Categories
Yeremia

Yeremia 23

Tawi La Haki

1 “Ole wao wachungaji wanaoharibu na kutawanya kondoo wa malisho yangu!” asemaBwana.

2 Kwa hiyo hili ndiloBwana, Mungu wa Israeli, analowaambia wachungaji wanaowachunga watu wangu: “Kwa sababu mmelitawanya kundi langu na kuwafukuzia mbali, wala hamkuwatunza, basi mimi nitawaadhibu kwa ajili ya uovu mliofanya,” asemaBwana.

3 “Mimi mwenyewe nitayakusanya mabaki ya kundi langu kutoka nchi zote ambazo nimewafukuzia, nami nitawarudisha katika malisho yao, mahali ambapo watazaa na kuongezeka idadi yao.

4 Nitaweka wachungaji juu yao ambao watawachunga, nao hawataogopa tena au kutishwa, wala hatapotea hata mmoja,” asemaBwana.

5 Bwanaasema, “Siku zinakuja,

nitakapomwinulia Daudi Tawi lenye haki,

Mfalme atakayetawala kwa hekima,

na kutenda lililo haki na sawa katika nchi.

6 Katika siku zake, Yuda ataokolewa

na Israeli ataishi salama.

Hili ndilo jina atakaloitwa:

BwanaHaki Yetu.

7 “Hivyo basi, siku zinakuja, wakati ambapo watu hawatasema tena, ‘Hakika kamaBwanaaishivyo, aliyewapandisha Waisraeli kutoka Misri,’

8 bali watasema, ‘Hakika kamaBwanaaishivyo, aliyewatoa wazao wa Israeli kutoka nchi ya kaskazini na nchi zote alizokuwa amewafukuzia,’ asemaBwana. Ndipo wataishi katika nchi yao wenyewe.”

Manabii Wasemao Uongo

9 Kuhusu manabii:

Moyo wangu umevunjika ndani yangu;

mifupa yangu yote inatetemeka.

Nimekuwa kama mtu aliyelewa,

kama mtu aliyelemewa na divai,

kwa sababu yaBwana

na maneno yake matakatifu.

10 Nchi imejaa wazinzi;

kwa sababu ya laana, nchi imekauka

na malisho yaliyoko nyikani yamekauka.

Mwenendo wa manabii ni mbaya

na mamlaka yao si ya haki.

11 “Nabii na kuhani wote si wacha Mungu;

hata hekaluni mwangu ninaona uovu wao,”

asemaBwana.

12 “Kwa hiyo mapito yao yatakuwa utelezi,

watafukuziwa mbali gizani

na huko wataanguka.

Nitaleta maafa juu yao

katika mwaka wa kuadhibiwa kwao,”

asemaBwana.

13 “Miongoni mwa manabii wa Samaria

nililiona jambo la kuchukiza:

Walitabiri kwa Baali

na kuwapotosha Israeli watu wangu.

14 Nako miongoni mwa manabii wa Yerusalemu

nimeona jambo baya sana:

Wanafanya uzinzi

na kuenenda katika uongo.

Wanatia nguvu mikono ya watenda mabaya,

kwa ajili hiyo hakuna yeyote

anayeachana na uovu wake.

Wote wako kama Sodoma kwangu;

watu na Yerusalemu wako kama Gomora.”

15 Kwa hiyo, hili ndiloBwanaMwenye Nguvu Zote asemalo kuhusu manabii:

“Nitawafanya wale chakula kichungu

na kunywa maji yaliyotiwa sumu,

kwa sababu kutokana na manabii wa Yerusalemu

kutokumcha Mungu kumeenea katika nchi yote.”

16 Hili ndiloBwanaMwenye Nguvu Zote asemalo:

“Msisikilize wanachowatabiria manabii,

wanawajaza matumaini ya uongo.

Wanasema maono kutoka akili zao wenyewe,

hayatoki katika kinywa chaBwana.

17 Huendelea kuwaambia wale wanaonidharau mimi,

‘Bwanaasema: Mtakuwa na amani.’

Kwa wale wote wafuatao ugumu wa mioyo yao,

wao husema, ‘Hakuna dhara litakalowapata.’

18 Lakini ni yupi miongoni mwao aliyesimama katika baraza laBwana

ili kuona au kusikia neno lake?

Ni nani aliyesikiliza

na kusikia neno lake?

