Categories
Mwanzo

Mwanzo 30

1 Raheli alipoona hamzalii Yakobo watoto, akamwonea ndugu yake wivu. Hivyo akamwambia Yakobo, “Nipe watoto, la sivyo nitakufa!”

2 Yakobo akamkasirikia, akamwambia, “Je, mimi ni badala ya Mungu, ambaye amekuzuia usizae watoto?”

3 Ndipo Raheli akamwambia, “Hapa yupo Bilha, mtumishi wangu wa kike. Kutana naye kimwili ili aweze kunizalia watoto na kwa kupitia yeye mimi pia niweze kuwa na uzao.”

4 Hivyo Raheli akampa Yakobo Bilha awe mke wake. Yakobo akakutana naye kimwili,

5 Bilha akapata mimba, naye akamzalia Yakobo mwana.

6 Ndipo Raheli akasema, “Mungu amenipa haki yangu, amesikiliza maombi yangu na kunipa mwana.” Kwa sababu hiyo akamwita Dani.

7 Bilha mtumishi wa kike wa Raheli akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mwana wa pili.

8 Ndipo Raheli akasema, “Nilikuwa na mashindano makubwa na ndugu yangu, nami nimeshinda.” Kwa hiyo akamwita Naftali.

9 Lea alipoona kuwa amekoma kuzaa watoto, alimchukua mtumishi wake wa kike Zilpa, naye akampa Yakobo awe mke wake.

10 Mtumishi wa Lea yaani Zilpa, akamzalia Yakobo mwana.

11 Ndipo Lea akasema, “Hii ni bahati nzuri aje!” Kwa hiyo akamwita Gadi.

12 Mtumishi wa kike wa Lea akamzalia Yakobo mwana wa pili.

13 Ndipo Lea aliposema, “Jinsi gani nilivyo na furaha! Wanawake wataniita furaha.” Kwa hiyo akamwita Asheri.

14 Wakati wa kuvuna ngano, Reubeni akaenda shambani akakuta tunguja, ambazo alizileta kwa Lea mama yake. Raheli akamwambia Lea, “Tafadhali nakuomba unipe baadhi ya tunguja za mwanao.”

15 Lakini Lea akamwambia, “Haikukutosha kumtwaa mume wangu? Je, utachukua na tunguja za mwanangu pia?”

Raheli akasema, “Vema sana! Yakobo atakutana nawe kimwili leo usiku, kwa malipo ya tunguja za mwanao.”

16 Kwa hiyo Yakobo alipokuja kutoka shambani jioni ile, Lea akaenda kumlaki, akamwambia, “Lazima ukutane nami kimwili. Nimekukodisha kwa tunguja za mwanangu.” Kwa hiyo akakutana naye kimwili usiku ule.

17 Mungu akamsikiliza Lea, naye akapata mimba akamzalia Yakobo mwana wa tano.

18 Ndipo Lea akasema, “Mungu amenizawadia kwa kumpa mume wangu mtumishi wangu wa kike.” Kwa hiyo akamwita Isakari.

19 Lea akapata mimba tena akamzalia Yakobo mwana wa sita.

20 Ndipo Lea aliposema, “Mungu amenizawadia kwa zawadi ya thamani sana. Wakati huu mume wangu ataniheshimu kwa sababu nimemzalia wana sita.” Kwa hiyo akamwita Zabuloni.

21 Baadaye akamzaa mtoto wa kike akamwita Dina.

22 Ndipo Mungu akamkumbuka Raheli, akasikia maombi yake na akafungua tumbo lake.

23 Akapata mimba na akamzaa mwana na kusema, “Mungu ameniondolea aibu yangu.”

24 Akamwita Yosefuna kusema, “Bwanana anipe mwana mwingine.”

Makundi Ya Yakobo Yaongezeka

25 Baada ya Raheli kumzaa Yosefu, Yakobo akamwambia Labani, “Nipe ruhusa nirudi katika nchi yangu.

26 Nipe wake zangu na watoto, ambao nimetumika kuwapata, nami niende zangu. Unajua ni kazi kiasi gani ambayo nimekufanyia.”

27 Lakini Labani akamwambia, “Ikiwa nimepata kibali machoni pako, tafadhali ukae. Nimegundua kwa njia ya uaguzi kwambaBwanaamenibariki kwa sababu yako.”

28 Akaongeza kumwambia, “Taja ujira wako nami nitakulipa.”

29 Yakobo akamwambia, “Unajua jinsi ambavyo nimekutumikia na jinsi ambavyo wanyama wako walivyolishwa vizuri chini ya uangalizi wangu.

30 Kidogo ulichokuwa nacho kabla sijaja kimeongezeka sana, nayeBwanaamekubariki popote nilipokuwa. Lakini sasa, ni lini nitashughulikia mambo ya nyumba yangu mwenyewe?”

31 Labani akamuuliza, “Nikupe nini?”

Yakobo akamjibu, “Usinipe chochote lakini kama utanifanyia jambo hili moja, nitaendelea kuchunga na kuyaangalia makundi yako.

32 Niruhusu nipite katika makundi yako yote leo niondoe humo kila kondoo mwenye mabakabaka au madoadoa, kila mwana-kondoo mweusi na kila mbuzi mwenye madoadoa au mabakabaka. Hawa watakuwa ujira wangu.

33 Uadilifu wangu utanishuhudia siku zijazo, kila utakapochunguza ujira ambao umenilipa mimi. Mbuzi yeyote wangu ambaye hana mabakabaka wala madoadoa, au mwana-kondoo ambaye si mweusi, atahesabika ameibwa.”

34 Labani akasema, “Ninakubali na iwe kama ulivyosema.”

35 Siku ile ile Yakobo akawaondoa beberu wote waliokuwa na mistari au madoadoa na mbuzi wake wote waliokuwa na mistari au madoadoa (wote waliokuwa na alama nyeupe juu yao) na wana-kondoo weusi wote, akawaweka chini ya uangalizi wa wanawe.

36 Kisha Labani akamwacha Yakobo kwa mwendo wa safari ya siku tatu kati yake na Yakobo, wakati Yakobo akiendelea kuchunga lile kundi la Labani lililobaki.

37 Hata hivyo, Yakobo, akachukua fito mbichi zilizokatwa wakati huo huo za miti ya mlubna, mlozi na mwaramoni akazibambua ili mistari myeupe ionekane katika fito hizo.

38 Kisha akaweka fito alizozibambua kwenye mabirika yote ya kunyweshea mifugo, ili ziwe mbele ya makundi walipokuja kunywa maji. Wanyama walipokuja kunywa maji, hali wakiwa wanahitaji mbegu,

39 wakapandwa hizo fito zikiwa mbele yao. Wanyama waliopata mimba mbele ya hizo fito walizaa wanyama wenye mistari, madoadoa na mabakabaka.

40 Yakobo akawatenga wadogo wa kundi peke yao, lakini akazielekeza nyuso za hao waliobaki kwenye wale wenye mistari na weusi waliokuwa mali ya Labani. Hivyo akatenga makundi yake mwenyewe, na wala hakuwachanganya na wanyama wa Labani.

41 Kila mara wanyama wenye nguvu walipohitaji mbegu, Yakobo aliweka zile fito kwenye mabirika mbele ya hao wanyama, ili wapandwe karibu na hizo fito,

42 lakini ikiwa wanyama walikuwa wadhaifu hakuziweka hizo fito. Hivyo wanyama wadhaifu wakawa wa Labani, na wanyama wenye nguvu wakawa wa Yakobo.

43 Kwa njia hii Yakobo akastawi sana, tena akawa na makundi makubwa, watumishi wa kike na wa kiume na ngamia na punda.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/GEN/30-a582da6d02c6ee2fa5cb91f4c76a4ae2.mp3?version_id=1627—

Categories
Mwanzo

Mwanzo 31

Yakobo Akimbia Kutoka Kwa Labani

1 Yakobo akawasikia wana wa Labani wakisema, “Yakobo amechukua kila kitu kilichokuwa cha baba yetu naye amepata utajiri huu wote kutokana na vile vilivyokuwa mali ya baba yetu.”

2 Yakobo akatambua kwamba moyo wa Labani kwake haukuwa kama ulivyokuwa mwanzo.

3 NdipoBwanaakamwambia Yakobo, “Rudi katika nchi ya baba zako na kwa watu wako, nami nitakuwa pamoja nawe.”

4 Hivyo Yakobo akatuma ujumbe kwa Raheli na Lea waje machungani yalikokuwa makundi yake.

5 Akawaambia, “Naona moyo wa baba yenu kwangu sivyo kama ulivyokuwa mwanzoni, lakini Mungu wa baba yangu amekuwa pamoja nami.

6 Mnajua kwamba nimemtumikia baba yenu kwa nguvu zangu zote,

7 hata hivyo baba yenu amenidanganya kwa kubadilisha ujira wangu mara kumi. Hata hivyo, Mungu hakumruhusu kunidhuru.

8 Kama alisema, ‘Wenye madoadoa watakuwa ujira wako,’ basi makundi yote yalizaa wenye madoadoa, kama alisema, ‘Wenye mistari watakuwa ujira wako,’ basi makundi yote yalizaa wenye mistari.

9 Hivyo Mungu amechukua mifugo ya baba yenu na amenipa mimi.

10 “Wakati fulani majira ya kuzaliana niliota ndoto ambayo niliinua macho na kuona kwamba wale mabeberu waliokuwa wakipanda kundi walikuwa wa mistari, madoadoa na mabakabaka.

11 Malaika wa Mungu akaniambia katika ndoto, ‘Yakobo.’ Nikamjibu, ‘Mimi hapa.’

12 Akasema, ‘Inua macho yako uone wale mabeberu wote wanaopanda kundi wana mistari, madoadoa au mabakabaka, kwa maana nimeona yale yote ambayo Labani amekuwa akikutendea.

13 Mimi ndiye Mungu wa Betheli, ulikomiminia ile nguzo mafuta na pale mahali uliponiwekea nadhiri. Sasa ondoka katika nchi hii mara moja urudi katika nchi uliyozaliwa.’ ”

14 Ndipo Raheli na Lea wakajibu, “Je bado tu tunalo fungu lolote katika urithi wa nyumba ya baba yetu?

15 Je, yeye hatuhesabu sisi kama wageni? Sio kwamba ametuuza tu, bali ametumia hata na vile vilivyolipwa kwa ajili yetu.

16 Hakika utajiri wote ambao Mungu ameuchukua kutoka kwa baba yetu ni mali yetu na watoto wetu. Hivyo fanya lolote lile Mungu alilokuambia.”

17 Ndipo Yakobo akawapandisha watoto wake na wake zake juu ya ngamia,

18 naye akawaswaga wanyama wote mbele yake pamoja na vitu vyote alivyokuwa amechuma huko Padan-Aramu kwenda kwa baba yake Isaki katika nchi ya Kanaani.

19 Labani alipokuwa amekwenda kukata kondoo wake manyoya, Raheli aliiba miungu ya nyumba ya baba yake.

20 Zaidi ya hayo, Yakobo alimdanganya Labani Mwaramu kwa kutokumwambia kwamba anakimbia.

21 Hivyo akakimbia pamoja na vitu vyote alivyokuwa navyo na kuvuka Mto Frati akaelekea nchi ya vilima katika Gileadi.

Labani Amfuatilia Yakobo

22 Siku ya tatu Labani akaambiwa kwamba Yakobo amekimbia.

23 Akiwachukua jamaa zake, akamfuatia Yakobo kwa siku saba na kumkuta kwenye nchi ya vilima katika Gileadi.

24 Ndipo Mungu akamjia Labani Mwaramu katika ndoto usiku na kumwambia, “Jihadhari usiseme neno lolote kwa Yakobo, liwe zuri au baya.”

25 Yakobo alikuwa amepiga hema lake katika nchi ya vilima katika Gileadi wakati Labani alipomkuta, Labani na jamaa yake wakapiga kambi huko pia.

26 Ndipo Labani akamwambia Yakobo, “Umefanya nini? Umenidanganya na umewachukua binti zangu kama mateka katika vita.

27 Kwa nini ulikimbia kwa siri na kunidanganya? Kwa nini hukuniambia ili nikuage kwa furaha na nyimbo za matari na vinubi?

28 Hata hukuniruhusu niwabusu wajukuu zangu na kuwaaga binti zangu. Umefanya kitu cha kipumbavu.

29 Nina uwezo wa kukudhuru, lakini usiku uliopita Mungu wa baba yako alisema nami, akaniambia, ‘Jihadhari, usiseme neno lolote kwa Yakobo liwe zuri au baya.’

30 Sasa umeondoka kwa sababu umetamani kurudi nyumbani kwa baba yako. Lakini kwa nini umeiba miungu yangu?”

31 Yakobo akamjibu Labani, “Niliogopa, kwa sababu nilifikiri ungeweza kuninyangʼanya binti zako kwa nguvu.

32 Lakini kama ukimkuta yeyote aliye na miungu yako, hataishi. Mbele ya jamaa yetu, angalia mwenyewe uone kama kuna chochote chako hapa nilicho nacho, kama kipo, kichukue.” Basi Yakobo hakujua kwamba Raheli alikuwa ameiba hiyo miungu.

33 Kwa hiyo Labani akaingia ndani ya hema la Yakobo na ndani ya hema la Lea na ndani ya hema la watumishi wawili wa kike, lakini hakukuta chochote. Baadaye alipotoka katika hema la Lea, akaingia hema la Raheli.

34 Basi Raheli ndiye alikuwa amechukua ile miungu ya nyumbani kwao na kuiweka katika matandiko ya ngamia na kukalia. Labani akatafuta kila mahali kwenye hema lakini hakupata chochote.

35 Raheli akamwambia baba yake, “Usikasirike, bwana wangu kwa kuwa siwezi kusimama ukiwepo, niko katika hedhi.” Labani akatafuta lakini hakuweza kuipata miungu ya nyumbani kwake.

36 Yakobo akakasirika na kumshutumu Labani, akisema, “Uhalifu wangu ni nini?” Akamuuliza Labani, “Ni dhambi gani niliyofanya hata unaniwinda?

37 Sasa kwa kuwa umepekua vitu vyangu vyote umepata nini kilicho cha nyumbani mwako? Kiweke hapa mbele ya jamaa yako na yangu, nao waamue kati yetu sisi wawili.

38 “Mpaka sasa nimekuwa pamoja nawe miaka ishirini. Kondoo wako na mbuzi wako hawajaharibu mimba, wala sijala kondoo dume kutoka makundi yako.

39 Sikukuletea mfugo aliyeraruliwa na wanyama pori, nilibeba hasara mimi mwenyewe. Tena ulinidai malipo kwa chochote kilichoibwa mchana au usiku.

40 Hii ndiyo iliyokuwa hali yangu: Niliumia kwa joto la mchana na baridi usiku, pia usingizi ulinipa.

41 Ilikuwa hivi kwa miaka ile ishirini niliyokuwa nyumbani kwako. Nilikutumikia miaka ile kumi na minne kwa ajili ya binti zako wawili, miaka sita kwa ajili ya makundi yako, nawe ulibadilisha ujira wangu mara kumi.

42 Kama Mungu wa baba yangu, Mungu wa Abrahamu na Hofu ya Isaki, hakuwa pamoja nami, hakika ungenifukuza mikono mitupu. Lakini Mungu ameona taabu yangu na kazi ngumu ya mikono yangu, naye usiku uliopita amekukemea.”

