Categories
Isaya

Isaya 49

Mtumishi Wa Bwana

1 Nisikilizeni, enyi visiwa, sikieni hili,

ninyi mataifa mlio mbali:

Kabla sijazaliwa,Bwanaaliniita,

tangu kuzaliwa kwangu, amelitaja jina langu.

2 Akafanya kinywa changu kuwa kama upanga ulionolewa,

katika uvuli wa mkono wake akanificha;

akanifanya kuwa mshale uliosuguliwa,

na kunificha katika podo lake.

3 Akaniambia, “Wewe u mtumishi wangu,

Israeli, ambaye katika yeye

nitaonyesha utukufu wangu.”

4 Lakini nilisema, “Nimetumika bure,

nimetumia nguvu zangu bure bila faida.

Hata hivyo linalonistahili liko mkononi mwaBwana,

nao ujira wangu uko kwa Mungu wangu.”

5 SasaBwanaasema:

yeye aliyeniumba tumboni kuwa mtumishi wake,

kumrudisha tena Yakobo kwake

na kumkusanyia Israeli,

kwa maana nimepata heshima machoni paBwana,

naye Mungu wangu amekuwa nguvu yangu;

6 yeye asema:

“Je, ni jambo dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu

ili kurejeza makabila ya Yakobo,

na kuwarudisha wale Waisraeli niliowahifadhi?

Pia nitakufanya uwe nuru kwa ajili ya watu wa Mataifa,

ili upate kuleta wokovu wangu hata miisho ya dunia.”

7 Hili ndilo asemaloBwana,

yeye Mkombozi na Aliye Mtakatifu wa Israeli,

kwake yeye aliyedharauliwa na kuchukiwa na taifa,

kwa mtumishi wa watawala:

“Wafalme watakuona na kusimama,

wakuu wataona na kuanguka kifudifudi,

kwa sababu yaBwana, aliye mwaminifu,

yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, aliyekuchagua wewe.”

Kurejezwa Kwa Israeli

8 Hili ndilo asemaloBwana:

“Wakati wangu uliokubalika nitakujibu,

nami katika siku ya wokovu nitakusaidia;

nitakuhifadhi, nami nitakufanya

kuwa agano kwa ajili ya watu,

ili kurudisha nchi

na kugawanyia urithi tena wale waliokuwa ukiwa,

9 kuwaambia mateka, ‘Tokeni nje,’

nao wale walio gizani, ‘Kuweni huru!’

“Watajilisha kando ya barabara

na kupata malisho yao juu ya kila kilima kilicho kitupu.

10 Hawataona njaa wala kuona kiu,

wala hari ya jangwani au jua halitawapiga.

Yeye mwenye huruma juu yao atawaonyesha njia,

na kuwaongoza kando ya chemchemi za maji.

11 Nitaifanya milima yangu yote kuwa barabara,

na njia kuu zangu zitainuliwa.

12 Tazama, watakuja kutoka mbali:

wengine kutoka kaskazini, wengine kutoka magharibi,

wengine kutoka nchi ya Sinimu.”

13 Pigeni kelele kwa furaha, enyi mbingu;

furahi, ee dunia;

pazeni sauti kwa kuimba, enyi milima!

Kwa maanaBwanaanawafariji watu wake,

naye atakuwa na huruma kwa watu wake walioumizwa.

14 Lakini Sayuni alisema, “Bwanaameniacha,

Bwana amenisahau.”

15 “Je, mama aweza kumsahau mtoto

aliyeko matitini mwake akinyonya,

wala asiwe na huruma

juu ya mtoto aliyemzaa?

Ingawa anaweza kusahau,

mimi sitakusahau wewe!

16 Tazama, nimekuchora kama muhuri

katika vitanga vya mikono yangu,

kuta zako zi mbele yangu daima.

17 Wana wako wanaharakisha kurudi,

nao wale waliokuteka wanaondoka kwako.

18 Inua macho yako ukatazame pande zote:

wana wako wote wanakusanyika na kukujia.

Kwa hakika kama vile niishivyo,

utawavaa wote kama mapambo,

na kujifunga nao kama bibi arusi,”

asemaBwana.

19 “Ingawa uliangamizwa na kufanywa ukiwa,

na nchi yako ikaharibiwa,

sasa nafasi itakuwa finyu kwa ajili ya watu wako,

nao wale waliokuangamiza watakuwa mbali sana.

20 Watoto waliozaliwa wakati wa msiba wako

bado watakuambia,

‘Mahali hapa ni finyu sana kwetu,

tupe eneo kubwa zaidi la kuishi.’

21 Ndipo utasema moyoni mwako,

‘Ni nani aliyenizalia hawa?

Nilikuwa nimefiwa, tena tasa;

nilikuwa nimehamishwa na kukataliwa.

Ni nani aliyewalea hawa?