19 Tazama, dhoruba yaBwana

itapasuka kwa ghadhabu,

kisulisuli kitazunguka na kuanguka

vichwani vya waovu.

20 Hasira yaBwanahaitageuka mpaka amelitimiza kusudi la moyo wake.

Siku zijazo mtalifahamu kwa wazi.

21 Mimi sikuwatuma manabii hawa,

lakini bado wamekimbia wakitangaza ujumbe wao.

Mimi sikusema nao,

lakini wametabiri.

22 Lakini kama wangesimama barazani mwangu,

wangetangaza maneno yangu kwa watu wangu,

nao wangewageuza kutoka njia zao mbaya

na kutoka matendo yao maovu.”

23 “Je, mimi ni Mungu aliyeko hapa karibu tu,”

Bwanaasema,

“wala si Mungu aliyeko pia mbali?

24 Je, mtu yeyote aweza kujificha

mahali pa siri ili nisiweze kumwona?”

Bwanaasema.

“Je, mimi sikuijaza mbingu na nchi?”

Bwanaasema.

25 “Nimesikia wanayoyasema manabii, hao wanaotabiri uongo kwa jina langu. Wanasema, ‘Nimeota ndoto! Nimeota ndoto!’

26 Mambo haya yataendelea mpaka lini ndani ya mioyo ya hawa manabii wa uongo, ambao hutabiri maono ya uongo ya akili zao wenyewe?

27 Wanadhani ndoto wanazoambiana wao kwa wao zitawafanya watu wangu walisahau jina langu, kama baba zao walivyolisahau jina langu kwa kumwabudu Baali.

28 Mwache nabii aliye na ndoto aseme ndoto yake, lakini yule aliye na neno langu na aliseme kwa uaminifu. Kwa maana jani kavu lina uhusiano gani na ngano?” asemaBwana.

29 “Je, neno langu si kama moto,” asemaBwana, “na kama nyundo ivunjayo mwamba vipande vipande?

30 “Kwa hiyo, niko kinyume na manabii wanaoibiana maneno kana kwamba ni yangu,” asemaBwana.

31 “Naam, mimi niko kinyume na manabii wanaotikisa ndimi zao wenyewe na kusema, ‘Bwanaasema.’

32 Kweli, niko kinyume na hao wanaotabiri ndoto za uongo,” asemaBwana. “Wanazisimulia na kuwapotosha watu wangu kwa uongo wao bila kujali, lakini sikuwatuma wala sikuwaamuru. Hawawafaidi watu hawa hata kidogo,” asemaBwana.

Maneno Ya Uongo Na Manabii Wa Uongo

33 “Wakati watu hawa, au nabii, au kuhani watakapokuuliza, ‘Mzigo waBwanani nini?’ wewe utawaambia, ‘Ninyi ndio mzigo. Nami nitawavua kama vazi, asemaBwana.’

34 Nabii, kuhani, au mtu yeyote akisema, ‘Huu ndio mzigo waBwana,’ nitamwadhibu huyo na nyumba yake.

35 Hivyo mnaambiana kila mmoja na mwenzake, au kwa mtu wa nyumba yao: ‘Bwanaamejibu nini?’ au ‘Bwanaamesema nini?’

36 Lakini kamwe msiseme tena, ‘Nina mzigo waBwana,’ kwa sababu kila neno la mtu binafsi linakuwa mzigo wake mwenyewe, na hivyo kupotosha maneno ya Mungu aliye hai,BwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wetu.

37 Hivi ndivyo utakavyoendelea kumuuliza nabii: ‘Bwanaamekujibu nini?’ au ‘Je,Bwanaamesema nini?’

38 Ingawa unadai, ‘Huu ndio mzigo waBwana,’ hili ndiloBwanaasemalo: Ulitumia maneno, ‘Huu ndio mzigo waBwana,’ hata ingawa nilikuambia kuwa kamwe usiseme, ‘Huu ni mzigo waBwana.’

39 Kwa hiyo, hakika nitakusahau na kukutupa mbali na uso wangu pamoja na mji niliowapa ninyi na baba zenu.

40 Nitaleta juu yako fedheha ya kudumu: yaani aibu ya kudumu ambayo haitasahaulika.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JER/23-7ce7ca3828ff1e73e6bddcedf17d0968.mp3?version_id=1627—

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *