Categories
Ufunuo

Ufunuo 18

Kuanguka Kwa Babeli

1 Baada ya haya nikaona malaika mwingine akishuka kutoka mbinguni, akiwa na mamlaka makuu na dunia ikamulikiwa na mngʼao wake.

2 Naye akalia kwa nguvu kwa sauti kubwa, akisema:

“Umeanguka! Umeanguka Babeli Mkuu!

Umekuwa makao ya mashetani

na makazi ya kila pepo mchafu,

makazi ya kila ndege na kila mnyama achukizaye.

3 Kwa maana mataifa yote yamekunywa

mvinyo wa ghadhabu ya uasherati wake.

Nao wafalme wa dunia wamefanya uzinzi nao,

nao wafanyabiashara wa dunia

wametajirika kutokana na wingi wa utajiri wake.”

4 Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni ikisema:

“Tokeni katikati yake, enyi watu wangu,

ili msije mkashiriki dhambi zake,

ili msije mkapatwa na pigo lake lolote;

5 kwa kuwa dhambi zake zimelundikana hadi mbinguni,

naye Mungu ameukumbuka uhalifu wake.

6 Mtendee kama yeye alivyotenda;

umlipe mara mbili kwa ajili ya yale aliyotenda.

Katika kikombe chake mchanganyie

mara mbili ya kile alichochanganya.

7 Mpatie mateso na huzuni nyingi sawa na

utukufu na anasa alizojipatia.

Kwa kuwa moyoni mwake hujivuna, akisema,

‘Mimi ninatawala kama malkia;

mimi si mjane, wala sitaona huzuni kamwe.’

8 Kwa hiyo mapigo yatampata kwa siku moja:

mauti, maombolezo na njaa.

Naye atateketezwa kwa moto,

kwa maanaBwanaMungu amhukumuye ana nguvu.

9 “Wafalme wa dunia waliozini naye na kushiriki anasa zake watakapoona moshi wa kuungua kwake, watamlilia na kumwombolezea.

10 Kwa hofu kubwa ya mateso yake, watasimama mbali na kulia na wakisema:

“ ‘Ole! Ole, ee mji mkubwa,

ee Babeli mji wenye nguvu!

Hukumu yako imekuja katika saa moja!’

11 “Wafanyabiashara wa dunia watalia na kumwomboleza kwa sababu hakuna anunuaye bidhaa zao tena:

12 Bidhaa za dhahabu, za fedha, za vito vya thamani na vya lulu, kitani safi, nguo za rangi ya zambarau, hariri, nguo nyekundu, aina zote za miti ya udi, na vifaa vyote vya pembe za ndovu, vifaa vyote vya miti yenye thamani kuliko yote, shaba, chuma na marmar,

13 bidhaa za mdalasini, vikolezi, za uvumba, manemane, na uvumba wenye harufu nzuri, za divai, na mafuta ya zeituni, za unga mzuri na ngano; ngʼombe na kondoo; farasi na magari; na miili na roho za wanadamu.

14 “Watasema, ‘Yale matunda ambayo roho yako iliyatamani yamekoma. Utajiri wako wote na fahari yako vimetoweka, wala haviwezi kupatikana tena kamwe!’

15 Wale wafanyabiashara waliotajirika kwa bidhaa hizo kutoka kwake watasimama mbali naye kwa hofu kubwa ya mateso yanayompata. Watalia na kuomboleza wakipiga kelele wakisema:

16 “ ‘Ole! Ole, ee mji mkubwa,

uliyekuwa umevikwa mavazi ya kitani safi,

ya rangi ya zambarau na nyekundu,

ukimetameta kwa dhahabu,

vito vya thamani na lulu!

17 Katika muda wa saa moja utajiri wote mkubwa

kama huu umeangamia!’

“Kila nahodha, na wote wasafirio kwa meli, na wote wapatao kipato chao kutokana na bahari, watasimama mbali.

18 Watakapouona moshi wa kuungua kwake watalia wakisema, ‘Je, kulipata kuwako mji mkubwa kama huu?’

19 Nao watajirushia mavumbi vichwani mwao, huku wakilia na kuomboleza, wakisema:

“ ‘Ole! Ole, ee mji mkubwa,

mji ambao wote wenye meli baharini

walitajirika kupitia kwa mali zake!

Katika saa moja tu ameangamizwa!

20 Furahia kwa ajili yake, ee mbingu!

Furahini watakatifu, mitume na manabii!

Mungu amemhukumu

kwa vile alivyowatendea ninyi.’ ”

21 Kisha malaika mmoja mwenye nguvu akainua jiwe kubwa kama la kusagia akalitupa baharini akisema:

“Hivyo ndivyo mji mkubwa Babeli

utakavyotupwa chini kwa nguvu

wala hautaonekana tena.

22 Nyimbo za wapiga vinubi na waimbaji,

wapiga filimbi na wapiga tarumbeta

kamwe hazitasikika tena ndani yako.

Ndani yako kamwe hataonekana tena fundi

mwenye ujuzi wa aina yoyote.

Wala sauti ya jiwe la kusagia

kamwe haitasikika tena.

23 Mwanga wa taa

hautaangaza ndani yako tena.

Sauti ya bwana arusi na bibi arusi

kamwe haitasikika ndani yako tena.

Wafanyabiashara wako walikuwa watu maarufu wa dunia.

Mataifa yote yalipotoshwa kwa uchawi wako.

24 Ndani yake ilionekana damu ya manabii na ya watakatifu

na wote waliouawa duniani.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/REV/18-5c6f9d4423132dd19237fa2f94162b51.mp3?version_id=1627—

Categories
Ufunuo

Ufunuo 19

Shangwe Huko Mbinguni

1 Baada ya haya nikasikia sauti kama ya umati mkubwa mbinguni wakipiga kelele wakisema:

“Haleluya!

Wokovu na utukufu na uweza ni vya Mungu wetu,

2 kwa maana hukumu zake

ni za kweli na za haki.

Amemhukumu yule kahaba mkuu

aliyeuharibu ulimwengu kwa uzinzi wake.

Mungu amemlipiza kisasi

kwa ajili ya damu ya watumishi wake.”

3 Wakasema tena kwa nguvu:

“Haleluya!

Moshi wake huyo kahaba unapanda juu

milele na milele.”

4 Wale wazee ishirini na wanne pamoja na wale viumbe wanne wenye uhai wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu Mungu, aliyekuwa ameketi kwenye kile kiti cha enzi. Wakasema kwa sauti kuu:

“Amen, Haleluya!”

5 Kisha sauti ikatoka katika kile kiti cha enzi, ikisema:

“Msifuni Mungu wetu,

ninyi watumishi wake wote,

ninyi nyote mnaomcha,

wadogo kwa wakubwa!”

6 Kisha nikasikia sauti kama ya umati mkubwa, kama sauti ya maji mengi yaendayo kasi na kama ngurumo kubwa ya radi wakipiga kelele wakisema:

“Haleluya!

Kwa maanaBwanaMungu wetu Mwenyezi anatawala.

7 Tufurahi, tushangilie

na kumpa utukufu!

Kwa maana arusi ya Mwana-Kondoo imewadia

na bibi arusi wake amejiweka tayari.

8 Akapewa kitani safi, nyeupe

inayongʼaa, ili avae.”

(Hiyo kitani safi inawakilisha matendo ya haki ya watakatifu.)

9 Ndipo malaika akaniambia, “Andika: ‘Wamebarikiwa wale walioalikwa kwenye karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo!’ ” Naye akaongeza kusema, “Haya ndiyo maneno ya kweli ya Mungu.”

10 Ndipo nikaanguka kifudifudi miguuni pake ili kumwabudu, lakini yeye akaniambia, “Usifanye hivyo! Mimi pia ni mtumishi mwenzako pamoja na ndugu zako walio na ushuhuda wa Yesu. Mwabudu Mungu! Maana ushuhuda wa Yesu ndio roho ya unabii.”

Aliyepanda Farasi Mweupe

11 Kisha nikaona mbingu imefunguka na hapo mbele yangu akiwepo farasi mweupe, ambaye yeye aliyempanda aliitwa Mwaminifu na Kweli. Yeye huhukumu kwa haki na kufanya vita.

12 Macho yake ni kama miali ya moto na juu ya kichwa chake kuna taji nyingi. Ana jina lililoandikwa ambalo hakuna mtu yeyote anayelijua isipokuwa yeye mwenyewe.

13 Amevaa joho lililochoviwa katika damu, na Jina lake ni “Neno la Mungu.”

14 Majeshi ya mbinguni walikuwa wakimfuata, wakiwa wamepanda farasi weupe, hali wamevaa mavazi ya kitani safi, nyeupe na nzuri.