Niliachwa peke yangu,

lakini hawa wametoka wapi?’ ”

22 Hili ndilo asemaloBwanaMwenyezi:

“Tazama, nitawaashiria watu wa Mataifa,

nitainua bendera yangu kwa mataifa;

watawaleta wana wako mikononi yao,

na kuwabeba binti zenu juu ya mabega yao.

23 Wafalme watakuwa baba zenu wa kuwalea,

na malkia wao watakuwa mama zenu wa kuwalea.

Watasujudu mbele yako nyuso zao zikigusa ardhi;

wataramba mavumbi yaliyo miguuni mwako.

Ndipo utajua ya kuwa Mimi ndimiBwana;

wale wanaonitumaini mimi hawataaibika.”

24 Je, nyara zaweza kuchukuliwa kutoka kwa mashujaa wa vita,

au mateka kuokolewa kutoka kwa watu wakali?

25 Lakini hili ndilo asemaloBwana:

“Naam, mateka watachukuliwa kutoka kwa mashujaa,

na nyara zitapokonywa kutoka kwa watu wakali.

Nitashindana na wale wanaoshindana nawe,

nami nitawaokoa watoto wako.

26 Nitawafanya wale wanaokuonea kula nyama yao wenyewe,

watalewa kwa damu yao wenyewe,

kama vile kwa mvinyo.

Ndipo wanadamu wote watajua

ya kuwa Mimi,Bwana, ni Mwokozi wako,

Mkombozi wako, niliye Mwenye Nguvu wa Yakobo.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/49-3756dc0655b9545f1a78eec34c6ba2cd.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 50

Dhambi Ya Israeli Na Utii Wa Mtumishi

1 Hili ndilo asemaloBwana:

“Iko wapi hati ya talaka ya mama yako

ambayo kwayo niliachana naye?

Au nimewauza ninyi kwa nani

miongoni mwa watu wanaonidai?

Kwa ajili ya dhambi zenu mliuzwa,

kwa sababu ya makosa, mama yenu aliachwa.

2 Nilipokuja, kwa nini hakuwepo hata mmoja?

Nilipoita, kwa nini hakuwepo hata mmoja wa kujibu?

Je, mkono wangu ni mfupi mno hata nisiweze kuwakomboa?

Je, mimi sina nguvu za kukuokoa?

Kwa kukemea tu naikausha bahari,

naigeuza mito ya maji kuwa jangwa;

samaki wake wanaoza kwa kukosa maji

na kufa kwa ajili ya kiu.

3 Ninalivika anga weusi na kufanya nguo ya gunia

kuwa kifuniko chake.”

4 BwanaMwenyezi amenipa ulimi uliofundishwa,

ili kujua neno limtegemezalo aliyechoka.

Huniamsha asubuhi kwa asubuhi,

huamsha sikio langu lisikie kama mtu afundishwaye.

5 BwanaMwenyezi amezibua masikio yangu,

nami sikuwa mwasi,

wala sikurudi nyuma.

6 Niliwapa mgongo wangu wale wanipigao,

mashavu yangu wale wangʼoao ndevu zangu;

sikuuficha uso wangu kutokana na fedheha

na kutemewa mate.

7 Kwa sababuBwanaMwenyezi ananisaidia,

sitatahayarika.

Kwa hiyo nimekaza uso wangu kama jiwe la gumegume,

nami ninajua sitaaibika.

8 Yeye anipatiaye haki yangu yu karibu.

Ni nani basi atakayeleta mashtaka dhidi yangu?

Tukabiliane uso kwa uso!

Mshtaki wangu ni nani?

Ni nani aliye mshtaki wangu?

9 NiBwanaMwenyezi anisaidiaye mimi.

Ni nani huyo atakayenihukumu?

Wote watachakaa kama vazi,

nondo watawala wawamalize.

10 Ni nani miongoni mwenu amchayeBwana,

na kulitii neno la mtumishi wake?

Yeye atembeaye gizani,

yeye asiye na nuru,

na alitumainie jina laBwana,

na amtegemee Mungu wake.

11 Lakini sasa, ninyi nyote mnaowasha mioto,

na kupeana mienge iwakayo ninyi kwa ninyi,

nendeni, tembeeni katika nuru ya moto wenu

na ya mienge mliyoiwasha.

Hili ndilo mtakalolipokea kutoka mkononi mwangu:

Mtalala chini kwa mateso makali.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/50-ebb04f50960cdafa3d3403a8043fd55d.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 51

Wokovu Wa Milele Kwa Sayuni

1 “Nisikilizeni, ninyi mnaofuatia haki

na mnaomtafutaBwana:

Tazameni mwamba ambako mlichongwa,

na mahali pa kuvunjia mawe ambako mlichimbwa;

2 mwangalieni Abrahamu, baba yenu,

na Sara, ambaye aliwazaa.

