkubwa Israeli? Hasha! Hakika kamaBwanaaishivyo, hakuna hata unywele wa kichwa chake utakaoanguka juu ya ardhi, kwa kuwa alifanya jambo hili leo kwa msaada wa Mungu.” Basi watu wakamwokoa Yonathani, wala hakuuawa.

46 Kisha Sauli akaacha kuwafuata Wafilisti, nao wakajiondoa na kurudi katika nchi yao.

47 Baada ya Sauli kujitwalia utawala katika Israeli, alipigana dhidi ya adui zake kila upande: Moabu, Waamoni, Edomu, wafalme wa Soba, na Wafilisti. Popote alipogeukia, aliwashinda.

48 Akapigana kishujaa na kuwashinda Waamaleki, akiikomboa Israeli kutoka mikono ya wale waliokuwa wamewateka nyara.

Jamaa Ya Sauli

49 Wana wa Sauli walikuwa Yonathani, Ishvi na Malki-Shua. Jina la binti yake mkubwa lilikuwa Merabu, naye mdogo aliitwa Mikali.

50 Jina la mkewe Sauli aliitwa Ahinoamu binti wa Ahimaasi. Jina la jemadari wa jeshi la Sauli aliitwa Abneri mwana wa Neri, naye Neri alikuwa babaye mdogo Sauli.

51 Babaye Sauli yaani, Kishi na Neri baba yake Abneri walikuwa wana wa Abieli.

52 Siku zote za utawala wa Sauli zilikuwa za vita vikali dhidi ya Wafilisti, na wakati wowote Sauli alimwona mtu mwenye nguvu au shujaa, alimchukua kwa utumishi wake.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1SA/14-55a7bac9810ae3dd74f8b23d12b13b31.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Samweli

1 Samweli 15

Bwana Anamkataa Sauli Asiwe Mfalme

1 Samweli akamwambia Sauli, “Mimi ndiye ambayeBwanaalinituma nikutie mafuta uwe mfalme juu ya watu wake Israeli, basi sasa sikiliza ujumbe kutoka kwaBwana.

2 Hili ndiloBwanaMwenye Nguvu Zote asemalo: ‘Nitawaadhibu Waamaleki kwa kile walichowatendea Israeli walipowavizia wakati walipanda kutoka Misri.

3 Basi sasa nenda ukawashambulie Waamaleki na kuwaangamiza kabisa pamoja na kila kitu kilicho mali yao. Usiwahurumie; waue wanaume na wanawake, watoto na wanyonyao, ngʼombe na kondoo, ngamia na punda.’ ”

4 Ndipo Sauli akawaita watu na kuwapanga huko Telaimu, askari wa miguu 200,000 pamoja na watu 10,000 kutoka Yuda.

5 Sauli akaenda katika mji wa Amaleki na kuwavizia bondeni.

6 Kisha akawaambia Wakeni, “Ondokeni, waacheni Waamaleki ili nisije nikawaangamiza ninyi pamoja nao, kwa kuwa ninyi mliwatendea mema Waisraeli wote wakati walipanda kutoka Misri.” Basi Wakeni wakaondoka, wakawaacha Waamaleki.

7 Ndipo Sauli akawashambulia Waamaleki toka Havila mpaka Shuri, hadi mashariki ya Misri.

8 Akamchukua Agagi, mfalme wa Waamaleki akiwa hai, nao watu wake wote akawaangamiza kabisa kwa upanga.

9 Lakini Sauli na hilo jeshi wakamhifadhi hai Agagi na kondoo na ngʼombe walio wazuri, mafahali na wana-kondoo walionona kila kitu kilichokuwa kizuri. Hivi vitu hawakuwa radhi kuviangamiza kabisa, bali kila kitu kilichodharauliwa na kilicho dhaifu wakakiangamiza kabisa.

10 Kisha neno laBwanalikamjia Samweli kusema:

11 “Ninasikitika kwamba nimemfanya Sauli kuwa mfalme, kwa sababu ameacha kunifuata mimi na hakutimiza maagizo yangu.” Samweli akafadhaika, naye akamliliaBwanausiku ule wote.

12 Asubuhi na mapema Samweli akaamka kwenda kukutana na Sauli, lakini akaambiwa, “Sauli amekwenda Karmeli. Huko amesimamisha mnara kwa heshima yake mwenyewe naye ameendelea na kuteremkia Gilgali.”

13 Samweli alipomfikia, Sauli akamwambia, “Bwanaakubariki! Nimetimiza yaleBwanaaliniagiza.”

14 Lakini Samweli akasema, “Nini basi huu mlio wa kondoo masikioni mwangu? Huu mlio wa ngʼombe ninaousikia ni kitu gani?”