43 Labani akamjibu Yakobo, “Wanawake hawa ni binti zangu, watoto hawa ni watoto wangu na makundi haya ni makundi yangu. Vyote unavyoviona ni vyangu. Lakini hata hivyo ninaweza kufanya nini kuhusu hawa binti zangu, au kuhusu watoto waliowazaa?

44 Njoo sasa na tufanye agano, wewe na mimi, na liwe kama shahidi kati yetu.”

45 Hivyo Yakobo akachukua jiwe, akalisimamisha kama nguzo.

46 Akawaambia jamaa yake, “Kusanyeni mawe.” Hivyo wakachukua mawe na kuyakusanya yakawa lundo, wakala chakula hapo karibu na hilo lundo.

47 Labani akaliita Yegar-Sahaduthana Yakobo akaliita Galeedi.

48 Labani akasema, “Lundo hili ni shahidi kati yako na mimi leo.” Ndiyo maana likaitwa Galeedi.

49 Pia liliitwa Mispa,kwa sababu alisema, “Bwanana aweke ulinzi kati yako na mimi wakati kila mmoja akiwa mbali na mwingine.

50 Kama ukiwatenda mabaya binti zangu au ukioa wake wengine zaidi ya binti zangu, hata ingawa hakuna hata mmoja aliye pamoja nasi, kumbuka kwamba Mungu ni shahidi kati yako na mimi.”

51 Pia Labani akamwambia Yakobo, “Hili ndilo lundo, na hii ndiyo nguzo niliyoisimamisha kati yako na mimi.

52 Lundo hili ni shahidi na nguzo hii ni shahidi, kwamba sitavuka lundo hili kuja upande wako kukudhuru, nawe kwamba hutavuka lundo hili na nguzo hii kuja upande wangu kunidhuru.

53 Mungu wa Abrahamu na Mungu wa Nahori, Mungu wa baba zao, aamue kati yetu.”

Hivyo Yakobo akaapa kwa jina la Hofu ya baba yake Isaki.

54 Yakobo akatoa dhabihu juu ya kilima na akawaalika jamaa zake kula chakula. Baada ya kula, wakalala huko.

55 Kesho yake asubuhi na mapema, Labani akawabusu wajukuu zake, binti zake na kuwabariki. Kisha akaondoka, akarudi nyumbani.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/GEN/31-e0fe49ce3caea1d72b29c266f40622fe.mp3?version_id=1627—

Categories
Mwanzo

Mwanzo 32

Yakobo Ajiandaa Kukutana Na Esau

1 Yakobo pia akaondoka akaenda zake, nao malaika wa Mungu wakakutana naye.

2 Yakobo alipowaona, akasema, “Hii ni kambi ya Mungu!” Kwa hiyo akapaita mahali pale Mahanaimu.

3 Yakobo akatuma wajumbe kumtangulia kwa Esau ndugu yake huko Seiri, katika nchi ya Edomu.

4 Akawaagiza akisema: “Hili ndilo mtakalomwambia bwana wangu Esau: ‘Mtumishi wako Yakobo anasema, nimekuwa nikiishi pamoja na Labani na nimekuwako huko mpaka sasa.

5 Ninao ngʼombe na punda, kondoo na mbuzi, watumishi wa kiume na wa kike. Sasa ninatuma ujumbe huu kwa bwana wangu, ili nipate kibali machoni pako.’ ”

6 Wajumbe waliporudi kwa Yakobo, wakamwambia, “Tulikwenda kuonana na ndugu yako Esau, naye sasa anakuja kukulaki akifuatana na wanaume 400.”

7 Kwa hofu kuu na huzuni, Yakobo akagawanya watu aliokuwa nao katika makundi mawili, pia akagawanya makundi ya kondoo na mbuzi, na vilevile ngʼombe na ngamia.

8 Yakobo alifikiri, “Kama Esau akija na kushambulia kundi moja, kundi lililobaki litaweza likanusurika.”

9 Ndipo Yakobo akaomba, “Ee Mungu wa baba yangu Abrahamu, Mungu wa baba yangu Isaki, EeBwana, ambaye uliniambia, ‘Rudi katika nchi yako na jamaa yako, nami nitakufanya ustawi,’

10 mimi sistahili fadhili na uaminifu wako wote ulionitendea mimi mtumishi wako. Nilikuwa na fimbo tu mkononi mwangu nilipovuka mto huu wa Yordani, lakini sasa ninayo makundi mawili.

11 Nakuomba, uniokoe na mkono wa ndugu yangu Esau, kwa maana ninaogopa kuwa atakuja kunishambulia, pia mama pamoja na watoto wao.

12 Lakini umeshasema, ‘Hakika nitakufanya ustawi na kuufanya uzao wako kuwa mwingi kama mchanga wa baharini ambao hauwezi kuhesabika!’ ”

13 Akalala pale usiku ule, miongoni mwa vitu alivyokuwa navyo, akachagua zawadi kwa ajili ya Esau ndugu yake:

14 Mbuzi waume ishirini na mbuzi wake 200, kondoo dume ishirini na kondoo wake 200.

15 Ngamia wake thelathini pamoja na ndama zao, ngʼombe wake arobaini na mafahali kumi, punda wake ishirini na punda waume kumi.

16 Akaviweka chini ya uangalizi wa watumishi wake, kila kundi peke yake na kuwaambia, “Nitangulieni na kuacha nafasi kati ya makundi.”

17 Akamwagiza yule aliyetangulia kuwa, “Ndugu yangu Esau atakapokutana nawe na kukuuliza, ‘Wewe ni wa nani? Unakwenda wapi? Wanyama hawa wote mbele yako ni mali ya nani?’

18 Ndipo utakaposema, ‘Ni mali ya mtumishi wako Yakobo. Ni zawadi ambazo zimetumwa kwa bwana wangu Esau, naye anakuja nyuma yetu.’ ”

19 Akamwagiza pia yule mtumishi wa kundi la pili, la tatu na yale mengine yote yaliyofuata akiwaambia, “Mtamwambia Esau maneno hayo hayo mtakapokutana naye.

20 Hakikisheni mmesema, ‘Mtumishi wako Yakobo anakuja nyuma yetu.’ ” Kwa kuwa alifikiri, “Nitaweza kumtuliza kwa zawadi hizi ninazotanguliza, hatimaye, nitakapomwona, huenda atanikubali.”

21 Kwa hiyo zawadi za Yakobo zilitangulia mbele yake, lakini yeye mwenyewe alilala kambini usiku ule.

Yakobo Ashindana Mweleka Na Mungu

22 Usiku ule Yakobo akaamka akawachukua wake zake wawili, watumishi wake wawili wa kike na wanawe kumi na mmoja na akavuka kivuko cha Yaboki.

23 Baada ya kuwavusha ngʼambo ya kijito, alivusha pia mali zake zote.

24 Kwa hiyo Yakobo akaachwa peke yake na mtu mmoja akashikana naye mweleka mpaka mapambazuko.

25 Yule mtu alipoona kuwa hawezi kumshinda, aligusa kiungio cha nyonga ya Yakobo kwa hiyo nyonga yake ikateguka wakati alipokuwa akishikana mweleka na yule mtu.

26 Ndipo yule mtu akasema, “Niache niende, kwa kuwa ni mapambazuko.”

Lakini Yakobo akajibu, “Sitakuacha uende usiponibariki.”

27 Yule mtu akamuuliza, “Jina lako nani?”

Akajibu, “Yakobo.”

28 Ndipo yule mtu akasema, “Jina lako halitakuwa tena Yakobo, bali Israeli,kwa sababu umeshindana na Mungu na watu pia, nawe umeshinda.”

29 Yakobo akasema, “Tafadhali niambie jina lako.”

Lakini akajibu, “Kwa nini kuniuliza Jina langu?” Ndipo akambariki huko.

30 Kwa hiyo Yakobo akapaita mahali pale Penieli,akasema, “Ni kwa sababu nimemwona Mungu uso kwa uso na bado maisha yangu yameokoka.”

31 Jua lilikuwa linachomoza Yakobo alipoondoka Penueli, naye alikuwa akichechemea kwa sababu ya nyonga yake.

32 Kwa hiyo mpaka leo Waisraeli hawali mshipa ulioungana na kiungio cha nyonga, kwa sababu kiungio cha nyonga ya Yakobo kiliteguliwa karibu na mshipa huo.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/GEN/32-9e30cac4943bbcb2650af7802393d885.mp3?version_id=1627—

Categories
Mwanzo

Mwanzo 33

Yakobo Akutana Na Esau

1 Yakobo akainua macho akamwona Esau akija na watu wake 400, kwa hiyo akawagawanya watoto kati ya Lea, Raheli na wale watumishi wake wawili wa kike.

2 Akawaweka wale watumishi wa kike na watoto wao mbele, Lea na watoto wake wakafuata, Raheli na Yosefu wakaja nyuma.

3 Yeye mwenyewe akatangulia mbele na kusujudu mara saba alipomkaribia ndugu yake.

4 Lakini Esau akamkimbilia Yakobo kumlaki na kumkumbatia, akamwangukia shingoni na kumbusu. Nao wakalia.

5 Esau akainua macho akawaona wale wanawake na watoto. Akauliza, “Hawa uliofuatana nao ni nani?”

Yakobo akamjibu, “Ni watoto ambao Mungu amempa mtumishi wako kwa neema.”

6 Kisha wale watumishi wa kike na watoto wao wakakaribia na kusujudu.

7 Kisha Lea na watoto wake wakaja na kusujudu. Mwisho wa wote wakaja Yosefu na Raheli, nao pia wakasujudu.

8 Esau akauliza, “Una maana gani kuhusu makundi hayo yote niliyokutana nayo?”

Akasema, “Ni ili kupata kibali machoni pako, bwana wangu.”

9 Lakini Esau akamwambia, “Ndugu yangu, tayari nina wingi wa mali. Ulivyo navyo viwe vyako mwenyewe.”

10 Yakobo akasema, “La hasha! Tafadhali, kama nimepata kibali machoni pako, upokee zawadi hii kutoka kwangu. Kwa maana kuuona uso wako, ni kama kuuona uso wa Mungu, kwa kuwa umenipokea kwa takabali kubwa.

11 Tafadhali ukubali zawadi iliyoletwa kwako, kwa kuwa Mungu amenineemesha na ninavyo vyote ninavyohitaji.” Kwa sababu Yakobo alisisitiza, Esau akapokea.

12 Ndipo Esau akasema, “Na tuendelee na safari, nitakuwa pamoja nawe.”

13 Lakini Yakobo akamwambia, “Bwana wangu unajua kwamba watoto ni wachanga na kwamba ni lazima nitunze hawa kondoo wake na ngʼombe wanaonyonyesha. Wakipelekwa kwa haraka hata kama ni kwa siku moja tu, wanyama wote watakufa.

14 Hivyo bwana wangu umtangulie mtumishi wako, wakati mimi nikija polepole kwa mwendo wa makundi yaliyo mbele yangu na mwendo wa watoto, mpaka nifike kwa bwana wangu huko Seiri.”

15 Esau akamwambia, “Basi na niwaache baadhi ya watu wangu pamoja nawe.”

Yakobo akauliza, “Lakini kwa nini ufanye hivyo, niache tu nipate kibali machoni pa bwana wangu.”

16 Hivyo siku hiyo Esau akashika njia akarudi Seiri.

17 Pamoja na hayo, Yakobo akaenda Sukothi,mahali alipojijengea makazi kwa ajili yake na mabanda kwa ajili ya mifugo yake. Hii ndiyo sababu sehemu ile inaitwa Sukothi.

18 Baada ya Yakobo kutoka Padan-Aramu, alifika salama katika mji wa Shekemu huko Kanaani na kuweka kambi yake karibu na mji.

19 Akanunua kiwanja kutoka kwa wana wa Hamori, baba wa Shekemu, kwa bei ya vipande mia vya fedha, ambapo alipiga hema lake.

20 Pale akajenga madhabahu na kupaita El-Elohe-Israeli.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/GEN/33-6452315bd46aef6827c859c7500164b2.mp3?version_id=1627—

Categories
Mwanzo

Mwanzo 34

Dina Na Washekemu

1 Basi Dina, binti wa Yakobo aliyezaliwa na Lea, akatoka nje kuwatembelea wanawake wa nchi ile.

2 Ikawa Shekemu mwana wa Hamori Mhivi, mtawala wa eneo lile alipomwona, akamchukua na kumnajisi.

3 Moyo wake ukavutwa sana kwa Dina binti Yakobo, akampenda huyu msichana na akazungumza naye kwa kumbembeleza.

4 Shekemu akamwambia baba yake Hamori, “Nipatie msichana huyu awe mke wangu.”

5 Yakobo aliposikia kwamba binti yake Dina amenajisiwa, wanawe walikuwa mashambani wakichunga mifugo yake, kwa hiyo akalinyamazia jambo hilo mpaka waliporudi nyumbani.

6 Kisha Hamori baba yake Shekemu akaenda kuzungumza na Yakobo.

7 Basi wana wa Yakobo walikuwa wamerudi kutoka mashambani mara tu waliposikia kilichotokea. Walikuwa wamejawa na huzuni na ghadhabu, kwa sababu Shekemu alikuwa amefanya jambo la aibu katika Israeli kwa kukutana kimwili na binti wa Yakobo, kitu ambacho hakingepasa kufanyika.

8 Lakini Hamori akawaambia, “Moyo wa mwanangu Shekemu umeelekea kwa binti yenu. Tafadhali mpeni awe mke wake.

9 Oaneni na sisi, tupeni binti zenu, nanyi mchukue binti zetu.

10 Mwaweza kuishi katikati yetu, nchi ni wazi kwenu. Ishini ndani yake, fanyeni biashara humu na mjipatie mali.”

11 Kisha Shekemu akamwambia baba yake Dina pamoja na ndugu zake, “Na nipate kibali machoni penu, nami nitawapa chochote mtakachosema.

12 Niambieni kiasi cha mahari na zawadi nitakayoileta, hata iwe kubwa kiasi gani, nami nitawalipa chochote mtakachodai. Nipeni tu huyu msichana awe mke wangu.”

13 Kwa sababu ndugu yao Dina alikuwa amenajisiwa, wana wa Yakobo wakajibu kwa udanganyifu walipozungumza na Shekemu pamoja na baba yake Hamori.

14 Wakawaambia, “Hatuwezi kufanya jambo kama hili, hatuwezi kumtoa dada yetu kwa mtu ambaye hakutahiriwa. Hiyo itakuwa aibu kwetu.

15 Tutakuruhusu kwa sharti moja tu, kwamba mtakuwa kama sisi kwa kuwatahiri wanaume wenu wote.

16 Kisha tutawapa binti zetu na sisi tutawachukua binti zenu. Tutaishi kwenu na tutakuwa watu wamoja nanyi.

17 Lakini mkikataa kutahiriwa, tutamchukua ndugu yetu na kuondoka.”

18 Pendekezo lao likawa jema kwa Hamori na Shekemu mwanawe.

19 Kijana mdogo, ambaye alikuwa ameheshimiwa kati ya wote walioishi nyumbani mwa baba yake, hakupoteza muda kufanya waliyoyasema, kwa sababu alikuwa amependezwa sana na binti Yakobo.

20 Kwa hiyo Hamori na Shekemu mwanawe walikwenda kwenye lango la mji kuzungumza na wenzao wa mjini.

21 Wakasema, “Hawa watu ni marafiki kwetu, tuwaruhusu waishi katika nchi yetu na kufanya biashara ndani yake, nchi ina nafasi tele kwa ajili yao. Tunaweza kuoa binti zao. Nao wanaweza kuoa binti zetu.

22 Lakini watu hao watakuwa tayari kukubali kuishi nasi kama watu wamoja nao kwa sharti kwamba wanaume wetu watahiriwe, kama wao.

23 Je, si mifugo yao, mali zao na wanyama wao wengine wote watakuwa wetu? Basi na tuwape kibali, nao wataishi miongoni mwetu.”

24 Wanaume wote waliotoka nje ya lango la mji walikubaliana na Hamori na Shekemu mwanawe na kila mwanaume katika mji ule akatahiriwa.

25 Baada ya siku tatu, wakati wote wakiwa wangali katika maumivu, wana wawili wa Yakobo, yaani Simeoni na Lawi, ndugu zake Dina, wakachukua panga zao na kuvamia mji ambao haukutazamia vita, wakaua kila mwanaume.

26 Wakawaua Hamori na Shekemu mwanawe kwa upanga kisha wakamchukua Dina kutoka nyumba ya Shekemu na kuondoka.

27 Wana wa Yakobo walipita juu ya maiti katika kuteka nyara mji ule ambamo dada yao alikuwa amenajisiwa.

28 Wakachukua kondoo na mbuzi, ngʼombe, punda na kila kitu kilichokuwa chao ndani ya mji ule na mashambani.

29 Walichukua utajiri wao wote pamoja na wanawake na watoto wao, wakachukua nyara kila kitu ndani ya nyumba zao.

30 Kisha Yakobo akawaambia Simeoni na Lawi, “Mmeleta taabu kwangu kwa kunifanya ninuke kama uvundo kwa Wakanaani na Waperizi, watu waishio katika nchi hii. Sisi ni wachache, kama wakiunganisha nguvu zao dhidi yangu na kunishambulia, mimi na nyumba yangu tutaangamizwa.”

31 Lakini wakamjibu, “Je, ilikuwa vyema kumtendea dada yetu kama kahaba?”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/GEN/34-5739f8e58f375adcb67498908a88b68a.mp3?version_id=1627—

Categories
Mwanzo

Mwanzo 35

Yakobo Arudi Betheli

1 Kisha Mungu akamwambia Yakobo, “Panda uende Betheli ukakae huko na ukamjengee Mungu madhabahu huko, Yeye aliyekutokea ulipokuwa unamkimbia Esau ndugu yako.”

2 Hivyo Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake pamoja na wote waliokuwa naye, “Iondoeni miungu ya kigeni ile iliyoko katikati yenu, jitakaseni na mkabadilishe nguo zenu.

3 Kisha njooni, twende Betheli, mahali nitakapomjengea Mungu madhabahu, aliyenijibu katika siku ya shida yangu, ambaye amekuwa pamoja nami popote nilipokwenda.”

4 Kwa hiyo wakampa Yakobo miungu yote ya kigeni waliyokuwa nayo, pamoja na pete zilizokuwa masikioni mwao. Yakobo akavizika chini ya mti wa mwaloni huko Shekemu.

5 Kisha wakaondoka, na hofu ya Mungu ikawapata miji yote iliyowazunguka. Kwa hiyo hakuna aliyewafuatia wana wa Yakobo.

6 Yakobo na watu wote waliokuwa pamoja naye wakafika Luzu (ndio Betheli), katika nchi ya Kanaani.

7 Huko akajenga madhabahu na akapaita mahali pale El-Betheli,kwa sababu mahali pale ndipo Mungu alipojifunua kwake alipokuwa akimkimbia ndugu yake.

8 Wakati huu Debora, mlezi wa Rebeka, akafa na akazikwa chini ya mti wa mwaloni ulioko chini ya Betheli. Kwa hiyo pakaitwa Alon-Bakuthi.

9 Baada ya Yakobo kurudi kutoka Padan-Aramu, Mungu alimtokea tena na kumbariki.

10 Mungu akamwambia, “Jina lako ni Yakobo, lakini hutaitwa tena Yakobo, jina lako utakuwa Israeli.” Kwa hiyo akamwita Israeli.

11 Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu Mwenyezi,ukazae na kuongezeka. Taifa na jamii ya mataifa itatoka kwako, nao wafalme watatoka viunoni mwako.

12 Nchi niliyowapa Abrahamu na Isaki nakupa wewe pia, nami nitawapa wazao wako baada yako.”

13 Kisha Mungu akapanda juu kutoka kwake mahali pale alipozungumza naye.

14 Yakobo akasimamisha nguzo ya jiwe mahali pale Mungu alipozungumza naye, akamimina sadaka ya kinywaji juu yake, pia akamimina mafuta juu yake.

15 Yakobo akapaita mahali pale Mungu alipozungumza naye Betheli.

Vifo Vya Raheli Na Isaki

16 Kisha wakaondoka Betheli. Walipokuwa umbali fulani kabla ya kufika Efrathi, Raheli akaanza kusikia uchungu na alipata shida kuu.

17 Alipokuwa katika shida hii katika kujifungua, mkunga akamwambia, “Usiogope, kwa sababu umempata mwana mwingine.”

18 Hapo alipopumua pumzi yake ya mwisho, kwa maana alikuwa akifa, akamwita mwanawe Benoni.Lakini babaye akamwita Benyamini.

19 Kwa hiyo Raheli akafa, akazikwa kando ya njia iendayo Efrathi (ndio Bethlehemu).

20 Juu ya kaburi lake, Yakobo akasimamisha nguzo, ambayo mpaka leo inatambulisha kaburi la Raheli.

21 Israeli akaendelea tena na safari yake na kupiga hema mbele mnara wa Ederi.

22 Wakati Israeli alipokuwa akiishi katika nchi ile, Reubeni mwanawe alikutana kimwili na suria wa baba yake aitwaye Bilha, naye Israeli akasikia jambo hili.

Yakobo alikuwa na wana kumi na wawili:

23 Wana wa Lea walikuwa:

Reubeni mzaliwa wa kwanza wa Yakobo,

Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari na Zabuloni.

24 Wana wa Raheli walikuwa:

Yosefu na Benyamini.

25 Wana waliozaliwa na Bilha mtumishi wa kike wa Raheli walikuwa:

Dani na Naftali.

26 Wana waliozaliwa na Zilpa mtumishi wa kike wa Lea walikuwa:

Gadi na Asheri.

Hawa walikuwa wana wa Yakobo, waliozaliwa kwake akiwa Padan-Aramu.

27 Yakobo akarudi nyumbani kwa baba yake Isaki huko Mamre, karibu na Kiriath-Arba (yaani Hebroni), ambapo walikuwa wameishi Abrahamu na Isaki.

28 Isaki aliishi miaka 180.

29 Kisha Isaki akapumua pumzi yake ya mwisho akafa, akakusanywa pamoja na watu wake akiwa mzee wa miaka mingi. Nao wanawe Esau na Yakobo wakamzika.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/GEN/35-bef0a453cbf819b0eaf4d4632d30171d.mp3?version_id=1627—

Categories
Mwanzo

Mwanzo 36

Wazao Wa Esau

1 Hivi ndivyo vizazi vya Esau (yaani Edomu).

2 Esau akaoa wake kutoka miongoni mwa wanawake wa Kanaani: Ada binti wa Eloni Mhiti, Oholibama binti wa Ana, mjukuu wa kike wa Sibeoni Mhivi,

3 pia akaoa Basemathi binti wa Ishmaeli, dada yake Nebayothi.

4 Ada akamzalia Esau Elifazi, Basemathi akamzaa Reueli,

5 Oholibama akamzaa Yeushi, Yalamu na Kora. Hawa ndio wana wa Esau waliozaliwa kwake huko Kanaani.

6 Esau akawachukua wake zake, watoto wake wa kiume na wa kike na wote wa nyumbani mwake, mifugo yake pamoja na wanyama wake wengine wote na mali yake yote ambayo alikuwa ameipata akiwa Kanaani, akahamia katika nchi iliyo mbali na Yakobo ndugu yake.

7 Mali zao zilikuwa nyingi sana kiasi kwamba haikuwa rahisi wao kuishi pamoja, nchi waliyokuwa wakiishi isingewatosha wote kwa ajili ya mifugo yao.

8 Kwa hiyo Esau (ambaye ni Edomu) aliishi katika nchi ya kilima huko Seiri.

9 Hawa ndio wazao wa Esau, baba wa Waedomu, katika nchi ya kilima cha Seiri.

10 Haya ndiyo majina ya wana wa Esau:

Elifazi, mwana wa Esau ambaye mkewe Ada alimzalia; na Reueli, mwana wa Esau ambaye mkewe Basemathi alimzalia.

11 Wana wa Elifazi ni:

Temani, Omari, Sefo, Gatamu na Kenazi.

12 Elifazi mwana wa Esau alikuwa pia na suria aliyeitwa Timna, ambaye alimzalia Amaleki. Hawa ndio waliokuwa wajukuu wa Ada mke wa Esau.

13 Wana wa Reueli ni:

Nahathi, Zera, Shama na Miza. Hawa ndio waliokuwa wajukuu wa Basemathi mkewe Esau.

14 Wana wa Oholibama binti Ana, mkewe Esau, aliyekuwa mjukuu wa Sibeoni, aliomzalia Esau ni:

Yeushi, Yalamu na Kora.

15 Hawa ndio waliokuwa wakuu miongoni mwa wazao wa Esau:

Wakuu wa wana wa Elifazi, mzaliwa wa kwanza wa Esau ni:

Temani, Omari, Sefo, Kenazi,

16 Kora, Gatamu na Amaleki. Hawa ndio waliokuwa wakuu waliotoka kwa Elifazi huko Edomu, waliokuwa wajukuu wa kiume wa Ada.

17 Wakuu wa wana wa Reueli, mwana wa Esau ni:

Nahathi, Zera, Shama na Miza. Hawa ndio wakuu waliotoka kwa Reueli huko Edomu, waliokuwa wajukuu wa kiume wa Basemathi mkewe Esau.

18 Wakuu wa wana wa Esau ambao mkewe Oholibama alimzalia ni:

Yeushi, Yalamu na Kora. Hawa ndio wakuu waliotoka kwa mke wa Esau, Oholibama binti Ana.

19 Hawa ndio waliokuwa wana wa Esau (ndiye Edomu), na hawa ndio waliokuwa wakuu wao.

20 Hawa ndio walikuwa wana wa Seiri, Mhori, waliokuwa wakiishi katika nchi ile:

Lotani, Shobali, Sibeoni, Ana,

21 Dishoni, Eseri na Dishani. Hawa ndio wana wa Seiri huko Edomu waliokuwa wakuu kwa Wahori.

22 Wana wa Lotani walikuwa:

Hori na Homamu. Timna alikuwa dada yake Lotani.

23 Wana wa Shobali walikuwa:

Alvani, Manahathi, Ebali, Shefo na Onamu.

24 Wana wa Sibeoni walikuwa:

Aiya na Ana. Huyu Ana ndiye aligundua chemchemi ya maji moto jangwani alipokuwa akichunga punda za Sibeoni baba yake.

25 Watoto wa Ana walikuwa:

Dishoni na Oholibama binti wa Ana.

26 Wana wa Dishoni walikuwa:

Hemdani, Eshbani, Ithrani na Kerani.

27 Wana wa Eseri walikuwa:

Bilhani, Zaavani na Akani.

28 Wana wa Dishani walikuwa:

Usi na Arani.

29 Hawa ndio waliokuwa wakuu wa Wahori:

Lotani, Shobali, Sibeoni, Ana,

30 Dishoni, Eseri na Dishani. Hawa ndio walikuwa wakuu wa Wahori, kufuatana na makundi yao, katika nchi ya Seiri.

Watawala Wa Edomu

31 Wafuatao ni wafalme waliotawala Edomu kabla ya mfalme yeyote wa Israeli kutawala:

32 Bela mwana wa Beori alikuwa mfalme wa Edomu. Mji wake uliitwa Dinhaba.

33 Bela alipofariki, Yobabu mwana wa Zera kutoka Bosra akawa mfalme baada yake.

34 Yobabu alipofariki, Hushamu kutoka nchi ya Watemani akawa mfalme baada yake.

35 Hushamu alipofariki, Hadadi mwana wa Bedadi, aliyeshinda Midiani katika nchi ya Moabu, akawa mfalme baada yake. Mji wake uliitwa Avithi.

36 Hadadi alipofariki, Samla kutoka Masreka akawa mfalme baada yake.

37 Samla alipofariki, Shauli kutoka Rehobothi ngʼambo ya Mto Frati akawa mfalme baada yake.

38 Shauli alipofariki, Baal-Hanani mwana wa Akbori akawa mfalme baada yake.

39 Baal-Hanani mwana wa Akbori alipofariki, Hadadi akawa mfalme baada yake. Mji wake uliitwa Pau, na mkewe aliitwa Mehetabeli binti Matredi, binti Me-Zahabu.

40 Hawa ndio wakuu waliotokana na Esau, kwa majina, kufuatana na koo zao na nchi zao:

Timna, Alva, Yethethi,

41 Oholibama, Ela, Pinoni,

42 Kenazi, Temani, Mibsari,

43 Magdieli na Iramu. Hawa ndio walikuwa wakuu wa Edomu, kufuatana na makazi yao katika nchi waliyoimiliki.

Huyu ndiye alikuwa Esau, baba wa Waedomu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/GEN/36-3b2cde05d94227532eeeb3958cc5e1eb.mp3?version_id=1627—

Categories
Mwanzo

Mwanzo 37

Ndoto Za Yosefu

1 Yakobo akaishi Kanaani katika nchi ambayo baba yake alikuwa ameishi.

2 Zifuatazo ni habari za Yakobo.

Yosefu, kijana wa miaka kumi na saba, alikuwa akichunga makundi ya kondoo na mbuzi pamoja na ndugu zake wa mama wengine, yaani wana wa Bilha na wana wa Zilpa wake za baba yake, naye akawa akimletea baba yake taarifa mbaya kuhusu hao ndugu zake.

3 Basi, Israeli akampenda Yosefu kuliko yeyote miongoni mwa kaka zake, kwani ni mwanawe wa uzeeni, akamshonea joho lililorembwa vizuri sana.

4 Ndugu zake walipoona kwamba baba yao anampenda Yosefu kuliko yeyote mwingine miongoni mwao, walimchukia na hawakusema naye neno lolote jema.

5 Yosefu akaota ndoto, naye alipowaeleza ndugu zake, wakamchukia zaidi.

6 Akawaambia, “Sikilizeni ndoto niliyoota:

7 Tulikuwa tukifunga miganda ya nafaka shambani, ghafula mganda wangu ukasimama wima, wakati miganda yenu ikiuzunguka na kuuinamia.”

8 Ndugu zake wakamwambia, “Wewe unakusudia kututawala? Hivi kweli wewe utatutawala sisi?” Wakaongeza kumchukia zaidi kwa sababu ya ndoto yake pamoja na yale aliyowaambia.

9 Kisha akaota ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake akisema, “Sikilizeni, nimeota ndoto nyingine, wakati huu jua, mwezi na nyota kumi na moja zilikuwa zinanisujudia.”

10 Alipomwambia baba yake pamoja na ndugu zake, baba yake akamkemea akisema, “Ni ndoto gani hii uliyoota? Hivi kweli mama yako na mimi na ndugu zako tutakuja kukusujudia wewe hadi nchi?”