Wakati nilipomwita alikuwa mmoja tu,

nami nikambariki na kumfanya kuwa wengi.

3 HakikaBwanaataifariji Sayuni,

naye atayaangalia kwa huruma magofu yake yote;

atayafanya majangwa yake yawe kama Edeni,

nazo sehemu zake zisizolimika ziwe kama bustani yaBwana.

Shangwe na furaha zitakuwako ndani yake,

shukrani na sauti za kuimba.

4 “Nisikilizeni, watu wangu;

nisikieni, taifa langu:

Sheria itatoka kwangu;

haki yangu itakuwa nuru kwa mataifa.

5 Haki yangu inakaribia mbio,

wokovu wangu unakuja,

nao mkono wangu utaleta hukumu kwa mataifa.

Visiwa vitanitegemea

na kungojea mkono wangu kwa matumaini.

6 Inueni macho yenu mbinguni,

mkaitazame dunia chini;

mbingu zitatoweka kama moshi,

dunia itachakaa kama vazi,

na wakazi wake kufa kama mainzi.

Bali wokovu wangu utadumu milele,

haki yangu haitakoma kamwe.

7 “Nisikieni, ninyi mnaojua lililo sawa,

ninyi watu ambao mna sheria yangu mioyoni mwenu:

Msiogope mashutumu ya wanadamu

wala msitiwe hofu na matukano yao.

8 Kwa maana nondo atawala kama vazi,

nao funza atawatafuna kama sufu.

Lakini haki yangu itadumu milele,

wokovu wangu kwa vizazi vyote.”

9 Amka, Amka! Jivike nguvu,

ewe mkono waBwana,

Amka, kama siku zilizopita,

kama vile vizazi vya zamani.

Si ni wewe uliyemkata Rahabu vipande vipande,

uliyemchoma yule joka?

10 Si ni wewe uliyekausha bahari,

maji ya kilindi kikuu,

uliyefanya barabara katika vilindi vya bahari

ili waliokombolewa wapate kuvuka?

11 Wale waliolipiwa fidia naBwanawatarudi.

Wataingia Sayuni wakiimba;

furaha ya milele itakuwa taji juu ya vichwa vyao.

Furaha na shangwe zitawapata,

huzuni na kulia kwa uchungu kutatoweka.

12 “Mimi, naam mimi,

ndimi niwafarijie ninyi.

Ninyi ni nani hata kuwaogopa

wanadamu wanaokufa,

wanadamu ambao ni majani tu,

13 kwamba mnamsahauBwanaMuumba wenu,

aliyezitanda mbingu

na kuiweka misingi ya dunia,

kwamba mnaishi katika hofu siku zote

kwa sababu ya ghadhabu ya mdhalimu,

ambaye nia yake ni kuangamiza?

Iko wapi basi ghadhabu ya mdhalimu?

14 Wafungwa waliojikunyata kwa hofu

watawekwa huru karibuni;

hawatafia kwenye gereza lao,

wala hawatakosa chakula.

15 Kwa maana Mimi ndimiBwana, Mungu wako,

ambaye huisukasuka bahari ili mawimbi yake yangurume:

BwanaMwenye Nguvu Zote ndilo jina lake.

16 Nimeweka maneno yangu kinywani mwako

na kukufunika kwa uvuli wa mkono wangu:

Mimi niliyeweka mbingu mahali pake,

niliyeweka misingi ya dunia,

niwaambiaye Sayuni,

‘Ninyi ni watu wangu.’ ”

Kikombe Cha Ghadhabu Ya Bwana

17 Amka, amka!

Simama, ee Yerusalemu,

wewe uliyekunywa kutoka mkono waBwana

kikombe cha ghadhabu yake,

wewe uliyekunywa mpaka kufikia machujo yake,

kikombe kile cha kunywea

kiwafanyacho watu kuyumbayumba.

18 Kati ya wana wote aliowazaa

hakuwepo hata mmoja wa kumwongoza,

kati ya wana wote aliowalea

hakuwepo hata mmoja wa kumshika mkono.

19 Majanga haya mawili yamekuja juu yako:

ni nani awezaye kukufariji?

Maangamizi, uharibifu, njaa na upanga:

ni nani awezaye kukutuliza?

20 Wana wako wamezimia,

wamelala kwenye mwanzo wa kila barabara,

kama swala aliyenaswa kwenye wavu.

Wamejazwa na ghadhabu yaBwana

na makaripio ya Mungu wako.

21 Kwa hiyo sikiliza hili, wewe uliyeteswa,

uliyelewa, lakini si kwa mvinyo.

22 Hili ndilo asemaloBwanaMwenyezi wako,

Mungu wako, yeye ambaye huwatetea watu wake:

“Tazama, nimeondoa mkononi mwako

kikombe kilichokufanya uyumbayumbe;

kutoka kikombe hicho,

kikombe cha kunywa cha ghadhabu yangu,

kamwe hutakunywa tena.

