Categories
2 Wathesalonike

2 Wathesalonike 2

Yule Mtu Wa Kuasi

1 Ndugu, kuhusu kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo na kukusanyika kwetu pamoja mbele zake, tunawasihi,

2 msiyumbishwe kwa urahisi wala msitiwe wasiwasi na roho wala neno au barua inayosemekana kuwa imetoka kwetu, isemayo kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwako.

3 Mtu yeyote na asiwadanganye kwa namna yoyote kwa maana siku ile haitakuja mpaka uasi utokee kwanza, na yule mtu wa kuasi adhihirishwe, yule ambaye amehukumiwa kuangamizwa kabisa.

4 Yeye atapingana na kujitukuza juu ya kila kitu kiitwacho Mungu au kinachoabudiwa, ili kujiweka juu katika Hekalu la Mungu, akijitangaza mwenyewe kuwa ndiye Mungu.

5 Je, hamkumbuki ya kwamba nilipokuwa pamoja nanyi niliwaambia mambo haya?

6 Nanyi sasa mnajua kinachomzuia, ili apate kudhihirishwa wakati wake utakapowadia.

7 Maana ile nguvu ya siri ya uasi tayari inatenda kazi, lakini yule anayeizuia ataendelea kufanya hivyo mpaka atakapoondolewa.

8 Hapo ndipo yule mwasi atafunuliwa, ambaye Bwana Yesu atamteketeza kwa pumzi ya kinywa chake na kumwangamiza kabisa kwa utukufu wa kuja kwake.

9 Kuja kwa yule mwasi kutaonekana kana kwamba ni kutenda kazi kwake Shetani ambaye hutumia nguvu zote, ishara, maajabu ya uongo,

10 na kila aina ya uovu kwa wale wanaoangamia kwa sababu walikataa kuipenda kweli wapate kuokolewa.

11 Kwa sababu hii, Mungu ameruhusu watawaliwe na nguvu ya udanganyifu, ili waendelee kuamini uongo,

12 na wahukumiwe wote ambao hawakuiamini ile kweli, bali wamefurahia uovu.

Simameni Imara

13 Lakini imetupasa sisi kumshukuru Mungu daima kwa ajili yenu, ndugu mpendwao na Bwana, kwa sababu Mungu aliwachagua ninyi tangu mwanzo ili mwokolewe kwa kutakaswa na Roho kwa kuiamini kweli.

14 Kwa kusudi hili Mungu aliwaita kwa njia ya kuhubiri kwetu Injili, ili mpate kushiriki katika utukufu wa Bwana Yesu Kristo.

15 Hivyo basi, ndugu wapendwa, simameni imara na myashike sana yale mafundisho tuliyowapa ikiwa ni kwa maneno ya kinywa au kwa barua.

16 Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe na Mungu Baba yetu, aliyetupenda na kwa neema yake akatupatia faraja ya milele na tumaini jema,

17 awafariji mioyo yenu na kuwaimarisha katika kila neno na tendo jema.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2TH/2-353c646b730e695a504f56d93075ec80.mp3?version_id=1627—

Categories
2 Wathesalonike

2 Wathesalonike 3

Hitaji La Maombi

1 Hatimaye, ndugu, tuombeeni ili Neno la Bwana lipate kuenea kwa haraka na kuheshimiwa kila mahali, kama vile ilivyokuwa kwenu.

2 Ombeni pia ili tupate kuokolewa kutokana na watu waovu na wabaya, kwa maana si wote wanaoamini.

3 Lakini Bwana ni mwaminifu, naye atawaimarisha ninyi na kuwalinda kutokana na yule mwovu.

4 Nasi tuna tumaini katika Bwana ya kuwa mnafanya na mtaendelea kufanya yale tuliyowaagiza.

5 Bwana aiongoze mioyo yenu katika upendo wa Mungu na katika saburi ya Kristo.

Onyo Dhidi Ya Uvivu

6 Ndugu, tunawaagiza katika Jina la Bwana Yesu Kristo, jitengeni na kila ndugu ambaye ni mvivu na ambaye haishi kufuatana na maagizo tuliyowapa.

7 Maana ninyi wenyewe mnajua jinsi iwapasavyo kufuata mfano wetu. Sisi hatukuwa wavivu tulipokuwa pamoja nanyi,

8 wala hatukula chakula cha mtu yeyote pasipo kukilipia. Badala yake tulifanya kazi kwa bidii usiku na mchana, ili tusimlemee mtu yeyote miongoni mwenu.

