Categories
Waamuzi

Waamuzi 13

Kuzaliwa Kwa Samsoni

1 Waisraeli wakafanya maovu tena mbele zaBwana. HivyoBwanaakawatia mikononi mwa Wafilisti kwa muda wa miaka arobaini.

2 Basi palikuwa na mtu mmoja wa Sora, aliyeitwa Manoa, wa kabila la Wadani, naye alikuwa na mke ambaye alikuwa tasa na hakuwa na mtoto.

3 Malaika waBwanaakamtokea huyo mwanamke na kumwambia, “Wewe ni tasa na huna mtoto, lakini utachukua mimba na utamzaa mtoto mwanaume.

4 Lakini ujihadhari sana usinywe mvinyo wala kileo kingine chochote, wala usile kitu chochote kilicho najisi,

5 kwa kuwa utachukua mimba na utamzaa mtoto mwanaume. Wembe usipite kichwani pake, kwa kuwa huyo mwana atakuwa Mnadhiri wa Mungu, aliyewekwa wakfu kwa ajili ya Mungu tangu tumboni mwa mama yake, naye ataanza kuwaokoa Waisraeli kutoka mikononi mwa Wafilisti.”

6 Ndipo huyo mwanamke akamwendea mumewe na kumweleza kuwa, “Mtu wa Mungu alinijia. Kule kuonekana kwake kulikuwa kama kwa malaika wa Mungu, wa kutisha sana. Sikumuuliza alikotoka wala hakuniambia jina lake.

7 Lakini aliniambia, ‘Utachukua mimba na utazaa mtoto mwanaume. Basi sasa, usinywe mvinyo wala kileo kingine chochote wala usile kitu kilicho najisi, kwa kuwa huyo mtoto atakuwa Mnadhiri wa Mungu tangu tumboni mwa mama yake mpaka kufa kwake.’ ”

8 Ndipo Manoa akamwombaBwana, akasema: “Ee Bwana, nakusihi, huyo mtu wa Mungu uliyemtuma kwetu aje tena ili atufundishe jinsi ya kumlea huyo mwana atakayezaliwa.”

9 Mungu akamsikia Manoa, naye malaika wa Mungu akamjia tena huyo mwanamke alipokuwa shambani, lakini mumewe Manoa hakuwepo.

10 Basi yule mwanamke akaenda haraka na kumwambia mumewe, “Tazama mtu yule aliyenitokea siku ile yupo hapa!”

11 Manoa akainuka akaandamana na mkewe. Alipomfikia yule mtu akamuuliza, “Je, wewe ndiye yule uliyesema na mke wangu?”

Akasema, “Mimi ndiye.”

12 Basi Manoa akamuuliza, “Wakati maneno yako yatakapotimia, masharti ya maisha ya mtoto huyu yatakuwa nini na kazi yake itakuwa ni nini?”

13 Malaika waBwanaakamjibu, “Mke wako hana budi kufanya yale yote niliyomwambia.

14 Kamwe asile kitu chochote kitakachotoka katika mzabibu, wala asinywe mvinyo wa aina yoyote wala kileo chochote wala asile kitu chochote kilicho najisi. Hana budi kufanya kila kitu nilichomwagiza.”

15 Manoa akamjibu yule malaika waBwana, “Twakuomba usubiri kwanza ili tuweze kuandaa mwana-mbuzi kwa ajili yako.”

16 Malaika waBwanaakamjibu, “Hata kama utanizuia, sitakula chochote kwako. Lakini ukitaka kuandaa sadaka ya kuteketezwa, mtoleeBwanahiyo sadaka.” (Kwa kuwa Manoa hakujua kuwa alikuwa malaika waBwana.)

17 Ndipo Manoa akamuuliza yule malaika waBwana, “Jina lako ni nani, ili kwamba tuweze kukupa heshima hapo hayo uliyonena yatakapotimia?”

18 Akamjibu, “Kwa nini unauliza Jina langu? Ni Jina la ajabu.”

19 Ndipo Manoa akamchukua mwana-mbuzi, pamoja na sadaka ya unga, naye akamtoleaBwanadhabihu hapo juu ya mwamba. Naye yule malaika waBwanaakafanya jambo la ajabu wakati Manoa na mkewe wakiwa wanaangalia:

20 Mwali wa moto kutoka hapo madhabahuni ulipowaka kuelekea mbinguni, malaika waBwanaakapaa ndani ya huo mwali. Manoa na mkewe, kwa kuona jambo hili, wakaanguka chini kifudifudi.

21 Malaika waBwanahakumtokea tena Manoa na mkewe. Ndipo Manoa akatambua kuwa huyo alikuwa malaika waBwana.

22 Manoa akamwambia mkewe, “Hakika tutakufa, kwa kuwa tumemwona Mungu.”

23 Lakini mkewe akamwambia, “IkiwaBwanaalikuwa amekusudia kutuua, asingelipokea sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya unga kutoka mikononi mwetu, wala asingelituonyesha mambo haya yote wala kututangazia mambo kama haya wakati huu.”

24 Yule mwanamke akazaa mtoto wa kiume akamwita jina lake Samsoni. Kijana akakua, nayeBwanaakambariki.

25 Roho waBwanaakaanza kumsukuma wakati alipokuwa huko Mahane-Dani, kati ya Sora na Eshtaoli.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JDG/13-e557ecacc6155f6b16ba1881e68206c8.mp3?version_id=1627—

Categories
Waamuzi

Waamuzi 14

Ndoa Ya Samsoni

1 Samsoni akateremkia Timna, akamwona mwanamke wa Kifilisti.

2 Alipopanda kutoka huko, akawaambia baba yake na mama yake, “Nimemwona mwanamke wa Kifilisti huko Timna; basi mnipe ili awe mke wangu.”

3 Baba yake na mama yake wakamjibu, “Je, hakuna mwanamke miongoni mwa jamaa yako au miongoni mwa ndugu zako, hata ulazimike kwenda kujitwalia mwanamke kutoka kwa hawa Wafilisti wasiotahiriwa?”

Lakini Samsoni akamwambia baba yake, “Nipatieni huyo kwa maana ndiye alinipendeza.”

4 (Baba yake na mama yake hawakujua kuwa jambo hili limetoka kwaBwana, kwani alikuwa akitafuta sababu ya kukabiliana na Wafilisti; kwa kuwa wakati huo walikuwa wakiwatawala Waisraeli.)

5 Samsoni akateremkia Timna pamoja na baba yake na mama yake. Walipofika kwenye mashamba ya mizabibu huko Timna, ghafula mwana simba akamjia akimngurumia.

6 Roho waBwanaakaja juu yake kwa nguvu, naye akampasua yule simba kwa mikono yake bila silaha yoyote kama vile mtu ampasuavyo mwana-mbuzi, wala hakumwambia baba yake wala mama yake aliyoyafanya.

7 Basi akateremka na kuongea na yule mwanamke, naye akampendeza Samsoni.

8 Baada ya muda aliporudi ili akamwoe, akatazama kando ili kuutazama mzoga wa yule simba, na tazama, kulikuwa na kundi la nyuki ndani ya ule mzoga wa simba na kulikuwa na asali;

9 akachukua asali mkononi mwake akaendelea huku akila. Alipowafikia baba yake na mama yake, akawapa ile asali nao wakala. Lakini hakuwaambia kuwa alitwaa asali kutoka kwenye mzoga wa simba.