23 Nitakiweka mikononi mwa watesi wako,

wale waliokuambia,

‘Anguka kifudifudi

ili tuweze kutembea juu yako.’

Ukaufanya mgongo wako kama ardhi,

kama njia yao ya kupita.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/51-f745b61a926dc7b2dcdcd68d4df3598b.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 52

1 Amka, amka, ee Sayuni,

jivike nguvu.

Vaa mavazi yako ya fahari,

ee Yerusalemu, mji mtakatifu.

Asiyetahiriwa na aliye najisi

hataingia kwako tena.

2 Jikungʼute mavumbi yako,

inuka, uketi kwenye kiti cha enzi, ee Yerusalemu.

Jifungue minyororo iliyo shingoni mwako,

ee Binti Sayuni uliye mateka.

3 Kwa kuwa hili ndilo asemaloBwana:

“Mliuzwa pasipo malipo,

nanyi mtakombolewa bila fedha.”

4 Kwa maana hili ndilo asemaloBwanaMwenyezi:

“Hapo kwanza watu wangu walishuka Misri kuishi,

hatimaye, Ashuru wakawaonea.

5 “Basi sasa nina nini hapa?” asemaBwana.

“Kwa kuwa watu wangu wamechukuliwa pasipo malipo,

nao wale wanaowatawala wanawadhihaki,”

asemaBwana.

“Mchana kutwa

jina langu limetukanwa bila kikomo.

6 Kwa hiyo watu wangu watalijua Jina langu;

kwa hiyo katika siku ile watajua

kwamba ndimi niliyetangulia kulisema.

Naam, ni mimi.”

7 Tazama jinsi miguu ya wale waletao habari njema

ilivyo mizuri juu ya milima,

wale wanaotangaza amani,

wanaoleta habari njema,

wanaotangaza wokovu,

wauambiao Sayuni,

“Mungu wako anatawala!”

8 Sikiliza! Walinzi wako wanapaza sauti zao,

pamoja wanapaza sauti zao kwa furaha.

WakatiBwanaatakaporejea Sayuni,

wataliona kwa macho yao wenyewe.

9 Pazeni sauti ya nyimbo za furaha pamoja,

enyi magofu ya Yerusalemu,

kwa maanaBwanaamewafariji watu wake,

ameikomboa Yerusalemu.

10 Mkono mtakatifu waBwanaumefunuliwa

machoni pa mataifa yote,

nayo miisho yote ya dunia itaona

wokovu wa Mungu wetu.

11 Ondokeni, ondokeni, tokeni huko!

Msiguse kitu chochote kilicho najisi!

Tokeni kati yake mwe safi,

ninyi mchukuao vyombo vyaBwana.

12 Lakini hamtaondoka kwa haraka,

wala hamtakwenda kwa kukimbia;

kwa maanaBwanaatatangulia mbele yenu,

Mungu wa Israeli atakuwa mlinzi nyuma yenu.

Mateso Na Utukufu Wa Mtumishi

13 Tazama, mtumishi wangu atatenda kwa hekima;

atatukuzwa, na kuinuliwa juu, na kukwezwa sana.

14 Kama walivyokuwa wengi

walioshangazwa naye,

kwani uso wake ulikuwa umeharibiwa sana

zaidi ya mtu yeyote

na umbo lake kuharibiwa

zaidi ya mfano wa mwanadamu:

15 hivyo atayashangaza mataifa mengi,

nao wafalme watafunga vinywa vyao kwa sababu yake.

Kwa kuwa yale ambayo hawakuambiwa, watayaona,

nayo yale wasiyoyasikia, watayafahamu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/52-60ccd17162f8f971ccf3535f61e23995.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 53

1 Ni nani aliyeamini ujumbe wetu,

na mkono waBwanaumefunuliwa kwa nani?

2 Alikua mbele yake kama mche mwororo

na kama mzizi katika nchi kavu.

Hakuwa na uzuri wala utukufu wa kutuvutia kwake,

hakuwa na chochote katika sura yake cha kutufanya tumtamani.

3 Alidharauliwa na kukataliwa na wanadamu,

mtu wa huzuni nyingi, ajuaye mateso.

Kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao,

alidharauliwa, wala hatukumhesabu kuwa kitu.

4 Hakika alichukua udhaifu wetu

na akajitwika huzuni zetu,

hata hivyo tulidhania kuwa amepigwa na Mungu,

akapigwa sana naye, na kuteswa.

5 Lakini alitobolewa kwa ajili ya makosa yetu,

alichubuliwa kwa ajili ya maovu yetu;

adhabu iliyotuletea sisi amani ilikuwa juu yake,

na kwa majeraha yake sisi tumepona.

6 Sisi sote, kama kondoo, tumepotea,

kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe,

nayeBwanaaliweka juu yake

maovu yetu sisi sote.