9 Tulifanya hivi, si kwa sababu hatukuwa na haki ya kupata msaada kama huo, bali ndio sisi wenyewe tuwe kielelezo.

10 Kwa maana hata tulipokuwa pamoja nanyi, tuliwapa amri kwamba: “Mtu yeyote asiyetaka kufanya kazi, hata kula asile.”

11 Kwa kuwa tunasikia kwamba baadhi ya watu miongoni mwenu ni wavivu. Hawafanyi kazi bali hujishughulisha na mambo ya wengine.

12 Basi watu kama hao tunawaagiza na kuwahimiza katika Bwana Yesu Kristo, kwamba wafanye kazi kwa utulivu kwa ajili ya chakula chao wenyewe.

13 Kwa upande wenu, ndugu, ninyi kamwe msichoke katika kutenda mema.

14 Ikiwa mtu yeyote hayatii maagizo yetu yaliyoko katika barua hii, mwangalieni sana mtu huyo. Msishirikiane naye, ili apate kuona aibu.

15 Lakini msimhesabu kuwa adui, bali mwonyeni kama ndugu.

Salamu Za Mwisho

16 Basi, Bwana wa amani mwenyewe awapeni amani nyakati zote na kwa kila njia. Bwana awe nanyi nyote.

17 Mimi, Paulo, ninaandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe. Hii ndio alama ya utambulisho katika barua zangu zote. Hivi ndivyo niandikavyo.

18 Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi nyote. Amen.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2TH/3-ff6d0d373cb935040c7ee8129426f3e7.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Timotheo

1 Timotheo Utangulizi

Utangulizi

Nyaraka za 1 na 2 Timotheo na ule wa Tito zinatambuliwa kama nyaraka za kichungaji zilizoandikwa na Paulo. Alimwandikia Timotheo msaidizi wake, ambaye alikuwa amemwacha huko Efeso kusahihisha matatizo kadhaa kuhusu mwenendo wa kanisa, uongozi wa kanisa, na mambo yaliyowahusu waumini. Paulo aliandika ili kumpa Timotheo maagizo kuhusu mambo haya, ili kanisa lifanye kazi yake vyema. Aliandika pia kumtia moyo Timotheo asichoke katika maisha yake ya Kikristo, bali aishi maisha ya ukamilifu kwa utukufu wa Mungu.

Timotheo alizaliwa huko Listra. Baba yake alikuwa Myunani, naye mama yake Myahudi ambaye alimfundisha Maandiko tangu utoto. Paulo alipofika Listra katika safari yake ya pili ya kitume, alimchagua Timotheo ambaye alishirikiana naye hadi mwisho wa huduma yake.

Mwandishi

Mtume Paulo.

Kusudi

Kumtia moyo na kumpa maelekezo Timotheo, ambaye alikuwa kiongozi mchanga, kuhusu utaratibu wa kanisa, imani na maadibisho.

Mahali

Pengine Filipi.

Tarehe

Kama mwaka wa 64 B.K.

Wahusika Wakuu

Paulo na Timotheo.

Wazo Kuu

Umuhimu wa kuwa na imani sahihi, mwenendo mnyofu, na pia uadilifu.

Mambo Muhimu

Kumwelekeza Timotheo kuhusu sifa na wajibu wa viongozi mbalimbali katika kanisa, na kumpa mwongozo katika wajibu wake wa kichungaji.

Mgawanyo

Maonyo kuhusu mafundisho ya uongo (

1:1-20

)

Mafundisho kuhusu maombi (

2:1-15

)

Sifa zinazowapasa waangalizi na wazee wa kanisa (

3:1-16

)

Maonyo na huduma (

4:1–5:25

)

Huduma ya Kikristo, na maagizo kwa Timotheo (

6:1-21

).

Categories
1 Timotheo

1 Timotheo 1

1 Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na ya Kristo Yesu tumaini letu.

2 Kwa Timotheo, mwanangu halisi katika imani:

Neema, rehema na amani itokayo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu.