10 Basi baba yake akateremka kumwona huyo mwanamke. Samsoni akafanya karamu huko, kama ilivyokuwa desturi ya vijana.

11 Watu walipomwona, wakaleta vijana wenzake thelathini ili kuwa pamoja naye.

12 Samsoni akawaambia, “Niwape kitendawili, mkiweza kunipa jibu katika muda wa siku hizi saba za karamu, nitawapa mavazi thelathini ya kitani na mavazi mengine mivao thelathini.

13 Lakini msipoweza kufumbua, ndipo ninyi mtanipa mavazi thelathini ya kitani na mavazi mengine mivao thelathini.”

Wakamwambia, “Tuambie hicho kitendawili, hebu na tukisikie.”

14 Akawaambia,

“Ndani ya mlaji,

kulitoka kitu cha kuliwa,

ndani ya mwenye nguvu,

kulitoka kitu kitamu.”

Kwa muda wa siku tatu hawakuweza kutoa jibu.

15 Siku ya saba, wakamwambia mkewe Samsoni, “Mbembeleze mumeo ili atueleze hicho kitendawili, la sivyo tutakuchoma moto wewe na wa nyumba ya baba yako. Je, mmetualika ili mpate kutunyangʼanya kile tulicho nacho?”

16 Basi mke wa Samsoni akalia mbele yake na kumwambia, “Unanichukia! Hunipendi kabisa. Umewategea watu wangu kitendawili, lakini mimi hujaniambia jibu.”

Samsoni akamwambia, “Wala sijamweleza baba yangu wala mama yangu, kwa nini nikufumbulie?”

17 Mkewe akalia kwa muda wa zile siku zote saba za karamu. Hivyo siku ile ya saba Samsoni akamweleza, kwa kuwa aliendelea kumsisitiza sana. Naye akawaeleza watu wake kile kitendawili.

18 Siku ya saba kabla ya jua kutua, watu wa mji wakamwambia Samsoni,

“Ni nini kitamu kama asali?

Ni nini chenye nguvu kama simba?”

Samsoni akawaambia,

“Kama hamkulima na mtamba wangu,

hamngeweza kufumbua

kitendawili changu.”

19 Ndipo Roho waBwanaakamjia Samsoni kwa nguvu. Akateremka mpaka Ashkeloni, akawaua watu waume thelathini miongoni mwa watu wa mji, akatwaa mali zao na nguo zao, akawapa watu wale waliofumbua kile kitendawili. Akiwa na hasira, akakwea kurudi nyumbani kwa baba yake.

20 Lakini huyo mke wa Samsoni akakabidhiwa kwa rafiki yake Samsoni ambaye alikuwa rafiki yake msaidizi siku ya arusi.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JDG/14-f00323398b7a329eeb02a5786f25f398.mp3?version_id=1627—

Categories
Waamuzi

Waamuzi 15

Kisasi Cha Samsoni Kwa Wafilisti

1 Baada ya kitambo kidogo, wakati wa mavuno ya ngano, Samsoni akachukua mwana-mbuzi, kwenda kumzuru mkewe. Akasema, “Nataka kuingia chumbani kwa mke wangu.” Lakini baba yake huyo mwanamke hakumruhusu kuingia.

2 Huyo baba mkwe wake akamwambia, “Nilikuwa na hakika kwamba ulimkataa, hivyo mimi nikampa rafiki yako. Je, mdogo wake wa kike si mzuri zaidi kuliko yeye? Mchukue huyo badala yake.”

3 Samsoni akawaambia, “Wakati huu, nitakapowadhuru Wafilisti, sitakuwa na lawama.”

4 Hivyo Samsoni akatoka akawakamata mbweha 300 na kuwafunga wawili wawili kwa mikia yao kila mmoja kwa mwingine. Kisha akafungia mwenge wa moto, kwenye mikia ya kila jozi moja ya mbweha aliyokuwa ameifunga,

5 akawasha ile mienge na kuwaachia wale mbweha katika mashamba ya Wafilisti ya nafaka zilizosimamishwa katika matita. Akateketeza matita ya nafaka zilizosimama, pamoja na mashamba ya mizabibu na viunga vya mizeituni.

6 Ndipo Wafilisti wakauliza, “Ni nani aliyetenda jambo hili?” Wakaambiwa, “Ni Samsoni, yule mkwewe Mtimna, kwa sababu alimchukua mkewe akampa mwenzake.”

Hivyo Wafilisti wakapanda wakamteketeza kwa moto yeye huyo mwanamke pamoja na baba yake.

7 Samsoni akawaambia, “Kwa kuwa mmetenda hivyo, hakika sitatulia mpaka niwe nimelipiza kisasi juu yenu.”

8 Akawashambulia kwa ukali kwa mapigo makuu na kuwaua watu wengi sana. Kisha akateremka na kukaa katika ufa kwenye mwamba wa Etamu.

9 Wafilisti wakapanda na kupiga kambi huko Yuda na kuenea huko Lehi.

10 Watu wa Yuda wakawauliza, “Kwa nini mmekuja kupigana nasi?”

Wakawajibu, “Tumekuja ili kumkamata Samsoni na kumtenda kama alivyotutendea.”

11 Ndipo watu 3,000 toka Yuda walipoteremka na kwenda kwenye ufa wa mwamba huko Etamu, na kumwambia Samsoni, “Je, hujatambua kuwa Wafilisti wanatutawala? Ni nini hiki ulichotutendea?”

Akawajibu, “Mimi nimewatendea tu kile walichonitendea.”

12 Wakamwambia, “Tumekuja kukufunga na kukutia mikononi mwa Wafilisti.”

Samsoni akawaambia, “Niapieni kuwa hamtaniua ninyi wenyewe.”

13 Wakamjibu, “Sisi hatutakuua, bali tutakufunga tu na kukutia mikononi mwao.” Basi wakamfunga kwa kamba mbili mpya. Wakamchukua toka huko kwenye ufa katika mwamba.

14 Alipokaribia Lehi, Wafilisti wakamjia wakipiga kelele. Roho waBwanaakamjia juu yake kwa nguvu. Kamba zilizomfunga mikono yake zikawa kama kitani iliyochomwa kwa moto, na vifungo vyake vikaanguka chini toka mikononi mwake.

15 Ndipo akaona mfupa mpya wa taya la punda, akanyoosha mkono, akauchukua na kuua nao Wafilisti wapatao 1,000.

16 Ndipo Samsoni akasema,

“Kwa taya la punda

malundo juu ya malundo.

Kwa taya la punda

nimeua watu 1,000.”

17 Alipomaliza kusema, akautupa ule mfupa wa taya; na mahali pale pakaitwa Ramath-Lehi.

18 Kwa kuwa alikuwa amesikia kiu sana, akamliliaBwanaakisema, “Umempa mtumishi wako ushindi huu mkuu. Je, sasa nife kwa kiu na kuangukia mikononi mwa hawa watu wasiotahiriwa?”

19 Bwanaakafunua shimo huko Lehi, pakatoka maji. Samsoni alipoyanywa, nguvu zikamrudia na kuhuika. Hivyo chemchemi ile ikaitwa En-Hakore,nayo iko mpaka leo huko Lehi.

20 Samsoni akawa mwamuzi wa Waisraeli katika siku za Wafilisti kwa muda wa miaka ishirini.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JDG/15-5084914edaac6c9703888ec24c8e2550.mp3?version_id=1627—

Categories
Waamuzi

Waamuzi 16

Samsoni Na Delila

1 Siku moja Samsoni alienda Gaza, akamwona mwanamke kahaba, naye akaingia kwake.

2 Watu wa Gaza wakaambiwa, “Samsoni amekuja huku!” Hivyo wakapazingira mahali pale nao wakamvizia usiku kucha, penye lango la mji. Wakanyamaza kimya usiku kucha, wakisema, “Tumvizie hadi mapambazuko, ndipo tutamuua.”

3 Samsoni akalala mpaka usiku wa manane. Akaondoka katikati ya usiku, akashika milango ya lango la mji pamoja na miimo yake miwili, akaingʼoa, makomeo yake na vyote. Akaviweka mabegani mwake na kuvipeleka mpaka kwenye kilele cha mlima ule unaokabili Hebroni.

4 Baada ya hayo akampenda mwanamke mmoja katika Bonde la Soreki aliyeitwa Delila.

5 Viongozi wa Wafilisti wakamwendea yule mwanamke na kumwambia, “Umbembeleze ili upate kujua siri za nguvu zake zilizo nyingi na jinsi tutakavyoweza kumshinda ili tuweze kumfunga na kumtiisha. Nasi kila mmoja wetu tutakupa shekeli 1,100 za fedha.”

6 Hivyo Delila akamwambia Samsoni, “Naomba niambie siri ya hizi nguvu zako nyingi na jinsi utakavyoweza kufungwa ili kukutiisha.”

7 Samsoni akamjibu, “Kama wakinifunga kwa kamba saba za upinde ambazo hazijakauka bado, hapo ndipo nitakapokuwa dhaifu kama mtu mwingine yeyote.”

8 Viongozi wa Wafilisti wakamletea yule mwanamke kamba saba za upinde ambazo hazijakauka bado, akamfunga nazo Samsoni.

9 Wakati watu wakiwa wanamvizia katika chumba cha ndani, yule mwanamke akamwambia, “Samsoni, Wafilisti wanakujia!” Lakini yeye akazikata zile kamba za upinde, kama vile uzi wa pamba unapoguswa na moto. Hivyo siri ya nguvu zake haikujulikana.

10 Ndipo Delila akamwambia Samsoni, “Umenifanyia mzaha na kuniambia uongo. Tafadhali niambie waweza kufungwa kwa kitu gani?”

11 Akamwambia, “Wakinifunga kwa uthabiti kwa kamba mpya ambazo hazijatumika, basi nitakuwa dhaifu kama mtu mwingine yeyote.”

12 Hivyo Delila akachukua kamba mpya na kumfunga nazo. Kisha akamwambia, “Samsoni, Wafilisti wanakujia!” Wale watu waliokuwa wanamvizia walikuwa katika chumba cha ndani. Lakini akazikata zile kamba zilizokuwa zimefunga mikono yake kama akatavyo uzi.

13 Ndipo Delila akamwambia Samsoni, “Mpaka sasa, umenifanyia mzaha na kuniambia uongo. Nieleze ni jinsi gani utakavyoweza kufungwa.”

Samsoni akamwambia, “Kama ukivisuka hivi vishungi saba vya nywele za kichwa changu katika mtande wa nguo na kukaza kwa msumari, ndipo nitakuwa dhaifu kama mtu mwingine yeyote.” Hivyo Samsoni alipokuwa amelala, Delila akachukua vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake na kuvifunga kwenye mtande wa nguo,

14 na kuvikaza kwa msumari.

Kisha akamwambia, “Samsoni, Wafilisti wanakujia!” Lakini akaamka kutoka usingizini na kuungʼoa ule msumari na ule mtande.

15 Ndipo Delila akamwambia, “Wawezaje kusema, ‘Nakupenda,’ wakati moyo wako haupo pamoja nami? Umenifanyia mzaha mara hizi tatu na hujaniambia siri ya hizi nguvu zako nyingi.”

16 Hatimaye, baada ya kuwa anamsumbua kwa maneno siku kwa siku na kumuudhi, roho yake ikataabika hata kufa.

17 Hivyo akamwambia yule mwanamke siri yake yote, akamwambia, “Wembe haujapita kamwe kichwani mwangu, kwa kuwa mimi ni Mnadhiri wa Mungu tangu tumboni mwa mama yangu. Kama nywele za kichwa changu zikinyolewa, nguvu zangu zitanitoka, na nitakuwa dhaifu kama mtu mwingine yeyote!”

18 Delila alipoona kuwa amemweleza siri yake yote, akatuma ujumbe kwa viongozi wa Wafilisti na kusema, “Njooni tena mara nyingine, maana amenieleza siri yake yote.” Basi viongozi wa Wafilisti wakaja kwa Delila, wakiwa na fedha mikononi mwao.

19 Delila akamfanya alale usingizi magotini pake, akamwita mtu akamnyoa vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake. Akaanza kumsumbua ili aamke nazo nguvu zake zikamtoka.

20 Yule mwanamke akamwita, “Samsoni, hao Wafilisti wanakujia!”

Akaamka toka usingizini akasema, “Nitatoka nje kama hapo awali, nitawakungʼutia mbali na kuwa huru.” Lakini hakujua kuwaBwanaamemwacha.

21 Basi Wafilisti wakamkamata, wakamngʼoa macho yake, wakamchukua wakamteremsha mpaka Gaza. Wakiwa wamemfunga kwa pingu za shaba, wakamweka ili asage ngano huko gerezani.

22 Wakati huo nywele za kichwa chake zikaanza kukua tena baada ya kunyolewa.

Kifo Cha Samsoni

23 Basi viongozi wa Wafilisti wakakusanyika pamoja ili kutoa kafara kwa mungu wao Dagoni na kufanya karamu, wakisema, “Mungu wetu amemtia adui yetu Samsoni mikononi mwetu.”

24 Watu walipomwona Samsoni wakamsifu mungu wao, wakisema:

“Sasa mungu wetu amemtia adui yetu

mikononi mwetu,

yule aliyeharibu nchi yetu

na kuwaua watu wengi miongoni mwetu.”

25 Mioyo yao ilipokuwa imefurahishwa wakasema, “Mleteni Samsoni aje acheze ili tufurahi.” Basi wakamleta Samsoni kutoka mle gerezani naye akacheza mbele yao.

Wakamweka kati ya nguzo mbili.

26 Samsoni akamwambia mtumishi aliyeshika mkono wake, “Niweke mahali ambapo ninaweza kuzigusa nguzo ambazo zinategemeza jengo ili nipate kuziegemea.”