7 Alionewa na kuteswa,

hata hivyo hakufungua kinywa chake;

aliongozwa kama mwana-kondoo

apelekwaye machinjoni,

kama vile kondoo anyamazavyo mbele ya wao wamkataye manyoya,

hivyo hakufungua kinywa chake.

8 Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa.

Nani awezaye kueleza kuhusu kizazi chake?

Kwa maana alikatiliwa mbali na nchi ya walio hai,

alipigwa kwa ajili ya makosa ya watu wangu.

9 Wakamfanyia kaburi pamoja na waovu,

pamoja na matajiri katika kifo chake,

ingawa hakutenda jeuri,

wala hapakuwa na hila kinywani mwake.

10 Lakini yalikuwa ni mapenzi yaBwana

kumchubua na kumsababisha ateseke.

IngawaBwanaamefanya maisha yake

kuwa sadaka ya hatia,

ataona uzao wake na kuishi siku nyingi,

nayo mapenzi yaBwanayatafanikiwa mkononi mwake.

11 Baada ya maumivu ya nafsi yake,

ataona nuru ya uzima na kuridhika;

kwa maarifa yake, mtumishi wangu mwenye haki

atawafanya wengi kuwa wenye haki,

naye atayachukua maovu yao.

12 Kwa hiyo nitamgawia sehemu miongoni mwa wakuu,

naye atagawana nyara pamoja na wenye nguvu,

kwa sababu aliyamimina maisha yake hadi mauti,

naye alihesabiwa pamoja na wakosaji.

Kwa kuwa alichukua dhambi za wengi,

na kuwaombea wakosaji.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/53-ace0856423d7685405dade8d355f362b.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 54

Utukufu Wa Baadaye Wa Sayuni

1 “Imba, ewe mwanamke tasa,

wewe ambaye kamwe hukuzaa mtoto;

paza sauti kwa kuimba, piga kelele kwa furaha,

wewe ambaye kamwe hukupata utungu;

kwa sababu watoto wa mwanamke aliyeachwa ukiwa ni wengi

kuliko wa mwanamke mwenye mume,”

asemaBwana.

2 “Panua mahali pa hema lako,

tandaza mapazia ya hema lako uyaeneze mbali,

wala usiyazuie;

ongeza urefu wa kamba zako,

imarisha vigingi vyako.

3 Kwa maana utaenea upande wa kuume

na upande wa kushoto;

wazao wako watayamiliki mataifa

na kukaa katika miji yao iliyoachwa ukiwa.

4 “Usiogope, wewe hutaaibika.

Usiogope aibu, wewe hutaaibishwa.

Wewe utasahau aibu ya ujana wako,

wala hutakumbuka tena mashutumu ya ujane wako.

5 Kwa maana Muumba wako ndiye mume wako,

BwanaMwenye Nguvu Zote ndilo jina lake,

yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli ni Mkombozi wako,

yeye anaitwa Mungu wa dunia yote.

6 Bwanaatakuita urudi

kana kwamba ulikuwa mke aliyeachwa na kuhuzunishwa rohoni;

kama mke aliyeolewa bado angali kijana

na kukataliwa,” asema Mungu wako.

7 “Kwa kitambo kidogo nilikuacha,

lakini kwa huruma nyingi nitakurudisha.

8 Katika ukali wa hasira

nilikuficha uso wangu kwa kitambo,

lakini kwa fadhili za milele

nitakuwa na huruma juu yako,”

asemaBwanaMkombozi wako.

9 “Kwangu mimi jambo hili ni kama siku za Noa,

nilipoapa kuwa maji ya Noa kamwe hayatafunika tena dunia.

Hivyo sasa nimeapa sitawakasirikia ninyi,

kamwe sitawakemea tena.

10 Ijapotikisika milima, na vilima viondolewe,

hata hivyo upendo wangu usiokoma kwenu hautatikisika,

wala agano langu la amani halitaondolewa,”

asemaBwana, mwenye huruma juu yenu.

11 “Ewe mji uliyeteswa, uliyepigwa kwa dhoruba na usiyetulizwa,

nitakujenga kwa almasi, nitaweka misingi yako kwa yakuti samawi.

12 Nitafanya minara yako ya akiki,

malango yako kwa vito vingʼaavyo,

nazo kuta zako zote za vito vya thamani.

13 Watoto wako wote watafundishwa naBwana,

nayo amani ya watoto wako itakuwa kuu.

14 Kwa haki utathibitika:

Kuonewa kutakuwa mbali nawe;

hutaogopa chochote.

Hofu itakuwa mbali nawe;

haitakukaribia wewe.

15 Kama mtu yeyote akikushambulia,

haitakuwa kwa ruhusa yangu;

yeyote akushambuliaye

atajisalimisha kwako.