Maonyo Dhidi Ya Walimu Wa Uongo

3 Kama nilivyokusihi wakati nilipokwenda Makedonia, endelea kubaki Efeso, ili kwamba upate kuwaagiza watu wasiendelee kufundisha mafundisho ya uongo

4 wala wasitoe muda wao kwa hadithi za kubuniwa na orodha za majina ya vizazi visivyo na mwisho, ambazo huchochea mabishano badala ya mpango wa Mungu utokanao na imani.

5 Kusudi la maagizo haya ni upendo utokao katika moyo safi, dhamiri njema na imani ya kweli.

6 Watu wengine wamepotoka kutoka haya na kugeukia majadiliano yasiyo na maana kwa kuwa,

7 wanataka kuwa walimu wa sheria, lakini hawajui mambo yale wanayosema wala hayo wanayoyatumainia kwa uthabiti.

8 Tunajua kwamba sheria ni njema ikiwa inatumika kwa halali kama ilivyokusudiwa.

9 Lakini tunajua ya kuwa sheria si kwa ajili ya wenye haki, bali kwa ajili ya wavunja sheria na waasi, kwa ajili ya wasiomcha Mungu na wenye dhambi, wasio watakatifu na wanaokufuru; kwa wale wawauao baba zao au mama zao, kwa wauaji,

10 kwa wazinzi na wahanithi, kwa wale wauzao watu, na kwa waongo na waapao kwa uongo, na kwa chochote kingine kilicho kinyume na mafundisho ya kweli,

11 ambayo yanakubaliana na Injili ya utukufu wa Mungu anayehimidiwa, ambayo mimi nimewekewa amana.

Neema Ya Mungu Kwa Paulo

12 Namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu, kwa sababu aliniona mwaminifu, akaniteua kwa kazi yake.

13 Ingawa wakati fulani nilikuwa mwenye kukufuru, mtesaji na mwenye jeuri, lakini nilipata rehema kwa sababu nilitenda hivyo kwa kutojua na kutoamini kwangu.

14 Neema ya Bwana wetu ilimiminwa juu yangu kwa wingi, ikiambatana na imani na upendo ulio katika Kristo Yesu.

15 Msemo huu ni wa kweli na unaostahili kukubalika, usemao kwamba: Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuokoa wenye dhambi, ambao mimi ndiye niliye mbaya kuliko wote.

16 Lakini kwa sababu hiyo nilipata rehema, ili katika mimi, niliyekuwa mwenye dhambi kuliko wote, Kristo Yesu apate kuonyesha uvumilivu wake usio na kikomo, ili niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini na wapate uzima wa milele.

17 Basi Mfalme wa milele, asiye na mwisho, asiyeonekana, aliye Mungu pekee, apewe heshima na utukufu milele na milele. Amen.

18 Mwanangu Timotheo, ninakupa agizo hili, kwa kadiri ya maneno ya unabii yaliyosemwa kukuhusu, ili kwa kuyafuata upate kupigana vita vizuri,

19 ukiishikilia imani na dhamiri njema, ambazo wengine wamevikataa, na hivyo wakaangamia kwa habari ya imani yao.

20 Miongoni mwao wako Himenayo na Aleksanda, ambao nimemkabidhi Shetani ili wafundishwe wasije wakakufuru.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1TI/1-409b6376652847daea82368653bf1b12.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Timotheo

1 Timotheo 2

Maagizo Kuhusu Kuabudu

1 Awali ya yote, nasihi kwamba dua, sala, maombezi na shukrani zifanyike kwa ajili ya watu wote:

2 kwa ajili ya wafalme na wale wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi kwa amani na utulivu, katika uchaji wote wa Mungu na utakatifu.

3 Jambo hili ni jema, tena linapendeza machoni pa Mungu Mwokozi wetu,

4 anayetaka watu wote waokolewe na wafikie kuijua kweli.

5 Kwa maana kuna Mungu mmoja na mpatanishi mmoja kati ya Mungu na wanadamu, yaani mwanadamu Kristo Yesu,

6 aliyejitoa mwenyewe kuwa fidia kwa ajili ya wanadamu wote: jambo hili lilishuhudiwa kwa wakati wake ufaao.

7 Nami kwa kusudi hili nimewekwa niwe mhubiri na mtume (nasema kweli katika Kristo wala sisemi uongo), mwalimu wa watu wa Mataifa katika imani na kweli.