15 Sauli akajibu, “Askari wamewaleta kutoka kwa Waamaleki, waliwaacha wale kondoo na ngʼombe wazuri ili kuwatoa dhabihu kwaBwana, Mungu wako, lakini tuliwaangamiza kabisa wengine wote.”

16 Samweli akamwambia Sauli, “Ngoja! Nami nitakuambia lileBwanaaliloniambia usiku huu.”

Sauli akajibu, “Niambie.”

17 Samweli akamwambia, “Ingawa zamani ulijiona mdogo machoni pako mwenyewe, Je, hukuwa kiongozi wa kabila za Israeli?Bwanaalikutia mafuta kuwa mfalme juu ya Israeli.

18 Naye akakutuma kwa kazi maalum, akisema, ‘Nenda ukaangamize kabisa wale watu waovu, wale Waamaleki, upigane nao vita mpaka utakapowaangamiza kabisa.’

19 Kwa nini hukumtiiBwana? Kwa nini ulivamia nyara na kufanya uovu machoni paBwana?”

20 Sauli akasema, “Lakini nilimtiiBwana. Nilikamilisha ile kazi ambayoBwanaalinituma. Niliwaangamiza Waamaleki kabisa na kumleta Agagi mfalme wao.

21 Askari walichukua kondoo na ngʼombe kutoka kwenye nyara, zile ambazo ni nzuri sana zimewekwa wakfu kwa Mungu, ili zitolewe dhabihu kwaBwanaMungu wako huko Gilgali.”

22 Lakini Samweli akajibu:

“Je,Bwanaanafurahia sadaka za kuteketezwa na dhabihu

kama vile kuitii sauti yaBwana?

Kutii ni bora zaidi kuliko dhabihu,

nako kusikia ni bora

kuliko mafuta ya kondoo dume.

23 Kwa maana kuasi ni kama dhambi ya uaguzi,

nao ukaidi ni kama uovu wa kuabudu sanamu.

Kwa sababu umelikataa neno laBwana,

naye amekukataa wewe

kuendelea kuwa mfalme.”

24 Ndipo Sauli akamwambia Samweli, “Nimetenda dhambi. Nimevunja amri yaBwanana maagizo yako. Niliwaogopa watu na kwa hiyo nikafanya walivyotaka.

25 Sasa ninakusihi usamehe dhambi yangu, nawe urudi pamoja nami, ili nipate kumwabuduBwana.”

26 Lakini Samweli akamwambia, “Sitarudi pamoja nawe. Umelikataa neno laBwana, nayeBwanaamekukataa wewe, usiendelee kuwa mfalme juu ya Israeli!”

27 Samweli alipogeuka ili aondoke, Sauli akangʼangʼania pindo la joho lake, nalo likararuka.

28 Samweli akamwambia, “Bwanaameurarua ufalme wa Israeli kutoka kwako leo, naye ameutia kwa mmoja wa majirani zako, aliye bora kuliko wewe.

29 Yeye aliye Utukufu wa Israeli hasemi uongo wala hana kigeugeu; kwa kuwa yeye si mwanadamu, hata abadili nia yake.”

30 Sauli akajibu, “Nimetenda dhambi. Lakini tafadhali niheshimu mbele ya wazee wa watu wangu na mbele ya Israeli; rudi pamoja nami, ili nipate kumwabuduBwanaMungu wako.”

31 Hivyo Samweli akarudi pamoja na Sauli, naye Sauli akamwabuduBwana.

32 Ndipo Samweli akasema, “Niletee Agagi mfalme wa Waamaleki.”

Agagi akaja kwake kwa ujasiri, akifikiri, “Hakika uchungu wa mauti umepita.”

33 Lakini Samweli akasema,

“Kama upanga wako ulivyofanya wanawake

kufiwa na watoto wao,

ndivyo mama yako atakavyokuwa

hana mtoto miongoni mwa wanawake.”

Naye Samweli akamuua Agagi mbele zaBwanahuko Gilgali.

34 Kisha Samweli akaenda Rama, lakini Sauli akapanda nyumbani kwake huko Gibea ya Sauli.

35 Hadi siku Samweli alipofariki hakwenda kumwona Sauli tena, ingawa Samweli alimwombolezea. NayeBwanaalihuzunika kwamba alimfanya Sauli kuwa mfalme juu ya Israeli.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1SA/15-d85ba7ed12adc5f74311c7e833e73f25.mp3?version_id=1627—