27 Basi lile jengo lilikuwa na wingi wa watu waume kwa wake; viongozi wote wa Wafilisti walikuwamo humo, na kwenye sakafu ya juu walikuwepo watu 3,000 waume kwa wake, waliokuwa wakimtazama Samsoni wakati anacheza.

28 Ndipo Samsoni akamwombaBwana, akasema, “EeBwanaMwenyezi, unikumbuke. Ee Mungu, nakusihi ukanitie nguvu mara hii moja tena, ili kwa tendo hili nipate kulipiza kisasi juu ya Wafilisti kwa ajili ya macho yangu mawili.”

29 Ndipo Samsoni akazikaribia zile nguzo mbili za katikati ambazo lile jengo lilikuwa linazitegemea. Akazishika moja kwa mkono wa kuume na nyingine mkono wa kushoto.

30 Samsoni akasema, “Nife pamoja na Wafilisti!” Ndipo akazisukuma zile nguzo kwa nguvu zake zote, lile jengo likaanguka juu ya viongozi na watu wote waliokuwamo mle ndani yake. Hivyo akawaua watu wengi wakati wa kufa kwake kuliko siku za uhai wake.

31 Basi ndugu zake na jamaa yote ya baba yake wakateremka kwenda kumchukua. Wakampandisha na kumzika kati ya Sora na Eshtaoli kwenye kaburi la Manoa baba yake. Naye Samsoni alikuwa mwamuzi wa Israeli kwa miaka ishirini.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JDG/16-0f1e09e10fdf89f88c4b5ede579fc4fa.mp3?version_id=1627—

Categories
Waamuzi

Waamuzi 17

Sanamu Za Mika

1 Palikuwa na mtu aliyeitwa Mika ambaye aliishi katika vilima vya Efraimu.

2 Akamwambia mama yake, “Zile shekeli 1,100za fedha zilizochukuliwa kwako, ambazo nilisikia ukizinenea maneno ya laana, hizi hapa; mimi ndiye niliyezichukua, lakini sasa ninakurudishia.”

Ndipo mama yake akamwambia, “Bwanana akubariki, mwanangu.”

3 Alipozirudisha zile shekeli 1,100 za fedha kwa mama yake, mama yake akamwambia, “Mimi nimeiweka fedha hii wakfu kwaBwanakwa ajili ya mwanangu kutengenezea kinyago cha kuchonga na sanamu ya kusubu. Mimi nitakurudishia wewe.”

4 Hivyo akamrudishia mama yake ile fedha, naye mama yake akachukua shekeli mia mbiliza hiyo fedha na kumpa mfua fedha, ambaye aliifanyiza kinyago na sanamu. Navyo vikawekwa ndani ya nyumba ya Mika.

5 Basi Mika alikuwa na mahali pa kuabudia miungu, akatengeneza naivera, pamoja na vinyago, na kumweka mmoja wa wanawe kuwa kuhani wake.

6 Katika siku hizo Israeli hawakuwa na mfalme, kila mmoja akafanya kama alivyoona vyema machoni pake mwenyewe.

7 Basi palikuwa na kijana mmoja wa Bethlehemu ya Yuda. Yeye alikuwa Mlawi aliyeishi miongoni mwa kabila la Yuda.

8 Huyu kijana akatoka katika mji huo wa Bethlehemu ya Yuda na kutafuta mahali pengine ambapo angeweza kuishi. Alipokuwa akisafiri, akafika nyumbani kwa Mika katika vilima vya Efraimu.

9 Mika akamuuliza, “Wewe umetoka wapi?”

Akamjibu, “Mimi ni Mlawi kutoka Bethlehemu ya Yuda, ninatafuta mahali pa kuishi.”

10 Ndipo Mika akamwambia, “Ishi pamoja nami, uwe baba yangu na kuhani wangu, nami nitakupa shekeli kumiza fedha, nguo na chakula.”

11 Hivyo yule Mlawi akakubali kuishi pamoja naye, naye huyo kijana akawa kwake kama mmoja wa wanawe.

12 Hivyo Mika akamweka wakfu huyo kijana Mlawi, naye huyo akawa kuhani wake na kuishi nyumbani mwake.

13 Ndipo Mika akasema, “Sasa najuaBwanaatanitendea mema, kwa kuwa Mlawi huyu amekuwa kuhani wangu.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JDG/17-1dba4344808cfa00d629d9fde9480c04.mp3?version_id=1627—

Categories
Waamuzi

Waamuzi 18

Wadani Wahamia Laishi

1 Katika siku hizo Israeli walikuwa hawana mfalme.

Katika siku hizo kabila la Wadani walikuwa wanatafuta mahali pao wenyewe pa kuishi, kwa sababu walikuwa hawajafika kwenye urithi wao miongoni mwa makabila ya Israeli.

2 Hivyo Wadani wakatuma mashujaa watano kutoka Sora na Eshtaoli ili kupeleleza nchi na kuichunguza. Hawa watu waliwakilisha koo zao zote. Waliwaambia, “Nendeni mkaichunguze hiyo nchi.”

Watu hao wakaingia katika nchi ya vilima ya Efraimu, nao wakafika nyumba ya Mika, ambako walilala usiku huo.

3 Walipofika karibu na nyumba ya Mika, waliitambua sauti ya yule kijana Mlawi; hivyo wakaingia humo na kumuuliza, “Ni nani aliyekuleta hapa? Unafanya nini mahali hapa? Kwa nini uko hapa?”

4 Akawaeleza yale Mika aliyomtendea, naye akasema, “Ameniajiri nami ni kuhani wake.”

5 Kisha wakamwambia, “Tafadhali tuulizie kwa Mungu kama safari yetu itafanikiwa.”

6 Yule kuhani akawajibu, “Enendeni kwa amani. Safari yenu ina kibali chaBwana.”

7 Basi hao watu watano wakaondoka na kufika Laishi, mahali ambapo waliwakuta watu wanaishi salama, kama Wasidoni, kwa utulivu na bila mashaka. Nchi yao haikupungukiwa na kitu chochote, hivyo wakawa tajiri. Pia walikaa mbali sana na Wasidoni, wala hawakushughulika na mtu yeyote.

8 Waliporudi kwa ndugu zao huko Sora na Eshtaoli, ndugu zao wakawauliza, “Mlionaje mambo huko?”

9 Wakajibu, “Twendeni, tukapigane nao! Tumeona kuwa nchi ni nzuri sana. Je, hamtafanya chochote? Msisite kupanda ili kuimiliki.

10 Mtakapokwenda huko mtakuta watu waliotulia walio salama, nayo nchi hiyo ni kubwa na Mungu ameitia mikononi mwenu, nayo ni nchi ambayo haikupungukiwa na kitu chochote kilicho duniani.”

11 Ndipo watu 600 toka ukoo wa Wadani, waliojifunga silaha za vita, wakaondoka Sora na Eshtaoli.

12 Walipokuwa wakisafiri wakapiga kambi huko Kiriath-Yearimu katika Yuda. Hii ndiyo sababu sehemu ya magharibi ya Kiriath-Yearimu inaitwa Mahane-Danimpaka leo.

13 Kutoka hapo wakaendelea mbele mpaka nchi ya vilima ya Efraimu na kufika katika nyumba ya Mika.

14 Ndipo wale watu watano waliopeleleza nchi ya Laishi wakawaambia ndugu zao, “Je, mwajua kuwa mojawapo ya nyumba hizi kuna naivera, sanamu ndogo za nyumbani, sanamu ya kuchonga na sanamu ya kusubu? Sasa basi fikirini mtakalofanya.”

15 Basi wakaingia humo na kwenda kwenye nyumba ya yule kijana Mlawi katika nyumba ya Mika na kumsalimu.

16 Wale Wadani 600, waliovaa silaha za vita, wakasimama penye ingilio la lango.

17 Wale watu watano waliokwenda kupeleleza nchi wakaingia ndani na kuchukua ile sanamu ya kuchonga, ile naivera, na zile sanamu nyingine ndogo za nyumbani pamoja na ile sanamu ya kusubu, wakati yule kuhani akiwa amesimama pale penye ingilio la lango pamoja na wale watu 600 waliokuwa wamejifunga silaha za vita.

18 Hao watu walipoingia katika nyumba ya Mika na kuchukua ile sanamu ya kuchonga, ile naivera, na zile sanamu nyingine ndogo za nyumbani, pamoja na ile sanamu ya kusubu, yule kuhani akawauliza, “Mnafanya nini?”

19 Wakamjibu, “Nyamaza kimya! Weka mkono wako juu ya kinywa chako na ufuatane nasi, uwe baba yetu na kuhani wetu. Si ni afadhali utumikie kabila na ukoo katika Israeli kama kuhani kuliko kumtumikia mtu mmoja na watu wa nyumbani mwake?”

20 Yule kuhani akafurahi. Akachukua ile naivera, zile sanamu nyingine ndogo za nyumbani, na sanamu ya kuchonga, naye akaenda pamoja na wale watu.

21 Ndipo wakageuka na kuondoka wakiwatanguliza mbele watoto wao wadogo, wanyama wao wa kufugwa na mali zao.

22 Walipokuwa wamesafiri umbali kidogo toka nyumbani kwa Mika, watu walioishi karibu na Mika wakaitwa wakakusanyika pamoja, nao wakawafikia Wadani.

23 Walipofuatilia wakipiga kelele Wadani wakawageukia na kumwambia Mika, “Una nini wewe hata ukaja na kundi la watu namna hii ili kupigana?”

24 Akawajibu, “Mmechukua miungu yote niliyoitengeneza, mkachukua na kuhani wangu, nanyi mkaondoka. Nimebaki na nini kingine? Mnawezaje kuniuliza, ‘Una nini wewe?’ ”

25 Wadani wakamjibu, “Usibishane na sisi, la sivyo watu wenye hasira kali watakushambulia, nawe na watu wa nyumbani mwako mtapoteza maisha.”

26 Basi Wadani wakaenda zao, naye Mika alipoona kuwa wana nguvu kumliko yeye, akageuka na kurudi nyumbani kwake.

27 Kisha wakachukua vile Mika alivyokuwa ametengeneza, na kuhani wake, wakaendelea hadi Laishi, dhidi ya watu walio na amani, wasiokuwa na wasiwasi. Wakawashambulia kwa upanga na kuuteketeza mji wao kwa moto.

28 Hapakuwa na yeyote wa kuwaokoa, kwa kuwa kulikuwa mbali sana na Sidoni na hawakuwa na ushirikiano na mtu mwingine yeyote. Mji ulikuwa kwenye bonde karibu na Beth-Rehobu.

Wadani wakaujenga upya huo mji na kuishi humo.

29 Wakauita ule mji Dani kwa kufuata jina la baba yao aliyezaliwa na Israeli, ingawa mji huo ulikuwa ukiitwa Laishi hapo kwanza.

30 Kisha Wadani wakajisimamishia sanamu ile ya kuchonga, naye Yonathani mwana wa Gershomu, mwana wa Mose pamoja na wanawe walikuwa makuhani wa kabila la Wadani mpaka nchi hiyo ilipotekwa.

31 Wakaisimamisha na kuiabudu hiyo sanamu ya kuchonga ya Mika aliyokuwa ameitengeneza, wakati wote ule nyumba ya Mungu ilipokuwa huko Shilo.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JDG/18-f990664498e6bac3f6606f1cfc9dfe99.mp3?version_id=1627—

Categories
Waamuzi

Waamuzi 19

Mlawi Na Suria Wake

1 Katika siku hizo Israeli hawakuwa na mfalme.

Basi Mlawi mmoja aliyeishi sehemu za mbali katika nchi ya vilima ya Efraimu, akamchukua suria mmoja kutoka Bethlehemu ya Yuda.

2 Lakini suria wake akafanya ukahaba dhidi yake, naye akamwacha akarudi nyumbani kwa baba yake huko Bethlehemu ya Yuda. Baada ya kukaa huko kwa muda wa miezi minne,

3 mume wake akaenda kumsihi ili arudi. Alikwenda na mtumishi wake na punda wawili. Yule mwanamke akamkaribisha nyumbani mwa baba yake, baba yake alipomwona akamkaribisha kwa furaha.

4 Baba mkwe wake, yaani, baba yake yule msichana, akamzuia ili akae, hivyo akakaa na huyo baba mkwe wake kwa siku tatu, wakila, wakinywa na kulala huko.

5 Siku ya nne wakaamka mapema naye akajiandaa kuondoka, lakini baba wa yule msichana akamwambia mkwewe, “Ujiburudishe kwa kula kitu chochote, ndipo uweze kwenda.”

6 Basi wakaketi wote wawili ili kula na kunywa pamoja. Baadaye baba wa msichana akamwambia, “Tafadhali ubakie usiku huu upate kujifurahisha nafsi yako.”

7 Basi yule mtu alipotaka kuondoka baba wa yule msichana akamsihi, basi akabaki usiku ule.

8 Asubuhi ya siku ya tano, alipoamka ili aondoke, baba wa yule msichana akamwambia, “Jiburudishe nafsi yako. Ngoja mpaka mchana!” Kwa hiyo wote wawili wakala chakula pamoja.

9 Basi wakati yule mtu alipoinuka aende zake, pamoja na suria wake na mtumishi wake, baba mkwe wake, yaani, baba wa yule msichana akamwambia, “Tazama sasa jioni inakaribia. Ulale hapa usiku unakaribia. Ukae, ukajifurahishe nafsi yako. Kesho unaweza kuamka mapema asubuhi na uende nyumbani kwako.”

10 Lakini akakataa kulala tena, akaondoka na kwenda mpaka Yebusi (ndio Yerusalemu), akiwa na punda wake wawili waliotandikiwa, pamoja na suria wake.

11 Alipokaribia Yebusi na usiku ukiwa umekaribia, mtumishi akamwambia bwana wake, “Haya sasa natuingie katika mji huu wa Wayebusi tulale humo.”

12 Lakini bwana wake akamjibu, “Hapana. Hatutaingia kwenye mji wa kigeni, ambao watu wake si Waisraeli. Tutaendelea mpaka tufike Gibea.”