8 Nataka kila mahali wanaume wasali wakiinua mikono mitakatifu pasipo hasira wala kugombana.

9 Vivyo hivyo nataka wanawake wajipambe kwa adabu na kwa heshima katika mavazi yanayostahili, si kwa kusuka nywele, kuvalia dhahabu, lulu au mavazi ya gharama kubwa,

10 bali kwa matendo mazuri kama iwapasavyo wanawake wanaokiri kuwa wanamcha Mungu.

11 Mwanamke na ajifunze kwa utulivu na kwa utiifu wote.

12 Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha au kuwa na mamlaka juu ya mwanaume. Mwanamke inampasa kukaa kimya.

13 Kwa maana Adamu aliumbwa kwanza, kisha Eva.

14 Wala si Adamu aliyedanganywa, bali ni mwanamke aliyedanganywa akawa mkosaji.

15 Lakini mwanamke ataokolewa kwa kuzaa kwake, kama wakiendelea kudumu katika imani, upendo na utakatifu, pamoja na kuwa na kiasi.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1TI/2-c6d36e0052ed47debe344c3ce3fddcba.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Timotheo

1 Timotheo 3

Sifa Za Waangalizi

1 Hili ni neno la kuaminiwa, kwamba mtu akitamani kazi ya uangalizi, atamani kazi nzuri.

2 Basi, imempasa mwangalizi awe mtu asiye na lawama, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi, anayejitawala, anayeheshimika, mkarimu, ajuaye kufundisha,

3 asiwe mlevi, wala mkali bali awe mpole, asiwe mgomvi wala mpenda fedha.

4 Lazima aweze kuisimamia nyumba yake mwenyewe vizuri na kuhakikisha kwamba watoto wake wanamtii na kuwa na heshima kwa kila njia.

5 (Kwa maana kama mtu hajui jinsi ya kusimamia nyumba yake mwenyewe, atawezaje kuliangalia kanisa la Mungu?)

6 Asiwe mtu aliyeokoka karibuni asije akajivuna na kuangukia kwenye hukumu ile ile ya ibilisi.

7 Inampasa pia awe na sifa njema kwa watu walio nje, ili asije akalaumiwa na kuanguka kwenye mtego wa ibilisi.

Sifa Za Mashemasi

8 Vivyo hivyo, mashemasi nao wawe watu wanaostahili heshima, wasiwe wenye kauli mbili au wenye kujifurahisha kwa mvinyo, wala wanaotamani faida isiyo halali.

9 Inawapasa kushikamana sana na ile siri ya imani kwa dhamiri safi.

10 Ni lazima wapimwe kwanza; kisha kama hakuna neno dhidi yao, basi na waruhusiwe kuhudumu kama mashemasi.

11 Vivyo hivyo, wake zao wawe wanawake wanaostahili heshima, wasio wasingiziaji, bali wawe na kiasi na waaminifu katika kila jambo.

12 Shemasi awe mume wa mke mmoja na inampasa aweze kusimamia watoto wake na watu wa nyumbani mwake vyema.

13 Wale ambao wamehudumu vyema katika huduma ya ushemasi hujipatia msimamo bora na ujasiri mkubwa katika imani yao ndani ya Kristo Yesu.

14 Ingawa ninatarajia kuja kwako hivi karibuni, ninakuandikia maagizo haya sasa ili kwamba,

15 kama nikikawia, utajua jinsi iwapasavyo watu kuenenda katika nyumba ya Mungu, ambayo ndiyo kanisa la Mungu aliye hai, lililo nguzo na msingi wa kweli.

16 Bila shaka yoyote, siri ya utauwa ni kubwa:

Alidhihirishwa katika mwili wa kibinadamu,

akathibitishwa kuwa na haki katika Roho,

akaonekana na malaika,

akahubiriwa miongoni mwa mataifa,

akaaminiwa ulimwenguni,

akachukuliwa juu katika utukufu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1TI/3-c6237f1099bd9ead7ce85c3ff80fef55.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Timotheo

1 Timotheo 4

Maagizo Kwa Timotheo

1 Roho asema waziwazi kwamba katika siku za mwisho baadhi ya watu wataiacha imani na kufuata roho zidanganyazo na mafundisho ya mashetani.

2 Mafundisho kama hayo huja kupitia kwa waongo ambao ni wanafiki, hali dhamiri zao zikiungua kwa kuchomwa moto.

3 Wao huwakataza watu wasioe na kuwaagiza wajiepushe na vyakula fulani, ambavyo Mungu aliviumba ili vipokewe kwa shukrani na wale wanaoamini na kuijua kweli.

4 Kwa maana kila kitu alichokiumba Mungu ni chema, wala hakuna kitu chochote cha kukataliwa kama kikipokewa kwa shukrani,

5 kwa sababu kimetakaswa kwa neno la Mungu na kwa kuomba.

Mtumishi Mwema Wa Yesu Kristo

6 Kama ukiwakumbusha ndugu mambo haya, utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu, uliyelelewa katika kweli ya imani na yale mafundisho mazuri uliyoyafuata.

7 Usijishughulishe kamwe na hadithi za kipagani na masimulizi ya uongo ya wanawake wazee; badala yake, jizoeze kuwa mtauwa.

8 Kwa maana mazoezi ya mwili yana faida kwa sehemu, lakini utauwa una faida katika mambo yote, yaani, unayo ahadi ya uzima wa sasa na ya ule ujao.

9 Hili ni neno la kuaminiwa tena lastahili kukubaliwa kabisa,

10 (nasi kwa ajili ya hili tunajitaabisha na kujitahidi), kwamba tumeweka tumaini letu kwa Mungu aliye hai, ambaye ni Mwokozi wa watu wote, hasa wale waaminio.

11 Mambo haya yaagize na kuyafundisha.

12 Mtu yeyote asikudharau kwa kuwa wewe ni kijana, bali uwe kielelezo kizuri kwa waumini katika usemi, mwenendo, upendo, imani na usafi.

13 Fanya bidii kusoma Maandiko hadharani, kuhubiri na kufundisha, mpaka nitakapokuja.

14 Usiache kutumia kipawa kilicho ndani yako, ambacho ulipewa kwa neno la unabii wakati wazee walikuwekea mikono.

15 Uwe na bidii katika mambo haya; ujitolee kwa ajili ya mambo haya kikamilifu, ili kila mtu aone kuendelea kwako.

16 Jilinde sana nafsi yako na mafundisho yako. Dumu katika hayo, kwa maana kwa kufanya hivyo, utajiokoa wewe mwenyewe pamoja na wale wanaokusikia.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1TI/4-ab3daa3e74806105fc1d4551fc41c28b.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Timotheo

1 Timotheo 5

Maagizo Kuhusu Wajane, Wazee Na Watumwa

1 Usimkemee mzee kwa ukali bali umshawishi kama vile angekuwa ni baba yako. Uwatendee vijana kama vile ndugu zako;

2 nao wanawake wazee uwatendee kama mama zako, na wanawake vijana kama dada zako, katika usafi wote.

3 Waheshimu wanawake wajane ambao ni wajane kweli kweli.

4 Kama mjane ana watoto ama wajukuu, hawa inawapasa awali ya yote wajifunze kutimiza wajibu wao wa kumcha Mungu katika matendo kwa kuwatunza wale wa jamaa zao wenyewe, na hivyo wawarudishie wema waliowatendea wazazi wao, kwa kuwa hivi ndivyo impendezavyo Mungu.

5 Mwanamke ambaye ni mjane kweli kweli, yaani, yeye aliyebaki peke yake huweka tumaini lake kwa Mungu naye hudumu katika maombi usiku na mchana akimwomba Mungu ili amsaidie.

6 Lakini mjane aishiye kwa anasa amekufa, ingawa anaishi.

7 Wape watu maagizo haya pia, ili asiwepo yeyote wa kulaumiwa.

8 Kama mtu hawatunzi wale wa jamaa yake, hasa wale wa nyumbani mwake mwenyewe, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko yeye asiyeamini.

9 Mjane yeyote asiwekwe kwenye orodha ya wajane isipokuwa awe ametimiza umri wa miaka sitini, na ambaye alikuwa mke wa mume mmoja,

10 awe ameshuhudiwa kwa matendo yake mema, aliyewalea watoto wake vizuri, aliye mkarimu, aliyewanawisha watakatifu miguu, aliyewasaidia wenye shida na aliyejitolea kwa ajili ya matendo mema ya kila namna.

11 Lakini kwa habari za wajane vijana usiwaweke kwenye orodha hiyo, maana tamaa zao za kimaumbile zikizidi kule kujitoa kwao kwa Kristo, watataka kuolewa tena.