16 “Tazama, ni mimi niliyemuumba mhunzi,

yeye afukutaye makaa kuwa moto,

na kutengeneza silaha inayofaa kwa kazi yake.

Tena ni mimi niliyemwambia mharabu

kufanya uharibifu mwingi.

17 Hakuna silaha itakayofanyizwa dhidi yako

itakayofanikiwa,

nawe utauthibitisha kuwa mwongo

kila ulimi utakaokushtaki.

Huu ndio urithi wa watumishi waBwana

na hii ndiyo haki yao itokayo kwangu,”

asemaBwana.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/54-8a15f0a458827af4e4b879f5f7f872ed.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 55

Mwaliko Kwa Wenye Kiu

1 “Njooni, ninyi nyote wenye kiu,

njooni kwenye maji;

nanyi ambao hamna fedha,

njooni, nunueni na mle!

Njooni, nunueni divai na maziwa

bila fedha na bila gharama.

2 Kwa nini kutumia fedha kwa kitu ambacho si chakula,

na kutaabikia kitu kisichoshibisha?

Sikilizeni, nisikilizeni mimi na mle kilicho kizuri,

nazo nafsi zenu zitafurahia utajiri wa unono.

3 Tegeni sikio mje kwangu,

nisikieni mimi, ili nafsi zenu zipate kuishi.

Nitafanya agano la milele nanyi,

pendo la uaminifu nililomwahidi Daudi.

4 Tazama, nimemfanya kuwa shahidi wa mataifa,

kiongozi na jemadari wa mataifa.

5 Hakika utaita mataifa usiyoyajua,

nayo mataifa yale yasiyokujua yataharakisha kukujia,

kwa sababu yaBwanaMungu wako,

yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli,

kwa maana amekutukuza.”

6 MtafuteniBwanamaadamu anapatikana;

mwiteni maadamu yu karibu.

7 Mtu mwovu na aiache njia yake,

na mtu mbaya na ayaache mawazo yake.

Yeye na amrudieBwana, naye atamrehemu,

arudi kwa Mungu wetu, kwa kuwa atamsamehe bure kabisa.

8 “Kwa kuwa mawazo yangu si mawazo yenu,

wala njia zenu si njia zangu,”

asemaBwana.

9 “Kama vile mbingu zilivyo juu kuliko dunia,

ndivyo njia zangu zilivyo juu kuliko njia zenu

na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.

10 Kama vile mvua na theluji

ishukavyo kutoka mbinguni,

nayo hairudi tena huko

bila kunywesha dunia

na kuichipusha na kuistawisha,

hivyo hutoa mbegu kwa mpanzi

na mkate kwa mlaji,

11 ndivyo lilivyo neno langu lile litokalo kinywani mwangu:

Halitanirudia tupu,

bali litatimiliza lile nililokusudia

na litafanikiwa katika kusudi lile nililolituma.

12 Mtatoka nje kwa furaha

na kuongozwa kwa amani;

milima na vilima

vitapaza sauti kwa nyimbo mbele yenu,

nayo miti yote ya shambani

itapiga makofi.

13 Badala ya kichaka cha miiba

itaota miti ya misunobari,

na badala ya michongoma

utaota mhadasi.

Hili litakuwa jambo la kumpatiaBwanajina,

kwa ajili ya ishara ya milele,

ambayo haitaharibiwa.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/55-979465adb21391b486fb7a9609b44d28.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 56

Wokovu Kwa Ajili Ya Wengine

1 Hili ndilo asemaloBwana:

“Dumisheni haki

na mkatende lile lililo sawa,

kwa maana wokovu wangu u karibu

na haki yangu itafunuliwa upesi.

2 Amebarikiwa mtu yule atendaye hili,

mtu yule alishikaye kwa uthabiti,

yeye ashikaye Sabato bila kuinajisi,

auzuiaye mkono wake usifanye uovu wowote.”

3 Usimwache mgeni aambatanaye naBwanaaseme,

“HakikaBwanaatanitenga na watu wake.”

Usimwache towashi yeyote alalamike akisema,

“Mimi ni mti mkavu tu.”

4 Kwa kuwa hili ndilo asemaloBwana:

“Kwa matowashi washikao Sabato zangu,

ambao huchagua kile kinachonipendeza

na kulishika sana agano langu:

5 hao nitawapa ndani ya Hekalu langu na kuta zake

kumbukumbu na jina bora

kuliko kuwa na watoto wa kiume na wa kike:

nitawapa jina lidumulo milele,

ambalo halitakatiliwa mbali.

6 Wageni wanaoambatana naBwana

ili kumtumikia,

kulipenda jina laBwana,

na kumwabudu yeye,

wote washikao Sabato bila kuinajisi

na ambao hushika sana agano langu:

7 hawa nitawaleta kwenye mlima wangu mtakatifu

na kuwapa furaha ndani ya nyumba yangu ya sala.