15 Kinywani mwake hutoka upanga mkali ambao kwa huo atayaangusha mataifa. “Atayatawala kwa fimbo yake ya utawala ya chuma.” Hulikanyaga shinikizo la mvinyo wa ghadhabu ya Mungu Mwenyezi.

16 Kwenye joho lake na paja lake pameandikwa jina hili:

Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana.

Mnyama Na Majeshi Yake Yashindwa

17 Nami nikamwona malaika amesimama ndani kwenye jua, akaita ndege wote warukao angani kwa sauti kuu, “Njooni, kusanyikeni kwa ajili ya karamu kubwa ya Mungu,

18 ili mpate kula nyama ya wafalme na ya majemadari, ya mashujaa, ya farasi na ya wapanda farasi, nyama ya wanadamu, wote walio huru na watumwa, wadogo na wakubwa.”

19 Kisha nikamwona yule mnyama na wafalme wa dunia pamoja na majeshi yao wakiwa wamekusanyika pamoja ili kufanya vita dhidi ya yule aliyempanda farasi pamoja na jeshi lake.

20 Lakini yule mnyama akakamatwa pamoja na huyo nabii wa uongo ambaye alikuwa amefanya ishara kwa niaba ya huyo mnyama, ambaye kwa ishara hizi aliwadanganya wale waliopokea chapa ya huyo mnyama na kuiabudu sanamu yake. Hawa wawili wakatupwa wakiwa hai ndani ya ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti.

21 Wale waliosalia waliuawa kwa upanga uliotoka kinywani mwa yule aliyekuwa amempanda farasi nao ndege wote wakajishibisha kwa nyama yao.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/REV/19-f5a2e21f2e70e7332e5a0e96f03d9a05.mp3?version_id=1627—

Categories
Ufunuo

Ufunuo 20

Utawala Wa Miaka Elfu Moja

1 Kisha nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni, akiwa ameshika ufunguo wa lile Shimo na mnyororo mkubwa mkononi mwake.

2 Akalishika lile joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ndiye ibilisi au Shetani, naye akamfunga kwa muda wa miaka 1,000.

3 Akamtupa katika lile Shimo, akamfunga humo na kulitia lakiri, ili kumzuia asiendelee kudanganya mataifa mpaka hiyo miaka 1,000 itimie. Baada ya hayo lazima afunguliwe kwa muda mfupi.

4 Kisha nikaona viti vya enzi vilivyokuwa vimekaliwa na hao waliopewa mamlaka ya kuhukumu, na nikaona roho za wale waliokatwa vichwa kwa sababu ya ushuhuda wa Yesu na kwa sababu ya neno la Mungu. Hawakuwa wamemsujudu huyo mnyama wala sanamu yake wala hawakupokea ile chapa yake kwenye vipaji vya nyuso zao au kwenye mikono yao. Wakawa hai na kutawala pamoja na Kristo miaka 1,000.

5 (Wafu waliosalia hawakufufuka mpaka ilipotimia hiyo miaka 1,000.) Huu ndio ufufuo wa kwanza.

6 Waliobarikiwa na walio watakatifu ni wale walio na sehemu katika ufufuo wa kwanza. Hao mauti ya pili haina nguvu juu yao, bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye kwa muda wa miaka 1,000.

Kuhukumiwa Kwa Shetani

7 Hiyo miaka 1,000 itakapotimia, Shetani atafunguliwa kutoka kifungoni mwake,

8 naye atatoka ili kuyadanganya mataifa yaliyopo katika pembe nne za dunia, yaani, Gogu na Magogu apate kuwakusanya tayari kwa vita. Idadi yao ni kama mchanga ulioko pwani.

9 Nao walitembea katika eneo lote la dunia, wakaizunguka kambi ya watakatifu na ule mji unaopendwa. Lakini moto ukashuka kutoka mbinguni na kuwateketeza.

10 Naye ibilisi aliyewadanganya akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti walikokuwa wametupwa yule mnyama na yule nabii wa uongo. Watateswa humo usiku na mchana, milele na milele.

Wafu Wanahukumiwa

11 Kisha nikaona kiti kikubwa cheupe cha enzi pamoja na yeye aliyeketi juu yake. Dunia na mbingu zikaukimbia uso wake wala mahali pao hapakuonekana.

12 Nami nikawaona wafu wakubwa na wadogo, wakiwa wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi na vitabu vikafunguliwa. Pia kitabu kingine kikafunguliwa ambacho ni kitabu cha uzima. Hao wafu wakahukumiwa sawasawa na matendo yao kama yalivyoandikwa ndani ya hivyo vitabu.