13 Akasema, “Haya, tujitahidi tufike Gibea au Rama, nasi tutalala katika mji mmojawapo.”

14 Hivyo wakaendelea na safari, jua likachwea walipokaribia Gibea ambao ni mji wa Benyamini.

15 Wakageuka ili kuingia na kulala Gibea. Wakaingia humo, wakaketi kwenye uwanja wa mji, wala hakuna mtu yeyote aliyewakaribisha kwake ili wapate kulala.

16 Jioni ile mtu mmoja mzee toka nchi ya vilima ya Efraimu, aliyekuwa anaishi huko Gibea (watu wa sehemu ile walikuwa Wabenyamini), akarudi kutoka kwenye kazi za shamba.

17 Alipotazama na kuwaona hao wasafiri katika uwanja wa mji, yule mzee akawauliza, “Ninyi mnakwenda wapi? Nanyi mmetoka wapi?”

18 Akamwambia, “Tumepita kutoka Bethlehemu ya Yuda, tunaelekea katika nchi ya vilima ya Efraimu, ambako ndiko ninakoishi. Nilikwenda Bethlehemu ya Yuda na sasa ninakwenda katika nyumba yaBwana. Hakuna mtu yeyote aliyenikaribisha katika nyumba yake.

19 Tunazo nyasi na chakula cha punda wetu na mkate na divai kwa ajili yetu sisi watumishi wako, yaani mimi, mtumishi wako mwanamke, pamoja na huyu kijana tuliyefuatana naye. Hatuhitaji kitu chochote.”

20 Yule mzee akawaambia, “Amani iwe kwenu! Karibuni nyumbani mwangu. Nitawapa mahitaji yenu yote, msilale katika uwanja huu wa mji.”

21 Hivyo akamwingiza nyumbani mwake na kuwalisha punda wake. Baada ya kunawa miguu yao, wakala na kunywa.

22 Walipokuwa wakijiburudisha, watu waovu wa mji huo, wakaizingira ile nyumba. Wakagonga mlango na kusema na yule mzee mwenye nyumba, “Mtoe nje yule mtu aliyeingia kwako, tupate kumlawiti.”

23 Yule mwenye nyumba akatoka nje na kuwaambia, “Hapana, ndugu zangu msiwe waovu namna hii, ninawasihi. Kwa kuwa huyu mtu ni mgeni wangu msifanye jambo hili la aibu.

24 Tazameni, hapa yupo binti yangu ambaye ni bikira na suria wa huyu mtu. Nitawatoleeni hawa sasa, mkawatwae kwa nguvu na kuwafanyia lolote mtakalo. Lakini kwa mtu huyu msimfanyie jambo ovu hivyo.”

25 Lakini wale watu hawakumsikia. Hivyo yule mtu akamtoa yule suria wake nje kwa wale watu, nao wakambaka na kumnajisi usiku ule kucha mpaka asubuhi. Kulipoanza kupambazuka wakamwachia aende.

26 Alfajiri yule mwanamke akarudi kwenye ile nyumba bwana wake alikokuwa, akaanguka chini mlangoni, akalala pale hata kulipopambazuka.

27 Bwana wake alipoamka asubuhi na kufungua mlango wa nyumba na kutoka nje ili kuendelea na safari yake, tazama, yule suria wake alikuwa ameanguka pale penye ingilio la nyumba na mikono yake ikiwa penye kizingiti cha chini.

28 Akamwambia yule suria, “Inuka, twende.” Lakini hakujibu. Yule bwana akamwinua akampandisha juu ya punda wake, wakaondoka kwenda nyumbani.

29 Alipofika nyumbani, akachukua kisu na kumkatakata yule suria kiungo kwa kiungo, sehemu kumi na mbili, na kuvipeleka hivyo vipande katika sehemu zote za Israeli.

30 Kila mtu aliyeona akasema, “Jambo la namna hii halijaonekana wala kutendeka, tangu Israeli walipopanda kutoka Misri. Fikirini juu ya jambo hili! Tafakarini juu ya jambo hili! Tuambieni tufanye nini!”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JDG/19-307054f35d3185fdf6c9741073e75436.mp3?version_id=1627—

Categories
Waamuzi

Waamuzi 20

Waisraeli Wapigana Na Wabenyamini

1 Ndipo Waisraeli wote kuanzia Dani hadi Beer-Sheba na wa kutoka nchi ya Gileadi wakatoka kama mtu mmoja wakakusanyika mbele zaBwanahuko Mispa.

2 Viongozi wote wa kabila za Israeli wakakaa kwenye nafasi zao katika kusanyiko la watu wa Mungu, askari 400,000 waendao kwa miguu wenye panga.

3 (Wabenyamini wakasikia kuwa Waisraeli wamepanda kwenda Mispa.) Ndipo Waisraeli wakasema, “Tuelezeni jinsi jambo hili ovu lilivyotendeka.”

4 Hivyo yule Mlawi, mume wa yule mwanamke aliyeuawa, akasema, “Mimi na suria wangu tulifika Gibea ya Benyamini ili tulale huko.

5 Wakati wa usiku watu wa Gibea wakanijia na kuizingira nyumba, wakitaka kuniua. Wakambaka suria wangu mpaka akafa.

6 Ndipo nikamchukua suria wangu, nikamkatakata vipande vipande na kuvipeleka katika nchi yote ya urithi wa Israeli, kwa kuwa wametenda uasherati mkubwa na jambo la aibu katika Israeli.

7 Sasa, ninyi Waisraeli wote, semeni na mtoe uamuzi wenu.”

8 Watu wote wakainuka wakasema, kama mtu mmoja, “Hakuna hata mmoja wetu atakayekwenda nyumbani. Wala hakuna hata mmoja wetu atakayerudi nyumbani kwake.

9 Sasa hili ndilo tutakaloitendea Gibea: Tutaikabili jinsi kura itakavyotuongoza.

10 Tutatoa watu kumi katika kila 100 kutoka kwenye kabila zote za Israeli, watu 100 katika watu 1,000 na watu 1,000 katika 10,000, ili waende wakalete mahitaji kwa ajili ya jeshi. Basi wakati jeshi litakapofika Gibea ya Benyamini, watawatendea yale wanayostahili, kwa ajili ya uovu huu wa aibu waliotenda katika Israeli.”

11 Hivyo wanaume wote wa Israeli wakakutanika pamoja na kujiunga kama mtu mmoja dhidi ya huo mji.

12 Makabila ya Israeli yakatuma watu kwenda katika kabila la Benyamini lote na kuwaambia, “Ni uovu gani huu wa kutisha uliotendeka katikati yenu?

13 Basi watoeni hao watu waovu kabisa walioko Gibea, ili tupate kuwaua na kuondoa uovu katika Israeli.”

Lakini Wabenyamini hawakuwasikia ndugu zao, Waisraeli.

14 Wakatoka katika miji yao, wakakutanika Gibea ili kupigana na Waisraeli.

15 Siku ile Wabenyamini wakakusanya watu 26,000 kutoka miji yao, waliojifunga panga, mbali na hao 700 waliochaguliwa miongoni mwa hao waliokaa Gibea.

16 Miongoni mwa hao askari wote kulikuwa na watu 700 bora waliochaguliwa watumiao mkono wa kushoto, kila mmoja wao aliweza kutupa jiwe kwa kombeo na kulenga unywele mmoja bila kukosa.