11 Ndugu zake wakamwonea wivu, lakini baba yake akaliweka jambo hilo moyoni.

Yosefu Auzwa Na Ndugu Zake

12 Basi, ndugu zake walikuwa wamekwenda kuchunga makundi ya baba yao karibu na Shekemu,

13 naye Israeli akamwambia Yosefu, “Kama ujuavyo, ndugu zako wanachunga makundi huko karibu na Shekemu. Njoo, nitakutuma kwao.”

Yosefu akajibu, “Vema sana, niko tayari.”

14 Kwa hiyo akamwambia, “Nenda uone kama mambo yote ni salama kwa ndugu zako na makundi, kisha uniletee habari.” Ndipo akamtuma Yosefu kutoka Bonde la Hebroni.

Yosefu alipofika Shekemu,

15 mtu mmoja akamkuta akizungukazunguka mashambani na akamuuliza, “Unatafuta nini?”

16 Akajibu, “Ninawatafuta ndugu zangu. Unaweza kuniambia wanachunga wapi makundi yao?”

17 Yule mtu akajibu, “Wamehama hapa. Nilisikia wakisema, ‘Twende Dothani.’ ”

Kwa hiyo Yosefu akawafuatilia ndugu zake na kuwakuta karibu na Dothani.

18 Ndugu zake walipomwona akiwa mbali, kabla hajawafikia, wakapanga shauri baya la kumuua.

19 Wakaambiana, “Yule mwota ndoto anakuja!

20 Njooni sasa, tumuue na kumtupa katika shimo mojawapo na tuseme kwamba mnyama mkali amemrarua. Kisha tutaona matokeo ya ndoto zake.”

21 Reubeni aliposikia jambo hili, akajaribu kumwokoa kutoka mikononi mwao akasema, “Tusiutoe uhai wake.

22 Tusimwage damu yoyote. Mtupeni katika shimo lililoko hapa jangwani, lakini msimguse.” Reubeni alisema hivyo ili amwokoe kutoka mikononi mwao, kisha amrudishe nyumbani kwa baba yake.

23 Kwa hiyo Yosefu alipowafikia ndugu zake, walimvua lile joho lake, lile joho lililorembwa vizuri alilokuwa amevaa.

24 Kisha wakamchukua wakamtupa katika shimo. Wakati huo shimo lilikuwa tupu, halikuwa na maji ndani yake.

25 Walipokaa ili wale chakula chao, wakainua macho wakaona msafara wa Waishmaeli ukija kutoka Gileadi. Ngamia wao walikuwa wamepakizwa mizigo ya vikolezo, uvumba na manemane, nao walikuwa njiani kuvipeleka Misri.

26 Yuda akawaambia ndugu zake, “Tutafaidi nini ikiwa tutamuua ndugu yetu na kuificha damu yake?

27 Njooni, tumuuze kwa hawa Waishmaeli. Tusimguse, kwa kuwa hata hivyo yeye ni ndugu yetu, nyama yetu na damu yetu wenyewe.” Ndugu zake wakakubali.

28 Kwa hiyo wale wafanyabiashara Wamidiani walipofika pale, ndugu zake wakamtoa Yosefu kutoka kwenye lile shimo, na kumuuza kwa shekeli ishiriniza fedha kwa wale Waishmaeli, ambao walimpeleka Misri.

29 Reubeni aliporudi kutazama kwenye lile shimo na kuona kwamba Yosefu hayupo, alirarua nguo zake.

30 Akawarudia ndugu zake na kusema, “Kijana hayuko mle! Nielekee wapi sasa?”

31 Kisha wakalichukua lile joho la Yosefu, wakachinja mbuzi na kulichovya katika damu.

32 Wakalichukua lile joho lililorembwa vizuri na kulipeleka kwa baba yao na kusema, “Tumeliokota hili joho. Uchunguze uone kama ni la mwanao.”

33 Baba yao akalitambua akasema, “Hili ni joho la mwanangu! Mnyama mkali amemrarua. Hakika Yosefu ameraruliwa vipande vipande.”

34 Kisha Yakobo akararua nguo zake, akavaa nguo ya gunia na kumwombolezea mwanawe kwa siku nyingi.

35 Wanawe wote na binti zake wakaja kumfariji, lakini hakukubali kufarijiwa. Akasema, “Hapana, nitamwombolezea mwanangu mpaka nimfikie kaburini.” Kwa hiyo baba yake akaendelea kumlilia.

36 Wakati ule ule, Wamidiani wakamuuza Yosefu huko Misri kwa Potifa, mmojawapo wa maafisa wa Farao, aliyekuwa mkuu wa ulinzi.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/GEN/37-7377bc119f8c5847bfc9b3118dbd2088.mp3?version_id=1627—

Categories
Mwanzo

Mwanzo 38

Yuda Na Tamari

1 Wakati ule, Yuda akawaacha ndugu zake, akaenda kuishi na Hira Mwadulami.

2 Huko Yuda akakutana na binti wa Kikanaani aitwaye Shua, akamwoa na akakutana naye kimwili,

3 akapata mimba, akamzaa mwana, ambaye alimwita Eri.

4 Akapata mimba tena, akamzaa mwana na kumwita Onani.

5 Akamzaa mwana mwingine tena, akamwita Shela. Huyu alimzalia mahali paitwapo Kezibu.

6 Yuda akampatia Eri, mzaliwa wake wa kwanza, mke aitwaye Tamari.

7 Lakini Eri, mzaliwa wa kwanza wa Yuda, alikuwa mwovu machoni paBwana, kwa hiyoBwanaakamuua.

8 Kisha Yuda akamwambia Onani, “Kutana kimwili na mke wa ndugu yako, na utimize wajibu wako kwake kama mke wa ndugu yako, ili umpatie ndugu yako uzao.”

9 Lakini Onani alijua kwamba uzao haungekuwa wake, kwa hiyo kila alipokutana kimwili na mke wa ndugu yake, alimwaga chini mbegu za kiume ili asimpatie ndugu yake uzao.

10 Alichofanya kilikuwa kiovu machoni paBwana, hivyo, piaBwanaakamuua Onani.

11 Kisha Yuda akamwambia Tamari mkwewe, “Ishi kama mjane nyumbani mwa baba yako mpaka mwanangu Shela atakapokua.” Kwa maana alifikiri, “Angeweza kufa pia kama ndugu zake.” Kwa hiyo Tamari alikwenda kuishi nyumbani kwa baba yake.

12 Baada ya muda mrefu mke wa Yuda binti wa Shua akafariki. Baada ya msiba, Yuda alikwenda Timna, kwa watu waliokuwa wakikata kondoo wake manyoya, naye alifuatana na rafiki yake Hira Mwadulami.

13 Tamari alipoambiwa, “Baba mkwe wako yuko njiani kwenda Timna kukata kondoo wake manyoya,”

14 alivua mavazi yake ya ujane, akajifunika kwa shela ili asifahamike, akaketi kwenye mlango wa Enaimu, ambao upo njiani kuelekea Timna. Akafanya hivyo kwa sababu aliona kwamba, ingawa Shela amekua, lakini alikuwa hajakabidhiwa kwake kuwa mkewe.

15 Yuda alipomwona alifikiri ni kahaba, kwa sababu alikuwa amefunika uso wake.

16 Pasipo kutambua kwamba alikuwa mkwe wake, akamwendea kando ya njia na kumwambia, “Njoo sasa, nikutane na wewe kimwili.”

Yule mkwewe akamuuliza, “Utanipa nini nikikutana nawe kimwili?”

17 Akamwambia, “Nitakutumia mwana-mbuzi kutoka kundi langu.”

Akamuuliza, “Utanipa kitu chochote kama amana mpaka utakapompeleka?”

18 Akamuuliza, “Nikupe amana gani?”

Akamjibu, “Pete yako na kamba yake pamoja na fimbo iliyo mkononi mwako.” Kwa hiyo akampa vitu hivyo kisha akakutana naye kimwili, naye akapata mimba yake.

19 Tamari akaondoka, akavua shela yake akavaa tena nguo zake za ujane.

20 Wakati ule ule, Yuda akamtuma rafiki yake Mwadulami apeleke yule mwana-mbuzi ili arudishiwe amana yake kutoka kwa yule mwanamke, lakini yule rafiki yake hakumkuta yule mwanamke.

21 Akawauliza watu wanaoishi mahali pale, “Yuko wapi yule kahaba wa mahali pa kuabudia miungu aliyekuwa kando ya barabara hapa Enaimu?”

Wakamjibu, “Hajawahi kuwepo mwanamke yeyote kahaba wa mahali pa kuabudia miungu hapa.”

22 Kwa hiyo akamrudia Yuda na kumwambia, “Sikumpata. Zaidi ya hayo, watu wanaoishi mahali pale walisema ‘Hapakuwahi kuwepo mwanamke yeyote kahaba wa mahali pa kuabudia miungu hapa.’ ”

23 Kisha Yuda akasema, “Mwache avichukue vitu hivyo, ama sivyo tutakuwa kichekesho. Hata hivyo, nilimpelekea mwana-mbuzi, lakini hukumkuta.”

24 Baada ya miezi mitatu Yuda akaambiwa, “Tamari mkweo ana hatia ya kuwa kahaba, na matokeo yake ana mimba.”

Yuda akasema, “Mtoeni nje na achomwe moto hadi afe!”

25 Alipokuwa akitolewa nje, akatuma ujumbe kwa baba mkwe wake kusema, “Nina mimba ya mtu mwenye vitu hivi.” Akaongeza kusema, “Angalia kama utatambua kwamba pete hii na kamba yake pamoja na fimbo hii ni vya nani.”

26 Yuda akavitambua na kusema, “Yeye ana haki kuliko mimi, kwa kuwa sikumkabidhi kwa mwanangu Shela ili awe mkewe.” Tangu hapo hakukutana naye kimwili tena.

27 Wakati ulipofika wa kujifungua, kukawa na wana mapacha tumboni mwake.

28 Alipokuwa akijifungua, mmoja akatoa mkono wake nje, kwa hiyo mkunga akachukua uzi mwekundu na kuufunga mkononi mwa yule mtoto, akasema, “Huyu ametoka kwanza.”

29 Lakini alipourudisha mkono wake ndugu yake akaanza kutoka, naye akasema, “Hivi ndivyo ulivyotoka kwa nguvu!” Akaitwa Peresi.

30 Kisha ndugu yake, aliyekuwa na uzi mwekundu mkononi, akatoka, naye akaitwa Zera.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/GEN/38-500dfeb3411bbd2a3b1fcf5503e0d91c.mp3?version_id=1627—

Categories
Mwanzo

Mwanzo 39

Yosefu Na Mke Wa Potifa

1 Wakati huu Yosefu alikuwa amechukuliwa mpaka Misri. Mmisri aliyeitwa Potifa aliyekuwa mmojawapo wa maafisa wa Farao, mkuu wa ulinzi, akamnunua Yosefu kutoka kwa Waishmaeli waliomleta Misri.

2 Bwanaalikuwa pamoja na Yosefu, naye akastawi, Yosefu akaishi nyumbani kwa bwana wake Mmisri.

3 Potifa alipoona kuwaBwanaalikuwa pamoja na Yosefu na kwambaBwanaalimfanikisha kwa kila kitu alichokifanya,

4 Yosefu alipata kibali machoni pa Potifa, akamfanya mhudumu wake. Potifa akamweka kuwa msimamizi wa nyumba yake, naye akamkabidhi kuwa mwangalizi wa kila kitu alichokuwa nacho.

5 Kuanzia wakati huo Potifa alipomweka Yosefu kuwa msimamizi wa nyumba na mali zake zote alizokuwa nazo,Bwanaaliibariki nyumba ya Mmisri huyo kwa sababu ya Yosefu. Baraka yaBwanailikuwa juu ya kila kitu alichokuwa nacho Potifa, nyumbani na shambani.

6 Kwa hiyo Potifa akamwachia Yosefu uangalizi wa kila kitu alichokuwa nacho, Yosefu alipokuwa katika uongozi, Potifa hakuwa na sababu ya kujishughulisha na kitu chochote isipokuwa chakula alichokula.

Yosefu alikuwa mwenye umbo zuri na sura ya kuvutia;

7 baada ya kitambo mke wa Potifa akamtamani Yosefu, akamwambia, “Njoo, ukutane nami kimwili!”

8 Lakini Yosefu akakataa. Akamwambia yule mwanamke, “Mimi nikiwa katika uongozi, bwana wangu hahusiki na kitu chochote katika nyumba hii, kila kitu alicho nacho amenikabidhi.

9 Hapa nyumbani hakuna aliye mkuu kuliko mimi. Bwana wangu hakunizuilia kitu chochote isipokuwa wewe, kwa kuwa wewe ni mke wake. Nitawezaje basi kufanya uovu huu na kutenda dhambi dhidi ya Mungu?”

10 Ingawa yule mwanamke aliendelea kumshawishi Yosefu siku baada ya siku, Yosefu alikataa kukutana naye kimwili wala kukaa karibu naye.

11 Siku moja Yosefu akaingia ndani ya nyumba kufanya kazi zake, wala hapakuwepo na mfanyakazi yeyote ndani ya nyumba.

12 Mke wa Potifa akashika vazi Yosefu alilokuwa amevaa, akamwambia, “Njoo tukutane kimwili!” Lakini Yosefu akaacha vazi lake mkononi mwa huyo mwanamke, akatoka nje ya nyumba akikimbia.

13 Yule mwanamke alipoona kwamba Yosefu amemwachia vazi lake mkononi na kukimbilia nje ya nyumba,

14 akawaita watumishi wake wa nyumbani, akawaambia, “Tazameni! Huyu Mwebrania ameletwa hapa kutudhihaki! Aliingia hapa ndani ili akutane nami kimwili, lakini nikapiga kelele.

15 Aliposikia kelele za kuomba msaada, akaacha vazi lake kando yangu akakimbilia nje.”

16 Yule mwanamke akaliweka lile vazi karibu naye mpaka Potifa aliporudi nyumbani.

17 Ndipo akamweleza kisa hiki, akisema: “Yule mtumwa wa Kiebrania uliyetuletea alinijia ili kunidhihaki.

18 Lakini mara nilipopiga kelele kuomba msaada, akaliacha vazi lake kando yangu akakimbia nje ya nyumba.”

19 Potifa aliposikia kisa hiki mkewe alichomweleza, akisema, “Hivi ndivyo mtumwa wako alivyonitenda.” Hasira ya Potifa ikawaka.

20 Potifa akamchukua Yosefu na kumweka gerezani, mahali ambapo wahalifu wa mfalme walikuwa wamefungwa.

Lakini wakati Yosefu alipokuwa huko gerezani,

21 Bwanaalikuwa pamoja naye, akamhurumia na kumpa kibali mbele ya msimamizi wa gereza.

22 Kwa hiyo msimamizi wa gereza akamweka Yosefu awe mkuu wa wafungwa pamoja na kusimamia yote ambayo yalitendeka mle gerezani.

23 Msimamizi wa gereza hakujishughulisha tena na kitu chochote kilichokuwa chini ya uangalizi wa Yosefu, kwa sababuBwanaalikuwa pamoja na Yosefu akimfanikisha kwa kila alichofanya.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/GEN/39-ee7c1009eac9f887c6ba4734ba611dad.mp3?version_id=1627—