Sadaka zao za kuteketeza na dhabihu zao

zitakubalika juu ya madhabahu yangu;

kwa maana nyumba yangu itaitwa

nyumba ya sala kwa mataifa yote.”

8 BwanaMwenyezi asema, yeye awakusanyaye

Waisraeli waliohamishwa:

“Bado nitawakusanya wengine kwao

zaidi ya hao ambao wamekusanywa tayari.”

Mashtaka Ya Mungu Dhidi Ya Waovu

9 Njooni, enyi wanyama wote wa kondeni,

njooni mle, ninyi wanyama wote wa mwituni!

10 Walinzi wa Israeli ni vipofu,

wote wamepungukiwa na maarifa;

wote ni mbwa walio bubu,

hawawezi kubweka;

hulala na kuota ndoto,

hupenda kulala.

11 Ni mbwa wenye tamaa kubwa,

kamwe hawatosheki.

Wao ni wachungaji waliopungukiwa na ufahamu;

wote wamegeukia njia yao wenyewe,

kila mmoja hutafuta faida yake mwenyewe.

12 Kila mmoja hulia, “Njooni, tupate mvinyo!

Tunywe kileo sana!

Kesho itakuwa kama leo,

au hata bora zaidi.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/56-27fcdddbb4db5bf23fb1c37da12ab46c.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 57

Ibada Ya Sanamu Ya Israeli Iliyo Batili

1 Mwenye haki hupotea,

wala hakuna hata mmoja awazaye hilo moyoni mwake;

watu wanaomcha Mungu huondolewa,

wala hakuna hata mmoja anayeelewa

kuwa wenye haki wameondolewa

ili wasipatikane na maovu.

2 Wale waendao kwa unyofu

huwa na amani;

hupata pumziko walalapo mautini.

3 “Lakini ninyi:

Njooni hapa, ninyi wana wa wachawi,

ninyi wazao wa wazinzi na makahaba!

4 Mnamdhihaki nani?

Ni nani mnayemcheka kwa dharau,

na kumtolea ndimi zenu?

Je, ninyi si watoto wa waasi,

uzao wa waongo?

5 Mnawaka tamaa katikati ya mialoni

na chini ya kila mti uliotanda matawi;

mnawatoa kafara watoto wenu kwenye mabonde

na chini ya majabali yenye mianya.

6 “Sanamu zilizo katikati ya mawe laini ya mabondeni ndizo fungu lenu;

hizo ndizo sehemu yenu.

Naam, kwa hizo mmemimina sadaka za vinywaji,

na kutoa sadaka za nafaka.

Katika haya yote,

niendelee kuona huruma?

7 Umeweka kitanda chako juu kwenye kilima kirefu kilichoinuka,

huko ulikwenda kutoa dhabihu zako.

8 Nyuma ya milango yako na miimo yako

umeweka alama zako za kipagani.

Kwa kuniacha mimi, ulifunua kitanda chako,

umepanda juu yake na kukipanua sana;

ulifanya patano na wale ambao unapenda vitanda vyao,

nawe uliangalia uchi wao.

9 Ulikwenda kwa Molekiukiwa na mafuta ya zeituni,

na ukaongeza manukato yako.

Ukawatuma wajumbe wako mbali sana,

ukashuka kwenye kaburilenyewe!

10 Ulikuwa umechoshwa na njia zako zote,

lakini hukusema, ‘Hakuna tumaini.’

Ulipata uhuisho wa nguvu zako,

kwa sababu hiyo hukuzimia.

11 “Ni nani uliyemhofu hivyo na kumwogopa

hata ukawa mwongo kwangu,

wala hukunikumbuka

au kutafakari hili moyoni mwako?

Si ni kwa sababu nimekuwa kimya muda mrefu

hata huniogopi?

12 Nitaifunua haki yako na matendo yako,

nayo hayatakufaidi.

13 Utakapolia kwa kuhitaji msaada,

sanamu zako ulizojikusanyia na zikuokoe!

Upepo utazipeperusha zote,

pumzi peke yake itazipeperusha,

Lakini mtu atakayenifanya kimbilio lake,

atairithi nchi

na kuumiliki mlima wangu mtakatifu.”

Faraja Kwa Wenye Majuto

14 Tena itasemwa:

“Jengeni, jengeni, itengenezeni njia!

Ondoeni vikwazo katika njia ya watu wangu.”

15 Kwa maana hili ndilo asemalo Aliye juu, yeye aliyeinuliwa sana,

yeye aishiye milele, ambaye jina lake ni Mtakatifu:

“Ninaishi mimi mahali palipoinuka na patakatifu,

lakini pia pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu

na mwenye roho ya unyenyekevu,

ili kuzihuisha roho za wanyenyekevu

na kuihuisha mioyo yao waliotubu.