17 Nao watu wa Israeli, mbali na hao wa Benyamini, wakakusanya watu waume 400,000, wenye kutumia panga, wote hao walikuwa mashujaa.

18 Waisraeli wakapanda Betheli na kumuuliza Mungu, “Ni nani miongoni mwetu atakayetangulia mbele yetu ili kupigana na Wabenyamini?”

Bwanaakawajibu, “Yuda ndiye atakayetangulia.”

19 Asubuhi yake Waisraeli wakaamka na kupiga kambi karibu na Gibea.

20 Waisraeli wakatoka kupigana na Wabenyamini, nao Waisraeli wakajiweka kwenye nafasi zao katika vita dhidi yao huko Gibea.

21 Wabenyamini wakatoka Gibea na kuwaua watu 22,000 wa Israeli siku ile.

22 Lakini Waisraeli wakatiana moyo kila mmoja na mwenzake, nao wakajiweka kwenye nafasi zao katika vile vita mara ya pili mahali pale walipokuwa wamejiweka mara ya kwanza.

23 Waisraeli wakapanda mbele zaBwanana kulia mbele zake mpaka jioni, nao wakamuulizaBwanawakisema, “Je, tupande tena kupigana vita na Wabenyamini, ndugu zetu?”

Bwanaakajibu, “Pandeni mkapigane nao.”

24 Ndipo Waisraeli wakawakaribia Wabenyamini siku ya pili.

25 Wakati huu, Wabenyamini walipotoka Gibea ili kupigana nao, wakawaua watu Waisraeli 18,000, wote wakiwa wamejifunga panga.

26 Ndipo Waisraeli, watu wote, wakapanda Betheli, huko wakakaa mbele zaBwanawakilia. Wakafunga siku ile mpaka jioni na kutoa sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya amani kwaBwana.

27 Nao Waisraeli wakauliza kwaBwana. (Katika siku hizo Sanduku la Agano la Mungu lilikuwa huko

28 na Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa Aroni, alikuwa anahudumu mbele za hilo Sanduku.) Wakauliza, “Je, tupande kwenda vitani kupigana tena na Wabenyamini ndugu zetu, au la?”

Bwanaakajibu, “Nendeni, kwa kuwa kesho nitawatia mikononi mwenu.”

29 Basi Waisraeli wakaweka waviziao kuizunguka Gibea.

30 Kisha Waisraeli wakapanda kupigana na Wabenyamini katika siku ya tatu na kujiweka kwenye nafasi zao dhidi ya Gibea kama walivyokuwa wamefanya hapo kwanza.

31 Wabenyamini wakatoka ili kukabiliana nao, Waisraeli wakawavuta Wabenyamini watoke katika mji. Wakaanza kupigana na kuua watu wapatao thelathini wa Israeli, kama walivyofanya nyakati nyingine, katika njia kuu, moja iendayo Betheli na nyingine Gibea.

32 Wabenyamini wakafikiri, “Wanapigwa mbele yetu kama hapo kwanza.” Waisraeli wakasema, “Sisi na turudi nyuma ili tuwavute wauache mji waende kuelekea barabarani.”

33 Watu wote wa Israeli wakaondoka kwenye sehemu zao na kujipanga huko Baal-Tamari, nao wale waviziaji wa Waisraeli, wakatoka hapo walipokuwa kwenye uwanda wa magharibi ya Gibea.

34 Ndipo watu 10,000 bora waliochaguliwa katika Israeli wote, wakaja kuishambulia Gibea. Vita vilikuwa vikali sana, hata Wabenyamini hawakutambua kuwa maangamizi yalikuwa karibu nao kwa kiasi hicho.

35 Bwanaakawashinda Wabenyamini mbele ya Waisraeli na siku ile Waisraeli wakawaua Wabenyamini watu waume 25,100, wote wakiwa wenye kujifunga silaha za vita.

36 Hivyo Wabenyamini wakaona kuwa wamepigwa.

Basi Waisraeli walikuwa wameondoka mbele ya Wabenyamini, kwa sababu Waisraeli waliwategemea hao waviziaji waliokuwa wamewaweka dhidi ya Gibea.

37 Wale waviziaji wakafanya haraka kuingia Gibea, wakasambaa na kuwaua watu wote wa mji kwa upanga.

38 Waisraeli walikuwa wamepatana na hao waviziaji kuwa wangefanya lipande wingu kubwa la moshi kutoka huo mji,

39 ndipo watu wa Waisraeli wangegeuka kupigana.

Watu wa Benyamini walikuwa wameanza kuwapiga na kuua watu wa Israeli (wapatao thelathini), hivyo wakafikiri, “Hakika tutawapiga, kama tulivyowashinda katika vita hapo kwanza.”

40 Lakini wakati lile wingu la moshi lilipoanza kupanda kutoka ule mji, Wabenyamini wakageuka na kuona moshi wa mji mzima unapaa juu angani.

41 Ndipo watu wa Israeli wakawageukia, nao Wabenyamini wakatiwa hofu, kwa kuwa walitambua kwamba maafa yamewajia.

42 Basi wakakimbia mbele ya Waisraeli kuelekea nyikani, lakini hawakuweza kukwepa vile vita. Nao watu wa Israeli waliotoka katika ile miji wakawaua huko.

43 Wakawazingira Wabenyamini pande zote, wakawafuatia na kuwapata hapo walipopumzika katika viunga vya Gibea upande wa mashariki.

44 Wakaanguka Wabenyamini 18,000 ambao wote ni mashujaa.

45 Walipogeuka na kukimbia kuelekea nyikani hata kufikia mwamba wa Rimoni, Waisraeli wakawaua watu 5,000 wakiwa njiani. Wakawafuata kwa kasi mpaka Gidomu huko wakawaua watu wengine 2,000.

46 Siku ile wakawaua Wabenyamini 25,000 waliokuwa mashujaa wa vita.

47 Lakini watu 600 wakakimbia kuelekea nyikani katika mwamba wa Rimoni, na kukaa huko muda wa miezi minne.

48 Waisraeli wakarudi na kuua watu wote wa Benyamini, pamoja na wanyama na kila walichokikuta. Pia kila mji waliouona waliuchoma moto.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JDG/20-1d0aea9297b47fd3777972a3a2c580af.mp3?version_id=1627—

Categories
Waamuzi

Waamuzi 21

Wabenyamini Watafutiwa Wake

1 Wana wa Israeli walikuwa wameapa kwa kiapo kule Mispa: “Hapana mtu yeyote atakayemwoza binti yake kwa Wabenyamini.”

2 Watu wakaenda Betheli, wakaketi mbele za Mungu mpaka jioni, wakapaza sauti zao, wakalia sana.

3 Wakasema, “EeBwana, Mungu wa Israeli, kwa nini jambo hili limewapata Waisraeli? Kwa nini kabila moja la Israeli limekosekana?”

4 Kesho yake asubuhi na mapema watu wakajenga madhabahu na kuleta sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani.