12 Nao kwa njia hiyo watajiletea hukumu kwa kukiuka ahadi yao ya kwanza.

13 Zaidi ya hayo, wajane kama hao huwa na tabia ya uvivu wakizurura nyumba kwa nyumba, wala hawawi wavivu tu, bali pia huwa wasengenyaji, wajiingizao katika mambo yasiyowahusu na kusema mambo yasiyowapasa kusema.

14 Hivyo nawashauri wajane vijana waolewe, wazae watoto na wasimamie nyumba zao, wasije wakampa adui nafasi ya kutushutumu.

15 Kwa maana kwa kweli wajane wengine wamepotoka ili kumfuata Shetani.

16 Lakini kama mwanamke yeyote aaminiye ana wajane katika jamaa yake, inampasa awasaidie wala si kuwaacha wakililemea kanisa, ili kanisa liweze kuwasaidia wale ambao ni wajane kweli kweli.

Wazee Wa Kanisa

17 Wazee wa kanisa wanaoongoza shughuli za kanisa vizuri wanastahili heshima mara mbili, hasa wale ambao kazi yao ni kuhubiri na kufundisha.

18 Kwa maana Maandiko husema, “Usimfunge maksai kinywa apurapo nafaka,” tena, “Mfanyakazi anastahili mshahara wake.”

19 Usiendekeze mashtaka dhidi ya mzee isipokuwa yawe yameletwa na mashahidi wawili au watatu.

20 Wale wanaodumu katika dhambi uwakemee hadharani, ili wengine wapate kuogopa.

21 Ninakuagiza mbele za Mungu na mbele za Kristo Yesu na mbele za malaika wateule, shika maagizo haya pasipo ubaguzi wala upendeleo.

22 Usiwe na haraka kumwekea mtu mikono wala usishiriki dhambi za watu wengine. Jilinde nafsi yako uwe safi.

23 Acha kunywa maji peke yake, tumia divai kidogo kwa sababu ya tumbo lako na maumivu yako ya mara kwa mara.

24 Dhambi za watu wengine ni dhahiri nazo zinawatangulia kwenda hukumuni; na dhambi za watu wengine zinawafuata nyuma yao.

25 Vivyo hivyo, matendo mema yako dhahiri, na hata yale ambayo si mema hayawezi kufichika.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1TI/5-964d1cc4c8192ccd44e575d926556537.mp3?version_id=1627—

Categories
1 Timotheo

1 Timotheo 6

Watumwa

1 Wale wote walio chini ya kongwa la utumwa inawapasa kuwahesabu mabwana zao kuwa wanastahili heshima yote, ili jina la Mungu lisitukanwe wala mafundisho yetu.

2 Wale watumwa ambao wana mabwana waaminio, haiwapasi kupunguza heshima yao kwa sababu wao ni ndugu. Badala yake, wawatumikie hata vizuri zaidi, kwa sababu wale wanaonufaika na huduma yao ni waaminio, ambao ni wapenzi wao. Fundisha mambo haya na uwahimize kuyafuata.

Mafundisho Ya Uongo Na Utajiri Wa Kweli

3 Ikiwa mtu yeyote atafundisha mafundisho mapotovu wala hakubaliani na mafundisho manyofu ya Bwana wetu Yesu Kristo na yale ya utauwa,

4 huyo amejivuna wala hajui kitu chochote. Yeye amejaa tamaa ya mabishano na ugomvi kuhusu maneno ambavyo matokeo yake ni wivu na mapigano, maneno ya ukorofi, shuku mbaya,

5 na kuzozana kusikokoma kati ya watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli, na ambao hudhani kwamba utauwa ni njia ya kupata faida.

6 Lakini utauwa na kuridhika ni faida kubwa.

7 Kwa kuwa hatukuja humu duniani na kitu chochote, wala hatuwezi kutoka humu na kitu.

8 Lakini kama tuna chakula na mavazi, tutaridhika navyo.

9 Lakini wale watu wanaotamani kuwa na mali kwa haraka huanguka kwenye majaribu, na wamenaswa na tamaa nyingi za kipumbavu zenye kudhuru, zinazowazamisha watu katika uharibifu na maangamizi.

10 Kwa maana kupenda fedha ndiyo shina moja la maovu ya kila namna. Baadhi ya watu wakitamani fedha, wameiacha imani na kujichoma wenyewe kwa maumivu mengi.