13 Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake, nayo mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Kila mtu akahukumiwa kulingana na yale aliyoyatenda.

14 Kisha mauti na Kuzimu zikatupwa katika ziwa la moto. Hii ndio mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto.

15 Iwapo mtu jina lake halikuonekana katika kile kitabu cha uzima, alitupwa ndani ya lile ziwa la moto.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/REV/20-a2dbaa73e8e7aa1a332b56554acf7b9f.mp3?version_id=1627—

Categories
Ufunuo

Ufunuo 21

Mbingu Mpya Na Nchi Mpya

1 Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya, kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza vimekwisha kupita, wala hapakuwepo na bahari tena.

2 Nikaona Mji Mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, ukiwa umeandaliwa kama bibi arusi aliyepambwa kwa ajili ya mumewe.

3 Nami nikasikia sauti kubwa kutoka kile kiti cha enzi ikisema, “Sasa makao ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atakaa pamoja nao. Yeye atakuwa Mungu wao nao watakuwa watu wake, naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.

4 Atafuta kila chozi kutoka macho yao. Mauti haitakuwepo tena, wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu, kwa maana mambo ya kwanza yamekwisha kupita.”

5 Naye yule aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi akasema, “Tazama, nayafanya mambo yote kuwa mapya!” Kisha akasema, “Andika haya, maana maneno haya ni ya kuaminika tena ni kweli.”

6 Akaniambia, “Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Yeye aonaye kiu nitampa kunywa kutoka chemchemi ya maji ya uzima bila gharama yoyote.

7 Yeye ashindaye atayarithi haya yote, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu.

8 Lakini waoga, wasioamini, wachafu, wauaji, wazinzi, wachawi, waabudu sanamu, pamoja na waongo wote, mahali pao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.”

9 Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na yale mabakuli saba ya hayo mapigo saba ya mwisho akaja akaniambia, “Njoo, nami nitakuonyesha bibi arusi, yaani, mke wa Mwana-Kondoo.”

10 Naye akanichukua katika Roho hadi kwenye mlima mkubwa na mrefu, akanionyesha ule Mji Mtakatifu, Yerusalemu, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu.

11 Ulikuwa ukingʼaa kwa utukufu wa Mungu kama kito chenye thamani sana, kama yaspi, safi kama kioo.

12 Ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu wenye malango kumi na mawili, pakiwa na malaika kumi na wawili kwenye hayo malango. Kwenye malango hayo yaliandikwa majina ya yale makabila kumi na mawili ya Israeli.

13 Kulikuwa na malango matatu upande wa mashariki, matatu upande wa kaskazini, matatu upande wa kusini na matatu upande wa magharibi.

14 Ukuta wa huo mji ulikuwa na misingi kumi na miwili, na juu yake yaliandikwa majina ya wale mitume kumi na wawili wa Mwana-Kondoo.

15 Huyo malaika aliyesema nami alikuwa na ufito wa dhahabu wa kupimia huo mji, malango yake na kuta zake.

16 Mji huo ulikuwa mraba, urefu wake ulikuwa sawa na upana wake. Akaupima huo mji kwa huo ufito akakuta una kama kilomita 2,200;urefu wake na upana wake na kwenda juu kwake vilikuwa sawa.

17 Akaupima ukuta wake, ulikuwa na unene wa dhiraa 144kwa kipimo cha kibinadamu ambacho huyo malaika alikuwa akikitumia.

18 Ukuta huo ulijengwa kwa yaspi hali mji wenyewe ulijengwa kwa dhahabu safi, ikingʼaa kama kioo.

19 Misingi ya kuta za mji huo zilipambwa kwa kila aina ya kito cha thamani. Msingi wa kwanza ulikuwa wa yaspi, wa pili yakuti samawi, wa tatu kalkedoni, wa nne zumaridi,

20 wa tano sardoniki, wa sita akiki, wa saba krisolitho, wa nane zabarajadi, wa tisa yakuti manjano, wa kumi krisopraso, wa kumi na moja hiakintho, wa kumi na mbili amethisto.

21 Yale malango kumi na mbili yalikuwa ni lulu kumi na mbili, kila lango lilikuwa limetengenezwa kwa lulu moja. Barabara kuu ya mji huo ilikuwa ya dhahabu safi ingʼaayo kama kioo.

22 Sikuona Hekalu ndani ya huo mji kwa sababuBwanaMungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo ndio hekalu lake.

23 Ule mji hauhitaji jua wala mwezi kuuangazia, kwa sababu utukufu wa Mungu ndio nuru yake na Mwana-Kondoo ndiye taa yake.

24 Mataifa yatatembea yakiangaziwa na nuru yake na wafalme wa duniani wataleta fahari yao ndani yake.

25 Malango yake hayatafungwa kamwe, kwa maana hakutakuwa na usiku humo.

26 Utukufu na heshima za mataifa zitaletwa humo.

27 Lakini kitu kichafu hakitaingia humo kamwe, wala mtu yeyote atendaye mambo ya aibu au ya udanganyifu. Bali watakaoingia humo ni wale tu ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/REV/21-bd5b856884801cce591a109561f60709.mp3?version_id=1627—

Categories
Ufunuo

Ufunuo 22

Mto Wa Maji Ya Uzima

1 Kisha yule malaika akanionyesha mto wa maji ya uzima, maangavu kama kioo yakitiririka kutoka kwenye kile kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo,

2 kupitia katikati ya barabara kuu ya huo mji. Kwenye kila upande wa huo mto kulikuwa na mti wa uzima utoao matunda ya aina kumi na mbili, ukizaa matunda yake kila mwezi. Nayo majani ya mti huo ni kwa ajili ya uponyaji wa mataifa.

3 Katika mji huo hakutakuwa tena na laana, bali kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kitakuwamo humo na watumishi wake watamtumikia,

4 nao watamwona uso wake na Jina lake litakuwa kwenye vipaji vya nyuso zao.

5 Usiku hautakuwako tena, wala hawatahitaji mwanga wa taa au wa jua, kwa maanaBwanaMungu atakuwa nuru yao, nao watatawala milele na milele.

6 Kisha yule malaika akaniambia, “Maneno haya ni ya kuaminika na kweli.Bwana, Mungu wa roho za manabii, alimtuma malaika wake kuwaonyesha watumishi wake yale ambayo hayana budi kutukia upesi.”

Bwana Yesu Anakuja

7 “Tazama, naja upesi! Amebarikiwa yeye ayashikaye maneno ya unabii wa kitabu hiki.”

8 Mimi, Yohana, ndiye niliyesikia na kuyaona mambo haya. Nami nilipokwisha kuyasikia na kuyaona, nilianguka chini nikasujudu miguuni pa yule malaika aliyekuwa akinionyesha mambo hayo.

9 Lakini yeye akaniambia, “Usifanye hivyo! Mimi ni mtumishi pamoja nawe na ndugu zako manabii na wote wanaoyashika maneno ya kitabu hiki. Msujudie Mungu!”

10 Kisha akaniambia, “Usiyafunge maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, kwa sababu wakati umekaribia.

11 Atendaye mabaya na aendelee kutenda mabaya, aliye mchafu na aendelee kuwa mchafu, yeye atendaye haki na aendelee kutenda haki, na yeye aliye mtakatifu na aendelee kuwa mtakatifu.”

12 “Tazama, naja upesi! Thawabu yangu i mkononi mwangu, nami nitampa kila mtu sawasawa na alivyotenda.

13 Mimi ni Alfa na Omega, wa Kwanza na wa Mwisho, Mwanzo na Mwisho.

14 “Wamebarikiwa wale wafuao mavazi yao, ili wapate haki ya kuuendea huo mti wa uzima na kuuingia huo mji kupitia kwenye malango yake.

15 Huko nje wako mbwa, wachawi, wazinzi, wauaji, waabudu sanamu, na kila mtu apendaye udanganyifu na kuufanya.

16 “Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu kushuhudia mambo haya kwa ajili ya makanisa. Mimi ndimi Shina na Mzao wa Daudi, ile Nyota ya Asubuhi ingʼaayo.”

17 Roho na bibi arusi wanasema, “Njoo!” Naye asikiaye na aseme, “Njoo!” Yeyote mwenye kiu na aje, na kila anayetaka na anywe maji ya uzima bure.

18 Namwonya kila mtu asikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki: Mtu yeyote akiongeza humo chochote, Mungu atamwongezea mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki.

19 Kama mtu yeyote akipunguza humo chochote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.

20 Yeye anayeshuhudia mambo haya asema, “Hakika, naja upesi!”

Amen. Njoo, Bwana Yesu.

21 Neema ya Bwana Yesu iwe na watakatifu wote. Amen.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/REV/22-1909eb4f43e6fc880212503a7b022f29.mp3?version_id=1627—