5 Ndipo Waisraeli wakasema, “Ni kabila lipi la Israeli ambalo halikufika katika mkutano kumkaribiaBwana?” Kwa kuwa walikuwa wameweka kiapo kikuu kuwa yeyote asiyefika mbele zaBwanahuko Mispa, kwa hakika angeuawa.

6 Basi Waisraeli wakaghairi kwa ajili ya ndugu zao Wabenyamini, wakasema, “Leo kabila moja limekatiliwa mbali na Israeli.

7 Sasa tutawezaje kuwapa mabinti zetu wawe wake zao kwa hao waliobaki maadamu tumeapa kwaBwanakuwa hatutawapa binti zetu kuwa wake zao?”

8 Ndipo wakasema, “Ni kabila lipi la Israeli ambalo halikufika mbele zaBwanahuko Mispa?” Wakagundua kuwa hakuna hata mmoja aliyetoka Yabeshi-Gileadi aliyefika kambini kwa ajili ya kusanyiko la mkutano.

9 Walipohesabu waliona hakuna mtu yeyote wa Yabeshi-Gileadi aliyekuwepo.

10 Ndipo mkutano wakatuma askari 12,000 na wakawaamuru kwenda Yabeshi-Gileadi na kuwaua wale wote waishio huko, walikuwepo wake na watoto.

11 Wakasema, “Hilo ndilo mtakalofanya. Ueni kila mtu mume na mke ambaye si bikira.”

12 Wakakuta kati ya watu walioishi Yabeshi-Gileadi wanawali mia nne ambao hawajakutana kimwili na mwanaume, nao wakawachukua kwenye kambi huko Shilo katika nchi ya Kanaani.

13 Ndipo mkutano ukatuma ujumbe wa amani kwa Wabenyamini huko katika mwamba wa Rimoni.

14 Basi Wabenyamini wakarudi nyumbani mwao, wakapewa wale wanawali wa Yabeshi-Gileadi waliowaponya. Lakini hawakuwatosha wanaume wote.

15 Waisraeli wakasikitika kwa ajili ya Wabenyamini, kwa kuwaBwanaameweka ufa katika makabila ya Israeli.

16 Viongozi wa kusanyiko wakasema, “Kwa kuwa wanawake wa Wabenyamini wameangamizwa, tufanyeje ili kuwapatia wake wale wanaume waliosalia?

17 Wale waliopona wa Wabenyamini ni lazima tuwape wake, ili wawe na warithi, ili kabila lolote katika Israeli lisifutike.

18 Hatuwezi kuwapa binti zetu kuwa wake, kwa kuwa sisi Waisraeli tumeapa kiapo hiki: ‘Alaaniwe mtu yeyote ampaye Mbenyamini mke.’ ”

19 Ndipo waliposema, “Tazama iko sikukuu ya kila mwaka yaBwanakatika Shilo, kaskazini ya Betheli na mashariki mwa ile barabara itokayo Betheli kwenda Shekemu, upande wa kusini wa Lebona.”

20 Hivyo wakawaelekeza Wabenyamini wakisema, “Nendeni mkajifiche kwenye mashamba ya mizabibu,

21 nanyi mwangalie. Wasichana wa Shilo watakapojiunga kwenye kucheza, ninyi tokeni kwenye hayo mashamba ya mizabibu na kila mmoja akamate mwanamke mmoja toka miongoni mwa hao wasichana wa Shilo na mwende nao katika nchi ya Benyamini.

22 Baba zao au ndugu zao waume watakapotulalamikia, tutawaambia, ‘Kuweni wakarimu kwetu, nanyi mturuhusu tuwe nao kwa kuwa hatukuweza kumpa kila mtu mke tulipopigana. Lakini ninyi pia hamna hatia, kwa kuwa hamkuwapa wao binti zenu kuwa wake.’ ”

23 Basi hivyo ndivyo Wabenyamini walivyofanya. Wakati wasichana walipokuwa wakicheza, kila mtu akamkamata msichana mmoja akamchukua akaenda naye ili awe mke wake. Kisha wakarudi katika urithi wao na kuijenga upya miji na kuishi humo.

24 Wakati huo Waisraeli wakaondoka sehemu ile na kwenda nyumbani kwao, kwenye makabila yao na kwa jamaa zao, kila mmoja kwenye urithi wake mwenyewe.

25 Katika siku hizo kulikuwa hakuna mfalme katika Israeli; kila mtu alifanya kile alichoona ni sawa machoni pake mwenyewe.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JDG/21-e914f4e9890b9c5cfa042af8d01944ee.mp3?version_id=1627—

Categories
Ruthu

Ruthu Utangulizi

Utangulizi

Kitabu hiki kimepewa jina la Ruthu, mhusika mkuu katika habari zilizoandikwa humu. Elimeleki na mkewe Naomi walilazimika kuhama kutoka Bethlehemu kwenda nchi ya Moabu. Muda mfupi baadaye Elimeleki akafariki, nao wanawe Maloni na Kilioni nao wakaoa wanawake wa Kimoabu, Ruthu na Orpa. Maloni na Kilioni wakafariki bila watoto. Naomi alipoamua kurudi nyumbani kwake katika nchi ya Yuda, aliwashawishi wakwe zake kurudi kwao. Ruthu alisisitiza kwenda pamoja naye, lakini Orpa aliamua kurudi nyumbani kwao.

Naomi na Ruthu walipofika Israeli, Ruthu alienda kutafuta riziki yao. Alijikuta katika mashamba ya mtu wa jamaa wa karibu wa Elimeleki, kwa jina Boazi, ambaye aliamuru Ruthu atunzwe na wafanyi kazi wake. Baada ya muda, Boazi alimwoa Ruthu. Ukoo wa ufalme wa Israeli ulioanza na Mfalme Daudi ulitoka ukoo huu. Baadaye Masiya, Yesu Kristo, anatajwa kuwa wa ukoo huu.

Mwandishi

Hajulikani, lakini mapokeo ya Kiyahudi yanasema Samweli ndiye mwandishi.

Kusudi

Kitabu cha Ruthu kinaonyesha jinsi watu watatu wanaweza kuwa na mwenendo thabiti na wa uadilifu kwa Mungu wakati jamii inayowazunguka imepotoka.

Mahali

Moabu na Bethlehemu.

Tarehe

Baada ya kipindi cha Waamuzi, 1375–1050 K.K.

Wahusika Wakuu

Naomi, Ruthu na Boazi.

Wazo Kuu

Uhusiano kati ya Naomi na mkwewe Ruthu unatupa kielelezo jinsi maisha ya kumcha Mungu yanapasa kuwa, na vile upendo wa kweli kwa jirani unavyoweza kuwa na matokeo ya baraka.

Mambo Muhimu

Kuambatana kwa Ruthu na Naomi kunaonyesha uaminifu wa Ruthu, ijapokuwa Naomi alimsihi arudi kwa watu wake baada ya kufiwa na mumewe. Kutokana na uaminifu huo, Ruthu anatajwa katika uzao wa Yesu kutokana na kuolewa na Boazi.

Mgawanyo

Naomi kuondoka Israeli, na kurudi kwake (

1:1-22

)

Ruthu anakaribishwa (

2:1–3:18

)

Boazi na Ruthu (

4:1-22

).