Vitu Vizuri Vya Imani

11 Lakini wewe, mtu wa Mungu, yakimbie mambo haya yote. Fuata haki, utauwa, imani, upendo, saburi na upole.

12 Pigana vile vita vizuri vya imani. Shika uzima wa milele ambao ndio ulioitiwa ulipokiri ule ukiri mzuri mbele ya mashahidi wengi.

13 Nakuagiza mbele za Mungu avipaye vitu vyote uhai, na mbele za Kristo Yesu ambaye alipokuwa anashuhudia mbele ya Pontio Pilato alikiri ukiri mzuri,

14 uishike amri hii bila dosari wala lawama mpaka kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo,

15 ambaye Mungu atamleta kwa wakati wake mwenyewe: yeye ahimidiwaye, aliye peke yake Mtawala, Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana,

16 yeye peke yake ambaye hapatikani na mauti, na anakaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa, ambaye hakuna mwanadamu aliyemwona wala awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye milele. Amen.

17 Waagize wale ambao ni matajiri wa ulimwengu huu waache kujivuna, wala wasiweke tumaini lao katika mali ambayo si ya hakika, bali waweke tumaini lao katika Mungu ambaye hutupatia vitu vyote kwa wingi ili tuvifurahie.

18 Waagize watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, pia wawe wakarimu na walio tayari kushiriki mali zao na wengine.

19 Kwa njia hii watajiwekea hazina kama msingi kwa ajili ya wakati ujao na hivyo watajipatia uzima, yaani, ule uzima ambao ni wa kweli.

Maelekezo Ya Binafsi Na Maombi Ya Baraka

20 Timotheo, linda kile kilichowekwa amana kwako. Epuka majadiliano yasiyo ya utauwa na mabishano ambayo kwa uongo huitwa elimu,

21 ambayo wengine kwa kujidai kuwa nayo wameiacha imani.

Neema iwe nanyi. Amen.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/1TI/6-dcb4942357e748a02afbf31adbcf6280.mp3?version_id=1627—

Categories
2 Timotheo

2 Timotheo Utangulizi

Utangulizi

Huu ulikuwa waraka wa mwisho kabisa wa Paulo. Baada ya kuandika waraka wa kwanza kwa Timotheo msaidizi wake, Paulo alikamatwa na kurudishwa gerezani huko Rumi. Katika waraka huu, Paulo alihisi fursa zake za kuhubiri Injili zilikuwa zikifikia kikomo. Alimkumbusha Timotheo kwamba hata kama maisha yake hapa duniani yangekoma, Mungu alikuwa amemwandalia maisha ya milele. Paulo pia alimkumbusha juu ya uaminifu wa Mungu ambaye alikuwa amemwongoza katika maisha yake yote. Aligusia nyakati za hatari ambazo zingekuja, na siku za taabu ambapo watu wangeiacha kweli na kupenda anasa kuliko kumpenda Mungu.

Alijitahidi kumtia moyo Timotheo na kumwimarisha kwa ajili ya kazi kubwa aliyokabidhiwa. Paulo alitamani kumwona Timotheo tena, akimwomba amletee vile vitabu alivyokuwa ameviacha Troa.

Mwandishi

Mtume Paulo.

Kusudi

Kumpa maelekezo ya mwisho, na kumtia moyo Timotheo, mchungaji wa kanisa la Efeso.

Mahali

Rumi.

Tarehe

Kati ya 66-67 B.K.

Wahusika Wakuu

Paulo, Timotheo, Luka, Marko.

Wazo Kuu

Barua hii inazungumzia uweza wa Mungu juu ya vitu vyote. Ingawa kuna mateso ambayo yataendelea kuongezeka, Mungu bado anatawala.

Mambo Muhimu

Kumwelekeza Timotheo ajitahidi kujionyesha kuwa amekubalika na Mungu, mtendakazi asiye na sababu ya kuona aibu, akilitumia kwa usahihi neno la kweli.

Mgawanyo

Shukrani za Paulo kwa ajili ya Timotheo (

1:1-5

)

Maagizo ya Paulo kwa Timotheo (

1:6–2:2

)

Sifa za mtumishi mwaminifu (

2:3-26

)

Mateso yajayo (

3:1-17

)

Maneno ya mwisho (

4:1-22

).