16 Sitaendelea kulaumu milele,

wala sitakasirika siku zote,

kwa kuwa roho ya mwanadamu

ingezimia mbele zangu:

yaani pumzi ya mwanadamu niliyemuumba.

17 Nilighadhibika na tamaa yake ya dhambi;

nilimwadhibu, nikauficha uso wangu kwa hasira,

na bado aliendelea katika njia zake za tamaa.

18 Nimeziona njia zake, lakini nitamponya,

nitamwongoza na kumrudishia upya faraja,

19 nikiumba sifa midomoni ya waombolezaji

katika Israeli.

Amani, amani, kwa wale walio mbali

na kwa wale walio karibu,”

asemaBwana. “Nami nitawaponya.”

20 Bali waovu ni kama bahari ichafukayo,

ambayo haiwezi kutulia,

mawimbi yake hutupa takataka na matope.

21 Mungu wangu asema,

“Hakuna amani kwa waovu.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/57-5d612401288fe3f4bde3fa1583fde07c.mp3?version_id=1627—

Categories
Isaya

Isaya 58

Mfungo Wa Kweli

1 “Piga kelele, usizuie.

Paza sauti yako kama tarumbeta.

Watangazieni watu wangu uasi wao,

na kwa nyumba ya Yakobo dhambi zao.

2 Kwa maana kila siku hunitafuta,

wanaonekana kutaka kujua njia zangu,

kana kwamba walikuwa taifa linalotenda lililo sawa,

na ambalo halijaziacha amri za Mungu wake.

Hutaka kwangu maamuzi ya haki,

nao hutamani Mungu awakaribie.

3 Wao husema, ‘Mbona tumefunga, nawe hujaona?

Mbona tumejinyenyekeza, nawe huangalii?’

“Lakini katika siku ya kufunga kwenu, mnafanya mnavyotaka

na kuwadhulumu wafanyakazi wenu wote.

4 Kufunga kwenu huishia kwenye magomvi na mapigano,

na kupigana ninyi kwa ninyi kwa ngumi za uovu.

Hamwezi kufunga kama mnavyofanya leo

na kutazamia sauti zenu kusikiwa huko juu.

5 Je, hii ndiyo aina ya mfungo niliouchagua,

siku moja tu ya mtu kujinyenyekeza?

Je, ni kwa kuinamisha kichwa chini kama tete,

na kwa kujilaza juu ya nguo ya gunia na majivu?

Je, huo ndio mnaouita mfungo,

siku iliyokubalika kwaBwana?

6 “Je, hii si ndiyo aina ya mfungo niliyoichagua:

kufungua minyororo ya udhalimu,

na kufungua kamba za nira,

kuwaweka huru walioonewa,

na kuvunja kila nira?

7 Je, sio kushirikiana chakula chako na wenye njaa

na kuwapatia maskini wasiokuwa na makao hifadhi,

unapomwona aliye uchi, umvike,

wala si kumkimbia mtu wa nyama na damu yako mwenyewe?

8 Ndipo nuru yako itajitokeza kama mapambazuko

na uponyaji wako utatokea upesi;

ndipo haki yako itakapokutangulia mbele yako,

na utukufu waBwanautakuwa mlinzi nyuma yako.

9 Ndipo utaita, nayeBwanaatajibu,

utalia kuomba msaada,

naye atasema: Mimi hapa.

“Kama ukiiondoa nira ya udhalimu,

na kunyoosha kidole na kuzungumza maovu,

10 nanyi kama mkimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi zenu

na kutosheleza mahitaji ya walioonewa,

ndipo nuru yenu itakapongʼaa gizani,

nao usiku wenu utakuwa kama adhuhuri.

11 Bwanaatakuongoza siku zote,

atayatosheleza mahitaji yako katika nchi kame,

naye ataitia nguvu mifupa yako.

Utakuwa kama bustani iliyonyweshwa vizuri,

kama chemchemi ambayo maji yake hayakauki kamwe.

12 Watu wako watajenga tena magofu ya zamani

na kuinua misingi ya kale;

utaitwa Mwenye Kukarabati Kuta Zilizobomoka,

Mwenye Kurejeza Barabara za Makao.

13 “Kama ukitunza miguu yako isivunje Sabato,

na kutokufanya kama vile upendavyo katika siku yangu takatifu,

kama ukiita Sabato siku ya furaha

na siku takatifu yaBwanaya kuheshimiwa,

kama utaiheshimu kwa kutoenenda

katika njia zako mwenyewe,

na kutokufanya yakupendezayo

au kusema maneno ya upuzi,

14 ndipo utakapojipatia furaha yako katikaBwana,

nami nitakufanya upande juu ya miinuko ya nchi

na kusherehekea urithi wa Yakobo baba yako.”

Kinywa chaBwanakimenena haya.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/58-c7382a8cff973714fa434a93b7cf7d85.mp3?version_id=1627—